Uchaguzi 2020 Hotuba ya Mkurugenzi Uchaguzi Dkt. Wilson Mahera Charles katika ufunguzi wa kikao cha Tume ya Taifa ya Uchaguzi na watoa huduma ya habari mitandaoni

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Apr 18, 2017
2,794
11,955
Hotuba ya Mkurugenzi Uchaguzi Dkt. Wilson Mahera Charles katika ufunguzi wa kikao cha Tume ya Taifa ya UIchaguzi na watoa huduma ya habari mitandaoni katika ukumbi wa Mikutano wa Mwl. J. K. Nyerere 15 SEPTEMBA, 2020

Wakurugenzi & Wakurugenzi Wasaidizi wa Idara,

Watoa huduma ya habari mitandaoni,

Watendaji wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi,

Wanahabari,

Mabibi na Mabwana.


Bwana Asifiwe,

Tumsifu Yesu Kristo,

Assalam Aleykum.


Napenda nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia uzima na kutuwezesha kukutana hapa siku ya leo kwa ajili ya kikao hiki muhimu. Kikao hiki ni muhimu kwa mustakabali wa nchi yetu hasa katika kipindi hiki tunapoelekea katika Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani wa mwaka 2020.

Kipekee, niwashukuru ndugu Watoa huduma ya habari mitandaoni kwa kuitikia wito na kuhudhuria kikao hiki ambacho kinakusudiwa, pamoja na mambo mengine, kutoa ufafanuzi wa masuala kadhaa yahusuyo michakato mbalimbali ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020. Karibuni sana.

Ndugu Watoa huduma ya habari mitandaoni;
Nitumie nafasi hii kuwashukuru kwa kuiwezesha Tume kutekeleza majukumu yake na kuiwezesha kuwa karibu na Wadau wa Uchaguzi kwa njia ya taarifa na habari mnazozitoa kwa wakati. Hali kadhalika, kuiwezesha Tume kutumia vyombo vyenu kwa ajili ya elimu ya mpiga kura na kufafanua hoja mbalimbali kutoka kwa wadau.

Mathalan, ipo mitandao ambayo imetoa nafasi ya kuchapisha/kutangaza habari/makala za kuelimisha umma kuhusu Tume na majukumu yake. Kupitia Redio na Runinga za mitandaoni, Tume imeshiriki vipindi mbalimbali vyenye kulenga kutoa elimu kwa wapiga kura. Ni dhahiri kwamba bila ushirikiano huo Tume isingeweza kufanikisha jambo hilo.

Ndugu Watoa huduma ya habari mitandaoni;
Kwa niaba ya Tume napenda kuwashukuru waandishi wa habari za mitandaoni, ambao ndio wanaofanya kazi kwa karibu zaidi nasi, na kila tunapowahitaji hawajawahi kusita kushirikiana nasi. Tumewaona daima wakitoa kipaumbele kwa shughuli na taarifa za Tume. Asanteni sana.

Ndugu Watoa huduma ya habari mitandaoni;

Tume inavitambua vyombo vyenu kwa sura mbili. Kwanza, kama daraja linalounganisha Tume na wadau kwa njia ya mawasiliano na pili, kama mojawapo ya Wadau muhimu wa Uchaguzi. Hivyo, mko hapa leo kama Wadau muhimu wa uchaguzi ili kwa pamoja tuweze kujadiliana kuhusu masuala mbalimbali ya Uchaguzi.

Napenda kuwafahamisha kuwa, hadi sasa Tume imefanya maandalizi mbalimbali ya Uchaguzi Mkuu. Hata hivyo, ili zoezi la uchaguzi lifanikiwe, kwa kiwango kikubwa linategemea sana ushirikiano wenu, katika kutoa taarifa na kuwaelimisha Wananchi juu ya umuhimu wa zoezi hili.

Katika muktadha huo, Tume inaamini kuwa mkipata uelewa mzuri wa michakato ya uchaguzi basi itakuwa rahisi kwenu kuwaelimisha na kuwahamasisha wananchi kupitia vyombo vyenu vya habari ili kushiriki kikamilifu katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.

Dhamira hiyo ndiyo iliyoisukuma Tume kuandaa kikao cha pamoja ili kupeana taarifa na kufahamishana kuhusu taratibu mbalimbali za uchaguzi. Vilevile, kupitia kikao hiki tutapata wasaa wa kujadili kuhusu taratibu na kanuni za utangazaji wakati wa uchaguzi mkuu.

Ndugu Watoa huduma ya habari mitandaoni;
Katika maandalizi ya Uchaguzi Mkuu, Tume imekamilisha uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ambao ulifanyika mara mbili kama inavyoelekezwa katika kifungu cha 15 (5) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 na kifungu cha 21 (5) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292.

Uboreshaji wa Daftari ulianza tarehe 18 Julai, 2019 na kukamilika 20 Juni, 2020. Katika kipindi hicho, awamu mbili za uboreshaji wa daftari zilifanyika, hali kadhalika uwekaji wazi wa daftari la awali.

Katika awamu zote mbili, uboreshaji ulifanyika katika vituo 37,814 vya kuandikisha wapiga kura. Katika zoezi hilo Jumla ya Wapiga Kura wapya 7,326,552 waliandikishwa sawa na asilimia 31.63 ya Wapiga Kura 23,161,440 walioandikishwa mwaka 2015. Aidha, Jumla ya Wapiga Kura 3,548,846 waliboresha taarifa zao na Wapiga Kura 30,487 waliondolewa kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kutokana na kukosa sifa kwa mujibu wa sheria. Baada ya kuwaondoa Wapiga Kura ambao taarifa zao zimejirudia, kwa hivi sasa Daftari lina jumla ya Wapiga Kura wapatao 29,188,347.

Kutokana na idadi hiyo ya wapiga kura, katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu kutakuwa na vituo 80,155 vya kupigia kura na kila kituo kimoja kitakuwa na Wapiga Kura wasiozidi 500.

Ndugu Watoa huduma ya habari mitandaoni;
Katika maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, hakukuwa na marekebisho katika Sheria za Uchaguzi. Hata hivyo, Tume imefanya maboresho ya Kanuni za Uchaguzi wa Rais na Wabunge za mwaka 2020 na Kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa (Uchaguzi wa Madiwani) za mwaka 2020. Hali kadhalika, imekamilisha Maelekezo ya Uchaguzi kwa ajili ya wadau mbalimbali na Watendaji wa Uchaguzi.

Ndugu Wahariri wa vyombo vya Habari;

Tume kupitia vyombo vyenu vya habari ilitangaza ratiba ya Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani na kama ambavyo mmesikia, Uchaguzi Mkuu umepangwa kufanyika siku ya Jumatano tarehe 28 Oktoba, 2020. Serikali kwa upande wake tayari imetoa tamko la kuitangaza siku hiyo kuwa ni siku ya mapumziko.

Kwa mujibu wa ratiba hiyo, uteuzi wa wagombea ulifanyika tarehe 25 Agosti, 2020.

Ndugu Watoa huduma ya habari mitandaoni;
Kwa mujibu wa ratiba ya uchaguzi, kipindi cha kampeni za uchaguzi kilianza tarehe 26 Agosti, 2020 na kinatarajiwa kumalizika tarehe 27 Oktoba, 2020 kwa upande wa Tanzania Bara. Kwa kuzingatia ratiba ya uchaguzi iliyotolewa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) Kampeni za uchaguzi kwa upande wa Tanzania Zanzibar zitaisha tarehe 26 Oktoba 2020 ili kupisha upigaji wa kura ya mapema ya Rais wa Zanzibar, Mwakilishi na Diwani.

Katika kipindi cha kampeni, vyama vya siasa vitapata fursa ya kuwanadi wagombea na kuelezea sera na Ilani za Uchaguzi za vyama vyenu. Katika eneo hili, uzoefu unaonyesha kuwa kipindi cha Kampeni kunakuwa na joto kali la kisiasa linatokana na baadhi ya watu kukosa uvumilivu wa kisiasa hali ambayo inaweza kuhatarisha amani na utulivu wa nchi. Kipindi hicho cha kampeni ndio ambacho vyombo vya habari mnapaswa kuwa makini kwa kuhakikisha kuwa haviwi chanzo cha joto hilo. Njia muafaka ya kuepukana na hilo, ni kuzingatia misingi ya maadili ya kazi yenu.


Ndugu Wahariri wa vyombo vya Habari;

Wote tunafahamu kuwa kampeni za uchaguzi zinasimamiwa na maadili ya uchaguzi, hivyo Tume kwa kushirikiana na Vyama vya Siasa pamoja na Serikali tuliandaa Maadili ya Uchaguzi ya mwaka 2020 ambayo yalisainiwa na pande zote mnamo tarehe 27 Mei, 2020. Ni matarajio yetu kuwa mtayasoma maadili hayo ili kujipatia uelewa.

Ndugu Watoa huduma ya habari mitandaoni;
Maadili hayo ya Uchaguzi, pamoja na mambo mengine, yanavitaka Vyama vya Siasa kufanya Kampeni za kistaarabu na kuepuka kufanya fujo au kuchochea vurugu ya aina yoyote katika mikutano ya vyama vingine; kutokutumia lugha ya matusi, kashfa, kejeli, udhalilishaji na vitisho au lugha inayochochea uvunjifu wa amani au kuashiria ubaguzi wa kijinsia, ulemavu, rangi au maumbile kwenye mikutano na kwenye shughuli zote za kampeni.

Pamoja na shughuli nyingine mnazozifanya, niwaombe kipindi cha kampeni kitumike pia kuwahamasisha wananchi hasa Wapiga Kura kushiriki katika kampeni hizo ili waweze kuwapima wagombea na hatimaye kujitokeza kwa wingi siku ya Kupiga Kura.

Ndugu Watoa huduma ya habari mitandaoni;

Maeneo mengine muhimu kwa wanahabari kuyafahamu ni bajeti ya uchaguzi na vifaa vya uchaguzi. Katika kuandaa na kuendesha Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, Tume iliandaa Bajeti ya kiasi cha Tsh. 331,728,258,035.00 zinazotarajiwa kutumika. Kwa kuzingatia kifungu cha 122 cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupitia Mfuko Mkuu wa Hazina, itagharimia shughuli zote za Uchaguzi kwa asilimia mia moja.

Katika eneo la vifaa vya uchaguzi Tume inaendelea na mchakato wa ununuzi wa vifaa mbalimbali sambamba na uchapishaji wa fomu, sheria za uchaguzi, kanuni na maelekezo. Jumla ya zabuni ishirini na tano (25) zimetangazwa ambazo zinahusisha uchapishaji wa nyaraka mbalimbali za uchaguzi, na ununuzi wa vifaa vya uchaguzi.

Eneo la Elimu ya Mpiga Kura ni eneo lingine muhimu katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu. Kwa mujibu kifungu cha 4C cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi Sura ya 343 Tume imepewa mamlaka ya kutoa Elimu ya Mpiga Kura nchi nzima, kuratibu na kusimamia Taasisi au Asasi zenye nia ya kutoa elimu hiyo.

Hivyo, Tume kwa upande wake imejipanga kutoa habari na elimu ya mpiga kura kwa njia mbalimbali ikiwemo matumizi ya Vyombo vya Habari. Katika eneo hili tunategema mchango wenu, Tume inaamimi mtafanya hivyo kwa kuwa mmeshirikiana nasi katika maeneo mengi yaliyotuwezesha kufanikisha majukumu yetu.

Ndugu Watoa huduma ya habari mitandaoni;
Niwaombe msichoke kuwasisitiza na kuwahimiza wadau na wananchi kwa ujumla kuzingatia Sheria za Uchaguzi, Kanuni na Maelekezo ya Tume. Tume nayo kwa upande wake itaendelea kuzingatia Sheria za Uchaguzi na Kanuni zilizotungwa chini yake katika michakato yote ya uchaguzi.

Aidha, nitoe rai kwenu kutenda haki sawa kwa vyama vyote na kuhakikisha mnawapa wagombea nafasi kutangaza na kunadi sera na ilani za vyama vyao. Ni matarajio ya Tume kuona kwamba vyombo vya habari vinatoa kipaumbele kwa masuala yanayoelekea kujenga umoja wa kitaifa badala ya taarifa na habari ambazo zinachochea vurugu. Tukumbuke kuwa Tanzania sio kisiwa, tusipotumia vizuri taaluma yetu basi kalamu zenu zinaweza kuiingiza nchi kwenye machafuko kama ilivyotokea katika maeneo mengine.

Ndugu Watoa huduma ya habari mitandaoni;

Tume inapenda kuwahakikishia kuwa itatoa taarifa kwa wakati kwa kadri itakavyowezekana na inatarajia kuona nanyi mkitoa taarifa hizo kwa usahihi, na kwa wakati. Tume inaahidi kuwapa ushirikiano pale mtakapohitaji ufafanuzi wa jambo lolote.

Tume pia itajitahidi kukutana nanyi ili kutoa taarifa juu ya hatua mbalimbali za mchakato wa uchaguzi. Lengo la haya yote ni kuona watanzania wanapata taarifa na hamasa ili mwishowe kila mwenye sifa ya kupiga Kura ajitokeze siku ya Uchaguzi.

Tume ina matumaini makubwa ya kufanikisha Uchaguzi huu kwa kutegemea ushiriki wenu katika hatua zote zilizosalia hadi kufikia siku ya uchaguzi. Imani hii inatokana na ushirikiano mlioonesha hususan wakati wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga kura.

Kwa mara nyingine, napenda kuwashukuru tena kwa kuitikia wito na kushiriki kikao hiki muhimu kwetu sote. Tume itaendelea kuwashirikisha kwa kadri itakavyowezekana na kama kawaida itasimamia uchaguzi huu kwa kuzingatia Katiba, Sheria, Kanuni na Taratibu mbalimbali zinazosimamia uendeshaji wa uchaguzi. Lengo likiwa ni kuhakikisha Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 unakuwa huru, wa uwazi, wa haki na wa kuaminika kwa kuweka mazingira sawa ya ushindani kwa wagombea na vyama vyote vya siasa vitakavyoshiriki.

Baada ya kusema hayo, sasa napenda kutamka rasmi kuwa kikao chetu kimefunguliwa.

ASANTENI KWA KUNISIKILIZA
 

Attachments

  • HOTUBA YA MKURUGENZI UCHAGUZI .pdf
    325.4 KB · Views: 8
NEC msitafute uchochoro kuwatupia lawama waandishi wa habari na tasnia ya Habari kwa ujumla nyie ndio mnataka kuingiza nchi kwe machafuko wagombea mliowaengua wote kwa maagizo toka juu warudisheni uchaguz uwe huru na haki haiwezekan wagombea wa ccm pekee ndio watimize vigezo vyote afu upinzan wakose vigezo acheni hizi sarakasi kaa vile mmewajazia fomu wagombea wa ccm bana 😡 😡 😡
 
Back
Top Bottom