HoloLens 2: Teknolojia ya Kufanya Kazi na Ana kwa Ana na Mtu Asiyeonekana

View attachment 1156332
Wakati teknolojia ya simu za mkononi zenye uwezo wa ‘touch screens’ ikiingia, kila mtu alikuwa akistaajabu kwamba utaweza vipi kubofya simu ambayo haina ‘buttons?’ yaani uguse tu kioo halafu mambo yawe yanaenda kama unavyotaka? Ilionekana kama ni kitu kisichowezekana.

Lakini sasa imeshakuwa kitu cha kawaida kabisa, kiasi kwamba simu zenye ‘buttons’ au vitufe vya kubonyeza, zinaonekana kupitwa na wakati, kila kitu ni ‘touch’!

Teknolojia hiyo imehama, hivi sasa siyo simu tu zenye touch screens, kuna laptop za kisasa ambazo kila kitu kinafanyika kwa kugusa kioo tu, lakini pia kuna televisheni za majumbani zenye touch screen.

Sasa kwa sababu ‘touch screens’ siyo kitu cha ajabu tena, wanasayansi wameendelea kuumiza vichwa kuja na kitu kikubwa zaidi na hapo ndipo ilipogunduliwa teknolojia iitwayo HoloLens.

Hii ni kama ‘touch screens’ tu lakini tofauti yake, wakati kwenye ‘touch screens’ ukilazimika kugusa kioo cha kifaa unachotumia, kwenye HoloLens, unavaa miwani yenye teknolojia kubwa ya kugeuza kila unachokiona kupitia miwani hiyo, kuwa touch screen.

Twende taratibu, yaani ni hivi; unavaa miwani maalum iliyotengenezwa kwa teknolojia ya hali ya juu, halafu ukiitazama miwani hiyo, eneo lote unaloliona mbele yako linakuwa ni ‘screen’, na jinsi ilivyotengenezwa kimaajabu, japokuwa unaivaa machoni, bado unaweza ‘ku-touch’ kwa mikono yako kila kinachoonekana kwenye screen.

Yaani unapoivaa, halafu mtu ambaye hajavaa miwani hiyo akikutazama, anaweza asielewe unafanya nini, au akahisi pengine umechanganyikiwa na ndiyo maana inashauriwa kwamba unatakiwa kuivaa ukiwa ndani ya chumba kilichotulia.

Sasa kwenye matumizi yake ndiyo utachoka! Miwani hii ina matumizi makubwa na mazito yanayoweza kukushangaza. Kazi yake kubwa ya kwanza, ni kukuunganisha na watu waliopo sehemu mbalimbali duniani kwa wakati mmoja, mnaweza kuunganishwa watu wawili, watatu au hata kumi ambao mpo sehemu tofauti duniani, wote mkajiona kama mpo ndani ya chumba kimoja.
View attachment 1156333
Unapounganishwa, unamuona mwenzako aliyevaa miwani kama yako, akiwa pembeni yako hata kama wewe upo Dar es Salaam na yeye yupo Washington DC, teknolojia inawaleta pamoja, tena sio kwa picha za kawaida, bali zenye kiwango cha 3D.

Kisha baada ya kuunganishwa, wote mnaweza kuanza kujadiliana kuhusu kitu kimoja, kutegemeana na muongoza mjadala anataka mjadili kuhusu nini. Kwa mfano, yawezekana mgonjwa yupo Dar es Salaam, anaumwa sana lakini madaktari wa hapa hawana uwezo, kwa hiyo wanawaunganisha madaktari waliopo China, India na Ujerumani.

Kwa wakati mmoja, wote watakuwa na uwezo wa kumtazama mgonjwa, kuchunguza taarifa zake za kina na kutoa ushauri wa nini kifanyike, tena siyo ushauri wa maneno tu, ushauri wa picha za video kuhusu nini kifanyike na kwa wakati gani! Wote watakuwa ni kama wapo wodini wakimtazama mgonjwa.

Sasa unaweza kuona kwamba ni mambo ambayo yapo mbali sana na yatachelewa kutekelezeka lakini kwa taarifa yako, teknolojia ya HoloLens, tayari ilishaanza kufanya kazi na sasa, Kampuni ya Microsoft imezindua toleo jipya la teknolojia hiyo, HoloLens 2 ambayo tofauti na toleo la mwanzo la majaribio, hii imeboreshwa maradufu.

Miwani hiyo, inatarajiwa kuanza kuuzwa kwa bei ya dola za Kimarekani 3,500 ambazo ni sawa na takribani shilingi milioni 8 za Kitanzania ikiwa na uwezo wa kuunganishwa na Wi-Fi, kwa hiyo cha msingi ni kuhakikisha mahali ulipo kuna intaneti yenye kasi, hilo likifanikiwa basi dunia nzima inakuwa machoni mwako, si kiganjani tena!
Hii teknolojia inaendana sambamba na 5G
 
Back
Top Bottom