Hotuba yangu jimboni Kigoma | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Hotuba yangu jimboni Kigoma

Discussion in 'Great Thinkers' started by Zitto, Aug 25, 2009.

 1. Zitto

  Zitto MP Kigoma Urban

  #1
  Aug 25, 2009
  Joined: Mar 2, 2007
  Messages: 1,197
  Likes Received: 109
  Trophy Points: 160
  Wakubwa salaam,

  Ninawaletea hotuba yangu jimboni Kigoma. Asante


  HOTUBA YA MBUNGE WA KIGOMA KASKAZINI NDUGU ZITTO ZUBERI KABWE KWENYE UFUNGUZI WA MKUTANO MKUU WA CHADEMA UCHAGUZI JIMBO LA KIGOMA KASKAZINI.


  KALINZI, AGOSTI15, 2009.


  Ndugu wajumbe, ninayo heshima kubwa kuwashukuru kwa jitihada mlizofanya kuhakikisha leo karibu viongozi wote wa vijiji vya jimbo la Kigoma Kaskazini tunakutana hapa kata ya Kalinzi kwa ajili ya Mkutano Mkuu wa CHADEMA. Natambua kuwa mnafanya kazi katika mazingira magumu, lakini mnafanya mambo makubwa sana..........

  Lakini zaidi nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutusaidia uhai hadi leo hii kupata fursa ya kufanya mkutano huu muhimu sana kwa mustakabali wa chama na hatima ya demokrasia, kuanzia ngazi za msingi, vijiji vyetu, kata, jimbo, na kimsingi Taifa kwa ujumla.

  Sote tunajua kuwa huu ni mkutano mkuu wa pili kikatiba tangu mnichague kuwa mbunge wa jimbo la Kigoma kaskazini mwaka 2005.

  Kuna wengi tulikuwa nao katika mkutano mkuu uliopita, lakini leo hatunao kwa sababu mbalimbali. Wapo waliotangulia mbele ya haki, Mwenyezi Mungu awalaze mahala pema! Wengine hatunao kwasababu hawakupata fursa kutokana na michakato ya chaguzi kwenye vijiji na kata zao;Na hiyo ndiyo demokrasia yenyewe tuliyoamua kufuata kama chama. Wapo ambao wamekwenda katika vyama vingine na wengine tunao hapa kama wajumbe wapya kutoka vyama vingine vya siasa. Sote sasa ni familia moja ya CHADEMA yenye lengo la kutoa uongozi mbadala na kuchochoea maendeleo katika Jimbo letu.

  Ndugu wajumbe;
  Wengi tumekuwa tukikutana, kuwasiliana na kujadili katika nyakati tofauti ninapokuwa kwenye ziara za jimbo letu, na hata nje ya jimbo letu katika harakati mbalimbli za kuchochea maendeleo. Ninawashukuru kwa kazi yote tuliyoifanya, na kwakuwa leo tumekutana tena, ni fursa basi kuangalia kwa pamoja kama tumefanikiwa kufanya nini kuelekea malengo tuliyo jiwekea.

  Ndugu wajumbe;
  Ni kazi ya Mkutano Mkuu wa chama kutafakari kuhusu kazi ambazo kama chama tumezifanya kuelekea malengo tuliyojiwekea. Chama chochote cha siasa kina kazi kuu za aina mbili; kuna kazi za chama ndani ya chama, na kuna kazi za chama kwenye jamii. Kazi za chama ndani ya chama ni majukumu yote ambayo tunayafanya kuhakikisha chama kinajiendesha, kinafanya vikao, kinatekeleza na kusimamia maamuzi ya vikao kwa lengo la kuhakikisha kinajenga mtandao imara wa chama kuanzia ngazi za msingi. Kwahiyo, tunapokutana leo kupima kazi tunazofanya kuelekea malengo yetu, tunapaswa kujiuliza tumefanya nini kuelekea ujenzi imara wa chama, tumefanya nini kuhakikisha uongozi wa pamoja ndani ya chama, tumefanya nini kuhakikisha tunawaunganisha zaidi wanachama kuanzia ngazi ya msingi, vijiji, kata mpaka jimbo.

  Kazi ya pili ya chama ni ujenzi wa chama kwenye jamii. Hii ni jumla ya majukumu yote ambayo viongozi tunayafanya kutetea na kuhakikisha maendeleo kwa jamii yetu..Hii ni kazi muhimu sana kwa chama. Ni muhimu kwasababu ni kazi hii inayomfanya mtu wa kawaida kuona sababu ya kujiunga na chama. Kwahiyo tunapokutana leo katika Mkutano Mkuu, tunapaswa kujiuliza,sasa ni takribani mwaka mmoja kuelekea uchaguzi, Tumefanya nini kutetea na kuhakikisha maendeleo kwa jamii tunamoishi?

  Ndugu wajumbe;
  Mnafahamu kwamba tangu kurejeshwa mfumo wa vyama vingi, ni kipindi hiki ambacho jimbo letu limefanikiwa kuongozwa na upinzani, tena kupitia chama chetu CHADEMA. Kwa hiyo Kigoma Kaskazini, CHADEMA ndio chama chenye Mbunge, ingawa sio chama tawala kwani hatuna madiwani wengi wala wenyeviti wa vijiji. Ndio maana ni lazima viongozi wawe na ujuzi wa kujua namna ya kuendesha siasa ukiwa chama chenye uwakilishi Bungeni. Nasema ni lazima kwasababu maswali mengi yanayohusu maendeleo ya jimbo hili ni sisi viongozi wa CHADEMA wenye jukumu la kutoa majibu yake. Nasema ni sisi, na sio mimi kwasababu siwezi kukutana na kila mwananchi ndani ya jimbo hili kumweleza tunafanya nini? Na Tumekwishafanya nini?. Ni jukumu la viongozi wote kujua wenyeviti wa vijiji kupitia CHADEMA wamefanya nini kuelekea malengo yetu? Madiwani kwa tiketi ya CHADEMA wamefanya nini kuelekea malengo yetu? Na Mbunge wa Jimbo lenu nimefanya nini kuelekea malengo tuliyojiwekea.

  Ndugu wajumbe;
  Mnakumbuka niliwaambia wakati wa kampeni mwaka 2005, kuwa haiwezekani sehemu zingine za nchi serikali inabandua lami na kuweka lami ilhali majimbo mengine mtoto anaweza kuzaliwa, kusoma shule ya msingi kijijini, sekondari kwenye kata, chuo cha ualimu kwenye wilaya, na kufanya kazi ndani ya wilaya hata kustaafu kabla ya kuona lami. Nikasema hili haliwezekani, na nikawaahidi kupigania ujenzi wa barabara ya Mwandiga Manyovu kwa kuwa nilijua kuna kila sababu ya barabara hii kujengwa kiwango cha lami, na hakuna sababu hata moja kuzuia hili.

  Niliposhika Ubunge wa Jimbo hili, nilikuta bajeti ya Barabara ya Mwandiga – Manyovu ni shilingi 800 milioni tu katika Bajeti ya mwaka 2005/2006. Nilikuta mpango wa serikali ya CCM ni kuweka lami inayoitwa ‘Otta Seal’ ambayo ni teknolojia ya Afrika Kusini. Nilikataa lami hii kwani haidumu na mvua tatu tu za Kigoma zingeweza kuondoa lami hiyo! Ndani ya Kamati za Bunge ya miundombinu na Fedha na Uchumi na ndani ya Bunge la Bajeti la 2006/2007 nilikataa kata kata mradi walioutaka na kubadili fedha hizo kwenda kufanya upembuzi yakinifu. Matokeo ya hatua hizo za Mbunge wa Jimbo la Kigoma Kaskazini ndio yanayoonekana leo katika mradi wa mabilioni ya ujenzi wa barabara ya Mwandiga – Manyovu. Bajeti zilizofuata niliweza kufuatilia na kuongeza fedha kutoka 800 milioni nilizozikuta mpaka Bilioni 7 mwaka 2009/2010.

  Napenda nimshukuru kwa dhati kabisa aliyekuwa Waziri wa Miundombinu ndugu Andrew Chenge na Katibu Mkuu ndugu Enos Bukuku kwa msaada mkubwa walionipa kuhakikisha tunajenga barabara hii kwa Lami. Napenda kumshukuru aliyekuwa Waziri wa Fedha ndugu Zakia Meghji kwa kuelewa tatizo letu na kutenga fedha. Nawashukuru sana TANROADS chini ya Mkurugenzi Mkuu ndugu Mrema kwa ushirikiano wanaoendelea kutoa katika Mradi huu.

  Nimepigania kuhakikisha hilo, mchakato wa ujenzi wa barabara umeanza, viongozi wa CCM wanaanza kuweweseka na kudai kuwa wanatekeleza ilani ya CCM. Mimi nawaambia viongozi wenzangu, mnapaswa kuwauliza ni wapi ndani ya Ilani ya CCM wameahidi kujenga barabara ya Mwandiga - Manyovu kwa kiwango cha lami?. Hakuna! Mimi najua nimefanya nini kuhakikisha hili linafanyika! Ndio sababu mlinichagua. Viongozi wa CHADEMA mnao wajibu wa kuwaliza viongozi hao wanaojipitisha huku kwa aibu na kudai eti ni Ilani ya CCM inayojenga barabara ya Mwandiga - Manyovu.

  Hii ni barabara ya kwanza ya kiwango cha lami kujengwa ndani ya jimbo hili na Mkoa huu tangu Tanzania ipate uhuru. Mnapaswa kuwauliza walikuwa wapi miaka yote hiyo wakumbuke leo? Mnapaswa kuwaliza, Mkoa wa kigoma tuna majimbo saba, huku sita yakiongozwa na CCM. Waulizeni kwanini hawakwenda kujenga majimbo yaliyo chini ya CCM?. Kwanini Kigoma Kaskazini, kwanini leo? Mimi najua ni kwanini Kigoma kaskazini, najua kwanini leo, ndio sababu mlinichagua!..Na ndio maana nawaambia, ninyi viongozi mna kila sababu ya kutembea kifua mbele kwa kazi hii!

  Ndugu wajumbe;
  Leo viongozi wote wa vijiji mko hapa. Wakati wa kampeni mwaka 2005, ni vijiji 5 tu kati ya 32 vilikuwa vimepimwa. Nikaahidi kuhakikisha vijiji vyote ndani ya jimbo langu vinapimwa ndani ya miaka 5 ya uongozi wangu. Leo ni mwaka mmoja kabla ya uchaguzi, Naomba niwaulize viongozi wa vijiji, Ni kijiji gani katika jimbo hili hakijapimwa? Haya ndio mambo mnapaswa kuwaambia wana CCM wanaojipitisha huku kudanganya wananchi kuwa mbunge wenu hafanyi kazi za jimbo. Waulizeni kwanini vijiji hivi havikupimwa miaka yote hii isipokuwa leo? Lazima muwaulize kwanini hawajafanya hivi Kasulu wala Kibondo?. Ina maana serikali ya CCM inawapenda wananchi waliochagua CHADEMA mkoani Kigoma kuliko majimbo walio chagua CCM? Msipowauliza na kuwaambia wananchi maswali haya mtakuwa hamkitendei haki chama chenu.

  Ndugu wajumbe;
  Niliwaambia mwaka mwaka 2005 wakati wa kampeni, nitatumia asilimia 30 ya mshahara wangu kuwasomesha watoto wa wanaotoka familia duni, zisizojiweza kabisa kiuchumi kama mchango wangu kwenu, kwani mimi nimezaliwa na kuishi katika familia duni, ninatambua mchango wa elimu katika kuinasua familia kutoka mduara wa ufukara uliokithiri. Nimekwenda shule kwa kutembea kwa mguu! Nilianza mara moja kutekeleza ahadi hiyo. Nimefanya hivyo, na mpaka sasa ninatoa zaidi ya asilimia 30 ya mshahara wangu. Na leo vijana 198 kutoka vijiji vyote vya jimbo langu wapo sekondari kwa mchango huo. Haya siyafanyi kwa bahati mbaya wala bahati nasibu! Ni mpango na nidhamira. Mkitaka kuona tofauti, waulizeni hata jirani zenu walio chini ya CCM, kwao wabunge wao wanasomesha watoto wangapi wa kimasikini? Kwao wamefanya nini?

  Ni muhimu mkawauliza hao wanaojipitisha jimbo hili kwa hoja za eti mbunge wenu hamko nae kila siku. Nilipogombea ubunge nilitoa ahadi, na nilijua nitapimwa kwa ahadi nilizotoa. Waulizeni kipi bora kati ya mbunge kuwa na wananchi kila siku jimboni au mbunge kusomesha watoto? Waambieni watoe hoja kuhusu ahadi nilizotoa. Mbunge niliyechukua nafasi yake mwaka 2005 alikuwa mbunge kwa miaka 15 na alikuwa anakaa sana jimboni. Ninyi mnajua hiyo miaka 15 tumepata maendeleo gani.

  Ndugu wajumbe;
  Kabla sijaingia madarakani, Tarafa ya Mwandiga haikuwa na kituo cha afya. Leo kituo cha afya kimeanza kujengwa tarafa ya Mwandiga. Tayari tumeshapata mchango wa Shirika la NHIF katika mradi huu.
  Niliahidi kuhakikisha tunajenga mabweni kwa wanafunzi wa kike, katika jimbo letu. Leo kwa ushawishi na mchango wangu wa moja kwa moja nimefanikisha ujenzi wa bweni la wanafunzi wa kike katika Shule ya Sekondari Bugamba kwa kushirikiana na Shirika la TANAPA. Mimi binafsi nimetoa fedha za ujenzi huu. Nasikia kuna baadhi ya watu CCM wanasema wao ndio wamejenga bweni hili. Aibu tupu hii kwani wao wanajua ni juhudi za nani. Tayari nimefanya mazungumzo na TANAPA ili mwaka huu wa fedha tujenge bweni katika Sekondari ya Bitale. Haya ndio maswala ambayo Mbunge anapaswa kupimwa nayo na ninyi kama viongozi wa CHADEMA vijijini lazima muhakikishe wananchi wanajadili na kukipima CHADEMA kwa ahadi zake. Na sio majungu yasiyopimika.

  Ndugu wajumbe;
  Kuna mengi tumeyafanya kwa kipindi kifupi na katika mazingira magumu. Nilipoingia madarakani tu, nilihakikisha wakulima wa kahawa wanapata soko la uhakika la kahawa ili kuongeza tija ya kilimo kwa maisha ya mkulima. Nikawaunganisha wakulima wa kahawa wa jimbo letu na soko la uhakika Marekani, na sasa kuna mradi wa milioni 300 kwa ajili ya kuboresha na kutafuta soko la kahawa. Wanachama wa chama cha ushirika cha KANYOVU chini ya uongozi dhabiti wa Mzee Yahaya Mahwisa wanajua juhudi hizi na mafanikio yake. Ni kazi hizi zinazonifanya niamini kwamba ninyi viongozi wa CHADEMA mna kila sababu ya kwenda kifua mbele kwasababu mengi tunayoyafanya leo, hayakufanyika wakati jimbo hili likiwa chini ya CCM, na hayafanyiki majimbo mengi ya jirani zenu chini ya CCM. Ni lazima muoneshe tofauti ya Maendeleo ya jimbo hili wakati wa CCM na wakati wa CHADEMA ili wananchi wapime.

  Ndugu wajumbe;
  Niliwaambia wakati wakati wa kampeni, kwamba ninataka kwa kipindi chote cha uongozi wangu wa jimbo hili, sura ya jimbo ibadilike ili nitakapomaliza muda wangu yabaki mambo ambayo mtayakumbuka na kurejea kipindi cha uongozi wa jimbo hili chini ya CHADEMA. Leo Mwandiga Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) limeanza mpango wa kujenga kituo kikubwa kabisa cha mabasi. Upembuzi umeanza kufanyika na michoro kuuchorwa kwa ajili ya mradi huu mkubwa sana wa mabilioni fedha na ambao utabadili kabisa sura ya Mkoa wa Kigoma.

  Leo tunaongea hapa, lakini ninawaambia ndani ya siku mbili , kata za Mwamgongo na Kagunga zitakuwa zimepata mawasiliano ya simu. Niliahidi kuhakikisha kuwa kunakuwa na mawasiliano ya simu katika Jimbo zima. Kampuni ya Zain imejenga minara Mwamgongo, Zashe na Kagunga. Jana nimezungumza kwa mara ya mwisho na ndugu zangu wa Zain na tumekubaliana kuwa siku nitakayokuwa kuwa Kagunga nitazungumza nao kwa kutumia simu yangu ya Zain.................... kutokea Kagunga! Haya ndio mnapaswa kunipa nayo, haya ndiyo mnapaswa kuipima kwayo CHADEMA.

  Kata ya kagunga walikuwa na changamoto ya Soko. Niliahidi katika Kampeni kuwa nitahakikisha kuwa tunapata soko Kagunga. Nilifuatilia suala hili ndani ya Bunge. Nilifuatilia suala hili katika vikao vya Madiwani. Soko limeanza kujengwa Kagunga na Kagunga haitakuwa ile ile tena. Maana kuna mradi mkubwa zaidi.

  Ndugu Wajumbe,
  Leo ninapozungumza nanyi kuna mradi mkubwa sana wa kujenga Gati Kagunga na hivyo kuifanya kuwa Bandari. Kwa juhudi zangu binafsi kama Mbunge nimehakikisha kuwa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) wanaingiza Kagunga katika miradi ya magati Ziwa Tanganyika. Mradi wa Gati la Kagunga utagharimu zaidi ya shilingi 600 milioni. Gati hili litachochea maendeleo Kagunga kwa kiasi kikubwa sana na kuufanya mpaka wa Kagunga kuchangamka kama ilivyo Namanga na Tunduru. Hii ndio kazi ya Mbunge wenu. Hii ndio kazi mnayopaswa kujivunia.......!

  Ndugu Wajumbe,
  Mimi niseme wazi, na nikiri kwamba nina majukumu mengi ya Kitaifa na Kimataifa. Nimekuwa mjumbe wa Kamati ya Uanzishwaji wa Afrika mashariki, Kamati ya kuchunguza mikataba ya madini nchini, nimekuwa kwenye timu ya kumshauri Rais wa Ujerumani kuhusu masuala ya uchumi wa bara la Afrika, Na sasa mimi ni Mwenyekiti wa mwenza wa Mtandao wa wabunge wanaoshughulikia migogoro ya kisiasa duniani, Mwenyekiti mwenza wangu ni mbunge katika bunge la Ujerumani. Yote haya yanakijengea heshima kubwa chama chetu, mkoa wetu, na hasa jimbo letu. Leo ukiwa mkoa wowote Tanzania ukisema natoka Kigoma, unaulizwa kwa Zitto Kabwe?

  Sasa kuna wana CCM wasio na hoja wanasema, eti mbunge wenu ni wa kitaifa, hawajali jimbo lake. Mimi nawaambia, ni kweli ninafanya majukumu mengi kama mbunge wa nchi hii. Wengine wanaweza kudhani nikiwa sipo Kigoma labda nipo Dar es Salaam. Lakini mimi nawaambia nimeumbwa kutumikia wananchi. Nikiwa sipo jimboni kwangu, nipo majimbo mengine tunaendesha harakati, tunatetea maslahi ya Taifa. Na ni kwasababu ya harakati hizo, Mbunge wenu nimejijengea heshima kubwa na uwezo wa kuibana serikali itekeleze baadhi ya mambo mnayoyaona jimboni hapa, ambayo hayafanyiki kwenye majimbo jirani yenu.

  Mimi ninawaapia, siwezi kuacha kupambana na viongozi wabovu ndani ya serikali ya CCM kama ilivyo Buzwagi, kwa propaganda za CCM eti kwasababu Buzwagi haipo Kigoma kaskazini. Hilo siwezi, na nipo tayari kuhukumiwa kwa hilo. Ninasema haya kwasababu ninaamini hata barabara hii ya lami ya Mwandiga - Manyovu , ambayo ni ya kwanza kujengwa Kigoma tangu uhuru , haijengwi kwa pesa za Halmashauri ya wilaya ya Kigoma. Ni serikali kuu, ambayo kama tutaiacha iendelee kupoteza mapato kwa ufisadi, miradi mingi mikubwa kama hii itakwama. Huwezi kuacha kumkamata fisadi eti kwasababu hajaiba Kigoma Kaskazini. Fedha za kodi zinazolipwa Buzwagi ndio zitakazojenga Barabara yetu Kigoma, fedha za malipo ya wafanyakazi katika migodi ya madini ndio zinazofanya NSSF wajenge miradi Kigoma ukiwemo mradi wa Kituo cha Mabasi cha Kimataifa Mwandiga. Mamlaka ya Bandari Tanzania inajenga Gati la Kagunga kwa fedha za tozo kwa waagizaji Bidhaa kutoka nje na kupitia Bandari ya Dar es Salaam yakiwemo makampuni ya Madini ambao Mbunge wenu amejipambanua kupambana nao ili nchi ifaidike na rasilimali ya madini.

  Ndugu Wajumbe,
  Hao wanaosema kuwa mimi ni Mbunge wa Taifa na hivyo nimeliacha jimbo ni wapuuzi wachache ambao hawajui nchi inaendeshwa namna gani. Kuwa Mbunge wa Taifa ni sifa kwenu ninyi maana Bunge lina wajumbe 320 na ni wachache sana ambao tunaonekana kuwa wa Taifa. Miradi yote hii ya maendeleo inayoendelea hivi sasa inakuja kwa sababu mimi ni Mbunge wa Taifa. Nimepata heshima ya kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mashirika ya Umma kwa sababu yenu. Msingenichagua kuwa Mbunge nisingepata heshima hizi ninazopata leo. Ninawashukuru sana. Asanteni. Hivyo, nipimeni na wabunge wengine ambao sio wa Taifa katika maendeleo!

  Ndugu wajumbe,
  Ninawatakia kila la kheri katika Mkutano Mkuu huu wa uchaguzi. Ninawaomba mchague viongozi ambao watapelekea chama chetu kushinda Vijiji vingi katika uchaguzi unaotukabili. Ninawaomba mchague viongozi ambao watatupelekea kushinda madiwani wengi zaidi. Mchague viongozi ambao watatupelekea kushinda Ubunge mwaka 2010. Ninajitahidi kwa kadri ya uwezo wangu kuhakikisha kuwa ninatimiza majukumu kwa vizuri ili yeyote atakayeteuliwa na CHADEMA kuwa Mgombea aweze kuwa na rekodi ya kujivunia na apate ridhaa ya kuwa Mbunge wetu.
  Asanteni kwa kunisikiliza.

  Kabwe Z. Zitto, Mb
  Mbunge wa Kigoma Kaskazini,
  Kalinzi, 15/8/2008.
   
  Last edited by a moderator: Aug 25, 2009
 2. M

  MC JF-Expert Member

  #2
  Aug 25, 2009
  Joined: Oct 5, 2007
  Messages: 751
  Likes Received: 28
  Trophy Points: 45
  Thanks Zitto kwa kuwaweka sawa wananchi wa Kigoma kaskazini, Maana Comment ya Pinda Bungeni kuhusu wewe kulisahau Jimbo la Kigoma kaskazini ilinishtua sana.
   
 3. K

  Kiranja JF-Expert Member

  #3
  Aug 25, 2009
  Joined: May 19, 2007
  Messages: 754
  Likes Received: 4
  Trophy Points: 0
  Hii ndio mbinu sahihi ya kukabiliana na propaganda. Huu ndio ukomavu.Safi sana
   
 4. Dilunga

  Dilunga JF-Expert Member

  #4
  Aug 25, 2009
  Joined: Apr 8, 2009
  Messages: 679
  Likes Received: 16
  Trophy Points: 0
  Nadhani tumelogwa.
   
 5. Malafyale

  Malafyale JF-Expert Member

  #5
  Aug 25, 2009
  Joined: Aug 11, 2008
  Messages: 11,214
  Likes Received: 3,626
  Trophy Points: 280
  Dilunga umekuja "kuchafua hali ya hewa hapa nahisi,anyway kutoa maoni yako ni haki yako ya msingi na ipo ndani ya katiba!

  Zitto kaza mwendo mkuu;tukijipanga vyema NEC-CCM itakutana sana 2011 kupanga tena kumdhibiti Spika,na wala si kukutana kupanga waone jinsi gani wataleta maendeleo kwa watz maana upinzani utakuwa unadhibiti bunge!

  Tunahitaji akina Zitto wengi bungeni!
   
 6. K

  Kiranja JF-Expert Member

  #6
  Aug 25, 2009
  Joined: May 19, 2007
  Messages: 754
  Likes Received: 4
  Trophy Points: 0
  Je, ilikuwa lazima kuwashukuru hao, hasa Chenge na Mrema? Jamani alama za nyakati zinasemaje?
   
 7. Kichuguu

  Kichuguu Platinum Member

  #7
  Aug 25, 2009
  Joined: Oct 11, 2006
  Messages: 7,203
  Likes Received: 867
  Trophy Points: 280
  Dilunga,

  Naungana nawe 100%.

  Mheshimiwa Zitto ametoa shukrani nzito sana kwa mafisadi kiasi cha kuwafanya wawe ni wa muhimu zaidi katika miradi hiyo kama vile walikuwa anatekeleza miradi hiyo kwa hiari yao. Ninadhani angewaambia wananchi wake straight kuwa alifanikiwa kuifanya serikali isikilize kilio chao na kutekeleza miradi hiyo anayotaja.


  Mambo mengine aliyaweka vizuri sana isipokuwa hilo hapo ambalo Dilunga kaengua
   
 8. Dilunga

  Dilunga JF-Expert Member

  #8
  Aug 25, 2009
  Joined: Apr 8, 2009
  Messages: 679
  Likes Received: 16
  Trophy Points: 0


  Ahsante Kichuguu kwa kuliona hilo, aksante.

  Zaidi ya Mkapa na Vithlani, hakuna kichwa kinachotafutwa Tanzania kikajibu shutuma za ubadhilifu kama kichwa cha Andrew Chenge.

  Zitto Kabwe, mbunge kiongozi wa upinzani, ameenda kuwaambia wananchi kwamba kwa kushirikiana na Ephraem Mrema aliyeilipisha TANROADS Sh bilioni 3.3 kwa kampuni illegal ya Norconsult na Zhakia Meghji aliyesaini makaratasi ya Billal wa EPA, Andrew Chenge amewajengea mabarabara!

  Kana kwamba kina Zhakia Meghji na Chenge walifanya hisani kutoa hela, hela zinazopita kwa idhini ya Bunge.

  Unalalamika Buzwagi, Buzwagi, Buzwagi halafu wakina Chenge waliosaini mikabata unaenda kuwauza kwa watu? Unasimama mbele za wananchi wenye disapointment na frustration unataja ``Chenge`` kwa ufahari kabisa?

  Labda ni Waganda walikasirika mwaka '79 wakatutafutia dawa, au Wakenya walinyunyiza kimiminika na helikopta ili tupwelee tuwaachie ardhi, lakini kuna mkono wa mtu, hatuwezi kuwa wazima. Anamsifu Chenge hadharani?
   
  Last edited: Aug 25, 2009
 9. Abdulhalim

  Abdulhalim JF-Expert Member

  #9
  Aug 25, 2009
  Joined: Jul 20, 2007
  Messages: 16,472
  Likes Received: 126
  Trophy Points: 160
  Kwa wale mnaomlalamikia Zitto kwa ku-acknowledge akina Chenge, Meghji etc, nadhani mnasahau kuwa utendaji wa serikali yetu ukoje na hasa hii lobbying ya waziwazi ya wabunge. Hili si suala la mbunge mmoja ni wote tu ni self-serving na nakuhakikishieni hakuna mbunge ambaye sio successful lobbyist anaweza kutetea kiti chake cha ubunge..Hizi ndio facts zilizopo ground-level..ukikaa kushinda nyuma ya computa yako huwezi kuyajua haya.

  Maendeleo ktk nchi yetu yanaenda kwa njia ya ku-lobby. Mbunge akiwa na urafiki na waziri wananchi mmeula, mbunge akichonga gega sana kwenye mjengo wananchi ya jimbo lake wanaula, mbunge akiteuliwa uwaziri ndio hivyo tena miradi inaletwa kwa staili ya vimemo.etc etc etc..
   
 10. Mkaguzi

  Mkaguzi JF-Expert Member

  #10
  Aug 25, 2009
  Joined: Sep 26, 2007
  Messages: 249
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 33
  Dilunga, nadhani ukomavu unahitajika zaidi kabla ya hukumu! Hapo zitto kaonyesha uungwana na ujasiri!
  Hata kama mtu ni fisadi na kuna zuri alikutendea huna budi kumshukuru!mabya mia haatakiwi kufuta mazuri kuumi ulotenda! mi nafkiri hadi jamaa kuwataja watakua waliplay role kubwa sana kumsaidia!
  Sema bahati mbaya kwa zito ni hao walokua stake holder katika maamuzi wanatuhuma za ufisadi!
  Ila cha msingi ambacho tunatakiwa kumshauri zitto ni kusoma alama za nyakati! Politics z not decent as he thinks! Smetimes u have to agree with time and accept sme facts though they might b painful!
   
 11. Abdulhalim

  Abdulhalim JF-Expert Member

  #11
  Aug 25, 2009
  Joined: Jul 20, 2007
  Messages: 16,472
  Likes Received: 126
  Trophy Points: 160
  Ktk larger picture unakosea.

  Serikali lazima iwe na roadmap yake kuyafikia malengo ya kimaendeleo sio kusubiria ma-lobbyst au mwanasiasa aseme. Serikali inapaswa kuwasikiliza na kuwatumia wataalamu na mikakati yao. Bila hivyo kila kitu kinakuwa ovuyovyo. Shaghalabaghala.

  Na sio ajabu unaweza kukuta akina Zitto wana-lobby kujengewa barabara ambayo haitoki nje ya mkoa yao! Nilikuwa Kigoma mwaka jana na nimejionea hali halisi ya kule. Sasa technically ni upotevu wa fedha za umma kujenga barabara ambayo haitoki. Kwa maoni yangu, mathalan kwenye ishu ya barabara, serikali ilitakiwa ihakikishe kwanza mikoa yote inafikika kwa njia ya barabara ya lami . Baada ya hapo nguvu ndio zielekezwe kuangalia makao makuu ya wilaya na miji.nk.nk.nk.
   
 12. Indume Yene

  Indume Yene JF-Expert Member

  #12
  Aug 25, 2009
  Joined: Mar 17, 2008
  Messages: 2,932
  Likes Received: 42
  Trophy Points: 145
  Mkuu kama walisaidia ikiwa moja ya majukumu yao, Zitto kwa niaba ya wananchi wa jimbo lake hakuwa hana budi kuwashukuru. Naamini walifanya hivyo kwa kutekeleza majukumu yao ambayo walikuwa wamepewa ndani ya serikali.
   
 13. Indume Yene

  Indume Yene JF-Expert Member

  #13
  Aug 25, 2009
  Joined: Mar 17, 2008
  Messages: 2,932
  Likes Received: 42
  Trophy Points: 145
  Kwenye ukweli lazima tuseme ukweli au tukubali. Siko hapa kuwatetea hao fisadiz lakini kama hiyo ilikuwa ni sehemu ya wajibu wao na wakatoa ushirikiano mzuri naamini Zitto alikuwa hana budi kuwashukuru kwa hilo kwa niaba ya wanajimbo wake. Pamoja na hilo bado wataendelea kubaki fisadiz tu.
   
 14. Dilunga

  Dilunga JF-Expert Member

  #14
  Aug 25, 2009
  Joined: Apr 8, 2009
  Messages: 679
  Likes Received: 16
  Trophy Points: 0
  Indume Yene,

  Kama utaniruhusu kifupi nitumie mifano ya misahafu kueleza ninachokisema.

  Ibilisi aliwahi kuwa Malaika Mwandamizi katika falme ya Mbinguni, akiitwa Lucifa. Alifanya kazi sawia mpaka siku moja akajiona anaweza kukalia kiti cha Mungu, akaingia katika uhasama na Mikaeli, Malaika Mwandamizi mwenzi, akashindwa vita, akatupwa duniani amelaaniwa kama nyoka. Ufunuo wa Yohana 12:7-10.

  Baada ya hapo hutasikia muumini yoyote akimsifu Ibilisi kwa kazi alizofanya akiwa Malaika Mwandamizi kabla hajaanguka. Ukifanya mawili, ukaharibu manane, huna cha kusifiwa. Umetoa mbili ukaiba nane!

  Andrew Chenge alikuwa mfujaji mkuu wa mali umma. Huwezi kumsifia kwa mawili matatu aliyofanya akiwa na majukumu ya uwaziri. Wananchi wengi wana kiu ya kumwona Chenge kizimbani, utakuwa huelewi hisia za watu ukianza kumshukuru na kumsifia sifia hadharani kwa kujenga mabarabara!

  Ukimshukuru mtu "kwa dhati kabisa" maana yake unajisikia una mzigo moyoni kwa fadhila uliyopewa, hutaweza kumwandama kama fisadi. Manake anamheshimu, wakikutana anamchekea, anamshukuru, hawezi kumsema, ameshasema alimfanyia fadhila. Zitto Kabwe wa upinzani anasema Chenge amewajengea Kigoma mabarabara?


   
 15. Kichuguu

  Kichuguu Platinum Member

  #15
  Aug 25, 2009
  Joined: Oct 11, 2006
  Messages: 7,203
  Likes Received: 867
  Trophy Points: 280
  Zitto ni mtu smart sana kutambua kuwa watu hawa hawakutoa ushirikiano huo kwa hisani zao kiasi cha kuhitaji kushukuriwa; nadhani hapa aliteleza kidogo
   
 16. Chakaza

  Chakaza JF-Expert Member

  #16
  Aug 25, 2009
  Joined: Mar 10, 2007
  Messages: 23,668
  Likes Received: 21,900
  Trophy Points: 280
  Kama ni hivyo nadhani tunaweza kumsamehe na kutomtafsiri vibaya.
  Tujenge tabia ya kuwakosoa na kuwapa moyo wapiganaji wetu.Tunawahitaji sana hao.
   
 17. Ntaramuka

  Ntaramuka Senior Member

  #17
  Aug 25, 2009
  Joined: May 2, 2008
  Messages: 169
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 33
  Safi sana mzee Zitoo, "GIVE THE DEVIL ITS DUE" hata kama mtu ni fisadi akifanya vizuri anasifiwa. Akina Chenge hatuwachukii kwa kuwa tu ni Chenge, mtu anahukumiwa kwa matendo yake.
   
 18. Fugwe

  Fugwe JF-Expert Member

  #18
  Aug 25, 2009
  Joined: Aug 21, 2008
  Messages: 1,680
  Likes Received: 230
  Trophy Points: 160
  Hoja mnazozitoa nadhani hamjamwelewa Mhe. Zitto. Sisi kama wapiga kula wake tunamwelewa. Hatumwelewi kwa kujisifu kwake la hasha tunamwelewa kwa yale ambayo amelifanyia jimbo lake ambalo serikali ya CCM ililisahau takribani kwa miongo yote. Zitto sisi wasomi wa jimbo tupo na wewe endeleza hayo, usijali hoja zisizo na kichwa wala Miguu, sisi tulioluwa tunatembea kwa miguu kutoka Kigoma mjini, Mwandiga, Kiganza, Bitale, Mkongoro, Kalinzi, au ukichepuka kidogo Matyazo na Mkabogo ndio tunaojua umuhimu wa barabara uliyopigania na sasa inajengwa. Hongera sana Mhe. Zitto.

  Vijana woter wa Jimbo la Kigoma kaskazini tuache wazee waliolemazwa na CCM, tunajua kuchambua mbichi na mbivu. Hatutahadaliwa na chama cha Mafisadi. tunataka kujenga jimbo letu na nchi yetu.

  HONGERA MHE. ZITTO
   
 19. Masanja

  Masanja JF-Expert Member

  #19
  Aug 25, 2009
  Joined: Aug 1, 2007
  Messages: 3,595
  Likes Received: 3,763
  Trophy Points: 280

  Exactly mkuu.

  Hapa swala si ufisadi. Kila mtu anajua kwamba Chenge et al ni mafisadi. LAKINI kama walitoa ushirikiano kwa Mh. Zitto jimbo lake likapata barabara ya lami tangu uhuru..huoni kwamba hana budi kuwashukuru? Ingwa walitekeleza wajibu wao..wangekataa jee? angewafanya nini? Hapa tunajifunza kwamba ukiwa aggressive na smart mambo yanawezekana. Kwani mbona wabunge wa CCM hawakupewa huo ushirikiano?

  Again, kwamba Chenge ni Fisadi au Meghji halina ubishi..lakini tunaangalia mchango wao katika kufanikisha maendeleo ya watanzania. It is wrong kuassume kwamba mtu akiwa fisadi hana lolote la maana. After all, wakina Chenge ni mafisadi lakini ndo walikuwa wasimamizi wa raslimali za taifa. Na ingawa ni mafisadi si wajinga kiasi hicho....

  Kichuguu et al, YOU SHOUDLD NOTE Zitto kuwashukuru waliomsaidia katika kufanikisha azma yake hata kama ni mafisadi..it doesnt mean is endorsing their fisadi behavior. Ni kuacknoledge kwamba along the way.....kuna watu walifanikisha azma ya wana Kigoma kupata lami-unfortunately wengi wao leo wanatuhumiwa kwa ufisadi. Ufisadi hauondoi hoja kwamba walimsaidia Mh. Zitto. Wangekataa....(after Zitto ni opposition) ingekuwaje? Absolutely Nothing!
   
 20. Next Level

  Next Level JF-Expert Member

  #20
  Aug 25, 2009
  Joined: Nov 17, 2008
  Messages: 3,159
  Likes Received: 17
  Trophy Points: 135
  Mkuu naomba nikuunge mkono kwenye post yako hapo juu! Ni kweli kina Dilunga wanaweza kuwa na point kwa malalamiko yao kwani mh.Zitto kawafagilia mafisadi hadharani. Lakini kumbuka kwa mtu mwenye akili timamu lazima utambue kuwa hizo sifa ni za kinafiki tu, ni kupaka mafuta kwa mgongo wa chupa......for political reasons....ndivyo siasa zetu hapa TZ zinavyoenda!

  So haina maana kwamba kuwasifia huko kunafuta habari za kifisadi na msimamo wa mheshimiwa kuhusu ufisadi wa kina Chenge, na pia hawa jamaa kuwa mafisadi hakufuti kabisa yale mazuri machache waliyoyafanya wakiwa viongozi hasa kwa jimbo la mh. kwa mazuri hayo ndicho kisehemu alichokisifia Mh. Zitto wakuu!
   
Loading...