Hongera Mh.Magdalena Sakaya, Mbunge wa Kaliua

Egnecious

JF-Expert Member
Jul 8, 2015
875
960
HONGERA MH. MAGDALENA SAKAYA, MBUNGE WA KALIUA
(Uwe somo kwa Wabunge wengine wa Upinzani)

Aprili 16, 2018

Moja kati ya mambo yanayoonesha dhahiri kwamba ni tatizo kubwa nchini Tanzania ni siasa za chuki, mihemko, vurugu na uhasama kati ya vyama vya upinzani vyenye ushirika kupitia mwavuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) dhidi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambachi ni chama tawala.

UKAWA ikiongozwa na kinara wake Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) inaendesha mapambano ya wazi yanayoonesha kiu na dhamira yake ya kutaka kushika dola na hivyo viongozi na wafuasi wake wamejipa kazi ya kutaka kuwaaminisha wananchi kuwa Serikali iliyopo madarakani hakuna inachokifanya, viongozi wake hawana akili, kila kinachofanywa na Serikali ni kibaya na kwa makusudi kabisa viongozi wa CHADEMA na washirika wao wamejiingiza kwenye kibarua cha kuwashambulia kwa matusi, kashfa na kejeli viongozi wa Serikali akiwemo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. John Pombe Magufuli.

Mwendo huu umepelekwa kila mahali hadi Bungeni ambako ni chombo muhimu kinachofanya kazi muhimu kwa Taifa ya kuisimamia na kuishauri Serikali hasa wakati huu wa vikao vya bunge la bajeti.

Kwa shauku kubwa mimi hufuatilia mienendo ya Bunge na Ijumaa iliyopita nilimsikiliza Mbunge wa Jimbo la Kaliua kwa tiketi ya Chama cha Wananchi (CUF) Mh. Magdalena Sakaya akichangia hoja. Alitumia muda wake wa dakika kumi kuzungumzia masuala muhimu ya maendeleo ya wananchi wa Jimbo lake.

Sakaya alijikita kuibana Serikali iongeze fedha katika Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA) tena ikiwezekana iwe asilimia 50 kwa 50 na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), hoja yake hapa ilikuwa TARURA ndio imebeba jukumu la kujenga barabara nyingi za vijijini ambazo zimekuwa kero kwa Watanzania wengi ambao ni masikini waishio vijijini na katika miji ambako TANROADS hawashughuliki na matatizo yao ya barabara.

Mh. Sakaya aliibana Serikali ipeleke fedha Kaliua kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa Hospitali ya Wilaya, alidai tayari halmashauri ya wilaya ya Kaliua imeshaanza ujenzi wa majengo ya hospitali hiyo na hivyo kuitaka Serikali ione umuhimu wa kuendeleza hapo ilipofikia halmashauri yake ya Kaliua.

Aliendelea kuibana Serikali ipeleke watumishi ili kupunguza uhaba wa watumishi unaoyakabili baadhi ya maeneo ya kutolea huduma kama vile zahanati na shule na pia akataka watumishi waliopo wapandishwe madaraja ili kuwaongezea morali ya kazi.

Mh. Sakaya aliendelea kutaka uwezeshaji wa vijana na wanawake kupitia mifuko ya maendeleo ya vijana na wanawake utiliwe mkazo, akambana Waziri Jenister Mhagama aangalie mifuko 17 inayoshughulikia vijana na wanawake inafanya nini. Kiu yake ni kutaka vijana na wanawake wa Kaliua wawezeshwe kuzalisha mali na kukabiliana na umasikini.

Katika uchangiaji huu Magdalena Sakaya pia alitoa mawazo yake na ushauri wake wa namna Serikali inavyoweza kufanikisha hayo japo kuwa kuna changamoto ya uwezo wa kibajeti. Aliongea kwa msisitizo na bila kuona haya, lakini hakutukana na wala hakukashifu na wala hakutishia. Alimwaga hoja nzito na kuwapigania wananchi waliomchagua.

Na hii sio mara ya kwanza kwa Mbunge Magdalena Sakaya kutoa michango ya kupigania wananchi, ni mpambanaji lakini siku zote amesimama kwenye hoja zenye msingi wa maendeleo na manufaa kwa wananchi. Kila akisema iwe Bungeni ama kwenye mahojiano nje ya bunge ama kwenye mikutano ya hadhara anazungumza kuhusu kero za wananchi na maendeleo yao

Kwangu mimi huu ndio wajibu hasa wa Mbunge na ni wajibu hasa wa mwasiasa wa upinzani. Hapa ndipo panaponoga na panapoonesha kweli tuna siasa zenye tija kwa nchi yetu.

KIOJA kikaja kwa Mbunge wa viti maalum wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) anayewakilisha mkoa wa Geita Mh. Upendo Peneza, yeye aliposimama tu akaanza kushambulia Serikali kwamba hakuna uhuru wa kufanya siasa, kuna mauaji, mara watu wanapotea, mara anataka Bunge Live, ikawa ni kubishana na Mwenyekiti wa Bunge Mh. Mussa Azan Zungu mpaka Mwenyekiti akatumia kanuni kumzuia asiongee tena.

Nikajiuliza maswali sasa Mbunge kama huyu ana maana gani? Mwanasiasa wa namna hii ana faida gani? Kapewa dakika kumi akatumia dakika 3 kubishana na kiti na mwisho wa siku akazuiwa kuzungumza.

Nikavuta picha ya wananchi wa Geita ambao wana mambo yao muhimu ya kusema Bungeni kama alivyofanya Magdalena Sakaya, kwamba walipata nafasi hiyo ya mambo yao kusemwa mbele ya kikao kinachoandaa bajeti lakini waliyemtuma hakusema akaishia kugombana na kiti.

Nikawaza tu hivi wananchi kama hawa watakapoona wananchi wa Jimbo jirani la Kaliua katika Mkoa wa Tabora wanapelekewa fedha za ujenzi wa hospitali wakati wao wanahaha na mahitaji ya matibabu, watakapokuwa wanaona wananchi majirani zao wanajengewa barabara zilizoombwa na Mbunge wao, watakapokuwa wanaona majirani zao wanaongezewa watumishi hospitalini na zahanati watajisikiaje?

Hapa ndipo Watanzania tunapaswa kuwa makini sana, wanasiasa wote duniani kote lengo lao kuu ni kutaka kushika dola, wanasiasa mahiri hutafuta kufikia lengo hilo kwa kujenga hoja zenye kuleta uongozi mbadala na wenye manufaa kwa maisha ya watu, lakini wanasiasa wasio mahiri hupambana kushika dola kwa siasa za fitina na uchonganishi ambazo uzoefu unaonesha matokeo yake ni mabaya na uwezekano wa kufanikiwa ni mdogo sana.

Siasa kama hizo zimefanywa sana na mwanasiasa wa upinzani Bw. Kiiza Besigye wa Uganda na mpaka sasa hakuna dalili za kufanikiwa kwake na wananchi wa Uganda kupitia sanduku la kura wanaonesha dhahiri bora waendelee na babu yao Mzee Yoweri Kaguta Museveni.

Siasa kama hizo zimefanywa na mwanasiasa wa upinzania Bw. Morgan Tsvangirai wa Zimbabwe nae hakufanikiwa mpaka mauti yamemkuta. Alishindwa kabisa kuwashawishi wananchi wa Zimbabwe na matokeo yake wakawa wanaendelea kumchagua Mzee Robert Mugabe hata kama alikuwa amechoka kabisa hadi chama chake tawala kilipoamua kumuondoa kwa busara na heshima na kumweka mwana ZANU PF mwingine na sio MDC.

Na siasa kama hizi zinafanywa na mwanasiasa wa upinzani Julius Malema wa Afrika Kusini na hakuna dalili kuwa yeye na chama chake watafanikiwa kushika madaraka zaidi ya kuhamasisha mapambano na fujo ambazo huzimwa kwa urahisi kabisa na vyombo vya dola.

Sasa moja kati ya mambo yanayotia doa siasa za upinzani Tanzania ni mwelekeo wa kuwekeza katika kupinga kila kinachofanywa na Serikali na kujenga siasa za uhasama dhidi ya dola.

Aina hii ya siasa husababisha madhara makubwa katika uongozi wa nchi kutokana na ukweli kwamba badala ya upinzania kuwa chombo kinachohoji na kukosoa Serikali iliyoko madarakani inakuwa ni genge la mashambulizi, kuparulana na kuwekeana uhamasama.

Matokeo ya hayo ni kuzaa Serikali inayopambana kwa kasi ileile au zaidi ya ile inayofanywa na upinzani, Serikali yenye ubabe na mwisho wa siku ni kutengeneza machafuko.

Mwandishi wa vitabu na mwanasiasa aliyewahi kuwa kiongozi wa upinzani wa New Zealand Dk. Donald Thomas Brash ameeleza katika moja ya maandiko yake kuwa upinzani hauna maana ya kupinga kila kitu kinachafanywa na Serikali, bali kuikosoa na kutoa njia mbadala wa namna ya kutoa uongozi na sio kupinga kila kinachofanywa na Serikali.

Nimekuwa nikifuatilia vikao vya Bunge vinavyoendelea mjini Dodoma, makosa haya yanaendelea na wabunge wa upinzani ni kama vile hawana hoja nyingine zaidi ya hoja za kushambuliwa Tundu Lissu, Miili iliyookotwa Coco Beach, Kuzuiwa mikutano ya Siasa, Kupotea kwa watu na kukamatwa kwa viongozi wa upinzani.

Najiuliza sana hivi kweli upinzani wa nchi hii hauna ajenda zenye mashiko kwa ajili ya Watanzania? Kila kiongozi wa upinzani analalamikia mambo yale yale kama vile wamekaririshwa, wanapoteza muda kubishana bungeni kwa ajenda hizo tu.

Na sio hayo tu, wakijitahidi basi ni kusubiri wapi watapinga yanayofanywa na Serikali na kuanzisha vurugu kubwa na vitisho vya kuvunja amani na utulivu wa nchi.

Ziko wapi hoja nzito za upinzani zilizokuwa zinajengwa enzi za akina Wilbrod Slaa na Akina Dk. Mvungi?

Hakuna anayesema kama kununua ndege ni makosa basi mbadala wake tufanyaje ili kuwa na shirika la ndege la Taifa? Kama kujenga reli ya kisasa ni makosa mbadala wake ni nini katika kupunguza tatizo la kusafirisha mizigo na abiria na kukuza biashara ya bandari ya Dar es Salaam.

Kama ujenzi wa viwanja vya ndege unafanywa kwa makosa, au utoaji wa fedha kwa ajili ya elimu bure au kuongeza fedha za dawa au kuongeza usambazaji wa maji, umeme na kujenga barabara ni makosa mbadala wake nini?

Mwisho, vikao vya bunge vinaendelea Dodoma Wabunge wa upinzani jipimeni, mwelekeo wenu huu una manufaa gani kwa Watanzania kwamba watashawishika kuwaoneni nyie ndio mtakaofaa kutoka mbadala wa uongozi wa nchi? Mnawahakikishiaje wananchi kuwa kwa staili hii mtakaposhika nchi mtajipanga kufanya maendeleo na sio kuwa walalamikaji?

Julius J. N
Dododma
 
Kila mtu anachangia kulingana na uchungu alionao kwenye mambo ya kitaifa kwahiyo sio lazima sana
 
Kwa hiyo alichoongea peneza kwako hakina maana au? Stori yako haijabalance kwani umeonekana lengo ni kuishambulia chadema kiaina ila umemtumia sakaya kama chambo.halafu hao unaoita wapinzani wa nje kama svangirai,malema,na besigye impact yao ni kubwa kama viongozi wa upinzani wa tz.ila pale serikali za kidikteka kama ulizoziorodhesha ikiwemo na ya tanzania zinashindwa ila zinalazimisha ushindi.serikali zote hizo hazipendwina raia wake bali na watu wanaofaidika na mfumo
 
Back
Top Bottom