Hotuba ya bajeti ya Mheshimiwa Kabwe Zuberi Zitto (Mb) waziri kivuli wizara ya fedha hii hapa

nice 2

JF-Expert Member
Joined
Aug 10, 2011
Messages
747
Points
0

nice 2

JF-Expert Member
Joined Aug 10, 2011
747 0
hotuba ya mheshimiwa kabwe zuberi zitto (mb) waziri kivuli wizara ya fedha na uchumi kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya wizara kwa mwaka wa fedha 2011/2012
see attachment....
 

nice 2

JF-Expert Member
Joined
Aug 10, 2011
Messages
747
Points
0

nice 2

JF-Expert Member
Joined Aug 10, 2011
747 0
HOTUBA YA MHESHIMIWA KABWE ZUBERI ZITTO (MB) WAZIRI KIVULI WIZARA YA FEDHA NA UCHUMI KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA KWA MWAKA WA FEDHA 2011/2012UTANGULIZIMheshimiwa Spika, naomba kumshukuru Mwenyezi Mungu, kwa kunipa afya na uzima na kuweza kusimama mbele ya Bunge ili kutoa maoni ya Kambi ya Upinzani Wizara hii, kwa mujibu wa Kanuni za Bunge kanuni ya 99(7), toleo la mwaka 2007.Mheshimiwa Spika, natoa pongezi na shukrani zangu za dhati kwako wewe binafsi, Naibu Spika pamoja na Wenyeviti wa Bunge kwa kazi kubwa waliyoifanya ya kuliongoza Bunge licha ya changamoto nyingi. Tukiwa tunakaribia mwisho wa Mkutano wa Nne wa Bunge la Kumi, nawapongeza Wabunge wote wa pande zote mbili za Bunge na wa vyama vyote kwa michango yao na changamoto mbalimbali walizotoa ndani ya Bunge. Ninaamini Serikali itafanyia kazi hoja mbalimbali ambazo wabunge wametoa na pia Wabunge watafanyia kazi majibu mbalimbali ambayo Serikali imeyatoa.Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo natoa shukrani zangu za dhati kwa Kiongozi wa Upinzani Bungeni pamoja na waheshimiwa wabunge wote wa Kambi ya Upinzani kwa ushirikiano waliouonyesha katika uwasilishaji wa Hotuba zote mbadala katika kipindi chote cha mkutano huu. Kwa uzito wa pekee nitambue ushiriki mkubwa wa Naibu Waziri Kivuli wangu Mhe. Christina Mughway (Mb) kwa kujituma kwake katika kazi za Wizara hii tunayoisimamia . Busara na hekima zake, ucheshi na uchapa kazi wake ni nguzo muhimu kwangu kama Kiongozi wake. Nakushukuru Sana Mheshimiwa Christina Mughwai.Mheshimiwa Spika, kipekee naomba kutoa pongezi na shukrani kwa Mawaziri vivuli wote kwa kazi kubwa waliyoifanya katika Mkutano Huu. Kwa niaba ya Uongozi mzima wa Kambi ya Upinzani nawaahidi wananchi wote kuwa hotuba zote za Mawaziri Vivuli zitahaririwa na kuchapishwa katika kitabu kimoja kwa ajili ya wananchi kufanya rejea na kujionea kazi iliyofanywa na Waheshimiwa Wabunge wa CHADEMA katika mkutano huu na kipindi hiki cha Bajeti ya mwaka 2011/2012.Mheshimiwa Spika, Mkutano huu wa Bunge ulikuwa na changamoto nyingi sana. Hata hivyo mkutano huu umeweka Rekodi kadhaa. Bunge limejijengea heshima zaidi kwa kuhakikisha Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini imeongezwa ili kutatua tatizo la Umeme, Bajeti ya Wizara ya Usafiri iliongezwa ili kufufua Reli na Usafiri wa Anga na hasa Shirika la ATCL na Azimio la Bunge la kuongeza muda wa Shirika la CHC liliboreshwa na kuwezesha shughuli ya kufuatilia zoezi la ubinafsishaji kuwa na ufanisi. Nakupongeza sana mheshimiwa Spika kwa uongozi wako mahiri. Ninaamini wale waliokuwa wanahojihoji uwezo wako sasa watafikiri mara mbili. Mungu akupe nguvu zaidi ili uendelee kuwa na msimamo wa kulinda hadhi na heshima ya Bunge letu.Mheshimiwa Spika, Pamoja na kuwapongeza Wabunge wote kwa mafanikio hayo, napenda kutoa pongezi maalumu kwa Wabunge Mhe. Januari Makamba na Mheshimiwa Peter Serukamba kama Wenyeviti wa Kamati zilizopelekea uboreshaji huu na Mhe. John Mnyika na Mheshimiwa Muhonga Ruhwanya kama Mawaziri vivuli ambao changamoto zao zilizaa matunda. Napenda kurudia ninalosema kila siku, Vijana hawa ni hazina kubwa kwa Taifa letu. Bila kujali itikadi za vyama vyetu, vijana hawa wamelitendea haki Taifa letu. Nawapongeza sana.Mheshimiwa Spika, Baada ya maelezo hayo ya utangulizi naomba sasa nipitie baadhi ya maeneo yaliyo chini ya Wizara ya Fedha na Uchumi na kutoa maoni ya kambi ya Upinzani.UBINAFSISHAJI WA MASHIRIKA YA UMMA TANZANIAMheshimiwa Spika, Wizara ya Fedha na Uchumi kupitia Shirika la CHC inasimamia sera ya ubinafsishaji wa Mashirika ya Umma. Sera ya ubinafsishaji iliyoanza kutekelezwa mwanzoni mwa miaka ya tisini pamoja na kuleta baadhi ya manufaa imekuwa ikilalamikiwa sana siku hadi siku na wananchi. Malalamiko mengi ni kwamba nchi yetu imetekeleza zoezi la ubinafsishaji vibaya, liligubikwa na Rushwa (briberization as termed by Joseph Stiglitz) na uuzaji holela wa mali za yaliyokuwa mashirika ya Umma kama majengo nk.Mheshimiwa Spika, Mashirika ya Umma mia tatu sitini (360) yalibainishwa (specified) kwa ajili ya ubinafsishaji mpaka Disemba 2009.Kati ya Mashirika hayo, Mia Tatu Thelathini na Moja (331)yamebinafsishwa na ishirini na tisa (29) yalikuwa katika hatua mbalimbali za kubinafsishwa. Mpaka muda huo pato la serikali kutokana na ubinafsishaji huo yalikuwa Shilingi billion 482. Hii maana yake ni wastani wa shilingi 1.5 bilioni kwa kila Shirika lililouzwa! Mheshimiwa Spika, ni takribani miaka ishirini sasa toka tuanze kutekeleza sera hiyo na mashirika mengi yakiwa yamebinafsishwa, na hivyo ni wakati mwafaka wa kufanya tathmini ya kina juu ya utekelezaji wa Sera ya Ubinafsishaji wa Mashirika ya Umma (Public Inquiry on Privatisation). Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali kuanza mchakato wa kufanya uchunguzi huu ili tuone mafanikio na matatizo ya sera hii kwa ajili ya kujifunza na pale inapowezekana kurekebisha makosa. Wananchi washirikishwe vya kutosha katika mchakato huu.Mheshimiwa Spika, utafiti uliofanywa mwaka 2007 na asasi ya AFRODAD (African Forum and Network on debt and development) ukitolea mfano wa Tanzania katika sera ya ubinafsishaji uligundua kuwa pamoja na matarajio ya serikali kuhusu ubinafsishaji bado haukuwashirikisha wananchi hata katika hatua ya kuwapa taarifa na kuwaelimisha kuhusu sera hiyo na pia wananchi wamekuwa na malalamiko ya mara kwa mara kuwa hawanufaiki na mafanikio ambayo serikali imekuwa ikiyatoa.Mheshimiwa Spika, zaidi ya hayo ubinafsishaji pamoja na uwekezaji kwa ujumla haujaweza kutanzua tatizo la ajira ambalo linawakumba vijana wengi huku kukiwa na malalamiko kuwa wabia hao wa maendeleo huwaajiri wageni wengi zaidi kinyume na sheria kama ambavyo ilijadiliwa katika hotuba ya bajeti ya Wizara ya Kazi na Ajira.Mheshimiwa Spika, pia mashirika mengi ya umma yaliyobinafsishwa wawekezaji wameshindwa kutekeleza mambo/masharti waliyokubaliana na serikali hii ikiwa ni pamoja na wao kufanya mambo mengine kinyume na makubaliano kwa mfano Kiwanda cha Urafiki Dar es Salaam ambapo mwekezaji kutoka China amekuwa akiuza baadhi ya mashine kama vyuma chakavu, Kiwanda cha kuzalisha mbao cha Tembo Chip board cha Mkumbara mkoani Tanga ambapo mwekezaji alianza kwa kuuza miti ya msitu bila kuendesha kiwanda na hivyo kusababisha mgogoro na wananchi baada ya kuvamia maeneo yao.Mheshimiwa Spika, hiyo ni baadhi ya mifano ambayo inaonyesha kushindwa kwa mashirika/taasisi zilizobinafsishwa hii ikiwa ni pamoja na baadhi ya wawekezaji/wabia kutoa taarifa za uongo/ zisizo sahihi juu ya uwezo wao kufufua na kuendesha taasisi zilizobinafsishwa kwao mathalani kiwanda cha kusindika nyama kilichopo Kawe Dar es Salaama cha Tanganyika Packers.Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani Bungeni inapendekeza, kama ilivyoelezwa hapo juu, kufanyika kwa uchunguzi maalumu kuhusu Utekelezaji wa sera ya Ubinafsishaji (Public Inquiry on privatisation).Mheshimiwa Spika, Mwezi Juni mwaka huu na katika Mkutano huu wa Nne, Bunge lako tukufu lilijadili na kupitisha Azimio la kuongeza muda wa Shirika la CHC baada ya kufanyia marekebisho Azimio lililoletwa na Serikali ambapo awali kulikuwa na nia ya kuunganisha Shirika hili na Ofisi ya Msajili wa Hazina. Uamuzi huu wa Bunge haukuwafurahisha baadhi ya watendaji wa Serikali. Hivi sasa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la CHC (kaimu) ndugu Methusela Mbajo amesimamishwa kazi kwa tuhuma za majungu kutoka kwa wanaojiita Wafanyakazi wa CHC. Tuhuma hizo ziliwasilishwa kwangu binafsi na kunakiliwa kwa Waziri Mkuu na Waziri wa Fedha. Kufuatia maagizo ya Waziri wa Fedha kwa Bodi ya Wakurugenzi wa CHC Mtanzania huyu kasimamishwa kazi na kwamba CAG ameombwa kuchunguza majungu yale kutoka kwa wanaojiita wafanyakazi wa Shirika la CHC.Mheshimiwa Spika, nilikuandikia barua kukuomba hatua mwafaka zichukuliwe kwani suala hili bado lipo katika mamlaka ya Bunge na kwa mujibu wa Sheria ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge, sheria namba 3 ya mwaka 1988 Maamuzi haya ya Waziri wa Fedha ni sawa na ‘contempt of Parliament’. Barua ya wanaojiita wafanyakazi wa CHC (niliyoandikiwa tarehe 24 Juni 2011, siku moja baada ya kupitishwa kwa Azimio la Bunge na kutuhumu Mawaziri kuwa walishawishiwa), Barua ya maelekezo ya Serikali (iliyosainiwa na ndugu Mmbaga, Msaidizi wa Waziri Mkuu ya tarehe 10 Agosti 2011) na Barua yangu ya majibu (18 Agosti 2011) niliyowapa zimewasilishwa mezani kwako kama vithibitsho na kwa hatua zaidi utakazoona inafaa.Mheshimiwa Spika, Bunge hili linapaswa kusimama imara kuzuia kuingiliwa kwa mamlaka yake na tawi la Utendaji. Mijadala ndani ya Bunge inalindwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tusipokuwa makini Bunge litaendelea kudharauliwa na hivyo kushindwa kufanya kazi yake ya kuwawakilisha wananchi, kutunga sheria na kuisimamia Serikali ipasavyo. Ninataka maelezo ya kina ya Waziri wa Fedha kwa nini amechukua hatua nilizoeleza hapo juu ilhali akijua jambo hili lipo mezani kwa Spika wa Bunge.USIMAMIZI WA MASHIRIKA YA UMMAMheshimiwa Spika, ukiangalia katika Fungu la 50, kasma 229900 (Other operating expenses) katika kasma ndogo ya 229931: (contigent liabilities) Serikali imetenga shilingi bilioni 35.7 zikiwa fedha za kulipia madeni na mahitaji ya dharura kwa Mashirika ya Umma. Vile vile katika fungu 21, kasma 229929, Serikali imetenga shilingi bilioni 26.4 kwa ajili ya kulipa fidia kwa mikataba mbalimbali ambayo serikali imeingia. Kwa vyovyote vile miongoni mwa mikataba hiyo ni pamoja ule wa Shirika la Reli na mingineyo. Hii inaonyesha kuwa Serikali inatumia fedha nyingi sana kwa ajili ya Mashirika ya Umma. Mheshimiwa Spika, Kwa hiyo basi usimamizi thabiti unatakiwa ili kulinda fedha hizi za Umma zinazotumika kwenye Mashirika ya Umma. Kinyume chake kumekuwa na usimamizi mbovu sana na unaopelekea Taifa kupoteza fedha nyingi sana kutokana na ubadhirifu katika Mashirika ya Umma. Hii ni kweli kwa Mashirika ambayo Serikali ina hisa nyingi (majority) na hata kule ambapo Serikali ina hisa chache. Mheshimiwa Spika, Lipo tatizo la serikali kushindwa kusimamia vizuri hisa zake kwenye Taaisisi/Mashirika ambayo serikali ina hisa chini ya asilimia hamsini na moja (51%). Hisa hizi zinasimamiwa kwa niaba ya Taifa na Ofisi ya Msajili wa Hazina. Muundo wa Ofisi hii ulikuwa unakwaza kazi ya kusimamia Mashirika ya Umma na hivyo Bunge lilifanya mabadiliko ya Sheria mwaka 2010 kuimarisha Ofisi ya Msajili wa Hazina. Mpaka leo mapendekezo ya muundo wa Utumishi hayajapata kibali ili Ofisi ifanye kazi ipasavyo. Tunaitaka Serikali ieleze ni lini kibali hiki kitatoka ili kuwezesha usimamizi bora wa Mashirika ya Umma.Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Msajili wa Hazina (TR) imekuwa dhaifu mno katika kusimamia mali za serikali Katika Mashirika. Mifano miwili ya namna hisa za Serikali zilivyouzwa itasaidia kuonyesha hali hii. Kampuni ya Oryx ilikuwa inamilikiwa na Serikali kwa asilimia hamsini mpaka mwaka 2004. Mwaka 2004, kupitia ofisi ya TR serikali iliuza hisa zake ambazo ni asilimia 50% kwa bei ya kutupa kwa thamani ya dola 2.5 milioni. Hivi sasa Oryx ni moja ya Kampuni inayofanya vizuri sana katika sekta ya Mafuta lakini hatuna umiliki tena na pesa kiduchu tulizopata zimekwishatumika!Mheshimiwa Spika, pia serikali ilikuwa na hisa katika kampuni ya simu za mkononi ya Mobitel ambayo kwa sasa inajulikana kama “tigo”. Katika hatua ya kushangaza na haina maelezo kabisa Serikali imeuza hisa zake asilimia kumi na sita (16%) kwa thamani ya dola 1.3 milioni mwaka 2006 na kwa sasa kampuni hiyo ni ya kigeni kwa asilimia mia moja jambo ambalo ni kunyume na sheria. Kampuni za Simu zinatakiwa kumilikiwa na Watanzania kwa sio chini ya Asilimia 35. Asilimia 16 ya hisa Tigo leo thamani yake ni zaidi ya kumi ya bei tuliyouza mwaka 2006.Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Msajili wa Hazina inashikilia hisa ‘minority’ za Serikali kwenye Kampuni zaidi ya 24 hapa nchini. Baadhi ya Kampuni hizi wala hazina wajumbe wa Bodi wanaowakilisha Serikali au Wajumbe ni maafisa wale wale wa Ofisi ya Msajili wa Hazina ambao hufikia hata kuhudhuria Bodi tatu mpaka tano kwa siku. Matokeo yake hawawezi kutoa maamuzi ya kibiashara na hivyo kutolinda Mali za Taifa vizuri. Mfano wa hivi majuzi ni sakata la uuzwaji wa Shirika la UDA ambapo Msajili wa Hazina hakuwahi kuteua Mjumbe wa Bodi kwa zaidi ya miaka 3 na ndio chanzo cha mgogoro wote wa Shirika la UDA unaoendelea hivi sasa.Mheshimiwa Spika, baada ya tathmini hiyo fupi, kambi ya upinzani tunapendekeza mambo yafuatayo ambayo tunaitaka serikali kuzingatia ili kuboresha usimamizi wa Mashirika ya Umma ili kuleta tija zaidi kama ifuatavyo;v Ofisi ya Msajili wa hazina (TR) ifumuliwe na ianzishwe ofisi ya Mashirika ya Umma ambayo itakuwa ni kama Wakala wa Serikali chini ya Wizara ya Fedha ikiwa ni chombo huru chenye kusimamia Mashirika yote ya Umma (Office of Public Enterprises – OPE)). Ofisi hii itasimamia Mashirika yote ya Umma ambayo Serikali ina hisa zaidi ya asilimia 51 (majority). Mashirika ambayo Serikali inamiliki hisa chini ya asilimia 51 (minority) yaundiwe Kampuni Hodhi (holding company) ambayo itasimamiwa na OPE ambayo sasa ni Ofisi ya Msajili wa Hazina. Hata hivyo ili kupunguza mlolongo wa Mashirika, Shirika la CHC linaweza kuongezewa majukumu na kuwa ‘National Holding Company’ na hivyo kumilikishwa hisa hizi na kuzifanyia biashara kwa tija.v Mashirika yaliyo katika Sekta nyeti kwa umma yasibinafsishwe tena na badala yake yaendelee kumilikiwa na Serikali kwa kuweka Menejimenti mahiri na kuwa na lengo la kuorodhesha hisa zao katika Soko la Hisa la Dar es Salaam ili kumilikisha wananchi na kuweka uwazi katika uendeshaji. Lazima kufikiria upya zoezi la kubinafsisha Mashirika yaliyo katika Sekta nyeti kwa wananchi kama TANESCO. Sekeseke la juzi la Mafuta liwe fundisho kwetu katika kuangalia sera za Uliberali zilizokuwa zinapigiwa debe na Mashirika ya Fedha ya kimataifa.OFISI YA TAIFA YA TAKWIMU TANZANIAMheshimiwa Spika, Chombo rasmi kinachojihusisha na kutafuta, kuandaa na kusambaza takwimu hapa Tanzania ni Ofisi ya Taifa ya Takwimu (Nation Bureau of Statistics). Ofisi ya Taifa ya Takwimu ni wakala wa serikali chini ya Wizara ya Fedha, na iliundwa kupitia Sheria ya Wakala wa Serikali Na. 30 ya mwaka 1997. Mheshimiwa Spika, Katika kupanga mipango ya maendeleo na kuandaa sera mbalimbali za nchi husika, upatikanaji wa takwimu rasmi zinazotokana na Kanuni na Mbinu za Kitaalamu iliyowekwa na Ofisi ya Takwimu ya Umoja wa Mataifa (United Nations Statistical Division) ni muhimu. Takwimu zote zilizo rasmi duniani hutolewa na Ofisi za Takwimu za nchi husika kupitia Sheria za Takwimu za nchi mbali mbali. Mapendekezo ya kuboresha utendaji wa Ofisi ya Takwimu.Mheshimiwa Spika, Kambi rasmi ya upinzani inapendekeza yafuatayo ili kuboresha utendaji wa Ofisi hii ya Takwimu ya Taifa; i. Taarifa mbali mbali za takwimu zitolewe kwa uwazi ikiwahusisha wanahabari na wataalamu wa kada mbalimbali kama vile wachumi na kuwepo mjadala wa wazi kuhusiana na taarifa hiyo. Kwa mfano taarifa za Robo mwaka kuhusu ukuaji wa uchumi ziwe zinatolewa mbele ya Waandishi wa Habari na kurushwa ‘live’ na Televisheni ya Taifa. Hii itasaidia sana kupasha habari za kiuchumi lakini pia kuwezesha wataalamu na Wanahabari za Uchumi kuwa hoji maswali Maafisa wa NBS. Hii hufanyika katika nchi kama za Uingereza na husaidia sana katika kutunga sera. ii. Kuwa na uhisiano wa moja kwa moja wa Ofisi ya Takwimu ya Taifa na ngazi za mikoa, halmashauri za wilaya, kata na vijiji kurahisisha upatikanaji wa takwimu ili zisaidie katika kupanga mipango ya maendeleo.MAMLAKA YA MAPATO TANZANIA (TRA)Mheshimiwa Spika, kambi ya upinzani tunasikitishwa na pungufu ya makusanyo madogo ya kodi na hii ni kutokana na serikali kushindwa kusikiliza maoni ya kambi ya upinzani tunayotoa kila mwaka ambapo tumekuwa tukitoa vyanzo mbadala vya kuongeza mapato.Mheshimiwa Spika, bei ya dhahabu katika soko la dunia imeongezeka mara dufu. Hadi kufikia tarehe 23/08/2011 bei ya dhahabu kwa mujibu wa mtandao wa gold-alert ilikuwa dola za kimarekani 1902.61 (kutokana na taarifa ya gazeti la Financial Times (ft.com) la leo 25 Agosti 2011, bei imeshuka mpaka dola 1760 kwa wakia moja). Hili ni ongezeko kubwa sana na hivyo kuna kila haja ya kuanghalia namna ya kurekebisha kodi kwenye rasilimali hiyo muhimu hapa nchini ili Taifa lifaidike na kupanda kwa bei ya dhahabu.Mheshimiwa Spika, kambi ya upinzani tunaitaka Mamlaka ya Mapato Tanzania kuanza mara moja kufanya utafiti wa namna bora ya kutoza kodi ya faida kwenye dhahabu (windfall tax) ili kuongeza mapato ya serikali kwa sababu wawekezaji wanapata faida mara dufu kwa sasa kwa sababu ya ongezeko hilo la bei. Matokeo ya tafiti hii yaletwe Bungeni kama muswada wa Sheria ili kurekebisha sheria za kodi na kutoza aina hii mpya ya kodi. Mheshimiwa Spika, Tunapendekeza, kwa kuwa Gharama ya kuzalisha wakia moja ya Dhahabu hapa nchini ni wastani wa dola za marekani 650, basi bei ya dhahabu ikiwa ya kati ya dola 1000 – 1300, mrahaba uwe mara mbili ya unaotozwa sasa, ikiwa kati ya dola 1301 – 1600 mrahaba uwe mara tatu ya unaotozwa sasa na ikiwa zaidi ya 1601 mrahaba uwe mara tano ya ule unaotozwa sasa. Kwa mfumo huu Taifa litafaidika na kupanda kwa Bei ya dhahabu katika soko la Dunia na pale ambapo bei zitashuka wawekezaji watalipa mrahaba wa kawaida. Mheshimiwa Spika, iwapo mfumo huu wa kodi katika madini ungekuwa unatumika sasa na ambapo Bei ya dhahabu imefikia zaidi ya dola 1900 kwa wakia, na Taifa letu linazalisha takribani Tani 60 ya dhahabu kwa mwaka, Serikali ingekusanya takribani shilingi 450 bilioni kama mrahaba. Hii ingetuwezesha hata kutokopa kwa ajili ya umeme wa dharura kama tunavyoelekea kufanya sasa. DENI LA TAIFAMheshmiwa Spika, kambi ya upinzani tunatambua kuwa nchi nyingi duniani zinakopa ili kuboresha huduma na miradi mbalimbali ya kimaendeleo na pia kuendesha shughuli za serikali pia. Katika hali isiyokuwa ya kawaida deni la taifa limeongezeka kwa kasi sana na hali hii sio kuachwa hivi hivi tu kwa sababu watakaoumia watanzania.Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Mdhibiti na Mkaguzi wa hesabu za serikali, deni la taifa liliongezeka kwa asilimia 38 kutoka trilioni 7.6 mwaka 2008 mpaka Tshs 10.5 trilioni mwaka 2009/2010, hadi kufikia mwisho wa mwezi Aprili 2011 kwa mujibu wa tamko la hali ya kifedha la Benki Kuu ya Tanzania la Juni 2011, deni la taifa lilikuwa dola za kimarekani milioni 11,455.4 sawa na shilingi trilioni 17.1 ambapo asilimia 80 ya deni hilo ni deni la nje.Mheshimiwa Spika, pamoja na umuhimu wa kukopa kama ambavyo mataifa mengine hufanya hivyo, kwetu sisi hii ni kasi kubwa mno ukilinganisha na ukuaji wa uchumi wa chi yetu kwa sababu ukopaji unategemea uwezo wa kulipa pia. Hii itasababisha mzigo huu wa madeni kubebwa na kizazi cha sasa na kijacho. Ukilinganisha na nchi nyingine za Afrika Mashariki, Tanzania bado ina viwango vidogo vya mikopo kama sehemu ya Pato la Taifa (debt/GDP ratio). Hata hivyo, wakati wenzetu wanakopa ili kuongeza uzalishaji (capital investments), sisi tunakopa kwa matumizi ya kawaida. Kambi ya Upinzani inapendekeza kuwepo kwa namna bora zaidi ya kuamua kuhusu mikopo ambayo Taifa linaingia ili kuhakikisha inaelekezwa katika uzalishaji mali.MIFUKO YA HIFADHI ZA JAMIIMheshimiwa Spika, Bunge lilipitisha sheria ya mamlaka ya Kudhibiti Mifuko yote ya hifadhi za jamii mwaka 2008 kwa lengo la kuangalia ni kwa namna gani mifuko hiyo inavyofanya kwa kuratibiwa vizuri na pia uwekezaji kwa kutumia fedha za wanachama wake unafanyika kwa vigezo vilivyowekwa. Kambi ya Upinzani inapongeza juhudi zinazoendelea za kuimarisha taasisi ya SSRA ili kuweza kusimamia Mifuko hii ya Umma vizuri na kuweka mazingira ya mifuko binafsi ya pensheni kuanzishwa.Mheshimiwa Spika, hivi sasa kuna mifuko mitano ya hifadhi ya jamii nchini yenye jumla ya wanachama 1,073,441. Kati ya hao Shirika la NSSF ilna wanachama 506,218 (47%), Shirika la PSPF lina wanachama 289,046 (27%), Shirika la PPF lina wanachama 160,068 (15%), Shirika la LAPF lina wanachama 73,833 (7%) na Shirika la GEPF ambalo lina wanachama 35,279 (4%). Idadi hii ya wanachama katika Mifuko yote ni sawa na asilimia 2.5 ya idadi ya watu waliopo nchini na ni asilimia 4.7 ya nguvu kazi yote iliyo katika sekta rasmi ya ajira. Hii inaonyesha kwamba watu wengi sana hawana mfumo wa hifadhi ya jamii (social security) licha ya kukua kwa kasi kwa watu wa Daraja la kati. Inakadiriwa kuwa asilimia 12 ya Watanzania ni daraja la kati kwa kipato.Mheshimiwa Spika, Kutokana na kuwa na uendeshwaji tofauti wa mifuko hiyo, kila mfuko umewekeza katika miradi mbalimbali kulingana na sera za uendeshaji wake. Mifuko hii imewekeza katika vitega uchumi vyenye thamani ya shilingi trilioni 2.8, ambayo ni takribani asilimia 8.7 ya Pato la Taifa kwa bei za sasa. NSSF inaongoza kwa kuwa na uwekezaji wenye thamani ya shilingi trilioni 1.03 (38%), PSPF inafuatiwa kwa kufanya uwekezaji wenye thamani ya shilingi bilioni 751 (27%), PPF uwekezaji wenye thamani ya shilingi bilioni 670 (24%), LAPF shilingi bilioni 206 (7%) na GEPF shilingi bilioni 82 (3%). Mheshimiwa Spika, Huu ni uwekezaji mkubwa sana na hii inadhihirisha ni kwa kiasi gani Tanzania ina mitaji ya kuweza kujiletea maendeleo yake. Narejea kuipongeza mifuko yote kwa uwekezaji wao katika ujenzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Chuo Kikuu cha Nelson Mandela Arusha na hivi karibuni kwa mfuko wa NSSF kuamua kuwezeka katika kuzalisha Umeme na hivyo kuelekea kuliokoa Taifa na mgawo wa Umeme, kulinda ajira za viwandani, kuongeza uzalishaji na hivyo ajira mpya na wanachama wengi zaidi wa mifuko.Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inapendekeza kwa Mifuko ya PSPF na PPF kuangalia namna ya kuwekeza katika maeneo yanayochochea ukuaji wa uchumi na hivyo kuzalissha ajira na kupata wanachama zaidi. Maeneo kama uwekezaji kwenye Bandari na Reli yanapaswa kuangaliwa kwani kutokana na Jiografia ya nchi yetu ni maeneo yanayoweza kuzalisha faida kubwa sana. Tunaitaka Serikali ilieleze Bunge kuna mipango gani katika Mashirika haya (PSPF na PPF) kuangalia maeneo mapya ya uwekezaji katika miundombinu na hasa Bandari.Mheshimiwa Spika, Mifuko ya hifadhi ya jamii imewekeza katika miradi ya ujenzi wa nyumba nafuu kwa ajili ya wanachama wao na pia wanachi kwa ujumla. Tunasisitiza Miradi hii isiwe Dar es salaam na Mwanza tu bali ienee nchi nzima kama ambavyo mfuko wa PSPF umeanza. Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani Bungeni bado inasisitiza ushauri wake kuwa Mifuko yote ya Hifadhi ya Jamii ihamishiwe Wizara ya Kazi na Ajira kama Wizara inayohusika na ‘social security’. Hata Mdhibiti wa Mifuko (SSRA) yupo chini ya Wizara ya Kazi. Mheshimiwa Spika, Hali kadhalika, hakuna sababu ya kuwa na utitiri wa mifuko mingi kama ilivyo sasa. Ipunguzwe na kubakia na mifuko miwili tu, mmoja wa wafanyakazi walio katika sekta binafsi na sekta isiyo rasmi na mwingine kwa wafanyakazi wa sekta ya umma. NSSF na PPF iunganishwe kuwa mfuko mmoja kwa ajili ya sekta binafsi na isiyo rasmi na PSPF, LAPF na GEPF iunganishwe na kushughulika na wafanyakazi wa Sekta ya Umma. HUDUMA KWA WASTAAFU KWA UJUMLAMheshimiwa Spika, pamoja na kuwa Mifuko ya hifadhi ya jamii inawekeza katika tekinolojia mbalimbali ili kuboresha utoaji wa huduma bado kuna changamoto. Inafahamika kuwa malipo bado yanachelewa kwa sababu mbalimbali katika ule mlolongo wa kutoa huduma hii. Kwa mfano hata pale hundi za mirathi zinapokuwa tayari na kufikishwa mahakamani kwa wajili ya kuwakabidhi warithi; wapo watendaji ambao huzifungia kabatini au kutafuta visingizio vyovyote vile ili mradi uwepo ugumu kwa mhusika kuzipata hundi hizo. Hii ni kero na ni chanzo cha rushwa. Mheshimiwa Spika, tatizo la kumbukumbu na michango ya watumishi nalo bado ni kero, japo juhudi za mapema kwa Waajiri na Mtumishi mmoja mmoja zinaweza kabisa kumaliza tatizo hili kama kutakuwa na mawasiliano kati ya Mtumishi/mwanachama, Mwajiri na Mfuko husika. Wananchi na wanachama kwa ujumla wawe karibu na Mifuko ili wapate taarifa zao mara kwa mara ili kama kuna mapungufu yeyote yarekebishwe mapema kabla ya muda wa kustaafu. Hii itapelekea malipo kufanyika haraka mara tu mwanachama anapostaafu.Madeni ya PSPF ya michango ya kabla ya Julai 1999Mheshimiwa Spika, watumishi wa umma wanaolipwa na Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSPF) wanapostaafu hulipwa mafao yao tangu kipindi walipoanza kazi, japo wao wameanza kuchangia kuanzia Julai 1999. Kipindi cha Julai 1999 kurudi nyuma ni deni ambalo serikali inapaswa kuulipa Mfuko huu wa PSPF. Kwa bahati mbaya deni hili lilikuwa halilipwi kwa kipindi chote tangu Mfuko uanzishwe hiyo Julai 1999, na limeendelea kukua na kuwa deni kubwa sana sasa; takriban Shs 3,380 Billioni. Mheshimiwa Spika, wizara ipongezwe kwanza; kwa kukubali kuwepo kwa deni hili na pili kwa kuanza kulipa sehemu ya deni husika (shs 716.6 Billioni). Jambo la msingi, Wizara iharakishe uhakiki wa sehemu kubwa ya deni lililosalia (shs 2,663.48 Billioni) ili ianze kulipa na kuuwezesha Mfuko kuwekeza katika maeneo yenye tija kwa nchi na Wanachama. Serikali ione suala hili kama suala nyeti maana tayari ‘acturials’ wameonyesha katika Hesabu za Mfuko wa PSPF kuwa mfuko huu ni ‘technically insolvent’. PPF Mheshimiwa Spika, Shirika la PPF limekuwa likifanya vizuri katika uwekezaji wake licha ya kuhudumia wastaafu wengi kuliko Mashirika mengine. Tunapenda kutoa pongezi za dhati kwa Shirika hili kwa kubuni na kutekeleza fao la Elimu. PPF ni mfuko pekee unaotoa fao la elimu kwa watoto wasiozidi miaka 4. Fao hili hutolewa endapo mwanachama atafariki dunia na amechangia miaka isiyopungua mitatu. Hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 2010 PPF ilikuwa imelipia zaidi ya watoto 1,105 kiasi cha Tshs 505,212,000. Ni vizuri mifuko mingine iangalie uwezekano wa kuanzisha fao hili ili kusaidia watoto wa nchi yetu ambao wazazi wao wameondoka duniani.Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani Bungeni inapenda kupata taarifa kuhusu agizo la kufanya ukaguzi maalumu kwa Shirika hili kuhusiana na malipo ya mafao kwa kada ya watumishi wa mikataba. Vile vile tumepata taarifa kuwa kuna wafanyakazi wa mfuko huu wamesimamishwa kazi kutokana na kutoa taarifa kuhusu malipo haya. Kambi ya Upinzani Bungeni inapenda kupata taarifa ya Serikali kuhusu suala hili.GEPFMheshimiwa Spika, Shirika la GEPF limeanza kuandikisha wanachama katika sekta isiyo rasmi. Zoezi hili limefikia wananchi wa kada ya chini kabisa na hivyo kuongeza idadi ya Watanzania walio katika mfumo wa Hifadhi ya Jamii. Hatua hii ni ya kupongeza sana. Kambi ya Upinzani inawataka GEPF wafike katika maeneo ya Wavuvi ili waweze kuchangia na kufaidika na mafao ya aina mbalimbali yanayotolewa.Nyongeza ya kiwango cha Pensheni ya kila mwezi kwa wastaafuMheshimiwa Spika, Serikali iliongeza viwango vya pensheni ilipwayo kwa wastaafu na kiwango cha chini kilipanda na kuwa shs 50,000/=. Wastaafu wanalalamika kuwa sasa unaanza mwaka wa tatu bado hawaioni nyongeza hiyo. Wakienda Wizarani wanaambiwa nendeni PSPF, wakienda PSPF wanaambiwa Wizara haijatoa hizo pesa ili PSPF iwaongezee/kuwalipa wastaafu hawa. Serikali itamke kuwa ni lini wastaafu hawa watalipwa? Kwa mujibu wa sheria iliyopo, nyongeza yeyote ya pensheni italipwa kutoka Mfuko mkuu wa serikali, kwa hiyo Wizara itoe majibu ni lini itamaliza kero hii, vinginevyo hili nalo ni deni ambalo litaendelea kukua na pengine kupeleke/kuanzisha mgogoro kama wa Wastaafu wa iliyokuwa Jumuia ya Afrika Mashariki ambao kila kukicha wazee wetu hawa wanaandama kwenda Hazina na Mahakamani.Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani imepata taarifa kwamba Wanajeshi wastaafu na hasa waliofikia ngazi ya Brigedia Jenerali wanalipwa pensheni ndogo sana. Inasemekana mwanajeshi aliyestaafu katika cheo ya Brigedia na kuendelea anapata pensheni ya shilingi 58,000 tu. Hiki ni kiasi kidogo sana kwa watu waliolitumia Jeshi na Taifa letu. Ninashauri kiwango hiki kiongezeke maradufu ili angalau wanajeshi wetu wiashi maisha yenye staha katika ustaafu.MASUALA YA JUMLAMheshimiwa Spika, kasma 229900, shilingi bilioni 100 zimetengwa kwa ajili ya dharura za kitaifa. Ni kweli kwamba kunaweza kuwa na dharura wakati wowote. Hata hivyo,shilingi bilioni 100 za dharura zimefikiwa kwa vigezo gani? Katika vitabu vya bajeti havionyeshi mwaka jana zilitengwa kiasi gani kwa dharura. Kambi ya Upinzani inataka maelezo ya Serikali.Mheshimiwa Spika, Ni vyema sasa tuanze utaratibu wa kupata takwimu ya jumla ya ruzuku ambazo Serikali inatoa kwa Mashirika na Taasisi za Umma. Takwimu zinakuwa ngumu kupatikana na hivyo kutoweza kudhibiti kikamilifu ruzuku hizi. Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali ieleze kwa mfano kwa mwaka huu wa fedha 2011/2012 Serikali itatoa ruzuku kiasi gani kwa taasisi na mashirika ya umma? Ni ofisi gani Hazina inayohusika na kugawa ruzuku hizi? Inawezekana ofisi ya Msajili wa Hazina badala ya kurekebishwa ikapewa jukumu hili la kugawa ruzuku.MIUNDO KANDAMIZI KWA WATUMISHI WA KADA YA UHASIBU SERIKALINIMheshimiwa Spika, kumekuwa na miundo kandamizi ya wahasibu Serikali kwa muda mrefu hivyo kusababisha wastaafu wakiwa mafukara kwa sababu ya mishahara midogo wanayolipwa. Muundo huo unaweka kigezo cha Mhasibu kupanda ngazi moja tu baada ya kuajiriwa katika maisha yake ya kazi iwapo hatapata shahada ya taaluma ya uhasibu (CPA). Huu ni unyanyasaji ambao hauwezi kuvumiliwa iwapo mhitimu wa shahada nyingine yeyote ile anapandishwa kila muda unapofika bila matatizo. Hiki ni kilio cha muda mrefu kwa wahasibu wote nchini. Taarifa zinazoletwa hapa Bungeni zinaandaliwa na wahasibu hawa ambao hawajatunukiwa shahada ya CPA, je inakuwaje taarifa hizo tunazikubali lakini waandaaji tunawawekea miundombinu kandamizi? Kambi ya Upinzani inamtaka Waziri alieleze Bunge ni wahasibu wangapi wana shahada ya CPA kwa sasa. Ni vyema utaratibu huu ukaangaliwa upya na kada hii ya uhasibu ikajiona kuwa mchango wake ni muhimu sana katika kulitumikia taifa hili. HITIMISHOMheshimiwa Spika, majukumu ya Wizara ya fedha ni makubwa na muhimu kwa nchi yetu. Majukumu haya yakisimamiwa vizuri tutaweza kupeleka mbele nchi yetu. Ninawataka watumishi wote wa Wizara ya Fedha na Taasisi zake wafanye kazi kwa bidii katika kusimamia uchumi wa nchi yetu. Uwajibikaji ndio suluhisho kubwa kwa matatizo ya rushwa, hongo, ubadhirifu na ufisadi. Kambi ya upinzani na Waziri kivuli wa Fedha na Uchumi atatupia jicho kali kuhakikisha kunakuwepo na uwajibikaji na kila mtumishi anajibu kwa matendo yake.Mheshimiwa Spika, Inasikitisha kwamba Taifa letu limepoteza miaka mitano ya mwanzo ya utawala wa Awamu ya nne kutokana na kelele nyingi za kisiasa. Kuna hatari kubwa sana kwamba miaka mitano ijayo inaweza pia kupotea. Ni lazima sote kwa pamoja bila kujali itikadi za vyama vyetu kuhakikisha tunafanyakazi kwa pamoja ili kuendeleza nchi yetu. Watawala watekeleze wajibu wao ipasavyo. Mheshimiwa Spika, ni muhimu sasa sote kama Taifa kuweka nguvu zetu zote na kuweka mazingira yanayochochea uwekezaji katika Gesi Asilia na Mafuta ufanikiwe. Tusipoteze muda huu kwani uwekezaji mkubwa katika Gesi Asilia utasaidia sana kupata umeme nafuu na wadau kwenye sekta wanasema Pato la Taifa litapanda kwa asilimia 40. Vile vile uwekezaji katika Mradi wa Mchuchuma na Liganga utaongeza Pato la Taifa kwa asilimia 25. Wizara ya Fedha na Uchumi iwe Wizara kiongozi kuhakikisha miradi hii haipotei kwani ikitekelezwa nchi yetu itakuwa na uchumi mkubwa zaidi kuliko nchi zote za Afrika Mashariki.Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani tutaendelea kuwa jicho la watanzania dhidi ya watawala, ninawataka Mawaziri Vivuli wote wafuatilie kwa karibu sana utendaji wa Mawziri katika maeneo yao ili kuhakikisha kuwa bajeti hii inatekelezwa kwa faida ya mwananchi wa kawaida. Uwaziri kivuli usiishie Bungeni wakati wa mikutano ya Bunge bali siku zote. Kila kauli inayotolewa na Waziri wa Serikali lazima Waziri Kivuli aitolee jibu na pale pa kupongeza papongezwe lakini pale pa kukosoa tukosoe kwa nguvu zetu zote. Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inasema ni lazima kuhakikisha Mawaziri wawe macho muda wote ili wale Mawaziri goi goi na wanaosinzia kila kukicha wapishe utumishi wa Umma na hivyo kuondoa vikwazo vya maendeleo ya nchi yetu. Pale ambapo Serikali hii ikianguka Mawaziri vivuli wawe tayari mara moja kuchukua majukumu ya Mawaziri wa Serikali na kuanza kazi bila kuchelewa.Mheshimiwa Spika, nawatakia wote sikukuu njema ya Eid el fitr,Kwa niaba ya Kambi ya Upinzani, naomba kuwasilisha.
..................................
Kabwe Zuberi Zitto (Mb)
Waziri Kivuli- Wizara ya Fedha.
25.08.2011
 

Forum statistics

Threads 1,353,877
Members 518,416
Posts 33,083,635
Top