Hongera Kikwete, kila la kheri Libya

singidadodoma

JF-Expert Member
Nov 11, 2013
4,394
1,536
UMOJA wa Afrika (AU) Jumapili iliyopita, ulimteua Rais wa Awamu ya Nne wa Tanzania, Jakaya Kikwete, kuwa msuluhishi wa umoja huo nchini Libya, kuchukua nafasi ya Dileita Mohamed Dileita wa Djibout, ambaye alishika nafasi hiyo tangu mwaka 2014.

Uteuzi huo wa Rais (mstaafu) Kikwete ni mwendelezo wa juhudi za Umoja wa Afrika, kurejesha amani katika taifa hilo la Afrika ya Kaskazini, ambalo liliingia katika machafuko baada ya kuondolewa na hatimaye kuuawa kwa kiongozi wake, Mummar Gaddafi, mwaka 2011.

Akitangaza uteuzi huo wa Kikwete, Kamishna wa Amani na Usalama wa AU, Smail Chergui, alisema Libya inahitaji msaada wa umoja huo ili kulirejesha taifa hilo katika hali ya utulivu na amani.

Ni imani yetu kwamba uteuzi wa Kikwete kuwa msuluhishi wa mgogoro wa taifa hilo utafungua ukurasa mwingine wa uwezo wa Afrika kutatua matatizo yao wenyewe.

Pamoja na imani na pongezi hizo kwa mwanadiplomasia huyo wa kimataifa, tunajua kuwa kazi ya kukutanisha na kupatanisha makundi mawili hasimu nchini humo ambayo kila moja linadai ndilo lenye uhalali wa kuongoza nchi hiyo, siyo nyepesi hata kidogo, ni kazi ngumu ambayo itahitaji, hekima, busara na uvumilivu.

Uhasama kati ya makundi hayo ambalo moja lina makao makuu yake katika mji wa Tobruk na jingine katika mji mkuu Tripoli, umesababisha maafa makubwa na mateso makali kwa wananchi wa taifa hilo lililowahi kuwa na nguvu Afrika na duniani kwa namna fulani, huku raia wake wengi wakihatarisha maisha yao kuvuka bahari kukimbilia Ulaya kupitia kisiwa cha Lampedusa nchini Italia, kilichoko maili 200 tu kutoka mpaka wa Libya.

Hali ya wakimbizi hao na jinsi wanavyohatarisha maisha yao kukimbia mapigano nchini mwao na kusambaratika kwa taifa hilo ni kielelezo kilichojitosheleza kwa Jumuiya ya Kimataifa kuchukua hatua za makusudi kuleta amani nchini humo. Ni vyema dunia ikaungana na Afrika, kumuunga mkono kwa dhati msuluhishi huyo ili wananchi wasio na hatia Libya wapate haki yao ya kuishi maisha yenye staha na utu. -


Raia Mwema
 
Back
Top Bottom