Hotuba ya kambi rasmi ya upinzani bungeni kuhusu muswada wa sheria ya huduma za habari 2016

figganigga

JF-Expert Member
Oct 17, 2010
25,491
54,884
HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI KATIKA WIZARA YA HABARI KATIKA WIZARA YA HABARI, UTAMADUNI, WASANII NA MICHEZO, MHESHIMIWA JOSEPH OSMUND MBILINYI (MB), AKIWASILISHA BUNGENI MAONI YA KAMBI RASMI YA UPINZANI KUHUSU MUSWADA WA SHERIA YA HUDUMA ZA HABARI YA MWAKA 2016 (MEDIA SERVICES ACT, 2016)

(Inatolewa chini ya Kanuni ya 86(6) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Januari, 2016)

_______________________________

  1. UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua nafasi hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kuendelea kunilinda na kuniimarisha katika jukumu hili kubwa la kuwaongoza watu wake. Pili ninawashuru sana wabunge wa chama changu – CHADEMA chini ya uongozi imara wa Mheshimiwa Freeman Aikaeli Mbowe (Mb) Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, kwa imani kubwa waliyoonesha kwangu kwa kunichagua kuwa mwakilishi wao katika Kamati Kuu ya chama Taifa. Mimi binafsi na kwa niaba ya wana Mbeya nakubali na kupokea kwa unyenyekevu heshima hii kubwa mliyonipa. Kwenu nyote nasema asante sana na ninawaahidi utumishi uliotukuka.

Mheshimiwa Spika, muswada huu wa huduma za habari ulioletwa bungeni unakuja kuua na kuzika kabisa haki na uhuru wa kupata habari kwa wananchi. Aidha, unakuja kuwafilisi wamiliki wa vyombo vya habari sambamba na kuwafunga waandishi na wahariri wa vyombo vya habari. Kwa ujumla muswada huu umelenga kusambaratisha kabisa tasnia ya habari.

Mheshimiwa Spika, katika hotuba yangu niliyoitoa hapa Bungeni tarehe 13 Mei, 2016 wakati nawasilisha maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuhusu bajeti ya Wizara hii nilisema kwamba wanazuoni wa masuala ya uhuru wa habari wanasema kwamba hakuna dikteta anayependa vyombo huru vya habari “every dictator dislikes free media” niliongeza pia kwamba jambo la kwanza ambalo hufanywa na utawala wa ki-dikteta ni kuminya uhuru na haki ya kupata habari.

Mheshimiwa Spika, nililazimika kufanya rejea ya wanazuoni hao kuandaa hotuba hiyo kwa sababu Serikali hii ya awamu ya tano mara tu baada ya kuingia madarakani ilianza kwa kasi kubwa kuvunja waziwazi kifungu cha 18 (d) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, inayosema kwamba: “Kila mtu anayo haki ya kupewa taarifa wakati wote kuhusu matukio mbalimbali muhimu kwa maisha na shughuli za wananchi na pia kuhusu masuala muhimu kwa jamii”. Tulishuhudia Serikali ikizuia matangazo ya moja kwa moja ya vikao vya Bunge kupitia televisheni ya Taifa; tulishuhudia magazeti kadhaa yakifutiwa usajili; tulishuhudia uhuru wa wananchi kukusanyika na kushiriki mikutano ya kisiasa ukikanyagwa na kupigwa marufuku, tulishuhudia sheria kandamizi ya makosa ya kimtandao ikutungwa ili kudhibiti mawasilano ya haraka miongoni mwa wananchi kupitia mitandao ya jamii na tulishuhudia pia waandishi mbalimbali wa makala wakifunguliwa mashtaka kwa kile kilichoitwa kutenda makosa ya uchochezi.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Serikali ilifanya hayo yote kinyume cha sheria, sasa inaleta sheria kandamizi kuliko zote ili kuhalilisha matendo hayo maovu dhidi ya wananchi wake yenyewe. Sheria inayopendekezwa imelenga kabisa kuwaziba midomo watanzania, waandishi wa habari, na wamiliki wa vyombo vya habari. Aidha, sheria hii inayopendekezwa inalenga kuwanyima wananchi haki na uhuru wa kupata habari bila kujali mipaka ya nchi kama ambavyo kifungu cha 18 cha Katiba kinavyoelekeza.

Mheshimiwa Spika, Muswada huu kwa namna yoyote ile unakiuka Katiba ya nchi. Nasema hivyo kwa sababu muswada huu umepunguza kwa kiasi kikubwa mno haki na uhuru wa wananchi kupata na kutoa habari iliyotolewa na Katiba ya nchi. Na kwa mujibu wa misingi ya kisheria, Katiba ndio sheria mama, na sheria zote lazima zifuate misingi ya Katiba. Sheria inayopingana na Katiba ni batili . Kwa sababu hiyo Mheshimiwa Spika, sheria hii inayopendekezwa ni batili tayari. Na hata kama itapitishwa kishabiki kukidhi malengo ya kidikteta ya Serikali hii ya awamu ya tano ya kuwaziba midomo na kuwaburuza watanzania ubatili huo hautaondoka.

Mheshimiwa Spika, katika mkutano wa nne wa Bunge la 11 kikao cha tarehe 15/09/2016 Serikali ilileta Bungeni muswada wa huduma ya Habari na kusomwa kwa mara ya Kwanza Bungeni, kwa lengo la kuwapa nafasi waheshimiwa wabunge pamoja na wadau mbalimbali wa habari kuupitia na kuufanyia tafakuri ya kina na hatimae kutoa ushauri kwa Serikali pale Kamati za Bunge zitakapokaa kuanzia tarehe 17/10/2016.

Mheshimiwa Spika, Muswada huu wa sheria sio muswada mpya kwa wale wote ambao wanafuatilia kwa makini hoja ambazo Serikali inaziandaa ili Bunge lizipitishe kuwa sheria. Ukweli ni kwamba Muswada huu wa Huduma za Vyombo vya Habari ulitolewa na Serikali kwa mara ya kwanza mwezi Oktoba mwaka 2006 na ukaondolewa Bungeni kutokana na ukweli kwamba wadau walikuwa hawakupata nafasi ya kushiriki katika kutoa maoni yao kwenye mchakato wa utayarishaji wa muswada huo, na kwakuwa Serikali ilikuwa imeleta miswada miwili Bungeni.

Mheshimiwa Spika, Wadau kupitia Baraza la Habari Tanzania walipeleka maoni yao kwenye muswada huu wa Huduma za vyombo vya Habari mwaka 2008 ili yazingatiwe katika uandishi wa Muswada huo.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa hadi mwaka 2011 Serikali ilikuwa bado inatafakari maoni yaliyopelekwa na wadau kwa lengo la kuboresha muswada huo hivyo wadau chini ya Baraza la Habari (MCT) walilazimika kuandika rasimu ya mapendekezo yao kuhusu muswada huo mwaka 2011 - yani “Stakeholders Proposals on the Media Services Bill 2011” na kuyawasilisha Serikalini. Mwaka 2015 Serikali ilileta tena muswada wao huo ili kupitishwa kwa hati ya dharura, lakini Bunge likakataa na ikailazimu Serikali kuurudisha ili wadau wapate nafasi ya kutoa maoni yao.

Mheshimiwa Spika, katika hali ya kushangaza serikali iliamua kupuuza agizo la Bunge lililowataka kuitisha vikao vya mashauriano na wadau mbalimbali ili waweze kutoa maoni yao kwa ajili ya kuuboresha muswada huo, badala yake waliamua kuuweka kabatini bila kufanyia kazi agizo la Bunge. Serikali hii ya awamu ya tano kwa kuwa ina nia ovu dhidi ya tasnia ya habari wameamua kuuleta tena muswada huo bila ya kushirikisha wadau wenyewe wa habari ili waweze kutoa maoni yao, hata pale ambapo wadau walipoomba muda zaidi ili waweze kutoa maoni yao kikamilifu walinyimwa.

Mheshimiwa Spika, katika mchakato wa kuujadili muswada huu katika Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii; kamati ilikuwa ikitoa maelekezo ya kuboresha vifungu mbalimbali vya muswada huu lakini Serikali ilikuwa haifanyi marekebisho hayo kama ilivyokuwa inaagizwa na kamati, jambo ambalo linadhihirisha nia mbaya ya Serikali juu ya tasnia ya habari hapa nchini.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inatoa rai kwa waheshimiwa wabunge wote bila kujali itikadi za vyama; kujua kuwa jukumu la kutunga sheria ni wajibu wa kikatiba na ni kazi ya Bunge hili na kwamba tunatakiwa kufanya hivyo kwa maslahi mapana ya taifa letu.

Mheshimiwa Spika, nadhani tumepata fundisho kwa kupitisha bajeti ya 2016/17 kwa ushabiki na sasa inatuangamiza sote b kila mtu analia ukata na Bunge linashindwa kutimiza majukumu yake ya kikatiba ya kuisimamia Serikali kutokana na ukosefu wa fedha. Kutokana na funzo hilo, safari hii tuache ushabiki wa kiitikadi ili tutunge sheria bora ya kusimamia tasnia ya habari kwa maslahi ya vizazi vya sasa na vya baadaye. Vinginevyo tutakuja kujuta kama tunavyojutia bajeti ya Serikali sasa hivi.

Mheshimiwa Spika, Muswada uliopo mezani unahusu kutunga sheria ya huduma za Habari kwa madhumuni ya kuweka utaratibu wa kisheria katika tasnia ya habari, kuunda bodi ya Ithibati ya wanahabari, kuunda Baraza Huru la Habari, kushughulikia masuala ya kashfa, makosa yanayohusiana na utangazaji na masuala yanayohusiana na hayo.

Mheshimiwa Spika, Muswada unapendekeza kuundwa kwa Baraza Huru la Habari. Hata hivyo, wajumbe wa Baraza hilo ni wateule wa Waziri. Aidha, kazi za Baraza zinafanywa na Bodi ambayo pia wajumbe wake wanateuliwa na Waziri. Kwa muundo huo, ni wazi kabisa kwamba Baraza hilo halitakuwa huru. Kambi Rasmi ya Upinzani Bugeni sheria iweke utaratibu wa kuwapata wajumbe wa Baraza na sio kumwachia waziri mamlaka hayo ili baraza hilo liweze kuwa huru kwali kama ambavyo jina la baraza hilo linajipambanua.

Mheshimiwa Spika, katika mapitio ya muswada hakijaonekana kifungu chochote kinachotoa ulinzi kwa waandishi wa habari. Imekuwa ni jambo la kawaida sasa kwa wanataaluma wa habari kupewa vitisho na wakati mwingine kudhuriwa miili yao na hata kuwawa kutokana na kazi ya kufichua uovu kupitia taaluma yao ya uandishi wa habari.

Mheshimiwa Spika, kutokana na ukweli huo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapendekeza kiwepo kifungu mahsusi cha kuwalinda wanahabari dhidi ya vitendo viouvu vinavyoweza kufanywa dhidi yao.

B: MAPITIO YA VIFUNGU

Mheshimiwa Spika, kifungu cha 3 cha muswada kinahusu tafsiri ya maneno kama ambavyo yatakuwa yanatoa maana kwenye sheria hii; neno:-

media” means the industry, trade of business of collecting,processing and dissemination of content through radio,television or newspaper, and includes online platforms. Kwa Kiswahili kama ilivyotumika kwenye muswada ni kwamba;

chombo cha habari za kielektroniki” maana yake ni aina ya mawasiliano ya maudhui kwa umma kwa njia ya televisheni,redio,video,sinema,magazeti yaliyotolewa mtandaoni au kwa njia nyingine yoyote ya kielektroniki na vifaa ikijumuisha mitandao ya kijamii na njia nyingine zinazoendana na hizo.

Mheshimiwa Spika, kwa tafsiri hiyo ni kwamba; hata wamiliki na waendeshaji wa mitandao ya kijamii ni lazima wapewe ithibati, kinyume cha hapo mitandao wanayoiendesha itakosa uhalali wa kuendeshwa na wamiliki hao. Lengo la serikali ni kuweka Uthibiti na usimamizi wa mitandao ya kijamii –hii ni mitandao kama Jamii Forums ,Blogs n.k kuwa chini ya udhibiti wa serikali na hili ndio maana serikali imeweka mitandao ya kijamii kama sehemu ya vyombo vya habari.

Mheshimiwa Spika, kifungu cha tatu kimeeleza maana ya Mitandao ya kijami kuwa ni …….’mawasiliano miongoni mwa watu kwa njia ya mitandao ambayo yameanzishwa na watu hao kwa ajili ya kubadilishana habari na taarifa katika mitandao na majukwaa mengine ya teknolojia ya kisasa’. Hii maana yake ni kuwa sheria hii inaenda kusimamia hata mawasiliano kwa njia ya Whatsap, Instagram, facebook, twitter na kila mmoja atafungwa na sheria hii. Kambi rasmi ya Upinzani inaona sheria hii ni mbaya na inalenga kudhoofisha tasnia ya habari nchini. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni haioni mantiki mathalani ya Admin wa group la Whatsap kuomba kibali au leseni ya kuwa admi kwa mujibu wa sheria hii inayopendekezwa.

Mheshimiwa Spika, katika mkutano wa nne wa Bunge ilipitishwa sheria ya Haki ya kupata taarifa (The Access to Information Act). Katika mkutano huu wa Bunge, leo Bunge lako tukufu tunajadili muswada wa sheria ya huduma za habari.

Mheshimiwa Spika, wakati akitoa ufafanuzi kuhusu hoja ya serikali kuhusu muswada wa haki ya kupata taarifa mheshimiwa Waziri wa Sheria na Katiba Dr Harrison Mwakyembe alisema kumekuwa na upotoshaji au kuchanganya maneno kuhusu haki ya kupata habari na kupata taarifa na kwa muktadha wa sheria hiyo ya “access to information” haikuwa na uhusiano wowote na masuala ya waandishi wa habari, rejea hansard ya mkutano wa nne, kikao cha kwanza cha tarehe 6 Septemba 2016.

Serikali Kuingilia Vyombo vya Habari

Mheshimiwa Spika, hivi karibuni katika nchi yetu tumeshuhudia kwa mara ya kwanza kufutwa kabisa kwenye usajili wa gazeti la Mawio. Aidha, tumeshuhudia radio 5 na Magic FM zikifungiwa kwa kosa la uchochezi na maamuzi yote hayo yamefanywa na Waziri wa Habari Nape Nnauye.

Mheshimiwa Spika, aidha zipo taarifa kuwa viongozi wa serikali wamekuwa wakipiga simu moja kwa moja kwenye vyombo vya habari kuelekeza habari ambazo zinatakiwa kutolewa kwa umma na vyombo hivyo vya habari. Katika taifa ambalo tumeamua kufuata misingi ya demokrasia na misingi ya haki za binadamu hii si dalili nzuri hata kidogo.

Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo kufanyika wakati mwingine kinyume kabisa cha misingi ya demokrasia na haki za binadamu, kifungu cha 7(1)cha muswada huu kinatoa wajibu kwa vyombo vya habari vya umma na binafsi. Katika kifungu cha 7(1)(b)(iv) kinavitaka vyombo vya habari vya binafsi kutangaza au kuchapisha habari ya masuala ambayo ni muhimu kadri serikali itakavyoelekeza.

Mheshimiwa Spika, kama vyombo vya habari binafsi vinafanya kazi kwa nia ya kupata faida, na hapo hapo serikali inao uwezo kuamuru habari flani ichapwe au itangazwe kwa maelekezo. Sekta binafsi yoyote ile inaendeshwa kwa faida inayopatikana tofauti na vyombo vya umma ambavyo hupata ruzuku ya serikali. Kifungu hiki cha muswada kitasababisha hasara kwa vyombo vya habari.

Mheshimiwa Spika, ni serikali hii ya CCM ambayo iliwahi kuleta muswada wa kuvitaka vyombo vya habari hasa Televisheni na Redio kila ikifika saa mbili usiku kurusha taarifa ya habari ya Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC). Hii ni kutokana na wananchi wengi kutoangalia au kusikiliza TBC kwa sababu inatoa matangazo yasiyo na weledi na yenye kupendelea Chama cha Mapinduzi. Haitashangaza kuona wamiliki wa vyombo vya habari binafsi wakikatazwa kurusha Bunge live kwa gharama zao na kuamriwa kuanza kurusha kipindi cha chereko cha TBC1.

Mheshimiwa Spika, kwa kifungu hiki cha muswada, maelekezo ya muswada ambao uliondolewa ndani ya Bunge lako tukufu umerudishwa kwa mlango wa uani. Sitamshangaa Waziri wa masuala ya habari akitoa maelekezo hayo mara tu baada ya muswada huu kuridhiwa na kuanza kutekelezwa kama sheria kamili.

Mheshimiwa Spika, ni maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani kuwa si tu kuwa kifungu hiki kitatia hasara vyombo binafsi vya habari bali pia kitatoa mwanya na uhalali wa kisheria kwa serikali kuelekeza namna ya kuandika habari kwenye vyombo mbalimbali vya habari kama ilivyoelezwa katika tuhuma ambazo zimeelekezwa dhidi ya serikali kuelekeza namna ya kuandika habari flani zenye maslahi nayo.

Mheshimiwa Spika, waswahili wana msemo wao maarufu wa “Mungu si athumani”, masharti yote yaliyokuwepo kwenye sheria ya haki ya kupata taarifa kama nilivyoeleza yamerudishwa katika muswada huu wa sheria. Hii ni uthibitisho kuwa sheria ya haki ya kupata taarifa na muswada huu wa sheria ya huduma za habari ni kama uhusiano wa kuku na yai kuhusiana na nini kilianza kati ya vitu hivyo viwili.

Mheshimiwa Spika, masharti yaliyopo katika kifungu cha 7(2) ni kikwazo kwa uhuru wa habari. Itakumbukwa kuwa tulieleza wakati wa kutoa maoni kwenye mjadala wa sheria ya haki ya kupata taarifa kuwa masharti hayo, mfano habari zinazoingilia uchunguzi wa vyombo vya uchunguzi, kutowezesha au kuhamasisha kufanya kosa la jinai, kutishia maslahi ya kibiashara ya Jamhuri ya Muungano, kuzuia au kusababisha madhara makubwa kusimamia uchumi n.k

Mheshimiwa Spika, pamoja maelezo hayo ya Waziri katika kifungu cha 7 kifungu kidogo cha 2 muswada huu wa huduma za habari umerudia upya kifungu cha 6 cha sheria za haki ya kupata taarifa, kifungu hicho cha Sheria kilileta mjadala mkubwa hapa Bungeni ambapo ilibainishwa na Waheshimiwa wabunge kutoka Kambi Rasmi ya Upinzani kuwa kifungu hicho kitakuwa ni kaburi la uhuru wa vyombo vya habari.

Mheshimiwa Spika, muswada huu umepiga marufuku kuchapisha ama kutangaza taarifa za Baraza la Mawaziri, hata kama mtu akipata nyaraka inayoonyesha kuwa uamuzi uliofanywa na Baraza la Mawaziri haukuzingatia maslahi ya Taifa kama ambavyo tumeshuhudia huko nyuma kwa mawaziri kufanya maamuzi yasiyokuwa na tija na wengine kufikishwa Mahakamani na kuhukumiwa vifungo kama ilivyotokea kwa Mawaziri Mramba na Yona, kwa sheria hii ukizichapisha taarifa kama hizo unakuwa umetenda kosa kwa mujibu wa kifungu cha 7(2)(c) Kifungu hiki kinaingilia uhuru wa kupashana habari, uhuru na haki ya wahariri. Ni vyema muswada huu ukaonyesha ni aina gani ya taarifa ambazo ni siri na hazitakiwi kuchapishwa badala ya kuacha kama ilivyo sasa.

Mheshmiwa Spika, pamoja na kifungu cha 7(3) kueleza kuwa ikitokea mgongano kati ya sehemu hiyo ndogo katika muswada huu na sheria zingine zilizotungwa na Bunge, sehemu hiyo ndogo ya muswada huu itatamalaki au kuzingatiwa haiondoi uhalisia kuwa masuala hayo yataua kabisa uhuru wa vyombo vya habari.

Mheshimiwa Spika, Serikali imeamua kuwa na aina ya waandishi wa habari ambao inawataka wao kama serikali na hii ni kutokana na kuanzishwa kwa bodi ya Idhibati kwa wanahabari Nchini , na ni bodi ambayo itakuwa inaundwa na serikali yenyewe. Kifungu cha 11 cha sheria hii kimeunda bodi hiyo ya UTHIBITI na sio Ithibati kama wanavyotaka umma uelewe. Waziri mwenye dhamana na masuala ya habari ndiye mwenye mamlaka ya kuteua wajumbe wa Bodi hii.

Bodi hii ya waziri imepewa mamla ka makubwa sana ikiwamo kuwasimamisha au kuwaondoa wanahabari waliothibitishwa katika orodha, kifungu cha 13 (a).

Mheshimiwa Spika, Adhabu imewekwa kubwa sana kuwa mtu akifanya makosa kwa mujibu wa sheria hii atapigwa faini ya kati ya shilingi milioni tano mpaka milioni 20 au kifungo cha miaka 3 na kisichozidi miaka mitano jela au vyote kwa pamoja. Jambo hili ni la hatari kwani sasa Bodi inajipa mamlaka ya kuhukumu na kutoza faini bila Mahakama .

Utoaji wa Leseni kwa Machapisho

Mheshimiwa Spika, Kifungu cha 8 cha muswada kinapaswa kuandikwa upya kwa sababu kinatoa mamlaka makubwa kwa Waziri kutengeneza Kanuni za namna ya kuomba leseni kwa mtu mwenye nia ya kuchapisha, kuuza, kutaka kuuza, kuingiza nchini chapisho lolote na pia kuweka masharti ya umiliki wa hisa kwa kampuni inayomilikiwa na raia wa kigeni.

Mheshimiwa Spika, masuala haya yanahitaji misingi ya kisheria kuainisha vigezo vya utoaji leseni na masuala yanayohusiana na umiliki wa hisa, ili kumpa Waziri mwenye dhamana ya habari apate mwelekeo na msingi wa kisheria kuliko kumwachia kila jambo kuhusiana na masuala ya utoaji leseni kwenye tasnia ya habari.

Mheshimiwa Spika, lengo la Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kupendekeza haya ni kuepuka matumizi mabaya ya mamlaka ya Waziri kutotumika vibaya katika utoaji wa leseni na masuala ya umiliki wa hisa.

Mheshimiwa Spika, kifungu cha 13 kinatoa mamlaka kwa Bodi kumsimamisha au kumuondoa mwandishi wa habari kwenye orodha ya waandishi wa habari. Kifungu hicho hakijaweka utaratibu wa mwandishi wa habari kukata rufaa dhidi ya maamuzi ya Bodi.

Mheshimiwa Spika, kifungu cha 18 (3) kinaweka masharti ya kupata kibali kwa mwandishi wa habari ambaye si mtanzania. Lazima serikali ielewe kuwa habari ina uhusiano mkubwa sana na muda. Muda ukipita na mwandishi huyo akajikuta kuthibitishwa na bodi hakutakuwa na maana yoyote ya kuja Tanzania kama habari husika imeshapitwa na wakati. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali kuweka ukomo wa muda wa kumthibitisha mwandishi wa habari kutoka nje na sio kuwa kama ilivyo.

Mheshimiwa Spika, Kifungu cha 50(2) kinaweka adhabu kwa mtu anayekutwa na chapisho la uchochezi atakuwa na hatia ya faini ya shilingi milioni mbili na isiyozidi milioni tano na au kifungo kisichopungua miaka miwili na kisichozidi miaka mitano. Kifungu hiki kina tofauti kati ya muswada wa kiingereza na wa Kiswahili.

Mheshimiwa Spika, muswada wa Kiswahili katika kifungu cha 50(2) kinazungumzia kukutwa na chapisho la “uasi” wakati muswada wa kiingereza unazungumzia kosa la kukutwa na chapisho la uchochezi pekee.

Mheshimiwa Spika, kifungu hiki hakitoi ulinzi wowote kwa watoa taarifa (whistle blowers) na kimsingi watoa taarifa hawatakuwa na uhuru wa kutoa nyaraka kwa vyombo vya habari kwa sababu akikutwa na nyaraka inaweza kutafsiriwa kwa maslahi ya dola kuwa ni ya kichochezi au uasi.

Mheshimiwa Spika, kwa kurudisha vifungu vya uchochezi vilivyokuwa kwenye sheria ya magazeti ya mwaka 1976 ni kwenda kinyume na mapendekezo ya Tume ya Nyalali ambayo ilipendekeza pamoja na sheria zingine kuwa sheria ya magazeti ya mwaka 1976 ni kikoloni na ifutwe.

Mheshimiwa Spika, vifungu vyote vya uchochezi vilivyopo katika muswada hii vinawanyima waandishi wa habari kufanya kazi zao kwa uhuru kwa mujibu wa taaluma yao. Mathalani uandishi wa habari za uchunguzi umewekwa kaburini na muswada huu.

Mheshimiwa Spika, Kifungu cha 52(1) kinatoa adhabu ya faini ya shilingi milioni 15 au kifungo cha miaka kwa Mkurugenzi au Afisa wa Kampuni au taasisi yoyote ambaye atakutwa na kosa kwa mujibu wa muswada huu. Hili ni janga hasa kwa wasemaji wa vyama vya siasa na taasisi zingine ambao kimsingi hutoa taarifa ambazo ni maamuzi ya vikao vya kikatiba kwa mujibu wa taratibu za taasisi yao.

Mheshimiwa Spika, Kifungu cha 58 kinatoa jukumu na kuwataka waajiri wa waandishi wa habari kuhakikisha kuwa waandishi wa habari wanakuwa na bima ya afya pamoja na kuhakikisha kuwa wanachangia katika mifuko ya hifadhi ya jamii. Jambo hili ni jema sana na Kambi Rasmi ya Upinzani inaliunga mkono, ila yatengenezwe mazingira na wamiliki wa vyombo vya habari kuhakikisha kwamba suala hili halitoathiri kwa njia yoyote ajira za waandishi au watumishi wa vyombo hivyo kwa sababu ya kushindwa kikidhi gharama za uendeshaji.

Kutaifisha mitambo ya kuzalisha magazeti na majarida

Mheshimiwa Spika, kifungu cha 50 vifungu vidogo vya (4)(5)(7)(8)(9)(10)(11) vinatoa mamlaka kwa Polisi kuchukua mashine iliyotumika kupiga chapa chapisho la uchochezi/uasi, kutaifisha au uchukua mashine iliyotumika katika kuchapa chapisho la uchochezi na fedha kutumika katika mfuko wa habari au kuzuia mashine husika isitumika kuchapisha machapisho yoyote.

Mheshimiwa Spika, kubwa katika yote vifungu hivyo vya sheria hii vinatoa uhalali kwa Polisi kutokuwa na kosa lolote hata ikitokea mashine ya uchapishaji imeharibika au kuharibiwa ikiwa mikononi mwao. Kambi Rasmi ya Upinzani inaona kuwa sasa serikali hii ya CCM inaligeuza Jeshi la Polisi kuwa chombo cha uharibifu badala ya kuwa chombo cha ulinzi wa raia na mali zao.

Mheshimiwa Spika, kitendo cha kuleta vifungu vinavyolipa jeshi la Polisi mamlaka kama haya ni ishara kuwa nchi yetu sasa inaelekea kwenye dola la kipolisi (Police State). Ni vema Polisi wakabaki na jukumu la usalama wa raia na mali zao kuliko kuwageuza kuwa matarishi wa kushikilia mali za wawekezaji. Kitendo hiki cha Waziri kuleta muswada kama huu kutaitia doa nchi yetu kitaifa na kimataifa. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali kufuta kifungu hicho.

Mheshimiwa Spika, lazima serikali ya CCM ijue kuwa teknolojia imekua kwa kasi sana kiasi kwamba mchapishaji wa magazeti au nyaraka zingine hana tena jukumu la kusoma na kuhakiki nyaraka inayoletwa kwa ajili ya uchapishaji. Lazima serikali ielewe kuwa siku hizi mambo yote hukamilika kwenye vyumba vya habari na wazalishaji hawana haki wala jukumu la kufanya masahihisho kwenye gazeti wanalopelekewa. Kwa mfano Command to print ni teknolojia inayotumika kwa sasa, na kwa kufanya hivyo mhariri wa habari anaweza kuelekeza computer za kiwandani kuanza kuzalisha magazeti akiwa kwenye chumba cha habari na sio kiwandani.

Mheshimiwa Spika, Si tu mhariri kuanza uzalishaji akiwa kwenye chumba cha habari bali teknolojia imefikia hatua ya kufungasha magazeti kwenye vifurushi tayari kwa kusafirisha kwenda kuuzwa. Mfano halisi ni kuwa hivi karibuni Kampuni ya Mwananchi Communication imeanza kuzalisha magazeti Mikoani na si Dar es Salaam, mathalani wanao mtambo wa kuzalisha magazeti Mwanza ambapo Mhariri akiwa chumba cha habari Dar es Salaam anaweza kuelekeza computer iliyoko kiwandani Mwanza kuanza uzalishaji na kufungasha magazeti tayari kwa usambazaji.

Mheshimiwa Spika, kwa maana hiyo ni ngumu sana kwa Mhariri wa uzalishaji kuwa sehemu zote hizo na kusimamia uzalishaji kiwandani na hivyo kumfanya mmiliki wa mashine au mtambo wa uchapishaji kuwa na hatia kisa tu amehusika katika uzalishaji wa nyaraka husika.

Mheshimiwa Spika, kinachoenda kutokea ni kuwa wamiliki wa mitambo hiyo hawatakubali tena kuviruhusu vyombo vya habari hasa magazeti kuzalisha magazeti yao kwenye mashine zao na hivyo kuua kabisa magazeti mengi ya watu binafsi.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali kuvifuta vifungu vyote ambavyo tumevirejea kwa sababu vinarudisha nyuma tasnia ya habari katika wakati wa mkoloni.

Mheshimiwa Spika, kampuni zinazojihusisha na uchapishaji wa magazeti hawafanyi kazi ya kuzalisha magazeti pekee, wanazalisha vitabu, majarida, mabango, note books, bahasha na vitu vingine kwa ajili ya matumizi mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, lazima serikali ikumbuke kuwa mitambo ya kuzalisha magazeti na nyaraka zingine ni sehemu ya ukuaji wa viwanda, sasa kama serikali imeweka sheria ya kutaifisha viwanda hivyo hali hiyo itarudisha nyuma uwekezaji kwenye sekta hiyo.

Mgawanyo wa kazi za Bodi ya ithibati na Baraza Huru la Habari

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inatambua kuwa Baraza la Habari (MCT) la sasa ni taasisi isiyokuwa na kiserikali ambayo ilianzishwa na wadau wa habari baada ya kuona ombwe katika tasnia ya habari. Ni wazi kuwa MCT ilifanya kazi nzuri pamoja na kuwa haikuwa na mamlaka ya moja kwa moja dhidi ya waandishi wa habari pindi linapotokea tatizo katika utekelezaji wa majukumu ya waandishi wa habari.

Mheshimiwa Spika, kuanzishwa kwa Bodi ya ithibati pamoja na Baraza Huru la Habari ni jambo jema ili kuwe na viwango na uangalizi pamoja na uratibu wa kitaaluma katika tasnia ya habari, lakini ili kuwe na ufanisi ni lazima kuwe na mgawanyo mzuri wa majukumu kati ya vyombo hivi viwili ili kusiwe na mkanganyika katika kutekeleza majukumu hayo.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inapendekeza kuwa kifungu cha 12 kinachoonesha kazi za Bodi kifanyiwe marekebisho ili kazi za Bodi zingine zifanywe na Baraza Huru la Habari. Mathalani suala la kutoa vitambulisho vya waandishi wa habari katika kifungu cha 12(a) libaki kwa Baraza Huru la Habari. Hii haitakuwa tofauti na Chama cha Wanasheria cha Tanganyika (TLS) ambao wanahusika kutoa vitambulisho kwa Mawakili lakini ithibati hufanywa na Baraza linaloratibu masuala ya elimu ya sheria pamoja na Jaji Mkuu.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani pia inapendekeza jukumu lililopo kifungu cha 12 (h) na kifungu cha 19 na 20 lifanywe na Baraza la Habari ili orodha ya waandishi wa habari itunzwe na Baraza kwa sababu, kimsingi wao ndio wanawafahamu waandishi wa habari na wanafanya nao kazi mara kwa mara.

Mheshimiwa Spika, katika masuala ya kinidhamu Kambi Rasmi ya Upinzani inapendekeza kuwa mchakato wa nidhamu kwa waandishi wa habari uanzie kwenye Baraza Huru la Habari ambao ndio wanaohusika na masuala ya kimaadili. Kwa maana hiyo kifungu cha 13 kioneshe kuwa katika Kutekeleza majukumu ya Bodi itakuwa na mamlaka ya kupokea mapendezo ya Baraza la Habari kuhusu nidhamu ya waandishi wa habari au kupokea rufaa kutoka kwa mwandishi wa habari baada ya uamuzi wa Baraza Huru la Habari. Hii itasaidia kuipunguzia Bodi jukumu la kuonekana kama chombo cha kipolisi cha Waandishi wa Habari.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inapendekeza kuwa Leseni za Waandishi wa habari zitolewe na Mkurugenzi wa habari isipokuwa kama Baraza limeshatoa ithibati Mkurugenzi wa habari hatakuwa na mamlaka ya kukataa kutoa leseni kwa Mwandishi wa Habari. Jambo hili halitakuwa tofauti na Mawakili ambapo baada ya kumaliza masomo kwenye Shule ya Sheria Tanzania na mamlaka za kuthibitisha zikimaliza kazi yake Cheti cha ithibati ya kufanya kazi hizo hutolewa na Msajili wa Mahakama Kuu.

Mheshimiwa Spika, ni lazima misingi ya utoaji wa leseni iwekwe wazi kama tulivyopendekeza hapo awali na sio kumuachia Waziri kutoa utaratibu kwa mujibu wa kifungu cha nane. Mamlaka hayo yanaweza kutumiwa vibaya na kuleta matatizo katika utekelezaji wa majukumu ya waandishi wa habari.

Mheshimiwa Spika, katika utaratibu wa kuwathibitisha waandishi wa habari wanaotoka nje ya nchi ambao si watanzania kwa mujibu wa kifungu 18(2) cha muswada, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapendekeza kazi hiyo ifanywe na Mkurugenzi wa Habari au Kamati ya Bodi ya ithibati kwa sababu inaonekana kwenye Jedwali kuwa Bodi itakuwa inakutana mara moja kila baada ya miezi mitatu. Kwa kuwa waandishi ambao si watanzania watakuwa wanakuja mara kwa mara.

Mheshimiwa Spika, mara baada ya mwandishi wa habari ambaye si Mtanzania kupata ithibati Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapendekeza kuwa Baraza Huru la Habari liwe na jukumu la kutoa kitambulisho kwa mwana habari husika.

Mafunzo kwa wanahabari

Mheshimiwa Spika, kifungu cha 21 cha muswada kinaanzisha mfuko wa mafunzo kwa waandishi wa habari. Kwa jinsi kifungu hicho kilivyo ni dhahiri serikali ya CCM haina dira na taaluma ya habari nchini. Kwa sababu kifungu hicho hakijatoa upana wa namna mafunzo ya wanahabari yatakavyofanyika.

Mheshimiwa Spika, kila taaluma ni muhimu kuwa na utaratibu wa mafunzo kwa wanataaluma husika. Mathalani kwa wahasibu na wanasheria wanao utaratibu wao wa mafunzo. Kwa upande wa Mawakili hata baada ya kupewa ithibati ya kufanya kazi za kiwakili kuna utaratibu wa mafunzo endelevu kila mwaka. Kambi Rasmi ya Upinzani inapendekeza kuwa muswada huu uanzishe shule ya waandishi wa habari ambapo watakuwa wanakwenda kupata mafunzo kabla ya kuthibitishwa.

Mheshimiwa Spika, si tu kuwa shule ya waandishi wa habari itasaidia kukuza maadili ya wanahabari bali itakuwa chachu ya kuwa na waandishi wa habari wenye weledi na wanaoaminika nchini.

Mheshimiwa Spika, katika hili Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapendekeza kuwa Bodi ya Ithibati isiwe tu na mamlaka ya ithibati kwa waandishi wa habari bali pia iwe na mamlaka ya ithibati kwa elimu inayotolewa na vyuo mbalimbali vya uandishi wa habari nchini pamoja na kusimamia utendaji wa shule ya waandishi wa habari kabla ya ithibati.

Mheshimiwa Spika, ni vema pia Bodi kwa kushirikiana na Baraza Huru la Habari likaweka viwango vya elimu kwa waandishi wa habari kabla ya kuthibitishwa kufanya kazi za habari na sio kumwachia mamlaka Waziri kuweka kiwango cha elimu kwenye Kanuni. Kitendo cha Muswada kutoweka kiwango cha elimu ni ishara kuwa serikali ina agenda ya siri na ikawa mwiba kwenye taaluma nzima ya habari. Kambi Rasmi ya Upinzani inapendekeza kiwango cha elimu kiwe angalau ngazi ya Diploma.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo muswada huu pia unatoa marufuku kwa waandishi wasiokuwa na ithibati kufanya kazi za habari. Hii itakuwa hatari kubwa mbeleni kwa kuwa kama Bodi itatoa ithibati kwa waandishi wa habari wenye Diploma au shahada pekee, maana yake ni kuwa waandishi wa habari wenye elimu ya ngazi ya cheti hawatakuwa na kazi za kufanya wala kujihusisha na kazi za uandishi wa habari.

Mheshimiwa Spika, ni vema viwango vya elimu vikawekwa na Sheria hii na kutafuta namna ya kuwaruhusu waandishi wa habari ambao hawajafika kiwango hicho cha elimu kuendelea kufanya baadhi ya majukumu kwenye habari kuliko kuacha kundi kubwa la waandishi likiwa mitaani.

Mheshimiwa Spika, baada ya kutoa uchambuzi huo niwashukuru wale wote ambao wameshiriki kwa njia moja au nyingine katika uchambuzi wa muswada huu pamoja na uandaaji wa maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.

Joseph Osmund Mbilinyi (Mb)

WAZIRI KIVULI NA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI

YA UPINZANI BUNGENI KATIKA WZARA YA

HABARI, UTAMADUNI, WASANII NA MICHEZO

4 Novemba, 2016
 
Huu muswaada utapita kama ulivyo licha ya mapungufu yote hayo kwasababu nchi hii watu hatuna uzalendo.

JamiiForums na watumiaji wake tujiandae.
 
Sugu ndio Waziri kivuli wa Habari????? Kweli Mungu alituepusha mwaka Jana Nchi isifanyiwe majaribio ya Utawala. Asante sana Mungu wetu!!
 
Hilo la kuhusu Bajeti na shirikisho la Bunge katika kutunga katiba likiinclude vyama vya upinzani ni sawa na kumpigia mbuzi gitaa kwa serikali ya CCM.

Hayo mawili ndio yalikuwa hot issues last year mwanzoni ila wenye nchi wakafanya fitina zao za wazi.
 
Sasa naona bwana juma pumba maharagwe kaamua kutubaka vizuri,yaani unabakwa huku umezibwa mdomo aisee kazi kweli kweli
 
Back
Top Bottom