Hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni Wizara ya Maji na Umwagiliaji kuhusu mapitio ya utekelezaji 2018/19

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Apr 18, 2017
2,797
11,959
HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI WIZARA YA MAJI NA UMWAGILIAJI KUHUSU MAPITIO YA UTEKELEZAJI KWA MWAKA WA FEDHA 2018/2019 NA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA KWA MWAKA WA FEDHA 2019/20
(Yanatolewa chini ya Kanuni za Bunge, Kanuni ya 99(9), toleo la mwaka 2016)

1.0 UTANGULIZI


1. Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, kwa kunijalia afya njema inayoniwezesha kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu kuwasilisha maoni na mapendekezo ya Kambi Rasmi ya Upinzani kwa Wizara hii.

2. Mheshimiwa Spika, kipekee kabisa naomba nichukue fursa hii adhimu kuwapongeza viongozi wakuu wa vyama vya Upinzani kwa mshikamano mkuu wanaouonesha katika kipindi hiki kigumu sana ambacho kufanya siasa nje ya CCM imekuwa ni kosa la jinai. Aidha, ni mshukuru Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani kwa kuendelea kuwa na imani na mimi katika majukumu ya kusimamia Wizara hii muhimu sana kwa maisha ya watanzania.

3. Mheshimiwa Spika, mwisho lakini sio kwa umuhimu mkubwa niwashukuru wanachama wote wa vyama shindani pamoja na wananchi wote kwa kuendelea kutuunga mkono katika mapambano ya kupigania demokrasia ya kweli katika nchi hii hasa uchaguzi ulio huru na haki. Kwani Kambi Rasmi ya Upinzani ina amini kuwa bila haki hakuna demokrasia, pia hakuna amani katika nchi.

2.0 MUUNDO NA MFUMO WA KISEKTA

4. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, inaungana na tamko la kaulimbiu za kitaifa na kimataifa kuhusu umuhimu wa maji. Kaulimbiu hizi ni kwamba; “Maji ni Haki ya Kibinaadamu, Maji ni Uhai, Maji ni Uchumi; Maji ni Msingi wa Amani”.

5. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaamini kwamba pamoja na kwamba maji ni huduma vile vile ni biashara. Ukweli ni kwamba kwa sasa hakuna huduma yoyote ya kijamii inayotolewa bure na Serikali, achilia mbali ukweli kwamba kodi zinazotolewa na wananchi wenyewe ndio zinaitwa fedha za Serikali. Pamoja na kodi bado Bunge limeidhinisha tozo ya shilingi 50 kwa kila lita ya mafuta kwa ajili ya uwekezaji kwenye maji.

6. Mheshimiwa Spika, kwa muktadha wa “huduma ya maji” hakuna eneo lolote katika Tanzania ambalo wanapata maji ya bomba au kutoka katika vyanzo vya maji safi na salama bila ya malipo ya aina yoyote. Hivyo huduma hii ya maji, iwe ni kwa matumizi ya majumbani, matumizi ya mifugo, matumizi ya viwandani au kwa matumizi ya kilimo, hiyo yote ni sehemu ya huduma ya maji ni gharama hivyo watumiaji wa maji hupatiwa kwa malipo ili kuchangia uzalishaji wa maji safi na salama. Lakini kwa kiingereza, tunasema water has an economic value.

7. Mheshimiwa Spika, Hivyo basi, kama ni biashara utolewaji wa huduma hiyo lazima kuwepo na ushindani ili mtumiaji wa huduma hiyo apate huduma iliyo bora zaidi. Kwa muktadha huo, sekta binafsi ni mdau muhimu sana katika utoaji wa huduma hii kwa wananchi.

8. Mheshimiwa Spika, umuhimu wa maji kwa ajili ya uhai wa watu, wanyama, mimea na mazingira kwa ujumla ni jambo lisilopingika. Bila ya maji, viumbe vyote vitapotea, mazingira yatakuwa mfu, na maendeleo ya kiuchumi na ya kijamii yatadumaa.

Kutokana na umuhimu wa maji, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa katika kikao chake cha tarehe 21 Desemba 2016 limeridhia kwa kauli moja miaka kumi ya utekelezaji wa Azimio jipya la Maji kwa Maendeleo Endelevu (Interational Decade (2018-2028) for Action- Water for Sustainable Development).

9. Mheshimiwa Spika, Dira ya Maendeleo ya Taifa (Tanzania Development Vision 2025) Pia Mpango wa pili wa Maendeleo wamiaka mitano 2016-2021 wa Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa viwanda ifikapo 2015, azma hii haiwezi kufikiwa iwapo changamoto za upatikanaji wa maji kwa matumizi ya nyumbani,kilimo na kwa ajili ya viwandani hazitajipiwa kikamilifu. Japokuwa dira imeweka malengo ya maendeleo ya kiuchumi, kisiasa na ustawi jamii ikiwa ni pamoja na malengo yanayogusa moja kwa moja Wizara na Sekta ya Maji na Umwagiliaji.

Baadhi ya malengo muhimu katika muktadha huu ni kama ifuatavyo:
i. Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati, ambapo wananchi wake wanafurahia amani na umoja wa kitaifa

ii. Upatikanaji wa maji safi na salama kwa wakazi wote. Ambapo kwa wakazi wa mijini watapata maji kwa asilimia 100 na kwa wakazi wa vijijini watapata maji safi na salama kwa agalau asilimia 90 ifikapo 2025.

iii. Kuhakikisha kwamba raslimali za maji ni endelevu ili kukidhi mahitaji ya kiuchumi na kijamii.

3.0 HALI YA MAJI KWA NCHI YETU

10. Mheshimiwa Spika, pamoja na upatikanaji na usambazaji wa maji safi na salama vijijini na mijini, bado Tanzania inakabiliwa na changamoto nyingi za usimamizi na uendelezaji wa rasilimali za maji. Tofauti na nchi nyingi majirani, nchi ya Tanzania imejaaliwa kuwa na rasilimali za kutosha za maji safi – mito, maziwa, maji ya kwenye miamba, na ardhioevu – za kutosheleza mahitaji yake yote ya sasa ya maji.

11. Mheshimiwa Spika, Takwimu za kitaifa za rasilimali za maji zilizopo zinaonesha kuwa kiasi cha maji kwa sasa kwa kila mtanzania ni wastani wa mita za ujazo 1,952 kwa mwaka. Pamoja na takwimu hizi ikumbukwe kuwa idadi ya watu imeongezeka kwa kasi katika miaka 25 iliyopita, vile vile matumizi ya maji sio tu yameongezeka bali yamebadilika kwa kiasi kikubwa kufuatia kuongezeka kwa shughuli za kiuchumi,kukua kwa miji,mabadiliko ya mfumo wa kilimo,biashara na viwanda. AMBAPO kilimo kinachukua wastani wa asilimia 89 ya rasilimali za maji,matumizi ya majumbani na ya taasisi ni asilimia 10 na viwandani ni asilimia 1 . Endapo hatua madhubuti za utunzaji wa vyanzo vya maji hazitachukuliwa mapema, kiasi hicho kinatarajiwa kupungua hadi kufikia mita za ujazo 883 mwaka 2035. Kiwango cha chini cha mahitaji ya maji kwa kila mtu kwa mwaka kinachokubalika kimataifa ni mita za ujazo 1,700

12. Mheshimiwa Spika, ni dhahiri hapa kama hatutachukua hatua stahiki si muda mrefu Tanzania inaweza kuwa kwenye tatizo kubwa la maji ambapo ukosefu wa maji linakuwa janga kubwa na hivyo kupelekea rasilimali hiyo kuwekewa utaratibu wa jinsi gani ya kugawanywa kwa kila familia, mifugo na kwa matumizi ya viwandani kama ilivyowahi kuwa kwa nishati ya umeme.

13. Mheshimiwa Spika, Mkakati wa Tanzania wa Kusaidia Rasilimali za Maji wa Mwaka 2006 unatambua umuhimu wa kipekee wa maji katika utendaji kazi wa sekta muhimu za kiuchumi na ustawi wa Watanzania. Mkakati huu unabainisha athari za uwekezaji duni katika: (a) usambazaji wa maji na huduma za usafi kama hitaji la msingi kwa maisha zalishi (b) uendelezaji wa kilimo cha umwagiliaji na uzalishaji wa umeme wa maji kwa ajili ya kuhakikisha upatikanaji wa chakula na nishati ya kutosha.

14. Mheshimiwa Spika, Mkakati huu unabainisha namna utendaji kazi wa sekta kuu za uchumi (nishati, kilimo, viwanda, mifugo, uchimbaji madini, utalii, na uvuvi) zinavyoathirika kutokana na ukame, mafuriko, na usimamizi duni wa rasilimali za maji. Pia, unasisitizia haja ya kufanya juhudi za haraka za kupanua uwekezaji katika uendelezaji na usimamizi wa rasilimali za maji, udhibiti mzuri wa rasilimali za maji, na ulinzi na uhifadhi wa vyanzo muhimu vya maji – mito, maziwa, maji ya kwenye miamba, na ardhioevu.

15. Mheshimiwa Spika, hivyo basi, ushahidi huo ni ukweli kabisa kuwa Maendeleo ya kijamii na kiuchumi yana uhusiano wa moja kwa moja katika upatikanaji wa rasilimali ya maji na utunzaji wa mazingira. Maji ni rasilimali inayomalizika kama haikutunzwa ili kuwa endelevu, hivyo maendeleo ya kilimo, mifugo, viwanda vyote vinatagemea upatikanaji wa uhakika wa rasilimali ya maji.
16. Mheshimiwa Spika,ni ukweli pia kuwa mahitaji ya matumizi ya maji yanazidi kuongezeka, japokuwa upatikanaji wa maji unazidi kupungua na mahitaji ya maji yanazidi kuongezeka kutokana na ukweli kuwa idadi ya watu inazidi kuongezeka, kutokuwa na mifumo mizuri ya kuhifadhi maji ya mvua (Inadequate rain-water storage), mabadiliko ya tabianchi pamoja na shughuli za kiuchumi ambazo hazizingatii utunzaji wa mazingira ambayo ndicho chanzo kikuu cha maji mengi ya mito yetu. Hivyo ni lazima kuwa na mkakati madhubuti wa kuhakikisha maji yaliyopo yanatumiwa kwa uagalifu na uendelevu.

17. Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na tatizo la maji ni lazima kuifanya rasilimali hii kutumika kwa uangalifu na kwa uendelevu baina ya makundi yote ya kijamii, Kambi Rasmi ya Upinzani inashauri kuwa; ni lazima mahitaji kwa kila kundi katika mfumo mzima wa uzalishaji(kilimo,mifugo,viwandani na majumbani) lijulikane mahitaji yake (water demand) kwa siku ni lita ngapi, hapo ndipo tunapoweza kupanga mgawanyo wa uendelevu; lazima kuwa na mipango ya muda mfupi,kati na muda mrefu ya kuvuna maji na matumizi yake.

4.0 UHIFADHI WA VYANZO VYA MAJI

18. Mheshimiwa Spika, Usimamizi wa vyanzo vya maji nchini unafuata taratibu za mipango shirikishi ya usimamizi wa rasilimali za maji kwenye Bodi za Maji za mabonde tisa yaliyopo nchini, ambapo saba katika hayo yanahusisha maji shirikishi kati ya nchi yetu na nchi jirani.
19. Mheshimiwa Spika, Changamoto kubwa iliyopo kwenye usimamizi wa rasilimali za maji ni kupungua na kuharibika kwa vyanzo vya maji kutokana na shughuli za kibinadamu, suala la uchafuzi wa vyanzo vya maji.Taarifa za uchafuzi kuanzia mwaka 2014(Joint water Sector Review)na tafiti nyingine za kitaalamkama zile za chuo kikuu cha Kilimo cha Sokoine na nyinginezo zinaonesha athari za uchafuzi mkubwa na hapa tunatoa baadhi ya maeneo yaliyoathirika kwa kiwango kikubwa. Katika maeneo ya vyanzo vya maji na katika misitu ya hifadhi ya maji (catchments forests and wetlands). Aidha, kupungua huko kunatokana na mabadiliko ya tabiananchi na hivyo kumeathiri shughuli za kijamii na kiuchumi na na kusababisha migogoro kwenye vyanzo vya maji. Hifadhi hizi zinawezesha upatikanaji wa maji juu na chini ya ardhi.

20. Mheshimiwa Spika, kwa muktadha wa mabonde tisa ya maji, Kambi Rasmi ya Upinzani inaona ni lazima na muhimu kuhifadhi vyanzo vya maji kwa mabonde hayo bila kusahau umuhimu wa kipekee wa uhifadhi wa vyanzo vya bonde la Rufiji ambalo chanzo chake ni mabonde ya Kilombero na Ruaha.

21. Mheshimiwa Spika, Ikumbukwe hapa kwamba, Mto Rufiji hupata maji yake mengi kutoka mito miwili mikuu—Kilombero na Ruaha Mkuu—na hasa Mto Kilombero, ambao huchangia theluthi mbili ya maji ya Mto Rufiji kabla hayajafika Stiegler’s Gorge. Hivyo ustawi wa Mto Rufiji unategemea ustawi wa Mto Rufiji; ambao nao pia unategemea (kwa asilimia 60) ustawi wa Mto Kilombero; hususan Bonde la Mto Kilombero.

22. Mheshimiwa Spika, Ni dhahiri, kwamba uwezekano wa Watanzania kupata umeme wa maji wa bei nafuu kutoka Stiegler’s Gorge, ni ndoto inayokaribia kuwa ya kweli endapo Serikali itashindwa kuchukua hatua za makusudi za kuhifadhi (conservation measures) Bonde la Mto Kilombero, kwani ustawi wa bonde hilo hivi sasa unasambaratishwa na shughuli za kibinadamu.
23. Mheshimiwa Spika, Wataalamu wanakubaliana kwamba, uharibifu wa mazingira ukiongeza na tatizo la sasa linaloikumba dunia nzima—mabadiliko ya tabianchi (climate change), vinaashiria kuwa muda si mrefu Bonde la Kilombero linaweza kupoteza sifa yake ya kuwa bonde adhimu la maji baridi ambalo ni kubwa kuliko yote duniani, lililokuwa linajaa maji misimu yote.

24. Mheshimiwa Spika, kitu pekee ambacho wataalamu hao wanatofautiana, ni muda uliobakia kabla Bonde hilo halijasambaratika kabisa. Ni muhimu Mheshimiwa Waziri aliambie Bunge kuhusu hali halisi ya Bwawa la Ngapemba lililopo katika Kata ya Utengule na lile la Kibasila ambayo ni makubwa na yamekuwepo kwa miaka mingi likiwa ni chanzo kikuu cha shughuli za kiuchumi kwa wanavijiji wanaozunguka Bonde la Kilombero. Bwawa hilo Ngapemba lililokuwa na ukubwa wa eka za mraba 1,000 na lililokuwa na hekaheka nyingi za uvuvi, sasa limenyauka na kusinyaa na kubakia eka chache sana za mraba.,

25. Mheshimiwa Spika, Utafiti uliofanywa na JET kuhusu hali ya mito kati ya Kihansi na Ifakara, unaonyesha kati ya mito 29 iliyokuwepo, sasa imebaki mito mitano tu, huku mito tisa ikiwa na maji yaliyotuama. Miongoni mwa mito hiyo mitano ambayo inatiririsha maji, ni Luipa, Mpanga na Mnyera ndio bado ina maji ya kutosha mwaka mzima.

Kwa hiyo, hali ya mito katika Bonde la Kilombero ni mbaya, na chanzo kikubwa cha hali hiyo ni uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya Tabianchi.

26. Mheshimiwa Spika, kwa muktadha huo ni kwa vipi uzalishaji wa umeme wa maji kwa mradi wa Stiegler’s Gorge utakuwa endelevu?

5.0 UHABA WA MAJI NA UCHAFUZI WA VYANZO VYA MAJI

27. Mheshimiwa Spika, uhaba wa maji katika maeneo mengi ya miji na miji midogo ni mkubwa sana ila kutokana na kutokuwepo kwa taarifa za uhakika tunashindwa kuweka takwimu za uhaba kwa kila eneo hadharani ili Serikali iweze kuzifanyia kazi. Lakini kwa taarifa za Uhakika tulizozikusanya na kuzithibitisha kutoka kwa Madiwani, Wenyeviti wa Serikali za Mitaa, na viongozi wa Chadema kwenye kata zote sita(6) na Mitaa 45 iliyopo Jimbo la Kibamba imebainika kwamba;

28. Mheshimiwa Spika, Mradi wa Usambazaji wa Maji unaofanywa na JAIL IRRIGATION haujakamilika mpaka leo mbali na naibu waziri kueleza ulikamilika 2016. Maeneo ya Kwa Mwakatundu, Kwa Nyembele, Kwafungo na Kwa Mndeme katika barabara ya Makabe na kwa Mangara barabara ya Mpiji MAGOE bomba kubwa la Inchi 10 halijaunganishwa mpaka hii leo.

29. Mheshimiwa Spika, hakuna Ujenzi wa TENKI ulioanza wala unaoendelea katika eneo la MSAKUZI (Kwa Paulo)kata ya MBEZI na MARAMBA MAWILI (Maarufu kama Manzese) kata ya MSIGANI na mbaya zaidi wananchi waliopaswa kuachia ardhi kwaajili ya Ujenzi huo wa Matenki hawajalipwa fidia hadi leo japokuwa maeneo yao yalifanyiwa uthamini Februari 2018. Baadhi ya Wananchi waliounganishiwa huduma ya Maji miezi 3 iliyopita katika mitaa ya LUIS, MSAKUZI KUSINI kata ya Mbezi mpaka leo hawajapata MAJI.

30. Mheshimiwa Spika, kuna maeneo yasiyo na maji kabisa katika kata zote sita (6) za jimbo la kibamba. MBEZI katika Mitaa 8 ya kata ya Mbezi, Mitaa ya Mpiji Magoe, Msumi, Makabe na Msakuzi hakuna kabisa Mtandao wa Maji wananchi hununua maji kati ya 18,000 hadi 20,000 kwa lita 1000. Katika mtaa wa Luis eneo la Upendo, Furaha, kwa Mkome na Maeneo ya Uzunguni hakuna kabisa Miundombinu.

31. Mheshimiwa Spika, kata GOBA-Katika mitaa 8 iliyopo kata hiyo, mtaa wa Muungano, Tegeta A, Matosa na Kibururu hakuna kabisa maji ya bomba. Mtaaa wa Kunguru 45% wanapata maji lakini maeneo ya Kitongwa, Kontena B na Kwa Ndambi kisiwani hakuna maji kwasababu presha ya maji ni ndogo sana na haiwezekani kuunganishiwa wateja wapya.Mtaa wa Kulangwa ambao unategemea maji kutoka Kisauke maji hutoaka mara 1 hadi 2 ndani ya mwezi mmoja na maeneo ya Jipe moyo, Mtambani, Mwishehe na Kimambo hakuna mtandao kabisa.

32. Mheshimiwa Spika, kata ya KWEMBE Katika mitaa 10 iliyopo kata ya Kwembe, Mitaa ya Kisopwa, Mpakani na Kingazi A hakuna mabomba kabisa. Mitaa ya Njeteni, Mloganzila maji hupatikana maeneo machache yasiyofika robo ya eneo la mtaa na maeneo maji yanatoka hutoka mara chache. Mtaa wa Msakuzi Miundombinu ni michache na haijawahi kutoa maji kabisa.

33. Mheshimiwa Spika, kata ya MSIGANI Katika Mitaa 5 iliyopo katika kata hiyo; Mtaa wa Msingwa, Maramba Mawili hakuna kabisa Mtandao wa Maji na Kwa Yusufu hakuna MAJI KABISA lakini mabomba yamesambazwa Mnarani na Mchungwani wakati Njeteni, Kwamakofia na Mbezi Hill hakuna hata miundombinu kabisa. Mtaa Temboni Kanisa la Udongo hakuna maji.

34. Mheshimiwa Spika, kata ya KIBAMBA-Katika Mitaa 5 ya kata hiyo; maeneo ya Magengeni - uwanjani, uwanjan kwenda shule ya msingi, mbuyuni kwenda malonga na msakati hayana Maji wala mtandao.

35. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inamtaka Mheshimiwa Waziri kulieleza Bunge ni lini wananchi hao ambao wanaishi kandokando ya Bomba kuu linalosambaza maji kutoka Ruvu kwenda maeneo mengine ya jiji lini watapatiwa maji ya uhakika?

36. Mheshimiwa Spika, kwa ushahidi wa uhakika uliotolewa na taasisi ya shahidi wa maji kuhusu uchafuzi wa maji kwenye mto Ngerengere ambao una mwaga maji yake kwenye mto Ruvu, ambao ni chanzo kikuu cha maji yanayotumiwa na wakati wa Mkoa wa Dar es salaam na hivyo kuhatarisha maisha ya maelfu ya wakazi wa jiji la Dar es salaam, Kibaha na Bagamoyo.

37. Mheshimiwa Spika, mto Ngerengere unapokea maji maji taka kutoka kwenye ukanda wa viwanda wa Morogoro pamoja na mfumo mzima wa maji taka ya mji wa morogoro (Morogoro Industrial complex and Morogoro Urban water supply and sewerage Authority-Moruwasa).

38. Mheshimiwa Spika, maji taka yanayoingia kwenye mto huo kutoka kwenye viwanda vya ngua na viwanda vya ngozi hayafai kabisa kutumika kwa matumizi ya nyumbani na kwa matumizi ya kilimo kutokana na kuwa na viwango vya juu vya kemikali hatarishi kwa viumbe hai.

39. Mheshimiwa Spika, kutokana na kutokuwa na chanzo mbadala cha maji kwa wakazi zaidi ya 5000 waishio kwenye maeneo ya Kipera, Kingolwira, Bomba la Zambia na Sanga Sanga wanalazimika kutumia maji ya mto huo kwa matumizi ya nyumbani na mashambani hivyo hivyo bila kutiwa dawa. Jambo hilo lina hatarisha usalama wa afya zao. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali itoe kauli kuhusiana na uchafuzi huo wa chanzo kikuu cha maji kwa mamilioni ya wakazi wa Dar Es Salaam sambamba na wale wajamii tajwa hapo juu.

6.0 MIRADI YA MAJI YA KIDUNDA,KIMBIJI

40. Mheshimiwa Spika, ukiangalia Randama ya Wizara inaonesha kuwa mradi wa Ujenzi wa Bwawa la Kidunda ili ukamilike unahitaji kiasi cha dola za Kimarekani milioni 215,. Kwa mwaka 2018/19 mradi wa Bwawa la Kidunda uliidhinishiwa jumla ya shilingi bilioni 3 lakini haikutoka hata shilingi na mwaka 2019/20 zimeombwa tena shilingi bilioni 3, na kwa mradi wa Mpera na Kimbiji mwaka 2018/19 ziliidhinishwa shilingi 14,109,999,000.00 lakini hazikutoka hata shilingi, mwaka 2019/20 zimeombwa tena shilingi bilioni 3. Kambi Rasmi ya Upinzani inasema, Serikali haina uhakika na nini hasa inataka kifanyike katika huo Mradi wa Mpera na Kimbiji kwani tofauti ya maombi ya Mwaka jana na mwaka huu ni kubwa sana pia kwa kuangalia hali halisi ya thamani ya shilingi kwa dola ya Kimarekani. Hii inapelekea kushindwa kufanya tathmini ya thamani ya fedha iliyotumika na kazi iliyofanyika.

41. Mheshimiwa Spika, kama ambavyo tumetangulia kusema, kuwa hakuna huduma ya bure na hivyo ukiangalia mwongozo wa biashara kwa mradi huo ni dhahiri inajulikana wanufaikaji ni wangapi na kwa muda gani uwekezaji huo utakuwa umerejesha fedha hizo. Kwa mantiki hiyo basi kushindwa kumalizia mradi huo ambao kwa sasa umeishachukua takriban miaka zaidi ya minane (8) na wakati huo huo thamani ya shilingi yetu dhidi ya dolla inazidi kuporomoka.

42. Mheshimiwa Spika, mtazamo huo wa Serikali maana yake ni kwamba miradi mingi ya huduma za jamii hazitakuja kukamilika kwa miaka ya karibuni hadi watu wenye muono wa kibiashara watakapo kuwa kwenye madaraka.

43. Mheshimiwa Spika, ukiangalia taarifa ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2017/19 (randama) uk. Wa 44 hadi uk. Wa 49 kuna miradi ya maji inayofanyiwa usanifu na mingine inayoendelea au mingine iliyokamilika (Mradi wa Same -wanga-Korogwe,Maji mkoa wa Kigoma, mradi wa maji wa Ntomoko, Maradi wa Chiwambo, mradi wa Ukarabati na ujenzi wa Mabwawa, Mradi wa Maji wa Lukululu n.k) lakini mingi haifanyi kazi na imetumia fedha nyingi na mingine inailazimu Wizara itoe maelekezo kuwa miradi mingine isitekelezwe na Halmashauri kutokana na sababu zao na hivyo mamlaka za maji za mikoa zihusishwe katika utekelezaji wake. Lakini hoja ya msingi ni je ikishatekelezwa ni mamlaka ipi itakuwa inaiendesha miradi hiyo? Hapa ndipo kutupia mpira kunapoanzia, kwani waendeshaji watasema haikujengwa kwa kiwango kinachohitaji na visingizo vingine kama hivyo.

44. Mheshimiwa Spika, tatizo sio uwezo mdogo wa Halmashauri,tatizo linaanzia Serikali Kuu ambao ndio waratibu, wasimamizi na walipaji. Hapa lipo tatizo la msingi la kutokuwa na vipaumbele vinavyogusa maja kwa moja maisha ya watanzania na maeneo yenye mchango mkubwa na wa haraka kwa maendeleo ya Taifa kwa ujumla. Wimbo wa Serikali inayodhamiria kujenga uchumi wa Viwanda utaendelea kuimbwa bila mafanikio ikiwa mwelekeo huu hautabadilika na kuwekeza kwenye miradi yenye kuchochea maendeleo halisi ya uchumi wetu kama kwenye maji.

45. Mheshimiwa Spika, tumesema maji ni uhai, ni umeme, ni kilimo cha uhakika,ni chakula ni mifugo, ni usafi na mazingira yetu. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaka kufahamu hivi mradi kama wa Kidunda wenye thamani ya dola za kimarekani milioni 215 unalinganishwa na nini hasa? Hivyo ilikuwa sahihi kuwekeza katika ununuzi wa Ndege za ATCL zaidi ya mara mbili ya fedha zilizotakiwa kukamilisha Bwawa la Kidunda litakalo toa ajira zaidi ya ATCL, kwani litatoa maji kwa ajili ya umwagiliaji, hususan kilimo cha miwa, viwandani,litainua uvuvi, litavutia watalii n.k Kwa muktadha huo Kambi Rasmi inahitaji maelezo ya Serikali kwanini hadi sasa mradi huo haupatiwi fedha ili ukamilike.

46. Mheshimiwa Spika, katika ujenzi wa miradi mikubwa Serikali inaweza kuingia katika ubia na Sekta binafsi na miradi kutekelezwa kwa utaratibu wa Kujenga mradi na kuuendesha na baadae kuurudisha Serikali (Build Operate and Transfer-BOT). Utaratibu huu kwa mazingira yetu ambayo Serikali imeshindwa kupata mikopo ya masharti nafuu-(concessional/soft loans) ndio utaratibu utakaokuwa suluhisho katika miradi ya maendeleo. Na katika hili mjenzi wa mradi kwa njia ya ubia naye ndiye atakuwa muendeshaji hadi fedha zao zilizowekwa kwa mujibu wa mkataba zitakaporudi na faida ndipo mradi utaendeshwa na mbia mwenza Serikali au wakala wake

47. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani kwa hili inasisitiza mikataba kuwa wazi na yenye tija baina ya wabia watakao husika katika utekelezaji na usimamizi wa miradi hiyo.

7.0 UZALISHAJI NA MAHITAJI YA MAJI MIJINI (Upatikanaji wa maji mijini)

48. Mheshimiwa Spika,hotuba ya mheshimiwa Waziri, aliyoitoa hapa Bungeni mwezi Mei, 2018 uk 8 aya ya 16 imetoa takwimu ya kukamilika kwa baadhi ya miradi ya maji kwa kipindi cha mwezi Machi 2017 hadi Machi 2018, ikionesha ongezeko la maji dhidi ya mahitaji kwa maeneo ya mijini. Hivyo imetulazimu kuchambua takwimu hizo kama ifuatavyo ili kuonesha hali halisi ya upatikaji wa maji kwa maeneo ya mijini kulingana na takwimu zilizotolewa na Waziri





Uzalishaji-(lita kwa milioni kwa siku)

Mahitaji-(lita kwa milioni kwa siku)

% ya Upungufu

Miji mkuu ya mikoa

404

646

37.4

Miji mikuu ya wilaya na miji midogo

100.6

277.8

63.7

Miradi ya maji ya kitaifa

67.2

125.6

46.5

Dar, na miji ya kibaha na Bagamoyo

504

544

7.35

Wastani wa upungufu wa uzalishaji kwa siku kwa mijini

38.74




Upatikanaji wa maji mijini

61.3

49. Mheshimiwa Spika, kutokana na takwimu hizo ni kuwa upatikanaji huo ni pale miradi inapokuwa imekabidhiwa kwa kuanza kutumika, lakini kutokana na mambo mbalimbali yaliyo ndani na nje ya uwezo wetu miradi hiyo inalazimika kufanyakazi chini ya kiwango au kusimamisha kabisa kufanya kazi. Hivyo tatizo la Upatikanaji wa maji kuzidi kuwa kubwa zaidi na takwimu ya 61.7% kushuka chini sana kutokana na ukweli kwamba ongezeko la watu kwa mwaka (Population growth rate), kwa makadirio ya mwaka 2017 ilikuwa ni asilimia 2.75.

Changamoto ya ubora wa maji (water quality); Usafi na uhakika wa upatikanaji wa maji. Aidha, upotevu wa maji kutokana na uharibifu wa miundombinu na uchakavu wa mabomba ni moja ya sababu dhahiri za kutilia shaka takwimu zinazoelezwa. Mfano DSM inaelezwa kuwa zaidi ya 49% ya maji hupotea njia, lakini kinachohesabiwa ni maji yanayotoka kwenye chanzo kuingia kwenye mitambo ya bomba.

8.0 UPOTEVU WA MAJI

50. Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa hotuba ya Mheshimiwa Waziri aliyoitoa hapa Bungeni mwezi Mei, 2018 uk wa 19 aya ya 19 changamoto kwa mamlaka zinazotoa hudma za maji ni upotevu wa maji. Takwimu zinaonesha kuwa upotevu wa maji kwa Jiji la Dar, Kibaha na Bagamoyo ni asilimia 49, Miji Mikuu ya Wilaya na Miji Midogo ni asilimia 39, Miji Mikuu ya mikoa ni asilimia 32. Sababu zilizotolewa kuhusiana na upotevu wa maji Rejea Randama ya Mpango wa Bajeti ya Wizara ya Maji kwa mwaka 2019/20- Uk. 47 na 48 kubwa ni uchakavu wa miundombinu ya mifumo ya usambazaji wa maji

51. Mheshimiwa Spika, kwa mahesabu hayo ni kwamba upatikanaji wa maji halisi kwa Jiji la Dar pamoja na Kibaha na Bagamoyo ni sawa na asilimia uzalishaji ukitoa asilimia ya upotevu. Hivyo kwa Jiji la Dar-es-Salaam sawa na upatikanaji wa maji halisi ni kwa asilimia 51 hapa ni kwa wale tu ambao tayari wako kwenye mtandao wa mabomba ya maji. Vivyo hivyo kwa miji mikuu ya mikoa, wilaya na miji midogo hali ni mbaya zaidi. Kwani ukichukulia asilimia ya upungufu kulingana na mahitaji halisi ya maji ambayo imeoneshwa kwenye jedwali hapo juu na utoe pia asilimia ya upotevu hali inazidi kuwa mbaya zaidi.

52. Mheshimiwa Spika, kwa hesabu za kawaida ni kuwa kwa wilaya na miji midogo asilimia ya upungufu kulingana na mahitaji halisi ni 63.7% na upatikanaji ni 36.3% wakati Hotuba ya Waziri kwa mwaka 2018/19 inasema upotevu ni 39%. Hii maana yake ni kuwa wilaya na miji midogo mingi, haina kabisa uhakika wa upatikanji wa maji.

53. Mheshimiwa Spika, lengo lililowekwa na ilani ya CCM iliyoiingiza madarakani Serikali ya awamu ya tano ya Rais Magufuli ni kuwa hadi 2020 Dar iwe na upatikanaji wa maji kwa asilimia 95 na miji mingine iwe ni asilimia 90. Kambi Rasmi ya Upinzani inauliza, Je kwa mwendo huu wa hali halisi ya maji tutafikia malengo?

9.0 MFUKO WA MAJI

54. Mheshimiwa Spika, mfuko wa maji unachangiwa kwa makato ya watumiaji wa bidhaa ya mafuta ya petrol kwa shilingi 50 kwa kila lita moja ili kuwa endelevu. Taarifa ya utekelezaji ya mwaka 2018/19 inaonesha kuwa mfuko umepata jumla ya shilingi bilioni 93.661 sawa na asilimia 59 ya makadirio ya mapato ya mwaka wa fedha 2018/19.

55. Mheshimiwa Spika, lengo lilikuwa ni kumtua mama ndoo ya maji lakini kwa makusanyo hayo maana yake kuna tatizo sehemu fulani kwa nini mapato hayakukamilika angalau kwa asilimia 90? lakini makato hayo hayawezi kuwa ya milele bila kuwepo kwa ukomo kuwa mfuko unaweza kujiendesha wenyewe, kama ni hivyo huo sio mfuko bali ni kitu kingine. Kwa dhana ya uendelevu ni lazima upatikanaji wa fedha zinazokuwa zimepangwa zifikie angalau asilimia 75 na kufikia asilimia 100, sasa makusanyo ya asilimia 59 na chini yake maana yake makato yataendelea kwa miongo kadhaa ijayo na watumiaji wa mafuta wataendelea kupata shida.

56. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inasema kuwa kutokukamilika kwa lengo angalau kwa asilimia 90 ni kutokana na msinyao wa uchumi unaoendelea kuikumba nchi yetu, jambo linalopelekea matumizi ya mafuta hasa petrol na dezeli kushuka

57. Mheshimiwa Spika, kwa dhana hiyo ya mfuko, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kupitia mfuko huo kuingia katika ubia na Sekta binafsi kuendesha miradi mikubwa ya maji kama vile miradi ya umwagiliaji, miradi ya marambo kwa ajili ya ufugaji na miradi ya maji kwa ajili ya matumizi ya majumbani. Kwa njia hii ni dhahiri mfuko utazidi kuwa endelevu na hivyo kupunguza kilio cha kila siku kuwa Serikali haina fedha. Ni ukweli kuwa maji ni huduma lakini vile vile ni biashara pia tena kubwa; suala hapa ni Serikali kuacha undumila kuwili na kufanyia kazi sera ya PPP kwa vitendo kwa maeneo yenye uhitaji mkubwa wa maji ya shughuli za kibiashara kama kilimo cha umwagiliaji na mifugo.

58. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inasisitiza uhusishwaji wa Sekta binafsi katika hatua zote za utoaji wa huduma za msingi hasa miradi ya maji, kwa kutokana na historia ya matumizi ya Serikali inaonesha kuwa sekta ya maji imetumia fedha nyingi sana lakini upatikanaji wa maji hauakisi thamani halisi ya fedha zilizowekezwa.

59. Mheshimiwa Spika, ukiangalia Randama uk. Wa 50 Serikali kwa kushauriwa na shirikia la Maendeleo la kimataifa la Uingereza (DFID) wamebuni mpango wa kuimarisha uendelevu wa Huduma ya maji vijiji-mfumo wa malipo kwa matokeo. Hii ni kutokana na miradi mingi kutokuwa endelevu na hivyo kuwa changamoto kubwa sana kwa Serikali.

60. Mheshimiwa Spika, jambo hili kwa kiasi kikubwa ni kutohusisha sekta binafsi na hivyo kukosekana kwa dhana nzima ya umiliki wa miradi hiyo, fedha za mikopo au ufadhili zinaonekana kutokuwa na mwenyewe (Kasumba ya Mali ya umma haina mwenyewe) kwa kuanzia na hatua za mwanzo kabisa za usanifu na utekelezaji wa miradi na inapofikia hatua ya uendeshaji ndipo balaa la ufujaji wa fedha linapogundulika. Tunatakiwa kuondoa kwanza kasumba hiyo kwa watendaji kwa kupitia umiliki na uendeshaji wa Sekta binafsi kwa miradi ya maji.

61. Mheshimiwa Spika, kuundwa kwa vyombo vya watumiaji maji (COWSOs) kuhusu uendeshaji na matengenezo ya miradi ya maji vijijini, Kambi Rasmi ya Upinzani inaona kuwa suala hili halitoweza kutoa suluhisho la tatizo lililopo katika miradi hiyo, kwani watumiaji hawana umiliki wowote kwa maana ya uchangiaji wakati mradi unaanza na kutekelezwa.

62. Mheshimiwa Spika, kuondokana na tatizo hili ni vema watumiaji wa maji wakashirikishwa toka mwanzo, mawazo na matamanio yao yakazingatiwa ili kuleta dhana ya ushirikishwaji kamili sio hila ya kubambikiwa miradi yenye matatizo toka siku ya kwanza ya kukabidhiwa.

10.0 UTAFUTAJI WA FEDHA ZA MIRADI YA MAJI

63. Mheshimiwa Spika, ukurasa wa 53 wa Randama ya mwaka 2018/19 ulionesha kuwa mbali na kupatikana na ahadi za dola za Kimarekani bilioni 1.93 kwa ajili ya utekelezaji wa Programu ya Pili ya maendeleo ya Sekta ya Maji, pia Serikali ilikamilisha majadiliano kwa ajili ya mikopo ya masharti nafuu yenye jumla ya dola za Kimarekani milioni 829.7.

64. Mheshimiwa Spika, Randama ya wizara fungu 49 kwa mwaka wa fedha 2019/20 uk.40 na 41 inaonesha kuwa fedha ambazo zimeishatafutwa kwa ajili ya miradi maji katika miji mbalimbali ni Euro milioni 313 kwa exchange rate ya Euro 1 shilingi 2,605.09 kama ilivyotolewa na BOT 15 April 2019 ni sawa na shilingi bilioni 815.4 au (815,393,170,000.00) hizo kutoka Benki ya KFW ya Ujerumani pamoja na Green Climate Fund. Kiasi cha Euro milioni 70 sawa na shilingi bilioni 182.4 au(182,356,300,000.00) Aidha, USD milioni 500 kutoka Serikali ya India, ambazo ni sawa na shilingi trilioni 1.12 au (1,115,050,000,000.00)

65. Mheshimiwa Spika, jumla ya fedha hizi kwa mahesabu yetu ni shilingi trilioni 2.12 au (2,117,024,970,000.00); Hizi ni fedha nyingi sana zinahitaji uangalizi wa karibu kwa kushirikisha wadau wakubwa katika miradi hiyo ambayo ni wananchi katika mchakato mzima wa kufuatilia na kuona thamani ya fedha hizo inapatikana.

66. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani kama ilivyosema katika Hotuba yetu ya Utumishi na Utawala Bora kwamba, tatizo kubwa la nchi yetu ni kukosekana kwa mifumo imara ya Ufuatiliaji na tathmini katika ufuatiliaji wa miradi ya maji vijijini kuna mfumo wa kidigitali uliotumia fedha nyingi katika uwekezaji wake wa WATER MAPPING SYSTEM lakini wahandisi wa maji hawatoi taarifa zenye uhalisia juu ya utendaji kazi wa miradi yote. Kambi Rasmi ya Upinzani inataka kupata maelezo ya kina ni kwanini Serikali inakosa takwimu za uhakikia kuhusiana na upatikanaji wa maji hapa nchini?

67. Mheshimiwa Spika, kuna mfumo mwingine wa EWURA ambao kila mwaka mamlaka hii hutoa taarifa za utendaji za mamlaka za maji kwenye miji na miji midogo, lakini kwa bahati mbaya watanaotakiwa kuchukua hatua wanakuwa ni sehemu ya utendaji mbovu wa mamlaka hizo.

68. Mheshimiwa Spika, takwimu zinaonesha kuwa tangu mwaka 2006- WSDP-I ilipoanza, jumla ya miradi 1810 ilipangwa kutekelezwa, lakini hadi sasa ni miradi 1493 ndiyo imekamilika na miradi 366 inaendelea kujengwa. Aidha, vituo vya kuchotea maji 123,888 vilijengwa lakini vinavyofanya kazi ni vituo 85,286 na vituo 38,602 havifanyikazi kabisa sawa na asilimia 31, Mheshimiwa Spika, huu ni udhaifu mkubwa sana ambao ni lazima utafutiwe ufumbuzi wa haraka.

69. Mheshimiwa Spika, katika miradi hiyo yote ni kuwa fedha zilikwishatolewa lakini matokeo yake wananchi wanaendelea kukosa maji. Kambi Rasmi ya Upinzani inaelewa kuwa hata hiyo miradi ambayo Serikali inasema kuwa imekamilika kwa ajili ya matumizi ya wananchi,uwezekano mkubwa ni kuwa iko pale lakini wananchi hawanufaiki nayo na hata ile inayofanyakazi bado mingine siyo kwa asilimia 100.

70. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inasikitika kwamba licha ya jitihada hizo za kutafuta mikopo lakini bado tunatatizo la uendelevu wa miradi, kama tulivyo shauri ni muda mwafaka sasa PPP itakayohusisha BOT ndilo litakalokuwa suluhisho la uendelevu wa miradi ya maji (kwa kilimo, matumizi ya nyumbani, mifugo na viwandani).

11.0 UWEKEZAJI MDOGO NA USIOAMINIKA KATIKA MIUNDOMBINU KWA AJILI YA SEKTA NYINGINE ZINAZOTUMIA MAJI.

71. Mheshimiwa Spika, Tanzania ina kiwango cha juu kabisa cha uwezo wa kuhifadhi maji asilia barani Afrika, lakini hakuna jitihada za makusudi na makini za kuwekeza katika eneo hili bali tunabaki kutegemea kudra za Mwenyezi Mungu.

72. Mheshimiwa Spika, mbali na uwekezaji mdogo katika kilimo cha umwagiliaji mahitaji ya maji kulingana na ongezeko na kupanuka kwa makazi ya watu yanazidi kuwa makubwa lakini rasilimali watu na fedha ni kidogo mno kukabiliana na mahitaji. Hivyo basi, Kambi Rasmi ya Upinzani inaona itakuwa ni vyema kuwekeza vya kutosha katika kuhakikisha miradi yote ambayo imeishaanza inamalizika kikamilifu na kwa wakati.

12.0 KIWANGO KIDOGO CHA URATIBU WA KISEKTA NA UWEZO WA KITAASISI.

73. Mheshimiwa Spika, Sekta hii bado inakabiliwa na tatizo la uratibu duni wa mipango na maendeleo miongoni na baina ya sekta. Utengano huu unasababisha kushughulikia kwa mtazamo finyu maji kama suala la kisekta (yaani, usambazaji wa huduma ya maji, usafi, na utupaji wa maji taka) badala ya kushughulikia maji kama kipaumbele kikubwa na kugharimia maendeleo na usimamizi wake kama kitovu cha mafanikio kwa sekta kadhaa kuu za uchumi. Jambo hili ni muhimu katika kufanikisha nguzo za ukuaji wa uchumi za Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupambana na Umaskini Tanzania (MKUKUTA) kukuza kipato binafsi, ubora wa maisha, na utawala bora.

13.0 MAPITIO YA BAJETI KWA MIRADI MAENDELEO YA MAJI KUANZIA 2015/16 HADI 2018/19

74. Mheshimiwa Spika, kwa Mwaka wa Fedha 2015/2016 Wizara ya Maji na Umwagiliaji Fungu 49 na Fungu 05 iliidhinishiwa jumla ya shilingi bilioni 565.9 au 565,862,426,195. Fungu 49, liliidhinishiwa jumla ya shilingi bilioni 512.5 au 512,235,736,000 kati ya fedha hizo shilingi bilioni 27 au 26,966,326,000 ni fedha za matumizi ya kawaida (fedha hizi zinajumuisha mishahara shilingi bilioni 18 au 17,960,716,000 na matumizi mengineyo shilingi bilioni 9 au 9,005,610,000). Na kiasi cha shilingi bilioni 485.3 au 485,269,410,000 zilitengwa kwa ajili ya bajeti ya maendeleo.

75. Mheshimiwa Spika, hadi kufikia mwezi Aprili 2019, fungu 49 lilikuwa limepokea fedha za maendeleo shilingi bilioni 137 au 136,900,281,752 tu kati ya shilingi bilioni 485.3 au 485,269,410,000 zilizotengwa ambazo ni sawa na asilimia 28 ya bajeti yote ya maendeleo.

76. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2016/17 Fungu 49 likiidhinishiwa jumla ya shilingi bilioni 938.3 au 938,246,195,000. Kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 913.8 au 913,836,029,000 ni kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo.

77. Mheshimiwa Spika, lakini hadi mwaka huo wa 2016 /17 unamalizika wizara fungu 49 ilipokea fedha za maendeleo jumla ya shilingi bilioni 231 au 230,997,934,672. tu sawa na asilimia 25.7 ya bajeti yote ya maendeleo.

78. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2017/18 fungu 49 liliidhinishiwa na Bunge fedha za maendeleoz jumla ya shilingi bilioni 624 au 623,606,748,000. Lakini hadi mwezi Machi 2018 fedha za maendeleo zilizokuwa zimepokelewa ni shilingi bilioni 135.2 au 135,191,256,566 tu, sawa na asilimia 22 ya fedha zote za bajeti ya maendeleo kwa Wizara ya Maji-fungu 49.

79. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka huu wa fedha 2018/19 bunge lilinaombwa kuidhinisha fedha za miradi ya maendeleo yenye jumla ya shilingi bilioni 673.2 au 673,214,033,677 kati ya fedha hizo shilingi bilioni 443.2 au 443,214,034,677.00 sawa na asilimia 66 zilikuwa ni fedha za ndani na shilingi bilioni 230 au 229,999,999,000.00 sawa na asilimia 34 zilikuwa ni fedha za nje.

80. Mheshimiwa Spika, hadi Mwezi February 2019 jumla ya shilingi bilioni 100.1 au 100,068,574,321.92 sawa na 15 ndizo zilizokuwa zimetolewa. Kati ya fedha hizo shilingi bilioni 95. 3 au 95,335,378,365.39 sawa na asilimai 22 ya fedha za ndani. Fedha za nje zilizotolewa ni shilingi bilioni 4.7 au 4,733,195,956.53 tu sawa na asilimia 2.06 ya fedha za nje. Takwimu hizi zinaonesha kuwa fedha za maendeleo zinazotolewa zinakuwa zikipungua kila mwaka hii ni dhahiri kuwa Maji sio kipaumbele kwa Serikali ya CCM.

81. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2019/20 wizara inaomba fedha za maendeleo jumla ya shilingi bilioni 610.5 au 610,469,888,530.00 kati ya fedha hizo shilingi bilioni 349.45 au 349,449,000,000.00 ni fedha za ndani na shilingi bilioni 261.021 au 261,020,888,530 ni fedha za nje. Bajeti ya maendeleo ni pungufu kulinganisha na ile ya mwaka 2018/19 kwa shilingi bilioni 62.7 au 62,744,145,147.00 sawa na asilimia 9.32

82. Mheshimiwa Spika, ukiangalia miradi ambayo imekosa fedha na iliyopatiwa fedha ni dhahiri kwamba tunachokipanga na kukipitisha hapa Bungeni, kinakuwa sio kinachopatiwa fedha; mfano mradi wa maji toka ziwa Viktoria kwenda Kahama-Shinyanga-Tabora ulitengewa shilingi bilioni 1 lakini hadi Mwezi Machi 2018 hakuna hata shilingi iliyokuwa imetolewa. Mradi wa Masasi-Nachingwea hakuna fedha yoyote iliyotolewa, Mradi wa Ujenzi wa Bwawa la Kidunda zilitengwa shilingi bilioni 10 lakini hakuna fedha iliyotolewa. Mradi wa kuboresha upatikanaji wa maji katika miji ya Same na Mwanga shilingi bilioni 12 lakini hadi Machi hakuna fedha iliyotolewa na Hazina. Mradi wa kupanua na kukarabati miradi ya maji vijijini ambayo inaendelea ya shilingi bilioni 20.7 hakuna fedha zilizotolewa hadi Machi 2018, (rejea Jedwali na.5 uk.14 hadi 16 wa Randama, fungu 49)

83. Mheshimiwa Spika, ukiangalia Randama ya mwaka 2018/19 uk. 15,16 & 17 utaona miradi mikubwa ya kitaifa Mradi wa maji makao makuu ya mikoa mipya,Mradi wa Masasi Nachingwea, Mradi wa Ziwa Viktoria, Kahama/Shinyanga na Tabora, Huduma za Maji Jijij la Dar-es-Salaam, Mradi wa maji Bwawa la Kidunda, Mradi wa maji Mpera na Kimbiji yote hiyo haikupewa hata shilingi. Hivyo Kambi Rasmi ya Upinzani inaona ni utaratibu wa Serikali sasa kuomba Bunge lipitishe fedha lakini haitoi fedha kama zilivyoombwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi husika. Jambo hili linazidisha madeni kwa Serikali kwani mara nying fedha hizo zinakuwa ni za mikopo ya kibiashara ya ndani au ya nje.

84. Mheshimiwa Spika, hapa kuna miradi ambayo toka imeanza kuandikwa kwenye vitabu vya bajeti ni zaidi ya miaka 7 sasa na bado haioneshi kama inamalizika, kama mradi wa bwawa la kidunda na Mpera na Kimbiji. Madhara yake ni kwamba gharama zinazidi kuongezeka kila kukicha kutokana na ukweli kwamba thamani ya shilingi yetu dhidi ya Dola ya Kimarekani inazidi kuporomoka. Kambi Rasmi ya Upinzani inaona ni muda mwafaka sasa kwa Serikali kabla ya kuanzisha miradi mipya tumalize miradi iliyopo tayari, kinyume cha hapo ni kuendelea kupoteza fedha za walipa kodi. (Matumizi mabaya ya fedha za walipa kodi)

85. Mheshimiwa Spika, Mradi wenye Thamani ya Shilingi Bilioni 6.66 Kuchelewa Ukamilishaji, Tarehe 25 Mei 2015 MWAUWASA iliingia mkataba na kampuni ya M/s Jassie& Company Limited wa Ujenzi wa Miundombinu ya Maji Safi na Majitaka katika Mji wa Geita wenye thamani ya Shilingi bilioni 6.66. Mradi huu ulipangwa kuanza mwezi Juni 2015 na kumalizika ndani ya siku 360. Hata hivyo, hadi mwezi Novemba 2017, mradi ulikuwa haujakamilika na mkandarasi ameshaondoka eneo la kazi. Kambi Rasmi ya Upinzani inasema kuwa hizi ni fedha za walipa kodi na matumizi kama haya yanapofanyika wahusika wanahamishwa toka eneo moja kwenda eneo lingine. Katibu Mkuu wa wakurugenzi wa wizara wapo ofisini wanazunguka kwenye viti vyao tu.

14.0 HUDUMA YA MAJI TAKA

86. Mheshimiwa Spika, utoaji wa huduma ya uondoaji wa majitaka mijini bado ni tatizo kubwa sana, hii ni kutokana na uwekezaji mdogo katika utoaji wa huduma hii. Takwimu zinaonesha kuwa ni miji 11 tu ndiyo yenye mifumo ya uondoaji wa maji taka, na ni asilimia 20 tu ya wakazi wa mijini ndio waliounganishwa na mtandao wa majitaka.

87. Mheshimiwa Spika, kama ambavyo tumekuwa tunashauri kwamba ni muda mwafaka haya maji taka yasafishwe na kuingizwa upya kwenye mfumo wa matumizi (recycling). Na tulitoa mfano wa Singapore kama nchi inayotumia vizuri rasilimali ya maji.

88. Mheshimiwa Spika, zipo mamlaka zimeanza utaratibu huu japokuwa kwa kiwango kidogo sana kama MUWASA. Ni vema miradi yote mikubwa inayojengwa sasa kuzingatia hoja hii kwa lazima kabisa toka hatua ya usanifu. Ipo miradi mikubwa sana inayoendelea mfano mradi wa Arusha, Same, Monduli,Tabora,Songea n.k ni vema Mheshimiwa Waziri akalieleza Bunge hili kama jambo hili limezingatiwa.

89. Mheshimiwa Spika, kwa muktadha huo, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kuanza kufikiria au kukaribisha wawekezaji wa kuweza ku-recycle majitaka ili hapo baadaye tuweze kuwa salama kwani viashiria vya upungufu wa maji viko wazi kabisa na jambo hilo halihitaji kubishaniwa au kufanyiwa tafiti.

90. Mheshimiwa Spika, kuna watu wanajiaminisha kuwa tuna maziwa makubwa hapa kwetu na hivyo maji sio tatizo, lakini wafahamu kwamba uwekezaji wa kuyatoa maji hayo kwenye hayo maziwa na kuyaleta kwenye miji mingi na gharama ya kufunga mitambo ya kusafisha maji hayo ni vitu viwili ambavyo uwezi kulinganisha.

15.0 UJENZI WA MAOFISI

91. Mheshimiwa Spika, ukiangalia Randama ya mwaka 2018/19 uk.51 kifungu cha 3.4.2.4 ukarabati na ujenzi wa majengo ya Wizara. Hili kwa kweli linatusumbua kwani, ujenzi wa maji house Dar es Dar es Salaam jengo lenye ghorofa 13 na pale pale kuna ujenzi wa Makao Makuu ya Wizara yatakuwa ni Dodoma. Jengo la Dar es Salaa, litakuwa ni kwa ajili ya watu gani? Hizi zote ni fedha ambazo zingetakiwa ziingie katika utoaji wa huduma. Kambi Rasmi ya Upinzani inaamini kabisa kuwa majengo bado ni mengi kwa watendaji kufanyia kazi na sio jambo la haraka kiasi cha kupelekea miradi ya maji kukosa fedha za kumalizia miradi hiyo. Kwa muktadha huo ni vyema jingo hilo likauzwa kama zilivyouzwa nyumba za Serikali miaka hiyo, ili fedha ziingizwe kuhakikisha upatikanaji wa maji mijini na vijijini.

92. Mheshimiwa Spika, sasa hivi utendaji katika Serikali unaunganishwa katika mtandao mkuu wa Utumishi, na pia malipo yote kwa huduma zinazotolewa na Serikali zinakuwa kwenye mfumo wa e-payment uliopo Hazina au TRA. Kwa muktadha huo inakuwaje taasisi za kutoa huduma kwa wananchi zinaweza kutumia Mamilioni ya shilingi kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi badala ya fedha hizo kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi? Mfano Mzuri ni MWAUASA ambao wametumia takriban Bilioni 1 kwa ujenzi wa Ofisi wakati wakazi wa Mji wa Mwanza wanapata shida ya maji, na wakati huo maji yamejaa ziwa viktoria. Rejea taarifa ya CAG 2016/17

16.0 HITIMISHO

93. Mheshimiwa Spika,maji ni muhimu kwa uhai wa binadamu na viumbe vingine na kwa hiyo, yanatakiwa kusimamiwa vizuri, pia maji ni hitaji muhimu kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi na hiyo wananchi wanayo haki ya kupata maji safi na salama.

94. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inatambua kwamba magonjwa yatokanayo na maji machafu yanasababisha vifo vingi kuliko vile vitokanavyo na vita na machafuko mengine ya kijamii duniani, kwa muktadha huo tutajikita katika uhifadhi endelevu wa vyanzo vya maji, na hili litafanyika kwa ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi.

95. Mheshimiwa Spika, tutahakikisha ubia imara kati ya sekta ya umma na binafsi katika kuwekeza kwenye miradi ya maji kwa mfumo wa anzisha, endesha na hamisha umiliki (Build Operate and transfer). Mfumo huu utatoa hakikisho la upatikanaji wa maji ya kutosha kwa matumizi ya majumbani, viwandani, wakulima, wanyama wafugwao na wale wa porini.
96. Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba kuwasilisha.

Devotha Mathew Minja(Mb)
K.n.y- Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani- Wizara ya Maji
02.05.2019
 

Attachments

  • HOTUBA YA MAJI 2019 FINAL.doc
    125 KB · Views: 22
Back
Top Bottom