HOTUBA ya leo Upinzani; PROF. Kahigi abainisha wazi udhaifu mkubwa Ikulu

Tumaini Makene

JF-Expert Member
Jan 6, 2012
2,642
6,071
HOTUBA YA MHESHIMIWA PROF. KULIKOYELA K.KAHIGI (MB), MSEMAJI MKUU WA KAMBI YA UPINZANI OFISI YA RAIS, KUHUSU MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA MWAKA 2011/2012 NA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA OFISI YA RAIS KWA MWAKA WA FEDHA 2012/2013 1. UTANGULIZI Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kutoa maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani kuhusu mapitio ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2011/2012 na mapendekezo ya mapato na matumizi Ofisi ya Rais kwa mwaka wa fedha 2012/2013, kwa mujibu wa Kanuni za Kudumu za Bunge, toleo la mwaka 2007, kanuni ya 99(7). Mheshimiwa Spika, kwa heshima kubwa natoa shukrani kwa Kiongozi wa Upinzani Bungeni kwa imani kubwa aliyo nayo kwangu, na hivyo kunikabidhi majukumu ya kuwa Msemaji Mkuu wa Kambi wa Ofisi ya Rais katika mapana yake. Nami natoa ahadi kwake kuwa nitajitahidi kwa kadri itakavyowezekana kutimiza majukumu yangu ndani na nje ya Bunge. Mheshimiwa Spika, mwisho lakini kwa umuhimu mkubwa, nawashukuru wafuatao: familia yangu yote, wana-CHADEMA pamoja na wale wasio Wana-Chadema katika Jimbo langu la Bukombe. Nawaomba wana-Bukombe wote tuendelee kushirikiana na kushikamana katika azma yetu ya kuleta mabadiliko katika maisha yetu. 1. OFISI YA RAIS, IKULU Mheshimiwa Spika, Ofisi hii ndiyo yenye dhamana ya kuangalia usalama wa nchi, na hivyo idara ya Usalama wa Taifa ipo chini ya Ofisi hii. Kambi ya Upinzani katika hotuba zake za nyuma tumekuwa tukiitaka Idara hii ya usalama kuzingatia jukumu lake la msingi la kuhakikisha maslahi ya nchi yanalindwa, badala ya kulinda maslahi ya viongozi kama ilivyo sasa. Mheshimiwa Spika, nchi yetu imeingia katika kashfa mbalimbali zinazohusu rasilimali za nchi hii kuporwa au viongozi waandamizi katika serikali kujiingiza na kushiriki katika mipango ya kuwaibia walipa kodi, lakini usalama wa Taifa hatujawahi kusikia popote kuwa wamehusika katika kuzuia mchakato huo japokuwa wanakuwa na taarifa za kutosha. Jambo hili linapelekea wananchi kukosa imani na idara hii na pengine kufikia hata kusema kuwa idara hii ndio mshiriki mkuu katika kufisidi raslimali za nchi hii. Mheshimiwa Spika, sasa hivi nchi yetu kiusalama si salama kama ambavyo Serikali inataka kuwaaminisha wananchi. Kitendo cha Wahabeshi kuingia tokea huko walikotoka hadi kuja kuonekana wamefia katikati ya nchi ni ushahidi wa moja kwa moja kuwa usalama wa nchi uko mashakani. Hivi usalama wa taifa na vikosi vyote vya ulinzi na usalama vilikuwa wapi hadi Wahabeshi wakavuka mpaka na kuendelea na safari hadi Kongwa? Aidha, kitendo cha kutekwa na kuteswa kwa Kiongozi wa Chama cha Madaktari nchini, Dr. Steven Ulimboka na vyombo vya usalama vipo ni dhahiri kuwa hali ya usalama ni ya mashaka. Hali ya usalama ni tete pia katika mipaka ya mikoa ya Kigoma na Kagera hususani kuhusiana na wahamiaji haramu. Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inasema hayo kwa kuwa Rais ndiye Amiri Jeshi Mkuu wa vyombo vyote vya usalama hapa nchini lakini kwa matukio hayo Ofisi ya Rais haijatoa kauli ya kina Bungeni ni kwa vipi watu wanaingia toka nje na wanasafiri hadi katikati ya nchi bila kujulikana. Au kuna mtandao wa vyombo vya usalama unaojihusisha na biashara hiyo ya kusafirisha watu, jambo ambalo ni hatari kwa usalama wa nchi yetu? Huu ni udhaifu mkubwa kwa idara ya usalama wa Taifa. Je, ni kutokana na watendaji kupata kazi bila ya kuzingatia vigezo vya weledi katika kazi husika, au kutokujua umuhimu na maana halisi ya idara hiyo kwa taifa letu? Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali kuiunda upya idara hii ya usalama wa taifa ili iendane na dhana husika ya kulinda maslahi ya nchi na wananchi wake. Ni muhimu kuwa watumishi waajiriwe kwa vigezo vya weledi. Madaraka ya Rais, Mfumo wa Uongozi wa Nchi na Mchakato wa Katiba Mpya Mheshimiwa Spika, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzaniaimetoa mamlaka makubwa sana kwa Rais, kuwa yeye ndiye mamlaka ya uteuzi na kufukuza kwa nafasi za juu katika sekta nzima ya utumishi wa umma. Wahusika katika nafasi hizo za uteuzi kwa kiasi kikubwa wamekuwa wakizitumia kwa kuifurahisha zaidimamlaka ya uteuzi badala ya kuitumikia jamii. Nafasi hizo ni pamoja na: Makatibu wakuu, wakurugenzi wa Halmashauri, wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya, watendaji wakuu wa taasisi mbalimbali, Mkuu wa Majeshi, Mkuu wa Jeshi la Polisi, mabalozi, wenyeviti wa bodi mbalimbali za taasisi za umma, n.k. Hivyo basi, Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inatoa rai kwa Watanzania kuwa jambo hili liwe ni hoja katika mchakato wa utoaji wa maoni ili katiba mpya iweke mfumo mpya wa uteuzi ambao utasimamia ufanisi wa utendaji wa viongozi na watendaji wa kuteuliwa. Mheshimiwa Spika, katika hotuba ya Kambi ya Upinzani kwa mwaka wa fedha 2011/12 tulihoji uhalali wa taasisi zinazoanzishwa na wake/waume wa Marais kuwa zao binafsi na sio za Serikali; hivyo, utumishi wa umma kwa ma-Rais unapokoma, wao wanahama na taasisi hizo, jambo ambalo hupelekea mke/mume wa Rais ajaye kuanzisha upya taasisi nyingine badala ya kuendeleza kazi za ile iliyokuwepo. Nanukuu sehemu ya hotuba hiyo: “Mheshimiwa Spika, kumeibuka mtindo wa wake za marais kuanzisha taasisi zao binafsi zisizo za kiserikali; lakini zinazotumia magari, jina na hadhi ya kiserikali (ya kuwa Mke wa Rais), kuvuta fedha za wafadhili kwa ajili ya kufanya kile kinachoitwa “kusaidia jamii”. Mifano ya taasisi hizi ni Taasisi ya Maendeleo ya Wanawake (WAMA) ya Mama Salma Kikwete na Mfuko wa Fursa Sawa kwa wote (EOTF) wa Mama Anna Mkapa. Mheshimiwa Spika, tabia ya kila mke wa rais kuanzisha taasisi yake tena baada tu ya mumewe kuingia madarakani, inatoa picha mbaya kuwa taasisi hizi huanzishwa kwa maslahi binafsi zaidi kuliko kusaidia jamii; kwa kuwa Mke wa Rais ni taswira ya Rais mwenyewe ambaye ndiye Kiongozi wa Nchi. Kambi ya Upinzani tunaona ipo haja kwa serikali kuandaa utaratibu rasmi wa kuwa na taasisi moja tu yenye nguvu itakayokuwa inaongozwa na mke au mume wa rais aliye madarakani kama mlezi, na kupokewa na wake au waume wa marais wajao, ili kuondoa picha hii mbaya ya kila mmoja kujianzishia taasisi au mfuko wake”. Mwisho wa Kunukuu. Mheshimiwa Spika, majibu ya hoja hii katika kitabu kilichotolewa na Ofisi ya Rais uk. 1-4 hayaridhishi kwani kwa bahati mbaya wamelinganisha vitu ambavyo kwa hali ya kawaida huwezi kuvilinganisha. Chungwa na nanasi yote ni matunda lakini huwezi kuyalinganisha! Huwezi kulinganisha mke wa Rais wa Tanzania na mke wa Rais wa Marekani, hawa wote ni wake wa ma-Rais lakini mfumo wa utawala wa Marekani ni tofauti na Tanzania. Mheshimiwa Spika, mwisho wa majibu kwa hoja hiyo, Serikali inasema, na nanukuu: “ushauri wa kuundwa kwa Taasisi moja itakayoratibiwa na wake au waume wa Marais umepokelewa na utafanyiwa kazi”. Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali ilieleze Bunge hili utekelezaji wa ushauri huu umefikia wapi? 2. TAASISI YA KUZUIA NA KUPAMBANA NA RUSHWA (TAKUKURU) Mheshimiwa Spika, taasisi hii muhimu ipo chini ya Ofisi ya Rais na inatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na. 11 ya mwaka 2007. Mheshimiwa Spika, kutokana na rushwa kuathiri maendeleo ya nchi yetu kwa kiasi kikubwa, Kambi ya Upinzani tunasisitiza kuwa ni wakati muafaka sasa kwa taasisi hii kuwa chombo huru kiutendaji na hata katika uteuzi wa mkurugenzi wake ili kuondoa dhana ya kukosa nguvu ya kuwachukulia hatua wala rushwa wakubwa au hata viongozi wa siasa wanaojihusisha na vitendo vya kifisadi. Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani tunapendekeza kuwa uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hii ufanywe na Kamati ya Taifa ya Uteuzi na athibitishwe na Bunge, pia taarifa za taasisi hii ziwe zinawasilishwa Bungeni kila mwaka na kujadiliwa na Bunge kama ilivyo sasa katika kujadili taarifa za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali. Tunatoa mwito kwa Watanzania wafikirie jambo hili ili iwe ni mojawapo ya hoja zitakazozingatiwa katika mchakato wa kuandikwa kwa Katiba mpya ambao ukusanyaji wa maoni unaanza rasmi leo. Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani tunaendelea kusisitiza kuwa bado kasi ya utendaji kazi wa taasisi hii hairidhishi kutokana na kuwa na mlundikano wa tuhuma mbalimbali za rushwa na kushindwa kufanyia kazi taarifa mbalimbali za rushwa kama zinavyowasilishwa hasa kipindi cha uchaguzi. Mathalani katika mwaka wa fedha unaoisha, TAKUKURU ilichunguza tuhuma 3,456 ambapo kati ya hizo ni tuhuma 727 tu ndio zilizokamilika. Mheshimiwa Spika, hivi karibuni kuna taarifa mbalimbali zilizotolewa na vyombo vya habari kwenye gazeti la The Citizen la tarehe 23/06/2012 na gazeti la Mwananchi la tarehe 26/06/2012 kuwa kuna baadhi ya viongozi wa serikali na baadhi ya wafanyabiashara nchini wenye akaunti mbalimbali katika benki nchini Uswisi na kuna fedha kiasi cha shilingi bilioni 315 ambazo ziliingizwa na makampuni mbalimbali ya nje ya uchimbaji madini na utafutaji mafuta zinazofanya kazi nchini. Mheshimiwa Spika, taarifa hizi ni nzito; sio za kupuuzwa, hasa na idara yetu ya usalama wa taifa pamoja na TAKUKURU. Pamoja na Waziri Mkuu kuiagiza TAKUKURU kufanya uchunguzi, Kambi ya Upinzani tunaitaka serikali itumie uzoefu wa nchi nyingine, kwa kuiomba mahakama ya Uswisi izilazimishe benki za huko walikoweka fedha zitoe majina ya wahusika na kiasi cha fedha walicho nacho katika benki hizo, ili wananchi wafahamu. Hii ni hatua ya kwanza. Hatua ya pili ni kuangalia je wamevunja sheria gani ya nchi? Kama ni viongozi wa umma ziangaliwe fomu za maadili ya umma kama fedha hizo walizitaja, kama ni za wizi basi zirejeshwe nchini; fedha hizo zinaweza kutumika kuboresha elimu au hata kuwalipa wazee wetu pensheni kama tulivyopendekeza kwenye hotuba yetu kuhusu bajeti ya mwaka 2012/2013. Mheshimiwa Spika, katika taarifa hiyo Kambi ya Upinzani tunaitaka serikali kulieleza Bunge lako tukufu katika mkutano huu wa Bunge unaoendelea wamiliki wa fedha hizo, zimepatikaje na hatua gani ambazo serikali itachukua dhidi ya watu hao. Pia tunaitaka serikali kupanua wigo wa uchunguzi ili kuzihusisha nchi za Afrika Kusini na nchi za Falme ya Kiarabu (UAE) ambapo mafisadi wengi wanatuhumiwa kuficha fedha na mali katika nchi hizo. Pia kila kiongozi wa kisiasa mwenye fedha na mali nje aangaliwe kama alitoa taarifa ya mali na fedha hizo kwenye fomu za maadili alizokwisha kuzijaza. Mheshimiwa Spika, kwa hatua ya sasa na jinsi rushwa inavyoathiri nchi hii ni vema serikali ikazingatia ushauri wetu wa mwaka uliopita kwenye hotuba ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kuwa na kitengo cha Usalama wa Taifa, ambacho pamoja na kazi zake nyingine, kitafanya kazi ya ujasusi wa kiuchumi kwa ajili ya kupata taarifa za wawekezaji mbalimbali ambao wanakuja nchini kuwekeza ili kuepukana na makampuni ya mifukoni kama ilivyokuwa Richmond. Ujasusi huu wa kiuchumi ujumuishe utafutaji wa fursa za kimaendeleo kwa ajili ya kuendeleza nchi yetu katika sekta mbalimbali. Mheshimiwa Spika, tatizo la rushwa linaloigusa serikali hii ndio msingi wa pendekezo la Kambi ya Upinzani la mara kwa mara kuhusu kufanya maboresho ya Idara ya Usalama wa Taifa. Taarifa za rushwa kubwa kama kashfa ya rada, rushwa ya Richmond, sakata la EPA na ufisadi wa IPTL ni ishara kuwa idara hii sio tena usalama wa taifa bali usalama wa baadhi ya viongozi wa serikali, chama chao na familia zao. Mheshimiwa Spika, katika hotuba ya Kambi ya Upinzani kwa mwaka uliopita tuliomba maelezo kuhusu watumishi waliohusika katika wizi wa Deep Green, Kagoda, mkataba wa IPTL na ufisadi mwingine. Naomba ninukuu sehemu ya hoja hiyo “Mheshimiwa Spika, aidha jitihada za dhati hazijaonekana za kushughulikia watumishi wa umma waliotajwa kwenye orodha ya mafisadi waliohusika na kashfa za Kagoda, Meremeta, Deep Green, Richmond, IPTL na mikataba mingine inayoendelea kulitia hasara Taifa letu” Mwisho wa kunukuu. Mheshimiwa Spika, kuhusu suala hilo, Serikali, kwenye uk. 32 wa kitabu cha majibu ya Ofisi ya Rais, ilisema, na nanukuu: “uchunguzi dhidi ya kashfa ya Kagoda, Meremeta na Deep Green unaendelea. Aidha, IPTL uchunguzi umepiga hatua kubwa”. Mwisho wa kunukuu. Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali kutoa taarifa kwa Bunge hili kuhusu uchunguzi wa ubadhirifu huo. Je, utakamilika lini, na watuhumiwa kufikishwa katika vyombo vya sheria lini? Kwani hivi sasa ni takribani miaka 10 toka kashfa ya Meremeta, Deep Green na Kagoda itolewe hadharani na IPTL ni takribani miaka 17. Huu ni muda tosha kabisa kwa taasisi makini kukamilisha kazi ya uchunguzi. Bunge kuhusishwa na vitendo vya rushwa Mheshimiwa Spika, kumekuwepo na vitendo vya kulidhalilisha Bunge ambapo zimetolewa tuhuma kadhaa na vyombo vya habari pamoja na waheshimiwa wenyewe kutuhumiana na wengine kukamatwa kwa tuhuma za rushwa. Ni dhahiri hata katika mchakato wa kuchagua wabunge la Afrika ya Mashariki kauli za vitendo vya rushwa zilitolewa na waheshimiwa wabunge. Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inaitaka TAKUKURU kuhakikisha kuwa pamoja na kuwakamata watuhumiwa wengine, iendelee kuchukua hatua kulisafisha jina la Bunge katika kashfa hii nzito inayoliondolea heshima mbele ya jamii. Suala la David Jairo na wenzake Mheshimiwa Spika, katika Bunge la Bajeti la mwaka uliopita wakati wa kujadili bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini, tuhuma za aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Ndugu David Jairo na wenzake kukusanya fedha bila kufuata utaratibu kwa ajili ya kupitisha bajeti ziliibuliwa na kulifanya Bunge kuazimia kuunda Kamati Teule kwa ajili ya kuchunguza suala hili. Mheshimiwa Spika, pamoja na Ofisi Kuu ya Utumishi wa umma, yaani Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi, kumsafisha Jairo na wenzake na hatimaye Jairo kurudishwa tena ofisini, Bunge lilitekeleza jukumu lake; na kupitia Kamati Teule uliyoiunda wewe mwenyewe, Bunge lilithibitishiwa kuwa utaratibu wa ukusanyaji wa fedha zile haukuzingatia sheria na taratibu. Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani tunahoji ni hatua gani ambazo TAKUKURU wameshachukua juu ya tuhuma dhidi ya Jairo na wenzake ambazo zilithibitishwa na Kamati ya Bunge lako tukufu. Kama hatua hazitachukuliwa dhidi yake ni dhahiri taasisi hii haitalitendea haki taifa hili na Bunge lako tukufu. 3. MFUKO WA MAENDELEO YA JAMII (TASAF) Mheshimiwa Spika, Mfuko wa Maendeleo ya Jamii kulingana na malengo yake ya kupunguza umaskini bado umeshindwa kujikita kwa walengwa kutokana na kukumbwa na changamoto za ubadhirifu wa rasilimali tengwa. Ubadhirifu huu umebainishwa katika ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali juu ya miradi ya maendeleo iliyotolewa tarehe 30Juni, 2011 kuhusu ukaguzi wa taarifa za fedha za miradi ya maendeleo kifungu cha 5.3.1 juu ya manunuzi ya vifaa ambavyo havikupokelewa. Changamoto zilizopo ni kutokuwepo kwa ushindani, kufanyika manunuzi bila mipango. Huu ni udhaifu wa Ofisi ya Rais kwa kusababisha hasara ya shilingi 50,275,000. Kambi ya Upinzani inaitaka serikali kuzingatia mapungufu haya na hatua stahiki zichukuliwe dhidi ya waliohusika na ubadhirifu huu. Mfuko wa Rais wa Kujitegemea (PTF) Mheshimiwa Spika, lengo la Mfuko wa Rais wa Kujitegemea (PTF) ni kuwasaidia wananchi wa kipato cha chini kwa kutoa mikopo yenye riba nafuu. Hata hivyo, mfuko umeshindwa kufikia malengo yake ikizingatiwa kwamba mikopo hutolewa kwa riba inayolingana na taasisi nyingine za kifedha. Kama mfuko huu unakopa katika benki kwa riba na baadaye kukopesha SACCOS ni kwa nini Mfuko huo usifanye kazi ya kutengeneza mazingira mazuri ya ukopeshwaji ili SACCOS na watu wengine wakope kwenye mabenki moja kwa moja? Kwani hapa inaonyesha kuwa Serikali inafanya kazi ya udalali na hivyo mzigo wa riba kumwangukia mkopaji wa mwisho ambaye ni mwananchi. Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inaitaka serikali kuheshimu dhamira ya kuwasaidia wananchi wa hali ya chini kiuchumi na kutekeleza nia njema ya kuanzishwa kwa mfuko huu ikiwa ni pamoja na kuwanufaisha walengwa, na hivyo, mfuko usitoze riba za kibiashara kama hali ilivyo hivi sasa. MKURABITA Mheshimiwa Spika, Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA) umekuwa ukitekelezwa kwa kasi ndogo kwa kuzingatia vigezo na tathmini zinazofanywa. Hali hii hupelekea wilaya nyingi kutofikiwa na mpango huu. Kambi ya Upinzani inaitaka serikali kusambaza mpango wa MKURABITA nchi nzima badala ya utaratibu ulivyo sasa. Tunaitaka Serikali iandae mpango-mkakati wa MKURABITA utakaoonesha jinsi Mpango huu utakavyotekelezwa nchi nzima, hatua kwa hatua. Mheshimiwa Spika, miongoni mwa matatizo yanayoukabili MKURABITA ni tatizo la mgongano wa kisheria kwa kipindi kirefu unaosababisha ugumu katika utekelezaji wa mpango huu. Sheria hizo ni sheria ya Ardhi, sura ya 113, sheria ya Ardhi ya vijiji, sura ya 114 na sheria ya Mipangomiji na. 8 ya mwaka 2007 ambazo ni miongoni mwa sheria zinazotumika katika kusimamia sekta ya ardhi. Mchakato wa kufanya marekebisho ya sheria hizi ulianza miaka iliyopita lakini mpaka sasa haujakamilika. Mheshimiwa Spika, taarifa iliyotolewa katika randama ya Ofisi ya Rais katika mafungu 20,30, 32,33,67,94 na 9 ukurasa 36 imeainisha, na nanukuu: “maandalizi ya maboresho ya sheria za ardhi na biashara yalikamilika mwaka 2008”. Kambi ya Upinzani inaitaka serikali kuharakisha mchakato wa miswada ya sheria hizi za ardhi na kuzileta bungeni ili zijadiliwe; maboresho ya sheria yataondoa dosari nyingi na kurahisisha utekelezaji wa MKURABITA. 4. MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA Tatizo la Watumishi Hewa Mheshimiwa Spika, kada ya Utumishi wa Umma imekumbwa na kashfa kubwa la watumishi Hewa. Tarehe 23 Machi, 2011, Rais Jakaya Kikwete alinukuliwa na magazeti ya The Guardian namba ISSN 0856- 5422 toleo 5083 na Daily News namba ISSN 0856 – 5422 toleo 10,302 akiagiza ukaguzi ufanyike katika idara zote za Serikali baada ya taarifa kwamba shilingi bilioni 9 za mishahara zimelipwa kwa watumishi hewa. Mheshimiwa Spika, suala la watumishi-hewa ni mbinu nyingine ambayo mafisadi ambao kimsingi ni wahujumu-uchumi, wanaitumia kutafuna fedha za umma bila jasho. Licha ya tatizo hili la watumishi hewa kuathiri malengo mahsusi ya bajeti ya Serikali, pia linapunguza ufanisi katika kada hii ya utumishi wa umma na hivyo kulisababishia taifa hasara kubwa. Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inalaani wizi huu wa fedha za umma unaofanywa katika utumishi wa umma huku viongozi waliopewa dhamana ya kusimamia fedha za umma wakibaki na mshangao badala ya kutoa majibu ya kiuwajibikaji. Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali, itoe taarifa rasmi ya hatua madhubuti ilizochukua kukomesha tatizo la watumishi hewa Serikalini, ikiwa ni pamoja na udhibiti wa malipo, na tunatoa rai kwamba wahusika wa kashfa hii wachukuliwe hatua kali mara moja ili liwe fundisho kwa yeyote aliye na nia ya kuchezea fedha za walipa kodi wa nchi hii. Kadhalika hii ni dalili wazi ya udhaifu wa Serikali kutokuwa na kumbukumbu sahihi za watumishi wake. Sekretarieti ya Ajira Mheshimiwa Spika, Serikali iliamua kuachana na sera yake ya D by D na hivyo kufanya ajira zote za umma kupitia Sekretarieti ya Ajira. Uamuzi huo kwa bahati mbaya sana umeanza pia kugusa ajira za Vyuo Vikuu Vya Umma! Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani tunaona mpango huu wa Sekretarieti ya Ajira ni vyema ihusike tu na watumishi wa umma wa Serikali kuu na sio Serikali za mitaa, au taasisi zingine za Serikali. Kwani uamuzi huo ni dhahiri unakinzana na Sheria zilizoanzisha taasisi hizo.
Mheshimiwa Spika, Sekretarieti ya Ajira kuchukua jukumu la kuajiri watumishi bila kujali ni wa Serikali Kuu, Serikali za Mitaa au taasisi za Serikali ni jambo la hatari la kuhodhi madaraka na ukiritimba usiotakiwa. Hii ni kutokana na ukweli kwamba chombo hicho kina kazi chache kama mfumo wa ugatuaji wa madaraka ungekuwa unafanya kazi kwa kadri ya uanzishwaji wake. Rai yetu ni kwamba taasisi ambazo kisheria zina mamlaka ya kuajiri ziachwe ziendelee kuajiri kama ambavyo zimekuwa zikifanya. Malipo ya Uzeeni yenye Utata Mheshimiwa Spika, malipo ya uzeeni kwa watumishi wa umma wastaafu ni jambo linalohitaji uangalizi makini kwani linaweza kutumiwa vibaya na watendaji na hivyo kupoteza fedha za umma. Kwa mujibu wa taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya mwaka 2011, ukokotoaji wa fedha za malipo ya uzeeni ulizidi kwa kiasi cha shilingi 539,201,733.63 na kiasi kilichopunjwa ni shilingi 106,007,774.81. Mheshimiwa Spika, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu ameeleza kwamba kama malipo ya uzeeni yangelipwa bila kukaguliwa basi Serikali ingepata hasara ya shilingi 539,201,733.63 na vilevile wazee wangelipwa pungufu ya shilingi 106.007, 774.81. Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inakemea vikali hali ya watendaji wa Serikali ya kutokuwa makini katika kutekeleza majukumu muhimu hasa yanayohusu fedha za umma. Kambi ya Upinzani inashawishika kuamini kwamba fedha nyingi za walipakodi wa Tanzania zinapotea kwa sababu ya uzembe wa watendaji wa Serikali. Tunaitaka Serikali kutoa taarifa ya hatua ilizochukua hadi sasa kutokomeza uzembe kama huu. Pensheni kwa Wahadhiri Wastaafu wa Vyuo Vikuu vya Umma Mheshimiwa Spika, hawa ni wale waliokuwa kwenye Utaratibu wa SSSS. Suala hili lilizungumzwa mwaka jana katika hotuba ya Kambi ya Upinzani. Utaratibu huu uliwahusu wahadhiri na maprofesa walioajiriwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kabla ya Julai 1978. Kwa mujibu wa utaratibu huu, mstaafu alipata malipo ya mkupuo mmoja tu, na hapati pensheni ya kila mwezi. Mheshimiwa Spika, utaratibu wa SSSS ulifutwa kuanzia Machi 2011. Hata hivyo, katika hatua hiyo serikali haikuwafikiria wahadhiri waliostaafu kabla ya tarehe hiyo. Serikali, katika majibu yake mwaka jana, ilisema kuwa serikali ilitaka kuwahamisha lakini wahadhiri wakakataa kuhama toka SSSS kwenda taratibu nyingine za hifadhi za jamii miaka ya nyuma. Mheshimiwa Spika, naomba kulifahamisha Bunge lako tukufu kuwa hakuna mahali popote wala wakati wowote ambapo serikali hii iliwauliza wahadhiri wa Vyuo Vikuu vya Umma jambo kama hili. Kwa hiyo dai hilo la serikali lilikuwa si sahihi, na sisi tunaelekea kuamini kuwa lilikuwa na lengo la kukwepa jukumu au kuudanganya umma. Mheshimiwa Spika, ukweli ni kwamba toka miaka ya 1990 hadi Machi 2011 wahadhiri wa Vyuo Vikuu vya Umma, kupitia vyama vyao, walihangaika na suala hili bila mafanikio. Mheshimiwa Spika, ni jambo la aibu kwa maprofesa/wahadhiri wazima kuhangaika baada ya kustaafu kwa kosa ambalo si lao wakati wanafunzi wao hawapati shida ya pensheni ya kila mwezi, na wote wakiwa wamefanya kazi chini ya serikali ya Chama cha Mapinduzi! Mheshimiwa Spika, kwa kuwa tayari serikali imeshaunda Mamlaka ya Udhibiti wa Hifadhi za Jamii, na kwa kuwa wahadhiri wa vyuo vikuu walifanya juhudi mapema kubadilisha utaratibu huo kuanzia miaka ya 1990 bali mafanikio yakaja yamechelewa kwa wengi wao waliostaafu kabla ya Machi 2011, na kwa kutambua mchango mkubwa ambao hawa watumishi wa vyuo vikuu wameutoa kwa taifa, Kambi ya Upinzani inaitaka serikali kuielekeza Mamlaka ya Udhibiti wa Hifadhi za Jamii kuanza kupanga jinsi ya kuwapatia pensheni ya kila mwezi wastaafu hawa. Tunaomba suala hili lichukuliwe kwa umuhimu wake, kwani hakuna mtu anayependa kuona anafanyiwa ubaguzi wa mafao kwa makosa ambayo si yake. Kupunguza Gharama za Uendeshaji wa Serikali Mheshimiwa Spika, kwa muda mrefu sasa Kambi ya Upinzani tumekuwa tukipinga ongezeko la matumizi ya Serikali hasa katika gharama za uendeshaji. Ukiangalia mfumo mzima wa Menejimenti ya Utumishi wa umma utaona kuwa muundo wake unaongeza gharama ambazo zingeweza kuepukwa. Kwa mfano shughuli za kada hii ya Utumishi wa Umma zinaratibiwa na vyombo vifuatavyo: Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Tume ya Utumishi wa Umma, Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma na Bodi ya Mishahara na Maslahi katika Utumishi wa Umma. Kazi za taasisi hizi zinazofanywa kwa ujumla ni zilezile za usimamizi wa Utumishi wa Umma na vilevile hazitimizi majukumu yake ipasavyo. Mheshimiwa Spika, nitatoa mfano wa jinsi taasisi hizi zisivyotimiza wajibu ipasavyo. Sekretarieti ya Ajira iliyoanzishwa baada ya marekebisho ya Sheria ya Utumishi wa Umma namba 18 ya 2007, pamoja na mujukumu mengine, ina majukumu yafuatayo: kuwatafuta wataalamu na kuwa na kanzidata kwa ajili ya ajira na kusajili wahitimu na wataalamu kurahisisha ajira. Mheshimiwa Spika, kwa kuwa uzoefu unaonesha kwamba Sekretarieti hii imekuwa ikitoa matangazo ya kazi tu bila hata kufanya usaili, Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali kupitia Ofisi ya Raisi Menejimenti ya Utumishi wa Umma kuonesha idadi ya wataalamu ambao wameshatafutwa na Sekretarieti ya Ajira na idadi ya wahitimu na wataalamu ambao tayari wamesajiliwa na wapo kwenye hiyo kanzidata ambayo imetajwa na sheria husika. Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inashauri kuwa na chombo kimoja kitakachoratibu mambo yote ya utumishi wa Umma. Faida ya kuwa na chombo kimoja ni kwamba usimamizi wake utakuwa ni rahisi na kwa jinsi hiyo kitakuwa na ufanisi. Migogoro baina ya Serikali na watumishi wake Mheshimiwa Spika, ingawa kuna sheria mbili nzuri, yaani Sheria namba 19 ya Majadiliano ya Pamoja katika utumishi wa umma ya mwaka 2003 inayoitaka serikali kuwashirikisha watumishi katika maamuzi kuhusiana na utumishi wa umma, na Sheria ya Mahusiano Kazini ya mwaka 2004, Serikali inasuasua katika utekelezaji wake na hivyo kusababisha migogoro na wafanyakazi na kuathiri huduma muhimu kwa jamii. Hotuba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, menejimenti ya utumishi wa umma, akiwasilisha bungeni makadirio ya matumizi ya fedha kwa mwaka 2009/2010, aliahidi mbele ya bunge kutekeleza maagizo ya sheria hizi, lakini matokeo yake hayatoshelezi. Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali kuzingatia sheria hizi na ishirikishe watumishi wa Umma katika maamuzi yanayowahusu watumishi hasa maslahi yao. Aidha, Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali ioanishe Sheria hizi iwe moja itakayo shughulikia na kulinda haki na maslahi ya wafanyakazi. Mheshimiwa Spika, madai ya watumishi wa umma yameongezeka kwa kasi huku yakichukua sura mpya ya migomo kama nyenzo ya kuishinikiza Serikali kutatua madai yao. Siku za hivi karibuni tumeshuhudia migomo ya madaktari wengi ambayo licha ya kuathiri uwajibikaji na ufanisi katika utumishi wa umma, imesababisha vifo vya Watanzania masikini wasio na hatia. Hata sasa kuna dalili za mgomo baridi wa madaktari ambapo hali ya huduma katika hospitali zetu sio nzuri hata kidogo. Pia kumekuwa na matishio ya migomo hasa watumishi wa kada ya ualimu. Mheshimiwa Spika, madai ya watumishi hawa ni pamoja na nyongeza ya mishahara kwa wale wenye stahili, malimbikizo ya mishahara, fedha za usumbufu wa uhamisho, fedha za likizo, mafao ya uzeeni kwa wastaafu, kupunguza kiwango cha kodi (PAYE) katika mishahara na kuweka mazingira bora ya utoaji wa huduma. Mheshimiwa Spika, kwa kuwa tumesikia kauli za upande mmoja tu wa Serikali, Bunge liingilie kati kuthibitisha kama madai haya ni halali au si halali. Kambi ya Upinzani inatoa ushauri kwa Serikali kuharakisha kushughulikia madai haya kwani dalili za migomo kwa watumishi wa umma zinazoendelea hivi sasa sio nzuri kwa uchumi wa nchi yetu, na pia sio dalili nzuri kwa amani ya nchi yetu. Ni matumaini ya Kambi ya Upinzani kuwa Serikali hii ya CCM ambayo imekuwa ikijiita sikivu basi na isikie sasa na kutatua madai ya watumishi wa umma. Mheshimiwa Spika, naomba kunukuu kauli ya Mtendaji Mkuu wa ESRF kuhusiana na mgomo wa Madaktari: “Maoni ya wengi kutokana na mgomo wa Madaktari wa Februari 2012, yalilenga zaidi kwenye kuboresha uwajibikaji wa viongozi katika Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii katika kushughulikia maslahi ya wafanya kazi wake; pamoja na kuangalia upya suala zima la malipo na mafao ya wafanyakazi katika sekta zote”. (Chanzo, Tovuti ya ESRF, http://esrf.or.tz/madaktari.pdf,) Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali kuliangalia jambo hili kwa makini kwani uwajibikaji wa viongozi katika sekta mbalimbali ni suala la msingi sana. Kwamba Serikali isiyowajibika kwa wananchi wake katika utoaji wa huduma za msingi, na huduma za msingi ni pana sana, maana yake ni kuwa Serikali hiyo inakuwa imekosa uhalali wa kuitawala jamii. Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali isiishie kwenye kuwawajibisha viongozi wa wizara husika, bali ilishughulikie suala la malipo na mafao kwa makini. Serikali isiishie tu kwa madaktari, bali iharakishe utekelezaji wa azma inayotajwa uk. wa 16 wa Mpango wa Maendeleo wa Miaka 5 (Toleo la Kiswahili Juni 2011) ya kupitia mishahara na marupurupu katika Utumishi wa Umma. Aidha, Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali iyafanyie kazi mapendekezo yaliyo katika Ripoti ya Tume ya Ntukamazina iliyowasilishwa kwa Rais Januari 2007. Lengo la Tume lilikuwa ni kuboresha mishahara na maslahi katika sekta ya utumishi wa umma, lengo hili likamilishwe na Serikali. Mheshimiwa Spika, sheria ya majadiliano ya pamoja ya mwaka 2003 na sheria ya mahusiano ya kazi, ya mwaka 2004, zinatoa mwongozo wa uwepo wa mabaraza ya mashauriano kati ya Serikali na watumishi. Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inasikitika kuona kuwa kipindi hiki chote ambacho kumekuwa na tishio la migomo toka kwa watumishi wa umma, mabaraza ya majadiliano ya watumishi katika sekta ya elimu, afya, Serikali za mitaa na Serikali kuu yalimaliza muda wake mwaka 2011. Hivyo basi, Kambi ya Upinzani inatoa rai kwa Serikali iharakishe kuhuisha upya mabaraza hayo ili yafanye kazi. Sambamba na hilo, mabaraza yakishaundwa yaache tabia iliyokuwepo awali ya kutokutimiza majukumu yake kikamilifu. Maagizo ya Bunge kwa Menejimenti ya Utumishi wa Umma Mheshimiwa Spika, katika kikao cha kujadili mapendekezo ya mpango na bajeti ya mwaka 2011/212 cha Juni, 2011 Bunge kupitia Kamati yake ya Kudumu ya Katiba, Sheria na Utawala iliiagiza Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma kutekeleza pamoja na mambo mengine majukumu yafuatayo: i. Kupanua wigo wa upatikanaji wa wataalamu na kuweka vivutio ili kuimarisha maadili ya Watumishi wa umma. ii. Kuangalia upya maslahi ya watumishi kwa kuoanisha hali ya maisha ya sasa ili kuwapunguzia makalli ya maisha watumishi wa Serikali na kuongeza uwajibikaji. iii. Kutilia mkazo Mfumo wa Tathmini Wazi ya Utendaji (Open Performance Appraisal System= OPRAS) kusaidia kurudisha nidhamu ya uwajibikaji. Mheshimiwa Spika, pamoja na serikali kuwa na muda wa kutosha na kutengewa fedha katika bajeti iliyopita bado haijatekeleza kikamilifu maagizo haya. Serikali ilichokifanya ni kutoa majibu mepesi kama vile “tunaandaa mkakati wa kutekeleza” ikiwa ni mwaka mmoja tangu maagizo yatolewe. Mheshimiwa Spika, kuhusu maslahi ya watumishi yanayoendana na hali ya maisha ya sasa, majibu ya Serikali ni kwamba inaendelea kuboresha maslahi na kwamba imeongeza kima cha chini hadi kufikia shilingi 135,000/= kwa mwezi. (Na kwamba kwenye mwaka wa fedha 2012/2013 kinatarajiwa kuongezeka mpaka shilingi 170,000/-). Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inaona kuwa Serikali sasa inakwenda kinyume kabisa na kaulimbiu yake ya “maisha bora kwa kila Mtanzania” kwani kiwango hiki ni kidogo sana na hakiendani kabisa na hali ya maisha ya sasa kutokana na mfumuko wa bei kuwa juu. Mheshimiwa Spika, ni dhahiri kuwa kiwango kidogo cha mshahara na maslahi kwa watumishi huchangia kwa kiasi kikubwa utovu wa uwajibikaji na ufanisi wa kiwango cha chini katika utumishi wa umma. Kwa kutambua jambo hili, Kambi ya Upinzani imekuwa ikipigania kima cha chini cha mshahara kipande hadi kufikia shilingi 315,000 lakini kwa masikitiko makubwa Serikali hii sikivu haijasikia hili hadi sasa. Rai yetu kwa watumishi wote wa umma, waendelee kupigania haki zao na sisi tutaendelea kuwaunga mkono. Mheshimiwa Spika, kuhusu Mfumo wa Tathmini Wazi ya Utendaji ni kwamba bado hautumiki ipasavyo, tofauti na Serikali inavyosema. Uzoefu unaonesha kuwa bado taasisi nyingi za Serikali hazitumii mfumo huu na taarifa za mtumishi bado zimekuwa zikishughulikiwa kwa siri na mtumishi hana nafasi ya kuona na kuhoji taarifa zilizo kwenye jalada lake. Matokeo ya tatizo hili ni mtumishi kukosa haki zake hasa pale anapopandishwa cheo/mshahara na kutopewa stahili hizo pamoja na kwamba taarifa zipo kwenye jalada. Wengine hupunjwa mafao yao ya kustaafu kwa kuwa taarifa zao sio sahihi. Kama mtumishi angekuwa anapata fursa ya kuangalia jadala lake angepata nafasi ya kutoa taarifa sahihi na hivyo kupata stahili zake ipasavyo. Inasikitisha kuwa kuna watumishi hadi wanastaafu hawajawahi kuona majalada yao. Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali kuwa na tabia ya kutekeleza kikamilifu maagizo inayopewa na kamati za bunge na ilete taarifa ya utekelezaji halisi uliofanyika na sio kuleta taarifa ya kwamba “mchakato unaendelea……” Usimamizi wa Utendaji Mheshimiwa Spika, miongoni mwa matakwa ya msingi ya ufanisi katika utumishi wa umma ni kwa watumishi kufanya kazi kwa bidii na kwa kujituma. Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani tuna wasiwasi kwamba desturi ya kufanya kazi “kwa mazoea” yaani kutofanya kazi kwa bidii imeshamiri katika sekta ya umma. Hali hii inasababishwa hasa na ukosefu wa usimamizi madhubuti wa utendaji kwa watumishi lakini pia kukata tamaa kwa watumishi kutokana na mshahara kutowiana na gharama za maisha. Matokeo ni kwa watumishi kubuni njia mbalimbali za kujipatia kipato na hivyo kukosa ufanisi katika ajira zao katika utumishi wa umma. (Kwa mfano walimu wa shule za msingi hufanya biashara mashuleni wakati wa masomo, na wahadhiri, katika vyuo vikuu vya umma hufanya ”kazi za muda” katika vyuo vingine tofauti na kule walikoajiriwa). Yote haya yanapunguza tija kwa kiasi kikubwa sana katika utumishi wa umma. Mheshimiwa Spika, haitoshi kujiridhisha na kuwa na watendaji wenye sifa, lakini ni lazima kujenga mfumo wa usimamizi wa utendaji wa watumishi hawa wenye sifa ili utendaji wao uwe na tija kwa taifa. Mfumo huu sio wa “kinyapara” wa kumsimamia mtumishi kwa kiboko ndipo afanye kazi, bali mfumo ambao utamjengea mtumishi utamaduni wa kuwajibika na aone fahari kufanya kazi. Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inapendekeza mfumo shirikishi ambao mtumishi pamoja na mkuu wake wa kazi watakuwa na mahusiano ya karibu na sio uhusiano ule wa “bosi” na “mtumishi” uliopo sasa hivi. Hali iliyopo sasa hivi ni kwamba wakubwa wamejifanya “miungu watu” na hivyo watumishi wanawaogopa mabosi wao na hivyo huwakwepa. Hali kama hii haiwezi hata mara moja kuongeza ufanisi katika utendaji kwa kuwa hakuna mawasiliano ya karibu kati ya watumishi na wakubwa wao wa kazi. Mheshimiwa Spika, motisha ya vitu na ya kauli kwa watumishi imeelezwa na wanazuoni wengi katika eneo la menejimenti ya rasilimaliwatu kuwa vichocheo muhimu vya utendaji mzuri wa watumishi. Kwa kuwa watumishi wengi hujishughulisha na kazi nyingine nje ya ajira zao muda ule ule wanaopaswa kuwa kwenye vituo vyao vya ajira, Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali kuongeza mishahara ya watumishi kwa kulingana na hali halisi ya maisha ili watumishi wafanye kazi kwa moyo na kuongeza tija na ufanisi katika kazi zao. Pia ni muhimu kuondoa malimbikizo ya mishahara kwa kuwalipa watumishi stahili zao kwa wakati mwafaka. Mapitio ya Bajeti Iliyopita Mheshimiwa Spika, mwaka 2011/2012 Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma ilitengewa shilingi 33,361,247,000 na mwaka huu wa fedha wanaomba shilingi 42,431,552,870 ikiwa ni ongezeko la shilingi 9,070,305,000 sawa na asilimia 27.2%. Mheshimiwa Spika, ongezeko hili ni kubwa ukizingatia kwamba majukumu yanayotekelezwa hayana tofauti sana na yale ya mwaka jana. Pia baadhi ya kazi zimeandikwa kwa ujumla mno, jambo ambalo linatoa mwanya wa kutofanya kazi hiyo kwa ufanisi: Kwa mfano mojawapo ya shughuli ni “Kuandaa tafiti 5 katika masuala mbalimbali” (fungu 32 uk. 11 na. xiv). Hii haioneshi shughuli mahsusi na hivyo kukaribisha utashi wa mtu binafsi badala ya msingi wa mwongozo. Tunaitaka serikali ieleze hizi tafiti ni tafiti gani? 5. CHUO CHA UTUMISHI WA UMMA Mheshimiwa Spika, kumbukumbu zinaonyesha kuwa tangu kuanzishwa kwake kama Wakala wa Serikali mwaka 2000, Chuo cha Utumishi wa Umma kimeendelea kukua na kujiimarisha katika utoaji wa huduma katika nyanja za utumishi, utawala, menejimenti na uongozi kwa utumishi wa umma. Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inasema kama chuo hiki kipo ni kwa vipi viongozi wateule wanashindwa kutenda kazi zao za kiuongozi? Baadhi ya viongozi wa umma wanajikita kutenda kazi zao kwa misingi ya ushabiki wa kisiasa jambo ambalo linaleta mitafaruku isiyo na maana miongoni mwa wanaowaongoza. Mheshimiwa Spika, viongozi wetu wengi ama hawafuati kwa dhati au hawaelewi miiko ya uongozi; ndiyo maana vitendo vya wizi na ubadhirifu wa mali za umma vinaendelea. Aidha, kuna upendeleo katika utoaji wa zabuni na mambo yasiyozingatia uadilifu wa utendaji katika sekta ya umma. Rushwa iliyokithiri katika sekta ya umma ni kielelezo tosha kuwa miiko ya uongozi si sehemu ya utamaduni wa sekta ya umma. Uenevu wa ufisadi unabainishwa na nukuu toka taarifa ya utafiti uliofanywa na TAKUKURU kuhusu ufisadi na utawala wa kitaifa ya mwaka 2009: “……. pamoja na juhudi zilizoorodheshwa hapo juu, ufisadi umeenea na ni kikwazo kikubwa cha juhudi za maendeleo; sababu kubwa ya ufisadi ni ulafi miongoni mwa watumishi wa umma na wafanyabiashara; katika baadhi ya vitengo vya utumishi wa umma ufisadi umegeuka kuwa njia ya maisha; asasi ambazo ni za msingi katika kulinda utawala bora kama polisi na mahakama ndizo zinazoongoza kwa kushiriki ufisadi.” Mwisho wa kunukuu Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inaitaka TAKUKURU kutoishia kufanya utafiti tu bali iende mbele zaidi kuweza kung’oa mizizi ya rushwa maeneo ambayo imeyafanyia utafiti, kinyume na hapo itakuwa ni kila mara kufanya tafiti za maeneo yanayoongoza kwa rushwa lakini hakuna suluhisho. Mheshimiwa Spika, takwimu zinaonyesha kuwa asilimia 69.6% ya watumishi wa umma ndio wanaodai rushwa ili watoe huduma kinyume na taarifa kuwa wananchi ndio wanaoanzisha au kushawishi utoaji wa rushwa. Na mara zote watumishi wa umma rushwa imebatizwa majina kama vile, malipo yasiyo rasmi, na jina hili ni lina umaarufu wa asilimia 94.4%, rushwa ya ngono ni asilimia 57.4%. (Chanzo, Taarifa Ya Utafiti Kuhusu Ufisadi Na Utawala Kwa Taifa ya Mwaka 2009 , juzuu 3: utafiti wa watumishi wa umma.)
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali kusisitiza ufundishwaji wa maadili na miiko ya utumishi wa umma. Taaluma ya utawala tu haitoshi. Maadili na miiko inayosimamia utendaji lazima ifunzwe vilivyo. La sivyo sekta ya utumishi wa umma itaendelea kushindwa kusonga mbele. 6. SEKRETARIETI YA MAADILI YA VIONGOZI WA UMMA Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani kupitia kwa Mhe. Zitto Zuberi Kabwe mwaka 2008, 2009, na 2010 tulileta muswada Bungeni kwa ajili ya kuboresha sheria ya maadili ya viongozi. Mheshimiwa Spika, Muswada huo ulipigwa danadana kwamba Serikali inafanyia kazi muswada wa sheria ya maadili ya viongozi. Lakini mpaka leo muswada huo haujawasilishwa Bungeni. Kuna haja kubwa ya kufanya marekebisho kwenye sheria ya maadili ili kuifanya kuwa ya uwazi zaidi na wananchi wawe na haki ya kujua mali wanazomiliki viongozi wao wa kisiasa. Mheshimiwa Spika, uwazi kwenye fomu za maadili ni moja ya suluhisho la kadhia ya ufisadi. Mgongano wa kimaslahi kati ya viongozi wa kisiasa na biashara zao ndio umetufikisha hapa tulipo leo. Hatusemi wanasiasa wasiwe wafanyabiashara, bali ni lazima kuweka wazi maslahi ya kibiashara ambayo wafanyabiashara walio kwenye siasa wanayo. Vinginevyo ufisadi utaendelea kushika kasi nchini siku hadi siku. Mheshimiwa Spika, idara hii ni muhimu sana hasa ukizingatia kuwa inahusika kuhakikisha kuwa viongozi wa umma wanazingatia maadili ya kazi katika utendaji wao kila siku. Mheshimiwa Spika, Sekretarieti hii ina changamoto kubwa sana ya kuongozwa na watumishi ambao wengi wao ni wastaafu kutoka katika mhimili wa Mahakama. Pamoja na kutambua mchango wa Majaji wastaafu wanaoongoza idara hii, Kambi ya Upinzani inaona ni muhimu sasa serikali kuchukua hatua ya kuwa na watumishi ambao hawajastaafu kwa ajili ya kuboresha utendaji na ufanisi katika kazi muhimu za idara hii. Mheshimiwa Spika, tatizo jingine kubwa linaloathiri utendaji wa idara hii ni kukosa bajeti ya kutosha kwa ajili ya kutimiza kazi zake kwa mujibu wa sheria. Taarifa zilizonukuliwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu katika taarifa ya mwaka 2011 zinaonyesha kuwa waliweza kuhoji viongozi 23 tu waliokiuka taratibu za utumishi wa umma na zaidi ya nusu ya madiwani wote nchini hawakuweza kuwasilisha taarifa zao na hawajachukuliwa hatua yoyote. Mheshimiwa Spika, ili kuboresha utendaji wa sekretarieti ya maadili ni vema serikali ikawapa uwezo wa kifedha na hivyo kuwawezesha kufanya kazi kwa uhalisia ikiwa ni pamoja na kuzifanyia uhakiki taarifa zinazotolewa na viongozi na watumishi wa umma kuhusu uhalali wa mali zao. Aidha, ni vema taarifa zote wanazopokea ziwekwe kwenye tovuti ili wananchi wapate taarifa badala ya kuwa na masharti magumu ya kisheria ya kukagua taarifa husika. 7. TUME YA UTUMISHI WA UMMA Mheshimiwa Spika, wajumbe waTume hii wameteuliwa na Rais na iko chini ya Rais na inawajibika kwa Rais, hivyo ni dhahiri haiwezi kufanya jambo lolote ambalo litakwenda kinyume na matakwa ya Rais. Huu ni upungufu mkubwa unaosababisha sekta ya utumishi wa umma kutokuwa huru na hivyo sekta ya utumishi wa umma kukosa uimara. Mheshimiwa Spika, mamlaka ya Rais kikatiba kwa kiasi kikubwa yanachangia kuivuruga sekta ya utumishi wa umma, kwa dhana kwamba nafasi nyingi na nyeti zinafanywa kuwa za kisiasa badala ya kiutendaji hivyo uwajibikaji wa watumishi hao unakuwa mgumu na badala yake wanafanya kazi kwa lengo la kumfurahisha mtu aliyefanya uteuzi huo. Kwa mfano, nafasi za makamishana wakuu wa taasisi nyeti, ukurugenzi na utendaji mkuu kwenye taasisi nyingi za Serikali uteuzi wake unakuwa sio wa wazi jambo linalopelekea kuwa hata uwajibishwaji wa watumishi hao na vyombo kama bodi zao unakuwa mgumu. Kambi ya Upinzani inaliona hili kuwa ni kasoro kubwa; linahitaji kuangalia na hatimaye kuwa jambo la kikatiba, Tunawaomba Watanzania watoe maoni kwenye mchakato wa kuandika Katiba Mpya kuhusiana na suala hili. Mheshimiwa Spika, Tanzania ya sasa haina upungufu wa watendaji wenye uwezo, lakini kuna tatizo kubwa katika taasisi zetu nyingi kwa watu ambao wamefikisha muda wa kustaafu kuongezewa muda na kuendelea kufanya kazi kwa mikataba. Kambi ya Upinzani inasisitiza kuwa Serikali idhibiti mtindo wa kuongezeana mikataba wakati mtu keshastaafu kwani inawanyima vijana fursa za kuonyesha vipaji na ubunifu wao, jambo linalopelekea kwenda nje ya nchi kutafuta kazi. Mheshimiwa Spika, naomba kunukuu mahojiano kati ya mtaalam wa utawala wa Chuo Kikuu cha Dar, Dr. Bana na Ndg.Andrew Schalkwyk ya tarehe 19 Novemba 2008, Nanukuu: “Nchini, desturi daima imekuwa kwamba walioteuliwa kwenye nafasi za makamishna wa utumishi wa umma,…… hawa ni watu waliostaafu……. Wastaafu ambao hawajachoka. Lakini unapoajiri mstaafu ili afanye kzi katika chombo muhimu kama Tume ya Utumishi wa Umma, kuna tatizo…. Watu hawa wamechoka… na pia watu hawa wamechoka na watu hawa tayari wametimiza muda wao wa kisheria kustaafu, hivyo hawawezi kutembelea maeneo yote ya nchi yetu”. Mwisho wa kunukuu. Mtaalamu huyuanaonyesha waziwazi kuwa mara nyingi mtu akiendelea kuongezewa muda wa kazi baada ya kustaafu ni hakika kuwa utendaji wake utakuwa na mapungufu. 8. MAHUSIANO YA SIASA NA DINI Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Rais, kupitia Wizara ya Mahusiano na Uratibu ndiyo yenye jukumu la kuangalia na kusimamia mahusiano mema kati ya Serikali na taasisi za dini na asasi za kiraia. Mheshimiwa Spika, katika majumuisho ya hotuba ya Waziri Mkuu, Waziri wa Nchi, Sera, Uratibu na Bunge akijibu hoja ya Kambi ya Upinzani kuhusiana na udini, ukabila na ukanda kuingizwa kwenye siasa, alitoa jibu rahisi kuwa wale wote wanaolalamika ndio wanajihusisha na jambo hilo. Huu ni mzaha ambao unaweza kuhatarisha umoja na mshikamano wa nchi hii. Mheshimiwa Spika, sehemu nyingi katika Afrika na kwingineko ambako machafuko yametokea kwa kiasi kikubwa yamesabishwa na watu kutumia udini au ukabila katika siasa. Hivyo basi wahusika wakuu katika maeneo haya wanatakiwa kukumbushwa mara kwa mara wajibu na umuhimu wa kusimamia kwa dhati umoja na mshikamano katika taasisi wanazoziongoza. Mheshimiwa Spika, hatari ya kuligawa Taifa sasa haiko katika siasa pekee, bali hata ndani ya dini zetu. Yanayowasukuma baadhi ya viongozi wetu wa dini kuendeleza na kukoleza vita hii ya ki-imani ni pamoja na udhaifu wa serikali kukemea na kuchukua hatua stahiki kadri matukio yanavyotokea. Kuna tuhuma nyingi vile vile kuwa baadhi ya viongozi wetu wa dini wametumiwa na kufadhiliwa na watu mashuhuri wakiwemo wafanyabiashara wakubwa kwa niaba ya viongozi wa kiserikali kueneza propaganda hizi kwa malengo ya kisiasa. Mheshimiwa Spika, vipo vyombo vya habari vinavyomilikiwa na taasisi za dini ambavyo wakati mwingine vimekuwa vikieneza uchochezi wa wazi dhidi ya dini nyingine bila mamlaka za kiserikali kuchukua hatua stahiki. Kambi ya Upinzani inaitaka serikali itoe tamko kukemea hali hii na iahidi ndani ya Bunge kutokuvumilia dini, kiongozi au muumuni yeyote wa dini yeyote atakayeshindwa kuheshimu haki ya mwenye imani tofauti. Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inaamini kuwa madhehebu ya dini yana haki ya kuhoji na kushauri utendaji wa Serikali na kutoa mwelekeo wao ni upi katika yale wanayoona ni tatizo na kupongeza wanapoona kuwa yamefanywa vizuri. Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inasisitiza ushauri ambao tumekuwa tukiutoa mara kwa mara kuwa sisi sote tuzingatie matakwa ya sheria ya usajili wa vyama vya siasa ya mwaka 1992 (Na. 8, kifungu cha 2) inayokataza vyama vya siasa kutetea au kuendeleza maslahi ya kidini, kikabila au kikanda. Kambi ya Upinzani inasisitiza aliyosisitiza Baba wa Taifa kwamba masuala ya udini na ukabila yanahitaji usimamizi makini. Aidha, Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali kufanya uchunguzi wa kina ili kubaini wale wote watakaobainika kuwa wanafanya siasa kwa kutumia udini, ukabila na ukanda wachukuliwe hatua kali. 9. OFISI YA RAIS –TUME YA MIPANGO
Mheshimiwa Spika, majukumu ya msingi ya Tume ya Mipango ni:
a. Kutoa dira na mwongozo wa uchumi wa Taifa; na
b. Kubuni sera za uchumi na mikakati ya mipango ya maendeleo ya Taifa pamoja na usimamizi wa uchumi na utafiti.

Mheshimiwa Spika, majukumu tajwa hapo juu ni makubwa sana japokuwa rasilimali watu katika ofisi hiyo ni ndogo kukidhi majukumu hayo. Ni ukweli ulio wazi kuwa Tume hii ndiyo iliyotoa Dira ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Miaka Mitano.

Mheshimiwa Spika, Tume ya Mipango, pamoja na kazi hizo za msingi, inahitajika kufanya kazi ya kuhakikisha kuwa inatayarisha mkakati wa kusimamia utekelezaji wa mipango hiyo.

Mheshimiwa Spika, taarifa za randama zinaonyesha kuwa ina watumishi 122 wakati mahitaji halisi ni watumishi 174. Tatizo hili linapelekea ukwamishwaji au utendaji kazi katika hali ngumu sana, jambo hili linaweza sababisha mipango yetu iwe ya kinadharia zaidi badala ya kiuhalisia.

Mheshimiwa Spika, bajeti ya Tume ya Mipango kwa mwaka wa fedha unaomalizika ilikuwa shilingi bilioni 8.039 na mwaka huu wa fedha imetengewa shilingi bilioni 8.007 ikiwa ni pungufu ya ile ya mwaka jana kwa shilingi milioni 32. Mbaya zaidi ni kwamba fedha zote zinazoombwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya Tume ni fedha kutoka nje. Tunapaswa kukumbuka kuwa kwa sasa tuna tatizo kubwa la fedha za nje kutokutolewa kwa wakati, jambo ambalo linapelekea kucheleweshwa kwa utekelezaji wa mipango yetu.

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali kuliangalia jambo hili la Tume kupewa mahitaji yake halisi ili ifanye kazi kama inavyotakiwa.

Mheshimiwa Spika, zipo dosari mbili ambazo tulizitaja katika hotuba ya Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani kwa Bajeti ya Taifa kwa mwaka 2012/2013. Dosari hizo ni:-
1. Mpango wa 2012/2013 haukuzingatia kwa ukamilifu Mpango wa Taifa wa Miaka Mitano.
2. Bajeti ya mwaka 2012/2013 haikuzingatia viwango na mgawanyo wa fedha kwa mujibu wa Mpango wa Taifa.
Kambi ya Upinzani inaitaka Tume ya Mipango, ambayo mwenyekiti wake ni Rais, kurekebisha dosari hizi ili kuwezesha maendeleo ya haraka ya Taifa letu.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo kwa niaba ya Kambi ya Upinzani naomba kuwasilisha.
……………………………………………………
Prof. Kulikoyela Kanalwanda Kahigi (Mb)
Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani Ofisi ya Rais,
02/07/2012
 
Mkuu hebu edit hii hotuba fasta. Unatuharibia computer zetu. Ya kwangu ime-stuck.
 
Back
Top Bottom