Hotuba ya msemaji mkuu wa Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni katika Wizara ya Fedha

Mwanahabari Huru

JF-Expert Member
Mar 9, 2015
14,243
34,899
HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI KATIKA WIZARA YA FEDHA NA MIPANGO MHESHIMIWA HALIMA JAMES MDEE (MB) AKIWASILISHA BUNGENI MAONI YA KAMBI RASMI YA UPINZANI KUHUSU MAPENDEKEZO YA MPANGO WA MAENDELEO WA TAIFA 2017/18

Inatolewa chini ya Kanuni ya 94(5) (a) ya Kanuni za Kudumu za Bunge,
Toleo la Januari, 2016
___________________________________
UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia sote afya na uzima na kutuwezesha kukutana tena katika Mkutano huu wa tano wa Bunge tukiwa salama. Aidha, nawapongeza viongozi viongozi wakuu wa CHADEMA na UKAWA kwa jumla kwa kazi kubwa wanayofanya ya kutetea na kulinda misingi ya demokrasia hapa nchini ambayo kwa sasa ipo katika majaribu makubwa.
Mheshimiwa Spika, kabla sijatoa maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuhusu mapandekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2017/18 uliopo mezani; napenda niweke rekodi sawa kuhusu uwasilishwaji wa Mpango. Kumekuwa na ukiukwaji mkubwa wa Katiba, Sheria na hata Kanuni za Bunge katika uwasilishaji wa Mapendekezo ya Mipango ya Maendeleo ya Taifa jambo ambalo limechangia kwa kiasi kikubwa utekelezaji hafifu wa Mipango hiyo.
Mheshimiwa Spika, wakati Kanuni ya 94(1) ya Kanuni za Kudumu za Bunge inaelekeza kwamba Bunge litakaa kama Kamati ya Mipango katika mkutano wake wa mwezi Oktoba Novemba kila mwaka ili kujadili na kuishauri Serikali kuhusu mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali katika mwaka wa fedha unaofuata; kifungu cha 21(2) cha Sheria ya bajeti ya mwaka 2015 kinaelekeza kwamba mapendekezo ya Mpango pamoja na makisio ya bajeti yatawasilishwa katika mkutano wa Bunge wa mwezi Februari kila mwaka au kama Bunge halipo kwenye mkutano katika mwezi wa februari basi katika wiki ya kwanza ya mkutano huo utakapoitishwa.
Mheshimiwa Spika, huu ni mgongano wa wazi kati ya Kanuni za Bunge na Sheria ya bajeti kuhusu uwasilishwaji wa Mpango na makisio ya bajeti katika mwaka wa fedha unaofuata. Uzoefu unaonyesha kwamba pale kunapotokea mgongano kati ya kanuni na sheria; sheria ndio husimama, lakini kwa hapa Bungeni mambo yamekuwa tofauti kwa sababu sheria imewekwa kando na badala yake Kanuni za Bunge ndio zimesimama.
Mheshimiwa Spika, tukizingatia matakwa ya kifungu cha 21(2) cha sheria ya bajeti, mapendekezo haya ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa yalitakiwa yawasilishwe katika Bunge la Jaunuari Februari. Na mantiki ya sheria ya bajeti hapa; kwa mujibu wa kifungu cha 21(3) cha sheria hiyo, ni kutoa mwanya wa kufanya tathmini ya utekelezaji wa bajeti kwa mwaka wa fedha unaoendelea (current financial year) na makisio ya hali ya uchumi kwa mika mitatu ya fedha inayofuatia. Na ili tathmini hiyo iweze kutoa mwanga wa mwelekeo wa utekelezaji wa bajeti basi angalau iwe ni tathmini ya robo ya pili au nusu ya kwanza ya mzunguko wa bajeti.
Mheshimiwa Spika, na Waheshimiwa Wabunge, tathmini iliwasilishwa hapa ni tathmini ya robo ya kwanza ya mzunguko wa bajeti ambayo inaishia tarehe 30 Septemba. Robo ya pili inayoishia tarehe 30 Disemba, haijaguswa kabisa kutokana na ukweli kwamba hatujafika huko. Kutegemea tathmini ya robo ya kwanza ambayo utekelezaji wake ni chini ya robo kwa ajili ya kufanya makisio ya miaka mitatu mfululizo ni kutumia vibaya maudhui ya tathmini na faida zake katika kusaidia kufanya makisio ya bajeti za miaka mitatu inayofuata.
Mheshimiwa Spika, kutokana na mgongano huo wa Kanuni za Bunge na Sheria ya bajeti, Kambi Rasmi ya Upinzani inatoa wito kwako wewe Mheshimiwa Spika, kuiagiza Kamati ya Kanuni kufanya marekebisho ya Kanuni ya 94(1) ili izingatie matakwa ya kifungu cha 21 (2) cha Sheria ya bajeti ya 2015 kwa ajili ya utekelezaji bora wa shughuli za Bunge kwa manufaa ya wananchi.

UONGOZI MBOVU UNAVYOCHANGIA KUYUMBA KWA UCHUMI
Mheshimiwa Spika, licha ya mbwembwe nyingi za Serikali ya awamu ya Tano, inayotokana na Chama kilichokaa madarakani toka mwaka 1961 tumeshuhudia;
‘Serikali iliyotengeneza watumishi hewa ikisitisha ajira kwa kigezo kuwa inafanya uhakiki wa watumishi wake, jambo hili limepelekea kuyumba kwa uchumi kwa baadhi ya familia ambazo zina watu wenye sifa ya kuajiriwa katika sekta ya umma kama vile waalimu,manesi na madaktari. Kusimamishwa huku kwa ajira kumewafanya nguvu kazi iliyokuwa na uwezowa kuzalisha kuishi kama ombaomba !

Serikali hii ikiwaumiza sana wafanyabiashara wakubwa na wa kati kwa kukamata mali zao kama Rais alivyofanya kwa kukamata mali za mfanyibiashara kwa kitanzania Salim Baharesa ,sukari yake ilishikiliwa na serikali bila kutoa sababu zozote zile na Rais aliamua kuachia sukari hiyo bila kutoa sababu zozote za maana kwa umma. Hali iko hivyo kwa wafanyabiashara wengi ambao akaunti zao Benki zimeshikiliwa na Serikali bila kuelezwa sababu, jambo linalopelekea kuporomoka kwa uchumi kwa kasi katika taifa letu.

Kambi rasmi inaunga mkono hatua za kisheria kuchukuliwa kwa wale wote waliokuwa wanahusika kwa namna moja au nyingine kuhujumu uchumi, lakini tunapinga kwa nguvu zote kwa dola kutumia mamlaka yake kuonea au kunyanyasa wafanyabiashara wanaofanya shughuli zao kwa kufuata sheria na taratibu za nchi!
Sekta ya kilimo imeathirika sana hasa kutokana na uamuzi wa Benki kuu kuzuia baadhi ya Benki kukopesha wakulima kama ilivyofanya kwa Benki ya Maendeleo ya kilimo kwa hoja kuwa kama wakiendelea kukopesha miradi ya kilimo hakuna uhakika wa mikopo hiyo kurejeshwa.
Sekta ya Hoteli na utalii iko ICU na hasa kutokana na uamuzi wa serikali kuanzisha kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kwenye huduma zote za utalii jambo ambalo limepelekea kushuka kwa idadi ya watalii wanaotembelea nchi yetu na hivyo kufanya hoteli zilizokuwa zinafanya biashara ya utalii pamoja na makampuni yaliyokuwa yakijihusisha na biashara ya utalii kwa ujumla.
Serikali za mitaa zimeathirika sana kutokana na uamuzi wa serikali kuamua kukusanya kodi ya Majengo kupitia TRA badala ya Halimashauri ambazo awali zilikuwa zikifanya jukumu hilo, na hasa ikizingatiwa kuwa uamuzi huu ulifanyika baada ya bajeti za Halimashauri kupitishwa na TAMISEMI na kuwa miongoni mwa vyanzo vya mapato ya Halimashauri husika. Ni mwezi wa nne sasa toka uamuzi huu ufanywe na serikali na kuthibitishwa na Bunge TRA haijaweza kukusanya kodi husika! Halmashauri ziko katika ukata Mkubwa sababu ni moja ya vyanzo vinavyotegemewa kwa shughuli za Maendeleo!

sekta ya afya imekuwa ikizorota kwa kasi kubwa .Hivi karibuni tumeshuhudia ukosefu mkubwa wa madawa, chanjo na vifaa tiba katika Hospitali zetu mbalimbali hapa nchini. Hali hii imepelekea wananchi kupoteza maisha kutokana na kukosekana kwa dawa na kundi la watoto limeathirika sana kutokana na kukosekana kwa chanjo kwenye hospitali zetu. Huku tukishuhudia mgongano wa kauli kati ya waziri wa afya na Makamu wa Rais. Waziri akidai dawa ziko tele.huku bosi wake akisema hali ni mbaya!
Sekta ya elimu ikizidi kwenda mrama baada ya Serikali ya matukio kudandia hoja ya elimu bure bila kuwa na maadalizi ya kutosha na ya kuweza kutekeleza ajenda hiyo. Hali katika shule za umma imekuwa mbaya sana kutokana na serikali kushindwa kupeleka fedha za uendeshaji kwenye shule hizo na hivyo kufanya suala zima la elimu ya msingi na Sekondari kuwa katika hali mbaya na huenda baada ya muda mfupi ujao shule hizi zinaweza kuanguka kutokana na kukosekana kwa fedha za uendeshaji.

Wakati kwenye maandiko ya mpango Serikali inajitapa kwamba itaendelea kutoa ruzuku ya uendeshaji (capitation)ya shilingi 10,000/= kwa kila Mwanafunzi kwa shule za Msingi/awali/maalum na shilingi 25,000/= kwa kila mwanafunzi wa sekondari wa kutwa na bweni.Ukweli ni kwamba kwa kipindi kiasi kinachotolewa kwa wastan huwa ni shilingi 1000 kwa shule za msingi na shilingi 7,000/= kwa shule za sekondari.

Mheshimiwa Spika, mwezi Septemba 2016, Serikali ilitenga fedha kwa ajili ya kugharimia elimu bure kiasi cha shilingi 18,777,000,000 ambapo kiasi cha shilingi 15,714,000,000 kinatakiwa kupelekwa Halimashauri na shilingi 3,063,000,000 zinatakiwa kupelekwa NECTA kwa ajili ya fidia ya mitihani.Kwa mujibu wa tovuti kuu ya takwimu huria ya serikali (www.pendadata.go.tz) takwimu za mwezi machi 2016 zinaonyesha kuwa serikali ina jumla ya shule za msingi 16,084 zenye jumla ya wanafunzi 8,340,128 kwa nchi nzima .
Kwa takwimu hizi za idadi ya wanafunzi maana yake ni kuwa serikali inatenga kiasi cha shilingi 1,884/= kwa mwezi kwa kila mwanafunzi wa shule ya msingi .
Tumeshuhudia, serikali ambayo Mgombea wake wa Urais wakati akiomba kura aliwaahidi watanzania kwamba hakuna mwanafunzi atakayekosa mkopo wa elimu ya juu,huku akiwashangaa watangulizi wake kwa kushindwa kulitafutia ufumbuzi huku akidai yeye ndio mwarobaini wa tatizo, ikiwanyima mkopo wanafunzi 27,053! katika vyuo vikuu mbalimbali nchini kwa mwaka huu wa masomo. Huku Wanafunzi waliopata Mikopo wakiwa 20,183 tu!!!!. Hakika watanzania wanaisoma namba Tuliposema tuanze kuujenga ukuta kuzuia udhalimu unaoendelea katika nchi yetu kuna ambao hawakutuelewaMkono wa chuma unagusa mmoja baada ya mwingine!

Aidha ikumbukwe kuwa, serikali inadaiwa na vyuo mbalimbali nchini kiasi cha shilingi bilioni 60.798 ambazo ni fedha za ada za wanafunzi walizokopeshwa lakini serikali haikupeleka mkopo huo kwenye vyuo husika kwa mwaka wa masomo 2015/16. Jambo hili linahitaji kufuatiliwa kwa kina kwani likiachwa kama lilivyo litasababisha vyuo kushindwa kujiendesha kwani na kugharimia gharama nyingine za uendeshaji

Tumeshuhudia Serikali ya CCM ikijitapa kutumbua majipuiliyoyatengeneza yenyewe kwa mbwembwe nyingi, kumbe nyuma ya pazia serikali hiyo hiyo inayalipa majipu hayo mishahara pamoja na marupurupu mengine kama kawaida! Mwezi Septemba kiasi cha shilingi 2,199,740,340 (bilioni 2.1) zilitengwa kwa ajili ya kuwalipa viongozi ambao walitumbuliwa kikiwemo kiasi cha shilingi 196,842,000 kama posho ya usumbufu.

SERIKALI YA AWAMU YA TANO YAANZA NA MDORORO WA UCHUMI
Mheshimiwa Spika, ni bahati mbaya kwamba mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka wa fedha 2017/18 yanaletwa mbele ya Bunge hili kujadiliwa na kupitishwa wakati ambapo hali ya uchumi wa nchi yetu ikiwa imeporomoka vibaya ndani ya kipindi cha mwaka mmoja tu tangu Serikali hii ya awamu ya tano iingie madarakani.
Kwa mujibu wa Taarifa Kuhusu Hali ya Uchumi wa Tanzania iliyotolewa na Benki Kuu ya Tanzania Septemba,2016 imeonyesha kuwa hali ya uchumi wa taifa inaenda mwendo wa kusuasua karibia katika sekta zote hapa nchini.
Taarifa hiyo inaonyesha kuwa Katika robo ya kwanza ya mwaka 2016, ukuaji wa Pato la Taifa unakadiriwa kukukua kwa asilimia 5.5 ikilinganishwa na ongezeko la asilimia 5.7 kipindi kama hicho mwaka 2015
Kuporomoka huku hakujawahi kufikiwa kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita kwani takwimu zinaonyesha kuwa katika robo ya kwanza tangu mwaka 2011 ukuaji wa pato la Taifa ulikuwa kama inavyoonekana kwenye mabano, 2011 (7.9), 2012 (7.1),2013(6.3),2014 (8.2) na 2015 (5.7)
Kwa mujibu wa ripoti hiyo shughuli zilizochangia ukuaji huu wa uchumi kwa kiasi kikubwa ni pamoja na kilimo (asilimia 11.7), biashara (asilimia 10.6), uchukuzi (asilimia 10.1), sekta ya fedha (asilimia 10.1) na mawasiliano (asilimia 10.0). Shughuli za kiuchumi zilizokua kwa kasi ya juu zaidi katika robo ya kwanza ya mwaka 2016 ni sekta ya fedha (asilimia 13.5), mawasiliano (asilimia 13.4), na utawala wa umma (asilimia 10.2)
Pamoja na taarifa hiyo kuonyesha kuwa uchumi unaimarika lakini wakati huohuo taarifa hiyo imeonyesha kuyumba kwa uchumi katika sekta zifuatazo;
Mikopo itolewayo na mabenki ya biashara kwenye sekta binafsi, imeendelea kushuka katika nusu ya kwanza ya mwaka 2016 na kuwa Shilingi bilioni 1,167.2, ikilinganishwa na ongezeko la Shilingi bilioni 1,577.5 la mwaka 2015 katika kipindi kama hicho.Hii maana yake ni kuwasekta binafsi imenyanganywa au imekosa takribani shilingi Bilioni 410.3 katika nusu ya kwanza ya mwaka 2016.Hali hii imepelekea mzunguko wa sarafu na noti mikononi mwa watu kushuka kutoka asilimia 18.8 Disemba 2015 na kufikia asilimia 6.7 Mwezi Julai ,2016.
Amana za wateja katika mabenki zilipungua kutoka shilingi trilioni 20.52 mwezi Desemba 2015 hadi kufikia shilingi trilioni 20.24 mwezi June 2016.
Katika miezi sita ya kwanza ya mwaka 2016, nakisi ya urari wa biashara ya bidhaa, huduma na uhamisho mali nchi za nje (current account deficit) ilipungua kwa asilimia 61.7 na kufikia nakisi ya dola za Kimarekani milioni 970.4, kutoka nakisi ya dola za Kimarekani milioni 2,532.5 mwaka 2015. Kupungua huko kulitokana zaidi na ongezeko la thamani ya bidhaa za viwandani, mapato yatokanayo na utalii na huduma za usafirishaji nje ya nchi, pamoja na kupungua kwa thamani ya bidhaa zilizoagizwa kutoka nje ya nchi hususan bidhaa za mitaji, na bidhaa za matumizi ya kawaida katika kipindi hiki
Hadi mwezi June 2016, akiba ya fedha za kigeni ilifikia dola za Kimarekani milioni 3,870.3 ambazo zinatosheleza kuagiza bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi kwa takriban miezi 4 tu ,hali ambayo hairidhishi hata kidogo kwa taifa ambalo halijatoka vitani nah ii imeendelea kusababisha kushuka kwa dhamani ya shilingi nchini
Deni la Taifa limeendelea kuongezeka kwa kasi

Mheshimiwa Spika, taarifa hiyo ya Benki Kuu inaendelea kuonyesha kwamba; shughuli za uchumi zinazohusu wananchi masikini zimeshuka kutoka kasi ya ukuaji ya 10.20% katika robo ya mwisho ya mwaka 2015 mpaka 2.7% katika robo ya kwanza ya mwaka 2016, ikiwa ni punguzo la 8% ndani ya kipindi kisichozidi miezi sita. Hii ina maanisha kwamba Wananchi wetu wanazidi kuzama kwenye dimbwi la umasikini na ufukara kwa kasi kubwa tangu awamu ya tano ya Serikali ya Chama Mapinduzi iingie madarakani
Mheshimiwa Spika, wakati Benki Kuu ya Tanzania inatoa takwimu hizi za kiuchumi zinazoonesha kuwa uchumi unasuasua; Serikali kupitia TRA imekuwa ikijigamba kwamba makusanyo ya mapato yameongezeka na kwamba uchumi uko imara.
Mheshimiwa Spika, kwa utafiti mdogo wa kiuchambuzi uliofanywa na Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ni kwamba; mapato ambayo TRA inasema yameongezeka ni hewa. Hii ni kwa sababu bandari ambayo ndio chanzo kikuu cha Mapato ya Serikali imekumbwa na mtikisiko mkubwa kutokana na mizigo inayoingia kupitia bandari hiyo kushuka kutoka tani hadi 25,000 kwa siku hadi tani chini ya 5,000 kwa siku.(- Rejea taarifa za TRA zinazoonyesha tozo mbali mbali kama ilivyoonyeshwa katika kurasa za mbele)
Mheshimiwa Spika, kinachoipa kiburi TRA na kujigamba kwamba mapato yameongezeka ni ujanja wa kuwalazimisha wafanyabiashara na walipa kodi wengine kulipa kodi ya mbele kabla ya muda wa kulipa kodi hiyo kufika. Imebainika kwamba kama mlipa kodi analipa kodi ya mwezi; sasa TRA inamshawishi kulipa kodi hiyo kwa miezi sita au mwaka bila kujali stability ya mapato ya mlipa kodi huyo. Hali kadhali mlipa kodi anayetakiwa kulipa kodi yake kwa mwaka sasa analazimika kulipa kodi hiyo kwa miaka mitatu au mitano kwa mkupuo mmoja. Kwa maneno rahisi ni Kwamba sasa Serikali inakopa kodi kwa wananchi. Hivyo inaonekana kuwa makusanyo ni mengi lakini kimsingi ni makusanyo ya miaka ya mbele, na sio ya mwaka huu wa fedha. Kwa hali hii sina hakika hiyo miaka ya mbele tutakuwa na makusanyo gani na sijui tutakuwa na akiba kiasi gani kuweza kuendesha nchi.
Mheshimiwa Spika, jambo jingine linalowafanya TRA wafikiri mapato yameongezeka ni kitendo cha kukusanya maduhuli (mapato yasiyo ya kodi) na kuyaingiza moja kwa moja kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali (Hazina) tofauti na ilivyokuwa hapo kabla.
Mheshimiwa Spika, Majigambo yote hayo ya Serikali na vyombo vyake vya ukusanyaji mapato kwamba mapato yameongezeka ni hila ya kuwahadaa wananchi ili Serikali hii ya awamu ya tano ipate uhalali kwa wananchi lakini kimsingi mapato yameshuka kwa kiwango kikubwa sana jambo ambalo pia limesababisha fedha kupotea katika mzunguko wake.
Mheshimiwa Spika, nyote ni mashahidi kwamba miezi michache iliyopita Rais alisema kwamba kuna watu wameficha fedha majumbani ndio maana fedha hazipo katika mzunguko. Aidha, Rais alitishia kuchapisha noti mpya ili hao walioficha fedha wapate hasara. Huo ni ushahidi kwamba hakuna fedha, na sababu yake kubwa ni kwamba hakuna mzunguko wa biashara na hivyo hakuna mapato. Sasa Serikali ituambie hayo mapato inayosema yameongezeka yametoka wapi ikiwa fedha imepotea kwenye mzunguko?
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kuwa wazi na kuwaambia wananchi ukweli kuliko kuwadanganya kuwa mapato yameongezeka wakati hali ya maisha inazidi kuwa ngumu. Aidha, Serikali izingatie demokrasia na utawala wa sheria. Hii misuli ya Serikali ya kutoa matamko kila kukicha na kukandamiza shughuli za kikatiba za kisiasa za vyama vya upinzani vinawatisha wawekezaji wakubwa na hivyo kuwafanya wazuie mitaji yao kuingia kwenye mzunguko kwa hofu kwamba pengine kutatokea machafuko ya kisiasa halafu wakapata hasara. Hivyo Rais, na vyombo vyake vya dola wajitazame upya mienendo yao katika kuendesha Serikali yamkini mienendo hiyo ndiyo imepelekea anguko hili la uchumi wa nchi yetu.

KUPOROMOKA KWA SHEHENA YA TRANSIT KATIKA BANDARI YA DAR ES SALAAM
Mheshimiwa Spika, hakuna mashaka tena kwamba shehena ya mizigo bandarini imepungua sana hivyo kuathiri mapato ya serikali. Majibu ya serikali katika hoja hii ni kwamba, wafanyabiashara wakwepa kodi wamekimbia bandarini hapo kutokana na kubanwa na serikali na hoja nyingine ni kwamba mizigo ya transiti imekuwa haivuki mipakani na hivyo kubakishwa hapa hapa nchini kwa matumizi ya ndani.
Mheshimiwa Spika, sababu tajwa hapo juu zina ukweli wake kwa kiwango fulani, lakini sio sahihi kwa 100%. Kuna sababu nyingine ambazo zinalalamikiwa kama chimbuko kwa bandari yetu kukimbiwa, na kama hatua zisipochukuliwa na tukiendelea kujidanganya, athari itakuwa kubwa sana:
Sababu zinazotajwa na wadau wakuu wa Bandari ni Pamoja na:
Uanzishwaji wa himaya ya forodha kati Tanzania na DRC. Ina maana shehena yote ya DRC ushuru ukusanywe wakati shehena hiyo ikiwa bandari ya Dar es salaam . Baadhi ya wafanyabiashara wanaona wanaweza pata hasara iwapo mzigo hautaweza fika DRC.
Uanzishaji wa sheria ya kutoza VAT katika huduma ya shehena ya Transiti inayopita katika bandari na mipaka ya Tanzania mfano. Wharphage, storage, customs rent, stevedoring ,transport shipping line delivery nk..katika kila huduma ,kuna ongezeko la 18% kinyume kabisa na Mkataba wa Viena Program OECD Organisation for economic cooperation ambao Tanzania ni Signatory. Kwa mfano kwa tozo ya wharphage peke yake, wakati bandari ya Mombasa wanatoza dola 70 za kimarekani kwa makasha ya futi 20, bandari ya Dar es salaam tunatoza dola 240. Halikadhalika wakati Mombasa wanatoza dola 105 (Import Transit) kwa makasha ya futi 40, Dar es salaam tunatoza dola 420.
Tozo za storage na customs warehosung rent (Hiki ni kitu kimoja lakini wameweka majina mawili tofauti ilimradi mtu alipe bila sababu ya msingi.
Taasisi ya Mkemia Mkuu wa serikali kwa shehena za kikemikali inatoza tozo kubwa kuliko nchi zingine. Tanzania inatoza dola 1 hadi 2 za kimarekani kwa kila tani moja ya shehena kulingana na aina ya kemikali. Kama kuna shehena ya tani 30,000 ina maana italipiwa zaidi ya dola 30,000 za kimarekani. Nchi nyingine kama Afrika Kusini wanatoza kila Bill of Lading dola 100 tu.
Muda mdogo wa bidhaa ya mafuta kukaa bandarini (wet cargo). South Africa inatoa siku 180, Msumbiji inatoa siku 90 , Tanzania siku inatoa 30. Siku 30 kiutendaji, kwa vyovyote hazitoshi kusafirisha mzigo.
Ongezeko la gharama za vibali vya usafirishaji kwenda nchi Jirani kwa malori ya Tanzania. TRA imepandisha toka dola zakimarekani 12 mpaka dola 200 kwa kila lori.
Kila container moja la futi 40, lina ongezeko la gharama ya dola za kimarekano 180.
Mheshimiwa Spika, kwa mwenendo huo ni wazi kwamba wafanyabiashara wengi wataikimbia bandari yetu. Kambi rasmi ya upinzani Bungeni inaitaka serikali kulieleza Bunge hili mikakati ambayo inafanya kulipatia ufumbuzi jambo hilo.





5. DENI LA TAIFA
Mheshimiwa Spika, taarifa za Mwongozo wa kutayarisha Mpango na Bajeti ya mwaka 2017/18 iliyotolewa na Wizara ya fedha na Mipango, Deni la Taifa likijumuisha deni la ndani na la nje) lilifikia dola za kimarekani milioni 18.614 (sawa na shilingi trillion 40.9) ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 9.8 kufikia Juni, 2016; ikilinganishwa na dola za kimarekani milioni 16.9 ( shilingi trillion 37.180) katika kipindi kama hicho mwaka 2015.(ongezeka la shilingi trillion 3.72 katika kipindi cha mwaka 1)
Mheshimiwa Spika, endapo deni hili litajumuishwa na madai ya mifuko ya hifadhi ya jamii (yanayokadiriwa kufikia trillion 3.2 ) na deni la nje la sekta binafsi la dola za kimarekani 2.829.3 (shilingi trillion 2.8 ) jumla ya Deni la taifa litakuwa Dola za kimarekani milioni 23.093 katika kipindi hicho, sawa sawa na shilingi za kitanzania trillion 50.8.
Mheshimiwa Spika, deni hili la sugu linazidi kukua kutokana na ukweli kwamba kile kinachoitwa kulipwa kwa deni la Taifa, sio kulipa kwa lengo la kupunguza deni, bali ni kupunguza makali ya kudaiwa kwa kulipia gharama za kusogeza mbele deni! Ukweli huu unadhihirika na maandiko ya serikali inayoonyesha kwamba kwa mwaka 2015/16, malipo ya deni la Taifa yalifikia shilingi trillion 4.996! ambapo malipo ya shilingi trillion 4.015 yalikuwa malipo ya deni la ndani na shilingi bilioni 980 yalikuwa ni malipo ya deni la nje.
Mheshimiwa Spika, kati ya fedha za deni la ndani ( trillion 4.015) zinazodaiwa kulipwa, shilingi tillion 3.006 zilikuwa ni kwa jili ya kuahirisha deni lililoiva na shilingi trillion 1.009 ilikuwa ni malipo ya riba!

6. UHIMILIVU WA DENI LA TAIFA
Mheshimiwa Spika, imekuwa ni kawaida kwa serikali kubadilisha takwimu za uhimilivu wa deni la Taifa ili kujipa uhalali wa kuendelea kukopa! Ikumbukwe kwamba wakati Mhe Jakaya Mrisho Kikwete anaingia madarakani kupitia CCM,mwaka 2005 deni la Taifa lilikuwa shilingi za kitanzania Trillion 7 tuMiaka 11 baadae chini ya utawala huu huu wa CCM, deni la Taifa limeongezeka na kufikia shilingi trillion 50!!
Mheshimiwa Spika, Ripoti ya ya marejeo ya kina ya mpango wa maendeleo wa miaka mitano (Comprehensive Review Report for Tanzania Five years Development Plan 2011/12 -2015/16) uk. 15 juu ya tathmini ya uhimilivu wa deni la taifa ( debt sustainability assessment) iliyofanyika septemba 2015 ilionyesha kuwa deni hilo ni himilivu na kwamba viashiria vya deni vinaonyesha kuwa thamani ya deni la nje kwa pato la Taifa ni 20.9% kwa mwaka ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 50%.
Mheshimiwa Spika, mwaka mmoja baadae , Serikali hiyo hiyo ya CCM kupitia Taarifa ya mwongozo wa kutayarisha mpango wa bajeti ya mwaka 2017/18 iliyotolewa na wizara ya fedha mwezi oktoba 2016, ikizungumzia uhimilivu wa Deni la Taifa imenukuu ripoti ile ile ya tathmini iliyofanyika mwezi septemba 2015 na kusema kwamba deni la taifa ni himilivu kwa kuwa thamani ya sasa ya deni la serikali kwa pato la Taifa ni 36.8 % kwa mwaka ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 74% !! Kambi ya rasmi ya upinzani inaitaka serikali ilieleze Bunge lako ukomo ni upi haswa? Asilimia 50% au 74%? Na ni nana anaweka ukomo wa kukopa, ni sisi kama nchi au Benki ya dunia?



Mheshimiwa Spika, kasi ya ukopaji wa mikopo mikubwa yenye masharti ya kibiashara unaonekana kuendelea, kwani taarifa zinaonyesha kwamba katika bajeti ya mwaka 2017/18 serikali inatarajia kukopa mikopo ya kibiashara licha ya kukiri katika maandiko yake kwamba kuongezeka kwa kasi kwa thamani ya deni dhidi ya Pato la Taifa tokea mwaka 2010 ni kielelezo cha uwezo mdogo wa kiuchumi wa kulipa.

MATAKWA YA KIKATIBA KUHUSU MPANGO WA TAIFA WA MAENDELEO
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Kanuni ya 94(1) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, toleo la Januari, 2016 Bunge hili limekaa kama Kamati ya Mipango, ili kukidhi matakwa ya ibara ya 63(3) (c) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kujadili na kuishauri Seirkali kuhusu mapendekezo ya utekelezaji wa Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali katika mwaka wa fedha unaofuata.
Mheshimiwa Spika, matakwa ya ibara ya 63(3) (c) ambayo Bunge hili linatakwa lifuate linapokaa kama Kamati ya Mipango ni Bunge kutekeleza madaraka yake, kwa kujadili na kuidhinisha mpango wowote wa muda mrefu au muda mfupi unaokusudiwa kutekelezwa katika Jamhuri ya Muungano, na kutunga sheria ya kusimamia utekelezaji wa mpango huo.
Mheshimiwa Spika, wakati Serikali ilipoleta mbele ya Bunge hili Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa wa miaka mitano 2016/17 2020/21, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni iliibua hoja ya kuitaka Serikali kuleta Bungeni Muswada wa Sheria ya kusimamia utekelezaji wa Mpango huo kama ibara ya 63(3) (c) ya Katiba inavyoelekeza.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani iliibua hoja hii kwa nia njema ya kuisaidia Serikali kuweka utaratibu mzuri wa kisheria wa utekelezaji wa Mpango huo kwa kudhibiti mianya yote inayoweza kukwamisha utekelezaji wa mpango huo ili Serikali ifikie malengo iliyokusudia kuyafikia katika mpango huo.
Mheshimiwa Spika, sababu kubwa iliyotolewa na Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni juu ya umuhimu wa kutekeleza matakwa ya Ibara ya 63(3)(c) ya Katiba ya kutunga sheria ya kusimamia utekelezaji wa mpango, ilitokana na ukweli kwamba; Mpango wa Kwanza wa Maendeleo wa Taifa wa miaka mitano 2011/12 2015/16 ulishindwa kufikia malengo yake kwa takriban asilimia 50 kutokana na kukosekana kwa sheria ya kusimamia utekelezaji wake na hivyo kusababisha mambo kufanywa hovyohovyo bila utaratibu.
Mheshimiwa Spika, ni bahati mbaya sana Serikali haikuona haja ya kuheshimu matakwa ya Katiba na kama desturi yake ikatumia vibaya wingi wa wabunge wa chama tawala kuupitisha Mpango ule bila kuutungia sheria ya utekelezaji. Ukiukaji huo wa Katiba ulifanyika pia wakati wa kupitisha mpango wa taifa wa maendeleo wa mwaka; kwa mwaka wa fedha 2015/16.
Mheshimiwa Spika, Serikali hii ya awamu ya tano imeanza vibaya mhula wake wa uongozi kwa kuivunja Katiba ya nchi. Ilianza kwa kukanyaga uhuru na haki za msingi za wananchi za kutoa maoni yao, kupata habari, kukusanyika, kushiriki mikutano halali ya kisiasa, kutumia fedha za umma bila idhini ya Bunge na sasa imeanza kukwepa agizo la wazi kabisa la Katiba la kutunga sheria ya kusimamia mpango wowote utakaotekelezwa katika Jamhuri ya Muungano.
Mheshimiwa Spika, hii si dalili nzuri hata kidogo kwa utawala huu wa awamu ya tano; na ni kiashiria cha kushindwa kwa Mpango wa Taifa wa Maendeleo unaopendekezwa kwa kuwa hakutakuwa na mwongozo wowote wa kisheria wa kusimamia utekelezaji wake. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, inaitaka Serikali kulieleza Bunge hili ni kwa nini inapuuza Katiba ya nchi kwa kukwepa kwa makusudi kuleta muswada wa sheria ya kusimamia utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Maendeleo?

MISINGI YA KIBAJETI KATIKA UTEKELEZAJI WA MPANGO WA
TAIFA WA MAENDELEO
Mheshimiwa Spika, ukiachilia mbali umuhimu wa uwepo wa sheria ya kusimamia utekelezaji wa Mpango, jambo jingine muhimu ni uwepo wa bajeti ya uhakika ya kugharamia miradi ya maendeleo.
Mheshimiwa Spika, wakati wa tathmini ya Mpango wa kwanza wa Maendeleo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ilisema kwamba; moja ya sifa kubwa ya Mpango wa kwanza wa Maendeo wa Miaka Mitano (2011/12 2015/16) ilikuwa ni kuweka msingi wa kibajeti ulioitaka Serikali kutenga asilimia 35 ya Mapato yake ya ndani kwa ajili ya ugharamiaji wa miradi ya maendeo. Mpango huo ulisema hivi: nanukuu, kwa kuelewa kuwa wakati wote kutakuwa na miradi ya uwekezaji nje ya mpango, serikali, kuanzia sasa, itakuwa inatenga asilimia 35 ya makadirio ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya kugharamia bajeti ya maendeleo kila mwaka mwisho wa kunukuu.
Mheshimiwa Spika, kutokana na ukweli kwamba Mpango huo haukutungiwa sheria ya utekelezaji kama Katiba ya nchi inavyoelekeza; Serikali ilijificha katika kichaka cha udhaifu huo; na matokeo yake kwa miaka yote mitano ya utekelezaji wa Mpango huo, Serikali haikuwahi hata mara moja kutenga asilimia 35 ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuna wakati mwingine haikutenga hata senti moja. Kwa mfano katika mwaka wa fedha 2012/13 Serikali haikutenga fedha yoyote kutoka katika mapato yake ya ndani kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo.
Mheshimiwa Spika, kutokana na Serikali kugoma kutoa asilimia 35 ya mapato yake ya ndani kutekeleza miradi ya maendeleo, miradi mingi ya maendeleo haikukamilika hadi mwisho wa muda wa utekelezaji wa Mpango huo.
Mheshimiwa Spika, kutokana na aibu ambayo Serikali iliipata kwa miaka yote mitano ya utekelezaji wa Mpango huo kwa kushindwa kutekeleza utaratibu iliyojiwekea yenyewe wa kutenga asilimia 35 ya Mapato yake ya ndani kugharamia mpango wa Maendeleo; safari hii Serikali imefuta kabisa utaratibu huo katika Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2016/17 2020/21) na kwa maana hiyo utaratibu huo hautakuwepo tena katika ugharamiaji wa miradi ya maendeleo kila mwaka.
Mheshimiwa Spika, tafsiri rahisi ya uamuzi wa Serikali hii ya CCM inayojinasibu kwa kauli ya hapa kazi tu kufuta msingi wa kibajeti wa kugharamia mpango wa maendeleo kila mwaka kwa kutenga asilimia 35 ya mapato yake ya ndani ni hofu ya kushindwa kutekeleza commitment hiyo kama ambavyo ilishindwa kufanya hivyo katika Mpango uliomaliza muda wake; lakini pia ni kukwepa kuwajibika au kuwajibishwa na Bunge kwa hofu hiyo hiyo ya kushindwa kutekeleza.
Mheshimiwa Spika, katika Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2016/17 Mpango ambao unaendelea kutekezwa hivi sasa; Serikali ilisema kwamba ilitenga shilingi trilioni 11.82 sawa na asilimia 40 ya bajeti yote kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo; lakini ukisoma kitabu cha Matumizi ya Fedha za Maendeleo (Public Expenditure Estimates Development Votes) VOLUME IV, fedha zilizotengwa ni shilingi trilioni 10.511. Katika hali hiyo, ni lazima kuwe na sheria itakayoibana Serikali kutekeleza kile inachoahidi hasa utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo ambao unatumia fedha za umma.
Mheshimiwa Spika, katika Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2017/18 Serikali imesema pia kwamba itaendelea na dhana ya kutenga asilimia 40 ya Bajeti yake kugharamia Mpango; akini imekwepa kueleza ni kaisi gani katika hiyo asilimia 40 kitakuwa ni fedha za ndani.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inasisitiza kiwango cha fedha za ndani kwa ajili ya kugharamia Mpango kiwekwe bayana kwa sababu Maendeleo ya nchi yatapimwa kwa uwezo wa nchi yenyewe kugharamia miradi yake ya maendeleo kwa kutumia fedha zake za ndani na sio kwa kutumia fedha za nje.

BAJETI HEWA NA UTEKELEZAJI HEWA WA MIRADI YA MAENDELEO
Mheshimiwa Spika, wakati bajeti kuu ya serikali kwa mwaka wa fedha 2016/17 inawasilishwa hapa Bungeni, Kambi Rasmi ya Upinzani ilibaini mapungugu makubwa katika bajeti hiyo, na kuliarifu Bunge lako tukufu kwamba bajeti hiyo ilikuwa ni bajeti hewa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ilitoa ushahidi wa kuthibitisha jambo hilo kwa kuonyesha jinsi ambavyo takwimu zilizoandikwa kwenye vitabu vya bajeti zilivyokuwa zikitofautiana kwa kiwango kikubwa. Kwa mfano, kitabu cha Mapato ya serikali katika mwaka wa fedha 2016/17 (Volume 1 Financial Statements and Revenue estimates for the year 1st July ,2016 to 30th June 2017) kilionyesha kuwa mapato yote ya serikali yaani mapato ya kodi , yasiyokuwa ya kodi ,mikopo na misaada ya kibajeti itakuwa jumla ya shilingi Trilioni 22.063.
Mheshimiwa Spika, wakati jumla ya makusanyo yote ya Serikali kwa mwaka 2016/17 ni trilioni 22.063; kitabu cha matumizi ya kawaida, (Volume II: Estimates of Public Expenditure Consolidated Fund Services for the year 1st July ,2016 to 30th June, 2017 na kitabu cha matumizi ya maendeleo Volume IV Public Expenditure Estimates Development Votes (part A) kama vilivyowasilishwa Bungeni,vinaonyesha kuwa matumizi yaliyoidhinishwa na Bunge ni jumla ya shilingi Trilioni 23.847; kwa mchanganuo kwamba: Fedha za Matumizi ya Kawaida (Volume II) ni shilingi 13,336,042,030,510 wakati fedha za Miradi ya Maendeleo (Volume IV) ni shilingi 10,511,945,288,575.
Mheshimiwa Spika; kwa kifupi, kwa mwaka wa fedha 2016/17, Serikali imepanga kukusanya jumla ya shilingi trilioni 22.063 ila imepanga kutumia shilingi trilioni 23.847, kiasi ambacho ni zaidi ya mapato yake kwa shilingi trilioni 1.783
Mheshimiwa Spika, bajeti ya Serikali iliyopitishwa hapa Bungeni kwa mwaka wa fedha 2016/17 ni kichekesho kitupu. Hii ni kwa sababu ukiosoma ukisoma sura ya bajeti iliyowasilishwa katika hotuba ya Waziri wa Fedha na Mipango utaona kwamba jumla ya makusanyo yote ni shilingi trilioni 29.539 na matumizi yote ni shilingi trilioni 29.539 lakini takwimu zilizoandikwa kwenye vitabu vya mapato na matumizi ni tofauti kama nilivyoonyesha hapo juu.
Mheshimiwa Spika, mkanganyiko huo wa takwimu za bajeti: kwamba Serikali itakusanya trilioni 29.5 na kutumia trilioni 29.5 lakini kwenye vitabu inaonekana itakusanya trilioni 22.063 na kutumia trilioni 23.8 ndio kunaifanya Kambi Rasmi ya Upinzani kuiita bajeti hiyo kuwa ni ‘bajeti hewa na kwamba mkanganyiko huo ndio kiashiria cha kwanza kikubwa; kwamba bajeti hiyo haitekelezeki. Kutotekelezeka kwa bajeti tafsiri yake ni kutotekelezeka kwa miradi ya maendeleo na ndio kufeli kwenyewe kwa Mpango wa Maendeleo wa Taifa. Aidha, sababu nyingine inayoifanya bajeti hiyo kuwa hewa ni kwa na vyanzo hewa vya mapato. Kwa mfano, kuingiza malipo ya kiinua mgongo cha wabunge ambacho kinatakiwa kulipwa mwaka 2020 kwa mujibu wa sheria na kukifanya kuwa chanzo cha mapato katika mwaka huu wa fedha 2016/17, hakuna jina lingine la kukiicha chanzo hicho cha mapato isipokuwa ni ‘chanzo hewa cha mapato kwa kuwa fedha hiyo itapatikana mwaka 2020 wakati wabunge watakapolipwa kiinua mgongo hicho.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa kumekuwa na vyanzo hewa vya mapato ambavyo vimepelekea kuwa na bajeti hewa, basi tutegemee pia kwamba utekelezaji wa miradi mingi ya maendeleo nao utakuwa hewa. Na kama tunatumia bajeti hewa kufanya mapendekezo ya Mpango wa Maendelo kwa mwaka wa fedha unaofuata na makisio ya bajeti kwa miaka mitatu mfululizo inayofuata, kuna hatari kubwa ya kuishia kuwa na Mpango dhaifu na makisio hewa ya bajeti kwa mika hiyo mitatu inayofuata.

MPANGO WA MAENDELEO WA TAIFA NA SEKTA YA KILIMO
Mheshimiwa Spika, sekta ya Kilimo ni miongoni mwa maeneo ambayo hayajawekewa mkazo kabisa na yamepuuzwa na serikali ya CCM . Sekta hii imekuwa ikidumaa siku hadi siku na katika hali ya kutia aibu hali ni mbaya kuliko hata ilivyokuwa wakati nchi inapata uhuru! Ni muhimu serikali ikaelewa kwamba bila kuwekeza katika kilimo, itakuwa ni ndoto wananchi wetu kutoka kwenye lindi la umasikini. Kama kilimo hakikaendelezwa ina maana kwamba inamaanisha kwamba maisha ya 75% ya watanzania iko matatani! Ripoti zinaonyesha kwamba Shughuli za kiuchumi za kilimo zilikuwa kwa kasi ndogo ya asilimia 2.3 mwaka 2015 ikilinganishwa na asilimia 3.5 mwaka 2014.Licha ya kuwa na mchango mkubwa katika pato la Taifa kwa kuchangia kwa asilimia 29.0 kwa mwaka 2015 zikifuatiwa na shughuli za ujenzi (13%), biashara na matengenezo (10.7%) na ulinzi na utawala 6.4%.
Mheshimiwa Spika, Mpango wa kwanza wa Maendeleo wa miaka mitano (2011-16) lengo lilikuwa kukuza shughuli za kilimo kwa wastani wa 6%,kiwango hiki kiliwekwa baada ya lile lengo la awali la 10% kuishia kwenye makaratasi. Kutokana na uwekezaji duni, kikaambulia kukua kwa kiwango cha wastani wa asilimia 3.4 tu! Na Mapitio ya mwenendo wa uchumi 2016/17 yanaonyesha kwamba sekta hii muhimu imeporomoka mpaka kufikia 2.3%!


Mheshimiwa Spika, baada ya serikali kushindwa vibaya kwenye Kilimo,sasa imekuja na hoja ya serikali ya viwada. Ni muhimu ikaeleweka kwamba Maendeleo ya sekta moja inategemea ukuaji wa sekta nyingine. Viwanda sio mbadala (Substitutive) wa Kilimo, bali ni sekta mbili zinazotegemeana. Viwanda/Kilimo haviwezi kukua bila kukuza / kuboresha sekta hizi mbili kwa pamoja . Kama Kilimo kitachukuliwa kuwa ni moyo wa nchi, basi viwanda itakuwa ni ubongo.
Mheshimiwa Spika, tusitegemee miujiza kama kwa miaka mitatu mfululizo kati ya kiasi cha shilingi 2,710 (shilingi trillion 2.7) kilichopangwa katika mpango kama kichocheo cha kufufua sekta hii muhimu, kiasi kilichopitishwa (approved budget) ni shilingi 371 bilioni (13.71 % ),na kiasi cha pesa kilichotolewa (actual budget released) ni shilingi bilioni 250.12 tu ! sawa na 9.23 % ya mahitaji yote.
Mheshimiwa Spika, mwelekeo wa Mpango, hauonyeshi dalili ya kulifanyia kazi hili! Uchumi unaonekana kukua kwa tarakimu, bila kuzalisha ajira nyingi wala kupunguza umasikini kutokana na ukweli kwamba Sekta zinazokuwa kwa kasi ni zile zinazotumia machine na mitambo. Sekta hizi haziajiri wafanyakazi wengi kama zile zinazotumia misuli mfano Kilimo, uvuvi na ufugaji. Sekta hii inatoa soko kwa sekta nyingine kama vile viwanda ,fedha, usafirishaji na biashara. Pia hutoa malighafi kwa sekta nyingine kama viwanda na huingiza fedha nyingi za kigeni. Kwa ufupi ni sekta yenye muingiliano mkubwa na sekta nyingine.
Mheshimiwa Spika, Mkurugenzi Mwendeshaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) akitoa utangulizi katika semina ya waheshimiwa wabunge kuhusu kuanzishwa kwa TADB alisema: “ili Tanzania ifanikiwe katika kupunguza umasikini na kujenga uchumi wa viwanda , ni lazima ifanye mapinduzi kwenye sekta ya Kilimo”.Ni ukweli unaouma kwamba viwanda haviwezi kuwepo bila malighafi. Bado uzalishaji kwa eneo ni mdogo,miundombinu kama barabara za vijijini,umwagiliaji na masoko ni duni, uwezo wa kupata fedha kutoka vyombo vya fedha ni mdogo,masoko ni shida ,halikadhalika uwezo wa kuongeza thamani kwa bidhaa za kilimo ni mdogo. Wakulima wadogo, kimsingi ndio wanalisha Taifa hili? Serikali imewekeza nini kwao ili kuwawezesha kuzalisha Zaidi na kuongeza kipato!!
Mheshimiwa Spika, zilianzishwa programu kadhaa kama vile TAFSID-Tanzania Agriculture and Food Security Investment Plan, SAGCOT- Southern Agricultural Growth Corridor of Tanzania ambazo lengo lilikuwa ni kukifanya kilimo kuwa cha kisasa na cha kibiashara kwa kuhusisha sekta binafsi jambo ambalo lingekuwa nguzo muhimu wa kuubadilisha uchumi wa Tanzania kutoka kutegemea kilimo na kuwa nchi ya viwanda. Mipango hii imebaki kwenye makaratasijapo chama ni kile kile, kila Rais anayeingia, anakuja vipaumbele vyake kwa kadiri akili yake inavyomuongoza!
Mheshimiwa Spika, halikadhalika ilianzishwa Benki ya Maendeleo ya kilimo. Benki hii ilianzishwa kwa lengo la kuiwezesha Tanzania kufikia mapinduzi ya kilimo. Uanzishwaji wa bank hii ilikuwa moja ya maazimio kumi ya KILIMO KWANZA yaliyofikiwa mwaka 2009 (Miaka 7 iliyopita). Na ilikuwa shughuli ya pili kwa umuhimu (Baada ya shughuli ya 1 ya kuongeza bajeti ya Serikali kwa ajili ya Kilimo kwanza )Kati ya shughuli 15 za nguzo ya pili ya Kilimo Kwanza ilidhamiriwa ilidhamiriwa TADP ianzishwe ikiwa na mtaji wa dola za kimarekani milioni 500 (kipindi kile shilling bilioni 800, sasa hivi Trilion 1.1).Fedha hizo zingepatikana iwapo serikali ingetenda bilioni 100 kila mwaka . Lengo likiwa ni kukopesha wakulima wadogo wadogo kwa masharti na riba nafuu!! Mpaka nasoma hotuba hii, benki hii muhimu ilipewa shilingi bilioni 60 tu mwezi April 2015. Na inasemekana kama hatua zisipochukuliwa haraka,kwa mgao huu itakapofika 2020 banki hii itashindwa kujiendesha.
Mheshimiwa Spika, kukosekana kwa mwendelezo wa mipango yetu kama nchi limekuwa ni tatizo kubwa sana, hivyo kuathiri kwa kiwango kikubwa maendeleo ya nchi na wananchi wake.
KAULI MBIU YA TANZANIA YA VIWANDA YAGEUKA KIINI MACHO
Mheshimiwa Spika, Kauli mbiu ya Tanzani ya Viwanda ndio iliyotawala sera za Mgombea Urais kupitia CCM katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, 2015. Kauli mbiu hiyo imechukuliwa kama ilivyo na kuwa Kauli Mbiu ya Mpango wa Pili wa Miaka Mitano wa Maendeleo wa Taifa 2016/17 hadi 2020/21.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani haikosoi kuweka viwanda kama kipaumbele cha Mpango kwa kuwa viwanda vitatoa ajira kwa watanzania walio wengi na hivyo kukuza pato la mtu mmoja mmoja (per capita income) ambalo ni muhimu katika ukuaji wa uchumi wa Taifa kwa ujumla. Jambo ambalo Kambi Rasmi ya Upinzani inashangazwa nalo ni kwamba zile mbwembwe na mihemko ya kwenye kampeni za Urais kwamba Tanzania itakuwa ya viwanda zimeyeyuka na nchi sasa imekosa kabisa mwelekeo kuhusu uhuishaji wa sekta ya viwanda.
Mheshimiwa Spika, nasema hivi kwa ujasiri, kwa sababu katika utekelezaji wa bajeti ya Wizara ya Viwanda na Biasharia kwa kwa kipindi cha robo ya kwanza ya mzunguko wa bajeti (Julai hadi Septemba, 2016), kati ya shilingi bilioni 40 zilizotengwa kwa ajili bajeti ya maendeleo, hakuna fedha yoyote ya maendeleo iliyotolewa kwa ajili ya miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa viwanda. Hii ni kwa mujibu wa Taarifa ya Utekelezaji wa Malengo ya Sekta ya Viwanda na Biasahara na Uwekezaji kwa kipindi cha Julai Septemba, 2016 iliyowasilishwa kwenye Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda na Biashara mwezi Oktoba, 2016.
Mheshimiwa Spika, Ikiwa robo ya kwanza yote ya mzunguko wa bajeti imeisha na hakuna hata senti moja iliyotolewa kutekeleza miradi ya maendeleo katika sekta ya viwanda, Serikali inakuwa na ujasiri gani wa kutumia tathmini hiyo ya kushindwa katika mapandekezo ya Mpango wa Maendeleo wa mwaka 2017/18?

Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nimeeleza hapo wali; sekta ya viwanda ikikua kwa viwango vinavyokusudiwa itapanua wigo wa ajira kwa vijana wa Tanzania. Hata hivyo, licha ya uhalisia huo, bado Serikali haijatilia mkazo miradi inayozalisha ajira kwa wingi. Kwa mfano taarifa ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango miradi itakayozingatiwa, ukiifanyia tathmini; ni mirandi ambayo siyo labour intensive, hivyo upatikanaji wa ajira bado utakuwa wa kusuasua.
Mheshimiwa Spika, ni ukweli kwamba Serikali ilikwisha ainisha maeneo ya uzalishaji kwa ajili ya uzalishaji bidhaa kwa mauzo ya nje ya nchi, lakini hadi sasa maeneo hayo bado Serikali haijamaliza kuyalipia fidia toka kwa wamiliki. Na kwa yale ambayo tayari fidia imekamilika ujenzi wa miundombinu ya uzalishaji bado haijaanza kujengwa.
Mheshimiwa Spika, kituo kikubwa cha biashara cha KURASINI LOGISTIC CENTRE cha ubia kati ya Tanzania na China (EPZ), ambapo tumefanya ulipaji fidia mkubwa kwa kuhamisha watu toka eneo husika lakini katika vipaumbele haioneshi. Jambo hili linatuonesha kwamba mradi huo unapingana na dhana nzima ya Tanzania ya Viwanda kwani kuruhusu mradi huo kuendelea ni sawa na kusaini mkataba wa EPA kati ya Jumuiya ya Afrika ya Mashariki na Jumuiya ya Ulaya.
Mheshimiwa Spika, kufunguliwa kwa kituo hicho maana yake ni kwamba Tanzania itakuwa nchi ya wachuuzi wa bidhaa kutoka Uchina na hivyo sisi kama nchi industrialization haitofanikiwa kwani kutokana na kiwango cha teknolojia walichonazo wachina katika uzalishaji viwandani hatutaweza kuzalisha bidhaa za kuweza kushindana na bidhaa zao.
Mheshimiwa Spika, Tanzania ya Viwanda haitapatikana kwa kauli mbiu za Viongozi bali itapatikana kwa sera madhubuti ambayo inaelekeza uwepo wa utawala bora katika sekta husika (rasilimali watu), mazingira wezeshi kwa uanzishaji wa viwanda pamoja na mgawo wa upendeleo wa rasilimali fedha kwa sekta husika. Aidha, kuandika nyaraka ni jambo moja na utekelezaji way yale yaliyomo kwenye nyaraka hizo ni jambo lingine. Kambi Rasmi ya Upinzani inapenda tujiulize ni kwa kiwango gani matakwa hayo yametekelezwa?
Mheshimiwa Spika, Kuhusu Biashara; Taarifa ya Benki ya Dunia ya Mwelekeo wa Ufanyaji Biashara Tanzania kwa mwaka ujao 2017 inaonesha kuwa Tanzania imeboresha mazingira ya biashara kutoka nchi ya 139 hadi ya 132. Hata hivyo; yapo mazingira ambayo yanaifanya Tanzania kuendelea kuwa nyuma katika uwekaji wa mazingira wezeshi ya biashara hasa katika uwekezaji.
Mheshimiwa Spika, Changamoto zilizotolewa katika taarifa hiyo ni mfumo wa kodi mgumu na usiotabirika ambapo wawekezaji ambao wanategemea kuja nchini wanashindwa kupima na kufanya tathmini yao kuhusu masuala yote ya kodi kabla ya kuleta mitaji yao nchini. Aidha, ufanyaji wa biashara nje ya mipaka yetu imetajwa kuwa ni changamoto ambayo inarudisha nyuma mazingira ya biashara.
Mheshimiwa Spika, imeonekana pia kuwa hakuna uhakika wa kuwalinda wawekezaji waliopo nchini. Changamoto hii si ya kupuuza kwa sababu toka serikali ya awamu ya tano iwepo madarakani, kwa kauli na matendo imeonesha kutowathamini wawekezaji waliopo nchini. Pamoja na changamoto ya baadhi ya mikataba katika sekta mbalimbali kuwa mibovu, ni ukweli pia kuwa ni serikali hii ya CCM ambayo ilishiriki kuingia kwenye mikataba hiyo na Rais wa sasa akiwa kwenye Baraza la Mawaziri kwa miaka ishirini.
Mheshimiwa Spika, ni vema taratibu zikafuatwa katika kuboresha mifumo na si kauli za kubeza wawekezaji na kusema nchi ilikuwa na ufisadi wakati Rais wa sasa hajashuka toka mbinguni kama malaika na kinyume chake alikuwa sehemu ya serikali hiyo. Kambi ya Upinzani kwa miaka mingi tumetoa maoni ya kuhakikisha kuwa mazingira ya biashara ni wezeshi kwa wawekezaji wa ndani na wa nje wanafanya biashara zao na serikali inanufaika na uwepo wao.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inashangaa kuona serikali hii ya hapa kazi ikijigamba kuwa inaipeleka nchi kuwa ya viwanda wakati biashara ya kimataifa imedorora na mfumo wa kodi umekuwa ni mgumu zaidi. Hii ni tofauti na nchi jirani ya Kenya ambayo ni miongoni mwa nchi kumi duniani zilizoboresha mazingira yake ya biashara.
NISHATI YA UMEME NA UCHUMI WA VIWANDA
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Mapendeko ya Mpango wa Taifa wa Maendeleo 2017/18, sekta ya viwanda ndio kipaumbele cha Mpango kwa ajili ya kukuza uchumi wa viwanda. Hata hivyo, ukuaji wa sekta ya viwanda unategemea sana ukuaji wa sekta ya nishati na hasa nishati ya umeme ili viweze kufanya kazi na kuzalisha kama inavyokusudiwa.
Mheshimiwa Spika, pamoja na kutegemeana huku kati ya sekta ya viwanda na sekta ya nishati, Serikali hii ya awamu ya tano haikulipa uzito stahiki sula la nishati ya umeme katika ukuaji wa viwanda nchini. Sekta ya nishati imewekwa kama kipaumbele cha mwisho katika mapandekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2017/18.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upnzani ina mtazamo kwamba; Kama Serikali ina nia thabiti ya kuhuisha viwanda katika nchi yetu; basi azma hiyo iende sambamba na uboreshaji wa miundo mbinu ya umeme ili kuwe na umeme wa uhakika wa kuweza kuendesha viwanda na kukidhi matumizi mengine ya wananchi. Kambi Rasmi inatoa angalizo hili kwa kuwa tumekuwa tukishuhudia umeme wa mgawo kabla hata ya kufanya mapinduzi ya viwanda; sasa baada ya viwanda hivyo vinavyosemwa kujengwa na kuanza kufanya kazi hali itakuwaje?
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa taarifa ya utafiti uliofanywa na Donna Peng & Rahmatallah Poudineh wa Oxford Institute for Energy Studies ya mwaka 2016; juu ya Bei Endelevu ya Umeme Tanzania (Sustainable Electricity Pricing for Tanzania) ni kwamba upungufu wa umeme nchini unatokana na upotevu wa umeme unaotokea katika usafirishaji na usambaza wa umeme. Taarifa hiyo inaonyesha pia kwaamba upotevu mkubwa wa umeme unatokea kwenye usambazaji, ambapo na uchakavu wa miundombinu ya umeme, mipango ya uzambazaji ya umeme isiozingatia mahitaji ya uwekezaji wa baadye ndiyo chanzo kikubwa cha upotevu huo.
Mheshimiwa Spika, kutoakana na hali hiyo, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kueleza bayana katika mapendekezo ya Mpango wa maendeleo wa 2017/18 namna itakavyokabiliana na tatizo la upungufu wa umeme nchini ili kukidhi mahitaji ya nishati inayohitajika viwandani na kwa matumizi ya wananchi majumbani.

MISNGI YA MPANGO NA BAJETI KWA MWAKA 2017/18
Mheshimiwa Spika, mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2017/18 yanaeleza kwamba katika kipindi cha 2017 2019/20 misingi ya mpango na bajeti ni pamoja na amani, usalama, utulivu na utangamano wa ndani na nchi jirani kuendelea kuimarishwa na kudumishwa.
Mheshimiwa Spika, mazingira ya kisiasa yaliyopo sasa hapa nchini ya Serikali kuzuia washindani wa kisiasa kufanyakazi za siasa ni ishara tosha kwamba mpango wa bajeti umejengwa kwenye msingi ambao tayari una ufa. Nchi hii ni ya watanzania wote na Katiba ya nchi inatambua uwepo wa siasa za ushindani. Siasa za ukosoaji na kukubali kukosolewa ndio msingi wa maendeleo. Hoja ya msingi ni kama wadau wa ndani hawaridhiki, je sifa za watu wa nje zinafaida gani?
Mheshimiwa Spika, tunu ya amani na utulivu, usalama na utangamano wa ndani vinajengwa juu ya msingi wa haki, uhuru na usawa miongoni mwa wananchi. Tunu hizo zinaimarishwa kunapokuwa na Serikali inayozingatia misingi ya kidemokrasia na utawala wa sheria katika kutekeleza majukumu yake. Inapotokea dola kutaka kuwa juu ya sheria na kuongoza kwa matamko ya mkuu wa Serikali, basi misingi hiyo ya kidemokrasia na utawala wa sheria inakuwa imevunjwa. Hali hiyo ni hatari kwa kuwa aliyenyimwa haki atakapoidia ataonekana kwamba ni mkorofi na kwa hiyo kutakuwa na hali ya uhasama kati ya vyombo vya dola na wananchi wanaodai haki.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inapenda kuweka rekodi sawa kuhusu mambo yafuatavyo:
Umma ndio wenye madaraka ya mwanzo na mwisho kuhusu hatima ya nchi yao na Serikali itapata uhalali na madaraka yake kutoka kwa wananchi. Na hili ni takwa la kikatiba.
Nguvu na Mamlaka ya Umma vitajenga na kudumisha Demokrasia kuendana na katiba.
Nguvu na Mamlaka ya Umma ndiyo msingi wa kuhoji na kuwajibisha uongozi uliochaguliwa kwa uhuru na kwa haki.
Nguvu na Mamlaka ya Umma ndiyo chombo cha kuwaamsha, kuwahamasisha, na kuwaelimisha Watanzania waimiliki, waitawale, wailinde, waiendeshe na waiendeleze nchi kwa ubunifu ili wanufaike nayo.
Mheshimiwa Spika napenda kumalizia hotuba yangu kwa kusema kwamba ni aibu kubwa kwa Serikali kupanga mipango ambayo inashindwa kuitekeleza. Kupanga ni kuchangua, hivyo Serikali iwe inapanga mipango ambayo ni realistic na ilete miswada hapa bungeni ya kusimamia utekelezaji wa mipago hiyo vinginevyo hotuba zetu zitaendelea kuwa hivi hivi na hatuataifika ndoto ya taifa ndoto ya kuondokana na umasikini na kuwa nchi ya watu wenye kipato cha kati.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba kutoa hoja.


Halima James Mdee (Mb)
WAZIRI KIVULI NA MSEMAJI MKUU WA
KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI KATIKA
WIZARA YA FEDHA NA MIPANGO
1 Novemba, 2016.
 
Mm bado nnaisoma namba maana mpk sasa hiv bado cjajua nmeifikia namba ipi maana nnaona giza tu...Asante baba jitaid kukaza mpk nione mwanga.
 
Mheshimiwa Spika, taarifa hiyo ya Benki Kuu inaendelea kuonyesha kwamba; shughuli za uchumi zinazohusu wananchi masikini zimeshuka kutoka kasi ya ukuaji ya 10.20% katika robo ya mwisho ya mwaka 2015 mpaka 2.7% katika robo ya kwanza ya mwaka 2016, ikiwa ni punguzo la 8% ndani ya kipindi kisichozidi miezi sita.
 
Back
Top Bottom