Hotuba ya kambi ya upinzani, wizara ya elimu na mafunzo ya ufundi

masalia

Member
Dec 20, 2012
24
26
TANZAMA PIA KIAMBATANISHO CHA MADAI HALISI YA WALIMU, (ATTACHED)


HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI YA UPINZANI MHE. SUSAN ANSELM JEROME LYIMO (MB), KUHUSU MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA 2012/2013 NA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI KATIKA WIZARA YA ELIMU NA MAFUNZO YA UFUNDI KATIKA MWAKA WA FEDHA 2013/2014



1. Utangulizi
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Kanuni ya 99, kanuni ndogo ya (9) ya Kanuni za Kudumu za Bunge Toleo la 2013, napenda kuchukua nafasi hii kuwasilisha maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi katika Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kwa mwaka wa fedha 2013/2014.

Mheshimiwa Spika,
Huko nyuma tumeonya mara nyingi juu ya hatari inayoinyemelea taifa letu kutokana na Serikali ya Chama cha Mapinduzi kuharibu mfumo wetu wa elimu. Tunasikitika kwamba maonyo yetu yote, ushauri na nasaha tulizotoa zilibezwa kwa kishindo ndani na nje ya bunge hili. Sasa si maonyo wala utabiri tena. Kuporomoka kwa mfumo wetu wa elimu ni dhahiri. Leo hii asilimia zaidi ya thelathini ya watanzania hawawezi kusoma wala kuandika. Wengi wa vijana wanaomaliza katika vyuo vyetu vya elimu ya juu hawaajiriki wala hawezi kujiajiri. Katika utafiti uliofanywa na shirika moja linalojihusisha na ajira jijini Dar es Salaam unaonyesha kuwa ni theluthi moja tu ya wahitimu katika vyuo vya elimu ya juu nchini wanaoweza kuajirika, kwa maana ya kushindana katika soko la ndani la ajira.

Mheshimiwa Spika,
Katika kipindi cha miaka saba ya utawala wa Rais Kikwete kiwango cha ufaulu katika ngazi ya msingi na sekondari kimeendelea kushuka huku kiwango cha kufeli kikipanda kwa kasi kubwa. Kwa mujibu wa takwimu za serikali zinazopatikana kwenye kitabu cha takwimu za elimu (Basic Statistics in Education in Tanzania), Katika kipindi hiki, kiwango cha KUFELI kimepanda kutoka asilimia 10.7 Rais Kikwete alipoingia madaraka hadi asilimia 50 mwaka 2010 alipomaliza awamu ya kwanza ya utawala wake. Awamu ya pili ya utawala wa Rais, Dokta Jakaya Mrisho Kikwete, umepandisha kiwango cha KUFELI hadi asilimia 65.5 katika mwaka 2012 kabla ya kubatilishwa kisiasa kwa matokeo ya kidato cha nne na kuwa asilimia 56.9. Wataalamu wa maswala ya elimu wanabashiri kwamba, kwa kuwa hakuna hatua zozote za maana zinazochukuliwa na serikali hii katika kurekebisha mambo, kiwango cha KUFELI kinaweza kupanda hadi kufikia asilimia 95 kama hakutakuwa na ujanja ujanja wa kufuta matokeo na kuyapanga upya kama Serikali hii ya CCM ilivyofanya siku chache zilizopita.



Mheshimiwa Spika,
Mwaka jana, nilisema Tanzania ni vyema ikawekwa kwenye kitabu cha maajabu ya dunia yaani “The Guiness Book of Records” kwa kuchagua baadhi ya watoto wasiojua kusoma na kuandika kidato cha kwanza, na mwaka huu hii “standardization” ya kisiasa ni kituko kingine ambacho sijui jumuiya ya kimataifa inatuelewaje kwa kuwa hata baada ya kufanya “standardization” ya kisiasa bado kiwango cha wanafunzi waliopata sifuri ni kikubwa sana na haijawahi kutokea katika historia ya Tanzania.

Mheshimiwa Spika,
Sababu za kuporomoka kwa mfumo wetu wa elimu zinajulikana na zimeainishwa katika tafiti mbalimbali zilizofanywa na mashirika mbalimbali na serikali yenyewe. Vilevile, mapendekezo juu ya hatua za kuchukua zimeainishwa sana na watafiti mbalimbali wakiwemo wataalamu wa serikali yenyewe. Kwa mfano, mwaka 2011, Serikali iliunda Kamati iliyokuwa na wajumbe kumi chini ya uenyekiti wa Ndugu Francis M. Liboy wa Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI) kuchunguza sababu za kushuka kwa kiwango cha ufaulu wa mtihani wa Taifa wa kidato cha nne mwaka 2010. Kamati ilitoa ripoti nzuri yenye kurasa 137 ambayo lisifiwa sana na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Mheshimiwa Dkt. Shukuru Kawambwa.


Mheshimiwa Spika,
Katika taarifa yake, Kamati iliainisha sababu nyingi zilizosababisha matokeo mabaya ya kidato cha nne ya mwaka 2010, zikiwemo sababu za kimfumo, uwezo wa usimamizi wa utekelezaji wa mitaala, upatikanaji wa vifaa na uboreshaji wa miundo mbinu. Ukisoma taarifa ya Kamati hiyo, utaona kwamba; sababu za kufeli na mapendekezo yaliyotolewa yanaakisi kwa kiasi kikubwa, sababu na mapendekezo yatakayotolewa na Tume ya Waziri Mkuu inayoendelea kumalizia kazi yake, kama yalivyodokezwa na Mheshimiwa Lukuvi katika taarifa yake aliyoitoa hapa bungeni hivi karibuni, isipokuwa katika swala la kufuta na kupanda upya matokeo ya kidato cha nne ya mwaka 2012. Utangulizi wa taarifa hii uliandikwa na aliyekuwa Katibu Mkuu wa WEMU, Profes Hamisi O. Dihenga, na Dibaji iliandikiwa na Waziri wa WEMU, Mheshimiwa Dkt. Shukuru Kawambwa.

Hata hivyo, taarifa ya Kamati hii haijawahi kutolewa hadharani hadi iliposambazwa hivi karibuni kwenye mitandao ya kijamii na wadau wakereketwa wa elimu. Sasa, ni wajibu wetu kama Kambi ya Upinzani kuhoji mambo yafuatayo:
· Kwa nini Serikali ilificha taarifa ya Kamati iliyoiunda kuhusu matokeo ya kidato cha nne ya mwaka 2010?
· Kwa nini serikali iliunda Kamati nyingine kufanya kazi ile ile iliyofanywa na Kamati iliyoundwa na serikali hiyo hiyo, chini ya usimamizi wa waziri mkuu huyo huyo na waziri wa elimu huyu huyu aliyepo leo?


Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, haiamini kwamba kuporomoka kwa mfumo wetu wa elimu ni kwa bahati mbaya. Wala Kambi ya Upinzani haiamini kwamba serikali hii haina uwezo wa kiraslimali na kimiundo mbinu wa kutatua matatizo ya elimu. Tunachoamini katika Kambi ya Upinzani ni kwamba kuporomoka kwa mfumo wa elimu hapa nchini ndio taswira halisi ya kushindwa kiuongozi kwa Serikali ya Chama cha Mapinduzi. Inabidi watanzania wenzetu waelewe kwamba hawa mliowakabidhi serikali hawawezi na kuendelea kuwaamini ni kuiweka elimu na nchi yetu rehani. Aidha, tusisahau kwamba uwepo wa CCM madarakani kunategemeana sana na idadi kubwa ya wananchi kuendelea na elimu duni. CCM wanajua kwamba uwepo wa idadi kubwa ya watu walioelimika vizuri ni kuhatarisha uwepo wake madarakani. Kwa hiyo, kuharibu mfumo wa elimu kunafanywa makusudi ili chama hiki kiendelee kubaki madarakani kiujanja ujanja. Serikali imezoea kufanya mambo mepesi na kukwepa mambo mazito katika taifa hili.


2. Mfumo wa elimu
Mheshimiwa Spika,
Tumetoa angalizo kwa miaka mingi sasa kwamba mfumo wetu wa elimu umepitwa na wakati. Mosi, watoto wetu wanaanza shule ya msingi kwa kuchelewa sana (6-9)na wanakaa shuleni kwa muda mfupi miaka saba(darasa la kwanza hadi la saba). Kiwango cha wastani duniani cha kukaa shuleni (compulsory)ni miaka tisa, lakini watoto wetu wanakaa miaka saba pekee. Matokeo yake wanamaliza wakiwa wadogo na bila kuwa na maarifa na stadi za msingi za kuwafanya wajitegemee. Ndio maana tumekuwa tukitoa mapendekezo kwamba mfumo wetu wa elimu upitiwe upya ili:
i) watoto waanze shule mapema. Kama tulivyopendekeza katika ilani ya CHADEMA ya Mwaka 2005 na 2010, watoto waanze shule wakiwa na umri usiozidi miaka sita.
ii) Wigo wa elimu ya msingi upanuliwe ili watoto wakae shuleni kwa elimu ya lazima kwa muda usiopungua angalau miaka tisa kama ilivyo katika nchi zingine katika bara la Afrika
iii) Elimu ya msingi lazima iunganishwe na elimu na mafunzo ya ufundi ili kwamba vijana wetu wamalizapo elimu ya msingi wawe na maarifa na stadi za kufanya kazi itakayowafanya wajitegemee popote walipo kama ilivyosisitizwa katika kipindi cha utawala wa awamu ya kwanza chini ya uongozi wa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Mheshimiwa Spika,
Ni bahati mbaya, kwamba, mawazo yetu hayajawahi kusikilizwa kwa sababu ya wivu wa kisiasa kwa kuogopa kuipa CHADEMA sifa kwa ubunifu. Matokeo yake tumeendelea kuwa na mfumo wa elimu uliopitwa na wakati na leo sote tunaona matokeo ya kuporomoka kwa mfumo wetu wa elimu. Hata hivyo, katika hali ambayo si ya kawaida, hatimaye serikali sasa imeamua kukubaliana na maoni ya CHADEMA na sera mpya ya Elimu imependekeza kubadili mfumo wetu wa elimu ikiwemo kupanua wigo wa elimu ya msingi.

Mheshimiwa Spika,
Baada ya maelezo hayo ya jumla, napenda sasa kutoa maoni ya Kambi ya Upinzani katika sekta na ngazi mbalimbali za elimu hapa nchini.

2.1 Elimu ya Awali
Mheshimiwa Spika,
Wataalamu wa elimu wanatuambia kwamba elimu ya awali ndio ngazi muhimu zaidi katika elimu kwa kuwa ndio inayotoa msingi wa elimu katika ngazi zinazofuata. Kwa hiyo wataalamu wa elimu duniani wamekuwa wakitoa wito kwa serikali kuwekeza katika elimu ya awali. Na kwa kweli nchi zilizowekeza vya kutosha katika elimu ya awali ndizo zenye mafanikio makubwa zaidi kielimu duniani kuliko zile zisizowekeza katika elimu ya awali.

Mheshimiwa Spika,
Kwa bahati mbaya sana, hapa kwetu elimu ya awali haijapewa kipaumbele cha kutosha, nah inajidhirisha kwenye randama kwa kuwa hakuna bajeti iliyotengwa kwa ajili ya elimu ya awali. Sera ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ya mwaka 1995, inaelekeza kwamba watoto wote wanapaswa kupitia elimu ya awali kabla ya kujiunga na elimu ya msingi. Sera hii pia inaelekeza kwamba kila shule ya msingi lazima iwe na darasa la elimu ya awali. Hata hivyo, kwa mujibu wa kitabu cha takwimu za elimu kinachotolewa kila mwaka na WEMU (BEST), ni asilimia 39.9 pekee ya watoto wenye stahili ya kujiunga na elimu hiyo, wanaojiunga na elimu hiyo, na kiwango hiki kimekuwa kikishuka badala ya kuongezeka. Kwa mfano, katika mwaka 2012, kiwango cha uandikishaji katika elimu ya awali kilishuka kwa asilimia 3.2 kutoka watoto 1,069,208 mwaka 2011 hadi watoto 1,034,729 katika mwaka wa 2012.



Mheshimiwa Spika,
Hali ya walimu katika elimu ya awali pia ni mbaya kwani, kwa wastani, mwalimu mmoja anafundisha watoto 114 kinyume na kiwango kinachopaswa cha mwalimu mmoja wanafunzi 25. Hali ni mbaya zaidi katika baadhi ya mikoa kama vile Dodoma, Kigoma na Morogoro ambapo mwalimu mmoja hufundisha watoto zaidi ya 600! (Tazama BEST 2012, uk. 13). Bahati mbaya hotuba ya Waziri wa WEMU aliyeisoma hivi punde haina mikakati yeyote ya maana itakayoweza kututoa hapa tulipo. Na hata rasimu ya sera mpya haioneshi mikakati ya kuboresha elimu ya awali


2.2 Elimu ya Msingi na Sekondari
Mheshimiwa Spika,
Pamoja na kwamba tumefanikiwa kama taifa kupanua uandikishaji wa watoto katika elimu ya msingi, na sasa tumefanikiwa kwa kiasi kuongeza udahili katika elimu ya sekondari, ubora wa elimu inayotolewa katika ngazi hizi umeendelea kuwa dhaifu kabisa. Ni bahati mbaya sana kwamba serikali ya CCM imeshindwa kutekeleza mapendekezo mbalimbali ya kitaalamu ambayo yamekuwa yakitolewa katika kuboresha elimu inayotolewa katika ngazi za msingi na sekondari.

Mheshimiwa Spika,
Maoni hayo ni pamoja na kuongeza idadi ya walimu wenye sifa stahiki, kuchochea motisha na mori wa kazi ya ualimu, pamoja na kuboresha mazingira ya kujifunzia. Baadhi ya tafiti za kimataifa zinaonyesha kwamba ni asilimia 4 pekee ya shule za sekondari zenye sifa au zinakidhi vigezo vya chini vya kuwa shule za sekondari. Ndio kusema kwamba, ni shule 160 pekee kati ya zaidi ya shule 4000 za sekondari nchini zenye kustahili kuitwa shule za sekondari. Kwa maneno mengine, shule za sekondari zinazostahili kuitwa sekondari hapa nchini hazizidi shule 160. Haishangazi basi kwamba watoto wanaopitia shule za umma za sekondari wanafeli kwa cha kiwango cha kutisha tunachokishuhudia leo.
Tunaendelea kutoa wito kwa serikali ya Chama cha Mapinduzi kutekeleza maoni, ushauri na mapendekezo ya wataalamu wa elimu katika kuboresha mfumo wa elimu hapa nchini.

2.3 Elimu ya Ufundi
Mheshimiwa Spika,
Elimu ya Ufundi ndio muhimili wa kutoa maarifa na stadi za kuweza kujitegemea. Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, kuna vyuo vya ufundi vipatavyo 248 hapa nchini vinavyomilikiwa na taasisi mbalimbali za serikali pamoja na mashirika ya watu binafsi na taasisi za kidini. Hata hivyo, vyuo hivyo kwa pamoja vina uwezo wa kuchukua wanafunzi wasiozidi 50,000 katika ngazi ya cheti ukilinganisha, kwa mfano, na wanafunzi 973,812 waliomaliza elimu ya msingi kwa mwaka 2012.

Mheshimiwa Spika,
Kwa mwaka huu wanafunzi 513,876 walichaguliwa kujiunga na elimu ya sekondari, sawa na asilimia 52.8 waliomaliza elimu ya msingi. Ndio kusema watoto 459,936 waliomaliza elimu ya msingi mwaka 2012 , sawa na asilimia 42.2, waliingia mitaani bila maarifa na stadi za msingi za kuwafanya wajitegemee.

Mheshimiwa Spika,
Kwa takwimu za hapo juu utaona kwamba vyuo vyetu vya elimu ya ufundi bado ni vichache na havikidhi haja ya mahitaji yaliyopo. Ndio maana CHADEMA ikaweka katika ilani yake mpango wa kuunganisha elimu ya msingi na elimu ya ufundi ili kila mwanafunzi anayepitia elimu ya msingi apate fursa ya kupata mafunzo maalumu ya ufundi kabla ya kumaliza ili aweze kupata maarifa na stadi zitakamuwezesha kujitegemea, kujiajiri, kuajirika na kupata utamaduni na tabia ya kupenda kazi. Bahati mbaya serikali hii ya Chama cha Mapinduzi haina mpango huu na kutokana na wivu wa kisiasa imeshindwa kunakili sera ya CHADEMA na kuitekeleza.


2.4 Elimu ya Juu
Mheshimiwa Spika,
Nchi yetu imepanua elimu ya juu katika ya miaka ya hivi karibuni na hasa katika kipindi hiki cha awamu ya nne ya Rais Kikwete. Kwa sasa tuna vyuo vikuu 28, vyuo vikuu vishiriki 22 na vituo na taasisi zenye hadhi ya elimu ya juu zipatazo 14. Kati ya vyuo vikuu na vyuo vikuu vishiriki vilivyopo nchini 36 (sawa na asilimia 72) vinamilikiwa na kuendeshwa na mashirika na taasisi binafsi, na serikali inamiliki na kuendesha vyuo 14 pekee, sawa na asilimia 28 ya vyuo vikuu na vyuo vikuu vishiriki vyote nchini.

Mheshimiwa Spika,
Kwa niaba ya Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni naomba nichukue nafasi hii kupongeza sana taasisi na mashirika binafsi na hasa taasisi za dini kwa kutoa mchango mkubwa kwa sekta ya elimu ya juu hapa nchini. Kwa kuwa vyuo hivi vinasomesha vijana wa kitanzania wanaolipa kodi kwa serikali hii, ni muhimu sana kuweka utaratibu utakaohakisha kwamba vyuo vya binafsi vinapata ruzuku maalumu ya serikali katika kuchangia na kupunguza makali ya gharama za uendeshaji. Jambo hili lilielezwa vizuri na kwa kina katika ilani ya CHADEMA ya mwaka 2010 na tutalizungumza tena katika ilani ya CHADEMA ya mwaka 2015 hadi kitakapoeleweka.

Mheshimiwa Spika,
Pamoja na kupanua wigo wa elimu ya juu hapa nchini, ubora wa elimu inayotolewa katika taasisi hizi bado ni wa wasiwasi mkubwa. Kuna viashiria vingi vinavyoonyesha kwamba ubora wa elimu ya juu nchini mwetu sio wa kuridhisha. Kiashiria kimojawapo ni uwezo wa vyuo vyetu kuhimili ushindani wa kimataifa. Vyuo vyetu vingi havionekani kabisa katika ligi ya mashindano ya vyuo vikuu duniani. Kwa mfano, kwa miaka takribani mitano mfufulizo ni vyuo viwili pekee vinavyoonekana katika vyuo bora 100 barani Afrika katika Mpango wa Kupima Vyuo Vikuu (World University Ranking) uliofanywa na mashirika ya Times Higher Education (Uingereza), Shanghai (China) na Webometrics. Vyuo hivi ni Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Hubert Kairuki. Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambacho ni bora Tanzania ni cha 1618 kati ya vyuo 2000 duniani vilivyoshindanishwa mwaka 2012. Vyuo vikuu vyetu sio miongoni mwa vyuo vikuu bora 1000 duniani!!

Mheshimiwa Spika,
Kuna sababu nyingi zinazokwamisha ubora wa elimu ya juu ambazo zimeelezwa vizuri katika maandiko ya wataalamu wa elimu nchini na nje ya nchi. Naomba kwa leo nitaje mambo mawili nayo ni ubora wa walimu(wahadhiri) na uhaba wa fedha.

Mheshimiwa Spika,
Ili kuwa mwalimu wa chuo kikuu uliyebobea sharti uwe na shahada ya uzamivu (Ph.D) katika eneo husika la kitaaluma. Katika walimu 3,755 waliopo katika taasisi mbalimbali za elimu ya juu hapa nchini, ni walimu 649 pekee wenye shahada za uzamivu sawa na asilimia 17! Upungufu huu unatokana kwa kiasi kikubwa na serikali kutokutoa kipaumbele katika kusomesha walimu wa vyuo vikuu. Kwa hiyo vyuo vikuu vingi vinategemea zaidi fedha za wafadhili wa nje katika kusomesha walimu wake, ambazo hazina uhakika. Ndio maana katika Ilani ya CHADEMA ya mwaka 2010 tulisema, na tutasema tena mwaka 2015, kwamba serikali iwekeze fedha za kutosha katika kusomesha walimu wa vyuo vikuu ili wapate viwango vinavyokubalika kimataifa. Hali ipo hivyohivyo katika upande wa utafiti. Fedha zinazotolewa kwa ajili ya utafiti ni kidogo sana na tafiti nyingi vyuo vikuu zinategemea ufadhili wa nje.

Mheshimiwa Spika,
Kumekuwa na uhaba mkubwa sana wa fedha za maendeleo na hata za matumizi mengineyo yaani OCs kwa vyuo vya elimu hapa nchini. Hali inayopelekea majengo ya vyuo vyetu hasa vile vya zamani kama UDSM, Ardhi, Sokoine, Mzumbe na Muhimbili kuonekana machakavu kwa kuwa ukarabati haufanywi kwa wakati. Idadi kubwa ya ongezeko la wanafunzi haliendi sambamba na ujenzi wa madarasa, vyoo, maktaba na mabweni. Matokeo yake wanafunzi wanaishi kwa taabu sana huku afya zao zikiwa mashakani. Na kwa wengine hali ya ufinyu wa sehemu za kulala vyuoni huwafanya wafanye matendo maovu yasiyokubalika katika jamii yetu.


Mheshimiwa spika
Fedha zinazopelekwa kwenye vyuo vyetu ni kidogo mno na zinapungua kadiri siku zinavyokwenda huku idadi ya wanafunzi ikiongezeka. Hali hii sio tu inaleta migomo isiyo ya lazima bali pia ina waweka watendaji wa vyuo hivyo njia panda.


3. Anguko la Elimu Nchini na Mustakabali wa Taifa

Mheshimiwa Spika, ni mwaka mmoja tu umepita tangu Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inayoongozwa na CHADEMA itoe angalizo kali kwa Serikali juu ya kasi kubwa ya kuporokoka kwa Elimu ya Tanzania na hivyo kuitaka Serikali kuchukua hatua madhubuti ili kuliepusha Taifa na balaa hilo. Hata hivyo, Serikali hii ya CCM imeendelea kupuuza ushauri mzuri inayopewana na Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na matokeo yake ni kwamba anguko la kipindi hiki ni kubwa kuliko maanguko yote yaliyowahi kutokea katika Historia ya Tanzania ambapo asilimia 56.9 ya wanafunzi waliofanya mtihani wa kidato cha nne mwaka 2012 walipata alama sifuri baada ya kukarabatiwa’standardization’.

Mheshimiwa Spika, matokeo ya mtihani wa kitaifa wa kidato cha nne mwaka 2012 yanaakisi kiwango cha juu cha kudorora kwa elimu nchini na matokeo ya Serikali ya CCM kuipuuza elimu. Pamoja na juhudi kubwa za serikali kubatilisha matokeo hayo bado ukweli umebaki palepale kama ambavyo wataalamu wa elimu walivyobashiri na kuonya zoezi hilo kuwa halina tija kwa taifa. Matokeo ya awali ambayo asilimia 65.5 walipata sifuri sasa imekuwa 56.9 yaani punguzo la asilimia 8.6 wakati wale wa daraja la nne waliokuwa asilimia 33.5 sasa imekuwa 28.1 sawa na ongezeko la asilimia 5.4 huku wale wa daraja la pili asilimia 1.8 na sasa ni 2.8 sawa na ongezeko la asilimia 1. Kwa wale wa daraja la kwanza walikuwa asilimia 0.5 na sasa ni 0.9 sawa na ongezeko la asilimia 0.4.

Mheshimiwa spika.
Kimsingi ukilinganisha matokeo haya utaona kwamba hayana tofauti ya maana (no significant difference)na yale ya awali kwa sababu daraja la kwanza hadi la tatu bado hawajafikia asilimia 10. Na hawa ndio wanaotegemewa kujiunga na elimu ya kidato cha tano! Lakini vilevile ni asilimia 33.5 tu ndio wamepata daraja la nne au theluthi ya watahiniwa wote ukilinganisha na asilimia 28.1 ya awali. Kwa ujumla asilimia 56.9 (57) ya watahiniwa wote wamepata daraja la sifuri ukilinganisha na 65.5 ya awali. Lakini kibaya zaidi bado asilimia 90.5 ya watahiniwa wamepata daraja la nne na sifuri katika matokeo mapya ukilinganisha na yale ya awali ya asilimia 93.6. Kwa maana hiyo bado zaidi ya nusu ya watahiniwa wote wa 2012 wamepaa daraja sifuri au wamefeli hata baada ya mabadiliko ya ripoti ya awali ya tume.

Mheshimiwa spika,
Ni wazi kwamba matokeo mapya yanakubaliana na mapendekezo na ushauri wa wadau mbalimbali wa elimu Tanzania kwamba matokeo ya awali hayakuwa na kasoro zozote na kwamba mfumo uliotumika haukuwa sababu ya matokeo hayo. Pamoja na kwamba kuna punguzo la asilimia ya waliofeli kwa asilimia 8.6 na hivyo kuwa asilimia 56.9 bado matokeo haya ni mabaya kuliko matokeo yote ya kidato cha nne kwa nchi hii toka tumepata uhuru. Na vile vile kama tatizo ni matumizi ya mfumo mpya wa ku grade, vipi hata haya yamekuwa mabaya kuliko ya mwaka 2011 yaliyotumia mfumo wa flexible grading na siyo fixed???

Mheshimiwa Spika,
Kwa uchambuzi huu ni wazi sasa kuwa ukweli ni lazima usemwe hata kama utauma namna gani ili Taifa lisonge mbele kwa kuwa ni dhahiri kuwa watoto wetu walifeli kwa sababu ya mfumo wetu wa elimu. Tunapenda kuionya serikali kuwa mchezo huu wa kisiasa uliochezwa ili kupunguza hasira za wananchi ni mchezo mchafu ambao haulipeleki Taifa letu mbele kwa kuwa hauelezei vyanzo vya matatizo makubwa yanayosababisha anguko la elimu nchini na mfumo wetu wa elimu.

Mheshimiwa Spika, kuna ushahidi wa kutosha kwamba Serikali inahusika sana kusababisha anguko kuu la matokeo ya kidato cha nne 2012. Na ushahidi huo ni kama ifuatavyo:

Mheshimiwa Spika, tarehe 14 Novemba, 2012 Kamishna wa Elimu Profesa E. P. Bhalalusesa alimwandikia Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa yenye kichwa cha habari “YAH: UTARATIBU WA MATUMIZI YA ALAMA ZA MAENDELEO YA MTAHINIWA NA VIWANGO VYA UFAULU KATIKA MITIHANI YA TAIFA”.

Mheshimiwa Spika, Katika barua hiyo, Kamishna wa Elimu alisema hivi: “Kutokana na maelezo ya barua yako, Wizara imeridhia mapendekezo ya uwiano wa alama za maendeleo ya wanafunzi (CA) na alama za mtihani wa mwisho kubadilishwa kutoka alama 50:50 na kuwa 30:70. Wizara inaridhia pia alama 15 zitokane na mtihani wa kidato cha pili kwa wanafunzi wa kidato cha nne. Aidha, wizara inataka mlete mchanganuo wa jinsi alama 15 zilizobakia zitakavyopatikana ili kuleta uelewa wa pamoja. Vivyo hivyo mchanganue mgawanyo wa alama za maendeleo ya mwanafunzi kwa kidato cha sita”

Mheshimiwa Spika, tarehe 12 Desemba, 2012, (mwezi mmoja baadaye) Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Selestine Gesimba alimwandikia barua Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Tanzania kama ifuatavyo:
“YAH: MAAGIZO YA KUHUSU UTARATIBU WA MATUMIZI YA VIWANGO VYA UFAULU KATIKA MTIHANI WA KIDATO CHA NNE NA SITA
Tafadhali rejea kikao cha tarehe 10/12/2012 kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Wizara kuhusu somo tajwa hapo juu.
Baada ya kupitia mapendekezo mliyowasilisha pamoja na majadiliano katika kikao husika naelekeza yafuatayo yafanyike.
i. Viwango vya Ufaulu vilivyopendekezwa na Baraza la Mitihani Tanzania vitumike kwa mitihani ya kidato cha nne 2012 na kidato cha sita kwa mwaka 2013 tu.
ii. Viwango vya kutunuku (grade range) vifanyiwe kazi zaidi ili kupunguza au kuondoa mlundikano (bunching) wa alama katika kundi moja
iii. Baraza la Mitihani Tanzania lifanye utafiti kuhusu matumizi ya alama za maendeleo kwa “O” Level na “A” Level na kutoa mapendekezo mapya ya matumizi ya alama za maendeleo ( Continuous Assessment)
Utekelezaji wa maagizo haya ufanyike mapema ili mapendekezo yaliyowasilishwa yaweze kuanza kutumika katika mwaka wa fedha 2013/2014”

Mheshimiwa Spika, mjumbe mmojawapo wa kikao kinachotajwa na barua hii, ni Profesa Sifuni Mchome ambaye alikuja kuwa mwenyekiti wa tume ya kuchunguza matokeo ya mtihani wa taifa wa kidato cha nne mwaka 2012 na kupendekeza matokeo hayo yafutwe. Wajumbe wengine walikuwa ni Dkt. Shukuru Kawambwa, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Selestine Gesimba, Kaimu Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na Profesa E. P. Bhalalusesa, Kamishna wa Elimu. Wote hawa ni maafisa wa Serikali ambao walishiriki kikamilifu kufanya maamuzi na kutoa maagizo ya kubadili mfumo wa kupanga matokeo ya kidato cha nne 2012 ambao sasa wanakimbia kivuli cha maamuzi yao na kulibebesha Baraza la Mitihani la Tanzania mzigo wa uvivu wao wa kufikiri na woga wa kuchukua hatua za kuwajibika kwa kujiuzulu kwa kushindwa kusimamia elimu ya Tanzania.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inayoongozwa na CHADEMA inakichulia kitendo cha Serikali kulitupia baraza la mitihani mzigo ili kuhalalisha makosa iliyoyafanya na kusababisha wanafunzi wa kidato cha nne 2012 kupata alama sifuri kwa zaidi ya asilimia 60 wakati Serikali ndiyo iliyokuwa ikitoa maagizo kwa baraza la mitihani, ni usaliti wa hila kwa baraza la mitihani. Aidha uamuzi wa Serikali wa kuyafuta matokeo ya kidato cha nne yaliyopitishwa na bodi ya NECTA chini ya uongozi wa Profesa Rwekaza Mukandala ulikwenda kinyume kabisa na misingi ya utaalamu na weledi (professionalism) na kwa misingi hiyo haukuwa na uhalali.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kutoa majibu mbele ya bunge hili, “standardization” iliyofanywa na Serikali kwa matokeo ya kidato cha nne inakwenda kumsaidia vipi mwanafunzi ambaye hakuandika chochote katika karatasi ya mtihani zaidi ya kuchorachora picha za ajabu na kuandika matusi? Na je! marekebisho haya, yanakwenda kusaidia vipi familia ambazo ziliathirika na matokeo haya kwa watoto wao kujiua kutokana kufeli mtihani huo?

Mheshimiwa Spika, kwa vyovyote vile mchakato wa uliobadili matokeo ya kidato cha nne hauna tija kwa taifa kwa kuwa unaturudisha nyuma. Itakumbukwa kwamba sababu zilizopelekea Serikali kupitisha matumizi ya viwango vipya vya ufaulu katika mitihani ya kidato cha nne na sita 2012/13 ni kwamba mfumo wa zamani ulikuwa haupandishi ubora wa elimu yetu. Kambi Rasmi ya Upinzani inaona kwamba uamuzi wa Serikali ya CCM kurudi kwenye mfumo wa zamani wa kupanga matokeo una lengo la kuendelea kudidimiza elimu ya nchi yetu jambo ambalo halikubaliki.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaishauri bodi ya NECTA kwamba kwa kuwa serikali imelazimisha mabadiliko ya matokeo ya kidato cha nne kinyume na miiko ya weledi wa bodi hiyo, basi bodi hiyo ijiuzulu ili kulinda heshima yake ya utaalamu na weledi kwa kutoruhusu maamuzi ya kisiasa kuathiri utendaji wa kitaalamu. Aidha kwa kufanya hivyo, Serikali itapata funzo la kuwajibika inapofanya makosa ya wazi kama haya.

Mheshimiwa Spika, Kauli ya Serikali iliyawasilishwa hapa bungeni tarehe 3 Mei, 2013 na Mhe. William Lukuvi kuhusu taarifa ya awali ya tume ya taifa ya kuchunguza matokeo ya mtihani wa taifa wa kidato cha nne 2012 ilisema hivi: “Maamuzi ya Baraza la Mawaziri yanalenga kutenda haki kwa walimu na wanafunzi ambao juhudi zao za kufundisha na kujifunza zimepimwa kwa kwa kutumia mfumo wa mpya ambao hawakupata fursa ya kushirikishwa na kuandaliwa”.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani haioni uhalisia wa kauli hii wala haioni nia ya dhati ya Serikali kuwasaidia wananchi kupata elimu bora kwa haki na kwa usawa kwani ni hivi majuzi tu katika Mkutano wa Kumi wa Bunge, ambapo hoja binafsi ya Mheshimiwa James Mbatia (Mb) kuhusu udhaifu ulioko katika sekta ya elimu nchini ilibezwa na Serikali kwa kutolewa majibu mepesi kinyume na kanuni za bunge na hatimaye kuyazima maazimio ya bunge ya kuinusuru elimu ya Tanzania yaliyokuwa yamependekezwa katika hoja hiyo.

Mheshimiwa Spika, ni katika mkutano huohuo wa Bunge ambapo hoja binafsi ya Mheshimiwa Joshua Nassari (Mb) kuhusu Baraza la Mitihani linavyoathiri elimu ya Tanzania iliondolewa katika orodha ya shughuli za mkutano wa kumi wa Bunge bila ridhaa ya mtoa hoja kinyume na kanuni ya 58(5) ya Kanuni za Kudumu za Bunge.

Mheshimiwa Spika, maazimio yaliyokuwa yameanishwa katika hoja zote mbili nilizozifanyia rejea hapo juu yalikuwa na tija sana katika kuuboresha mfumo wa elimu hapa Tanzania na pia yalikuwa yanatoa suluhu kwa tatizo la kushuka kwa ufaulu wa wanafunzi ambalo linaongezeka kila mwaka.

Mheshimiwa Spika, kitendo cha Serikali ya CCM chini ya mwavuli wa wingi wa wabunge wake bungeni, cha kuzivuruga hoja hizi na hivyo kusababisha maazimio ya bunge juu ya hoja hizi kutotekelezwa ni udhaifu mkubwa sana kwa chama kinacho tawala cha CCM na Serikali yake na ni ushahidi uliokamilika kwamba Elimu kwao sio kipaumbele cha taifa.

Mheshimiwa Spika, niwe mkweli na muwazi kwamba Serikali ambayo Elimu sio kipaumbele cha Taifa, haiwafai watanzania kwa karne hii. Hivyo Kambi Rasmi ya Upinzania inaionya Serikali kuacha kabisa kufanya mzaha na elimu ya taifa hili kwani ikiendelea kufanya mchezo na elimu kama ilivyo sasa, italiingiza taifa kwenye msiba mkubwa wa umasikini mkuu ambao matanga yake hayaishi leo wala kesho bali ni ya miaka mingi ijayo. Aidha kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inawapa angalizo wananchi wote wa Tanzania kwamba haya yote yanatokea kwa kuwa Serikali ya CCM haijaiweka Elimu kuwa kipaumbele cha taifa na kwamba umefika wakati wa kufanya mabadiliko makubwa ya mfumo wa utawala kwa kuchagua chama chenye nia ya dhati ya kuleta mabadilko kitakachounda Serikali inayojali elimu ya watoto wao na bila shaka chama hicho hakiwezi kuwa CCM tena.

4. Gharama za Elimu Nchini?
Mheshimiwa Spika,
Wote tunatambua kuwa kupata elimu ni haki ya kila mtanzania. Vilevile, natambua kuwa soko huria limeshamiri katika sekta zote nchini ikiwemo elimu. Lakini kinachosikitisha, wote tunaelewa kipato cha watanzania wengi. Na mwalimu Nyerere alionya kuwa tukishabaguana katika elimu tutakuwa na matabaka. Na kimsingi hapo ndipo tulipofika. Haiwezekani serikali ishindwe kudhibiti gharama za elimu hapa nchini katika ngazi zote. Kwa mfano inawezekanaje mwenye shule aamue kupandisha ada kwa shilingi milioni moja ghafla? Inawezekanaje vyuo vya elimu ya juu vilipishe wanafunzi wao fedha nyingi kuliko kiwango kinachotolewa na bodi ya mikopo? Mfano chuo cha St Joseph Songea wanapaswa kulipa chuo shilingi 2,750,000/= huku bodi ya mikopo ikiwapatia shilingi 1,043,000/= hivyo kujikuta wakilipa shilingi 1,707,000/=. Hivi ni watoto gani wa wakulima wataweza kulipa fedha hii? Na kibaya zaidi vijana hawa wanasoma masomo ya sayansi yaani (Bachelor of Science and Technology in Agriculture). Je tutafanikisha Kilimo Kwanza kama tunapoteza vijana wenye uwezo wa kusomea taaluma hii?

Mhesimiwa Spika
Sambamba na shule binafsi umejitokeza utata mkubwa kuhusiana na ongezeko kubwa la ada kwa shule ya serikali ya Arusha School tofauti na wenzao wa Olympio. Wazazi na walezi wameandika barua kwa watendaji wa wizara lakini hadi ninapozungumza hawajajibiwa na hawaelewi hatma ya watoto wao. Swali la kujiuliza; kama shule hii iko chini ya Wizara ni kwa nini ada zinapanda kiholela na ni kwa nini kwa shule hiyo tu?
Ni vyema serikali iangalie utaratibu mzima wa kugharamia elimu hapa nchini ili wazazi, walezi na wadau wote wa elimu waelewe vizuri

5. Changamoto katika Sekta ya Elimu na Tatizo la Kupanga Vipaumbele vya Bajeti ya Elimu

Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na HakiElimu 2011, hali ya mazingira katika shule zetu kuanzia elimu ya awali mpaka sekondari ni mbaya kwa kujifunzia. Uwiano wa mwalimu mwenye sifa kwa mwanafunzi elimu ya awali umebaki kuwa 1:124 badala ya 1:25; uwiano wa matundu ya vyoo kwa wanafunzi msingi unakadiriwa kuwa 1:56 badala ya 1:25 kwa wavulana na 1:55 badala ya 1:20 kwa wasichana. Mrundikano wa wanafunzi darasani ni mkubwa mno, wastani kwa nchi nzima ni 1:70 badala ya 1:40, uhaba wa madawati unafikia asilimia 49.1 kwa sasa ikiwa ni upungufu wa takribani madawati 1,879,806 kati ya 3,893,338 yanayohitajika. Shule za sekondari pia zinaathiriwa na changamoto za namna hii pamoja na tatizo la uhaba wa mabweni, maabara, vitabu na walimu wa masomo ya sayansi. Pia hamasa ya mioyo ya walimu kujitolea na kuridhika na ualimu iko chini sana. Changamoto hizi zinatupa ishara kuwa shule zetu za umma (msingi na sekondari) si shule ambazo zinaweza kumfanya mwanafunzi afundishwe na ajifunze ipasavyo.



Mheshimiwa Spika ,
Ni jambo ola kushangaza kuona hata shule za vipaji maalumu kama Mzumbe hawana vyoo hali iliyopelekea vijana hawa kuacha masomo na kuandamana hadi kwa Mkuu wa Mkoa. Kama shimo moja la choo linatumika kwa wanafunzi 150 hivi kweli tunawapeleka wapi watoto wetu?

Mheshimiwa Spika, ni wazi kuwa changamoto hizi zina uhusiano wa moja kwa moja na upangaji wa vipaumbele vyetu na maamuzi ya matumizi ya rasilimali za taifa. Ikiwa tunataka kutoka hapa tulipo kwenda mahali bora zaidi ni lazima upangaji wa bajeti katika sekta ya elimu uangaliwe kwa makini sana kwa kuwashirikisha wadau wote wa sekta ya elimu ili kutatua changamoto za sekta ya elimu. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka sasa serikali kuacha visingizio vya uhaba wa bajeti na wahisani kukwamisha utekelezaji wa mipango ya kuikwamua elimu. Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inatoa mapendekezo yafuatayo katika upangaji wa bajeti katika sekta ya elimu 2013/2014.
i. Tatizo la Wanafunzi kutojua Kusoma na Kuandika
Mheshimiwa Spika, hili bado ni tatizo kubwa na hadi sasa serikali haijawa na mkakati maalumu wa kuondoa tatizo hili. Shule za msingi kwa madarasa yote bado zina wanafunzi wasiojua kusoma na kuandika. Hali hii imejitokeza pia katika baadhi ya shule za sekondari licha ya serikali kudai itawabaini na kuwaondoa. Tatizo hili lazima lianze kufanyiwa kazi kwa kuwa na mpango maalumu wa kuwasaidia wanafunzi wasiojua kusoma na kuandika. Mpango huu lazima uwashirikishe wadau wote wa sekta ya elimu hasa wazazi ili watambue majukumu yao katika kuondoa tatizo hili.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa elimu ya awali ni msingi wa mwanafunzi katika kujifunza kusoma na kuandika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inayoongozwa na CHADEMA inataka kuona bajeti hii ikitilia mkazo uwekezaji katika elimu ya awali hasa kuwa na walimu bora na vifaa vya kujifunzia na kufundishia. Uwekezaji katika elimu ya awali utachangia sana kuondoa tatizo sugu la kuwa na wanafunzi wasiojua kusoma na kuandika katika shule za msingi.

Mheshimiwa Spika,
Tunatambua kuwa ni majuzi tu waheshimiwa wabunge wamepitia rasimu ya sera ya elimu na msisitizo umewekwa kwenye elimu ya awali lakini cha ajabu bado mkakati wake hauoneshi ni jinsi gani itawaandaa walimu wa shule hizi. Utaratibu wa sasa ni walimu wale wale wa msingi hufundisha na awali. Hili ni tatizo kwa kuwa watoto hawa wana mahitaji maalum na hivyo wanahitaji walimu maalumu waliopita katika vyuo maarufu kama Montesori ili kuwalea vizuri watoto hawa wajitambue na kupenda shule hasa ikizingatiwa hapa ndipo ubongo wa mtoto unapokuwa kwa kasi kubwa.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inatambua kwamba katika Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM III), Serikali imeazimia kuanzisha fungu maalumu katika bajeti ya elimu (separate budget line) kwa ajili ya elimu ya awali na kutenga asilimia 20 ya matumizi yake ya kawaida kwa ajili ya sekta ya elimu huku asilimia 60 ya fedha zitakazotengwa kwa ajili ya sekta kuelekezwa katika elimu ya awali na msingi. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inayoongozwa na CHADEMA inaitaka Serikali kutekeleza mpango huu katika bajeti ya mwaka wa fedha 2013/2014.

ii. Uhaba wa Fedha na Wataalamu Idara ya Ukaguzi wa Shule
Mheshimiwa Spika,
Ripoti ya tathmini ya Mpango wa pili wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM) inaonesha kutofikiwa kwa malengo ya ukaguzi wa shule hivyo kuziacha shule nyingi bila kukaguliwa. Sababu kubwa ya kutofikiwa kwa malengo ya ukaguzi ni uhaba wa fedha unaosababisha upungufu wa vitendea kazi na wataalamu wa ukaguzi. Mwaka 2011/12 shule za msingi zilizokaguliwa ni 3,061 tu kati ya 7,200 zilizopangwa kukaguliwa ( sawa na silimia 42.5). Aidha, sekondari 935 (43.3%) zilikaguliwa kati ya 2,100 zilizopangwa kukaguliwa.


Mheshimiwa Spika,
Hii ni kusema kwamba ni asilimia 19.1 pekee kati ya shule za msingi nchini ambazo hukaguliwa na asilimia 21.4 tu ya sekondari ambazo hukaguliwa kwa mwaka. Tafsiri hapa ni kuwa uwezo wa fungu la ukaguzi katika bajeti ni kukagua asilimia 20 tu ya shule zake zote, asilimia 80 ya shule hazipati fursa ya kukaguliwa kutokana na uhaba wa bajeti. Athari za shule kutokaguliwa ni nyingi, utendaji wa walimu kutopimwa, utekelezwaji wa mitaala, maendeleo ya shule na wanafunzi kutopimwa. Kama ukaguzi haufanyiki kwa nini tunashangaa wanafunzi kufeli au kumaliza elimu ya msingi na kufaulu mitihani ilihali hawajui kusoma na kuandika?

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inayoongozwa na CHADEMA inaitaka Serikali katika bajeti ya Elimu ya 2013/2014 kutoa kipaumbele katika kuimarisha ukaguzi wa shule. Aidha, Serikali itenge fungu la kutosha kwa ajili ya ukaguzi, kwa kuwa tumeona athari ya shule kutokaguliwa katika matokeo mabaya ya wahitimu wa darasa la saba, kidato cha pili na cha nne 2012 na tusingependa kuona haya yakijirudia.

Mheshimiwa Spika
Kwa kuwa kiengo kimekuwa hakitengewi fedha za kutosha, watumishi wake ambao kimsingi wanapaswa kuwa mashuleni kuhakiki ufundishaji na ufundishwaji, wameishia kukaa ofisini kwa kuwa hawana vitendea kazi vya kuwafikisha huko. Kwa mfano kanda yenye shule za sekondari 430 na vyuo vya ualimu kupatiwa shilingi milioni 4 kwa mwaka ni jambo lisiloelezeka na ni kichekesho kwani fedha hii haitoshi ukarabati wa magari mawili ya kanda achilia mbali mafuta!

Hivi kama kazi mojawapo ya ukaguzi ni kufuatilia na kuhakiki ubora wa elimu, na bila kufika na kuona na kutoa ushauri kwa watoa maamuzi ni vigumu sana kujua kinachoendelea ndani na nje ya madarasa yetu.

Mheshimiwa spika,
Ni kwa muda mrefu sasa serikali kupitia wizara hii iliahidi kuanzisha wakala wa ukaguzi na jambo hili likakolezwa na Rais Dkt. Kikwete wakati wa mkutano wake na viongozi wa shule binafsi TAMOGOSCO kule Mbeya 31/4/2013. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali ilieleze bunge hili ni lini sasa wakala huu utaanza? Hii ni kwa kuwa wakaguzi huishia kutoa ushauri na si kutekeleza au kuchukua hatua kwa yale mapungufu wanayokutana nayo.

iii. Uhaba wa Fedha za Ruzuku shuleni
Mheshimiwa Spika, ili kuinua ubora wa elimu serikali iliazimia kutoa ruzuku kwa kila mwanafunzi kupitia MMEM & MMES; shilingi 10,000/= kwa mwanafunzi shule ya msingi na shilingi 20,000/= kwa mwanafunzi wa sekondari kila mwaka. Hata hivyo, mujibu wa utafiti uliofanywa na HakiElimu 2012, ni wastani wa shilingi 6,025/= tu ambazo hufika shuleni badala ya shilingi 10,000/= kwa msingi na wastani wa shilingi 14,178/= pekee badala ya shilingi 20,000/= zilizoahidiwa kwa kila mwanafunzi wa Sekondari. Hali hii imekwamisha shughuli nyingi za maendeleo ya mwanafunzi shuleni, vitabu havinunuliwi kwa wakati, nyenzo za kufundishia na fedha za uendeshaji wa shule hazitoshi. Katika baadhi ya shule hasa katika Mkoa wa pwani, fedha za capitation grants zinazopelekwa ni shilingi 2,000 kwa mwanafunzi wa shule ya msingi. Fedha hizi, licha ya kuwa kidogo mno kwa mahitaji, bado zinakatwa tena kwa ajili ya michezo ya UMITASHUMTA na hivyo kiasi kinachobakia hakiwezi kufanya chochote. Matokeo yake ni kwamba wazazi wanalazimishwa kulipa michango mbalimbali ya shule jambo ambalo ni kero kubwa kwa wananchi.

MheshimiwaSpika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inayoongozwa na CHADEMA inaitaka Serikali kutenga kiwango kamili cha 10,000/= na 20,000/= kwa mujibu wa ahadi na kuhakikisha kuwa fedha hizo zinatolewa zote kwa shule husika. Aidha Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kuzingatia mfumuko wa bei wakati wa kutoa fedha za ruzuku kwa kuwa mfumuko wa bei umekuwa ukiathiri pia uwezo wa shilingi katika kufanya manunuzi. Itakumbukwa kuwa upangaji wa kiwango hiki cha ruzuku ulifanyika 2002-2006 wakati mfumuko wa bei ukiwa katika wastani wa 4.4% wakati leo wastani wa mfumuko wa bei ni takriban asilimia 14.9%[1], hii ikiwa ni mara tatu zaidi ya wastani wa mfumuko wa bei wa kipindi fedha za ruzuku zilivyopendekezwa.



iv. Upangaji na Usimamizi wa Fedha za Umma.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Hotuba ya Waziri wa Fedha iliyotolewa tarehe 9 Juni, 2011, Serikali ilitoa ahadi ya kupunguza bajeti ya matumizi ya kawaida ili kuongeza bajeti za miradi ya maendeleo. Hata hivyo bado Wizara ya Elimu imeendelea kutenga fedha nyingi katika matumizi ya kawaida huku eneo la “matumizi mengineyo” likiendelea kutengewa fedha nyingi zaidi. Takwimu zinaonesha bajeti ya matumizi ya kawaida ya wizara imeongezeka kutoka bilioni 523.8 mwaka 2011/12 hadi bilioni 631.9 mwaka 2012/13, sawa na ongezeko la asilimia 20; wakati fedha za matumizi mengineyo (posho, mafuta, safari, samani na ukarimu) ikiongezeka kutoka bilioni 207 mwaka 2011/12 hadi bilioni 386 mwaka 2012/13 sawa na ongezeko la asilimia 86.

Mheshimiwa Spika kwa mwaka wa fedha 2013/2014 Bajeti ya matumizi ya kawaida imeshuka kutoka shilingi bilioni 631.9 kwa mwaka 2012/2013 hadi kufikia shilingi bilioni 617.08 huku bajeti ya matumizi mengineyo (posho, mafuta,safari, samani na ukarimu) ikipungua kidogo kutoka shilingi bilioni 386 kwa mwaka 2012/2013 hadi kufikia shilingi bilioni 384.6 kwa mwaka 2013/2014.

Mheshimiwa Spika,
Licha ya kupungua kidogo kwa matumizi mengineyo (tofauti ya bilioni 2), bajeti ya maendeleo (ambayo ndio roho ya elimu yetu) imeporomoka kutoka shilingi bilioni 92.6 kwa mwaka 2012/2013 hadi kufikia shilingi bilioni 72.6 kwa mwaka 2013/14 (tofauti ya shilingi bilioni 20). Lengo la kupunguza matumizi mengineyo (na yasiyo ya lazima, ilikuwa ni kuongeza bajeti ya maendeleo ili kuleta maendeleo katika sekta ya elimu. Kwa maana hiyo, lengo hilo halijatimizwa.

Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa bajeti ya sekta ya elimu umekuwa si mzuri pia. Licha ya serikali kudai kuwa haina fedha za kutatua changamoto zinazoikabili sekta ya elimu, bado kumekuwa na usimamizi mbaya wa hata zile fedha kidogo zinazopangwa. Kwa mfano, Ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya mwaka 2010/2011 ilibaini kuwa fedha zilizotolewa kwa miradi ya MMEM na MMES hazikutumiwa na Halmashauri kutekeleza miradi hiyo. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inayoongozwa na CHADEMA inaitaka Serikali kuachana na matumizi kawaida yasiyo ya lazima katika bajeti ya 2013/2014 na badala yake fedha hizo zitumike kutatua changamoto muhimu kama urekebishaji wa maslahi ya walimu kama vile nyumba, mishahara na posho ya mazingira magumu ya kazi, na ukaguzi wa shule,

Mheshimiwa Spika, hatua hii itasaidia kurudisha morali wa ufundishaji na kupunguza matatizo ya ufaulu nchini. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inayoongozwana CHADEMA inaitaka Serikali kuwa na tabia ya kupanga bajeti kwa kuainisha vipaumbele vichache vinavyotekelezeka. Hii ni kwa sababu Serikali haiwezi kutatua matatizo yote kwa wakati mmoja, hivyo ni muhimu Serikali ijenge utamaduni wa kuteua vipaumbele vichache katika bajeti kwa kila mwaka wa fedha ili kutatua changamoto za sekta ya elimu. Bajeti hii lazima ieleze bayana mikakati ya Wizara kuboresha usimamizi na ufanisi wa fedha za umma hasa katika kuhakikisha fedha zinafika kwa walengwa kwa wakati, zinatumika kama zilivyopangwa na zinatumika ipasavyo kwa mantiki ya kuleta thamani iliyokusudiwa (value for money).


6. MASLAHI NA STAHILI ZA WALIMU NCHINI
Mheshimiwa Spika, tofauti na Kauli Mbiu ya Serikali hii ya CCM ya “Maisha Bora kwa Kila Mtanzania”, sasa Serikali imeyafanya maisha ya watanzania kuwa magumu zaidi kwa kutoboresha maslahi na mishahara ya walimu. Aidha madai ya walimu yamezidi kujilimbikiza jambo linalowafanya walimu wazidi kuishi kwa tabu. (Tazama kiambatanisho namba 1 kuhusu malimbikizo ya madai ya walimu nchi nzima ambayo ambayo hayajalipwa hadi mwezi Mei, 2013.

Mheshimiwa Spika,
Madai haya ni ya tangu 2007. Mwaka 2009 Serikali ilifanya uhakiki wa madai ya walimu na kupata Jumla ya shilingi bilioni 52 ambapo shilingi bilioni 32 ni madai ya mishahara na shilingi bilioni 20 ni madai yasiyo ya mishahara (kama vile likizo, uhamisho, matibabu, gharama za masomo nk). Serikali imejitahidi sana kulipa madai yasiyo ya mishahara. Madai ya mishahara yameendelea kulipwa kwa kasi ndogo sana. Kwa mfano katika uhakiki wa mwaka 2009 katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro, jumla ya walimu 364 waliodai jumla ya shilingi milioni 417 ni walimu 25 tu wamepwa jumla ya shilingi milioni 40 hadi sasa. Mfano huu wa kasi ndogo ya kulipwa ni kwa nchi nzima. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali, kuwalipa walimu haki yao kwani kwa kutowalipa kunaweza kuwa sababu kubwa ya kuporomoka kwa elimu kama tunavyoshuhudia sasa kutokana na walimu kuvunjika moyo kwanza kwa kulipwa mishahara midogo sana ukilinganisha na kada nyingine za utumishi wa umma lakini pia licha ya kupunjwa, walimu hawalipwi stahili zao kwa wakati.

Mheshimiwa Spika, Mara baada ya Rais Jakaya Mrisho Kikwete kuingia madarakani 2005, aliunda tume kadhaa ikiwa ni pamoja na Tume ya kuboresha mishahara ya watumishi wa umma iliyoongozwa na Mheshimiwa Deogratius Ntukamazina (Mb). Jambo la kushangaza badala ya kuboresha mishahara ya watumishi wa umma, tarehe 1 Disemba 2009, serikali kupitia ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumisi wa Umma, iliandaa waraka namba C/AC.44/45/01/84, wenye kichwa cha habari kisemacho “UTARATIBU WA KUWABADILISHA KAZI (RECATEGORIZATION)/KUPANDISHA CHEO WALIMU WA SHULE ZA SERIKALI AMBAO WAMEJIENDELEZA KIELIMU.

Mheshimiwa Spika, waraka huo unaagiza kuwa walimu ambao walishaajiriwa na serikali wakienda masomoni wanaporudi kutoka masomoni, wafanyiwe utaratibu wa kupandishwa vyeo kwa majina (recategorization) lakini mishahara yao waliyofikia iondolewe na badala yake warudishwe nyuma hadi kwenye mishahara ya walimu wanaoanza kazi. Kwa maana nyingine ni kwamba umri wa mwalimu kukaa kazini unafutwa (deletion of seniority in service).

Mheshimiwa Spika, kwa ufafanuzi ni kwamba, walimu wamegawanyika katika makundi au kada tatu zifuatazo:-
i. Walimu: Hawa ni walimu wenye elimu ya kidato cha nne na mafunzo ya ualimu katika ngazi ya cheti na wanaajiriwa ili kufundisha katika shule za msingi. Mwalimu anayeajiriwa kwa mara ya kwanza katika kada hii (Preservice), huanza na mshahara wa ngazi ya TGTS B na hupanda mpaka ngazi ya mshahara wa TGTS E ambayo ndiyo ukomo (Bar) wake. Hawezi kupanda tena kwenda cheo kinginne cha mshahara mpaka atakapofungua ukomo huo kwa kuongeza kiwango chake cha elimu kutoka ngazi ya kidato cha nne na mafunzo ya ualimu ya ngazi ya cheti kwenda kiwango cha elimu ya kidato cha sita na mafunzo ya ualimu ya ngazi ya Stashahada (Diploma) au Shahada (Degree) ya chuo kikuu. Na ataendelea kuwa mwalimu wa shule za msingi kwa kupewa majukumu yanayoendana na kiwango chake cha elimu.

ii. Maafisa elimu wasaidizi: Hawa ni walimu wenye elimu ya kidato cha sita na mafunzo ya ualimu katika ngazi ya Stashahada (Diploma) na wanaajiriwa ili kufundisha katika shule za sekondari au katika vyuo vya ualimu vya ngazi ya cheti. Walimu hawa wanapoajiriwa kazini kwa mara ya kwanza (Preservice), huanza na mshahara wa ngazi ya TGTS C na hupanda vyeo vya mshahara mpaka ngazi ya TGTS F ambayo ndiyo ukomo (Bar) wake. Hawezi kupanda tena kwenda cheo kingine cha mshahara mpaka atakapofungua ukomo huo kwa kuongeza kiwango chake cha elimu kutoka kidato cha sita na mafunzo ya ualimu ya ngazi ya Stashahada (Diploma) na kufikia kiwango cha elimu na mafunzo ya ualimu ya kiwango cha Shahada (Degree) ya Chuo kikuu.

iii. Maafisa elimu: Hawa ni walimu wenye elimu na mafunzo ya ualimu katika ngazi ya Shahada (Degree) ya chuo kikuu na wananjiriwa ili kufundisha katika katika shule za sekondari na katika vyuo vya ualimu vya cheti na Diploma. Walimu hawa wanapoajiriwa kwa mara ya kwanza (Preservice), huanza na cheo cha mshahara cha TGTS D na hupanda mpaka cheo cha mshahara cha TGTS I ambayo ndiyo ukomo (Bar) wake. Hawezi kupanda tena cheo cha mshahara mpaka atakapoongeza kiwango chake cha elimu kutoka Shahada (Degree) kwenda Shahada au Stashahada ya uzamili (Masters Degree/Post Graduate Diploma).

Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa waraka unaolalamikikwa na walimu ni kwamba:-
Mwalimu wa shule ya msingi mwenye mshahara wa TGTS E (Tsh.720, 000/=), akijiendeleza kielimu ka kupata Diploma, abadilishiwe muundo kwa kuitwa Afisa Elimu Msaidizi daraja la II lakini mshahara wake ushushwe kutoka Tsh.720,000/= mpaka Tsh. 370,000/= ambayo ni TGTS C, daraja ambalo mwalimu wa diploma anayeajiriwa kwa mara ya kwanza huanzia.
Na kama mwalimu huyo huyo alikuwa amejiendeleza kutoka cheti na kwenda Degree badala ya Diploma basi anapewa cheo cha jina kwa kuitwa Afisa Elimu daraja la II lakini mshahara wake unashushwa kutoka Tsh. 720,000/= mpaka Tsh. 532,000/= ambayo ni TGTS D, daraja ambalo huanzia mwalimu mwenye degree anapoajiriwa kwa mara ya kwanza. Wakati huo endapo mwalimu huyo aliyejiendeleza kielimu alikuwa na Diploma na alikuwa bado hajafkia ukomo wa mshahara kwa mujibu wa kiwango chake cha elimu, tukimwita ni mwalimu X, anaposhushwa mshahara kwenda Tsh. 532,000/= au Tsh. 370,000/=, mwalimu Y mbaye hajajiendeleza kielimu anapandishwa mshahara wake kwenda Tsh. 930,000/=.

Mheshimiwa spika, baada ya walimu nchini kupinga kwa nguvu zote Waraka huo, Serikali iliwadanganya walimu kwamba imefuta waraka huo kwa kuandika waraka mwingine wenye namba CAC.44/45/O1/A/121 wa tarehe 20 Disemba 2011 kwa kichwa cha habari kile kile na maudhui kandamizi kuliko hata waraka ule wa kwanza.

Mheshimiwa Spika, baada ya kuhuishwa kwa waraka namba C/AC.44/45/01/84 kwa kutumia waraka namba CAC.44/45/O1/A/121, tatizo linaloendelea sasa ni kwamba, walimu wote waliojiendeleza kielimu, badala ya kupandishwa madaraja ya mishahara, sasa wanafanyiwa ‘recategorization’ mpya na wanabakizwa kwenye madaraja yale yale na wanatakiwa kukaa kwenye madaraja hayo kwa muda wa miaka mingine mitatu zaidi ndipo wapande madaraja ya mshahara. Huu ni uonevu na ubaguzi mkubwa sana kwa walimu wanaojiendeleza.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, kama kuna walimu wawili, (mwalimu X na mwalimu Y), ambao waliajiriwa pamoja na wanapanda madaraja ya mishahara pamoja na wana kiwango cha elimu cha kimoja (tuseme Diploma) na kama mwaka wao wa kupandishwa madaraja ni 2013, tofauti inajitokeza kama ifuatavyo:

Ikiwa mwalimu X amejiendeleza kielimu na kupata degree, wakati mwalimu Y hajajiendeleza kielimu wote wawili wako kwenye daraja la mshahara la TGTS- E lenye mshahara wa Tsh. 748,000/= kwa mwezi. Kwa mujibu wa Waraka namba CAC.44/45/O1/A/121, mwalimu Y ambaye hajajiendelea kielimu anaruhusiwa kupanda kutoka TGTS E (748,000/=) kwenda ngazi ya mshahara TGTS F yenye mshahara wa Tsh. 930,000/= kwa mwezi na mwalimu X ambaye amejiendeleza kielimu anabadilishiwa muundo kwa kuondoa jina la Afisa Elimu Msaidizi na kupewa jina la Afisa Elimu daraja la II lakini anazuiliwa kupanda daraja la mshahara, atabaki kwenye msahahara wa TGTS –E (Tsh. 748,000/=) kwa muda wa miaka mingine mitatu zaidi.

Mheshimiwa Spika, kwa vyovyote vile, mpango huu wa Serikali ya CCM ya kuwabana walimu wasinufaike na matunda ya elimu yao hata pale wanapojibana na kujisomesha katika mazingira magumu kwa kutowapandisha madaraja ya mishahara ni udhalimu na unyonyaji dhidi ya walimu, na sumu mbaya itakayoiua elimu ya Tanzania kwa kuwa huwezi kuzungumzia elimu bila kuwagusa walimu.
Mheshimiwa Spika, kabla ya kuandikwa kwa waraka huu kandamizi, utaratibu uliokuwa ukitumika kuwapandisha walimu madaraja ya mishahara ulizingatia zaidi umri wa mwalimu kazini, utendaji wa kazi uliokuwa bora pamoja na kiwango chake cha elimu. Aidha, mwalimu alipojiendeleza kielimu alistahili kupanda cheo kutoka kada moja kuingia kwenye kada nyingine bila kujali ni mwajiriwa wa muda mrefu au ni mwajiriwa wa hivi karibuni.
Mheshimiwa Spika, kutokana na ukandamizaji huo, wapo walimu ambao watastaafu wakiwa bado hawajapata manufaa ya elimu yao waliyojiendelezea na wakati huo huo Bodi ya Mikopo ya wanafunzi wa Elimu ya juu tayari imeshaingiza makato ya 8% kwenye mishahara yao kama marejesho ya mkopo wakati elimu hiyo haina tija kwa walimu kimapato. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inayoongozwa na CHADEMA inaitaka Serikali kuwatendea haki walimu waliojiendeleza kielimu kwa kuwapandisha madaraja ya mishara haraka iwezekanavyo ili kuwapa motisha wa kufanya kazi kwa bidii na pia kuwavutia walimu wengine kujiendeleza kielimu ili kuinua ubora wa elimu hapa nchini.
Mheshimiwa Spika, kabla ya tarehe 1 Disemba 2009, utaratibu uliokuwa unatumika kuwapa walimu miundo na kuwapandisha madaraja haukuwa ukilalamikiwa kama huu ulioletwa na waraka namba C/AC.44/45/01/84 na waraka namba CAC.44/45/O1/A/121. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kufuta mara moja nyaraka zote mbili zilizotajwa hapo juu na kurejea kwenye utaratibu wa kuwapandisha walimu madaraja ya mishahara uliokuwepo kabla kwa kuwa nyaraka za sasa ni kandamizi na zinalenga kuwakatisha walimu tamaa ya kujiendeleza kielimu na hivyo kuwaongezea umasikini na kuendelea kudidimiza elimu ya Tanzania.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa sheria ya Utumishai wa Umma namba 8 ya mwaka 2002 kifungu cha 6(4) kama ilivyorekebishwa na sheria namba 18 ya 2007 na kanuni za utumishi wa Umma za mwaka 2003 kifungu cha 6(h), mwenye mamlaka ya kuwapandisha walimu madaraja ni Tume ya Utumishi wa Walimu (TSD), lakini sasa hivi tangu nyaraka za kuwakandamiza walimu zilipoanza kuandikwa na serikali, Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya, miji na majiji ndiyo wanaowapandisha na kuwashusha walimu madaraja ya mishahara. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kulieleza Bunge hili, ni nani mwenye mamlaka ya kisheria ya kuwapandisha walimu madaraja ya mishahara na ni sheria ipi inatumika kuwapandisha walimu madaraja ya mishahara?
Mheshimiwa Spika, wapo pia walimu wa shule za msingi waliojiendeleza kielimu na wamekuwa wakihamishiwa shule za sekondari, bila kulipwa haki na maslahi yao ya uhamisho kwa madai kuwa idara ya shule za msingi na idara ya shule za sekondari zote ziko chini ya mwajiri mmoja ambaye ni Mkurugenzi wa Halmashauri/Manispaa/Jiji. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kueleza bunge hili; inawezekana vipi shule za msingi na shule za sekondari kuunganishwa pamoja wakati katika Wizara ya Elimu Makao makuu, idara hizi zimetengana na kila moja inajitegemea? Je utunzaji wa kumbukumbu za walimu hawa utakuwaji ikiwa taarifa za walimu wa shule za msingi ziko Idara ya msingi Wizarani wakati walimu wenyewe wamehamishiwa sekondari? Aidha Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka kujua ni kwa nini walimu wa shule za msingi wanapohamishwa kutoka kituo kilichokuwa cha shule ya msingi na kwenda kituo cha shule ya sekondari hawalipiwi fedha za uhamisho?
Mheshimiwa Spika, licha ya Serikali kuwakandamiza walimu wanaojiendeleza kwa kutowapandisha madaraja ya mishahara, bado Serikali hii ya CCM imeendelea kuwabagua walimu kwa kuwalipa mishahara tofauti walimu wenye kiwango kimoja cha Elimu. Kwa mfano; Mwalimu mwenye shahada ya kwanza akiajiriwa kufundisha shule ya Sekondari huitwa Afisa Elimu Daraja la II na huanza na ngazi ya mshahara TGTS – D (sh. 532,000/=) wakati mwalimu mwenye kiwango hichohicho cha elimu akiajiriwa katika chuo cha ualimu huitwa mkufunzi na huanza na mshahara wa TGTS – E (sh. 720,000/=)
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inayoongozwa na CHADEMA inaitaka pia Serikali kulieleza bunge hili kama hii ni haki na inatumia vigezo gani kuwalipa walimu wenye kiwango kimoja cha elimu mishahara tofauti.


7. CHAMA CHA WALIMU NA MANUFAA YAKE KWA WALIMU
Mheshimiwa Spika, madhumuni ya kuanzishwa kwa Chama cha Walimu (CWT) yalikuwa ni kutetea maslahi ya walimu. Hata hivyo kwa siku za karibuni kumekuwa na malumbano ambayo yanapelekea baadhi ya walimu kutaka kujitoa. Walimu lazima wafahamu kuwa umoja ni nguvu na waelewe kuwa hakuna watumishi wengi hapa nchini zaidi yao. CHADEMA inaamini kuwa penye wengi hapakosi matatizo hivyo ni vizuri CWT wakae pamoja na kuangalia matatizo yao ya ndani ili waweze kutatua matatizo lukuki yanayowakabili walimu hapa nchini.


8. VITABU VYA ELIMU NA MCHANGO WAKE KATIKA KUKUZA AU KUPUNGUZA UBORA WA ELIMU
Mheshimiwa Spika, vitabu ni nyenzo muhimu sana katika utoaji wa elimu. Vitabu vya kiada na ziada vinapaswa kuwa na ubora unaokubalika ili elimu itakayopatikana katika vitabu hivyo iweze kuwa bora pia. Kwa mantiki hiyo, vitabu vina nafasi kubwa sana katika kuboresha elimu lakini pia vitabu viliyoandikwa kiholela bila kuzingatia viwango na mitaala husika vina nafasi kubwa pia ya kuporomosha ubora wa elimu.
Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia umuhumu wa vitabu katika kuboresha elimu, Serikali kupitia waraka wake namba 2 wa mwaka 1998, iliunda Kamati ya kuidhinisha vitabu na vifaa vya elimu (EMAC) ili kutoa ithibati baada ya kujiridhisha kuwa machapisho ya vitabu yamekidhi viwango vinavyotakiwa.
Mheshimiwa Spika, mfumo wa kuidhinisha kitabu, unaanza kwa sekretarieti kuwapa watathimini kupitia miswaada ya vitabu inayoletwa na mchapishaji. Kwa bahati mbaya sana wataathimini hawa huwa hawapatikani kwa njia ya ushindani ulio wazi jambo linaloashiria rushwa na ufisadi katika eneo hili.
Mheshimiwa Spika, hali ya kutokuwa na uwazi katika kuwapa watathimini miswada ya vitabu halina afya hata kidogo katika kupata machapisho yenye ubora. Ikumbukwe kuwa mapendekezo ya wataathimini ndiyo huwasilishwa katika kikao cha EMAC kwa ajili ya kupitishwa au kukataliwa.

Mheshimiwa Spika, Upatikanaji wa Mtathimini anayepitia muswada wa kitabu kwa njia isiyo ya ushindani wa wazi inatoa mwanya wa uteuzi wa kirafiki usiozingatia ujuzi wa somo, ambapo hatima yake ni kuwa na vitabu vinavyo danganya wanafunzi. Mfano mzuri ni kitabu cha Uraia darasa la saba kilichochapwa na kampuni ya “Educational Books Publishers” ambacho katika ukurasa wa 145 kinadanganya watoto kuhusu uwepo wa shirika la GATT ambalo limekufa na kuzikwa miaka kumi na nane iliyopita. Aidha kitabu cha “40 Big Lies in Civics for Tanzania schools” kilichoandikwa na mwandishi nguli na mtafiti Huruma K. Joseph kinafafanua kwa kirefu makosa mbalimbali ambayo baadhi yake yamebarikiwa na EMAC.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni inataka kujua ni hatua gani zimechukuliwa kwa uzembe wa unaofanywa na wataathimini wa miswada ya vitabu na ubabaishaji wa wajumbe wa EMAC katika utungaji wa vitabu?.

Mheshimiwa Spika, kumekuwa na malalamiko kutoka kwa baadhi ya wachapishaji kuwa Sekretarieti ya EMAC imekuwa ikiikakalia miswaada ya vitabu “isiyowekewa asali” na kugoma kuiwasilisha katika vikao vya kamati licha ya kukidhi alama zinazotakiwa. Kambi rasmi ya upinzani inaweza kuthibitisha miswada ambayo imekaa kwenye ngazi ya sekretarieti takribani miaka mitatu sasa. Aidha, Kambi rasmi ya upinzani inaweza kuthibitisha pasipo shaka muswada uliyokataliwa (reject) katika ngazi ya sekretarieti ingawa alama zake zilitosha kupata ithibati yenye masharti (conditional approval). Kambi rasmi ya Upinzani inaitaka serikali ichunguze na kuchukua hatua madhubuti kwa Maafisa wanaoendekeza ubinafsi huu.

Mheshimiwa Spika, Kamati hii ambayo inapaswa kukaa vikao vinne kwa mwaka, imekuwa wakati mwingine ikikaa kikao kimoja kwa mwaka. Hii imesababisha kuwepo kwa wachapishaji ambao wanaamua kuingiza vitabu sokoni bila kuwa na ithibati ambavyo baadhi vimekuwa na makosa yanayotisha. Ushahidi juu ya hili ni kitabu cha uraia kidato cha pili kilichotolewa na kampuni ya Nyambari Nyangwine kinachoainisha wenyeviti wa vijiji kuwa eti theluthi yao ni wajumbe katika baraza la madiwani la halmashauri ya wilaya (Civics for secondary schools book 2 p.41), na kile cha historia darasa la sita cha Adamson Educational Publishers kinachoonyesha makao makuu ya Tanzania kwa sasa yapo Nairobi (Historia darasa la 7uk. 84). Uwepo wa vitabu hivi vya kiada visivyo na ithibati ya EMAC ni dhahiri vinamweka katika hali mbaya Mheshimiwa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi kutokana na kauli yake ndani ya Bunge lako tukufu, kuwa vitabu vyote vinavyotumika katika shule za msingi, sekondari na vyuo vya ualimu vinaithibati ya EMAC. Kauli hii ya waziri aliitoa pale alipokuwa akijibu hoja ya Mheshimiwa James Mbatia (MB) juu ya udhaifu katika mfumo wa elimu.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inataka kujua kama huo ndio bado msimamo wa waziri ili Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni iweze kuwasilisha kama ushahidi vitabu vya kiada zaidi ya thelathini (30) vya kampuni ya Adamson Educational Publishers, ambavyo vimekuwa vikitumika mashuleni bila kuwa na ithibati. Moja ya maajabu ya vitabu hivi vya Adamson ni kupotosha historia kwa kumtaja Mohammed Shamnte kuwa ndiye aliyekuwa kiongozi wa ASP na si Seikh Abeid Amani Karume (Historia darasa la 6 uk. 28) na kwamba eti utawala wa kijerumani Tanganyika ulianza wakati wa vita vya majimaji ((Historia darasa la 6 uk. 28). Kambi rasmi inataka kujua kama Mheshimiwa waziri anabariki uozo huu au anatangaza kupiga marufuku matumizi ya vitabu hivi.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inapendekeza kuwa ili kufuta mizaha hii katika elimu mambo yafuatayo yafanyike:
a) Serikali ipanue idadi ya wafanyakazi katika sekretarieti angalau kila somo liwe na mjumbe mmoja katika sekretarieti.

b) Vikao vya EMAC vikae kama inavyotakiwa, yaani mara nne kwa mwaka.
c) Hatua za kinidhamu zichukuliwe kwa wajumbe wa sekretarieti na kamati pale inapoonekana kuna ukiukaji wa maadili au uzembe wa makusudi unaopelekea kuidhinisha vitabu vyenye makosa yasiyovumilika.
d) Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) ambalo hupitia na kuidhinisha miswada unayoondikwa kwa lugha ya kiswahili kabla ya kupelekwa sekretarieti,ishindanishwe na Taasisi zingine za Kiswahilli kama vile Taasisi ya Uchunguzi ya Kiswahili (TUKI), na Baraza la Kiswahili la Zanzibar (BAKIZA). Hii itaisukuma kufanya kazi kwa ufanisi kuliko sasa ambapo hupitisha maneno ya Kiswahili yanayolalamikiwa na wadau.
e) inayowasilishwa kwake. Kambi rasmi ya upinzani inataka ushindani wa wazi katika kuwapata wataathimini wa EMAC.
f) Aidha muda wa kujadili miswada ya vitabu pamoja na mapendekezo ya watathmini ni kidogo sana jambo ambalo linazidi kudhoofisha ubora wa vitabu. Kikao cha EMAC chenye wajumbe kumi na wanne huupitia muswada wenye kurasa hadi 200 kwa dakika zisizozidi kumi. Baada ya kuupitia muswada hujadiliana kwa dakika 10-20

9. MAPENDEKEZO MUHIMU YA KUBORESHA SEKTA YA ELIMU NCHINI

Mheshimiwa Spika, ili kuboresha sekta ya elimu nchini, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapendekeza mambo yafuatayo yafanyike:

i. Serikali ianzishe bodi ya wataalamu wa ualimu (Tanzania Teachers’ Professional Board – TTPB kama zilivyo taaluma nyingine kama uhasibu (NBAA), uhandisi, utabibu n.k. ili bodi hii iwe inaratibu na kupanga vigezo vya mtu kuitwa mwalimu katika ngazi ya ujuzi wake. Bodi hii pia itahusika na kusimamia nidhamu na maadili ya taaluma ya ualimu nchini na pia itahusika na ukaguzi wa shule ili kuona kama walimu wanazingatia mwongozo wa taaluma yao. Chombo hiki kiwe na mamlaka kisheria kuwasajili walimu na kuwapa leseni za kufundisha.

ii. Serikali iongeze kiwango cha ufaulu kwa wanaotaka kujiunga na vyuo vya ualimu baada ya kuhitimu kidato cha nne, kutoka daraja la nne hadi daraja la tatu kwa ngazi ya cheti. Aidha wanaotaka kujiunga na vyuo vya ualimu baada ya kuhitimu kidato cha sita, wawe na ufaulu wa daraja la pili badala ya daraja la tatu kama ilivyo sasa. Hii itasaidia kupata walimu wenye uwezo mkubwa kitaaluma, na hivyo kuinua ubora wa elimu yetu.

iii. Serikali iweke usawa wa mishahara kwa wahitimu wenye viwango sawa vya elimu kwa mfano cheti, stashahada na shahada kati ya walimu na watumishi wa kada nyingine. Hii itasaidia vijana waone ualimu kama fani nyingine
iv. Serikali iweke utaratibu wa kuwapa motisha walimu kwa kuruhusu watato wa walimu wasiozidi watatu kusoma bure katika shule za sekondari na wapewe mikopo bila masharti ya kusomama katika vyuo vya elimu ya juu ikiwa watakuwa wamefaulu na kuwa na sifa ya kujiunga na elimu ya sekondari na vyuo hivyo ili kuwaondolea walimu mizigo mikubwa ya kulipa ada za sekondari na vyuo pamoja na kodi za nyumba kwa kutumia mishahara midogo wanayolipwa.
v. Serikali ianzishe chombo cha udhibiti wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi (Tanzania Education and Training Regulatory Authority - TETRA) kitakachoweka viwango vya ubora wa elimu kwa mujibu wa mitaala iliyopitishwa na Serikali, kudhibiti utungaji, usahihishaji na upangaji wa matokeo ya mitihani, kudhibiti gharama za elimu (ada na michango mingine) baina ya shule na taasisi nyingine za elimu za uma na binafsi ili kuwa na mfumo mmoja wa elimu unaoeleweka kuliko sasa ambapo kuna tofauti kubwa za kimfumo baina ya shule na taasisi za elimu binafsi na zile za umma.

10. Hitimisho
Mheshimiwa Spika,
Hakuna nchi yoyote iliyoendelea hapa duniani bila kuwekeza kwenye elimu. Malaysia inajivunia maendeleo yake kwa kuwa iliwekeza kwa vitendo katika elimu na ndio maana nchi nyingi ikiwemo Tanzania imekwenda kujifunza kwao mambo mbalimbali. Wakati umefika sasa wa serikali ya CCM kuwekeza kimkakati katika elimu na si kwa maneno. Sekta ya elimu iko katika sekta sita za vipaumbele kupitia ‘Big Results Now’, lakini kinachosikitisha sioni bajeti ya mwaka huu ikijibu changamoto za elimu hapa nchini hasa ikizingatiwa kuwa asilimia zaidi ya 50 inakwenda kwenye bodi ya mikopo ya elimu ya juu.

Mheshimiwa Spika, ni vyema serikali ielewe maana ya msemo huu ‘ “if education is expensive, try ignorance” yaani kama elimu ni aghali , jaribu ujinga. Imefika wakati sasa wote kwa pamoja kama taifa tuseme “ELIMU KWANZA” mengine baadaye na hivyo nguvu zetu zote zielekezwe kwenye elimu.

Mheshimiwa Spika,
Ni dhahiri kwamba kuporomoka kwa elimu hapa nchini, pamoja na sababu nyingi zilizotajwa na tume mbalimbali za uchunguzi, kuna tatizo pia la ki-uongozi katika Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi. Ni dhahiri vile vile kwamba hatuwezi kupiga hatua mbele kwa kuendelea na viongozi wale wale ambao matatizo yalitokea mikononi mwao. “Problems can not be solved by the same level of thinking which created them”(Malcom X). Kwa mananeo mengine, Kambi Rasmi ya Upinzani inamtaka Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Mhe. Dkt. Shukuru Kawambwa na naibu wake Mhe. Philipo Mulugo, watumie busara zao na kujipima kama kweli pamoja na majanga makubwa yaliyotokea katika elimu ambayo madhara yake yatadumu kwa vizazi vingi, wanastahili kuendelea kuongoza wizara hivyo.

Mheshimiwa Spika,
Wahenga walisema ada ya mja hunena lakini Mwungwana ni kitendo. Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni bado ina imani kwamba Waziri wa Elimu na Naibu wake wataonyesha uungwana na uzalendo zaidi kwa nchi yetu kama watawajibika kutokana na hitilafu zilizotokea katika sekta ya elimu hapa nchini hata kama makosa na hitilafu hizo hawakuzifanya wao wenyewe moja kwa moja. Lakini kwa ajili ya kuonesha uwajibikaji wa ki-uongozi na kuonesha kwamba wanajali misingi ya utawala bora na pia kulinda heshima yao mbele ya jamii hawana budi kuwajibika kwa dhamana waliyopewa. Kufanya hivyo si fedheha hata kidogo bali ni ushujaa na ukomavu katika uongozi. Rais Mstaafu Alli Hassani Mwinnyi alifanya hivyo alipokuwa Waziri wa Mambo ya Ndani kwa makosa yaliyofanywa na watu wengine lakini aliwajibika na kulinda heshima yake na hatimaye alikuja kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. “Wadau wote wa Elimu wakiwajibika kikamilifu kwa majukumu waliyopewa, kutakuwa na mabadiliko mazuri makubwa sana katika Mfumo wa Elimu yetu”

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema haya kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, na watanzania wote wanaopenda kuona taifa letu likisonga mbele kwa kasi ya kumwondoa adui ujinga na kuona Serikali inaboresha mfumo wa elimu kwa kuwekeza kwa vitendo katika elimu, naomba kuwasilisha.

________________________________
Susan Anselm Jerome Lyimo (Mb)
MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI NA WAZIRI KIVULI WA ELIMU NA MAFUNZO YA UFUNDI
Tarehe 4 Juni, 2013


[1] Tazama Taarifa ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu NBS, September 2012.
 

Attachments

  • Hotuba ya Upinzani,Elimu.pdf
    360.5 KB · Views: 292
  • madai halisi ya walimu.pdf
    116.1 KB · Views: 282
Leo tuko busy na Rasimu ya katiba mpya. Labda kama ungetufanyia favour ya kutuwekea summary (spoon feeding).

Lakini nafikiri ilivyokwenda shule itakuwa Dr. Kitilya Mkumbo ameshiriki kuindaa, but, no disrespect to Suzan Lyimo
 
Du kiwango cha kufeli kimeongezeka kutoka asilimia 10 mpaka 57 that means kiwango cha ufaulu kimeshuka kutoka asilimia 90 mpaka 43 na kinatarajiwa kushuka mpaka 5%,ehee jeikei unaua elimu ndgu fukuza kina mulugo na kawambwa.
 
well said mama hakika hili ndilo hotuba nzuri kuhusu elimu kuwai kusomwa nimependa sana maneno yako ya mwisho kwamba matatizo hayawezi kusuluishwa kwa kutumia fikra zile zilizokuza tatizo na pia hao kawaumbwa na huyo aliyefoji vye WAJIUZULU HARAKA.
 
nikiwa kama mdau wa elimu nampongeza sana msemaji wa kambi rasmi ya upinzani kwani ni nzuri iliyosheni kila aina ya uhalisia japo tumepigwa upofu na rasimu ya katiba ila ukweli unabaki pale pale kuwa kwenye kada hii kuna matatizo mengi sana.Hongara sana Suzan Lymo
 
Kamanda umenena, kama elimu ni ghali tujaribu basi ujinga. Elimu inapaswa kupewa kipaumbele kwa maendeleo ya taifa. Itikadi zikae pembeni tuangalie taifa na nchi yetu kwanza
 
Kamanda umenena, kama elimu ni ghali tujaribu basi ujinga. Elimu inapaswa kupewa kipaumbele kwa maendeleo ya taifa. Itikadi zikae pembeni tuangalie taifa na nchi yetu kwanza
Nyie bavicha mbona mnajitukana hadi mnatukana viongozi wenu,make kuna mambo mnayosema yanawahusu viongozi wenu.
 
Akinajosefu mbowe nao wamo kwenye kufelisha hawa wanafunzi kwa kuharibu matokeo kwa maksudi.
 
Serikali ni noma, inajua kwa sasa watu wako bize na rasimu ya katiba mpya ndo fursa za kupitisha wizara mbovu. Haya bwana.
 
Back
Top Bottom