Hotuba ya Kikwete ya Kulifungua Bunge la 10

Dickson Ng'hily

JF-Expert Member
Oct 22, 2010
451
485
HOTUBA YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE, AKIFUNGUA RASMI BUNGE JIPYA LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, DODOMA, 18 NOVEMBA 2010

Mheshimiwa Spika,

Napenda nianze kwa kukupongeza wewe kwa kuchaguliwa kuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hongera sana!

Hakuna asiyejua kwamba unao ujuzi, uwezo, uzoefu, na umahiri wa kutosha wa kutekeleza majukumu ya Spika wa Bunge letu. Nafarijika sana kwamba sisi katika Chama cha Mapinduzi tumeijengea heshima na kuitengenezea historia nchi yetu kwa kuiwezesha kuwa na Spika mwanamke wa kwanza tangu uhuru. Haukuwa uamuzi rahisi. Lakini tulipoona wamejitokeza wanawake watatu wazito wenye uwezo kushika Uspika kuomba nafasi hiyi kupitia Chama chetu, tukasema fursa ndio hii sasa ya kuondoa dhana kwamba mwanamke hawezi
kukabidhiwa kuongoza mhimili wa dola. Kwa uamuzi huu, tumepiga hatua kujenga fahari ya mwanamke katika nchi yetu na tumeonyesha kwa vitendo kwamba wanawake ni sawa kabisa na wanaume kwa uwezo. Hii sio mara ya kwanza kwa CCM kufanya uamuzi wa aina hii na haitakuwa mara ya mwisho.

Napenda kuchukua fursa hii kumshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Samuel Sitta kwa kazi nzuri aliyoifanya ya kuliongoza Bunge la Tisa. Nina imani kabisa kwamba kazi nzuri aliyoifanya itaendelezwa na Spika mpya ambaye alipata fursa ya kufanya kazi chini yake, akiwa Naibu wake, kwa miaka mitano. Binafsi namuahidi Spika wetu mpya ushirikiano wangu, pamoja na ushirikiano wa Serikali yangu nitakayoiunda.

Mheshimiwa Spika,

Napenda pia kutoa pongezi kwenu nyote, Waheshimiwa Wabunge, kwa kuaminiwa na wananchi na kuchaguliwa kuwa wawakilishi wao katika Bunge hili.

Hiyo ni heshima kubwa mliyopewa. Nawatakieni kila la heri mnapojiandaa hivi sasa kuonyesha kuwa kweli mmestahiki heshima hiyo.

Wajibu wa Wapinzani Bungeni

Nawapongeza Wabunge wa vyama vya upinzani. Chama cha Mapinduzi ni chama kikubwa na chenye nguvu kuliko vyote nchini. Ni kazi kubwa kweli kupambana nacho. Hivyo, mnastahili pongezi za pekee kwa kuongeza idadi ya wabunge. Imani yangu ni kwamba wingi wenu tafsiri yake ni dhamana zaidi na mchango zaidi kwenye kusukuma mbele maendeleo ya nchi yetu na sio fursa kubwa zaidi ya kulaumu, kushambulia, kubeza, na kupambana. Watanzania wenzetu wamewachagua wakiamini hali zao za maisha zitabadilika na kuwa bora zaidi. Uhodari wenu hautapimwa kwa kauli kali au kutema cheche hapa Bungeni wala kwa umahiri wa kuainisha matatizo ya nchi yetu. Tutapimwa kwa mchango wetu katika kuboresha hali za maisha ya wapiga kura wetu: wapate huduma ya afya, maji, umeme, barabara, na huduma nyinginezo, na kipato chao kiongezeke. Hilo ndilo wananchi wanalotarajia.

Mheshimiwa Spika,

Serikali ndio inayopanga mipango ya maendeleo na kuitekeleza. Wajibu huo tutautimiza kwa umakini katika kila kona ya nchini yetu, bila kubagua kama wananchi wa eneo fulani wamechagua chama cha upinzani au la. Wananchi wote hata kwenye majimbo ya wapinzani ni watu wa Serikali na wako chini ya utawala wa Serikali. Tunachotegemea kutoka kwenu ni ushirikiano na ushauri kwa Serikali ili tupange mipango hiyo vizuri na kuitekeleza kwa ufanisi.

Sisi katika CCM tunawashukuru ndugu zetu hawa wa vyama vya upinzani kwa kutupa changamoto katika uchaguzi huu ulioisha. Tumejifunza tumeteleza wapi, na tunajipanga kuvirudisha viti tulivyovipoteza na kuongeza vingine zaidi. Tunawashukuru kwamba mmetushtua mapema na kutupa fursa ya kujipanga upya wakati bado tukiwa ni Chama tawala.

Mheshimiwa Spika,

Narudia tena shukrani zangu kwa wananchi kwa kunirejesha mimi na Chama Cha Mapinduzi katika uongozi wa nchi yetu. Maelezo yake ni ya aina tatu tu.
Kwanza, ni kwamba Watanzania wanaienzi na kuithamini rekodi na historia ya Chama chetu katika dhamana ya uongozi wa nchi yetu.
Pili, wameridhika na kazi tuliyoifanya na mafanikio tuliyoyapata katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.
Na, tatu, wamekubaliana na hoja tulizozitoa kwenye kampeni kote nchini, na wana imani, juu ya mipango yetu ya kukabiliana na changamoto za nchi yetu na kusukuma gurudumu la maendeleo kama tulivyoahidi kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka huu.

Nawashukuru wana-CCM wenzangu wote, kuanzia viongozi wa kitaifa hadi kwenye mashina, na wapenzi na washabiki wa CCM kote nchini kwa kuutafuta na kuuwezesha ushindi tulioupata. Kazi yetu mbele yetu ni kutimiza ahadi zetu kwa Watanzania na kufanya tathmini ya kina ya uchaguzi huu na kujipanga upya, kujiimarisha upya kwa kujenga upya umoja, upendo na mshikamano ndani ya Chama chetu ili tuendelee kukamata dola katika chaguzi zijazo. Mbio za kusaka ushindi wa mwaka 2015 tunazianza sasa.

Mheshimiwa Spika,

Nawashukuru Wabunge kwa uteuzi wangu wa Waziri Mkuu, Mheshimiwa.......... Wengi wenu mnamjua vizuri. Naomba Waheshimiwa Wabunge mumpe ushirikiano mkubwa akiwa Kiongozi wa Shughuli za Serikali Bungeni. Naomba pia muwape ushirikiano unaostahili Mawaziri nitakaowateua. Nisaidieni kuwashtua watakapokuwa wanasuasua, lakini pia wapongezeni wakifanya vizuri.






Uchaguzi Umekwisha

Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge,

Uchaguzi Mkuu sasa umekwisha. Sasa ni wakati wa kufanya kazi tulizotumwa na wananchi. Wajibu wa wanasiasa wote, ndani na nje ya ukumbi huu, ni kuacha malumbano yasiyokuwa na msingi, ambayo wananchi walio wengi wanaona hayana tija kwao, na kufanya kazi wanazotazamiwa kuzifanya. Nchi yetu ni maskini. Baada ya muda mrefu wa kampeni, wananchi wamekinai malumbano ya kisiasa. Sasa wanataka tufanye kazi ya kumaliza matatizo yanayowakabili na kuwaletea maisha bora.

Bahati nzuri Serikali yangu iliyopita imeweka mazingira mazuri ya kuongeza kasi kwenye safari ya kuelekea kwenye maisha bora. Dhamira yetu, sasa kama ilivyokuwa huko nyuma, ni kuwaletea maisha bora Watanzania. Haijabadilika na haitabadilika. Tumepiga hatua kubwa lakini kwasababu tunaanzia kutokea kiwango cha chini sana cha umaskini, itachukua muda
matunda ya kazi yetu kuanza kuonekana. Lakini lazima tuendelee na safari hiyo kwa ari zaidi, nguvu zaidi na kasi zaidi.

Vipaumbele 11

Mheshimiwa Spika,

Katika ujumla wake, katika kutekeleza majukumu yake, na katika kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM mwaka 2010, Serikali nitakayounda itasukumwa na vipaumbele 11:

1. Kuhakikisha kwamba nchi yetu inaendelea kuwa na umoja, amani na usalama, na Muungano wetu unaendelea kuimarika.

2. Kujenga misingi ya uchumi wa kisasa wa Taifa linalojitegemea kwa kuchukua hatua madhubuti za kuharakisha zaidi mapinduzi ya kilimo, ufugaji, uvuvi na viwanda. Nataka tuanze safari ya kuelekea kuwa taifa la uchumi wa kati, ambalo viwanda ndio mhimili mkuu.

3. Kuongeza jitihada na mipango zaidi ya kuwawezesha kiuchumi wananchi hasa wa hali ya chini, ili waweze kushiriki na kunufaika na uchumi wetu unaokua. Lakini vilevile tutaweka mkazo katika kulitambua na kuliwezesha kwa namna yake kundi la wajasiriamali wa tabaka la kati ili waweze kushiriki katika uwekezaji mkubwa katika nchi yetu.

4. Kutumia fursa ya kijiografia ya nchi yetu kwa kuifanya lango kuu la biashara na usafirishaji kwa nchi za Afrika ya Mashariki, Kusini na Kati, hasa kwa kuimarisha ufanisi wa reli na bandari zetu.

5. Kuongeza jitihada za kuhakikisha Taifa letu linanufaika zaidi na rasilimali za asili za nchi yetu kuanzia madini, misitu, wanyamapori hadi vivutio mbalimbali vya utalii.

6. Kuweka mkazo sasa kwenye kuboresha elimu ya msingi na sekondari, na kupanua elimu ya ufundi na elimu ya juu, hasa katika masomo ya sayansi.

7. Kuongeza jitihada za kupanua na kuboresha huduma muhimu za kijamii hasa huduma za afya na maji, na huduma za kiuchumi hasa umeme, miundombinu ya usafirishaji na mawasiliano na huduma ya fedha.

8. Kuimarisha utawala bora, utawala wa sheria, na demokrasia nchini, hasa kwa kuongeza kasi ya mapambano dhidi ya rushwa, matumizi mabaya ya madaraka, na ubadhirifu wa mali ya umma; na kuendelea kuviwezesha kirasilimali, kitaasisi/kimuundo na kisheria vyombo vya kutoa na kusimamia haki nchini;

9. Kuipa dola na vyombo vyake husika uwezo mkubwa zaidi wa kupanga mipango ya uchumi na kusimamia uchumi wa nchi kwa ufanisi, bila kuingilia sekta binafsi, ili kulinda maslahi ya nchi yetu na watu wake.

10. Kulinda mafanikio tuliyoyapata katika nyanja zote tangu uhuru wa nchi yetu, ikiwemo katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, na kukamilisha yale tuliyoyaahidi mwaka 2005 ambayo, kwa sababu moja au nyingine, hatukuweza kuyakamilisha katika miaka hii mitano.

11. Kuendelea kuimarisha mahusiano mazuri yaliyopo baina ya nchi yetu na majirani zetu, na mataifa mengine duniani, pamoja na taasisi mbalimbali za kimataifa, na kuendelea kutafuta marafiki wapya kwa manufaa ya nchi yetu.

Mheshimiwa Spika,

Amani, Umoja, Ulinzi na Usalama

Katika miaka mitano iliyopita, tumefanikiwa kudumisha amani na utulivu wa nchi yetu na umoja baina ya Watanzania wote na kati ya pande mbili za Muungano wetu. Jukumu la kwanza la Serikali nitakayoiunda ni kuhakikisha kuwa Tanzania inaendelea kuwa nchi moja, watu wake wanabakia wamoja, na amani na utulivu unaendelea kutawala.

Hatari ya Uchaguzi 2010 kwa Umoja

Naomba nirudie kuelezea kusononeshwa na kusikitishwa kwangu na baadhi ya
viongozi wa dini na wanasiasa waliowataka Watanzania wawachague watu kwa dini zao. Jambo hili linapaswa kukemewa kwa nguvu zote na kila mmoja wetu. Nawaomba viongozi wa kisiasa ambao vitendo hivi vya kibaguzi vilifanywa na vinafanywa kwa niaba yao au kwa kuwanufaisha wao wasikae kimya. Watoe kauli kukemea uovu huu. Hapa nchini Watanzania wenye dini mbalimbali wanafanya kazi pamoja, wanasaidiana, wanashirikiana katika shughuli mbalimbali za kijamii bila kujali dini zao, wanaishi pamoja.

Tusikubali zipandikizwe mbegu za chuki baina ya Watanzania.

Nawapongeza na kuwashukuru Watanzania kwa kukataa kugawanywa kwa misingi ya dini katika uchaguzi huu. Narudia wito wangu kwamba sasa viongozi wote wa siasa, wa dini, wanahabari, viongozi wa kimila, kijamii na wengineo wanaoipenda nchi yetu, tuungane kuziba nyufa na kutibu majeraha yaliyoletwa na uchaguzi huu.

Muungano

Mheshimiwa Spika,

Napenda tena kuchukua fursa hii kuwapongeza Wazanzibari wote kwa kufanikisha muafaka wa kihistoria, uliowezesha kufanyika uchaguzi kwa amani na utulivu na hatimaye kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Dhamira yangu ya kumaliza mpasuko wa kisiasa Zanzibar niliyoitoa siku ya kuzindua Bunge la Tisa tarehe 30 Disemba 2005, imetimia! Tunawatakia kila heri watu wa Zanzibar waendelee kudumisha umoja huo kwa manufaa ya Wazanzibari wote.

Hali mpya ya kisiasa Zanzibar inajenga mazingira mazuri ya kuzidisha maradufu jitihada zetu za kuimarisha Muungano wetu ili uendelee kuzinufaisha pande zote mbili za Muungano. Tutaimarisha taasisi na taratibu za kushughulikia matatizo ya Muungano ili ziweze kutekeleza wajibu na majukumu yake kwa ufanisi zaidi.

Usalama wa Raia

Mheshimiwa Spika;

Katika miaka mitano iliyopita, tumejitahidi kuimarisha hali ya usalama wa raia. Uhalifu hata hivyo bado upo. Katika miaka mitano ijayo tutaendelea na wembe huo huo. Tutaendelea kuviimarisha vyombo vyetu vya ulinzi na usalama kifedha, rasimali watu, vifaa na mafunzo ili kuviongezea uwezo na ufanisi wa kutimiza majukumu ya ulinzi wa mipaka yetu na usalama wa raia na mali zao.

Kujenga Misingi ya Uchumi wa Kisasa wa Taifa Linalojitegemea

Mheshimiwa Spika;

Azma yetu kuu ni kujenga uchumi wa kisasa wa Taifa linalojitegemea na uchumi unaowanufaisha walio wengi. Hili ndilo jukumu letu la msingi katika kipindi cha miaka mitano ijayo. Katika kipindi hiki, tutaendeleza uchumi wa soko kwa kutengeneza mazingira mazuri kwa ajili ya kuongeza uzalishaji, ukuaji wa uchumi na ustawi wa biashara na kuwekeza katika sekta muhimu za uchumi kama vile miundombinu, huduma za kiuchumi na huduma za kijamii.

Tutahakikisha pia viashiria vya afya ya uchumi mkuu (macroeconomics indicators) vinabaki katika hali imari. Lengo kuu ni kuongeza pato la wastani la kila Mtanzania na kupunguza umaskini.


Kuleta Mapinduzi ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi

Kilimo

Mheshimiwa Spika,

Watanzania wengi bado wanategemea kilimo kwa maisha yao. Katika miaka mitano iliyopita, tumedhihirisha dhamira yetu ya dhati ya kuleta mapinduzi ya kilimo nchini. Katika miaka mitano ijayo, tutaongeza kasi ya kutekeleza Programu ya Maendeleo ya sekta ya Kilimo*, (ASDP), pamoja na mkakati wa Kilimo Kwanza. Tutaendelea kuongeza bajeti ya kilimo na kuhakikisha mambo ya msingi katika kuleta mapinduzi ya kilimo yanazingatiwa.

Mheshimiwa Spika,

Pamoja na yote haya, pia tutaanza kutekeleza mkakati wa kuanzisha Ukanda wa Kusini ya Tanzania wa Kukuza Kilimo (Southern Agricultural Growth Corridor of Tanzania (SAGCOT) utakaohusihsa mikoa ya Rukwa, Mbeya, Iringa, na Morogoro. Utekelezaji wa Mpango huu utaiwezesha Tanzania kuwa ghala la Chakula katika ukanda wa huu wa Afrika.

Mifugo

Mheshimiwa Spika,

Wafugaji hatutawaacha nyuma. Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita tumechukua hatua madhubuti za kuboresha mifugo kwa kujenga majosho, malambo, kuimarisha uhamilishaji, kuongeza madume bora, kutoa dawa za ruzuku, na mambo mengineyo.

Katika miaka mitano ijayo tutatekeleza Programu Kabambe ya Maendeleo ya Mifugo na Ufugaji. Programu hii itahusisha uendelezaji wa maeneo ya malisho, uchimbaji na ujengaji wa malambo, mabwawa, majosho na huduma za ugani kama vile wataalam, madawa na vifaa ili wafugaji wetu waondokane na ufugaji wa kuhamahama.

Uvuvi

Tunataka kuelekeza nguvu zetu pia katika kuanza safari ya kuleta mapinduzi ya uvuvi nchini ili kuwaongezea wavuvi kipato, lishe bora na kuiwezesha sekta hiyo kuchangia zaidi kwenye pato la taifa. Tutabuni na kutekeleza Mpango wa Maendeleo wa Sekta ya Uvuvi kwa lengo la kuhimiza matumizi ya zana na maarifa ya kisasa katika uvuvi na ufugaji wa samaki nchini ili uvuvi wetu uwe endelevu na wenye tija kubwa.

Kuleta Mapinduzi ya Viwanda

Mheshimiwa Spika;

Nchi nyingi zilizoendelea duniani zimefanikiwa kupata maendeleo hayo kutokana na mapinduzi ya viwanda.

Katika miaka mitano ijayo dhamira yetu ni kuongeza na kuvutia viwanda vitakavyosindika mazao na kutumia madini kutengeneza bidhaa zenye ubora na viwango vya kimataifa. Tumedhamiria pia kutumia madini yetu kuanzisha viwanda vikubwa (heavy industries) kama vile kutengeneza bidhaa zitokanazo na chuma hapa hapa nchini; mbolea itokanayo na gesi asilia na madini ya fosfati; saruji; na viwanda vya kuongeza thamani vitu vitokanavyo na madini ya kung’aa kama dhahabu na Tanzanite.

Tutaendelea kuimarisha na kutenga maeneo zaidi ya viwanda vitakavyozalisha na kuuza nje (EPZ/SEZ). Maeneo haya yatapunguza gharama za uzalishaji na kuhakikisha kuwa miundombinu na huduma nyingine za kiuchumi zinapatikana pasipo matatizo na hivyo kuchochea maendeleo ya viwanda.

Kuongeza Jitihada na Mipango ya Kuwawezesha

Wananchi Kiuchumi

Mheshimiwa Spika;

Katika kujenga uchumi wa nchi yetu, hatutafanikiwa bila kuwawezesha wananchi na sekta binafsi kushiriki kikamilifu. Vilevile, uchumi wetu unaokua lazima uwashirikishe na uwanufaishe wananchi walio wengi.

Katika miaka mitano iliyopita tulifanya jitihada kubwa ya uwezeshaji wa wananchi kwa kuanzisha mifuko na programu mbalimbali za mikopo. Matokeo yake tumeshudia kuongezeka kwa SACCOS nyingi nchini na mikopo itolewayo.

Katika miaka mitano ijayo, tutaongeza fedha zaidi kwa ajili ya mikopo ya wajasiriamali, lakini pia tutahakikisha kwamba mikopo hii inawafikia na kuwanufaisha watu wengi zaidi kote mijini na vijijini.

Tutaongeza pia jitihada za kuwajali vijana wetu wanaozunguka mijini kutafuta riziki. Kwanza tutawajengea majengo ya kuendesha shughuli zao wafanyabiashara wadogo (Machinga Complex). Tutaongeza majengo mapya Dar es Salaam na baadaye tutaendelea na miji mingine mkuu hatua kwa hatua. Pili, tutawasihi wajiunge kwenye vikundi ili tuweze kuwatambua na kuwakopesha mitaji.

Lakini tutafanya zaidi ya kuwawezesha wajasiriamali wadogo wadogo. Tunataka sasa tulenge kuwawezesha wafanyabiashara wa tabaka la kati ili waweze kushiriki katika uwekezaji mkubwa katika nchi yetu. Kwa ajili hiyo, tutaimarisha mifuko mbalimbali ya uwezeshaji na tutaijengea uwezo zaidi Benki ya Raslimali na kuanzisha Benki ya Kilimo ili ziweze kutoa mikopo kwa wananchi wengi zaidi.

Kutumia Fursa ya Kijiografia Kuifanya Tanzania

Lango Kuu la Biashara

Mheshimiwa Spika;

Nchi yetu imejaaliwa kuwa na rasilimali nyingi. Lakini ipo rasilimaji moja muhimu ambayo hatujaitumia ipasavyo. Nayo ni jiografia ya nchi yetu. Tanzania imepakana na nchi za Maziwa Makuu na Afrika ya Kati, ambazo zinategemea bandari na miundombinu yetu kusafirisha bidhaa zao na huduma za mawasiliano kupitia mkongo wa kimataifa na mkongo wetu.

Kwasasa, biashara ya usafirishaji (transit trade) inatuingizia fedha nyingi zaidi kuliko kilimo. Tunataka tunufaike zaidi na biashara hii. Lakini tunaweza tu kunufaisha kama bandari zetu zitakuwa na ufanisi wa hali ya juu na reli na barabara zetu zitakuwa kwenye hali nzuri.

Bandari:

Mheshimiwa Spika;

Ukweli ni kwamba uwezo na ufanisi wa Bandari ya Dar es Salaam ni mdogo ukilinganisha na mahitaji ya sasa. Katika miaka mitano iliyopita, tulianza kazi ya kukabiliana na changamoto za ufanisi wa bandari yetu. Lakini dawa kamili ipo kwenye kuipanua bandari yenyewe na kujenga nyingine. Katika miaka mitano ijayo, kwa kushirikiana na wawekezaji katika sekta binafsi, tunataka tuanze mchakato wa ujenzi wa bandari nyingine eneo la Mwambani/Tanga na Bagamoyo, ambayo pia itahudumia maeneo ya EPZ/SEZ.

Tutafanya pia upanuzi na uboreshaji wa Bandari ya Mtwara. na kuanza mikakati ya Tutaboresha pia bandari zetu za Kigoma, Mbamba Bay, Kasanga, Mwanza, Musoma na Nansio na kuimarisha usafiri kwenye maziwa yetu ili tuweze kuhudumia wananchi wetu na nchi jirani kwa usafiri na usafirishaji wa uhakika.

Reli:

Mheshimiwa Spika;

Reli zetu bado haziko katika hali nzuri. Reli yetu ya Kati ni chakavu na ina viwango duni kwa sababu haijaboreshwa miaka mingi. Reli ya TAZARA pia inahitaji ukarabati na ununuzi wa injini na mabehewa ya kutosha. Katika miaka mitano iliyopita, tumehangaika sana na kurekebisha matatizo ya reli yetu. Naomba nikiri kwamba hatukufanikiwa kama nilivyotarajia. Tumepania kwamba, katika miaka mitano ijayo, tuchukue hatua sahihi kwa kuwa sasa tumejifunza.
Malengo yetu katika miaka mitano ijayo ni kukarabati reli ya TAZARA na kuboresha Reli ya Kati ili ifikie viwango vya kimataifa (standard gauge) kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza na Kigoma na kujenga reli mpya kutoka Isaka hadi Kigali, Rwanda na Bujumbura, Burundi.

Barabara:

Mheshimiwa Spika;

Katika miaka mitano iliyopita tumejitahidi sana kujenga kwa kiwango cha lami barabara zinazounganisha mikoa na zinazounganisha nchi yetu na nchi jirani. Kazi hiyo imefanyika kwa bidii sana kwa kiasi kikubwa tukitumia fedha za ndani za bajeti. Katika miaka mitano ijayo Ilani ya Uchaguzi ya CCM inatuagiza kumalizia miradi ya ujenzi wa barabara za lami zenye urefu wa kilometa 2,502.6 na kuanza miradi ya ujenzi mpya na ukarabati kwa kiwango cha lami barabara zenye urefu wa kilometa 5,285. Pia tutafanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa miradi ya barabara zenye urefu wa kilometa 3,202. Tutaendelea kuimarisha Mfuko wa Barabara ili tuweze kujenga na kukarabati barabara za vijijini ili ziweze kupitika mwaka mzima.

Tanzania kama Kitovu (Hub) cha Biashara

Mheshimiwa Spika;

Kwa kuboresha njia za mawasiliano na nchi zinazotutegemea kijiografia, hatutaishia kwenye kupitisha tu bidhaa zinazozalishwa nje, bali tutaweza pia kuuza bidhaa zinazozalishwa Tanzania kwenye nchi za Maziwa Makuu, EAC na SADC. Nafasi yetu kijiografia vilevile inatupa upendeleo katika kuvutia viwanda na kuwa kitovu (hub) cha kuuza bidhaa zetu mbalimbali
tunazozalisha na zile ambazo tunanunua na kisha kuziuza tena nje (re-export ).

Kuhakikisha kuwa Taifa Letu Linanufaika zaidi na

Raslimali za Asili

Mheshimiwa Spika;

Kama nilivyosema, Tanzania imejaliwa kuwa na raslimali nyingi za asili. Tuna madini ya aina mbalimbali na rasimali-asili nyingi, hasa za misitu. Hizi ni rasilimali ambazo ni lazima tuzitumie vizuri ili nchi yetu inufaike nazo. Katika miaka mitano ijayo, tunataka kuziba kila mwanya unaofanya tusinufaike zaidi na rasilimali za nchi yetu. Tutazilinda maliasili zetu na kuhakikisha hazivunwi hovyo, na hata pale tunapoamua kuvuna, basi taifa linufaike zaidi.

Madini

Katika hotuba yangu ya kuzindua Bunge la Tisa tarehe 30 Disemba 2005 niliahidi kufanya jitihada kuhakikisha kwamba nchi yetu inanufaika zaidi na utajiri wa madini tuliojaliwa na Mwenyezi Mungu. Kazi hiyo tuliianza katika kipindi cha miaka mitano iliyopita. Tuliandaa Sera ya Madini ya 2009, tulitunga Sheria mpya ya Madini ya 2010, kuanzisha Wakala wa Ukaguzi wa Madini, na kuanza kutenga maeneo kwa ajili ya wachimbaji wadogo na kuwapatia leseni ili nao watambulike. Pia, tumehamasisha wachimbaji wadogo waunde
vikundi vya ushirika ili tuweze kuwakopesha mitaji, vifaa na masoko. Haya yote yamesaidia kuifanya nchi yetu inufaike na madini tuliyonayo. Lakini bado tunaweza kunufaika zaidi.

Katika miaka mitano ijayo, tutaendelea kuimarisha Shirika la Taifa la Madini (STAMICO) ili Serikali nayo iweze kushiriki katika umiliki wa migodi mikubwa na ya kati na hivyo kunufaika zaidi. Tutaendelea kutenga maeneo kwa ajili ya wachimbaji wadogo na kuwaendeleza. Ili kuongeza mapato kutoka sekta ya Madini, tutaimarisha uwezo wa Serikali katika usimamizi wa madini, kuvutia wawekezaji katika uongezaji thamani madini.

Kuboresha Huduma za Jamii na Huduma za Kiuchumi

Mheshimiwa Spika;

Serikali iliyo na dhamira ya kweli ya kuwaletea maisha bora wananchi ni ile inayowekeza kwenye huduma za kijamii na kiuchumi. Nafarijika na mafanikio ambayo tumeyapata katika kipindi cha miaka mitano iliyopita licha ya changamoto ambazo bado zipo.

Elimu

Mheshimiwa Spika,

Katika Sekta ya elimu, tutaendelea kupanua fursa za elimu kwa ngazi zote lakini pia sasa kuweka mkazo kuboresha elimu inayotolewa kwa katika ngazi zote.

Tumefanya upanuzi mkubwa hasa wa elimu ya sekondari na elimu ya juu, na zipo changamoto zilizotokana na mafanikio haya. Mojawapo ni changamoto ya upungufu wa walimu. Tutaendelea kupanua na kuimarisha mafunzo ya ualimu kwa ngazi zote. Dhamira yetu ni kumaliza kabisa tatizo la uhaba wa walimu nchini ndani ya miaka hii mitano.

Licha ya kuongeza walimu, tutajitahidi kuboresha maslahi yao kila mwaka. Tutaendelea kulipa madeni yao na tutahakikisha kwamba hatulimbikizi tena. Kwa upande wa vitabu, tutaendelea kununua na kusambaza vitabu vya kiada kwa lengo la kufikia uwiano wa mwanafunzi mmoja kitabu kimoja ifikapo 2015. Kwa kushirikiana na wananchi tumedhamiria kujenga Maabara za Sayansi kwa sekondari zetu zote na kujenga hosteli.

Vilevile, tutabuni na kutekeleza Mpango Kabambe wa Ujenzi wa Nyumba za Walimu kwa gharama isiyopungua shilingi bilioni 250 katika miaka mitano ijayo. Aidha, tumedhamiria kuanza safari ya kutimiza azma yetu ya kuwa na Chuo cha Ufundi katika kila Wilaya ifikapo mwaka 2015.

Kwa upande wa Elimu ya Juu, tutaiboresha elimu yetu ya juu kupitia Mpango wetu mpya wa Maendeleo wa Elimu ya Juu tutakaoutekeleza. Dhamira yetu ni kupanua fursa za elimu ya juu na kuongeza ubora wa elimu hiyo ili ikidhi viwango na utashi wa soko la ajira nchini na kimataifa.

Vilevile, katika miaka mitano ijayo, tutakamilisha ujenzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma ili kifikie lengo lake la kuwa na wanafunzi 40,000. Lakini tunataka sasa tuanze ujenzi vyuo vikuu vingine viwili yaani Chuo Kikuu cha Kilimo cha Mwalimu Nyerere Butiama, Musoma na Chuo Kikuu cha Udaktari, yaani Chuo Kikuu cha Udakatari. Zaidi ya hapo tutakamilisha matayarisho ambayo tumeyaanza ya ujenzi wa hospitali ya kufundishia pale Mlonganzila.

Pia tutaendelea kuboresha na kukarabati miundombinu ya vyuo vyetu vikuu vingine na taasisi nyingine za Elimu ya Juu nchini.

Afya

Mheshimiwa Spika,

Katika Sekta ya Afya, tutaongeza kasi ya kutekeleza Mpango wetu wa miaka 10 wa Maendeleo ya Afya ya Msingi ili katika miaka mitano ijayo Watanzania wapate huduma ya Afya iliyo bora zaidi. Kwa kushirikiana na wananchi tumedhamiria kujenga zahanati katika kila kijiji, kituo cha afya katika kila kata na kuhakikisha kuwa kila halmashauri ya wilaya, mji,
manispaa na jiji ina hospitali yake na hospitali za mikoa zibakie kutoa huduma za rufaa kutoka hospitali za wilaya.

Natambua kwamba bado kuna tatizo la watumishi wachache katika sekta ya afya. Tutaendelea na kazi tuliyoianza ya kuongeza na kupanua vyuo vya kufundisha madaktari, wauguzi na watumishi wengine ili kuendana na upanuzi wa vituo vya kutolea huduma za afya.

Lazima pia tuendelee na tuongeze kasi ya kupambana na maradhi hasa yale yanayoua watanzania wengi kama malaria, UKIMWI, kifua kikuu, maradhi ya moyo, saratani, figo, mishipa ya fahamu, maradhi mengine yanayowasumbua Watanzania. Tumedhamiria kutokomeza malaria ifikapo 2015.

Maji

Mheshimiwa Spika,

Pamoja na juhudi kubwa tulizozifanya katika kuboresha huduma ya upatikanaji maji nchini, uhaba wa maji bado ni tatizo kubwa katika maeneo mengi nchini. Sasa tumedhamiria kulivalia njuga tatizo hili. Tunawashukuru wenzetu wa Benki ya Dunia kwa msaada wao mkubwa kwenye Sekta hii. Lakini sasa na sisi tutatia nguvu yetu kubwa zaidi.

Ukiondoa uwekezaji kwenye sekta, lipo tatizo la kupotea kwa vyanzo vya maji. Tutaielekeza Mikoa na Halmashauri zote kuendelea kuchukua hatua madhubuti za kutunza vyanzo vya maji, mabonde ya mito na usafi wa mazingira ikiwa ni pomoja na kuchukua hatua zitakazowezesha mito hiyo kuanza kutiririka tena.

Uboreshaji wa Makazi

Mheshimiwa Spika;

Watanzania wengi bado wanaishi katika makazi duni. Katika kipindi cha miaka mitano ijayo serikali itajielekeza kupambana na umaskini wa makazi. Serikali itaandaa Mpango wa Maendeleo ya Makazi wa miaka kumi utakaokeleza dhamira yetu ya kushirikiana na sekta binafsi kujenga na kuboresha makazi ya wafanyakazi na kuwahamasisha wananchi vijijini kuboresha makazi yao.

Nishati

Mheshimiwa Spika;

Pamoja na kupambana na changamoto nyingi katika kipindi cha miaka mitano ikiwemo changamoto ya ukame, tumefanya juhudi kubwa katika uzalishaji na usambazaji wa umeme nchini. Tumepunguza utegemezi mkubwa kwa umeme wa maji. Tunategemea katika miaka mitano ijayo kuongeza megawati 640 za umeme kwenye gridi ya Taifa. Tutaendelea na jitihada za kuunganisha mikoa yote kwenye gridi ya taifa na kupeleke umeme kwenye makao makuu ya wilaya zote nchini. Aidha, tutaendelea kuliimarisha shirika la TANESCO na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ili uzalishaji na usambazaji wa umeme mijini na vijijini ufanyike kwa kasi zaidi. Tumedhamiria katika miaka mitano ijayo kuongeza idadi ya Watanzania wanaopata umeme kutoka asilimia 14 hadi asilimia 30.

Utawala Bora

Mheshimiwa Spika,

Katika miaka mitano iliyopita, tumefanya mengi katika kuimarisha utawala bora, utawala wa sheria, na demokrasia nchini. Katika miaka mitano ijayo, tutafanya zaidi.

Tutakuwa wakali zaidi katika kudhibiti nidhamu ya watumishi wa umma. Tutawataka watumishi wa umma pamoja na viongozi katika Wizara, Halmashauri na Idara na Taasisi za Serikali kuhakikisha maamuzi yanafanyika kwa haraka na utekelezaji wa kazi za umma unapewa msukumo na kasi mpya. Juu ya hili, tutaongeza uwajibikaji katika matumizi ya raslimali za umma.

Taasisi zetu za kupambana na maovu katika jamii, hasa TAKUKURU na Polisi tutaendelea kuziimarisha ili zitimize majukumu yao vizuri.

Tutaendelea kuwateua Majaji wapya, kuajiri Mahakimu wapya, Waendesha Mashtaka na kukamilisha mchakato wa kutenganisha kazi ya upelelezi na kuendesha mashtaka. Tutaendendelea kujenga majengo mapya ya Mahakama katika ngazi zote na ofisi za waendesha mashtaka.

Tatizo sugu la uwezo wetu wa kusimamia mikataba tutalipatia ufumbuzi. Tutaendelea kutoa mafunzo kwa wanasheria wa Serikali pamoja na maofisa wa serikali katika sekta mbalimbali ili wawe mahiri zaidi na makini katika kujadili, kufunga na kusimamia mikataba ya Serikali.

Kuimarisha Demokrasia

Mheshimiwa Spika;

Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita tumeshuhudia kukua kwa demokrasia kwa kasi kubwa. Tutaendelea kupanua na kuimarisha uhuru wa wananchi, vyombo vya habari, asasi za kiraia na mtu mmoja mmoja kujieleza na kutoa maoni.

Tutaendelea kuviimarisha vyombo vyetu vya uwakilishi wa wananchi yaani Bunge na Mabaraza ya Halmashauri. Dhamira yetu ni kuvijengea uwezo mkubwa zaidi wa kujenga hoja zenye manufaa kwa wananchi na taifa kwa ujumla.


Tutajitahidi sana kuhakikisha kwamba dhana ya upinzani kama sehemu ya utawala wa nchi inaeleweka vyema. Hatutayafumbia macho mambo mema yatakayosemwa na wapinzani kwa sababu tu yametoka kwenye kambi ya upinzani.

Tutayapokea na kuyafanyia kazi kwa vile natambua kuwa lengo letu ni moja la kuijenga nchi yetu. Lakini pia hoja zitakazosukumwa na nguvu na mashinikizo hizo tutazikataa.

Vyombo vya Habari

Mheshimiwa Spika,

Katika miaka mitano iliyopota, tumeshuhudia kupanuka kwa uhuru wa vyombo vya habari. Mimi binafsi ni mpenzi mkubwa wa uhuru huu na ni mvumilivu sana wa mawazo tofauti. Hata hivyo nimesononeshwa sana na mwenendo wa baadhi ya vyombo vya habari.

Najua kwamba baadhi ya vyombo vya habari vikijitahidi kuwa makini na baadhi ya waandishi wakijitahidi kuwa waadilifu. Lakini sote pia hapa tunajua kwamba baadhi ya waandishi wa habari na vyombo vya habari vimetiwa mifukoni na wanasiasa, wafanyabiara na vingine vinasukuma ajenda za wamiliki wao. Hali hii imechangia kuchafua mahusiano baina ya watu na baina ya makundi katika jamii.

Jukumu la kwanza la kurekebisha hali hii ni la wanataaluma wenyewe, yaani waandishi wa habari. Mnajuana, kaeni myazungumze. Msikubali kununuliwa ili kubomoa au kujenga mtu au kundi. Lakini pia tambueni kwamba hii ni nchi yenu pia, na kumbukeni kwamba sio dhana sahihi kwamba ukiwa mwandishi wa habari basi unaweka uzalendo au utaifa wako pembeni. Kote duniani, tena hata kule kwenye uhuru mkubwa wa vyombo vya habari, bado uzalendo na utaifa unawekwa mbele na waandishi wa habari. Ukibomoa Tanzania kwa kalamu yako
hauitwi jasiri bali unaonekana kituko.

Jukumu la pili ni kwa wamiliki wa vyombo hivi na wahariri wao. Jengeni uwezo wa waandishi wenu wa habari, himizeni uadilifu katika kazi hii muhimu, na msitoe mashinikizo kwa waandishi kukiuka miiko na maadili ya taaluma.

Jukumu la tatu ni la Serikali. Serikali inaweka sheria na taratibu zinamiliki uendeshaji wa taaluma na biashara ya vyombo vya habari. Ndani ya miezi sita tutaleta Sheria mpya ya Vyombo vya Habari ambayo itazingatia haja ya kupanua uhuru wa vyombo vya habari lakini pia ambayo itatoa wajibu mkubwa zaidi kwa vyombo vya habari na waandishi kuzingatia maadili ya taaluma ya uandishi wa habari na kutoa fursa ya haraka zaidi kwa wale wanaochafuliwa na vyombo vya habari kutafuta na kupata haki katika vyombo vya sheria kwa haraka zaidi kulivyo ilivyo sasa.

Wanawake Katika Nafasi za Uongozi

Mheshimiwa Spika;

Katika Bunge lililopita niliahidi kwamba Serikali yangu itachukua hatua za kuongeza ushiriki wa wanawake katika nafasi mbalimbali za uongozi.

Kazi hiyo tumeifanya vizuri. Bunge hili ndio la kwanza tangu uhuru lenye asilimia kubwa zaidi ya wanawake. Kazi hii tutaendelea nayo. Sote tushirikiane kuwajengea uwezo wanawake kushiriki na kushinda katika chaguzi mbalimbali. Natoa wito kwa asasi zinazohusika na harakati za wanawake pamoja na vyama vya siasa kubuni mikakati itakayowawezesha wanawake kugombea, kuteuliwa na kushinda uchaguzi.

Mapambano Dhidi ya Rushwa

Mheshimiwa Spika;

Katika miaka mitano iliyopita tumefanya kazi kubwa ya kupambana na rushwa na matumizi mabaya ya madaraka. Tumebuni na kuutekeleza mkakati wa kupambana na rushwa, tumetunga sheria mpya na kali zaidi ya kuzuia na kupambana na rushwa, tumeanzisha taasisi mpya ya kupambana na rushwa (TAKUKURU) na kuipa uwezo mkubwa zaidi, tumewachukulia hatua kali za kuwapeleka mahakamani watu wote waliodhihirika kujihusisha na vitendo vya rushwa, bila kujali nyadhifa au nafasi zao katika jamii. Tutaendelea kukaza kamba.

Lakini kama mjuavyo, mapambano dhidi ya rushwa hayawezi kufanikiwa bila jamii kuichukia kwanza rushwa yenyewe. Katika hotuba yangu ya uzinduzi wa Bunge lililopita, niliwahimiza na kuwachochea Watanzania waichukie rushwa. Nafurahi kwamba lengo letu limetia. Watanzania sasa wamehamasika kuichukia rushwa. Naomba tuendelee hivyo hivyo. Na tuzisaidie taasisi zetu za kupambana na rushwa kufanya kazi zake.

Dola kuwa na Uwezo Mkubwa wa Kupanga na Kusimamia Mipango ya Uchumi

Mheshimiwa Spika;

Katika dunia ya sasa ya utandawazi na uchumi wa soko huria, usimamizi wa karibu wa Serikali ni muhimu ili kuhakikisha kuwa shughuli za kiuchumi zinaendeshwa bila ghiliba, dhuluma na udanganyifu. Majukumu ya Serikali ni pamoja na kuandaa sera, kutunga sheria na kudhibiti mwenendo wa sekta binafsi ili kuhakikisha ushindani wa haki. Ili kufanikisha haya, tunahitaji Serikali yenye nguvu, inayoweza kudhibiti sekta binafsi bila kuiathiri sekta
hiyo kiutendaji. Pia ni muhimu Serikali iwe na mpango madhubuti wa kupanga, kusimamia utekelezaji na kufanya tathmini ya utekelezaji na ufikiaji malengo tuliyojiwekea.

Tumeunda Tume ya Mipango itakayotusaidia siyo tu kuratibu utekelezaji wa ajenda ya miaka mitano bali pia kuweza kuratibu hatua tunazohitaji kukamilisha katika kipindi hiki ili kukamilisha vipindi viwili vya miaka mitano itakayofuata. Tunatarajia pia kuwa Tume hii itaweza kuwa chombo kikuu cha kufanya tathmini ya hatua tutakazopiga kila mwaka na matokeo yake katika maeneo ya vipaumbele ili kuchochea utekelezaji wa ajenda hii pamoja
na ajenda ya muda mrefu. Majukumu hayo ya Tume ya Mipango yatasaidia sana kuhakikisha kuwa Serikali inasimamia kwa karibu maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini.

Michezo na Utamaduni

Katika miaka mitano iliyopita tumejitahidi kuboresha mchezo wa mpira wa miguu. Bado hatujafikia kiwango cha juu lakini mwanga unaonekana. Sasa tutaelekeza nguvu zetu katika michezo mingine hususan riadha, ngumi na netiboli. Nimetoa mchango wangu na nitaendelea kutoa mchango wangu katika maendeleo ya michezo ya aina yote nchini.

Vilevile, katika kipindi hiki tutaendelea kuunga mkono juhudi za wasanii na hasa katika kuhakikisha kuwa wanapata malipo stahiki kwa jasho lao.

Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa

Mheshimiwa Spika,

Tutaendelea kuisimamia Sera yetu ya Mambo ya Nje inayotilia mkazo diplomasia ya uchumi ili kuimarisha uhusiano wetu wa kiuchumi na kisiasa na mataifa mengine duniani. Tunataka nchi rafiki na mashirika ya kikanda na kimataifa yaendelee kuunga mkono juhudi zetu za kujiletea maendeleo.

Na kwakweli nitakuwa mwizi wa fadhila kama sitazishukuru nchi wahisani na mashirika ya fedha ya kimataifa yaliyotuunga mkono katika jitihada zetu za kuleta maendeleo katika miaka mitano iliyopita. Napenda niwahakikishie kuwa tutaendelea kuwa wazi kwao, na kushirikiana nao, ili fedha zinazopatika zilete manufaa makubwa zaidi. Wakati tunaendelea na jitihada za kupunguza utegemezi kwa wahisani, tutaendelea kuhitaji sana msaada wao katika kipindi hiki cha miaka mitano ijayo.

Mheshimiwa Spika,

Tutaendelea kushiriki kikamilifu katika kukuza ushirikiano wa Afrika Mashariki (EAC), SADC na Umoja wa Afrika (AU). Tutaendelea kuimarisha Utengamano wa Afrika Mashariki kwa kutekeleza Itifaki ya Soko la Pamoja lililoanza rasmi tarehe 1 Julai 2010 na kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kuanzisha Umoja wa Sarafu. Aidha, tutaendelea kuwahamasisha Watanzania wenzetu hasa wafanyabiashara kuchangamkia fursa zitokanazo na kupanuka na
kuimarika kwa utengamano wa Afrika Mashariki na ushirikiano wa SADC.

Tutaendelea kudumisha urafiki na ujirani mwema na mataifa yanayotuzunguka na kutoa mchango wetu katika masuala ya amani na maendeleo kwenye Ukanda wetu, barani Afrika na duniani kwa ujumla. Tutaendelea kushiriki katika shughuli mbalimbali za Umoja wa Mataifa na vyombo vyake mbalimbali, pamoja na mikutano ya kikanda na kimataifa inayotuhusu kwa namna ambayo sauti ya nchi yetu itazidi kusikika na kuheshimika. Katika mahusiano yetu ya kimataifa, tutaendelea kuweka mbele Uhuru wa nchi yetu, heshima ya
nchi yetu, na maslahi ya nchi yetu.

Hitimisho

Mheshimiwa Spika

Nimesema mengi, lakini pia mengi nimeyaacha. Ni vigumu, katika muda tulionao na stamina sote tuliyojaliwa nayo, nikasema yote. Naomba niishie hapa. Nimetoa kwa muhtasari sana mwelekeo na vipaumbele vitakavyoongoza Serikali nitakayoiunda.

Katika siku chache zijazo nitaunda Baraza la Mawaziri. Dhamira yangu ni kwamba tupate Serikali makini, yenye watu waadilifu na wachapakazi. Watu ambao wataongoza utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwa umahiri mkubwa, ambao wataondoa urasimu katika Serikali na ambao watashirikiana vizuri nanyi Wabunge ili kila mmoja wenu, bila kujali Chama anachotoka, atimize ahadi zake kwa wananchi wake. Nawaomba muwape ushirikiano Mawaziri hawa ili tutimize azma hii.

Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge,

Kwa miaka mitano iliyopita, nimefarijika kujionea ari na moyo mkubwa waliokuwa nao wananchi katika kuchangia maendeleo yao. Hata wale ambao hawakuwa na chochote cha kutoa, walitoa jasho lao na kushirikiana na Serikali Kuu na Serikali za Mitaa kufanya kazi za maendeleo ikiwemo ujenzi wa shule za Sekondari za Kata. Kazi yetu kubwa tuliowekwa madarakani kwa kura za wananchi ni kuhakikisha kwamba moto huo wa maendeleo hauzimiki.

Nimalizie kwa kuwahimiza Watanzania wenzangu kwamba sote leo hii tuamue kukusanya nguvu zetu, akili zetu na maarifa yetu yote, kama ndugu wa Taifa moja, na kuamua kwa dhati kuifanya Tanzania iwe nchi bora. Nchi hii ni yetu sote. Sio nchi ya Chama tawala, sio nchi ya watu walio Serikalini.

Ikiharibika, maumivu ni yote sote. Ikitengemaa, faraja ni yetu sote. Inawezekana, Timiza Wajibu Wako.

Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge

Asanteni sana kwa kunisikiliza.

Mungu Ibariki Afrika.

Mungu Ibariki Tanzania.
 
Mapambano Dhidi ya Rushwa

Mheshimiwa Spika;

Katika miaka mitano iliyopita tumefanya kazi kubwa ya kupambana na rushwa na matumizi mabaya ya madaraka. Tumebuni na kuutekeleza mkakati wa kupambana na rushwa, tumetunga sheria mpya na kali zaidi ya kuzuia na kupambana na rushwa, tumeanzisha taasisi mpya ya kupambana na rushwa (TAKUKURU) na kuipa uwezo mkubwa zaidi, tumewachukulia hatua kali za kuwapeleka mahakamani watu wote waliodhihirika kujihusisha na vitendo vya rushwa, bila kujali nyadhifa au nafasi zao katika jamii. Tutaendelea kukaza kamba.

Lakini kama mjuavyo, mapambano dhidi ya rushwa hayawezi kufanikiwa bila jamii kuichukia kwanza rushwa yenyewe. Katika hotuba yangu ya uzinduzi wa Bunge lililopita, niliwahimiza na kuwachochea Watanzania waichukie rushwa. Nafurahi kwamba lengo letu limetia. Watanzania sasa wamehamasika kuichukia rushwa. Naomba tuendelee hivyo hivyo. Na tuzisaidie taasisi zetu za kupambana na rushwa kufanya kazi zake.
KIKWETE haya ni masihara kwa watanzania.
 
Uboreshaji wa Makazi


Mheshimiwa Spika;


Watanzania wengi bado wanaishi katika makazi duni. Katika kipindi cha miaka mitano ijayo serikali itajielekeza kupambana na umaskini wa makazi. Serikali itaandaa Mpango wa Maendeleo ya Makazi wa miaka kumi utakaokeleza dhamira yetu ya kushirikiana na sekta binafsi kujenga na kuboresha makazi ya wafanyakazi na kuwahamasisha wananchi vijijini kuboresha makazi yao.

Ilani ya CHADEMA hiyo mzee !!!
 
Ilani ya CHADEMA hiyo mzee !!!

Hiyo ni kweli kabisa. Hata mabadiliko yaliyofanyika ni madogo mno. CCM kama mnataka kutekeleza ilani ya CHADEMA wawape na mpango kazi kwani msije mkaiga vya wenzenu halafu mkaishia njiani.
 
Nawashukuru Wabunge kwa uteuzi wangu wa Waziri Mkuu, Mheshimiwa.......... Wengi wenu mnamjua vizuri. Naomba Waheshimiwa Wabunge mumpe ushirikiano mkubwa akiwa Kiongozi wa Shughuli za Serikali Bungeni. Naomba pia muwape ushirikiano unaostahili Mawaziri nitakaowateua. Nisaidieni kuwashtua watakapokuwa wanasuasua, lakini pia wapongezeni wakifanya vizuri.

Hivi Jk alikuwa anaenda Dodoma kabla hajajua jina la Waziri Mkuu? Au ndiyo utaratibu katika uandishi wa hotuba za Rais? au hotuba ilitungwa kabla ya waziri mkuu kuidhinishwa? Kwani editing hairuhusiwi ili kujaza nafsi wazi?
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom