Hotuba ya kambi ya upinzani wizara ya mawasiliano, sayansi na teknolojia

masalia

Member
Dec 20, 2012
24
26
HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI MHESHIMIWA SUSAN JEROME LYIMO (MB) KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA KATIKA WIZARA YA MAWASILIANO, SAYANSI NA TEKNOLOJIA KWA MWAKA WA FEDHA 2013/2014



Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua nafasi hii kwa mujibu wa Kanuni ya 99, kanuni ndogo ya 9 ya Kanuni za Kudumu za Bunge toleo la 2013, kutoa maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya fedha, katika Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, kwa mwaka wa fedha 2013/2014 .
Mheshimiwa Spika, Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia inawajibu wa kusimamia utafiti, utungaji na utekelezaji wa Sera ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEKNOHAMA). Wizara hii pia, ina jukumu la kusimamia mawasiliano ya posta, na ya njia ya simu. Vilevile inajukumu la kupata na kutumia teknolojia, kuendeleza wataalamu wa ndani katika fani za sayansi na teknolojia; kufanya utafiti wa mawasiliano, sayansi na teknolojia, kusaidia uvumbuzi, na kuongeza ufanisi.
Muheshimiwa Spika, Dira ya wizara hii ni kuwa na jamii ya watanzania wenye maarifa na uwezo wa kisayansi, kiteknolojia na wa ki-uvumbuzi, kwa maendeleo endelevu ya kiuchumi na hivyo kuweza kukabiliana na ushindani wa kimatifa.
Mheshimiwa Spika, licha ya tamko zuri la dira ya wizara hii, Kambi Rasmi ya Upinzani inasikitika kwamba, Serikali hii haitekelezi kwa vitendo tamko hili jambo ambalo limeifanya nchi yetu kuendelea kuwa nyuma katika medani za sayansi na technolojia na hivyo kuendelea kuwa soko la “mawazo ya kisayansi” na bidhaa zinazotokana na uvumbuzi wa kisayansi na technolojia. Nia aibu kwa taifa kwamba wakati elimu ya mataifa yaliyoendele inalenga kuwawezesha watu wao kuvumbua vitu mbali mbali vya kumpunguzia binadamu ugumu wa maisha kupitia sayansi na teknolojia, sisi elimu yetu inalenga kumfundisha mtanzania namna ya kutumia vifaa vinavyotokana uvumbuzi kisayansi na teknolojia ya nchi zilizoendelea. Jambo hili linamfanya mtanzania aendelee kuwa tegemezi kifikra kwa kuwa elimu yake ni katika kutumia tu na si katika kugundua vitu vipya.
Mheshimiwa Spika, nasema hivi kwa uchungu mkubwa kwa kuwa sioni jitihada za makusudi zikichuliwa ili kubadili taifa letu kutoka hali duni tuliyo nayo sasa, na kulipeleka katika hali nzuri zaidi kwa njia ya sayansi na teknolojia. Sina hakika pia kama teknolojia ya mawasiliano tuliyo nayo sasa, na iliyoenea sehemu kubwa ya nchi, inatumika katika kuleta mapinduzi ya kiuchumi ili kulinusuru taifa na umasikini uliokithiri. Hii ni kwa sababu, katika hotuba ya Bajeti ya Kambi Rasmi ya Upinzani ya mwaka wa fedha 2012/2013, Kambi Rasmi ya Upinzani ilibaini mapungufu katika Wizara hii muhimu na kuitaka Serikali kuchukua hatua ili mawasiliano, sayansi na teknolojia viweze kutumika katika kuleta mabadiliko ya kimaendeleo hapa nchini lakini mwitikio wa Serikali umeendelea kuwa ni ule wa kusua . Miongoni mwa masuala muhimu ambayo Kambi Rasmi ya Upinzani illitaka Serikali kufanya kwa mwaka wa fedha unaomalizika ni pamoja na yafuatayo:
1. Kuibua vipaji vya ubunifu na uvumbuzi wa ki-teknolojia miongoni mwa wanafunzi na wananchi wenye vipaji maalumu, na kuweka mkakati wa kuviendeleza vipaji hivyo ili kuondokana na utegemezi wa teknolojia za kigeni,
2. Tuliitaka Serikali kutoa taarifa (progressive report) juu ya utekelezaji wa Mtandao wa Taifa wa Elimu na Utafiti (National Education and Research Network-NERN),
3. Tuliitaka Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuongeza wigo wa mapato yanayotokana na makampuni ya simu nchini, na kuitaka serikali ufute misamaha ya kodi kwa makampuni ya simu nchini.
4. Tuliitaka TCRA itoe bei elekezi kwa makampuni ya simu, ili wananchi wasiendelee kunyonywa gharama kubwa za matumizi ya simu,
5. Tuliitaka Serikali kuthibitisha kama ni kweli Jeshi la Polisi lilinunua mtambo Gi2 unaotumika kufanya “sms spoofing’’ na madhumuni ya kufanya manunuzi hayo. Aidha, tuliitaka Serikali pia kuweka sheria ya kuthibiti matumizi ya taarifa za “sms spoofing” hapa nchini, kama zilivyofanya nchi ya Australia na Uingereza.

6. Tuliitaka Serikali iandae utaratibu wa kisheria wa kupata mapato kutoka katika mifumo ya malipo ya kieletroniki kwa mfano “Mobile Money Transfer” kama vile M-PESA kwa Kampuni ya Simu ya Vodacom, Tigo Pesa kwa Kampuni ya simu ya Tigo, Air Tel Money kwa Kampuni ya Simu ya Air Tel.
7. Tuliitaka Serikali kuiongezea pesa Tume ya Sayansi na Teknolojia ili iweze kufanya kazi zake kwa ukamilifu na kwa ufanisi.
Mheshimiwa Spika, kabla ya kujielekeza katika masuala mahususi ya mwaka mpya wa bajeti wa 2013/2014 unaotarajiwa kuanza mapema tarehe 1 Julai, 2013, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inayoongozwa na CHADEMA, inaitaka Serikali kutoa taarifa (progressive report) ya utekelezaji wa hoja za Kambi Rasmi ya Upinzani (zilizoorodheshwa hapo juu), ilizoitaka Serikali itekeleze tangu mwaka uliopita wa bajeti.
HAKI YA MAWASILIANO NA KUPATA HABARI
Mheshimiwa Spika, Kupata habari na mawasiliano ni moja ya haki za binadamu. Mikataba ya Kimataifa ya Haki za Binadamu inatoa haki ya kupata habari na mawasiliano. Kwa mujibu wa Ibara ya 19 ya Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa (The International Covenant on Civil and Political Rights)1966 “ wananchi wanahaki ya kupata habari na mawasiliano”.
Mheshimiwa Spika, sio mikataba ya kimataifa peke yake inayotambua haki hii, bali pia Ibara ya 18(b)(c) na (d) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977, inatamka wazi kwamba “kila mtu anayo haki ya kutafuta, kupokea na kutoa habari bila kujali mipaka ya nchi. Mwananchi ana haki ya kuwasiliana bila kuingiliwa, na ana haki ya kupewa taarifa kuhusu matukio yanayogusa maisha yake na shughuli muhimu za maisha yake”.
Mheshimiwa Spika, Pamoja na haki hii kutamkwa wazi na Katiba ya nchi yetu, na Mikataba ya Kimataifa, Serikali imekuwa ikiwanyima wananchi haki hii kwa makusudi kupitia “hila” mbalimbali kama ifuatavyo:
i. Kuhama Kutoka kwenye Mfumo wa Analojia kwenda kwenye Mfumo wa Dijiti.
Mheshimiwa Spika, Mamlaka ya Uthibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA) iliamuru vituo vyote vya Televisheni nchini kuzima mitambo ya analojia na kuvilazimisha kuingia kwenye mfumo mpya na wakisasa wa Digitali ambao unatumia Ving’amuzi kupata mawimbi ya “Televisheni”.
Mheshimiwa Spika, uamuzi huo uliwaathiri sana wananchi na taifa kwa ujumla kwani kulikuwa hakuna maandalizi ya kutosha, na pia wananchi wengi hasa wa vijijini wameshindwa kununua ving’amuzi hivyo na kwa jinsi hiyo kukosa haki yao ya kikatiba ya kupata habari.
Mheshimiwa Spika, TCRA imechangia sana tatizo hili kwa kuwa mpaka sasa haijaweka udhibiti wa bei wala usambazaji wa Ving’amuzi na hivyo kuacha hali ya ushindani usio na afya kwa watumiaji wa huduma za ving’amuzi. Ving’amuzi vimekuwa vikiuzwa kwa bei ya juu ambayo inafanya watanzania masikini kushindwa kununua na hivyo kuwakosesha haki yao ya Kikatiba ya kupata mawasiliano. Aidha, TCRA haidhibiti usambazaji wa ving’amuzi jambo ambalo limesababisha kutokupatikana kwa ving’amuzi katika baadhi ya maeno, na hivyo kuleta usumbufu mkubwa kwa wananchi wanaotaka kununu Ving’amuzi hivyo.
Mheshimiwa Spika, Mbaya zaidi, baadhi ya ving’amuzi kwa muda mrefu tangu kuzimwa kwa mitambo ya analojia vimekuwa havirushi matangazo ya vituo vya televisheni vya ndani ya nchi, na cha ajabu katika taarifa ya Wizara kwa umma, Wizara iliwataka wananchi ambao hawapati matangazo ya vituo vya television vya ndani ya nchi wawasiliane na wauza ving’amuzi hili wapate suluhisho;
Mheshimiwa Spika, kwa msisitizo naomba kuinukuu sehemu ya taarifa hiyo kama ifuatavyo: “Serikali inapenda kuwakumbusha wananchi kuwa katika maeneo ambayo tayari kuna matangazo ya televisheni katika mfumo wa dijitali, watumiaji wa televisheni wanatakiwa kuhakikisha kuwa wanapata matangazo ya televisheni zote zenye leseni za kitaifa bila gharama yoyote ile ya ziada mbali na gharama ya kununua king’amuzi (kisimbuzi) ambacho kinawezesha kuona matangazo katika mfumo mpya wa utangazaji wa dijitali. Stesheni hizo ni TBC1, ITV, Star TV, Channel 10, na East African TV. Endapo matangazo ya televisheni ya vituo hivyo hayapatikani, wananchi wawasiliane mara moja na watoa huduma za ving’amuzi ili kuwasaidia kupatia ufumbuzi’’ Taarifa hii ilitolewa na kutiwa siani na Mhe. Profesa Makame Mbarawa Waziri Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia tarehe 2 Aprili, 2013.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inasikitishwa sana na tangazo la Wizara kwamba wananchi ambao hawaoni matangazo ya vituo vya televisheni za ndani wawasiliane na wasambaza ving’amuzi. Hii ni kwa sababu Serikali ndio iliyotoa leseni kwa wasambazaji wa ving’amuzi, na ndio inayojua masharti ya leseni hizo. Hivi Mwananchi masikini wa kijijini kwa mfano wa kijiji cha Mwamgongo, kule Kigoma au yule wa Liwale kule Lindi atapa wapi nguvu na mamlaka ya kuyaambia makampuni ya usambaziji kwamba king’amuzi chake hakioneshi matangazo ya kituo cha televisheni cha ndani ya nchi?
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inayoongozwa na CHADEMA inaitaka Serikali kupitia Wizara hii kuacha mara moja kufanya mzaha na haki ya wananchi ya kupata habari. Aidha Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kutoa agizo leo hii kwa Makampuni ya usambazaji wa ving’amuzi kuhakisha kwamba vituo vya TBC1, ITV, Star TV, Channel 10, na East African TV ambavyo vina leseni ya kitaifa vinaendelea kurusha matangazo yake bure kupitia ving’amuzi kama ilivyokuwa katika makubaliano ya wasambazaji wa vin’ngamuzi, wamiliki wa vituo tajwa vya televisheni na TCRA.

MAWASILIANO YA SIMU ZA VIGANJANI
Mheshimiwa Spika, Pamoja na TCRA kuzitaka kampuni za utoaji huduma za simu Tanzania kupunguza gaharama za kupiga simu na kutuma ujumbe mfupi wa maneno, makampuni hayo bado yana bei ya juu, hasa kupiga simu toka mtandoa mmoja kwenda mwingine, (interconnection charges) hali inayosababisha wananchi kumiliki simu au line zaidi ya moja. Mbaya zaidi makampuni ya simu yamekuwa yakiwatoza wateja pale wanapopiga simu kwenda huduma kwa mteja (customer care service) na hakuna viwango vyenye mlingano kati ya kampuni moja na nyingine. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kupitia mdhibiti wa mawasiliano ya simu TCRA kukataza mara moja makampuni ya simu kuwatoza wateja pale wanapo piga simu ili kupata huduma kwa wateja (customer care services) kwakuwa wateja wanapofanya hivyo huwa wana jambo aidha la kiufundi au la kiutaratibu wanalotaka kusaidiwa na kampuni husika, na hakuna faida yoyote ya kifedha mpiga simu anayopata kwa kuomba msaada wa maelezo kutoka kwa customer care.


UTANGAZAJI REDIONI NA KWENYE LUNINGA
Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa Sheria ya Utangazaji ‘the Broadcasting Services Act’, TCRA inawajibu wa kusimamia pamoja na mambo mengine maudhui ya matangazo kama ilivyoainishwa na kanuni za udhibiti wa maudhui ya utangazaji za mwaka 2005 [the Broadcasting Services (Content) Regulations 2005].
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa kanuni hizo, vituo vya redio na television vinakatwazwa kurusha matangazo yenye maudhui ya kibaguzi kam vile rangi, kabila, dini na aina zote za ubaguzi. Aidha kanuni hizo zinakataza vyombo vya utangazaji kuibua chuki baina ya makundi tofauti katika jamii, na wakati wote kulinda umoja, uhuru, na maslai ya Taifa, na kudumisha maadili ya kitaifa.

Mheshimiwa Spika, kanuni hizo pia zinavitaka vyombo vya utangazaji kuwalinda watoto katika matangazo yao dhidi ya lugha za matusi, na picha zisizofaa. Adhabu inayotolewa na Kanuni ya 28 ya kanuni hizi kwa kituo kitakachokiuka kanuni hizi ni faini kiasi cha million tano tu.
Mheshimi wa Spika, pamoja na kuwepo kwa kanuni hizi tangu mwaka 2005, vyombo vya utangazaji, redio na luninga vimekuwa vikivunja kanuni hizo, kwa kuonesha picha na kurusha matangazo yenye lugha ya matusi, zenye kuchochea chuki za kidini, na kisiasa, zinazo zorotesha maadili na kutishia umoja wa kitiafa. Hivi karibuni kituo cha redio cha Clouds Fm kilipigwa faini kwa kosa la kushabikia mambo ya ushoga, jambo amabalo ni kinyume na maadili ya Taifa letu. Vituo vingine viwili vya redio Imani FM na Kwa Neema FM navyo vimefungiwa. Kambi Rasmi ya Upinzani inahoji; ni lini Serikali ‘sikivu’ ya CCM itaanza kuona kwamba vituo vingi vya televisheni na redio nchini vinaonesha picha na kurusha matangazo yaliyojaa maudhui yaliyopotoka kimaadili ili kuchukua hatua stahiki?
Mheshimiwa Spika, kwa hali ilivyo sasa kwenye vituo vyetu vya redio na televisheni ni ushahidi mwingine unaodhirisha ni namna gani Serikali ya CCM ilivyoshindwa kusimamia maadili ya Taifa letu, imeshindwa kusimamia maadili ya kisiasa, na sasa inaacha watoto wetu waharibiwe kimaadili kwa kuviachia vitu vya redio na television kurusha picha na matangazo ambayo yanachochea mmomonyoko wa maadili.
MALIPO YA TOZO ZA MINARA YA SIMU KWA HALMASHAURI
Mheshimiwa Spika, katika taarifa ya utekelezaji wa maagizo ya Kamati ya Miundombinu kwa mwaka wa fedha unaomalizika, ni kwamba, Wizara ilitakiwa kuwasiliana na TAMISEMI kuhusu kutofautiana kwa tozo mbalimbali za minara ya simu (land levy) zinazotozwa na Halmashauri hapa nchini kwa lengo la kuwianisha tozo hizo ili zifanane.
Mheshimiwa Spika, pamoja na Wizara kuandaa mwongozo kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu-TAMISEMI ambao utaweka viwango vya kufanana vya tozo, Wizara imeenda mbele zaidi kuweka utaratibu wa kuwa na taasisi moja itakayo kusanya tozo kwa niaba ya Halmashauri zote kisha kuzigawa kwa Halmshauri husika.
Mheshimiwa Spika, kwa utaratibu huu ni wazi kwamba taasisi (agency) itakayokusanya tozo kwa niaba ya Halmashauri itahitaji gharama za uendeshaji na hivyo ni dhahiri itafanya makato toka kwa tozo zinazokusanywa na matokeo yake ni kupunguza kiasi cha mapato ambacho Halamshauri ingekusanya moja kwa moja. Kambi Rasmi ya Upinzani inayoongozwa na CHADEMA inaitaka Serikali, kurekebisha Mwongozo uliotolewa na TAMISEMI kwa kuwa na kiwango kimoja cha tozo, na kuondoa taasisi moja ya ukusanyaji mapato kwani, kwa utaratibu wa kisheria uliopo Halmashauri inaweza kukusanya mapato yake yenyewe; na makampuni ya simu yanazo ofisi mikoani na hivyo wanaweza kulipa tozo hizo bila usumbufu wowote.
MICHEZO YA BAHATI NASIBU KWENYE MITANDAO YA SIMU
Mheshimiwa Spika, Makampuni ya simu yamekuwa na utaratibu wa kufanya “promosheni” zinazohusisha kuwakata pesa wateja wanaoshiriki promosheni hizo. Hata hivyo kumekuwa na malalamiko toka kwa watumiaji wa simu za mkononi kwamba mara kadhaa wameingizwa kwenye promosheni hizo bila ridhaa zao na hivyo kukatwa pesa hali inayopelekea kupata hasara na usumbufu mkubwa. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kupitia TCRA na Bodi ya Kusimamia Michezo ya Kubahatisha ya Taifa kuyataka makampuni ya simu kuweka utaratibu mzuri wa kucheza michezo hiyo ili kuondoa usumbufu kwa wateja.
Mheshimiwa Spika, Baadhi ya makampuni ya simu yamekuwa yakitoa huduma duni sana, na hivyo kuleta usumbufu kwa wateja. Mathalani kuna wakati kampuni fulani inaweza kupoteza kabisa “network” katika mkoa, au mji fulani na hivyo kukwamisha kabisa mawasiliano, bila kutoa taarifa wala kuomba radhi wateja wake.
Mheshimiwa Spika, katika zama, hizi ambazo mawasiliano ya simu yanawezesha shughuli karibu zote, kiuchumi, kijamii na kiusalama hali ya kukatika kwa “network” ina hatarisha usalama wa maisha ya watanzania, ukizingatia mtandao wa simu unawezesha sio tu mawasiliano bali pia huduma za kibenki za watumiaji wake.
UHIFADHI, NA UTUMAJI PESA KWA NJIA YA SIMU
Mheshimiwa Spika, Maendeleo ya sayansi na teknolojia yametufikisha mahali simu za kiganjani zimekuwa benki na makampuni ya simu yamekuwa taasisi za kifedha hapa nchini. Malipo mengi yanafanywa kupitia huduma za M-pesa,Tigo-pesa, Airtel-Money, Z-pesa na kadhalika.
Pamoja na mamillion ya pesa yanayotumwa kila siku kupitia njia hii, na makato ambayo makampuni ya simu na mawakala wao wanayapata na kujichumia faida isiyo na kifani kupitia miamala hiyo Serikali haipati hata senti tano (5 Cent) kama kodi kutokana na biashara hii, lakini wakati huo huo Serikali hii imekuwa ikitoza taasisi nyingine za kifedha kama benki kodi chungu mzima. Kambi Rasmi ya Upinzani inayoongozwa na CHADEMA inaishangaa Serikali hii ya CCM inayojiita makini, kwa kushindwa kuandaa utaratibu utakao iwezesha Serikali kupata faida kutoka na miamala ya pesa kwa njia ya simu ili kuchangia ongezeko la pato la taifa. Na katika hili Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inasisitiza sheria ya tozo itakapotungwa isilenge kuwapa mzigo watumiaji/ wateja wa mihamala hii, badala yake makampuni ya simu ndio walipe kodi na ushuru kwa serikali, bila kuathiri wateja.
Mheshimiwa Spika, izingatiwe kwamba leseni za utoaji huduma za mawasilaino ya simu hutolewa kwa makampuni na TCRA, lakini leseni za utoaji huduma za pesa kwa njia ya simu hutolewa na Benki Kuu ya Tanzania kwa mujibu wa Sheria ya Benki na Taasisi za Kifedha ya mwaka 2006 (Banking and Financial Institutions Act 2006). Hivyo Serikali lazima ielewe kwamba biashara hizi mbili ni biashara tofauti, watoaji leseni wake ni tofauti; hivyo serikali lazima ipate mapato tofauti kutoka makampuni haya, katika biashara ya mawasiliano, na biashara ya pesa kwa njia ya simu.
UHALIFU WA MITANDAONI (CYBER CRIME)
Mheshimiwa Spika, Kumeibuka wimbi kubwa la uwizi kwa njia ya mtandao. Mamilioni ya pesa yameibwa kwenye taasisi mbalimbali, hasa mabenki, machine za kutolea pesa (ATM) na miamala mingine inayofanyika kwa njia ya kompyuta vimeendelea kuzitia hasara taasisi za kifedha nchini. Kwa mfano, tarehe 14 mwezi Febuari mwaka 2013 watuhumiwa wa wizi wa fedha kiasi cha shilingi milioni 500 kupitia kwenye ATM, walikamatwa mkoani Mwanza. Huu ni mfano mmoja tu, lakini kesi za uwizi kwa njia ya ATM zimekuwa zikiripotiwa kila mara katika maeneo tofuauti nchini.
Mheshimiwa Spika, pamoja na wizi, kuna uhalifu mwingine unaofanyika kwa njia ya mtando kwa mfano, ubadhirifu kwa njia ya kompyuta (computer fraud), kuingilia mawasiliano (haking) nakadhalika.
Mheshimiwa Spika, waathirika wa uhalifu huu ni pamoja na taasisi za kiserikali, mabenki, biashara binafsi, vyuo vya elimu, wanasiasa wanaofanyiwa ushushushu, na jamii kwa ujumla. Pamoja na hali hii, Tanzania haina Sheria mahususi inayodhibiti uhalifu kwa njia ya mtandao. Mabadiliko madogo yalifanywa kwenye Sheria ya Ushahidi (the Law of Evidence Act) na Sheria ya Kanuni za Adhabu (the Penal Code) hazitoshi kudhibiti aina zote za uhalifu kwa njia ya mtando; hivyo Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali ilete muswada wa Sheria mahususi kwa madhumuni ya kudhibiti uhalifu huu wa kimtandao.
Mheshimiwa Spika, katika hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani tulihoji juu ya kuwepo kwa taarifa za Jeshi la Polisi kuhusika na ununuzi wa mtambo wa kijasusi wa Gi2 unaotumika kufanya ‘’sms spoofing’’ yaani kutuma ujumbe mfupi wa maneno kwa kutumia namba ambayo kiualisia mwenye namba hiyo hajatuma ujumbe huo, isipokuwa ni kuingilia kihalifu mawasiliano (cyber trespass) ambapo mtumaji anafanya “ impersonation”.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya upinzani inataka kujua ni lini Serikali itaweka sheria ya kudhibiti matumizi ya taarifa za “sms spoofing” hapa nchini ama kukubaliana na matumizi yake au kupiga marufuku kama walivyofanya nchi ya Australia na Uingereza.
KUONGEZA PATO LA TAIFA KUPITIA MAWASILIANO
Mheshimiwa Spika, katika hotuba ya bajeti ya Wizara hii ya mwaka 2012/13 Wizara iliahaidi kuanza kutumia mtambo wa kuhakiki mawasiliano (Tarrif Monitoring System-TMS) ili kuhakiki mapato yanayotokana na mawasiliano ya simu. Wizara ilijinadi kwamba imeanza mchakoto huo mwezi juni mwaka 2012. Kambi Rasmi ya Upinzani inataka kujua ni hatua gani mchakato huo umefikia?
Mheshimiwa Spika, katika kiambatanisho namba 2. cha hotuba ya bajeti ya mwaka jana ya Wizara hii chenye kichwa UWEKEZAJI NA MCHANGO WA WATOA HUDUMA ZA SIMU ZA MKONONI KUPITIA TEKNOLOJIA YA GSM TANZANIA, Wizara ilishindwa kutoa taarifa za kikodi za kampuni za simu za TIGO,AIRTEL, ZANTEL kwenye baadhi ya aina ya kodi. Taarifa ya kodi ya Makampuni (Corporate tax) iliyolipwa na Kampuni ya TIGO hazikupatikana, taarifa ya malipo kwenye mfuko wa mawasiliano kwa wote (2009-2011) za kampuni ya Zantel hazikupatikana, taarifa za kiasi cha fedha zilizotumwa (mobile money transaction) cha kampuni ya AIRTEL, na Zantel hazikupatikina, Taarifa za mchango wa kijamii (Corporate Social Responsibility) wa kampuni ya Zantel hazikupatikana.
Mheshimiwa Spika, Kitendo cha Serikali hii ya CCM kushindwa kupata takwimu ambazo nyingine zinatakiwa kutolewa na makampuni kisheria ni muendelezo wa uthibitisho wa kushindwa kwa Serikali hii kutawala Taifa hili. Kitendo cha Serikali kushindwa kupata taarifa hizi kuna ashiria uzembe na rushwa.
SERIKALI KUMILIKI TTCL KWA 100%
Mheshimiwa Spika, Serikali imeanza mchakato wa kumiliki Shirika la Mawasiliano ya Simu la Taifa (TTCL) kwa asilimia mia moja (100%) kwa kununua asilimia 35% ya hisa za M-bia mwenza kampuni ya AIRTEL. Kambi Rasmi ya Upinzani inakubaliana na hatua hii kwa kuzingatia umuhimu wa Wananchi kupitia Serikali kumiliki sekta ya mawasiliano ya simu kwa umuhimu na unyeti wake. Hata hivyo Kambi Rasmi ya Upinzani inataka Serikali kuweka wazi tathimini ya bei ya hisa za AIRTEL kabla ya ununuzi wa hisa hizo na mkataba wa mauzino hayo uwekwe wazi na uridhiwe na Bunge lako tukufu, ili kuziba mianya ya ufisadi, na kulipa Bunge haki yake ya kuisimamia Serikali.
UVUMBUZI WA KISAYANSI
Mheshimiwa Spika, naomba kunukuu sehemu ya hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani iliyowasilishwa ndani ya Bunge hili tukufu katika mwaka wa fedha 2012/13 kuhusu rai ya Kambi Rasmi ya Upinzani kuibua na kuendeleza vipaji maalumu vya kisayansi na teknlojia miongoni mwa wanafunzi wetu na wananchi wengine wenye vipaji hivyo. Sehemu ya hotuba hiyo inasema hivi: “Mheshimiwa Spika, hakuna mkakati wa kuibua na kuwendeleza wabunifu katika kuibua na kuendeleza Teknolojia hapa nchini. Pamoja na nchi yetu kuonekana kuwa na vijana wenye uwezo wa hali ya juu katika kubuni na kuendeleza Teknolojia itakayoweza kuinua uchumi wa nchi, serikali imeshindwa kutambua fursa hiyo na kuwaendeleza wabunifu hao. Mfano ni kijana Frank Waya kupitia kipindi cha Jenerali on Monday kinachorushwa na Televisheni ya Channel Ten ameonyesha uwezo mkubwa katika kubuni Teknolojia ambayo ikiendelezwa itasaidia sana taifa katika kuleta maendeleo.

Mheshimiwa Spika, kupitia kipaji alichonacho, ameweza kuonyesha jinsi Teknolojia ya simu inavyoweza kutumika katika kutengeneza mfumo wa kuzuia vyombo vya moto kutoungua kutokana na shoti ya umeme na hata kutumia simu kwa ajili ya umwagiliaji wa bustani na shamba kwa kutumia pampu ya maji hata mtu akiwa mbali na shamba au bustani. Pia ameonyesha uwezo wa kutengeneza inventor inayoweza kukaa na umeme kwa siku 7 baada ya umeme wa Tanesco kukatika. Hiki ni kipaji cha hali ya juu ambacho kikitumiwa vizuri na kuendelezwa, kitasaidia taifa hili kupiga hatua ya kimaendeleo.

Kambi ya Upinzani inataka kupata majibu kuna mkakati gani wa serikali wa kuhakikisha kuwa vipaji kama hivi vinaendelezwa katika nchi yetu, na je wenye vipaji kama hivi ni nani mwenye wajibu na jukumu la kuviendeleza na kuvikuza

Mheshimiwa Spika, ni mwaka mmoja umepita sasa tangu Kambi Rasmi ya Upinzani itoe rai hii kwa Serikali kuibua na kendeleza vipaji vya namna hii. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka kujua Serikali kwa kipindi cha mwaka mmoja uliopita, imeibua na kuendeleza vipaji vingapi ili kutimiza dira na dhima ya wizara hii ya kuwajengea uwezo wananchi wa kisayansi, kiteknolojia na ki-uvumbuzi ili kukabiliana na ushindani wa kimataifa na hivyo kuleta maendeleo endelevu ya kiuchumi?

Mheshimiwa Spika, Katika muhtasari wa taarifa ya utekelezaji (Perfomance Review 2012/2013) Wizara ilieza kuwa Serikali inatumia Tume ya Sayansi na Tekinolojia kufanya tathimini ya ugunduzi ili kuweza kurasimisha ugunduzi huo, na kwamba inaanda sera ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu, na kwamba kuna sheria inaandaliwa ili kuwahamasisha, kuwasimamia na kuwalinda wagunduzi.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kutumia sheria ambayo tayari ipo, Sheria ya Usajili wa Uvumbuzi, ya mwaka 1994, Sura ya 217 ya sheria zetu. [the Patents (Registration) Act, 1994 Cap 217] ambayo kwa mujibu wa jina refu (long title) ya sheria hiyo, madhumuni ya sheria hiyo ni; Sheria ya kusajili uvumbuzi, kuweka mazingira bora ya kuhamasisha uvumbuzi na ugunduzi ili kuwezesha kupata teknolojia katika misingi ya usawa kupita, kutoa na kuratibu uvumbuzi, kutoa vyeti vya bidhaa gunduliwa, na vyeti vya ugunduzi. kwa kiingereza “An Act to provide for the Patents Registration so as to make better provisions for the promotion of inventivity and innovation for the facilitation of the acquisition of technology on fair terms through the grant and regulation of patents, utility certificates and innovation certificates”.
Mheshimiwa Spika, kama serikali inaona vifungu vya sheria hii ambayo tayari inatumika havitoshi, ni vyema ikaileta sheria hii Bungeni ili tuifanyie marekebisho kwani ni wazi kusubiri mpaka mchakato wa maandalizi ya sera na sheria mahususi unachelewesha uendelezaji wa vipaji vya wabunifu wetu, hasa kwa kuzingatia kuwa Serikali hii imekuwa madarakani kwa miaka zaidi ya 50 na haijawahi kuona umuhimu wa kuwa na sheria hii kwa wakati wote huo.

TEKNOLOJIA YA BIO METRICK VOTERS REGISTER
Muheshiwa Spika, Dunia imeshuhudia mikanganyiko na migongano iliyohatarisha amani na utulivu wa nchi kadhaa zilizojaribu kutumia mtambo wa Bio Metrick Voters Register katika chaguzi zake mbali mbali, mifano ya hivi karibuni ni ya Nchi za Ghana na Kenya. Mitambo ya aina hii inatumia teknolojia ya juu inayotaka mazingira mazuri yaliyoandaliwa. Katika mazingira ya nchi masikini, yenye kitekinolojia duni na ambayo hata robo ya eneo la nchi haina umeme kama Tanzania, ni jambo linaloshangaza kuona tunataka kutumia teknolojia hii. Ni lazima tukumbuke msemo usemao, ukiona mwenzio kanyolewa, wewe tia maji.
Mheshimiwa Spika, Bila kujali hali duni ya kiteknolojia inayoikabili nchi yetu, Serikali ya CCM kupitia tume ya uchaguzi imeanza mchakato wa kununua mtambo wa Biometrick Voters Register (BVR) kwa mabilioni ya fedha za wahisani. Kambi Rasmi ya Upinzani inayoongozwa na CHADEMA inaitaka serikali iache mara moja mpango huo na badala yake ifanye marekebisho kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
Mheshimiwa Spika, ninayasema haya kwakuzingatia kuwa, ukiacha riporti kadhaa zinazoelezea uduni wa maendeleo ya kisayansi na teknolojia nchini, sisi wote humu ni mashaidi kwamba asilimia 80 ya maeneo tunayotoka hayana umeme.

TUME YA TAIFA YA SAYANSI NA TEKNOLOJIA
Mheshimiwa Spika, Tume ya Sayansi na Teknolojia inawajibu wa kusimamia na kuratibu tafiti za kisayansi na teknolojia. Pamoja na tafiti nyingi zilizifanywa na wanasayansi mbalimbali nchini. Matokeo ya tafiti hizo zimekuwa haziwafikii walengwa. Mathalani tafiti zinazogusa sekta ya kilimo, zimeendelea kuishia kwenye vitabu, na kushindwa kuwafikia wakulima vijijini. Hili linatokana na kukosekana kwa uratibu kwa upande wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH).
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2012/2013 Serikali ilitenga kiasi cha bilioni 26 na milioni 476 na 961 elfu (26,479,961,000), kwa ajili ya utafiti. Hata hivyo, kiwango hicho cha fedha kimepungua katika bajeti ya mwaka 2013/2014 ambapo serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 16.5 tu kwa ajili ya utafiti. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kutoa maelezo mbele ya Bunge hili ni kwa nini fedha za utafiti zinapungua wakati jukumu kubwa la Tume ya Sayansi na Teknolojia ni kufanya utafiti?

TAASISI ZA MAFUNZO YA SAYANSI NA TEKNOLOJIA
Mheshimiwa Spika, kuna ulazima wa kupandishwa hadhi kwa Taasisi za mafunzo za Sayansi na Teknolojia nchini. Kupandishwa hadhi kwa taasisi zetu na kuwa vyuo vikuu vinavyotoa shahada za ngazi mbalimbali sio tu itaongeza fursa za kujiendeleza kimasomo kwa wanasayansi wetu nchini, lakini pia itakuza wigo wa maendeleo ya sayansi na teknolojia nchini na hivyo kuleta maendeleo ya kiuchumi, na kukuza ustawi wa wananchi, ukizingatia kuwa tunahitaji wataalamu wa ndani katika sekta ya sayansi na teknolojia ili kulisaidia taifa kujitegemea.
Mheshimiwa Spika, Taasisi ya Sayansi na Teknolojia-Mbeya bado haijapata ithibati ya kudumu toka Tume ya Vyuo vikuu, ili kuwa Chuo kikuu kamili, Kambi Rasmi ya Upinzani inayoongozwa na CHADEMA inaitaka Serikali kutamka mbele ya Bunge hili kuwa ni lini taasisi hiyo itapata ithibati ya kudumu, kwa kuzingatia umuhimu wa kuwa na Vyou vingi vya Sayansi na Teknolojia nchini kama nilivyoeleza hapo juu.
Mheshimiwa Spika, Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam (DIT) ni moja ya taasisi kongwe nchini. Hata hivyo, pamoja na taasisi hii kuwepo kwa miaka mingi, kasi ya kukua kwake sio ya kuridhisha, ukilinganisha na umri wake. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kuongeza kasi ya ukuaji na kuiwezesha DIT kuwa na matawi kila mkoa, kama zinavyofanya taasisi nyingine za kitaaluma nchini, husasani vyuo vikuu.
Mheshimiwa Spika, taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela-Arusha ni taasisi mpya kiumri. Ili kukuza na kuiendeleza taasisi hii serikali inao wajibu wa kuitengea fedha za kutosha katika bajeti hii ili kuijengea uwezo wa kiutendaji.
Mheshimiwa Spika, maendeleo na mafanikio katika taasisi za taaluma za sayansi na teknolojia nchini zinategemea kwa kiasi kikubwa maandalizi ya wanafunzi yanayo paswa kufanywa katika ngazi za chini za elimu yao. Kwa hali hilivyosasa ambapo wanafunzi wa shule za msingi wanasoma masomo ya sayansi bila kuwa n mahabara wala maktaba, wanasoma somo la TEHAMA bila kuwa na kompyuta- na asilimia zaidi ya 90 ya shule za msingi hazina umeme, ni wazi hawawezi kuwa na uwezo wala motisha ya kupenda kusoma masomo ya sayansi. Hali hiyo pia imetamalaki kwenye shule za sekondari.
Mheshimiwa Spika, kama hali hii ya wanafunzi kutoandaliwa mazingira ya kupenda masomo ya sayansi itaendelea kukua na kukomaa, utafika wakati taasisi zetu za sayansi na teknolojia zitakosa wanafunzi wa kitanzania wa kuwadahili, na hivyo taasisi zetu ama zitakufa, au zitaishia kudahili wanafunzi kutoka nchi za nje.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Wizara ishirikiane na Wizara ya Elimu kuweka mazingira yenye afya kwa ustawi wa masomo ya sayansi hili kuhamasisha wanafunzi kupenda masomo ya sayansi. Aidha Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kuweka vivutio kwa wanafunzi wa masomo ya sayansi kama vile kuwalipia karo wanafunzi wa sayansi ngazi za sekondari na kuwapa mikopo asilimia mia moja kwa wale watakaoendelea na masomo ya juu katika taasisi za sayansi na vyuo vikuu.

MGAWANYO WA FEDHA ZA MAENDELEO YA 2013/2014
Mheshimiwa Spika, Wizara hii imetengewa kiasi cha millioni mia mbili 200,000,000 kwa uanzishaji wa vituo vya jamii vya mawasiliano Vijijini, lakini kwa mujibu wa idadi, ukubwa na umuhimu wa kazi zilizipongwa katika fungu hili ni wazi kuwa kiasi hicho cha fedha ni kidogo sana na hakiwezi kukidhi malengo yanakusudiwa. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali iongeze pesa kwenye fungu hili ili kuchagiza maendeleo ya mawasiliano ya Internet vijijini kwa mustakhabali wa mendeleo ya vijiji vyetu.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani naomba kuwasilisha.

_______________________________________
Susan Jerome Lyimo (Mb)
MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI
NA
WAZIRI KIVULI WA MAWASILIANO, SAYANSI NA TEKNOLOJIA.

Imesomwa leo, tarehe 3 Juni, 2013
 

Attachments

  • hotuba ya Kambi ya Upinzani mawasiliano sayansi na teknolojia.doc
    101.5 KB · Views: 75
Back
Top Bottom