Roving Journalist

JF Roving Journalist
Apr 18, 2017
2,746
11,877
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kulihutubia Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.



UPDATES:
Rais Samia ameshaingia ndani ya jengo la bunge na sasa Spika wa Bunge Job Ndugai anafuata taratibu za kiitifaki kabla ya Rais kutoa hotuba yake.

HOTUBA YA RAIS SAMIA
"Nawasalimu kwa jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,"

SSH2.jpg
SHUKRANI
"Mheshimiwa Spika mbali ya kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema na rehema zake, imekuwa ni miaka takribani sita imepita tangu niondoke kwenye jengo hili adhimu la bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hivyo leo ninayo furaha ya kurudi tena na kupata fursa ya kulihutubia bunge ambalo limenilea limenijenga, limeninoa na ni bunge hili lililofanya uwezo wangu uonekane na wote mpaka kushika nafasi hii niliyonayo."

“Nawashukuru sana Marais Wastaafu, uwezo wangu wa Uongozi uliibuliwa na Rais Karume aliyenipa nafasi ya Uwaziri, malezi haya yaliendelezwa na Dr.Kikwete aliyenipa Uwaziri na baadaye Makamu Mwenyekiti wa Bunge la Katiba, nimshukuru pia Hayati Magufuli kwa kuniamini."

"Kuniamini kwa Hayati Magufuli kuwa Mgombea Mwenza wake kumeniwezesha leo hii kuwa Mwanamke wa Kwanza Tanzania kushika nafasi ya Umakamu wa Rais na hatimaye sasa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania”

“Nimekuja kulihutubia Bunge baada ya Nchi yetu kupita kwenye kipindi kigumu, kama inavyokumbukwa March 17 Taifa letu lilipata msiba mkubwa wa kuondokewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Hayati Magufuli,hivyo tusimame kumuombea Mpendwa wetu”

“Mapenzi ya Watanzania kwa Hayati Magufuli yalidhihirika katika kipindi cha maombolezo ambapo wengi walijitokeza kumuaga, namshukuru Mungu kwa kutupitisha salama kwenye kipindi cha mabadiliko ya Uongozi, dhamana hii ni kubwa na yenye mitihani mingi”

Ni ukweli kwamba Hayati Dkt. Magufuli alikuwa kiongozi jasiri na shupavu mwenye maono ambaye aliipenda Nchi yetu. Natumia fursa hii kutoa pole tena kwa Mama wa Rais, Mama mjane Janeth, Watoto na familia. Pia, natoa pole kwa Bunge hili na kwa Watanzania wote.

Nakishukuru Chama changu cha CCM kwa kunijengea uwezo mkubwa na wakati wote kimeniamini kwani wasingeniamini nisingekuwa mbele yenu. Nawashukuru Viongozi mbalimbali wa Chama na Serikali na nawashukuru kwa dhati Marais wastaafu wote na Viongozi wakuu wa Kitaifa.

Niseme wazi, kwa uwezo wangu wa uongozi uliibuliwa na Amani Karume aliyenipa nafasi ya Uwaziri katika kipindi changu nikiwa Mjumbe wa Baraza la Mawaziri Zanzibar Malezi yaliendelezwa na Jakaya Kikwete aliyenipa Uwaziri na baadaye kuwa Makamu M/Kiti wa Bunge la Katiba.

Nalishukuru Bunge kwa ushirikiano mkubwa ambao limenipa tangu nilipochukua dhamana ya kuongoza Nchi yetu. Nalishukuru kwa kupitisha adhimio la kunipongeza na kuahidi ushirikiano. Pia, kupitisha pendekezo langu la kumpitisha Dkt. Mpango kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Rais samia pia Kamshukuru Rais wa Zanzibar, Vyombo vya Ulinzi na usalama pamoja na Wageni wote waalikwa, Vyombo vya habari na Watanzania wote kwa kumuamini na kumuunga mkono. Aidha, baada ya shukrani Rais Samia amesema yafuatayo:

DIRA NA MUELEKEO WA SERIKALI YA AWAMU YA SITA
Dira na mwelekeo wa Serikali ya Awamu ya 6 utakuwa ni kudumisha yale ya Serikali zilizopita. Tutaendeleza mema na kuibua yaliyo mapya. Jambo la kwanza ambalo tutalipa kipaumbele ni kuendelea kulinda na kudumisha Tunu za Taifa letu. Amani, Umoja na Mshikamano.

Amani na Umoja ni Msingi Mkuu ndani ya Taifa lolote. Hivyo nawasihi Watanzania kila mmoja tushirikiane kuzilinda na kuzitunza Tunu hizi. Tanzania ni yetu sote. Kila mmoja wetu anao wajibu wa kuhakikisha anazilinda na kuzitunza Tunu hizi.

“Niliwahi kusema na leo narudia tena kwamba Mimi na Hayati Magufuli ni kitu kimoja, kwahiyo mengi ambayo nimepanga kuyatekeleza ni yale ambayo yalielezwa na Hayati Magufuli wakati akilizindua Bunge hili”.

Pia, tunakusudia kuelekeza nguvu kubwa katika ukuzaji wa Uchumi. Taifa letu limepata mafanikio makubwa kiuchumi hususan miaka 5 iliyopita. Takwimu zinaonyesha kwa Tanzania Uchumi wetu tumeusimamia kwa wastani wa 6.9% na kudhibiti Mfumuko wa Bei kwa 4.4%. Na kupuza umasikini kwa kiwango cha asilimia 26.6%.

Muhimu zaidi Mwaka jana mwezi julai Taifa letu lilifanikiwa kuingia Uchumi wa Kati ambapo Pato la Wastani wa kila Mtanzania limeongezeka hadi kufikia dola 1080 zaidi ya kigezo cha dola 1036 cha kuingia kwenye kundi hilo. Hayo bila shaka ni mafanikio makubwa. Jitihada zaidi zinahitajika ili kuongeza kasi ya ukuaji Uchumi na kupambana na umasikini nchini. Hii ni kwa sababu licha ya mafanikio tuliyoyapata kasi ya ukuaji wa uchumi bado ni ndogo.

UKUAJI WA UCHUMI NA UWEKEZAJI
Wataalamu wa Uchumi wanatueleza kwamba ili kuweza kupambana na umasikini uchumi wetu unatakiwa ukue kwa angalau asilimia 8 kwa mwaka. lakini kutokana na Dunia kukumbwa na janga la Corona, kiuhalisia takwimu zinaonesha kwa chumi nyingi duniani zimeshuka. Tanzania nayo imeathirika kutoka wastani wa ukuaji wa uchumi wa 6.9% hadi 4.7%.

Hii inamaanisha kwamba katika miaka mitano ijayo tunahitajika uwekezaji mkubwa sana katika sekta za uzalishaji na zinazotoa ajira kwa wingi. Hatua mahsusi tutakazozichukua katika kukuza uwekezaji ni pamoja na kufanya marekebisho kadhaa katika sera, sheria na kanuni zetu na kuondoa vifungu vitakavyosababisha vikwazo katika kukuza uwekezaji.

“Tutarudisha imani ya Wawekezaji na kutoa vivutio kwa Wawekezaji, tunalalamikiwa sana, kumekuwa na mchakato mrefu Watu wanapotaka kuwekeza Tanzania, Serikali ya Awamu ya Sita tunakwenda kukomesha hili na Uwekezaji utakwenda kwa haraka”.

Kuna ucheleweshwaji wa vibali kwa Wafanyabiashara wa Kigeni, kuna usemi unasema ukiona Mtu Mzima analia ujue kuna jambo, tutashughulikia hili huku tukilinda maslahi ya Taifa. Tutachukua hatua madhubuti kuboresha mazingira ya biashara, kutoa vivutio kwa Wawekezaji.

ULIPAJI WA KODI
“Tutaweka mifumo rafiki ulipaji kodi , ningependa kuona Wafanyabiashara wanalipa kodi bila matumizi ya nguvu wakitambua kwamba kodi ni maendeleo yao, kumekuwa na matumizi ya nguvu wakati wa ukusanyaji kodi hili tutalikomesha”.

''Watanzania wachache ndio wanaolipa kodi, hivyo kuna haja ya kutanua wigo wa walipa kodi, ningependa kuona wafanyabiashara, wawekezaji na wananchi wanalipa kodi bila shuruti na bila matumizi ya nguvu wakitambua kwamba kodi ni maendeleo yao''

“Mashirika mengi ya Umma yanaendeshwa kwa kusuasua, ikifika wakati wa kutoa gawio Serikalini Viongozi wa Mashirika hayo wanahangaika kutafuta gawio wakihofia nafasi zao, tutaboresha Mashirika ya Umma ili yawe na tija na kuzalisha faida”.

KUHUSU KILIMO NA UFUGAJI
Tunakusudia kuongeza maeneo ya Ufugaji, lengo likiwa ni kuepusha Wafugaji kuhama hali inayopelekea uharibifu wa mazingira na migogoro ya ardhi Tunatarajia kununua meli 8 za uvuvi ili zishiriki ktk Uvuvi wa Bahari Kuu, nne zitafanya kazi Zanzibar na nne Tanzania Bara.

Tunalenga kuachana na uchungaji wa kuhama hama kwani hauna tija. Katika ufugaji huu Ng'ombe hanenepi wala Mchungaji hanenepi - Katika miaka hii mitano tutawekeza katika kutoa Elimu ya Ufugaji wa kisasa na kuongeza uzalishaji wa vyakula vya mifugo viwandani.

Sekta ya Kilimo kwa sasa inachangia asilimia 100 ya chakula kinacholiwa nchini, asilimia 60 ya malighafi za Viwandani, asilimia 27 ya Pato la Taifa na asimilia 25 ya Fedha za Kigeni. Hata hivyo bado Sekta hii inakabiliwa na changamoto nyingi.

''Katika miaka mitano tunayokwenda nayo tutaendelea kuongeza nguvu kuhakikisha kilimo kinakuwa na tija, ikiwemo kuwa na mbegu bora, kuboresha afya ya udongo, pamoja na kuziwezesha taasisi za kilimo kwa kuzipa fedha ili ziweze kuzalisha kwa tija''.

Ili kukuza zaidi Sekta ya Kilimo hatuna budi kufungamanisha Sekta ya Kilimo na Sekta ya Viwanda. Viwanda vinawahakikishia wakulima soko la mazao yao - Tutaendeleza jitihada za kuhamasisha ujenzi wa Viwanda hususani vinavyotumia malighafi za hapa Nchini.

Tunafahamu Nchi yetu imebarikiwa Vivutio vya Utalii, ambapo Sekta hii ya Utalii imeajiri Watanzania milioni 4 - Mafanikio mengi yamepatikana ikiwemo kuongezeka kwa mapato kutoka dola za Kimarekani bilioni 1.9 mwaka 2015 hadi dola bilioni 2.6 mwaka 2019

USAFIRI WA ANGA NA ATCL
Katika Usafiri wa Anga, tutaendelea kupanua na kukarabati Viwanja vya Ndege Mikoani ikiwemo kujenga Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa hapa Makao Makuu, Dodoma. Pia, tutaendelea kulilea Shirika letu la Ndege ATCL kimkakati ili lijiendeshe kibiashara.

''Kuilea ATCL kimkakati ni pamoja na kuangalia uwezekano wa kutoa unafuu wa madeni na baadhi ya kodi na tozo kama inavyofanyika kwenye nchi nyingine ili liweze kukua na kuweka mahesabu yake sawa, kwasasa halina thamani kwasababu ya kurithi madeni makubwa ya nyuma''.

''Kama serikali tunakwenda kulitua mzigo mkubwa shirika letu la ATCL ili liweze kukua, tutajitahidi kuepuka mambo yote yasiyo na tija kwa shirika letu, hatutakubali kuona shirika linaendelea kupata hasara baada ya uwekezaji mkubwa tuliofanya'' .

Tunakwenda kufanya utafiti wa kina ili kuhakikisha tutakaowaamini kuliendesha Shirika letu la Ndege wana weledi na uwezo wa kuliendesha shirika hili kibiashara. Pia, tutakamilisha Ujenzi wa Mradi wa Kufua Umeme wa Mwl. Nyerere ili nchi kuwa na nishati ya kutosha.

MAWASILIANO NA TEHAMA
Uchumi na shughuli nyingi duniani kwa sasa zinafanyika kupitia TEHAMA, nasi Tanzania tunapaswa kufikia huko - Katika kipindi cha miaka mitano tumepanga kuboresha na kufikisha huduma ya Mkongo wa Taifa katika Ngazi za Wilaya.

Tunapanga kuongeza wigo wa matumizi ya Mawasiliano ya Kasi yaani 'Broadband' kutoka asilimia 45 ya sasa hadi 80 mwaka 2025. Aidha, tutaongeza watumiaji wa intaneti kutoka asilimia 43 ya sasa hadi 80% mwaka 2025. Pia, tutaboresha Mawasiliano ya Simu nchi nzima.

KUHUSU AFYA NA COVID-19

A. Afya

Serikali itaboresha Huduma za Afya na kupunguza vifo vya Mama na Mtoto kwani hatupendi kuona watu wakifariki kwa sababu zinazoweza kuepukika. Ninasikitishwa sana Watanzania milioni 8.2 tu (sawa na 14% ya Watanzania wote) ndio wenye Bima ya Afya.

Serikali itaboresha Huduma za Afya na kupunguza vifo vya Mama na Mtoto kwani hatupendi kuona watu wakifariki kwa sababu zinazoweza kuepukika. Ninasikitishwa sana Watanzania milioni 8.2 tu (sawa na 14% ya Watanzania wote) ndio wenye Bima ya Afya.

B. Covid-19
Hadi sasa hakujapatikana kinga ya Ugonjwa wa Covid 19, tumeunda Tume maalumu ambayo itashirikiana na Taasisi za Afya kuliangalia suala hili kiundani na kutoa mapendekezo ya namna ya kupambana na janga hili.

Wakati tukisubiri majibu ya Kamati ya Wataalamu wa Corona iliyoundwa, nichukue fursa hii kuwataka Watanzania kuchukua tahadhari kwani ulinzi wa afya yako, unaanza na wewe mwenyewe, usisubiri tamko la Serikali.

UHURU NA DEMOKRASIA
Katika kulinda Uhuru wa Kidemokrasia nakusudia kukutana na Viongozi wa Siasa - Uhuru na Demokrasia ni Msingi wa Amani katika nchi na hakuna Uhuru wa Kidemokrasia usiosimamiwa na Sheria. Niwaombe Watanzania kufanya mambo yetu kwa kufuata Sheria.

MAJI
Ninakwenda kufanya marekebisho makubwa kwa Wahandisi wa Maji Mikoani. Fedha nyingi zimekuwa zikitoka lakini kumekuwa na kusuasua. Waziri wa Maji ile kauli yako ya 'ukinizingua tunazinguana' inarudi kwako. Tunakwenda kutunisha Mfuko wa Maji na kuondosha utendaji mbovu.

Tatizo kwenye maji ni kusuasua. Walioshindwa kutuletea maji na kutumia fedha nyingi wakae upande tuingize damu mpya. Lengo ni kufikisha maji kwa asilimia 95 Mijini na asilimia 85 Vijijini ifikapo mwaka 2025. Tupeleke maji kwa Wananchi kwa haraka.

Lingine tutakalolifanya ni utunzaji wa Vyanzo vya Maji pamoja na mazingira. Kwa maeneo ambayo hayana kabisa vyanzo vya maji tunakwenda kuchimba visima vya kuvuna maji ya mvua - Pia, tutaziimarisha Kamati za Maji Mitaani na Vijijini ili ziweze kusimamia miradi yao.

UCHONGANISHI KUHUSU KIFO CHA HAYATI MAGUFULI
Kila Mtu Duniani atapata umauti na kila mauti ina sababu. Nimeona kwenye Mitandao taarifa za uchonganishi - Taarifa tuliyopewa na Madaktari ya kifo cha Magufuli ni Tatizo la Moyo. Nimekua naona mitandaoni wanasema fulani na fulani wamempa sumu, waache hili.

Wanaosema mitandaoni kuwa Hayati Magufuli alipewa sumu, mara fulani na fulani walitega kitu, kama wana taarifa za maana waje tuwasikilize, lasivyo waache kuleta uchonganishi. Kama wanafanya hivyo kwasababu hatutowapata warudi kwa Mungu wajiulize je, wanafanya sawa?

Wanaoleta uchonganishi kwenye Mitandao nadhani wanafanya hivyo kwasababu wanajua hatutoweza kuwapata - Wanatumia mifumo hiyo huko kwingine ambayo bado hatujawa na uwezo wa kuwatafuta, lakini niwaambie tutawatafuta

RAIS MWANAMKE
Hii ni mara ya 1 kwa Taifa letu kupata Rais Mwanamke na hivyo najua kuna watu wenye wasiwasi kwamba kutokana na jinsia yangu sitaweza kuyatimiza niliyoyasema hapa. Naomba nitumie Bunge hili kusema kwamba Mwenyezi Mungu hakuumba ubongo dhaifu kwa mwanamke.

KUWAKOSOA VIONGOZI
Haya niliyoyasema hapa sio kwamba nakwenda kuyafanya peke yangu. Nitakaa na kushirikiana na wenzangu. Tukosoeni pale inapobidi na naomba mtukosoe vikali sana. Mawaziri wangu wakileta vitu visivyoeleweka wakosoeni vikali sana, lakini wakosolewe kwa lugha ya kibunge.

Kuna baadhi ya watu wameenza kulegalega na wizi umeanza kushamiri kwenye baadhi ya maeneo. Nataka niwaambie kwamba mwendo ni ule ule.

Niwaonye wale wote wanaosimamia mali za Umma, ukwepaji kodi, ubadhirifu, kukemea uzembe na uvivu kuwa yameondoka kutokana na kuondoka kwa Hayati Magufuli - Amekwenda peke yake, lakini maoni na mikakati tunaifanyia kazi.

FULL TEXT HOTUBA YA RAIS SAMIA SULUHU....


HOTUBA YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHESHIMIWA SAMIA SULUHU HASSAN, WAKATI WA KULIHUTUBIA BUNGE LA 12 LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

DODOMA, 22 APRILI 2021



Mheshimiwa Spika;

Baada ya kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa Neema na Rehma zake, niruhusu niseme kuwa ni miaka takriban 6 imepita tangu niondoke kwenye Jengo hili adhimu – Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nikiwa Mbunge. Hivyo basi, leo ninayo furaha kurudi tena na kupata fursa hii ya kulihutubia Bunge hili ambalo limenilea, limenijenga, kuninoa na kufanya uwezo wangu uonekane na wote mpaka kuweza kushika nafasi hii niliyonayo. Nimefarijika kuona baadhi ya wenzangu niliokuwa nao bado wapo ndani ya Bunge hili. Lakini, nimepata faraja zaidi baada ya kuziona sura mpya zenye ari na matumaini ya kuwatumikia Watanzania.

Mheshimiwa Spika;

Nashukuru sana kwa ukarimu wako pamoja na Waheshimiwa Wabunge kunikaribisha leo hii ndani ya Bunge hili. Nimekuja kulihutubia Bunge hili baada ya nchi yetu kupita kwenye kipindi kigumu cha historia ya uongozi. Kama itakavyokumbukwa, tarehe 17 Machi 2021, Taifa letu lilipatwa na msiba mkubwa wa kuondokewa na aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. Kwa sababu hiyo, kabla sijaendelea mbele na hotuba yangu, naomba sote tusimame kwa dakika moja tumuombee Hayati Rais Magufuli. Mwenyezi Mungu aipumzishe Roho yake mahali pema peponi. Amina.


Hayati Rais Dkt. Magufuli alikuwa Kiongozi hodari, jasiri na shupavu; mwenye maono, ambaye aliipenda nchi yetu na kuitumikia kwa uaminifu na uadilifu mkubwa. Hivyo basi, napenda nitumie fursa hii kurudia tena kutoa pole nyingi sana kwa familia, hususan Mama Suzan Magufuli, Mama wa Marehemu; Mjane wa Hayati Dkt. Magufuli, Mama Janet Magufuli; watoto, ndugu pamoja na jamaa. Napenda pia kutoa pole kwa Bunge hili Tukufu ambalo kabla awe Rais alikuwa mwenzenu kwa miaka 20. Aidha, kama ivyofahamika, kwa mujibu wa Katiba yetu, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni sehemu ya Bunge hili. Hivyo basi, sina budi kulipa pole Bunge hili.

Nitumie fursa hii pia kurudia kuwapa pole nyingi Watanzania wote kwa kumpoteza Kiongozi wetu mpendwa. Kwa hakika, Taifa letu limeondokewa na mmoja wa viongozi mahiri, mzalendo, mwana mwema wa Tanzania ambaye tulimpenda na tunathamini mchango wake kwa taifa. Mapenzi haya ya Watanzania yalidhihirika wazi kipindi cha maombolezo na mazishi ambapo sote tulishuhudia idadi kubwa ya wananchi waliojitokeza kumuaga.


Mheshimiwa Spika,

Kufuatia kifo cha Hayati Rais Dkt. Magufuli; tarehe 19 Machi, 2021; kwa kuzingatia Katiba ya nchi yetu, niliapishwa kushika hatamu za uongozi wa Taifa letu. Hivyo basi, napenda, kwanza kabisa, kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kulipitisha salama Taifa letu kwenye kipindi cha mabadiliko ya uongozi wa Nchi. Mimi binafsi, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kushusha kudra yake kwangu mimi mja wake, kwani dhamana hii ni kubwa na yenye mitihani mingi. Hivyo, namwomba Mwenyezi Mungu anisaidie.

Napenda pia nikishukuru Chama changu, Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambacho kimenijengea uwezo mkubwa na wakati wote kimeniamini. Kama nisingeaminiwa na Chama changu, huenda leo, nisingekuwa mbele ya Bunge hili kulihutubia. Nawashukuru pia Viongozi mbalimbali wa Chama na Serikali, ambao wamenilea na kunijengea uzoefu na pia kujiamini. Na hapa naomba niwashukuru kwa moyo wa dhati kabisa, Waheshimiwa Marais Wastaafu wote pamoja na Viongozi wote Wakuu wa Kitaifa kwa kuwa nami bega kwa bega katika nyadhifa zangu mbalimbali za utumishi nilizopitia na kushika.

Kipekee kabisa, napenda kutambua mchango na malezi ya Waheshimiwa Marais Hayati Dkt John Magufuli na Marais Wastaafu Amani Abeid Karume na Jakaya Mrisho Kikwete. Niseme wazi kuwa uwezo wangu wa uongozi uliibuliwa na Mhe. Amani Karume aliyenipa nafasi ya Uwaziri katika kipindi changu cha mwanzo na cha pili nikiwa Mjumbe wa

Baraza la Wawakilishi la Zanzibar. Malezi haya ya uongozi yaliendelezwa na Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete alienipa Uwaziri katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na baadaye kuniamini kwenye nafasi ya kuwa Makamu Mwenyekiti wa Bunge la Katiba. Fursa hii ilinipa nafasi ya kuwajua na kufanya kazi na baadhi yenu humu ndani na ndiyo fursa iliyonitambulisha kwa Watanzania.

Nimshukuru sana, ingawa hatuko naye duniani, Hayati Rais Dkt. Magufuli kwa kuniamini kuwa Mgombea Mwenza wake kwenye Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015 na Mwaka 2020; na hatimaye kuniwezesha kuwa Mwanamke wa Kwanza nchini kushika wadhifa wa Makamu wa Rais na sasa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.


Mheshimiwa Spika;

Nalishukuru Bunge lako Tukufu kwa ushirikiano mkubwa ambao limenipa tangu nimechukua dhamana ya kuliongoza Taifa letu. Nalishukuru sana Bunge kwa kupitisha Azimio la Kunipongeza na kuniahidi ushirikiano; lakini pia kwa kuridhia pendekezo langu kuhusu jina la Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Philip Isdor Mpango. Namshukuru kwa kukubali uteuzi huo na kwamba sasa amejipanga kuchapa kazi kweli kweli.

Siwezi kuhitimisha shukran zangu bila kuwashukuru viongozi wengine wa Serikali kwa ushirikiano mkubwa walionipa tangu nimekabidhiwa dhamana ya kuliongoza Taifa letu. Namshukuru Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi pamoja na Serikali yake, tumeanza kufanyakazi kwa ukaribu zaidi.

Namshukuru Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa; Namshukuru Mheshimiwa Jaji Mkuu na kupitia yeye Mhimili wa Mahakama; nawashukuru Waheshimiwa Mawaziri; Katibu Mkuu Kiongozi Ndugu Hussein Kattanga; Wakuu wa Mikoa; Makatibu Wakuu pamoja na viongozi wengine wote wa Serikali. Kwa namna ya pekee, navishukuru Vyombo vya Ulinzi na Usalama, ambavyo kwa ari kubwa vinaendelea kulinda amani na usalama wa nchi yetu na mipaka yake.

Napenda pia niwashukuru Viongozi wetu wa Dini ambao wakati wote wamekuwa wakifanya dua na sala kuliombea Taifa letu. Nawashukuru viongozi wa Vyama vya Siasa kwa ushirikiano wanaonipa. Navishukuru Vyombo vya Habari kwa kuendelea kutoa taarifa na kuwaelimisha Watanzania kuhusu masuala mbalimbali yanayojitokeza nchini. Mwisho, lakini sio kwa umuhimu, nawashukuru Watanzania wote kwa kuendelea kuniamini na kuiunga mkono Serikali.

Mheshimiwa Spika;

Mwaka huu, nchi yetu imetimiza miaka 57 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar pamoja na Muungano wetu na tutasheherekea miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara. Katika kipindi hicho, mafanikio mengi makubwa yamepatikana. Napenda nitumie fursa hii, kuzishukuru na kuzipongeza Awamu zote za Uongozi wa nchi yetu; kuanzia Awamu ya Kwanza iliyoongozwa na Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere; Awamu ya Pili ya Mzee Ali Hassan Mwinyi; Awamu ya Tatu ya Hayati Mzee Benjamin William Mkapa; Awamu ya Nne ya Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete; pamoja na Awamu ya Tano iliyoongozwa na Mtangulizi wangu, Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli; kwa mafanikio hayo. Kwa upande wa Zanzibar, nazishukuru awamu zote nane za uongozi kwa kujenga Ustawi na Maendeleo kwa Wananchi wa Zanzibar mpaka hatua iliyofikia.

Nami nataka, hapa mwanzoni kabisa, nilieleze Bunge hili Tukufu pamoja na Watanzania kwa ujumla, kuwa, Dira na Mwelekeo wa Serikali ya Awamu ya Sita itakuwa “Kudumisha mazuri ya Awamu zilizopita, Kuyaendeleza mema yaliyopo

na Kuleta mengine mapya
. Na hii, kimsingi, ndiyo dhana na maana halisi ya kaulimbiu/salamu yetu ya “Jamhuri ya Muungano wa Tanzania – Kazi Iendelee”. Tutaenzi na kuendeleza mambo yote mazuri; lakini pia tutafanya mabadiliko pale itakapobidi kwa lengo la kukuza ufanisi na tija; huku tukiongozwa na Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Mwaka 2025; Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2020 – 2025; Mpango wa Tatu wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano; Ajenda ya Maendeleo ya Afrika ya mwaka 2063 na

Ajenda ya Dunia ya Malengo ya Maendeleo Endelevu ya mwaka 2030.

Na katika hilo, Mheshimiwa Spika utakumbuka kuwa, wakati akizindua Bunge hili, tarehe 13 Novemba, 2020; Rais wa Awamu ya Tano, Hayati Dkt. Magufuli alieleza mambo mengi muhimu ambayo yangepewa kipaumbele na Serikali ya Chama Cha Mapinduzi kwenye miaka hii mitano, kwa kuzingatia Ilani yetu ya Uchaguzi ya Mwaka 2020 - 2025. Hivyo basi, kwa kuwa nilishiriki kikamilifu katika kuinadi Ilani hiyo; na kwa kuwa, kama nilivyowahi kusema, na leo nataka nirudie tena kuwa, mimi na Hayati Rais Dkt. Magufuli tulikuwa kitu kimoja. Kwa sababu hiyo, mambo mengi ambayo Serikali ninayoingoza imepanga kuyatekeleza ni yale ambayo yalielezwa na Hayati Rais Dkt. Magufuli wakati akilizindua Bunge hili.

Mheshimiwa Spika;

Naomba sasa uniruhusu nitaje baadhi ya masuala muhimu ambayo Serikali ya Awamu ya Sita itayapa kipaumbele kwenye miaka hii mitano.


Jambo la kwanza na muhimu kabisa tutakalolipa kipaumbele kwenye miaka hii mitano ni kuendelea kulinda na KUDUMISHA TUNU ZA TAIFA letu, yaani Amani, Umoja na Mshikamano, Uhuru wa nchi yetu, Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar pamoja na Muungano wetu. Kama mnavyofahamu, amani na umoja ni msingi mkuu wa maendeleo katika Taifa lolote. Hivyo basi, nawasihi sana Watanzania wenzangu tushirikiane kwa pamoja katika kulinda tunu hizi. Tanzania ni yetu sote; kila mmoja wetu anao wajibu wa kuhakikisha anazilinda na kuzitetea tunu hizi mahali popote alipo.

Mheshimiwa Spika;

Mbali na kulinda na kuzitunza tunu za Taifa letu, tunakusudia kuelekeza nguvu kubwa katika KUSIMAMIA UKUZAJI UCHUMI. Kama mnavyofahamu, kwenye miaka ya hivi karibuni, hususan kwenye miaka mitano iliyopita, Taifa letu limepata mafanikio makubwa ya kiuchumi. Tumesimamia ukuaji uchumi kwa wastani wa asilimia 6.9 kwa mwaka; tumedhibiti mfumko wa bei kwa wastani wa asilimia 4.4; na kupunguza umasikini hadi kufikia asilimia 26.6. Muhimu zaidi, mwaka jana, mwezi Julai 2020, Taifa letu lilifanikiwa kuingia kwenye Kundi la Nchi za Uchumi wa Kati, ambapo Pato la wastani wa kila Mtanzania limeongezeka hadi kufikia Dola za Marekani 1,080, zaidi ya kigezo cha Dola za Marekani 1,036 cha kuingia kwenye Kundi hilo. Haya, bila shaka, ni mafanikio makubwa.

Lakini, pamoja na mafanikio hayo makubwa, ni wazi kuwa jitihada zaidi zinahitajika ili kukuza uchumi na kupambana na umasikini nchini. Hii ni kwa sababu, licha ya mafanikio yaliyopatikana, kasi ya ukuaji uchumi bado ni ndogo. Wataalam wa Uchumi wanatueleza kwamba, ili kuweza kupambana na umasikini, uchumi wetu unatakiwa ukuwe angalau kwa asilimia 8 kwa mwaka. Lakini, kutokana na Dunia kukumbwa na janga la Corona, ki-uhalisia takwimu zinaonesha kwamba chumi nyingi duniani zimeshuka. Tanzania nayo imeathirika kwa kushuka kwa kiwango cha uchumi kutoka wastani wa asilimia 6.9 hadi asilimia 4.7. Hii inamaanisha kwamba katika miaka mitano ijayo kunahitajika uwekezaji mkubwa katika sekta za uzalishaji na zitazotoa ajira kwa wingi.

Hatua mahsusi zitakazochuliwa katika kukuza Uwekezaji, ni pamoja na kufanya marekebisho kadhaa katika Sera, Sheria na kanuni zetu na kuondoa vifungu vitakavyobainika kusababisha vikwazo katika kukuza uwekezaji. Tutaendelea kuboresha sera zetu za Uchumi wa Jumla pamoja na sera za fedha, na kuhakikisha viashiria vyote vya uchumi; ikiwemo thamani ya sarafu yetu, mfumko wa bei pamoja na viwango vya riba; vinabaki kwenye hali ya utulivu. Sambamba na hilo, hatutokuwa tayari kuvumilia Uvivu, Uzembe, Wizi na Ubadhirifu wa Mali na Fedha za Umma.

Aidha, tutachukua hatua madhubuti za kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini ili kuivutia sekta binafsi kushiriki vizuri kwenye shughuli za kiuchumi. Mwelekeo utakuwa kurudisha imani kwa wawekezaji na kutoa vivutio kwa wawekezaji mahiri (Strategic Investors), ikiwa ni pamoja na kuwezesha uwekezaji kufanyika kwa haraka.

Kutakuwa na Sifa na matakwa maalum yatakayowekwa kwa uwazi katika kutambua miradi ya kimkakati itakayostahiki vivutio vya kikodi au vivutio vyenginevyo. Suala la upatikanaji wa mitaji nalo halina budi kuangaliwa kwa umakini mkubwa.

Kama mnavyofahamu, ili sekta binafsi iweze kushiriki vizuri, hatuna budi kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara. Nchi yetu imekuwa ikilalamikiwa kwa kutokuwa na mazingira mazuri ya biashara na uwekezaji, ikiwemo kutokuwa na sera zinazotabirika, utaratibu wa kodi usio na utulivu, urasimu mwingi katika kutoa huduma kwa wawekezaji, na matatizo mengine yanayokwamisha ustawi wa biashara na uwekezaji.

Hivyo basi, Serikali ya Awamu ya Sita inakusudia kufanya maboresho makubwa kwenye eneo hilo. Kwanza, tutahakikisha tunatekeleza kikakamilifu Mpango wetu wa Kuboresha Mazingira ya Biashara nchini. Zaidi ya hapo,

Nimeiweka Wizara ya Uwekezaji chini ya uangalizi wa Waziri Mkuu ili kurahisisha uratibu wa pamoja na ukaribu katika kuhakikisha tunaondoa urasimu kwenye masuala ya Uwekezaji, ikiwemo kutoa vibali na leseni ndani ya muda mfupi na masuala ya upatikanaji wa ardhi kwa uwekezaji. Na katika hilo, narudia wito wangu wa kujenga Dirisha Moja la mfumo wa kutoa Huduma kwa Mtandao.

Tunakusudia kufanya mageuzi ya kiutendaji kwenye mfumo wa utozaji na ukusanyaji wa kodi, kuweka mfumo utakaorahisisha na kuvutia walipa kodi, na kutengeneza wigo mpana zaidi wa walipa kodi ikilinganishwa na walipa kodi waliopo leo. Tumejitahidi sana katika awamu ya tano kuongeza makusanyo ya kodi kutoka wastani wa shilingi bilioni 850 mwaka 2015 hadi kufikia wastani wa shilingi trilioni 1.9 hivi sasa. Makusanyo haya yanatokana na Kodi ya Forodha asilimia 40 na Kodi za ndani asilimia isiyozidi 20. Hii
ina maana kwamba ni watanzania wachache ndio wanaolipa kodi kati ya Watanzania wanaokaribia milioni 60. Hivyo basi, kuna kila haja ya kutanua wigo wa walipa kodi, na vile vile, kuweka mifumo rafiki ya ulipaji na ukusanyaji wa kodi. Ningependa kuona Wafanyabiashara, Wawekezaji na Wananchi wanalipa kodi bila shuruti na matumizi ya nguvu, wakitambua kwamba kodi ni maendeleo yao.

Tunadhamiria pia kufanya mapitio na uchambuzi wa kina kwenye uendeshaji wa Mashirika ya Umma, tukiwa na lengo la kuyafanya yaweze kujiendesha kwa faida. Mashirika yaliyo mengi yanaendeshwa kwa kusuasua kiasi kwamba unapofika muda wa kutoa gawio la faida Serikalini, uongozi na Bodi za Mashirika wanahaha kunusuru ajira zao.

Vilevile, tutaendelea kufanya kazi kwa karibu sana na Sekta Binafsi kwa kutambua kuwa wao ndiyo kiini cha ukuaji wa uchumi. Kwa kudhihirisha hilo, pamoja na mambo mengine, Serikali tunashirikiana na Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF) kuanzisha mfumo wa kupokea na kushughulikia changamoto za wawekezaji nchini kwa njia ya mtandao. Lengo la Mfumo huo ni kurahisisha ushughulikiaji wa changamoto za wawekezaji kwa njia ya haraka na kuleta ufanisi katika kuwahudumia. Kumekuwa pia na malalamiko mengi kwenye upatikanaji wa vibali vya kazi kwa wageni. Kuna msemo unasema ukimuona mtu mzima analia ujue lipo jambo. Hapa napo kwa kuwa malalamiko yamezidi hatuna budi kuliangalia upya suala hili, huku tukilinda maslahi ya Taifa.

Ni imani yangu kuwa hatua hizi, pamoja na nyingine ambazo sikuzitaja, zitavutia wawekezaji na wafanyabiashara wengi ikiwemo wa ndani, kuwekeza kwenye sekta mbalimbali nchini na hivyo kusaidia juhudi za Serikali za kukuza uchumi, kupambana na umasikini na kukabiliana na tatizo la ajira.

Mheshimiwa Spika;

Kama unavyofahamu, zaidi ya asilimia 65 ya Watanzania ni Wakulima, ambao wanajishughulisha na KILIMO CHA MAZAO, UFUGAJI NA UVUVI. Hivyo basi, ni ndoto kwetu kufikiria kwamba tutaongeza kasi ya kukuza uchumi na kukabiliana na umasikini bila ya kuelekeza nguvu kubwa katika sekta hizo. Ni kweli, kwenye miaka iliyopita, tumeweza kupata baadhi ya mafanikio kwenye sekta ya kilimo. Mathalan, sekta hii kwa sasa inachangia asilimia 100 ya chakula nchini, asilimia 60 ya malighafi za viwandani, asilimia 27.7 ya Pato la Taifa na asilimia 25 ya fedha za kigeni.

Hata hivyo, pamoja na mafanikio hayo, sekta ya kilimo bado inakabiliwa na matatizo mengi, lakini kubwa zaidi ni udogo wa tija au uhaba wa mavuno. Nimeeleza hivi punde kuwa, zaidi ya asilimia 65 ya Watanzania ni wakulima lakini mchango wao kwenye Pato la Taifa ni asilimia 27 tu. Hii inatokana na tija ndogo inayopatikana kwenye kilimo cha mazao mbalimbali hasa mazao ya biashara. Kwa mfano; kilimo cha mahindi chenye tija kinawezesha uvunaji wa tani 8 kwa hekta, lakini kwa hapa kwetu wastani wa uzalishaji ni tani 1.9 tu. Aidha, tunazalisha pamba kilo 250 kwa ekari moja wakati zipo nchi wanazalisha kati ya kilo 1,000 hadi kilo 1,250 kwa ekari. Na hali hii ipo kwenye mazao takriban yote.

Ukiachilia mbali tija ndogo kwenye kilimo cha mazao, nchi yetu, licha ya kushika nafasi ya pili kwa mifugo Barani Afrika, sekta ya mifugo inachangia asilimia 7.4 kwenye Pato la Taifa. Mwaka 2019/2020 tulizalisha tani 701,679 za nyama na lita bilioni 3 za maziwa. Hii inatokana na matumizi madogo ya mbinu za kisasa za ufugaji. Mathalan, ng’ombe wetu kwa wastani wanazalisha lita 3 za maziwa; wakati kwa kutumia mbinu za kisasa wanaweza kuzalisha lita 20 hadi lita 30 kwa siku. Ng’ombe wetu wengi wanatoa nyama isiyozidi wastani wa kilo 150; lakini mahali kwingine duniani ng’ombe wanafikisha kilo 500 – 600 za nyama.

Kwa upande uvuvi, nako hali iko vivyo hivyo. Licha ya kuwa na maeneo mengi makubwa yenye kufaa kwa uvuvi, ikiwemo mwambao wenye urefu wa takriban kilometa 1,400, maziwa makubwa pamoja na mito mingi, mauzo yetu ya samaki nje ya nchi ni madogo na wakati mwingine nchi yetu inaendelea kuagiza samaki kutoka nje. Hii inadhihirisha kuwa tija kwenye sekta ya kilimo bado ni ndogo sana.

Hivyo basi, kwenye miaka hii mitano, tutaelekeza nguvu kubwa katika kujenga misingi imara wa sekta ya kilimo kwa lengo la kuongeza tija. Tutajitahidi kuwekeza katika kilimo cha biashara, kuongeza uzalishaji wa mbegu bora kwa kuongeza uwekezaji kwa Taasisi za Serikali za TARI na ASA ili zizalishe na kuhamasisha matumizi ya mbegu bora kwa wakulima. Taasisi hizo tutazipa fedha za kuanzia kama mtaji na tutazitaka ziendelee kuzalisha kibiashara. Hii itarahisisha upatikanaji wa mbegu bora na kupunguza gharama za kuagiza mbegu kutoka nje.

Shughuli nyingine kwenye sekta hii ni upatikanaji wa mbolea ya kutosha na kwa wakati, kuboresha afya ya udongo, kukuza huduma za utafiti na huduma za ugani, kujenga masoko Imara kwa kujenga miundombinu na mfumo na kuwezesha uuzaji wa mazao ya kilimo nje ya nchi, pamoja na upatikanaji wa mikopo yenye riba nafuu. Tutaongeza pia eneo la kilimo cha umwagiliaji kutoka hekta 561,383 hadi hekta milioni 1.2 ifikapo mwaka 2025 ili kupunguza kilimo cha kutegemea mvua. Tutakamilisha ujenzi wa skimu za umwagiliaji zilizopo na kuhakikisha zinafanya kazi kwa tija. Na hapa nataka kueleza kuwa Serikali itaanza kutoza ada kwa wakulima wanaotumia skimu hizo ili kugharamia gharama za usimamizi na uendeshaji. Vile vile, tutaendeleza ujenzi wa vihenge na maghala maeneo mbalimbali nchini ili kuondoa tatizo la upotevu wa mazao baada ya kuvunwa.

Kuhusu ufugaji, kama nilivyowahi kusema, tunalenga kuachana na uchungaji wa kuhamahama. Katika kutimiza azma hii, tutaelekeza nguvu kubwa katika kuhamasisha ufugaji wa kisasa. Tutajielekeza kwenye uzalishaji kwa njia ya uhamilishaji kwa lengo la kubadili kosaafu (breed) ya mifugo yetu, ili kuwawezesha wafugaji kuwa na mifugo michache yenye sifa za uzalishaji mkubwa uwe wa Nyama au Maziwa na kuongeza tija. Tutaongeza vituo vya kuzalisha mbegu bora na pia kuongeza uzalishaji wa chakula cha mifugo viwandani kutoka tani 900,000 hadi tani milioni 8, kama ilivyoelekezwa kwenye Ilani yetu ya Uchaguzi. Vilevile, tunakusudia kuongeza maeneo ya ufugaji kutoka hekta 2,788,901 za sasa hadi hekta 6,000,000. Lengo ni kupunguza tabia ya sasa ya wafugaji kuhamahama, ambayo inasababisha uharibifu mkubwa wa mazingira pamoja na kuzusha migogoro kati yao na wakulima.

Kwa upande wa uvuvi, tutaimarisha usimamizi wa uvuvi wa Bahari Kuu ili Taifa letu linufaike na rasilimali zake. Na katika hilo, tumepanga kununua Meli 8 za Uvuvi kwa kushirikiana na Shirika la IFAD ili zishiriki katika uvuvi wa Bahari Kuu, ambapo meli 4 zitafanya kazi upande wa Zanzibar na 4 upande wa Tanzania Bara. Aidha, tunakusudia kujenga bandari kwa ajili ya meli zitakazofanya uvuvi katika maeneo ya ukanda wa Pwani. Tunajipanga kuanza utengaji wa vizimba vya kuvua samaki baharini, utoaji wa vibali vya uvuvi katika bahari kuu na uwekezaji katika zana bora za kuvulia pamoja na uanzishaji wa viwanda vya uchakataji wa samaki na mazao mengine ya majini.

Sambamba na hayo, tunakusudia kuendelea kuimarisha Benki ya Maendeleo ya Kilimo ili kuiwezesha kutoa mikopo yenye riba nafuu kwa wakulima, wafugaji na wavuvi. Zaidi ya hapo, tunakusudia kuliangalia kwa karibu zaidi suala la Bima ya kilimo na kuliwekea misingi imara.

Mheshimiwa Spika;

Ili kukuza sekta ya kilimo, hatuna budi pia kuifungamanisha na SEKTA YA VIWANDA. Kama nilivyosema awali kwamba kilimo kinachangia kwa kiasi kikubwa malighafi ya viwandani, aidha, viwanda vinawahakikishia wakulima soko kwa mazao yao. Kwa bahati nzuri, kwenye miaka mitano iliyopita, tuliweza kuhamasisha ujenzi wa viwanda vingi nchini, kati yao vikiwemo vya kusindika mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi.

Hivyo basi, Serikali ya Awamu ya Sita itaendeleza jitihada za kuhamasisha ujenzi wa viwanda nchini, hususan vile vinavyotumia malighafi za ndani. Tunakusudia pia kutenga maeneo ya viwanda kulingana na mazao yanayozalishwa. Aidha, njia nyingine itakayotumika kuongeza kasi ya viwanda nchini ni kutenga na kuendeleza maeneo huru ya biashara, ambapo kipaumbele kitakuwa kwenye maeneo ya mipakani au maeneo yenye miundombinu thabiti ya usafiri, kama reli, bandari na barabara zinazotuunganisha na nchi jirani. Na katika hilo, suala la Kongani (Industrial Parks) ni muhimu sana katika kuchochea ujenzi wa viwanda na pia kuiwezesha nchi yetu kunufaika na vyema fursa za kibiashara, ikiwemo kupitia itifaki mbali mbali kama vile EAC, SADC, Eneo Huru la Biashara la Afrika; n.k.

Mheshimiwa Spika;

SEKTA YA MADINI
, ambayo kwa sasa imetoa ajira zipatazo milioni 1.5, ina nafasi kubwa ya kuchochea ukuaji uchumi nchini. Kwenye miaka mitano iliyopita, tumepata mafanikio makubwa kwenye sekta hii. Mchango wake kwenye Pato la Taifa umeongezeka kutoka asilimia 3.4 mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 5.2 mwaka 2019. Mapato yake yaliongezeka kutoka shilingi bilioni 168 mwaka 2014/2015 hadi shilingi bilioni 527 mwaka 2019/2020. Zaidi ya hapo, mwaka 2019, sekta ya madini iliongoza kwa kuliingizia Taifa fedha nyingi za kigeni, Dola za Marekani bilioni 2.7.

Serikali ya Awamu ya Sita inakusudia kuendeleza mafanikio hayo kwa kusimamia Sheria yetu ya Madini ya mwaka 2017, kuendelea kuziba mianya ya utoroshaji wa madini yetu, tutaendelea kuangalia kwa umakini mkubwa na kuondoa vikwazo vya uwekezaji katika sekta hii, ili kuvutia na kurahisisha mijadala ya Serikali kuingia ubia na wachimbaji wakubwa Duniani. Tutaendelea pia kuimarisha masoko na minada ya uuzaji madini, kuhamasisha ujenzi wa viwanda vya uchenjuaji, uyeyushaji, usafishaji na utengenezaji wa bidhaa za madini. Mkazo utawekwa kwenye ubora na ufanisi wa teknolojia. Tutawaendeleza wachimbaji wadogo na kuwapatia mafunzo, mikopo pamoja na vifaa. Vilevile, Tutaliimarisha zaidi Shirika la Taifa la Madini (STAMICO) ili lishiriki kikamilifu kwenye shughuli za madini. Hatua hizi naamini, zitaifanya sekta ya madini ikuze mchango wake kufikia asilimia 10 ya Pato la Taifa ifikapo mwaka 2025.

Mheshimiwa Spika;

Sekta nyingine ambayo tutaipa mkazo mkubwa kwenye miaka hii mitano ni UTALII. Kama mnavyofahamu, nchi yetu imebarikiwa kuwa ni vivutio vingi vya utalii na sekta hii imeajiri takriban watu milioni 4. Kwenye miaka mitano iliyopita, mafanikio mengi yamepatikana kwenye sekta ya utalii, ikiwemo kuongezeka kwa idadi ya watalii waliotembelea nchini kutoka milioni 1.1 mwaka 2015 hadi watalii milioni 1.5 mwaka 2019. Mapato nayo yaliongezeka kutoka Dola za Marekani bilioni 1.9 mwaka 2015 hadi kufikia Dola za Marekani bilioni 2.6 mwaka 2019.

Hivyo basi, kwenye miaka hii mitano, pamoja na uwepo wa janga la Corona, tunalenga kuendeleza mafanikio yaliyopatikana, kwa kuongeza idadi ya watalii hadi kufikia milioni 5 mwaka 2025 na mapato kutoka Dola za Marekani bilioni 2.6 za sasa hadi Dola za Marekani bilioni 6. Hatua ambazo tunakusudia kuzichukua ni pamoja na kupanua wigo wa vivutio vya utalii, ikiwemo kukuza utalii wa mikutano, malikale na fukwe; ambapo tunakusudia kujenga miundombinu ya kuwezesha meli za utalii kuzuru nchini. Tutahamasisha pia wawekezaji kuwekeza kwenye miundombinu ya utalii, ikiwemo hoteli, ili kupunguza gharama za malazi. Tunajipanga kusomesha vijana wengi katika taaluma ya utalii ili waweze kuendesha maeneo mbali mbali ya sekta bila kutegemea wataalamu kutoka nje.


Mheshimiwa Spika;

Ili kuchochea shughuli za kiuchumi na uzalishaji nilizozitaja (yaani kilimo, viwanda, madini na utalii) tutaendeleza jitihada za kuimarisha MIUNDOMBINU YA USAFIRI, ambayo ni moyo wa ukuzaji uchumi. Kwenye miaka mitano iliyopita, jitihada kubwa zilifanyika za kuimarisha usafiri wa barabara, reli, maji na anga. Jumla ya kilometa 3,537 za barabara za lami zilijengwa pamoja na madaraja makubwa 12.

Usafiri wa reli kutoka Dar es Salaam – Tanga – Moshi – Arusha ulifufuliwa pamoja na kuanza ujenzi wa Reli ya Standard Gauge kutoka Dar es Salaam hadi Makutopora (Dodoma), ambapo kipande cha Dar es Salaam – Morogoro kimefikia asilimia 91 na Morogoro – Makutupora zaidi ya asilimia 58.2 hadi kufikia mwezi Aprili 2021.

Kwa upande wa usafiri wa maji, umefanyika upanuzi mkubwa wa Bandari za Dar es Salaam, Tanga na Mtwara pamoja na ujenzi wa Bandari Kavu ya Kwala Mkoani Pwani. Kwenye Ziwa Victoria, tumejenga chelezo, tumekarabiti meli mbili (MV. Victoria na MV. Butiama) pamoja na kujenga meli mpya. Katika Ziwa Tanganyika, umefanyika upanuzi na ukarabati mkubwa wa Bandari za Kigoma, Kalema, Kasanga na Kabwe; na kwenye Ziwa Nyasa zimejengwa meli mpya tatu na kufanya upanuzi wa Bandari za Kiwira na Itungi. Kuhusu usafiri wa anga, jumla ya viwanja vya ndege 11 vimepanuliwa ama kukurabatiwa na ndege mpya 11 zimenunuliwa.

Kwenye miaka hii mitano, tutatekeleza yaliyoagizwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwa kuendeleza ujenzi wa miundombinu hiyo ya usafiri. Tutaendelea kukamilisha ujenzi wa Bandari za Dar es Salaam, Tanga, Mtwara na Kigoma, kujenga barabara, hususan kwenye maeneo ya kimkakati, ambako shughuli za uzalishaji zinafanyika. Tukamilisha pia ujenzi wa madaraja makubwa, likiwemo la Kigongo – Busisi, Wami, Tanzanite na Pangani. Kwa upande wa reli, tutakamilisha ujenzi wa reli ya Dar es Salaam – Makutupora na kuanza ujenzi wa vipande vingine, kikiwemo cha Mwanza – Isaka (lot5); Makutupora – Tabora (Lot 3); Tabora – Isaka (Lot

na baadaye Tabora – Kaliua – Kigoma na Kaliua – Mpanda. Aidha, tunakusudia kuimarisha usafiri wa TAZARA kwa lengo la kuiongezea ushindani Bandari yetu ya Dar es Salaam na pia kunufaika na fursa nyingine za kiuchumi.

Kwa upande wa usafiri wa majini, tutakamilisha ujenzi wa meli mpya na kuanza ukarabati wa meli ya mabehewa (yaani Ferry Wagon) kwenye Ziwa Victoria na pia kuikarabati meli ya Mv. Liemba na kuanza ujenzi wa meli mpya kwenye Ziwa Tanganyika. Kuhusu usafiri wa anga tutaendelea na upanuzi wa viwanja vya ndege mikoani, na kujenga Kiwanja kipya cha Kimataifa cha Msalato hapa Makao Makuu Dodoma. Aidha, tutaendelea kulilea Shirika letu la Ndege (ATCL) kimkakati ili liweze kujiendesha kwa ufanisi. Ninaposema kimkakati ni pamoja na kuangalia uwezekano wa kutoa unafuu wa madeni na baadhi ya kodi na tozo, kama inavyofanyika kwenye nchi nyingine, ili liweze kukua. Shirika letu linaonekana kupata hasara kutokana na mzigo mkubwa wa madeni ya nyuma. Sote tunafahamu kuwa biashara ya ndege ni ngumu. Tutajitahidi kusoma mwenendo wa biashara hii ulimwenguni na kuepuka mambo yote yasiyo na tija kwa shirika letu. Hatutakubali kuona Shirika linaendelea kupata hasara baada ya uwekezaji mkubwa tulioufanya. Tutafanya uchambuzi wa kina ili watu watakaoendesha Shirika wawe na weledi na ujuzi wa biashara. Zaidi ya hapo, tutawekeza kwenye kupata rasilimali watu wenye uwezo na weledi wa kuendesha shirika kibiashara.

Mheshimiwa Spika;

Mbali na miundombinu hiyo migumu, tutaimarisha pia miundombinu laini, hususan miundombinu ya TEKNOLOJIA YA MAWASILIANO. Kama inavyofahamika, dunia ipo kwenye Mapinduzi ya Nne ya Viwanda, ambayo yanaongozwa na sekta ya Teknolojia ya Mawasiliano (TEHAMA), na kwa maana hiyo, Uchumi wa dunia pamoja na shughuli nyingi duniani, kwa sasa, zinafanyika kwa kutumia TEHAMA. Hivyo basi, sisi Tanzania nasi hatuna budi kuweka mkazo mkubwa katika kukuza sekta hii.

Kwa msingi huo, tumepanga, kwenye miaka hii mitano, pamoja na masuala mengine, kuongeza kasi ya kufikisha miundombinu ya Mkongo wa Taifa kwenye maeneo mengi ya nchi yetu, hususan katika ngazi za Wilaya, na pia kuongeza wigo wa matumizi ya mawasiliano ya kasi (yaani broadband) kutoka asilimia 45 ya sasa hadi asilimia 80 ifikapo mwaka 2025. Aidha, kuongeza watumiaji wa internet kutoka asilimia 43 ya sasa hadi asimilia 80 mwaka 2025; na pia, kuboresha upatikanaji wa mawasiliano ya simu nchi nzima. Tutatoa kipaumbele kwenye masuala ya utafiti na ubunifu kwenye

TEHAMA pamoja na kuimarisha usalama kwenye masuala ya Mawasiliano.

Mheshimiwa Spika;

Kwenye miaka mitano iliyopita, tumepata mafanikio makubwa kwenye SEKTA YA NISHATI. Tumeongeza uzalishaji umeme hadi kufikia Megawati 1602.3; ambapo mahitaji ya juu ya umeme kwa nchi yetu kwa sasa ni Megawati 1,200. Tumefanikiwa pia kufikisha umeme kwenye vijiji 10,294, sawa na asilimia 83.3 ya vijiji 12,317 vilivyopo. Tumeanza pia utekelezaji wa mradi mkubwa wa umeme wa Bwawa la Mwalimu Nyerere utakaozalisha Megawati 2,115. Mradi huu kwa sasa umefikia asilimia 45.

Hivyo basi, Serikali ya Awamu ya Sita itaendeleza jitihada za kuimarisha upatikanaji wa nishati nchini, ikiwemo kukamilisha ujenzi wa Bwawa la Nyerere, na kufikisha umeme kwenye vijiji 1,974 vilivyobakia. Tunajipanga kuanza kutekeleza miradi ya kuzalisha umeme wa maji ya Ruhudji Megawati 358; Rumakali Megawati 222; Kikonge Megawati 300 na pia umeme wa gesi asilia Mtwara Megawati 300; Somanga Fungu Megawati 330, Kinyerezi III Megawati 600 na Kinyerezi IV Megawati 300. Kutokana na kasi ya mabadiliko ya tabianchi, tunahitaji kuchanganya vyanzo vya nishati ili kuwa na uhakika wakati wote. Hivyo basi, tutaangalia uwezekano wa kutekeleza miradi ya nishati jadidifu (jua, upepo, jotoardhi) kwa kuwa vyanzo hivi ni endelevu. Tunatarajia katika miaka hii mitano kuzalisha Megawati 1,100 kupitiavyanzo hivyo.

Katika hatua nyengine, tutaendelea kutekeleza miradi ya kujenga njia za kusafirisha umeme kutoka Bwawa la Nyerere hadi kituo kikuu Chalinze na njia zinazoelekea kwenye maeneo ambayo hayajaunganishwa na Gridi ya Taifa ili kupunguza gharama za kuzalisha umeme wa mafuta na umeme unaopotea. Sambamba na hayo, tunatarajia kuanza utekelezaji wa Miradi ya kielelezo ya Bomba la Mafuta kutoka Hoima nchini Uganda hadi Bandari ya Tanga lenye urefu wa kilometa 1,445 pamoja na Mradi wa Kusindika Gesi Asilia (LNG) Mkoani Lindi. Mradi huu umechukua muda mrefu; hivyo, tunakwenda kumaliza majadiliano ili Mradi huu uanze kutekelezwa.

Mheshimiwa Spika;

Mbali na shughuli hizo za kuchochea ukuaji uchumi nilizozitaja, katika kipindi hiki cha miaka mitano, tutaendelea kuimarisha na kuboresha HUDUMA ZA JAMII, hususan afya, elimu na maji. Kuhusu AFYA, kama mnavyofahamu, kwenye miaka mitano iliyopita tumepata mafanikio makubwa, ikiwemo kujenga vituo vya kutolea huduma za afya 1,887 (zikiwemo zahanati 1,198, vituo vya afya 487, hospitali za wilaya 99, Hospitali za Rufaa za Mikoa 10 na Hospitali za Rufaa za Kanda 3).

Katika miaka hii mitano mpaka 2025, tutaimarisha upatikanaji wa huduma za afya kwa kuendelea kujenga miundombinu, kuongeza watumishi, vifaa tiba, dawa na vitendanishi. Aidha, juhudi za kupunguza vifo vya wajawazito na watoto zitaendelezwa. Nilipokuwa Makamu wa Rais nilizindua Kampeni ya ‘Jiongeze Tuwavushe Salama’ ili kutilia mkazo uwajibikiaji wa wadau wote katika kupunguza vifo vya mama na mtoto. Hivyo, huu ni mradi wangu wa moyoni kabisa. Binafsi, huwa nasikitishwa sana kusikia mwanamke anapoteza maisha wakati wa kujifungua kwa sababu ambazo zingeweza kuzuilika.

Tutaelekeza pia nguvu katika kinga na tiba, ikiwemo kwa magonjwa yasiyoambukiza, ambayo yanasababisha vifo vingi na kugharimu Serikali fedha nyingi. Tutaimarisha pia huduma za matibabu ya kibingwa na kuzipeleka huduma hizi kwenye Hospitali za Rufaa za Mikoa. Tutaimarisha utoaji wa huduma za matibabu kwa wazee; na kutaweka mipango maalum kuhudumia makundi yenye magonjwa adimu. Tutaimarisha Mifuko ya Taifa ya Bima ya Afya ili kufikia lengo la Bima ya Afya kwa wote. Kwa sasa ni watu 8,224,271 sawa na asilimia 14 tu ya Watanzania ndio wanaotumia Bima ya Afya. Vilevile tutahamasisha ujenzi wa viwanda vya kutengeneza dawa, vitendanishi, vifaa tiba pamoja na chanjo mbali mbali.

Kuhusu ugonjwa wa corona, kama mnavyofahamu, ugonjwa huu umeathiri dunia nzima na ubaya zaidi ni kwamba janga hili linapungua na kurudi katika mifumo tofauti tofauti. Mpaka sasa bado hakujawa na dalili za kupatikana kwa tiba ya maradhi haya. Njia pekee iliyopo ni kujikinga na kuchukua hatua mbali mbali za tahadhari. Hapa nchini tumekuwa tukifuata miongozo kadhaa ya kinga inayotolewa na wataalam, na kwa kutumia njia zetu za tiba asilia tumeweza kwa kiasi kikubwa kushusha kiwango cha maambukizi. Hapa nchini, tumeamua kuunda Kamati ya Wataalamu ambao kwa kushirikiana na taasisi za Afya Duniani na zile za Kikanda za EAC na SADC wataliangalia suala hili kwa undani, kufanya uchambuzi wa kina na kutoa mapendekezo ya hatua za kuchukua na jinsi ya kuendelea kupambana na maradhi hayo. Hivyo, wakati tukisubiri majibu ya Kamati iliyoundwa, napenda kutumia fursa hii kutoa wito kwa Watanzania kuendelea kuchukua tahadhari zote kama zinavyoshauriwa na wataalam. Nawaomba kila mmoja awajibike kwani ulinzi wa afya yako unaanza na wewe mwenyewe.

Kwenye Sekta ya ELIMU, katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, udahili wa wanafunzi katika ngazi za elimu Msingi na Sekondari uliongezeka kwa kiwango kikubwa kutokana na Sera ya elimu bila malipo. Ongezeko hilo limeilazimu Serikali kuweka nguvu kwenye ujenzi wa miundombinu ya elimu, kuongeza idadi ya walimu hasa walimu wa sayansi na hisabati, na kusambaza vitendea kazi mashuleni. Kumekuwa na ongezeko la kiwango cha mfuko wa elimu ya juu ambao umeongeza pia idadi ya vijana wanaoingia vyuo vikuu. Awamu ya sita itaendeleza kazi nzuri iliyofanywa miaka mitano iliyopita. Aidha tutajielekeza katika kufanya mapitio ya Sera ya Elimu ya mwaka 2014 na kufanya marekebisho kwenye Mitaala iliyopo ili ielekezwe kwenye kutoa elimu ujuzi kulingana na mazingira ya nchi na soko la ajira.

Kwa upande wa MAJI, licha ya mafanikio yaliyopatikana kwenye miaka mitano iliyopita; tatizo la maji bado ni kubwa kwenye maeneo mengi nchini. Hali hii inachangiwa na usimamizi usioridhisha wa miradi, na vile vile, matumizi mabaya ya fedha zinazotengwa kwa ajili ya upatikanaji wa maji safi na salama. Miradi mingi imekuwa ikitekelezwa kwa kutumia fedha nyingi; lakini baada ya muda mfupi maji hayapatikani. Hivyo basi, katika miaka hii mitano, tutaweka mkazo mkubwa katika kuimarisha usimamizi kwenye utekelezaji wa miradi ya maji. Na katika hilo, nakusudia kufanya mabadiliko makubwa kwa Wahandisi wa Maji wa Mikoa, ambao hawafanyi kazi vizuri. Lengo letu ni kufikia
azma ya kufikisha maji kwa wananchi kwa asilimia 95 mijini na asilimia 85 vijiji ifikapo mwaka 2025.

Lakini, ili kuweza kufikisha maji kwa Watanzania wengi, hatuna budi kuhakikisha tunalinda na kutunza vyanzo vyetu vya maji. Aidha, kwa maeneo yasiyokuwa na vyanzo vya maji, tutajielekeza katika ujenzi wa mabwawa ya kuvuna maji ya mvua. Vilevile, Kamati za Maji za Mitaa na Vijiji zinaimarishwa ziweze kutimiza majukumu yao ipasavyo. Zaidi ya hapo, tutatafuta vyanzo vingine vya kutunisha Mfuko wa Maji.

Mheshimiwa Spika;

Kwa upande wa Mahusiano na Ushirikiano na Mataifa mengine na Taasisi za Ki dunia, Serikali ya Awamu ya Sita imejipanga kutekeleza shughuli za Kidiplomasia kuendana na Sera ya Diplomasia ya Uchumi. Hivyo basi, tutaimarisha na kukuza Uhusiano na Mataifa mengine pamoja na jumuiya za kikanda na Taasisi za Kimataifa.

Ili kutimiza azma hiyo, tunakusudia kuimarisha utendaji kazi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki pamoja na Balozi zetu zilizoko nchi mbali mbali duniani, kwa kuajiri watumishi wenye sifa na weledi wa kazi na kusambaza vitendea kazi, pamoja na kutumia kiuchumi majengo na viwanja ambavyo ni mali ya Tanzania vilivyoko nje ya nchi. Kwa madhumuni ya kuwezesha utekelezaji mzuri wa Diplomasia ya Uchumi, tutafungua na kuanzisha pia Balozi mpya, Konseli pamoja na Vituo vya Biashara kwenye nchi na miji ya kimkakati ili kutangaza vivutio vyetu vya utalii, kuvutia uwekezaji na kutafuta masoko ya bidhaa zetu. Tutafanya uchambuzi wa kitaalamu utakaobaini nafasi ya kila ofisi ya ubalozi katika kukuza biashara, uwekezaji na utalii.

Uchambuzi huo ndio utatumika kupanga maafisa kulingana na uwezo wa kila Ubalozi.

Zaidi ya hapo, tutaendelea kushiriki kikamilifu kwenye shughuli za kimataifa, ikiwemo ushiriki wetu kwenye kulinda amani duniani. Tunakusudia pia kufanya mapitio ya Sera ya Mambo ya Nje ya mwaka 2000 ili iendane na mahitaji ya sasa ya dunia.

Mheshimiwa Spika;

Maeneo mengine ni pamoja na kuendelea kulinda misingi ya demokrasia na uhuru wa watu pamoja na vyombo vya habari. Kama mnavyofahamu, uhuru na demokrasia ni msingi wa amani katika nchi na pia vinasaidia kuchochea maendeleo ya kisiasa, kiuchumi na kijamii. Hata hivyo, naomba niseme kuwa, hakuna uhuru ama demokrasia isiyolindwa na kusimamiwa na Sheria, Taratibu na Kanuni. Hivyo basi, pamoja na demokrasia na uhuru wa watu, niwaombe Watanzania tujidhatiti kufanya shughuli zetu tukizingatia masharti ya sheria za nchi. Hapa nakusudia kukutana na Viongozi wa vyama vya Siasa Tanzania ili kwa pamoja tuweke mwelekeo wa kuendesha shughuli za kisiasa zenye tija na maslahi kwa nchi yetu.

Katika hatua nyingine, Tutashirikiana pia na Mhimili wa Mahakama katika kuimarisha mifumo ya utoaji haki, ikiwemo kuendelea kujenga miundombinu ya mahakama, kuongeza idadi ya majaji na mahakimu, na kukuza matumizi ya TEHAMA ili kuongeza kasi ya usikilizaji wa kesi na uwekaji mzuri wa kumbukumbu. Niombe Mahakama yetu na vyombo vya utoaji haki kuzielekeza zaidi nafsi zetu katika kutenda na kuhukumu yaliyo ya haki kwa wananchi. Na katika hilo, tutaendelea kuziimarisha taasisi nyingine za usimamiaji haki ikiwemo Ofisi ya Mwanasheria Mkuu, Wakili Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Polisi, TAKUKURU, Magereza, n.k.

Mheshimiwa Spika;

Serikali ya Awamu ya Sita kama ilivyokuwa awamu ya tano, itaendeleza jitihada za kuimarisha nidhamu na uwajibikaji kwenye utumishi wa umma. Tunakusudia kuimarisha taasisi na pia kuweka mifumo ya uwajibikaji, ambayo itahakikisha kwamba viongozi na watumishi wa umma katika ngazi zote wanawekewa malengo yanayopimika. Mfumo uliopo sasa ikiwemo mikataba kati ya kiongozi na walio chini yake pamoja na OPRAS tutaiangalia upya. Tutawapima viongozi na watumishi kwa namna wanavyotimiza majukumu yao. Hatutawaonea aibu viongozi na watumishi wazembe, wezi na wabadhirifu wa mali za umma. Tutaendeleza pia juhudi za kupambana na rushwa kwenye utumishi wa umma. Wajibu huu wa wafanyakazi wa umma ni lazima uendane na haki zao. Hivyo basi, tutasimamia mageuzi katika Utumishi wa Umma na kutazama maslahi ya watumishi, ikiwemo suala la upandishaji vyeo na mishahara.

Tutaendelea pia na jitihada za kuwawezesha wananchi kiuchumi, hususan wanawake, vijana na wenye ulemavu. Na katika hilo, tutaendelea kutoa mikopo ya asilimia 10 kupitia mapato ya ndani ya Halmashauri (wanawake asilimia 4, vijana asilimia 4 na wenye ulemavu asilimia 2) pamoja na kuimarisha Mifuko mingine ya Uwezeshaji Wananchi. Tutaendelea pia kuboresha mazingira ya kufanya biashara kwa wajasiriamali wadogo (machinga, mama lishe, baba lishe, waendesha boda, bajaji, n.k.), ikiwemo kwa kuwatengea maeneo mazuri ya biashara na kuwawekea miundombinu pamoja na kuviboresha Vitambulisho vyao ili viwe na taarifa muhimu zitakazowawezesha kuendesha shughuli zao kwa uhuru bila kubughudhiwa; lakini pia kutambulika kwenye Taasisi mbali mbali wanakofuata huduma.

Mheshimiwa Spika;

Sekta ya sanaa, michezo na utamaduni inakua kwa kasi kubwa hivi sasa. Vijana wetu wengi wamepata ajira kupitia sekta hii. Hivyo basi, kama ilivyoahidiwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020 – 2025, kwenye miaka hii mitano, tunakusudia kuikuza zaidi sekta hii, hususan kwa kuimarisha usimamizi wa masuala ya Hati Miliki ili wasaniii waweze kunufaika na kazi zao; tutahuisha Mfuko wa Utamaduni na Sanaa ili kuwasaidia wasanii wetu, ikiwemo kupata mafunzo na mikopo. Aidha, tutaanza kidogo kidogo kuanza kutenga fedha kwa ajili ya kuziandaa Timu zetu za Taifa, zikiwemo za wanawake. Tumechoka kuwa kichwa cha mwandawazimu kwenye michezo.

Masuala mengine ambayo yatapewa kipaumbele na Serikali ya Awamu ya Sita ni kuendeleza ujenzi wa Makao Makuu ya Serikali Jijini Dodoma. Aidha, kwa kuzingatia vigezo na sifa tutakuza usawa wa jinsia kwa kuwateua wanawake wengi zaidi kwenye nafasi mbalimbali za uongozi. Zaidi ya hapo, tutazidisha mapambano dhidi ya dawa za kulevya; uendelezaji na uboreshaji wa makazi wa wananchi, ambapo tutahakikisha vifaa vya ujenzi vinapatikana kwa gharama nafuu na mikopo ya ujenzi inapatikana kwa riba nafuu; tutaimarisha taasisi zetu za utafiti na kuendelea kushughulikia kero mbalimbali za wananchi, ikiwemo migogoro ya ardhi.

Tutaweka mkazo katika kushughulikia masuala ya Mazingira na Mabadiliko ya Tabianchi ili kupunguza athari zinazotokana na mabadiliko hayo kwa maisha ya watu na shughuli zao za kiuchumi na kijamii. Kitaifa, mbali na Sheria yetu ya Mazingira ya mwaka 2004, Bunge liliridhia Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi wa Paris. Tutaendelea kushirikiana na mataifa mbalimbali katika kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi. Tayari tumeandaa Mpango wa Utekelezaji wa Makubaliano ya Paris 2021-2026 unaolenga kujenga uwezo katika kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi katika sekta za kilimo, mifugo, misitu, nishati, uvuvi, maji, utalii, makazi, afya, miundombinu na pia kukabiliana na maafa.

Mheshimiwa Spika;

Ili kutimiza masuala hayo yote niliyoeleza, Bunge hili lina umuhimu wa pekee sana. Kama mnavyofahamu, mbali na kutunga sheria, Bunge lina wajibu wa kuisimamia Serikali. Aidha, ninyi Wabunge ni wawakilishi wa wananchi na kwa maana nyingine, ninyi ni sauti ya wananchi. Hivyo, sitegemei kuona Bunge hili likijieleza kujadili masuala ambayo hayana manufaa kwa Taifa letu. Na hili nalisema kwa vile natambua, bila ya ushirikiano wa Bunge hili, itakuwa vigumu sana kwa Serikali kuweza kutekeleza masuala yote niliyoyaeleza.

Hivyo basi, napenda kutumia fursa hii kuliomba Bunge hili Tukufu kutoa ushirikiano kwa Serikali. Tukoseeni pale inapobidi. Mawaziri wakileta vitu visivyoeleweka wakososolewe lakini kwa staha. Nami naahidi kuwa Serikali itakuwa tayari, wakati wote, kupokea ushauri wenu na pia ushauri wa watu wengine wenye nia ya kuiletea maendeleo nchi yetu. Nitumie pia fursa hii kuwaomba wananchi pia, kuendelee kuiunga mkono Serikali kwa kudumisha amani, kuchapa kazi kwa bidii na bila kusahau kulipa kodi, ili kwa pamoja tuweze kutimiza tuliyoyakusudia.

Mheshimwa Spika;

Kabla sijahitimiza hotuba yangu, naomba kueleza masuala mawili. Kwanza, naomba kutumia jukwaa hili la Bunge lako Tukufu kuwaonya wale wote wanaodhani kuwa usimamizi wa mali ya umma kwa maslahi ya wananchi, kukataa ukwepaji wa kodi, wizi, na kukemea uzembe vitasimama kwa sababu tu Rais Magufuli hayupo. Napenda kuwaambia kwamba wanajidanganya. Hatuko tayari kurudi nyuma. Kama mtu ana dhamira ya kuendeleza vitendo hivyo basi ni kwa gharama yake.

Pili, tangu kifo cha mpendwa wetu, Hayati Rais Dkt. Magufuli kumetokea tabia ya watu kuzusha maneno ya uchonganishi kwenye mitandao. Mtakumbuka kuwa, Serikali ilikwishatoa taarifa kwamba, Hayati Dkt. Magufuli alifariki kwa ugonjwa wa udhaifu wa moyo. Kwa hiyo, taarifa zinazotolewa kwenye mitandao kwamba kuna watu wamehusika ni uzushi mtupu. Hivyo basi, natoa onyo kwa watu wanaoeneza uzushi huo kuacha mara moja kwa vile Serikali itawatafuta kokote walipo.

Mheshimiwa Spika;

Hii ni mara ya kwanza kwenye historia ya Taifa letu kupata Rais Mwanamke. Kwa sababu hiyo, ninajua, watakuwepo baadhi ya watu wachache wenye wasiwasi kwamba kutokana na jinsia yangu sitoweza kuyatimiza yote niliyoyasema hapa. Nataka nitumie jukwaa hili kuwaondoa hofu kwamba kwanza, Mwenyezi Mungu hakuumba Ubongo hafifu kwa mwanamke na Ubongo wenye uwezo mkubwa kwa mwanaume. Makuzi na umakini wa akili hutegemea jamii inayokuzunguka na shughuli unazokuwa nazo. Nataka nikuhakikishieni kuwa nimekuzwa kwenye jamii sahihi na kwamba nina uzoefu wa kutosha kwenye Serikali na kwenye Chama changu cha Siasa CCM.

Hivyo basi, ninajiamini kuwa ninao uwezo wa kuliongoza Taifa hili. Pili, kazi hii sitoifanya peke yangu bali nitashirikiana na Watanzania wote. Wito wangu kwa Watanzania, tushirikiane, tushikamane na kuwa kitu kimoja katika kulijenga Taifa letu. Binafsi naamini, tukiwa na upendo, mshikamano na kuheshimiana, na kwa msaada wa Mwenyezi Mungu, tutaweza kufika kule ambako sote tunamani tufikie.


Baada ya kusema hayo Mheshimiwa Spika nimalizie kwa kumuomba Mungu alibariki Bunge hili pamoja na Wabunge wake! Mungu aibariki Tanzania!

Nawasalimu kwa jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.


“Ahsanteni sana kwa Kunisikiliza”


ssh3.jpg

ssh6.jpg

ssh5.jpg

ssh7.jpg

ssh4.jpg
 
Tuna mengi tunataka kuyasikia:

1. Kodi zinazozingatia hali halisi ya biashara.
2. Utawala wa sheria.
3. Mazingira rafiki kwa investors.
4. Mazingira wezeshi kwa wajasiriamali.
5. Ajira Mpya
6. Maisha bora kwa wafanyakazi.
7. Kupandisha kima cha chini cha mshahara bara kama Zanzibar.
8. Huduma bora za Afya.. Bima ya wote
9. Elimu bure yenye Tija.
10....
11.....
12.....
13......
 
Sawa.

Ngoja tusubiri.

Mama awazibe mdomo wale wanaompangia cha kusema. Naona kina Zitto kule Twitter wanatumia nguvu kubwa kutaka kuingiza ushawishi wa mama aseme nini leo.

Mtu yoyote mwenye akili anajua ATCL is there strategically. Sio kila kitu kwenye nchi lazima kitoe ama kiwe na faida.
 
24 Reactions
Reply
Back
Top Bottom