Hotuba ya kambi ya upinzani - wizara ya uchukuzi (full text) | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Hotuba ya kambi ya upinzani - wizara ya uchukuzi (full text)

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by mndeme, Aug 3, 2011.

 1. m

  mndeme JF-Expert Member

  #1
  Aug 3, 2011
  Joined: Sep 2, 2008
  Messages: 322
  Likes Received: 3
  Trophy Points: 35
  HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI YA UPINZANI MHESHIMIWA MHONGA SAID RUHWANYA (MB) WIZARA YA UCHUKUZI KUHUSU MPANGO NA MAKADIRIO YA MATUMIZI YA BAJETI, KWA MWAKA WA FEDHA 2011/2012

  UTANGULIZI
  Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Kambi ya Upinzani naomba nitoe maoni ya Kambi ya Upinzani kuhusu hotuba ya bajeti ya Wizara ya Uchukuzi kwa mwaka wa fedha 2011/2012 kwa mujibu wa Kanuni za Bunge Kanuni ya 99(7) toleo la Mwaka 2007.
  Mheshimiwa Spika, kwanza nichukue fursa hii kutoa shukrani zangu za dhati kwa Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni Mhe. Freeman Aikael Mbowe kwa kuniteua kuwa Waziri Kivuli wa Wizara ya Uchukuzi. Namshukuru kwa miongozo yake na uongozi thabiti akishirikiana na Naibu wake Mhe. Zitto Zuberi Kabwe pamoja na Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani Mhe. Tundu Antiphas Lissu.
  Mheshimiwa Spika, napenda pia kuwashukuru wananchi wa mkoa wa Kigoma hasa akina mama kwa imani yao kwangu na kunipitisha ili kuwa mgombea ubunge kwa viti maalum, na hatimaye kuwa mbunge. Aidha, nishukuru kwa ushirikiano mkubwa wanaonipa katika kazi zangu. Natoa ahadi kwenu kuwa nitazidi kusimamia yale yote mliyonituma niyafanye.
  Mheshimiwa Spika, mwisho lakini kwa umuhimu mkubwa naomba pia kumshukuru Mama yangu mpenzi Kuruthum Mohamed pamoja na ndugu na jamaa zangu wote kwa kunipa moyo pale mikikimikiki ya kisiasa inapokuwa katika hali ya juu.
  Mheshimiwa Spika, Kambi ya upinzani Bungeni bila ya woga wala upendeleo imekuwa ikisema ukweli kuhusiana na jinsi Taifa letu linavyoongozwa na kufichua maovu yote kwa lengo la kuhakikisha kuwa mlipa kodi wa Tanzania anapata maendeleo kulingana na thamani ya kodi anayolipa.
  MASUALA YA JUMLA

  Mheshimiwa Spika, Sekta ya uchukuzi ni miongoni mwa sekta za kimkakati katika uchumi wa Tanzania. Nafasi ya kijiografia ya Tanzania inatoa upendeleo wa kipekee kwa sekta hii kuwa sekta kichocheo kwa ukuaji wa uchumi wa Taifa letu. Sekta hii hutengeneza mazingira mazuri yanayosaidia kusukuma maendeleo katika shughuli nyingine za kiuchumi na inatengeneza ajira nyingi sana. Sekta hii inajumuisha usafiri wa Reli, Barabara, Anga na usafiri wa Majini. Hapa Tanzania, Sekta hii ni mojawapo ya sekta zinazokua kwa kasi na mchango wake katika pato la Taifa ni takribani asilimia 5.1; hii ni takribani mara mbili ya mchango wa sekta ya madini katika GDP na zaidi ya mara nne ya mchango wa sekta ya uvuvi katika uchumi. Ukuaji huu wa asilimia 5.1 maana yake ni kuwa sekta hii imechangia shilingi trilioni 1.6 katika uchumi wa nchi kwa mwaka 2010.
  Mheshimiwa Spika, bajeti iliyotengwa kwa ajili ya kuimarisha sekta ya uchukuzi ni ndogo mno kulinganisha na majukumu ya Wizara. Kwa mwaka 2011/2012 fedha za maendeleo zilizotengwa ni shs. Bilioni 167.98, kati ya fedha hizo shs.bilioni 95 ni fedha za ndani na shs bilioni 72.98 ni fedha za wadau wa maendeleo. Mahitaji halisi ya fedha za maendeleo ni shs.bilioni 492.02
  Mheshimiwa Spika, kati ya majukumu ya msingi yaliyomo katika sera ya uchukuzi ya mwaka 2003 ni kuhakikisha usafirishaji wa bidhaa zinazopitia kwenye bandari zetu kwenda nchi jirani ni salama. Kambi ya Upinzani inaona hili litawezeshwa vizuri kama bidhaa hizo zitasafirishwa kwa kutumia usafiri wa reli badala ya barabara.
  Mheshimiwa Spika, sera ya uchukuzi imeweka wazi kile ambacho Kambi ya Upinzani katika hotuba yake mbadala ilisisitiza, yaani kukuza uchumi katika maeneo ya vijijini, hasa maeneo ambayo yanatoa mazao kwa wingi. (Sera ya uchukuzi ya mwaka 2003, kifungu cha 3:4:1).

  USAFIRI WA NCHI KAVU
  Mheshimiwa Spika, wananchi wengi wanatumia aina hii ya usafiri katika kutimiza majukumu yao ya kila siku – iwe kwa mabasi, treni au magari madogo. Lakini kwa safari ndefu, yanayotumika zaidi ni mabasi. Inasemekana kwamba mabasi mengi yanayotumika hapa nchini yanatokana na malori yaliyobadilishwa bodi na kutengenezwa kuwa mabasi. Mabasi yanayopatikana kutokana na hali hii, mara nyingi huwa hayana ubora na mengine yanakosa sifa ya kuweza kubeba abiria.
  Mheshimiwa Spika, miji yenye mabasi mengi yanayotoa huduma kutoka mkoa mmoja kwenda mwingine ni DSM mabasi 7573, Mbeya mabasi 1433, Mwanza mabasi1152. Miji hii haina tatizo la usafiri kutokana na barabara kuwa nzuri. Lakini kuna mikoa ambayo ina matatizo ya usafiri wa reli pia barabara ni mbaya sana, hivyo hata idadi ya mabasi yanayotoa huduma katika mikoa hiyo si kubwa; Rukwa mabasi 52, Manyara 51, Bukoba 21, Tabora 18, Lindi 54 na Kigoma 152. Serikali iharakishe kutengeneza barabara ili wananchi wapate usafiri ambao utakuwa wa haraka, lakini pia reli ni muhimu hasa kwa baadhi ya mikoa.
  Mheshimiwa Spika, ajali nyingi za barabarani zimesababisha watanzania wengi kupoteza maisha, na kumekuwepo na vyombo vingi vya kuzuia ajali, ikiwemo speed governor ambayo imeshindwa. Lakini kwa sasa kuna mpango mpya ulioletwa na Kampuni ya U-Track ambao kwa mantiki hauna tofauti na unaotumiwa na Jeshi la polisi-matrafiki maarufu kama tochi tofauti ni kwamba U-track unategemea sana minara ya simu za mikononi na Vodacom ni wadau wakubwa katika hilo.
  Mheshimiwa Spika, mamlaka inayodhibiti usafiri wa nchi kavu na majini (SUMATRA) imehusika vipi katika hili, mkataba una unaonyesha kuwa TABOA ndio walioingia makubaliano na U-Track Africa Ltd, kampuni ambayo kwa taarifa zilizopo ni kuwa imeshindwa kutoa tija nchini Kenya na uwezo wake ni mdogo sana. Ajali zinazotokea si za mabasi ya abiria tu bali ni magari ya aina zote, hivyo TABOA kuchukua jukumu la SUMATRA ni kosa kubwa, SUMATRA ndio wasajili wa magari yote yanayobeba abiria sio TABOA. Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali kulieleza Bunge kwa nini mambo yanayosababisha wananchi kuongezewa bei ya nauli bila kuhusisha asasi zilizoundwa kisheria kwa kazi yanatendeka bila Serikali kutoa taarifa?
  Mheshimiwa Spika; Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) ni taasisi muhimu katika kuandaa madereva, wataalamu wa sekta ya usafirishaji pamoja na kutoa ushauri wa kitaalamu kwa mamlaka mbalimbali katika kuboresha usafiri. Hata hivyo, chuo hicho kimekuwa kikikabiliwa na tuhuma na migogoro mbalimbali pamoja na matatizo ya kiutendaji hali inayoathiri ufanisi wa chuo hicho. Kambi ya upinzani inaitaka serikali kueleza namna ambavyo imeshughulikia matatizo mbalimbali katika Chuo hicho pamoja na kuwa na mkakati wa kukiboresha kwa ajili ya manufaa kwa taifa.

  Shirika la usafiri Dar Es Salaam (UDA).

  Mheshimiwa Spika, Serikali ilikuwa inamiliki asilimia 100 ya hisa za UDA. Mwaka 1983 Msajili wa Hazina alitoa Hisa 51% kwa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa madhumuni ya kwamba Jiji liboreshe na kuendeleza usafiri wa kisasa Jijini. Hivyo Serikali ilibakiwa na Hisa 49%. Kwa Tangazo la Serikali (Government Notice) Na. 543 la 1997, UDA iliwekwa chini ya Tume ya Rais ya Kurekebisha Mashirika ya Umma (PSRC) kwa lengo la kubinafsishwa.

  Mheshimiwa Spika, PSRC ilitangaza uuzaji wa Hisa za Serikali katika UDA ambapo kati ya wawekezaji waliojitokeza hakupatikana mwekezaji mahiri wa kununua hisa hizo. Zoezi hili lilirudiwa tena bila mafanikio, na hadi PSRC inamaliza muda wake mwezi Desemba, 2007 na shughuli zake kuchukuliwa na CHC, mwekezaji mwenye sifa alikuwa bado hajapatikana.
  Mheshimiwa Spika, Mwaka 2008 ilijitokeza Kampuni ya Simon Group ikiwa na nia ya kununua Hisa za Serikali. Simon Group alitambulishwa na Bodi ya UDA kwenye Kamati ya Bunge ya Miundombinu. Wizara ya Fedha baada ya kupata taarifa za kupatikana kwa mnunuzi wa Hisa za Shirika la UDA iliishauri Wizara ya Miundombinu iandae Waraka wa Baraza la Mawaziri ili kupata kibali cha Serikali cha kutekeleza azma hiyo. Mchakato huu haukukamilika kwa sababu Wadau walishauri kuwa Kampuni ya Simon Group ishindanishwe, na mwekezaji atakayepatikana afanyiwe tathmini.
  Mheshimiwa Spika, Wakati mchakato wa maandalizi ya Waraka ukiendelea, Bodi ya UDA bila kuihusisha Serikali (Msajili wa Hazina) zilipatikana taarifa kuwa hisa ambazo zilikuwa hazijagawiwa (unalloted shares) zimeuzwa kwa Kampuni ya Simon Group, hisa 7,880,000 kwa shilingi 1,142,643,935/= kwa mkataba uliosainiwa tarehe 11 Februari 2011.
  Mheshimiwa Spika, Kampuni ya Simon Group ilitakiwa ilipe shilingi Milioni 400 kama “commitment fee” kwenye akaunti binafsi ya Mwenyekiti wa Bodi kwa sababu iliambiwa kuwa akaunti za UDA zilikuwa na “overdraft” kwa wakati huo. Waliambiwa kuwa mara akaunti za UDA zitakapokuwa na fedha na overdraft kumalizika, hiyo “commitment fee” ingehamishiwa kwenye akaunti ya UDA. Inadaiwa kuwa kiasi cha shilingi milioni 320 zililipwa kwa utaratibu huo. Lakini hadi Kampuni ya Simon Group ilipochukua uongozi wa UDA, fedha hizo zilikuwa bado hazijahamishiwa kwenye akaunti ya UDA.
  Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa vifungu vya mkataba huo, ilitakiwa mkutano mkuu maalum wa kampuni (extra ordinary General Meeting) ufanyike ndani ya wiki mbili tangu mkataba huo ulipotiwa saini ili Kampuni ya Simon Group itambulishwe kwa Wanahisa wengine, bodi ya UDA iliyopo ivunjwe na iundwe Bodi mpya na menejimenti ya UDA ikabidhiwe kwa Simon Group. Hata hivyo, mkutano huu maalum haukufanyika kama ilivyotarajiwa.
  Mheshimiwa Spika, mkutano maalum wa wanahisa uliohudhuriwa na Simon Group na Halmashauri ya Jiji ulifanyika tarehe 10 Juni 2011. Katika mkutano huu, Msajili wa Hazina hakuhudhuria. Kwenye mkutano huu; Meneja Mkuu wa UDA alisimamishwa kazi, wajumbe wa Bodi ya UDA (Iddi Simba, Bakari King’obi na Salum Mwanking’inda) walisimamishwa, mamlaka ya wanaosaini akaunti za UDA kutoa pesa yalitenguliwa na Simon Group alipewa mamlaka ya kuiendesha UDA.
  Mheshimiwa Spika, kambi ya Upinzani imebaini kuwa Mkutano uliofanyika tarehe 10 Juni, 2011 kati Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam na Wajumbe kutoka Kampuni ya Simon Group haukuitishwa kihalali kwa sababu ulikiuka Katiba (Articles of Association) ya UDA (Kifungu cha 45) na kikao hicho kilikuwa hakina akidi (quorum) kwa kukosekana Msajili wa Hazina. Kwa hiyo, kikao hicho cha tarehe 10 Juni 2011 kilikuwa hakina mamlaka ya kufanya maamuzi, na maazimio yote yaliyofikiwa katika kikao hicho na hivyo yalikuwa batili.
  Aidha, kambi ya upinzani imebaini kuwa Serikali kwa kipindi cha zaidi ya miaka mitatu imekuwa haina uwakilishi kwenye Bodi ya UDA. Hali hii iliifanya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kuwa na maamuzi makubwa katika UDA na Serikali kushindwa kufahamu ni nini kilichokuwa kinaendelea ndani ya Kampuni ya UDA. Pia, kwa kipindi chote hiki haujawahi kufanyika mkutano wa wanahisa wa kila mwaka (Annual General Meeting) au mkutano maalum (extra ordinary General Meeting).
  Mheshimiwa Spika, kutokana na mwenendo huu ni dhahiri kuwa kumekuwa na ubadhirifu mkubwa ndani ya uendeshaji wa shirika la UDA na hali hii inapaswa kufanyiwa kazi mapema kwani inavyoonyesha ni kuwa uuzaji huu wa hisa na ubadilishaji wa uendeshaji wa shirika , unaelekea katika kutaka kutumia mali za UDA kwa masilahi binafsi zaidi badala ya kuliimarisha shirika hili.
  Kambi ya Upinzani, inataka kupata majibu yafuatayo juu ya suala hili:
  (i) Nini msimamo /tamko la serikali katika suala hili na haswa ikizingatiwa kuwa mkataba ulioingiwa haukushirikisha wanahisa muhimu.
  (ii) Je, wizara imechukua hatua gani mpaka sasa kuhusiana na waliohusika kwenye suala hili?
  (iii) Mali za UDA zilikuwa na thamani kiasi gani? Na ni lini tathimini ya mali hizo ilifanyika, na ni nani walihusika katika kugharimia utathimini huo?

  SHIRIKA LA RELI TANZANIA (TANZANIA RAILWAYS
  CORPORATION – TRC)
  Mheshimiwa Spika; Reli ya Kati ni kichocheo kikubwa sana cha uchumi kwa wananchi wanaoishi katika mikoa ambayo imeunganishwa na reli hii, na pia ni kiunganishi kikubwa kati ya bandari na nchi ambazo hazina bandari. Hivyo, basi jambo la kwanza ni kuiboresha reli ya sasa ili ifanye kazi kwa uwezo mkubwa kusafirisha abiria na mizigo. Kwa miaka ya hivi karibuni, shirika letu hili limeyumba sana kutokana na uendeshwaji mbovu wa shirika hili, na uchakavu wa miundombinu.
  Mheshimiwa Spika, bajeti iliyoombwa mahitaji halisi kwa fedha za matumizi ya kawaida ni sh Bilioni 63.68 na fedha iliyotengwa na Serikali ni shs, milioni 900 kiasi ambacho ni pungufu sana ya fedha iliyoombwa. Je, kwa hali kama hii kuna jambo linaweza fanyika? Kambi ya Upinzani kwa kuona umuhimu wa reli yetu, ilitenga kiasi cha shilingi bilioni100 katika bajeti mbadala kuliwezesha shirika la Reli Tanzania kufanya kazi yake ya msingi ya kusafirisha mizigo na abiria.
  Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali kutoa ufafanuzi ni jinsi gani mtandao wa mawasiliano wa fiber optic unaoanzia Dar es Salaam hadi Mwanza unaomilikiwa na Shirika unavyotumika kibiashara na kama hautumiki kibiashara, kuna mpango gani wa mtandao huo kutumika kibiashara?
  Mheshimiwa Spika, moja ya sababu zinaoongeza gharama za uendeshaji wa shirika la reli ni tozo ya mafuta yanayoendeshea injini za shirika; tozo hiyo ni kwa ajili ya mfuko wa barabara. Kambi ya Upinzani haioni sababu ya shirika la reli kuchangia mfuko wa barabara, kwani ni kuwaimarisha washindani wa shirika hilo ambao ni wasafirishaji wa mizigo kwa njia ya barabara. Kama makampuni ya madini yanasamehewa kulipa tozo hiyo wakati ni watumiaji wa barabara ni kwanini shirika la reli nalo lisisamehewe kulipa tozo hiyo?

  Mheshimiwa Spika, kutokana na sababu mbalimbali TRL ikiwa chini ya menejimenti ya RITES Ltd kwa takribani miaka mitatu imeshindwa kwa kiasi kikubwa kuhakikisha kuwa miundombinu ya reli, injini za treni, mabehewa ya mizigo na ya abiria pamoja na mali zote zilizokabidhiwa kwake vinafanyiwa matengenezo na kukarabatiwa kama ilivyoainishwa kwenye Concession Agreement. Kwa sababu hizi hali ya sasa ya miundombinu ya reli, injini za treni, mabehewa ya mizigo na ya abiria pamoja na mali zingine ni mbaya sana.
  Mheshimiwa Spika, TRL ilipoanza kazi tarehe 1 Octoba, 2007 ilikabidhiwa jumla ya injini 79, mabehewa ya mizigo 1,357 na mabehewa ya abiria 97 yaliyokuwa yakitumiwa na TRC. Lakini badala yake TRL kwa makusudi iliamua kukodisha injini za treni 25 na mabehewa ya abiria 23 kutoka India.
  Hata hivyo, kutokana na kutofanyiwa matengenezo, kati ya injini 79 zilizokabidhiwa TRL na serikali tarehe 1 Octoba 2007, ni injini 39 tu zinazofanya kazi hivi sasa tena zikiwa chini ya kiwango cha ubora, huku injini 40 zikiwa zimekufa kutokana na kutokarabatiwa.
  Mheshimiwa Spika, Kati ya mabehewa 1,357 ya mizigo ni 638 tu yanayofanya kazi na kati ya mabehewa 97 ya abiria ni 45 tu yanayofanya kazi na kwamba yote hayo yako chini ya kiwango cha ubora. Kwa upande wa mabehewa ya mizigo1,357 yaliokabidhiwa TRL hadi sasa mabehewa 719 hayafanyi kazi, na kwa upande wa mabehewa ya abiria 97 mabehewa 52 hayafanyi kazi.
  Mheshimiwa Spika, Kwa ujumla hali hii ilisababisha hadi kufikia mwezi Aprili, 2010 toka kubinafsishwa TRC shirika hilo limepata hasara ya Shilingi bilioni 98.386 kutokana na kushuka kwa usafirishaji wa mizigo kutoka tani laki 5.7 zilizosafirishwa mwaka 2007 hadi kufikia tani laki 2.7 mwaka 2010.
  Mheshimiwa Spika, treni za abiria kutoka Dar es Salaam kwenda Kigoma na Mwanza zilipungua kutoka treni nne kwa wiki hadi kufikia treni moja kwa wiki kwenda Kigoma pekee mwaka 2010. Hali hii ilipelekea idadi ya wasafiri wa treni kupungua, kwa mfano, abiria 290,046 walisafiri mwaka 2010, wakati mwaka 2009 walisafiri abiria 543,000, hii inaonyesha upungufu wa abiria 252,954 karibu na nusu ya abiria waliosafiri mwaka 2009 sawa na 46.6%. Hii ni aibu kwa Serikali inayotarajia kusherekea kutimiza miaka 50 ya uhuru, badala ya kwenda mbele tunarudi nyuma.

  Mheshimiwa Spika, makubaliano ya Serikali katika ukodishaji wa TRC yalikuwa ni kuboresha sekta ya usafirishaji kwa njia ya reli kupitia utendaji wenye tija kutoka kwenye sekta binafsi. Serikali ilitarajia pia kuwa TRL ingewekeza kwenye miundombinu ya reli, injini za treni, mabehewa na vifaa mbalimbali vya kufanyia kazi ili kuongeza uwezo na ufanisi katika sekta ya usafiri wa reli.
  Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inasema kuwa kitendo cha TRL kutelekeza injini 79 zilizokuwa zikitumiwa na TRC na kuamua kukodisha injini chakavu toka INDIA ni hujuma ambayo tunadhani inatakiwa iwe mojawapo ya ajenda katika kadhia nzima ya uvunjwaji wa mkataba na urejeshwaji wa hisa ambazo RITES wanamiliki.

  Mheshimiwa Spika, Mpango wa Biashara wa RITES/TRL uliowasilishwa Serikalini ulionyesha kutakuwepo na treni sita za abiria kwa wiki kuanzia Dar es salaam kwenda Kigoma na Mwanza. TRL ilitarajiwa kuanza kupata faida kuanzia mwaka wa kwanza wa biashara, lakini Mwaka huohuo wa 2007 TRL ilipata hasara ya Shilingi bilioni 4.87, mwaka 2008 hasara ilikuwa Shilingi bilioni 26.914, mwaka 2009 hasara ilikuwa Shilingi bilioni 56.532 na hasara iliyopatikana mwaka 2010 mpaka kufikia mwezi Aprili ilikuwa Shilingi bilioni 10.07.

  Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Serikali imeamua kuchukua hisa zote za kampuni ya reli Tanzania, Serikali haina budi kuiwezesha TRL kuwekeza katika miradi muhimu ya maendeleo, mtaji wa kufanyia kazi pamoja na kulipa madeni yote ambayo yataachwa na menejimenti ya RITES kama ilivyo kubaliwa katika makubaliano ya kuvunja mkataba.
  Mheshimiwa Spika, mawasiliano kati ya RITES na Serikali invoice na. 055 ya mwezi Julai 2011, inaonyesha kuwa Serikali hadi sasa bado inailipa RITES Management Service Fee ya dolla za Marekani US$10,982 kwa mwezi. Pia Invoice na. 056 ya julai ya dolla za Marekani 40,498.20,kama fedha za mishahara kwa watumishi wanne wa RITES, Pesa hizo Zilitakiwa ziingizwe akaunti na. 0011407376, AXIS BANK MUMBAI INDIA.

  Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali kutoa ufafanuzi wakati mkataba na RITES ulishavunjwa. Inakuwaje RITES waendelee kulipwa wakati mkataba umeishavunjwa? Aidha, serikali inatakiwa kulipia matengenezo ya injini aina ya 88 class kiasi cha dolla za kimarekani 1,538,000 tarehe 30 Septemba 2011( EXTRACT FROM DEED OF SETTLEMENT BETWEEN RITES & GOT barua ya tarehe 20.07.2011 iliandikwa na HL Chaudhary, Mkurugenzi Mtendaji wa TRL). Kambi ya Upinzani inaona huu ni mchezo wa kuigiza ambao Serikali inawafanyia watanzania kama mkataba umevunjwa ni kwa vipi ndg. Chaudhary bado ndiye Mkurugenzi Mtendaji na nyaraka zote zinazohusiana na shirika hilo anaendelea kuzimiliki yeye?
  Kambi ya Upinzani inaomba kupata maelezo ni kwa vipi pale mbia anaposhindwa kutimiza masharti yaliyomo kwenye mkataba na alipwe pale mkataba utakapovunjwa?
  Mheshimiwa Spika, kumbukumbu za Serikali zinaonyesha kuwa tumeingia gharama kiasi cha shilingi bilioni 63.68 katika kufidia kuvunjwa kwa mkataba baina ya TRC na RITES ya India. Kambi ya Upinzani inasema ili kuwa makini na masuala ya matumizi ya fedha za wananchi ni lazima wahusika wakuu wa mkataba ulioingiwa, nao wawajibishwe kwa uzembe kama ambavyo waheshimiwa Basil Pesambili Mramba na Daniel Yona pamoja na Grey Mgonja walivyofunguliwa mashtaka ya kulitia Taifa hasara.
  Mheshimiwa Spika, Jambo hili likiachwa bila ya wahusika kuchukuliwa hatua itaonekana kuwa sheria zina bagua (double standards) katika kushughulikia wale wote wanaoliingizia hasara taifa letu au wahujumu uchumi.

  Mheshimiwa Spika, kuna reli iendayo ukanda wa Kaskazini (Tanga, Kilimanjaro) ambayo kwa muda mrefu imeshindwa kufanya kazi na hivyo kusababisha usafirishaji wa mizigo kutumia njia ya barabara jambo linalosababisha uharibifu wa mara kwa mara wa barabara zetu. Ni tarajio letu kuwa sasa ni muda mwafaka wa Serikali kuunganisha usafiri wa reli kati ya Dar es Salaam, Tanga na Kilimajaro hii itasaidia kwa kiasi kikubwa kuokoa fedha za matengenezo ya mara kwa mara ya barabara na kupunguza ajali za mara kwa mara zinazosababishwa na malori ya mizigo katika njia hiyo.

  Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inashauri yafuatayo kama mpango wa muda mfupi wa kuliimarisha shirika la reli:
  [i.] Serikali iwekeze Mtaji kutoka katika vyanzo vya ndani ya nchi kama vile kuwashirikisha wadau ambao wako tayari.
  [ii] Serikali kuunda upya Bodi ya wataalamu wa mambo ya reli, Menejimenti adilifu na mifumo mipya ya kiutawala ya kuendesha RELI
  [iii]Ukarabati wa NJIA YA RELI, MITAMBO, INJINI NA MABEHEWA ya abiria na mizigo ufanywe na wataalamu Wazalendo.
  [iv] Kwa kuwa tatizo kubwa ni Injini za kuvuta mabehewa tunashauri Serikali inunue Injini haraka iwezekanavyo kwani gharama ya Injini moja ni kati ya Usd 2,000,000 na usd 2,500,000.
  [v] Kwa kuwa Ufanisi wa Bandari ya Dar es salaam,Tanga Kigoma na Mwanza utatokana na Reli hivyo basi tunapendekeza Kampuni ya Reli na Bandari ziungane kama ilivyokuwa wakati wa Jumuiya Ya Afrika ya Mashariki.
  [vi] Kuboresha mazingira ya kufanyia kazi, maslahi ya wafanyakazi ikiwa ni pamoja na mishahara , madai mbali mbali n.k
  [vii] Kuwe na mafunzo kwa watumishi ya mara kwa mara [skill upgrading]
  Mheshimiwa Spika, kuna mawasiliano ya barua kati ya wizara ya Uchukuzi ya tarehe 19, Julai 2011 yenye kumbukumbu Na.WUC/GEN/2011/89 iliyokwenda kwa KAMPUNI ya Glasgow International General Trading International LLC, YA Dubai kuhusiana na kukaribishwa kwa kampuni ya IPEX ambayo ni kampuni dada, kwenye kikao na wizara cha tarehe 27/Julai 2011 kwa ajili ya kujadiliana na ikiwezekana kusaini MOU kati ya serikali na mwekezaji huyu kwa ajili ya matengenezo na uendeshaji wa reli zetu.
  Mheshimiwa Spika, zipo taarifa kwamba serikali imesaini MOU na kampuni ya Dubai (HLG) kwa ajili ya kufanyia marekebisho reli ya kati na mnamo tarehe 05/07/2011 kampuni ya HABTOOR LEIGHTON GROUP ya Dubai, waliandika barua kwenda kwa Cansulate General wa Tanzania ndugu Cleophas Kasenza Ruhumbika wa Dubai kuhusu mkataba kati ya serikali na kampuni hii (MOU) ambayo ilikuwa inaishia tarehe 4 Agusti 2011 ili aweze kuongezewa muda wa miezi 3 hadi Novemba 4 ,2011 .
  Sababu walizotoa kwenye barua yao ni pamoja na kuhitaji muda zaidi kwa ajili ya kwenda kuwasiliana na taasisi mbalimbali za kifedha ili waweze kupata fedha za kutekeleza ujenzi huo,
  Kambi ya Upinzani inahoji, hivi serikali inatumia vigezo gani katika kuingia mikataba na makampuni mbalimbali ya nje na haswa ikizingatiwa kuwa hii kampuni inaonyesha dhahiri kuwa haina fedha ni mpaka waweze kukopa na wameshindwa kupata mkopo hadi muda wa MOU unamalizika.
  Mheshimiwa Spika,wakati tunahangaika kuvunja mkataba na RITES wakati huohuo tunaenda haraka mbele kutafuta mbia mwingine, Kambi ya Upinzani inataka kujua serikali imezingatia mazingira yaliyosababisha mkataba na RITES kuvunjwa? Je, Masilahi ya taifa yanazingatiwa?
  Mheshimiwa Spika, mnamo tarehe 13-21 Juni 2011 benki ya dunia ilituma wataalamu wake kuja Tanzania kwa ajili ya kufuatailia hali ya shirika letu la reli na kikubwa walikuwa wanakuja kukagua kama tunastahili kupata mkopo wa dola 150 milioni ambazo tuliomba, na hii inathibitishwa na barua ya tarehe 06 Juni 2011 yenye kumbukumbu Na.CA230/505/01/93 iliyosainiwa na F.Mwanyika kwa niaba ya katibu mkuu wa wizara kwenna kwa mameneja wa RAHCO na TRL.
  Mheshimiwa Spika, miongoni mwa mambo ambayo mameneja hawa walitakiwa kutengeneza ni pamoja na mpango kazi (constructive business plan) na mpango wa kusimamia mradi husika (project implementation plan).
  Kambi ya Upinzani , tunataka kupata majibu hivi ni kweli kuwa shirika letu la reli halina mpango kazi ? na kama haupo kwanini tunawalipa RITES ?walikuwa wanafanya nini kwa muda wote wa mkataba?
  Je, Serikali ilifanikiwa kupata mkopo huu wa benki ya dunia? Na kama ndio fedha hizo zimeigizwa kwenye bajeti hii? Na zitatumika kufanya jambo gani?
  Shirika la reli la Tanzania na Zambia (TAZARA)

  Mheshimiwa Spika, ufanisi wa reli hii umepungua kwa kiasi kikubwa kutokana na kupungua kwa kiasi kikubwa cha injini zake na kuchakaa kwa mabehewa kulikochangiwa kwa kiasi kikubwa kwa bajeti finyu na migomo ya wafanyakazi inayohusiana na ubaguzi ki-maslahi kati ya wafanyakazi wa Tanzania na Zambia. Mwaka 2010 wasafiri walikuwa 757,987 ikilinganishwa na 794,983 mwaka 2009 ukiwa ni upungufu wa asilimia 4.7%. Barabara zimeendelea kuharibika kutokana na kubeba mizigo mizito inayotoka na kupelekwa mikoa ya Nyanda za juu kusini pamoja na nchi jirani ya Zambia hasa shaba, mbao, vyuma na cement.
  Kambi ya upinzani, tunataka kupata majibu juu ya malalamiko kuhusiana na mkataba ambao TAZARA kwa upande wa Zambia waliingia na shirika la reli la Zambia RSZ ambao uliridhiwa na bodi mwezi mei 2011 , kwa ajili ya shirika hilo kuendesha shughuli za TAZARA na mwaka wa fedha 2009/2010 RSZ waliweza kuchukua asilimia 44 ya mapato ya TAZARA ambayo yalikuwa US$ 38 milioni. Je? Katika mkataba huu serikali ilishiriki kwa kiasi gani? Na nini manufaa ya mkataba huu kwa taifa la Tanzania.

  MAMLAKA YA USAFIRI WA ANGA- (TANZANIA CIVIL AVIATION AUTHORITY – TCAA)
  Mheshimiwa Spika, mamlaka ya usafiri wa anga ni moja kati ya mamlaka muhimu sana katika kuchangia mapato ya Taifa. Kwa mantiki hiyo, hapana budi kwa serikali kupitia wizara ya Miundombinu kuitilia maanani mamlaka hii na kuipatia kila msaada ili ibaki kuwa miongoni mwa mihimili mikuu ya uchumi wa Taifa.
  Mheshimiwa Spika, mamlaka hii inakabiliwa na changamoto ya udhaifu wa miundombinu muhimu katika kutekeleza majukumu yake. Karibu viwanja vingi vikiwemo vile vinavyomilikiwa na TANAPA na Idara ya Wanyama Pori ni changamoto na kikwazo kinachowafanya watalii wasifike kwa urahisi kwenye vivutio muhimu vilivyomo nchini mwetu. Kwa hivyo Kambi ya Upinzani inaitaka serikali pamoja na hali inayoelezwa kuwa uchumi wetu ni duni, lazima itoe kipaumbele katika kuboresha miundombinu hiyo. Ikumbukwe kuwa shilingi hutafutwa kwa shillingi. Bila kuwekeza watalii wala fedha haiwezi kuja tu!

  Mheshimiwa Spika, gharama kubwa ya kununua na kukarabati mitambo ya kuongozea ndege bado nayo ni changamoto inayoikabili mamlaka. Hii inatokana na mabadiliko makubwa na ya haraka ya Teknolojia na utaalamu katika mitambo ya kuongoza ndege. Sambamba na hili, mamlaka lazima iwapatie wafanyakazi wake mafunzo ya mara kwa mara ili waendane na mabadiliko hayo.

  Mheshimiwa Spika, kwa kipindi cha takriban miaka 12 kampuni iliyopewa dhamana ya kuendeleza uwanja wa ndege wa Kilimajaro imewekeza kiasi cha dolla za kimarekani milioni 4 tu sawa na sh. Bilioni 6, wakati imekusanya jumla ya sh.bilioni 56.94 kutoka vyanzo mbalimbali katika uwanja huo. Kushindwa kuuweka uwanja huo katika mazingira bora na ya kisasa ni kasoro kubwa itakayosababisha uwanja huo kukosa kabisa ndege za nje kutua.
  Mheshimiwa Spika, badala ya serikali kuendeleza porojo za kujenga uwanja wa ndege wa kimataifa wa Misenye, mkoani Kagera na uwanja wa kimataifa wa ndege wa Bukoba Mjini eneo ambalo lina umbali wa takribani Km 50 kama ambavyo Rais wa Jamhuri ya Muungano, Jakaya Kikwete alivyoahidi wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu uliyopita, serikali iachane na porojo hizo na badala yake iwekeze katika ukarabati mkubwa katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kilimanjaro.

  Mheshimiwa Spika, hatua hii ya kuachana na porojo za ujenzi wa uwanja wa ndege wa Misenyi na Bukoba Mjini ni muhimu kwa kuwa jirani zetu wameanza kujenga uwanja wa ndege wa kisasa eneo la Taveta mpakani mwa Tanzania na Kenya kwa lengo la kukiua kabisa kiwanja cha ndege cha Kilimanjaro na hivyo biashara yote inayohusiana na usafiri wa anga kati ya Afrika ya Mashariki na mataifa mengine kuwa vituo vyake Nairobi, Mombasa na Taveta , jambo ambalo litaathiri kwa kiwango kikubwa biashara ya utalii nchini.
  Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali kupanga kibiashara zaidi ili kukabilina na ushindani wowote wa kibiashara ambao unatishia sekta zetu muhimu za kiuchumi. Serikali haina budi kuboresha huduma (ground handling facilities) zinazosababisha wafanyabiashara wetu wa bidhaa zinayowahi kuharibika kwenda uwanja wa Ndege wa Nairobi kwa ajili ya kufuata huduma hiyo huko.

  Mheshimiwa Spika, TCAA waliweka ushindani katika viwanja vyote vya ndege isipokuwa KIA katika suala la ‘ground handling’ ambapo ni Kampuni moja tu ya Swissport inaruhusiwa kutoa huduma. Kwa sababu ya ukiritimba ni rahisi kwa kampuni hii kukataa kutoa huduma kwa makampuni mengine yenye wateja na hata kufanya huduma hizo kuwa ghali sana. Wizara iseme ni lini itaondoa ukiritimba huu ili kuongeza ufanisi katika huduma za usafiri wa anga.
  USAFIRFI WA ANGA
  Shirika la ndege ya Tanzania ( ATCL)
  Mheshimiwa Spika, ni dhahiri kuwa hauwezi kuzunguzmzia usafiri wa anga hapa nchini bila ya kuzungumzia Shirika la ndege ya Taifa letu (ATCL). Shirika hili ndilo kioo cha Taifa nje ya nchi, hivyo basi Serikali haina budi kufanya kila iwezalo kuhakikisha shirika letu linafanyakazi.
  Mheshimiwa Spika, tathmini ya ufanisi katika Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) ilibaini mambo yafuatayo ambayo yamesababisha Kampuni hii kushindwa kabisa kujiendesha:
  • Shirika inakabiliwa na madeni yanayofikia shilingi 23.3 bilioni
  • Kampuni ina mtaji hasi wa shilingi 14 bilioni, hivyo inahitaji kupatiwa mtaji
  • Kuanzia mwaka 2007/2008 serikali ilisitisha rasmi utoaji wa ruzuku ya shilingi milioni 500 kwa mwezi kwa ATCL hivyo kuiacha Kampuni bila msaada au ruzuku yoyote.
  • Ukiritimba uliokidhiri katika kufanya maamuzi yahusuyo shirika.
  • Kwa zaidi ya miaka mitano sasa Serikali imetafuta mwekezaji wa kuwekeza kwenye ATCL bila mafanikio.

  Mheshimiwa Spika, jitihada za makusudi zinatakiwa kufanywa ili kuiokoa ATCL ili hata kama mwekezaji atapatikana aikute Kampuni ikiwa inajiendesha, hivyo basi Kambi ya Upinzani inaungana kukazia mapendekezo yaliyotolewa na Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) kuwa:
   Serikali kuchukua madeni yote ya ATCL na baada ya hapo kutoa mtaji (unaofikia dola za kimarekani 31 bilioni) wa kuanza kuliendesha Shirika hili ikiwa ni pamoja na kutoa dola laki saba ili kuirudisha ndege ya ATCL iliyopo kwenye matengenezo ili ianze kufanya kazi mara moja.
   Serikali kuangalia uwezekano wa kuunda upya Bodi na Menejimenti ya ATCL ili iweze kukabiliana na changamoto zilizopo kwenye Shirika hilo kwa haraka na kwa ufasaha imetoa mapendekezo yake kuhusu ufufuaji wa ATCL kwenye sehemu ya maoni katika taarifa hii.
  Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani katika hotuba yake ya bajeti mbadala ilipendekeza Shirika letu la Ndege lirudi tena kwenye biashara, hivyo ilitenga sh. Bilioni 200 kulifufua upya shirika la ndege la ATC. Hata hivyo, tunashauri kwamba Serikali iangalie uwezekano wa kurekebisha umiliki wa Shirika la Ndege la Taifa kwa kuhusisha Taasisi za Umma ambazo zinafaidika zaidi katika biashara zao kutokana na uwepo wa shirika la ndege la Taifa. Pia tunaitaka Serikali itoe maelezo ndege iliyokuwa ikitoa huduma kati ya Dar –Kigoma kupitia Tabora iko wapi?
  Mheshimiwa Spika, kwa sasa ndege za Pecision hazitui uwanja wa Tabora na Kigoma kutokana na viwanja hivyo kutokuwa na viwango. Hivi sasa ni vigumu sana kusafirisha wagonjwa wanaohitaji huduma ya haraka katika hospitali za rufaa. Hii kauli ya miaka mingi ya Serikali kuwa itaukarabati uwanja wa ndege wa Kigoma ni hadithi ambayo tunauliza itatekelezwa lini?
  Mheshimiwa Spika, tunamtaka Mheshimiwa Waziri wakati wa majumuisho atueleze yafuatayo:
  a) Kwa kiasi gani mpango huu umefanikiwa?
  b) Ni makampuni gani binafsi yaliyoshirikishwa katika mpango huu na katika maeneo gani?
  c) Faida gani na kiasi gani imepatikana kutokana na ushiriki wa sekta binafsi katika mpango huu?
  USAFIRI WA MAJINI
  Mheshimiwa Spika, tuna wasiwasi juu ya suala zima la usimamizi na ukaguzi wa vyombo vya usafiri wa majini, kama vile meli na maboti. Tunaitaka serikali kupitia SUMATRA iweke utaratibu ulio wazi na makini juu ya usimamizi na ukaguzi wa vyombo vya usafiri wa majini. Taarifa ya hali ya uchumi inaonyesha kuwa ajali zilizotokea baharini na katika maziwa na kusababisha kupotea watu 54 mwaka 2010 kulinganisha na watu 40 mwaka 2009. Kambi ya Upinzani inaliona hili kuwa ni kutokuwepo kwa mfumo wa ukaguzi wa mara kwa mara kwa vyombo vinavyofanya safari baharini na maziwani.
  MAMLAKA YA BANDARI
  Mheshimiwa Spika, mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), ni miongoni mwa mihimili muhimu ya taifa katika kukuza na kuinua uchumi wa nchi, aidha bandari hii inahudumia takribani nchi 6. Umuhimu wa Mamlaka hiyo, unatokana na kuingizia serikali mapato ya kutosha. TPA inasimamia bandari kuu tatu nchini zilizopakana na bahari ya Hindi. Hizi ni Tanga, Mtwara na Dar es Salaam ambayo ndio kubwa na kitovu cha biashara zote za kimataifa. Pia TPA inasimamia bandari nyinginezo ndogondogo kama vile Kilwa, huku kukiwepo mkakati wa kupanua bandari ya Bagamoyo. Bandari nyingine ziko katika maziwa Nyasa, Tanganyika na Victoria kukiwepo bandari kama vile Mbambabay, Itungi, Kigoma, Mwanza, Kemondo, Bukoba na Musoma. Awali bandari hizo zilikuwa chini ya lililokuwa Shirika la Reli Tanzania (TRC).
  Mheshimiwa Spika, Hiyo ndio maana kaulimbiu ‘Bandari ni Lango la Biashara’ hutumika sana kwa maana ya umuhimu wake katika kukuza biashara na uchumi kitaifa, na hii ndiyo bahati ambayo nchi yetu imepewa na Mwenyezi Mungu kwa kulinganisha na nchi jirani zetu. TPA kupitia vyanzo vyake, imekuwa ikikusanya mapato kusaidia maendeleo ya nchi, licha ya kukabiliwa na changamoto nyingi na hasa malalamiko yahusuyo utendaji kazi wake usioridhisha.

  Mheshimiwa Spika, Miongoni mwa malalamiko ya muda mrefu, ni mizigo kukaa muda mrefu bandarini, mrundikano wa makontena na wizi wa vipuri vya magari unaodaiwa kufanyika katika bandari ya Dar es Salaam, Changamoto nyingine ni kuongezeka kwa meli katika bandari hiyo kutoka nje na ushindani uliopo na bandari za Mombasa, Afrika Kusini na Msumbiji. Hivyo, Kambi ya Upinzani inaiasa Mamlaka kukaa kibiashara zaidi ili kukabiliana na changamoto hizo.

  Mheshimiwa Spika, taarifa ya Benki ya Dunia ya Julai 2011 inaonyesha kuwa msongamano wa mizigo katika bandari ya Dar es Salaam ulikuwa ukiliingizia hasara taifa letu ya dolla za Kimarekani milioni 2 kwa siku kwa mwaka 2009. Hii ni hasara kubwa sana kwa nchi change ambayo inapambana kuondokana na umasikini, Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali iwaeleze wananchi ni mkakati upi umewekwa kumaliza hasara hii?

  Mheshimiwa Spika, taarifa ilitolewa na jarida ya “the Econimist, 2009” inasema kuwa China imeamua kuwekeza katika kupanua miundombinu ya bandari za Uganda na Kenya ili kupata urahisi wa kusafirisha malighafi yake toka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo badala ya kutegemea bandari ya Dar es Saalam ambayo imejaa ukiritimba. Kambi ya Upinzani inaona nchi yetu haikukaa kiushindani katika kuimarisha na kuendeleza vile vitu ambavyo sisi tunavyo kwa kulinganisha na jirani zetu na mwisho wake ni kupoteza fursa zetu kiuchumi, kama inavyotokea kwenye shirika la ndege na sasa kwenye bandari ya Dar es Salaam.

  Mheshimiwa Spika, takwimu zinaonyesha kuwa mamlaka ya usimamizi wa bandari ilihudumia shehena zenye uzito wa tani 10,045,462 kwa mwaka 2010 ambazo ni ongezeko la asilimia 12.4 ukilinganisha na mwaka 2009. Ongezeko hili linatokana na uingizaji mkubwa wa shehena za magari, mafuta, mbolea na ngano kwa ajili ya nchi jirani. Ongezeko kubwa lilitokea katika bandari ya Dar es Salaam. Shehena katika bandari za Kigoma na Mtwara zilipungua kutokana na kupungua kwa mazao yanayosafirishwa nje ya nchi, kukosekana kwa meli zinazofanyakazi katika mwambao wa bahari ya hindi.

  Mheshimiwa Spika, kukosekana kwa meli maalum ya kubeba mabehewa katika ziwa viktoria na Tanganyika nalo ni tatizo kubwa sana linalosababisha utendaji wa bandari kuwa wa hali ya chini. Aidha, kukosekana kwa miundombinu imara ya kuunganisha bandari na vyanzo vya shehena nalo ni tatizo kubwa.

  Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa serikali ni kuwa tathmini ya upanuzi wa bandari ya Kigoma umekamilika na wizara hiyo kupitia msimamizi wa Bandari ya Kigoma na kuwasilisha maombi ya dola milioni 10 za Marekani katika Shirika la JICA baada ya kuonyesha nia ya kugharamia mradi huo. Aidha JICA wanafanya tena tathimini halisi nyingine ya mradi huo huo. Kambi ya Upinzani inataka kuelewa ni nini maana ya tathmini kufanywa mara mbilimbili, je huu sio ucheleweshwaji wa muda usio na msingi wowote? Muda ni mali pindi upoteapo si rahisi kuupata tena!!!
  Mheshimiwa Spika, taarifa ya Benki ya Dunia inasema kuwa upanuzi wa bandari yetu ya Dar es Salaam kwa kushirikiana na sekta binafsi unashindikana kutokana na kuingiliwa na wanasiasa na hivyo kusababisha nchi yetu kuzidi kupoteza fursa za kibiashara na nchi jirani hasa Uganda, Rwanda, Burundi na DRC.


  Ujenzi wa Gati (Berths) 13 na 14 Bandari ya DSM.
  Mheshimiwa Spika, kuna pendekezo la kujenga gati kwenye mlango namba 13 na 14 na ambazo zitajengwa kutokana na mkataba ambao umesainiwa kati ya serikali ya Tanzania na ile ya China wa kupata mkopo kutoka Exim Benki ya China ambao unafikia kiasi cha dola za kimarekani US$ 525 Milioni.
  Mheshimiwa Spika, upembuzi yakinifu uliofanywa na CPCS Transcom ambao ulifanyika mwaka 2009 ulionyesha kuwa kujenga Gati hizo gharama zake zilikuwa ni kiasi cha dola za Kimarekani 280 milioni, ila kwa sasa gharama hizo zimepanda hadi kufikia dola milioni 525 na hizi gharama zinapigiwa chapuo na kampuni la Ujenzi la kichina ambalo linaitwa China Road &Bridge, hizi ni gharama kubwa mno ukilinganisha na gharama ambazo zinatumika katika ujenzi kama huo ambao unafanyika katika bandari ya Mombasa kule Kenya.
  Mheshimiwa Spika, ukiangalia utaweza kuona kuwa mradi huu wa upanuzi wa bandari yetu unafanyika huku tukipata mkopo kutoka China na hapo hapo kampuni za kichina ndio zimefanya upembuzi wa ujenzi na kuja na gharama kubwa ukilinganisha na hali halisi na hata hivyo kampuni za kichina ndio zinataka kupewa kazi kwa ajili ya ujenzi wa Gati husika.
  Kambi ya Upinzani inaona kuwa ili kuweza kujenga Gati hizi na kuweza kuimarisha bandari yetu hatua zifuatazo zichukuliwe:
  (i) Kandarasi kwa ajili ya ujenzi iwe ya wazi na itangazwe ili makampuni yaweze kushindanishwa na hivyo tuchague aliye na gharama nafuu zaidi na mwenye sifa ndio apewe kazi ya ujenzi huo.
  (ii) Tutumie mfumo wa kujenga Gati hizi kwa mfumo wa ‘Built-Operate-Transfer’ BOT. Na hili litavutia mitaji kutoka sekta binafsi na hivyo ujenzi uweze kufanyika.
  (iii) Kuchukua Mkopo huu wa US$ 525 milioni wenye masharti haya ni wizi mkubwa wa mchana kwani tutakuwa tunalipia madeni makubwa kuliko inavyotakikana na ambayo tungeweza kuyapunguza .Na haswa ikizingatiwa kuwa fedha hizi zote zitaelekezwa China kwani masharti yake ni kuwa lazima mkandarasi atoke China.

  Hali ya usalama katika Bandari ya DSM
  Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inasikitishwa na hali ya usalama katika bandari ya Dar es Salaam ambayo hutumiwa si tu na wananchi wetu bali hata nchi jirani kama zile za Burundi, Zambia, Rwanda na Congo. Hii ni kutokana na wizi wa mali za wananchi na watu wengine ambao wanatumia bandari hiyo.
  Mheshimiwa Spika, taarifa tulizonazo ni kuwa baada ya Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania kushauriana na wadau wa bandari ya Dar es Salaam, alimuagiza Inspecta Jenerali wa Polisi (IGP) kupeleka kikosi maalumu cha asikari polisi kwa kuwa kitengo hicho kilikuwa chini ya Auxiliary Polisi na hivyo kutoweza kukidhi haja ya ulinzi katika eneo hilo
  Mheshimiwa Spika, kuna taarifa kuwa Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) aliweza kuunda kikosi hicho mnamo tarehe 17/11/2009 kwa barua yenye Kumb. Na. PHQ AD,21/VOL.XVIII/227 na tayari walisharipoti kwenye kikosi cha Marine Dar Es Salaam ila mpaka sasa kutokana na mkurugenzi wa Bandari kukaidi kwa malengo anayoyajua yeye binafsi, askari hao wamekuwa wapo kituoni bila kupangia kazi za kufanya na wanaendelea kulipwa mishahara bila kazi yeyote wanayofanya.
  Mheshimiwa Spika, hata baada ya IGP kupeleka kikosi maalumu cha askari 51katika eneo hilo, taarifa zinaeleza kuwa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Bandari amekataa kuwapa ushirikiano kwa madai kuwa anajitosheleza kiulinzi hata baada ya Rais kuagiza kufanya hivyo. Hata hivyo upo ushahidi wa wizi wa makontena na vitu vingine ulioripotiwa katika kikosi maalumu cha polisi hao wa bandari Dar es Salaam ambao hata hivyo haujafanyiwa kazi.

  Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani tunaitaka serikali kutoa majibu ya kina juu ya tuhuma hizi zinazoelekezwa kwa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Bandari kwa kuwakingia kifua watuhumiwa wa wizi unaofanywa na watumishi wa bandari na wengine walio karibu nae, na pia kukaidi agizo la Rais la kuunda kikosi maalumu cha polisi kwa ajili ya kuboresha ulinzi wa eneo tajwa.
  Kambi ya Upinzani, tunataka kupewa taarifa juu ya yaliko Makontena yaliyoibiwa Bandarini na taarifa zake kufunguliwa RB kwenye kituo cha Police Marine na kisha faili hizo kupelekwa kituo cha polisi Kilwa Road, baadhi ya namba za RB hizo ni MUD/RB/51/11 hadi MUD/RB/56/11 na MUD/RB/106/11 hadi MUD/RB/113/11. Ni jukumu la chombo gani kulinda mali za raia?
  Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL)
  Mheshimiwa Spika, Kampuni ya Huduma za Meli imeendelea kutoa huduma katika maeneo ya Ziwa Victoria, Ziwa Nyasa na Ziwa Tanganyika. Kampuni hii imejiendesha kwa muda mrefu bila kupata fedha toka Serikali jambo ambalo kwa kiasi kikubwa imechangia uchakavu wa Meli zinazohudumiwa na shirika hili. Kutokufanyiwa matengenezo ya mara kwa mara kwa meli hizo umesababisha shirika kuendeshwa kwa madeni. Hadi sasa shirika linahitaji jumla ya shs. Bilioni 1.6 ili kulipia madeni yanayolikabili shirika hilo.
  Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali kuliwezesha shirika hili kimkakati ili liweze kutoa usafiri wa viwango kwenye maziwa ya Victoria, Nyasa na Tanganyika. Mizigo mingi inayotoka Bandari ya Dar es Salaam kwenda nchi jirani, usafiri wa uhakika wa meli ndio suluhisho pekee la usalama na uhakika. Aidha, Kambi ya Upinzani inashauri kuwepo na umiliki wa pamoja kati ya Halmashauri za wilaya husika kwa meli zinazotoa huduma kwenye maziwa tajwa na Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL).


  MAMLAKA YA HALI YA HEWA TANZANIA - (TANZANIA METOROLOGICAL AGENCY- TMA)
  Mheshimiwa Spika, mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania ni chombo muhimu sana katika kutoa huduma hapa nchini. Na mikakati ya serikali katika kuunda mamlaka nchini ni kuweza kufanya shughuli zake kibiashara. Ili kutimiza majukumu yake, TMA lazima ijipinde katika kupanga mikakati ambayo itawawezesha kukabiliana na changamoto ambazo zina wakwaza.
  Mheshimiwa Spika, moja kati ya majukumu ya mamlaka hii ni kufanya uchunguzi wa hali ya hewa ya anga za juu. Katika kulitekeleza hili, Mamlaka ilikuwa inategemea vituo vyake vitatu ambavyo viwili kati ya hivyo – kile cha Kigoma na Mtwara havifanyi kazi kwa sasa. Vituo hivyo vinahitaji matengenezo ya gharama kubwa.
  Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inaitaka serikali iiwezeshe mamlaka hii kifedha ili imudu kufanya matengenezo ya vituo hivyo kwa ajili ya kupata uwezo wa kutekeleza majukumu yake ipasavyo.
  Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, TMA haina budi kuwezeshwa ili ikidhi dhamira yake kuu ya kutoa huduma za hali ya hewa zilizo bora zitakazokidhi matarajio ya wadau na hivyo kulinda maisha yao, mali zao, mazingira na kusaidia katika kuondoa umaskini nchini.
  Mheshimiwa Spika, kwa kuwa nia ya mamlaka hii ni kuwa kitovu bora cha utoaji huduma za hali ya hewa zenye hadhi ya kimataifa ifikapo 2015, Kambi ya Upinzani inaitaka serikali itimize ahadi yake ya kuipatia TMA Rada mpya ya kisasa ambayo itaendana na wakati huu wa ongezeko la Tekinolojia na hivyo kuiwezesha kukidhi malengo yake.

  Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani ina imani kwamba kama serikali itakuwa makini kuzipatia ufumbuzi changamoto zinazoikabili TMA – kama vile kuboresha mitambo ya uchunguzi, mifumo ya mawasiliano, miundombinu ya uchoraji na uchambuzi wa taarifa, kupata kompyuta yenye uwezo mkubwa wa kuendesha mifumo ya utabiri wa WRF na High Resolution Model (HRM), pamoja na yale niliyoyaeleza katika ibara ya hapo juu, Mamlaka hii itaweza kufanya shughuli zake kwa ufanisi, kibiashara na hivyo kuondokana na kutegemea ruzuku ya serikali. Watanzania watapata tabiri ya uhakika ya hali ya hewa na hivyo kupanga shughuli zao, hasa za kilimo kitaalamu zaidi.

  Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo kwa niaba ya Kambi ya Upinzani, naomba kuwasilisha.


  ..........................................
  Mhonga Said Ruhwanya (Mb)
  Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani-Wizara ya Uchukuzi.
  03.08.2011
   
 2. T

  Technology JF-Expert Member

  #2
  Aug 3, 2011
  Joined: Oct 19, 2010
  Messages: 733
  Likes Received: 138
  Trophy Points: 60
  I have just wasted my time reading line by line! nthing really serious in here
   
 3. g

  gonja Member

  #3
  Aug 4, 2011
  Joined: Jan 28, 2011
  Messages: 41
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 13
  <br />
  <br />
  What did u expect and its missing.give your views so tht u add what u thnk is missing in the report
   
Loading...