(Hoja Yangu) CUF wameuziwa mbuzi kwenye gunia!

jamadari

JF-Expert Member
Feb 13, 2010
295
92
WIKI hizi chache zilizopita nimeamua kuvunja mwiko ambao mara kadhaa tumekumbushwa kuwa tusiuvunje. Katika makala hii naendelea kuvunja mwiko huu.
Kama mtu nisiyejali mikwara na kejeli za wale ambao wanaamini kuwa wana haki pekee ya kuzungumzia masuala ya Zanzibar, nimeona nijitolee kusema kile ambacho wengi wao hawataki kukisikia kwa sababu wanazozijua wao. Nimeona niwe mbebaji tena wa habari mbaya kwa Chama cha CUF katika kile ambacho wao wanaamini kitaleta "maridhiano" visiwani humo.
Chama cha Mapinduzi (CCM) kimekubali kuridhia kuundwa kwa serikali ya Mseto visiwani humo kwa sababu moja tu; nayo ni kuhakikisha kuwa kamwe hakiwezi kuondolewa katika nafasi ya kushika madaraka ya uongozi wa kisiasa huko Zanzibar.
Serikali ya Mseto (au ya Umoja wa Kitaifa kama wengi wanavyoiita) ndiyo njia pekee na ya uhakika zaidi ya Chama cha Mapinduzi kubakia katika uongozi wa visiwa hivyo endapo Chama kingine (a.k.a CUF) kitashinda uchaguzi huo.
Kwa kukumbatia wazo la kuundwa kwa serikali ya mseto, Chama cha Wananchi (CUF), kimsingi, kimeridhia kwamba hakiwezi kuunda serikali yake bila kuhusisha Chama cha Mapinduzi.
Hii ina maana ya kwamba CUF kikishinda uchaguzi visiwani humo hakiwezi kutekeleza sera zake ambazo kilizipendekeza kwa wapiga kura isipokuwa kwa kuwashirikisha CCM.
Kuna ubaya gani?
Mtu ambaye hasomi vizuri ninachosema jibu lake la kwanza ni; kwani kuna ubaya gani kama vyama hivi vinashirikiana? Ubaya uliopo ni kwamba kwa miaka zaidi ya 40 sasa, Chama cha Mapinduzi (ASP kabla ya kuungana) kimeweza kutawala visiwa hivyo na kutekeleza sera zake na kusimamia mambo yake bila kukubali serikali ya mseto wakati hali ya mgawanyiko wa kisiasa walikuwa wanaijua tangu zamani.
Kuanzia chaguzi zote za Zanzibar kuna ushahidi wa wazi kuwa visiwa hivyo vimegawanyika kisiasa na kimaslahi kiasi kwamba wazo la mseto lilikuwa ni njia pekee ya kujaribu kutawala visiwa hivyo.
Kwa miaka yote hii baada ya kuipindua serikali ya mseto ya Shamte, ASP na CCM baadaye hawakuona ulazima wowote wa kujaribu kuunda umoja wa kitaifa.
Hawakuona ulazima huo mwaka 1995, hawakuona ulazima huo 2000 na hawakuona ulazima huo 2005. Ulazima huo unaonekana sasa kwa sababu kuna uwezekano mkubwa zaidi wa Chama cha CUF kushinda uchaguzi wa Rais mwaka huu, na kama hilo litatokea CCM haiko tayari kuona kuwa kinawekwa pembeni ya uongozi kwa kuachia CUF kuunda serikali yake.
Kwa maneno mengine, ubaya mkubwa ni kuwa badala ya kuwa na mgongano wa kugombania madaraka ambao tumeuona miaka hii iliyopita, tutakachokiona baada ya kuundwa kwa serikali ya mseto ni ‘kugombania' kutumia madaraka.
Je ni sera za chama gani zitatekelezwa pale inapoundwa serikali ya mseto? Itakuwaje kama chama cha CUF kina wingi wa wabunge na kimeshinda kura kinapojaribu kutekeleza sera zake na CCM inaona kuwa sera hizo si nzuri kwa Zanzibar na wamekubaliana kushiriki katika serikali hiyo? Itakuwaje mapendekezo ya wajumbe wa CCM yatakapokataliwa na CUF?
Kama tunaweza kujifunza kutoka nchi nyingine, kinachotokea ni chama kinachopuuzwa huamua kujitoa kwenye serikali ya mseto, na hivyo kusababisha mgogoro mwingine wa kikatiba.
Tuone huo muundo wa serikali ya mseto utakavyotakiwa kuwa tunaweza kuanza kushuhudia yale tunayoyaona Canada, Israeli na nchi nyingine zenye mifumo ya kuruhusu serikali za umoja wa kitaifa; yaani chaguzi za mara kwa mara kila chama kinapojitoa katika serikali ya umoja wa kitaifa.
Anayepoteza ni CUF
Jambo moja wazi ni kuwa kwa kukubali kuwepo kwa serikali ya mseto, chama cha CUF ndicho kinachopoteza zaidi kuliko kupata. Ni chenyewe ndicho kinalazimishwa kufungwa mikono yake na kulazimishwa kuunda serikali ya mseto wakati kimeshinda uchaguzi.
Ni wao (CUF) wanaopoteza kutumia ridhaa yao waliyopewa na wananchi kuongoza. Anayenufaika, kwa kweli, katika mpango huu ni CCM; kwani kwa kukubali kuundwa kwa serikali ya mseto CCM imehakikishiwa kuendelea kubakia madarakani na imekataa kukiachia CUF uongozi wa Zanzibar endapo kitashinda.
Kama Chama cha Mapinduzi upande wa Bara hakilazimishwi kuunda serikali ya mseto (umoja wa kitaifa) kwa sababu kinaamini kuwa kinakubalika zaidi na kimepewa mlango wa wazi wa kutawala na kutekeleza sera zake huku wapinzani wakibakia kupiga kelele majukwaani na kwenye vyombo vya habari, kwa nini chama hicho hicho kisikubali kuwa Visiwani nao wananchi wake wana haki ya kuongozwa na chama kilichoshinda?
Kwa nini waone ni wazo zuri kuwa na serikali ya mseto Zanzibar lakini siyo Bara isipokuwa kwa sababu wanajua kwamba kule Zanzibar wanaweza kweli kushindwa; kwani mwamko wa kisiasa Zanzibar ni wa muda mrefu na wenye kina cha hoja na sera zaidi kuliko Bara.
Mbinu hii itatumika hata Bara
Kwa mtu yeyote anayeweza kuona mbali anaweza kuona kuwa mbinu hii itatumika hata Bara vile vile. Endapo kabla ya uchaguzi huu mkuu wa mwaka huu kutaonekana dalili ya CCM kuangushwa katika kiti cha urais na kupoteza viti vingi vya wabunge, msishangae kuona kuwa CCM wanapendekeza kuwepo kwa serikali ya umoja wa kitaifa Tanzania Bara!
Lengo litakuwa ni lile lile kwamba kamwe CCM isiondolewe kabisa katika kumbi za wenye madaraka Tanzania.
Kuikataa serikali ya mseto siyo kukataa mapatano
Kuna baadhi ya wanasiasa ambao wanataka wananchi waamini kwamba kukataa serikali ya mseto ni sawa na kukataa maridhiano au mapatano ya kweli. Watu hawa wamewaaminisha Wanzanzibar kuwa mazungumzo ya maridhiano ni lazima yaendane na serikali ya mseto.
Hili si kweli. Wananchi wa Zanzibar, kama walivyo wananchi wa Tanzania nzima, wanastahili mazingira bora ya kisiasa ambayo yatawahakikishia kuwa wanafanya kampeni za kisiasa kwa uhuru, wanapiga kura kwa uhuru na matokeo yanapatikana kwa uhuru.
Nina uhakika wa asilimia 101 kwamba endapo mazingira huru ya uchaguzi, miundo mbinu bora ya kisiasa na usimamizi wa haki wa sheria vitawekwa Zanzibar, basi, wananchi watakuwa tayari kupokea matokeo yoyote ya uchaguzi; kwani watajua yamepatikana kwa haki kabisa na kwa uwazi.
Kugawanyika nusu kwa nusu si msingi serikali ya mseto
Mojawapo ya visingizio vya kukubali serikali ya mseto ni kugawanyika kwa wapiga kura kiasi kwamba hakuna anayepata kura nyingi. Kwa haraka haraka hii inaweza kuwa ni kama sababu ya kutaka kuundwa kwa serikali ya mseto. Lakini ni lazima tutambue kuwa kugawanyika kwa jamii na wapiga kura ndio msingi wa demokrasia.
Demokrasia ya watu wasiogawanyika siyo demokrasia ya kweli. Msingi mkubwa wa utawala wa demokrasia ni kuweza kuwashawishi wale ambao hawakubaliani na wewe ili wakubaliane na wewe na wakuchague.
Kama sera za chama fulani ni nzuri na zenye mantiki, basi, zitavutia mashabiki wa chama kile na wale wa vyama vingine na hata wale wasio na vyama; pale inapotokea kuwa sera za vyama fulani zinakaribiana sana au zinatofautiana sana kiasi cha kugawa watu nusu kwa nusu; maana yake ni kwamba uwezekano wa kubadilisha madaraka kila baada ya uchaguzi unakuwa ni mkubwa sana.
Nitatoa mifano kwa kuangalia Marekani ambapo vyama vya Democrat na Republican ndivyo vyenye nguvu zaidi. Ninaangalia kura za mtu mmoja mmoja na siyo ya Baraza la Kuchagua Rais.
Mwaka 1992 Bill Clinton alishinda urais wa Marekani kwa kupata asilimia 43 dhidi ya 37.4 za George H. Bush; huku Ross Perot akichukua asilimia 18.9. - Democrat wakachukua nchi toka kwa Republican.
Mwaka 1996 Bill Clinton alipata asilimia 49.2 ya kura zote wakati Bob Dole alipata asilimia 40.7 na Ross Perot akapata asilimia 8.4 – Democrat wakaendeleza kushikilia nchi.
Rais Bush alipogombea tena mwaka 2004 alishinda kwa kupata asilimia 50.7 ya kura zote dhidi ya John Kerry aliyepata asilimia 48.3. – Republican wakachukua nchi mara ya pili tena.
Rais Barack Obama katika ushindi wake wa kihistoria wa 2008 alipata asilimia 52.9 dhidi ya zile za John McCain za asilimia 45.7 – Democrat wakachukua nchi toka kwa Republican.
Hii ina maana ya kwamba kugawanyika karibu nusu kwa nusu kwenye taifa siyo jambo baya kama CCM na CUF wanataka wananchi waamini.
Kugawanyika kwa namna hii ni kuzuri kwa taifa kwani kutatoa nafasi kwa CUF na CCM kupishana madaraka kila baada ya miaka mitano kutegemea na nani anauzika vizuri, nani sera zake ni bora zaidi na nani wananchi wanamuamini kuboresha maisha yao.
Kwa kulazimisha serikali ya mseto kama walivyofanya wanawanyima wananchi nafasi ya kupima uongozi wa chama kimoja na kukibadilisha na kingine.
CUF wasikubali serikali ya mseto isiyo na masharti
Baada ya kusema haya sina budi kutoa mapendekezo yangu kuhusu suala hili na jinsi gani tunaweza kuweka uwezekano wa kuwepo kwa serikali ya mseto (iwe Bara au Visiwani) bila kuilazimisha kwa mshindi kiholela.
Narudia kauli hii hapa: tunaweza kuweka uwezekano wa kuwepo kwa serikali ya mseto (iwe Bara au Visiwani) bila kuilazimisha kwa mshindi kiholela. Haya ni mapendekezo yangu tu yanaweza kusahihishwa na kuboreshwa zaidi.
Kwanza kabisa: Uundwaji wa serikali ya mseto utegemee asilimia ya ushindi. Mshindi wa yeyote wa kiti cha urais anayepata kura chini ya asilimia 55 atalazimika kuunda serikali ya mseto kwa kuchagua asilimia 45 ya manaibu waziri kutoka chama au vyama vinavyofuatia kwa mgawanyo wa asilimia ya kura zao (kama CUF inapata asilimia 30 basi itatoa manaibu asilimia 30, kama TLP inapata asilimia 5 basi itatoa manaibu asilimia 5 n.k)
Pili, Chama kinachopata ushindi wa kati ya asilimia 50 na asilimia 55, basi, kitaunda serikali ya mseto pamoja na kuteua manaibu itatoa nafasi za uwaziri kamili kwa asilimia tano.
Tatu, hakuna chama kitakachounda serikali yoyote kikipata kura chini ya asilimia 50 isipokuwa kwa kushirikiana na chama kingine au vingine hadi kifikishe zaidi ya asilimia 50 au zaidi. Endapo hilo haliwezekani ndiyo serikali ya mseto ya umoja wa kitaifa inaundwa huku nafasi za juu za uongozi wa taifa zikigawanywa kwa vyama vilivyopata kura nyingi zaidi. Bila kuweka kanuni tunachoshuhudia ni kuchezea demokrasia
Endapo wana CUF watakubali kichwa kichwa kuundwa kwa serikali ya mseto watajikuta wanafungwa na sharti hilo kiasi kwamba watashindwa kutekeleza ahadi zao kwa wananchi.
Pendekezo bora ni kutokuwa na mseto
Pendekezo langu kubwa zaidi ni kuwa CUF wasikubali kuwepo kwa serikali ya mseto isipokuwa walilie mabadiliko ya mfumo wa uchaguzi, kampeni, na utangazaji matokeo. Walilie na kupigania uwazi, usawa, na haki katika uchaguzi na hasa utendaji huru wa tume za uchaguzi, uhuru wa vyombo vya dola, na matumizi ya haki ya vyombo vya habari katika kampeni.
Lakini Kama ni wanademokrasia wa kweli walilie kuwa atakayeshinda ndiye aunde serikali apendavyo. Lakini ushindi ni lazima uwe katika mazingira huru ya kisiasa na ya haki kwa wote.
Wasipofanya hivyo basi kitakachotokea ni kile kisemwacho "papa mkaange kwa mafuta yake" na "kitanzi jitie mwenyewe". Kwa kukubali serikali ya mseto, CUF wameuziwa mbuzi kwenye gunia na wao na mashabiki wao wanafikiri wamepata, ngoja wafike nyumbani.
hs3.gif



 
That was a hard choice better results need time and tolerance. Agreeing to disagree is always there for some matters, the bottom line we don't want someone to die just because of of any avoidable reason. As time past we have learn a lot generational violence should be avoided in any cost, mutual concert is necessary. aNGALIA KENYA rAILA NI pM LAKINI HAPATI USINGIZI JUST BECAUSE HE IS NOT A PRESDENT
 
jamadari,

Ni vigumu sana kusoma "article" isiyo na nukta wala koma!, na hata paragraph!.

Iweke vizuri halafu tusome na kuchangia

 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom