Hotuba ya Waziri Mkuu kuliahirisha Bunge!!! | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Hotuba ya Waziri Mkuu kuliahirisha Bunge!!!

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by Kasheshe, Nov 7, 2008.

 1. Kasheshe

  Kasheshe JF-Expert Member

  #1
  Nov 7, 2008
  Joined: Jun 29, 2007
  Messages: 4,690
  Likes Received: 91
  Trophy Points: 145
 2. Mzee Mwanakijiji

  Mzee Mwanakijiji Platinum Member

  #2
  Nov 7, 2008
  Joined: Mar 10, 2006
  Messages: 31,362
  Likes Received: 6,393
  Trophy Points: 280
  Hotuba ya Mheshimiwa Mizengo Pinda (mb), Waziri Mkuu wakati wa kutoa hoja ya kuahirisha mkutano wa kumi na tatu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano waTanzania, Tarehe 7 Novemba 2008, Dodoma

  UTANGULIZI

  1. Mheshimiwa Spika, kabla ya kutoa hoja ya kuliahirisha Bunge lako Tukufu, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kufikia salama siku ya leo. Namshukuru kwa kutuwezesha wote kukamilisha shughuli zote zilizopangwa kufanyika katika Mkutano huu wa Kumi na Tatu.

  Pongezi

  2. Mheshimiwa Spika, napenda nitumie fursa hii ya mwanzo kabisa kuvipongeza Vyama vyote vilivyoshiriki katika Uchaguzi Mdogo wa Jimbo la Tarime uliofanyika tarehe 12 Oktoba 2008, kufuatia Kifo cha Mpendwa wetu, Mheshimiwa Chacha Wangwe. Kwa njia ya pekee, napenda kumpongeza kwa dhati kabisa, Mheshimiwa Charles Nyanguru Mwera (Mb.) kwa kushinda Uchaguzi huo kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo – CHADEMA. Nawapongeza Wananchi wa Tarime ambao pamoja na changamoto nyingi wakati wa Kampeni hatimaye walikamilisha Uchaguzi kwa kupiga kura kwa amani, utulivu na mshikamano.

  Nawapongeza wote kwa maamuzi yao ya Kidemokrasia waliyotumia kuchagua mtu wanayempenda awawakilishe kwenye Bunge hili. Napenda kuchukua nafasi hii kuwakumbusha Watanzania wote kuwa wajibu wa KIDEMOKRASI ni kulumbana kwa hoja na siyo mapigano, vitisho au vurugu. Katika chaguzi zetu tuepuke mambo yote yanayoweza kuvuruga amani na utulivu wetu.

  3. Mheshimiwa Spika, niungane na Waheshimiwa Wabunge wenzangu kumpongeza Mheshimiwa Pindi Hazara Chana, Mbunge wa Viti Maalum kwa kuchaguliwa kuwa Mjumbe kwenye Baraza la Chuo Kikuu cha Sayansi za Afya Muhimbili. Vilevile, napenda kuwapongeza Mheshimiwa Beatrice Matumbo Shelukindo, Mbunge wa Kilindi; Mheshimiwa Benson Mwailugula Mpesya, Mbunge wa Mbeya Vijijini; na Mheshimiwa Dkt. Ali Tarab Ali, Mbunge wa Konde kwa kuchaguliwa kuwa Wajumbe kwenye Bodi ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania.

  4. Kwa wote waliochaguliwa tunawapongeza sana. Ni mategemeo yetu sote kuwa watawakilisha Bunge hili na Watanzania wote kwa ujumla vizuri katika Bodi za Taasisi hizo. Ninaamini kwamba uwezo wanao na ndio maana wamechaguliwa.

  5. Mheshimiwa Spika, katika Mkutano huu wa Kumi na Tatu, Waheshimiwa Wabunge walipata nafasi ya kuuliza Serikali jumla ya Maswali 121 ya Msingi na mengine mengi ya Nyongeza. Nitumie fursa hii kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote walioweza kuuliza Maswali ambayo kwa ujumla wake yalilenga katika kujua na kuhimiza shughuli za Maendeleo katika Majimbo, Sekta zinazohusika na maendeleo za Kitaifa. Aidha, nawashukuru Mawaziri na Naibu Mawaziri wa Sekta zilizohusika kwa kutoa majibu ya maswali hayo kwa ufasaha na kwa ufanisi wa hali ya juu. Nawapongeza pia Waheshimiwa Wabunge kwa maswali yao 19 ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu

  6. Mheshimiwa Spika, katika Mkutano huu Waheshimiwa Wabunge waliweza kujadili na kupitisha Miswada ifuatayo:

  i) Muswada wa Sheria ya Kurekebisha Sheria ya Bodi ya Usajili wa Makandarasi wa Mwaka 2008, [The Contractors Registration (Amendment) Bill, 2008];
  ii) Muswada wa Sheria ya Utoaji wa Miliki za Sehemu za Majengo wa Mwaka 2008, [The Unit Title Bill, 2008];

  iii) Muswada wa Sheria ya Mikopo ya Nyumba wa Mwaka 2008, [The Mortgage Financing (Special Provisions) Bill, 2008];

  iv) Muswada wa Sheria ya Biashara ya Ngozi wa Mwaka 2008 [The Hides, Skins and Leather Trade Bill, 2008];

  v) Muswada wa Sheria ya Ustawi wa Wanyama wa Mwaka 2008 [The Animal Welfare Bill, 2008];

  vi) Muswada wa Sheria ya Kutoa Fidia kwa Wafanyakazi wa Mwaka 2008 [The Workers Compensation Bill, 2008];

  vii) Muswada wa Sheria ya Afya ya Akili wa Mwaka 2008 [The Mental Health Bill, 2008]; na

  Bunge lako Tukufu pia lilijadili na kuridhia:

  i) Azimio la Bunge kuhusu Kumpongeza Rais Mteule wa Marekani, Mheshimiwa Barrack Obama kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa 44 wa Marekani; na

  ii) Azimio la Bunge kuhusu Upanuzi wa Hifadhi ya Ziwa Manyara.

  7. Vilevile, Bunge lako Tukufu lilipokea Taarifa za Serikali zifuatazo:

  i) Taarifa ya Kamati ya Rais ya Kuishauri Serikali kuhusu Usimamizi wa Sekta ya Madini;

  ii) Taarifa ya Utekelezaji wa Azimio la Bunge Kuhusu Utendaji Usioridhisha wa Kampuni ya Tanzania (International Containers Terminal Services (TICTS); na
  iii) Taarifa ya Utekelezaji wa Azimio la Bunge Juu ya Utendaji Usioridhisha wa Shirika la Reli Tanzania [Tanzania Railways Limited (TRL)] Uliofanywa na Kampuni ya Rites ya India.

  Mwisho, Bunge lako Tukufu lilipokea Kauli za Serikali na Hoja za Waheshimiwa Wabunge ambazo ziliwasilishwa hapa Bungeni.

  8. Mheshimiwa Spika, napenda kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote walioshiriki kupokea, kujadili na kutoa ushauri kuhusu Miswada, Maazimio na Taarifa mbalimbali zilizowasilishwa hapa Bungeni wakati wa Mkutano huu. Michango yao itazingatiwa na itasaidia kuboresha juhudi za Serikali katika kuwaletea Wananchi maendeleo.

  Madini

  9. Mheshimiwa Spika, katika Mkutano huu, Bunge lako Tukufu limepata nafasi ya kujadili Taarifa ya Kamati ya Rais ya Sekta ya Madini iliyoongozwa na Mheshimiwa Jaji Mark Bomani. Bila shaka Waheshimiwa Wabunge watakubaliana nami kwamba Kamati ilifanya kazi nzuri na kwa umakini mkubwa. Mapendekezo yaliyotolewa yataisaidia Serikali kuboresha Sekta hii muhimu kwa maendeleo ya uchumi wa Nchi yetu. Baadhi ya mapendekezo na ushauri uliotolewa yatatekelezwa kwa kipindi cha muda mfupi na mengine yatahitaji muda mrefu kidogo kutekelezwa. Napenda nilihakikishie Bunge lako Tukufu kwamba, Serikali imeanza utekelezaji wa baadhi ya mapendekezo na tutakuwa tunaliarifu Bunge lako hatua tutakazokuwa tunachukua kila wakati. Mapendekezo mengine kama ya kurekebisha Sera na Sheria ya Madini yanaendelea kufanyiwa kazi, kwani Mchakato wa kurekebisha Sheria na Sera ulishaanza hata kabla ya kuundwa kwa Kamati ya Jaji Bomani.

  10. Mheshimiwa Spika, ni lazima tukubaliane kwamba, ili Sekta ya Madini itoe mchango mkubwa zaidi katika maendeleo ya uchumi wetu na kuongeza ajira nyingi, tunahitaji kuyaongezea thamani Madini yetu hapa Nchini.

  11. Nilipotembelea Namibia hivi karibuni, nilijionea Kiwanda cha Kukata na Kusafisha Almasi ambacho kinafanya kazi nzuri ya kuongeza thamani Madini ya Almasi kwa kutumia Almasi ghafi inayozalishwa Namibia jambo ambalo limeipatia Namibia fedha nyingi pamoja na ajira. Hata hivyo, ili kuongeza Madini thamani kunahitajika uwekezaji mkubwa na uhakika wa malighafi za kutosha. Hizi ni baadhi tu ya changamoto ambazo hatuna budi kukabiliana nazo. Ni katika kufanya mabadiliko makubwa kwenye Sekta ya Madini tunaweza kuanza na sisi kushirikiana na Sekta Binafsi kuongeza thamani Madini hapa Nchini badala ya kuyauza ghafi. Tunalifuatilia suala hili kwa ukaribu mkubwa na nina imani tutafanikiwa.

  12. Nichukue fursa hii kuishukuru kwa dhati Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini kwa kuichambua vyema Taarifa ya Jaji Bomani na kutoa mapendekezo yake mazuri kwa Serikali. Vilevile, niwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote kwa kuchangia kikamilifu katika mjadala wa Taarifa hii na niwahakikishie kwamba michango yenu itafanyiwa kazi inayostahili. Nawasihi wote tuvute subira ili Wataalam wapate nafasi ya kuyashughulikia mapendekezo yenu ambayo nina imani yatasaidia sana katika jitihada zinazoendelea za kuboresha Sekta ya Madini.

  Kilimo

  13. Mheshimiwa Spika, tarehe 16 – 18 Oktoba 2008, nilishiriki katika Mkutano wa Kuhamasisha Uzalishaji wa Mazao ya Kilimo uliofanyika Mkoani Morogoro ambao ulihusisha Mikoa ya Ruvuma, Iringa, Mbeya, Rukwa, Morogoro na Kigoma. Lengo kuu lilikuwa ni kuweka Mikakati ya namna ya Kuongeza Uzalishaji wa Mazao hapa Nchini hususan kupitia utekelezaji wa Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo – ASDP.

  14. Tuliona ni vema kuanza na Mikoa hii sita katika mchakato huu kwa sababu mbalimbali, lakini kubwa ni kwamba Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini ya Ruvuma, Rukwa, Iringa na Mbeya, ndiyo Mikoa ambayo kihistoria imekuwa na mchango mkubwa katika uzalishaji wa mazao ya chakula na hivyo kuifanya ijulikane kama "The Big Four". Mkoa wa Morogoro ulijumuishwa na Mikoa hii ya Nyanda za Juu Kusini kutokana na changamoto uliopewa na Mheshimiwa Rais kuwa Ghala la Taifa la Chakula. Vilevile, Mkoa wa Kigoma nao ulijumuisha kutokana na fursa ilizo nazo katika Kilimo zinazofanana sana na Mikoa hiyo mingine mitano.

  15. Mheshimiwa Spika, takwimu za uzalishaji za mwaka 2007/2008 zinaonyesha kuwa Mikoa hii sita inachangia Tani milioni 3.9, sawa na asilimia 36 ya mahitaji ya chakula Nchini. Kitaifa uzalizalishaji ulifikia Tani milioni 10.78 za chakula kwa mwaka huo. Matarajio ni kwamba kufanikiwa kwa Mikoa hii sita katika Kilimo itakuwa chachu kwa Mikoa mingine kutumia mbinu na Mikakati iliyofikiwa kwenye Mkutano huo ili kuongeza uzalishaji kwa Nchi nzima. Dhamira yetu ni kufanya Mikutano mingine kama huu kwa Mikoa mingine kwa kuzingatia hali ya Mikoa inayofanana Kijiografia na Hali ya Hewa.

  16. Mheshimiwa Spika, Uongozi wa Nchi yetu katika ngazi zote Vijiji, Kata, Tarafa, Wilaya na Mkoa lazima utuwezeshe kutekeleza yale tuliyojifunza kwa vitendo zaidi. Mambo hayo ambayo hatuna budi kuyafuatilia kwa karibu ni haya yafuatayo.

  i) Kuongeza Tija

  17. Mheshimiwa Spika, imejidhihirisha kuwa Kilimo cha Tanzania bado kina tija ndogo sana na hivyo mavuno hayalingani kabisa na kiasi cha eneo linalolimwa. Kwa mfano, wakati Wakulima wengi sasa hivi wanazalisha mahindi wastani wa Tani 1.2 kwa hekta, lakini kama Kanuni za Kilimo Bora zitatekelezwa wanaweza wakaongeza uzalishaji.

  Takwimu za mwaka 2007/2008 zinaonyesha kuwa tulilima mahindi hekta milioni 2.88 na tukavuna Tani Milioni 3. Lakini kama tungetekeleza Kanuni za Kilimo Bora, ilitakiwa kuzalisha Tani 5 kwa Hekta na kuvuna Tani milioni 14.4 katika eneo hilo hilo. Hivyo, uzalishaji huu wa mahindi unathibitisha kuwa tija ni ndogo sana.

  18. Mheshimiwa Spika, ni wajibu wetu Viongozi na Wataalam kumsaidia Mkulima kuongeza Tija ili aweze kupunguza umaskini na kuongeza akiba ya Hifadhi ya Chakula cha Taifa. Lengo ni kuongeza uzalishaji ili eneo dogo linalotumika litoe mazao mengi kwa kutimiza Kanuni za Kilimo Bora. Mfano Mkulima anaweza kuongeza uzalishaji kutoka magunia 12 ya sasa kwa Hekta na kufikia takriban magunia 30.

  ii) Upatikanaji wa Pembejeo

  19. Mheshimiwa Spika, suala la upatikanaji wa Pembejeo za Kilimo, bei kubwa, usambazaji na matumizi yasiyo sahihi bado ni tatizo. Upatikanaji wa Mbolea, Mbegu Bora pamoja na Madawa ya Viatilifu hayakidhi mahitaji. Kwa mfano, mahitaji ya aina mbalimbali ya Mbolea yanakadiriwa kuwa ni Tani 400,000 kwa mwaka. Mwaka 2007/2008 zilipatikana Tani 211,000, sawa na asilimia 53 ya mahitaji.

  20. Kwa Msimu wa Kilimo wa Mwaka 2008/2009 hadi mwishoni mwa Oktoba 2008, kiasi cha Mbolea kilikuwa Tani 188,600 tu. Kiwango cha mbolea ya tani 150,000 kitauzwa kwa bei ya Ruzuku. Hiki ni kiasi kidogo kwa kuzingatia kwamba Msimu wa Kilimo ndiyo umekaribia. Hata hivyo, Serikali imeongeza kiasi cha fedha kwa ajili ya Pembejeo kutokana na fedha za EPA kama Mheshimiwa Rais alivyoahidi katika Hotuba yake aliyoitoa hapa Bungeni. Ni matumaini yangu nyongeza hii italeta mabadiliko katika suala zima la upatikanaji wa Pembejeo Nchini na hivyo kuongeza uzalishaji.

  21. Mheshimiwa Spika, kutokana na upungufu wa upatikanaji wa Mbolea Nchini, Serikali imetoa udhamini kwa Kampuni ya Mbolea Tanzania – Tanzania Fertilizer Company, ili waweze kuagiza Mbolea zaidi ambayo tayari imekwishaagizwa na tutaipata hivi karibuni na kusambazwa.

  22. Mwaka huu, tutaanza kutumia mfumo wa VOCHA. Lengo ni kuhakikisha kwa kiasi kikubwa mbolea ya ruzuku inawafikia na kuwanufaisha Wakulima moja kwa moja. Ninaelewa ugumu wa utaratibu kukubalika hivi sasa kutokana na uwezo wetu mdogo wa kuwafikia Wakulima wengi. Mwanzo wa jambo lolote huwa mgumu. Wito wangu kwa Viongozi na Wananchi wote ni kuwa tuukubali utaratibu huu uanze ili tupate uzoefu. Uzoefu tutakaoupata utatusaidia sana katika kufanya maboresho ili kuweza kukidhi mahitaji ya Mbolea kwa Wakulima hapa Nchini. Mfumo wa VOCHA ni bora kuliko tuliotumia mwaka jana kwa sababu mbolea ya ruzuku inawafikia Wakulima moja kwa moja na hivyo kumfanya kila Mkulima atumie mbolea.

  Natoa Wito kwa Waheshimiwa Wabunge wote washiriki katika kuwaelimisha Wakulima umuhimu wa matumizi ya mfumo wa VOCHA. Tukishirikiana kwa pamoja Mfumo huu wa VOCHA utafanikiwa na hivyo kuwanufaisha Wakulima.

  iii) Kuongeza na Kusambaza Huduma za Ugani

  23. Mheshimiwa Spika, pamoja na uhaba wa Maafisa Ugani, ni lazima wale waliopo watekeleze wajibu wao wa kuwezesha Wakulima kupata Elimu itakayowawezesha kutekeleza Kanuni za Kilimo Bora. Pamoja na upungufu wa Maafisa Ugani katika Mikoa, Maafisa Ugani waliopo wanaweza kuleta mabadiliko makubwa ya Kilimo chetu, kama watasimamiwa vizuri na kupewa vitendea kazi. Kwa mfano, Mkoa wa Mbeya una Maafisa Ugani 488; Morogoro 355; Iringa 428; Ruvuma 201; Rukwa 202 na Kigoma 204. Pamoja na upungufu uliopo, lakini Wataalam hawa waliopo wakitumiwa vizuri, wakawezeshwa kwa kupewa vitendea kazi kama vile Pikipiki na zaidi ya yote wao wenyewe wakawa na Mpango wa Kazi na wakijituma na kutimiza wajibu wao, Mapinduzi ya Kilimo Tanzania yanawezekana kabisa.

  24. Vilevile, tunazo Taasisi za Umma kama Magereza, Kambi za Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Vyuo vya Kilimo na Mifugo, Vyuo vya Maendeleo ya Jamii ambavyo ni lazima viwe vitovu vya Mapinduzi ya Kilimo Nchini. Ni muhimu katika vita hii tukatumia kila nguvu kazi iliyopo. Ni jukumu la kila Halmashauri kuhakikisha inatoa mafunzo ya msingi ya Kanuni za Kilimo Bora kwa Vijana wasiopungua 20 katika kila Kijiji watakaosaidia katika utoaji elimu hiyo kwa Wakulima chini ya usimamizi wa Maafisa Ugani. Aidha, upo umuhimu wa kuanzisha Mabaraza ya Kilimo ya Kata ambayo yatatoa msukumo mkubwa katika Kilimo. Vilevile, Sekta Binafsi ishirikishwe katika kutoa huduma za Ugani kwa Wakulima na Wafugaji ili kuongeza uzalishaji wa mazao. Nitamuomba Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika kutoa maelekezo mahususi namna Mabaraza ya Kilimo ya Kata yatakavyofanya kazi.

  25. Mheshimiwa Spika, kila Mkurugenzi wa Halmashauri Nchini ahakikishe kuwa Maafisa Ugani wanaacha kukaa Ofisini na badala yake wawafuate Wakulima popote walipo ili kujionea shughuli zao za Kilimo na kutoa ushauri stahiki.

  Wawe na Ratiba ya Kazi na Daftari la Wakulima wanaowahudumia. Kama vile Madaktari wanavyokuwa na Daftari la Wagonjwa na kila siku wanajua watawaona Wagonjwa wangapi na saa ngapi, ni muhimu na Maafisa Ugani wafanye hivyo. Kama vile Walimu walivyo na Daftari la kuandaa Vipindi vya kila siku, Maafisa Ugani nao wawe na Daftari linaloonyesha Mpango wa Kazi wa kila siku. Wakurugenzi wa Halmashauri waweke vigezo vya tathmini kwa Maafisa Ugani wote na wahakikishe usimamizi mzuri na ufuatiliaji unakuwepo wakati wote. Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Wilaya wafuatilie taarifa za Madaftari ya Maafisa Ugani wajue wanafanya nini. Vilevile, Halmashauri zihakikishe zinawapatia Maafisa Ugani makazi karibu na maeneo ya Wakulima ili wawe karibu katika kutoa ushauri kwa Wakulima.

  iv) Teknolojia na Utafiti

  26. Mheshimiwa Spika, ili kuleta kweli Mapinduzi ya Kilimo Nchini hatuna budi kuchukuwa hatua za makusudi za kuongeza ushirikiano wa karibu kati ya Watafiti, Wagani na Wakulima. Lazima Wataalam mbalimbali wahakikishe kuwa matokeo ya tafiti zao yanawafikia Wakulima na kwa wakati. Aidha, lazima kuweka taratibu itakayowezesha Teknolojia sahihi kutangazwa na kuenezwa kwa Wakulima ili kuongeza uzalishaji.

  Kuhusu uzalishaji wa Mbegu Bora, nimeelekeza Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika ihusishe na kushirikisha Taasisi za Serikali kama Magereza na Jeshi la Kujenga Taifa ili mashamba yao, yatumike kikamilifu kuongeza uzalishaji wa Mbegu Bora, ambazo asilimia 75 sasa hivi tunaagiza kutoka Nchi za nje.

  v) Umwagiliaji

  27. Mheshimiwa Spika, Kilimo cha Umwagiliaji Maji bado kipo chini sana kulingana na maeneo ambayo yanaweza kutumika katika Kilimo cha Umwagiliaji. Kwa mfano, Mkoa wa Morogoro una jumla ya Mito 143 inayotiririsha maji mwaka mzima. Lakini kati ya hekta 123,500 zinazofaa kwa Kilimo cha Umwagiliaji, ni hekta 8,800 tu ndizo zinazotumika, sawa na asilimia 7.0 ya eneo lote linalofaa kwa Kilimo cha Umwagiliaji. Tatizo hili lipo karibu Mikoa yote Nchini.

  28. Kitaifa tunazo hekta milioni 29.4 ambazo tunaweza kuendesha Kilimo cha Umwagiliaji, lakini hivi sasa tunatumia jumla ya hekta 290,000, sawa na asilimia 1 tu hapa Nchini. Takwimu hizi zinaonyesha kuwa bado Kilimo cha Umwagiliaji hatujakipa umuhimu mkubwa. Lazima tukubali kwamba hapa bado kuna udhaifu. Hivi sasa tumeomba fedha kwa ajili ya Kilimo cha Umwagiliaji. Lazima tuzitumie vizuri na kwa ufanisi. Hivyo, naagiza Kilimo cha Umwagiliaji kipewe kipaumbele hasa katika miradi inayoibuliwa na Wananchi Wilayani kupitia DADPs. Wataalamu wa Kilimo wawasaidie Wananchi kuibua miradi katika maeneo yao. Serikali kwa upande wake itaangalia Wataalam wa Kanda watakavyoelekezwa kusaidia Wakulima.

  29. Mheshimiwa Spika, Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo ina nafasi nzuri katika kuleta Mapinduzi ya Kijani. Pamoja na kuwa ASDP inatoa msukumo mkubwa katika Kilimo, bado Wananchi hawajaelimishwa na kuhamasishwa kuibua miradi mizuri na yenye kuweza kuleta mabadiliko ya haraka katika Kilimo. Kwa mfano, hivi sasa Wananchi wengi wameanza kupata ufahamu wa Matrekta Madogo, lakini hawakuwa wamepata elimu na fursa ya kuibua miradi ya aina hiyo. Jukumu la Viongozi na Wataalam ni kuipeleka Programu hii karibu zaidi na Wananchi na kuwaelimisha ili waweze kuibua miradi mizuri itakayoongezea tija.

  30. Mheshimiwa Spika, kwa upande wa mazao ya biashara, lazima tuwasaidie pia Wakulima katika kuongeza tija kwa mazao kama vile Korosho, Kahawa, Tumbaku na Pamba. Hatuna tena muda wa kusubiri, bali Mikoa husika ichukue hatua za kuhakikisha uzalishaji wa mazao haya unaongezeka, kupata bei nzuri na kujumuisha mazao haya kwenye Mipango ya Maendeleo ya Kilimo ya Wilaya DADPs ili kupata ruzuku ya Serikali. Uzalishaji wa Kahawa, kwa mfano, hivi sasa Nchini ni sawa na kilo 200 kwa hekta ikilinganishwa na lengo la kilo 500 kwa hekta, zilizopo katika Mkakati wa Kuendeleza Zao la Kahawa.

  31. Mheshimiwa Spika, ili kuongeza tija ya zao kama Kahawa, ni lazima kupanda kwa wingi miche bora ambayo imefanyiwa utafiti na Kituo cha Utafiti cha TaCRI na kuonyesha ongezeko la tija kwa mwaka. Ni lazima sasa kila Mkoa unaolima zao la Kahawa kuanzisha bustani za miche bora za mazao ya biashara katika maeneo ya Wakulima ili miche hiyo iwafikie Wakulima haraka. Aidha, ni lazima kuwahimiza kutumia Pembejeo, hasa mbolea za Viwandani na samadi ambayo inapatikana katika maeneo ya Wafugaji yaliyo karibu na mazao haya ya biashara. Wakuu wa Mikoa, Wilaya na Wakurugenzi wa Wilaya wajipange vizuri ili waweze kufikia malengo.

  32. Mheshimiwa Spika, tumejifunza mengi kwa kutumia mfano wa Mikoa Sita ya awali tuliyoanzia nayo. Kutokana na hali ya Kilimo ilivyo, Uongozi wa Mikoa kwa kushirikiana na Viongozi wa Wilaya waweke utaratibu wa kujipima. Kuwepo na Mikutano ya kutathmini maendeleo ya Mipango yao ili kujua wamefika wapi na kama kuna matatizo wapange jinsi ya kuyatatua. Sekretarieti za Mikoa zijipange vizuri ili kuweza kuzisimamia Halmashauri katika majukumu yake hasa suala la uzalishaji. Halmashauri ziwe na mikakati mizuri ya uzalishaji badala ya kuwa watumiaji wa fedha tu, na Vijiji vibadilike kutoka kuwa Vijiji vya Utawala na kuwa Vijiji vya Uzalishaji na Maendeleo. Ni lazima tubadilike kimtazamo na kiutendaji kama tunataka kubadili Kilimo chetu.

  Nitapenda kujua kila nikifika kwenye ziara Mikoani ni kwa kiasi gani mabadiliko katika Kilimo yametokea na uzalishaji umeongezekaje. Mkuu wa Mkoa na Mkuu wa Wilaya asiyeweza kuongoza mabadiliko hayo hawezi kutusaidia katika kazi hii. Tutawapima kwa vigezo vya mabadiliko katika Sekta za Maendeleo ya Wananchi. Tuanze kwa kuanzisha Mashindano ya Kilimo na kutoa tuzo kwa Mwananchi mmoja mmoja, Vijiji, Wilaya na hata Mikoa itakayoonyesha kwa vitendo mabadiliko ya tija kwenye Kilimo. Tuzo hizi zitatolewa wakati wa Sikukuu ya Nane Nane Kitaifa. Mashindano hayo lazima yaanze mwaka 2009.

  33. Mheshimiwa Spika, nimeongelea sana Kilimo. Lakini kwa Sekta ya Mifugo, Serikali imefanya jitihada za kuboresha Sekta hiyo. Pamoja na mambo mengine, Serikali imeendelea kutoa Chanjo, kujenga Majosho, Malambo na ununuzi wa dawa mbalimbali za Mifugo. Kwa mfano, Serikali imejenga na kukarabati jumla ya Malambo 158 kupitia Miradi ya PADEP na DADEPs. Aidha, Serikali imeendelea na jitihada zake za kuboresha Ranchi za Taifa kwa ajili ya uzalishaji bora. Hata hivyo, Serikali inakabiliwa na changamoto nyingi katika Sekta ikiwemo ukosefu wa ardhi ya malisho ya kutosha. Hali hii imeleta migogoro mikubwa kati ya Wakulima na Wafugaji ambayo imesababisha uvunjaji wa amani, utulivu, mshikamano na umwagaji wa damu. Ili kuondokana na tatizo hili, tunahitaji kutenga maeneo kwa ajili ya Kilimo na Ufugaji na kuyamilikisha. Ardhi ipimwe na ijulikane imetengwa kwa shughuli gani. Hii itatusaidia katika kupunguza migogoro inayoendelea kutokea kati ya Wakulima na Wafugaji. Mgogoro unaoendelea hivi sasa katika Wilaya ya Kilosa ni kutokana na kutokuwepo kwa mpango wa matumizi bora ya Ardhi. Kuanzia sasa, naziagiza Halmashauri za Wilaya kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika; na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi waanze na kukamilisha zoezi hili ili tupunguze migogoro ya Wakulima na Wafugaji. Vilevile, nawasihi Wananchi ambao ni Wakulima na Wafugaji kuvumiliana kuishi kwa amani na kila upande kutumia eneo lake, hivyo kuepusha migogoro, uvunjaji wa amani, umwagaji wa damu na vifo visivyokuwa vya lazima.

  34. Mheshimiwa Spika, Nchi yetu inahitaji kuisimamia vizuri rasilimali ya Uvuvi ili kuhakikisha kuwa Sekta ya Uvuvi inatoa mchango wake katika Kupunguza Umaskini kwa Wananchi wetu. Usimamizi mzuri wa Sheria za Uvunaji wa Maliasili za Bahari na Maziwa utasaidia kuongeza Pato la Taifa kutoka Sekta hii. Hivyo, Serikali inasisitiza kwamba Leseni za shughuli za Uvuvi ambazo nyingi hutolewa na Halmashauri za Wilaya zinapaswa kuwa na masharti yanayoonyesha zana, vifaa vya kila aina vya Uvuvi na mahali zana hizo zinapotumika kwa urahisi wa ufuatiliaji. Ningependa kuwakumbusha Wavuvi wote Nchini kuwa wazitumie Ofisi zetu zinazohusika na shughuli za Uvuvi, hasa Maafisa Uvuvi kuhakikisha kuwa wanapata ushauri na ufafanuzi kuhusu masuala yanayohusu Leseni za Uvuvi ili kupunguza matatizo yanayoweza kujitokeza.

  Nawasihi Wavuvi na Wadau wote wa Uvuvi Nchini kusoma kwa makini na kutekeleza yaliyomo kwenye Kauli ya Serikali kuhusu Waraka wa Uvuvi Kuzuia Zana za Uvuvi Haramu Nchini kama ulivyowasilishwa kwenye Mkutano wa Kumi na Mbili wa Bunge la Bajeti na Mheshimiwa Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi.

  Elimu

  35. Mheshimiwa Spika, wakati tunakaribia kufikia mwisho wa mwaka 2008, tunatarajia kwamba Vijana wetu waliofanya Mtihani wa Darasa la Saba watapata majibu yao wakati wowote. Jumla ya Wanafunzi 1,017,865 walifanya mtihani huo ambapo tunatarajia Wanafunzi 631,076, sawa na asilimia 62 watafaulu. Aidha, tunatarajia Wanafunzi takriban 504,860, sawa na asilimia 80 ya waliofaulu watachaguliwa kuingia Sekondari. Hata hivyo, taarifa za awali zinaonyesha kuwa idadi ya madarasa yanayohitajika ni takriban 12,622 kwa wastani wa Wanafunzi 40 kwa darasa. Wakati tunasubiri matokeo, ni lazima tujiweke tayari kupokea Wanafunzi wote watakaofaulu ili waweze kujiunga na Sekondari. Tunao uzoefu wa miaka takriban mitatu iliyotangulia katika kuhimizana kujenga madarasa na Shule za Sekondari za kutosha kuwapokea wote watakaofaulu. Tumefanya vizuri katika kipindi hicho tufanye vizuri katika kipindi kijacho. Kwa hiyo, napenda kutumia nafasi hii kuwakumbusha Wakuu wa Mikoa na Watendaji wote kuwa zoezi hili la kupanua elimu yetu na kuongeza idadi ya Wanafunzi wanaojiunga na Sekondari ni endelevu. Halihitaji kusukumwa na Viongozi wa Kitaifa. Ni wajibu wa Viongozi wa Mikoa na Wilaya kuhakikisha kuwa wanazo Shule na Madarasa zaidi yatakayotosheleza kupokea Wanafunzi wote watakaofaulu. Itakuwa aibu kwa Mkoa wowote ule utakaoshindwa kupeleka Wanafunzi wake wote watakaofaulu eti kwa vile hakuna madarasa.

  Nawaagiza Wakuu wa Mikoa na Wilaya zote kuhakikisha kuwa Wanafunzi wote watakaofaulu wanapata nafasi ya kujiunga na Kidato cha Kwanza mwakani. Tusisubiri kutoa visingizio na sababu za kushindwa. Jambo hili linawezekana, kila Kiongozi atimize wajibu wake.

  36. Mheshimiwa Spika, moja ya kipimo cha kupima ubora wa elimu yetu ni ufaulu wa Wanafunzi katika mitihani ya Kitaifa. Walimu, Wazazi na Wataalam wengine wa elimu wanapata faraja wanapoona matokeo ya elimu ya Wanafunzi ni mazuri. Kwa mfano, tunayo rekodi nzuri ya ufaulu wa Wanafunzi waliofanya Mtihani wa Kidato cha Nne kwa mwaka 2007 ambapo kati ya Watahiniwa 192,127 waliofanya Mtihani, waliofaulu Madaraja I – IV walikuwa 162,509, sawa na asilimia 86.2 ikilinganishwa na 116,647 sawa na asilimia 82.3 waliofaulu mwaka 2006 katika Madaraja hayo. Mategemeo ni kwamba matokeo yatakuwa mazuri zaidi kwa mwaka huu 2008. Hiyo ndiyo fahari yetu sote, kwani hutuwezesha kujipima kama Watoto wetu wanaweza kushindana katika soko la ajira au lile la elimu ya juu ndani na nje ya Nchi.

  37. Pamoja na kujivunia matokeo hayo mazuri, lakini sote tumesikia tukio la kuvuja kwa Mtihani wa Hisabati wa Kidato cha Nne mapema mwezi Oktoba 2008. Hatutarajii kwamba kufanya kwetu vizuri katika mitihani hii ni matokeo yanayotokana na ujanja wa kupata majibu ya mitihani kabla.

  38. Taarifa za kuvuja kwa mitihani ni jambo la aibu na ilipokelewa kwa mshituko mkubwa sio tu kwa Watahiniwa, bali pia kwa Wazazi na Wananchi wote kwa ujumla. Hali hii inatokana na ukweli kwamba kama Taifa tukijenga dhana ya uvujaji wa mitihani ni dhahiri inaathiri aina ya Wataalam watakaopatikana katika Nchi yetu kwa miaka ijayo. Tukijenga utamaduni huu wa uvujaji wa mitihani katika ngazi hii Wataalamu wetu hawataweza kushindana katika soko la ajira na katika Vyuo vya Elimu ya Juu. Vilevile, tunawajengea watoto wetu misingi mibovu ya maisha yao. Napenda kuwaasa Wazazi na Wananchi kwa ujumla kwamba tusishabikie wala kuruhusu utamaduni huu wa Wizi wa Mitihani. Ni aibu kubwa kwa Mzazi kushiriki kwa kumpa fedha Mtoto wake ili akanunue mitihani mitaani. Tusikubali kuwapotosha Watoto wetu, kwani kwa kufanya hivyo tunawatumbukiza katika shimo la kujiharibia maisha. Vilevile, Vyombo vya Habari vitusaidie kupiga vita mapungufu haya. Visiwe mashabiki, bali viwaongoze Vijana wetu kuwajengea tabia ya kutokimbilia mitihani inayonunuliwa mitaani. Tuwajengee Watoto mazingira na tabia ya kujifunza kwa bidii kuwa ndio mlango wa kufaulu na hivyo kupata Wanafunzi Bora ambao ndio watakuwa Wataalam bora wa Nchi hii kwa siku zijazo.

  39. Mheshimiwa Spika, pamoja na kuchunguza tukio hilo, Serikali itatumia matokeo ya Uchunguzi huo kuimarisha Baraza la Mitihani la Taifa ili tabia hii tuweze kuikomesha.

  Madeni na Madai ya Walimu

  40. Mheshimiwa Spika, katika Mkutano wa Kumi na Mbili wa Bunge, Serikali iliahidi kwamba ingelipa madeni mbalimbali ya Walimu. Hadi mwezi Septemba 2008, Serikali iliweza kulipa Malimbikizo ya Mishahara ya Walimu yenye jumla ya Shilingi Bilioni 7.4. Aidha, hadi tarehe 29 Oktoba 2008, malimbikizo ya Shilingi Bilioni 2.3 yalikuwa yamefikishwa Hazina tayari kwa kulipwa. Pamoja na Serikali kulipa madai hayo, na kuendelea na zoezi la uhakiki, bado Walimu kupitia Chama chao waliona madai yanachelewa kulipwa na hivyo kuamua kugoma. Wakati akihutubia Taifa, tarehe 31 Oktoba 2008, Mheshimiwa Rais alieleza kwa kirefu chanzo cha mgomo huo. Mheshimiwa Rais aliahidi na kuagiza Madai ya Walimu yote yahakikiwe na Walimu wenye stahili waanze kulipwa.

  41. Mheshimiwa Spika, kutokana na madai hayo, Serikali ilifanya uhakiki wa kina na hadi kufikia tarehe 4 Novemba 2008, Uhakiki wa madai ya Walimu ulikuwa umekamilika katika Halmashauri za Wilaya, Miji na Majiji 129 kati ya Halmashauri za Wilaya, Miji na Majiji 133 zilizopo. Halmashauri za Wilaya na Miji ambazo zilikuwa bado ni Ilala, Temeke, Kinondoni na Manispaa ya Dodoma. Uhakiki wa madai ya Walimu katika Halmashauri na Manispaa hizo nao utakamilika muda mfupi ujao.

  42. Napenda kutumia nafasi hii kuzielekeza Halmashauri zote kukamilisha zoezi hili na kutekeleza Maagizo ya Mheshimiwa Rais akiwa ziarani Mkoa wa Tabora kwa umakini. Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ikishirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI wahakikishe usimamizi wa karibu ili matatizo ya madai na madeni ya Walimu hayatokei tena. Vilevile, natoa Wito kwa Walimu wachache ambao walionekana kudanganya, kujenga utamaduni wa kuwasilisha madai ya kweli ya stahili zao. Kwa kufanya hivyo, itarahisisha uhakiki wa madeni haya na kupunguza kero ya kucheleweshwa kwa malipo kwa wenzao ambao wamekuwa wakidai malipo halali.

  Mikopo ya Wanafunzi

  43. Mheshimiwa Spika, tatizo la utoaji wa mikopo limekuwa likijitokeza Nchini katika miaka ya karibuni tangu utaratibu huu uanze. Utoaji wa mikopo unaongozwa na Sheria ya Bodi ya Mikopo Na. 9 ya mwaka 2004 pamoja na Kanuni na Miongozo iliyowekwa na Serikali. Sheria ya Mikopo pia inaweka bayana masharti ya kutoa mikopo. Hivyo, utaratibu wa kuwabaini wasio na uwezo na wale wenye uwezo unatokana na Sheria. Utaratibu wa kung'amua uwezo wa kiuchumi ndiyo njia pekee iliyopo kwa sasa ya kuwatambua Wanafunzi wenye uwezo kulingana na hali zao kiuchumi. Sera ya uchangiaji pia inalenga kutumia rasilimali kidogo za Serikali ili kuwawezesha Wanafunzi wengi zaidi kupata Elimu ya Juu.

  44. Mheshimiwa Spika, kwa utaratibu wa kawaida, gharama za Elimu zinatakiwa kuchangiwa kati ya Wazazi na Serikali. Kwa mfano, Nchini Kenya wastani wa Wanafunzi 120,000 wameandikishwa (kudahiliwa) kwenye Vyuo Vikuu Nchini humo, lakini wanaopata mkopo ni 10,000 tu. Kwa upande wa Uganda, kati ya wastani wa Wanafunzi 30,000 wanaodahiliwa kwa mwaka ni 4,000 tu ndio wanaopata mkopo kutoka Serikalini. Kwa upande wa Tanzania, Wanafunzi 60,000 wanapata mikopo kati ya Wanafunzi 80,000 waliodahiliwa katika vyuo mbalimbali vinavyotoa Elimu ya Juu katika mwaka wa fedha wa 2008/2009. Kazi hii iliyofanyika ukilinganisha na wenzetu wa Kenya na Uganda ni kubwa na inastahili pongezi kwa Serikali. Lazima tujipongeze kwa kazi nzuri ambayo imefanyika kusomesha Watoto wetu.

  45. Mheshimiwa Spika, Sera ya Uchangiaji inalenga kutumia rasilimali na fedha kidogo za Serikali ili kuwawezesha Wanafunzi wengi zaidi kupata Elimu ya Juu. Kwa hiyo, sio busara Serikali kuwalipia asilimia 100 hata wale Wanafunzi wanaotoka kwenye familia zenye uwezo. Kwa kufanya hivyo, kwa Bajeti ya mwaka 2008/2009 ya Shilingi Bilioni 119, ni Wanafunzi 42,000 tu ndio wangeweza kukopeshwa badala ya 60,000 wanaopata sasa hivi. Kwa maneno mengine, kuwapatia Wanafunzi wote 60,000 mkopo wa asilimia 100, kiasi cha Shilingi Bilioni 163.7 zingehitajika. Kwa upande mwingine, utaratibu huu umewasaidia sana Wazazi wasio na uwezo. Mimi najiuliza, ni kwa nini Mtoto wa Waziri Mkuu au Spika au Mbunge au wa Mfanyabiashara Maarufu ambao wanao uwezo wa kusomesha Watoto wao katika Vyuo Vikuu wafaidike na utaratibu huu ambao tuna uwezo nao badala ya kusaidia wasio na uwezo?

  46. Mheshimiwa Spika, tuelewe kwamba, Sera ya Uchangiaji Gharama za Elimu ya Juu si jambo geni kwa Nchi nyingi Duniani. Hapa kwetu, utaratibu huu hauko katika Elimu ya Juu pekee, bali uko katika Elimu ya Sekondari, Vyuo na pia katika huduma nyingine za jamii kama vile Afya, Maji na Nishati. Mchango wa Serikali katika Elimu ya Juu ni mkubwa ukilinganisha na mkopo wa Mwanafunzi kwa ajili ya Elimu ya Juu. Kwa ujumla gharama wanazolipa Wanafunzi wa Vyuo vya Elimu ya Juu ni za chini sana ukilinganisha na gharama halisi.

  47. Gharama halisi ya Kozi ya Udaktari wa Binadamu kwa mfano kwa Chuo Kikuu cha Muhimbili ni Shilingi Milioni 4.3, lakini Mwanafunzi hulipa Shilingi Milioni 1.0 tu kwa mwaka kupitia kwenye mkopo anaopewa (kwa wasio na uwezo).

  48. Ada halisi kwa Kozi ya Udaktari wa Wanyama, Chuo Kikuu cha Sokoine ni Shilingi Milioni 3.2 kwa mwaka, lakini Mwanafunzi hulipa Shilingi Milioni 1.2 tu. Kwa upande wa Shahada ya Biashara, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, gharama halisi ni Shilingi Milioni 3, lakini Mwanafunzi hulipa Shilingi Milioni 1.25 tu.

  49. Pamoja na kutolipa ada halisi, mikopo wanayolipa Wanafunzi kwa kipindi cha miaka 10 huwa haina riba. Hii ina maana kuwa thamani ya fedha wanazolipa Wanafunzi ni kidogo sana ukilinganisha na thamani ya fedha wakati walipokopa. Kwa hali ya kawaida, hii mikopo ilitakiwa ilipiwe riba kwa Wanafunzi, lakini kwa sasa Serikali inabeba mzigo huo. Hatuna uchaguzi mwingine, bali kuendelea kuchangia gharama za elimu ili Wanafunzi wengi zaidi wapate Elimu ya Juu. Napenda nirudie kusema kwamba Serikali wakati wote itakuwa mstari wa mbele kuhakikisha Wanafunzi wanapata kile wanachostahili kujiendeleza kielimu. Naomba mtamke kuwa Wanafunzi wale wanaotaka Wanafunzi wote kupewa mikopo asilimia 100 haiwezekani. Mheshimiwa Spika haiwezekani Serikali kuwalipia Watoto wa Waziri Mkuu, Spika, Wabunge na Wafanyabiashara wakubwa.

  Migomo na Maandamano Nchini

  50. Mheshimiwa Spika, katika siku za hivi karibuni, Nchi yetu pia imeshuhudia matukio kadhaa ya Migomo na Maandamano yanayofanywa na Vikundi mbalimbali kwa kile kinachoelezwa kuwa ni njia mojawapo ya Vikundi hivyo kudai haki zao. Matukio ya aina hiyo ni pamoja na Migomo na Maandamano ya Wanafunzi wa Vyuo Vikuu, Migomo ya Wafanyakazi wa Kampuni ya Reli Tanzania, Migomo ya Madaktari na Wauguzi katika Hospitali ya Rufaa ya Muhimbili, Migomo ya Wafanyakazi wa NMB, Maandamano na tishio la Mgomo wa Walimu, Maandamano ya waliokuwa Wafanyakazi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, na Migomo midogo midogo katika maeneo mbalimbali ya Sekta Binafsi.

  51. Mheshimiwa Spika, kimsingi, Serikali haipingi kufanyika kwa Migomo na Maandamano ambayo yanafuata Kanuni na Taratibu zilizowekwa Kisheria. Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini Na. 6 ya Mwaka 2004 inatoa Uhuru wa Wafanyakazi kugoma ila tu wafuate Taratibu na Kanuni. Hata kwa upande wa Maandamano, yanaruhusiwa ila tu kwamba yanapaswa kupata Kibali cha Polisi.

  52. Hata hivyo, kwa baadhi ya matukio ya hivi karibuni ambayo tumeyashuhudia, zipo dalili zinazoashiria kuwa baadhi ya Vikundi vinavyohusika na kuandaa Maandamano na Migomo vimefanya hivyo bila ya kufuata Sheria. Aidha, baadhi ya Maandamano na Migomo hiyo imetishia Usalama, Amani, Utulivu na Mshikamano wa Nchi yetu na hivyo kulazimisha Vyombo vya Dola kuingilia kati.

  53. Mheshimiwa Spika, ikumbukwe kuwa Maandamano na Migomo yote ya Wafanyakazi inayotokea sehemu za kazi hasa zile zinazohusika na utoaji wa huduma muhimu kwa jamii, inaleta athari kubwa kwa Taasisi husika na Uchumi wa Nchi kwa ujumla. Kwa mfano, Mgomo uliofanywa na Wafanyakazi wa Kampuni ya Reli Tanzania ulisababisha Wananchi wengi kupata usumbufu na kuchelewa kufika wanakokwenda na wengine kukatiza safari zao. Vilevile, shehena za mizigo zilikwama na hivyo kuwasababishia Wafanyabiashara hasara kubwa na zaidi ya yote, kudumaza shughuli za kiuchumi zinazotegemea Sekta ya Mawasiliano na Uchukuzi Nchini.

  54. Vilevile, Mgomo wa Madaktari Wanafunzi wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ulisababisha Wagonjwa wengi wasio na hatia kukosa huduma muhimu za tiba. Maandamano yaliyofanywa na Wastaafu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambao tarehe 28 Oktoba 2008 walifunga barabara za Ali Hassan Mwinyi na ile ya Umoja wa Mataifa, Jijini Dar es Salaam, ni dhahiri yalisababisha kero kubwa kwa Wananchi wengi ambao kwa njia moja au nyingine hawahusiki na wala sio Wadau kwa madai ya Wastaafu hao.

  55. Mheshimiwa Spika, ni muhimu kujiuliza kama ni busara Makundi ya Wafanyakazi wa Taasisi mbalimbali Nchini kutumia Migomo katika kutetea maslahi yao, bila wahusika kutoa muda wa kutosha wa majadiliano wala kujali maslahi ya Umma na Wananchi wanaowahudumia. Ukweli ni kwamba, hasara na athari kubwa za Migomo pamoja na usumbufu, kero na mateso wanayopata Wananchi na Taifa kwa ujumla na kuzorota kwa utekelezaji wa Mipango ya Maendeleo kutokana na Migomo hiyo, haziwezi kulinganishwa na madai ya makundi ya Wafanyakazi wachache wanaoongoza Migomo hiyo.

  56. Mheshimiwa Spika, napenda kusisitiza kwamba Wafanyakazi, Wanafunzi na Wananchi wengine wowote wanaoitisha na kufanya Migomo ni vyema watambue kuwa pamoja na Serikali kuruhusu Migomo katika mazingira fulani Kisheria, ni lazima maslahi ya Umma yazingatiwe na kulindwa kwanza. Serikali inatoa wito kwa Makundi yote Nchini kuacha kutumia Migomo kama njia pekee ya kupata haki, kwani Migomo ina athari nyingi kama nilivyokwishaeleza. Kwa misingi hiyo, Serikali haitawavumilia Wahusika wanaochochea Migomo isiyo ya lazima na isiyofuata Sheria, Taratibu na Kanuni kwani ina athari kubwa kiuchumi na inahatarisha Amani, Utulivu na Usalama wa Nchi yetu. Vyama vya Wafanyakazi vilivyopewa dhamana ya kisheria kutetea haki za Wafanyakazi pamoja na kudumisha mahusiano mazuri kazini, vina wajibu mkubwa wa kuepusha Migomo isiyo ya lazima. Ni vyema Vyama hivyo vifanye kazi zake kwa kufuata Taratibu zinazokubalika Kisheria.

  57. Vivyo hivyo, Serikali haitavumilia Watendaji wake wote wanaosababisha au kushindwa kutatua kero za Wananchi hadi Wananchi wafikie hatua ya kufikiria migomo wakati uwezo wa kutatua kero zao wanao. Jukumu la Serikali iliyoko madarakani ni kuzipatia ufumbuzi kero mbalimbali za Wananchi kulingana na uwezo uliopo.

  58. Napenda nitumie fursa hii kusisitiza Maelekezo ya Mheshimiwa Rais kwa kuwaomba Wananchi wote kujenga dhana na utamaduni wa uvumilivu. Tujenge utamaduni uliokomaa Kidemokrasia. Mimi ninaamini kwamba migogoro yote ina njia inayofaa katika kuitatua. Tuzungumze. Tukubaliane. Kwa njia hiyo tunaweza kuepusha athari ambazo zingeweza kuepukika. Hebu tukae kwa pamoja tufikirie tena jinsi ya kupunguza matatizo haya.

  Matatizo ya Watu Wenye Ulemavu

  59. Mheshimiwa Spika, niruhusu nizungumzie kidogo kuhusu matatizo ya Walemavu Nchini. Inakadiriwa kwamba Nchi yetu ina Watu wenye Ulemavu wapatao Milioni 3.5. Hawa wanajumuisha Walemavu wa Viungo, Wasioona, Viziwi, Ulemavu wa Akili, Ulemavu mchanganyiko na Ulemavu mwingine. Serikali inatambua umuhimu wa Watu wenye Ulemavu katika maendeleo ya Nchi yetu. Hata hivyo, ipo dhana iliyojengeka miongoni mwetu kwamba Watu wenye Ulemavu hawawezi kazi wala shughuli yoyote. Dhana hii si sahihi hata kidogo na ni dhana potofu. Dhana hii potofu inapingana na mambo makubwa ambayo Walemavu wanaweza kufanya kuchangia maendeleo ya Taifa. Kwa mfano, sote tuliona jinsi Watu wenye Ulemavu walivyoleta msisimko kwenye michezo ya Olimpiki iliyomalizika kule Nchini China hivi karibuni.

  60. Kila Mwananchi ana haki sawa Kisheria ya kushiriki kikamilifu katika mambo muhimu yanayomhusu yeye Mwenyewe na Jamii nzima kwa ujumla. Watu wenye Ulemavu wana haki ya kupata mahitaji ya msingi sambamba na Wananchi wengine wasio na ulemavu. Kimsingi, hawa ni Wenzetu katika jamii ambao kwa maumbile yao wanahitaji maangalizi ya pekee katika jamii. Kwa maana hiyo, ni wajibu wa Serikali kuhakikisha mahitaji yao yanapatikana.

  61. Mheshimiwa Spika, Takwimu zinaonyesha kwamba, hadi sasa, Serikali ina Vituo vya Watu wenye Ulemavu wa aina mbalimbali vinavyotoa Elimu na Mafunzo ya Ufundi kama ifuatavyo:
  Moja: Shule za Msingi Maalum kwa Wasioona tatu (3); Ulemavu wa Akili tano (5); Ukiziwi kumi (10); na Ulemavu wa Viungo tano (5);

  Pili: Shule za Sekondari kwa Wasioona kumi na tano (15); Ulemavu wa Akili mbili (2); Ulemavu wa Viungo tatu (3); na Ukiziwi nane (8);

  Tatu: Vyuo vya Ufundi kwa Wasioona kimoja (1); na Ulemavu mchanganyiko sita (6).

  Serikali inavihudumia Vituo hivi takriban 58 kwa kuandaa Walimu wa Elimu Maalum; Kutoa vifaa vya kufundishia; Kutoa nyenzo za kujimudu; Kuboresha miundombinu katika mazingira ya shule; na kutoa chakula, malazi na huduma za msingi.

  62. Mheshimiwa Spika, napenda nitumie nafasi hii kuihakikishia jamii ya Watu wenye Ulemavu na Wananchi wote kwa ujumla kwamba Serikali inawajali na inatambua matatizo yao. Aidha, Serikali imeandaa Mikakati ya kukabili matatizo hayo ya Watu wenye Ulemavu Nchini. Kubwa katika hili ni Kuandaa Mapendekezo ya Marekebisho ya Sheria Na. 2 ya Mwaka 1982 ili kutoa nafasi ya kuboresha zaidi huduma kwa Watu wenye Ulemavu katika nyanja za Ajira, Miundombinu, Elimu na Upatikanaji wa Vifaa kwa urahisi.

  63. Kupitia Bunge hili naomba kuziagiza Wizara zinazohusika na huduma za Walemavu ikiwemo Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii; Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi; Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma; na Wizara ya Fedha na Uchumi kushirikiana kukamilisha Miongozo yote inayohusu Watu wenye Ulemavu Nchini. Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii iratibu zoezi hili na nipate Taarifa ya Utekelezaji kabla ya Mkutano wa Kumi na Nne wa Bunge.

  Utunzaji wa Mazingira

  64. Mheshimiwa Spika, Uhai na Ustawi wa Nchi yetu unategemea kwa kiasi kikubwa Hifadhi na Utunzaji wa Mazingira. Ukizunguka sehemu mbalimbali za Tanzania utakuta sehemu mbalimbali zimechomwa moto na unaweza kudhani yapo mashindano maalum ya uchomaji moto nchini. Kumekuwa na utamaduni miongoni mwa Watanzania Wakulima na Wafugaji wa kuchoma moto maeneo mbalimbali Vijijini. Wakulima huchoma moto nyasi kwa ajili ya kurahisisha utayarishaji wa mashamba wakati Wafugaji huchoma moto ili kuwezesha majani mabichi kuchipua kwa ajili ya Mifugo yao. Vilevile, kuna sehemu za Nchi ambapo wana imani kuwa anayechoma moto na kuwaka kwa muda mrefu ana mkono mzuri. Utamuduni huu umepitwa na wakati. Kuchoma moto hovyo kunaharibu mimea ambayo mingine huwa ni mazao ya chakula na hivyo kuleta ukame na njaa. Matokeo ya ukame na njaa ni kuongezeka kwa umaskini. Uchomaji wa moto hovyo huua viumbe hai wanaoishi kwenye majani na ardhini. Wataalam wanatueleza kuwa viumbe hivyo ni muhimu kwa kurutubisha ardhi.

  65. Mheshimiwa Spika, kuna uharibifu wa Mazingira unaoendelea kufanywa kwenye vyanzo vya maji. Miti inakatwa hovyo na vyanzo hivyo vimekuwa malisho maarufu ya idadi kubwa ya mifugo. Matokeo ya kufanywa hivyo ni kukauka kwa vyanzo hivyo vya maji. Lakini tujiulize itakuwaje binadamu, wanyama na mimea vitapokosa maji? Ni wazi kuwa maji ni uhai na bila maji hakuna uhai.

  66. Tumeharibu sana mazingira, hali hii imesababisha maeneo mengi kukosa mvua na kuwa na upungufu wa uzalishaji wa mazao. Ni muhimu Wananchi wakazidi kufahamishwa madhara yatokanayo na kuchoma moto hovyo na kuharibu vyanzo vya maji. Halmashauri ziwe na Sheria zinazodhibiti uchomaji moto hovyo, uharibifu wa vyanzo vya maji na mazingira kwa ujumla wake. Sheria hizo zisimamiwe na kutekelezwa kwa kushirikisha Viongozi wa Vijiji, Kata na Wilaya. Pia, ni wakati sasa wa kuelekeza rasilimali za kutosha katika kulinda uhai wa viumbe hai vyote ikiwa ni pamoja na sisi Wanadamu. Tupande miti mara kwa mara kwenye vyanzo vya maji, mashamba yetu, nyumba zetu, kando kando ya barabara, n.k. Pamoja na Siku ya Kupanda Miti Kitaifa, ni vizuri kila Mkoa ukawa na siku maalum ya kupanda miti inayoendana na hali yake ya Hewa. Badala ya kuwa na mashindano ya kuharibu mazingira tuwe na mashindano ya kulinda mazingira katika ngazi ya Kijiji, Kata, Wilaya, Mkoa na Taifa. Natumaini kila mmoja wetu atajisikia vizuri kuzungukwa na uoto wa asili na ikiwa upatikanaji wa maji halitakuwa tatizo kwenye jamii. Hilo liwe ndilo lengo letu kuu.

  Hitimisho

  67. Mheshimiwa Spika, wakati tunatekeleza malengo ya Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini Tanzania (MKUKUTA), tuelekeze nguvu zetu kutumia fursa zilizopo kutekeleza Mkakati huu. Twendeni tukawahimize Wananchi kushiriki katika Maendeleo yao. Mambo ya Msingi ambayo napenda kuyasisitiza ni haya yafuatayo:
  Moja: Tunayo nafasi nzuri ya kutumia rasilimali zilizopo hususan Madini kuinua uchumi wetu. Tutumie nafasi iliyopo kwa kuyaongezea thamani Madini yetu badala ya kuyauza ghafi. Tuanze kwa kushirikiana na Sekta Binafsi. Kwa kufanya hivyo tutafanikiwa;

  Pili: Tunatoka Bungeni wakati Msimu wa Kilimo umekaribia. Twendeni tukasukume Mapinduzi ya Kilimo. Wakuu wa Mikoa, Wilaya, Wakurugenzi wa Wilaya, Madiwani tusukume hili ili iwe dhambi kutozingatia Kanuni Bora za Kilimo. Tuanze kufuatilia kwa karibu upatikanaji wa Pembejeo muhimu kwa Kilimo ikiwemo Mbolea, Mbegu Bora, na Madawa ya Kuuwa Wadudu waharibifu, ili kuongeza tija.

  Tatu: Tujenge dhana ya uvumilivu. Tuepuke kujenga tabia ya kuona kwamba Maandamano na Migomo ndiyo njia ya kutatua migogoro. Bado Serikali yetu ni nzuri, inajitahidi kukamilisha mahitaji yote ya Walimu, Wastaafu mbalimbali na matatizo ya Wanafunzi. Kubwa tuwe na Subira na tushirikiane.

  Nne: Tushirikiane kuwasaidia Watu wenye Ulemavu, kwani ni sehemu ya jamii yetu. Tuwape moyo, tuwasaidie pale inapobidi ili waweze kushiriki katika kujiletea maendeleo yao.

  68. Mheshimiwa Spika, leo hii tunahitimisha Mkutano wa Kumi na Tatu wa Bunge. Tumebakiza Mikutano takriban Saba (7) kabla ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2010. Sisi sote, kila mmoja wetu ndani ya Bunge hili bila kujali Itikadi ya Chama chake ni lazima ujiulize, kuwepo kwetu ndani ya Bunge hili tumewasaidiaje Wananchi wetu tunaowawakilisha. Ni vema kila mmoja wetu kuanza kujifanyia tathmini mwenyewe ya kitu gani alichokifanya cha kuwaondolea Wananchi Umaskini.

  Je, umeshiriki vipi katika kuwaondolea Wananchi kero ambazo zinawakabili. Kila mmoja ajipime mwenyewe kujua kama kuwepo kwake ndani ya Bunge hili ametumia muda wake katika kupunguza Kero za Wananchi au ndio amewazidishia ukali wa Maisha. Twendeni nyumbani tukatumie muda wetu kutafakari yote yale ambayo yanatuhusu tuyafanye kwa Manufaa ya Wananchi wetu.

  69. Mheshimiwa Spika, nimalizie kwa kuwashukuru wote waliosaidia katika kufanikisha Mkutano huu. Nakushukuru kwa namna ya pekee wewe Mheshimiwa Spika, na Naibu Spika kwa kutuongoza vizuri. Nawashukuru Wenyeviti wa Bunge kwa msaada mkubwa walioutoa kuliongoza Bunge hili.

  Nawashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa michango yenu mbalimbali wakati wa kujadili Miswada tuliyoipitisha katika Mkutano huu. Namshukuru Kaimu Katibu wa Bunge, Dkt. Thomas Kashilillah na Wasaidizi wake pamoja na Wataalam wa Serikali kwa kazi nzuri ya kutoa misaada ya Kitaalam na huduma mbalimbali katika kufanikisha Mkutano huu. Navipongeza Vyombo vya Habari kwa kuwafikishia Wananchi habari ya yale yaliyojitokeza hapa Bungeni kwa Wakati na Usahihi. Mwisho, nawapongeza madereva wote kwa kuwaendesha Viongozi na Wataalam wote kwa umakini mkubwa na hivyo kuwaepusha na ajali. Wote Asanteni Sana!

  70. Mheshimiwa Spika, leo ni tarehe 7 Novemba 2008. Katika kipindi cha takriban mwezi mmoja na nusu tutakuwa tumefikia mwisho wa mwaka 2008. Ni matumaini yangu kwamba Inshallah Muumba Wetu atatujalia sote kama tulivyo kumaliza mwaka huu na kuuanza mwaka mwingine salama. Napenda nitumie nafasi hii kuwatakieni wote Heri, Baraka na Fanaka tele za Sikukuu ya Krismas na Mwaka Mpya wa 2009!

  71. Nawatakia wote safari njema ya kurejea kwenye Majimbo yenu na nyumbani kwenu.

  72. Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo haya mafupi, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu sasa liahirishwe hadi tarehe 27 Januari 2009, siku ya Jumanne Saa 3:00 Asubuhi, litakapokutana tena kwa ajili ya Mkutano wa 14 kwenye Ukumbi huu hapa Dodoma.

  73. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.
   
 3. Mzee Mwanakijiji

  Mzee Mwanakijiji Platinum Member

  #3
  Nov 7, 2008
  Joined: Mar 10, 2006
  Messages: 31,362
  Likes Received: 6,393
  Trophy Points: 280
  Hotuba ya Mheshimiwa Mizengo Pinda (mb), Waziri Mkuu wakati wa kutoa hoja ya kuahirisha mkutano wa kumi na tatu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano waTanzania, Tarehe 7 Novemba 2008, Dodoma

  UTANGULIZI

  1. Mheshimiwa Spika, kabla ya kutoa hoja ya kuliahirisha Bunge lako Tukufu, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kufikia salama siku ya leo. Namshukuru kwa kutuwezesha wote kukamilisha shughuli zote zilizopangwa kufanyika katika Mkutano huu wa Kumi na Tatu.

  Pongezi

  2. Mheshimiwa Spika, napenda nitumie fursa hii ya mwanzo kabisa kuvipongeza Vyama vyote vilivyoshiriki katika Uchaguzi Mdogo wa Jimbo la Tarime uliofanyika tarehe 12 Oktoba 2008, kufuatia Kifo cha Mpendwa wetu, Mheshimiwa Chacha Wangwe. Kwa njia ya pekee, napenda kumpongeza kwa dhati kabisa, Mheshimiwa Charles Nyanguru Mwera (Mb.) kwa kushinda Uchaguzi huo kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo – CHADEMA. Nawapongeza Wananchi wa Tarime ambao pamoja na changamoto nyingi wakati wa Kampeni hatimaye walikamilisha Uchaguzi kwa kupiga kura kwa amani, utulivu na mshikamano.

  Nawapongeza wote kwa maamuzi yao ya Kidemokrasia waliyotumia kuchagua mtu wanayempenda awawakilishe kwenye Bunge hili. Napenda kuchukua nafasi hii kuwakumbusha Watanzania wote kuwa wajibu wa KIDEMOKRASI ni kulumbana kwa hoja na siyo mapigano, vitisho au vurugu. Katika chaguzi zetu tuepuke mambo yote yanayoweza kuvuruga amani na utulivu wetu.

  3. Mheshimiwa Spika, niungane na Waheshimiwa Wabunge wenzangu kumpongeza Mheshimiwa Pindi Hazara Chana, Mbunge wa Viti Maalum kwa kuchaguliwa kuwa Mjumbe kwenye Baraza la Chuo Kikuu cha Sayansi za Afya Muhimbili. Vilevile, napenda kuwapongeza Mheshimiwa Beatrice Matumbo Shelukindo, Mbunge wa Kilindi; Mheshimiwa Benson Mwailugula Mpesya, Mbunge wa Mbeya Vijijini; na Mheshimiwa Dkt. Ali Tarab Ali, Mbunge wa Konde kwa kuchaguliwa kuwa Wajumbe kwenye Bodi ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania.

  4. Kwa wote waliochaguliwa tunawapongeza sana. Ni mategemeo yetu sote kuwa watawakilisha Bunge hili na Watanzania wote kwa ujumla vizuri katika Bodi za Taasisi hizo. Ninaamini kwamba uwezo wanao na ndio maana wamechaguliwa.

  5. Mheshimiwa Spika, katika Mkutano huu wa Kumi na Tatu, Waheshimiwa Wabunge walipata nafasi ya kuuliza Serikali jumla ya Maswali 121 ya Msingi na mengine mengi ya Nyongeza. Nitumie fursa hii kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote walioweza kuuliza Maswali ambayo kwa ujumla wake yalilenga katika kujua na kuhimiza shughuli za Maendeleo katika Majimbo, Sekta zinazohusika na maendeleo za Kitaifa. Aidha, nawashukuru Mawaziri na Naibu Mawaziri wa Sekta zilizohusika kwa kutoa majibu ya maswali hayo kwa ufasaha na kwa ufanisi wa hali ya juu. Nawapongeza pia Waheshimiwa Wabunge kwa maswali yao 19 ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu

  6. Mheshimiwa Spika, katika Mkutano huu Waheshimiwa Wabunge waliweza kujadili na kupitisha Miswada ifuatayo:

  i) Muswada wa Sheria ya Kurekebisha Sheria ya Bodi ya Usajili wa Makandarasi wa Mwaka 2008, [The Contractors Registration (Amendment) Bill, 2008];
  ii) Muswada wa Sheria ya Utoaji wa Miliki za Sehemu za Majengo wa Mwaka 2008, [The Unit Title Bill, 2008];

  iii) Muswada wa Sheria ya Mikopo ya Nyumba wa Mwaka 2008, [The Mortgage Financing (Special Provisions) Bill, 2008];

  iv) Muswada wa Sheria ya Biashara ya Ngozi wa Mwaka 2008 [The Hides, Skins and Leather Trade Bill, 2008];

  v) Muswada wa Sheria ya Ustawi wa Wanyama wa Mwaka 2008 [The Animal Welfare Bill, 2008];

  vi) Muswada wa Sheria ya Kutoa Fidia kwa Wafanyakazi wa Mwaka 2008 [The Workers Compensation Bill, 2008];

  vii) Muswada wa Sheria ya Afya ya Akili wa Mwaka 2008 [The Mental Health Bill, 2008]; na

  Bunge lako Tukufu pia lilijadili na kuridhia:

  i) Azimio la Bunge kuhusu Kumpongeza Rais Mteule wa Marekani, Mheshimiwa Barrack Obama kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa 44 wa Marekani; na

  ii) Azimio la Bunge kuhusu Upanuzi wa Hifadhi ya Ziwa Manyara.

  7. Vilevile, Bunge lako Tukufu lilipokea Taarifa za Serikali zifuatazo:

  i) Taarifa ya Kamati ya Rais ya Kuishauri Serikali kuhusu Usimamizi wa Sekta ya Madini;

  ii) Taarifa ya Utekelezaji wa Azimio la Bunge Kuhusu Utendaji Usioridhisha wa Kampuni ya Tanzania (International Containers Terminal Services (TICTS); na
  iii) Taarifa ya Utekelezaji wa Azimio la Bunge Juu ya Utendaji Usioridhisha wa Shirika la Reli Tanzania [Tanzania Railways Limited (TRL)] Uliofanywa na Kampuni ya Rites ya India.

  Mwisho, Bunge lako Tukufu lilipokea Kauli za Serikali na Hoja za Waheshimiwa Wabunge ambazo ziliwasilishwa hapa Bungeni.

  8. Mheshimiwa Spika, napenda kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote walioshiriki kupokea, kujadili na kutoa ushauri kuhusu Miswada, Maazimio na Taarifa mbalimbali zilizowasilishwa hapa Bungeni wakati wa Mkutano huu. Michango yao itazingatiwa na itasaidia kuboresha juhudi za Serikali katika kuwaletea Wananchi maendeleo.

  Madini

  9. Mheshimiwa Spika, katika Mkutano huu, Bunge lako Tukufu limepata nafasi ya kujadili Taarifa ya Kamati ya Rais ya Sekta ya Madini iliyoongozwa na Mheshimiwa Jaji Mark Bomani. Bila shaka Waheshimiwa Wabunge watakubaliana nami kwamba Kamati ilifanya kazi nzuri na kwa umakini mkubwa. Mapendekezo yaliyotolewa yataisaidia Serikali kuboresha Sekta hii muhimu kwa maendeleo ya uchumi wa Nchi yetu. Baadhi ya mapendekezo na ushauri uliotolewa yatatekelezwa kwa kipindi cha muda mfupi na mengine yatahitaji muda mrefu kidogo kutekelezwa. Napenda nilihakikishie Bunge lako Tukufu kwamba, Serikali imeanza utekelezaji wa baadhi ya mapendekezo na tutakuwa tunaliarifu Bunge lako hatua tutakazokuwa tunachukua kila wakati. Mapendekezo mengine kama ya kurekebisha Sera na Sheria ya Madini yanaendelea kufanyiwa kazi, kwani Mchakato wa kurekebisha Sheria na Sera ulishaanza hata kabla ya kuundwa kwa Kamati ya Jaji Bomani.

  10. Mheshimiwa Spika, ni lazima tukubaliane kwamba, ili Sekta ya Madini itoe mchango mkubwa zaidi katika maendeleo ya uchumi wetu na kuongeza ajira nyingi, tunahitaji kuyaongezea thamani Madini yetu hapa Nchini.

  11. Nilipotembelea Namibia hivi karibuni, nilijionea Kiwanda cha Kukata na Kusafisha Almasi ambacho kinafanya kazi nzuri ya kuongeza thamani Madini ya Almasi kwa kutumia Almasi ghafi inayozalishwa Namibia jambo ambalo limeipatia Namibia fedha nyingi pamoja na ajira. Hata hivyo, ili kuongeza Madini thamani kunahitajika uwekezaji mkubwa na uhakika wa malighafi za kutosha. Hizi ni baadhi tu ya changamoto ambazo hatuna budi kukabiliana nazo. Ni katika kufanya mabadiliko makubwa kwenye Sekta ya Madini tunaweza kuanza na sisi kushirikiana na Sekta Binafsi kuongeza thamani Madini hapa Nchini badala ya kuyauza ghafi. Tunalifuatilia suala hili kwa ukaribu mkubwa na nina imani tutafanikiwa.

  12. Nichukue fursa hii kuishukuru kwa dhati Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini kwa kuichambua vyema Taarifa ya Jaji Bomani na kutoa mapendekezo yake mazuri kwa Serikali. Vilevile, niwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote kwa kuchangia kikamilifu katika mjadala wa Taarifa hii na niwahakikishie kwamba michango yenu itafanyiwa kazi inayostahili. Nawasihi wote tuvute subira ili Wataalam wapate nafasi ya kuyashughulikia mapendekezo yenu ambayo nina imani yatasaidia sana katika jitihada zinazoendelea za kuboresha Sekta ya Madini.

  Kilimo

  13. Mheshimiwa Spika, tarehe 16 – 18 Oktoba 2008, nilishiriki katika Mkutano wa Kuhamasisha Uzalishaji wa Mazao ya Kilimo uliofanyika Mkoani Morogoro ambao ulihusisha Mikoa ya Ruvuma, Iringa, Mbeya, Rukwa, Morogoro na Kigoma. Lengo kuu lilikuwa ni kuweka Mikakati ya namna ya Kuongeza Uzalishaji wa Mazao hapa Nchini hususan kupitia utekelezaji wa Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo – ASDP.

  14. Tuliona ni vema kuanza na Mikoa hii sita katika mchakato huu kwa sababu mbalimbali, lakini kubwa ni kwamba Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini ya Ruvuma, Rukwa, Iringa na Mbeya, ndiyo Mikoa ambayo kihistoria imekuwa na mchango mkubwa katika uzalishaji wa mazao ya chakula na hivyo kuifanya ijulikane kama “The Big Four”. Mkoa wa Morogoro ulijumuishwa na Mikoa hii ya Nyanda za Juu Kusini kutokana na changamoto uliopewa na Mheshimiwa Rais kuwa Ghala la Taifa la Chakula. Vilevile, Mkoa wa Kigoma nao ulijumuisha kutokana na fursa ilizo nazo katika Kilimo zinazofanana sana na Mikoa hiyo mingine mitano.

  15. Mheshimiwa Spika, takwimu za uzalishaji za mwaka 2007/2008 zinaonyesha kuwa Mikoa hii sita inachangia Tani milioni 3.9, sawa na asilimia 36 ya mahitaji ya chakula Nchini. Kitaifa uzalizalishaji ulifikia Tani milioni 10.78 za chakula kwa mwaka huo. Matarajio ni kwamba kufanikiwa kwa Mikoa hii sita katika Kilimo itakuwa chachu kwa Mikoa mingine kutumia mbinu na Mikakati iliyofikiwa kwenye Mkutano huo ili kuongeza uzalishaji kwa Nchi nzima. Dhamira yetu ni kufanya Mikutano mingine kama huu kwa Mikoa mingine kwa kuzingatia hali ya Mikoa inayofanana Kijiografia na Hali ya Hewa.

  16. Mheshimiwa Spika, Uongozi wa Nchi yetu katika ngazi zote Vijiji, Kata, Tarafa, Wilaya na Mkoa lazima utuwezeshe kutekeleza yale tuliyojifunza kwa vitendo zaidi. Mambo hayo ambayo hatuna budi kuyafuatilia kwa karibu ni haya yafuatayo.

  i) Kuongeza Tija

  17. Mheshimiwa Spika, imejidhihirisha kuwa Kilimo cha Tanzania bado kina tija ndogo sana na hivyo mavuno hayalingani kabisa na kiasi cha eneo linalolimwa. Kwa mfano, wakati Wakulima wengi sasa hivi wanazalisha mahindi wastani wa Tani 1.2 kwa hekta, lakini kama Kanuni za Kilimo Bora zitatekelezwa wanaweza wakaongeza uzalishaji.

  Takwimu za mwaka 2007/2008 zinaonyesha kuwa tulilima mahindi hekta milioni 2.88 na tukavuna Tani Milioni 3. Lakini kama tungetekeleza Kanuni za Kilimo Bora, ilitakiwa kuzalisha Tani 5 kwa Hekta na kuvuna Tani milioni 14.4 katika eneo hilo hilo. Hivyo, uzalishaji huu wa mahindi unathibitisha kuwa tija ni ndogo sana.

  18. Mheshimiwa Spika, ni wajibu wetu Viongozi na Wataalam kumsaidia Mkulima kuongeza Tija ili aweze kupunguza umaskini na kuongeza akiba ya Hifadhi ya Chakula cha Taifa. Lengo ni kuongeza uzalishaji ili eneo dogo linalotumika litoe mazao mengi kwa kutimiza Kanuni za Kilimo Bora. Mfano Mkulima anaweza kuongeza uzalishaji kutoka magunia 12 ya sasa kwa Hekta na kufikia takriban magunia 30.

  ii) Upatikanaji wa Pembejeo

  19. Mheshimiwa Spika, suala la upatikanaji wa Pembejeo za Kilimo, bei kubwa, usambazaji na matumizi yasiyo sahihi bado ni tatizo. Upatikanaji wa Mbolea, Mbegu Bora pamoja na Madawa ya Viatilifu hayakidhi mahitaji. Kwa mfano, mahitaji ya aina mbalimbali ya Mbolea yanakadiriwa kuwa ni Tani 400,000 kwa mwaka. Mwaka 2007/2008 zilipatikana Tani 211,000, sawa na asilimia 53 ya mahitaji.

  20. Kwa Msimu wa Kilimo wa Mwaka 2008/2009 hadi mwishoni mwa Oktoba 2008, kiasi cha Mbolea kilikuwa Tani 188,600 tu. Kiwango cha mbolea ya tani 150,000 kitauzwa kwa bei ya Ruzuku. Hiki ni kiasi kidogo kwa kuzingatia kwamba Msimu wa Kilimo ndiyo umekaribia. Hata hivyo, Serikali imeongeza kiasi cha fedha kwa ajili ya Pembejeo kutokana na fedha za EPA kama Mheshimiwa Rais alivyoahidi katika Hotuba yake aliyoitoa hapa Bungeni. Ni matumaini yangu nyongeza hii italeta mabadiliko katika suala zima la upatikanaji wa Pembejeo Nchini na hivyo kuongeza uzalishaji.

  21. Mheshimiwa Spika, kutokana na upungufu wa upatikanaji wa Mbolea Nchini, Serikali imetoa udhamini kwa Kampuni ya Mbolea Tanzania – Tanzania Fertilizer Company, ili waweze kuagiza Mbolea zaidi ambayo tayari imekwishaagizwa na tutaipata hivi karibuni na kusambazwa.

  22. Mwaka huu, tutaanza kutumia mfumo wa VOCHA. Lengo ni kuhakikisha kwa kiasi kikubwa mbolea ya ruzuku inawafikia na kuwanufaisha Wakulima moja kwa moja. Ninaelewa ugumu wa utaratibu kukubalika hivi sasa kutokana na uwezo wetu mdogo wa kuwafikia Wakulima wengi. Mwanzo wa jambo lolote huwa mgumu. Wito wangu kwa Viongozi na Wananchi wote ni kuwa tuukubali utaratibu huu uanze ili tupate uzoefu. Uzoefu tutakaoupata utatusaidia sana katika kufanya maboresho ili kuweza kukidhi mahitaji ya Mbolea kwa Wakulima hapa Nchini. Mfumo wa VOCHA ni bora kuliko tuliotumia mwaka jana kwa sababu mbolea ya ruzuku inawafikia Wakulima moja kwa moja na hivyo kumfanya kila Mkulima atumie mbolea.

  Natoa Wito kwa Waheshimiwa Wabunge wote washiriki katika kuwaelimisha Wakulima umuhimu wa matumizi ya mfumo wa VOCHA. Tukishirikiana kwa pamoja Mfumo huu wa VOCHA utafanikiwa na hivyo kuwanufaisha Wakulima.

  iii) Kuongeza na Kusambaza Huduma za Ugani

  23. Mheshimiwa Spika, pamoja na uhaba wa Maafisa Ugani, ni lazima wale waliopo watekeleze wajibu wao wa kuwezesha Wakulima kupata Elimu itakayowawezesha kutekeleza Kanuni za Kilimo Bora. Pamoja na upungufu wa Maafisa Ugani katika Mikoa, Maafisa Ugani waliopo wanaweza kuleta mabadiliko makubwa ya Kilimo chetu, kama watasimamiwa vizuri na kupewa vitendea kazi. Kwa mfano, Mkoa wa Mbeya una Maafisa Ugani 488; Morogoro 355; Iringa 428; Ruvuma 201; Rukwa 202 na Kigoma 204. Pamoja na upungufu uliopo, lakini Wataalam hawa waliopo wakitumiwa vizuri, wakawezeshwa kwa kupewa vitendea kazi kama vile Pikipiki na zaidi ya yote wao wenyewe wakawa na Mpango wa Kazi na wakijituma na kutimiza wajibu wao, Mapinduzi ya Kilimo Tanzania yanawezekana kabisa.

  24. Vilevile, tunazo Taasisi za Umma kama Magereza, Kambi za Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Vyuo vya Kilimo na Mifugo, Vyuo vya Maendeleo ya Jamii ambavyo ni lazima viwe vitovu vya Mapinduzi ya Kilimo Nchini. Ni muhimu katika vita hii tukatumia kila nguvu kazi iliyopo. Ni jukumu la kila Halmashauri kuhakikisha inatoa mafunzo ya msingi ya Kanuni za Kilimo Bora kwa Vijana wasiopungua 20 katika kila Kijiji watakaosaidia katika utoaji elimu hiyo kwa Wakulima chini ya usimamizi wa Maafisa Ugani. Aidha, upo umuhimu wa kuanzisha Mabaraza ya Kilimo ya Kata ambayo yatatoa msukumo mkubwa katika Kilimo. Vilevile, Sekta Binafsi ishirikishwe katika kutoa huduma za Ugani kwa Wakulima na Wafugaji ili kuongeza uzalishaji wa mazao. Nitamuomba Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika kutoa maelekezo mahususi namna Mabaraza ya Kilimo ya Kata yatakavyofanya kazi.

  25. Mheshimiwa Spika, kila Mkurugenzi wa Halmashauri Nchini ahakikishe kuwa Maafisa Ugani wanaacha kukaa Ofisini na badala yake wawafuate Wakulima popote walipo ili kujionea shughuli zao za Kilimo na kutoa ushauri stahiki.

  Wawe na Ratiba ya Kazi na Daftari la Wakulima wanaowahudumia. Kama vile Madaktari wanavyokuwa na Daftari la Wagonjwa na kila siku wanajua watawaona Wagonjwa wangapi na saa ngapi, ni muhimu na Maafisa Ugani wafanye hivyo. Kama vile Walimu walivyo na Daftari la kuandaa Vipindi vya kila siku, Maafisa Ugani nao wawe na Daftari linaloonyesha Mpango wa Kazi wa kila siku. Wakurugenzi wa Halmashauri waweke vigezo vya tathmini kwa Maafisa Ugani wote na wahakikishe usimamizi mzuri na ufuatiliaji unakuwepo wakati wote. Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Wilaya wafuatilie taarifa za Madaftari ya Maafisa Ugani wajue wanafanya nini. Vilevile, Halmashauri zihakikishe zinawapatia Maafisa Ugani makazi karibu na maeneo ya Wakulima ili wawe karibu katika kutoa ushauri kwa Wakulima.

  iv) Teknolojia na Utafiti

  26. Mheshimiwa Spika, ili kuleta kweli Mapinduzi ya Kilimo Nchini hatuna budi kuchukuwa hatua za makusudi za kuongeza ushirikiano wa karibu kati ya Watafiti, Wagani na Wakulima. Lazima Wataalam mbalimbali wahakikishe kuwa matokeo ya tafiti zao yanawafikia Wakulima na kwa wakati. Aidha, lazima kuweka taratibu itakayowezesha Teknolojia sahihi kutangazwa na kuenezwa kwa Wakulima ili kuongeza uzalishaji.

  Kuhusu uzalishaji wa Mbegu Bora, nimeelekeza Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika ihusishe na kushirikisha Taasisi za Serikali kama Magereza na Jeshi la Kujenga Taifa ili mashamba yao, yatumike kikamilifu kuongeza uzalishaji wa Mbegu Bora, ambazo asilimia 75 sasa hivi tunaagiza kutoka Nchi za nje.

  v) Umwagiliaji

  27. Mheshimiwa Spika, Kilimo cha Umwagiliaji Maji bado kipo chini sana kulingana na maeneo ambayo yanaweza kutumika katika Kilimo cha Umwagiliaji. Kwa mfano, Mkoa wa Morogoro una jumla ya Mito 143 inayotiririsha maji mwaka mzima. Lakini kati ya hekta 123,500 zinazofaa kwa Kilimo cha Umwagiliaji, ni hekta 8,800 tu ndizo zinazotumika, sawa na asilimia 7.0 ya eneo lote linalofaa kwa Kilimo cha Umwagiliaji. Tatizo hili lipo karibu Mikoa yote Nchini.

  28. Kitaifa tunazo hekta milioni 29.4 ambazo tunaweza kuendesha Kilimo cha Umwagiliaji, lakini hivi sasa tunatumia jumla ya hekta 290,000, sawa na asilimia 1 tu hapa Nchini. Takwimu hizi zinaonyesha kuwa bado Kilimo cha Umwagiliaji hatujakipa umuhimu mkubwa. Lazima tukubali kwamba hapa bado kuna udhaifu. Hivi sasa tumeomba fedha kwa ajili ya Kilimo cha Umwagiliaji. Lazima tuzitumie vizuri na kwa ufanisi. Hivyo, naagiza Kilimo cha Umwagiliaji kipewe kipaumbele hasa katika miradi inayoibuliwa na Wananchi Wilayani kupitia DADPs. Wataalamu wa Kilimo wawasaidie Wananchi kuibua miradi katika maeneo yao. Serikali kwa upande wake itaangalia Wataalam wa Kanda watakavyoelekezwa kusaidia Wakulima.

  29. Mheshimiwa Spika, Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo ina nafasi nzuri katika kuleta Mapinduzi ya Kijani. Pamoja na kuwa ASDP inatoa msukumo mkubwa katika Kilimo, bado Wananchi hawajaelimishwa na kuhamasishwa kuibua miradi mizuri na yenye kuweza kuleta mabadiliko ya haraka katika Kilimo. Kwa mfano, hivi sasa Wananchi wengi wameanza kupata ufahamu wa Matrekta Madogo, lakini hawakuwa wamepata elimu na fursa ya kuibua miradi ya aina hiyo. Jukumu la Viongozi na Wataalam ni kuipeleka Programu hii karibu zaidi na Wananchi na kuwaelimisha ili waweze kuibua miradi mizuri itakayoongezea tija.

  30. Mheshimiwa Spika, kwa upande wa mazao ya biashara, lazima tuwasaidie pia Wakulima katika kuongeza tija kwa mazao kama vile Korosho, Kahawa, Tumbaku na Pamba. Hatuna tena muda wa kusubiri, bali Mikoa husika ichukue hatua za kuhakikisha uzalishaji wa mazao haya unaongezeka, kupata bei nzuri na kujumuisha mazao haya kwenye Mipango ya Maendeleo ya Kilimo ya Wilaya DADPs ili kupata ruzuku ya Serikali. Uzalishaji wa Kahawa, kwa mfano, hivi sasa Nchini ni sawa na kilo 200 kwa hekta ikilinganishwa na lengo la kilo 500 kwa hekta, zilizopo katika Mkakati wa Kuendeleza Zao la Kahawa.

  31. Mheshimiwa Spika, ili kuongeza tija ya zao kama Kahawa, ni lazima kupanda kwa wingi miche bora ambayo imefanyiwa utafiti na Kituo cha Utafiti cha TaCRI na kuonyesha ongezeko la tija kwa mwaka. Ni lazima sasa kila Mkoa unaolima zao la Kahawa kuanzisha bustani za miche bora za mazao ya biashara katika maeneo ya Wakulima ili miche hiyo iwafikie Wakulima haraka. Aidha, ni lazima kuwahimiza kutumia Pembejeo, hasa mbolea za Viwandani na samadi ambayo inapatikana katika maeneo ya Wafugaji yaliyo karibu na mazao haya ya biashara. Wakuu wa Mikoa, Wilaya na Wakurugenzi wa Wilaya wajipange vizuri ili waweze kufikia malengo.

  32. Mheshimiwa Spika, tumejifunza mengi kwa kutumia mfano wa Mikoa Sita ya awali tuliyoanzia nayo. Kutokana na hali ya Kilimo ilivyo, Uongozi wa Mikoa kwa kushirikiana na Viongozi wa Wilaya waweke utaratibu wa kujipima. Kuwepo na Mikutano ya kutathmini maendeleo ya Mipango yao ili kujua wamefika wapi na kama kuna matatizo wapange jinsi ya kuyatatua. Sekretarieti za Mikoa zijipange vizuri ili kuweza kuzisimamia Halmashauri katika majukumu yake hasa suala la uzalishaji. Halmashauri ziwe na mikakati mizuri ya uzalishaji badala ya kuwa watumiaji wa fedha tu, na Vijiji vibadilike kutoka kuwa Vijiji vya Utawala na kuwa Vijiji vya Uzalishaji na Maendeleo. Ni lazima tubadilike kimtazamo na kiutendaji kama tunataka kubadili Kilimo chetu.

  Nitapenda kujua kila nikifika kwenye ziara Mikoani ni kwa kiasi gani mabadiliko katika Kilimo yametokea na uzalishaji umeongezekaje. Mkuu wa Mkoa na Mkuu wa Wilaya asiyeweza kuongoza mabadiliko hayo hawezi kutusaidia katika kazi hii. Tutawapima kwa vigezo vya mabadiliko katika Sekta za Maendeleo ya Wananchi. Tuanze kwa kuanzisha Mashindano ya Kilimo na kutoa tuzo kwa Mwananchi mmoja mmoja, Vijiji, Wilaya na hata Mikoa itakayoonyesha kwa vitendo mabadiliko ya tija kwenye Kilimo. Tuzo hizi zitatolewa wakati wa Sikukuu ya Nane Nane Kitaifa. Mashindano hayo lazima yaanze mwaka 2009.

  33. Mheshimiwa Spika, nimeongelea sana Kilimo. Lakini kwa Sekta ya Mifugo, Serikali imefanya jitihada za kuboresha Sekta hiyo. Pamoja na mambo mengine, Serikali imeendelea kutoa Chanjo, kujenga Majosho, Malambo na ununuzi wa dawa mbalimbali za Mifugo. Kwa mfano, Serikali imejenga na kukarabati jumla ya Malambo 158 kupitia Miradi ya PADEP na DADEPs. Aidha, Serikali imeendelea na jitihada zake za kuboresha Ranchi za Taifa kwa ajili ya uzalishaji bora. Hata hivyo, Serikali inakabiliwa na changamoto nyingi katika Sekta ikiwemo ukosefu wa ardhi ya malisho ya kutosha. Hali hii imeleta migogoro mikubwa kati ya Wakulima na Wafugaji ambayo imesababisha uvunjaji wa amani, utulivu, mshikamano na umwagaji wa damu. Ili kuondokana na tatizo hili, tunahitaji kutenga maeneo kwa ajili ya Kilimo na Ufugaji na kuyamilikisha. Ardhi ipimwe na ijulikane imetengwa kwa shughuli gani. Hii itatusaidia katika kupunguza migogoro inayoendelea kutokea kati ya Wakulima na Wafugaji. Mgogoro unaoendelea hivi sasa katika Wilaya ya Kilosa ni kutokana na kutokuwepo kwa mpango wa matumizi bora ya Ardhi. Kuanzia sasa, naziagiza Halmashauri za Wilaya kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika; na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi waanze na kukamilisha zoezi hili ili tupunguze migogoro ya Wakulima na Wafugaji. Vilevile, nawasihi Wananchi ambao ni Wakulima na Wafugaji kuvumiliana kuishi kwa amani na kila upande kutumia eneo lake, hivyo kuepusha migogoro, uvunjaji wa amani, umwagaji wa damu na vifo visivyokuwa vya lazima.

  34. Mheshimiwa Spika, Nchi yetu inahitaji kuisimamia vizuri rasilimali ya Uvuvi ili kuhakikisha kuwa Sekta ya Uvuvi inatoa mchango wake katika Kupunguza Umaskini kwa Wananchi wetu. Usimamizi mzuri wa Sheria za Uvunaji wa Maliasili za Bahari na Maziwa utasaidia kuongeza Pato la Taifa kutoka Sekta hii. Hivyo, Serikali inasisitiza kwamba Leseni za shughuli za Uvuvi ambazo nyingi hutolewa na Halmashauri za Wilaya zinapaswa kuwa na masharti yanayoonyesha zana, vifaa vya kila aina vya Uvuvi na mahali zana hizo zinapotumika kwa urahisi wa ufuatiliaji. Ningependa kuwakumbusha Wavuvi wote Nchini kuwa wazitumie Ofisi zetu zinazohusika na shughuli za Uvuvi, hasa Maafisa Uvuvi kuhakikisha kuwa wanapata ushauri na ufafanuzi kuhusu masuala yanayohusu Leseni za Uvuvi ili kupunguza matatizo yanayoweza kujitokeza.

  Nawasihi Wavuvi na Wadau wote wa Uvuvi Nchini kusoma kwa makini na kutekeleza yaliyomo kwenye Kauli ya Serikali kuhusu Waraka wa Uvuvi Kuzuia Zana za Uvuvi Haramu Nchini kama ulivyowasilishwa kwenye Mkutano wa Kumi na Mbili wa Bunge la Bajeti na Mheshimiwa Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi.

  Elimu

  35. Mheshimiwa Spika, wakati tunakaribia kufikia mwisho wa mwaka 2008, tunatarajia kwamba Vijana wetu waliofanya Mtihani wa Darasa la Saba watapata majibu yao wakati wowote. Jumla ya Wanafunzi 1,017,865 walifanya mtihani huo ambapo tunatarajia Wanafunzi 631,076, sawa na asilimia 62 watafaulu. Aidha, tunatarajia Wanafunzi takriban 504,860, sawa na asilimia 80 ya waliofaulu watachaguliwa kuingia Sekondari. Hata hivyo, taarifa za awali zinaonyesha kuwa idadi ya madarasa yanayohitajika ni takriban 12,622 kwa wastani wa Wanafunzi 40 kwa darasa. Wakati tunasubiri matokeo, ni lazima tujiweke tayari kupokea Wanafunzi wote watakaofaulu ili waweze kujiunga na Sekondari. Tunao uzoefu wa miaka takriban mitatu iliyotangulia katika kuhimizana kujenga madarasa na Shule za Sekondari za kutosha kuwapokea wote watakaofaulu. Tumefanya vizuri katika kipindi hicho tufanye vizuri katika kipindi kijacho. Kwa hiyo, napenda kutumia nafasi hii kuwakumbusha Wakuu wa Mikoa na Watendaji wote kuwa zoezi hili la kupanua elimu yetu na kuongeza idadi ya Wanafunzi wanaojiunga na Sekondari ni endelevu. Halihitaji kusukumwa na Viongozi wa Kitaifa. Ni wajibu wa Viongozi wa Mikoa na Wilaya kuhakikisha kuwa wanazo Shule na Madarasa zaidi yatakayotosheleza kupokea Wanafunzi wote watakaofaulu. Itakuwa aibu kwa Mkoa wowote ule utakaoshindwa kupeleka Wanafunzi wake wote watakaofaulu eti kwa vile hakuna madarasa.

  Nawaagiza Wakuu wa Mikoa na Wilaya zote kuhakikisha kuwa Wanafunzi wote watakaofaulu wanapata nafasi ya kujiunga na Kidato cha Kwanza mwakani. Tusisubiri kutoa visingizio na sababu za kushindwa. Jambo hili linawezekana, kila Kiongozi atimize wajibu wake.

  36. Mheshimiwa Spika, moja ya kipimo cha kupima ubora wa elimu yetu ni ufaulu wa Wanafunzi katika mitihani ya Kitaifa. Walimu, Wazazi na Wataalam wengine wa elimu wanapata faraja wanapoona matokeo ya elimu ya Wanafunzi ni mazuri. Kwa mfano, tunayo rekodi nzuri ya ufaulu wa Wanafunzi waliofanya Mtihani wa Kidato cha Nne kwa mwaka 2007 ambapo kati ya Watahiniwa 192,127 waliofanya Mtihani, waliofaulu Madaraja I – IV walikuwa 162,509, sawa na asilimia 86.2 ikilinganishwa na 116,647 sawa na asilimia 82.3 waliofaulu mwaka 2006 katika Madaraja hayo. Mategemeo ni kwamba matokeo yatakuwa mazuri zaidi kwa mwaka huu 2008. Hiyo ndiyo fahari yetu sote, kwani hutuwezesha kujipima kama Watoto wetu wanaweza kushindana katika soko la ajira au lile la elimu ya juu ndani na nje ya Nchi.

  37. Pamoja na kujivunia matokeo hayo mazuri, lakini sote tumesikia tukio la kuvuja kwa Mtihani wa Hisabati wa Kidato cha Nne mapema mwezi Oktoba 2008. Hatutarajii kwamba kufanya kwetu vizuri katika mitihani hii ni matokeo yanayotokana na ujanja wa kupata majibu ya mitihani kabla.

  38. Taarifa za kuvuja kwa mitihani ni jambo la aibu na ilipokelewa kwa mshituko mkubwa sio tu kwa Watahiniwa, bali pia kwa Wazazi na Wananchi wote kwa ujumla. Hali hii inatokana na ukweli kwamba kama Taifa tukijenga dhana ya uvujaji wa mitihani ni dhahiri inaathiri aina ya Wataalam watakaopatikana katika Nchi yetu kwa miaka ijayo. Tukijenga utamaduni huu wa uvujaji wa mitihani katika ngazi hii Wataalamu wetu hawataweza kushindana katika soko la ajira na katika Vyuo vya Elimu ya Juu. Vilevile, tunawajengea watoto wetu misingi mibovu ya maisha yao. Napenda kuwaasa Wazazi na Wananchi kwa ujumla kwamba tusishabikie wala kuruhusu utamaduni huu wa Wizi wa Mitihani. Ni aibu kubwa kwa Mzazi kushiriki kwa kumpa fedha Mtoto wake ili akanunue mitihani mitaani. Tusikubali kuwapotosha Watoto wetu, kwani kwa kufanya hivyo tunawatumbukiza katika shimo la kujiharibia maisha. Vilevile, Vyombo vya Habari vitusaidie kupiga vita mapungufu haya. Visiwe mashabiki, bali viwaongoze Vijana wetu kuwajengea tabia ya kutokimbilia mitihani inayonunuliwa mitaani. Tuwajengee Watoto mazingira na tabia ya kujifunza kwa bidii kuwa ndio mlango wa kufaulu na hivyo kupata Wanafunzi Bora ambao ndio watakuwa Wataalam bora wa Nchi hii kwa siku zijazo.

  39. Mheshimiwa Spika, pamoja na kuchunguza tukio hilo, Serikali itatumia matokeo ya Uchunguzi huo kuimarisha Baraza la Mitihani la Taifa ili tabia hii tuweze kuikomesha.

  Madeni na Madai ya Walimu

  40. Mheshimiwa Spika, katika Mkutano wa Kumi na Mbili wa Bunge, Serikali iliahidi kwamba ingelipa madeni mbalimbali ya Walimu. Hadi mwezi Septemba 2008, Serikali iliweza kulipa Malimbikizo ya Mishahara ya Walimu yenye jumla ya Shilingi Bilioni 7.4. Aidha, hadi tarehe 29 Oktoba 2008, malimbikizo ya Shilingi Bilioni 2.3 yalikuwa yamefikishwa Hazina tayari kwa kulipwa. Pamoja na Serikali kulipa madai hayo, na kuendelea na zoezi la uhakiki, bado Walimu kupitia Chama chao waliona madai yanachelewa kulipwa na hivyo kuamua kugoma. Wakati akihutubia Taifa, tarehe 31 Oktoba 2008, Mheshimiwa Rais alieleza kwa kirefu chanzo cha mgomo huo. Mheshimiwa Rais aliahidi na kuagiza Madai ya Walimu yote yahakikiwe na Walimu wenye stahili waanze kulipwa.

  41. Mheshimiwa Spika, kutokana na madai hayo, Serikali ilifanya uhakiki wa kina na hadi kufikia tarehe 4 Novemba 2008, Uhakiki wa madai ya Walimu ulikuwa umekamilika katika Halmashauri za Wilaya, Miji na Majiji 129 kati ya Halmashauri za Wilaya, Miji na Majiji 133 zilizopo. Halmashauri za Wilaya na Miji ambazo zilikuwa bado ni Ilala, Temeke, Kinondoni na Manispaa ya Dodoma. Uhakiki wa madai ya Walimu katika Halmashauri na Manispaa hizo nao utakamilika muda mfupi ujao.

  42. Napenda kutumia nafasi hii kuzielekeza Halmashauri zote kukamilisha zoezi hili na kutekeleza Maagizo ya Mheshimiwa Rais akiwa ziarani Mkoa wa Tabora kwa umakini. Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ikishirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI wahakikishe usimamizi wa karibu ili matatizo ya madai na madeni ya Walimu hayatokei tena. Vilevile, natoa Wito kwa Walimu wachache ambao walionekana kudanganya, kujenga utamaduni wa kuwasilisha madai ya kweli ya stahili zao. Kwa kufanya hivyo, itarahisisha uhakiki wa madeni haya na kupunguza kero ya kucheleweshwa kwa malipo kwa wenzao ambao wamekuwa wakidai malipo halali.

  Mikopo ya Wanafunzi

  43. Mheshimiwa Spika, tatizo la utoaji wa mikopo limekuwa likijitokeza Nchini katika miaka ya karibuni tangu utaratibu huu uanze. Utoaji wa mikopo unaongozwa na Sheria ya Bodi ya Mikopo Na. 9 ya mwaka 2004 pamoja na Kanuni na Miongozo iliyowekwa na Serikali. Sheria ya Mikopo pia inaweka bayana masharti ya kutoa mikopo. Hivyo, utaratibu wa kuwabaini wasio na uwezo na wale wenye uwezo unatokana na Sheria. Utaratibu wa kung’amua uwezo wa kiuchumi ndiyo njia pekee iliyopo kwa sasa ya kuwatambua Wanafunzi wenye uwezo kulingana na hali zao kiuchumi. Sera ya uchangiaji pia inalenga kutumia rasilimali kidogo za Serikali ili kuwawezesha Wanafunzi wengi zaidi kupata Elimu ya Juu.

  44. Mheshimiwa Spika, kwa utaratibu wa kawaida, gharama za Elimu zinatakiwa kuchangiwa kati ya Wazazi na Serikali. Kwa mfano, Nchini Kenya wastani wa Wanafunzi 120,000 wameandikishwa (kudahiliwa) kwenye Vyuo Vikuu Nchini humo, lakini wanaopata mkopo ni 10,000 tu. Kwa upande wa Uganda, kati ya wastani wa Wanafunzi 30,000 wanaodahiliwa kwa mwaka ni 4,000 tu ndio wanaopata mkopo kutoka Serikalini. Kwa upande wa Tanzania, Wanafunzi 60,000 wanapata mikopo kati ya Wanafunzi 80,000 waliodahiliwa katika vyuo mbalimbali vinavyotoa Elimu ya Juu katika mwaka wa fedha wa 2008/2009. Kazi hii iliyofanyika ukilinganisha na wenzetu wa Kenya na Uganda ni kubwa na inastahili pongezi kwa Serikali. Lazima tujipongeze kwa kazi nzuri ambayo imefanyika kusomesha Watoto wetu.

  45. Mheshimiwa Spika, Sera ya Uchangiaji inalenga kutumia rasilimali na fedha kidogo za Serikali ili kuwawezesha Wanafunzi wengi zaidi kupata Elimu ya Juu. Kwa hiyo, sio busara Serikali kuwalipia asilimia 100 hata wale Wanafunzi wanaotoka kwenye familia zenye uwezo. Kwa kufanya hivyo, kwa Bajeti ya mwaka 2008/2009 ya Shilingi Bilioni 119, ni Wanafunzi 42,000 tu ndio wangeweza kukopeshwa badala ya 60,000 wanaopata sasa hivi. Kwa maneno mengine, kuwapatia Wanafunzi wote 60,000 mkopo wa asilimia 100, kiasi cha Shilingi Bilioni 163.7 zingehitajika. Kwa upande mwingine, utaratibu huu umewasaidia sana Wazazi wasio na uwezo. Mimi najiuliza, ni kwa nini Mtoto wa Waziri Mkuu au Spika au Mbunge au wa Mfanyabiashara Maarufu ambao wanao uwezo wa kusomesha Watoto wao katika Vyuo Vikuu wafaidike na utaratibu huu ambao tuna uwezo nao badala ya kusaidia wasio na uwezo?

  46. Mheshimiwa Spika, tuelewe kwamba, Sera ya Uchangiaji Gharama za Elimu ya Juu si jambo geni kwa Nchi nyingi Duniani. Hapa kwetu, utaratibu huu hauko katika Elimu ya Juu pekee, bali uko katika Elimu ya Sekondari, Vyuo na pia katika huduma nyingine za jamii kama vile Afya, Maji na Nishati. Mchango wa Serikali katika Elimu ya Juu ni mkubwa ukilinganisha na mkopo wa Mwanafunzi kwa ajili ya Elimu ya Juu. Kwa ujumla gharama wanazolipa Wanafunzi wa Vyuo vya Elimu ya Juu ni za chini sana ukilinganisha na gharama halisi.

  47. Gharama halisi ya Kozi ya Udaktari wa Binadamu kwa mfano kwa Chuo Kikuu cha Muhimbili ni Shilingi Milioni 4.3, lakini Mwanafunzi hulipa Shilingi Milioni 1.0 tu kwa mwaka kupitia kwenye mkopo anaopewa (kwa wasio na uwezo).

  48. Ada halisi kwa Kozi ya Udaktari wa Wanyama, Chuo Kikuu cha Sokoine ni Shilingi Milioni 3.2 kwa mwaka, lakini Mwanafunzi hulipa Shilingi Milioni 1.2 tu. Kwa upande wa Shahada ya Biashara, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, gharama halisi ni Shilingi Milioni 3, lakini Mwanafunzi hulipa Shilingi Milioni 1.25 tu.

  49. Pamoja na kutolipa ada halisi, mikopo wanayolipa Wanafunzi kwa kipindi cha miaka 10 huwa haina riba. Hii ina maana kuwa thamani ya fedha wanazolipa Wanafunzi ni kidogo sana ukilinganisha na thamani ya fedha wakati walipokopa. Kwa hali ya kawaida, hii mikopo ilitakiwa ilipiwe riba kwa Wanafunzi, lakini kwa sasa Serikali inabeba mzigo huo. Hatuna uchaguzi mwingine, bali kuendelea kuchangia gharama za elimu ili Wanafunzi wengi zaidi wapate Elimu ya Juu. Napenda nirudie kusema kwamba Serikali wakati wote itakuwa mstari wa mbele kuhakikisha Wanafunzi wanapata kile wanachostahili kujiendeleza kielimu. Naomba mtamke kuwa Wanafunzi wale wanaotaka Wanafunzi wote kupewa mikopo asilimia 100 haiwezekani. Mheshimiwa Spika haiwezekani Serikali kuwalipia Watoto wa Waziri Mkuu, Spika, Wabunge na Wafanyabiashara wakubwa.

  Migomo na Maandamano Nchini

  50. Mheshimiwa Spika, katika siku za hivi karibuni, Nchi yetu pia imeshuhudia matukio kadhaa ya Migomo na Maandamano yanayofanywa na Vikundi mbalimbali kwa kile kinachoelezwa kuwa ni njia mojawapo ya Vikundi hivyo kudai haki zao. Matukio ya aina hiyo ni pamoja na Migomo na Maandamano ya Wanafunzi wa Vyuo Vikuu, Migomo ya Wafanyakazi wa Kampuni ya Reli Tanzania, Migomo ya Madaktari na Wauguzi katika Hospitali ya Rufaa ya Muhimbili, Migomo ya Wafanyakazi wa NMB, Maandamano na tishio la Mgomo wa Walimu, Maandamano ya waliokuwa Wafanyakazi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, na Migomo midogo midogo katika maeneo mbalimbali ya Sekta Binafsi.

  51. Mheshimiwa Spika, kimsingi, Serikali haipingi kufanyika kwa Migomo na Maandamano ambayo yanafuata Kanuni na Taratibu zilizowekwa Kisheria. Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini Na. 6 ya Mwaka 2004 inatoa Uhuru wa Wafanyakazi kugoma ila tu wafuate Taratibu na Kanuni. Hata kwa upande wa Maandamano, yanaruhusiwa ila tu kwamba yanapaswa kupata Kibali cha Polisi.

  52. Hata hivyo, kwa baadhi ya matukio ya hivi karibuni ambayo tumeyashuhudia, zipo dalili zinazoashiria kuwa baadhi ya Vikundi vinavyohusika na kuandaa Maandamano na Migomo vimefanya hivyo bila ya kufuata Sheria. Aidha, baadhi ya Maandamano na Migomo hiyo imetishia Usalama, Amani, Utulivu na Mshikamano wa Nchi yetu na hivyo kulazimisha Vyombo vya Dola kuingilia kati.

  53. Mheshimiwa Spika, ikumbukwe kuwa Maandamano na Migomo yote ya Wafanyakazi inayotokea sehemu za kazi hasa zile zinazohusika na utoaji wa huduma muhimu kwa jamii, inaleta athari kubwa kwa Taasisi husika na Uchumi wa Nchi kwa ujumla. Kwa mfano, Mgomo uliofanywa na Wafanyakazi wa Kampuni ya Reli Tanzania ulisababisha Wananchi wengi kupata usumbufu na kuchelewa kufika wanakokwenda na wengine kukatiza safari zao. Vilevile, shehena za mizigo zilikwama na hivyo kuwasababishia Wafanyabiashara hasara kubwa na zaidi ya yote, kudumaza shughuli za kiuchumi zinazotegemea Sekta ya Mawasiliano na Uchukuzi Nchini.

  54. Vilevile, Mgomo wa Madaktari Wanafunzi wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ulisababisha Wagonjwa wengi wasio na hatia kukosa huduma muhimu za tiba. Maandamano yaliyofanywa na Wastaafu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambao tarehe 28 Oktoba 2008 walifunga barabara za Ali Hassan Mwinyi na ile ya Umoja wa Mataifa, Jijini Dar es Salaam, ni dhahiri yalisababisha kero kubwa kwa Wananchi wengi ambao kwa njia moja au nyingine hawahusiki na wala sio Wadau kwa madai ya Wastaafu hao.

  55. Mheshimiwa Spika, ni muhimu kujiuliza kama ni busara Makundi ya Wafanyakazi wa Taasisi mbalimbali Nchini kutumia Migomo katika kutetea maslahi yao, bila wahusika kutoa muda wa kutosha wa majadiliano wala kujali maslahi ya Umma na Wananchi wanaowahudumia. Ukweli ni kwamba, hasara na athari kubwa za Migomo pamoja na usumbufu, kero na mateso wanayopata Wananchi na Taifa kwa ujumla na kuzorota kwa utekelezaji wa Mipango ya Maendeleo kutokana na Migomo hiyo, haziwezi kulinganishwa na madai ya makundi ya Wafanyakazi wachache wanaoongoza Migomo hiyo.

  56. Mheshimiwa Spika, napenda kusisitiza kwamba Wafanyakazi, Wanafunzi na Wananchi wengine wowote wanaoitisha na kufanya Migomo ni vyema watambue kuwa pamoja na Serikali kuruhusu Migomo katika mazingira fulani Kisheria, ni lazima maslahi ya Umma yazingatiwe na kulindwa kwanza. Serikali inatoa wito kwa Makundi yote Nchini kuacha kutumia Migomo kama njia pekee ya kupata haki, kwani Migomo ina athari nyingi kama nilivyokwishaeleza. Kwa misingi hiyo, Serikali haitawavumilia Wahusika wanaochochea Migomo isiyo ya lazima na isiyofuata Sheria, Taratibu na Kanuni kwani ina athari kubwa kiuchumi na inahatarisha Amani, Utulivu na Usalama wa Nchi yetu. Vyama vya Wafanyakazi vilivyopewa dhamana ya kisheria kutetea haki za Wafanyakazi pamoja na kudumisha mahusiano mazuri kazini, vina wajibu mkubwa wa kuepusha Migomo isiyo ya lazima. Ni vyema Vyama hivyo vifanye kazi zake kwa kufuata Taratibu zinazokubalika Kisheria.

  57. Vivyo hivyo, Serikali haitavumilia Watendaji wake wote wanaosababisha au kushindwa kutatua kero za Wananchi hadi Wananchi wafikie hatua ya kufikiria migomo wakati uwezo wa kutatua kero zao wanao. Jukumu la Serikali iliyoko madarakani ni kuzipatia ufumbuzi kero mbalimbali za Wananchi kulingana na uwezo uliopo.

  58. Napenda nitumie fursa hii kusisitiza Maelekezo ya Mheshimiwa Rais kwa kuwaomba Wananchi wote kujenga dhana na utamaduni wa uvumilivu. Tujenge utamaduni uliokomaa Kidemokrasia. Mimi ninaamini kwamba migogoro yote ina njia inayofaa katika kuitatua. Tuzungumze. Tukubaliane. Kwa njia hiyo tunaweza kuepusha athari ambazo zingeweza kuepukika. Hebu tukae kwa pamoja tufikirie tena jinsi ya kupunguza matatizo haya.

  Matatizo ya Watu Wenye Ulemavu

  59. Mheshimiwa Spika, niruhusu nizungumzie kidogo kuhusu matatizo ya Walemavu Nchini. Inakadiriwa kwamba Nchi yetu ina Watu wenye Ulemavu wapatao Milioni 3.5. Hawa wanajumuisha Walemavu wa Viungo, Wasioona, Viziwi, Ulemavu wa Akili, Ulemavu mchanganyiko na Ulemavu mwingine. Serikali inatambua umuhimu wa Watu wenye Ulemavu katika maendeleo ya Nchi yetu. Hata hivyo, ipo dhana iliyojengeka miongoni mwetu kwamba Watu wenye Ulemavu hawawezi kazi wala shughuli yoyote. Dhana hii si sahihi hata kidogo na ni dhana potofu. Dhana hii potofu inapingana na mambo makubwa ambayo Walemavu wanaweza kufanya kuchangia maendeleo ya Taifa. Kwa mfano, sote tuliona jinsi Watu wenye Ulemavu walivyoleta msisimko kwenye michezo ya Olimpiki iliyomalizika kule Nchini China hivi karibuni.

  60. Kila Mwananchi ana haki sawa Kisheria ya kushiriki kikamilifu katika mambo muhimu yanayomhusu yeye Mwenyewe na Jamii nzima kwa ujumla. Watu wenye Ulemavu wana haki ya kupata mahitaji ya msingi sambamba na Wananchi wengine wasio na ulemavu. Kimsingi, hawa ni Wenzetu katika jamii ambao kwa maumbile yao wanahitaji maangalizi ya pekee katika jamii. Kwa maana hiyo, ni wajibu wa Serikali kuhakikisha mahitaji yao yanapatikana.

  61. Mheshimiwa Spika, Takwimu zinaonyesha kwamba, hadi sasa, Serikali ina Vituo vya Watu wenye Ulemavu wa aina mbalimbali vinavyotoa Elimu na Mafunzo ya Ufundi kama ifuatavyo:
  Moja: Shule za Msingi Maalum kwa Wasioona tatu (3); Ulemavu wa Akili tano (5); Ukiziwi kumi (10); na Ulemavu wa Viungo tano (5);

  Pili: Shule za Sekondari kwa Wasioona kumi na tano (15); Ulemavu wa Akili mbili (2); Ulemavu wa Viungo tatu (3); na Ukiziwi nane (8);

  Tatu: Vyuo vya Ufundi kwa Wasioona kimoja (1); na Ulemavu mchanganyiko sita (6).

  Serikali inavihudumia Vituo hivi takriban 58 kwa kuandaa Walimu wa Elimu Maalum; Kutoa vifaa vya kufundishia; Kutoa nyenzo za kujimudu; Kuboresha miundombinu katika mazingira ya shule; na kutoa chakula, malazi na huduma za msingi.

  62. Mheshimiwa Spika, napenda nitumie nafasi hii kuihakikishia jamii ya Watu wenye Ulemavu na Wananchi wote kwa ujumla kwamba Serikali inawajali na inatambua matatizo yao. Aidha, Serikali imeandaa Mikakati ya kukabili matatizo hayo ya Watu wenye Ulemavu Nchini. Kubwa katika hili ni Kuandaa Mapendekezo ya Marekebisho ya Sheria Na. 2 ya Mwaka 1982 ili kutoa nafasi ya kuboresha zaidi huduma kwa Watu wenye Ulemavu katika nyanja za Ajira, Miundombinu, Elimu na Upatikanaji wa Vifaa kwa urahisi.

  63. Kupitia Bunge hili naomba kuziagiza Wizara zinazohusika na huduma za Walemavu ikiwemo Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii; Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi; Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma; na Wizara ya Fedha na Uchumi kushirikiana kukamilisha Miongozo yote inayohusu Watu wenye Ulemavu Nchini. Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii iratibu zoezi hili na nipate Taarifa ya Utekelezaji kabla ya Mkutano wa Kumi na Nne wa Bunge.

  Utunzaji wa Mazingira

  64. Mheshimiwa Spika, Uhai na Ustawi wa Nchi yetu unategemea kwa kiasi kikubwa Hifadhi na Utunzaji wa Mazingira. Ukizunguka sehemu mbalimbali za Tanzania utakuta sehemu mbalimbali zimechomwa moto na unaweza kudhani yapo mashindano maalum ya uchomaji moto nchini. Kumekuwa na utamaduni miongoni mwa Watanzania Wakulima na Wafugaji wa kuchoma moto maeneo mbalimbali Vijijini. Wakulima huchoma moto nyasi kwa ajili ya kurahisisha utayarishaji wa mashamba wakati Wafugaji huchoma moto ili kuwezesha majani mabichi kuchipua kwa ajili ya Mifugo yao. Vilevile, kuna sehemu za Nchi ambapo wana imani kuwa anayechoma moto na kuwaka kwa muda mrefu ana mkono mzuri. Utamuduni huu umepitwa na wakati. Kuchoma moto hovyo kunaharibu mimea ambayo mingine huwa ni mazao ya chakula na hivyo kuleta ukame na njaa. Matokeo ya ukame na njaa ni kuongezeka kwa umaskini. Uchomaji wa moto hovyo huua viumbe hai wanaoishi kwenye majani na ardhini. Wataalam wanatueleza kuwa viumbe hivyo ni muhimu kwa kurutubisha ardhi.

  65. Mheshimiwa Spika, kuna uharibifu wa Mazingira unaoendelea kufanywa kwenye vyanzo vya maji. Miti inakatwa hovyo na vyanzo hivyo vimekuwa malisho maarufu ya idadi kubwa ya mifugo. Matokeo ya kufanywa hivyo ni kukauka kwa vyanzo hivyo vya maji. Lakini tujiulize itakuwaje binadamu, wanyama na mimea vitapokosa maji? Ni wazi kuwa maji ni uhai na bila maji hakuna uhai.

  66. Tumeharibu sana mazingira, hali hii imesababisha maeneo mengi kukosa mvua na kuwa na upungufu wa uzalishaji wa mazao. Ni muhimu Wananchi wakazidi kufahamishwa madhara yatokanayo na kuchoma moto hovyo na kuharibu vyanzo vya maji. Halmashauri ziwe na Sheria zinazodhibiti uchomaji moto hovyo, uharibifu wa vyanzo vya maji na mazingira kwa ujumla wake. Sheria hizo zisimamiwe na kutekelezwa kwa kushirikisha Viongozi wa Vijiji, Kata na Wilaya. Pia, ni wakati sasa wa kuelekeza rasilimali za kutosha katika kulinda uhai wa viumbe hai vyote ikiwa ni pamoja na sisi Wanadamu. Tupande miti mara kwa mara kwenye vyanzo vya maji, mashamba yetu, nyumba zetu, kando kando ya barabara, n.k. Pamoja na Siku ya Kupanda Miti Kitaifa, ni vizuri kila Mkoa ukawa na siku maalum ya kupanda miti inayoendana na hali yake ya Hewa. Badala ya kuwa na mashindano ya kuharibu mazingira tuwe na mashindano ya kulinda mazingira katika ngazi ya Kijiji, Kata, Wilaya, Mkoa na Taifa. Natumaini kila mmoja wetu atajisikia vizuri kuzungukwa na uoto wa asili na ikiwa upatikanaji wa maji halitakuwa tatizo kwenye jamii. Hilo liwe ndilo lengo letu kuu.

  Hitimisho

  67. Mheshimiwa Spika, wakati tunatekeleza malengo ya Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini Tanzania (MKUKUTA), tuelekeze nguvu zetu kutumia fursa zilizopo kutekeleza Mkakati huu. Twendeni tukawahimize Wananchi kushiriki katika Maendeleo yao. Mambo ya Msingi ambayo napenda kuyasisitiza ni haya yafuatayo:
  Moja: Tunayo nafasi nzuri ya kutumia rasilimali zilizopo hususan Madini kuinua uchumi wetu. Tutumie nafasi iliyopo kwa kuyaongezea thamani Madini yetu badala ya kuyauza ghafi. Tuanze kwa kushirikiana na Sekta Binafsi. Kwa kufanya hivyo tutafanikiwa;

  Pili: Tunatoka Bungeni wakati Msimu wa Kilimo umekaribia. Twendeni tukasukume Mapinduzi ya Kilimo. Wakuu wa Mikoa, Wilaya, Wakurugenzi wa Wilaya, Madiwani tusukume hili ili iwe dhambi kutozingatia Kanuni Bora za Kilimo. Tuanze kufuatilia kwa karibu upatikanaji wa Pembejeo muhimu kwa Kilimo ikiwemo Mbolea, Mbegu Bora, na Madawa ya Kuuwa Wadudu waharibifu, ili kuongeza tija.

  Tatu: Tujenge dhana ya uvumilivu. Tuepuke kujenga tabia ya kuona kwamba Maandamano na Migomo ndiyo njia ya kutatua migogoro. Bado Serikali yetu ni nzuri, inajitahidi kukamilisha mahitaji yote ya Walimu, Wastaafu mbalimbali na matatizo ya Wanafunzi. Kubwa tuwe na Subira na tushirikiane.

  Nne: Tushirikiane kuwasaidia Watu wenye Ulemavu, kwani ni sehemu ya jamii yetu. Tuwape moyo, tuwasaidie pale inapobidi ili waweze kushiriki katika kujiletea maendeleo yao.

  68. Mheshimiwa Spika, leo hii tunahitimisha Mkutano wa Kumi na Tatu wa Bunge. Tumebakiza Mikutano takriban Saba (7) kabla ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2010. Sisi sote, kila mmoja wetu ndani ya Bunge hili bila kujali Itikadi ya Chama chake ni lazima ujiulize, kuwepo kwetu ndani ya Bunge hili tumewasaidiaje Wananchi wetu tunaowawakilisha. Ni vema kila mmoja wetu kuanza kujifanyia tathmini mwenyewe ya kitu gani alichokifanya cha kuwaondolea Wananchi Umaskini.

  Je, umeshiriki vipi katika kuwaondolea Wananchi kero ambazo zinawakabili. Kila mmoja ajipime mwenyewe kujua kama kuwepo kwake ndani ya Bunge hili ametumia muda wake katika kupunguza Kero za Wananchi au ndio amewazidishia ukali wa Maisha. Twendeni nyumbani tukatumie muda wetu kutafakari yote yale ambayo yanatuhusu tuyafanye kwa Manufaa ya Wananchi wetu.

  69. Mheshimiwa Spika, nimalizie kwa kuwashukuru wote waliosaidia katika kufanikisha Mkutano huu. Nakushukuru kwa namna ya pekee wewe Mheshimiwa Spika, na Naibu Spika kwa kutuongoza vizuri. Nawashukuru Wenyeviti wa Bunge kwa msaada mkubwa walioutoa kuliongoza Bunge hili.

  Nawashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa michango yenu mbalimbali wakati wa kujadili Miswada tuliyoipitisha katika Mkutano huu. Namshukuru Kaimu Katibu wa Bunge, Dkt. Thomas Kashilillah na Wasaidizi wake pamoja na Wataalam wa Serikali kwa kazi nzuri ya kutoa misaada ya Kitaalam na huduma mbalimbali katika kufanikisha Mkutano huu. Navipongeza Vyombo vya Habari kwa kuwafikishia Wananchi habari ya yale yaliyojitokeza hapa Bungeni kwa Wakati na Usahihi. Mwisho, nawapongeza madereva wote kwa kuwaendesha Viongozi na Wataalam wote kwa umakini mkubwa na hivyo kuwaepusha na ajali. Wote Asanteni Sana!

  70. Mheshimiwa Spika, leo ni tarehe 7 Novemba 2008. Katika kipindi cha takriban mwezi mmoja na nusu tutakuwa tumefikia mwisho wa mwaka 2008. Ni matumaini yangu kwamba Inshallah Muumba Wetu atatujalia sote kama tulivyo kumaliza mwaka huu na kuuanza mwaka mwingine salama. Napenda nitumie nafasi hii kuwatakieni wote Heri, Baraka na Fanaka tele za Sikukuu ya Krismas na Mwaka Mpya wa 2009!

  71. Nawatakia wote safari njema ya kurejea kwenye Majimbo yenu na nyumbani kwenu.

  72. Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo haya mafupi, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu sasa liahirishwe hadi tarehe 27 Januari 2009, siku ya Jumanne Saa 3:00 Asubuhi, litakapokutana tena kwa ajili ya Mkutano wa 14 kwenye Ukumbi huu hapa Dodoma.

  73. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.
   
 4. kamonga

  kamonga Senior Member

  #4
  Nov 7, 2008
  Joined: Feb 13, 2008
  Messages: 170
  Likes Received: 1
  Trophy Points: 35
  Blah blah blah ............and the beat goes on.......
  cha muhimu ni ni fanaka za siku kuu na heri ya mwaka mpya.
  Tanzania needs Blessings .......heavy ones
   
 5. Lunyungu

  Lunyungu JF-Expert Member

  #5
  Nov 8, 2008
  Joined: Aug 7, 2006
  Messages: 8,836
  Likes Received: 75
  Trophy Points: 145
  Nilisema JK kakimbia na hotuba hakuna kazi zaidi na Bunge linaenda nyumbani mkanishambulia je sasa ukweli bado mnauita uzushi nyie akina Kashehe kwamba badala ya siku 21 sasa imekuwa siku 14?
   
 6. SaidSabke

  SaidSabke JF-Expert Member

  #6
  Nov 8, 2008
  Joined: Sep 28, 2006
  Messages: 1,969
  Likes Received: 223
  Trophy Points: 160
  I suspect that u are confused kila la kheri
   
 7. P

  Pakacha JF-Expert Member

  #7
  Nov 8, 2008
  Joined: Apr 15, 2008
  Messages: 816
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 33
  Bunge hili ni la Tanganyika au Jamhuri ya Muungano wa Tanzania? Umesikia humo hata kutajwa wale wa upande wa pili. Katiba hiyo!. Sasa isiwe kwa OIC tu?
   
 8. kamonga

  kamonga Senior Member

  #8
  Nov 11, 2008
  Joined: Feb 13, 2008
  Messages: 170
  Likes Received: 1
  Trophy Points: 35
  Thanks for noticing, ....birds of the same feather...........
   
 9. J

  JokaKuu Platinum Member

  #9
  Nov 11, 2008
  Joined: Jul 31, 2006
  Messages: 12,805
  Likes Received: 5,098
  Trophy Points: 280
  ..Kenya wana population ndogo kuliko Tanzania, lakini wanapeleka wanafunzi wengi zaidi ktk vyuo vikuu.

  ..kulingana na PM Pinda, Wakenya wana uwezo kuliko Watanzania ktk kuchangia wenyewe elimu ya Chuo Kikuu.

  ..sidhani kama Watanzania tunapaswa kuzifurahia hizo data za Waziri Mkuu hata kidogo. nadhani zina ishara mbaya kwamba:elimu yetu ina matatizo na Watanzania wengi hawa-qualify kwenda chuo kikuu, vilevile Watanzania tuna hali mbaya ya kiuchumi kuweza kuchangia elimu ya chuo kikuu.
   
Loading...