Hotuba ya Waziri Mwakyembe ktk Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari - May 03, 2017

Informer

JF-Expert Member
Jul 29, 2006
1,599
6,669
HOTUBA YA MHE. DKT. H.G. MWAKYEMBE, WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO, KATIKA MAADHIMISHO YA SIKU YA UHURU WA VYOMBO VYA HABARI DUNIANI TAREHE 3 MEI, 2017, MWANZA.


-Mhe. John Mongella, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza;

-Wah. Mabalozi na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa: natambua uwepo wa Mwakilishi wa taasisi za UN, Alvaro Rodriguez, Kaimu Balozi wa Marekani, Virginia Blaser, Mkuu wa UNESCO nchini, Bi. Zulmira Rodrigues; Mwakilishi wa EU Bal. Roeland Van de Geer; Mwakilishi wa Friedrich Elbert Stiftung, Bw. Michael Schlulteiss;

-Mwenyekiti wa MISA-TAN, Salome Kitomari;

-Wawakilishi wa UTPC, MISA, TEF; TMF; MOAT; TAMWA; & MCT;

-Wawakilishi wa mashirika na taasisi mbalimbali;

-Wahisani wa maendeleo;

-Wanataaluma mliopo hapa;

-Wanahabari, watangazaji na wadau wa habari nchini,

-Mabibi na mabwana.



Awali ya yote, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kukutana hapa siku ya leo. Katika kuadhimisha siku hii adhimu ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani, mlimwalika Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ambaye kutokana na kubanwa na majukumu mengine ya kitaifa, amenituma mimi kujumuika nanyi siku ya leo. Pamoja na kumwakilisha Mhe. Rais hapa, sitasoma hotuba aliyokuwa ameandaliwa, bali nitajielekeza kwenye machache niliyoyaandaa jana jioni na leo asubuhi kutokana na mawasilisho mbalimbali hapa.

Wah. viongozi, wanahabari wenzangu: Serikali inatambua umuhimu wa siku hii ya leo ambayo ilitangazwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka 1993 kufuatia pendekezo la Mkutano Mkuu wa 26 wa UNESCO la mwaka 1991 lililotokana na Azimio la Windhoek la waandishi wa habari wa Afrika la mwaka huohuo wa 91 kuhusu maadhimisho ya uhuru wa vyombo vya habari. Azimio hilo vilevile liliridhia kuanzishwa kwa Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika (MISA) ambayo wote tunajua mchango wake katika kupigania uhuru wa vyombo vya habari, maadili na weledi katika tasnia ya uandishi wa habari.

Ndugu wanahabari, mazungumzo yangu na nyie leo asubuhi, si ya kunyoosheana vidole na kupimana nguvu, la hasha. Kwani hayo yalishafanyika huko nyuma na matokeo yake mnayafahamu kupita mimi ambaye nilikuwa nje ya tasnia hii kwa miaka mingi. Mazungumzo yangu ni ya kujenga jukwaa la mawasiliano yenye tija kati ya vyombo vya habari na Serikali. Nimesukumwa na kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu: "Wajibu adhimu wa wanahabari katika ujenzi wa jamii zenye amani, usawa na shirikishi" na hivyo "Wajibu wa Kuwalinda Wanahabari" dhidi ya manyanyaso mbalimbali.

Ukipitia vyombo mbalimbali vya habari na mitandao ya jamii kwa siku kadhaa sasa, unauona

mjadala mpana duniani kote ambao umeyapitia matukio kadhaa ya waandishi kunyanyaswa duniani na mazingira hasi katika baadhi ya nchi, wanayofanyiakazi. Kwa ujumla nimeziona sababu kuu nne zinazojitokeza sana kwenye mjadala huu:

i. ukosefu katika baadhi ya nchi wa misingi imara ya kikatiba/ kisheria ya kulinda uhuru wa kutafuta, kupata au kupokea na kusambaza habari;

ii. uelewa unaopishana katika jamii kutambua na kuthamini wajibu adhimu walionao waandishi wa habari katika kuhabarisha, kuelimisha, na hivyo kufanikisha utekelezaji wa dhana ya kikatiba ya uwajibikaji wa serikali kwa umma;

iii. vyombo vya habari kutawaliwa na msukumo mkubwa wa kibiashara LAKINI bila kuzingatia weledi! Hivyo, vyombo vingi vinategemea huduma ya cheap labour kujiendesha na matokeo yake tunayajua;

iv. sera za uhariri za baadhi ya vyombo vya habari kukataa dhana ya mipaka ya uhuru wa habari kwa imani kwamba hiyo ni censorship na hivyo kujiingiza kwenye mivutano isiyoisha na Serikali na waathirika wa uhuru huo usio na mipaka.

Hali hii inaigusa Tanzania vilevile katika maeneo kadhaa kama wasemaji wengi walivyojieleza hapa . Nianze na suala la mazingira ya kisheria: je, na sisi tuna tatizo la kukosa misingi imara ya kikatiba na kisheria ya kulinda uhuru wa habari? Jibu litatokana na uchambuzi mfupi nitaoufanya sasa hivi.

Ibara ya 18(b) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inasema kila mtu anayo haki ya kutafuta, kupokea na kutoa habari bila ya kujali mipaka ya nchi. Ukiisoma ibara hii peke yake, unauona uhuru usio na kigugumizi wala mipaka, lakini tafsiri sahihi ya Katiba ni TAFSIRI OANISHI (harmonious interpretation) inayosema "kifungu chochote kile cha Katiba ni sehemu ya vifungu kadhaa vinavyohusiana ambavyo ni kwa kuviangalia kwa pamoja, utapata maudhui ya kila kipengele".

Hivyo basi ukiisoma ibara ya 18(b) ya Katiba na vipengele vingine vya Katiba hususan ibara ya 30(1) unapata ujumbe kuwa katika kutumia haki na uhuru tulionao ibara ya 18(b), tuna wajibu vilevile kuheshimu haki na uhuru wa wengine na maslahi ya Taifa. Huu ndo mpaka pekee muhimu wa kuzingatia sisi kama waandishi wa habari na watangazaji, na mpaka huu hauko Tanzania tu, ni universal. Masharti haya yanaendana na ya ibara maarufu ya 19 (Article 19) ya Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa (International Covenant on Civil and Political Rights) ambao Tanzania tumeuridhia.

Waandishi na watangazaji tunapovuka mpaka huo kwa makusudi, tena bila kuomba radhi kama uungwana unavyodai pale tunapoandika au kutangaza uvumi usio wa kweli, ndivyo tunavyojenga uhasama na watu ambao hawakustahili kujenga uhasama na vyombo vya habari. Nawafahamu watu wengi ambao wangetamani kwenda mahakamani, lakini wanachelea mlolongo wa taratibu za kimahakama na muda mrefu ambao mahakama zinawezachukua kuhitimisha madai yao. Hivyo huishia kujenga hisia hasi dhidi ya tasnia hii.

Tatizo linakuwa kubwa kutokana na vyombo vya habari vingi nchini kutawaliwa na msukumo mkubwa wa kibiashara bila kuzingatia weledi! Hivyo, vyombo vingi vinategemea huduma ya cheap labour kujiendesha na matokeo yake yanaeleweka: incessant defamation of characters, kuchafua watu bila tahadhari za kiuandishi, kunukuu watu out of context, kiasi cha kuwafanya hata watu waliokuwa na imani na media kupoteza imani na wajibu adhimu wa vyombo vya habari. Nataka kumwambia kaka yangu Salim Salim kuwa makanjanja kamwe hawawezi kuwa "critical minds" katika kipindi hiki cha mabadiliko makubwa ya kijamii, sayansi na teknolojia!

Kalamu yako mwandishi wa habari ina nguvu ya pekee: inajenga, inabomoa. Kalamu yako inapotetea chenye haki, uwe na uhakika kuwa baraka za wengi ziko nawe, na kwa kuwa sauti ya wengi ni sauti ya Mungu (vox populi vox Dei), una baraka na ulinzi wa Mungu. Kalamu yako inapotetea haramu, inapopindisha ukweli kwa rushwa na kumwonea mnyonge, mwenye haki, ujue unawaudhi wengi na hivyo unamwudhi Mungu! Naomba nisisitize kuwa katika kuadhimisha siku hii ya Uhuru wa Vyombo vya Habari yenye Kauli Mbiu ya "Wajibu adhimu wa wanahabari katika ujenzi wa jamii zenye amani, usawa na shirikishi" na hivyo "Wajibu wa Kuwalinda Wanahabari," naomba kusisitiza kuwa Mlinzi wa Kwanza wa Mwandishi wa Habari (wote sisi hapa ni waumini) ni Mwenyezi MUNGU. Mlinzi wa pili ni unadhifu, weledi wa kazi yako mwenyewe! You can never go wrong by doing what's right.

Zinapotokea changamoto, kamwe tusibebwe na hisia, mihemko, tukaacha taaluma yetu na kugeuka wanaharakati na mara nyingine hata wapiga ramli tunaojua kilichotokea hata kabla uchunguzi haujafanywa! Tutaiingiza nchi yetu kwenye machafuko bila sababu. Kama kuna dalili za mchezo mchafu, tuzame kwenye uchunguzi. Vyombo vyetu hivihivi vya habari vimeweka historia katika nchi hii, mara kadhaa vimefichua uozo ambao Serikali haikuujua na baadaye hatua madhubuti zikachukuliwa! Hebu tufungue ukurasa mpya wa mawasiliano zaidi kuliko hisia.

Nimeiagiza Idara yetu ya habari kutengeneza utaratibu wa kudumu wa mawasiliano ya karibu na wahariri na waandishi wa habari angalau mara moja kwa mwezi siyo tu kwa lengo la kupeana taarifa za yaliyojiri Serikalini, lakini vilevile udhaifu unaojitokeza katika zoezi la kutafuta, kupokea na kusambaza taarifa. Jukwaa hilo, liwe na uwezo wa kujadili udhaifu huo, uwezo wa kumwita waziri au kiongozi yeyote kupitia Idara ya Habari kutoa ufafanuzi wa taarifa fulani zinazoenea au kuchukua hatua kwa udhaifu uliojitokeza ili kujenga kuaminiana. Nina uhakika kupitia utaratibu huu, waandishi wa Tanzania tutaepusha maamuzi ya Serikali yasiyo shirikishi kuhusu tasnia ya habari, na tutaepusha vilevile maamuzi ya jazba ambayo baadhi yake yanavunja Katiba ya nchi k.m. kumfungia kiongozi fulani asiandikwe au kunukuliwa popote ni kujichukulia sheria mkononi kama wafanyavyo tunaowaeleza kuwa "wananchi wenye hasira kali" (mob justice). Siyo tu kwamba tunaingilia mamlaka ya utoaji haki yasiyo yetu, bali vilevile sisi tunawanyima wananchi haki yao ya kikatiba ya kupewa taarifa wakati wote kama ilivyoainishwa chini ya Ibara ya 18(d) ya Katiba yetu.

Serikali inatambua na inajitaji mchango wa vyombo vya habari katika harakati za kuleta maendeleo. Mapambano dhidi ya rushwa, ufisadi, ujangili, utoroshaji maliasili zetu, utakatishaji fedha, madawa ya kulevya kwa mfano, yanahitaji mchango wa vyombo vya habari, lakini si kwa hisia tu, bali uchunguzi wa kina. Vyombo vya habari vyenye ushahidi, sio ule wa juu kabisa wa kimahakama katika masuala ya jinai, (wa bila shaka yoyote - beyond reasonable doubt) bali wenye ushawishi wa kutosha (on a balance of probabilities), vina wajibu wa kuwafichua bila woga wahusika wote. Natamka kwenu kuwa nitatetea na kulinda investigative journalism, habari za uchunguzi.

Katika jamii yoyote ya kidemokrasia, vyombo huru vya habari na visivyoweza kuyumbishwa na watu wachache wanaolinda maslahi yao binafsi, ni silaha muhimu sana katika kuhamasisha utawala bora na maendeleo. Serikali, kwa kutambua changamoto za upatikanaji wa taarifa hasa kwenye taasisi za umma, tuliamua kupeleka Bungeni na kupitisha sheria mbili muhimu; Sheria ya Huduma za Habari na Sheria ya Haki ya Kupata Taarifa na ambazo zote zimeanza kufanyakazi na zinahakikisha uhuru wa wanahabari kukusanya, kuhariri na kupata taarifa muhimu za kuzisambaza kwa wananchi. Aidha tumezindua hivi karibuni tovuti kwa kila halmashauri nchini ili kuboresha mawasilinao na wananchi. Waandishi na watangazaji mtusaidie kutaja Halmashauri ambazo taarifa zake hazihuishwi, ni zilezile za wakati wa ufunguzi wa tovuti Dodoma! Ni waandishi pekee wa habari na watangazaji, hasa Klabu za Waandishi wa Habari zilizo na uwakilishi kila sehemu nchini, mtakaosaidia tovuti hizi zisigeuke kuwa magofu ya habari bali majokofu ya habari.

Nitumie fursa hii vilevile kuwakumbusha watendaji wote Serikalini tutekeleze sheria hizo mbili kwa kutoa ushirikiano mkubwa kwa vyombo vya habari katika kuvipa taarifa na habari za utekelezaji. Pengine moja ya faida kubwa ya utaratibu nilioagiza uanzishwe na Idara ya Habari wa mawasiliano ya karibu na wahariri na waandishi wa habari angalau mara moja kwa mwezi, ni kuwataja watendaji ambao ni vikwazo katika kutekeleza sheria hizo mbili na zingine ili Serikali ichukue hatua.

Serikali ya Awamu ya Tano imekuwa ikitilia mkazo ukuzaji wa viwanda nchini kama chachu ya maendeleo na kuboresha Maisha ya Watanzania kupitia ongezeko la ajira. Waandishi wa habari naa watangazaji tunalo jukumu kubwa kuhakikisha kuwa taarifa na habari mbalimbali zinazohusiana na ukuaji na maendeleo ya uchumi viwanda zinawafikia wananchi wote na hasa wale waishio vijijini.

Najua kwamba kupitia Wizara ya Habari na hasa Idara yetu ya Habari MAELEZO kumeshaanza mazungumzo na baadhi ya vyombo vya habari kuanzisha madawati maalum ya kuhakikisha habari za uchumi wa viwanda zinaandikwa ipasavyo. Naomba sote tushirikiane kufanikisha hili, na nawapongeza wote waliokwishaanza kutekeleza.

Ni lengo la Serikali kuhakikisha kuwa taaluma ya uandishi wa habari inakuzwa ili kufikia viwango wa kimataifa na ndio maana utaona kwenye sheria hiyo ya Huduma za Habari kunaanzishwa mfuko maalumu wa kuwaendeleza wanahabari kitaaluma ili kukidhi matakwa hayo na tunakuja pia na mfumo wa ithibati kwa wanahabari.

Serikali pia inatoa maagizo kwa taasisi zote zinazotoa mafunzo kwa waandishi wa habari wazingatie weledi na maelekezo ya sheria hiyo ya Huduma za Habari pamoja na Kanuni zake za mwaka 2017 ili kuwa na waandishi wenye weledi uliotukuka ili kutoa habari zenye maslahi mapana ya nchi.

Serikali itahakikisha pia haki za waandishi wa habari na hasa zinazohusiana na masilahi yao kazini ikiwemo zile zinazowalinda wakati wa kutekeleza majukumu yao zinazingatiwa kwa mujibu wa sheria za nchi. Kwa upande wa waajiri katika sekta ya habari pia ni wakati sasa wa kuhakikisha kuwa haki hizo za waajiriwa wao zinazingatiwa bila kuanza kushikana mashati. Sisi tunaamini kuwa uwepo wa sheria nzuri za vyombo vya habari na upatikanaji wa taarifa ni chachu kubwa ya maendeleo katika nchi. Sheria hizo haziwezi kutekelezwa bila ushirikishwaji wa kina wa wadau husika.

Nimeongea mengi, inatosha kwa leo ila nimalizie kuhusu mitandao ya kijamii ambayo imekuwa changamoto kubwa kwenu mnaotafuta habari na kusambaza kwa misingi ya kitaaluma. Zitumienintaarifa hizo kama tetesi za kutafutia habari za kweli ama sivyo mtajikuta mko mahakamani kila siku. Upatikanaji wa taarifa sahihi ndio ufunguo kwa utoaji suluhisho kwa matatizo yanayotukabili. Na kama kuna vyombo vya kutetea eneo hili, kwa hakika vyombo vya habari vina nafasi ya kipekee kabisa.

Ni imani yangu kuwa jukumu la vyombo vya habari kuhakikisha kuwa mambo yanakwenda sawa hapa nchini litazidi kuwa kubwa na hasa kutokana ka kukua kwa teknolojia ya upashanaji habari.

Tafiti zinaonesha kuwa usomaji wa magazeti kwa nchi za magharibi unapungua kwa kasi sana kutokana na matumizi wa intaneti, lakini hilo bado halijawa tatizo kubwa hapa nchini. Mimi ninaamini na mnaweza kunikosoa, kwamba aina zote za upashanaji habari kama magazeti, redio, televisheni na intaneti zinapanuka kwa karibu kasi sawa. Ushauri wangu kwenu ni kutumia taarifa za mitandao kwa tahadhari kubwa.

Ndugu wanahabari wenzangu, nihitimishe kwa maneno niliyosema mwanzoni: Mbali na Mwenyezi Mungu, mlinzi mkuu wa mwanahabari yeyote ni ukweli, unadhifu, na weledi wa kazi yake!

Concerns zenu nyingi nimezisikia, napanga kukutana na nanyi ndani ya mwezi huu au ujao tuangalie ni nini tukifanye kwa pamoja. Tuongelee hizo changamoto za kodi, kanuni za mitandao, mkanganyiko wa usajili wa vyombo vya habari vya kijamii, malalamiko kuhusu qualifications za wanahabari huku tukidai teknolojia inakimbia sana nk.

Nawatakia Maadhimisho Mema!
 
Kwanza tujikite kwenye dhana ya demokrasia kwamba ni neno la kilatin demos lilitafsiriwa kuwa ni utawala wa watu, Abraham likolin yeye akatafsir kuwa demokrasia ni utawala wa watu uliowekwa na watu kwa ajili ya watu.
Kwa namna nyingine watu wanaiweka serikali madarakani kwa utaratibu waliojiwekea ili iwahudumie na sio iwatese.
Turudi kwenye mada
1. Kwa kuwa serikali zote za kidemokrasia huwekwa na watu, watu hao wana haki ya kutoa maoni yao juu ya kinachoendelea kwa mustakabali wa nchi yao sio lazima maoni yawe yale yanaoupendeza utawala.
Vyombo vya habari viwe huru, vitoe fursa sawa ya habar bila kujali kuwa huyu ana mawazo tofauti na serikali au vipi. Je hapa kwetu habar za upinzan zinatangazwa ktk media za uma kama tbc, kila siku utasikia mkuu huyu wa wilaya mara mkuu wa mkoa mara rais mara sijui serikal imefanya hivi mara sijui waziri.....
Kwa hyo kwa kuhitimisha tunaweza kusema kua kwa kuwa sis tumeiweka serikal madarakan bac tuna haki ya kusema
 
Back
Top Bottom