Mzee Mwanakijiji
Platinum Member
- Mar 10, 2006
- 33,476
- 39,995
Na. M. M. Mwanakijiji
Mtu anaweza kukudharau kwa vitu vingi sana; anaweza kukudharau kwa sababu huvai nguo kama za kwake, huna gari kama lake, unaishi maisha duni, au hata huzungumzi kwa ufasaha kama yeye. Dharau kubwa walizonazo watu dhidi ya wengine zinahusiana hasa na hadhi (status), mali (material wealth) na hali ya kijamii (social condition). Dharau hizi kubwa tatu zinawafanya wenye hadhi ya juu, au wenye mali zaidi au wenye kuonekana juu katika jamii wakati mwingine kuwaona wale wasio kama wao kama watu walio "chini yao". Inapuzungumzwa chini yao si kama mtu ambaye anakufikia kwa chini labda miguuni au magotini; la hasha ni kuwa 'beneath you" yaani kama ni chini ya soli zako.
Lakini dunia imejawa na mifano ya watu waliodhaniwa wako chini ambao kutokana na juhudi zao au mchanganyiko wa vitu mbalimbali wakajikuta na wao wananyanyuka kutoka huko "chini" na kupanda ngazi na kuwa juu. Wakati mwingine ni hawa hawa ambao waliwahi kuwa chini ndio ambao nao wakishafika juu huanza kuonesha dharau kwa walio chini yao. Bila ya shaka wengine ambao wametoka chini na kufika juu huwa na mtazamo wa huruma na simanzi kwa walio chini na hujitahidi kuwanyanyua.
Wakati mwingine mtu mwenye dharau hizi kubwa tatu hawezi kuridhika anapoona aliye chini naye ameanza kunyanyuka. Wapo ambao wanaweza kutumia njia mbalimbali ili kuhakikisha wale walio chini wanaendelea kuwa chini iwe kihadhi, hali au mali. Na hawa hutumia njia nyingi sana kuhakikisha wale walio chini hawawafikii pale juu. Hivyo, huwekwa vikwazo viwe vya sheria au kanuni kuhakikisha kuwa aliye chini anaendelea kuwa chini.
Tawala nyingi duniani zimejengwa kwa msingi huo. Kwamba wale ambao wanatawala huamini kuwa wanapasa kutawala au wana haki ya kutawala na hivyo huwaona watawaliwa wao kuwa wako chini. Matokeo yake watawala wa aina hii duniani hufanya kila wawezalo kuhakikisha kuwa watawaliwa hawainuki na kutaka kuwa juu ya watawala. Kwa muda - hasa kama watawaliwa hawajafunguka kifikra - hali hii (status quo) hukubalika na yumkini hata kwa vizazi na vizazi. Vipo vizazi vya watu katika jamii mbalimbali duniani ambao wamekubali hali hiyo kuwa ni haki au stahiki yao.
Hata hivyo utaona kuwa jamii ya watu yenye kutawaliwa kwa msingi huo kwa kweli kabisa haidharauliwi kwa mambo hayo matatu bali jambo moja tu - akili. Kuna hisia kwa watawala kuwa wao wana "akili sana" kiasi kwamba ndio maana wanatawala na wale watawaliwa hawana "akili kihivyo" ndio maana wanatawaliwa. Matokeo yake watawala huanza kuwaangalia watawaliwa kwa dharau; dharau ya kuwaona kuwa hawastahili hata kuwahoji, kuwauliza au kuwakatalia. Watawala hao huamini kuwa wanaweza kufanya lolote, vyovyote na kwa yeyote na watawaliwa waliokubali hilo huamini wanaweza kufanyiwa lolote, vyovyote na yeyote kutoka kona za watawala.
Ni hili ambalo hatimaye huwa msingi wa mgongano kati ya watawala na watawaliwa. Kwamba watawaliwa ambao "wamefunguka" wanapoamua kukataa au kuwakatalia watawala. Hakuna kitu ambacho kinawashangaza watawala kama watawaliwa wasiokubali hadhi, hali na mali yao duni. Inawashangaza kwa sababu hawaamini kama watawaliwa wanaweza kuwa na "akili" za kujitambua kuwa wao ni nani. Tena watawala wanaweza hata kuzungumza kwa dharau; utasikia wanasema "wananchi wetu hawajui" au "inabidi tuwaelimishe kwanza wananchi" au "wananchi wanadanganywa na upinzani"; kimsingi wanaona wananchi hawana akili ya kuweza kufikiria wenyewe na kuamua kutenda kutokana na matokeo ya fikara zao.
Ni dharau inayoshangaza sana kwani hawa watawala wanawadharau watu wale ambao wamewapoa wao madaraka. Yaani, walipowapa madaraka (kwa kuwachagua na kufanya kazi kulipa mishahara yao) wananchi hawana hawana akili za kutambua wanapoburuzwa au kudanganywa au kuuziwa maneno na ahadi hewa! Walikuwa na akili walipopiga kura lakini walipotaka kujua kura zao zinafanyaje kazi wananchi hawa hawaaminiwi!
Sasa, wananchi ambao wanaamini kuwa watawala ndio wana akili zaidi kuliko wao hawawezi kamwe kuwahoji watawala wao. Watathubutu vipi wakati watawala ndio "elite"? Wananchi ambao wameambiwa "hawajui" au "hawana uwezo wa kujua" wataweza vipi kuhoji watawala kuhusu fedha, utendaji, au sera fulani fulani. Mara nyingi wananchi wanaojaribu kufanya hivyo hunyamazishwa kwa kuambiwa "serikali imejizatiti" au "serikali inajipanga" au "serikali iko mbioni"! Mtu ambaye ana akili akiuliza "mbona mmekuwa mkisema mnajizatiti, kujipanga na kuwa mbioni tangu mwaka elfu mia tisa kweusi?" watawala hapo hucharuka na kumuona huyo mtu kama mleta majungu, anachonganisha watu na "anajifanya anajua sana" wengine wanamuita "kimanyi"
Ndugu zangu, kwa nchi yetu hapa ndipo ilipochangamoto ya kizazi kipya cha Watanzania. Je wataendelea kuambiwa na kupigishwa stori na watawala mpaka lini? NI kwa muda gani wananchi wenye akili wataendelea kuambiwa visingizio na sababu zisizo na kichwa wala miguu na wao wakakubali? Ni jinsi gani waandishi wa habari wanaweza kukaa chini na kusikiliza masimulizi ambayo hayaingii kichwani lakini wanashindwa kuhoji au kukataa kwa sababu wanaogopa labda wataonekana wanakimbelembele. Au mtu anaweza kuelezea vipi waandishi ambao wanaenda kusikiliza "mkutano wa waandishi wa habari" na kushika kalamu na vinasa sauti zao na baadaye wanaondoka bila hata kutaka kuuliza maswali? Mtu akishakudharau akili anaweza kukuambia lolote!
Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere aliwahi kusema lile neno maarufu - mtu mweye akili akikushauri jambo la kipumbavu akijua kuwa na wewe una akili halafu na wewe ukakubali atakudharau. Ni kweli; lakini mimi naweza kusema mtu mwenye akili akifikiria kuwa wewe huna akili halafu akakuambia jambo la kipumbavu na wewe ukakubali basi amethibitisha kukudharau kwake. Ndio maana mojawapo ya maneno tuliyojifunza wakati wa kupigania huru bado yanarindima kiukweli - tumedharauliwa kiasi cha kutosha! Lakini ukiangalia sana utaona kuwa Watanzania bado hawajachoshwa kudharauliwa; walichoshwa kudharauliwa na wazungu tu! Leo hii wanapodharauliwa na watawala weusi hawawezi hata kuhoji; hawawezi kukataa na kwa hakika hawawezi hata kuonesha kuwa wanatambua wamedharauliwa!
Mpaka kizazi cha watakaokataa kudharauliwa na watawala kitakapoinuka. Kwa mbali naweza kukiona kizazi hicho kikichukua nafasi yake taratibu. Angalia vijana, angalia madaktari, angalia wafanyakazi - wapo kati yao kundi la wale wasiokubali kudharauliwa na watawala. Je waweza kujua kama wewe hujali kudharauliwa na unakubali kudharauliwa? Naam!
Jiulize ukisikia "serikali imesema" mwitikio wako ni nini? je unahoji? Je unapima kama inaingia akilini? je unaona kuna vitu haviko sawa? au unafunga mjadala na kukubali bila kuhoji?
Niandikie: mwanakijiji@jamiiforums.com