HONGERENI MABILIONEA WA TANZANIA BY Christopher Nyenyembe | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

HONGERENI MABILIONEA WA TANZANIA BY Christopher Nyenyembe

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by mukizahp2, Aug 22, 2012.

 1. mukizahp2

  mukizahp2 JF-Expert Member

  #1
  Aug 22, 2012
  Joined: Jul 28, 2012
  Messages: 635
  Likes Received: 94
  Trophy Points: 45
  NANI kawaambia kuwa Tanzania ni nchi masikini, na tangu lini nchi iliyosheheni rasilimali za kila aina ikawa masikini?

  Huu ni uvumi tu unaotumiwa na mabingwa wa wizi ili watu wanyonge wazidi kulia ilihali uchumi wao ukiwaneemesha mafisadi wachache.

  Tangu lini nchi masikini ikazungukwa na mabilionea walioamua kuficha fedha zao nchi za nje, na hao hao ndio wanaorudi kwa wananchi wakitamka kwa vinywa vyao kuwa Tanzania haiwezi kuendelea kama wananchi wake hawafanyi kazi kwa bidii.

  Aidha, ndio hao walioaminiwa na umma kuwa kupewa kwao madaraka yamegeuka na kuwa shubiri kwa watu masikini na hawaoni haja ya kuwatumikia wananchi kwa moyo wa dhati, wakijua wazi kuwa umasikini wa Watanzania ni moja ya silaha kubwa ya wao kuendelea kutawala.

  Haiwezekani kiasi kikubwa cha fedha zaidi ya trilioni 12 zifichwe kwenye mabenki ya nje, hususani nchini Uswisi, kwani kiasi hicho cha fedha kama kingekuwa kwenye mzunguko wa ndani, lazima kwa kiasi kikubwa mabadiliko ya kiuchumi yangeonekana.

  Kibaya zaidi, utoroshaji haramu wa fedha na kuhifadhiwa kwenye mabenki ya nje kunazinufaisha zaidi nchi hizo zilizoendelea, kwa kuwa wananchi wao wanapata fursa ya kukopa na kuzifanyia kazi fedha hizo huku Watanzania wakiendelea kuwa masikini.

  I wapi Tanzania yenye neema kwenye lindi la umasikini wa kujitakia, huku watu wakizingirwa na kauli tata za kina nani waliotorosha fedha na kuzificha nje?

  Ni kina nani hao ambao wanatajwa kwa mafumbo ilihali wapo na wanajulikana?

  Haiwezekani kila siku nchi inaibuka na tuhuma nzito zinazoendelea kuwalevya Watanzania, na hakuna hatua zozote zinazochukuliwa dhidi ya mabilionea wa nchi hii, walioamua kuiba rasilimali za nchi, wamejitajirisha na hawataki kuondoka madarakani wakihofia kuumbuana.

  Serikali inayojiaminisha kuwa inaongoza nchi kwa uwazi na uadilifu, ni mara ngapi watu wamejikuta wakitamkiwa kashfa nzito, lakini ndiyo kwanza wahusika wanazidi kujichimbia kwenye jahazi la uongozi na kwamba wanakipenda sana Chama Cha Mapinduzi.

  Ni mapinduzi ya aina gani yanayohitajika kati ya watu wanyonge na matajiri bilionea?

  Je, ni aina gani ya mapinduzi ya kiuchumi wanayohitaji Watanzania chini ya genge la wezi na mafisadi wa fedha za umma, huku idadi kubwa ya Watanzania wakipoteza maisha kwa kukosa huduma bora za kijamii?

  Ni lini CCM na serikali yake watakuwa tayari kujisafisha dhidi ya tuhuma hizi nzito za utoroshaji haramu wa fedha na kwenda kuzificha nje ya nchi?

  Ipo haja ya kuwaumbua mabilionea hao ili nchi iweze kurudisha heshima yake.

  Haiwezekani ndani ya nchi moja kuna kundi la watu wanaoishi kama wafalme, huku idadi kubwa ya Watanzania wakiishi kama watumwa kwa kisingizio cha kujivunia amani na utulivu walionao.

  Kwa maana hiyo, kutokana na kauli ya Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina (CCM) safari hii serikali inapaswa kupasua jipu ili wale wote waliotajwa moja kwa moja kujihusisha na ufisadi na utoroshaji wa rasilimali za nchi kwenda nje hawapaswi kutetewa na chama chao ama serikali yao.

  Na kwa kauli iliyotolewa na Zitto Kabwe, lazima iwe na mashiko, wahusika wanapaswa kutajwa mara moja na ninavyojua sio rahisi kwao kuweza kujisalimisha kwa kuwa ndani ya genge hilo la mafisadi, kuna vigogo wazito na hao ndio wanaolindana usiku na mchana ili wasijulikane.

  Kama Mpina na Zitto wameamua kujitoa mhanga dhidi ya kundi hilo hatari, watakuwa mashujaa wa nchi hii, lakini wakiogopa kuwataja watakuwa kwenye kundi la watu ambao thamani yao kwa nchi yao haitakumbukwa milele na milele kwa wao kuogopa kusema ukweli.

  Uozo wa aina hii na ufisadi uliokubuhu, ni hatari sana kwa maendeleo ya nchi yenye kila kitu, na inayopaswa kupigiwa mfano na mataifa mengine kwa kuwa na kila kitu. Lakini haki ya Mungu ni aibu Tanzania kuitwa masikini ilihali kuna kila kitu.

  Aibu hii inamuegemea zaidi rais kwa kuwa, siku zote amekuwa akifanya safari za kwenda nje, kuomba misaada ya fedha kwa nchi wahisani ambao wanatucheka kwa kuwa wanajua fika matrilioni ya fedha zilizofichwa kwenye nchi zao.

  Kumbe fedha wanazotukopesha ni zile zile zilizofichwa na mafisadi wetu kwenye mabenki yao, wakishakopesha na riba juu, tunawalipa na kurudisha tena fedha zetu kwao.

  Mafisadi wetu wapo kimya wanaangalia mchezo unaochezwa na rais wa kuzipigia magoti nchi tajiri zinazotunza fedha haramu za nchi masikini.

  Kwa mfumo huu wa kwenda kukopa fedha zetu zilizofichwa na Watanzania wenzetu kwenye mabenki ya nje, kamwe hakuwezi kuliacha taifa hili salama, wa kuwa litaendelea kuongozwa na kundi la watu wachache wenye kiburi cha pesa.

  Wananchi wanapaswa kushangaa na kujiuliza kama kweli kiasi kikubwa cha fedha kipo nje na wakati huo mgogoro mkubwa wa uchumi unaelezwa kuikumba Tanzania, hapo ndipo somo la mwalimu mjinga linapotolewa kwa wanafunzi werevu.

  Haiwezekani wengi tulie kilio cha mamba ndani ya maji, huku kundi la wachache wakicheka na kudharau umma wa Watanzania kwa umasikini wao, wakijua wazi kuwa wizi mkubwa wa mali za umma umechangia kwa kiasi kikubwa kuwafikisha watu hapa tulipo.

  Udhaifu mkubwa unaonekana wazi kwenye vyombo vya dola vyenye majukumu ya kudhibiti ubadhirifu wa mali za umma, na ni wazi kuwa ushahidi mkubwa wa hali bora za maisha na matumizi mabaya ya fedha haramu unaonekana kwa staili ya maisha ya watu walio kwenye kundi la mafisadi.

  Kwa mazingira hayo, lazima niwape pongezi mabilionea wa Tanzania kwa kufanikiwa kuwa vinara wa kutorosha fedha za nchi hii masikini na kwenda kuzificha kwenye mabenki ya nje.

  Endeleeni kufanya hivyo kwa kuwa si rahisi kwa watu wa kawaida na masikini kufahamu kuwa wameibiwa.

  Kwa kuwa nawapa pongezi, najua kuwa kitendo cha kuendelea kuzificha fedha hizo nje, kitaendelea kuifanya Tanzania iwe nchi ya omba omba siku zote, na hiyo ndiyo moja ya sifa tunayojivunia ya kwenda kuomba nje na rais anaporudi mnakuwa wa kwanza kwenda kumpokea uwanja wa ndege.

  Mnafanya hivyo sio tu kwa kutambua kuwa safari yake imezaa matunda baada ya kukopeshwa fedha kutoka kwenye benki mlizoficha fedha haramu, pia mnajua kuwa riba inayolipwa kwenye mikopo hiyo inaingia kwenye akaunti zenu na hapo ndipo mnapozidi kuneemeka.

  Kama kweli hayo yametendeka na utafiti uliofanywa na Shirika la Global Financial Integrity ukionesha fedha nyingi zimetoroshwa katika kipindi cha serikali ya awamu ya nne kutoka mwaka 2005 hadi 2009, basi Rais Jakaya Kikwete ana kila sababu ya kuwataja mafisadi hao, na asisubiri taarifa ya vyombo vya ndani kwa kuwa vimeshindwa kufanya kazi na kueleza ukweli juu ya kadhia hiyo mbaya.


  [​IMG]

  cnyenyembe@yahoo.com 0754 301 864, 0715 301 864[​IMG] [​IMG]
   
 2. Takalani Sesame

  Takalani Sesame JF-Expert Member

  #2
  Aug 22, 2012
  Joined: Jun 24, 2008
  Messages: 588
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 33
  Mkuu mpangilio wako unachosha sana kusoma. Samahani kama umekwazika.
   
Loading...