Hotuba ya Kikwete kwenye sherehe za miaka 38 ya CCM imebeba ujumbe mzito

Jk leo amezungumza mengi kwenye sherehe za miaka 38 ya kuzaliwa CCM lakini kwa wale wadau wanaojua siasa kwa kina basi amezungumzia masuala ya Urais na kusema CCM inataka mtu safi hivyo CCM inaweza kushawishi mtu kugombea na sio lazima kuwapa wale ambao wanautaka urais kwa lazima, ukimsikiliza kwa makini JK ameumia muda mwingi kusifia kazi nzuri anayofanya Kinana.


  • Awataka wana CCM kuepuka fedha za moto
  • Kila mmoja akumbuke ahadi zake
  • Awataka wana CCM kuwa mstari wa mbele kuhimiza watu kujiandikisha
  • Anukuu maneno ya Baba wa Taifa yanayosema 'Rais wa nchi yetu anaweza toka Chama chochote lakini Rais bora atatokea CCM'
04.jpg

Mwenyekiti wa CCM Taifa,Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akivishwa skafu na kijana wa chipukizi mara baada ya kuwasili kwenye uwanja wa Maji Maji kuadhimisha sherehe za miaka 28 ya kuzaliwa CCM ambapo Kitaifa zilifanyika mkoani Ruvuma na kuhudhuliwa na Viongozi mbali mbali.

15.jpg

Mwenyekiti wa CCM Taifa,Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akikatiza uwanjani baada ya kumaliza zoezi la kukagua gwaride la chipukizi za miaka 38 ya kuzaliwa CCM ambapo Kitaifa zilifanyika mkoani Ruvuma na kuhudhuliwa na Viongozi mbali mbali wa ndani na nje ya nchi.

18.jpg

Vijana wa Chipukizi wakionyesha ukakamavu wakati wa sherehe za kuzaliwa CCM zilizofanyika kwenye uwanja wa Maji Maji mjini Songea mkoani Ruvuma.

35.jpg

Mwenyekiti wa CCM Taifa,Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akihutubia wananchi wa Songea mjini kwenye uwanja wa Maji Maji wakati wa kuadhimisha sherehe za miaka 38 ya kuzaliwa CCM ambapo Kitaifa zilifanyika mkoani Ruvuma na kuhudhuliwa na Viongozi mbali mbali pamoja na wananchi.

28.jpg

Kepteni John Komba akiongoza bendi ya TOTkutumbuiza wananchi wa Songea mjini waliofurika kwa wingi kwenye maadhimisho ya sherehe za miaka 38 kuzaliwa kwa CCM.

60.jpg

Diamond akiwapungia mkono wananchi waliofurika kwenye uwanja wa Maji Maji wakati alipokuwa akiwasili tayari kutumbuiza kwenye sherehe za miaka 38 ya kuzaliwa CCM.



8.jpg

Diamond akiimba Asu pamoja na Abdul Msimbano kwenye sherehe za miaka 38 ya kuzaliwa kwa CCM.

40.jpg


Msanii Diamond akiwaburudisha wananchi kwenye uwanja wa maji maji.
 

security guard

JF-Expert Member
Sep 27, 2011
799
603
HOTUBA YA MWENYEKITI WA CCM TAIFA, MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE, KATIKA SHEREHE ZA KUTIMIZA MIAKA 38 YA CCM, KWENYE UWANJA WA MAJIMAJI, SONGEA - RUVUMA,
TAREHE 01 FEBRUARI, 2015


Ndugu Philip Mangula, Makamu Mwenyekiti wa CCM;
Mheshimiwa Mizengo Peter Pinda, Waziri Mkuu na mjumbe wa Kamati Kuu;
Mheshimiwa Anne Makinda, Spika wa Bunge na Mjumbe wa Kamati Kuu;
Ndugu Abdulrahman Kinana, Katibu Mkuu wa CCM;
Ndugu Mike Mukula, Makamu Mwenyekiti wa NRM ya Uganda na ujumbe wake;
Waheshimiwa Wajumbe wa Kamati Kuu;
Mheshimiwa Oddo Mwisho, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Ruvuma;
Waheshimiwa Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa;
Wajumbe wa Sekretarieti ya CCM;
Ndugu Verena Shumbusho, Katibu wa CCM Mkoa wa Ruvuma;
Wenyeviti wa Jumuiya za CCM;
Viongozi, wananchama na wapenzi wa CCM;

CCM Oyee!

Naomba nianze kwa kuwashukuru na kuwapongeza wenyeji wetu kwa mapokezi mazuri, hususan napenda kuwatambua wananchi, viongozi na wana-CCM wa Mkoa wa Ruvuma wakiongozwa na Mwenyekiti wao ndugu Oddo Mwisho, Katibu wa Mkoa Mama Verena Shumbusho, Mkuu wa Mkoa na Mjumbe wa Kamati ya Siasa Ndugu Said Mwambungu. Nawapongeza kwa maandalizi mazuri ya sherehe hizi. Hakika zimefana sana. Hii ni mara ya pili sherehe hizi kuadhimishwa mkoani hapa. Mara ya kwanza ilikuwa mwaka 1991 wakati wa kuazimisha miaka 14 ya CCM.

Tunatambua kuwa mmefanya kazi kubwa ya maandalizi mpaka mmeweza kufanikisha shughuli ya leo kwa kiwango cha juu. Waswahili wanasema "Usione vinaelea Vimeundwa". Napenda kutumia nafasi hii kutoa pongezi maalum kwa Katibu Mkuu Abdulrahman Kinana kwa uongozi wake makini uliowezesha mambo kuwa mazuri kiasi hiki. Hongera sana kwa hili na kwa kazi nyingi nzuri unazofanya kwa maslahi ya Chama chetu na nchi yetu.

Leo ni siku ya furaha kwangu na kwa viongozi na wanachama wenzangu wa CCM kote nchini ya kusherehekea na kuadhimisha miaka 38 ya kuzaliwa kwa Chama cha Mapinduzi. Tunastahili kuisherehekea siku hii kwa nderemo na vifijo kwa sababu ya mafanikio makubwa ambayo Chama chetu kimeendelea kupata ndani ya Chama na katika kuliongoza taifa letu. Katika miaka 38 ya uhai wake Chama chetu kimezidi kuimarika na kimeendelea kuliongoza vyema taifa letu: kuna amani, utulivu na maendeleo yanayoonekana.

Tumeeendelea kuaminiwa na kutumainiwa na Watanzania. Kama ilivyothibitika na ushindi wa kishindo katika chaguzi zote tangu mfumo wa vyama vingi uanze mwaka 1995 mpaka sasa. Hata mwaka huu itakuwa hivyo hivyo. Dalili ya mvua ni mawingu: ushindi mnono tulioupata kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ni dalili tosha kwamba Oktoba, 2015 watani zetu hawana chao.

Ninaposema hivyo nawaomba wana CCM wenzangu tusibweteke tukadhani kwamba ndiyo tumekwishafika. Bado safari ndiyo kwanza tumeianza na inaweza kuwa na changamoto zake. Lazima tufanye kazi tena kazi kubwa sana ndipo tutakapojihakikishia ushindi. Nguvu ya ushindi inaanzia kwenye Chama. Huu ni mwaka ambao kazi ya Chama ndani ya Chama na kazi ya Chama ndani ya umma inatakiwa ifanyike kwa nguvu zaidi na kwa ari kubwa zaidi. Lazima tuhakikishe tunao umoja wa dhati na kwamba wanachama wetu wanakuwa na mwamko wa hali ya juu wa kukipigania Chama katika kutafuta na kupata ushindi kwa Udiwani, Ubunge, Uwakilishi, Urais wa Zanzibar na Urais wa Muungano.

Huu ni mwaka ambao wanachama na viongozi wanatakiwa kuhakikisha kuwa wanakutana mara kwa mara kwa mujibu wa Katiba na hata zaidi kuzungumzia mikakati ya kupata ushindi na kuitekeleza. Huu ni mwaka ambao lazima tuhakikishe kuwa tunazo rasilimali na nyenzo za kutuwezesha kufanya kazi ya Chama ndani ya umma na kuwapatia ushindi wagombea wa Chama chetu.

Huu ni mwaka ambao kazi ya Jumuiya za Chama ya kukiwezesha Chama kuungwa mkono na jamii pana ya Watanzania walio vijana, wanawake na wazazi inafanyika kwa umahiri na ufanisi wa hali ya juu.

Bila ya shaka, ndugu zangu mtayakumbuka maneno niliyoyasema kwa kuyarudia kuwa "Mwisho wa uchaguzi mmoja ndiyo mwanzo wa uchaguzi mwingine". Najua baadhi yenu mmezingatia na kuchukua hatua za kufanya maandalizi mapema ya uchaguzi wa mwaka huu mara baada ya kumaliza uchaguzi wa mwaka 2010. Hao nawapongeza. Lakini wapo viongozi na wanachama ambao hawajafanya chochote. Hawa, wananisikitisha kwa athari mbaya na hatari ya kupoteza ushindi wanayokiletea Chama chetu.

Naomba kila mmoja wetu ajipime yupo fungu gani. Kama upo kwenye kundi la kwanza lililokwishaanza maandalizi natoa pongezi nyingi. Nawaomba muendelee kukamilisha ipasavyo. Kwa wale ambao wapo kundi la wale ambao maandalizi yao ni ya kiwango kidogo au hawajaanza kabisa lazima waanze na wakati ni huu. Usikawie, unatakiwa kufanya kazi kwa ari zaidi, nguvu zaidi na kasi zaidi kama ilivyo kauli mbiu ya CCM. Yapo mambo kadhaa ya kufanya ambayo tulikwishaambiana tufanye. Miongoni mwao ni lile agizo la kutaka kila ngazi ya Chama na hasa Wilaya na Mikoa kuwa na Mfuko wa Uchaguzi. Wakati wake ndio huu sasa wa mfuko huo kufanya kazi iliyokusudiwa. Naomba tujiulize wangapi wanayo mifuko hiyo na wangapi hawana. Kwa wale walionayo wahakikishe ina rasilimali za kutosha. Kama hazitoshi waweke mikakati ya kuitunisha mifuko hiyo. Kwa wale ambao hawajaanzisha wachune bongo kuhusu namna ya kupata fedha za kuendeshea shughuli za uchaguzi. Sina budi kuwatahadharisha kuwa msichukue fedha ambazo zitazua matatizo.

Ndugu viongozi na ndugu wanachama;
Huu ni mwaka wa kutambua ahadi zipi tulizotoa zimetimizwa na zipi bado. Kwa zile ambazo hazijakamilika wajibu wetu ni kuweka mikakati ya kuzikamilisha. Kwa zile ambazo hazitakamilika tutafute maelezo sahihi ya kutoa kwa wadau wa huduma hiyo. Naamini hazitakuwa nyingi za kuchosha. Mwaka huu siyo mzuri kwenda na madeni lukuki ya ahadi. Yanaweza kutupunguzia ushindi wetu.

Huu ni mwaka wa kuongeza ukubwa wa jeshi letu la ushindi kwa kuongeza wananchama wapya. Natambua tatizo la upungufu wa kadi lakini najua mipango thabiti iliyopo ya kuleta kadi nyingi za kutosha wale waliopo nje. Tujiepushe na kuingiza mamluki hivyo taratibu za kuingiza wanachama zizingatiwe ipasavyo.

Ndugu Viongozi;
Ndugu Wananchi;
Jambo lingine kubwa na muhimu sana kufanya mwaka huu ni kuwatembelea wanachama na wananchi na kuzungumza nao. Hatujaifanya vizuri sana kazi hii lakini hatujachelewa. Sina budi kutoa pongezi maalum kwa Katibu Mkuu wa CCM kwa ufanisi mkubwa aliopata kwa jambo hili. Sote hatuna budi kuiga mfano wake mzuri. Tuache kukaa maofisini tutoke kuzungumza na watu kuwashawishi waunge mkono na kuipigia kura CCM katika uchaguzi ujao. Kila Ofisi ya Mkoa na kila Ofisi ya Wilaya inalo gari la kuwawezesha kufanya kazi hiyo. Tafadhali fanyeni hivyo, kwani bila ya kufanya hivyo hakuna uhakika wa kupata ushindi. Kilichobakia kwa upande wetu ni kutafuta vipando kwa Ofisi za Kata na Matawi. Tusaidiane pale inapowezekana.

Uandikishaji wa Wapiga Kura

Ndugu wana CCM na ndugu Wananchi;

Jambo lingine muhimu katika kutafuta ushindi ni kupatikana kwa wapiga kura. Chama chetu kama vilivyo vyama vingine, hatuna budi kuwahimiza wanachama wetu, wapenzi wetu na wananchi wengine wajitokeze kwa wingi kujiandikisha kupiga kura. Mwaka huu wenye kadi mpya za mpiga kura ndiyo watakaoruhusiwa kupiga kura katika uchaguzi mkuu na katika kura ya maoni kuhusu Katiba Inayopendekezwa.

Asiyejiandikisha hatapata fursa ya kushiriki kura ya maoni na uchaguzi mkuu. Kwa sababu hiyo nawaomba viongozi na wanachama wa CCM wawe ndiyo wa kwanza kujitokeza kujiandisha. Pia wawe mstari wa mbele kuwahimiza wananchi wengine kujiandikisha. Nawaomba jambo hili mlipe uzito mkubwa kwani safari ya kutafuta na kupata ushindi inaanzie kwenye kupata wapiga kura hususani wapiga kura wanaounga mkono Chama chetu na wagombea wetu.

Kura ya Maoni

Ndugu wananchi;
Kama mjuavyo, jambo kubwa lililo mbele yetu ni kura ya maoni kuhusu Katiba Inayopendezwa itakayofanyika tarehe 30 Aprili, 2015. Maandalizi yote husika yanaendelea kufanyika ili kuwezesha kura hiyo kutekelezwa kama ilivyopangwa. Kama nilivyokwishaeleza hivi punde uandikishaji wa wapiga kura ni miongoni ma maandalizi hayo. Mengine ni uchapishaji na usambazaji wa Katiba Inayopendekezwa.

Yapo mambo kadhaa ambayo nawasihi viongozi na wanachama wenzangu mfuatilie kwa karibu ili yasiwapite. Yale tunayoyajua tuwaambie. Miongoni mwa mambo muhimu sana ambayo Chama hakina budi kujipanga vizuri ni kuhusu kutoa elimu kwa umma kuhusu Katiba Inayopendekezwa na kampeni ya Kura ya Maoni. Watani zetu watatoa elimu hasi kuhusu Katiba Inayopendekezwa, sisi tutoe elimu chanya.

Wenzetu watataka Katiba Inayopendekezwa isipite. Sisi tupige kampeni ikubalike. Nilisema siku ile Dodoma wakati wa kukabidhiwa Katiba Inayopendekezwa na narudia tena leo kwamba Katiba Inayopendekezwa imebeba maslahi mapana ya taifa letu. Hatujawahi kuwa na Katiba kama hii Inayopendekezwa. Misingi ya historia ya nchi yetu yaani kule tulikotoka, tulipo sasa na tuendako imezingatiwa vizuri. Katiba hiyo inatambua maslahi ya makundi yote nchini na kuyawekea utaratibu mzuri wa kutekelezwa. Wakulima, wafugaji, wavuvi, wanawake, vijana, wasanii, wafanyakazi, wazee na watoto wametambuliwa kwa kina na upana zaidi kuliko Katiba ya sasa.

Katiba Inayopendekezwa imeshughulikia kero za Muungano na kujenga mazingira bora zaidi kwa Muungano wetu kuimarika. Yale mambo yaliyokuwa yanaikwaza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na kuukwaza Muungano yamepatiwa ufumbuzi mwafaka. Sasa Zanzibar itaendesha na kushughulikia mambo yake kwa uhuru mkubwa zaidi.

Ndugu wananchi;

Kwa maoni yangu sioni sababu ya kuikataa Katiba Inayopendekezwa. Hatuna budi kutambua kuwa tukiikataa Katiba Inayopendekezwa, Katiba ya sasa itaendelea kutumika mpaka hapo mchakato mwingine utakapomalizika miaka mingi ijayo. Viongozi wa vyama vinne vya siasa wamesikika wakisema watasusia kushiriki katika kura ya maoni na kuwataka wanachama wao wasishiriki. Kauli hiyo imenisikitisha sana ingawaje haikunishangaza hasa tukikumbuka waliyoyafanya wakati wa Bunge la Katiba. Mimi nawaomba washiriki.

Nawasihi wananchi wasiwasikilize. Wao wakitaka kususia waacheni wasusie lakini nyie jitokezeni kupiga kura. Nawasihi msikubali kupoteza mema mengi yaliyo katika Katiba Inayopendekezwa ati kwa sababu tu hakuna Serikali Tatu walizokuwa wanazitaka. Kama kweli wananchi wa Tanzania wanakereketwa na Serikali Tatu watathibitisha hiyo kwenye kura ya maoni.

Naomba msibabaishwe wala kudanganywa na watu wanaotaka kuturudisha nyuma kutoka katika hatua kubwa muhimu tutakazopiga kwa kuikubali Katiba Inayopendekezwa. Tusikubali kubaki nyuma.

Uchaguzi Mkuu

Ndugu wananchi;
Kama mjuavyo mwezi Oktoba, 2015 nchi yetu itafanya uchaguzi mkuu wa Madiwani, Wabunge, Wawakilishi, Rais wa Zanzibar na Rais wa Jamhuri ya Muungano. Uchaguzi wa mwaka huu ni wa kihistoria kwa nchi yetu kwani tunachagua Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mimi nataka Rais huyo awe mwana CCM. Sisi sote katika CCM tunataka Rais atoke katika Chama chetu kwa sababu kama alivyousia Baba Wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere "Rais wa nchi yetu anaweza kutoka Chama chochote lakini Rais bora atatoka CCM".

Huu ni usia mzito wenye maono ya mbali. Tusiupuuze wosia huu bali tuuenzi. Sisi katika Chama cha Mapinduzi tuwe mstari wa mbele katika kuuenzi wosia huu kwa kupata mgombea aliye bora wa kupeperusha bendera ya CCM katika uchaguzi ujao. Mgombea ambaye wananchi wakisikia jina lake likitajwa watasema naam, hapo sawa, hapo barabara. Lakini tukiteua mgombea ambaye watu wataguna na kusema hata huyu? Tutakuwa tumemuangusha Muasisi wa Chama chetu na taifa letu katika wosia wake. Bila shaka laana yake tutaipata. Na hilo likitokea itakuwa hasara kubwa kwa taifa letu na msiba kwa CCM. Nchi itayumba.

Lazima tuhakikishe kuwa hatutafika huko. Watu wazuri wapo wa kutosha katika CCM na naamini tunawajua. Kama hawajajitokeza tuwashawishi wafanye hivyo. Ndugu zangu, tusifanye ajizi katika jambo hili kubwa na la msingi kwa Chama chetu. Kushinda chaguzi za dola katika sehemu zetu mbili za Muungano ndiyo madhumuni makuu ya kuundwa na kuwepo kwa CCM.

Napenda kuwahakikishia wanachama wa CCM na wananchi kuwa, Chama cha Mapinduzi ni Chama kilichokomaa, kilicho makini na imara. Tunao utaratibu unaoeleweka na kutabirika wa kuwapata wagombea. Inazo kanuni na vigezo vya wazi vya kuwapata viongozi walio bora, na tunavyo vikao rasmi vya kuchuja na kuteua wagombea kwa kuzingatia kanuni, taratibu na maadili ya Chama chetu. Hivyo basi, hapataharibika jambo.

Naomba niwahakikishie kwamba CCM itawapatia Watanzania wagombea bora ambao hawatawapa wananchi mashaka wala kigugumizi cha kuwachagua. Tutafanya hivyo kwa nafasi ya Rais wa Muungano, Rais wa Zanzibar, Wabunge, Wawakilishi na Madiwani. Nawaomba wagombea wazingatie na kuheshimu masharti ya Katiba ya Chama, Kanuni na Madili ya uteuzi kwa wanaotaka kuteuliwa kugombea nafasi katika chaguzi za dola. Asiyezingatia hayo asije akakilaumu Chama bali ajilaumu mwenyewe kwa makosa aliyoyafanya.

Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi wa CCM

Ndugu wananchi;
Miezi minne iliyopita nilifanya ziara ya mkoa huu wa Ruvuma kukagua shughuli za maendeleo. Nimefurahishwa sana na jitihada za kujiletea maendeleo zinazofanywa na wananchi wa mkoa huu na mafanikio mnayoendelea kuyapata. Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM na mipango mbalimbali ya serikali unakwenda vizuri, kiasi cha kuwastajabisha hata wale waliokuwa na mashaka na wasio tutakia mema.

Yako mambo mengi tuliyoahidi kufanya ambayo tumeyakamilisha na mengine utekelezaji wake unaendelea vizuri. Kilio cha miaka mingi cha wananchi wa mkoa huu kuhusu barabara kimefanyiwa kazi vya kutosha. Ujenzi wa barabara ya Namtumbo – Songea na Peramiho - Mbinga kwa kiwango cha lami umekamilika. Tunaendelea na ujenzi wa barabara ya Namtumbo – Tunduru na Tunduru – Mangaka ili kuunganisha mkoa wa Mtwara na Ruvuma kwa barabara za lami. Aidha, mipango ya kujenga barabara ya Mbinga – Mbambabay kwa mkopo wa Benki ya Maendeleo ya Afrika imefikia mahali pazuri. Kwa upande wa usafiri katika Ziwa Nyasa hivi sasa mchakato wa ujenzi wa chelezo cha kujengea meli ya ziwa hilo kule kwenye bandari ya Itungi, Kyela unaendelea vizuri. Ujenzi wa chelezo ukishakamilika ujenzi wa meli utaanza.

Kwa upande wa umeme tunaendelea na ujenzi wa njia ya umeme ya msongo wa Kv 220 kutoka Makambako kuja Songea na hadi Mbinga na Namtumbo. Ujenzi wa njia hii ya umeme utakapokamilika utawahakikishia wakazi wa mji wa Songea na mkoa wa Ruvuma umeme wa uhakika. Tumechelewa kidogo kwa sababu ya kubadilisha ukubwa wa njia kutoka msongo wa Kv 132 tuliyotaka kujenga awali hadi Kv 220. Aidha, usambazaji wa umeme vijijini unaendelea kwa kasi katika maeneo yote nchini. Tunataka ifikapo June, 2015 zaidi ya vijiji 5,336 viwe vimepatiwa umeme. Kati ya vijiji hivyo zaidi ya vijiji 300 ni vya mkoa wa Ruvuma. Haya ni mafanikio makubwa na ya kutia moyo.

Kuhusu sekta ya Afya nako pia tumepata mafanikio makubwa katika utoaji wa huduma ya afya kwa Watanzania. Kwa hapa Songea nimekwishatoa maelekezo kwa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kuanza mchakato wa ujenzi wa hospitali mpya ya Mkoa wa Ruvuma na hii iliyopo sasa iwe ni hospitali ya Manispaa ya Mji wa Songea. Halmashauri ya Manispaa ya Songea iharakishe kutenga eneo la kutosha kwa ajili ya ujenzi wa hospitali hiyo ya mkoa ambayo itakuwa ni ya rufaa kwa yale ambayo hospitali za Wilaya zitashindwa kumudu.

Haya ni maeneo machache tu ambayo yanaonyesha hatua kubwa tuliyopiga katika utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi na maendeleo ya mkoa huu. Ukweli ni kwamba Ruvuma ya miaka 10 iliyopita siyo Ruvuma ya leo. Ninyi nyote ni mashahidi wa mambo haya. Mwenye macho haambiwi tazama.

Ndugu wananchi;
Jambo la mwisho ambalo napenda kulizungumzia ambalo nilishalizungumzia kwenye hotuba yangu ya mwaka mpya inahusu ununuzi wa mazao ya wakulima. Nilieleza siku ile kuwa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) ilikuwa bado haijalipa shilingi bilioni 89 kwa wakulima kwa mazao yao iliyonunua. Nilielezea kutokufurahishwa kwangu na hali hiyo na kuagiza Wakala kulipa deni hilo.

Nimeambiwa kuwa tayari shilingi bilioni 15 zimeshatolewa na hapa Ruvuma mmepata shilingi bilioni 8. Hivi karibuni shilingi bilioni 36 zitatolewa na kubaki shilingi bilioni 38 ambazo zitalipwa mwezi Machi.

Jambo lingine ambalo tunaendelea nalo kulishughuikia katika Serikali ni kupata masoko mengine kwa mazao ya wakulima. Kama nilivyosema NFRA haiwezi kununua mazao yote ya wakulima nchini. Uwezo wake ni kuhifadhi tani 240,000 wakati uzalishaji wa mahindi hapa Ruvuma ni tani 993,350. Hata kama NFRA ingeamua kununua mahindi yote kutoka mkoa wa Ruvuma peke yake isingeweza kuyamaliza.

Nimewaagiza viongozi wa mkoa wa Ruvuma na mikoa yote nchini washirikiane na Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika na Wizara ya Viwanda na Biashara kutafuta masoko mengi kwa ajili ya mahindi, mpunga na mtama wa wakulima ndani na nje ya nchi.

Tunakokwenda

Ndugu wana CCM;
Mafanikio ya miaka 38 ya Chama chetu yasitufanye tubweteke. Bado tunayo kazi kubwa mbele yetu. Ili tuendelee kuongoza dola hatuna budi tuendelee kuwa tumaini na kimbilio la wananchi wetu. Inatupasa kuwa waaminifu kwa ahadi zetu na watiifu kwa matakwa yao. Kubwa sana, tunatakiwa tuwe tayari wakati wote kubadilika na kwenda na wakati. Tunaweza kufanya hivyo ikiwa tutaendelea kukuza demokrasia ndani ya Chama chetu na kuruhusu na kuvumilia tofauti za mitazamo. Hiyo ndiyo siri ya uhai wa CCM ambayo hatuna budi kuendeleza.

Tunapoanza safari ya kuelekea mwaka wa 39, hatuna budi sasa kuelekeza nguvu zetu kwenye kuondoa utegemezi wa kifedha kutoka kwenye ruzuku na michango ya wafanyabiashara. Kutegemea misaada na michango si mambo endelevu na huo hauwezi kuwa ni mkakati wa kutumainiwa wa kuimarisha Chama chetu. Wakati mwingine michango hii imetugharimu ndani ya Chama chetu. Lazima tuwe wabunifu katika kutafuta vyanzo vya mapato ikiwa ni pamoja na rasilimali zetu nyingi tulizonazo ili kuwezesha Chama kujitegemea. Tayari yako mawazo yaliyoibuliwa kutokana na kazi nzuri ya Kamati iliyoongozwa na Mjumbe wa Kamati Kuu na Mweka Hazina wetu Mheshimiwa Zakhia Meghji tumeagiza yatekelezwe. Naomba mtimize ipasavyo wajibu wenu.

Hitimisho

Ndugu wana CCM;
Leo ni siku ya furaha kwetu sote. Wakati tukisherehekea mafanikio yetu tuwakumbuke pia waasisi wetu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, aliyekuwa Mwenyeti wa TANU na Ndugu Sheikh Aboud Jumbe aliyekuwa Mwenyekiti wa ASP kwa busara, hekima na uamuzi wao uliotukuka uliowezesha kuzaliwa kwa CCM. Tunawakumbuka pia wale wote waliotangulia mbele ya haki ambao walijitoa maisha yao kujenga CCM.

Hatuna budi kuwaenzi kwa kutoa mchango mkubwa zaidi mwaka ujao na miaka mingi ijayo. Tuhakikishe kuwa tunaimarisha Chama chetu na kutenda mema kwa ajili ya nchi yetu na watu wake. Hili linawezekana ikiwa kila mtu atatimiza wajibu wake. Kidumu Chama cha Mapinduzi!

Asanteni sana kwa kunisikiliza.
 
Hao watu walikwenda kumuona diamond na siyo kumsikiliza kukwete na hilo liko wazi
 
Nimefanya Kazi Ktk Mgodi Wa Bulyanhulu Gold Mine Uliopo Kahama,huko Ndo Nilipata Siri Nyingi Sana Za Jinsi CCM ilivyo ya ajabu.

Kwa Siku Mgodi Wa Bulyanhulu Unaingiza Faida Ya $2.5milions,serikali Ya CCM Inalipwa Royalty Ya %3 Out Of The Entire Earnings,ikaja Kuongezewa Ikawa %4 Yaani In Short Dhahabu Inavunwa Bure,wanachoambulia Wafanyakazi Ni Magonjwa Ya Kudumu Ambayo Mwisho Wake Ni Kifo,nataka Niwaambie Ukweli Watanzania Wenzangu,wawekezaji Si Wabaya Mi Nimekaa Nao Sana,wana Huruma Sana,serikali Ndo Mbaya,kwa Mfano Wakati Wanaanza Kuchimba Walitaka Kulipa initial Basic Pay Ya Sh Mil 3.2 Mkapa Akagoma, ushahidi Upo.

Miaka 53 Ya Uhuru Taifa Bado Hoi Kiuchumi Na Raslimali Zote Tulizonazo Leo CCM Wanafanya Birthday Bila Aibu Wakati Taifa Lipo Uchi Kiuchumi,hii Ni Sawa Na Kumfanyia Birthday Mwanao Aliyemahututi Hosp Kalazwa,viongozi Wa CCM Hawana Aibu Akili Zao Karibia Wote Zimepigwa Ganzi,hadi Sasa Taifa Halina Mwelekeo Sahihi,kila Kitu Hapa Tanzania Ni Sintofahamu, hakuna Ajuaye Kesho Itakuwaje,labda Nape.
 
ikiwa chama tawala kinawatumia watu wanaojisifia kwa uzinzi katika shughuli zake na kuwalipa hela nyingi, basi vita dhidi ya ukimwi inakuwa ndoto kabisa.

Duniani kote hata uwe na kipaji cha hali ya juu kiasi gani kama hauna maadili mema huwezi kuweka katika national stage. Mfano John terry kuondolewa ukapten wa timu ya taifa, Mchezaji wa american football USA kufungiwa kwa kumpiga mchumba wake (later married to her).

Only in Tanzania unaweza kuwa na sifa mbaya laikini ukasifiwa na kila mtu, kwa kuwa unaweza kucheza mpira (ngasa na mkanda wa ngono), Kuimba kama Nasibu, nk. vijana wetu wanaiga haya mambo, maana wanaamini ndio yanaleta sifa na kufamika.
 
Naomba uni PM huo ushahidi wa basic payments tafadhali. Nafanya research ya extractive industry.
 
Majizi tu hayo hamna lolote. yanasherekea kwa jinsi plans za ku plunder nchi yetu adhim ilivyofanikiwa. Ukiangalia hilo nenguaji la kiume utadhabi roba la lumbesa kumbe mtu. alivyojaaa mtumbo na kichwa kingekuwa hivyo, basi tanzania ingekuwa kama peponi
 
Jk hajawahi kuwa serious.... Sintokaa kuamini chohote asaemacho namuombea sana aishi kutambua unafiki wake
 
Jambo la kujivunia walilonalo ni polisisiemu kuua watu kwenye maandamano ya kudai haki! R.I.P DAUD MWANGOSI
 
Nyerere ndo rais wa kwanza na mwisho toka ccm aliyekuwa mzalendo na mwenye upendo wa dhati na taifa letu! Wengine waliofuata ni waigizaji tu kama waigizaji wengine.
 
Ndugu zangu wana jamvi napenda kuwapongeza kwa mawazo mazuri mnayofanya humu ndani jamvini kwetu. ninaomba niweke ghiriba na uongo wanaotumia maccm kwa sasa hapa mkoani Ruvuma hasa yale aliyotudanganya Kikwete jana kwenye Sherehe za kuadhimisha kwa miaka 38 ya kuzaliwa kwa CCM.

Na niseme tu kwa mshangao mkuubwa na nilishanga sana badaya kusikia wa sherehe hizo zitaadhimihwa ta. 01/02/2015 toauti na miaka mingine ambapo sherehe hizo huadhimishwa kila tar. 05/02 waka huu imekuwa tofauti saa
Leo kwa kila aliyeikiliza hotua ya M/kii wao Kikwete atauwa amesikia utapeli mkubwa aliout e atika viwanja vya majimaji, amesema amesema hivi anwaagiza viongozi kuhakiksha kuwa mahini ya wakulima yaanunliwa na wae ambao awanidai serikali wanalipwa pesa zao.

Hiki ni kiini macho na utapeli wa hali ya juu sana. ndugu zangu wanajamii wangu, huyu jamaa mwaka jana alipofika mkani hapa aliwahidi wakulim kuwa wakulima wangeuza mazao yao Tsh. 500/= kwa kilo ifikapo mwezi wa agosti 2014 hayo ayakufanyika zaidi sana waliwakopa wakuma tenakwamikataa ya akina Car peterz kwa wakti wa ukoloni.

Zaidi bwana Nchimbi amewatia hasira sana wana Ruvuma hasa pale alipomdangnya kikwete kuwa amepata mdhmdhamin wa timu ya majimaji na ametoa Thsh. Mil. 15 huku akijua majimaji kwa sasa ina ukata wa fedha nazinazotumika wa sasa ni pea a wadau wanaochanga ili kuona majimaji yao inapanda daraja msimu huu.

Kwa maneno yale aliyoyasema ni kwamba watu amewavunja sana moyo kwani sasa ndo tunamini kabisa ni kweli akina Masamaki na Mohamed Mchele wanakula pesa ya wachezaji na ndo maan hawafanyi vizuri hivi sasa. lakini pia nimeshangaa sana kuona mpango wao wa kurudsha kadi na bendera feki za chademahawajafanya labda baada ya kugundua zimchukuliwa na majasi wa chadema tena ofsi ya CCM MKOA.
 
Eti Kikwete mwizi wa escrow anataka raisi ajaye awe "msafi", what a joke. Yeye sio msafi, ametumia maafisa wa Ikulu na familia yake kuiba hela za escrow pale Stanbic then wajinga wachache kwa njaa zao wanaamini kuwa kikwete aliyeingia madarakani kwa hela za EPA ataongoza mchakato safi kuleta raisi safi toka katika ukoo wa Panya
 
JK hajawahi na hawezi kuongea jambo la maana....unaweza dhani la maana utekelezaji ukaja kuwa 0%
 
Nimefanya Kazi Ktk Mgodi Wa Bulyanhulu Gold Mine Uliopo Kahama,huko Ndo Nilipata Siri Nyingi Sana Za Jinsi CCM ilivyo ya ajabu.Kwa Siku Mgodi Wa Bulyanhulu Unaingiza Faida Ya $2.5milions,serikali Ya CCM Inalipwa Royalty Ya %3 Out Of The Entire Earnings,ikaja Kuongezewa Ikawa %4 Yaani In Short Dhahabu Inavunwa Bure,wanachoambulia Wafanyakazi Ni Magonjwa Ya Kudumu Ambayo Mwisho Wake Ni Kifo,nataka Niwaambie Ukweli Watanzania Wenzangu,wawekezaji Si Wabaya Mi Nimekaa Nao Sana,wana Huruma Sana,serikali Ndo Mbaya,kwa Mfano Wakati Wanaanza Kuchimba Walitaka Kulipa initial Basic Pay Ya Sh Mil 3.2 Mkapa Akagoma,ushahidi Upo,

maelezo yako yameniuma sanaa..
 
Back
Top Bottom