R.B
JF-Expert Member
- May 10, 2012
- 6,296
- 2,575
A. UTANGULIZI
- Mheshimiwa Spika, kufuatia taarifa iliyowasilishwa leo hapa Bungeni na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu likubali kupokea, kujadili na kupitisha mpango na makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa Mwaka wa Fedha wa 2017/18.
- Mheshimiwa Spika, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia afya njema sisi Waheshimiwa Wabunge wote na hivyo kutuwezesha kuendelea na utekelezaji wa majukumu yetu ya kitaifa ndani na nje ya Bunge. Kwa uwezo wake Mwenyezi Mungu, Bunge limeendelea kutekeleza majukumu yake ya kikatiba likiwemo la kuisimamia na kuishauri Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
- Mheshimiwa Spika, nichukue fursa hii kuwapongeza kwa dhati viongozi wetu wa kitaifa kwa jinsi wanavyojituma katika kutatua matatizo na changamoto mbalimbali za Taifa letu na hatimaye kuwaletea wananchi maendeleo. Viongozi hao wameendelea kutoa miongozo ambayo kila mara imekuwa ikilenga kuwaondolea wananchi kero mbalimbali katika maeneo yao. Dhamira hii imedhihirika wazi kwa jinsi Serikali ya Awamu ya Tano inavyoshughulikia masuala yenye maslahi ya kitaifa yakiwemo ya vita dhidi ya rushwa, madawa ya kulevya, ubadhirifu wa mali za Umma, malipo hewa pamoja na kurudisha uwajibikaji Serikalini.
- Mheshimiwa Spika, kwa namna ya pekee nitumie fursa hii kumshukuru na kumpongeza Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali yake jinsi anavyochukua hatua za kusimamia na kulinda rasilimali za Taifa hasa madini.
- Mheshimiwa Spika, naomba pia kumpongeza Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kazi yake nzuri anayoendelea kuifanya tangu alipoteuliwa. Aidha, nampongeza Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb.) kwa jinsi anavyoendelea kusimamia kwa karibu shughuli za Serikali tangu Serikali ya Awamu ya Tano ilipoingia madarakani. Ni wazi kuwa Viongozi wetu hao wa kitaifa kwa kipindi kifupi walichokaa madarakani wamefanya kazi nzuri na kubwa kwa kutoa na kutekeleza miongozo makini ya kulisaidia Taifa letu. Tuwaombee wote kwa Mwenyezi Mungu ili waendelee na kasi hiyo ambayo imekuwa ni chachu ya mabadiliko katika nyanja mbalimbali na hatimaye nchi yetu iweze kupiga hatua za kimaendeleo kwa kasi kubwa zaidi.