HOTUBA: Waziri wa Habari, Nape Nnauye akiwasilisha Makadirio ya Bajeti ya Mapato na Matumizi 2022/23

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Apr 18, 2017
2,801
11,961
Waziri wa Habari Nape Nnauye akiwasilisha Makadirio ya Bajeti ya Mapato na Matumizi 2022/23

Laini za simu
Aprili, 2021 - laini 52,965,816
Aprili, 2022 - Laini 55,365,239
Sawa na ongezeko la 4.5%

Watumiaji wa intaneti
Aprili, 2021 – Watu Milioni 29.1
Aprili, 2022 – Watu Milioni 29.9
Wawa na ongezeko la 2.7%

Watumaji, wapokeaji pesa mtandaoni (simu)
Aprili, 2021 watu 27,326,938
Aprili, 2022 - Watu 35,749,298
Sawa na ongezeko la 30.8%

----------------------

HOTUBA YA WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI MHESHIMIWA NAPE MOSES NNAUYE (MB.), AKIWASILISHA BUNGENI MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA KWA MWAKA WA FEDHA 2022/23

A. UTANGULIZI

Mheshimiwa Spika
,

Kufuatia taarifa iliyowasilishwa humu Bungeni na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, ninaomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu likubali kupokea na kujadili Taarifa ya Utekelezaji wa Mpango na Bajeti ya Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa Mwaka wa Fedha 2021/22.

Aidha, ninaomba Bunge lako Tukufu lijadili na kupitisha Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa Mwaka wa Fedha 2022/23.

Naomba hotuba yangu yote iingie kwenye kumbukumbu za Bunge kama ilivyowasilishwa mezani.

Mheshimiwa Spika,

Awali ya yote nichukue fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutujalia uhai na afya njema; na kutuwezesha sote kuwepo hapa kushiriki katika Mkutano huu wa saba wa Bunge la kumi na mbili.

Mheshimiwa Spika,

Kabla ya yote, nichukue fursa hii kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa uongozi wake madhubuti katika kipindi hiki cha zaidi ya mwaka mmoja ambacho kimekuwa na maendeleo na uwekezaji mkubwa katika sekta zote zinazogusa Maendeleo ya watu nchini.

Kwa hakika katika kipindi cha Mwaka mmoja wa uongozi wake kama Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameonyesha Uzalendo, Uwezo, Ujasiri, Uhodari na Mapenzi yake makubwa kwa nchi yetu na wananchi wake.Hatua kadhaa za kisera na kiutendaji alizochukua katika kipindi kifupi cha uongozi wake zimekuwa na mwangwi mkubwa uliopeleka Matumaini kwa waliokata tamaa,umepeleka upendo mahali palipo nyemelewa na chuki, umepeleka heshima mahali paliponyemelewa na dharau.

Utendaji huu uliotukuka umezigusa pia sekta za Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na wadau wake. Mheshimiwa Rais kwa makusudi tarehe 12 Septemba 2021 akaanzisha wizara inayojitegemea kwa ajili ya kushughulikia sekta za Habari,Mawasiliano na Teknolojia ya Habari,Muundo ambao umeongeza ufanisi katika kuzihudumia sekta husika.

Wizara inatambua matarajio makubwa waliyonayo wananchi ya kufikishiwa huduma za Habari na Mawasiliano kama ilivyofafanuliwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020 - 2025.

Mheshimiwa Spika,

Wizara hii ndio inayosimamia Mapinduzi ya Kidijitali nchini. Mapinduzi ya Kidijitali ndio yanayoweka msingi wa kulipeleka Taifa kwenye Uchumi wa Kidijitali unaowezeshwa na kuendeshwa na TEHAMA. Katika uchumi wa kidigitali, Sekta zote hufanya kazi kwa pamoja, kwa ushirikiano na muingiliano zikiwezeshwa na mazingira bora ya kidigitili. Mapinduzi haya yanawezeshwa na misingi muhimu ikiwemo Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na Mifumo ya Mawasiliano.

Mifumo hii imerahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi zikiwemo utunzaji, utumaji na upokeaji wa fedha (Financial Inclusion), usambazaji wa bidhaa, uwepo wa vyombo vya kisasa vya upashanaji Habari pamoja na uimara wa uhuru husika. Aidha, Uchumi wa Kidigitali unawekewa mazingira bora ya Kiudhibiti, kiuwekezaji na atamizi kwa ajili ya uanzishwaji na uendelezaji wa Kampuni changa za ubunifu (Startups).

Mheshimiwa Spika,

Wizara ina jukumu la kutunga na kusimamia Sera zinazohusiana na masuala ya Habari, Mawasiliano, na Teknolojia ya Habari, kuratibu na kusimamia vyombo vya Habari, Mawasiliano ya Posta na Simu, kuendeleza tafiti na ubunifu kwenye masuala ya TEHAMA, kuendeleza wataalam wa TEHAMA, Kuendeleza na kusimamia miundombinu ya Mawasiliano nchini.

Utekelezaji wa majukumu haya kutaiwezesha Tanzania kuimarika katika kushiriki uchumi wa kidijitali katika kufikia Mapinduzi ya Nne ya Viwanda (4th Industrial Revolution) yanayowezeshwa na kuendeshwa na TEHAMA na pia kuwa na jamii inayopata taarifa sahihi kama Mheshimiwa Rais alivyobainisha kwenye Hotuba yake aliyotoa hapa kwenye Bunge lako Tukufu tarehe 22 Aprili, 2021.

Mheshimiwa Spika,

Ninaomba nikupongeze wewe binafsi na Mheshimiwa Naibu Spika kwa kuchaguliwa na Waheshimiwa Wabunge kuongoza Bunge la 12. Ninapenda kulishukuru Bunge lako Tukufu kwa ushirikiano wao wakati wote ninapotekeleza majukumu yangu ikiwa ni pamoja na kuwasilisha taarifa mbalimbali kuhusu Wizara. Ninapenda kuwahakikishia kuwa, Wizara yangu itaendelea kutoa ushirikiano unaohitajika ili kufikia malengo ya maendeleo ya Taifa na ya mwananchi mmoja mmoja.

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari itaendelea kuhimiza matumizi ya TEHAMA katika kuharakisha utoaji huduma, kufanya biashara, uzalishaji viwandani na kutoa elimu kwa wananchi ili kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi na kujiletea maendeleo binafsi na ya Taifa kwa ujumla.

Aidha, kwa namna ya pekee nimshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuniamini na kuniteua kuongoza Wizara hii. Naomba kuwashukuru wapiga kura wa Jimbo la Uchaguzi la Mtama kwa kuendelea kunipa ushirikiano katika kujiletea maendeleo kwenye Jimbo letu; nawashukuru wadau mbalimbali kwa ushrikiano wao wakati wa kutimiza kazi zangu, bila kuisahau familia yangu kwa kuendelea kunipa ushirikiano katika kutekeleza majukumu yangu kwa Watanzania.

Mheshimiwa Spika,

Kwa upekee niishukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu inayoongozwa na Mheshimiwa Seleman Moshi Kakoso Mbunge wa Jimbo la Mpanda Vijijini na Makamu Mwenyekiti Mheshimiwa Anne Kilango Malecela Mbunge wa Jimbo la Same Mashariki. Wizara imenufaika sana na umahiri, uzoefu, umakini na ushirikiano wa Kamati hii katika kuchambua, kushauri na kufuatilia majukumu yanayosimamiwa na Wizara.Ninapenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba maoni, ushauri na mapendekezo yaliyotolewa na Kamati yamezingatiwa kikamilifu katika Hotuba hii.

Mheshimiwa Spika
,

Kwa masikitiko makubwa niungane na Waheshimiwa Wabunge wenzangu kutoa pole kwa ndugu, jamaa, marafiki na wananchi kwa kuondokewa na viongozi mbalimbali wakiwemo aliyekuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa na Mbunge wa Jimbo la Ushetu kwa tiketi ya CCM Elias John Kwandikwa, aliyekuwa Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu na Mbunge wa Jimbo la Ngorongoro kwa tiketi ya CCM William Ole Nasha, aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Konde Zanzibar kwa tiketi ya Chama cha ACT -Wazalendo, Khatib Said Haji na ailyekuwa Mbunge wa Viti Maalum kupitia CCM, Mkoa wa Rukwa, Irene Alex Ndyamkama. Ninaomba Mwenyezi Mungu azilaze roho za marehemu mahali pema peponi. Amina.

Mheshimiwa Spika,

Wizara inasimamia Taasisi Nane zilizogawanyika kwenye umahsusi wa Huduma, udhibiti, mfuko, mashirika ya kibiashara na taasisi wezeshi. Taasisi hizo ni: Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA); Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL); Shirika la Posta Tanzania (TPC); Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC); Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN); Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF); Tume ya TEHAMA (ICTC); na Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano (TCRA-CCC). Hotuba hii itaelezea kwa ufupi masuala mbalimbali yanayotekelezwa na Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari pamoja na taasisi inazosimamia.

B. MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA MPANGO NA BAJETI YA WIZARA YA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI NA TAASISI ZAKE KWA MWAKA WA FEDHA 2021/22

Ukuaji wa Sekta ya Habari na Mawasiliano

Mheshimiwa Spika
,

Kulingana na Kitabu cha Hali ya Uchumi wa Taifa cha mwaka 2020, Sekta ya Habari na Mawasiliano imekua kwa kasi ya asilimia 8.4 mwaka 2020. Ukuaji huu unathibitishwa na ongezeko la upatikanaji na matumizi ya huduma za mawasiliano na kusambaa kwa huduma zitolewazo na vyombo vya habari. Kulingana na uchambuzi uliofanywa na Wizara, Mwaka 2021 asilimia 69 ya ardhi ya Tanzania inafikiwa na huduma ya mawasiliano ya simu za kiganjani.

Mheshimiwa Spika,

Sekta ya Mawasiliano imeendelea kukua, takwimu zinaonyesha kuwa laini za simu zilizosajiliwa zimeongezeka kutoka 52,965,816 Mwezi Aprili, 2021 hadi kufikia laini 55,365,239 Mwezi Aprili, 2022 sawa na ongezeko la asilimia 4.5. Watumiaji wa intaneti wameongezeka kutoka Milioni 29.1 Mwezi Aprili, 2021 hadi kufikia Milioni 29.9 Mwezi Aprili, 2022 sawa na ongezeko la asilimia 2.7. Watumiaji wa huduma za kutuma na kupokea pesa kwa njia ya mtandao wa simu wameongezeka kutoka 27,326,938 Mwezi Aprili, 2021 hadi kufikia 35,749,298 mwezi Aprili, 2022 sawa na ongezeko la asilimia 30.8. Aidha, Watoa huduma wa Miundombinu ya Mawasiliano wamefikia 23 ukilinganisha na watoa huduma 19 Mwezi Aprili, 2021 (hii ni sawa na ongezeko la asilimia 21.1).

Watoa huduma wa huduma za ziada (Application Services and Value Added Services) wamefikia 102 ukilinganisha na watoa huduma 66 Mwezi Aprili, 2021 (ongezeko la asilimia 54.5). Pia, Bei ya mwingiliano kati ya watoa huduma (Voice interconnection Charges) imeshuka kutoka Shilingi 2.6 kwa dakika mwaka 2021 hadi Shilingi 2.0 kwa dakika mwaka 2022 (punguzo la asilimia 23.1). Vituo vya kurusha matangazo ya redio vimeongezeka kutoka vituo 200 mwaka 2021 hadi kufikia vituo 210 Mwezi Aprili, 2022 na vituo vya kurusha matangazo ya runinga vimeongezeka kutoka vituo 50 mwaka 2021 na kufikia vituo 56 Mwezi Aprili, 2022.

Cable Television zimeongezeka kutoka 40 Mwezi Aprili, 2021 na kufikia 59 Mwezi Aprili, 2022 na magazeti yameongezeka kutoka 272 na kufikia 284 Mwezi Aprili, 2022. Serikali imeendelea kuweka mazingira rafiki ya matumizi ya teknolojia za Utangazaji hasa maudhui mtandaoni ambayo pia yamechangia kuongeza ajira kwa vijana. Hadi kufikia Mwezi Aprili, 2022 televisheni mtandao zimeongezeka kutoka 552 hadi 663 sawa na ongezeko la asilimia 20.1, blogu zimeongezeka kutoka 134 hadi 148 sawa na ongezeko la asilimia 10.4 na redio mtandao zimeongezeka kutoka 25 hadi 27 sawa na ongezeko la asilimia 8.0.

Mheshimiwa Spika,

Takwimu za mwezi Aprili, 2022, zinaonesha kuwa asilimia 95 ya Watanzania wapo kwenye maeneo yenye mtandao wenye uwezo wa kutoa huduma za simu za sauti na jumbe fupi, yaani 2G network kupitia minara 12,228. Aidha, asilimia 68 ya Watanzania wapo kwenye maeneo yenye Mtandao wenye uwezo wa kutoa huduma za intaneti ya kasi ya 3G kupitia minara 11,753 na asilimia 45 wapo kwenye maeneo yenye Mtandao wa 4G kupitia Minara 6,656.

Hata hivyo pamoja na kwamba asilimia 68 wapo kwenye maeneo yenye huduma ya intaneti, ni asilimia 27 tu ya watumiaji wa huduma za mawasiliano wenye simu janja au vifaa vingine vya mawasiliano (laptop, tablets, iPad, n.k.) vyenye uwezo wa kutumia intaneti. Jitihada za serikali kuondoa kodi kwenye vifaa vya simu katika mwaka wa fedha 2021/22, pamoja na watoa huduma kutengeneza taratibu mbalimbali za kuwakopesha wateja wao simu kumeongeza idadi ya simu janja kwa takribani asilimia 2 tu kulinganisha na mwaka uliopita.

Matumizi ya TEHAMA pamoja na teknolojia zinazoibukia kama Artificial Intelligence (AI), Internet of Things (IoT), Blockchain na nyinginezo yanawezesha ujenzi wa miji ya kisasa na endelevu. Haya yote yanahitaji miundombinu thabiti na intaneti ya kasi. Upatikanaji na utumiaji wa huduma ya intaneti ya 4G kwa wananchi wengi unatarajiwa kuleta mageuzi makubwa katika uchumi wa kidigiti. Serikali imeendelea kuweka mazingira wezeshi kwa watoa huduma/wawekezaji

kujenga Miundombinu ya Mawasiliano ya Intanenti ya kasi ili kuongeza wigo (coverage) wa mitandao na kuimarisha ubora wa huduma za Mawasiliano ili kufikisha intaneti ya kasi kwa asilimia 80 ya Watanzania ifikapo mwaka 2025.

Mheshimiwa Spika,

Pamoja na uwezo wa kuridhisha wa Intaneti ya 4G na uwekezaji unaondelea, Serikali kupitia TCRA imeshachukua hatua za kutengeneza Mkakati wa kuchochea miundombinu inayowezesha intaneti ya kasi ya 5G. Mkakati huu unahusisha pamoja na mambo mengine kupanga na kuweka masafa yatakayowezesha uwekezaji kwenye mitandao ya 5G. Serikali kupitia TCRA ipo tayari kutoa Masafa kwa watoa huduma ambao wangependa kufanya majaribio ya teknolojia ya 5G (5G Trials). Utaratibu wa kugawa masafa yaliyobainishwa kutumika kwa teknolojia ya 5G utakuwa wa ushindani (Transparent & Competitive Process).

Ukusanyaji wa Mapato

Mheshimiwa Spika
,

Hadi kufikia tarehe 30 Aprili, 2022 Wizara imekusanya jumla ya Shilingi 41,098,538,762.15 kutokana na mauzo ya huduma za Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano ambayo ni sawa na asilimia 82.2 ya makadirio ya makusanyo ya Shilingi bilioni 50; na kiasi cha Shilingi 8,621,793,488 kutokana na tozo ya kuongeza salio kwenye laini za simu sawa na asilimia 2.2 ya lengo la Shilingi bilioni 446.3.

Aidha, Idara ya Habari-MAELEZO imekusanya Shilingi 354,190,750 kutokana na mauzo ya picha za Viongozi Wakuu wa nchi na picha ya Baba wa Taifa, vitambulisho, machapisho na ada ya mwaka ya magazeti sawa na asilimia 199 ya lengo la Shilingi milioni 178.02. Kuvuka kwa malengo ya makusanyo kumetokana na kuuzwa kwa wingi kwa picha za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania baada ya kuapishwa.

Bajeti iliyoidhinishwa na Bunge Mwaka wa Fedha 2021/22

Mheshimiwa Spika,

Katika Mwaka wa Fedha 2021/22 iliyokuwa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari iliidhinishiwa kutumia kiasi cha Shilingi 246,384,551,000. Kati ya fedha hizo Shilingi 4,984,770,000 iliidhinishwa kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na Shilingi 241,399,781,000 iliidhinishwa kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo. Aidha, Idara ya Habari - MAELEZO na Taasisi za TBC na TSN ilikuwa imetengewa bajeti ya jumla ya Shilingi 23,744,630,000 kutoka Mfuko Mkuu wa Serikali, ambapo Shilingi 17,743,630,000 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Shilingi 6,001,000,000 ni kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo.

Bajeti ya Matumizi ya Kawaida

Mheshimiwa Spika,

Hadi kufikia tarehe 30 Aprili, 2022 Wizara imepokea na kutumia jumla ya Shilingi 6,947,838,745.79 sawa na asilimia 84 ya fedha zilizotengwa. Kati ya fedha za matumizi ya kawaida zilizopokelewa Shilingi 2,288,345,600.00 ni za Mishahara na Shilingi 4,659,493,145.79 ni Matumizi Mengineyo.

Bajeti ya Miradi ya Maendeleo

Mheshimiwa Spika,

Hadi kufikia tarehe 30 Aprili, 2022 Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari (Fungu 68) imepokea jumla ya Shilingi 129,713,798,179.86 kwa ajili ya utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo ambayo ni asilimia 53.7 ya fedha zilizotengwa.

Utekelezaji wa Majukumu ya Wizara

Mheshimiwa Spika,

Kwa Mwaka wa fedha wa 2021/2022 Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) imeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya kufikisha huduma za mawasiliano vijijini na mijini kusiko na mvuto kibiashara. Hadi sasa utekelezaji wa miradi hiyo upo katika hatua mbalimbali ambapo ujenzi wa minara 181 (passive part) umekamilika na kwa sasa hivi watoa huduma wapo katika hatua za kuagiza vifaa vya kurushia mawimbi ya simu na hatimaye kuwashwa kwa minara hiyo. Minara hii inategemewa kuwashwa kabla ya mwezi Oktoba 2022.

Mheshimiwa Spika,

Serikali kupitia UCSAF imengia makubaliano na watoa huduma za mawasiliano kwa ajili ya kujenga minara 161 Tanzania Bara na Visiwani. Minara hii itajengwa katika maeneo ya mipakani, Maeneo ya Ofisi za Wakurugenzi wa Halmashauri ambazo zilikuwa hazina huduma za mawasiliano pamoja na Zanzibar. Ujenzi wa minara hii upo katika hatua mbalimbali. Kwa upande wa Zanzibar ujenzi wa minara 42 upo katika hatua za ukamilshwaji ambapo ujenzi wa minara hiyo unatarajiwa kukamilika mwezi Juni, 2022. Kwa upande wa miradi mingine 119 ujenzi ipo katika hatua za awali ikiwa ni pamoja na kutafuta maeneo kwa ajili ya ujenzi pamoja na kutafuta wakandarasi. Utekelezaji wa majukumu katika maeneo mengine ni kama ifuatavyo:

Eneo la Mawasiliano

Mheshimiwa Spika
,

Katika Mwaka wa Fedha 2021/22 Wizara katika Eneo la Mawasiliano imetekeleza majukumu yafuatayo:

i. Kuanza maandalizi ya kuhuisha Sera ya Mawasiliano ya Simu ya Mwaka 1997 na Mkakati wa Utekelezaji wa Sera ya Taifa ya TEHAMA.

ii. Kuendelea kuratibu ujenzi wa jengo la Makao Makuu ya Umoja wa Posta la Afrika (Pan Africa Postal Union – PAPU) jijini Arusha lenye urefu wa ghorofa 18. Ujenzi wa jengo kwa ujumla wake umefikia asilimia 65;

iii. Kuendeleza mashirikiano ya Kikanda na Kimataifa ambapo Wizara imeshiriki Mkutano Mkuu wa Umoja wa Posta Duniani (UPU) uliofanyika tarehe 9 – 27 Agosti, 2021 Abidjan, Ivory Coast; ambapo chaguzi mbalimbali za viongozi na Mabaraza zilifanyika na Tanzania kufanikiwa kushinda nafasi ya Ujumbe wa Baraza la Utawala ; na Baraza la Uendeshaji la Posta kwa kipindi cha miaka minne (2021 - 2025). Sambamba na hilo, Tanzania imepata nafasi ya Kuongoza Kamati ya Huduma za Posta na Biashara Mtandao ya Umoja wa Posta Duniani.

iv. Kuendelea kuratibu jitihada za ufikishaji wa huduma za mawasiliano ya simu katika maeneo ambayo bado hayajafikiwa na yenye mawasiliano hafifu. Masuala yaliyofanyika ni pamoja na: ukaguzi wa hali ya mawasiliano katika maeneo mbalimbali ikiwemo eneo la Pori Tengefu la Loliondo lenye kata 15, visiwa 171 vya Ziwa Victoria, maeneo ya Kanda ya Ziwa, Kanda ya Juu Kusini, Kanda ya Kati na Pwani. Maeneo yaliyobainishwa yatafikishiwa huduma kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote. Aidha, katika kuratibu jitihada hizi za ufikishaji wa huduma za mawasiliano, Wizara imeandaa Mkakati wa Kuimarisha Mawasiliano wa kipindi cha miaka minne (2021/22 - 2024/25) ili kuboresha huduma za mawasiliano nchini.

v. Kufanya mapitio ya sekta ndogo ya utangazaji na mfumo wa leseni ili kuweka mazingira wezeshi kwa maendeleo ya sekta..

vi. Wizara imetoa leseni 25 kwa ajili ya kutoa huduma mbalimbali kupitia Sekta ya Mawasiliano na TEHAMA.

Eneo la Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA)

Mheshimiwa Spika
,

Katika Mwaka wa Fedha 2021/22 Wizara imetekeleza majukumu yafuatayo:-

i. Kukamilisha uaandaaji wa Mkakati wa Taifa wa intaneti yenye kasi (National broadband Strategy);

ii. Kuandaa Mwongozo wa Kitaifa wa Kushughulikia masuala ya uhalifu wa mtandao unaoongeza uratibu wa pamoja kwa taasisi zote zinazoshughulikia masuala ya uhalifu ya kimtandao.

iii. Kuingia Mkataba wa Mashirikiano na TANESCO kwa ajili ya kufanya kazi pamoja ya kupitisha miundombinu ya mawasiliano kwenye nguzo za umeme kwa lengo la kuongeza mtandao wa mawasiliano na wa umeme. Hatua hii imepunguza gharama za ujenzi wa Mkongo na kuharakisha mradi huu ambapo zilikuwa zijengwe Kilomita 1,880 lakini kutokana na Mkataba huu zitajengwa Kilomita 4,442 na kufikisha jumla ya Kilomita 12,761 za Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano.

iv. Kuratibu utengenezaji wa Mfumo wa kutunza na kuchakata taarifa za kesi na matukio ya uhalifu wa usalama mtandao “cybercrimes module” inayowezesha matukio ya uhalifu kutunzwa na kufuatilia mwenendo wa mashtaka husika hadi kukamilika wake;

v. Kutoa Mafunzo kwa Waendesha Mashtaka, Wachunguzi na Wapelelezi 197 pamoja na mafunzo ya kutumia “cybercrimes module” kwa watumishi 470 wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka;

vi. Kukamilisha uandaaji wa rasimu ya Mkakati wa Uchumi wa Kidijitali (Digital Economy Strategic Framework) kwa ajili ya kuchochea matumizi ya TEHAMA kwenye sekta zote za uchumi;

vii. Kukamilisha uandaaji wa Mwongozo wa Mageuzi ya Kidijitali (Digital Transformation Guideline) kwa ajili ya kutoa mwongozo wa Taasisi zote nchini wa kuelekea uchumi wa kidijitali;

viii. Kukamilisha uandaaji wa Programu ya Mafunzo ya TEHAMA yatakayopelekea kuongeza ujuzi na ubobezi wa wataalamu wa ndani ili kuendana na mahitaji ya sasa ya Uchumi wa Kidijitali;

ix. Ukamilishwaji wa Mkakati wa Taifa wa Elimu kwa Umma wa Usalama Mtandao (National Cyber Security Communication Strategy), 2021/22 – 2024/25; na

x. Kukamilisha na kuingia Makubaliano ya Ushirikiano kwenye maeneo ya TEHAMA na nchi ya Rwanda. Aidha, majadiliano na nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Uganda, Kenya, Marekani, Ujerumani, Uturuki na Falme za Kiarabu yanaendelea.

Xi. Kuanza mchakato wa kuhamishia shughuli za ujenzi,usimamizi na uendeshaji wa Mkongo wa Taifa wa mawasiliano kwa Shirika la Mawasiliano la Taifa (TTCL).

Eneo la Habari-MAELEZO

i. Kuisemea Serikali kuhusu utekelezaji wa Sera, Mikakati, Miradi na Programu zinazotekelezwa na Serikali kupitia Msemaji Mkuu wa Serikali. Jumla ya taarifa 18 zimetolewa kupitia vyombo vya habari.

ii. Kuratibu ratiba za Mawaziri na Viongozi kuzungumza kupitia Runinga na pia kukutana na Waandishi wa Habari kuelezea mafanikio na utekelezaji wa Serikali ya Awamu ya Sita katika Wizara zao.

iii. Kuandaa, kuchapisha na kusambaza nakala 5,000 za Jarida la Nchi Yetu lenye kuelezea mafanikio na utekelezaji wa mwaka immoja wa Serikali ya Awamu ya Sita tangu iingie madarakani tarehe 19 Machi, 2021. Kutokana na mahitaji ya toleo hili kuwa makubwa, Wizara imechapisha nakala nyingine 10,000 na kuzisambaza katika ofisi mbalimbali za Serikali, Sekta binafsi pamoja na kuwapatia wananchi;

iv. Kukusanya na kusambaza habari kuhusu utekelezaji wa miradi ya Serikali, ambapo Jumla ya habari 3,411, Makala 37, habari picha 529 katika magazeti, habari 49 katika Runinga, habari 1,600 katika “blogs” na mitandao ya kijamii zilichapishwa na kutangazwa;

v. Kuendelea kuhamasisha Vyombo vya Habari vya Nje ya nchi kuitangaza Tanzania ambapo vyombo vya habari vya nje vikiwemo CCTV, DW, BBC, Voice of Amerika, Xinhua na CGTV vilishiriki katika kuitangaza Tanzania na shughuli za utekelezaji wa Serikali;

vi. Katika kuimarisha uhuru wa vyombo vya habari; Serikali imetoa jumla ya leseni mpya 19 kwa magazeti hivyo kufanya Jumla ya vyombo vya Habari vilivyosajiliwa kufikia 285.

vii. Kuhuisha Kanuni za Utangazaji kwa njia ya Kidijitali za Mwaka 2018 ili kuruhusu watoa huduma wanaotoa maudhui ya bila malipo kwa wananchi (Free to Air – FTA) kubebwa katika visimbuzi vya kulipia; na

viii. Kuendelea kuratibu maandalizi ya Mkakati wa Taifa wa Mawasiliano (National Communication Strategy – NCS).

ix. Kuratibu Mkutano wa siku ya Uhuru wa vyombo vya habari Duniani ambao kwa Afrika ulifanyikia jijini Arusha Tanzania.

Utekelezaji wa Masuala Mengine

Mheshimiwa Spika,

Katika Mwaka wa Fedha 2021/22 Wizara imetekeleza majukumu mengine kama ifuatavyo:

ix. Kuhuisha sheria tatu (3) na Kanuni nne (4) za Sekta; sheria zilizohuishwa ni Sheria ya EPOCA ya Mwaka 2010; Sheria ya Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) ya Mwaka 2006; na Sheria ya Posta ya Mwaka 1993. Sheria hizi zimehuishwa ili kuboresha utendaji wa Taasisi husika na mazingira ya huduma za mawasiliano. Kanuni zilizohuishwa ni Kanuni za Leseni za Mwaka 2018; Kanuni za Utangazaji Kidijitali za Mwaka 2018; Kanuni za Maudhui ya Mtandaoni za Mwaka 2020; na Kanuni za Utangazaji Redioni na kwenye Runinga.

x. Kuratibu na kusimamia uandaaji wa Nyaraka za Baraza la Mawaziri za kutunga Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (Personal Data protection) na Sheria ya TEHAMA na kuhuisha Sheria ya Huduma ya Habari;

xi. Kuhuisha Mpango Mkakati wa Wizara kwa kipindi cha miaka mitano (2021/22 – 2025/26) kujumuiasha Idara ya Habari-MAELEZO;

xii. Kuajiri Mtumishi mmoja (1), kupandisha vyeo watumishi 46, kufanyika uhamisho wa watumishi 27 kutoka Taasisi mbalimbali za Serikali. Aidha, Muundo mpya wa Wizara umeandaliwa baada ya kuanzishwa kwa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari;

xiii. Kuandaa Mpango wa vihatarishi wa Wizara na rejesta ya vihatarishi (risk register) na Mafunzo ya vihatarishi kwa watumishi wote wa Wizara yametolewa;

xiv. Bodi za Wakurugenzi wa Taasisi tatu (3) ambazo ni Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Tume ya TEHAMA, na Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) zimeteuliwa; na

xv. Usimamizi wa ujenzi wa Jengo la Makao Makuu ya Wizara – Mtumba, lenye ghorofa saba ambapo hivi sasa lipo katika hatua ya ghorofa ya kwanza.

Utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo

Mradi wa Ujenzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano

Mheshimiwa Spika,

Mradi wa Ujenzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano umekusudiwa kupanua mawasiliano ya simu na intaneti nchini na nchi zinazotuzunguka katika kufanikisha mapinduzi ya kidijitali. Katika kipindi kinachoishia Mwezi Aprili, 2022 kazi zifuatazo zimefanyika:

i. Kukamilika kwa ujenzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano Kilomita 265 (Itigi – Manyoni - Rungwa);

ii. Kukamilika kwa Ujenzi wa Kilomita 72 za Mkongo wa kuunganisha Ofisi za Serikali (Kikombo – Mtumba – Msalato);

iii. Kukamilika kwa Ujenzi wa Kilomita 72 za Mkongo wa Taifa kwenye eneo la Mtambaswala kuunganisha Tanzania na Msumbiji;

iv. Kukamilika kwa Upembuzi yakinifu kuunganisha Mkongo wa Taifa na nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na nyaraka ya zabuni zimeandaliwa;

v. Kukamilika kwa kazi ya kukarabati Kilomita 105 za ujenzi wa mkongo Arusha – Namanga kupitia miundombinu ya TANESCO;

vi. Kukamilika kwa Ujenzi wa Kituo cha Kutolea Huduma za Mkongo wa Taifa kwenye Mji wa Serikali Mtumba;

vii. Kukamilika kwa taratibu za manunuzi za kuwezesha ujenzi wa Kilomita 4,442 za Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, upanuzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kutoka kiwango cha 200G hadi 800G na kujenga vituo vipya 37 na upanuzi wa vituo 75 vya kutolea huduma za Mkongo ambapo mikataba 22 yenye thamani ya Shilingi Bilioni 141 imesainiwa. Aidha, utekelezaji huu utafikisha Mkongo katika Wilaya 23 nchini.

viii. Kukamilika kwa Upanuzi wa Mkongo wa Taifa kwenye vituo 5 vya Kigoma, Arusha, Babati, Tunduma na Mbeya vyenye jumla ya kadi za kuchakata huduma (line processing cards) 30; na

ix. Kukamilika kwa kazi ya kuhamisha Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano wenye urefu wa Mita 250 eneo la Mkazi – Katavi kutokana na kujengwa kwenye eneo la makazi ya watu.

Mradi wa Mfumo wa Anwani za Makazi

Mheshimiwa Spika
,

Kufuatia malengo ya Serikali ya kukamilisha Anwani za Makazi kabla ya Sensa ya Watu na Makazi itakayofanyika Mwezi Agosti, 2022, katika Kikao kazi cha Wakuu wa Mikoa kilichofanyika tarehe 08 Februari, 2022; Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan alielekeza Mfumo wa Anwani za Makazi kutekelezwa kwa Mfumo wa Operesheni, aliyoipa jina la “OPERESHENI ANWANI ZA MAKAZI”. Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI zimeendelea na utekelezaji wa Mradi chini uratibu wa Ofisi ya Waziri Mkuu.

Katika Mwaka wa Fedha 2021/22 shughuli nyingine zilizotekelezwa ni pamoja na:

i. Kuunda Programu Tumizi (Mobile application) ya Mfumo iliyoongeza ufanisi katika matumizi na utekelezaji wa Mfumo. Programu Tumizi imetumika katika kukusanya taarifa za barabara/ mitaa/ njia, makazi na wakazi sambamba na kumuongoza mtu kutoka anwani ya makazi moja kwenda anwani ya makazi nyingine;

ii. Semina ya kujenga uelewa kuhusu Mfumo wa Anwani za Makazi imetolewa kwa Viongozi 483 ambao ni Wakuu wa Mikoa; Katibu Tawala wa Mikoa; Wenyeviti na Wakurugenzi wa Halmashauri; na Wajumbe wa ALAT; sambamba na Wataalam 616 wa Mikoa na Halmashauri

iii. Hadi kufikia tarehe 18 Mei, 2022 jumla ya anwani za makazi 12,339,471 zimekusanywa na kuingizwa kwenye Programu Tumizi. Idadi ya Anwani zilizokusanywa ni asilimia 106.53 ya lengo la jumla ya Anwani 11,583,564 zilizopangwa kukusanywa katika Mikoa yote nchini. Aidha, kazi ya kuweka miundombinu ya Anwani za makazi inaendelea kote nchini ambapo jumla ya nguzo mpya 74,040 zimesimikwa kati ya 672,952 zinazotarajiwa sawa na asilimia 11 kwa makadirio ya chini kwa wastani wa nguzo 2 kwa kila barabara na jumla ya vibao vya namba za nyumba 906,206 vimebandikwa kati ya 10,537,253 vinavyohitajika sawa na asilimia 9 kama ilivyokuwa jana tarehe 18 Mei, 2022.

Mradi wa Tanzania ya Kidijitali

Mheshimiwa Spika
,

Mradi wa Tanzania ya Kidigitali una thamani ya Dola za Marekani Milioni 150 na ulisainiwa rasmi tarehe 19 Agosti, 2021. Mradi huu unalenga kuboresha na kukuza maunganisho ya ndani na ya kimataifa ili kuweza kufikisha huduma za mawasiliano pamoja na utoaji wa huduma mbalimbali za Serikali kwa Wananchi. Vilevile, mradi huu unalenga kuboresha ubunifu pamoja na kuwajengea uwezo wataalam wa TEHAMA nchini.

Kazi zilizotekelezwa ni:-

i. Ukamilishaji wa ujenzi wa jengo la Ofisi ya Mradi katika eneo la Area D na kuanza kutumika rasmi tarehe 01 Oktoba, 2021;

ii. Kukamilisha usanifu na kuandaa mahitaji ya kuwezesha ununuzi wa bando la intaneti ya Serikali (Government internet bandwidth) kwa ajili ya matumizi ya Taasisi za Umma;

iii. Kukamilisha usanifu na kuandaa mahitaji kuwezesha kujenga na kuboresha Mtandao wa TEHAMA unaounganisha Taasisi za Serikali (GovNET);

iv. Kukamilisha ukusanyaji wa mahitaji kuwezesha kujenga na kupandisha hadhi minara 150 ya mawasiliano kutoka teknolojia ya 2G kwenda 3G/4G ili kuwezesha huduma za intaneti yenye kasi kwenye maeneo hayo;

v. Kukamilisha manunuzi ya vifaa na programu endeshi za kuboresha vituo mahiri vya kuhifadhia Data (National Internet Data Centre - NIDC na Government Data Centre);

vi. Kufanya tathmini ya maeneo ya kujengewa uwezo kwa watumishi wa TEHAMA Serikalini ambapo jumla ya watumishi 450 watapatiwa mafunzo ya muda mfupi na watumishi 50 watapatiwa mafunzo ya muda mrefu; na

vii. Kufanya maandalizi ya kuwezesha ujenzi wa Chuo cha TEHAMA ambapo eneo lenye ukubwa wa Hekta 400 limepatikana eneo la Nala, Jijini Dodoma.

Mheshimiwa Spika,

Utekelezaji wa Majukumu ya Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari umeainishwa katika Ukurasa wa 27 hadi 63 wa Kitabu cha Hotuba ya Bajeti.

C. MPANGO NA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA KWA MWAKA WA FEDHA 2022/23

Makadirio ya Mapato ya Wizara

Mheshimiwa Spika
,

Katika Mwaka wa Fedha 2022/23, Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari (Fungu 68) inakadiria kukusanya kiasi cha Shilingi 150,700,000,000 ambazo zitatokana na mauzo ya huduma za Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, tozo itokanayo na kuongeza salio la simu, usajili wa Magazeti, ada ya mwaka ya Magazeti, vitambulisho vya Waandishi wa Habari na machapisho ya picha, mabango na majarida.

MALENGO YA BAJETI YA WIZARA YA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI

Mheshimiwa Spika
,

Kama nilivyoeleza awali, Wizara yangu inasimamia Mapinduzi ya Kidijitali na kuimarisha uhuru wa vyombo vya habari nchini. Mapinduzi ya Kidijitali ndio yanayoweka Msingi wa kulipeleka Taifa kwenye Uchumi wa Kidijitali unaowezeshwa na kuendeshwa na TEHAMA. Ili kuwezesha mageuzi na mapinduzi haya kwenye Sekta zote za Uchumi na Kijamii, Wizara imepenga kufanya mabadiliko na maboresho makubwa kwenye Sekta ili kuendana na mageuzi haya ikiwemo kuharakisha uendelezaji na usimamiaji miundombinu ya TEHAMA, Mawasiliano, Posta na Habari kama vile Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, anwani za makazi, mitambo ya utangazaji na Posta.

Vilevile, kufanya mapinduzi kwenye Taasisi za Sekta; kuimarisha mashirikiano na Sekta binafsi, kuendeleza tafiti na ubunifu kwenye masuala ya TEHAMA, kuwajengea uwezo watumishi kuendana na mapinduzi haya, kuwezesha Sekta nyinginezo kuelekea kwenye mapinduzi haya ya kidijitali; na kuimarisha uhuru wa vyombo vya habari. Aidha, Wizara imekusudia kufanya mageuzi kwenye taasisi zake ikiwemo TCRA kuwa mlezi na mwezeshaji zaidi wa watoa huduma za Mawasiliano na habari. kufanya mageuzi kwenye Shirika la Posta Tanzania na Shirika la Mawasiliano ili kutoa huduma zake kimapinduzi na kwa weledi.

Eneo la Mawasiliano

Mheshimiwa Spika,

Katika Mwaka wa Fedha 2022/23, Wizara imepanga kutekeleza majukumu yake kama ifuatavyo:-

i. Kufanya mapitio ya Sera ya Taifa ya Mawasiliano ya Simu ya Mwaka 1997;

ii. Kukamilisha kazi ya kuhuisha Sera ya Taifa ya Posta ya Mwaka 2003 na maandalizi ya Mkakati wa utekelezaji;

iii. Kuandaa Mkakati wa utekelezaji wa Sera ya Taifa ya TEHAMA ya Mwaka 2016;

iv. Kufanya mapitio ya Sheria za Kisekta na Kanuni zake;

v. Kusimamia utendaji wa Taasisi zilizo chini ya Wizara;

vi. Kuimarisha ushirikiano wa Sekta Kitaifa, Kikanda na Kimataifa;

vii. Kusimamia uboreshaji wa huduma za mawasiliano ya simu na Posta ili kufikia wananchi wote;

viii. Kuendelea kutekeleza Mfumo wa Anwani za Makazi nchini;

ix. Kusimamia utekelezaji wa mradi wa Huduma Pamoja;

x. Kusimamia upembuzi yakinifu utakaowezesha biashara Mtandao (e-Commerce); na

xi. Kuratibu masuala ya kukuza uwekezaji katika Sekta ya Mawasiliano.

Eneo la Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA
)

Mheshimiwa Spika
,

Katika Mwaka wa Fedha 2022/23 Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari inatarajia kutekeleza majukumu yake kama ifuatavyo:-

i. Kukamilisha uandaaji wa Mkakati wa Kitaifa wa Uchumi wa Kidijitali (National Digital Economy Strategy) na kusimamia utekelezaji wake;

ii. Kuratibu na kuwezesha ujenzi wa Mfumo wa TEHAMA kuratibu utendaji kazi wa Wizara;

iii. Kusimamia utekelezaji wa Mkakati wa Kitaifa wa Usalama wa Mitandao (National Cyber Security Strategy);

iv. Kusimamia utekelezaji wa Mkakati wa Mtandao wa TEHAMA wenye kasi zaidi (National Broadband Strategy);

v. Kuendelea kuwaendeleza wataalamu 200 kwenye maeneo ya TEHAMA yenye uhaba wa ujuzi;

vi. Kuandaa na kusimamia utekelezaji wa Miongozo ya kuimarisha masuala ya utafiti na ubunifu katika TEHAMA;

vii. Kuendelea kuimarisha usalama wa mitandao, kuongeza udhibiti wa taarifa binafsi na kupunguza uhalifu wa mitandao kwa kushirikiana na Vyombo vya Usalama,

viii. Kuimarisha mashirikiano na mashirika ya mawasiliano ya Kikanda na Kimataifa; na

ix. Kukamilisha mchakato wa kuhamishia ujenzi,usimamizi na uendeshaji wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kwa Shirika la Mawasiliano nchini (TTCL).

x. Kupitia upya utaratibu unaotumika katika usimamizi wa Data Center.

Eneo la Habari – MAELEZO

i. Kukusanya taarifa na kuisemea Serikali kuhusu utekelezaji wa Sera, Mikakati, Miradi na Programu inazozitekeleza;

ii. Kufanya mapitio ya Sera ya Habari na Utangazaji ya Mwaka 2003 ili kuifanya iendane na mabadiliko katika Sekta ya Habari;

iii. Kufanya mapitio katika Sheria ya Huduma za Habari ya Mwaka 2016 na Kanuni zake za Mwaka 2017;

iv. Kuanzisha Bodi ya Ithibati ya Wanahabari, Baraza Huru la Habari na Mfuko wa Mafunzo kwa Wanahabari;

v. Kusimamia utekelezaji wa Sera,Sheria na kanuni mbalimbali za Habari na Utangazaji nchini.

vi. Kuchapa nakala 12,794 za Picha za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nakala 12,794 za Picha za Baba wa a Taifa Mwl. Julius K. Nyerere, nakala 4,000 za Jarida la Nchi Yetu na nakala 2,000 za Bango la Baraza la Mawaziri (Cabinet posters);

vii. Kuchapa na kutoa leseni za magazeti na vitambulisho vya waandishi wa Habari;

viii. Kutoa miongozo na kufanya tathmini ya utoaji taarifa kwa umma kwa kila Taasisi;

ix. Kuhamasisha Vyombo vya Habari vya nje ya nchi katika kuitangaza Tanzania;

x. Kuanza Utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Mawasiliano (National Communication Strategy – NCS);

xi. Kuanzisha Kipindi Maalum cha Ongea na Waziri; na

A xii. Kujenga Studio maalum kwa ajili ya Vipindi vya Moja kwa Moja vya redio na runinga.

Miradi Itakayotekelezwa na Wizara kwa Mwaka wa Fedha 2022/23

I: Mradi wa Ujenzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano

Mheshimiwa Spika

Wizara imeanza mchakato wa kuhamishia shughuli za Kujenga na kuendesha Mkongo wa taifa wa mawasiliano kwa Shirika la mawasiliano nchini TTCL. Mchakato huu utakamilika mwanzoni mwa mwaka wa fedha wa 2022/2023.

Katika Mwaka wa Fedha 2022/23 Wizara imekadiria kutumia Shilingi 149,700,000,000 ambapo Shilingi 149,000,000,000 ni fedha za ndani na Shilingi 700,000,000 ni fedha za nje kwa ajili ya kutekeleza kazi ya ujenzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano. Fedha hizi zitatumika kujenga Kilomita 1,600 za Mkongo na Vituo vipya 15 vya kutolea huduma za Mkongo ili kuongeza wigo wa utoaji wa huduma za Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano hadi kufikisha ngazi za Wilaya nchini. Ujenzi huu utawezesha kufikisha huduma za Mkongo kutoka Wilaya 81 kati ya Wilaya 139.

Mheshimiwa Spika
,

Shughuli nyingine zitakazotekelezwa kwenye Mradi huu ni:

i. Kufanya Ujenzi wa Mkongo wa majini kiasi cha Kilomita 60 kuunganisha Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kupitia Ziwa Tanganyika;

ii. Kufanya tathmini ya Ujenzi wa Kituo cha kuhifadhi Data Zanzibar;

iii. Kuwajengea uwezo wataalam 150 kwenye TEHAMA;

iv. Kuendelea kuimarisha usalama wa mitandao, kuongeza udhibiti wa matumizi ya taarifa binafsi na kupunguza uhalifu wa mitandao kwa kushirikiana na Vyombo vya Ulinzi na Usalama;

v. Kukamilisha Nyaraka za Baraza la Mawaziri kuhusu Mapendekezo ya Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi, Sheria ya TEHAMA na Mkataba wa Jumuiya ya Umoja wa Afrika wa Usalama wa Mtandao na Ulinzi wa Taarifa Binafsi (Malabo Convention);

vi. Kuelimisha umma kuhusu Mkakati wa Usalama Mtandaoni;

vii. Kuwezesha utendaji kazi wa Kamati za Kiufundi kwa ajili ya usimamizi wa Mradi wa Mkongo wa Taifa wa mawasiliano;

viii. Kufanya ufuatiliaji na tathmini ya mradi pamoja na ununuzi wa vitendea kazi kwa ajili ya usimamizi wa mradi; na

ix. Kuandaa Mpango Mkuu (Master Plan) wa utekelezaji wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano.

II: Mfumo wa Anwani za Makazi

Mheshimiwa Spika
,

Katika Mwaka wa Fedha 2022/23 Wizara imekadiria kutumia Shilingi 40,000,000,000 fedha za ndani kwa ajili ya kuendelea na utekelezaji wa Mfumo wa Anwani za Makazi. Shughuli zitakazotekelezwa ni pamoja na:

i. Kuhakiki miundombinu iliyowekwa wakati wa Operesheni Anwani za Makazi ili kuhakikisha viwango vimezingatiwa;

ii. Kuhakiki taarifa zilizokusanywa kwenye Operesheni Anwani za Makazi;

iii. Kuboresha Kanzidata na Programu Tumizi ya Mfumo;

iv. Kuendelea kuunganisha Mfumo wa Anwani za Makazi na Mifumo mingine ya kutoa huduma za kijamii;

v. Kutoa elimu kwa umma; makundi maalum ya kijamii kuhusu manufaa na matumizi sahihi ya Mfumo na kujengea uwezo Taasisi za umma na binafsi kutoa huduma kupitia Mfumo;

vi. Kutunga Sheria ndogo za kuwezesha ujenzi na matumizi ya Mfumo, mapitio ya Sheria ya EPOCA na Kanuni zake kuwezesha matumizi ya Mfumo;

vii. Kununua servers mbili (2) kwa ajili ya kuhifadhi taarifa za Mfumo na vifaa vya kuwezesha matumizi ya Mfumo;

viii. Kuandaa mwongozo ya namna mpya ya kufanya biashara kwa kutumia Mfumo;

ix. Kutengeneza Mkakati wa usimamizi, uendeshaji na uendelezaji wa Mfumo; na

x. Kuwezesha ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa Mfumo.

III: Mradi wa Tanzania ya Kidijitali (Digital Tanzania)

Mheshimiwa Spika,

Mradi wa Tanzania ya Kidijitali unalenga kuleta mabadiliko ya Kidijitali kwa kuwezesha maunganisho ya Kijiditali ya Kikanda na Kimataifa na hatimaye kukuza Uchumi wa Kidijitali (Digital Economy). Matokeo ya mradi huu ni pamoja na kuongeza na kubuni ajira zitakazotokana na ubunifu wa TEHAMA, ukuzaji wa viwanda vidogo vidogo (SMEs na SMMEs); kukuza ustadi wa wataalamu wa ndani ya Serikali na waliopo nje ya Serikali; na kuongeza uwezo wa utoaji wa Huduma za Serikali kwa kuwezesha uwepo wa intaneti bora ya bei nafuu na ya uhakika kwa ajili ya matumizi ya Serikali ili kumnufaisha mwananchi. Mradi huu utaanza kujenga chuo mahiri cha TEHAMA nchini (Digital Technology Institute). Aidha, mradi huu utapelekea Mawasiliano kwenye maeneo mapya 763 ambapo kiasi cha Shilingi Bilioni 111.59 kitatumika kupitia mradi huu.

Mheshimiwa Spika,

Katika Mwaka wa Fedha 2022/23 Wizara inakadiria kutumia kiasi cha Shilingi 39,300,000,000 ikiwa ni fedha za nje kwa ajili ya kutekeleza shughuli zifuatazo:-

i. Kujenga kituo kimoja (1) cha kukuza taaluma na ubunifu katika TEHAMA na vituo vidogo vitano (5) kwenye kila Kanda;

ii. Kuwezesha ununuzi, ugavi na ufungaji wa vifaa katika kituo kimoja (1) kikubwa na vituo vidogo vitano (5) vya kukuza taaluma na ubunifu katika TEHAMA;

iii. Kuwezesha ununuzi wa ‘bandwidth’ kwa ajili ya matumizi ya intaneti ya Serikali;

iv. Kusimika mitambo kwa ajili ya kuboresha Kituo cha Taifa cha Kutunzia Data (NIDC);

v. Kukarabati vituo 10 vya Huduma Pamoja;

vi. Kujenga mfumo wa kitaifa utakaorahisisha ukusanyaji wa takwimu za TEHAMA;

vii. Kujenga, kupanua na kuboresha miundombinu iliyopo ya intaneti yenye kasi (broadband) inayomilikiwa na Serikali (GovNET) na kuunganisha taasisi 100 kwenye Miundombinu hiyo na kufikisha taasisi 390 zilizounganishwa;

viii. Kutekeleza programu ya uelimishaji umma kuhusu mradi;

ix. Kujenga maabara tatu (3) kwa ajili ya kufufua (refurbishment) vifaa vya TEHAMA katika Mikoa ya Arusha, Dar es Salaam na Mwanza;

x. Kujenga minara ya mawasiliano 150 kwenye Kata 150 ili kuwezesha huduma za mawasiliano nchini;

xi. Kufanya mapitio na kuhuisha Sera, Sheria na Kanuni za Sekta ya TEHAMA;

xii. Kuwajengea uwezo wataalam wa TEHAMA nchini kwa kuwapatia watalaam 200 mafunzo ya muda mfupi na wataalam 10 mafunzo ya muda mrefu; na

xiii. Kufanya tathmini ya kuainisha mahitaji na usanifu wa kujenga mfumo wa kuwezesha biashara mtandao.

IV: Mradi wa Kuendeleza Ubunifu na Utengenezaji wa Vifaa vya TEHAMA

Mheshimiwa Spika
,

Katika Mwaka wa Fedha 2022/23 Wizara inakadiria kutumia Shilingi 3,300,000,000 fedha za ndani kwa ajili ya kutekeleza Mradi wa Kuendeleza Ubunifu na Utengenezaji wa Vifaa vya TEHAMA. Fedha hizo zinaombwa kwa ajili ya kutekeleza shughuli zifuatazo:

i. Kujenga Kituo cha Kuendeleza Wataalam, tafiti na ubunifu wa TEHAMA na kufanya maandalizi ya ujenzi wa makao makuu ya Tume ya TEHAMA;

ii. Kukiendeleza kituo cha kuendeleza kampuni changa za TEHAMA (ICT startups) cha Dar es Salaam na kujenga vituo viwili (2) vya Kanda vya kutengeneza bidhaa za TEHAMA;

iii. Kuanzisha Vituo vya Ubunifu na Atamizi TEHAMA katika Wilaya mbili (2) nchini;

iv. Kutengeneza mfumo jumuishi utakaounganisha usajili na uendelezaji wa wataalam na wabunifu TEHAMA nchini (ICT human capital development system); na

v. Kuwezesha shughuli za ufuatiliaji na tathmini ya Mradi.

V: Mradi wa Upanuzi wa Usikivu kwa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC)

Mheshimiwa Spika,

Mradi wa Upanuzi wa Usikivu kwa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) unalenga kuboresha upanuzi wa usikivu wa Shirika Nchi nzima. Kwa Mwaka wa Fedha 2022/23 Wizara inakadiria kutumia Shilingi 13,136,500,000 kwa ajili ya kutekeleza shughuli zifuatazo.

i. Upanuzi wa Usikivu redio za TBC kwenye maeneo yasiyokuwa na ausikivu nchini;

ii. Ukarabati wa ofisi, ununuzi wa Mitambo na vifaa vya utangazaji vya Chaneli ya Tanzania Safari;

iii. Kuimarisha muonekano wa Televisheni kwa kuongeza ung’aavu wa picha;

iv. Kuwezesha ununuzi na ufungaji wa mfumo wa kupokea na kuchanganya picha studio na matukio ya nje (Tricaster System, CG and Monitoring);

v. Ujenzi jengo la Makao Makuu ya TBC Dodoma na ukarabati wa majengo ya Ofisi yaliyopo;

vi. Kuwezesha ununuzi wa Magari ya kurushia matangazo mubashara ya Redio (TBCTaifa naTBCFM) na Televisheni (TBC1, TB2 na TBConline) na pia Magari kwa ajili ya Shughuli nyingine za Utangazaji;

vii. Kuwezesha ununuzi wa vifaa 18 vya kurushia Matangazo mubashara ya Redio nje ya studio;

viii. Ununuzi wa mitambo 10 na vifaa vya kurushia matangazo mubashara ya Televisheni (TBC1, TBC2 na Ofisi za Kanda);

ix. Ukarabati, uhifadhi, uhamishaji na uboreshaji wa studio za Ukombozi wa Nchi Kusini mwa Afrika katika jengo la utangazaji Barabara ya Nyerere kwa ajili ya Makumbusho ya maktaba ya picha na sauti;

x. Ufungaji wa mifumo ya uhariri, upokeaji na urushaji wa Matangazo kupitia mifumo ya TEHAMA (Robotic Intergrated News system with international news Monitoring); na

xi. Kuwezesha ununuzi wa mitambo na vifaa kwa ajili ya TBC Mtandaoni na televisheni ya Kiingereza ya online.

VI: Mradi wa Kufunga Mtambo Mpya wa Kisasa wa Uchapaji

Mheshimiwa Spika
,

Mradi huu unalenga kuwezesha Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) kufunga mtambo mpya na wa kisasa wa uchapaji ambao utakuwa ni chanzo kikubwa cha mapato ya Kampuni. Mtambo huu unatarajiwa kuboresha mwonekano wa magazeti ya Serikali na hivyo kuvutia wasomaji na watangazaji na pia kufanya uchapaji wa kibiashara kwa bidhaa mbalimbali chapishi kwa wateja wa ndani na nje ya nchi. Katika Mwaka wa Fedha 2022/23 Wizara inakadiria kutumia kiasi cha Shilingi 9,400,940,000 fedha za ndani kwa ajili ya kuwezesha ufungaji wa mitambo tajwa.

VII: Mradi wa Habari kwa Umma

Mheshimiwa Spika
,

Mradi huu unalenga kukusanya, kuchakata, kuandaa na kusambaza habari na taarifa kwa wananchi kuhusu mafanikio ya utekelezaji wa shughuli za Serikali ikiwemo Sera, Mikakati, Miradi na Programu zinazotekelezwa na Serikali. Vilevile, mradi unakusanya taarifa za mrejesho kutoka kwa wananchi kwa lengo la kupata maoni ya wananchi katika utekelezaji wa majukumu yake. Katika Mwaka wa Fedha 2022/23 Wizara inakadiria kutumia kiasi cha Shilingi 940,940,000 fedha za ndani kwa ajili ya kutekeleza mradi huu.

Mheshimiwa Spika,

Mipango itakayotekelezwa na Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa Mwaka wa Fedha 2022/23 imebainishwa kwa kina katika Ukurasa wa 74 hadi 84 wa kitabu cha hotuba ya bajeti.

D. SHUKRANI

Mheshimiwa Spika
,

Kwa moyo wa dhati ninapenda kuwashukuru wale wote walioshiriki kunisaidia kutekeleza majukumu yangu katika Wizara hii. Kipekee niwashukuru Mheshimiwa Mhandisi Kundo Andrea Mathew (Mb.), Naibu Waziri; Dkt. Jim Yonazi, Katibu Mkuu na, Mohammed Khamis Naibu Katibu Mkuu. Aidha, nawashukuru Wakurugenzi na Wakuu wa Vitengo katika Wizara yangu, Wenyeviti wa Bodi za Wakurugenzi za Taasisi zilizo chini ya Wizara; Viongozi wa Taasisi na wafanyakazi wote wa Wizara na Taasisi kwa kufanya kazi kwa bidii kuhakikisha kuwa Wizara yetu inakuwa chachu ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii kupitia Habari na TEHAMA.

Mheshimiwa Spika,

Naomba nichukue fursa hii kwa upekee niweze kuwashukuru Washirika wa Maendeleo ambao Serikali imekuwa ikishirikiana nao katika utekelezaji wa shughuli za maendeleo zinazohusiana na Sekta ya Mawasiliano. Washirika hao ni: Shirika la Umoja wa Mataifa la Mawasiliano (ITU); Shirika la Umoja wa Posta Duniani (UPU); Shirika la Umoja wa Posta Afrika (PAPU); Benki ya Dunia (WB) kupitia dirisha la Wakala wa Maendeleo ya Kimataifa (IDA), Ubalozi wa China nchini na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD). Aidha, kwa dhati kabisa, nawashukuru Wakandarasi wetu wote wanashirikiana na Wizara kutekeleza miradi inayosimamiwa na Wizara. Ninaamini wataendelea kuongeza juhudi na maarifa katika azma yetu ya kuchagiza Uchumi wa Kidijiti nchini.

Mheshimiwa Spika
,

Ningependa pia kuzishukuru Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kwa ushirikiano katika masuala ya Kikanda yanayohusu Sekta hii. Kwa kipindi cha Mwaka wa Fedha 2022/23, Wizara yangu itaendelea kuimarisha ushirikiano na Washirika wa Maendeleo na wadau wengine ili kuhakikisha kuwa Sekta ya Mawasiliano inachangia katika kutimiza Dira ya Taifa ya kufikia Uchumi wa Kati wa Juu ifikapo Mwaka 2025.

Mheshimiwa Spika,

Naomba kwa upekee pia niwashukuru vyombo vya habari vya ndani na nje ya nchi yetu kwa ushirikiano mkubwa walioonyesha katika kipindi cha utekelezaji wa shughuli zetu kama Wizara. Wanahabari ni wadau muhimu katika wizara yetu. Nawashukuru kipekee kabisa kampuni zote za simu nchini, kwa kuendelea kuwekeza kwenye huduma hii, kutoa ajira, kulipa kodi na kutoa huduma za teknolojia mbalimbali katika maisha ya kila siku nchini.

E. MUHTASARI WA MAOMBI YA FEDHA YA WIZARA YA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI KATIKA MWAKA WA FEDHA 2022/23

Mheshimiwa Spika,

Katika Mwaka wa Fedha 2022/23, Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari inaomba kuidhinishiwa jumla ya Shilingi 282,056,786,000.00 kwa mchanganuo ufuatao:-

i) Kiasi cha Shilingi 26,279,346,000.00 ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida ambapo Shilingi 17,249,317,000.00 ni kwa ajili ya Mishahara na Shilingi 9,030,029,000.00 ni kwa ajili ya Matumizi Mengineyo.

ii) Kiasi cha Shilingi 255,777,440,000.00 kinaombwa kwa ajili ya utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo ambapo Shilingi 215,777,440,000.00 ni Fedha za Ndani na Shilingi 40,000,000,000.00 ni Fedha za Nje.

Mheshimiwa Spika, hotuba hii inapatikana katika tovuti ya Wizara ambayo ni WMTH | Mwanzo.

Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.

Haya

Kuna kununua simu mpya hapa. Eh!
 
Mheshimiwa Spika​
,​

Mkuu Roving Journalist , asante sana kwa uzi huu wa bajeti yetu. Ila mpaka leo ndio umechangiwa na wachangiaji idadi hii!. Duh...!.
P
 
Back
Top Bottom