Hongera Serikali: Ukweli kuhusu Bajeti ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 2021/2022

Baraka Mina

JF-Expert Member
Sep 3, 2020
581
574
Kwema wanajamvi, tumshukuru Mwenyezi Mungu kwa uzima na afya. Poleni na majukumu mbalimbali ya kulijenga taifa, Moja kwa moja naomba niende kwenye mada.

Wahenga walisema "Hakuna marefu yasiyokuwa na ncha", baada ya mjadala mrefu juzi Juni 22, 2021 Bunge la Tanzania lilipitisha na kuidhinisha Bajeti Kuu ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania shilingi trilioni 36.68 (36,681,897,765,000) kwa mwaka wa fedha 2021/2022 ambapo wabunge 361 sawa na 94% walipiga kura ya ndiyo, wabunge 23 sawa na 6% walipiga kura isiyo ya maamuzi (hawajakataa wala kukubali) na wabunge 5 hawakuwepo wakati wa zoezi hilo la upigaji kura. Ikumbukwe kwamba bajeti ya mwaka wa fedha 2021/2022 ina ongezeko la 4% ikilinganishwa na bajeti ya mwaka wa fedha wa 2020/2021 iliyokuwa ni shilingi trilioni 34.8.

Nilimsikiliza kwa makini Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) wakati akijibu hoja kwa ajili ya kuhitimisha mjadala wa Bajeti Kuu ya Serikali kabla ya Bunge kuidhinisha Bajeti hiyo Bungeni jijini Dodoma, kwa hakika Serikali inahitaji kupewa pongezi za dhati kwa jinsi ilivyojipambanua namna ambavyo itaenda kuitekeleza bajeti hii na kuhakikisha inaleta maendeleo jumuishi na endelevu

Kuna baadhi ya hoja (mambo) wengi wetu tulizielewa vibaya kutokana na tafsiri tofauti zilizoenea sambamba na kukosa taarifa sahihi na huu hapa chini ndiyo ukweli kuhusu bajeti hii.​
  • KODI YA MAJENGO KUPITIA MITA ZA LUKU
Kodi hii haitatozwa kwa kila mwenye umeme na wala kwa matumizi ya umeme bali maeneo ambayo yatatozwa ni yale yaliyoainishwa yenye sifa kisheria, hivyo namba za mita za luku za wananchi ambao hawatakiwi kulipa zitaondolewa katika mfumo (blacklisted). Sambamba na hilo kodi hii italipwa na mmiliki wa nyumba na sio ya mpangaji. Kama ilivyokuwa inakusanywa kwa njia ya kawaida (physical) ukusanyaji uleule unapelekwa katika njia ya kielektroniki kwa sababu teknolojia imekuja ili kurahisisha kazi.

Serikali imeeleza kuwa kodi hii haitatozwa kwa kila mwenye umeme na wala kwa matumizi ya umeme kwa sababu kodi ingetozwa kwa matumizi ya umeme gharama za uzalishaji wa umeme zingeongezeka na hivyo kuleta adha kwa Wananchi.​
  • MAKATO YA SIMU KWENYE MUDA WA MAONGEZI
Makato hayatafanyika kila siku bali ni pale tu mtu anapoweka muda wa maongezi. Makato yataanzia shilingi 5 kwa wanaotumia shilingi 1000/= kwenda chini mpaka shilingi 222 kwa wanaotumia 100,000/= na kuendelea.

Mhe. Mwigulu Nchemba alisisitiza kuwa nchi hii (Tanzania) itajengwa na watanzania wenyewe, ni lazima tubebe majukumu hayo (ulipaji wa kodi) kama watanzania kwa sababu majukumu hayo ni yetu na nchi yetu ina matatizo pamoja na jitihada kubwa ambazo zimefanyika. Kila hatua ya maendeleo tunayoifanya inatuletea changamoto zaidi; ndivyo utaratibu wa maendeleo ulivyo.
  • WIZARA YA UJENZI NA UCHUKUZI
Serikali imetenga nyongeza ya bilioni 322 kwa ajili ya kufungua maeneo ambayo hayapitiki (hayana barabara) katika maeneo ya mijini na vijijini. Kila jimbo la uchaguzi litapata si chini ya bilioni 1 kwa ajili ya barabara hizi.

Barabara za vijijini zimekuwa ni kilio kikubwa kwa muda mrefu. Kutengwa kwa fedha hizi ambazo zitatumika kujenga barabara za vijijini ili zikae muda mrefu kutasaidia usafiri wa uhakika kwa wananchi, usafirishaji wa bidhaa na kuanza kusogeza huduma karibu na wananchi sambamba na kuiwezesha TARURA kifedha na kiutaalamu ili ifanye kazi kwa ufanisi zaidi.​
  • WIZARA YA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA
Serikali imetenga nyongeza ya bilioni 70 ili kuwapeleka chuo wanafunzi 11,000 waliokosa mkopo mwaka 2020 na wanafunzi 10,000 wanaokadiriwa kuwa wangekosa mkopo mwaka 2021. Kutengwa kwa fedha hizi kutawezesha wanafunzi wote waliodahiliwa katika vyuo vikuu nchini na kuomba mkopo katika Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) kuweza kupata mikopo na kutimiza azma yao ya kupata elimu ya juu na kuongeza wasomi wa kada mbalimbali nchini.

Pia Serikali imetenga nyongeza ya bilioni 125 kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya vyumba vya madarasa (maboma) 10,000 kwa wanafunzi wanaoingia kidato cha kwanza, kila halmashauri itapata maboma yasiyopungua 10. Wanafunzi wengi waliofaulu wamekuwa wanashindwa kwenda kujiunga na kidato cha kwanza katika shule za Serikali kwa sababu hakuna nafasi au miundombinu haitoshi.

Ikumbukwe kuwa mwaka kesho (2022) taifa linaenda kupata toleo la kwanza la wanafunzi wanaoenda kumaliza darasa la saba na kuanza kidato cha kwanza ambao waliandikishwa kupitia elimu bila malipo kwa shule ya msingi. Fedha hizi ni sehemu ya hatua nzuri kukabiliana na uhitaji wa vyumba vya madarasa nchini.​
  • WIZARA YA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO
Serikali imetenga nyongeza ya bilioni 100 kwa ajili ya zahanati kwenye vijiji na kata (maboma ya afya). Fedha hizi zitahakikisha ujenzi ulioanza na ujenzi mpya unakamilika katika maeneo husika na wananchi hususan maeneo ya vijijini wanapata huduma bora za afya.

Pia Serikali imetenga nyongeza ya bilioni 50 kwa ajili ya vifaa tiba pamoja na dawa. Utekelezaji huu utaenda sambamba na suala la bima kwa wote.​
  • WIZARA YA MAJI
Serikali imetenga nyongeza ya bilioni 207 kwa ajili ya shughuli za maji na utaratibu wa visima na mabwawa. Kwa sasa Serikali inajielekeza katika utaratibu wa kisima kwa kila kijiji kama ilivyo kwa umeme.

Pia fedha hizi zinatarajia kufanya ununuzi wa magari ya kujimba visima na greda za kuchimba mabwawa.

Mbali na hoja hizo hapo juu, Serikali imesisitiza kuwa inazingatia mambo yote yanayoikabili nchi yetu sambamba na miradi ya kimkakati ambayo ni lazima ipate fedha; Serikali imeona vyema ikafanya utaratibu wa kupata fedha kiasi (fedha za ndani) lakini kwa wakati huohuo itafute mikopo yenye masharti nafuu ambayo haitaipa mzigo mkubwa wa deni kwa taifa letu.

Ndugu watanzania wenzangu kazi ya kujenga nchi yetu lazima ifanywe na sisi sote.​

Nawasalimu kwa jina la Jamhuri Ya Muungano wa Tanzania.

 
kazi iendelee......

kilicho baki sasa ni kwa watendaji.

mawaziri, makatibu wakuu, wakuu wa mikoa, wa wilaya, wakurugenzi, madiwani n.k, watendaji wote wanao wajibu wa kusimamia fedha za miradi, hatutegemei kutokee ubadhirifu wa fedha za walipa kodi.

Hongera kwa Mhe. Rais Mama Samia kwa kudhamiria kuwaletea maendeleo ya kweli watanzania wote.
mabilioni ya TARURA yamemwagwa kila jimbo sasa kazi kwa wabunge na madiwani wetu kuhakikisha fedha zinatumika ktk malengo yaliyo kusudiwa.
tunategemea barabara zote kurekebishwa.
 
kazi iendelee......

kilicho baki sasa ni kwa watendaji.

mawaziri, makatibu wakuu, wakuu wa mikoa, wa wilaya, wakurugenzi, madiwani n.k, watendaji wote wanao wajibu wa kusimamia fedha za miradi, hatutegemei kutokee ubadhirifu wa fedha za walipa kodi.

Hongera kwa Mhe. Rais Mama Samia kwa kudhamiria kuwaletea maendeleo ya kweli watanzania wote.
mabilioni ya TARURA yamemwagwa kila jimbo sasa kazi kwa wabunge na madiwani wetu kuhakikisha fedha zinatumika ktk malengo yaliyo kusudiwa.
tunategemea barabara zote kurekebishwa.
Kwa hakika tunawategemea viongozi watendaji wahakikishe wanaitekeleza bajeti hii kwa vitendo.
Mafanikio makubwa yanakuja
 
Naomba niulize swali dogo mkuu,ikiwa natakiwa kulipa kodi ya shilingi 10,000 kwa mwaka kwa kibanda ninachokimiliki je makato yangu yakifikia kiwango hicho ndani ya muda wa miezi mitatu mtasitisha makato kwangu hadi mwaka unaofuata? Au mtaendelea kukata no matter what?
 
Naomba niulize swali dogo mkuu,ikiwa natakiwa kulipa kodi ya shilingi 10,000 kwa mwaka kwa kibanda ninachokimiliki je makato yangu yakifikia kiwango hicho ndani ya muda wa miezi mitatu mtasitisha makato kwangu hadi mwaka unaofuata? Au mtaendelea kukata no matter what?
Kupitia namba ya malipo (control number) suala hilo linawezekana. Kwa maelezo zaidi waweze kuwasiliana na mamlaka husika.
 
3 Reactions
Reply
Back
Top Bottom