Hotuba ya Mh. Mbatia (MB) kuhusu mapato na matumizi ya wizara ya ujenzi 2016/17

Feb 24, 2016
33
8
MAONI YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI MHESHIMIWA JAMES FRANCIS MBATIA (MB) KUHUSU MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA YA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO KWA MWAKA WA FEDHA WA 2016/2017

(Yanatolewa chini ya Kanuni za Bunge, Kanuni ya 99(9), toleo la mwaka 2016)

1.0 UTANGULIZI

Mheshimiwa Spika, kabla ya yote, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya njema na kuniwezesha kusimama mbele ya Bunge hili ili niweze kutoa maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni (KRUB), kuhusu Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa mwaka fedha 2016/2017.

Mheshimiwa Spika, naomba nitumie fursa hii nitoe shukrani zangu za dhati kwa kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni Mheshimiwa Freeman Aikaeli Mbowe(Mb) kwa kuniteua kuwa msemaji wa wizara hii. Aidha napenda kumshukuru Mheshimiwa Willy Qambalo(Mb) Naibu Waziri Kivuli na mbunge wa Karatu kwa ushauri na maoni yake yaliyofanikisha kuandaa hotuba hii.

Mheshimiwa Spika, kwa unyenyekevu mkubwa nawashukuru wapiga kura wa jimbo la Vunjo kwa kunichagua kwa asilimia 73 kuwa Mbunge wao, nawahakikishia utumishi wenye kuzingatia misingi ya kukuza utu wao na Taifa kwa ujumla. Kwa namna ya pekee natoa shukrani zangu kutoka moyoni kwa famila yangu, ndugu, jamaa na marafiki wote kwa msaada wa hali na mali wanaonipatia katika kutekeleza majukumu yangu.


2.0 SEKTA YA UJENZI NCHINI

Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kupitia Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi) imekabidhiwa majukumu ya kutekeleza Mipango ya msingi ya ujenzi, matengenezo ya barabara, vivuko, nyumba na majengo ya serikali lakini kwa bahati mbaya, Serikali hii imeshindwa kutimiza ahadi zake ipasavyo na badala yake jamii ya Kitanzania sasa inashuhudia ongezeko la msongamano wa magari hususani katika Jiji la Dar es Salaam, Mwanza, Arusha na Mbeya; Ucheleweshaji wa kumalizika miradi ya ujenzi pamoja na ongezeko la gharama za miradi ambazo kwa kiasi kikubwa hutokana na uwepo wa masilahi binafsi ya wachache katika nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, pia tumeshuhudia barabara nyingi za vijijni hasa kipindi hiki hazipitiki kabisa kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha au ujenzi wa barabara usiokidhi viwango. Ubovu wa barabara hizi unasababisha adha kubwa kwa watanzania hasa waishio vijijini.

Mheshimiwa Spika, katika kitabu chake cha Binadamu na Maendeleo Ukurasa wa 29 aya ya pili, Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere anafafanua maana ya maendeleo.

“maendeleo maana yake ni maendeleo ya watu. Mabarabara, majumba, kuongeza mazao, na vitu vingine vya aina hii siyo maendeleo; ni vyombo vya maendeleo. Barabara mpya inampanulia mtu uhuru wake kama ataitumia kusafiri. Kuongeza idadi ya majengo ya shule ni maendeleo kama majengo hayo yanaweza kutumika, kuongeza ujuzi na elimu ya watu.

...Maendeleo yasiyokuwa maendeleo ya watu yanaweza yakawapendeza wataalamu wa historia wa mwaka 3000; lakini kwetu hayana maana kwani hayahusiani na maisha ya kesho tunayoyajenga.”

Mheshimiwa Spika, Serikali ya Chama cha Mapinduzi (CCM) imekuwa ikitaja kwa mbwembwe kilometa za barabara zilizojengwa kwa kiwango cha lami, wakati ambao wananchi wengi wanakumbana na adha ya usafiri kutokana na ubovu wa barabara hizo. Kwa mfano; wakulima kushindwa kusafirisha mazao yao kupeleka sokoni, kina mama kufariki njiani wakati wa kwenda kupata huduma za matibabu au kujifungua, kuongezeka kwa vifo vinavyosababishwa na ajali za barabarani n.k

Mheshimiwa Spika, barabara za lami zilizojengwa tangu tupate uhuru mwaka 1961 kwa kiwango cha lami ni wastani wa asilimia 16 tu ya barabara zote nchini zenye urefu wa zaidi ya kilometa 35,000.Kwa kasi hii italigharimu Taifa zaidi ya miaka 62 ijayo kukamilisha ujenzi wa kilometa 29,432 ambao ni sawa na asilimia 84 ya barabara zote zilizosalia kujengwa kwa kiwango cha lami nchini bila kujumulisha barabara mpya zinazosanifiwa mara kwa mara.

Mheshimiwa Spika, aliyekuwa Waziri wa Wizara ya Ujenzi ambaye kwa sasa ni Rais wa serikali ya awamu ya tano, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiwasilisha hotuba yake katika bunge la 10, kuhusu mapato na matumizi ya wizara ya ujenzi kwa mwaka wa fedha 2015/2016, alikiri hapa bungeni kuwa Serikali ya CCM katika awamu ya nne ilishindwa kutekeleza ilani zao kikamilifu za uchaguzi za mwaka 2005 mpaka mwaka 2015, kwa kujenga barabara nchini kwa kiwango cha lami zenye urefu wa kilometa 5,568 sawa na asilimia 31 kwa lengo walilojiwekea la kujenga barabara zenye urefu wa kilometa 17,762.

Mheshimiwa Spika, ninaomba kunukuu sehemu ya hotuba hiyo;

Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha serikali ya awamu ya nne, serikali imepata mafanikio makubwa katika kuboresha miundombinu ya barabara na madaraja nchini. Katika kipindi hicho, barabara zenye urefu wa jumla ya kilometa 17,762 zimekuwa katika hatua mbalimbali za utekelezaji ambapo barabara zenye urefu wa jumla ya kilometa 5,568 zimekamilika kujengwa kwa kiwango cha lami. Aidha, barabara zenye urefu wa jumla ya kilometa 3,873 zimeendelea kujengwa kwa kiwango cha lami. Katika kipindi hicho, barabara zenye urefu wa jumla ya kilometa 4,965 zimefanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina na serikali inatafuta fedha za kuzijenga kwa kiwango cha lami. Vilevile, upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara zenye jumla ya kilometa 3,356 unaendelea”

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka serikali hii ya awamu ya tano, kutoa maelezo ya kina mbele ya bunge hili ina mipango gani ya uhakika na endelevu ya kukamilisha ujenzi wa barabara hizo kwa viwango vinavyokubalika kimataifa na kwa kuzingatia vipaumbele kwa misingi ya kitaalamu, badala ya ahadi nyingi zisizotekelezeka.

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa bajeti ya wizara kwa mwaka 2016/17, Sekta ya Ujenzi fungu 98 imetengewa jumla ya shilingi 2,176,204,557,000/- kwa ajili ya miradi ya maendeleo ambayo ni ya kimkakati na isiyo ya kimkakati. Na kati ya fedha hizo shilingi 1,831,365,922,000/- ni fedha za ndani na zilizobaki ni kutoka nje.

Mheshimiwa Spika, naomba kunukuu sehemu ya hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kwa mwaka 2015/16;

Mheshimiwa Spika, kwa upande mwingine Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inamtaka Waziri kuacha mbwembwe nyingi bali aeleze kuwa madeni hayo ya Billioni zaidi ya 800 yanatoka kwenye barabara zipi? Yatalipwaje? Na riba ni kiasi gani?


Mheshimiwa Spika, hata kwa mwaka huu wa fedha, bajeti ya maendeleo ni 890,572,000.00 kwa Wizara na taasisi zilizo chini ya Wizara huku madeni yakiwa zaidi ya Bilioni 800. Hivyo hakuna uhalisia kati ya fedha za maendeleo zinazoombwa na madeni husika”.


Mheshimiwa Spika, bajeti hii ya ujenzi fungu 98 ni sawa na asilimia 18.41 ya bajeti nzima ya maendeleo, hivyo basi Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inamtaka Waziri atoe mchanganuo hapa bungeni kati ya fedha hizo ni kiasi gani kimetengwa kwa ajili ya kulipia madeni ya wakandarasi, kiasi gani ni kwa ajili ya kuanzisha miradi mipya na ni kiasi gani ni kwa ajili ya ukarabati wa barabara na madaraja?

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imeomba kupewa takwimu hizo, kwani taarifa ya utekelezaji inaonesha kuwa miradi ya kimkakati inahusu ujenzi na ukarabati wa barabara, madaraja na vivuko. Hii itasaidia bunge hili kutekeleza wajibu wake kikatiba wa kuisimamia serikali kwa niaba ya wananchi ambao ndiyo walipa kodi.

2.1 HASARA YA SHILINGI BILIONI 5.6 ILIYOSABABISHWA NA TANROADS

Mheshimiwa Spika, TANROADS imebainika kuwa na utendaji mbovu kama ambavyo Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) alivyobaini juu ya usimamizi mbovu katika mikataba ya ujenzi wa barabara na madaraja ambapo ilikuwa chini ya iliyokuwa wizara ya Ujenzi katika Serikali ya awamu ya nne.

Mheshimiwa Spika, TANROADS wakati wa kipindi hicho, iliitia hasara Serikali ya jumla ya Shilingi 5,616,652,051 kutoka kwenye riba (interest) inayoongezeka kila siku kutokana na TANROADS kuchelewa kuwalipa wakandarasi 11 kati ya kipindi cha mwaka 2012 na mwaka 2015 kwa mujibu wa Ripoti ya CAG ya Hesabu za Serikali kuu akikagua taarifa za fedha kwa mwaka ulioishia tarehe 30 Juni 2015 iliyotolewa mwezi Machi 2016 (Ukurasa wa 134 na 135).

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inajiuliza kama serikali ya awamu ya tano inafanya kazi yake kwa haki, uadilifu, uwazi na usawa kwa wote, na hasa kwa kile kinachojulikana kama utumbuaji majipu, swali hapa ni nani amfunge paka kengele? au mkuki mtamu kwa nguruwe mchungu kwa binadamu?

2.2 UBORESHAJI NA UTUNZAJI WA BARABARA NCHINI

‘Super Single Tyre’

Mheshimiwa Spika, utafiti unaonesha matairi haya (super single tyres) yanaharibu barabara. Matairi haya yameanza kutumika takribani miaka mitano iliyopita na mzigo uliokuwa unabebwa na matairi 24 sasa unabebwa na matairi 12. Matokeo yake ni uharibifu mkubwa wa barabara. Uamuzi wa kuruhusu matairi haya haukuwa na busara maana barabara zetu hazijabuniwa kuhimili shinikizo la uzito (excessive pressure) linalotokana na matairi haya. Serikali izuie mara moja matumizi ya matairi haya ili kuzinusuru barabara zetu lakini pia kuokoa fedha za walipa kodi zinazotumika kurekebisha mara kwa mara barabara hizo na kunyima fursa maeneo mengine kupata barabara za kiwango cha lami.

2.3. WAKALA WA MAJENGO TANZANIA

Mheshimiwa Spika, Wakala wa Majengo ulianzishwa mwezi Mei mwaka 2002 chini ya Sheria Na. 30 ya mwaka 1997 ya Wakala za Serikali. Lengo la kuanzisha Wakala wa majengo ni kuwezesha kuwa na nyumba bora zaidi za kuishi watumishi wa Serikali wakiwa kazini na baada ya kustaafu kwa kujenga nyumba na kuwakopesha; kujenga majengo ya Serikali kwa kuzingatia viwango vilivyowekwa na kuyatunza; na pia kutoa huduma za ushauri wa kitalaam kuhusiana na majengo.

2.3.1 NYUMBA ZA SERIKALI ZILIZOUZWA

Mheshimiwa Spika, wakala huyu wa majengo ndiye mhusika mkuu katika kuhakikisha nyumba za Serikali zinakuwa katika hali nzuri kwa watumishi wa serikali kuishi. Katika muktadha huo kambi Rasmi ya Upinzani inalikumbusha Bunge kwamba, kati ya mwaka 2002 mpaka 2004 Serikali iliuza nyumba zipatazo 7,921 na mpaka mwaka 2008 Serikali ilikuwa imejenga nyumba 650 tu.

Mheshimiwa Spika, katika biashara hiyo kwa kuuza zilizokuwa mali ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), ilipata Sh. 252,603,000/- sasa inahitaji kusaka nyumba zaidi ya mara dufu ya kiasi hicho kujenga nyumba za fidia. Kwa mujibu wa taarifa ya utekelezaji wa maazimio ya Bunge juu ya uuzaji wa nyumba za serikali kinyume cha taratibu, serikali itatumia Sh. 677,606,000/- kujenga nyumba mpya ili zirejeshwe kwa Tamisemi, Rejea taarifa ya Serikali Bungeni tarehe 25 April 2008.

Mheshimiwa Spika, Kwa vile hata wale waliouziwa nyumba hizo, kuna taarifa kati yao wapo walioziuza na kujipatia faida kubwa kinyume na mikataba ya mauzo hayo, KRUB inapendekeza wanyang’anywe nyumba hizo kwa kukiuka mikataba na malengo ya mauzo.


Mheshimiwa Spika, Kumbukumbu za taarifa rasmi za Bunge zinaonesha kwamba Serikali ilitoa taarifa ndani ya Bunge hili kuwa, kuna Kamati iliundwa kuchunguza mchakato wa mauzo ya Nyumba ya Serikali na Kamati hiyo ilitegemewa kumaliza kazi mwezi Februari, 2007, lakini hadi Bunge la tisa na Bunge la Kumi linamaliza uhai wake hakuna taarifa iliyotolewa na Serikali. KRUB, inaitaka serikali ya awamu ya tano irejeshe nyumba hizo.


Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Hansard ya Tarehe 25 Aprili, 2008 MKUTANO WA KUMI NA MOJA Kikao cha Kumi na Nne Bunge kwa kauli moja baada ya mjadala mkubwa wa hoja binafsi iliyowasilishwa na aliyekuwa Mbunge wa Vunjo Mhe. ALOYCE BENT KIMARO iliyohusu Serikali Kurejesha nyumba zake zilizouzwa kienyeji na hivyo kuisababishia Serikali hasara kubwa na Hoja hiyo ikaungwa mkono na Bunge likapitisha azimio, naomba kunukuu azimio hilo;

KWA HIYO BASI, Bunge linaazimia kwamba Serikali ifanye yafuatayo:

Itekeleze mara moja bila kusita, Agizo la Rais kurejesha nyumba zilizouzwa kinyume cha utaratibu na kwa watu ambao hawakuwa Watumishi wa Serikali wakati huo na vilevile nyumba ambazo hazikupaswa kuuzwa kama zile zilizopo kwenye maeneo ya Utawala wa Serikali; Irejeshe kwenye umiliki wake nyumba hizo zilizouzwa kinyume na utaratibu;

Itoe orodha ya nyumba zake ambazo ziliuzwa kwa watu ambao sio Watumishi wa Serikali kinyume na utaratibu na pia zile ambazo hazikupaswa kuuzwa kutokana na unyeti wa kazi za Watumishi wa Serikali wanaostahili kutumia; na ichukue hatua kwa wale ambao hawajalipia na mikataba yao ya kuuziwa nyumba irejewe hakikisha kuwa malipo hayo yanalipwa mara moja ama mikataba yao kufutwa na nyumba kurejeshwa kwenye miliki ya Serikali”.


Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kutekeleza azimio hilo la Bunge, na kwa njia hiyo ile kauli mbiu ya hapa kazi tu, iweze kutafsiriwa kwa vitendo. Tunajua uuzwaji huo ulisimamiwa na Wizara aliyokuwa akiiongoza yeye na kuna uwezekano mkubwa kwamba alisimamia maamuzi ambayo hakuwa na uwezo wa kuyakiuka. Sasa ni muda sahihi Mhe Rais Magufuli kurekebisha kasoro alizozisimamia na katika mchakato huo ili kurejesha imani katika jamii. Tukumbuke kuwa Rais Kikwete alielekeza nyumba hizo zirudishwe Serikalini lakini alikosa uthubutu wa kusimamia kauli yake.


3.0 SEKTA YA UCHUKUZI

3.1 UPANUZI WA UWANJA WA NDEGE WA JULIUS NYERERE (TERMINAL THREE)

Mheshimiwa Spika, itakumbukwa kuwa Bunge lako tukufu lilipitisha bajeti ya upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere. Upanuzi huo wa kituo cha tatu (Terminal three) unahusishwa na harufu kubwa ya ufisadi.

Mheshimiwa Spika, kuna tuhuma kwamba mtu ambaye alikuwa ni dalali katika mchakato mzima wa Tanzania kupatiwa mkopo wa ujenzi wa uwanja huo, ulighubikwa na mazingira tatanishi, ambapo dalali alifanikiwa kupata asilimia 30 ya mkopo huo kama Kamisheni yake inayofikia takribani dola za Kimarekani milioni 100 zaidi ya shilingi bilioni 200 za Tanzania , hivyo basi, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kuliangalia suala hili kwa undani na kuleta taarifa hapa Bungeni, au kwenye kamati husika ya Bunge.


3.2. UFISADI KATIKA VIVUKO NA MADARAJA NCHINI

3.2.1.Ununuzi wa Kivuko Kibovu cha Dar es Salaam -Bagamoyo

Mheshimiwa Spika, Kivuko kutoka Dar es Salaam kwenda Bagamoyo ni jipu ambalo limeiva kwa viwango vyote na sasa linatakiwa litumbuliwe mara moja. Ni dhahiri kuwa Kivuko cha Dar es Salaam kwenda Bagamoyo kilichonunuliwa na TEMESA chini ya uongozi wa waziri wa Ujenzi wa serikali ya awamu ya nne ambaye ndiye Rais wa Tanzania wa sasa.

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) katika Hesabu za Serikali kuu akikagua Taarifa za fedha kwa mwaka ulioishia tarehe 30 Juni 2015 iliyotolewa mwezi Machi 2016 (Ukurasa wa 132 na 133), alibaini ununuzi wa boti feki na mbovu uliofanywa na TEMESA na kugharimu Dola za Marekani 4,980,000 sawa na shilingi 7,916,955,000 kupitia mkataba namba AE/006/2012-13/HQ/G/CN-39 uliosainiwa tarehe 25 April 2013 kati ya TEMESA kwa niaba ya Serikali na Mzabuni M/s Johs.Gram-Hanssen Bergensgade.

Mheshimiwa Spika, CAG alibaini masuala makuu mawili kuhusu ununuzi huo wa kivuko feki na kibovu cha Dar es Salaam – Bagamoyo. Jambo la kwanza CAG alibaini kasi ya kivuko hicho ni tofauti na kasi iliyotakiwa kuwepo, jambo la pili ni kuwa cheti cha kukikubali kivuko hicho kilikuwa hakijatolewa kinyume na Kanuni ya 247 ya Manunuzi ya Umma. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inahoji, tabibu wa kutumbua jipu hili yuko wapi? Au msemo usemao kuwa “mganga hajigangi” unatumika hapa?

3.3 HALI YA RELI NCHINI

3.3.1. Kuimarisha Reli ya Kati na matawi yake

Mheshimiwa Spika, reli ya kati ya Tanzania ikiboreshwa, ina nafasi ya pekee ya kutawala soko la usafirishaji wa abiria na mizigo ya ndani na kwa nchi jirani kama Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo - DRC, Burundi ,Rwanda na Uganda na kuongeza pia mapato ya Bandari ya Dar es Salaam na Tanga .

Mheshimiwa Spika, tunahitaji mtazamo mpya wa kisasa na wa upeo wa miaka 50 ijayo. Tunahitaji reli ambayo itaendana na mazingira tuliyonayo ya ukubwa wa nchi na fursa tuliyonayo ya nchi zilizotuzunguka zinazotegemea bandari zetu. Swala kubwa la kuzingatia ni mwendo kasi na uwezo wa kubeba uzito mkubwa. Na ndio maana hoja ya kwanini Tanzania inahitaji reli ya kisasa ‘standard gauge’ sasa na siyo baadaye.

Mheshimiwa Spika, kuna mtazamo kuwa na reli ya kisasa tunahitaji chuma cha reli chenye uzito wa pound 90 hadi 100 au zaidi kwa matarajio ya miaka 50 ijayo. Tukumbuke kwamba uwekezaji wa reli ni uwekezaji mkubwa na hivyo unatakiwa ulenge muda mrefu.

Mheshimiwa Spika, tunashauri reli ijengwe kwa mtazamo wa mbali wa zaidi ya miaka 50 ijayo, tuanze na reli moja sambamba na hii iliyopo, lakini mpango uwe kuwa na zaidi ya reli moja hapo baadaye ili kuwezesha usafirishaji katikati ya Tanzania na nchi jirani kuwa wa muda mfupi zaidi, ili kuzivuta nchi jirani kuona reli yetu ndiyo ya pekee ya kuwafikishia mizigo yao kwa muda mfupi na kwa usalama zaidi, ikiwepo sababu za kiutendaji.


Mheshimiwa Spika, Ujenzi wa ‘Standard Gauge’ uende sambamba na kuimarisha mawasiliano katika kuendesha shughuli za reli ili kuongeza ufanisi.


Mheshimiwa Spika, kuchelewa kwetu kujenga reli mpya sasa italigharimu taifa hili na vizazi vijavyo; Kwanza. itafanya tushindwe kufaidika na bandari zetu ipasavyo, hata tukija kuamua kujenga baadaye gharama zitakuwa kubwa mno kuliko hivi sasa, na si ajabu ikawa ngumu kupata wawekezaji, na hata kama tutafanikiwa bado tutakuwa na kazi ya kuwapata wateja ambao watakuwa wameshazoea kupitisha mizigo yao sehemu nyingine. Wakati wa kufanya uamuzi ni sasa na gharama ya kushindwa kufanya uamuzi sasa ni kubwa mno.

Mheshimiwa Spika, ili kufupisha muda wa ujenzi, kuwe na wakandarasi ambao watapewa vipande vidogo vya takribani kilomita 200 ambavyo vitajengwa kwa wakati mmoja ili kuwezesha reli hii ikamilike kwa haraka.


Mheshimiwa Spika, kuongezeka kwa thamani ya dola na kasi ya mabadiliko ya kiuchumi na kiteknolojia duniani kunasababisha pia gharama za ujenzi wa reli kupanda, kadri taifa linavyochelea kufanya maamuzi ya ujenzi wa reli ya kisasa basi hata gharama zitakuwa kubwa mno kuliko hivi sasa, na si ajabu ikawa ngumu kupata wawekezaji wenye unafuu, na hata kama tutafanikiwa bado tutakuwa na kazi kubwa ya kuweza kukabiliana na ushindani hasa kwa nchi jirani ambazo nazo zimeanza na nyingine zinakaribia kukamilisha ujenzi wa reli za kisasa. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inashauri tufanye maamuzi sasa kwa masilahi endelevu ya mama Tanzania.

3.3.2. Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA)

Mheshimiwa Spika, Reli ya Tazara iliyojengwa miaka ya 1970 ikitokea Dar es Salaam hadi New Kapirimposhi Zambia, uwezo wake wa kusafirisha mizigo na abiria umeshuka sana kutokana na sababu kama zile zile za Reli ya Kati.

Mheshimiwa Spika, Reli hiyo yenye uwezo wa kubeba tani milioni tano kwa mwaka, hivi sasa inaweza kubeba tani 100,000 tu kwa mwaka, sababu kubwa ni uchakavu wa miundombinu kama vile njia ya reli, injini na mabehewa.

Mheshimiwa Spika, ili TAZARA iweze kujiendesha kibiashara inatakiwa isafirishe zaidi ya tani 600,000 za mizigo kwa mwaka (break even point), hata hivyo Tazara kwa muda mrefu imekuwa ikisafirisha mizigo chini ya tani 100,000 za mizigo kwa mwaka kutokana na changamoto kadhaa;

i. Ucheleweshaji wa mizigo bandarini

ii. Miundombinu chakavu

iii. Muda mrefu wa usafirishaji wa mizigo.

Mheshimiwa Spika, ni dhahiri TAZARA haitaweza kujiendesha kwa faida kama mabadiliko makubwa ya kiutawala hayatafanyika. Ni aibu na fedheha kwa Serikali kulipa mishahara ya watumishi wa shirika ambalo lilikuwa na uwezo mkubwa. Tazara ina uongozi usiozingatia utawala bora, uwazi na uwajibikaji.

Mheshimiwa Spika, miaka michache iliyopita wafanyakazi wa Tazara waliibua tuhuma nzito dhidi ya Mameneja waandamizi saba (7) ndani ya Tazara. Aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi, Mhe. Omar Nundu aliwasimamisha kazi ili kupisha uchunguzi. Katika Mazingira yenye utata Mheshimiwa Harson Mwakyembe alipokabidhiwa wizara hiyo aliwarudisha kazini watendaji hao akidai kuwachukulia hatua za kisheria lakini hadi leo hatua hizo hazijawahi kuchukuliwa, watendaji wako kazini na shirika linaendelea kuporomoka. KRUB, inajiuliza ni kwa nini kunakuwa na hali ya kutunishiana misuli baina ya Mawaziri? Kwani jambo kama hilo pia lilitokea kwenye Bodi ya Mamlaka ya Bandari, Mhe Harrison Mwakyembe aliivunja bodi aliyoikuta na kuteua mpya, Mhe. Samuel Sitta alipoingia akaivunja hiyo bodi na kuteua mpya. Kuna nini hapa ambacho ni siri ya Mawaziri?

Mheshimiwa Spika, ikiwa Serikali ina nia ya dhati ya kupiga vita ubadhirifu inakuwaje watu waliotuhumiwa kwa kuchota kiasi kikubwa cha fedha wanalindwa na wale wanaotakiwa kuwachukulia hatua. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inamtaka Waziri aliangalie vizuri suala hili la uongozi wa Tazara.

3.4 HALI YA BANDARI NCHINI

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, inaamini kuwa ili kuongeza ufanisi wa bandari zetu ni lazima kuimarisha miundombinu ya reli na barabara zinazozunguka bandari ili kuondoa mizigo inayosongamana bandarini kwa haraka na ufanisi. Aidha, Mamlaka ya Bandari (TPA) na Mamlaka ya Mapato (TRA) zinatakiwa kuwekeza kikamilifu kwenye mifumo ya kieletroniki , ili kupunguza muda wa usafiirshaji wa mizigo na hasa ile ya nchi jirani (Transit goods) , ambao hivi sasa ni mkubwa kutokana na mizani na vituo vingi vya ukaguzi vilivyopo barabarani. Kupunguza muda wa usafirishaji, kutavutia watu wengi zaidi kutumia bandari za Tanzania.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inashauri kuwa na kituo kimoja cha ukusanyaji wa mapato (Single point tax collection) cheye ufanisi na utaalamu unaokubalika kimataifa ili kupunguza ucheleweshwaji na usumbufu wa kuondoa mizigo kutoka bandarini na kurahisisha ukusanyaji wa mapato kwa kufanya kazi kwa saa 24 kwa siku kwa mamlaka zote zinazohusika.



3.4.1 BANDARI KAVU YA SOGA

Mheshimiwa Spika, kuna mwekezaji aliyeshafanya mawasiliano na Serikali kutumia eneo la Soga kujenga bandari kavu. Eneo hilo lipo katikati ya Reli ya Tazara na Reli inayosimamiwa na Mamlaka ya reli (RAHCO) na hivyo ingekuwa rahisi kuchukua mizigo kutoka bandarini kupitia reli ya Tazara na Reli ya Kati. Hii ingefanya mizigo yote ya ndani na nje (transit goods) iwe inachukuliwa eneo hili la Soga na hivyo kuondoa msongamano wa malori ya mizigo jijini Dar es Salaam na bandarini. Aidha, Tazara na TRL zote zingenufaika na mpango huu, ikiwa ni pamoja na TRA kuweza kukusanya kodi zake kwa ufanisi (single point of tax collection) pamoja na kupunguza uzito kandamizi katika barabara za mijini.

Mheshimiwa Spika, pamoja na faida zote hizi, bado Serikali inaonekana kuwa na kigugumizi na kusitasita kana kwamba muda unatusubiri. Serikali ifanye maamuzi ya haraka kwa vitu ambavyo vina manufaa kwa nchi. Subiri subiri hii itakuja kuigharimu Serikali, kama ambavyo imekuwa kwa miradi mingi ambayo Serikali ilichukua muda kufanyia maamuzi.

3.4.2 BANDARI YA DAR ES SALAAM

Uwezo wa Bandari ya Dar es Salaam dhidi ya Bandari shindani kwa mfano Bandari ya Mombasa iliyoko nchin Kenya


Bandari ya Dar Es Salaam

Bandari ya Mombasa

Tani kwa Mwaka

Milioni 13

Milioni 22

Ujazo wa Kontena kwa Mwaka

600,000

800,000

Gati (Birth) zilizopo

11

19

Chanzo: www.tanzaniaports.com; Https://En.wikipedia.org/wiki/port of dar es salaam; www.kpa.co.ke


3.4.3 BANDARI YA TANGA

Mheshimiwa Spika, kupitia fursa ya bomba la mafuta la nchi ya Uganda kupitia bandari ya Tanga, ni wakati sasa Serikali iwekeze katika bandari hii na ifungue ukanda wa kiuchumi wa kaskazini. Bandari hii inaweza kutumika zaidi kwa ajili ya mizigo iendayo Uganda, Kenya, Kongo, Burundi, Rwanda na Sudan ya Kusini.

3.4.4 BANDARI YA MTWARA NA MTWARA CORRIDOR

Mheshimiwa Spika, Serikali iangalie upya ukanda huu wa kusini mwa Tanzania ikiwa ni pamoja na kutafuta wawekezaji kwa kuwa ukanda huu utafungua fursa nyingi sana za kiuchumi kwa wananchi wa maeneo hayo.



Bandari ya Mtwara kama Kituo Mbadala cha Kupakulia na Kupakia Mafuta.

Mheshimiwa Spika, shehena yamafuta yaliyosafishwa hadi hivi sasa yanafikia tani 3.6 milioni kwa mwaka. Ukizingatia kasi ya ukuaji wa uchumi wetu mahitaji ya mafuta yatazidi tani million 6 kwa mwaka kwa kipindi kisichozidi miaka 10 ijayo. Hii inaleta uhitaji mkubwa kwa bandari ya Mtwara kuwa kituo kingine kikuu cha kupokea mafuta yaliyosafishwa ili kuhudumia ukanda wa Kusini pamoja na nchi jirani kama Malawi , Zambia , Msumbiji na Kongo. Kuwa na kituo kikubwa cha kushusha na kuhifadhi mafuta, itasaidia pia kuwa rahisi kuhudumia nchi kama Shelisheli na Komoro pamoja na mikoa iliyopo pembezoni mwa bahari ya Hindi kama vile Tanga, Dar es Salaam, Pwani, Lindi, Mtwara na nchi ya Zanzibar.

Mheshimiwa Spika, hali ilivyo sasa kituo cha kupakulia na kujaza mafuta kwenye malori kilichopo Kurasini (Kurasini Oil Jet – KOJ), kinazidiwa siku hadi siku, kwahiyo ni wakati muafaka wa kuwa na kituo kingine. Hii ina maana kuwa kufunguliwa kwa kituo hiki kitasaidia mambo yafuatayo;

· Kutapunguza msongamano wa magari yanayokuja kuchukua mafuta bandari ya Dar es salaam, zaidi ya malori 5,000 hadi 6,000 kwa mwezi.

· Kutapunguza muda wa usafirishaji wa bidhaa hiyo, kwasababu hivi sasa inachukua takribani siku 4 kwa lori moja kuweza kujaziwa mafuta kutoka Kurasini - KOJ kwa sababu ya msongamano na foleni ya kupakia.

· Gharama za usafirishaji zitakuwa chini kwa sababu ya umbali ambao unakatwa kwa kuwa na kituo kikuu cha mafuta katika bandari ya Mtwara na hivyo kusababisha bidhaa hii kupatikana katika mikoa ya kusini kwa bei sawa na Dar es salaam, kwa wastani wa shilingi 400 chini ya kiwango wanachonunulia mafuta hivi sasa. Hii itasababisha mikoa ya kusini kuokoa takribani shilingi billioni 1.2 kwa mwezi.

· Hii itachochea pia nchi za jirani kuitumia zaidi bandari hii, katika kuagiza na kuhifadhi bidhaa hii kutokana na unafuu utakaokuwa unapatikana.

· Unafuu wa mafuta utanufaisha uwekezaji kwa mfano viwanda vya sementi unaofanywa kwenye ukanda huo. Bidhaa kama sementi inayozalishwa na kiwanda cha Dangote itakuwa bei nafuu , kama bidhaa za mafuta ya petroli zitachukuliwa moja kwa moja kutoka Mtwara badala ya Dar es Salaam.

· Itawanufaisha pia wawekezaji wanaofanya utafiti na uchimbaji wa gesi katika ukanda huo.

· Itapunguza msongamano wa malori ya mafuta ambao umezoeleka hivi sasa jijini Dar es Salaam na barabara kuu ya Mororogoro.

· Itachangia katika kuongeza fursa za ajira na kuchochea uchumi katika ukanda huu wa kusini.

· Itaokoa mamilioni ya shillingi ambayo Serikali inalazimika kupoteza kutokana na Meli kusubiri kwa muda mrefu kupakua mafuta kwenye SBM1 (Sub Marine Point 1).

· Kuimarisha usalama wa nchi (National Security) kwa Kuwa na kituo kikuu kikubwa cha pili cha kupakulia mafuta, ambacho kitasaidia kama kutakuwa na tatizo lolote lile kwenye kituo cha Dar es salaam ( KOJ au SBM1 ), nikiyaja tu faida zake kwa uchache.

4.0 SEKTA YA MAWASILIANO

4.1. KAMPUNI YA SIMU YA TAIFA-TTCL

Mheshimiwa Spika, pamoja na umuhimu na kukua kwa sekta ya mawasiliano nchini bado ni ajabu leo hii Kampuni ya Simu ya Taifa letu (TTCL) ni sawa na kichwa cha mwendawazimu. Katika maoni yetu mwaka jana, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, ilitoa hoja nyingi zilizohitaji majibu kuhusiana na utendaji na hujuma zinazofanywa ili kuikwamisha Kampuni ya Simu ya Taifa kuendelea kutekeleza majukumu yake na kukabiliana na soko la ushindani katika utoaji wa huduma za mawasiliano nchini na barani Afrika.

Mheshimiwa Spika, katika hotuba ya msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani kwa mwaka 2015/16 sehemu ya hotuba alitoa maoni yafuatayo;

Mheshimiwa Spika, Kampuni ya Simu Tanzania TTCL ilianzishwa kwa mujibu wa sheria Na.20/1993 na kusajiliwa kwa Hati Na. 24490 kuwa ni Kampuni ya Umma (Parastatal Organization) mpaka leo.

Mheshimiwa Spika,tarehe 23/2/2001, Serikali ilikodisha hisa za Kampuni ya Simu Tanzania TTCL kwa Kampuni ya Mobile System International (MSI) ya Netherlands. Hisa zilizokodishwa ni 35% kwa kulipiwa shilingi bilioni 111 sawa na Dolar za Marekani Milioni Sitini ($ 60milion) kwa wakati huu, malipo hayo ni sawa na hisa 17.5%; lakini serikali ikawapa MSI kuongoza Kampuni. Vile vile MSI hawakulipa pesa yote kwa mujibu wa Mkataba, lakini walipewa umiliki wa ukodishaji wa hisa 35% za hisa za TTCL.

Mheshimiwa Spika, hoja ya Msingi ambayo Kambi Rasmi ya Upinzani inataka Waziri alieleze Bunge na Watanzania wote ni kwa vipi HISA zinaweza kukodishwa? Hili la Tanzania kukodisha hisa kwa anayeitwa mwekezaji ni maajabu katika tasnia nzima ya uchumi na uhasibu”.

Mheshimiwa Spika, mnamo tarehe 26.05.2015 wakati wa kuhitimisha hoja yake aliyekuwa Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, wakati wa Bunge kukaa kama kamati ya matumizi alishindwa kujibu hoja ya Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani-Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia kuhusu Serikali kununua hisa zake asilimia 35 kwa thamani ya shilingi bilioni 14.9.

Mheshimiwa Spika, Bunge kwa kusikiliza na kutathmini hoja zilizotolewa, aliyekua Spika wa Bunge la 10 Mheshimiwa Anne Makinda (Mb) aliunda kamati ndogo ya Bunge ikiongozwa na Mheshimiwa Zarina Madabida kufanya kazi ya kiuchunguzi kuhusiana na hujuma zinazofanyika kwenye Kampuni hiyo ya simu. Taarifa hiii inapatikana kwenye HANSARD ya tarehe tajwa hapo juu. Kambi Rasmi ya Upinzani inataka kujua iwapo taarifa ya Kamati hiyo ndogo ya iliyokuwa kamati ya Miundombinu iliwasilishwa kwa Mheshimiwa Spika? Ikiwa taarifa hiyo haikuwasilishwa mpaka Bunge la 10 linafikia ukomo wake basi ipo haja sasa ya Bunge hili kuchunguza kwa umakini matatizo ya mikataba iliyoingiwa na Serikali kwa niaba ya TTCL na makampuni binafsi juu ya utoaji wa huduma.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inalitaka Bunge hili kuunda kamati maalum sambamba na kuangalia utendaji na mikataba ya TTCL na makampuni mengine ya simu pamoja na ushiriki wa TTCL kwenye mkongo wa Taifa, umiliki wa mkongo huo na mkataba wa TTCL na kampuni ya SEACOM katika uendeshaji au utoaji wa huduma kwa wateja.

4.2 MFUKO WA MAWASILIANO KWA WOTE-UCSAF

Mheshimiwa Spika, Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote ulianzishwa na Serikali kwa Sheria Na. 11 ya mwaka 2006 ambayo ilipewa jukumu kuu la kupeleka mawasiliano vijijini.

Malengo ya Mfuko kama yalivyoainishwa na sheria ni kama ifuatavyo:-

1. Kuhakikisha upatikanaji wa huduma ya mawasiliano katika maeneo ya vijijini na maeneo ya mijini yenye mawasiliano hafifu;

2. Kuhamasisha ushiriki wa sekta binafsi na serikali katika utoaji wa huduma za mawasiliano kwa wote katika maeneo ya vijijini na maeneo ya mijini yenye mawasiliano hafifu;

3. Kuhamasisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika maeneo ya vijijini na maeneo ya mijini yenye mawasiliano hafifu;

4. Kutengeneza mfumo kwa ajili ya upatikanaji wa mitandao ya mawasiliano na huduma rahisi na zenye ufanisi katika uzalishaji na upatikanaji katika soko la kiushindani;

5. Kuhamasisha utoaji wa huduma bora katika viwango nafuu na kuhakikisha kuwa teknolojia ya habari na mawasilianpo inapatikana vijijini na sehemu za mijini zenye mawasiliano hafifu kwa bei nafuu; na

6. Kuhakikisha upatikanaji wa huduma za wote kwa kuboresha upatikanaji wa huduma za mawasiliano kupitia ushiriki wa sekta binafsi.

Mheshimiwa Spika, changamoto za utoaji wa huduma za mawasiliano vijijini ni pamoja na ukosefu wa umeme wenye uhakika katika maeneo ya vijijini. Hivyo basi wakala huyu anashirikiana vipi na wakala wa Umeme vijijini (REA) katika kuhakikisha kuwa umeme wa uhakika unapatikana kwa wakati na hivyo lengo lake la uwepo wa mawasiliano rahisi na ya uhakika linafikiwa?

Mheshimiwa Spika, kinyume cha hapo ni dhahiri kwamba fedha za Mfuko wa Mawasiliano (UCSAF) zitazinufaisha zaidi kampuni za simu binafsi wakati lengo lake la msingi litashindwa kufikiwa.

Mheshimiwa Spika, niukweli kwamba makampuni ya simu yanayofanya shughuli zake hapa nchini ndio wachangiaji wakubwa wa mfuko kwa mujibu wa sheria iliyoanzisha mfuko huo, hivyo basi kitendo cha kutokuchangia au Mfuko kushindwa kukusanya michango hiyo ni kosa kisheria. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka kujua ni kwani Mfuko umeshindwa kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 3.5 toka kwa makampuni ya simu?

4.3. HALI YA HUDUMA ZA MAWASILIANO YA SIMU NCHINI

Mheshimiwa Spika, inakadiriwa kuwa mawasiliano ya huduma ya simu yamezalisha takribani shilingi trillion 2 kwa mwaka 2015 peke yake. Kwa kiasi kikubwa mawasiliano ya simu yamekuwa yanaendeshwa na makampuni binafsi nchini.

Pamoja na sekta hii ya mawasiliano hasa ya simu kuchangia kwa mapato makubwa, juhudi za serikali kuhakikisha mawasiliano ya simu za mikononi yanapatikana mpaka vijijini zimekuwa ndogo sana. Aidha, makampuni binafsi na serikali zimeshindwa kuwekeza kwenye minara na hivyo kusababisha mawasiliano kuwa ya shida au hamna kabisa katika baadhi ya maeneo nchini hasa vijijini.

Mheshimiwa Spika, mawasiliano ya simu za mkononi yanahitaji uwekezaji mkubwa katika minara . Tanzania yenye eneo la mraba la kilometa za mraba 945,087 ni kubwa kwa makampuni binafsi pekee kuweza kuweka minara. Ni dhahiri kuwa kampuni hizi hujenga minara katika maeneo ambayo yana faida kwao kibiashara na kuacha maeneo mengine yasiyo ya kifaida kwao bila ya minara ya mawasiliano.

Mheshimiwa Spika, pato la kawaida la mtumiaji yaani ‘average revenue per user’ [ARPU] limepungua kutoka dola 10 miaka 15 iliyopita hadi kufikia dola 2, hii pia imechangiwa na kodi kubwa zinazotozwa na Serikali na kuzipunguzia kampuni za mawasiliano kuwekeza zaidi. Ikumbukwe kuwa Tanzania ni nchi ya pili baada ya nchi ya Gabon kutoza kodi nyingi kwa makampuni ya mawasiliano ya simu za mkononi.

Mheshimiwa Spika, athari hizi zimesababisha baadhii ya kampuni za simu kuachana kabisa na kuwekeza na kuendeleza minara ya mawasiliano. Wameuza minara kwa kampuni nyingine binafsi na wao kuzikodi kutoka kampuni hizo, kwa lengo la kupunguza matumizi. Na kwa kuwa kampuni hizi zinazouziwa minara zipo zaidi kibiashara, itakuwa vigumu kuwekeza kwenye sehemu kama vijijini ambazo hakuna masilahi makubwa ya kibiashara.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaamini kuwa iwapo TTCL itanunua, kuwekeza na kuendesha minara ya mawasiliano na kuikukodisha kwa kampuni za simu kama Tigo, Vodacom, Airtel, Zantel, Smile nk., badala ya kuacha kampuni nyingine za binafsi kufanya shughuli hiyo TTCL itaongeza tija na kuweza kujiendesha bila hasara.

Aidha, iwapo Serikali itawekeza vya kutosha katika minara ya mawasiliano, itarahisisha mipango ya kuanzisha na kusambaza mawasiliano hata katika maeneo ambayo yanaonekana kwa sasa, hayana mvuto wa kibiashara. Kwa kufanya biashara hii ya minara kutakuwa hamna tofauti na kama TTCL inavyofanya sasa, kununua njia za mawasiliano ya ‘internet’ na kuziuza kwa makampuni ya ndani, au kama ambavyo walivyojenga mkongo wa mawasiliano (fibre optic), karibia kila wilaya ya nchi hii na kukodisha mkongo huo kwa makampuni mengine ya simu.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, Serikali ya Rwanda imejenga minara maeneo ya vijijiini na kuikodisha hiyo minara kwa kampuni za simu. Uwekezaji huu ni wa faida kubwa kwa nchi, kwa sababu itasaidia kuwa kichocheo kwa kampuni za simu kueneza wigo wao kufikia kila mwananchi na kuongeza ushindani wa kuboresha ubora wa mawasiliano. Tanzania ina kila nafasi na uwezo wa kuweza kuboresha sekta ya mawasiliano ya simu na kuyasambaza kwa wananchi wake kwa gharama nafuu zaidi.

4.4. SHERIA YA MAKOSA YA MTANDAO NAMBA 14 YA MWAKA 2015

Mheshimiwa Spika, Ikumbukwe kwamba wakati Bunge la Jamhuri ya Muungano linapitisha sheria hiyo tarehe 1.4.2015, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ilipinga kupitishwa kwa sheria hiyo kwani kulikuwa na vifungu ambavyo vilikuwa vinaminya uhuru wa utoaji na upokeaji wa taarifa kwa njia ya mtandao na baadhi ya wabunge wake waliwasilisha majedwali ya marekebisho kwa ajili ya kufuta au kurekebisha vifungu kandamizi, lakini kwa wingi wa wabunge wa CCM walipinga marekebisho hayo. Hansard ya terehe tajwa inaonesha.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni bado inaendelea kuamini kuwa sheria hiyo ya makosa ya kimtandao kama hakiufutwa basi inatakiwa kufanyiwa marekebisho makubwa ili iweze kukidhi malengo yake badala ya kuwa kikwazo kwa utoaji na upataji wa habari kwa njia za kimtandao.

Mheshimiwa Spika, zipo kila dalili zinazoonesha kuwa Sheria hiyo kandamizi ilitungwa kwa mashinikizo ya Chama tawala kuelekea uchaguzi mkuu wa 2015 kutokana na kasi ya vijana ambao wengi ndio watumiaji wa mitandao ya kijamii nchini ambao wengi walikuwa wakiunga mkono upinzani. Mara baada ya kumalizika uchaguzi mkuu, ushahidi unaonesha kuwa Sheria hii mbaya ilitungwa kwa makusudi ya kuwabana watanzania ambao wapo tayari kukosoa utendaji mbovu wa awamu ya tano na kuleta utawala wa kiimla na kidikteta katika taifa hili changa ambalo mpaka sasa halijafanikiwa kuwa taifa la uchumi wa kati.

Mheshimiwa Spika, kitendo cha MCC kuiondoa Tanzania kama mnufaika wa misaada yake kinatokana na tamko la uamuzi wa Bodi ya Wakurugenzi ya MCC iliyotolewa tarehe 28 Machi 2016 kuwa mojawapo ya sababu za Tanzania kuondolewa katika MCC ni uwepo wa Sheria ya Makosa ya Mitanado ambayo imetumika kama mojawapo ya njia za kuminya uhuru wa mawazo, ikiwemo kukamatwa kwa baadhi ya watu kwa makosa yanayohusiana na mitandao kipindi cha uchaguzi. Zaidi, tamko hilo lilieleza kuwa mazingaombwe na marudio ya uchaguzi wa Zanzibar tarehe 20 Machi 2016 na Sheria kandamizi ya Makosa ya Mitandao vinakinzana na azma ya uwepo wa demokrasia na uchaguzi huru na wa haki. Hivyo MCC ikatangaza kuvunja utekelezaji wa mpango wa pili wa maendeleo wa MCC kwa kushirikiana na Tanzania. Mojawapo wa sekta zilizokua zikipokea fedha za MCC ni sekta ya ujenzi wa miundombinu. Baadhi ya miradi iliyokuwa inafadhiliwa na MCC kwa Sekta ya Ujenzi nchini Tanzania ni pamoja na;

- Mradi wa Barabara, Kilometa 67 kutoka Songea – Namtumbo

- Mtwara Corridor

- Tanga – Horohoro

- Tunduma

- Mafia Island aiport

5. HITIMISHO

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo naomba kuhitimisha kwa kusema kuwa kinachofanywa sasa na serikali ya awamu ya ya tano ya kukimbizana barabarani na kwenye vyombo vya habari na mfumo wa kifisadi (kutumbua majipu), ni matokeo ya kulea mifumo mibovu miaka mingi iliyopita bila kuzingatia ushauri ambao tumekuwa tukiutoa katika Bunge hili. Ni vema Serikali ya awamu ya tano ikaanza kuweka mifumo endelevu inayojali na kukuza utu wa mama Tanzania. Dhambi ya kutumikia mfumo ni mauti kwa taifa letu.

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, naomba kuwasilisha.


James Francis Mbatia (Mb),

Waziri Kivuli wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano,

17 Mei 2016
 
Back
Top Bottom