dubu
JF-Expert Member
- Oct 18, 2011
- 3,500
- 3,481
UTANGULIZI:
Naanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu; Mtukufu, Muumba wa Ulimwengu na vyote vilivyomo, kwa kuturuzuku neema ya uhai, afya na uwezo wa kukutana leo hii tarehe 5 Aprili, 2016, katika tukio hili muhimu kwa mustakbali wa nchi yetu na maendeleo ya wananchi wake.
Tunawaombea dua wenzetu waliotangulia mbele ya haki, Mwenyezi Mungu awasamehe makosa yao na awape malazi mema peponi. Kadhalika, kwa wale wenzetu waliopata mtihani wa maradhi mbali mbali, tunamuomba Mola wetu awape uzima, ili waendelee kushirikiana nasi katika shughuli za ujenzi wa Taifa letu.
Mheshimiwa Spika,
Tumekutana katika shughuli hii muhimu ya kulizindua Baraza la Wawakilishi la Tisa, tangu lilipoanzishwa miaka 36 iliyopita ikiwa ni hatua muhimu ya kukuza demokrasia, uwakilishi wa wananchi na kuimarisha utawala bora nchini. Tunamuomba Mola wetu atupe uwezo na hekima, ili tuweze kutumia busara na maarifa katika kutekeleza majukumu yetu ya kikatiba na kisheria kwa ajili mafanikio ya wananchi wa Zanzibar, kwa kuzingatia mamlaka kilichopewa chombo hiki muhimu, katika Sura ya Tano ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, pamoja na kanuni nyengine zinazoongoza Baraza hili.
Baada ya kumshukuru Mola wetu Subhana Wataala na kulitakia baraka Baraza letu la Tisa la Wawakilishi tunalolizindua leo, napenda niitumie fursa hii ili nimpongeze kwa dhati Mheshimiwa Zubeir Ali Maulid kwa kuchaguliwa kuwa Spika wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar. Kuchaguliwa kwako kwa kura nyingi kuongoza mhimili huu wa dola, ni kielelezo cha imani waliyonayo waheshimiwa wajumbe kwako kutokana na hekima, busara, uadilifu, taaluma na uzoefu wako. Hapana shaka wala khofu kuwa waheshimiwa wawakilishi watashirikiana nawe katika kuyatekeleza majukumu yako na kuleta ufanisi katika utendaji wa Baraza hili Tukufu.
Kadhalika, natoa shukurani kwa Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza hili la Wawakilishi, kwa kuamua kwa dhati kugombea nafasi ya ujumbe wa Baraza la Wawakilishi kwa lengo la kuja kuwatumikia wananchi wa Zanzibar. Aidha, nakupongezeni kwa kuchaguliwa na wananchi huku mkielewa kuwa ushindi huo una maana ya kuchukua dhamana ya kuwatumikia wananchi tunaowawakilisha na Wazanzibari wote. Wananchi waliokuchagueni wana imani na mategemeo makubwa kwenu katika kushirikiana nao kwenye suala zima la kuwaletea maendeleo. Mwenyezi Mungu akuwezesheni kuyakidhi matarajio hayo ya wananchi wetu. Naamini kwa dhati ya moyo wangu kwamba mtafanya kazi zenu kwa kushirikiana na kwa kuzingatia matakwa ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 na kanuni za Baraza la Wawakilishi.
Mheshimiwa Spika,
Kwa mara nyengine, natoa shukurani zangu za dhati kwa wananchi wote wa Zanzibar kwa kupiga kura kwa amani katika uchaguzi wa marudio hapo tarehe 20 Machi, 2016 na kukichagua Chama cha Mapinduzi na wagombea wake wote na tukashinda kwa kishindo. Wananchi waliitumia vyema haki yao ya kidemokrasia ya kuwachagua viongozi wao na hasa nyinyi Waheshimiwa Wawakilishi mnaounda Baraza la Tisa la Wawakilishi. Nakupongezeni sana kwa kuchaguliwa kwenu.
Kwa mara nyengine, natoa shukurani zangu za dhati kwa Chama changu, Chama cha Mapinduzi, kwa kuniamini na kuniteua, kukiwakilisha katika kuwaomba ridhaa wananchi wa Zanzibar ya kunichagua niwe Rais wa Zanzibar, katika uchaguzi wa tarehe 20 Machi, 2016. Natoa shukurani kwa CCM, Viongozi, Wanachama, Wapenzi wa CCM wa ngazi mbali mbali na wananchi kwa kuniunga mkono na kukiwezesha chama chetu kupata ushindi wa asilimia 91.4. Matokeo haya yamekiwezesha chama chetu kupata mamlaka ya kuunda tena Serikali, kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya 1984. Hatua hiyo, itatupa fursa ya kuitekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020 pamoja na sera na mipango mengine ya maendeleo ambayo tulianza kuitekeleza katika kipindi cha kwanza cha Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba.
Kadhalika, natoa shukurani kwa viongozi wa vyama vyote vya siasa vilivyoshiriki katika uchaguzi na kuheshimu uamuzi wa wananchi wa kuwachagua viongozi wao katika uchaguzi uliokuwa huru na haki. Aidha, shukurani zangu maalum nazitoa kwa vyombo vyote vya ulinzi na usalama vya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kusimamia ulinzi wa nchi yetu katika kipindi chote cha kabla ya uchaguzi, wakati wa uchaguzi hadi hivi leo. Vile vile, naipongeza Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC); kwa kutekeleza vyema majukumu yake ya kisheria na kikatiba, hali ambayo iliwawezesha wananchi kupata haki yao ya kupiga kura kwa amani, salama na utulivu mkubwa.
Mheshimiwa Spika,
Kwa sasa, uchaguzi umekwisha na wananchi wamekipa tena Chama cha Mapinduzi ridhaa ya kuiongoza Zanzibar. Nasaha zangu kwenu, Waheshimiwa Wawakilishi na wananchi wote, ni kuwa tuendeleze umoja wetu na mshikamano kwa maslahi ya wananchi wote bila ya ubaguzi wa aina yoyote kwani sote ni wamoja na uchaguzi usiwe chanzo cha kuhasimiana na kukwamisha malengo yetu ya kuongeza kasi ya maendeleo nchini.
KAZI ILIYO MBELE YETU
Mheshimiwa Spika,
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba, katika kipindi chake cha pili itaweka vipaumbele kwa sekta mbali mbali kwa kuzingatia Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya CCM ya mwaka 2015 – 2020 pamoja na ahadi nilizozitoa kwa wananchi, wakati nikiomba ridhaa ya kunichagua pamoja na wagombea wenzangu wa Chama cha Mapinduzi katika Uchaguzi Mkuu uliomalizika. Tuna kila sababu ya kushirikiana katika kutekeleza majukumu yetu, jambo ambalo ni muhimu katika kuimarisha huduma za jamii, amani, umoja na mshikamano baina yetu, pamoja na kutekeleza wajibu wetu wa kudumisha na kuendeleza shabaha ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya tarehe 12 Januari, 1964.
Katika kuelezea kazi iliyo mbele yetu, nitaeleza kwa ufupi tu pale ambapo itakuwa lazima kuyaeleza mambo tuliyoyafanya na tukapata mafanikio makubwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita; kwani mambo hayo nilikwishayaeleza kwa kina katika hotuba yangu niliyoiwasilisha wakati nilipolivunja Baraza la Nane la Wawakilishi tarehe 26 Juni, 2015.
UCHUMI
Mheshimiwa Spika,
Ukuzaji wa uchumi ni wajibu wa msingi wa Serikali ili iweze kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi na kuwaletea maendeleo. Ninashukuru kuona kwamba, tunaanza Kipindi cha Pili, cha Awamu hii ya Saba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (2015–2020), tukiwa tumepiga hatua kubwa katika kujenga misingi imara ya kuimarisha uchumi wetu. Katika kipindi cha miaka mitano ya kwanza, kasi ya ukuaji wa uchumi ilikua ni ya kuridhisha, ambapo katika mwaka 2015 uchumi wetu ulikua kwa asilimia 6.6. Kasi hii ya ukuaji Pato la Taifa imechangiwa zaidi na kuimarika kwa sekta ya huduma, sekta ya viwanda, kuongezeka kwa idadi ya watalii walioingia nchini pamoja na kuendelea kuwepo kwa hali ya amani na utulivu.
Pato la Taifa liliweza kuongezeka kutoka TZS bilioni 1,050.8 mwaka 2010 kufikia TZS bilioni 2,133.5 mwaka 2014, sawa na ongezeko la asilimia 103. Aidha, Pato la Mtu binafsi liliongezeka kutoka TZS 856,000 sawa na Dola za Kimarekani 613 mwaka 2010 hadi kufikia TZS milioni 1.552 sawa na Dola za Kimarekani 939 mwaka 2014. Kasi ya mfumko wa bei imeendelea kushuka kutoka asilimia 6.1 mwaka 2010 kufikia asilimia 5.6 mwaka 2014 na asilimia 5.7 mwaka 2015. Katika kipindi chote hicho, kasi ya mfumko wa bei iliendelea kudhibitiwa na kuwa katika wastani wa tarakimu moja.
Lengo la Serikali ninayoiongoza, ni kuhakikisha kuwa kasi ya ukuaji wa uchumi inafikia asilimia 8-10 katika miaka mitano ijayo. Shabaha yetu tufikie kiwango cha uchumi wa nchi zenye kipato cha kati, kama ilivyoelekezwa na kusisitizwa katika Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya CCM ya mwaka 2015-2020, Dira ya Maendeleo 2020 pamoja na mipango mingine ya maendeleo.
Tutahakikisha kwamba tunaimarisha ustawi wa wananchi kwa kuongeza zaidi Pato la Mtu binafsi kutoka kiwango tulichokifikia hivi sasa, cha wastani wa TZS milioni 1.552 sawa na Dola za Kimarekani 939 hadi kufikia kiwango cha Pato la Mtu binafsi kwa nchi zenye kipato cha kati ambacho kinaanzia Dola za kimarekani 1,046.
Katika kipindi cha mwaka 2010/2011 hadi mwaka 2014/2015, tumeweza kwa kiasi kikubwa kuongeza ukusanyaji wa mapato kutoka TZS bilioni 181.4 hadi TZS bilioni 362.8, sawa na ukuaji wa asilimia 100 kwa kipindi hicho. Haya ni mafanikio makubwa na napenda kutumia fursa hii kuipongeza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) kwa juhudi kubwa walizochukua za kuimarisha ukusanyaji wa Mapato.
Dhamira ya Serikali katika kipindi hiki cha pili, cha Awamu ya Saba ni kuongeza ukusanyaji wa mapato ya ndani kutoka TZS bilioni 362.8 mwaka 2014/2015 hadi kufikia TZS bilioni 800 ifikapo mwaka 2020/2021. Waheshimiwa Wajumbe tuna wajibu na kazi kubwa ya kufanya ili tuweze kuyafikia malengo hayo na Zanzibar iweze kwenda sambamba na kasi ya ukuaji wa uchumi wa nchi nyingi zinazoendelea.
Mheshimiwa Spika,
Licha ya mafanikio makubwa tuliyoyapata katika ukusanyaji wa Mapato, imani yangu ni kuwa bado tunaweza kuongeza ukusanyaji wa mapato kwa kiasi na kwa kasi kubwa zaidi. Matumaini yangu ni kuwa katika kipindi cha pili, watendaji wa Taasisi zetu muhimu za kukusanya mapato hasa Bodi ya Mapato ya Zanzibar (ZRB), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Taasisi zilizoko bandarini, viwanja vya ndege na Wizara zenye vyanzo vya mapato wataongeza kasi katika kusimamia majukumu yao, wakitambua kuwa Serikali itakuwa inafuatilia utendaji wao kwa karibu na kwa umakini zaidi. Ufanisi katika mambo hayo ndio utakaotuwezesha kuyafikia malengo tuliyojiwekea katika Dira ya Maendeleo ya mwaka 2020.
Hatua hii itakuwa muhimu katika kupunguza utegemezi wa wahisani hatua kwa hatua ili baadae tuweze kujitegemea katika kupanga na kutekeleza mipango yetu ya maendeleo katika miaka ijayo. Tutafanya kila tuwezalo liliomo kwenye uwezo wetu ili tufanikiwe. Tumeamua kubana matumizi kwa kuyaondoa na kutoyafanya mambo ambayo si ya lazima.
Katika kipindi hiki, tutajitahidi kupanga vipaumbele vichache vinavyotekelezeka kwenye wizara zetu, kwa kutumia uwezo tulio nao na mapato yetu. Tunataka tuanze kujitegemea na hilo ni lazima tuliweze. Nataka Mawaziri na Makatibu Wakuu washirikiane katika kulifanikisha jambo hili. Tutaendelea kupokea misaada kutoka kwa wahisani wetu pale tutakapopewa na tutashirikiana nao kwa ajili ya maendeleo yetu.
Mheshimiwa Spika,
Mipango yote ya nchi yetu, inasimamiwa na kuratibiwa na Tume ya Mipango ya Zanzibar. Katika mwaka 2015, Serikali kupitia Tume ya Mipango imeratibu mapitio ya Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini (MKUZA II) unaomaliza muda wake mwezi wa Juni 2016. Kazi hii inafanywa kwa kuwashirikisha wahusika mbali mbali kuhakikisha kuwa mpango wa muda wa kati ujao, unakuwa wenye ufanisi zaidi. Serikali itaanza kutumia rasmi mkakati huo mpya, kuanzia bajeti ya mwaka 2016/17.
Mkakati huo utaendeleza mageuzi ya kiuchumi na kijamii ili kutuwezesha tufikie uchumi wa kipato cha kati ifikapo mwaka 2020. Katika kipindi hiki hadi mwaka 2020, mkakati utajikita katika kuimarisha uchumi endelevu kwa kukuza uzalishaji kwenye sekta ya kilimo, utalii na viwanda vidogo vidogo. Vile vile, mkakati huo utaimarisha rasilimali watu, ubora wa huduma za jamii ikiwemo elimu, afya, mazingira endelevu na misingi imara ya utawala bora.
MIRADI YA MASHIRIKIANO BAINA YA SEKTA YA UMMA NA SEKTA BINAFSI (PPP)
Mheshimiwa Spika,
Serikali inatambua umuhimu wa kuishirikisha Sekta Binafsi katika kuleta na kusimamia maendeleo ya kijamii na kiuchumi. Miradi ya PPP, itaongeza ajira, uimarishaji wa huduma na ukuaji wa uchumi. Kadhalika, hii ni njia bora ya kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa fedha za kuendeshea miradi. Ili kuleta ufanisi kwa miradi ya PPP, Serikali imefuta Sheria Namba 1 ya mwaka 1999 ya Miradi ya Maridhiano na imetunga Sheria mpya ya PPP; Namba 8 ya mwaka 2015.
Katika kipindi cha miaka mitano ijayo, Serikali itatekeleza Miradi ya PPP, baada ya kuifanyia Upembuzi Yakinifu miradi 10 ya awali ikiwemo Ujenzi wa Kituo cha daladala Kijangwani, Mradi wa Uendelezaji wa Soko la Mwanakwerekwe, Mkokotoni, Kinyasini, Soko la Mombasa kwa Unguja na Kengeja kwa Pemba. Miradi mengine ni Kituo cha Mikutano cha SUZA, Mradi wa Ujenzi wa Nyumba katika Mji Mkongwe pamoja na Mradi wa Hifadhi ya Mji wa Ng’ambo. Kadhalika, miradi mengine itakayotekelezwa ni Kuendeleza Vivutio vya Utalii katika eneo la Bandari ya Malindi, Uanzishwaji wa Kituo cha Usarifu wa Mazao, Kuanzishwa kwa Viwanda vya Usarifu wa Mazao ya Baharini, Kuendeleza Viwanja vya Ndege pamoja na Ujenzi wa viwanja vya michezo ya aina mbali mbali. Ninaihimiza na ninaishajiisha Sekta Binafsi ijiandae kutumia fursa hizo kikamilifu.
MATOKEO KWA USTAWI (RESULTS FOR PROSPERITY-R4P)
Mheshimiwa Spika,
Katika utekelezaji wa Mpango wa Matokeo kwa Ustawi, mnamo mwaka 2014, Serikali iliandaa programu maalum za utekelezaji wa shughuli mbali mbali kupitia utaratibu wa Maabara katika Sekta ya utalii, Uimarishaji wa biashara na Upatikanaji wa rasilimali fedha. Utekelezaji wa programu hizi umefikia hatua ya Kukamilika kwa Sera na Sheria ya Mashirikiano baina ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi, Kuandaliwa kwa Rasimu ya Mkakati wa Mawasiliano ya Utalii, Kuanzishwa kwa mchakato wa Mfumo wa Kisasa wa Upatikanaji wa Soko kwa kutumia Mtandao unaotegemewa kuwa na lugha 5 za Kimataifa, pamoja na Kukamilika na Kuidhinishwa kwa Mpango Mkuu wa Matumizi ya Ardhi.
Hatua nyengine ni kuandaliwa kwa Rasimu ya Awali ya Mapendekezo ya Sera ya Maendeleo ya Wajasiriamali, kutayarishwa kwa Rasimu ya Mapitio ya Sheria ya Uwekezaji ambayo inaendelea kufanyiwa kazi pamoja na kuanza kwa matayarisho ya ununuzi wa Mashine za Kisasa za Kutolea Risiti (EFD) kwa lengo la uimarishaji wa ukusanyaji wa mapato. Kwa sasa, Serikali imo katika matayarisho ya Maabara ya elimu na afya zinazotarajiwa kufanyika mwaka huu. Serikali imejiandaa vya kutosha katika kutekeleza programu zitakazoibuliwa na matokeo yatakayoafikiwa na wataalamu katika maabara, kwa sekta nyenginezo, katika kipindi chote cha miaka mitano ijayo. Programu hizo zitaleta msukumo na kuongeza ufanisi katika juhudi zetu za kukuza uchumi, ajira na kupunguza umasikini.
UWEKEZAJI VITEGA UCHUMI
Mheshimiwa Spika,
Katika kuendeleza juhudi za kukuza uchumi, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kupitia Mamlaka ya Ukuzaji Vitega Uchumi Zanzibar (ZIPA), imeweza kuitangaza Zanzibar kama kituo muhimu kwa wawekezaji, ndani na nje ya nchi. Zanzibar imeweza kuwavutia wawekezaji katika miradi mbali mbali ya gharama kubwa kutokana na fursa za uwekezaji zilizopo, mazingira mazuri kwa wawekezaji na biashara, pamoja na kuimarika kwa utawala bora nchini.
Mheshimiwa Spika,
Katika kuendeleza juhudi za kuvutia uwekezaji katika Maeneo Huru ya Uchumi ya Fumba, Serikali imefunga mkataba na Bakhresa Group of Companies ili kujenga miundo mbinu katika eneo ambalo Mpango Mkuu wa Uwekezaji umeshaidhinishwa katika kipindi hiki cha miaka 5. Jumla ya kilomita 13 za barabara kuu zimeanza kujengwa ambazo zitagharimu jumla ya TZS. bilioni 15.6 na barabara ndogo zenye urefu wa kiasi cha kilomita 20 zitajengwa kwa kiwango cha lami zitakazogharimu TZS. bilioni 20.
Jumla ya miradi mikubwa mitano (5) itajengwa kwenye eneo hilo, katika kipindi hiki. Miradi hiyo ni ujenzi wa Miji ya Kisasa wa Kibiashara “Fumba Satellite City” katika eneo la Fumba, ujenzi wa Mji wa kisasa wa Makaazi “Fumba Town Development” katika eneo la Nyamanzi, ujenzi wa Mji wa kisasa wa Nyumba za Biashara na Makaazi pamoja na ujenzi wa Maeneo ya Kupumzikia Watu “Fumba Uptown Living” katika eneo la Fumba.
Vile vile, eneo lenye ukubwa wa hekta 102 limetengwa huko Fumba, kwa ajili ya ujenzi wa viwanda ambapo viwanda viwili vya ujenzi wa nyumba katika vijiji vya Kororo na Nyamanzi tayari vimeshajengwa. Aidha, mtambo wa lami umeshafungwa katika eneo la Kororo na kiwanda cha maziwa kimeshaanza kazi. Katika uimarishaji wa eneo hili, vile vile, kitajengwa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa na eneo maalum la kiuchumi pamoja na Gati ya mizigo na abiria.
Vile vile, Kampuni ya S.S. Bakhresa “Group of Companies” tayari imepata ruhusa na inaendelea na hatua mbali mbali za uwekezaji mkubwa katika maeneo ya Mtoni Marine - Maruhubi. Mradi huo unajumuisha ujenzi wa Hoteli kubwa ya nyota tano; Maeneo ya michezo ya maji (Water Park); “Marina” na kujenga Kisiwa chenye nyumba za watu wenye kipato cha juu (Chapwani Paradise Island) Kusini mwa Kisiwa cha Chapwani.
Mheshimiwa Spika,
Kwa upande wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Mradi wa ujenzi wa mji wa kisasa wa kibiashara pamoja na hoteli kubwa ya nyota tano umekwishaanza kutekelezwa huko Matemwe na unatarajiwa kugharimu jumla ya Dola za Marekani milioni 800. Kampuni ya “Pennyroyal ya Gibralter” ndiyo inayotekeleza mradi huo.
Aidha, mnamo mwezi wa Novemba 2015, Serikali ilifunga Mkataba na Kampuni ya “Quality Group Limited” ambayo itaanzisha mradi mkubwa wa kuendeleza Hoteli ya Bwawani na maeneo yaliyoizunguka. Mradi huo utawekeza mtaji wa Dola za Marekani kiasi cha Milioni 200 na utahusisha kulifanyia matengenezo makubwa jengo la Hoteli ya Bwawani na kuwezesha upatikanaji wa huduma za hoteli za nyota tano. Jengo hili la hoteli litaimarishwa ili kuhifadhi kielelezo cha mafanikio cha Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya 1964. Majengo ya biashara ya ghorofa na maduka makubwa ya kisasa (Shopping malls) yatajengwa pamoja na Kituo cha Mikutano ya Kimataifa, Maeneo ya Michezo na Soko la Bidhaa zinazozalishwa Zanzibar.
Ni matumaini yangu kwamba Wajumbe wa Baraza hili, mtashirikiana na Serikali katika kuhakikisha mipango hii muhimu ya uwekezaji inatekelezwa ipasavyo na malengo ya Zanzibar ya kuwa na uchumi wa kati yanafikiwa kwa manufaa ya nchi yetu na watu wake.
Mheshimiwa Spika,
Katika kipindi cha miaka mitano ijayo, Serikali kupitia Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF) itaendelea na ujenzi wa nyumba za kisasa uliokwishaanza katika eneo la Mbweni - Unguja, ambao unajumuisha majengo 18 ya ghorofa 7 kila moja. Majengo hayo yatakapomalizika yatakuwa na jumla ya vyumba 252. Ujenzi huu unatarajiwa kukamilika katika kipindi cha miaka mitatu. Vile vile, kwa kushirikiana na Umoja wa Watu Wenye Ulemavu Zanzibar (UWZ), ZSSF itajenga nyumba 128 za gharama nafuu katika eneo linalomilikiwa na umoja huo wa UWZ lilioko Mombasa - Zanzibar.
Zaidi ya hayo, Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (ZSSF), italifanyia matengenezo makubwa jengo la ‘CHAWAL’ tunaloliita “Jumba la Treni” liliopo Darajani. Ujenzi huu unategemewa kuanza hivi karibuni. Aidha, Serikali inaandaa mpango na inaendelea na mazungumzo na wawekezaji mbali mbali kwa ajili ya kuliendeleza eneo la Darajani kwa ujenzi wa maduka makubwa ya kisasa ya biashara.
Kwa upande wa eneo la Michenzani, Serikali kupitia ZSSF imeandaa awamu ya pili ya mradi wa uimarishaji wa eneo la hilo baada ya kukamilika kwa Mnara wa kumbukumbu ya Miaka 50 ya Mapinduzi na bustani yake. Serikali imejipanga kujenga maduka ya kisasa (shopping malls) na sehemu za kupumzikia katika eneo hilo.
Mheshimiwa Spika,
Wahenga walisema, “Ukipata chungu kipya, usitupe cha zamani”. Katika kipindi kijacho, Serikali itahakikisha inachukua hatua madhubuti katika kuuhifadhi Mji Mkongwe, ili uendelee kuwa kivutio cha utalii na kubakia katika orodha ya Mji wa Urithi wa Dunia. Tutaendelea kuyafanyia ukarabati majengo mbali mbali ya kihistoria. Vile vile, tutakamilisha mradi wa ZUSP wa ujenzi katika eneo la Mizingani, utiaji wa taa za barabarani katika barabara mbali mbali, ujenzi wa misingi ya maji machafu katika Mji wa Unguja, Mji wa Chake chake, Wete na Mkoani kwa Pemba. Kupitia Baraza hili Tukufu, nataka niwahimize viongozi wa Manispaa, Mabaraza ya Miji, Halmashauri za Wilaya, Mamlaka ya Mji Mkongwe na Taasisi zote zinazoshughulika na usafi wa Miji na usimamizi wa biashara, waongeze jitihada katika kuimarisha usafi wa Mji na kusimamia sheria na nidhamu ya uendeshaji wa shughuli za biashara. Usafi ni jambo la lazima katika maisha yetu na hapana mbadala wake. Kwa hivyo, wale wote waliopewa dhamana ya kusimamia usafi katika Miji yetu, wajue kuwa wanachukua dhamana kubwa na watawajibishwa endapo watashindwa kutimiza wajibu wao katika kipindi hiki.
UIMARISHAJI WA MIJI KWA KUZINGATIA MKAKATI WA MATUMIZI YA ARDHI ZANZIBAR - 2015
Mheshimiwa Spika,
Katika mwaka 2015, tulikamilisha Mkakati wa Matumizi ya Ardhi Zanzibar (National Spatial Development Strategy - 2015). Katika Mkakati huu, Miji Kumi na Nne (14) itapangwa, ikiwemo Mji wa Zanzibar, Chake-Chake, Wete, Mkokotoni, Konde na Kengeja. Kati ya Miji hiyo, Serikali imekamilisha mipango ya miji mitano ambayo ni Mji wa Zanzibar, Nungwi, Mkokotoni, Chwaka na Makunduchi. Matayarisho ya mipango ya miji ya Chake-Chake na Wete imeshaanza.
Vile vile, katika mwaka uliopita, Serikali ilikamilisha Mpango Mkuu wa Mji wa Zanzibar. Katika Mpango huo, Serikali imeamua kuanzisha eneo jipya la Biashara na Utamaduni. Eneo lote kutoka Darajani hadi Kariakoo na kutoka Maisara hadi Kinazini litapagwa upya ili kuanzisha ujenzi wa nyumba za ghorofa, kuweka kituo kipya cha mabasi, kuongeza sehemu mpya za maduka na biashara na kujenga sehemu mpya za bustani. Aidha, Mji wa Zanzibar utakuwa na miji mitatu mipya; Chuini kwa upande wa Kaskazini, Tunguu kwa upande wa Mashariki na Fumba kwa upande wa Kusini. Mipango hii inafanywa kuhakikisha kuwa Zanzibar inaendelea ikiwa na uwiyano wa kiuchumi, kijamii na kimazingira, ili kufikia lengo lake la Milenia na kuelekea katika Malengo Mapya ya Maendeleo Endelevu (Sustainable Development).
BIASHARA
Mheshimiwa Spika,
Sekta ya biashara ina umuhimu mkubwa kwa kuchochea maendeleo na kukuza ajira kwa watu wa Zanzibar. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika awamu zote imekuwa ikichukua hatua za kuiimarisha na kuiiongezea ufanisi sekta hii. Katika kipindi cha pili, cha Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Saba, Serikali itahakikisha kuwa inaendelea kuimarisha mazingira na wepesi wa kuendesha shughuli za biashara hapa Zanzibar. Nitahakikisha kuwa tunafanikiwa kukuza biashara za ndani, biashara kati ya Zanzibar na Tanzania Bara na kati ya Zanzibar na nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na Mataifa mengine ya nje. Lengo letu ni kuongeza bidhaa zitakazouzwa Tanzania Bara ili zivuke kiwango cha mwaka 2014/15, cha bidhaa zenye thamani TZS. Milioni 2,203.8. Kadhalika, tuvuke kiwango cha bidhaa zenye thamani ya TZS. milioni 133,591.7 zilizosafirishwa kwenda nchi za nje mwaka 2014/2015.
Ili kuyafikia malengo hayo, Serikali itaendelea kutoa elimu kwa wafanyabiashara juu ya fursa zilizopo na utumiaji mzuri wa masoko yaliyopo Tanzania pamoja na Jumuiya za Kiuchumi ambazo Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni mwanachama. Serikali itaanzisha ujenzi wa Kituo cha Biashara cha Kimataifa katika eneo la Nyamanzi na itaendelea kuwahamasisha wafanyabiashara na wajasiriamali wa Zanzibar ili washiriki katika maonesho ya biashara ya Kimataifa yatakayofanyika hapa Zanzibar na nchi mbali mbali.
Katika kudhibiti ubora wa bidhaa na huduma zinazotolewa na wananchi, Serikali itaimarisha Taasisi ya Viwango ya Zanzibar iliyoanzishwa kwa mujibu wa Sheria Namba 1 ya Viwango ya Zanzibar ya mwaka 2011, kwa kuanza ujenzi wa Ofisi na Maabara ya kisasa katika eneo la Maruhubi ili kuimarisha ufanisi wa taasisi hiyo.
Mheshimiwa Spika,
Kwa kutambua umuhimu wa zao la karafuu kwa uchumi na historia ya Zanzibar na watu wake, Serikali inaendeleza juhudi mbali mbali za kuliimarisha zao hili. Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, tumepata mafanikio makubwa katika kulifufua zao hilo. Tulianzisha mpango maalum wa miaka 10 wa kulifufua na kuliendeleza zao hili na kwa kulifanyia mageuzi makubwa Shirika la ZSTC ambalo kwa sasa linaendeshwa kwa ufanisi mkubwa.
Kwa mara nyengine, nawaahidi wananchi kuwa Serikali itaendelea kuwalipa wakulima wa karafuu asilimia 80 ya bei ya karafuu ya soko la dunia kama nilivyoahidi katika kipindi kilichopita. Serikali itaendelea kuwapa mikopo na miche wakulima kutoka kwenye vitalu tulivyovianzisha. Tutaendeleza vita dhidi ya magendo na tutaendelea kuliimarisha Shirika la ZSTC, ili liendelee kusimamia vizuri biashara ya karafuu na viungo vyengine ili lijiendeshe kibiashara na liendelee kupata faida. Wito wangu kwa wananchi na wakulima wa karafuu ni kuwa, tushikamane katika kuyaendeleza mafanikio haya. Vile vile, Serikali itaendeleza ujenzi wa barabara za ndani zinazoelekea kwenye maeneo yenye karafuu nyingi. Jumla ya barabara nne zitajengwa kwenye maeneo mbali mbali katika kipindi hiki.
Mheshimiwa Spika,
Katika kipindi hiki, Serikali itaendeleza utaratibu wa kudhibiti ubora wa karafuu za Zanzibar (Branding) ili kumnufaisha mkulima wa zao la karafuu. Hatua ya awali ya vyeti vya kudhibiti ubora kutoka “TBS” na “Tan-cert” umepatikana. Usajili utapangwa kwa wakulima pamoja na wanaojishughulisha na biashara ya zao la karafuu kwa ajili ya kuwawezesha kwa kuwapatia misaada mbali mbali. Jitihada zitafanywa ili waweze kuendesha shughuli zao kwa ufanisi pamoja na kuwalipa fidia wale wanaopata ajali katika uchumaji wa karafuu. Shirika litaweka utaratibu wa kuwepo kwa karafuu kwa mfumo wa kilimo hai (Organic cloves).
Mazao mengine ya mfumo wa kilimo hai tayari yameshaandaliwa utaratibu wake. Mazao hayo ni Pilipili hoho, Pilipili manga, na Mdalasini kazi ya kutoa elimu ya ulimaji wa mazao hayo inaendelea. Maeneo ambayo yamepatiwa elimu hai ni Matemwe (Pilipili hoho) na Dayamtambwe na Gando (Mdalasini na Pilipili manga).
VIWANDA
Mheshimiwa Spika,
Nafahamu kwamba, tunaanza kipindi cha pili cha Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba ikiwa bado tumekabiliwa na changamoto nyingi katika kuiendeleza sekta ya viwanda. Miongoni wa sababu za kuwepo kwa changamoto hizo ni uchache wa rasilimali tulizonazo hapa Zanzibar ambazo zingeweza kutumika zikiwa ni malighafi kwa kuendeleza viwanda vya aina mbali mbali. Wakati wa kampeni za Uchaguzi wa mwaka 2015, katika nyakati mbali mbali nilielezea kuhusu juhudi pamoja na mipango yetu ya kuendeleza viwanda, hasa viwanda vya kusindika samaki, mazao ya kilimo na mifugo, viwanda vya ushoni na viwanda vyengine vidogo vidogo.
Nataka niwahakikishie wananchi kuwa katika kipindi cha miaka mitano ijayo, nitasimamia utekelezaji wa ahadi hiyo niliyoitoa wakati wa Kampeni huku tukishirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tutazidisha kasi ya kutafuta wawekezaji wenye mitaji mikubwa, uwezo na dhamira ya kweli ya kujenga viwanda katika eneo huru la huko Micheweni vitakavyokuwa na uwezo mkubwa wa kutoa ajira kwa vijana wetu, kama tulivyokwishaanza kwa eneo la Fumba. Kadhalika, Serikali itaendeleza viwanda katika Maeneo Maalum ya Kiuchumi (SEZ) na kuwavutia wawakezaji wenye mitaji mikubwa kuwekeza katika miundombinu ya viwanda vinavyotoa ajira kwa wingi.
UTALII
Mheshimiwa Spika,
Ni jambo la kutia moyo kuona kwamba tumemaliza miaka mitano ya kwanza tukiwa tumepata mafanikio makubwa katika kuiendeleza sekta ya utalii ambayo hivi sasa ndiyo sekta kiongozi katika uchumi wetu. Jitihada zetu za kuendeleza utalii kwa wote na kufikia azma yetu ya kuufanya utalii kuwa sekta kiongozi ya uchumi, zimeweza kuzaa matunda. Tumeweza kuongeza idadi ya watalii, kutoka 132,836 mwaka 2010 hadi kufikia 311,891 mwaka 2014. Hata hivyo, idadi ya watalii waliotembelea Zanzibar katika mwaka 2015 ni 294,243.
Katika kipindi cha miaka mitano ijayo, tutaongeza kasi ya kuiimarisha sekta ya utalii ili tuweze kulifikia lengo lililobainishwa katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015 – 2020, la kufikia idadi ya watalii 500,000, wanaoitembelea Zanzibar kwa mwaka, ifikapo mwaka 2020. Serikali itaongeza kasi ya utekelezaji wa Matokeo kwa Ustawi (Results for prosperity), mafanikio ya utalii kwa wote, kushajiisha ushiriki wa wananchi katika sekta ya utalii na kuhusisha sekta zetu zote za kiuchumi na shughuli za utalii. Serikali itaongeza kasi katika kuvitangaza vivutio vyetu vya utalii pamoja na uzuri wa Zanzibar na ukarimu wa watu wake katika masoko mapya katika Bara la Ulaya, Marekani, Mashariki ya Kati na Mashariki ya Mbali.
Mheshimiwa Spika,
Tutaendelea kuwashajiisha wawekezaji ili waje wawekeze katika ujenzi wa hoteli za kisasa na utoaji wa huduma huku tukiwa tumeelekeza nguvu kubwa katika kuimarisha utalii unaozingatia hifadhi ya mazingira na kuulinda utamaduni wetu. Katika kipindi hiki, Chuo cha Utalii cha Maruhubi kitaunganishwa na Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), ili kuimarisha utoaji wa mafunzo ya utalii kwa kutoa shahada za fani mbali mbali. Mafunzo haya yatasaidia katika kuimarisha sekta ya utalii na kuongeza ajira za vijana.
Katika kipindi cha miaka mitano ijayo, Serikali itaongeza juhudi za kuziimarisha sehemu za kihistoria na kufanya matengenezo ya Makumbusho pamoja na kufanya uhifadhi wa mapango ya asili kwa lengo la kuyatunza na kuchochea shughuli za utalii. Kadhalika, Serikali itaendeleza utekelezaji wa Mpango wa Uhifadhi wa Mambo ya Kale na kuanzisha Taasisi ya Nyaraka na Kumbukumbu za Kale pamoja na vituo vya kuhifadhia kumbukumbu katika kila Mkoa.
KILIMO
Mheshimiwa Spika,
Sekta ya kilimo ina umuhimu mkubwa na inachangia asilimia 31 katika Pato la Taifa (GDP). Kilimo huchangia katika kuwawezesha wananchi walio wengi kujikimu kimaisha na kuwapatia uhakika wa chakula na lishe bora. Sekta ya kilimo ilipata mafanikio makubwa katika kipindi kilichopita kutokana na utekelezaji wa miradi na programu mbali mbali za kilimo. Tutayaendeleza mafanikio pamoja na kuzitafutia ufumbuzi changamoto zinazoendelea kuwakabili wakulima wetu. Katika kipindi cha miaka mitano ijayo, Serikali itaendelea kuimarisha sekta ya kilimo kwa kuendelea kutoa ruzuku ya asilimia 75 ya gharama za pembejeo za kilimo na huduma za matrekta kwa wakulima kama tulivyoanza katika kipindi cha kwanza. Aidha, Serikali itaendeleza programu za mapinduzi ya kilimo na usimamizi wa rasilimali za misitu na kuongeza idadi ya mabwana/mabibi shamba kutoka 172 mwaka 2014 hadi kufikia mmoja kwa kila shehia ifikapo mwaka 2020. Vile vile, tutaendeleza mafunzo kwa wakulima na kutilia mkazo matumizi ya kanuni za kilimo bora katika uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara pamoja na matumizi ya zana za kisasa.
Vile vile, kilimo cha mpunga cha umwagiliaji maji kitaimarishwa kwa kuzingatia Mpango Mkuu wa Kilimo cha Umwagiliaji maji na kuimarisha eneo la hekta 2,105 za miundo mbinu ya umwagiliaji maji katika bonde la Cheju, Kilombero na Chaani kwa Unguja, Mlemele na Makwararani kwa Pemba. Maeneo hayo yanategemewa kuzalisha tani za mpunga 25,260 ifikapo 2018. Katika miaka mitano ijayo, minazi na mikarafuu itapandwa zaidi pamoja na uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara hasa manjano, hiliki, tangawizi, pilipili manga, kungu manga, kilimo cha alizeti na kuanzisha mazao mapya ya biashara. Kadhalika, vituo vya huduma za udhibiti wa maradhi vitaimarishwa, hasa vya mazao, wadudu waharibifu pamoja na ukaguzi na karantini dhidi ya maradhi na wadudu waharibifu wa mimea na mifugo ili kudhibiti maradhi ya mimea na mifugo hapa Zanzibar.
Mheshimiwa Spika,
Vile vile, Serikali itaendeleza utafiti wa mbegu za mazao ya chakula, biashara, mboga na matunda na kuhakikisha kwamba matumizi ya takwimu na matokeo ya utafiti huo, yanawafikia wakulima na yanatumika katika kufanya uamuzi. Katika kipindi hiki, eneo la Kibonde mzungu, litaandaliwa kwa kilimo cha mbegu za mpunga. Kadhalika, Chuo cha Kilimo Kizimbani, kitaimarishwa ili kiongeze idadi ya wataalamu wa kilimo na mifugo nchini kwa kukiunganisha na Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), ili kiweze kutoa masomo ya shahada kwa kuwa Chuo Kikuu Kishiriki. Vile vile, Serikali katika kipindi hiki itasimamia utekelezaji wa Sheria ya Hifadhi ya Taifa ya chakula ili kujikinga na baa la njaa na ukosefu wa chakula na lishe. Maghala ya kuhifadhia chakula matatu (3) yatakamilishwa katika kipindi hiki na kuanza kutumika.
Kadhalika, Serikali itaihamasisha sekta binafsi ijenge viwanda vya usarifu wa mazao, ili kuongeza thamani na ubora wa mazao ya mboga na matunda, na kadhalika, ili kukuza kipato cha wakulima na kurahisisha upatikanaji wa soko. Serikali imetiliana saini Mkataba na Kampuni ya Mahindra-Mahindra ya India kwa ajili ya ununuzi wa matrekta mapya katika kipindi hiki. Taratibu za ununuzi wa matrekta hayo tayari yameanza. Vile vile, kiwanda cha matrekta cha Mbweni kitatumika kwa ajili ya kuyaunganisha matrekta ya Mahendra ili baadae yauzwe kwenye soko la nje yakisafirishwa kutokea Zanzibar.
MIFUGO
Mheshimiwa Spika,
Sekta ya ufugaji inaendelea kuwa na mchango mkubwa katika kukuza uchumi na kutoa ajira kwa wananchi wengi wa Unguja na Pemba. Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba, katika kipindi chake cha kwanza iliiendeleza sekta ya ufugaji kwa kauli mbiu ya “Mapinduzi ya Ufugaji”, yaliyolenga kuwa na ufugaji wenye tija na kuongeza ubora wa mazao ya mifugo. Sekta ya ufugaji inakabiliwa na changamoto ya uhaba wa ardhi kutokana na kuongezeka kwa idadi ya watu na kupanuka kwa shughuli za maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Katika kipindi cha miaka mitano ijayo, Serikali itaendelea kuhimiza na kuimarisha ufugaji wa ng’ombe wa maziwa na nyama, ufugaji wa mbuzi pamoja na kuku wa nyama na mayai, ili kuongeza tija na kipato cha wafugaji. Katika kulifanikisha lengo hilo, Serikali itasimamia utekelezaji wa sera, sheria na programu mbali mbali za elimu kwa wafugaji, ili kuwawezesha wafugaji wadogo kutekeleza kanuni za ufugaji wa kisasa na kuongeza uzalishaji wa mazao ya mifugo kwa lengo la kukidhi mahitaji ya viwango vya soko la ndani na nje.
Mheshimiwa Spika,
Kadhalika, Serikali itaviimarisha vituo vya utafiti na huduma za kinga na tiba za mifugo na kuwapa wafugaji huduma za upandishaji wa ng’ombe kwa shindano, ili kupata mbegu bora pamoja na kuhamasisha sekta binafsi kutoa huduma za afya na pembejeo za mifugo. Aidha, Serikali itawahamasisha wawekezaji wa ndani na nje wawekeze katika sekta ya mifugo na viwanda vya usindikaji wa mazao ya mifugo pamoja na kuongeza uwezo wa kitaalamu kwa wafanyakazi wa sekta ya mifugo nchini.
UVUVI NA MAZAO YA BAHARINI
Mheshimiwa Spika,
Uvuvi na uzalishaji wa mazao ya baharini ni miongoni mwa shughuli muhimu za kiuchumi zinazofanywa na wananchi wengi wanaoishi katika maeneo ya karibu na bahari. Kwa kutambua umuhimu wa shughuli hizi, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba, katika kipindi chake cha kwanza (2010 – 2015) ilichukua jitihada mbali mbali za kuimarisha sekta ya uvuvi na mazao ya baharini kwa ufanisi mkubwa.
Mheshimiwa Spika,
Katika kipindi cha miaka mitano ijayo, Serikali itaendeleza juhudi katika kusimamia utekelezaji wa Sera na Sheria za Uvuvi ili kuimarisha usimamizi wa rasilimali za bahari na uhifadhi wa mazingira na kuendeleza jitihada za kuwahamasisha wavuvi wadogo katika kuanzisha vikundi vya ushirika na kuwapatia mafunzo na mikopo nafuu ya zana za kisasa ili kuongeza mapato yao.
Vile vile, Serikali itaandaa mpango na mazingira ya kuvutia Sekta Binafsi kuwekeza katika uvuvi wa bahari kuu, utengenezaji wa boti za uvuvi, ujenzi wa vyumba vya baridi (cold rooms) pamoja na viwanda vya kusindika samaki. Aidha, wavuvi hasa vijana watahamasishwa na kupatiwa mafunzo na zana za kisasa zitakazowawezesha kuvua katika kina kirefu cha maji.
Serikali itanunua vihori 500 vya kuchukulia mwani na kuvisambaza kwa wakulima wa mwani 3,000 Unguja na Pemba ili kuongeza uzalishaji wa mwani. Aidha, itawahamasisha wafugaji wa samaki, chaza, kaa, kamba na majongoo ili kuendeleza uzalishaji wa mazao hayo. Vile vile, juhudi zitachukuwa katika kutafuta masoko kwa mazao ya baharini. Aidha, tutasimamia Mpango Shirikishi wa Maeneo ya Hifadhi ya Bahari yakiwemo maeneo ya Tumbatu, Chumbe – Bawe, Minai kwa Unguja na Kisiwa Panza, Kokota na Mwambe kwa upande wa Pemba. Tutahakikisha kwamba jamii inayozunguka maeneo hayo inanufaika na uhifadhi huo.
Kwa kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tutaandaa Sera ya Uvuvi wa Bahari Kuu ili kuwavutia wawekezaji wa ndani na wa nje wawekeze katika Sekta ya Uvuvi wa bahari kuu, wajenge viwanda vya kusindika samaki, waanzishe Chuo cha Mafunzo ya Uvuvi na wajenge Bandari ya Uvuvi. Tayari Kampuni ya Hairu ya Sri Lanka imetiliana saini Makubaliano ya Awali ya kuanzisha uwekezaji katika uvuvi kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Vile vile, Serikali imetiliana saini mkataba na Shirika la Kimataifa la Kilimo na Chakula (FAO) kwa ajili ya kuanzisha Mradi wa kuendeleza shughuli za ufugaji wa samaki, utakaogharimu Dola za Kimarekani milioni 3.23. Mradi huu utatekelezwa kwa kipindi cha miaka mitatu na utajumuisha ujenzi wa kituo cha kuzalisha vifaranga vya samaki, huko Beit-el-Ras. Fedha za mradi huo zitatolewa na Serikali ya Korea kupitia Shirika la Ushirikiano wa Maendeleo la Kimataifa la Korea ( KOICA).
ARDHI
Mheshimiwa Spika,
Ardhi ni rasilimali muhimu katika nchi ambapo kwa kuzingatia umuhimu wake, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar tangu Awamu ya Kwanza ilizingatia haja ya rasilimali hiyo kumilikiwa na Serikali. Kwa kuzingatia udogo wa ardhi tuliyonayo, Serikali imetilia mkazo umuhimu wa matumizi bora ya ardhi kwa kuandaa Sera na Sheria za mipango ya matumizi yake. Katika miaka mitano ya mwanzo ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba, ilipanga na ilitekeleza mikakati mbali mbali iliyolenga katika kuimarisha matumizi bora ya ardhi na kupunguza migogoro ya ardhi nchini.
Katika kipindi hiki cha pili cha miaka mitano, Serikali itaendelea na juhudi zake za kuimarisha matumizi ya ardhi na kutatua migogoro iliyobakia na kuimarisha huduma za Mahakama za Ardhi katika Mikoa yote ya Unguja na Pemba. Tutaendelea kuwaelimisha wananchi juu ya umuhimu wa kutambua na kufuata sheria mbali mbali za ardhi zinazohusiana na utambuzi, upimaji na usajili wa ardhi. Aidha, Serikali, itaendeleza kazi ya upimaji wa viwanja na utoaji wa hati kwa ajili ya matumizi mbali mbali ya kiuchumi na kijamii, kwa kuzingatia mpango wa kitaifa wa Matumizi bora ya Ardhi.
Mheshimiwa Spika,
Waheshimiwa Wajumbe, mna jukumu la kushirikiana na viongozi wa Shehia zenu katika majimbo yenu, Uongozi wa Wilaya, Mkoa na Serikali kuu, ili kwa pamoja tuhakikishe kuwa Zanzibar inatekeleza mpango wa matumizi bora ya ardhi yanayozingatia uhifadhi wa mazingira. Vile vile, tunafanya jitihada za kuiondoa migogoro ya ardhi ambayo haina tija kwa maendeleo yetu. Napenda nitoe indhari kuwa Serikali haitomvumilia kiongozi wa ngazi yoyote ambaye atajijengea tamaa na akajiingiza katika migogoro ya ardhi au akashindwa kutatua migogoro iliyopo katika dhamana yake. Si siri kwani wapo baadhi ya viongozi waliojiingiza katika matatizo ya ardhi na kusababisha mzozo mkubwa kwenye jamii. Migororo ya ardhi ni kadhia ambayo tunataka tuimalize katika kipindi hiki cha miaka mitano ijayo. Kwa hivyo, nawatahadharisha viongozi watakaopewa dhamana ya kushughulikia masuala ya ardhi wayazingatie maelezo yangu haya.
MAZINGIRA
Mheshimiwa Spika,
Kila mmoja wetu anafahamu umuhimu wa mazingira kwa ajili ya kizazi cha sasa na kijacho na uharibifu wa mazingira ni tishio kwa maisha yetu. Katika miaka mitano iliyopita, Serikali ilichukua juhudi mbali mbali za kuimarisha uhifadhi wa mazingira. Katika kipindi cha miaka mitano ijayo, Serikali italiangalia upya, suala la uchimbaji mawe na mchanga na ukataji ovyo wa minazi. Serikali itaandaa mbinu mpya katika kulishughulikia suala hilo. Nitahakikisha kuwa juhudi za uhifadhi wa mazingira zinaendelea kupata ufanisi huku tukitambua kuwa dunia imekabiliwa na changamoto mbali mbali zitokanazo na uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabia ya nchi. Changamoto hizo zimekuwa na athari zaidi na katika nchi za Visiwa.
Serikali itaendelea kuhamasisha upandaji wa miti, ushajiishaji wa matumizi ya aina nyengine ya nishati na itatilia mkazo zaidi katika kufanya tathmini ya athari za mazingira katika miradi ya uwekezaji. Tutaendelea kuiridhia mikataba iliyowekwa na Jumuiya za Kimataifa yenye lengo la kuhifadhi mazingira. Matumaini yangu ni kuwa watendaji wa idara na taasisi zinazoshughulikia masuala ya mazingira watawajibika ipasavyo ili tuweze kuyafikia malengo haya tuliyojiwekea.
VYAMA VYA USHIRIKA NA SACCOS
Mheshimiwa Spika,
Serikali katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, iliwahamasisha wananchi kuanzisha vyama vya Ushirika na SACCOS kwa lengo la kuwawezesha kukabiliana na tatizo la ajira na kupambana na umasikini wa kipato. Katika kipindi hicho, Serikali iliviendeleza vikundi vya ushirika kwa kuvipatia mafunzo, mikopo na kuvifanyia ukaguzi. Aidha, katika kipindi hicho Serikali ilianzisha Mfuko wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ambao ilitoa mikopo 286 yenye thamani ya TZS milioni 436.2. Mikopo hiyo iliwanufaisha wananchi wapatao 8,976.
Mheshimiwa Spika,
Katika kipindi cha miaka mitano ijayo, Serikali itayaendeleza mafanikio yaliyopatikana pamoja na kuendelea kuimarisha Mfuko wa Uwezeshaji wa Wananchi Kiuchumi ili kuongeza uwezo wake wa kutoa mikopo kwa wajasiriamali na wafanyabiashara wadogo. Sambamba na juhudi hizo, Serikali itakiimarisha kituo cha kulelea wajasiriamali kilichoko Mbweni pamoja na kuendelea kutoa mafunzo mbali mbali kwa lengo la kuwajengea wananchi uwezo wa kujiajiri na kuondokana na umasikini.
Aidha, Serikali itaanzisha vituo 10 vya huduma za biashar; kimoja kila Wilaya ili kuongeza tija katika shughuli za wajasiriamali na wafanyabiashara wadogo pamoja na kutoa mikopo 5,000 yenye thamani ya TZS. bilioni 2.5. Mikopo hii itawanufaisha jumla ya wananchi 50,000 kutoka kwenye makundi mbali mbali ya wananchi hususan wanawake, vijana na watu wenye walemavu.
KAZI, AJIRA NA UTUMISHI WA UMMA
Mheshimiwa Spika,
Suala la ajira bado ni changamoto katika nchi yetu kama ilivyo katika Mataifa mengine. Tuna matumaini makubwa ya kupata mafanikio katika ongezeko la nafasi za kazi katika kipindi kijacho kutokana na mikakati tuliyojipangia. Miaka mitano iliyopita, zilipatikana nafasi za ajira 5,370 katika taasisi mbali mbali za serikali na nafasi 25,006 katika sekta binafsi zikijumuisha ajira za nje ya nchi.
Tutahakikisha jitihada za Serikali za kutekeleza mageuzi ya uchumi zinafanikiwa katika sekta ya utalii na viwanda kwa kuwashajiisha wawekezaji. Tutahakikisha kwamba sekta binafsi inaimarishwa na kuwa chanzo kikuu cha ajira. Vyama vya ushirika navyo vitaunganishwa ili viwawezesha wananchi kubadili maisha yao ili wajiendeleze kiuchumi. SACCOS na Asasi ndogo za fedha zitaimarishwa na kupatiwa mafunzo ya kitaalamu, uongozi na kuwaongezea mitaji, ili ziweze kutekeleza shughuli zake kwa ufanisi kwa lengo la kuongeza ajira.
Mheshimiwa Spika,
Serikali itaendelea na jitihada zake za kuimarisha maslahi ya wafanyakazi pamoja na mazingira ya kufanyia kazi. Tutaendelea kuimarisha miundo ya utumishi, ili wafanyakazi waendelee kufaidika na elimu, uwezo na uzoefu walioupata wakiwa kazini pamoja na viwango vya elimu walivyonavyo. Hata hivyo, nataka nikumbushe kuwa, wafanyakazi sote tufahamu kuwa mshahara ni matunda na tunzo mtu anayopata kutokana na juhudi aliyoifanya katika uzalishaji. Kuna baadhi ya watu wamejenga tabia ya kudai mishahara mikubwa na kuilaumu Serikali kuwa haipandishi mishahara bila ya wao kuwa na ari na dhamira ya kweli ya kujitahidi kufanya kazi na kuzalisha.
Natumai kuwa watu wa aina hiyo wataiacha tabia hiyo ambayo haina manufaa kwa maendeleo yetu. Kwa pamoja tunawajibika kulitekeleza kwa vitendo agizo langu nililolitoa mwaka 2011, mara tu baada ya kuingia madarakani kuwa “tubadilike na tusifanye kazi kwa mazoea”. Tulijitahidi kubadilika na kuyaondoa mazoea. Lakini ni ukweli usiopingika matatizo bado yapo, viwango vya utendaji na nidhamu kazini bado havijaongezeka sana. Ni jukumu letu tufanye kazi kwa bidii na tuipende kazi. Kwani wapo baadhi ya wafanyakazi ambao hawapendi kufanyakazi (kwa vitendo vyao), na wengine hawataki kufanyakazi, lakini wao ndio wa mwanzo wanaotaka mishahara mikubwa, posho nzuri, safari za kila wakati na kuhudhuria kwenye semina na mikutano kila mara.
Wapo baadhi ya wafanyakazi kwenye taasisi muhimu zinazotoa huduma kwa wananchi, ambao hawajali kazi zao na wanakwepa wajibu wao. Upo ushahidi kutoka kwa baadhi ya wananchi kwamba wanapokwenda kutaka huduma wanadharauliwa, wanapuuzwa, wananyanyaswa na wengine hutakiwa watoe kitu chochote. Baadhi ya wafanyakazi wenye tabia hizi walichukuliwa hatua za kinidhamu, lakini bado hawajajirekebisha. Wafanyakazi wa namna hii huwavunja moyo wananchi na hupelekea wananchi waichukie Serikali yao bila ya sababu za msingi.
Zaidi ya hayo, wapo baadhi ya watumishi wenye tabia ya kutoroka kazini, kuchelewa na hawazijali kanuni ziliopo za utumishi wa umma. Wao hujifanya wababe mbele ya viongozi wao. Wafanyakazi wenye sifa mbaya nilizozielezea katika kipindi hiki tutawachukulia hatua watakapobainika na kama hapana budi tutawafukuza kazini. Hatuwezi kuwa na wafanyakazi waliokuwa hawana nidhamu. Sasa basi, imetosha. Waliopewa dhamana ya kuziongoza Idara mbali mbali za Serikali watapaswa watekeleze wajibu kwa kuwasimamia wafanyakazi walio chini yao. Pindi kama hawatawawajibisha wafanyakazi wao, basi watawajibishwa wao. Lengo letu liwe kutoa huduma kwa wananchi, kwani sote tunawajibika kwao; kwa kuzingatia misingi ya utawala bora.
Mheshimiwa Spika,
Nataka niwahakikishie wananchi kuwa nitatekeleza ahadi nilizozitoa wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu mwaka 2015, za kuimarisha maslahi ya wafanyakazi katika sekta mbali mbali ukiwemo utoaji wa kima cha chini cha mshahara cha TZS. 300,000 kwa mwezi ndani ya kipindi cha mwaka mmoja baada ya kuingia madarakani. Kadhalika, ahadi yangu kwa Idara Maalum za SMZ ya maslahi yao yalingane na wenzao wa SMT ipo pale pale. Tumuombe Mwenyezi Mungu atupe uwezo wa kukusanya mapato vizuri, ili Serikali ipate uwezo wa kuzitekeleza ahadi hizo.
Serikali itaimarisha zaidi huduma za Hifadhi ya Jamii kwa wanachama wake kwa kubuni utoaji wa mafao mapya na kuongeza kiwango cha malipo ya kiinua mgongo na pensheni. Madeni ya viinua mgongo vya wafanyakazi waliostaafu tutayalipa, tunawaomba wastaafu wawe na subira. Sina shaka Mheshimiwa Spika, kwamba juhudi hizi za kuimarisha utawala bora zinaungwa mkono na zitapata baraka zote katika Baraza lako.
MIUNDOMBINU
Mheshimiwa Spika,
Miundombinu ya kiuchumi ikiwemo barabara, bandari na viwanja vya ndege ina mchango muhimu katika kuongeza kasi ya kukua kwa uchumi wa nchi na kuimarisha huduma za jamii katika shughuli zao za kila siku. Katika kipindi kilichopita, jumla ya barabara zenye urefu wa kilomita 124.7 kwa Unguja zilijengwa kwa viwango mbali mbali, na kilomita 203.4 za barabara zimejengwa huko Pemba.
Kwa lengo la kuimarisha zaidi miundombinu ya barabara katika kipindi cha miaka mitano ijayo, Serikali itaendeleza kazi ya utunzaji na matengenezo ya barabara zilizokwishajengwa na kufanya marekebisho katika maeneo yanayotuama maji ya mvua na kuathiri ubora wa barabara hizo. Kadhalika, tutakamilisha ujenzi wa barabara ya Jendele – Cheju-Kaebona (km 11.7) na barabara ya Koani hadi Jumbi (km 6.3) kwa kiwango cha lami kwa Unguja na barabara ya Ole hadi Kengeja (km 35), Makanyageni hadi Kangani (km 6.5), Finya hadi Kicha (km 8.8) na barabara kutoka Mgagadu hadi Kiwani (km 7.6) kwa kiwango cha lami kwa upande wa Pemba.
Kadhalika, Serikali itajenga jumla ya kilomita 160.8 za barabara kwa kiwango cha lami kwa Unguja katika maeneo mbali mbali ya Mikoa yote na jumla ya kilomita 51.1 kwa kiwango cha lami huko Pemba kwa maeneo yote ya Mikoa ya Pemba. Barabara zote hizi zimefafanuliwa vizuri kwenye Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu na mipango yake ya ujenzi tayari imepangwa. Kazi nyengine zitakazoshughulikiwa na Serikali ni kuendeleza kazi ya uwekaji wa taa za kuongozea magari kwa kuweka taa katika sehemu sita, ili kupunguza msongamano katika baadhi ya maeneo ya miji hasa katika mji wa Unguja, Wete na Chake chake. Vile vile, karakana kuu ya Serikali itaimarishwa kwa mashirikiano na sekta binafsi kwa lengo la kuongeza ufanisi na utoaji wa huduma bora za kiufundi kwa taasisi mbali mbali za Serikali na watu binafsi.
Mheshimiwa Spika,
Kwa lengo la kuiendeleza sekta ya usafiri wa anga katika kipindi cha miaka mitano ijayo, Serikali itakamilisha ujenzi wa jengo jipya la abiria katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Abeid Amani Karume (AAKIA), ili kuongeza idadi ya abiria wanaotumia kiwanja hicho pamoja na kiwango cha mizigo ili kuongeza mapato ya Serikali. Kiwanja cha ndege cha Pemba nacho kitapanuliwa ili ziweze kutua ndege kubwa za aina ya Boeing 737, jengo la abiria litajengwa upya na miundombinu na huduma za abiria, ndege na mizigo katika Kiwanja cha Ndege cha Pemba itaimarishwa. Vile vile, huduma za umeme zitaimarishwa na kukamilisha kazi ya ujenzi wa uzio wa kiwanja hicho. Serikali, vile vile itaendelea kuwapatia mafunzo na vifaa vya kisasa wafanyakazi wa Viwanja vya Ndege vya Unguja na Pemba pamoja na kuimarisha huduma za zimamoto na usalama wa viwanja vya ndege.
Katika nchi za Visiwa kama Zanzibar, usafiri wa baharini ni shughuli muhimu; jambo linalosababisha haja ya kuwepo kwa bandari za kisasa ambazo huwa ni milango mikuu ya biashara na chachu ya ukuaji wa uchumi na ustawi wa wananchi kwa jumla. Katika kipindi changu cha kwanza, jitihada za kuziimarisha bandari zetu na shughuli za usafiri wa baharini zilichukuliwa na kuleta mafanikio makubwa.
Mheshimiwa Spika,
Kwa lengo la kuimarisha bandari, katika kipindi cha miaka mitano ijayo, Serikali itatekeleza mradi wa ujenzi wa bandari mpya ya kisasa ya kuhudumia mizigo katika eneo la Mpigaduri itakayoanza kujengwa baadae mwaka huu kwa mkopo kutoka Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China. Vile vile, bandari ya Malindi itaendelezwa kwa kuongeza vifaa vya huduma kwa abiria pamoja na mizigo. Bandari ya Mkoani Pemba itaendelezwa kwa kuipatia vifaa vya kisasa vya kuhudumia abiria na mizigo. Aidha, bandari ya Wete nayo inatarajiwa kujengwa kwa juhudi za sekta binafsi, ambapo muwekezaji amejitokeza na yupo tayari kuifanya kazi hiyo. Kadhalika, Gati ya Mkokotoni nayo itajengwa kwa kukamilisha kazi ya ujenzi wa jeti kwa ajili ya huduma za usafiri wa wananchi hasa wa Tumbatu na usafirishaji wa mizigo kwa majahazi.
Shirika la Meli na Uwakala, litafanyiwa mabadiliko makubwa ili liweze kujiendesha kibiashara na kununua meli nyengine mpya ya abiria ndogo na moja ya mafuta. Aidha, kuhusu kuziimarisha huduma za usafiri wa baharini, Serikali itahakikisha kuwa inaendelea kusimamia utekelezaji wa Sheria na Kanuni za usafiri wa baharini ili kupunguza ajali za vyombo vya baharini kwa kuimarisha utendaji wa Mamlaka ya Usafiri wa Baharini (ZMA).
NISHATI
Mheshimiwa Spika,
Upatikanaji wa nishati ya uhakika ni muhimu katika kuimarisha ukuaji wa uchumi na ustawi wa maendeleo ya wananchi. Mabadiliko na mafanikio makubwa tumeyafikia nchini katika kuimarisha sekta ya nishati katika kipindi cha miaka mitano iliyopita mijini na vijijini, Unguja na Pemba. Visiwa vyote viwili sasa vina nishati ya umeme wa uhakika. Umeme tayari umefikishwa kwenye vijiji 129 na kwenye visiwa vidogo vidogo kadhaa.
Katika kipindi cha miaka mitano ijayo, Serikali itaendelea na juhudi za kuufikisha umeme katika vijiji na visiwa vidogo vidogo, vilivyobakia ikiwemo Kisiwa cha Fundo ambapo huduma hizi zinatarajiwa kupatikana katika mwaka wa fedha 2016/2017. Juhudi za kutafuta umeme wa nishati mbadala zimefikia hatua kubwa kwa kushirikiana na washirika wa maendeleo ambapo utafiti wa kutumia upepo unaendelea. Aidha, Shirika la Umeme la Zanzibar (ZECO) litafanyiwa mabadiliko, ili liweze kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi na kujiendesha kibiashara.
UCHIMBAJI WA MAFUTA NA GESI
Mheshimiwa Spika,
Natanguliza shukurani zangu kwa waliokuwa Wajumbe wa Baraza la Nane la Wawakilishi kwa mijadala ya kina waliyoiendesha juu ya suala zima la uchimbaji wa mafuta na gesi. Juhudi zao zimetuwezesha kuifikia hatua hii nzuri. Rasimu ya mswada wa sheria ya mafuta na gesi hivi sasa ipo katika hatua nzuri na matumaini yangu ni kuwa baada ya muda si mrefu italetwa katika Baraza hili tukufu la Wawakilishi wa Zanzibar kwa ajili ya kujadiliwa na kupitishwa.
Kwa mara nyengine tena, napenda nimpongeze kwa dhati, Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, kwa kuhakikisha kwamba, kabla ya kuondoka kwake madarakani suala la Zanzibar kuchimba mafuta yake wenyewe linapatiwa ufumbuzi. Tulishirikiana kwa dhati katika kulipatia ufumbuzi suala hili. Hivi sasa, Zanzibar ina uwezo wa kisheria wa kuchimba mafuta yake kwa mujibu wa Sheria Namba 21 ya mwaka 2015 iliyopitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Sina shaka, Baraza hili la Tisa litasimama imara katika kuendeleza pale tulipofika katika kipindi kilichopita na litaharakisha katika utungaji wa sheria tunazozihitaji ili tuweze kuyachimba mafuta na gesi na kufaidika na nishati hizi muhimu.
HUDUMA ZA JAMII
Mheshimiwa Spika,
Uimarishaji wa huduma za jamii ikiwemo elimu, afya, huduma za maji safi na salama ni miongoni mwa majukumu muhimu ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika awamu zake zote saba.
ELIMU
Mheshimiwa Spika,
Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Serikali iliizingatia huduma ya elimu kuwa ni haki ya msingi kwa kila mwananchi na nyenzo muhimu ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Serikali ilichukua hatua za kuimarisha ubora wa elimu inayotolewa kuanzia ngazi ya elimu ya maandalizi, msingi, sekondari, elimu ya juu na elimu inayotolewa katika vituo vya mafunzo ya amali, vyuo vya ualimu na Chuo Kikuu cha SUZA.
Mheshimiwa Spika,
Katika kipindi cha miaka mitano ijayo, Serikali itayaendeleza mafanikio hayo katika sekta ya elimu pamoja na kuchukua hatua za kuimarisha elimu katika ngazi mbali mbali. Kuhusu Elimu ya Maandalizi, Serikali itasimamia utekelezaji wa Sera ya Makuzi na Malezi ya Mtoto na itaanzisha vituo 150 vya Tucheze Tujifunze katika Wilaya nne za Unguja na Pemba.
Kwa upande wa Elimu ya Msingi, Serikali itaongeza kiwango halisi cha uwandikishaji hadi kufikia asilimia 100 mwaka 2020, itajenga skuli mpya 10 za ghorofa katika maeneo yenye upungufu na msongamano mkubwa wa wanafunzi. Vile vile, Serikali itakamilisha ujenzi wa madarasa yaliyoanzishwa kwa nguvu za wananchi. Lengo la kutoa elimu bila ya malipo katika elimu ya msingi kwa kutowachangisha wazazi michango yoyote, litaendelezwa kutekelezwa. Kadhalika, Serikali itaendelea kulipia gharama za mitihani ya kidatu cha tatu na mitihani ya Taifa kwa watahiniwa wa Kidatu cha Nne na cha Sita. Hatua hii ina lengo la kuwaondolea wazazi mzigo wa kuchangia huduma za elimu ya watoto wao.
Mheshimiwa Spika,
Serikali itajenga vituo vipya vya Mafunzo ya Amali huko Makunduchi kwa Unguja na Daya Mtambwe huko Pemba. Aidha, mafunzo ya ualimu yataimarishwa katika ngazi mbali mbali. Katika kipindi hiki ujenzi wa dakhalia katika Chuo Kikuu cha Taifa (SUZA) utaanza na ujenzi wa Chuo Kikuu kipya katika eneo la Dole utaanza kwa kushirikiana na Serikali ya Saudi Arabia. Vile vile, nafasi za masomo ya elimu ya juu zitaongezwa kwa kuuimarisha Mfuko wa Bodi ya Mikopo, ili lengo la kuwanufaisha wanafunzi 22,404 ifikapo mwaka 2020 liweze kufanikiwa.
Katika kipindi kijacho, Serikali itaongeza idadi ya watu wanaojua kusoma, kuandika na kuhesabu pamoja na kuimarisha Elimu Mjumuisho kwa ajili ya watoto wenye mahitaji maalumu. Vile vile, Serikali itaimarisha na itaendeleza michezo na utamaduni maskulini ambapo kipindi cha miaka mitano ijayo somo la michezo litaanzishwa katika skuli sita za sekondari zilizoteuliwa. Skuli nne Unguja na mbili huko Pemba.
AFYA
Mheshimiwa Spika,
Sekta ya afya ni muhimu katika kuimarisha afya za wananchi wetu ili waweze kushiriki kikamilifu katika shughuli zao za kila siku na kutoa mchango wao katika kuleta maendeleo nchini. Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Serikali ya Awamu ya Saba ilichukua hatua mbali mbali katika kuziimarisha huduma za afya ambapo huduma hizi zinapatikana si zaidi ya kilomita tano ya makaazi ya kila mwananchi.
Katika kipindi cha miaka mitano ijayo, Serikali itaongeza jitihada za kuziimarisha huduma za afya kwa kuendelea kuishirikisha sekta binafsi. Azma yetu ya kuifanya hospitali ya Mnazi Mmoja kuwa ya Rufaa itaendelezwa kwa kuzikamilisha zile huduma muhimu ambazo bado zinashughulikiwa. Hivi sasa Serikali inakamilisha utaratibu wa matibabu ya saratani na utibabu wa maradhi ya figo. Vile vile, huduma za uchunguzi wa maradhi zitaimarishwa kwa ununuzi wa vifaa vya kisasa kama “Magnetic Resonance Imaging (MRI)”, mashine ya uchunguzi wa “DNA” na vyengine. Vile vile, idadi ya madaktari na mabingwa wa fani mbali mbali itaongezwa.
Kadhalika, Serikali itatekeleza mpango wake wa kujenga Hospitali ya kisasa ya Rufaa katika eneo la Binguni Unguja. Ujenzi wa Hospitali ya Abdalla Mzee unaoendelea hivi sasa unatarajiwa kukamilika ifikapo Septemba, 2016. Hospitali ya Wete Pemba nayo itaimarishwa ili hospitali zote mbili zifikie daraja na kiwango cha Hospitali za Mkoa. Aidha, Hospitali ya vijiji ya Makunduchi na Kivunge kwa Unguja zimefika hatua kubwa ya kuwa Hospitali za Wilaya na kazi bado inaendelea kufanywa. Kazi kama hiyo inafanyika kwa hospitali ya Vitongoji na Micheweni.
Mheshimiwa Spika,
Vile vile, Serikali itaendeleza jitihada za kuimarisha Huduma ya Afya ya Mama na Mtoto kwa kuendeleza ujenzi wa majengo mapya ya wodi ya wazazi na wodi ya watoto unaoendelea sasa katika Hospitali Kuu ya Mnazi mmoja. Jumla ya vituo 19 vya afya ya msingi Unguja na Pemba vitafanyiwa matengenezo makubwa na kuvipatia vifaa vya kisasa ili kupunguza kiwango cha vifo vya mama na mtoto. Mapambano dhidi ya maradhi ya Malaria, UKIMWI, kifua kikuu na ukoma na maradhi mengine ya kuambukiza na yasiyokuwa ya kuambukiza yanaendelezwa kwa mafanikio. Kiwango cha maradhi ya malaria bado kipo chini ya asilimia moja. Utoaji wa elimu ya afya kwa wananchi unaendelezwa vizuri, ili kupunguza ongezeko la maradhi ya saratani, kisukari na shinikizo la damu.
Serikali vile vile, itakiimarisha Chuo cha Taaluma za Sayansi ya Afya kwa kukiunganisha na Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar, ili kiweze kutoa wataalamu wenye elimu ya kiwango cha shahada; katika fani mbali mbali. Kadhalika, madaktari na madaktari mabingwa wa fani mbali mbali watapatiwa mafunzo ili tuweze kujitosheleza na mahitaji yaliyopo. Vile vile, idadi ya madaktari wanaofundishwa katika kitivo cha udaktari katika Chuo Kikuu cha SUZA na vyengine itaongezwa; ili lengo la Serikali lililowekwa kwenye Mpango wa Afya wa mwanzo hapo 1965 wa daktari mmoja ahudumie watu 6,000 liweze kufikiwa. Hivi sasa daktari mmoja anahudumia watu 8,885 (1:8885).
Vile vile, tafiti mbali mbali katika maeneo ya Afya ya mama na mtoto, maradhi ya kuambukiza na yasiyoambukiza zitaendelezwa pamoja na mifumo ya utoaji huduma za afya. Huduma za matibabu ya wagonjwa walioathirika na dawa za kulevya na afya ya akili zitaimarishwa na kujenga kituo maalumu kwa waathirika wa dawa za kulevya. Serikali itaongeza bidii katika kukabiliana na matumizi ya dawa za kulevya ili kuwanusuru vijana ambao ni nguvu kazi ya Taifa. Aidha, Serikali itaimarisha upatikanaji, ugawaji, usambazaji na udhibiti wa dawa, vifaa vya utibabu, dawa za uchunguzi wa maradhi na “reagents” zenye ubora. Vile vile, Serikali itaandaa Sheria ya Uanzishaji wa Mfuko wa Bima ya Afya na kusimamia utekelezaji wa mfuko huo. Kadhalika, Serikali itaandaa utaratibu mzuri wa namna wananchi watakavyochangia huduma za afya wanapoelezwa kufanya hivyo. Hivi sasa hakuna mpango unaofahamika katika jambo hili.
MAJI
Mheshimiwa Spika,
Mafanikio makubwa yamepatikana katika kuimarisha huduma za maji safi na salama kupitia miradi na programu mbali mbali za maji mijini na vijijini. Katika kipindi kilichopita hadi mwishoni mwa mwaka 2015 hali ya upatikanaji wa maji safi na salama imefikia asilimia 87 kwa mijini na asilimia 70 kwa vijijini.
katika kipindi cha miaka mitano ijayo, Serikali itaendelea kuimarisha usambazaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi kutoka asilimia 87 mwaka 2015 hadi asilimia 97 mwaka 2020 kwa mijini na kutoka asilimia 70 mwaka 2015 hadi asilimia 85 kwa vijijini ifikapo mwaka 2020. Vile vile, itaendeleza jitihada za kuimarisha miundombinu ya maji ili kupunguza upotevu wa maji. Vyanzo vya maji vitahifadhiwa, vitatunzwa na vitalindwa pamoja na maeneo ya kuhifadhia maji. Vile vile, wananchi watahamasishwa juu ya umuhimu wa uhifadhi, utumiaji na uchangiaji wa huduma ya maji safi na salama. Utafiti wa matumizi ya nishati ya jua katika visima na vyanzo vya maji utafanywa, kwa lengo la kupatikana huduma hizi kwa ufanisi.
VYOMBO VYA HABARI
Mheshimiwa Spika,
Vyombo vya habari vina umuhimu mkubwa katika kuhamasisha shughuli za maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kisiasa pamoja kupanua uhuru na haki ya wananchi ya kupata taarifa. Katika kipindi cha miaka 5 ijayo, Serikali itahakikisha kwamba uhuru wa vyombo vya habari unaendelea kuimarishwa na vyombo hivyo vinatimiza wajibu wake kwa weledi na kuzingatia maadili ya kazi zao. Serikali itaimarisha matumizi ya TEHAMA na kuendeleza mageuzi ya sekta ya Habari, ili kuongeza ufanisi na weledi.
Vile vile, Shirika la Habari la Zanzibar (ZBC) litaimarishwa kwa kulipatia mitambo, vifaa vya kisasa ili kuukamilisha utaratibu wa matumizi ya “Digital” kwa TV na Redio. Aidha, mafunzo ya wafanyakazi wake katika kada mbali mbali yatatolewa ndani na nje ya nchi. Tutaendelea kuwashajihisha wawekezaji ili wawekeze katika vyombo vya habari binafsi.
Mheshimiwa Spika,
Kuhusu Kiwanda cha Upigaji Chapa na Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali, Serikali itakiimarisha na kukiongezea vifaa na wataalamu. Vile vile, Serikali itakiimarisha Chuo cha Uandishi wa Habari ili kiwe chachu ya kuendeleza tasnia ya habari na kuendeleza vipaji vya uandishi wa habari. Hata hivyo, tasnia ya habari imekabiliwa na changamoto ya matumizi mabaya ya intaneti na mitandao ya kijamii. Matarajio yangu ni kuwa wakati utakapofika mtahakikisha mnajadili na mnairidhia Sheria ya Makosa ya Matumizi ya Mitandao ya Mwaka 2015 iliyopitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili sheria hii iweze kutumika hapa Zanzibar. Lengo letu tuwe na matumizi ya mitandao yanayozingatia sheria, heshima, faragha na haki za wananchi pamoja na utunzaji wa siri za Serikali.
UTAMADUNI NA MICHEZO
Mheshimiwa Spika,
Kwa kutambua kuwa utamaduni ni nyenzo muhimu katika kulinda na kudumisha mapenzi, umoja, mila, desturi na silka njema katika jamii, Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi ilichukua juhudi mbali mbali za kuendeleza na kulinda utamaduni wetu.
Katika kipindi hiki cha pili, Serikali itaendelea na juhudi za kuulinda, kuudumisha na kuutangaza utamaduni wa Mzanzibari kwa kuendelea kuandaa matamasha ya utamaduni. Aidha, tutawaelimisha wananchi hasa vijana juu ya matumizi bora ya mitandao pamoja na kufanya ukaguzi wa kazi za sanaa mbali mbali. Tutaendelea na jitihada za kuimarisha lugha ya Kiswahili na kuzifanya lahaja za Zanzibar kuwa ni chimbuko la Kiswahili fasaha. Vile vile, tutaendelea kuimarisha tasnia ya sanaa kwa kuongeza kasi ya kutafuta na kukuza vipaji vya wasanii pamoja na kuimarisha maslahi yao kwa kuimarisha mfumo uliopo wa matumizi ya hakimiliki.
Mheshimiwa Spika,
Vile vile, tutazidisha juhudi zetu katika kuyaendeleza mafanikio tuliyoyapata katika sekta ya michezo kwa kuyaimarisha mashindano ya riadha ya Wilaya na kuliimarisha Bonanza la michezo la vikundi vya mazoezi. Jitihada zetu za kuimarisha michezo katika maskuli, bila ya shaka zitafanikiwa. Kadhalika, tutakamilisha matengenezo ya Kiwanja cha Mao Tse Tung na kujenga viwanja vya michezo kwa kila Wilaya. Tutahamasisha ushiriki wa michezo na ufanyaji wa mazoezi ya viungo kama ni hatua muhimu ya kuimarisha afya za wananchi. Tutaendeleza michezo ya asili ya Zanzibar, ikiwemo mashindano ya resi za ngalawa, bao, karata, mchezo wa ng’ombe na mengineyo.
Watu wenye ulemavu nao tutawahamasisha kwa kuwapatia vifaa pamoja na vyama vya michezo vinavyohusika, ili waweze kushiriki kikamilifu katika kuendeleza michezo. Wasanii wataendelea kusaidiwa, wataendelezwa na wale walioijengea nchi yetu heshima katika ulimwengu wa utamaduni, wataenziwa na watapewa heshima yao.
KUYAENDELEZA MAKUNDI MAALUM
VIJANA
Mheshimiwa Spika,
Serikali inatambua umuhimu wa kundi la Vijana kuwa ni rasilimali na nguvukazi ya Taifa. Vijana walioandaliwa vyema na kujipanga vizuri wanao mchango mkubwa katika kukuza uchumi na maendeleo ya jamii. Changamoto kubwa inayowakabili vijana mijini na vijijini ni ukosefu wa ajira, kukosa ujuzi na maarifa ya kisasa pamoja na mitaji, hivyo kushindwa kujiendeleza na kutekeleza wajibu wao wa kushiriki katika ujenzi wa uchumi wa kisasa.
Serikali ilichukua hatua mbali mbali za kuwaendeleza vijana katika kipindi kilichopita. Kwa lengo la kuzipatia ufumbuzi changamoto zinazowakabili vijana, Serikali katika kipindi kijacho cha miaka mitano, itachukua hatua za kuuimarisha mfuko maalum wa vijana, ili vijana wengi zaidi waweze kunufaika na mfuko huo na kwenye kazi mbali mbali pamoja na kujiajiri katika kilimo cha kisasa na kuanzisha "green house' moja kwa kila Wilaya. Aidha, Serikali itawahamasisha vijana 5,000 waliomaliza vyuo Vikuu kuanzisha vikundi vya uzalishajimali na utoaji wa huduma na kuwapatia mafunzo na mikopo ili waweze kujiajiri. Kadhalika, Baraza la Vijana litaendelezwa, ili kuongeza ushiriki wa vijana katika ngazi mbali mbali za uamuzi. Aidha, jitihada za Serikali za kuongeza ajira kwa kushirikiana na sekta binafsi, zitaendelezwa.
WANAWAKE
Mheshimiwa Spika,
Ni dhahiri kuwa wanawake wana uwezo mkubwa katika kuchochea kasi ya maendeleo ya kiuchumi, kisiasa na kijamii. Serikali katika kipindi kilichopita, iliwaendeleza wanawake kwa lengo la kuwapa uwezo wa kutumia fursa zilizopo katika kujiendeleza kiuchumi, kijamii na kisiasa.
Kwa lengo la kuwawezesha wanawake kiuchumi, kijamii na kisiasa katika miaka mitano ijayo, Serikali itayaendeleza yale mafanikio yote yaliyopatikana. Vile vile, itaendelea kusimamia upatikanaji wa haki za wanawake na kupiga vita mila na desturi zinazowabagua au kuwadhalilisha na kusimamia utekelezaji wa sheria na mikataba yote ya Kimataifa inayohusu ustawi wa wanawake. Aidha, Serikali itaanzisha jumla ya vikundi 500 vya wanawake na kuwapatia mafunzo ya ujasiriamali pamoja na mikopo ili waweze kujiajiri wenyewe. Kadhalika, kituo kiliopo Kibokwa cha kuwafundisha wanawake kutengeneza vifaa vya umeme wa jua kitaendelea kuimarishwa ili kiwafundishe wanawake wengi zaidi. Vile vile, kampeni ya kupinga udhalilishaji wanawake na watoto itaendelezwa kwa kasi, ili hatimae matatizo haya yasiwepo kwenye jamii zetu.
WAZEE
Wazee ni hazina na chem chem ya busara na hekima katika jamii kutokana na uzoefu walionao katika maisha. Serikali inaheshimu mchango wa wazee katika maendeleo yetu pamoja na malezi na maadili mema wanayoyatoa kwenye jamii yetu.
Katika kipindi cha miaka mitano ijayo, Serikali itaongeza juhudi katika kuziimarisha huduma za kijamii na mahitaji muhimu wanayopewa wazee wanaotunzwa katika nyumba za wazee za Unguja na Pemba. Kadhalika, Serikali itaanza kutekeleza Mpango wa kuwapatia Pencheni maalum wazee wote waliofikia umri wa miaka 70 bila ya kujali historia ya kazi walizokuwa wakizifanya. Vile vile, Serikali itaandaa utaratibu maalum wa kuwapatia wazee huduma za matibabu bure.
WATOTO
Mheshimiwa Spika,
Watoto wana haki ya kulindwa na kuishi vizuri bila ya matatizo na ni sehemu muhimu ya wanajamii. Watoto wetu wanayo haki ya kuishi, kutoa mawazo yao, kupata lishe bora, kupata haki ya elimu na kutobaguliwa kwa namna yoyote. Serikali katika miaka mitano iliyopita ilizingatia umuhimu huo na ilitekeleza mipango ya kuwapatia watoto haki zao za msingi.
Ili kuhakikisha haki za watoto zinaendelea kulindwa, katika kipindi kijacho Serikali itayaendeleza yale mafanikio yote yaliyopatikana. Vile vile, itaziimarisha Mahkama za watoto na kusimamia uanzishwaji na uendeshaji wa mabaraza ya watoto na kamati za wazazi katika Shehia, Wilaya na Mikoa yote ya Zanzibar, ili kupinga vitendo vya udhalilishaji dhidi ya watoto. Kadhalika, jitihada zetu za kupiga vita ajira za watoto zitaendelezwa pamoja na kusimamia utekelezaji wa sheria na mikataba ya Kimataifa inayohusu haki, usawa na hifadhi ya mtoto.
WATU WENYE ULEMAVU
Mheshimiwa Spika,
Watu wenye ulemavu wana haki kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya 1984, kutambuliwa utu wao, kuendelezwa, kuheshimiwa, kushirikishwa na kulindwa dhidi ya vitendo vinavyowabagua. Katika kipindi hiki, tutaendeleza kusimamia utekelezaji wa mipango na programu mbali mbali zenye lengo la kuwaendeleza watu wenye ulemavu. Mfuko wa Watu Wenye Ulemavu tuliouanzisha kipindi kilichopita utaimarishwa na tutahakikisha kuwa huduma muhimu na mahitaji ya nyenzo zote pamoja na dawa zinapatikana bila ya malipo. Aidha, tutaendeleza na utoaji wa mafunzo na elimu kwa wazazi, walezi na walimu juu ya namna ya kuwakuza watoto wenye ulemavu na tutayazingatia makaazi yao wanayoishi.
DEMOKRASIA NA UTAWALA BORA
Mheshimiwa Spika,
Demokrasia na utawala bora ni nguzo na nyenzo muhimu katika ujenzi wa jamii yenye umoja, mshikamano, uadilifu na uwajibikaji. Kwa lengo la kuimarisha utawala wa sheria, Serikali imefanya jitihada kubwa ya kuziimarisha taasisi zinazosimamia utawala bora, watendaji wake pamoja na mazingira ya kufanyia kazi.
Katika kipindi cha miaka mitano ijayo, Serikali itaongeza kasi katika kuziendeleza juhudi hizo kwa lengo la kuongeza ufanisi. Pamoja na mambo mengine, Serikali ina mpango wa kujenga wa jengo jipya la Mahkama Kuu huko Tunguu, kukamilisha ujenzi wa Mahkama ya Watoto Mahonda na kuyafanyia matengenezo makubwa majengo ya mahkama ya Mfenesini, Mwanakwerekwe na Wete na kuzisogeza huduma za Mahkama karibu na wananchi.
Mheshimiwa Spika,
Katika kusimamia maadili ya viongozi na nidhamu ya utumishi, Serikali katika kipindi kilichopita ilianzisha Sheria ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Namba. 1 ya 2012 na Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Namba 8 ya mwaka 2015. Kufuatia sheria hiyo, Serikali ilianzisha Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi na hivi karibuni nitaianzisha Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma.
Katika kipindi hiki, nitahakikisha kwamba Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma, inafanya kazi ipasavyo ili viongozi wote waliotajwa katika sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma wanatangaza mali zao kwa mujibu wa sheria hio. Kila kiongozi atatakiwa atekeleze wajibu wake kwa wakati uliowekwa. Katika kupambana na rushwa na uhujumu wa uchumi, Serikali haitomvumilia mtu yeyote atakayebainika kuzibeza na kutaka kuzirudisha nyuma jitihada za Serikali kutokana na udhaifu wake wa kimaadili.
Hapana asiyejua kuwa rushwa ni adui wa haki na Mwenyezi Mungu ameikataza rushwa. Katika kulikemea jambo hili, Mwenyezi Mungu katika aya ya 188 ya Surat Al-Baqarah ametuasa kwa kusema:”Wala msiliane mali zenu kwa batili na kuzipeleka kwa mahakimu ili mpate kula sehemu ya mali ya watu kwa dhambi, na hali mnajua”. Kadhalika, ipo hadithi mashuhuri ambapo, Mtume Muhammad (SAW) amesema kwamba: “Mwenyezi Mungu amemlaani mtoa rushwa na mpokeaji rushwa na anaeshuhudia na anaeandika”.
Lakini Serikali nayo inaichukia na inaipiga vita, ndio maana tunafanya jitihada za kushughulika nayo na tumelazimika kutunga Sheria ya Kuzuia na Rushwa na Uhujumu Uchumi. Kwa upande mwengine, wananchi nao wanaichukia rushwa na hawavipendi vitendo vinavyoambatana nayo. Wapo wananchi wanaovijua vitendo vinavyoashiria rushwa ambavyo vinafanywa katika maofisi yetu, inasemekana baadhi yao wanadiriki kuvisema. Tutawachunguza viongozi na watumishi wanaofanya vitendo hivyo, kwa kuzingatia sheria na taasisi zake, ili tuujue ukweli na hatimae tuchukue hatua. Iwapo mambo hayo yanayofanyika, wanayoyasema baadhi ya wananchi; ndio hayo yanayoitwa majipu, basi nataka niahidi, tutayatumbua na moyo wake tutautoa.
Nataka niwahakikishie wananchi kwamba, kauli yangu hii si maneno matupu bali yataambatana na vitendo.
Mheshimiwa Spika,
Vile vile, katika jitihada zetu za kusimamia matumizi bora ya fedha za umma, Serikali itadhibiti na kuzuwia safari za nje za kikazi zisizo za lazima. Semina, kongamano na mikutano inayofanywa kwa kutoa posho wakati wa saa za kazi, itawekewa utaratibu mpya. Serikali itahakikisha kuwa ubora wa miradi inayotekelezwa na ununuzi wa vifaa na huduma mbali mbali zinalingana na thamani ya fedha zilizotumika (Value for Money). Zipo taarifa kwamba kuna ubabaishaji mkubwa unafanyika, katika ununuzi wa vifaa na nyenzo. Ni jukumu la Watendaji Wakuu na wale wote wenye dhamana ya manunuzi na kuidhinisha miradi, kuzingatia Sheria Namba 9 ya 2005 ya Manunuzi na Uondoshaji wa Mali za Umma, wahakikishe kwamba taratibu zote za manunuzi zinafuatwa.
Nachukua nafasi hii, kuwahimiza viongozi watakaopewa nyadhifa mbali mbali kuwa wabunifu katika kupanga na kutekeleza mipango iliyo kwenye dhamana walizokabidhiwa. Ni vigumu kwenda katika kasi tunayoitaka ikiwa kila kiongozi atategemea maelekezo na mipango kutoka kwa Rais au Makamu wake ndipo atekeleze wajibu wake. Nawahimiza viongozi watakaopewa dhamana kutumia utaalamu wao kwa kuleta maendeleo na lazima waielewe mipango na sheria zinazohusiana na majukumu waliyopewa na taasisi wanazozifanyia kazi na kuzitekeleza ipasavyo. Lazima waifanye kazi ya kuwasimamia watumishi walio chini yao na wale watakaozikiuka sheria na taratibu watapaswa wawachukulie hatua na kuwawajibisha. Kama hawatafanywa hivyo, basi na wao watawajibishwa.
Mheshimiwa Spika,
Katika utekelezaji wa utawala bora, nitaendelea kuhakikisha kuwa Mihimili yetu Mitatu, (Serikali, Baraza la Wawakilishi na Mahkama), kila mmoja unafanya kazi ukiwa huru na kwa mujibu wa sheria zilizobainishwa katika Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984. Tutahakikisha kila muhimili unapata fedha za kuendesha shughuli zake kwa mujibu wa uwezo wa Bajeti ya Serikali na si zaidi ya hilo. Hapatakuwa na fedha za ziada, zaidi ya zile zitakazopitishwa katika bajeti.
BARAZA LA WAWAKILISHI
Mheshimiwa Spika,
Kwa mara nyengine tena, nakupongezeni Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza hili kwa kuchaguliwa na wananchi ili muwawakilishe katika Baraza hili la Tisa. Sote tunafahamu kwamba ili ushinde nafasi ya Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi, panahitajika juhudi na ujasiri mkubwa. Aidha, mgombea anahitaji busara, hekima, uvumilivu, ufasaha na uwezo wa kujieleza na mapenzi kutoka kwa wananchi. Hapana shaka, nyinyi mnapendwa na ni chaguo la wananchi. Kwa msingi huo, mtaithamini heshima waliyokupeni wananchi kwa kukuchagueni ili muwaongoze na mshirikiane nao katika jitihada za kuiletea maendeleo ya nchi yetu. Kazi iliyo mbele yetu ni kushikamana katika kuwahudumia wananchi kwa kuzingatia maadili ya uongozi na sheria mbali mbali zinazotuongoza.
Ni matumaini yangu kuwa mtatekeleza wajibu wenu kwa kuzingatia kifungu cha 88(a-d) cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 na kanuni za Baraza la Wawakilishi ziliopo; utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020 pamoja na mipango mengine ya maendeleo. Chombo hiki kinaendeshwa kwa taratibu za sheria na kanuni. Kwa hivyo, kila mjumbe anawajibika kuzifuata na kutekeleza majukumu yake kufuatana na sheria na kanuni hizo.
Nimefarajika kwa kuwepo mchanganyiko mzuri wa Waheshimiwa Wajumbe wapya pamoja na wale wa zamani, wenye uzoefu wa shughuli za Baraza la Wawakilishi. Mchanganyiko huo, unanipa matumaini makubwa kwamba shughuli za Baraza zitapata ufanisi mkubwa. Waheshimiwa Wajumbe wenye uzoefu, hamna budi kuwasaidia na kuwaongoza wajumbe wapya na wao wawe tayari kujifunza kutoka kwenu. Aidha, nimeridhishwa na kuwepo kwa idadi kubwa ya wajumbe wanawake na vijana katika Baraza hili, jambo ambalo limeongeza fursa ya uwakilishi wa makundi haya yenye idadi kubwa ya watu katika jamii yetu. Hongereni sana.
Naamini kwamba mtarejesha imani waliyokupeni wananchi wa Zanzibar, kwa kuunga mkono juhudi zangu za kupambana na rushwa, ubadhirifu na uhujumu wa uchumi katika nchi yetu. Kadhalika, mtafanya hivyo kwa michango mtakayoitoa katika Baraza hili na kwa vitendo kwa utekelezaji wa Sheria ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu wa Uchumi na Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma. Naelewa kwamba nyinyi ni makini na mahiri na sina shaka mtatekeleza wajibu wenu ipasavyo.
IDARA MAALUM ZA SMZ
Mheshimiwa Spika,
Idara Maalum za SMZ zimeonesha umahiri, ukakamavu na umakini wao katika kutekeleza Sera ya CCM ya kulinda na kudumisha amani nchini katika kipindi chote cha miaka mitano iliyopita. Idara Maalum zimeshirikiana vya kutosha na Vikosi vya Ulinzi na Usalama vya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuzima majaribio pamoja na kukomesha viashirio vya uvunjaji wa amani nchini.
Idara hizi ziko mstari wa mbele katika kutoa huduma za jamii kwa wananchi hasa elimu na afya kupitia taasisi, skuli, vyuo na hospitali zilizoanzishwa ndani ya vituo vya Idara Maalum. Vile vile, zimekuwa zikishiriki kikamilifu katika michezo ambapo zimefanikiwa kutwaa ubingwa katika mashindano mbali mbali.
Katika kipindi cha miaka mitano ijayo, Serikali itazidi kuziimarisha Idara Maalum za SMZ kwa kuwapatia watendaji wake mafunzo, vifaa vya kisasa na kuimarisha maslahi yao kadri hali itakavyoruhusu ili kuwawezesha kutekeleza majukumu ipasavyo. Nitatekeleza ahadi yangu niliyoitoa kwao wakati wa Kampeni za uchaguzi ya kuangalia upya maslahi yao ili yalingane na wenzao wa SMT kwa lengo la kuwapunguzia ukali wa maisha na kuongeza ufanisi katika kazi zao. Kama nilivyoeleza hapo mwanzo kwamba, suala hili litategemea uwezo wa Serikali katika kukusanya mapato. Uamuzi si tatizo na tayari nishaufanya.
USHIRIKIANO NA NCHI NYENGINE NA WAZANZIBARI WANAOISHI NJE
Mheshimiwa Spika,
Katika uongozi wangu, nitahakikisha Zanzibar, ikiwa ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inaendelea kuwa na uhusiano na mashirikiano mema na nchi mbali mbali duniani pamoja na Mashirika ya Kimataifa juu ya masuala mbali mbali ya kiuchumi, kisiasa na kijamii. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuimarisha ushirikiano na Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na Jumuiya nyengine za Kikanda ambazo Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni mwanachama.
Katika kipindi cha pili cha Awamu ya Saba, nitahakikisha tunazidi kukiimarisha Kitengo maalum nilichokianzisha cha kuratibu masuala ya Wazanzibari Wanaoishi Nchi za Nje ili kiendelee kuwashajiisha kushiriki katika shughuli za maendeleo ya nchi yetu. Nitaendelea kukutana nao kila ninapopata fursa ya kuzitembelea nchi wanazoishi, ili tubadilishane mawazo kwa maslahi ya nchi yetu. Tumedhamiria kuandaa Kongamano la Kimataifa la Wanadiaspora mwezi Agosti, 2016 ambalo litawashirikisha Wanadiaspora wa Zanzibar kwa jumla wanaoishi katika mataifa mbali mbali. Lengo la Kongamano hilo, ni kuushajiisha ushiriki wa Watanzania katika kupanga na kutekeleza mipango mbali mbali ya maendeleo ya nchi yetu.
Napenda nitoe shukurani zangu za dhati kwa “Wanadiaspora” kwa michango mikubwa wanayoendelea kuitoa, ya hali na mali, kwa ajili ya kuendeleza sekta za kiuchumi na kijamii hasa kuendeleza elimu, afya, biashara na uwekezaji. Nawaomba waendelee kuwa pamoja nasi kwani; ‘Mtu Kwao ndio Ngao’.
KUWAUNGANISHA WANANCHI WA ZANZIBAR
Mheshimiwa Spika,
Miongoni mwa majukumu tuliyoyatekeleza kwa ufanisi katika kipindi chote cha miaka mitano ya kwanza ni kuendeleza mshikamano, umoja na mapenzi baina ya watu wa Zanzibar bila ya kujali rangi, kabila, dini na itikadi zao za kisiasa. Mafanikio tuliyoyapata ni matunda ya kushiriki kila mmoja wetu katika kudumisha na kujenga mshikamano tukiwa na imani ya dhati kwamba Wazanzibari sote ni wamoja. Kuwepo kwa amani na utulivu ni mambo yaliyotupelekea kudumisha umoja wetu na kupata maendeleo makubwa.
Lazima nikiri kwamba dhamana ya kusimamia udugu na mshikamano tulionao ina changamato nyingi. Lakini changamoto hizo tumeweza kuzipatia ufumbuzi kwa sababu sote tuliufahamu wajibu wetu na tuliongozwa na hekima, busara na subira. Tulifahamu kwamba suala la amani, umoja na mshikamano tunajifanyia wenyewe na hatumfanyii mtu yeyote. Hii ndio siri ya mafanikio yetu.
Kwa kuzingatia hayo, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kutekeleza dhamana yangu, kwa kipindi chote cha miaka mitano na leo hii, Zanzibar iko salama na yenye utulivu mkubwa. Namuomba Mola atuvushe kwa salama katika kipindi cha miaka mitano ijayo na katika awamu nyengine zote zinazokuja. Nataka nikuhakikishieni nyinyi Waheshimiwa Wajumbe, niwahakikishie wananchi wote wa Zanzibar na Watanzania wote kwamba, nitaendelea kuwa muumini wa kweli wa amani na utulivu; na kufanya kila linalowezekana kwa ajili ya kuwaunganisha wananchi wa Zanzibar kwa lengo la kuimarisha udugu na mapenzi miongoni mwetu, ili nchi yetu iweze kupiga hatua zaidi za maendeleo.
Mheshimiwa Spika,
Nitaendelea kuyalinda maslahi ya Zanzibar na watu wake na kutimiza wajibu wangu wakati wote, bila ya kumuonea muhali mtu yeyote, kumfanyia chuki au kuogopa kama nilivyokula kiapo nilipoapishwa kuwa Rais. Kwa yeyote atakaejaribu kuibeza Katiba ya Zanzibar ya 1984 na kuchezea amani na utulivu tulio nao nitapambana nae. Nitaendelea kutumia hekima na busara kwa ajili ya kuyalinda Mapinduzi ya tarehe 12 Januari, 1964 na kuyalinda maslahi ya Zanzibar na watu wake.
Nayasema haya kwa dhati ya moyo wangu. Hii ndio imani yangu na ninaamini kuwa nyote mko tayari kwa kuyalinda Mapinduzi ya tarehe 12 Januari, 1964 na kuyatetea maslahi ya Zanzibar na watu wake na Tanzania kwa jumla.
Nafarijika kuona kwamba viongozi wa dini zilizopo nchini na wananchi wote wenye kuifahamu historia na kuitakia mema nchi yetu na Muungano wetu wapo pamoja nasi katika kudumisha amani itakayotupelekea kuyafikia malengo ya Mapinduzi yetu Matukufu ya tarehe 12 Januari, 1964. Kwa misingi huo, sote tuelewe kuwa suala la kudumisha mshikamano ni la kila mmoja wetu wakiwemo viongozi wa Serikali, vyama vya siasa, madhehebu ya dini na viongozi wengine katika jamii na wananchi wote kwa jumla. Kila mwananchi hana budi atii, ayaheshimu matakwa ya Katiba ya Zanzibar ya 1984, Sheria zake na kanuni mbali mbali zilizotungwa katika kuendesha shughuli za kiserikali na kijamii. Huu ni wajibu wetu hatuwezi kuukwepa na hatuna budi lazima tuutekeleze.
Mheshimiwa Spika,
Sote tunafahamu kwamba tarehe 20 Machi, 2016, tulikuwa na Uchaguzi Mkuu wa marudio ulioendeshwa na kusimamiwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya 1984 na Sheria ya Uchaguzi Nambari 11 ya mwaka 1984. Madhumuni ya uchaguzi huo yalikuwa ni kuchaguliwa kwa viongozi wa vyama vya siasa wakataoingoza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.
Katika Uchaguzi Mkuu huo wa Marudio wa tarehe 20 Machi, 2016 nafasi ya Rais iligombewa na vyama 14 vya siasa na hakukuwa na Chama chochote zaidi ya Chama cha Mapinduzi, kilichopata matokeo ya kura za Uchaguzi wa Rais kwa zaidi ya asilimia 10. Mimi nikiwa Mgombea wa Urais wa CCM, nilipata asilimia 91.4. Kadhalika, hakukuwa na Chama cha siasa zaidi ya CCM chenye wingi wa Viti vya Majimbo katika Baraza la Wawakilishi. Kwa kuzingatia msingi huo, na kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 39(3) cha Katiba ya Zanzibar ya 1984, hakuna Chama cha siasa ambacho kinakidhi masharti ya kustahiki kutoa Makamo wa Kwanza wa Rais ili kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Huo ni uamuzi wa wananchi wa kukipa ushindi mkubwa Chama cha Mapinduzi na hawakutoa nafasi ya kumchagua Makamu wa Kwanza wa Rais. Huo ni uamuzi wao wa kidemokrasia. Kadhalika, uteuzi wa nafasi ya Makamo wa Pili wa Rais umewekewa masharti na kifungu cha 39(6),
kuwa:-
(i)Atateuliwa kutoka miongoni mwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi.
(ii)Atoke katika chama anachotoka Rais. Uteuzi nilioufanya wa kumteua Makamu wa Pili wa Rais umekidhi matakwa ya kifungu cha 39(6) cha Katiba ya Zanzibar ya 1984.
Nimelazimika nilieleze jambo hili la kikatiba, kwa sababu wapo waliodhani kuwa yupo Mgombea anayestahiki kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais, lakini Rais amekataa kumteua na hivyo Katiba imekiukwa. Nililolifanya, la kumteua Balozi Seif Ali Iddi kuwa Makamo wa Pili wa Rais ni sahihi na ni kwa mujibu wa Katiba na nimechukua hatua ya kuunda Serikali kwa kuzingatia Katiba ya Zanzibar ya 1984.
Mheshimiwa Spika,
Nataka niwahakikishie Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza lako tukufu, kwamba Serikali nitakayoiunda itasimamia misingi ya haki, uwajibikaji, uwazi na usawa kwa wananchi wote, bil ya kumbagua mtu yeyote kutokana na itikadi yake, dini yake, jinsia au eneo analotoka. Mimi ni Rais wa wananchi wote wa Zanzibar. Nitashirikiana na viongozi mbali mbali, wa vyama vya siasa, viongozi wa dini, na kadhalika. Zanzibar ni yetu sote, viongozi wa vyama vya siasa tuna jukumu la kushikamana na kuwatumikia wananchi kwa ajili ya maendeleo yao.
Nataka nirudie ule usemi wangu wa mwanzo kwamba, viongozi jukumu letu hivi sasa, kila mmoja wetu na sote kwa pamoja tufanye kazi kwa bidii na maarifa tupate maendeleo tunayoyakusudia. Uchaguzi umekwisha na washindi wamepatikana ambao wataiongoza nchi yetu kwa kipindi cha miaka mitano ijayo, hadi hapo utakapofanyika uchaguzi mwengine mwaka 2020.
KUIMARISHA MUUNGANO
Mheshimiwa Spika,
Suala la kulinda na kudumisha Muungano wetu wa Serikali mbili, kwangu halina mbadala. Nitaendelea na juhudi za kudumisha Muungano wetu wa Tanganyika na Zanzibar wa Serikali mbili, ulioasisiwa mwaka 1964 ambao unatimiza Miaka 52 ifikapo tarehe 26 Aprili 2016.
Waheshimiwa Wajumbe, tuna wajibu wa kuhakikisha kwamba Serikali zetu mbili, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zinaendelea kuimarisha mashirikiano na kufanya kazi kwa umoja na ukaribu zaidi katika kupanga na kuitekeleza mikakati ya uchumi na mipango mengine ya maendeleo. Nitaiongoza vyema Zanzibar na kuhakikisha kwamba tunaimarisha mashirikiano, udugu na mapenzi baina ya watu wa pande mbili hizi. Nitaendelea kushirikiana na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kudumisha hali ya amani na utulivu, iliyodumu tangu kuundwa kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Aprili, 1964.
Mheshimiwa Spika,
Kutokana na kazi nzuri ya kuzipatia ufumbuzi changamoto au kero mbali mbali za Muungano wetu, iliyofanywa katika kipindi kilichopita, ni mambo machache tu ndio yaliyobaki kupatiwa ufumbuzi. Kwa yale mambo yanayohitaji taratibu za kisheria, naamini kwamba Baraza lako, Mheshimiwa Spika, litatimiza wajibu wake ipasavyo. Kwa kufanya hivyo, mtachangia kwa kiasi kikubwa katika kuudumisha Muungano wetu na kuwarahishia wananchi kutekeleza shughuli zao za kiuchumi na kijamii.
MWISHO
Mheshimiwa Spika,
Namalizia hotuba yangu kwa kukupongeza kwa mara nyengine tena Mheshimiwa Spika, kwa kuchaguliwa kuliongoza Baraza hili. Nakutakia mafanikio katika kutekeleza majukumu yako mazito yenye umuhimu kwa maendeleo ya nchi yetu. Vile vile, napenda kukupongezeni kwa mara nyengine tena, Waheshimiwa Wajumbe, kwa heshima kubwa mliyopewa na wananchi ili muwaongoze na muwawakilishe katika Baraza hili. Natoa pongezi kwa Waheshimiwa wote waliochaguliwa katika nafasi mbali mbali za uongozi pamoja na watendaji wote wa Baraza hili, wakiongozwa na Katibu wa Baraza la Wawakilishi Dkt. Yahya Khamis Hamad. Nakutakieni kila la kheri na mafanikio katika kuwatumikia wananchi wote kwa jumla.
Natoa shukurani maalum kwa wamiliki wa vyombo vya habari na watendaji wao kwa mashirikiano yao na kutangaza habari zinazohusu nchi yetu na hafla hii ya uzinduzi wa Baraza hili. Shukurani za pekee ziwaendee wananchi wote kwa jumla kwa kunisikiliza kwa utulivu kwa muda wote niliokuwa nikiwasilisha hotuba yangu. Namuomba Mwenyezi Mungu aturahisishie utekelezaji wa majukumu tuliyopewa, atuzidishie mapenzi na mshikamano baina yetu na aijaze baraka na neema nchi yetu.
Baada ya kusema hayo, sasa natamka kwamba Baraza la Tisa la Wawakilishi la Zanzibar limezinduliwa Rasmi, leo tarehe 05 Aprili, 2016.
MUNGU IBARIKI ZANZIBAR
MUNGU IBARIKI TANZANIA
MUNGU IBARIKI AFRIKA
Ahsanteni kwa kunisikiliza.