Hotuba ya Balozi Seif Ali Idd, Baraza la Wawakilishi likifungwa

figganigga

JF-Expert Member
Oct 17, 2010
25,492
54,890
balozi.jpg
Mh.Makamo wa pili wa Rais Z'bar Balozi Seif akitoa hutuba ya kufunga baraza la wawakilishi Chukwani

1.0Mheshimiwa Spika, sina budi kuanza hotuba yangu hii kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu Mwingi wa Rehema kwa kutujaalia uhai uzima, afya njema na kutuwezesha kumaliza Mkutano huu wa 20 wa Baraza la Wawakilishi la Nane kwa mafanikio makubwa. Aidha, nachukua nafasi hii kukupongeza na kukushukuru wewe Mheshimiwa Spika, kwa umahiri na umakini wako mkubwa wa kuliendesha Baraza hili Tukufu kwa kipindi chote cha Uongozi wako.

Sisi sote ni mashahidi wa namna ulivyodhihirisha uwezo na uzoefu wako wa kuliongoza Baraza hili katika kuisimamia na kuishauri Serikali juu ya utekelezaji wa mipango mbali mbali ya kuwaletea wananchi wetu maendeleo. Kwa kweli umetuongoza vizuri. Pia, napenda kumshukuru Mheshimiwa Naibu Spika pamoja na Waheshimiwa Wenyeviti wote wa Baraza kwa kukusaidia ipasavyo katika kuviendesha vikao vya Baraza hili.

2.0Mheshimiwa Spika, naomba kutoa shukrani za pekee pamoja na kumpongeza kwa dhati kabisa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein kwa uongozi wake uliojaa hekima na busara kubwa ambao umeiwezesha nchi yetu kuzikabili changamoto za kiuchumi na kisiasa na kupiga hatua za kimaendeleo. Aidha, napenda kuchukua fursa hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa imani yake kwangu ya kuniteua kushika nafasi ya Makamu wa Pili wa Rais katika kipindi cha kwanza cha Serikali ya Awamu ya Saba chini ya uongozi wake.

3.0Mheshimiwa Spika, vile vile napenda kumshukuru sana Makamu wa Kwanza wa Rais Mheshimiwa Maalim Seif Sharif Hamad kwa kumsaidia na kumshauri Mheshimiwa Rais katika kuiongoza nchi yetu. Aidha, namshukuru Mheshimiwa Makamu wa Kwanza wa Rais kwa mashirikiano yake makubwa kwangu binafsi na kwa Ofisi yangu katika kutekeleza mipango na malengo yaliyowekwa na Serikali. Hakika katika kipindi hiki cha miaka mitano, Serikali ya kwanza yenye mfumo wa Umoja wa Kitaifa imefanya kazi nzuri sana ya kuiletea nchi yetu maendeleo.

4.0Mheshimiwa Spika,nachukua fursa hii pia kuwashukuru na kuwapongeza Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri kwa kuwasilisha bajeti za Wizara zao na kujibu vizuri na kwa umakini mkubwa hoja mbali mbali zilizotolewa na Waheshimiwa Wawakilishi.

Ni matumaini yangu kwamba, Waheshimiwa Wajumbe na wananchi waliokuwa wakifuatilia kwa karibu zaidi mijadala ya mkutano huu wamefaidika na majibu na ufafanuzi uliotolewa. Vile vile, nawashukuru na kuwapongeza sana Waheshimiwa Wajumbe wote wa Baraza lako Tukufu kwa michango, mapendekezo na ushauri wao waliotoa wakati wa kuzijadili Hotuba za Bajeti zilizowasilishwa hapa Barazani. Nawashukuru Wajumbe wote kwa kuzipitisha bajeti hizo bila ya pingamizi zozote.

Kwa kweli katika mikutano yote ya Baraza lako tukufu, mkutano huu ulikuwa wa kupigiwa mfano kwa kupitisha bajeti zote kwa urahisi. Upitishaji wa bajeti hizo ulikuwa rahisi zaidi kwa sababu ya kutumia mfumo mpya wa bajeti ulioitwa "Program Based Budget" (PBB). Buti hazikuwa nyingi mara hii ukifananisha na bajeti zilizopita. Nawashukuru sana Wajumbe kwa ushirikiano wao.

5.0Mheshimiwa Spika, kwa masikitiko makubwa naomba kuchukuwa fursa hii kuwakumbuka wenzetu waliokwishafika mbele ya haki ambao walikuwa Wajumbe wa Baraza hili. Wajumbe hao ambao wametutoka katika kipindi cha miaka mitano (5) hii ni Marehemu Mussa Khamis Silima aliyekuwa Mwakilishi wa Jimbo la Uzini ambae alifariki tarehe 23 Agosti, 2011, Marehemu Salum Amour Mtondoo aliyekuwa Mwakilishi wa Jimbo la Bububu ambae alifariki tarehe 15 Machi, 2012, Marehemu Salmin Awadh Salmin aliyekuwa Mwakilishi wa Jimbo la Magomeni aliyefariki tarehe 19 Februari, 2015 na Marehemu Ali Khamis Abdalla aliyekuwa Spika Mstaafu alifariki tarehe 8 Agosti, 2014.

Viongozi hao walikua mahodari, wenye msimamo thabit, makini na shupavu na walijitolea kwa hali na mali katika kuwatumikia wananchi kwa kipindi chote cha uhai wao. Hatuna budi kuyaenzi na kuyaendeleza yale yote mema ambayo wenzetu hao wametuachia kwa manufaa ya nchi yetu. Kwa niaba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar naendelea kuwapa pole Waheshimiwa Wajumbe, wanafamilia na wananchi wote kwa ujumla kwa misiba hii. Sisi sote ni waja wake Mwenyezi Mungu na bila ya shaka marejeo yetu ni kwake. Mwenyezi Mungu azilaze roho za marehemu mahala pema peponi. Amin.

6.0Mheshimiwa Spika, kama tunavyoelewa kwamba Mkutano huu wa 20 ni mkutano wa mwisho kabla ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu hapo tarehe 25 Oktoba, 2015. Hivyo, natoa shukurani za dhati kwako wewe Mheshimiwa Spika, viongozi wote na wafanyakazi wa Baraza kwa mashirikiano makubwa katika kuliendesha Baraza katika kipindi chote cha miaka mitano (5). Nawapongeza Waheshimiwa Mawaziri, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu, Wakurugenzi na Wakuu wa Mashirika yote ya Umma kwa bidii na juhudi kubwa katika kutekeleza majukumu yao waliyopangiwa.

Jambo ambalo limechangia sana katika hatua za maendeleo tuliyopata katika nchi yetu. Nawashukuru wananchi wote wa Zanzibar kwa utulivu wao na mashirikiano yao na Serikali katika harakati za kuiletea maendeleo nchi yetu. Ni imani yangu kwamba, wananchi wote wataendelea kuiamini na kuiunga mkono Serikali yao inayoongozwa na Rais kutoka CCM, na watashiriki katika harakati za Uchaguzi Mkuu ujao kwa upendo, amani na utulivu uliokwisha jengeka miongoni mwa jamii yetu.

7.0Mheshimiwa Spika, mafanikio tuliyoyapata katika Kipindi cha Kwanza cha Awamu ya Saba katika Sekta mbali mbali ikiwemo Sekta ya Afya, Elimu, Utalii, Maji na Miundombinu na Mawasiliano na katika Sekta za Uzalishaji (viwanda, kilimo, mifugo na uvuvi) ni ya kupigiwa mfano na tuna kila sababu ya kumpongeza Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein kwa mafanikio haya makubwa. Mafanikio haya makubwa yametokana na utekelezaji sahihi wa Ilani ya CCM ya mwaka 2010 – 2015. Sina shaka kwa mafanikio haya, Rais Shein atarudi tena kuiongoza Serikali hii yenye mfumo wa Umoja wa Kitaifa.

8.0Mheshimiwa Spika, kama tunavyojua kwamba Baraza la Wawakilishi la Zanzibar ni moja kati ya mihimili mitatu ya nchi yetu ambalo ndilo lenye Mamlaka ya Kutunga Sheria na Kusimamia Utekelezaji wa Shughuli za Umma kama ilivyoainishwa katika Kifungu cha 5 A (1) na (2) cha Katiba ya Zanzibar ya 1984.

9.0Mheshimiwa Spika, Baraza hili la Nane hadi sasa limeshafanya jumla ya mikutano 20. Katika mikutano hiyo, jumla ya maswali ya msingi 1,630 na maswali ya nyongeza 3,277 yameulizwa kwa Serikali na kujibiwa. Aidha, Baraza limefanikiwa kujadili na kupitisha Miswada ya Sheria 63 na hatimaye kutungwa Sheria kutokana na Miswada hiyo. Pia, Baraza hili limeidhinisha Bajeti ya Serikali na Mawizara mara tano (5) hadi sasa. Bajeti ambazo zimesaidia kufanikisha kupatikana kwa maendeleo makubwa nchini mwetu.

10.0Mheshimiwa Spika, vile vile, Baraza hili la Nane liliunda jumla ya Kamati Teule tano (5) ambazo zilikuwa kama zifuatazo:-
a.Kamati Teule ya Kuchunguza Baraza la Manispaa.
b.Kamati Teule ya Kuchunguza Utendaji wa Shirika la Umeme (ZECO).
c.Kamati Teule ya Kuchunguza mambo mbali mbali yaliyoibuka kwenye majadiliano ya Bajeti ya mwaka 2011/2012.
d.Kamati Teule ya Kuchunguza Migogoro ya Ardhi.
e.Kamati Teule ya Kuchunguza Upotevu wa Nyaraka.
Ripoti za Kamati Teule zote ziliwasilishwa Serikalini na kuchukuliwa hatua zilizostahili.

11.0Mheshimiwa Spika, Baraza pia lilipokea na kujadili hoja binafsi za Wajumbe kama ifuatavyo:-

a.Hoja ya Mhe. Hamza Hassan Juma, Mwakilishi wa Jimbo la Kwamtipura, inayohusu Mkopo wa Elimu ya Juu.
b.Hoja ya Mhe. Hija Hassan Hija, Mwakilishi wa Jimbo la Kiwani, inayohusu Utendaji wa Shirika la Umeme (ZECO).

c.Hoja ya Mhe. Mgeni Hassan Juma, Mwakilishi Viti Maalum, inayohusiana na vitendo vya Udhalilishaji wa Watoto, Zanzibar.

d.Hoja ya Mhe. Jaku Hashim Ayoub, Mwakilishi wa Jimbo la Muyuni inayohusiana na Uimarishaji wa Huduma za Afya zinazotolewa kwa wananchi wa Zanzibar, na

e.Hoja ya Mhe. Hamad Masoud Hamad, Mwakilishi wa Jimbo la Ole inayohusu Ucheleweshaji wa Upatikanaji wa Vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi.

Hoja zote hizo zilipokelewa na Baraza lako tukufu, kujadiliwa na kutolewa maamuzi stahili.

12.0Mheshimiwa Spika, moja kati ya mambo makubwa na muhimu yaliyofanyika ndani ya Baraza hili la Nane ni Wajumbe wa Baraza lako kushiriki katika Bunge Maalum la Katiba kwa lengo la kuandaa Katiba Inayopendekezwa. Napenda kuchukua fursa hii kuwapongeza Waheshimiwa Wajumbe wote kwa ushiriki wao uliowezesha kupatikana kwa Katiba Inayopendekezwa ambayo hivi sasa inasubiri kupigiwa kura ya maoni na wananchi.

Katiba hii inayopendekezwa imesaidia kutatua kero nyingi zilizokuwa zinalalamikiwa na upande wa Zanzibar. Miongoni mwa kero hizo ni kutolewa kwa suala la mafuta na gesi asilia kutoka kwenye orodha ya mambo ya Muungano. Katiba hiyo imelitoa suala la mafuta na gesi asilia kutoka kwenye orodha hiyo. Kero hiyo ni miongoni mwa kero nyingi zilizokuwa zinalalamikiwa ambazo tayari zimekwisha patiwa ufumbuzi kupitia Katiba Inayopendekezwa.

MAFANIKIO YA SERIKALI YA AWAMU YA SABA:


13.0Mheshimiwa Spika, katika kipindi hiki cha Awamu ya Saba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar yenye Muundo wa Umoja wa Kitaifa tumeshuhudia maendeleo makubwa ya kisiasa, kiuchumi na kijamii. Kwa upande wa kisiasa, Serikali imeweza kuimarisha umoja wa kitaifa na mshikamano wa wananchi wetu bila ya kujali itikadi zao za kisiasa. Hali ambayo imepelekea kuimarika kwa uvumilivu wa kisiasa miongoni mwa viongozi na wanachama wa vyama vya siasa na wananchi kwa ujumla.

14.0Mheshimiwa Spika, kwa upande wa maendeleo ya kiuchumi, hali ya uchumi wetu imeimarika kwa kasi na umekua kutoka asilimia 5.2 mwaka 2010 hadi asilimia 7.4 mwaka 2015. Ukuaji huo unatokana na kuimarika kwa sekta ya kilimo, misitu, uvuvi, viwanda na utalii. Kasi ya mfumko wa bei imepungua kutoka asilimia 6.1 mwaka 2010 hadi kufikia asilimia 5.6 mwaka 2014.Hali hii inatokana na kuongezeka kwa uzalishaji wa ndani unaotokana na juhudi zilizochukuliwa na Serikali katika kuwapatia ruzuku za pembejeo wakulima wetu. Katika kipindi hiki cha miaka mitano (2010 – 2015), Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetoa fidia ya jumla ya Shs. 7,129,591,148 za kuendeleza kilimo, kwa ajili ya ununuzi wa mbolea, madawa, mbegu na kutoa huduma za matrekta kwa wakulima.

15.0Mheshimiwa Spika, kilimo bado kinaendelea kuwa ni mhimili mkuu wa uchumi wetu na ndicho kinachotoa ajira kwa wananchi walio wengi, kwa kutambua hilo Serikali imeweza kutekeleza programu na miradi mbali mbali ya kilimo. Juhudi hizi zimepelekea kuimarika utoaji wa elimu kwa wakulima wa mazao ya chakula, biashara, viungo na matunda, matumizi ya pembejeo, matumizi ya zana za kisasa za kilimo ikiwemo matrekta na miundombinu ya umwagiliaji maji mashambani.

16.0Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuliimarisha na kuliendeleza zao la karafuu kwa kuotesha miche na kugaiwa bure kwa wakulima wetu Unguja na Pemba. Aidha, wakulima wetu wameendelea kupatiwa taaluma ya kilimo bora cha karafuu ikiwemo uimarishaji wa vitalu vya miche ya mikarafuu, uchanganyaji wa mazao mengine (mixed cropping), uvunaji na uanikaji bora wa zao hili. Lengo ni kuhakikisha upatikanaji wa karafuu kwa wingi na zenye viwango vitakavyoipatia nchi yetu bei nzuri katika soko la dunia, ndiyo maana Serikali inawahamasisha wakulima kuyaweka mashamba yao ya mikarafuu katika hali ya usafi. Serikali kwa upande wake inajitahidi kuyaweka mashamba ya Serikali ya mikarafuu katika hali ya usafi.

17.0Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kushirikiana na Kampuni ya Bakhressa imeendelea na juhudi za kumarisha maeneo huru ya kiuchumi ya Fumba. Mpango ulokuwepo ni kuendeleza eneo la Fumba uwe miongoni mwa miji ya kibiashara nchini. Kupitia jitihada hizo, ujenzi wa miundombinu ya barabara, maji na umeme unaendelea, na kwa kuanzia barabara mbili zenye urefu wa kilomita 4.2 ujenzi umekamilika. Aidha, Kiwanda cha kuzalisha bidhaa zitokanazo na maziwa kinafanya kazi na kinaendelea kutoa ajira kwa vijana wetu.

18.0Mheshimiwa Spika, Sekta ya Utalii imeendelea kuimarika. Idadi ya watalii walioingia nchini imeendelea kuongezeka mwaka hadi mwaka na kufikia watalii 274,619 mwaka 2015. Ongezeko hili linatokana na kuimarika kwa miundombinu ya utalii pamoja na hali ya amani na utulivu uliopo nchini. Nawaomba viongozi na wananchi wote kuendelea kudumisha amani katika nchi yetu hasa katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu ili utalii wetu uzidi kuimarika na uchumi wetu uzidi kukua. Serikali inawahakikishia watalii wetu hao usalama wao kwa kipndi chote ambacho watakuwa nchini mwetu.

Katika kuimarisha zaidi Sekta hii ya Utalii, Serikali imeamua kuibadilisha mandhar ya Hoteli ya Bwawani, hoteli ambayo ina historia kubwa baada ya kupatikana mwekezaji ambaye yuko tayari kuibadilisha hali hiyo. Mazungumzo baina ya Serikali na mwekezaji yamefikia mbali na sasa bado tu Serikali kumkabidhi mradi huo kwa mwekezaji na kufunga naye mkataba.

19.0Mheshimiwa Spika, Sekta ya Miundombinu nayo imepata mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na ujenzi wa barabara mpya kwa kiwango cha lami zenye urefu wa kilomita 243.85 kwa Unguja na Pemba. Vile vile barabara zenye urefu wa kilomita 39.3 zimejengwa kwa kiwango cha kifusi. Aidha, barabara zenye urefu wa kilomita 656 zimefanyiwa matengenezo mbali mbali. Ni matumaini yangu kwamba, ujenzi wa barabara hizi utasaidia ukuaji wa uchumi wa nchi yetu, hivyo napenda kutoa wito kwa watumiaji wa barabara hizi na wananchi kwa ujumla kuzitunza kwa faida yetu na vizazi vyetu vijavyo. Wale wenzetu wenye tabia ya kuchoma barabara hizo kwa makusudi waiache tabia hiyo kwani inaigharimu Serikali fedha nyingi kuzitengeneza tena barabara hizo. Serikali itawachukulia hatua kali waharibifu hao.

20.0Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kushirikiana na wadau wa Sekta ya Usafiri Baharini imeendelea kuimarisha usafiri wa baharini kwa kujenga majengo mapya ya kuhudumia abiria katika bandari ya Malindi Unguja. Aidha, Serikali imeshanunua meli mpya huko Korea yenye uwezo wa kuchukua abiria 1,200 na tani 200 za mizigo ambayo inatarajiwa kuwasili mwishoni mwa mwezi wa Julai mwaka huu. Aidha, Serikali imeendelea kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwa kuendeleza dhamira ya ujenzi wa bandari mpya, kubwa na ya kisasa katika maeneo ya Mpigaduri ambapo hatua za uchambuzi yakinifu, michoro pamoja na makubaliano ya ujenzi huo na kampuni ya China Habour Engeneering Companyyamekamilika. Vile vile, Serikali inaendelea na utaratibu wa kuziendeleza bandari zetu zote za Unguja na Pemba. Uamuzi wa ujenzi wa bandari ya Mpiga Duri ulifanywa na Serikali ya Awamu ya Tano kuendelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita, na Serikali ya Awamu ya Saba ndiyo iliyoendeleza mradi huo kwa kutafuta wafadhili wa kuijenga bandari hiyo.

Ilani ya CCM ya mwaka 2010 – 2015 kifungu 143 (e) inasema:

"Kusimamia utekelezaji wa Mpango Mkuu (Master Plan) wa bandari ya Malindi, ikijumuisha huduma za bandari huru na kuendelea kutafuta uwezo wa kujenga bandari mpya ya kibiashara ya Mpiga Duri". Mhe. Rais anafanya kazi kubwa sana kuhakikisha kuwa mradi unatekelezwa na ndiyo tumefikia hapa tulipo. Mradi huu utaanza kujengwa mara tu mradi wa Terminal II utakapokamilika. Hivyo, Serikali itakayokuja itauendeleza tu mradi huu na siyo kuuanzisha.

21.0Mheshimiwa Spika, kwa upande wa usafiri wa anga, Serikali imejenga maegesho na njia za kupitia ndege katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Abeid Amani Karume. Vile vile, ujenzi wa jengo jipya la abiria la kiwanja hicho unaendelea vizuri na unatarajiwa kukamilika mwezi wa Oktoba mwaka huu. Aidha, Serikali inaendelea na uimarishaji wa Uwanja wa Ndege wa Sheikh Abeid Amani Karume - Pemba kwa kuuwekea taa na kuufanyia matengenezo katika njia yake ya kurukia na kutulia ndege. Kukamilika kwa ujenzi huo kutaimarisha utoaji wa huduma za abiria na mizigo katika viwanja vyetu vyote nchini.

22.0Mheshimiwa Spika, mafanikio makubwa yameweza kupatikana katika Sekta ya Elimu katika ngazi zote kuanzia elimu ya awali, msingi, sekondari na elimu ya juu. Miongoni mwa mafanikio hayo ni kupunguza tatizo la upungufu wa walimu, maabara, vitabu vya kiada na ziada pamoja na uhaba wa madarasa na samani. Aidha, Serikali imefanikiwa kwa asilimia 100 kuwaandikisha wanafunzi wote waliotarajiwa kuanza darasa la kwanza mwaka 2015.

23.0Mheshimiwa Spika, Serikali pia imeendeleza ujenzi wa skuli za sekondari na kukamilisha ujenzi wa skuli za msingi ambazo zimekuwa zikianzishwa na wananchi wenyewe katika maeneo mbali mbali ya nchi yetu. Sambamba na mafanikio hayo, Serikali imeendelea kuwapatia mikopo ya elimu ya juu wanafunzi ili kuwawezesha kujiunga na vyuo mbali mbali ndani na nje ya nchi. Aidha, Serikali imekuwa ikishirikiana na Vyuo Vikuu vilivyopo Zanzibar ili kuongeza fani za masomo kuanzia ngazi ya Shahada ya Kwanza na kuendelea ili kupata wataalamu wa fani mbali mbali.

24.0Mheshimiwa Spika, kupitia Baraza lako Tukufu napenda kutoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na Serikali katika jitihada za ujenzi na usimamizi wa skuli katika maeneo yao. Aidha, natoa wito kwa wale wote waliopatiwa mikopo ya elimu ya juu kulipa mikopo hiyo ili kuwawezesha wanafunzi wengine kupata huduma hiyo.

25.0Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na juhudi zake za kupambana na magonjwa mbali mbali ya kuambukiza na yasiyo ya kuambukiza. Zanzibar imekuwa mfano kwa nchi za Afrika Mashariki na dunia kwa kuweza kutokomeza ugonjwa wa Malaria. Aidha, Serikali inaendelea kuiimarisha Hospitali ya Mnazi Mmoja kwa kujenga na kuweka vifaa vya kisasa ili kuipandisha daraja na kuwa hospitali ya Rufaa na Kwa upande wa Hospitali za Kivunge, Makunduchi na Chake Chake kuwa Hospitali za Wilaya. Hospitali za Abdalla Mzee Mkoani na Hospitali ya Wete zinaimarishwa ili ziweze kupandishwa daraja na kuwa Hospitali za Mkoa. Katika mwendelezo wa kuimarisha huduma ya afya kwa wananchi wetu, Serikali imezipatia hospitali vifaa vya kisasa pamoja na usambazaji wa dawa kwa wananchi. Vile vile Serikali ya Awamu ya Saba kwa kushirikiana na Washirika wa Maendeleo imeweza kujenga Bohari Kuu ya Dawa ya kisasa ambayo ni mfano katika nchi za Afrika Mashariki na Kati.

26.0Mheshimiwa Spika, UKIMWI na Dawa za Kulevya ni miongoni mwa matatizo yanayoathiri makundi mbali mbali ya watu, hasa vijana. Katika suala la UKIMWI, kiwango cha mambukizi kimeendelea kubakia kuwa asilimia 0.6 na idadi ya watu walioambukizwa virusi vinavyosababisha UKIMWI (VVU) waliosajiliwa ni 7,820. Kati ya hao watu 5,375 wanapata huduma ya ARV. Katika kuendeleza mapambano dhidi ya UKIMWI, Serikali imechukuwa hatua mbali mbali, zikiwemo kuimarisha huduma za tiba, huduma za kuzuia maambukizi ya mama kwenda kwa mtoto. Aidha, Serikali imesambaza mashine tatu mpya za CD4 ambazo zimepelekwa katika Hospitali ya Mnazi Mmoja, Mwembeladu, na Kivunge, na mashine aina mbili za "Haematology" na "Chemistry" zimesambazwa katika Hospitali za Micheweni, Makunduchi, na Mwembeladu. Pia, Serikali imeimarisha vituo vya ushauri nasaha na upimaji wa VVU.

Vile vile, Serikali kwa kushirikiana na Taasisi zisizo za Serikali (NGOs) inaendelea na shughuli za kuelimisha jamii juu ya mapambano dhidi ya UKIMWI na kupunguza unyanyapaa kwa watu wanaoishi na VVU. Pia, vituo vinavyotoa huduma ya ushauri nasaha na upimaji wa VVU vimeongezeka kutoka vituo 87 mwaka 2012 hadi kufikia vituo 91 mwaka 2015. Kati ya hivyo, Unguja 58 na Pemba 33. Vile vile, Serikali inaendelea kuwahamasisha wananchi kuwa na tabia ya kupima afya zao na kujiepusha na maambukizi mapya ya UKIMWI.

27.0Mheshimiwa Spika, kwa upande wa tatizo la dawa za kulevya, Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais inasimamia utekelezaji wa Sheria ya Udhibiti wa Dawa za Kulevya Namba 12 ya mwaka 2011. Mpango Maalum (Road Map) wa Utekelezaji wa Sheria hiyo umeandaliwa na unatekelezwa kwa kushirikisha wadau kutoka Taasisi mbali mbali za Serikali na zisizo za Serikali ili kuhakikisha kwamba michango mbali mbali inatolewa kudhibiti uingizaji, usafirishaji, usambazaji na matumizi ya dawa za kulevya. Vile vile, Serikali imeandaa Sera ya Dawa za Kulevya na kufanya mikutano na vyombo vya kusimamia sheria (Law Enforcement Agency) ili kukuza mashirikiano na vyombo hivyo katika kudhibiti Dawa za Kulevya.

28.0Mheshimiwa Spika, ujenzi wa Kituo Maalumu cha Kurekebisha Vijana walioathirika na Dawa za Kulevya katika eneo la Kidimni, Wilaya ya Kati unaendelea.Aidha, Nyumba za Marekebisho ya Tabia (Sober Houses) 13 zimeanzishwa ambazo zimetoa huduma kwa vijana 1,020 kwa Unguja na Pemba. Serikali imechukua jitihada kubwa ya kuziendeleza nyumba hizo ili ziweze kutoa huduma zinazostahiki. Serikali kupitia Vituo vya Ushauri Nasaha imeendelea kutoa ushauri nasaha kwa waathirika wa dawa za kulevya. Pia, taaluma juu ya athari za Dawa za Kulevya imetolewa katika Shehia mbali mbali za Unguja na Pemba, Vikosi vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na Skuli kupitia mikutano, makongamano, semina pamoja na utoaji wa kalenda na vipeperushi.

29.0Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kushirikiana na Washirika wa Maendeleo inaendelea na jitihada zake za kuwapatia wananchi wake huduma bora ya maji safi na salama. Katika kutimiza azma hiyo, Serikali ya Awamu ya Saba imetekeleza Miradi 10 na Programu mbili (2) za kuwapatia wananchi wake maji safi na salama pamoja na kuendeleza Mpango wa Kulinda Vyanzo vya Maji Unguja na Pemba. Vile vile, Serikali imeifanyia matengenezo makubwa miundombinu ya usambazaji maji katika maeneo mbali mbali mjini na vijijini ili kuhakikisha kuwa huduma ya maji inapatikana kwa wananchi wakati wote bila ya usumbufu.

Serikali imechukua hatua maalumu ya kuziondosha mita 41 za TUKUZA zilizokuwepo katika visima mbali mbali vya miradi ya maji ili kuwaondoshea kero wananchi na kuhakikisha wanapata huduma ya maji safi na salama bila ya usumbufu.

30.0Mheshimiwa Spika, ili kuhakikisha kwamba Zanzibar inakua na umeme wa uhakika, Serikali imesimamia kikamilifu utekelezaji wa mradi wa kujenga njia ya pili ya umeme inayopita chini ya bahari kutoka Ras Kiromoni Tanzania Bara hadi Fumba Unguja. Pamoja na hatua hiyo, Serikali pia imo katika juhudi ya kutafuta miradi ya umeme mbadala, kwa kutumia ama jua, upepo au mawimbi ya baharí, hii itategemea na utafiti unaofanywa kujua ni aina gani ya umeme unatufaa kwa mazingira ya nchi yetu.

Aidha, kwa msaada wa Serikali ya Norway, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeunganisha umeme toka Majani Mapana, Tanga hadi Wesha huko Pemba ili wananchi wa Pemba wapate umeme wa uhakika. Umeme huu una nguvu ya 20MW, hadi sasa ni matumizi ya 6MW tu ndiyo yaliyofikiwa. Waya huu unaweza kuishi kwa muda wa miaka 30 hadi 40. Umeme huu umeanza kutumika kuanzia mwaka 2010.

31.0Mheshimiwa Spika, katika kuendeleza matumizi bora ya ardhi nchini (Land use Planning), Serikali imekamilisha Mpango Mkuu wa Kitaifa wa Matumizi Bora ya Ardhi wa Zanzibar. Utekelezaji wa Mpango huu utasaidia kupunguza matumizi holela ya ardhi. Sambamba na Mpango huo, Serikali imetayarisha Sheria ya kuanzisha Kamisheni ya Ardhi itakayosimamia matumizi yote ya ardhi nchini. Aidha, Serikali imeendelea kuziimarisha mahakama za ardhi kwa kuzipatia vitendea kazi na kuziongezea idadi ya Mahakimu. Juhudi zote hizi zimelenga katika kupunguza tatizo la migogoro ya ardhi hapa nchini. Ni matumaini yangu Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza lako watasaidia kuhakikisha kuwa migogoro ya ardí inakuwa historia nchini mwetu.

MAMBO YALIYOJADILIWA KATIKA MKUTANO WA 20:


32.0Mheshimiwa Spika, Mkutano huu wa 20 ulikuwa ni mkutano wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2015/2016 ambapo Bajeti ya Serikali, Mpango wa Maendeleo pamoja na bajeti za Wizara zote ziliwasilishwa, kujadiliwa na kupitishwa. Aidha, katika Mkutano huu jumla ya maswali ya msingi 72 na maswali ya nyongeza 174 yaliulizwa na Waheshimiwa Wajumbe na kujibiwa na Waheshimiwa Mawaziri. Pia, Mswada wa Sheria Namba 9 ya 2015 ya Kutoza Kodi na Ushuru na Kurekebisha Sheria Nyengine za Fedha na Sheria za Kodi Zinazohusiana na Ukusanyaji na Udhibiti wa Mapato ya Serikali na Mambo Mengine Yanayohusiana na Hayo, uliwasilishwa, kujadiliwa na kupitishwa na Baraza lako Tukufu.

Vile vile, Baraza lilijadili na kupitisha Sheria Namba 10 ya 2015 ya Kuidhinisha Makisio na Matumizi ya Shilingi Mia Nane na Thalathini, Mia Tatu na Sitini Milioni na Laki Tatu kutoka Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali kwa mwaka wa fedha unaoishia tarehe 30 Juni, 2016 na kuruhusu Utoaji na Uhaulishaji wa Fedha Hizo pamoja na Mambo Yanayohusiana na Hayo.

33.0Mheshimiwa Spika, pamoja na jukumu muhimu la Mkutano huu la kuwasilisha, kujadili na kupitisha Bajeti ya Serikali, Mpango wa Maendeleo pamoja na bajeti za Wizara zote, Baraza pia lilipata fursa ya kujadili hoja mbali mbali zilizowasilishwa na Waheshimiwa Wajumbe. Miongoni mwa hoja hizo ni pamoja na hoja ya ukarabati wa nyumba za Mji Mkongwe, mapambano dhidi ya udhalilishaji na ukatili wa kijinsia, migogoro na unyanyasaji wa wafanyakazi katika makampuni na hoja inayohusiana na malipo ya posho na stahiki za walimu.

34.0Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na juhudi ya kuzipatia ufumbuzi hoja mbali mbali zilizotolewa na Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza lako Tukufu. Suala la ukarabati wa Mji Mkongwe, Serikali tayari imeshafanya tathmini na jumla ya nyumba 26 zimegundulikana kuwa mbovu na zinahitaji ukarabati mkubwa. Kutokana na uwezo wa Serikali wa kuzikarabati nyumba hizo kuwa mdogo, imeamua kuziuza baadhi ya nyumba hizo. Aidha, katika kusimamia suala la udhalilishaji na unyanyasaji wa kijinsia, Serikali itaendeleza mashirikiano na wananchi katika kupambana udhalilishaji wa aina zote nchini. Hivyo, Serikali inawaomba wananchi waendeleze mashirikiano baina yao na Serikali yao katika kuwafichua wale wote wanaofanya vitendo vya udhalilishaji.

35.0Mheshimiwa Spika, katika kulishughulikia tatizo la migogoro na unyanyasaji wa wafanyakazi katika makampuni hasa ya kitalii, Serikali kupitia Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais Kazi na Utumishi wa Umma inaendelea kuwakumbusha wamiliki wa mahoteli kufuata kanuni na sheria za kazi zilizopo nchini na kuwacha kuwanyanyasa wafanyakazi wao. Aidha, Serikali inawataka waajiriwa wa makampuni hayo kuwasilisha malalamiko yao Wizarani ili Wizara ichukuwe hatua zinazofaa. Vile vile, kwa upande wa malipo ya stahiki na maposho kwa walimu waliosimamia mitihani iliyopita, Serikali tayari imeshalipa stahiki na maposho kwa baadhi ya walimu na hatua za kuwakamilishia stahiki na maposho kwa walimu waliobakia zinaendelea.

36.0Mheshimiwa Spika, harakati za Uchaguzi Mkuu wa 2015 tayari zimeanza kwa Vyama vya Siasa kutafuta wagombea wa nafasi mbali mbali za uongozi wa nchi yetu. Ni muhimu kwetu sisi viongozi kuzidi kuwanasihi wafuasi wetu na wananchi kwa ujumla kujiepusha na aina zote za vitendo vitavyoweza kupelekea uvunjifu wa amani na usalama wa nchi yetu. Ni imani yangu kwamba, tunaweza kuchaguana bila ya kutukanana, kugombana, kuchukiana, kuhasimiana au kufanya vurugu za aina yoyote ile.

Hii ni nchi yetu sote na hivyo, usalama na amani ni muhimu kwetu sote. Mafanikio yetu tuliyoyapata kwa muda mrefu na maendeleo yetu yanategemea kudumu kwa hali ya amani na utulivu katika nchi yetu. Nawasihi wananchi wote watumie haki yao ya kidemokrasia kuchagua viongozi makini wenye nia ya dhati na uwezo wa kuwatumikia na kuwaletea maendeleo wananchi. Serikali itahakikisha ulinzi na usalama unaimarika na haitokuwa tayari kumvumilia mtu yeyote au kikundi chochote kitakachovunja sheria na kuhatarisha amani na utulivu wa nchi yetu. Tusifikirie hata siku moja kuwa vikundi vinavyojitayarisha au kutayarishwa kufanya vitendo vya kuhatarisha amani ya nchi kuwa vinaikomoa Serikali bali vinajikomoa vyenyewe. Tunawaomba wazazi kuwadhibiti vijana wao ili wasijiingize katika vitendo vya uvunjifu wa amani.

37.0Mheshimiwa Spika, kabla ya kumalizia hotuba yangu, naomba kwa mara nyengine tena nikushukuru wewe binafsi kwa jinsi ulivyoliendesha Baraza kwa umakini na uadilifu mkubwa. Narudia kuwashukuru pia, Mheshimiwa Naibu Spika, Wenyeviti wa Baraza na Wenyeviti wa Kamati za Kudumu kwa kutekeleza majukumu yao vyema katika kipindi chote cha miaka mitano (5). Vile vile, nawashukuru Waheshimiwa Mawaziri, Naibu Mawaziri, Waheshimiwa Wajumbe wote wa Baraza la Wawakilishi, Makatibu Wakuu wa Wizara zote na Watendaji wote wa Serikali kwa utendaji wao mzuri uliotuletea mafanikio makubwa katika nchi yetu.

38.0Mheshimiwa Spika, kwa aina ya pekee namshukuru Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mheshimiwa Mohamed Aboud Mohamed, Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu, Afisa Mdhamini, Wakurugenzi na Watendaji wote wa Ofisi yangu kwa namna walivyonipa mashirikiano na kunisaidia katika kutekeleza majukumu yangu. Aidha, napenda kuwashukuru wake zangu Bi. Pili Juma Iddi na Bi. Asha Suleiman Iddi na familia zangu kwa ujumla kwa namna walivyonipa moyo, kunivumilia na kunisaidia katika kipindi chote nilichotumikia nchi yetu katika nafasi hii ya Makamu wa Pili wa Rais.

Zaidi namshukuru sana Bi. Asha kwa namna alivyonisaidia katika shughuli za Jimbo langu la Kitope wakati nikiwa na shughuli nyingine za Kitaifa. Pia, napenda kuwashukuru sana wananchi wangu wa Jimbo la Kitope kwa kushirikiana nami katika kipindi chote cha miaka mitano kwa nia ya kuliletea Jimbo letu maendeleo. Nawaomba waniunge tena mkono nitakapokwenda kuomba ridhaa yao ya kuwatumikia.

39.0Mheshimiwa Spika, navishukuru vyombo vyote vya habari vilivyoshirikiana nasi katika Baraza hili wakiwemo wataalamu wetu wanaotafsiri kwa lugha ya alama waliowawezesha wenzetu wenye matatizo ya kusikia kufuatilia mijadala na shughuli mbali mbali za Baraza. Pia, namshukuru Katibu wa Baraza la Wawakilishi na wafanyakazi wote wa Baraza hili kwa maandalizi mazuri ya mikutano yote. Kwa aina yake napenda kumshukuru sana Mhasibu wa Baraza kwa kazi nzuri alizofanya katika kipindi chote cha miaka mitano kuwahudumia vizuri Wajumbe wa Baraza.

40.0Mheshimiwa Spika, nawatakia kila la kheri Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza lako Tukufu watakaopata nafasi ya kurudi Majimboni kuomba ridhaa ya wananchi kuchaguliwa tena kuingia Baraza líjalo. Nawatakia kheri katika mchakato huo na ni matumaini yangu kwamba wengi wetu tutarudi tena katika Baraza hili kuendelea kuwatumikia wananchi. Lakini pia nawatakia kila la kheri wale Wajumbe ambao hawatopata bahati ya kurudi tena Barazani hapa, nawaombea wafanikiwe katika mambo watakayoamua kuyafanya hapo baadae.

41.0Mheshimiwa Spika, mwisho napenda kuchukua nafasi hii kuelezea masikitiko yangu kwa lile jambo lililotokea Barazani huku tarehe 23 Juni, 2015 kwa Mawaziri na Wajumbe wengine wa Baraza lako tukufu kutoka Chama cha CUF kuamua kutoka nje ya Baraza wakati Baraza lilipotaka kupitisha sheria ya matumizi kutokana na Bajeti zilizowasilishwa Barazani. Kitendo hiki hakikuwatendea haki wananchi kwani kama sheria ya matumizi isingepita maana yake Serikali ingeshindwa kuwatumikia wananchi na kuwaletea maendeleo kwa vile isingekuwa na fedha.

42.0Mheshimiwa Spika, napenda kuwapongeza kwa dhati Waheshimiwa Mawaziri na Wajumbe wengine wa Baraza lako tukufu kutoka Chama cha Mapinduzi kwa kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha kuwa sheria ya matumizi inapita. Kitendo hicho kilikuwa cha kizalendo na kimeonyesha upendo kwa wananchi wetu. Hongereni sana.

43.0Mheshimiwa Spika, kwa vile Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Ali Mohamed Shein leo tarehe 26 Juni, 2015 saa 9.30 jioni atakuja kulihutubia Baraza hili na baadae kutoa tamko la kulivunja, sasa kwa ruhusa yako naomba kutoa hoja ya kuliakhirisha Baraza lako Tukufu hadi hapo saa 9.30 barabara za jioni.

44.0 Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.
 
Back
Top Bottom