Homa ya mgunda: ‘Msile vibudu, kuleni nyama iliyopikwa vizuri’

Lady Whistledown

JF-Expert Member
Aug 2, 2021
603
791
Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Hezron Nonga, akizungumza jana na waandishi wa habari jijini hapo, alisema panya sio mnyama anayetakiwa kuliwa na binadamu kwa kuwa ni benki ya vimelea vya ugonjwa huo.

Aidha, wamesisitizwa kununua nyama iliyochinjwa kwenye machinjio na kuuzwa kwenye mabucha yaliyosajiliwa na Bodi ya Nyama nchini. “Mimi kama daktari wa masuala ya wanyama, hivyo naelekeza jamii ya Watanzania tuepuke kula panya sababu ni chanzo cha maradhi mengi, huyu panya ni benki ya vimelea vya ugonjwa huu wa mgunda, pia wachukue tahadhari ya popo wanaoingia kwenye nyumba ni hatari wana magonjwa mengi,” alisema.

Alisema, kuna uvumi unaowatia hofu Watanzania kwamba wasile nyama kutokana na kuibuka kwa ugonjwa huo jambo ambalo sio kweli, kinachotakiwa ni kupikwa na kuchomwa vizuri. Prof. Nonga alisema pia maziwa, mayai na maji ya kuchemshwa yanapaswa kupikwa vyema.

“Njia pekee ya maambukizi ya mgunda ni kula nyama ambayo haijaiva vizuri, nitoe rai kwa wananchi kutokutaharuki na kuacha kula nyama na badala yake wahakikishe nyama wanayokula imeiva vizuri,” alisisitiza.
Alisema ulaji wa nyama ndiyo njia rahisi ya kukabiliana na utapiamlo kutokana na takwimu kuonyesha kuwa nchini Tanzania mtu mmoja anakula kilo 15 kwa mwaka huku mapendekezo ya kimataifa ni kilo 50 kwa mwaka.

“Ulaji wa nyama bado tupo chini hivyo ni muhimu kula nyama, lakini ni nyama ipi ni ile ambayo kwanza imechinjwa kwenye machinjio ya serikali, kwa kuwa imepimwa na wataalamu na imepigwa muhuri kuuzwa kwenye maduka ambayo yamezingatia vigezo vya Bodi ya Nyama, lakini hiyo nyama ipikwe na kuiva vizuri,” alisema.

Alisema utafiti uliofanyika nchini unaonyesha kuwa maambukizi ya ugonjwa huo yalishawahi kutokea kwa binadamu na wanyama. “Inaonyesha kwa wanyama wa kufugwa ni ng’ombe, mbuzi, nguruwe, mbwa na paka katika mikoa ya Morogoro, Kilimanjaro, Tanga, Dar es Salaam, Katavi, Mwanza, Singida, Kagera na Mbeya waligundulika kuwa na maambukizi,” alisema.

“Matibabu ya ugonjwa huu kwa wanyama ni dawa ya anti-biotic aina ya doxycline au penicillin, tunasisitza mnyama wako apate chanjo, kutochunga maeneo ya maambukizi kama vile kwenye hifadhi za wanyamapori, kudhibiti panya kwenye mazingira ya mifugo.”

Kwa upande wake, Msajili wa Bodi ya Nyama nchini, Dk. Daniel Mushi, alisema bodi hiyo inaendelea kufanya ukaguzi kwenye mabucha mbalimbali nchini na kuyafunga yasiyokidhi vigezo na yatakayobainika kuuza nyama isiyothibitishwa na wataalamu. “Nawasihi Watanzania wasile nyama za vibudu kwa kuwa ni hatari mnaweza kupata maambukizi ya ugonjwa huu,” alisema.

Chanzo: Nipashe
 
0 Reactions
Reply
Top Bottom