Hotuba ya Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya ofisi yake 2020/2021

The Sheriff

JF-Expert Member
Oct 10, 2019
613
1,776
HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI KATIKA OFISI YA RAIS – TAMISEMI, MHESHIMIWA JAPHARY RAPHAEL MICHAEL (MB), AKIWASILISHA BUNGENI MAONI YA KAMBI RASMI YA UPINZANI KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA KATIKA OFISI HIYO, KWA MWAKA WA FEDHA 2020/2021

Inatolewa chini ya Kanuni ya 99(9) ya Kanuni za Kudumu za Bunge,

Toleo la Januari, 2016

_____________________

UTANGULIZI

1. Mheshimiwa Spika
, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema, kwa kunijalia uhai,afya njema na kunipa nguvu hivyo kuweza kusimama mbele ya Bunge lako tukufu ili kutoa maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya fedha katika Ofisi ya Rais - TAMISEMI kwa mwaka wa fedha 2020/2021 na pia kuangalia utekelezaji wa bajeti ya Wizara hii kwa mwaka wa fedha 2019/20.

2. Mheshimiwa Spika, kwa heshima kubwa nitoe pongezi kwa vyama vyote vya ushindani kwa kuendelea kuwepo na kuendelea kutimiza jukumu kubwa la kuiwajibisha serikali kwa wananchi kwa vile uwepo wao umesababisha baadhi ya mambo kufanyika hata kama sio kwa weledi na ufanisi ambao ungetamalaki kama nchi hii ingeongozwa na Serikali ya chama tofauti na CCM.

3. Mheshimiwa Spika, nitoe pole na hongera nyingi sana kwanza kwa viongozi waandamizi wa CHADEMA kwa madhila ambayo wamekutana nayo, kwa kipindi cha takriban miaka miwili na nusu kuwa katika mahakama kwa kesi ambayo tunaamini ilikuwa na lengo la kudhalilisha sheria ya vyama vya siasa. Pili ni kwa watanzania wote kwa umoja wao kuhakikisha wanachangia viongozi wote wa CHADEMA ambao walipatikana na hatia na hivyo kuamuliwa kulipa faini ya shilingi milioni 350. Asanteni sana Watanzania kwa kuifanya Demokrasia na utawala bora kushinda majaribu.

4. Mheshimiwa Spika, aidha napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa wananchi wa Jimbo la Moshi Mjini kwa ushirikiano walionipatia katika kipindi chote ambacho nimekuwa Mbunge sambamba na kipindi ambacho nilikuwa Mayor wa Halmashauri hiyo. Nawaomba tuendelee kushikamana katika kuhakikisha MOSHI inaendelea kuwa mahali salama katika kuendeleza uchumi wa wananchi wake na pia sehemu ya kutoa uongozi uliotukuka kwa wananchi wake, hilo wana-MOSHI mnaliona na sio jambo la kushawishiwa ili kuliona.

5. Mheshimiwa Spika, Mwisho lakini kwa umuhimu mkubwa ni kwa familia yangu, ambayo imenivumilia sana kwa kipindi chote ambacho nimekuwa nje ya familia kwa ajili ya kutimiza wajibu wangu kwa Chama na kwa Bunge, nasema asanteni sana na tuendelee kuvumiliana katika hilo.

B. MAPITIO YA MAJUKUMU YA OFISI YA RAIS TAMISEMI

6. Mheshimiwa Spika
, baada ya kutoa utangulizi huo, naomba sasa kuanza kupitia utendaji wa Wizara hii kwa kadri ambavyo itawezekana kutokana na ukweli kwamba Wizara hii ni serikali ambayo kwa mujibu wa KATIBA ya Tanzania Ibara ya 145 na 146 inatakiwa kutekeleza majukumu yake kufuatana na maelekezo ya Katiba na pia kwa sheria zilizotungwa na Bunge, bila ya hila ya kupoka mamlaka za wananchi.

7. Mheshimiwa Spika, Ibara tajwa za Katiba ndio kichocheo kikubwa cha uanzishwaji wa Sera ya Ugatuaji wa Madaraka kutoka Serikali Kuu kwenda Serikali za mitaa(Kwa wananchi) na sheria zikatayarishwa na maboresho yakafanyika kwa fedha nyingi za wananchi wenyewe, lakini sasa kinachoendelea ni hila za kupoka mamlaka hayo na kuyarejesha Serikali Kuu, jambo hili litaelezwa hapo baadae.

8. Mheshimiwa Spika, Duniani kote Serikali za mitaa zina majukumu makubwa ya kijamii, kisiasa na kiuchumi kwa kulingana na taratibu, kanuni na sheria zinazoiongoza jamii husika. Kwa Tanzania sheria ndogo (by laws) utungwa na baraza la madiwani ambalo ndicho chombo cha uwakilishi wa wananchini kwenye Halmashauri husika. Ili Halmashauri zitimize wajibu wake wa kutoa huduma kwa jamii zinahitajika kuwa na uwezo wa kukusanya rasilimali mali, fedha pamoja na rasilimali watu.

9. Mheshimiwa Spika, Mbali ya majukumu hayo ya utoaji wa huduma za msingi, pia katika nchi yetu halmashauri zimeongezewa wigo wa majukumu kama vile kupunguza umasikini katika jamii, kupunguza vifo vya mama na mtoto, kupambana na Ukimwi pamoja na virusi vyake, na sasa tungetegemea Halmashauri zetu zinakuwa na uwezo wa kupambana na mlipuka wa Corona, kuhakikisha njaa katika jamii inakuwa ni historia. Mbali na ongezeko la majukumu kwa Serikali za mitaa, bado halmashauri zetu hazina uwezo wa kifedha kuweza kutelekeza majukumu yake kwa kikamilifu (PMO-RALG, 2013; Repoa, 2008; URT, 2016 and LGCDP, 2010).

10. Mheshimiwa Spika, Kutokana na ufinyu huo wa rasilimali kwa Halmashauri zetu inazilazimu kutegemea uwezeshwaji kutoka Serikali Kuu, jambo ambalo linaathiri sana utendaji wa Halmashauri zetu katika kukabiliana na mahitaji ya wananchi.

11. Mheshimiwa Spika, uendeshaji au uhuru wa mabaraza ya madiwani katika kupanga na kuamua mgawanyo wa rasilimali zao kwa mujibu wa vyanzo vya mapato ambavyo vipo kisheria sio jambo la hisani, bali ni jukumu lao la kisheria, hivyo kitendo cha kupoka madaraka hayo ni kutokuwatendea haki wananchi. Aidha ni vyema tukafahamu vizuri uhusiano wa HAKI na SHERIA katika uendeshaji wa nchi, na msingi mkubwa wa kuendesha nchi au taasisi yoyote ni HAKI, sheria zinakuja baadae, kwani kuna wakati sheria zetu zinatungwa kwa hila ili kutimiza matakwa ambayo sio ya HAKI.

12. Mheshimiwa Spika, mojawapo ya majukumu ya msingi ya OR-TAMISEMI ni kama ilivyoainishwa kwenye Hati Idhini ya mgawanyo wa majukumu ya Wizara za Serikali ni; kusimamia utekelezaji wa Sera ya Ugatuaji Madaraka (D by D), na kuziwezesha Mamlaka za Serikali za Mitaa kutekeleza majukumu yake ya kisheria; hivyo basi,

13. Mheshimiwa Spika, katika ugatuaji wa madaraka hatuwezi kuongelea jambo hilo bila ya kuangalia uwezo wa Halmashauri zetu kifedha, na nguvu ya kujitegemea katika muktadha mpana ambao msingi wake mkuu ni uwezo wake wa kujitegemea kifedha. Katika hili ni vyema tuangalie sheria zinazotoa mwanya wa kupata fedha (vyanzo vya mapato) na kwa jinsi gani uwezo wa kujitegemea unavyofifishwa kwa makusudi ili wananchi waendelee kuwa masikini.

14. Mheshimiwa Spika, Vyanzo vya mapato ya Mamlaka za Serikali za Mitaa vimeainishwa katika vifungu Na. (6) hadi (9) vya Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa Na. 9 ya mwaka 1982 yaani (The Local Government Finance Act, No. 9 of 1982).Kulingana na Sheria ya Fedha Na. 9 ya mwaka 1982 ya Serikali za Mitaa iliyorekebishwa na Sheria ya Fedha Na. 15 ya mwaka 2003 yaani (The Finance Act No. 15 of 2003), Serikali za Mitaa hazitozi kodi ya Mapato bali kodi hiyo hutozwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania( TRA). Ni muhimu sana, tupewe tathmini ya hali za Halmashauri zetu katika kutimiza majukumu yake ya msingi kama ambavyo tumeyaainisha hapo awali tangu Serikali ya awamu ya tano iinge madarakani? Thathmini hiyo ni lazima ijibu swali la nia njema ya kupeleka madaraka kwa wananchi (d by d) iliyoanzishwa na Serikali ya awamu ya tatu na kuendelezwa na ile ya awamu ya nne.

15. Mheshimiwa Spika, ni vyema kwa ufupi tukaorodhesha vyanzo vya mapato kama vilivyokuwepo kabla ya vingine vikubwa kupokwa na Serikali kuu, kwa sababu ambazo zilikuwa ni za kisiasa zaidi kuliko za kimaendeleo na dhana nzima ya uwepo wa Serikali za mitaa kwa mujibu wa Ibara za 145 na 146 za Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kambi Rasmi ya Upinzani inaona hali ilivyo sasa katika dhana nzima ya kuhakikisha halmashauri zetu zinajitegemea nchi yetu ina utawala lakini inakosa uongozi.

C. VYANZO VYA MAPATO KWA MUJIBU WA SHERIA

16. Mheshimiwa Spika,
ifuatayo ni orodha ya vyanzo vya mapato, ambavyo ni nguzo ya kuimarisha dhana nzima ya Ugatuzi wa Madaraka (D by D) mbali na kuwa na uwezo wa kumiliki rasilimali watu katika muktadha wa utawala na fedha.

A. Taxes on Property
i. Property rates.-

B. Taxes on Goods and Services
Crop cess (maximum 5% of farm gate price)
Forest produce cess

C. Taxes on Specific Services
i. Guest house levy

D. Business and Professional Licenses
Commercial fishing license fees
Intoxicating liquor license fee
Private health facility license fee
Taxi license fee
Plying permit fees
Other business licenses fees

E. Motor Vehicles, Other Equipment and Ferry Licenses
Vehicle license fees -
Fishing vessel license fees

F. Other Taxes on the Use of Goods, Permission to Use Goods
Forest produce license fees
Building materials extraction license fee
Hunting licenses fees
Muzzle loading guns license fees
Scaffolding / Hoarding permit fees

G. Turnover Taxes
i. Service levy

H. Entrepreneurial and Property Income
Dividends
Other Domestic Property Income
Interest
Land rent

I. Administrative Fees and Charges
Market stalls / slabs dues
Magulio fees
Auction mart fees
Meat inspection charges
Land survey service fee
Building permit fee
Permit fees for billboards, posters or hoarding
Tender fee
Abattoir slaughter service fee
Artificial insemination service fee
Livestock dipping service fee
Livestock market fee
Fish landing facilities fee
Fish auction fee
Health facility user charges
Clean water service fee
Refuse collection service fee
Cesspit emptying service fee
Clearing of blocked drains service fee
Revenue from sale of building plans
Building valuation service fee
Central bus stand fees
Sale of seedlings
Insurance commission service fee
Revenue from renting of houses
Revenue from renting of assets
Parking fees-

J. Fines, Penalties and Forfeitures
Stray animals penalty
Share of fines imposed by Magistrates Court
Other fines and penalties

17. Mheshimiwa Spika, Maelezo au ufafanuzi wa utendaji kazi wa Serikali za mitaa umetolewa katika sheria zilizotungwa na Bunge, yaani sheria ya “the Local Government (District Authorities) Act, and the Local Government (Urban Authorities) Act” ya mwaka mwaka 1982.

18. Mheshimiwa Spika, katika taarifa ya utafiti wa utekelezaji wa sheria hiyo, unaonyesha Serikali Kuu imeshindwa kuweka mkakati uliowazi na makini wa kufanikisha matakwa ya Kikatiba na Kisheria. Katika uchambuzi huo kwa ngazi ya mkakati wa utekelezaji umeeleza kuwa;hakuna mpango mahususi unaohusiana na ugatuaji madaraka unaonesha majukumu na mipaka ya serikali kuu na serikali za mitaa. “There is no explicit implementation plan regarding decentralisation. The separation between central government matters and local affairs is not established”[1].

19. Mheshimiwa Spika, Vigezo au viashiria vilivyoonyesha mkanganyiko kwa Sera ya Ugatuaji wa Madaraka kwa mujibu wa andiko hilo ni: Transfer of competencies and sector-based policies: Serikali za mitaa hapa nchini sio taasisi inayojitegemea kama inavyotakiwa kuwa kwa mujibu wa Katiba na sheria. Uhawilishwaji wa raslimali watu katika serikali za mitaa ni matakwa ya Serikali kuu na si matakwa ya Serikali za mitaa, pili Uteuzi na ajira kwa watumishi hufanywa na Serikali kuu kupitia kwa kilinachoitwa-“local Government Service Commission”. Hivyo jambo hilo husababisha mamlaka za Serikali za mitaa kutokuwa na uwezo wa kuajiri au kufukuza mtumishi hadi pale Mamlaka iliyofanya uteuzi au uajiri kufanya hivyo.

20. Mheshimiwa Spika, Mojawapo ya sababu za kushindwa kufanya vizuri katika hutoaji wa huduma za msingi kwa wananchi kwa halmashauri nyingi hapa nchini inatokana na kukosa au kutokuwa na uwezo kwenye Utawala na Fedha katika kutoa maamuzi yanayohusu maendeleo ya Halmashauri zao. Badala yake maamuzi mengi ya Kiutawala na kifedha yanatolewa na Serikali Kuu,na utendaji wa Halmashauri nyingi kwa sehemu kubwa unaingiliwa na wakuu wa mikoa na wakuu wa Wilaya.

21. Mheshimiwa Spika, ni vizuri Serikali ya awamu ya tano ikatazama juhudi iliyofanywa na serikali za awamu zilizotangulia husana awamu ya tatu nay a nne, ambazo zilifanikiwa kukabribia lengo na dhana nzima la ugatuaji wa madaraka kama linavyoelezwa katika Ibara ya 154 na 146 lakini kwa bahati mbaya tumerudi nyuma miaka takriba 25 iliyopita.

22. Mheshimiwa Spika, Nyenzo muhimu inayotumiwa na Serikali katika kuhakikisha kuwa inazidi kuhodhi madaraka ya Serikali za mitaa ni kuhodhi watumishi waandamizi (senior Staffs) wa Serikali za mitaa walio kwenye sekta za utawala, afya, fedha, Kilimo n.k wote hawa huteuliwa kutoka Serikali Kuu.

23Mheshimiwa Spika, Idara ya Serikali za Mitaa baadhi ya majukumu yake ya msingi ili kuimarisha demokrasia na utawala bora ni pamoja na Kusimamia shughuli za utawala bora, kukuza demokrasia, ushirikishwaji wa wananchi na Ugatuaji wa Madaraka kwa Umma (D by D);Kuwezesha maandalizi na Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani, Kusimamia matumizi ya rasilimali katika Mamlaka za Serikali za Mitaa; Kuratibu na kusimamia utekelezaji wa shughuli za utoaji wa Huduma za Afya ya Msingi, Lishe na Ustawi wa Jamii katika Mamlaka za Serikali za Mitaa; Kuratibu na kusimamia Utekelezaji wa shughuli za utoaji wa Elimu katika Mamlaka za Serikali za Mitaa; na Kuratibu na kusimamia mkakati wa kuongeza juhudi za ukusanyaji wa mapato na matumizi katika Mamlaka za Serikali za Mitaa.

24. Mheshimiwa Spika shughuli hizo haziwezi kufanikiwa ikiwa kila kitu kinategemea kutoka serikali kuu, kutokana na ukweli kwamba halmashauri zetu hazina vyanzo vya mapato vya uhakika kwani vimepokwa na Serikali kuu.

25. Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inasisitiza kuwa uwezeshaji wa kweli utatokana na Mapinduzi ya kidemokrasia (Nguvu ya Umma), uwezeshaji utaletwa na watu kwa ajili ya watu. Uwezeshaji hapa utaanzia kwa watu wenyewe kwa kuangalia watu wanataka nini na sio dola kuamua kwa niaba ya wananchi. Misaada toka kwenye taasisi na asasi za Serikali itasaidia pale tu ambapo jamii itakuwa tayari kwa misaada hiyo na tayari ina mipango yake ya maendeleo. Kinyume na hapo ni kupoteza raslimali nyingi bila ya kuwepo matunda.

26. Mheshimiwa Spika, Serikali inatakiwa ielewe kwamba vyanzo ilivyo vipora kutoka Halmashauri ndio vilikuwa vyanzo vikubwa na nguzo imara ya kuzifikisha Halmashauri nyingi kufikia malengo ya kuondokana na utegemezi wa Serikali kuu katika kutimiza majukumu yake ya msingi ya kuwahudumia wananchi.

27. Mheshimiwa Spika, ikumbukwe kuwa ardhi ndiyo rasilimali pekee ambayo kila Halmashauri katika nchi inaimiliki. Ardhi ndiyo chanzo cha mapato cha uhakika kwa kila Halmashauri ya nchi hii, hivyo basi Serikali Kuu kujaribu kufifisha uwezo wa makusanyo ya chanzo hiki ni kuifanya halmashauri kushindwa kabisa kutoa huduma za msingi kwa wananchi wake.

28. Mheshimiwa Spika, Halmashauri zinatakiwa kuchukua 30% ya kodi ya Ardhi, hivyo inapotokea kuwa Serikali Kuu inachukua fedha hizo na urejeshaji wake unakuwa ni pale itakapojiridhisha kuwa zinahitajika, hilo sio sahihi kwa maendeleo ya wananchi.

29. Mheshimiwa Spika, Chanzo hicho cha mapato ya halimashauri kinachotokana na kodi ya ardhi kama makusanyo ya ndani (own source) ni muhimu sana katika kuzifanya halimshauri zikabiliane na changamoto mbali mbali za kuhudumia wananchi.

30. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaona kuwa ukusanyaji ufanywe na Halmashauri kama ambavyo illikuwa inafanyika miaka yote na ziada au hitaji la fedha la Serikali lipelekwe na Halmashauri na sio kinyume chake.

UTAWALA NA UENDESHAJI WA MABARAZA YA MADIWANI

31. Mheshimiwa Spika,
dhana nzima ya ugatuzi wa madaraka kutoka Serikali kuu kwenda Serikali za mitaa inatoa madaraka kwa utawala na upangaji wa mipango kwenye wilaya kwa baraza la madiwani.

32. Mheshimiwa Spika, Tamisemi ndio mlezi wa Halmashauri ikihusishwa na mabaraza ya madiwani pia, lakini imeshindwa kukemea mambo ambayo yameshika kasi kwa siku za karibuni ya kuhakikisha wale wote waliopewa ridhaa na wananchi ya kuendesha Halmashauri hizo katika uchaguzi wa Oktoba 2015, hasa wale kutoka vyama nje ya CCM wanafanyiwa hila na kuondolewa.

33. Mheshimiwa Spika, ni aibu kubwa kwa Serikali inayojinasibu kuwa ni ya kidemokrasia na inafuata misingi ya utawala bora, kwa makusudi kushindwa hata kuona au kutekeleza dhana ndogo ya madaraka kwa umma, pale ambapo wananchi wanatoa ridhaa kwa chama cha Upinzani kutoa Mwenyekiti wa kuongoza Halmashauri, mara tu anaondolewa kwa hila.

34. Mheshimiwa Spika, hivi ni kweli kati ya halmashauri takriban 134 zilizopo hapa nchini ni Wenyeviti au Mameya wanaotoka vyama vya Upinzani tu ndio wenye shida na hivyo kuondolewa? Kambi Rasmi ya Upinzani inasema hizo hila zinazofanywa na wakuu wa mikoa za kuwaondoa Mameya au Wenyeviti wa Halmashauri ni kipimo kwa Waziri Mwenye dhamana kama kweli anawajibika kwa jamii na kufuata utekelezaji wa sera ya D by D au la. Tukumbuke kwamba Meya sio mtendaji kwa nafasi yake na stahili zake zote anazipata kwa Mkurugenzi(DED), hivyo kwa hali ya kawaida ubadhirifu wa Meya unatoka wapi na Mkurugenzi kubakia akiwa ni msafi na mchapa kazi?

35. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inasema, kwa mfumo huu ambao umeibuka katika Serikali ya awamu ya tano ya kuhakikisha inasigina Katiba na sheria zake ni ishara mbaya sana katika kufikia lengo la kuwa na Serikali za mitaa zenye nguvu. Tukumbuke kwamba toka mfumo wa vyama vingi uanze hapa nchini, kuna halmashauri kama vile Karatu, Kigoma, Ujiji, Bariadi, Moshi Mjini, Musoma Mjini, Tarime ambazo zilikuwa chini ya Upinzani katika serikali za awamu ya tatu na ya nne lakini hatujawahi kusikia hiki kinachoitwa kuondolewa kwa wenyeviti wa halmashauri hizo eti kwa matumizi mabaya ya ofisi. Ni muhimu sana Serikali ya awamu ya tano iheshimu maamuzi ya wananchi hata wanapochagua wawakilishi wao kutoka vyama vya upinzani.

UWEZO WA HALMASHAURI ZETU KUKABILIANA NA JANGA LA UGONJWA WA CORONA

36. Mheshimiwa Spika
, Halmashauri ndizo zenye watu, na shughuli nyingi za kijamii na za kiuchumi zinafanyika zaidi kwenye maeneo yao. Shughuli za kiuchumi kama vile usafirishaji wa abiria kwa boda boda, bajaji, daladala, masoko katika maeneo mbalimbali n.k. Maeneo na vituo vya kuabudia.

37. Mheshimiwa Spika, udhibiti wa ugonjwa huu kwa kiasi kikubwa kinga yake tunaambiwa ni usafi na kujitenga au kuzuia misongamano ya watu katika maeneo mbalimbali ya kijamii na kibiashara. Hoja yetu ya Msingi ni kutaka kupata maelezo ni kwa vipi Halmashauri zetu zimejipanga kwa uwezo wa kifedha wa kuzuia maambukizi kuenea katika maeneo takriban yote yenye mkusanyiko wa watu?

38. Mheshimiwa Spika, ni kwa vipi pale itakapohitajika kuwapo na vituo vya “isolation”, matayarisho yake kwa sasa yako vipi na kwa kila halmashauri ina mkakati gani kuhakikisha inakabiliana na maambukizi badala ya kutegemea Serikali Kuu ambayo nayo uwezo wake unaweza kuwa ni mdogo. Ni kwa kiasi gani kila halmashauri ina uwezo wa kuhakikisha vyakula kwenye masoko yake vinauwezo wa kuhimili kipindi ambacho eneo husika linaweza kuwa kwenye karantini?

39. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inatoa rai kwa Serikali kwamba, ni vyema kujiandaa vilivyo kupambana ili kuepusha madhara makubwa pale mapambano yatakapoanza. Hivyo kinga ni bora kuliko tiba.

HUDUMA ZA AFYA YA MSINGI
40. Mheshimiwa Spika, takwimu zinaonesha kuwa watu bilioni 4, ambao ni zaidi ya nusu ya idadi ya watu duniani, hawana huduma za msingi za afya. Changamoto hii ya afya duniani zinawakabili zaidi watu katika nchi za kipato cha chini na cha kati (Least and Middle Income Countries-LMICs). Mpango wa Afya Duniani unachangia Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa kwa kutumia teknolojia ya Ada Global Health Initiative kwa manufaa ya dunia. Ushirikiano baina ya mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs), serikali za nchi za kipato cha chini na cha kati (LMICs), na mashirika ya kimataifa ya afya kwa lengo la kusaidia kuongeza upatikanaji wa taarifa za afya za kibinafsi na kuboresha utoaji wa huduma ya msingi ya afya kwa wale ambao wanaihitaji zaidi inafanyika kwa njia ya kidigital chini ya taasisi ya Ada Global Health Initiative.

41. Mheshimiwa Spika, Ada Global Health Initiative katika mtandao wake inaonesha kuwa, watu bilioni nne wanakosa upatikanaji wa huduma za msingi za afya duniani. Kuna upungufu wa wahudumu wa afya milioni saba duniani ambapo asilimia sabini na tano ya upungufu huo unapatikana maeneo ya vijijini katika nchi zinazoendelea. Aidha kuna upungufu mkubwa wa madaktari magonjwa ya akili katika nchi za kipato cha chini na cha kati. Takwimu zinaonesha kwamba uwiano ni madaktari 0.5 kwa wagonjwa 100,000. Takwimu hizo zinapaswa kutusukuma sisi watanzania kuitathmini hali ya huduma ya afya za msingi katika nchi yetu.

42. Mheshimiwa Spika, huduma za afya ni msingi mkuu wa maendeleo katika uendeshaji wa Serikali za mitaa, na utoaji wa hduma hizo ni mojawapo ya jukumu la msingi la halmashauri zetu. Vituo vya afya na Zahanati ndizo ngazi za kwanza za afya zinazoigusa jamii moja kwa moja. Kwa sababu hii, wauguzi na wafanyakazi wengine wa vituo hivyo hujulikana kama Wahudumu wa Afya. Wahudumu hao ni wawakilishi wa mfumo mzima wa huduma za afya kwa jamii na ndiyo wanaojenga hisia za jamii kuhusu uwezo, huduma na ufanisi wa wafanyakazi wa afya. Vile vile ndiyo macho na masikio ya kada nyingine za afya katika jamii. Wahudumu hao ni viungo muhimu kwa mawasiliano na pia ni viungo muhimu katika utekelezaji.

43. Mheshimiwa Spika, katika mfumo wa utawala ulivyo sasa ni dhahiri kuwa kwa sasa kutokana na takwimu toka kwa asasi zinazojihusisha na afya ni kwamba ubora na upatikanaji wa huduma za afya kuna upungufu wa 52% ya wataalam wa sekta ya afya hapa nchini, jambo ambalo linaathiri utoaji wa huduma za msingi katika sekta ya afya. Iwekwe wazi kwamba ajira zilizotolewa na serikali za takriban watumishi wa afya 7,680 sio kama inaondoa upungufu bali inaziba pengo ambalo lilitokea baada ya kuondoa takriban watumishi 7,300 katika zoezi lililoendeshwa la kuondoa vyeti feki. Nje ya upungufu huo bado kuna watumishi kuugua, vifo kwa watumishi na matatizo mengine ya kijamii yanayowakumba watumishi katika sekta ya afya, na hivyo kuzidisha upungufu na kupelekea utolewaji duni wa huduma za msingi katika afya. Huduma za afya katika maeneo ya vijijini hasa zahanati na vituo vya afya zimeathiriwa sana na upungufu mkubwa wa rasimali watu -Human Resource in Health- (HRH)[2].

44. Mheshimiwa Spika, tatizo la upungufu wa rasimali watu katika ngazi za chini limepelekea kuwepo kwa msongamano mkubwa wa wagonjwa kwenye Hospitali za mikoa na rufaa hapa nchini. Kambi Rasmi ya Upinzani inasisitiza kuwa madhara haya yote ni kutokana na Serikali kuu kuua kabisa mfumo wa kuzipa halmashauri uwezo wa kuajiri watendaji na badala yake ajira zote kuletwa Serikali kuu. Vile vile ni matokeo ya upokaji wa vyanzo vya mapato katika ngazi ya Halmashauri na hivyo kuzifanya kukosa uwezo wa kutoa huduma za msingi kwa wananchi wake.

45. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inasisitiza na kuhimiza ushiriki wa Sekta binafsi katika kuboresha utoaji na upatikanaji wa huduma za afya mijini na vijijini ili kupunguza mzigo kwa Halmashauri zetu.

ZAHANATI/KITUO CHA AFYA KILA KIJIJI/ KATA

46. Mheshimiwa Spika,
azma ya Serikali kwa mujibu wa sera ya afya ya 2007 ni Kuwa na jamii yenye afya bora na ustawi ambayo itachangia kikamilifu katika maendeleo binafsi na ya nchi. Kujenga ushirikiano kati ya sekta ya umma, sekta binafsi, mashirika ya dini, asasi za kijamii na jamii katika kutoa huduma za afya na Kuhakikisha kuwa huduma za afya ya msingi zinapatikana na kutolewa katika mfumo madhubuti na kushirikisha jamii, kwa kuzingatia sheria na miongozo iliyopo.

47. Mheshimiwa Spika, Katika kuimarisha yote hayo kwa muktadha wa upatikanaji wa huduma bora za afya, Serikali kwa kushirikiana na wadau itahakikisha kuwa kila kijiji kina zahanati na kila kata ina kituo cha afya ili kuleta uwiano katika utoaji wa huduma za afya kwa wananchi. Jambo hili ni katika Kukidhi matarajio ya wananchi kwa kuwa na huduma bora za afya.[3]

48. Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa sera hiyo ulianzishwa toka Bunge la tisa na wananchi walipewa hamasa na wakajitoa sana kujenga maboma (vituo vya afya kila kata ambavyo havikuezekwa) mengi sana. Lakini Serikali ilishindwa kutimiza ahadi yake ya kuezeka na kumalizia matenegezo mengine ili vituo hivyo vianze kazi. Takwimu zinaonesha kuwa hadi sasa Serikali bado inadaiwa takriban shilingi 184,184,497,000.00 zikiwa na kumalizia maboma ya zahanati/vituo vya afya pamoja na shule. Kambi Rasmi ya Upinzani inataka kupata mchanganua ni kiasi gani hasa ni kwa afya na shule? Hii ni ishara kubwa kabisa kuwa afya ya watanzania sio kipaumbele kwa Serikali ya CCM, kwa hali ya kawaida kama wananchi wametimiza ahadi yao inakuwaje Serikali inashindwa kutimiza kulingana na makubaliano?

ELIMU MSINGI NA SEKONDARI

49. Mheshimiwa Spika
, moja ya jukumu la TAMISEMI ni kusimamia na kuendesha elimu ya awali, msingi na Sekondari. Katika kusimamia huko ni kuhakikisha ubora wa elimu yetu unakuwa kwa kiwango ambacho kinakubalika kwa mazingira yetu ya ndani na pia kwa mazingira ya nje ya nchi, ubora au kiwango cha elimu kinachangiwa na mambo mengi, ambayo kwa muktadha wetu ni dhahiri kabisa tunashindwa, kwa kufahamu au kutokufahamu kuwa kufanya hivyo basi tunaporomosha wenyewe ubora au kiwango cha elimu hasa kwa shule zetu zinazosimamiwa na TAMISEMI.

50. Mheshimiwa Spika, ujenzi wa nchi ambayo inategemea kuwa bora duniani kwa kiwango kikubwa unategemea jinsi gani mfumo wake wa elimu ya awali hadi sekondari ulivyo imara na kuweza kutoa wahitimu ambao ni shindani na wabunifu kwa mazingira yanayowazunguka.

51. Mheshimiwa Spika
,Ni kweli kuwa matokeo mabaya katika shule zetu za awali hadi Sekondari kwa kulinganisha na yale ya shule binafsi, kwa kiwango kikubwa inatokana na uhaba na uduni wa miundombinu ya kufundishia wanafunzi, ukaguzi unaofanywa na wale wanaotakiwa kutimiza majukumu hayo na inakwenda mbele zaidi ya hapo ni kwa walimu kukosa furaha kutokana na kutopewa stahili zao za msingi na pia unyanyapaa wanaokutana nao kutoka kwa viongozi wa kisiasa kwenye maeneo yao ya kazi.

52. Mheshimiwa Spika, kwa muktadha wa hotuba yetu tunaongelea kidogo kuhusu bajeti inayotolewa na Serikali kuu kwenye kuboresha miundombinu ya kufundishia, ukaguzi na motisha kwa walimu. Kuna mambo mengi ikiwemo uwiano wa mwalimu na wanafunzi katika ufundishaji darasani, upatikanaji wa vifaa vya kufundishia (mazingira ya kufundishia na kujifunza kwa mwanafunzi n.k)

53. Mheshimiwa Spika, ni ukweli kabisa kuwa ubora wa elimu kwa sasa unazidi kudidimia japokuwa tunaambiwa ufaulu unaongezeka, jambo hili linatia mashaka sana, kwani wanafunzi katika shule zetu za awali hadi sekondari wameongezeka sana na ufaulu kwa shule zetu unapangwa kulingana na namna matokeo wanavyotaka yawe na sio “pass mark point” za chini na za juu kwa kila somo ziwe ni ngapi ili mwanafunzi awe amaefaulu kwa madaraja yaliyopangwa.

54. Mheshimiwa Spika, ni ukweli kwamba wanafunzi bado wanajifunzia katika mazingira magumu (miundombinu ya kusomea) na hili linatokana na uwekezaji mdogo unaofanywa na Serikali ambao hauoneshi dhamira ya kweli ya kuipeleka nchi yetu kuwa taifa shindani katika medani za kimataifa. Kambi Rasmi ya Upinzani inauliza ni kwanini hapo zamani wakaguzi walikuwa wanafanyakazi zao kwa umakini na umahiri na hivyo shule zetu ziliweza kufanya vyema, au ni kwanini shule za binafsi zinafanya vyema kuliko za Serikali? Tuna uhakika majibu yatatolewa lakini ni majibu ya kuficha ukweli uliopo.

55. Mheshimiwa Spika, ni ukweli kuwa ubora wa jambo unaendana moja kwa moja na gharama inayotumika, hivyo ni lazima Serikali iwekeze vyema katika eneo hili la kuimarisha elimu yetu ya awali, msingi na sekondari, jambo hili la uwekezaji halitakiwi “kuwa-compromised” na uwekezaji kwenye maeneo mengine kama ambavyo Serikali ya awamu ya tano inafanya. Nia nje ya Tanzania njema ya kesho inatokana na maamuzi ya uwekezaji kwenye elimu ya juzi, jana na leo.

56. Mheshimiwa Spika, mfumo wetu wa elimu unaendana sana na mfumo wa uendeshaji wa Serikali, umegubikwa na usiri mkubwa katika mambo ya msingi ambayo yanaharibu kizazi chetu cha leo na kesho na hivyo kuifanya Tanzania ya kesho na kesho kutwa isiweze kutabirika. Kambi Rasmi ya Upinzani inasema kuwa hatuwezi kuwa na elimu bora kama rasimali fedha na watu havitengwi kwa viwango toshelevu.

57. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaona dhana mpya ya elimu (new concept on education is basing on competency based approach) itakuwa suluhu kwa nchi yetu kwa kuanza kuitimia kuanzia shule za awali, msingi na sekondari, japokuwa sio mpya kwani zamani ilikuwa inatumika katika shule zetu lakini watawala wakaitupilia mbali. Nchi za Scandnavia na Asia zimepiga hatua kubwa katika sekta ya elimu kwa dhana hiyo.

58. Mheshimiwa Spika, Katika dhana mpya ya elimu ni kwamba inamtayarisha mwanafunzi kuelimika kwa kupata; kwanza uelewa (knowledge) wa kupata na kutumia taarifa mbalimbali, pili kuwa na uwezo(ability) wa kufanya tafakuri ya jambo; na tatu kupata ujuzi (skills) ujuzi wa kushirikia katika kutafuta suluhisho. Uwezeshaji huo wa elimu ili aweze kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa jamii na uchumi wa nchi.

59. Mheshimiwa Spika, Aidha, dhana mpya ya malengo ya elimu kama inavyotumika kwa nchi za Scandnavia na Asia ni kumuandaa mwanafunzi kutumia mafundisho aliyopewa shuleni kuwa tayari katika kutafuta ufumbuzi wa matatizo yanayotokea dunia. Competency based inasisitiza elimu itakayotolewa iweze kutoa suluhisho kwenye matatizo (problem solving skills) katika ulimwengu tunaoishi kama vile kuongezeka kwa idadi ya watu, kukua kwa teknolojia na matatizo mengine katika jamii. Aidha, katika kuwa na competency base katika elimu, ni muhimu kuangalia uhusiano kati ya mwalimu na mwanafunzi.

60. Mheshimiwa Spika, Ni ukweli kwamba katika elimu yetu kuna “mismatch” kati ya Mitaala na ujuzi unaohitajika katika soko la ajira. Hoja ya msingi ni je kwa Tanzania elimu yetu ya awali, msingi na sekondari inamuandaa mwanafunzi katika kupambana na matatizo na kutoa suluhisho kwa matatizo tuliyo nayo katika jamii yetu na ina muwezesha kuishi bila kutegemea msaada wa mtu mwingine? Je, mhitimu huyo anachangiaje katika uchumi wetu mchanga? Ni muda mwafaka sasa kuangalia jinsi ya kuimarisha ubora wa elimu yetu ya msingi na sekondari.

61. Mheshimiwa Spika, takwimu zinaonesha kuwa kwa mwaka wa fedha 2018/19 uthibiti ubora wa shule ulipangiwa shilingi bilioni 1.5 lakini hadi mwaka huo unamalizika fedha hizo hazikutolewa, vivo hivyo shilingi bilioni 25 zilitengwa kwa ajili ya kuimarisha ubora wa shule za sekondari (Secondary Education quality Improvement Programme-SEQUIP) na mradi huo haukupewa kiasi chochote cha fedha.

62. Mheshimiwa Spika, eneo la uthibiti ubora wa elimu limeathiri sana hali ya ukaguzi wa shule zetu, takwimu zilizotolewa na asasi inayojihusisha na elimu (Haki Elimu) zinaonesha kuwa kwa mwaka wa fedha 2018/19 utafiti kwa shule za msingi 5,723 kati ya shule 17,174. Ni asilimia 33 tu ya shule ndizo zilizo kaguliwa. Maana yake kwa mwaka huu wa 2020 kuna uwezekano mkubwa shule zilizo kaguliwa zikawa ni chini au ikawa ni mara mbili ya zile zilizo kaguliwa mwaka wa fedha 2018/19.

63. Mheshimiwa Spika, kwa upande wa shule za sekondari ni shule 1,185 kati ya shule zote 4,779 za sekondari. Hii ikiwa na maana kuwa ni asilimia 25 tu ndizo zilizo kaguliwa. Kambi Rasmi ya Upinzani inasisitiza tena, ni vyema Serikali ikawekeza katika kuhakikisha ubora wa elimu na hilo ndio uwekezaji wa katika kupata Tanzania bora ya kesho na keshokutwa.

64.Mheshimiwa Spika, Katika suala la miundombinu nalo limekuwa kama kidonda ndugu kwani toka awamu ya awamu ya nne kampeni ya ujenzi wa shule za kata ulipoanza, ni jambo jema na wananchi waliitikia na walijitolea sana kwa ujenzi wa mashule(maboma) ili serikali imalizie ujenzi ambao nguvu za wananchi ziliishia, lakini hadi leo takwimu za TAMISEMI zinaonesha kuwa bado serikali haijamalizia ujenzi wa maboma yaliyojengwa kwa nguvu za wananchi. Jambo hili la Serikali kushindwa kukamilisha mkataba wake na wananchi ni kuwakatisha tama wananchi katika masuala ya kujitolea, takwimu za Tamisemi zinaonesha kiasi cha shilingi 184,184,497,000/- bado hakijatolewa kwa ajili ya umaliziaji wa maboma ya shule na zahanati/ vituo vya afya. Kambi Rasmi ya Upinzani inataka kufahamu kati ya hizo, Maboma ya shule zinadaiwa kiasi gani na afya ni kiasi gani?

WAKALA WA BARABARA MIJINI NA VIJIJINI (TARURA)

65. Mheshimiwa Spika
, kulingana na sheria iliyopitishwa na Bunge, ni kuwa Wakala huyu wa Barabara Mijini na Vijijini katika utendaji kazi wake hawajibiki kwa namna yoyote kwenye Baraza la madiwani au kwa Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri. Tukumbuke kwamba eneo la kazi la TARURA liko chini ya mamlaka ya Baraza la Madiwani na Mkurugenzi wa Halmashauri. Hivyo utendaji kazi wa TARURA kwa njia moja au nyingine unakosa chombo cha usimamizi wa kazi zake. TARURA kiutendaji inawajibika kwa chombo au mamlaka gani? Kwa vyovyote vile vile haiwezekani kuondoa madiwani katika kushauri na kusimamia matengenezo ya barabara zilizo ndani ya kata husika.

66. Mheshimiwa Spika, Baraza la madiwani (kupitia kamati yake ya fedha) kabla ya uwepo wa TARURA linakuwa ziara kila mwezi ya kukagua miradi yote ambayo iko kwenye matengenezo. Lakini kutokana na TARURA kuzaliwa utaratibu huo wa kikanuni umekwisha na barabara za vijijini kwenye kata zimebakia bila ya kuwa na “mwenyewe”kwani diwani hana tena uwezo wa kumsimamia makandarasi.

67. Mheshimiwa Spika,
kwa kuwa waheshimiwa madiwani pamoja na mambo mengine ndio wanaofahamu kwa undani ni barabara gani na umuhimu wake kwa wananchi kwenye kata husika na matengenezo yake yanaweza kufanyikaje kulingana na majira ya mwaka. Hivyo kutokuhusishwa kwa wananchi katika suala hili na kuachwa kuwa ni jukumu la TARURA badala ya kupunguza gharama na kujenga kwa ubora zaidi limeongeza gharama na ubora wa miundombinu inayojengwa umekuwa hafifu zaidi.

68. Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani inasema, tulifanya makosa katika sheria ya uanzishwaji wake kutokutambua uwepo wa Baraza la madiwani na Mkurugenzi wa Halmashauri katika kile kinachoitwa “check and balance” ya TARURA, hivyo basi turekebishe sheria ya TARURA ili pamoja na kazi zake ushirikishwaji na uwajibikaji wake uwe kwenye ngazi ya Halmashauri kupitia vyombo vyake.

69. Mheshimiwa Spika,
kwa upande wa maduhuli yanayokusanywa na TARURA (Ushuru wa maegesho) bado ni mdogo sana katika uendeshaji wake, japokuwa ni mdogo lakini bado TARURA inalazimika kuwasilisha maduhuli hayo moja kwa moja kwenye mfuko wa Barabara (Tanzania Road fund), na baadae aombe fedha kutoka kwenye mfuko huo ili kutekeleza majukumu yake.

70. Mheshimiwa Spika, katika utaratibu huu wa kupeleka kwenye mfuko mkuu, baadae unaomba tena kwenye mfuko mkuu ili uweze kutumia kulingana na bajeti ambayo tayari ipo, ni mfumo wa kiukiritimba mno na sheria ya Mfuko wa barabara namba 220 sehemu ya 2 kifungu kifungu cha 2 inatakiwa kufanyiwa marekebisho, kwani badala ya kwenda mbele tunarudishwa nyuma kwa sheria ambazo tumezitunga sisi wenyewe.

71. Mheshimiwa Spika, uhalisi ni kwamba wakala huyo ana majukumu makubwa mno yanayohitaji fedha za kutosha kutekeleza wajibu wake kulingana na hali halisi ya uharibikaji wa barabara zetu za vijijini na mijini hasa katika kipindi hiki cha mvua kubwa sana ambazo zinaendelea kunyesha nchi nzima(masika). Na ukweli ni kuwa wanaofahamu ni wapi barabara inahitaji matengenezo ya haraka ni madiwanipamoja na mkurugenzi wao, sana nao hawana wajibu wowote kwa TARURA. Hii ni shida kubwa sana ambayo inatakiwa kutolewa ufumbuzi wa haraka.

72. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2020/21 wakala umetengewa jumla ya shilingi 344,556,044,824.00 kati ya fedha hizo za ndani ni shilingi 275,034,159,00.00 na za nje ni shilingi 69,521,885,824.00. Lakini kulingana na hali halisi ya mvua zilivyo nyesha na uharibifu mkubwa wa miundombinu ya ulifanyika kwa barabara zilizokuwa zinahudumiwa na halmashauri ni dhahiri kuwa kiasi cha fedha kilichoombwa hakitaleta matokeo chanya yoyote katika kuifanya TARURA kutimiza majukumu yake.

73. Mheshimiwa Spika, Fedha ambazo TAMISEMI inaomba kuidhinishiwa Shilingi 275,034,159,000.00 ni fedha za ndani kwa ajili ya kazi za TARURA, zitatumika kutekeleza kazi zifuatazo:- i) Ujenzi na matengenezo ya barabara za vijijini na mijini zenye urefu wa kilomita 22,746.41 ambapo kilomita 13,450.43 ni matengenezo ya kawaida, kilomita 5,858.88 ni matengenezo ya maeneo korofi na kilomita 3,437.1 ni matengenezo maalum; na ii) Ujenzi na ukarabati wa madaraja 99, makalvati 256 na mifereji ya maji kilomita 78.

74. Mheshimiwa Spika, kama katika bajeti ya 2019/20 zilitengwa jumla ya shilingi 42,112,000,000.00 kwa ajili ya kufanya matengenezo ya baraza zenye urefu wa KM 86.6 tu, sasa hiyo bajeti iliyo tengwa kutengeneza kilometa takriban KM 22,746.41pamoja na ujenzi na ukarabati wa madaraja 99, makalavat 256 na mifereji ya maji yenye urefu wa KM 78? Huu ni utani ambao mwisho wake ni kuhakikisha wananchi wanashindwa kutoka huko waliko kwenda maeneo mengine ya nchi hii, fikiria pia mvua nyingi ambazo zimenyesha na zinaendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu.

75. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani kama ambavyo tumesema awali barabara zilizokuwa zinahudumiwa na Halmashauri zetu zinaweza kuhudumiwa pia na TARURA lakini kama ikiwa chini ya Baraza na vyanzo vya mapato ya ndani halmashauri vikatumika kuiongezea nguvu.

76. Mheshimiwa Spika,
kuna jambo lingine ambalo ni la ajabu na tunaona litakwaza utendaji wa TARURA,kwa hali halisi tuliyoieleza hapo awali, inakuwaje TARURA inapanga bajeti yake bila ushirikishwaji wa baraza la madiwani au ofisi ya Mkurugenzi? Inawezekana bajeti inayoombwa na TARURA ni kwaajili ya kulipata posho na mishahara na sio kwa lengo la kujenga na kukarabati miundombinu ya barabara vijijini na mijini. Bajeti hiyo inayoombwa haina chembe ya ushirikishwaji wa wanufaikaji wa miundombinu inayotarajiwa kujengwa.

WAKALA WA MAJI NA MAJI TAKA VIJIJINI-RUWASA

78. Mheshimiwa Spika
, ni ukweli kwamba idadi ya watu Tanzania imeongezeka na inazidi kupamba moto, toka watu milioni 12.3 mwaka 1967 hadi watu milioni 44.9 mwaka 2012, na sasa takriban watu milioni 55 mwaka 2019. Na kati ya hao asilimia 30 wanaishi mijini na asilimia takriban 70 wanaishi vijijini. Ina kadiriwa kwamba ifikapo 2050[4], idadi ya watu kwa Tanzania itakuwa milioni 137 na asilimia 50 watakuwa wanaishi mijini. Hivyo basi ni vyema kuweka miundombinu inayoweza kukidhi mahitaji ya ukuaji wa idadi ya watu kwa muda uliopo na ujao.

79. Mheshimiwa Spika, changamoto iliyopo kwa RUWASA ni sawa na zingine, kwani kitendo cha kuondoa mfumo ambao ulikuwa unajaribu kubadilisha mtazamo wa wanannchi katika kumiliki miradi yao ya maendeleo kuanzia ngazi za kubuni hadi kuendesha imeondoka, na hivyo miradi hii ya maji itaonekana sio ya wananchi bali ni mali ya Serikali. Hili ni kosa ambalo ni muendelezo wa makosa yanayofanywa na Serikali hii ya awamu ya tano kupoka mamlaka ya wananchi na kutarudisha Serikali Kuu.

80. Mheshimiwa Spika, Miradi ya maji na huduma zingine za kijamii zinatakiwa zibuniwe na wananchi, kujengwa kwa ushiriki wa wananchi na uendeshaji pia wananchi washirikishwe ili dhana nzima ya uendelevu iwepo. Kinyume cha hapo ni kuharibu rasilimali na fedha za walipa kodi. Kambi Rasmi ya Upinzani inatafakari sana kuhusu dhana hii mpya ya Serikali ya awamu ya tano ya kupora madaraka ya wananchi kupitia Baraza la madiwani. Sasa kama huduma za maji zimeondolewa na huduma za barabara zimeondolewa, je bado kuna umuhimu wa kuwa na wawakilishi wa wananchi katika baraza la madiwani? Au uwepo wa madiwani ni muhimu kama huduma zote muhimu ambazo utatuzi wake unahusisha wananchi wenyewe zinatwaliwa na Serikali Kuu?

UTEKELEZAJI WA BAJETI 2019/20 NA MAOMBI YA FEDHA 2020/21

81. Mheshimiwa Spika,
kwa mwaka wa fedha, 2019/20 Tamisemi, kwa upande wa maendeleo zilitengwa jumla ya Shilingi 496,563,123,910.00 na fedha za ndani zikiwa ni Shilingi 286,738,400,000.00 na Shilingi 209,824,723,910.00 zikiwa ni fedha za nje. Hadi kufikia mwezi February, 2020 fedha zilizokuwa zimetolewa kwa miradi ya maendeleo ni shilingi 196,078,940,851.00 sawa na asilimia 68.4 zikiwa ni fedha za ndani na shilingi 281,660,973,484.00 sawa na asilimia 86.6 zikiwa ni fedha za nje.

82. Mheshimiwa Spika, Kwa mwaka wa fedha 2020/21, OR – TAMISEMI inaomba kuidhinishiwa makadirio ya jumla ya Shilingi 413,579,583,000.00 kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo ikiwa ni pungufu ya shilingi 82,983,540,910.00 kwa kulinganisha na zile zilizoidhinishwa mwaka jana. Kati ya fedha hizo, Shilingi 276,534,159,000.00 ni fedha za ndani na Shilingi 137,045,424,000.00 ni fedha za nje ikiwa ni pungufu ya shilingi 72,779,299,910.00 kulinganisha na zilizotengwa mwaka 2019/20.

HITIMISHO

83. Mheshimiwa Spika
, ni ukweli uliowazi kuwa TAMISEMI ni wizara ambayo inahudumia watanzania wote ikiwa na lengo la kuifanya kuwa na mamlaka kamili kwa mujibu wa Ibara ya 145 na 146 sambamba na sera ya ugatuaji wa madaraka.

84. Mheshimiwa Spika, kitendo chochote kitakachofanyika cha kuiondolea TAMISEMI hasa mabaraza ya halmashauri uhuru wao katika kuhakikisha yanatoa huduma kwa wananchi, ni kitendo ambacho hakitoleta maendeleo kwa wananchi wengi, na hivyo kinapingana na dhana nzima ya wananchi kuwa ndio wenye mamlaka ya kuamua, kupanga na kushiriki katika mchakato mzima wa kujiletea maendeleo.

85. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani mara zote imekuwa ikishauri na kutahadharisha juu ya azma ya Serikali inayopoka madaraka ya wananchi na kuyarudisha Serikali Kuu kuwa ni kuharibu kabisa mfumo wa kuipeleka nchi yetu kuwa nchi ya uchumi wa kati na nchi inayotegemea viwanda. Kwa bahati mbaya sana Serikali ya CCM imeshindwa kuielewa dhana hiyo ya wanachi kuwa wamiliki na wasimamizi wa mipango na miradi yao ya maendeleo.

86. Mheshimiwa Spika, jambo hilo la kupoka uhuru na vyanzo vikubwa vya mapato kwa halmashauri, limesababisha halmashauri nyingi kushindwa kujiendesha na hivyo kushindwa kutoa huduma za msingi kwa wananchi. Hivyo basi kuwa tegemezi na ombaomba kwa Serikali kuu.

87. Mheshimiwa Spika,
kwa kuwa mwaka huu ni mwaka wa uchaguzi, tunawataka watanzania ambao wametuelewa hasa katika dhana nzima ya kutoa uhuru kamili kwa Serikali za mitaa kupitia mabaraza ya madiwani, tuungane wote kurejesha kile ambacho Serikali ya awamu ya tatu ilikianzisha cha kufanya maboresho ya Serikali za mitaa ili kuwa Imara katika kuleta maendeleo kwa wananchi.

88. Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani, naomba kuwasilisha.


Japhary R. Michael(Mb)
Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani-Ofisi ya Rais, TAMISEMI.
08/04/2020
 
TARURA wabunge wa upinzani hamuonyeshi maturity hata kidogo.
Tarura anaripoti kwa mratibu wa mkoa ambaye ni sehemu ya idara chini ya ofisi ya Mkuu WA mkoa. Ambaye pia ni serikali ya mitaa hivyo mtakutana kwenye vikao vya RCC.

Mngetaka vinginevyo mngeshauri wakati wanaunda sheria,

Ugatuzi na Uhuru WA serikali za mitaa ulipingwa tangu miaka ya 1980s kuwa haziwezi kujiendesha na wakati parokia za kikatoliki zinajitegemea 100% na zingine kwa ruzuku ndogo Leo wamealiamsha ni vizuri.
Ugatuzi huo na Uhuru uendane na utendaji mzuri wa watendaji wake hasa wakuu wa mikoa kwani ni sehemu ya serikali za mitaa na nafasi yake ni ya kisiasa lkn haigombewi; hilo hamjalitazama poleni sana.

RUWASA bado hamjafikiri vema.


Tukumbuke, upinzani si hotuba nzuri na maneno ya kuvutia Bali ni nguvu inayonyesha nia ya kubadili na kuhakikisha mabadiliko yanatokea.
Mkifeli hilo hasa bungeni umaana unapotea.
 
Back
Top Bottom