Hotuba ya bajeti Nishati; Miradi ya Rufiji na gesi itaumiza nchi: Mnyika aonya

CHADEMA

JF-Expert Member
Apr 13, 2013
488
2,467
HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI KATIKA WIZARA YA NISHATI, MHESHIMIWA JOHN JOHN MNYIKA (MB), AKIWASILISHA BUNGENI MAONI YA KAMBI RASMI YA UPINZANI KUHUSU MAPITIO YA BAJETI KWA MWAKA WA FEDHA 2018/2019 PAMOJA NA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA KATIKA WIZARA HIYO, KWA MWAKA WA FEDHA 2019/2020
Inatolewa chini ya Kanuni ya 99(9) ya Kanuni za Kudumu za Bunge,
Toleo la Januari, 2016
UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema, kwa kunijalia uhaina kunipa nguvu na uwezo wa kusimama mbele ya Bunge lako tukufu ili kutoa maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya wizara Nishati kwa mwaka wa fedha 2019/2020.

Mheshimiwa Spika, Pili napenda kuwashukuru na kuwapongeza sana wabunge wote wa upinzani na viongozi wote wa CHADEMA kwa ujasiri wao wa kuendelea kuchapa kazi bila woga licha ya mazingira magumu ya kufanya siasa hapa nchini. Aidha, nawatia moyo wale wote waliokamatwa na kuwekwa kizuizini magerezani; walioumizwa na kujeruhiwa kwa sababu tu ya kutumia haki yao ya kikatiba ya kushiriki shughuli za kisiasa. Napenda kuwaambia wasikate tamaa kwani mateso wanayoyapata ni kielelezo cha ukombozi wa watanzania walio wengi.

Mheshimiwa Spika, kwa upekee kabisa napenda kuwashukuru wabunge na wadau mbalimbali ambao kwa namna moja au nyingine wamenisaidia katika kufanikisha hotuba hii, siwezi kuwataja wote lakini naomba kuwatambua na kuthamini mchango wa HakiRasiliamali, Asasi mbalimbali ndani na nje ya Nchi, wadau mbalimbali kwa nafasi zenu pamoja na wanataaluma mbalimbali mlionipatia michango yenu, Natambua haya yote ni kwa maslahi mapana ya Taifa na uzalendo wenu kwa Nchi yetu! Namshukuru Naibu Waziri Kivuli wa Nishati Mheshimiwa Jesca Kishoa (Mb) kwa ushirikiano wake katika maandalizi ya hotuba hii na majukumu mengine ya Wizara yetu ya Nishati. Kwa wote ambao sijawataja kwa majina lakini nyuma ya pazia mmekuwa nguzo yetu Nasema Asanteni na Mwenyezi Mungu awabariki!

Mheshimiwa Spika, Hii ni bajeti ya nne ya Serikali hii ya awamu ya tano ambapo imebaki bajeti moja tu ya mwaka wa fedha 2020/2021. Hata hivyo katika utaratibu wa mzunguko wa Bajeti za Serikali, Bajeti hii ni ya mwisho kwa serikali hii ya awamu ya Tano chini ya Chama Cha Mapinduzi kwa kuwa awamu ijayo itakuwa chini ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA. Hata hivyo, pamoja na kwamba imebaki bajeti ya takriban miaka miwili Serikali hii imalize muhula wake wa miaka mitano madarakani utekelezaji wa bajeti zilizotangulia umekuwa ni wa kusuasua jambo ambalo limeathiri sana sekta Nishati, hadi sasa hakuna mradi wowote uliokamilika kupunguza au kuhakikisha Tanzania kuna umeme wa uhakika.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa mara zote Serikali imeonesha kushindwa katika Sera zake, Sera Mbadala za Chadema ni kuhakikisha kunakuwepo na uzalishaji wa Nishati ya Uhakika na Endelevu, kuwepo na umakini na weledi katika usambazaji Nishati na Matumizi Endelevu ya Nishati.

Mheshimiwa Spika, Sera za Chadema zinatokana na ukweli kwamba CHADEMA tunatambua kuwa nishati ni muhimu kwa ajili ya maisha bora kwa wananchi na kwamba Nishati ni nyenzo muhimu ya uzalishaji katika sekta mbalimbali za uchumi. Kwa hiyo, ni muhimu kuhakikisha uwepo wa nishati ya uhakika kwa ajili ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi. CHADEMA inatambua kwamba Tanzania imejaliwa vyanzo vingi vya nishati ikiwa ni pamoja na umeme wa biomasi, gesi asilia, umeme wa nguvu za maji, Makaa ya mawe na vyanzo vya nishati jadidifu kama umeme unaotokana na jotoardhi(Geothermal) umeme wa nguvu ya upepo na umeme wa nguvu ya jua. Lakini pamoja na uwepo wa vyanzo vingi vya nishati ni sehemu ndogo sana ya vyanzo hivyo ambayo imekuwa inatumiwa na kuendelezwa ipasavyo kutokana na sera mbovu za serikali ya Chama Cha Mapinduzi.

Mheshimiwa Spika, ni kutokana na kupwaya huko kwa sera za Chama Cha Mapinduzi, ambazo hazitoi uhakika wa Nishati hapa nchini tangu uhuru hadi sasa, Chadema tunakuja na Sera mbadala ambapo tutahakikisha kuwa Nchi inakuwa na Nishati ya Uhakika, yenye gharama nafuu na endelevu na itakayokuwa inapatikana kwa urahisi katika sekta zote za uchumi. Kufikia lengo hili, CHADEMA tutahakikisha unafanyika utafiti wa kina kuhusu vyanzo mbalimbali vya nishati na hatimaye kutunga sera ya Taifa ya Nishati itakayoendana na Sera nyingine za kiuchumi na kijamii. Aidha ili kuhakikisha umeme unaozalishwa unatumika kwa tija na ufanisi, CHADEMA tutaweka mfumo wa ugatuaji katika uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme kwa kushirikiana na Sekta binafsi.
Mheshimiwa Spika, kutokana na Sera hii, wananchi watanufaika kutokana na uwepo wa teknolojia mpya na Nishati jadidifu gharama za matumizi ya nishati hiyo zitapungua na hivyo kuifanya jamii ya watu wengi hasa wanaoishi mbali na gridi ya Taifa au mbali na Miji kunufaika. Wananchi watanufaika pia kwa kuwa na umeme wa uhakika kwa matumizi ya majumbani na viwandani, kutokana na vyanzo vingi vya Nishati vilivyopo nchini na hivyo kuipelekea Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati. Kwa utangulizi huo, mheshimiwa Spika, Maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni yamezingatia matakwa ya sera mbadala baada ya sera za Chama Cha Mapinduzi na Serikali yake kushindwa kutatua kero za Nishati kwa watanzania kwa zaidi ya Miaka hamsini ya uhuru sasa. Aidha madhaifu, upungufu, ufisadi na uwezo mdogo wa Serikali kutekeleza miradi ambayo ingeondoa kero ya Nishati kwa watanzania ni dalili tosha kuonesha kwamba Sera za Serikali ya Chama Cha Mapinduzi zimefikia kikomo na hivyo watanzania wamejiandaa na wako tayari kwa Sera Mbadala.
MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA SHUGHULI ZA WIZARA YA NISHATI KWA MWAKA WA FEDHA 2018/2019.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2018/2019 Wizara ya Nishati ilikadiria kukusanya na kutumia shilingi 1,692,286,014,000 kati ya fedha hizo, fedha zilizopitishwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo ni shilingi 1,665,141,000,000 na shilingi 27,145,014,000 zilikuwa ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida. Hadi kufikia mwezi Disemba, 2018, Serikali ilitoa jumla ya kiasi cha shilingi bilioni 275.40 kwa ajili ya shughuli za Maendeleo.
Mheshimiwa Spika; Kambi Rasmi ya Upinzani inasisitiza kwamba uwezo wa serikali kutoa fedha za Miradi ya Maendeleo hauridhishi kutokana na Sera zilizopitwa na wakati za Serikali ya Chama Cha Mapinduzi, kwa Bajeti hii matatizo ya Nishati Tanzania yataishaje na wakati serikali iko taabani kifedha?
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2019/2020 Wizara inakadiria kutumia shilingi 2,142,793,309,000 ambapo kati ya makadirio hayo shilingi 2,116,454,000,000 ni kwa ajili ya fedha za maendeleo na shilingi 26,339,309,000 ni fedha kwa ajili ya matumizi ya kawaida kutokana na vyanzo vya ndani na nje ya nchi. Aidha wizara inatarajia kukusanya shilingi, 1,956,372,000,000 kutoka vyanzo vya ndani na shilingi 160,082,000,000 kutoka nje ya nchi. Hata hivyo takwimu za wizara zinaonesha kwamba makusanyo ya maduhuli yanayotarajiwa kukusanywa kwa mwaka wa fedha Fedha 2019/2020 ni bilioni 612,370,725,000 sawa na ongezeko la 55.5% kwa mwaka wa fedha 2018/2019.
SEKTA NDOGO YA UMEME.
Mheshimiwa Spika, Sekta ndogo ya umeme nchini inasimamiwa na Shirika la Umeme Nchini, TANESCO. Kama inavyofahamika Serikali kupitia TANESCO imekuwa kwa kipindi kirefu sasa ikitekeleza miradi miradi mbalimbali ya kuzalisha, kusafirisha na kusambaza umeme. Majukumu makubwa ya TANESCO ni kuzalisha/kununua, kusafirisha, kusambaza na kuuza umeme na ili kutekeleza majuku haya TANESCO inapaswa kuwekeza katika miradi mipya ya uzalishaji, usafirishaji, usambazaji na kufanya tafiti za vyanzo mbalimbali vya nishati ya umeme ikiwemo nguvu za maji, gesi asilia, makaa ya mawe, nishati jadidifu, kuendeleza na kuimarisha miundombinu ya usafirishaji wa umeme, kuendeleza na kuimarisha miundombinu ya usambazaji, uuzaji umeme na huduma kwa wateja, kufua na kuimarisha mitambo ya umeme inayomilikiwa na Shirika na kununua umeme kutoka kwa wazalishaji binafsi na nchi jirani.
Mheshimiwa Spika, kutokana na majukumu hayo ya shirika la umeme nchini, ni dhahiri kwamba kuzalisha ama kununua, kusafirisha, kusambaza na kuuza umeme ni majukumu ambayo shirika hili linayatekeleza na hivyo limezidiwa na mzigo huo. Kutokana na muktadha huo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inatachambua upungufu katika ufanisi wa kiutendaji na changamoto za Tanesco katika sekta hii ndogo ya umeme.
Shirika la umeme nchini TANESCO na mwenendo usioridhisha kifedha
Mheshimiwa Spika, Kwa miaka kadhaa, TANESCO imekuwa na mwenendo usioridhisha kwa kupata hasara mfululizo. Kwa mwaka wa fedha 2015/2016 hasara iliyopatikana ilikuwa Shilingi bilioni 346.40; na kwa hesabu za miezi 18 hadi mwaka wa fedha ulioishia Juni 2015, hasara ilikuwa Shilingi bilioni 124.46. na hadi kufikia mwa 2018 hasara ilikuwa imefikia shilingi bilioni 346. Mwenendo wa hasara umekuwa ukichangiwa na hali isiyoridhisha ya maji ya kuzalisha nguvu ya umeme pamoja na ongezeko la gharama za uzalishaji. Mfululizo wa hasara hizo una athari kubwa kwenye Mtaji wa Shirika, hivyo kulifanya kutokopesheka ili kukidhi mahitaji yake ya kifedha.

Mheshimiwa Spika, Kwa hesabu zilizoishia tarehe 30 Juni 2016, madai yameongezeka kwa asilimia 23, hadi Shilingi bilioni 958 kutoka Shilingi bilioni 738 zilizoripotiwa kwenye hesabu zilizoishia tarehe 30 Juni 2015. Kwa upande mwingine, thamani ya wadaiwa ilipungua hadi Shilingi bilioni 330.55 kwa hesabu zilizoishia tarehe 30 Juni 2016, kutoka Shilingi bilioni 440.66 zilizoripotiwa mwaka wa fedha ulioishia tarehe 30 Juni 2015.

Usimamizi wa kampuni binafsi za uzalishaji umeme na gharama za kuiuzia TANESCO

Mheshimiwa Spika, Shirika la umeme Tanzania, TANESCO katika jitihada za kuhakikisha kunakuwa na upatikanaji wa uhakika wa umeme nchini, shirika liliingia mikataba na makampuni binafsi yanayozalisha umeme kwa lengo la kuiuzia TANESCO. Aidha taarifa ambazo kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inazo ni kwamba, TANESCO inanunua umeme kwa bei ya wastani wa shilingi 544.65 kwa kila unit na kuuza kwa shilingi 279.35 na hivyo kulifanya shirika kupata hasara ya shilingi 265.3 kwa kila unit.
Mheshimiwa Spika, kabla ya kusitishwa kwa mkataba na kampuni ya Symbion, TANESCO ilikuwa inalipa jumla ya dola za Marekani milioni 16.36 kama capacity charge kwa makampuni yanayozalisha umeme wa dharura. Taarifa ambazo Kambi Rasmi ya Bunge lako Tukufu inazo zinaonesha kwamba Kwa sasa, Shirika linatumia Dola za Marekani milioni 9.75 kwa mwezi kununua umeme kutoka Aggreko, Songas na IPTL.

Mheshimiwa Spika, Bei za nishati ya umeme inayotozwa na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) zinadhibitiwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA) kila robo mwaka baada ya mapitio ya gharama halisi za uzalishaji. Aidha kwa mujibu wa taarifa ambazo Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inazo ni kuwa mapitio ya kila robo mwaka ya bei ya nishati ya umeme hayahusishi madeni yaliyojitokeza kabla ya kuanzishwa kwa utaratibu wa mapitio ya bei ya umeme ya robo mwaka. Hivyo, utaratibu huu Mheshimiwa Spika, hauiwezeshi TANESCO kulipa madeni yote inayodaiwa.
Mheshimiwa Spika, bei ya umeme inayopitishwa na EWURA haionyeshi gharama halisi zilizotumiwa na TANESCO jambo linaloathiri uwezo wa TANESCO katika kulipa madeni yanayolikabili Shirika.
Mheshimiwa Spika; Kambi Rasmi ya Bunge lako Tukufu inaishauri Serikali kupitia EWURA kuzipitia kwa umakini gharama za umeme ili kuhakikisha kuwa gharama zote za uzalishaji wa umeme zinahusishwa, ili hatimaye, kusaidia upatikanaji wa faida baada ya uwekezaji wenye lengo la kuboresha huduma na kuongeza matokeo chanya kwa TANESCO.
Mheshimiwa Spika, Kwenye Kampuni ya Umeme Tanzania (TANESCO) CAG alibaini kuwa, eneo la Ubungo Complex lilipewa Songas mwaka 2004 wakati Songas ilipoanza shughuli zake nchini Tanzania. TANESCO ilipatiwa hisa 10,000 katika kampuni ya Songas kama malipo kwa ajili ya Ubungo Complex; pia, Songas ilichukua yaliyokuwa madeni ya TANESCO yaliyotokana na ununuzi wa mitambo ya kuzalisha umeme kwa gesi pamoja na mitambo husika iliyopo Ubungo Complex. Hata hivyo, hakuna ushahidi unaoonesha kuwa Ubungo Complex pamoja na mali nyingine ilizopewa Songas Limited zilithaminishwa kabla uhamishaji haujafanyika.
Madeni ya Shirika la Umeme nchini TANESCO.
Mheshimiwa Spika, TANESCO inashindwa kukusanya madeni ambayo inapaswa kulipwa na hivyo kuzua maswali mengi ambayo hayana majibu. Taarifa ambazo Kambi Rasmi ya Upinzani inazo zinaonesha kwamba TANESCO inaidai Hospital ya Tumaini jumla ya Dola za Marekani Milioni 9.4 sawa zaidi ya shilingi bil 18 zilizotokana na madai ya kodi ya pango tangu mwaka 1998. Pamoja na kwamba mwaka 2016 TANESCO ilishinda kesi na mahakama ikaamua Hospital ya Tumaini kulipa fedha hizo na kuondoka kwenye Jengo la TANESCO lakini hadi mwaka jana Tanesco wenyewe walikuwa hawajachukua hatua zozote. Kutokana na taarifa hizo, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka majibu ya serikali iwapo Tanesco wameshalipwa fedha hizo na kama bado ni kwa nini wameshindwa kulipwa hizo fedha wakati wanajiendesha kwa hasara mwaka hadi mwaka.
Fidia ya ucheleweshaji wa malipo ya kampuni ya Pan African Energy yenye thamani ya dola za kimarekani milioni 10.43

Mheshimiwa Spika, Mkataba wa Usambazaji wa Gesi (Gas Supply Agreement) baina ya TANESCO na Kampuni ya Uzalishaji Gesi ya Pan African (PAET), unaeleza kuwa endapo kutatokea mgogoro wa kiasi chochote cha malipo, kiasi hicho kinatakiwa kuwekwa kwenye Akaunti ya Pamoja (Escrow Account) hadi pale mgogoro utakapotatuliwa.

Mheshimiwa Spika, Kinyume na hapo, fidia ya ucheleweshaji wa malipo itatozwa. Kutoka mwaka 2011 hadi 2016 TANESCO imekuwa na mgogoro dhidi ya baadhi ya malipo ya usambazaji wa gesi ya PAET yenye thamani ya dola za kimarekani milioni 6.48. Hadi tarehe 30 Juni 2016, TANESCO ilikuwa inadaiwa kiasi cha Dola za Kimarekani milioni 71.38 na PAET; Kuchelewa kulipa deni hilo kwa wakati kutapelekea TANESCO kulipa fidia ya ucheleweshaji kwa PAET yenye thamani ya Dola za Kimarekani Milioni 10.43.

Kesi zinazoliandama Shirika la umeme nchini-TANESCO
Mheshimiwa Spika, Mnamo mwezi Septemba 2010, TANESCO ilishtakiwa na Benki ya Standard Chartered ya Hong Kong (SCBHK) kulipa kiasi cha Dola za Kimarekani milioni 258.7 kilichotokana na madai ya malipo ya uzalishaji wa umeme pamoja na fidia ya kutolipa madai ya uzalishaji umeme na uharibifu uliosababishwa na TANESCO kutoilipa IPTL kwa wakati.

Mheshimiwa Spika, maamuzi ya mwisho yaliyotolewa tarehe 12 Septemba, 2016 yaliitaka TANESCO kuilipa SCBHK, ikijumuisha fidia ya kiasi cha Dola za Kimarekani 148.4, baada ya hukumu hiyo, TANESCO ilipinga maamuzi hayo kwa kukata rufaa Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Kibiashara (ICSID) kisha kuwasilisha utetezi wake tarehe 21 Agosti 2017, ambapo baadaye SCBHK iliwasilisha pingamizi juu ya utetezi huo wa TANESCO.

Mheshimiwa Spika, tangu kipindi hicho, TANESCO imekuwa ikitumia gharama kubwa za uendeshaji wa kesi hiyo, Shilingi bilioni 3.65 kwa mwaka wa fedha 2014/2015 na Shilingi bilioni 3.93 kwa mwaka wa fedha 2015/2016. Hata hivyo, suala hili litarejeshwa kwa mamlaka za kisheria za ndani ambapo utekelezaji wake kisheria utazingatia uwezo wa kulipa wa TANESCO. Licha ya kiasi kikubwa cha fedha zinazotumika kwenye kesi hiyo, hakuna uhakika wa kushinda.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka Serikali kutoa taarifa hapa Bungeni kuhusu kesi zote ambazo zinaendelea na zilizokamilika dhidi ya TANESCO na gharama ambazo shirika limeingia ikihusisha gharama ambazo zinatarajiwa kulipwa katika kesi ambazo TANESCO imeshindwa kama zipo ili umma wa watanzania wajue kwa kuwa zitalipwa kwa fedha za walipa kodi wa Tanzania.

Uunganishaji wa Huduma za Umeme

Mheshimiwa Spika, kumekua na malalamiko makubwa ya gharama za uunganishaji wa huduma za umeme pamoja na mlolongo wa uunganishaji kwa wateja ambao tayari wameshakamilisha taratibu za kuunganishiwa umeme. Ukiachana na gharama za uunganishaji wa umeme, bado kumekua na usumbufu wa uunganishaji wa wateja kwa wakati kwa visingizio mbalimbali wakati ambao wateja wa umeme huwa wameshakamilisha malipo na kufuata taratibu za uunganishaji wa huduma hiyo.


Mheshimiwa Spika, kutokana na malalamiko hayo; kwa mujibu wa ripoti ya Benki ya Dunia kuhusu Kufanya Biashara Tanzania mwaka 2019 (Doing Business 2019), Tanzania imeshika nafasi ya 83 kati ya nchi 190 duniani katika viwango vya wateja kuunganishiwa umeme (Getting Electricity)

Mheshimiwa Spika, mara baada ya mteja kupewa makadirio ya gharama za uunganishaji, mteja hutakiwa kufanya malipo kwa awamu iwapo ataomba kwa kuingia mkataba na TANESCO kwa kulipia gharama hizo kwa awamu. Na ikiwa TANESCO itashindwa kumuunganisha mteja kwa muda uliotakiwa, itawajibika kumtaarifu mteja mapema. Lakini kumekuwa na malalamiko makubwa ya watumiaji wa umeme juu ya kushindwa kwa TANESCO kufuata taratibu zilizowekwa .Aidha, kwa maeneo ya vijijini ambapo huduma za uunganishaji wa umeme zinafanywa chini ya REA kumekua na malalamiko ya mazingira ya uunganishaji wa huduma za umeme ambapo wananchi mbalimbali wamelalamikia kuwa wenye uwezo wa kutoa rushwa ndio ambao wanapewa kipaumbele cha kuunganishwa huduma hiyo.

Mheshimiwa Spika, ni dhahiri kuwa kushindwa kwa shirika la umeme nchini katika kusambazia na kuwaunganishia wananchi huduma ya umeme ni kutokana na kuelemewa kwa shirika hilo katika utoaji wa huduma hiyo. Kambi ya Upinzani inapendekeza kuwepo kwa soko huria kwa wasambazaji wa huduma ya umeme ili kupunguza urasimu wa uunganishaji na hivyo kulipatia faida shirika hilo ambalo sasa linakosa mapato kutokana na kuelemewa katika kuunganishia wateja wapya huduma ya umeme.

Kiwango kidogo cha kaya zilizounganishwa kwenye huduma ya umeme.

Mheshimiwa Spika; kwa mujibu wa ripoti ya utafiti wa hali ya upatikanaji wa umeme nchini, uliofanywa na Shirika la umeme Tanesco kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS, 2016), idadi ya kaya zilizounganishiwa huduma ya umeme ni asilimia 32.8 pekee kwa upande wa Tanzania bara.

Mheshimiwa Spika; kati ya asilimia hizo 32.8 ya kaya zilizounganishwa na huduma ya umeme, asilimia 65.3 ya kaya ni za mjini na asilimia 16.9 ya kaya ni za vijijini. Hii maana yake ni kuwa asilimia 83.1 ya kaya za vijijini hawana umeme wa kawaida. Wakati huo huo maeneo ya mijini ni asilimia 34.7 ya kaya ambazo hazijunganishwa na huduma ya umeme.

Mheshimiwa Spika; kuzalisha umeme mwingi, sio kigezo cha kuunganisha kaya zote na huduma ya umeme. Endapo asilimia 34.7 ya kaya katika maeneo ya mijini hawana huduma ya umeme, maana yake ni kuwa hawawezi kumudu gharama za kuunganishiwa umeme kwa kuwa na kipato duni au kutokuwa na kipato kabisa cha kumudu gharama hizo.

Mheshimiwa Spika; mwaka 2016, kwa kati ya kaya zote zilizounganishwa na huduma ya umeme, asilimia 31.5 ya kaya zililipia chini ya shilingi 100,000 ili kuunganishwa na huduma ya umeme, wakati asilimia 23.8 ya kaya zililipa kati ya shilingi 100,000 na 299,999 na asilimia 31.4 walilipa kati ya shilingi 300,000 na 499,999 kuunganishiwa umeme. Ukweli mchungu ni kuwa chini ya asilimia moja tu ndio walimudu kulipia zaidi ya shilingi milioni moja.

Mheshimiwa Spika; Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali, kufikiria tena gharama zake za kuunganisha umeme kwa kaya ambazo zina kipato duni au zisizo na kipato kabisa ili kaya hizo ziweze kumudu gharama za kuunganishiwa umeme kulingana na uwezo wa kaya husika.



Mikoa iliyoshika mkia kwa kaya zake kuunganishwa na umeme
Mheshimiwa Spika; Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kuanzisha operation maalumu kuhakikisha kuwa mikoa ambayo haikufanya vizuri katika kaya zilizounganishwa na huduma ya umeme zinaongeza juhudi katika hatua za makusudi kusaidia wananchi wa maeneo hayo kuunganishwa na huduma ya umeme.

Mheshimiwa Spika; Katika utafiti wa hali ya umeme (2016), mkoa wa Rukwa ndio ulishika mkia katika kaya zilizounganishwa na huduma ya umeme kwa kaya asilimia 8.7 pekee zilizounganishwa na umeme. Mikoa mingine ni pamoja na Simiyu
(11.5 %), Shinyanga (12.8 %), Geita (14.0 %), Songwe (15.9 %) na Kigoma (16.2 %).

Mheshimiwa Spika; mikoa iliyoongoza kwa kuwa na kaya nyingi zilizounganishwa na huduma ya umeme ni pamoja na Dar es Salaam (75.2 %), Njombe (50.5) na Kilimanjaro (42.6%)




Ufanisi mdogo wa TANESCO kufanya matengenezo ya mitambo ya kufua umeme
Mheshimiwa Spika, Ukaguzi wa ufanisi kwa shirika la TANESCO umefanyika na imebainika kuwa Shirika lina ufanisi duni wa kufanya matengenezo ya mitambo ya kuzalishia umeme. Matokeo ya ukaguzi huo yalichapishwa mwezi Machi, 2019.

Mheshimiwa Spika, ukaguzi huo ulitokana na ukweli kuwa kumekuweko mwenendo usioridhisha wa upatikanaji wa umeme nchini, kutokana na kukatika mara kwa mara kwa umeme katika mikoa yote iliyounganishwa kwenye gridi ya Taifa, kuwepo kwa mitambo na miundombinu ya umeme wa maji iliyopitwa na wakati, na msukumo mdogo wa kutoa kiapumbele kwenye matengenezo ya mitambo ya kuzalisha umeme.

Mheshimiwa Spika, ilibainika kuwa kwa mujibu wa mpango kazi wa TANESCO wa mwaka (2017/18-2020/21) katika kifungu cha 1.3.1.1(a) TANESCO inapaswa kufanya marekebisho na matengenezo ya mitambo yote ya kuzalisha umeme ili kuhakikisha kuwa muda wote mitambo inafanya kazi ya kuzalisha umeme na kuhakikisha kuwa vipuri vya matengenezo vinapatikana kila vinapohitajika.

Mheshimiwa Spika, katika ukaguzi ule ilibainika kuwa TANESCO haitekelezi ipasavyo mpango kazi wake kwenye eneno la matengenezo ya mitambo ya kufua umeme. Mfumo wa manunuzi kule ambako TANESCO inaendesha mitambo ya kufua umeme haukutekelezwa na TANESCO yenyewe haikujisumbua kufanya utafiti wa bei za soko la manunuzi ya vipuri.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kulieleza Bunge ni kwanini TANESCO imeshindwa kutekeleza mpango kazi wake iliyojiwekea yenyewe?

Mheshimiwa Spika, Pia Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali iwaeleze Watanzania imejipanga kiwango gani kuhakikisha kuwa manunuzi ya vipuri vya mitambo ya kufua umeme yanafanyika kwa wakati ili kuwaondolea Watanzania mateso na adha ya kukatika umeme mara kwa mara kwenye mikoa yote iliyounganishwa na gridi ya Taifa.


Zabuni 7 za matengenezo ya mitambo ya kufua umeme ambazo hazikutekelezwa kwa mwaka wa fedha 2017/18 kwa kukosa fedha

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa CAG, zipo zabuni takribani 7 zenye thamani ya shilingi bililioni 2.308 ambazo hazikutekelezwa na TANESCO kutokana na ufinyu wa Bajeti.

Mheshimiwa Spika, zabuni hizo ni pamoja na zabuni ya manunuzi ya vipuri na huduma ya gesi na mita za vituo ya Tender No. PA/001/17-18/HQ/G/29 for supply of
spare parts and services of gas pressure
reduction and metering station yenye thamani ya Shilingi Milioni 80; Zabuni ya vipuri vya mtambo wa kufua umeme yaani Tender No. PA/001/17-18/HQ/G/53 for supply of spare parts for caterpillar Generators yenye thamani ya shilingi milioni 420

Mheshimiwa Spika, zabuni nyingine zilizokwama kutokana na ukata wa TANESCO ni pamoja na zabuni ya kupata vifaa vya uendeshaji na matengenezo ya mitambo yaani Tender No. PA/001/17-18/HQ/G/55 for Supply of tools for operation & maintenance of
caterpillar power plants yenye thamani ya shilingi milioni 600; zabuni Tender No. PA/001/17-18/HQ/G/56 for supply of tools for Mirrlees Blackstone generators yenye thamani ya shilingi milioni 100. Zabuni nyinginezo zilizokwama ni pamoja na zabuni ya vifaa vya uendeshaji na matengenezo Tender No. PA/001/17-18/HQ/G/57 for supply of tools for operation &maintenance yenye thamani ya shilinigi bilioni 1, na zabuni ya Tender No. PA/001/17-18/HQ/G/61 for supply of steam cleaners for use in service of isolated
stations yenye thamani ya shilingi milioni 80 na zabuni ya saba ni yenye thamani ya shilingi milioni 28 Tender No. PA/001/2017-18/HQ/N/19 for Hiring of scaffolding and canvas covering of Gas Turbine No. 1 for Level B Maintenance”

Mheshimiwa Spika; shughuli zote za matengenezo ya mitambo ya kufua umeme kwa mwaka wa fedha 2017/18 hazikufanyika kutokana ha zabuni hizo kutotekelezwa.

Mheshimiwa Spika; Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka Watanzania wajue kuwa hali ya kifedha ya Shirika lao la umeme ni hoi bin taaban, na hivyo hali ya kukatika mara kwa mara kwa umeme itaendelea inatokana na sera mbovu za Serikali ya CCM kushindwa kusimamia uendeshwaji wa faida wa Shirika la umeme nchini kwa zaidi ya miaka 50 tangu nchi yetu ipate uhuru.



SHIRIKA LA UMEME NCHINI- TANESCO LIGAWANYWE

Mheshimiwa Spika, Kwa kipindi kirefu sasa TANESCO inajiendesha kwa hasara kutoka serikali ya awamu ya nne ambapo TANESCO ilikuwa ikipata hasara ya shil124. Takwimu zinaonesha kwamba baada ya kuingia madarakanai kwa serikali ya awamu ya Tano, shirika hili limekuwa likipata hasara kubwa zaidi ambapo hadi mwaka 2017 TANESCO ilipata hasara ya shilingi 346 sawa na ongezeko la bilioni 122.

Mheshimiwa Spika, hasara hiyo inatokana na upungufu wa maji ya uzalishaji umeme pamoja na gharama za uendeshaji wa shirika la umeme nchini. Pamoja na hayo madeni ya TANESCO yameongezeka kwa zaidi ya 23% kutoka shilingi bil 738 katika kipindi cha serikali ya awamu ya nne hadi kufikia shilingi shilingi bil 958 katika utawala wa serikali ya awamu ya Tano.

Mheshimiwa Spika, kwa nyakati mbalimbali Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni pamoja na wadau wengine tumependekeza mikakati mingi ya kulinusuru shirika la umeme nchini, kama ambavyo nchi nyingine Dunia zinafanya na moja ya mapendekezo ambayo hadi sasa tunapendekeza ni kuligawa shirika la umeme nchini na kupata mashirika mawili.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapendekeza kwamba shirika la umeme nchini TANESCO ligawanywe na yapatikane mashirika mawili. Shirika moja lishughulikie maswala ya uzalishaji wa umeme nchini wakati jukumu la kusambaza umeme nchini likiwa chini ya usimamizi wa shirika lingine. Mapendekezo haya mheshimiwa spika yatapunguza mzigo kwa TANESCO ambayo inahusika na majukumu ya kuzalisha/ kununua, kusafirisha kusambaza na kuuza umeme na kupelekea mzigo wa changamoto lukuki katika kuyatekeleza majukumu hayo.

MIRADI YA KUZALISHA UMEME
Ujenzi wa Mradi wa Rufiji (Rufiji Hydro Power Project)
Mheshimiwa spika, kwa mujibu wa taarifa za Serikali, lengo la kutekeleza mradi huu ni kuzalisha umeme wa jumla ya MW 2,100 kwa kutumia maji (hydro Power Plant) katika bonde la mto Rufiji ambako serikali inadai utekelezwaji wa mradi huu utakuwa ni kichocheo muhimu katika kuiwezesha Tanzania kufikia azma yake ya kuwa nchi ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025
Msimamo wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuhusu Mradi wa Rufiji (Rufiji Hydro Power Project)
Mheshimiwa Spika, Pamoja na kukubaliana na dhana ya kuzalisha umeme wa MW 2100 Kambi Rasmi Bungeni haikubaliani na namna utekelezwaji wa Ujenzi wa Mradi wa Rufiji Hydro Power Project unavyofanyika kwenye eneo la mradi lililoteuliwa na Serikali hivi sasa kwa sababu mbali ambazo nitazieleza hapa chini.
Gharama za kiuchumi za ujenzi wa Mradi huo kwa wakati mmoja
Mheshimiwa Spika, Kwa mwaka wa fedha 2018/2019 pekee, serikali kupitia hotuba ya waziri wa Nishati alieleza mpango wa serikali wa kujenga mradi huu katika aya ya 22 na 23 ya hotuba yake. Katika aya ya 23 Mheshimiwa Waziri wa Nishati alisema katika kipindi cha mwaka 2018/2019 serikali itaendelea kutekeleza mradi huu na shughuli zitakazofanyika ni pamoja na mosi, ujenzi wa kambi na Ofisi za wafanyakazi, pili, ujenzi wa bwawa yaani (main dam and spillways) na Tatu, ujenzi wa njia kuu za kupitishia maji (tunnels). Serikali ilisema fedha za ndani shilingi billion 700 zimetengwa katika mwaka wa fedha 2018/2019 kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa kazi hizo na kwamba utekelezaji wa shughuli za ujenzi wa mradi ulitarajiwa kuanza mwezi Julai, 2018 kwa mkandarasi kuanza kazi za awali kwa miezi mitatu na kufuatiwa na ujenzi wa miundombinu ya mradi unaotarajiwa kukamilika katika kipindi cha miezi 36.
Mheshimiwa spika, ukisoma taarifa ya wizara kuhusu utekelezaji wa mpango na bajeti ya wizara ya Nishati kwa kipindi cha mwaka 2018/2019 waziri anasema Wizara ya Fedha na Mipango imetenga cash jumla ya shilingi bilioni 984 ambazo taratibu za malipo zinaendelea ili zilipwe kwa mkandarasi wa Mradi wa Rufiji kabla ya mwishoni mwa mwezi April, 2019 kama malipo ya awali (advance payment) katika mradi huo
Mheshimiwa Spika, kwa maneno mengine ni kwamba sasa Serikali ilipanga kulipa fedha kwa ongezeko la shilingi bilioni 284 bila idhini ya Bunge lako tukufu kwa kazi zile zile za ujenzi wa kambi na Ofisi za wafanyakazi, ujenzi wa bwawa (main dam and spillways) na ujenzi wa njia kuu za kupitishia maji (tunnels) ambazo serikali ilisema Mkandarasi atatekeleza kwa miezi 36.
Mheshimiwa Spika, Serikali ya awamu ya Tano inaongoza kwa kukiuka taratibu na sheria za nchi. Kwenye mradi huu serikali imetoa wapi nyongeza ya Billioni 284 ambazo hazikupitishwa na Bunge hili? Kwamba Serikali sasa haizingatii matakwa ya Ibara ya 99 ya Katiba na kanuni ya 110 ya Kanuni za Bunge kuhusu makadirio ya matumizi ya nyongeza. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kuliambia Bunge hili, Billioni 284 zinazodaiwa kulipwa kwenye mradi zimetoka wapi, zimeongezeka kufanya shughuli gani na kwanini Serikali haikufuata matakwa ya makadirio ya matumizi ya nyongeza?
Muda na ongezeko la gharama halisi za Ujenzi wa Mradi wa umeme wa Bonde la Mto Rufiji
Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa Mkakati wa Mwongozo wa mabadiliko ya sekta ya usambazaji wa umeme nchini wa mwaka 2014 mpaka 2025 (Electricity Supply Industry Reform Strategy Roadmap), uwezo wa kuzalisha umeme unatakiwa kuongezeka kutoka Megawati 1,583 mwaka 2014 mpaka kufikia Megawati 10,000 mwaka 2025, ili kuiwezesha nchi kufikia uchumi wa kati sambamba na dira ya Maendeleo ya Taifa (Vision 2025).
Mheshimiwa Spika, mradi huu wa umeme wa mto Rufiji tunaambiwa na Serikali kuwa utakamilika ndani ya kipindi cha miezi 36 (sawa na miaka mitatu kwanzia sasa) na utaweza kuzalisha megawiti 2,100, kiasi ambacho ni asilimia 21.0 ya lengo la kufika kuwa nchi ya uchumi wa kipato cha kati. Wakati ujenzi unakamilika ndani ya miezi 36 kama tulivyoaminishwa na Serikali, itakuwa imesalia miaka miwili tu kufikia mwaka 2025, hivyo shabaha ya kufikisha uzalishaji wa megawi 10,000 ifikapo mwaka 2025 bado ni ndoto za mchana ambazo Serikali yetu inaendelea kuota.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo uchambuzi wa gharama za mradi wa umeme wa maji wa mto Rufiji, zilizofanywa na Odebrecht (2012) na iliyokuwa wizara ya Nishati na Madini (2016), walikadiria kuwa mradi utajengwa kwa vipindi vya miaka tisa awamu ya kwanza na miaka mitatu kwa awamu ya pili, hii inafanya idadi ya muda wa ujenzi kuongezeka kutoka miezi 36 ya awali hadi miaka 12 ambayo ni sawa na miezi 144.
Mheshimiwa Spika, Katika uchambuzi huo wa gharama za ujenzi wa mradi wa umeme wa mto Rufiji, miezi 36 ambayo imeripotiwa na Serikali, haitawezekana kuumaliza huu mradi hivyo kuufanya kuwa moja ya miradi mikubwa nchini itakayoigharimu nchi kiwango kikubwa cha fedha za walipa kodi kwa kuwa gharama za mwisho wa mradi zitakuwa kubwa kulikoni gharama ziliziainishwa wakati mradi unaanza!
Mheshimiwa Spika, katika uchambuzi huo, kunakadiriwa kuwa kwa aina ya miradi mikubwa kama huu, gharama za mradi zinakaridiwa kuongezeka kwa asilimia 30 (cost overruns) tangu hatua za ujenzi kuanza mpaka kuja kumalizika.
Mheshimiwa Spika, mwaka 2016 gharama za awali za mradi zilikadiriwa kufikia dola bilioni 3.738 sawa na Shilingi Trilioni 7.5. Endapo gharama za ujenzi wa mradi zitaongezeka (cost overruns) kwa asilimia 30% basi gharama za mradi wa Umeme wa Mto Rufiji zitaongezeka mpaka kufikia dola za marekani bilioni 9.852 ifikapo mwaka 2027, kiasi ambacho kama (exchange rate ya mwaka 2019 ikitumika, shs. 2330) basi kiasi hicho kitakuwa ni sawa na Shilingi Trilioni 22.95.
Mheshimiwa Spika, kupanga ni kuchangua, Shilingi Trilioni 22.95 ni sawa na asilimia 69.3 ya Bajeti nzima ya mwaka wa fedha 2019/20 inayopendekezwa na Serikali ya CCM. Kama bajeti kila mwaka wa fedha itaongezeka kwa asilimia 1.9 (maana mwaka wa fedha 2018/19, bajeti ilikuwa ni Shilingi Trilioni 32.48) na mwaka 2019/20 bajeti inayopendekezwa ni Shilingi Trilioni 33.10; basi gharama za ujenzi wa mradi wa umeme wa Mto Rufiji zikiwa Trilioni 22.95 ifakapo mwaka 2027 basi itakuwa ni sawa na asilimia 60 ya bajeti tarajiwa kwa mwaka wa fedha 2027/28, ambayo itakuwa ni Shilingi Trilioni 38.071

Mheshimiwa Spika, kwa uchambuzi huu uliofanywa na Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, basi mradi huu wa umeme wa mto Rufiji utakuwa ni aina nyingine za maamuzi yanayoenda kuiweka nchi katika hali mbaya ya kifedha na itakuwa ni hatua kubwa sana ya Serikali ya awamu ya tano, kuhujumu uchumi wa nchi kwa kuzingatia kuwa mradi unatekelezwa na mkandarasi kutoka nje na hivyo sehemu kubwa ya malipo itaondoka kutoka mzunguko wetu wa ndani wa kifedha.
Mheshimiwa Spika, nitoe wito tu kwa Serikali hii ya awamu ya tano; kufikiria upya na kutupa majibu ya namna gani wanajipanga na ugharimiaji wa gharama zinazokadiriwa kuongezeka katika ujenzi wa mradi huu kwa kuwa umekwisha anza kutekelezwa. Hatutaki ije Serikali ya awamu ya Sita, kwa vyoyote itakavyokuwa iwe ni Serikali itakayoongozwa na Chadema ama chama kingine chochote ilazimike kufanya maamuzi tofauti wakati nchi ikiwa tayari imeshaathirika kufuatia upungufu wa kiutendaji katika Serikali ya awamu ya tano.
Sababu za kimazingira
Mheshimiwa Spika, imesemwa mara nyingi na watalamu mbalimbali kwamba Mradi huu utaathiri Selous Game Reserve ambayo ni moja ya World Heritage Sites na hivyo ujenzi katika eneo hili utaathiri ecology ya Selous kwa kuathiri mazingira hatimaye yataathiri uchumi na maisha ya watu. Mradi huo utazuia tani milioni 16.6 za virutubisho vya Ardhi kwa mwaka, hivyo kusababisha mmomonyoko wa Ardhi kwenye delta ya Rufiji.
Mheshimiwa Spika, ipo pia hoja ya eneo ambalo mradi husika utatekelezwa ambalo ni kilomita za mraba 1,200. Eneo hili ni kubwa na litaufanya mradi kuwa ni bwawa kubwa kuliko yote Afrika Mashariki na kuzua hofu ya kukausha maziwa madogo madogo yote ya eneo la jirani, litaathiri utalii, kukomba rutuba yote ya ardhi ya eneo hilo hadi kwenye Delta ya Rufiji na hivyo kuua samaki na kuathiri uvuvi wa samaki kamba na kamba koche wanaotegemewa na watu zaidi ya laki mbili wa eneo hili.
Mheshimiwa Spika, Mradi huu unaotekelezwa, unatekelezwa kinyume cha mikataba ya kulinda urithi wa asili (World Heritage) ambayo Tanzania tumesaini. Kwa kutekeleza mradi huu tunaingia katika ongezeko la matumio mbalimbali ambayo Tanzania tunafanya yanayokiuka mikataba mbalimbali pamoja na sheria pia zikiwemo ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu, Lakini haishangazi kuona serikali ikikasirika iambiwapo kwamba wanaongoza kuvunja sheria na mikataba ambayo kama Taifa tulikubali kushirikiana na Dunia.

Mheshimiwa Spika, Sera za uchumi za Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) hazieleweki kabisa, awali mradi wa umeme wa Stiglers Gorge uliasisiwa tangu enzi za Nyerere na haukutekelezwa kutokana na sababu za kimazingira na mpango wa Tanzania Power System Master Plan (2016 update) umeonesha mradi huo kuwa ni chaguo la mwisho endapo miradi mingine mikubwa ikiwa imeshatekelezwa na mahitaji ya ziada ya umeme yangeibuka. Katika mpango huo imetajwa miradi mbalimbali ya maji ambayo ingepaswa kuanza kutekelezwa na pia imetajwa pia miradi ya gesi ambayo ingetekelezwa sanjari na miradi mipya ya maji. Tangu kuingia madarakani kwa serikali hii ya awamu ya Tano hakuna anayezungumzia tena miradi mingine ya muda mrefu zaidi ya umeme wa maji wala miradi ya umeme wa gesi na sasa tunaambiwa kipaumbele kikuu ni umeme wa Stigglers, Tunaomba kufahamu zipi hasa sababu za Serikali kuacha miradi ya kuzalisha umeme ambayo ilikuwa tayari katika mkondo wa utekelezaji na kuanza mradi mmoja mkubwa mpya ?

Madai ya ufisadi katika ujenzi wa Mtandao wa usambazaji umeme kwa ajili ya Mradi wa umeme Mtwara.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani ina taarifa ya madai ya ufisadi ambao inaelezwa kuwa ulifanywa wakati wa ujenzi wa mtandao wa usambazaji wa umeme Mtwara (MEP) yaliyopelekea kampuni ya M/S Wentworth Gas Limited pamoja na kampuni zake kufanya kazi zake bila kuzingatia masharti ya mikataba ya Tariff Equalisation Fund na MICRA, na pia ukafanyika ununuzi wa mitambo ya umeme bila kumshirikisha mthamaini mkuu wa Serikali. Ilipendekezwa kwamba Serikali ilipaswa kurejeshewa kutoka kwa kampuni ya wentworth Gas Limited (Umoja Light Co. Ltd) kiasi cha Dola za kimarekani 8,426,819.33. Hadi sasa hakuna taarifa kama kiasi hicho cha fedha kimesharejeshwa kama ilivyoshauriwa na ni hatua gani za ki uwajibikaji zimechukuliwa.
WAKALA WA NISHATI VIJIJINI- (REA)
Mheshimiwa Spika, wakala wa Nishati Vijijini ulianzishwa kwa sheria ya Nishati Vijijini Na.8 ya mwaka 2005 na kuanza rasmi Mwezi Oktaba 2007, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Nishati. Lengo la uanzishwaji wa REA lilikiwa ni kuwapatia wananchi waishio vijijini nishati bora. Pamoja na umuhimu wa wakala huyu bado Serikali haijaonesha kwa vitendo kuwa ina nia ya kusaidia wakala huyu ili aweze kuimiza majukumu yake kikamilifu na hasa linapokuja suala la kuupatia fedha kama zinavyoombwa na zinavyopitishwa na Bunge lako tukufu.
Mheshimiwa Spika, takwimu zinaonesha kuwa Serikali imekuwa haitimizi wajibu wake wa kuipatia REA fedha kama zinavyotengwa na kuidhinishwa na Bunge hili, kwa mfano Mwaka 2009/2010, fedha zilizopitishwa zilikuwa ni shilingi bilioni 39.55 na kiwango cha fedha zilizotolewa ni shilingi bilioni 22.14 sawa na 56%. Mwaka 2010/2011 kiasi cha fedha kilichotengwa ni shilingi bilioni 58.883 na kiasi cha fedha kilichotolewa ni shilingi bilioni 14.652 sawa na 25%, mwaka 2011/2012 kiasi kilichotengwa ni shilingi bilioni 71.044 na kiasi cha fedha kilichotolewa ni shilingi bilioni 56.748 sawa na 80%, mwaka 2012/2013 kiasi cha fedha kilichotengwa ni shilingi bilioni 53.158 na kiasi cha fedha kilichotolewa ni shilingi bilioni 6.757 sawa na 13%.
Mheshimiwa Spika, Kwa mwaka wa fedha 2015/2016 wakala alitengewa jumla ya shilingi 420,492,701,200/- kwa ajili ya kutekeleza majukumu yake. Lakini kwa mujibu wa taarifa ya utendaji ya Wakala ni kwamba hadi Desemba 2015 zilikuwa zimepokelewa jumla ya shilingi 141,163,133,226/- tu ambazo ni sawa na asilimia 34.
Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2016/17 wakala ulipitishiwa fedha za maendeleo jumla ya shilingi 382,840,122,792/-, taarifa ya wakala iliyotolewa Januari, 2017 takwimu zake zinaonyesha kuwa jumla ya miradi 13 inayoendelea kutekelezwa yenye thamani ya shilingi 1,210,050,878,902 kama mikataba yake ilivyosainiwa, hadi sasa fedha zilizotolewa na Serikali ni shilingi 1,019,957,110,048.20 na kiasi kilicho baki ni shilingi 190,093,768,854. Hiki ni kiasi kikubwa cha fedha, na ni miradi iliyoingiwa mikataba tu, lakini REA ina miradi mingi kwa kulingana na bajeti zilizopitishwa na Bunge pamoja na Mpango wa Maendeleo wa Taifa.
Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2017/18 hadi kufikia February 2018 jumla ya shilingi bilioni 249.33 zilikuwa zimepokelewa sawa na asilimia 49.9 ya shilingi 499,090,426,000/- ambazo kati ya hizo shilingi 469,090,426,000/- zilikuwa ni fedha za ndani na shilingi 30,000,000,000/- fedha za nje kama zilivyopitishwa na Bunge.
Mheshimiwa Spika, Kwa mwaka 2018/19 Bunge liliidhinisha jumla ya shilingi bilioni 412.08 kwa ajili ya Mfuko wa Nishati Vijijini ili kugharamia miradi ya maendeleo na uendeshwaji wa wakala wa Nishati Vijijini. Katika fedha hizo kiasi cha shilingi bilioni 395.61 sawa na 96% zilitengwa kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo. Aidha hadi kufikia mwezi February 2019 wakala wa Nishati ulikuwa umepokea jumla ya shilingi bilioni 302.61 sawa na 126%. Sababu inayotolewa ni kwamba fedha zilitolewa zaidi kuzidi matarajio kutokana na washirika wa maendeleo kutoa fedha zaidi ikilinganishwa na ukomo wa bajeti ya fedha za nje iliyotengewa Mfuko wa Nishati Vijijini na kwamba wafadhili walitoa kutokana na ahadi (commitment) ambazo walishaingia na serikali katika kufadhili miradi ya BTIP VEI, Ujazilizi, Makambako Songea, REA III Mzunguko wa kwanza na ile ya nje ya gridi. Kinachozua maswali ni kwanini Wizara haikuwa na makadirio ya fedha hizi wakati ilikuwa tayari na ahadi hizo (commitment) kutoka kwa wahisani hao wakati bajeti husika haikuwa na makadirio hayo.
Mheshimiwa Spika, Mwaka 2019/2020 wakala unaomba kuidhinishiwa jumla ya shilingi bilioni 423.1 ikiwa ni ongezeko la bilioni 10.3
Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa Mpango Kabambe wa Usambazaji Umeme Vijijini Awamu ya Tatu ambao umegwanywa katika vipengele vinne(4) ambavyo ni sehemu ya REA III, inaonesha kuwa Miradi ya Usambazaji Umeme kwenye maeneo ambayo yameshafikiwa na Miundombinu ya Umeme (DENSIFICATION) unakadiriwa kuwa utatumia jumla ya shilingi bilioni 2,000/- na utatekelezwa kwa kipindi cha miaka 5 ya fedha. Na vijiji vitakavyonufaika ni 4,395 Mheshimiwa Spika, hizi densification zimegawanywa katika awamu II kulingana na idadi ya vijiji vinavyohitajika kupatiwa umeme.
Mheshimiwa Spika, ni ukweli kuwa REA inatumia fedha nyingi sana katika kutekeleza wajibu wake. Kwa kuwa kila mradi ili utekelezeke ni lazima kuwepo na andiko la kuonesha costs benefits analysis. Kwa kuwa fedha za walipa kodi wa ndani na wengine ambao wanasaidia katika kutekeleza miradi hii fedha zinatumika, kwa mahesabu ya haraka haraka kwa kuanzia mwaka wa fedha 2008/09 hadi 2018/19 takriban zimekwisha tengwa jumla ya shilingi 2,199,772,249,992/- ambazo ni fedha nyingi sana. Kambi Rasmi ya Upinzani inataka Serikali itoe maelezo ni baada ya muda gani uwekezaji unaofanywa na REA utaanza kurudisha mtaji uliowekezwa huko (return on investment) kwa kuwa yamekuwepo matukio katika nchi yetu ya Serikali kuwekeza kwenye miradi yenye kuingiza hasara mingine uwekezaji ukifanyika bila hata ya kuwepo kwa mchanganuo wa kibiashara.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa taarifa ya utekelezaji wa REA (Final Report- Mid-term Review of the Capacity Development Project of the Rural Energy Agency, Tanzania) iliyotolewa na Swedish International DevelopmentCooperation Agency (Sida) inaonesha kuwa kati ya miradi yote inayotekelezwa na REA, miradi 234 sawa na asilimia (72.9%) inatekelezwa na TANESCO ikiwa na gharama ya shilingi bilioni 289 na miradi 87 sawa na 27.1% ilitekelezwa na wakandarasi wengine. Kati ya fedha hizo Tanesco ilipatiwa asilimia 89 na wakandarasi wengine walipatiwa 2% ya kile walichotakiwa kupatiwa. Hii inaonesha kuwa fedha nyingi zinazotengwa na REA zinapelekwa kutekelezwa miradi inayotekelezwa na TANESCO.

Mheshimiwa Spika, ukiangalia miradi mingi ya REA inayotekelezwa na TANESCO ni ile ya grid electrification ya kutekeleza Mpango Kabambe wa Usambazaji Umeme Vijijini (Turnkey Operation Projects).Miradi mingine ya inayohusu nishati ya umeme inayotokana na Jua, Upepo, maji katika maporomoko madogo madogo na n.k (solar, wind, biogas, hydro etc) bado miradi hiyo upatikanaji fedha kutoka REA unasuasua sana.
Mheshimiwa Spika, Ukweli ni kwamba miradi hiyo ya nishati Jadidifu (renewable energy) ndio inaweza kuwa mkombozi kwa mazingira yetu halisia badala ya kutegemea umeme unaozalishwa na kusambazwa na Tanesco.Hivyo basi ni Rai ya Kambi Rasmi ya Upinzani kwa REA kuhakikisha kipaumbele wanapewa wakandarasi ambao wanahusika na uzalishaji umeme kutokana na nishati Jadidifu.

Mheshimiwa Spika, kutokana na taarifa hiyo ni kwamba REA ndiyo inaiendesha TANESCO, fedha zote zinazokatwa kwenye mafuta na gharama za kununua umeme ili zipelekwe REA kwa lengo la kusambaza umeme vijijini ambapo TANESCO haijafika, kwa mlango wa nyuma fedha hizo zinarudishwa TANESCO kupitia njia ya kuwapatia kandarasi TANESCO ili watimize wajibu wao wa kuwapatia wananchi umeme.



Mheshimiwa Spika, kwa ukweli huo ni vyema REA ikafanyiwa tathmini upya na kuangalia inatakiwa ishughulikie miradi ya aina gani katika kutimiza majukumu yake kwa mujibu wa sheria.

WIZI WA FEDHA ZA REA KUPITIA MALIPO YA ZIADA TZS BIL.97, 935,493.04 (USD 44,725.53)

Mheshimiwa Spika, Mapitio ya mkaguzi na mdhibiti wa Hesabu za Serikali CAG, taarifa ya Machi, 2017 inaonesha kwamba wakala wa Nishati ya Umeme Vijijini REA ilifanya malipo ya ziada ya dola za Marekani USD 91,168.48 kwa HIFAB badala ya kulipa Dola za Marekani USD 9,218.48 na hivyo kufanya malipo ya ziada ya jumla ya dola za Marekani USD 81,950. Taarifa ya mwisho inaonesha kwamba jumla ya Dola za Marekani 44,725.53 hazijarejeshwa REA.

Mheshimiwa Spika, kitendo cha REA kulipa HIFAB fedha nyingi na za ziada kuliko kiasi kilichopaswa kulipwa ni wizi kama ulivyo wizi mwingine na ni vitendo ambavyo Serikali ya Chama Cha Mapinduzi imekuwa ikivikumbatia, hadi sasa ulipaji huo ambao ni uhujumu wa Miradi ya Taifa na Uhujumu Uchumi lakini hadi sasa, bado Fedha hizo hazijarejeshwa REA, Pili, hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa dhidi ya wahujumu uchumi hawa pamoja na tambo za serikali kuanzisha mahakama ya uhujumu uchumi nchini. Kambi Rasmi ya Upinzani Nchini inaitaka Serikali kuwaambia walipa kodi wa Tanzania sababu zilizosababisha REA wakawalipa HIFAB zaidi ya Dola za Marekani 81,950, wahusika ni akina nani kama siyo wizi unaofanywa na Vigogo na hatua zilizochukuliwa dhidi ya waliohusika na uhujumu huo.

REA IMESHINDWA KUKUSANYA JUMLA YA TZS 7,433,600,000 KUTOKA TANESCO:
Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa Tangazo la Serikali No.147 la tarehe 22 April 2011, TANESCO walitakiwa kutuma 3% ya gharama za mauzo ya umeme ya LUKU kwa kila mwezi REA na malipo ya 5% kwa adhabu ikiwa TANESCO watashindwa kufanya malipo hayo kwa muda. Hata hivyo REA ilishindwa kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 7,433,600,000 kutoka TANESCO pamoja na jitihada mbalimbali ambazo zimefanywa.

REA KUSHINDWA IMESHINDWA KUSIMAMIA MRADI WA UMEME KATIKA MKOA WA KAGERA (REA Phase II)
Mheshimiwa Spika, mwezi wa Februari Mwaka 2014, REA iliingia mkataba na M/S Urban & Rular Engineering service wa Thamani ya shilingi bilioni 110.8 kwa mradi wa usambazaji na kuunganisha umeme kwa wateja katika wilaya za Muleba, Karagwe, Kyerwa, Biharamulo, Ngara, Misenyi na Bukoba. Muda wa kukamilisha mradi huo ilikuwa tarehe 27/8/2015, lakini muda ulisogezwa mbele hadi tarehe 28/08/2016. Hata hivyo ilibainika kwama mpaka Oktoba 2018 vijiji 65 vilikuwa havijaunganishwa umeme. Aidha vijiji 50 vilivyounganishwa havikuwa kwenye makubaliano ya mkataba na jumla ya wateja 1317 waliokuwa wamelipa gharama za umeme ila bado hawajaunganishwa.

Mheshimiwa Spika, toka mwaka 2014 hadi mwaka 2018 ni kipindi cha miaka minne, bado mkandarasi hajamaliza kazi aliyokusudia kukamilisha mwaka 2015, na Serikali ipo na inafahamu jambo hili, haya ndiyo mazingira yanayopelekea Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kusema Miradi hii inagubikwa na mazingira ya ufisadi na Serikali haina uwezo wa kutosha wa kusimamia shughuli za maendeleo kwa maslahi ya nchi hii.


UKIUKWAJI WA SHERIA YA MANUNUZI YA UMMA NA TAASISI YA REA
Mheshimiwa Spika, uchunguzi uliofanywa kwenye mikataba mitatu yenye thamani ya Bilioni 984.3 ulibaini kwamba, REA iliingia mkataba na kampuni ya SMEC ambayo haikusajiliwa na bodi ya wakandarasi na hivyo kuleta mashaka kwa mkataba husika, pia zabuni ya kupata wakandarasi ilitangazwa kabla ya maandalizi ya nyaraka na usanifu wa mradi kukamilishwa na mshauri.

Mheshimiwa Spika, katika uchunguzi huo pia ilibainika kwamba majadiliano na mapendekezo ya wazabuni kupewa kandarasi hayakufanyika vizuri. Aidha makisio ya vifaa vilivyohitajika kutokana na BOQ ni vichache kuliko vilivyoorodheshwa katika mikataba yote sita iliyosainiwa na wakandarasi na jumla ya tofauti ya shilingi bilioni 99 kwa mikataba yote sita. Vijiji 55 ambavyo vilikuwa vimeshapata umeme viliingizwa tena kwenye mikataba ili wakandarasi waitekeleze katika mikoa ya Tanga, Mwanza, Arusha, Shinyanga na Manyara, pamoja na hayo mikataba ilikuwa na utata nani anawajibika kulipia gharama za kuingiza vifaa nchini. Ukiukwaji huu unafanywa katika kipindi ambacho watanzania ambao ni walipa kodi wakiaminishwa na Serikali kwamba Serikali yenyewe ni safi na kwamba iko kwa ajili ya kutetea wanyonge, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ingependa kufahamu hatua stahiki zilizochukuliwa dhidi ya matumizi haya mabaya ya fedha za umma na madai ya ufisadi katika mikataba hiyo.

TAKWIMU ZA UPATIKANAJI WA UMEME CHINI YA MRADI WA
UMEME VIJIJINI (REA)
Mheshimiwa Spika, katika kutoa takwimu za upatikanaji wa umeme chini ya mradi wa Umeme Vijijini (REA) kumekua na upotoshaji mkubwa wa Takwimu unaolenga kuonesha mafanikio katika utoaji wa huduma hiyo wakati kwa uhalisia wananchi wengi hawajafikiwa na huduma hizo za REA.

Mheshmiwa Spika, ni dhahiri kuwa wananchi wa sasa sio wajinga kama ambavyo amenukuliwa mara kadhaa Mhe. Rais. Ikumbukwe kuwa miradi hii ya REA ilianzishwa kwa lengo la kuunganisha na kusambaza umeme vijijini Tanzania ambavyo ni zaidi ya vijiji 12000. Lakini katika Takwimu zinazotolewa kwa umma juu ya vijiji vilivyounganishwa na umeme haviendani na uhalisia wa kaya ambazo zimeunganishwa ama kufikiwa na huduma za umeme. Kwa mfano; katika uchunguzi uliofanywa na Kambi ya Upinzani na pia kutokana na taarifa za wabunge wake walio katika kamati yako ya Nishati na Madini imegundua upikwaji mkubwa wa takwimu unaofanywa chini ya wizara ya Nishati na kupotosha umma.


Mheshimiwa Spika; kwa uhalisia miradi ya REA inapofika katika Vijiji husika, mkandarasi hutakiwa kuunganisha umeme katika vijiji vilivyo ndani yascope inayotolewa na wataalamu. Aidha, ikiwa katika kata au tarafa moja kuna vijiji 11 na vilivyo ndani ya Scope ya REA ni vijiji vitatu (3) basi TAKWIMU hizo husoma jumla ya vijiji vyote ndani ya kata au tarafa kuwa vimeunganishwa na umeme wakati kiuhalisia ni vijiji 3 tu ndio vyenye umeme. Na ili kuepukana na kuupotosha umma kwa kutoa takwimu ambazo hazina uhalisia Kambi ya Upinzani kwa nyakati tofauti imeendelea kupendekeza kwa michango ya wabunge wake na maoni yake kuwa takwimu za uunganishwaji wa umeme vijijini ufanywe kwa kutumia kaya zilizofikiwa na si kwa kutumia vijiji ambavyo havitoi uhalisia wa kitakwimu.

Mradi wa Usambazaji Umeme katika maeneo ambayo yameshafikiwa na Miundombinu ya UMEME (Densification)
Mheshimiwa Spika, mradi huu unahusisha kuongeza wigo wa usambazaji wa umeme katika vijiji, vitongoji na maeneo ambayo tayari yana miundombinu ya umeme. Mradi huu umetekelezwa kwa awamu mbili ambapo awamu ya kwanza (Densification Round I) ilianza mwaka 2017 na (Densification Round II )ilianza Julai 2018 na ulikadiriwa kugharimu kiasi cha shilingi Bilioni 62 1 . Mradi huu ulilenga kuunganisha vitongoji vilivyomo katika vijiji 4090. Lakini katika Randama ya Bajeti ya Wizara haijawekwa wazi utekelezaji wa mradi huu na iwapo umetengewa tena bajeti kwa mwaka 2019/2020.
SEKTA NDOGO YA NISHATI JADIDIFU
HEKAYA JUU YA UZALISHAJI WA UMEME WA UPEPO

Mheshimiwa Spika, ni dhahiri kuwa kuendelea kuwa na vyanzo vichache vya nishati hakuwezi kutimiza azma ya Serikali ya viwanda hasa ukizingatia kuwa maeneo mbalimbali nchini yana jiografia tofauti lakini pia uwezekano wa kuzalisha umeme kwa kupitia vyanzo vingine tofauti na maji (hydropower energy generation) na jua (solar enegy generation). Mikoa kama ya Singida, Iringa, Kilimanjaro ni mojawapo ya maeneo yenye upepo mkali ambao unaweza kuzalisha umeme na ukatumika kama nishati mbadala na hivyo kupunguza msongamano wa watumiaji wa umeme wa maji.
Mheshimiwa Spika, tangu kuingia kwa awamu ya tano tumesikia simulizi kutoka kwa mawaziri na manaibu waziri wanaotumikia wizara ya nishati juu ya utekelezaji wa umeme wa upepo kwa maeneo yalitajwa awali. Ikumbukwe kuwa November 2016, aliyekuwa naibu waziri wa iliyokua wizara ya nishati na madini ambaye sasa ni Waziri wa Wizara ya Nishati Dr. Medard Kalemani akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum kutoka Singida Mhe. Jessica Kishoa (CHADEMA) alinukuliwa kuwa ujenzi wa mradi wa uzalishaji wa umeme wa upepo utaanza ifikapo Aprili 2017 na kukamila mwaka 2019 baada ya majadiliano kati ya TANESCO na kampuni ya Wind East Africa Limited kukamilika mwezi Desemba 2016 na kuwa mradi huo ungefanyika kwa ubia wa Wind East Africa Ltd na wabia wengine watatu ambao ni Six Telecoms (Tanzania), kampuni ya Kimataifa ya Aldwych ya nchini Uingereza pamoja na moja ya wajumbe wa Benki ya Kimataifa (IFC) na ungegharimu jumla ya kiasi cha Dola za Kimarekani milioni 264.77.

Mheshimiwa Spika, Sasa ni Mei 2019 ikiwa ni miezi takribani 30 baada ya ahadi ya Mhe. Kalemani mbele ya bunge lako tukufu, Kambi ya Upinzani Bungeni inahoji Je mradi huu wa umeme wa upepo umekamilika na kuzinduliwa lini? Serikali inajinasibu kuwa Hapa Kazi Tuhuku ikishindwa kutekeleza ahadi zake na kuendela kusema uongo ndani ya bunge lako. Ni hekaya gani mpya Serikali itatoa hivi sasa kuhusu mradi huu na mingine ya upepo hapa nchini?

UCHAKAVU WA MIUNDOMBINU YA UMEME

Mheshimiwa Spika, pamoja na huduma za umeme kuendelea kutekelezwa bado kuna changamoto kubwa ya uchakavu wa miundombinu ya umeme na hivyo kusababisha athari kubwa kwa watumiaji. Uchakavu wa miundombinu ya umeme hupelekea kukosekana kwa huduma za umeme kwa maeneo mbalimbali na hivyo kukwamisha huduma nyingine za kiuchumi na kijamii.
Mheshimiwa Spika, pamoja na kuwepo kwa Mradi wa TEDAP wa kuboresha njia za usambazaji umeme (Tanzania Energy Development and Access Project) katika mikoa ya Arusha, Dar Es Salaam na Kilimanjaro ambayo imelenga kufanya marekebisho katika vituo vya kupozea umeme kwa kuboresha miundombinu na mitambo; ipo haja ya Serikali kuwekeza katika kubadilisha nguzo za mbao ambazo ndio kero kubwa sana na kusababisha usumbufu kwa watumiaji wa umeme. Kwa nyakati tofauti, ndani ya BUNGE lako tumejaribu kushauri na kutoa maoni ya umuhimu wa kubadilisha matumizi ya nguzo za mbao kupeleka kwenye nguzo za zege ili kuzuia uchakavu wa mara kwa mara na gharama, lakini bado tunaona kiasi kikubwa cha nguzo za mbao zikiwa zinaendelea kuwepo kama njia ya usafirishaji wa umeme.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inalitaka Bunge lako kuiagiza wizara ya Nishati kusitisha mara moja uagizaji wa mbao za umeme na kuendelea kuunganisha umeme kwa mbao hizo na badala yake kuwekeza katika miundombinu imara ya nguzo za zege ambazo zinatatua changamoto ya uchakavu kwa maeneo mengi ya nchini hasa maeneo ambayo yanasumbuliwa na mvua kubwa na mmomonyoko wa udongo.

Programu ya Nishati Endelevu kwa Wote (Sustainable Energy for All-SE4ALL)

Mheshimiwa Spika, malengo ya Programu hii ni kuhakikisha kuwa watanzania wote wanafikiwa na huduma za nishati hususan umeme ifipako mwaka 2030 kama ilivyoelezwa katika Randama ya Wizara ya Nishati. Jambo la kushangaza katika Randama hii ni Wizara kurudia maneno na Bajeti kama ambavyo iliwasilisha kwa mwaka 2018/19. Ukiangalia kiasi kilichotengwa kwa mwaka huu wa 2019/20 cha jumla ya shilingi Bilioni 3 (ambapo fedha za ni ni Bilioni 2.5 na fedha za ndani ni Milioni 500) kiasi ambacho ni sawa na kilichotengwa kwa mwaka huu unaoisha wa fedha.

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inahoji iwapo wataalamu wa wizara wanazingatia weledi katika uwasilishaji wa makadirio ya bajeti na utekelezaji wa shughuli zake au inaweka tu kiwango cha fedha ili Serikali ionekane kuwa na miradi ya utekelezaji na kuongezeka kwa bajeti za wizara?

SEKTA NDOGO YA MAFUTA NA GESI ASILIA
Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC)
Mheshimiwa Spika, Wataalamu wawili wa Shirika la Petroli Tanzania (TPDC) wakati wakiwasilisha mada kwenye semina ya wahariri iliyofanyika Bagamoyo walisema kwa nyakati tofauti kuwa Tathmini za kitaalamu na uzoefu wa masuala ya uziduaji na mapato ya rasilimali ya mafuta na gesi, yanaonesha pasipo shaka kuwa nchi za Afrika mapato yake hayawezi kuwa zaidi ya asilimia 25 ya pato la Taifa na hivyo ni makosa kufikiri kuwa nchi itaenda mbele sana kwa kutegemea gesi na mafuta pekee, ila kwa kuchechemua sekta nyingine za uchumi. Wakiwasilisha mada mbili ya Mapitio ya Sekta Rasilimali Gesi Asilia Historia yake, Hali ya Sasa na Mipango ya Baadaye na ya Mapitio ya Matumizi, na Mkondo wa Chini wa Gesi Asilia wameonesha wazi tatizo kubwa limezuka nchini la kutawala matarajio yaliyokithiri.

Mheshimiwa Spika, Wataalamu hao wanasema kulifanyika makosa kutoa kauli zilizokithiri wakati mambo bado yako mbali na hali ya uchumi hairuhusu kirahisi kuwekeza kutokana na mdororo wa uchumi duniani kufuatia sababu hasi lukuki zinazoendelea kudumaza mahitaji ya mafuta duniani, ikiwemo kuongezeka uzalishaji mafuta Marekani na kuanza kuuza mafuta yake katika soko la dunia na hivyo kupunguza mahitaji katika soko la dunia kwa asilimia 25.
Mheshimiwa Spika, Sababu nyingine ni kwamba, wakati huu dunia imeshuhudia matumizi makubwa ya teknolojia kule Marekani na Canada kufanya mabanzi ya mchanga (shale) kutengeneza mafuta, hivyo kuleta tafrani na utata kwa wawekezaji na kudhuru maendeleo ya miradi ghali ya gesi kama hiyo ya Tanzania ambayo gesi yake nyingi iko ndani baharini tcf 47.08 kilomita 120 toka nchi kavu kwenye kina cha mita 4000 na ile iliyoko nchi kavu ni tcf 8.04 na hivyo uendelezaji wake ni tatizo.
Mheshimiwa Spika, wataalam walifafanua kuwa mafuta ndio yanayofanyika kibiashara duniani kote, huku gesi asilia bado ikifanyika kieneo kidogo na hivyo bei ya mafuta ndio inayoamua uwekezaji katika sekta ya nishati. Matokeo yake ni kuanguka kutoka zaidi ya dola 100 miaka miwili iliyopita na kuwa chini ya dola 40 kwa pipa la mafuta mwaka huu. Hivyo kuuathiri uwekezaji wa Lindi kwani Msumbiji nayo imegundua gesi nyingi ya kiasi cha zaidi ya tcf 200 ukifananisha na tcf 57.2 ya Tanzania na hivyo kuwa mshindani mkubwa kwenye uwekezaji.

Mheshimiwa Spika, kuongeza kuwa ushindani wa kupata mitaji na kuvutia wawekezaji katika bara la Afrika, ni jambo gumu linalohitaji ushawishi mkubwa na hivyo kufanya watawala kuwa na wakati mgumu kufanya maamuzi sahihi kwa kuvutwa na kushawishiwa na matumizi ya mbinu mbalimbali kuweza kushawishi (lobby) na kuondokana na hali ya mkwamo mbele ya wananchi wao. Pamoja na hali hiyo bado Serikali iliyoko madarakani imeendelea kuwa na baadhi ya wanasiasa wenye kuwaita wawekezaji kuwa ni mabeberu na wanyonyaji wa rasilimali ya nchi badala ya kutafuta namna bora ya kufanya nchi na wananchi kunufaika na rasilimali ambazo Mwenyezi Mungu ameijalia nchi yetu.
Mheshimiwa Spika,Statoil na mshirika wake ExxonMobil walifanya ugunduzi mkubwa wa gesi asilia katika visima vya Zafarani, Lavani, Tangawizi, Piri, Giligilani na Mronge katika Kitalu namba 2, chenye eneo la takriban kilometa za mraba 5,500, ambalo lipo umbali wa zaidi ya kilometa 100 kutoka ufukweni katika kina cha maji kati ya meta 1,500 hadi 3,000.
Mheshimiwa Spika, kwa sasa Tanzania imeishagundua akiba ya gesi yenye futi za ujazo zaidi ya trilioni 57 imegundulika.
Mheshimiwa Spika, si rahisi kusafirisha gesi katika hali yake ya kawaida, ni lazima kuisindika kwa kuibadili kuwa katika hali ya kimiminika (Liquefied Natural Gas LNG), hivyo mtambo wa LNG una umuhimu mkubwa kwa biashara ya gesi kwa kusafirisha kwenye soko la kimataifa pamoja na matumizi ya ndani. Ni ukweli kwamba, katika ujenzi wa mtambo wa LNG, gharama zote zitalipwa na wawekezaji wakati serikali jukumu lake ni kutoa ardhi mahali mtambo huo utakapojengwa inaonekana jambo hilo kwa mwaka huu 2018/19, Serikali imetenga jumla ya shilingi 6,500,000,000/- ikiwa ni fedha za kulipa fidia kwa waathirika wa makazi katika eneo la mradi na pia zikiwa ni fedha za kufanya tafiti ili kusaidia timu ya Majadiliano (GNT). Suala hilo halikuanza mwaka ambao tunamaliza utekelezaji wake na katika mwaka mpya wa fedha Serikali imerudia tena kuja na mapendekezo hay ohayo. Hoja ya msingi hasa ni je wawekezaji ambao fedha za majadiliano tayari zimetengwa wapo tayari?

Mheshimiwa Spika, tulikwisha oneshwa manufaa faida katika kutumia gesi asilia katika kuendeshea magari badala ya kutumia mafuta ya petrol, kwamba Unafuu katika bei ya kununulia nishati hii ni rahisi zaidi ya asilimia 45 kulinganisha na bei ya mafuta ya petroli. Ulinganifu wa gesi asilia na petrol. Kilo 1 ya gesi asilia iliyoshindiliwa ni sawa na lita 1.54 ya petrol, bei ya kilo moja ya gesi asilia ni ndogo kuliko lita moja ya Petrol. Pia, gharama za ukarabati (service) wa magari zinapungua endapo utatumia gesi asilia badala ya mafuta ya petroli. Hii ni kwa sababu gesi asilia ni safi, muwako wake hauna masizi (carbon) kulinganisha na mafuta, hivyo itachukua muda mrefu kufanya ukarabati wa gari linalotumia gesi asilia (kilomita 5000) ukilinganisha na gari linalotumia mafuta (kilomita 3000).

Mheshimiwa Spika, TPDC walikwisha anza kuleta vifaa vya kuwezesha magari kutumia gesi asilia badala la Petrol au Dizeli na tukapewa matumaini kuwa kituo cha kujazia gesi kwenye magari kimejengwa Ubungo. Lakini hadi sasa Bunge halifahamu chochote kuhusu mradi huo mkubwa wa matumizi ya gesi asilia kwenye vyombo vya usafiri na majumbani. Hivyo basi, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kutoa ufafanuzi wa Mradi huo ambao ulikuwa ni mkombozi kwa wamiliki wa vyombo vya usafiri na watumiaji wa gesi majumbani.


Changamoto za Madeni na Ukusanyaji usioridhisha

Mheshimiwa Spika, Sheria ya Petroli ya Mwaka 2015, inatoa madaraka kwa Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini, TPDC kusimamia na kuendeleza sekta ya Mafuta na Gesi asilia kwa niaba ya Serikali. Katika kutekeleza hayo, sheria tajwa hapo juu, imeipa TPDC jukumu la kuhakikisha inaendesha kibiashara shughuli za Mkondo wa juu, yaani utafutaji mafuta na gesi, Mkondo wa kati ( uchakataji na usafirishaji mafuta na gesi) pamoja na Mkondo wa Chini ( usambazaji gesi na mafuta kwa watumiaji). Kwa maana hiyo, kazi za TPDC ni pamoja na kusimamia shughuli za utafutaji, uendelezaji na usambazaji wa Mafuta na Gesi Asilia Nchini.
Mheshimiwa Spika, Pamoja na umuhimu wa mamlaka ya TPDC bado inakabiliwa na changamoto kadhaa zikiwemo changamoto za Madeni na Ukusanyaji usioridhisha wa wadaiwa. Kwa taarifa ambazo Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inazo zinaonesha kuwa hadi kufikia Juni 30, 2018, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) ilipata hasara ya Shilingi bilioni sitini na Nne na Milioni Mia Tano Arobaini na Tatu (64,543,000,000) huku ikiwa na madeni yanayofikia shilingi Trilioni Tatu, bilioni Mia tano na Arobaini na Nne, Milioni Mia Nane Tisini na Mbili (3,544,892,000,000) hivyo kuwa katika moja ya mashirika yenye hali mbaya ya kifedha. Aidha deni hilo limesababisha makampuni yenye mkondo wa juu kutishia kuzuia kuuza Gesi Asilia kwa TPDC kwa sababu ya kushindwa kulipia Ankara zake kwa wakati. Kambi Rasmi ya Upinzani pamoja na kusikitika juu ya hasara inayoendelea kupata shirika, inapenda kufahamu mkakati wa serikali wa kulifanya shirika hili lisijiendeshe kwa hasara.

Mheshimiwa Spika, wakati TPDC ikipata hasara hiyo, taarifa zinaonesha kuwa, hadi kufikia Disemba 2018, TPDC ilikuwa inadai jumla ya shilingi bilioni 527.096. Wadaiwa Sugu wakiwa ni Shirila la Umeme Tanzania, TANESCO, Kampuni ya kuzalisha umeme ya SONGAS, Kampuni ya Ndovu Resources ltd na Kampuni ya Kilimanjaro Oil ltd na wadaiwa wengine. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka kupata majibu kutoka kwa Serikali, kuhusu mkakati wa makusudi wa kuhakikisha wadaiwa hawa sugu wanalipa madeni yake ili kuliwezesha sharika la Maendeleo ya Petroli Tanzania kufanya shughuli zake kwa mujibu wa sheria.

Uwekezaji Mdogo TPDC katika Shughuli za Maendeleo
Mheshimiwa Spika, Uwekezaji kwa ajili ya shughuli za Maendeleo ya shirika nao unapata changamoto ya Ufinyu wa bajeti, uwekezaji mdogo TPDC na utashi wa kisiasa. Changamoto hizi ni miongoni mwa sababu zinazokwamisha ufanisi katika utekelezaji wa mikakati inayojiwekea. Kwa mfano, Mwaka 2016, Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini (TPDC) iliandaa Mpango Kabambe wa Matumizi ya Gesi Asilia (NGUMP 2016 Natural Gas Utilization Master Plan). Mpango huu uliainisha kwa kina usambazaji wa Gesi Asilia Nchini. Hata hivyo, mpango huu umekua ukisuasua kutekelezeka hadi leo kwa sababu ya ukosefu wa rasilimali fedha, kutokana na ukosefu wa utashi wa kisiasa, sasa usambazaji wa Gesi Asilia inakumbwa na changamoto wakati Taifa inaonekana linaelekeza nguvu zake katika maeneo mengine, wakati mradi huu haukukamilika kwa ukamilifu wake. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kuhakikisha Mpango wa Matumizi ya Gesi Asilia nchini unatekelezwa kwa ukamilifu.

Majadiliano yasiyo na kikomo

Mheshimiwa Spika, Kwa kipindi kirefu sana, kupitia taarifa zinazotolewa na Wizara ya Nishati, kumekuwepo kwa majadiliano yasiyo na kikomo kwa Serikali na Wawekezaji. Hii inaathiri utekelezaji wa mikakati ya baadhi ya shughuli za Gesi Asilia iliyopo katika hatua mbalimbali za utekelezaji. Mathalani Utelezaji wa Mradi wa Kusindika Gesi Asilia kwenye Hali ya Kimiminika (Liquefied Natural Gas Plant-LNG). Vivyo hivyo majadiliano haya yasiyo na kikomo, yanasababisha ucheleweshwaji wa uwekezaji wa mitaji ya kigeni (FDI) ambayo ni kichocheo cha uchumi na maendeleo ya miradi mbali mbali nchini. Lakini pia upatikanji wa FDIs ungeisaidia Serikali kuelekeza rasilimali zaidi katika sekta zilizo na ufinyu wa Bajeti hasa katika maeneo ya kimkakati ya kijamii. Ni maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kwamba, Serikali ilipatie shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kipaumbele katika uwekezaji ili iweze kutekeleza majukumu yake ya kisheria kama inavyotakiwa, ufinyu wa bajeti na uhaba katika uwekezaji kunalifanya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kuwa tegemezi na kushindwa kuhimili ushindani kwa kasi inayohitajika katika biashara.

Mheshimiwa Spika, mnamo tarehe 2 Desemba, 2013, aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini wakati huo Prof. Sospeter Muhongo na ujumbe wake nchini Algeria, alisema kuwa makubaliano yamefikiwa baina ya Tanzania na Algeria ya kuanzisha kampuni ya Ubia itakayohusika na ujenziwa miundombinu ya kusambaza umeme na Kampuni ya Ubia ya kujenga mtambo wa kusindika gesi ya Liquefied Natural Gas (LNG) na kuiuza gesi kwa wananchi kwa kutumia mitungi.

Mheshimiwa Spika, Katika hatua nyingine, tuliambiwa kuwa Mawaziri hao waaliziagiza kampuni za mafuta na gesi likiwemo Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na kampuni za mafuta na gesi za Algeria za NAFTAL na SONATRAC kukamilisha majadiliano ya kuanzisha kampuni ya ubia ya kujenga mtambo wa LPG na kuuza gesi hiyo kwa wananchi kwa kutumia mitungi, ambapo kampuni zote za ubia zimetakiwa kuanza kazi ifikapo Januari, 2015.

Mheshimiwa Spika, ni muda mwafaka sasa Bunge hili kupewa mrejesho wa makubaliano yaliyofikiwa baina ya nchi zetu hizi yamefikiwa hatua gani ya utekelezaji?

Mheshimiwa Spika, wakati huohuo Waziri wakati huo, Profesa Sospeter Muhongo alizindua ofisi za Liquefied Natural Gas LNG Tanzania jijini Dar es Salaam. LNG ni muunganiko wa makampuni matano ya BG Group, Statoil, ExxonMobil, Ophir na Pavilion kwa ajili ya kufanikisha mipango itakayopelekea ujenzi wa kiwanda cha kuchakata gesi. Makampuni hayo yanayounda LNG yatashirikiana na serikali kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli Nchini (TPDC) na Wizara ya Nishati.

Mheshimiwa Spika, hizo hadithi kwa kiasi kikubwa zimepelekea kuaminisha wananchi kuwa tunakwenda kwenye uchumi wa Gesi na wimbo huo unaendelea kuimbwa na Serikali iliyopo madarakani wakati uhalisia wa jambo hilo haupo.

Malipo yasiyostahili kwa kampuni ya Maurel & Prom ya dola za kimarekani milioni 27.18

Mheshimiwa Spika, Maurel & Prom (operator, 48.06% interest) ni kampuni inayoendesha visima viwili vya gesi vilivyopo Mnazi Bay vinavyo peleka gesi pale kituo cha Madimba Mtwara (processing centre -operated by GASCO, a subsidiary of TPDC) linapoanzia Bomba la Gesi asilia kati ya Mtwara na Dar es Salaam.

Mheshimiwa Spika, Kifungu cha 15.1 cha Makubaliano ya Mauziano ya Gesi (GSA) uliosainiwa Sept. 12, 2014, kati ya TPDC na Maurel & Prom (M&P) kinataka TPDC kuweka dhamana ya fedha kwa kuweka kiasi cha fedha kwenye akaunti ya pamoja (Escrow) au kwa Barua ya Mkopo kutoka Benki (letter of credit) au kwa mkataba wa dhamana ya malipo (payment guarantee agreement).

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa ukaguzi wa CAG umebaini kuwa, TPDC ilitoa kiasi cha Dola za Kimarekani milioni 27.18 (sawa na Shilingi bilioni 56.70) kwa kulipa akaunti ya M & P kinyume na masharti tajwa hapo juu huku ikichukulia fedha hizo kama malipo ya awali (prepayment). Pia, ilibainika kuwa fedha zilizolipwa kwa M&P zilikopwa kutoka Benki ya Maendeleo ya TIB.

Mheshimiwa Spika, Ukosefu wa makubaliano rasmi juu ya namna fedha za dhamana zinavyotakiwa kuhifadhiwa unaiweka TPDC kwenye nafasi mbaya endapo kutatokea mgogoro wowote. Pia, kukopa fedha kwa lengo la kuweka dhamana kunaongeza gharama kwa taasisi kwa sababu ya riba. Mtindo huu wa kuendesha taasisi zetu ndio umekuwa ukisababisha taasisi zetu kutokupiga hatua za kwenda mbele. Kambi Rasmi ya Upinzani inaadharisha uwepo mwingine wa IPTL kutokana na mkataba huo kuingiwa kwenye mazingira yenye kuacha mashaka baina ya Serikali na Kampuni hiyo ya Kifaransa.

Masuala ya ujumla kuhusu matumizi ya gesi asili nchini:
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka serikali kupitia wizara ya Nishati kutekeleza mpango kabambe wa TPDC (NGUMP 2016) ili kuwezesha miundombinu ya Gesi Asilia kujengwa na kuharakisha matumizi ya Gesi Asilia katika kaya na pia kupunguza mahitaji ya matumizi ya Mkaa na kuni hasa kwa mikoa mikubwa ambapo mahitaji huongezeka kila siku kwa ajili ya shughuli za kiuchumi.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaishauri Serikali kutoa kipaumbele katika uwekezaji wa vitalu vya kimkakati vya asilia vilivyopo chini ya mamlaka ya TPDC kwa kuharakisha mazungumzo na wawekezaji ili kufikia muafaka wa kupata uwekezaji wenye manufaa na pia kujali muda kwa kutumiafursa ipasavyo, kwa kuwa Kambi Rasmi inaamini kwamba kuendelea kuchelewa kuwekeza kunaweza kutoa fursa kwa nchi nyingine zenye gesi kama nchi ya Msumbiji na kulikosesha taifa faida nono.

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, shirika la maendeleo ya Petroli nchini liweke juhudi za kutosha katika utafutaji wa masoko ya uhakika kwa ajili ya usambazaji wa Gesi Asilia. Katika bajeti ya mwaka wa fedha 2018/2019 serikali ilikuwa inakusudia kuunganisha viwanda takribani kumi pamoja na kaya zaidi ya 2000 katika miundombinu ya Gesi Asilia. Kwa vyovyote vile shabaha hizo haziridhishi kwa kuzingatia idadi ya viwanda ambavyo serikali kwa nyakati mbalimbali imetoa takwimu zake na idadi ya kaya za watanzania, ni wajibu wa Serikali kupitia TPDC kuhakikisha malengo yanatimia.
Miradi ya Gesi Asilia nchini.
Utekelezaji wa miradi ya gesi asilia na makadirio yake 2018/2019/2020.
Mheshimiwa Spika, Mradi wa kusindika Gesi Asilia kwenye hali ya kimiminika unaofahamika kwa lugha ya kigeni kama, Liquefied Natural Gas (LNG) ni miongoni mwa Miradi iliyopangwa kutekelezwa katika Mwaka wa fedha 2019/20. Ili kutekeleza mradi huu, Serikali imetenga bajeti ya Shilingi bilioni 6.5 kwa ajili ya kutekeleza zoezi la ulipaji fidia, kufanya tafiti mbalimbali za kiuchumi ili kusaidia timu ya Serikali katika majadiliano na wawekezaji. Katika hali ya kushangaza, Mradi huu ulipendekezwa kama ulivyo kwa Mwaka wa fedha 2018/19 kwa bajeti ya kiwango cha Shilingi bilioni 6.5. Mradi huu umekuwa katika majadiliano tangu miaka 2 iliyopita na hakuna taarifa za kutosha kuhusu maafikiano na hatua zilizofikiwa katika majadiliano baina ya Serikali na wawekezaji. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ina maoni kwamba Serikali lazima itambue na kuzingatia muda katika utekelezwaji wa miradi ya Maendeleo, aidha Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni tunaitaka Serikali kutolea ufafanuzi wa bajeti inayopangwa kila mwaka na ufanisi wake kwa kuwa hakuna taarifa za kina zinatolewa kuhusu Miradi mbalimbali, ukiwemo huu.
Ujenzi wa miundombinu ya usambazaji wa gesi asilia katika jiji la Dar es salaam.


Mheshimiwa Spika, Mradi huu unalenga kujenga miundombinu ya kusambaza gesi asilia katika jiji la Dar es Salaam na ili kutekeleza mradi huu, Bajeti ya Shilingi bilioni moja na Milioni Mia Moja (1,100,000,000) zimetengwa kwa Mwaka wa fedha 2019/20. Katika bajeti ya mwaka wa fedha 2018/2019 mradi kama huu uliwekwa pia kwa bajeti ya Shilingi Bilioni 2 zilizotengwa. Kwa kuwa Miradi hii ni ya watanzania, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaungana na watanzania na wadau mbalimbali na kupendekeza kwamba Serikali itoe maelezo na taarifa kuhusu hatua za usambazaji wa gesi asilia katika maeneo husika, kuliko kuandika tu, majina ya miradi kwa kujirudia kutoka mwaka mmoja wa fedha kwenda mwaka mwingine wa fedha.

Bomba la gesi kutoka Mtwara - Dar es salaam Tanga-Mwanza-Kagera- Uganda

Mheshimiwa Spika, Bomba la kusafirisha Gesi asilia kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam lilijengwa na Kampuni ya China Petroleum and Technology Development Company (CPTDC) kwa gharama ya takriban Dola za Kimarekani takriban bilioni 1.283 ambapo kati ya hizo, dola za Kimarekani bilioni 1.225 zilipatikana kama mkopo wa masharti nafuu kutoka Benki ya Exim ya China. Marejesho ya mkopo huo yalitegemea kupatikana kwenye mauzo ya gesi asilia baada ya kukamilika kwa mradi wa ujenzi wa bomba na kuanza kutumika kibiashara.
Mheshimwa Spika, kwa sasa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) ndilo mteja mkuu wa gesi asilia; ambapo anatumia wastani wa futi za ujazo milioni 46.61 kwa siku, sawa na asilimia sita (6%) tu ya ujazo wa bomba; ambapo, kiasi hicho ni pungufu futi za ujazo milioni 737.39 kwa siku ili kujaza bomba. Matumizi haya ni tofauti na makubaliano ya awali ambayo ilikua TANESCO liweze kutumia takribani futi za ujazo milioni 80 kwa siku kama ilivyokuwa kwenye makubaliano ya mkataba wa mauziano ya gesi asilia (GA).
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Bunge lako tukufu inapenda kupata ufafanuzi kutoka Serikali kuhusu jitihada ambazo Serikali imechukua ili kuhakikisha wateja zaidi wa gesi asilia wanapatikana ili mkopo uweze kulipwa kabla ya marekebisho ya ulipaji ambayo yataongeza gharama kubwa kwa Serikali.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inafahamu kwamba mkataba wa mauziano ya gesi asilia kati ya TPDC na TANESCO uko wazi kwamba TANESCO itatumia gesi asilia kwenye mitambo yake sita (6) ya kuzalisha umeme ya Kinyerezi I, Kinyerezi II, Ubungo I, Ubungo II, Tegeta kwa kima cha chini cha matumizi cha futi za ujazo milioni 80 kwa siku na futi za ujazo milioni 138.8 kwa siku kama kiwango cha juu. Hata hivyo, hadi sasa kiwango cha matumizi ya gesi asilia kuzalisha umeme hakilingani na kilichokubaliwa katika mkataba; kwa sasa matumizi ni kiwango cha asilimia thelathini na nne (34%) ya kiasi cha gesi yote iliyolengwa kutumiwa na TANESCO.
Mheshimiwa Spika, Mitambo mingine iliyokuwa imekadiriwa kutumia kiasi cha (66%) bado haijaanza kutumika; na haijulikani ni lini mitambo hiyo itaanza kutumia gesi asilia.
Mheshimiwa Spika, tukumbuke kwamba gharama za ujenzi wa Bomba hilo toka Mtwara hadi Dar ulikuwa ni mkopo toka Exim Bank ya China na mkopo huo unatakiwa kulipwa, hoja ya msingi ni kwamba matumizi ya gesi hiyo bado ni kidogo kulinganisha na mahitaji yake.
Mheshimiwa Spika, ukianangalia Randama uk 68 inaonesha kuwa mradi huu unahusu ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi asilia kutoka Dar es Salaam kwenda Uganda kupitia Tanga, bomba hilo linatakiwa kutumia mkuza uliopo wa Bomba la mafuta ghafi kutoka Uganda hadi Tanzania.
Mheshimiwa Spika, kwa maana rahisi ni kuwa Bomba jipya linalojengwa ni kutoka Dar hadi Tanga, na gesi asilia iliyopo ni kwamba matumizi yake hapa kwetu yameishatosheleza na zaida ndiyo inatakiwa ipelekwe Uganda.
Mheshimiwa Spika, katika mradi huo zimetengwa jumla ya shilingi 1,500,000,000/- kwa ajili ya upembuzi yakinifu utakaoonesha gharama halisi za mradi na namna bora ya kutekeleza mradi huo.
Mradi wa kusafirisha Gesi Asilia kutoka Dar Es Salaam Tanzania hadi Uganda
Mheshimiwa Spika, Mradi huu unahusisha ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi asilia kwenda Nchini Uganda kutokea Dar es Salaam, bomba hilo litakwenda sambamba na bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki linalotoka Hoima Uganda hadi Chongoleani-Tanga (Tanzania) na Serikali imetenga Bajeti ya Shilingi 800,000,000 Mwaka 2019/20. Hatahivyo, mradi huu pia ulitengewa Shilingi Bilioni 1.5 katika Mwaka 2018/19 kwa ajili ya Upembuzi Yakinifu. Tunashauri Serikali kufafanua bajeti nzima kwa ajili ya mradi huu na pia kutoa ufafanuzi wa hatua za utekelezaji wa bajeti zinazopangwa kila mwaka.
MATUMIZI YA GESI ASILIA KWENYE MAGARI
Mheshimiwa Spika, taarifa zilizopo ni kwamba upembuzi yakinifu kwa ajili ya kuweka mtandao wa mabomba ya kusambaza gesi na vituo vya kujazia gesi magari ulifanyika toka mwaka 2006/2007 na kuhusisha magari 8,000 na makazi yapatayo 30,000. Ujenzi wa mradi huo ulitarajiwa kuanza Julai 2015 ambapo zoezi la kumtafuta Mkandarasi pamoja na fedha za ujenzi takribani Dola za Marekani milioni 76 zilikuwa zikihitajika.
Mheshimiwa Spika, randama uk. 27 inaonesha kuwa kwa mwaka 2017/18 TPDC imeedelea na juhudi za kutafuta wateja zaidi wa gesi asilia kwa ajili ya matumizi ya viwandani pamoja na ujenzi wa miundombinu ya kusambazia gesi hiyo kwa wateja. Usambazaji wa gesi asilia kwenye viwanda vya Mkuranga ulitengewa shilingi 6,274,252,000/- lakini hadi mwezi Machi, 2018 hakuna hata shilingi iliyokuwa imetolewa.

Mheshimiwa Spika, aidha, bomba hilo linalosambaza gesi limehusisha uunganishaji wa nyumba 70 tu katika mtandao wa gesi asilia. Kwa mwaka huu wa bajeti 2018/19 jumla ya nyumba 60 zilipangwa kuunganishwa katika maeneo ya Mikocheni na Mwenge, na imetengwa jumla ya shilingi 1,500,000,000/-.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inataka kupatiwa ufafanuzi kuhusu uwekezaji wa shilingi bilioni 1.5 katika usambazaji wa gesi kwa nyumba 60 tu kwa mwaka. Hili la kusambaza miundombinu ya matumizi ya gesi asilia majumbani katika Jiji la Dar Es Salaam, mikoa ya Mtwara na Lindi ambako gesi asilia inaanzia lazima lionekane likifanyika kwa haraka ili baadae ifuatie mikoa mingine.
Miradi ya Usafirishaji wa Mafuta.
Mradi wa bomba la Mafuta kutoka Hoima Chongoleani
Mheshimiwa Spika, Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi ni Mradi wa Sekta binafsi unatekelezwa katika nchi mbili (Uganda na Tanzania). Mradi huo uliokadiriwa kugharimu Dola za Marekani 3.55 bilioni na kuleta ajira za kati ya watu 6,000 na 10,000 ndani ya miaka mitatu (3). Mafuta Ghafi ya Hoima (ya aina yake), yatasafirishwa kutoka Uganda kwenda sokoni nchi za nje,kupitia Tanzania. Mradi wa Bomba umbali wake ni kilometa 1,445 ambapo kilometa 298 zitakuwa nchini Uganda, na kilometa 1,147 zitakuwa nchini Tanzania.

Mheshimiwa Spika, taarifa zinasema kuwa katika mchakato huo wa mradi ni dhahiri kuwa shughuli kadhaa za uchumi katika sehemu litakapoptia Bomba hilo na mwisho wake zitaimarika zaidi.

Mheshimiwa Spika, kutokana na ukweli kwamba kilometa za urefu za bomba hilo zipo nchini Tanzani, na kati ya fedha Dola za Kimarekani 3.55 zilizotarajiwa kutumika ili kukamilisha mradi huo, Kwa kuwa sekta binafsi inatarajiwa kushiriki kikamilifu, sekta hiyo itaunganishwa na TPSF. Kambi Rasmi ya Upinzani inauliza, Serikali inachangia kiasi gani katika fedha tajwa hapo juu na Sekta binafsi inatakiwa kuchangia kiasi gani? Kwani kwa mujibu wa Randama inaonesha kuwa mwaka huu wa fedha zimetengwa jumla ya shilingi 54,200,000,000/- kwa ajili ya ujenzi wa Bomba la mafuta toka Uganda hadi Tanga. Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani imedokezwa kwamba mazungumzo juu ya mradi huu yameanza kukwama kutokana na sababu mbalimbali, hivyo inataka maelezo iwapo taarifa hizi ni sahihi na ni upi ufumbuzi wa mkwamo huo?

Mradi wa bomba la kusafirisha Mafuta ghafi la Africa Mashariki kutoka Uganda hadi Tanga Tanzania (EACOP):

Mheshimiwa Spika, Mradi huu ni mwendelezo wa ujenzi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Nchini Uganda hadi Tanzania, ambapo, bajeti ya Shilingi 7,000,000,000 zimetengwa kwa ajili ya kukamilisha majadiliano ya kimkataba kati ya Nchi washirika Uganda na Tanzania) na makampuni yaliyowekeza kwenye mradi huu (Total SA na Tullow Plc).

Mheshimiwa Spika, katika hali inayozua maswali mengi taarifa za Serikali zinaonesha kwamba, katika bajeti ya Mwaka 2018/19, Shilingi bilioni 54 zilitengwa kwa ajili ya kazi na majukumu yanayofanana na majukumu yanayotarajiwa kutekelezwa mwaka huu. Pamoja na jitihada za Serikali katika mradi huu, ili kukuza Uwazi na Uwajibikaji katika utekelezaji wa mradi huu, tunafahamu majadiliano haya yamechukua sura mpya na hivyo basi tunashauri Serikali iweke wazi hatua za makubaliano zilizofikiwa hadi sasa, na kipi kinakusudiwa kwenye majadiliano haya mapya. Pia ijulikane jumla ya fidia zitakazolipwa na mchango wa kila Nchi wabia katika utekelezaji wa Mradi.

Mheshimiwa Spika; Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inazo taarifa za kuanza kwa utekelezaji wa mradi huo katika hatua za awali yaani Surveys (Geological Survey, Geophyisical Survey, na GeoTechnical Survey); tunaiomba Serikali ilipatie Bunge lako tukufu hali ya mambo ilivyo katika hatua hizi za awali za utekelezaji wa mradi huo wa Bomba la Mafuta kutoka Uganda kuja Chongoleani Tanga.

Mheshimiwa Spika; Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kulieleza Bunge lako tukufu ni ajira kiasi gani zimeshaanza kutolewa kwa raia wa Tanzania, na endapo Serikali imepata mapato yoyote kutoka kwenye makampuni yaliyokuwa yakitekeleza hatua hizo za tafiti za awali kabla ya ujenzi kuanza.

Mheshimiwa Spika; pia Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kueleza kwa undani juu ya uzingatiaji wa sera, sheria na kanuni za local content katika uwekezaji mkubwa kama huu. Serikali ilileze Bunge lako tukufu ni kwa kiasi gani makampuni ya Kitanzania yameanza kushiriki katika hatua za awali za mradi huu.

Matumizi ya Gesi inayotokana na Petroli (Liquified Petroleum Gas LPG)
Mheshimiwa Spika, Kwa upande wa gesi ya kupikia (LPG), jumla ya tani 65,522 ziliingizwa nchini kwa ajili ya matumizi ya ndani, mwaka 2014, na kwa mwaka wa fedha 2015 ziliagizwa tani 70,063 sawa na ongezeko la asilimia 7 kwa kulinganisha na uagizaji wa mwaka 2014, na mwaka 2016 ziliagizwa tani 90,296 sawa na ongezeko la asilimia 29 kwa kulinganisha na uagizaji wa mwaka 2015.

Mheshimiwa Spika, ni ukweli kwamba sasa hivi wafanyabiashara wanazidi kuwekeza mitaji katika biashara hii ya gesi itokanayo na mafuta (LPG) ili kuhakikisha kuwa wanakwenda kutosheleza soko ambalo bado ni kubwa sana hapa nchini. Kwa hili Kambi Rasmi ya Upinzani inaona lingekuwa jambo la msingi kama mitaji ya hawa wafanyabiashara ingekuwa-mobilized pamoja kuweza kuwa na uagizaji wa pamoja (Bulk Procurement) wakati huu ambapo bado taifa linasubiria kujengwa kwa mtambo wa kuchakata gesi (LNG) ili nchi yetu kuanza kutumia mitungi ya gesi ya hapa nchini sanjari na mitungi ya gesi itokanayo na mafuta (LPG) kutoka nje.

Mheshimiwa Spika, inaonesha kuwa matumizi ya LPG kwa nchi yetu ni kidogo sana kwa kulinganisha ma majirani zetu wa Kenya, ambao matumizi ni mara nne ya matumizi yetu. Matumizi ya gesi kwa nchi za kusini mwa jangwa la Sahara ni wastani wa of 2.3Kg kwa mwaka, kwa mujibu wa taarifa ya of World LPG Association (WLPGA),kwa kulinganisha na wastani wa matumizi ya 55Kg kwa mwaka kwa nchi za Africa ya Kaskazini.



Mheshimiwa Spika, wakati wastani kwa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahala ni matumizi ni 2.3kg kwa mwaka, Tanzania matumizi ni wastani wa 1.4kg kwa mwaka, wastani ambao ni chini na nchi ambazo tuko nazo kundi moja.

Mheshimiwa Spika, mfano mzuri ni ulinganisho wa gunia moja la mkaa linalouzwa kwa shilingi 40,000/- hadi 60,000/- na mtungi wa gesi ya mafuta (LPG) wa kilo 15 unaouzwa kati ya shilingi 45,000/- hadi 55,000/- kulingana na eneo. Hivyo basi kama tukiwa na mkakati mzuri wa kuhamasisha matumzi ya gesi itokanayo na mafuta (LPG), ikiwemo kuwa na bei elekezi ni dhahiri tutaokoa misitu yetu.

Mheshimiwa Spika, tumeweka takwimu hizo kuonesha ni jinsi gani matumizi ya nishati Kuni ilivyo kubwa kwa nchi yetu na wakati huo hakuna mkakati wote wote wa kuhamasisha matumizi ya nishati gesi kwa matumizi ya nyumbani ili kukabiliana na mabadiliko ya Tabianchi.
MADENI YA WAKANDARASI
Mheshimiwa Spika, Kwa muda mrefu miradi ya Wizara ya Nishati imeendela kukwama ama kutokutekelezwa kwa wakati kutokana na kucheleweshwa kwa malipo ya wakandarasi na hivyo kupelekea kuwa na madeni makubwa ya wakandarasi na hivyo kushindwa kuendana na kasi ya miradi hiyo. Kusua sua kwa miradi ya REA kunatokana na changamoto kubwa ya Wizara kutowalipakwa wakati Wakandarasi kama ambavyo inaelekezwa katika mikataba baina yao. Pamoja na lawama zinazotolewa na Wizara kwa wakandarasi wa miradi ya REA kuwa hawana uwezo wa kutekeleza miradi hiyo; Kambi Rasmi ya Upinzani inahoji ikiwa shida ni wakandarasi kutokidhi vigezo; ni kwa nini wanashinda zabuni iwapo hawana uwezo wa kukamilisha miradi hiyo? Ikumbukwe kuwa kwa nyakati tofauti tumeshuhudia Raisi na Mawaziri wakisitisha mikataba ya wakandarasi wasio na uwezo wa kutekeleza majukumu yao ya kimkataba. Iwapo katika utekelezaji wa miradi ya REA shida ni wakandarasi ni kwa nini wakandarasi hao wasisitishiwe mikataba kwa kushindwa kuitekeleza?

Mheshimiwa Spika, ikumbukwe kuwa wakati wa ukaguzi wa miundombinu ya awamu ya tatu ya REA mwezi Machi 2018, Mhe. Waziri aliahidi kuwa watasitisha mikataba ya wakandarasi watakaoshindwa kuunganisha umeme kwa vijiji vilivyo kwenye miradi. Kambi ya Upinzani inahoji; toka atoe tamko hilo je, Mpaka sasa ni wakandarasi wangapi wamesitishiwa mikataba? Na je, toka kuanza kwa utekelezaji wa awamu ya tatu REA, Wizara imeweza kulipa kiasi gani cha malimbikizo ya madeni ya miradi iliyopita ya REA?

Mheshimiwa Spika, katika mjadala wa Bajeti ya Nishati katika Bunge lako kwa Bajeti ya mwaka 2018/19 tulishuhudia kisanga cha mawaziri wa Nishati na Fedha kwa kutupiana lawama za ucheleweshaji wa Fedha za miradi ya REA huku wizara ya Fedha ikidai kuwa haijawahi kuchelewesha fedha za miradi na zote hupelekwa kwa wakala wa umeme vijijini (REA) kwa wakati. Naomba nimnukuu Naibu waziri wa Fedha, Mhe. Ashatu Kijaji kuwa kwa mwaka wa fedha wa 2017/18, julai REA ilipelekewa shilingi Bilioni 21.5, Agosti ikapelekwa shilingi Bilioni 36.7 na Septemba ilipelekwa shilingi Bilioni 35. Na kwa maneno yake, kuanzia Julai hadi Aprili 2018 REA walikuwa wamepewa jumla ya Bilioni 99.9. Kambi ya Upinzani Bungeni inapenda kuhoji, iwapo REA inapelekewa fedha kwa wakati ni kwa nini wakandarasi wanaendelea kuidai?
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inalitaka Bunge lako kuweka mkakati wa kukutana na wakandarasi wa miradi ya REA kupitia kamati ya kisekta ya Nishati na Madini ili kuweza kuweka bayana mapungufu ya kikandarasi yanasababisha kuwa na utekelezaji hafifu wa miradi ya REA na kuleta ripoti katika Bunge lako kabla ya kuhitimisha Bunge la Bajeti ya mwaka 2019/2020.


HITIMISHO.
Mheshimiwa Spika, kutokana na Serikali kutokuwa na utaratibu wa kutekeleza miradi yake ikakamilika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inashauri kwamba kwa maeneo ambayo gesi ilishaanza kuvunwa ambako ni Mnazi Bay na SongoSongo, serikali iwe na mkakati kabambe wa kuuza gesi kwa ajili ya matumizi mbalimbali. Takwimu zinaonesha kwamba gesi inayotumika kwa mwaka mzima ni kati ya aslimia 4.8 na 6 tu ya uwezo wa Bomba. Hii ni hasara kwa Taifa ikizingatiwa kuwa bomba la gesi limejengwa kwa mkopo wenye riba.
Mheshimiwa Spika, Sambamba na hilo, lazima serikali izingatie mgawanyo wa rasilimali fedha kwa sekta mbalimbali nchini kwa sababu kurundika rasilimali nyingi kwenye miradi michache kunaweza kusababisha kudumaa kwa miradi mingine ya maendeleo utakaosababishwa na ufinyu wa mgawanyo wa rasilimali fedha. Urundikwaji wa rasilimali fedha kwenye miradi michache kunathirika katika makadirio ya bajeti ya 2019/2020 katika Wizara ya Nishati ukijumlisha na Ujenzi zinachukua zaidi ya 50% ya bajeti yote ya nchi.
Hivyo, nihitimishe kwa kutaka Serikali kutekeleza mambo matano: Mosi; mikataba yote mikubwa inayohusu Ujenzi wa Mradi wa Umeme wa Rufiji (Stigglers Gorge) iletwe na kujadiliwa na Bunge. Pili, Tathmini ya Kimazingira na Upembuzi yakinifu kuhusu mradi tajwa iletwe na kujadiliwa na Bunge. Tatu, Mikataba yote mikubwa kuhusu Ujenzi wa Bomba kutoka Mtwara Mpaka Dar Es Salaam iwasilishwe na kupitiwa na Bunge. Nne, Serikali iwasilishe Bungeni Taarifa ya Utekelezaji wa Mapendekezo ya Kamati ya Bunge iliyoundwa na Spika (wakati huo Anna Makinda) kuchunguza kuhusu mgogoro kati ya wananchi na Serikali Mtwara juu ya ujenzi wa Bomba la Gesi. Tano, Serikali iwasilishe Bungeni Taarifa ya Utekelezaji wa maoni na mapendekezo ya Kamati iliyoundwa na Spika (Mheshimiwa Job Ndugai) kuchunguza mikataba na utafutaji na uvunaji wa gesi asili.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo naomba kuwasilisha.

...
John John Mnyika, (Mb)
MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI
WIZARA YA NISHATI

28/05/2019
 
Wataalamu wa bajeti hiki alichosoma mnyika Ni bajeti? Spika Ndugai nkuulize swali hi ndio bajeti mbadala ya Upinzani ya wizara ya nishati na madini? Ndugai umeniangusha ulichopokea Sio bajeti ya Upinzani loooo
 
Ni mradi gani wa maendeleo uliponya nchi..bora imepigwa chini ni upuuzi mtupu na wastage of time wa mambo ya bunge. Warudi wakamalizie muda majimboni kabla ya kuondoka kabisa 2020
 
1 Reactions
Reply
Back
Top Bottom