Hoja ya Lissu ya kukataa marekebisho ya sheria yaungwa mkono na wabunge wa CCM | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Hoja ya Lissu ya kukataa marekebisho ya sheria yaungwa mkono na wabunge wa CCM

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by Mpaka Kieleweke, Feb 2, 2012.

 1. Mpaka Kieleweke

  Mpaka Kieleweke JF-Expert Member

  #1
  Feb 2, 2012
  Joined: Feb 27, 2007
  Messages: 4,137
  Likes Received: 67
  Trophy Points: 145
  MAONI YA MSEMAJI WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI, WIZARA YA SHERIA NA KATIBA, MHESHIMIWA TUNDU A.M. LISSU (MB.)KUHUSU MUSWADA WA SHERIA YA MAREKEBISHO YA SHERIA MBALIMBALI (NA. 2) YA MWAKA 2011 (WRITTEN LAWS (MISCELLANEOUS AMENDMENTS) BILL (NO. 2), 2011)UTANGULIZI
  Mheshimiwa Spika,Muswada ya Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na. 2) wa mwaka 2011 (The Written Laws (Miscellaneous Amendments) Bill (No. 2), 2011) ulichapishwa katika Gazeti la Serikali la tarehe 4 Novemba, 2011. Muswada huu umesomwa kwa Mara ya Kwanza na hatua zake zote kwa mujibu wa kanuni ya 93(2) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, 2007 juzi tarehe 31 Januari, 2012. Aidha, kabla ya kusomwa kwa mara ya kwanza, Muswada huu ulishapelekwa kwenye Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala kwa ajili ya kujadiliwa na Kamati hiyo. Hii ilikuwa kinyume na matakwa ya kanuni ya 83(1) ikisomwa pamoja na kanuni ya 84(1) ya Kanuni za Bunge zinazoelekeza Muswada wowote wa Sheria ambao umetangazwa katika Gazeti kupelekwa kwenye Kamati husika baada ya Kusomwa kwa Mara ya Kwanza. Kwa mujibu wa Kanuni za Bunge hili tukufu, Muswada wa Sheria ambao umetangazwa katika Gazeti hauwezi kupelekwa katika Kamati husika bila kwanza Bunge zima kupatiwa taarifa rasmi juu ya Muswada wenyewe kwa kupitia Muswada Kusomwa kwa Mara ya Kwanza.

  Mheshimiwa Spika, Utaratibu uliotumika kuwasilisha Muswada huu Bungeni na kuujadili hauna tofauti yoyote ya kimsingi na utaratibu wa kuwasilisha miswada kwa Hati ya Dharura chini ya kanuni ya 93(3) ya Kanuni za Bunge. Hii ni kwa sababu, lengo, madhumuni na athari ya matumizi ya kanuni ya 93(2) na 93(3) ni kufupisha muda unaotumika katika utungaji wa sheria kwa kudhibiti mjadala Bungeni. Kama nilivyowahi kusema wakati wa kujadili Muswada wa Sheria ya Uendeshaji Mahakama, 2011 katika Mkutano wa Tatu wa Bunge hili tukufu:

  "Muda wa kutunga sheria ukifupishwa maana yake ni kwamba Wabunge na wadau mbali mbali hawatapata muda wa kutosha wa kuusoma, kuuchambua, kuuelewa Muswada wa Sheria na kuchangia katika uboreshaji wake. Kwa sababu hizi, utaratibu huu hutumika tu ili kupitisha sheria zinazohitajika wakati wa maafa, vita au dharura nyingine za aina hiyo. Kwa maana nyingine, utaratibu wa kutumia hati ya dharura katika kutunga sheria ni utaratibu usiokuwa wa kidemokrasia lakini ambao unahalalishwa pale kunapokuwepo na dharura ya kweli inayohitaji sheria itungwe haraka ili kukabiliana nayo."

  Kama nilivyoeleza wakati huo, matokeo ya kutumia kanuni ya 93(2) na (93(3) ya Kanuni za Bunge ni kuwa na sheria zinazotungwa haraka haraka na kwa hiyo "... zinakosa uhalali wa kisiasa kwa sababu ya kukosa ushiriki wa Wabunge na wadau wengine. Vile vile, sheria hizo zinakuwa na makosa mengi kwa sababu ya kukosekana umakini katika kuzitunga na utekelezaji wake kisiasa na kisheria unakuwa mgumu.

  Aidha, sheria za aina hiyo zinafisha demokrasia na uwajibikaji wa Serikali kwa Bunge na kwa wananchi kwa sababu jukumu la kikatiba la Bunge kama baraza la kutunga sheria na la kusimamia serikali linageuzwa kuwa ni la kupiga muhuri maamuzi na mapendekezo yanayoletwa na Serikali. Mwishowe, Bunge la aina hiyo linakosa hadhi na heshima kwa wananchi na hivyo kukaribisha aina nyingine za siasa za nje ya Bunge.
  "

  Mheshimiwa Spika, Kwa vile ulichapishwa katika Gazeti tarehe 4 Novemba, 2011, Muswada huu ungeweza kuwasilishwa kwa ajili ya Kusomwa kwa Mara ya Kwanza katika Mkutano wa Tano wa Bunge hili tukufu Ulioanza tarehe 8 Novemba, 2011. Hii ingeipa Kamati husika, Wabunge wote na wadau wengine nje ya Bunge muda wa kutosha kufanya maandalizi kwa ajili ya mjadala wa kuupitisha katika Mkutano huu wa Bunge. Badala yake, Bunge hili tukufu sasa linatakiwa kuujadili na kuupitisha Muswada – ambao hauna sababu yoyote ya dharura - siku mbili tu baada ya Kusomwa kwa Mara ya Kwanza. Kwa sababu ya kuongezeka kwa hatari ya Bunge hili tukufu kugeuzwa kuwa la kugonga muhuri miswada na mapendekezo ya Serikali, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaishauri Kamati ya Uongozi pamoja na wewe mwenyewe,

  Mheshimiwa Spika, kutumia mamlaka yenu chini ya kanuni za 80(5) na (6) na 93(2)(b) ya Kanuni za Bunge kulinda mamlaka, hadhi na heshima ya Bunge hili tukufu kwa kuhakikisha kwamba miswada ya sheria isiyokuwa na dharura yoyote inawasilishwa, kujadiliwa na kupitishwa kwa kutumia utaratibu wa kawaida uliowekwa na Sehemu ya Nane ya Kanuni za Bunge.
  Mheshimiwa Spika, Sasa ninaomba, kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani, kujadili mapendekezo ya marekebisho ya sheria mbali mbali yaliyoko katika Muswada huu.
  MAREKEBISHO YA SHERIA YA BODI YA MIKOPO YA WANAFUNZI WA ELIMU YA JUU, SURA YA 178 YA SHERIA ZA TANZANIA
  Mheshimiwa Spika, Muswada unapendekeza kufanya marekebisho katika vifungu kadhaa vya Sheria ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu, Sura ya 178 ya Sheria za Tanzania. Kwanza, inapendekezwa kurekebisha kifungu cha 5 cha Sheria hiyo kwa kuongeza idadi ya wajumbe wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu kutoka wajumbe kumi na tatu walioko chini ya Sheria ya sasa hadi wajumbe kumi na nne. Hii inafanywa kwa kuongeza mwakilishi wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania na mwakilishi wa wanafunzi wa taasisi za elimu ya juu za umma; na kupunguza uwakilishi wa watu mashuhuri wenye utaalamu na uzoefu katika uendeshaji wa taasisi za elimu ya juu.

  Kwa mujibu wa Sheria ya sasa, Tume ya Vyuo Vikuu na wanafunzi wa taasisi za elimu ya juu za umma hawana uwakilishi katika Bodi ya Mikopo.
  Pamoja na inayoonekana kuwa nia njema ya kutoa fursa ya uwakilishi wa taasisi hizi katika Bodi ya Mikopo, hakuna ushahidi wa kuthibitisha kwamba kutokuwepo kwao kumeathiri utendaji wa Bodi ya Mikopo. Aidha, hakuna uhakika kwamba uwepo wao katika Bodi ya Mikopo utaiongezea Bodi hiyo tija yoyote. Hii ni kwa sababu, kwa mujibu wa kipengele cha 9 cha Nyongeza ya Sheria ya Bodi ya Mikopo, maamuzi ya Bodi hayawezi kubatilishwa kwa sababu tu ya kutokuwepo kwa mjumbe, au kutokana na mapungufu ya uteuzi wa mjumbe yeyote.

  Vile vile, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imepata taarifa kwamba licha ya kuwa wajumbe wa Bodi ya Mikopo kwa mujibu wa Sheria ya sasa, mwakilishi wa wanafunzi wa taasisi za elimu ya juu za binafsi amekuwa haalikwi kwenye vikao vya Bodi kwa nyakati mbalimbali. Hii ina maana kwamba kuongeza uwakilishi wa wanafunzi wa taasisi za umma wakati wawakilishi wenzao wa taasisi za binafsi hawashirikishwi kwenye vikao vya Bodi hakutatatua matatizo mbalimbali ya Bodi ya Mikopo.
  Mheshimiwa Spika, Sehemu ya pili inayopendekezwa kurekebishwa ni kifungu cha 7 cha Sheria ya Bodi ya Mikopo. Kifungu hiki kinaainisha mamlaka mbalimbali ya Bodi ya Mikopo.

  Hapa inapendekezwa kurekebisha kifungu cha 7(i) kwa kuipa Bodi mamlaka ya kuamua idadi ya juu ya wanafunzi wanaostahili kupatiwa mikopo kila mwaka "kwa kuzingatia ukomo wa bajeti ya Serikali." Kwa mujibu wa Madhumuni na Sababu za Muswada huu, kwa sasa Sheria "... inaelekeza mikopo itolewe kufuatana na vigezo vya ukopeshaji ... ambavyo vinaruhusu wanafunzi wengi kukopeshwa bila kuzingatia ukomo wa bajeti...."

  Pendekezo hili linaleta dhana potofu kwamba Bodi inatoa mikopo kwa wanafunzi wengi bila kuzingatia ukomo wa bajeti inayotolewa kwa Bodi kwa ajili hiyo.
  Ukweli, kama Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo alivyoieleza Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala, ni kwamba Bodi ya Mikopo inazingatia ukomo wa bajeti ya Serikali kwa sababu Serikali ndiyo chanzo pekee cha fedha za mikopo ya wanafunzi zinazotolewa na Bodi. Kwa hiyo, hata bila kuwepo kwa maneno ‘kwa kuzingatia ukomo wa bajeti ya Serikali' kwenye Sheria hii, Bodi ya Mikopo inalazimika kuendelea kuzingatia ukomo wa bajeti ya Serikali katika kutoa mikopo kwa wanafunzi!

  Kwa sababu hiyo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaamini kwamba sababu halisi ya pendekezo hili ni kuipa Bodi ya Mikopo na Serikali kinga ya kisiasa dhidi ya tuhuma kwamba imeshindwa kutatua matatizo makubwa ya mikopo ya wanafunzi ambayo yamepelekea migogoro isiyoisha kati ya Serikali na wanafunzi karibu taasisi zote za elimu ya juu nchini.

  Mheshimiwa Spika, Sehemu ya tatu inayopendekezwa kurekebishwa ni kuiongezea Bodi ya Mikopo mamlaka ya kutoa ruzuku (grants), msaada wa masomo (bursary) na fedha za kusomea (scholarships). Hata hivyo, utekelezaji wa lengo hili zuri unaelekea kukanushwa na kufifishwa na sharti la ‘uwepo wa fedha' ambalo limewekwa katika pendekezo la kifungu kipya cha 7(j) cha Sheria ya Bodi ya Mikopo. Kama imeshindikana kuwapa wanafunzi mikopo wanayoihitaji kila mwaka kwa madai ya uhaba wa fedha, Bodi ya Mikopo itatumia muuajiza gani kupata fedha za kutoa ruzuku, fedha za msarifu na misaada ya masomo ambayo kwa kawaida hutolewa bure kwa wanafunzi wanaostahili?

  Pendekezo la kifungu kipya cha 7(k) nalo linatia mashaka makubwa juu ya utekelezaji wake. Kifungu hicho kinapendekeza kuipa Bodi ya Mikopo mamlaka ya kuomba na kupatiwa taarifa za wanufaika wadaiwa wa mikopo kutoka kwenye mifuko ya hifadhi za jamii kama vile LAPF, NSSF, POPF na PSPF. Masharti haya yatazihusu pia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA). Kwa vile hakuna masharti kwa taasisi zote hizi kuisaidia Bodi ya Mikopo kukusanya madeni ya wanufaika wadaiwa, kama ilivyo kwa waajiri kwa mujibu wa vifungu vya 20 na 21 vya Sheria ya Bodi ya Mikopo, haieleweki ni kwa namna gani taarifa za wanufaika wadaiwa zilizoko kwenye mifuko ya hifadhi za jamii au BRELA au TRA "[zi]tarahisisha urejeshwaji wa mikopo inayodaiwa", kama inavyodaiwa kwenye Madhumuni na Sababu za Muswada huu.

  Mheshimiwa Spika, Eneo la tano lenye utata linahusu mapendekezo ya marekebisho ya vifungu vya 16 na 17 vya Sheria ya Bodi ya Mikopo. Kifungu cha 16 kinaipa Bodi wajibu kisheria wa kutoa mikopo kwa wanafunzi; mamlaka ya kupanga asilimia ya gharama za elimu ya juu ambayo mwanafunzi atatakiwa kuchangia; na kinachomtaka mwanafunzi kuchangia kiwango cha fedha sawa na asilimia ambayo imepangwa na Bodi. Kwa mujibu wa mapendekezo ya marekebisho, mikopo sasa itatolewa kwa wanafunzi waliodahiliwa moja kwa moja kwenye taasisi ya elimu ya juu baada ya kumaliza elimu ya sekondari.

  Aidha, inapendekezwa kwamba wanafunzi wanaotokea makazini hawatastahili kupewa mikopo, ijapokuwa makatazo haya hayatawahusu wanafunzi waliodahiliwa kusomea ‘taaluma za kipaumbele cha kitaifa.'
  Kwa upande mwingine, kifungu cha 17 kinaainisha sifa mbalimbali anazotakiwa kuwa nazo mwombaji wa mkopo. Sasa inapendekezwa kwamba licha ya sifa hizo, Bodi ya Mikopo inatakiwa iangalie pia uwezo wa kitaaluma wa mwombaji, mahitaji yake na udahili katika taaluma za kipaumbele kitaifa. Vile vile Bodi inatakiwa kuangalia mwenendo wa zamani wa mwombaji katika kulipa ada katika shule za sekondari; uwezo wa kifedha wa mzazi au mlezi; na hali ya kifamilia kwa maana ya uyatima au ulemavu wa mwombaji.

  Hata hivyo na licha ya masharti haya mapya, Bodi inatakiwa kuwapa kipaumbele wanafunzi waliodahiliwa katika kozi za kipaumbele kitaifa zilizoainishwa katika Nyongeza ya Pili inayopendekezwa kuingizwa katika Sheria. Kozi zinazotajwa katika Nyongeza hiyo ni pamoja na ualimu wa sayansi na hisabati, sayansi, sayansi za udaktari na uhandisi. Nyingine ni sayansi za kilimo, mifugo, udaktari wa mifugo na hisabati

  .
  Mheshimiwa Spika, Mapendekezo haya yanazua maswali mengi ambayo Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kuyajibu mbele ya Bunge hili tukufu. Kwanza, mapendekezo ya marekebisho ya kifungu cha 16 yanakinzana moja kwa moja na masharti ya kifungu cha 17 cha Sheria ya sasa. Hii ni kwa sababu, wakati marekebisho yanapendekeza wanafunzi waliotokea makazini wasipewe mikopo isipokuwa tu kama wamedahiliwa kusomea taaluma za kipaumbele kitaifa, kifungu cha 17(1)(e) cha Sheria ya sasa kinampa haki ya kufikiriwa kupatiwa mkopo kila mwanafunzi anayeendelea na masomo na ambaye amefaulu mitihani ya kumwezesha kuendelea na masomo kwa mwaka au hatua ya masomo inayofuata. Kifungu hiki hakijaguswa kabisa na mapendekezo ya marekebisho ya kifungu cha 17. Kwa sababu ya ukimya huu,

  Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali itoe tamko rasmi mbele ya Bunge hili tukufu kama athari za kupitishwa kwa mapendekezo ya ibara ya 6 ya Muswada huu ni pamoja na kurekebisha, by implication, masharti ya kifungu cha 17(1)(e) ya Sheria ya sasa kwa kadri inavyowahusu wanafunzi waliotokea makazini. Vile vile, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali itamke hadharani kama wanafunzi wanaotokea makazini, na ambao kwa mujibu wa kifungu cha 17(1)(e) cha Sheria ya sasa wanastahili kupatiwa mikopo, watanyimwa mikopo hiyo endapo mapendekezo ya marekebisho ya kifungu cha 16 yatapitishwa na kuwa sheria.

  Mheshimiwa Spika, Athari ya pili ya kupitishwa kwa mapendekezo ya marekebisho ya vifungu vya 16 na 17 vya Sheria ya Bodi ya Mikopo itakuwa ni kuingiza ubaguzi mkubwa katika mfumo wa utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu katika nchi yetu. Kwa mfano, wanafunzi wanaotokea makazini sasa wataweza kunyimwa mikopo wakati wanafunzi wanaotokea shule za sekondari moja kwa moja watakuwa na haki ya kupata mikopo hata kama wote wanasomea taaluma zile zile! Aidha, wanafunzi waliodahiliwa katika kile kinachoitwa ‘kozi za kipaumbele kitaifa' watakuwa na haki ya kupatiwa mikopo wakati wanafunzi wenzao waliodahiliwa katika kozi nyingine zilizoruhusiwa na Serikali kupitia Tume ya Vyuo Vikuu hawatakuwa na haki hiyo. Na kama ni hivyo, kwa nini Serikali isitangaze wazi kwamba ni marufuku kwa wanafunzi wa Kitanzania kusomea taaluma ambazo Serikali inaziona sio za ‘kipaumbele kitaifa!

  Mheshimiwa Spika, Mapendekezo haya yataleta ubaguzi mkubwa pia kati ya masikini na matajiri hapa nchini, na kati ya wanafunzi wanaotokea vijijini na wale wanaotokea mijini. Hii ni kwa sababu hakuna mtu anayeweza kubishia ukweli kwamba shule za sekondari za kata ambazo zimejengwa kwa maelfu katika maeneo ya vijijini ni shule za watoto wa masikini ambao kwa kiasi kikubwa wanaishi vijijini. Vile vile, hakuna anayeweza kubishia ukweli kwamba shule hizo zina upungufu mkubwa wa karibu kila kitu kinachotakiwa katika elimu ya sekondari, kuanzia walimu wa masomo yote, vyumba vya madarasa, maabara kwa ajili ya masomo ya sayansi, maktaba, vitabu, madawati, mabweni, chakula, maji, umeme, n.k.

  Aidha, hakuna anayeweza kubishia ukweli kwamba shule nyingi za binafsi na za Serikali zinazoongoza kwa ubora wa miundo mbinu yake na ubora wa mahitaji ya kitaaluma ndizo zinazoongoza kwa viwango vya ufaulu na ndizo zinazosomesha wanafunzi wanaotoka kwenye familia tajiri na/au za wenye kipato kikubwa. Nyingi ya shule hizi pia ziko maeneo ya mijini au pembezoni mwa miji na kwa hiyo zimeunganishwa na miundo mbinu bora ikilinganishwa na shule za vijijini.
  Kwa sababu za upungufu wa mahitaji haya muhimu kielimu, ufaulu wa wanafunzi wa shule za sekondari za kata ni wa chini sana kulinganisha na ufaulu wa wanafunzi wa shule za sekondari za binafsi au za Serikali zilizoko kwa kiasi kikubwa katika maeneo ya mijini.

  Kwa mapendekezo ya marekebisho ya kifungu kipya cha 17(3)(a)(i) cha Sheria ya Bodi ya Mikopo, itakuwa ndoto kwa wanafunzi wanaotoka katika familia masikini za vijijini na mijini na ambao wamesomea katika shule za sekondari za kata kupatiwa mikopo kwa sababu ya ufaulu wa chini kwa ujumla wa shule hizo, na kwa sababu ya ufaulu wa chini katika masomo ya sayansi ambao utawazuia wanafunzi hao kusomea ‘taaluma za kipaumbele kitaifa.'
  Kwa upande mwingine, kwa mapendekezo haya, ni wanafunzi wanaotoka familia zenye vipato vikubwa na wanaoishi maeneo ya mijini na kusomea katika shule bora za binafsi na za Serikali ndio pekee watakaokuwa na haki ya kupatiwa mikopo na Bodi ya Mikopo kwa sababu ya viwango vyao vikubwa vya ufaulu katika masomo yote kwa ujumla na hasa hasa katika masomo ya sayansi. Na endapo mapendekezo haya yatapitishwa na kuwa sheria, Bunge hili tukufu na Serikali ya Chama cha Mapinduzi itakuwa imetimiza kile kilichoandikwa katika maandiko matakatifu kwamba ‘aliyenacho ataongezewa na asiyekuwa nacho atanyang'anywa hata kile kidogo alicho nacho'!

  Mheshimiwa Spika, Ibara ya 13(2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 inatamka wazi kwamba "ni marufuku kwa sheria yoyote iliyotungwa na mamlaka yoyote katika Jamhuri ya Muungano kuweka sharti lolote ambalo ni la ubaguzi ama wa dhahiri au kwa taathira yake." Ibara ya 13(5) inatafsiri neno ‘kubagua' kumaanisha "... kutimiza haja, haki au mahitaji mengineyo kwa watu mbalimbali kwa kuzingatia ... pahala walipotokea ... au hali yao ya maisha kwa namna ambayo watu wa aina fulani wanafanywa ... dhaifu au duni na kuwekewa vikwazo au masharti ya vipingamizi ambapo watu wa aina nyingine wanatendewa tofauti au wanapewa fursa au faida iliyoko nje ya masharti au sifa za lazima...."

  Vile vile, ibara ya 11(2) inatamka wazi kwamba "kila mtu anayo haki ya kujielimisha, na kila raia atakuwa huru kutafuta elimu katika fani anayopenda hadi kufikia upeo wowote kulingana na stahili na uwezo wake." Zaidi ya hayo, ibara ya 11(3) inaitaka Serikali kufanya "... jitihada kuhakikisha kwamba watu wote wanapata fursa sawa na za kutosha kuwawezesha kupata elimu na mafunzo ya ufundi katika ngazi zote za shule na vyuo vinginevyo vya mafunzo."

  Mheshimiwa Spika, Ni jana tu Bunge hili tukufu limepitisha azimio la kuridhia Mkataba wa Vijana wa Afrika wa mwaka 2006. Ibara ya 2(2) ya Mkataba huo inazitaka nchi wanachama kuchukua "... hatua zinazofaa kuhakikisha vijana wanalindwa dhidi ya aina zote za ubaguzi kutokana na hali ... walizo nazo." Hata kabla wino uliotumika kuandikia azimio hilo haujakauka Bunge hili tukufu linaombwa kupitisha sheria ambayo itaongeza ubaguzi kati ya vijana masikini na matajiri na kati ya vijana wanaosomea shule za kata zilizoko vijijini na wale wanaosomea shule za binafsi na/au za serikali zilizoko mijini!

  Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kutoa kauli mbele ya Bunge hili tukufu kuhusu mapendekezo ya marekebisho ya vifungu vya 16 na 17 ambayo ni ya kibaguzi kwa ‘dhahiri na kwa taathira yake', na kwa hiyo yanakiuka Katiba yetu. Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kulithibitishia Bunge hili tukufu kwamba ubaguzi huu katika mfumo wa utoaji wa mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu nchini unalenga kurekebisha matatizo gani mahususi katika jamii yetu ili uweze kuhesabika kuwa sio ‘ubaguzi' kwa minajili ya ibara ya 13(5) ya Katiba yetu.

  Na kama Serikali itashindwa kutoa maelezo ya kuridhisha juu ya mapendekezo haya ya kibaguzi katika Sheria ya Bodi ya Mikopo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inawaomba Waheshimiwa Wabunge wote, bila kujali itikadi au kambi za kichama, wapige kura ya nafsi (conscience) zao kukataa kupitisha Muswada huu kuwa sheria.

  Mheshimiwa Spika, Mfumo wa utoaji mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu nchini umekuwa na migogoro mingi na inayoelekea kuwa sugu. Kiashiria kikuu cha migogoro hii ni migomo ya mara kwa mara ya wanafunzi wa taasisi karibu zote za elimu ya juu hapa nchini ambayo imepelekea masomo kukatishwa, vyuo vikuu vingi kufungwa na wanafunzi wengi kufukuzwa vyuoni na wengine wengi kukamatwa na kufunguliwa mashtaka ya jinai mahakamani.

  Aidha, vyuo vingi vimekuwa kama uwanja wa mapambano vyenye kukaliwa kwa nguvu za kijeshi na vikosi vya kuzuia ghasia vya Jeshi la Polisi. Militarization hii ya vyuo vikuu vya nchi yetu imeenda sambamba na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu za wanafunzi.
  Mheshimiwa Spika, Katika mazingira haya, mwezi Machi mwaka jana Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete aliteua Tume chini ya uenyekiti wa Profesa Makenya Maboko wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ili kuchunguza kiini na sababu za migogoro isiyoisha katika vyuo vyetu vikuu pamoja na mfumo mzima wa utoaji mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu hapa nchini. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inazo taarifa kwamba Tume ya Profesa Maboko ilikamilisha kazi yake baada ya kufanya uchunguzi ndani na nje ya nchi yetu na kuwasilisha ripoti yake kwa Mheshimiwa Rais mnamo mwezi Oktoba, 2011.

  Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ilitegemea – kwa kuzingatia unyeti na udharura wa hali ya sasa katika vyuo vyetu vikuu – kwamba Serikali ingewasilisha ripoti ya Tume ya Profesa Maboko hapa Bungeni sambamba na Muswada huu ili iwasaidie Waheshimiwa Wabunge kuelewa kiini na sababu za matatizo ya mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu na kuweza kuchangia katika uboreshaji wa Muswada huu.
  Hata hivyo, Mheshimiwa Spika, licha ya jitihada nyingi, sio Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala wala Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni iliyopatiwa nakala ya ripoti ya Tume hiyo. Kwa sababu hiyo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kutoa kauli kwa Bunge hili tukufu ni kwa nini ripoti ya Tume ya Profesa Maboko imefichwa hadi sasa hivi, licha ya kutumia mamilioni ya fedha za walipa kodi wa Tanzania.

  Aidha, Serikali itoe kauli ni lini, kama nia hiyo ipo, ripoti hiyo itatolewa hadharani ili sisi wawakilishi wa wananchi tuweze ‘kuisimamia na kuishauri' ipasavyo Serikali juu ya masuala ya mikopo kwa wanafunzi wa taasisi za elimu ya juu hapa nchini, kama ilivyo wajibu wetu kwa mujibu wa ibara ya 63(2) ya Katiba ya nchi yetu.
  MAREKEBISHO YA SHERIA YA KUZUIA BIASHARA YA MADAWA YA KULEVYA, SURA YA 95 YA SHERIA ZA TANZANIA
  Mheshimiwa Spika, Inapendekezwa kwamba Sheria ya Kuzuia Biashara Haramu ya Madawa ya Kulevya, Sura ya 95 ya Sheria za Tanzania irekebishwe ili kuongeza adhabu kwa makosa kadhaa yanayohusiana na madawa ya kulevya. Inapendekezwa, kwa mfano, kwamba adhabu ya kosa la kupatikana na madawa ya kulevya au mchanganyiko wa madawa hayo, au la kufanya au kushindwa kufanya tendo au kitu chochote kuhusiana na madawa ya kulevya iwe ni kifungo cha maisha. Adhabu ya sasa kwa makosa hayo, kwa mujibu wa kifungu cha 16(1)(a) cha Sheria ya Kuzuia Madawa ya Kulevya, ni faini ya shilingi milioni kumi au mara tatu ya thamani ya madawa au mchanganyiko wa madawa hayo katika soko au yoyote iliyo kubwa zaidi katika faini hizo, au kifungo cha maisha au vyote viwili, yaani kifungo cha maisha na faini.

  Inapendekezwa pia kuongeza adhabu ya kosa la kufanya biashara ya madawa ya kulevya kuwa kifungo cha maisha. Adhabu ya kosa hilo, kwa mujibu wa kifungu cha 16(1)(b) cha Sheria ya sasa, ni faini ya shilingi milioni kumi au mara tatu ya thamani ya madawa hayo katika soko au yoyote iliyo kubwa zaidi katika faini hizo, na kifungo kisichopungua miaka ishirini hadi kifungo cha maisha. Makosa mengine ambayo yanapendekezwa kuongezewa adhabu ni pamoja na kuvuta, kunusa au kutumia madawa ya kulevya kwa namna nyingine; kuvuta, kunusa au kutumia madawa hayo ndani ya nyumba, chumba au mahala pengine; kukutwa na kiko au vifaa vingine vinavyotumika kuvutia, kunusia au kutumia madawa hayo.

  Endapo mapendekezo ya Muswada huu yatapitishwa na kuwa sheria, adhabu ya makosa hayo itakuwa faini ya shilingi milioni moja au kifungo cha miaka kumi au vyote viwili, yaani kifungo na faini.
  Adhabu hii ni sawa na adhabu ya makosa hayo hayo chini ya kifungu cha 16(2)(a) na (b) cha Sheria ya sasa ambacho kinapendekezwa kufutwa. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni haifahamu hasara au matatizo yaliyokuwa yanatokana na makosa hayo kuwekwa katika kifungu cha Sheria. Vivyo hivyo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni haijafahamishwa juu ya faida, kama ipo, ya kuyahamisha makosa hayo na adhabu zake kutoka kifungu cha 16(2)(a) na (b) kwenda kifungu cha 17A kinachopendekezwa na Muswada huu.

  Inaelekea pendekezo la marekebisho ya kifungu hiki yameletwa Bungeni bila kuzingatia ufinyu wa muda wa Bunge hili tukufu na kwa hiyo Kambi Rasmi ya Upinzani inapendekeza mapendekezo haya yasikubaliwe.
  Mheshimiwa Spika, Muswada huu unapendekeza pia kuongeza adhabu ya makosa ya wamiliki, watumiaji au wasimamizi wa majengo au vyombo vya usafiri wanaoruhusu majengo au vyombo vyao kutumiwa kuandaa au kuzalisha madawa ya kulevya; au wanaokutwa na vyombo au vifaa vya kutengenezea madawa ya kulevya. Adhabu ya sasa ya makosa hayo ni faini ya shilingi milioni moja au kifungo cha miaka kumi au vyote viwili, yaani kifungo na faini.

  Adhabu inayopendekezwa katika kifungu kipya cha 17B ni kifungo cha maisha.
  Mheshimiwa Spika, Ni vizuri na ni busara kwa Bunge lako tukufu kuhoji sababu halisi za mapendekezo ya kuongeza adhabu za makosa haya. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inakubaliana na maelezo ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, Mheshimiwa William Vangimembe Lukuvi kwamba "matumizi na upatikanaji wa dawa za kulevya bado ni tatizo kubwa hapa nchini." Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inafahamu hatari kwa nchi yetu, na madhara kwa jamii yetu kutokana na matumizi ya madawa ya kulevya; na hivyo umuhimu wa kuendelea kupiga vita biashara na matumizi haramu na hatari ya madawa ya kulevya hapa nchini.

  Mheshimiwa Spika, Wakati wa uchambuzi wa Muswada huu, Kamati ya Sheria, Katiba na Utawala ya Bunge lako tukufu ilipata ushuhuda kutoka kwa Kamishna Christopher J. Shekiondo wa Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya nchini. Katika ushuhuda wake, Kamishna Shekiondo aliieleza Kamati kwamba ni muhimu kwa adhabu za makosa ya madawa ya kulevya zikaongezwa kama inavyopendekezwa kwa sababu tatizo la biashara hii haramu na matumizi ya dawa hizi imekuwa ikiongezeka hapa nchini.

  Kwa sababu hiyo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni haitakuwa inakosea kwa kuamini kwamba hii ndiyo sababu au rationale pekee ya mapendekezo ya kuongeza adhabu hizi kama inavyopendekezwa na Muswada huu.
  Mheshimiwa Spika, Sababu na rationale ya kuongeza adhabu kwa makosa ya madawa ya kulevya kama inavyopendekezwa haiendani na hali halisi ya tatizo la biashara na matumizi ya madawa ya kulevya nchini.

  Aidha, maelezo aliyoyatoa Kamishna Shekiondo kwenye Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala hayalingani na ushahidi uliopo katika taarifa mbalimbali rasmi zilizoandaliwa na Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya na kuwasilishwa kwenye Bunge lako tukufu kwa mujibu wa kifungu cha 6 cha Sheria ya Kuzuia Biashara Haramu ya Dawa za Kulevya. Kwa mfano, katika Taarifa ya Hali ya Dawa za Kulevya ya Mwaka 2010, Tume hiyo imeonyesha kwamba kiasi cha bangi kilichokamatwa mwaka 2010 ni tani 4.03 ikilinganishwa na tani 964.1 zilizokamatwa mwaka 2004. Vile vile, wastani wa kiasi cha bangi kilichokamatwa kila mwaka katika kipindi cha miaka mitano kufikia mwaka 2010 ulikuwa ni tani 80.4 ukilinganishwa na wastani wa tani 441.8 zilizokamatwa kwa mwaka kati ya 2001 na 2005.


  Mheshimiwa Spika, Taarifa za Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya zinaonyesha pia kupungua kwa biashara ya mandrax, morphine, bangi iliyosindikwa na bangi kavu katika kipindi cha miaka kumi kati ya mwaka 2000 na 2010. Ni kweli kwamba takwimu za Tume zinaonyesha kuongezeka kwa biashara ya madawa ya heroin na cocaine. Kwa mfano, kiasi cha heroin kilichokamatwa kimeongezeka kutoka kilo 5.3 mwaka 2000 hadi kilo 185.8 mwaka 2010. Vile vile, kiasi cha cocaine kilichokamatwa katika kipindi hicho kimeongezeka kutoka kilo 2.104 mwaka 2000 hadi kilo 62.966 mwaka 2010, ikiwa "... ni takriban mara mbili zaidi ya kiasi chote kilichowahi kukamatwa katika kipindi cha miaka kumi iliyotangulia." Aidha, idadi ya kesi zinazotokana na madawa ya heroin imeongezeka kutoka kesi 160 mwaka 2000 hadi kesi 317 mwaka 2009 na ile ya cocaine imeongezeka kutoka kesi 36 mwaka 2000 hadi kesi 336 mwaka 2009.

  Hata hivyo, Mheshimiwa Spika, Takwimu za Tume zinaonyesha kwamba idadi ya watuhumiwa wa makosa wa biashara ya heroin imepungua kutoka watuhumiwa 412 mwaka 2001 hadi watuhumiwa 15 mwaka 2010 na wale wa biashara ya cocaine wamepungua kutoka watuhumiwa 251 mwaka 2008 hadi watuhumiwa 8 mwaka 2010. Hii ni licha ya kuongezeka kwa kiwango cha madawa hayo kinachokamatwa.

  Mheshimiwa Spika, Kitu kimoja ambacho hakionyeshwi na Taarifa pamoja na takwimu zote za Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Biashara ya Dawa za Kulevya ni idadi ya watuhumiwa waliopatikana na hatia ya makosa haya mahakamani. Kamishna Shekiondo alipoulizwa juu ya jambo hili kwenye Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala alijibu kwamba ni mtu mmoja tu ambaye amepatikana na hatia ya makosa haya katika kipindi chote cha Taarifa za Tume! Kamishna Shekiondo alielezea sababu ya hali ya kustaajabisha kuwa ni rushwa iliyokithiri katika mahakama zetu ambapo alisema watuhumiwa wengi wamekuwa wakiachiliwa huru kwa sababu ya kutoa rushwa mahakamani.

  Mheshimiwa Spika, Kama kauli ya Kamishna Shekiondo kuhusiana na sababu za watuhumiwa wa biashara haramu ya dawa za kulevya kutopatikana na hatia mahakamani ni ya kuaminiwa, basi ni wazi kwamba tatizo la kuendelea kushamiri kwa biashara haramu ya dawa za kulevya nchini halitokani na udogo wa adhabu zilizowekwa na Sheria ya sasa kwa makosa hayo bali ni rushwa na uozo ulioko mahakamani na kwenye mamlaka za uandaaji na uendeshaji mashtaka ya makosa hayo.

  Na kwa maana hiyo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaamini kwamba dawa ya tatizo la rushwa na ufisadi katika taasisi hizo haiwezi kuwa kuongeza adhabu za makosa hayo bali kuzisafisha mahakama na taasisi za uandaaji na uendeshaji mashtaka ili kuondokana na rushwa na ufisadi huo!

  Kwa sababu hiyo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni haiwezi kuunga mkono mapendekezo ya marekebisho ya Sheria ya Kuzuia Biashara Haramu ya Dawa za Kulevya yaliyoko kwenye Muswada huu kwani hayalengi kuondoa kiini cha tatizo ambacho ni rushwa na ufisadi .
  MWISHO

  Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaridhika na Maoni na Ushauri wa Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala kuhusiana na mapendekezo ya marekebisho mengine ya Sheria yaliyoko kwenye Muswada huu na haioni haja ya kuyarudia maoni na ushauri huo. Napenda kuchukua fursa hii kuwashukuru wajumbe wote wa Kambi Rasmi ya Upinzani chini ya uongozi wa Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni Mheshimiwa Freeman A. Mbowe kwa ushauri na ushirikiano uliowezesha maandalizi ya hoja hii.

  Aidha, napenda kuchukua fursa hii kuwashukuru wajumbe wa Kamati ya Sheria, Katiba na Utawala, chini ya uongozi wa Mwenyekiti wake Mheshimiwa Pindi Hazara Chana, kwa michango yao mbali mbali wakati wa kujadili Muswada huu.
  Vile vile nichukue fursa hii kumshukuru Msaidizi wa Masuala ya Kibunge, Oliver Mwikila, kwa msaada na ushauri wa kitaalam uliofanikisha maandalizi ya hoja hii. Mwisho naomba nichukue fursa hii kuwashukuru viongozi, wanachama na wapenzi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na wananchi wote wa Tanzania ambao wameendelea kutuunga mkono na kututia nguvu katika kipindi hiki muhimu katika historia ya nchi yetu. Msimamo wetu ni ule ule: hakuna kulala mpaka kieleweke!

  Mheshimiwa Spika,
  ---------------------------------------------------------------

  Tundu Antiphas Mughwai Lissu

  MSEMAJI & WAZIRI KIVULI, SHERIA, KATIBA NA UTAWALAKAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI
   
 2. Mpaka Kieleweke

  Mpaka Kieleweke JF-Expert Member

  #2
  Feb 2, 2012
  Joined: Feb 27, 2007
  Messages: 4,137
  Likes Received: 67
  Trophy Points: 145
  Bunge limeipiga chini hoja ya serikali hivyo imeshindwa tena kwa mara ya pili siku ya leo.
   
 3. k

  kabuga Member

  #3
  Feb 2, 2012
  Joined: Nov 19, 2011
  Messages: 78
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  Safi sana Lisu we need a person like you
   
 4. Mr Rocky

  Mr Rocky JF-Expert Member

  #4
  Feb 2, 2012
  Joined: Oct 10, 2007
  Messages: 15,186
  Likes Received: 570
  Trophy Points: 280
  safi sana aise
   
 5. OSOKONI

  OSOKONI JF-Expert Member

  #5
  Feb 2, 2012
  Joined: Oct 20, 2011
  Messages: 10,800
  Likes Received: 3,884
  Trophy Points: 280
  summarize ndugu acha copy and paste
   
 6. N

  Nikupateje JF-Expert Member

  #6
  Feb 2, 2012
  Joined: Dec 22, 2009
  Messages: 1,314
  Likes Received: 106
  Trophy Points: 160
  Hakukuwa a jinsi ambavyo CCM wangepitisha hili wakati kupitisha Tundu Lissu kaonyesha kuwa ni kuvunja kanuni.
   
 7. Bitabo

  Bitabo JF-Expert Member

  #7
  Feb 2, 2012
  Joined: Sep 27, 2011
  Messages: 1,896
  Likes Received: 124
  Trophy Points: 160
  Wale waliosema Chadema wamekimbia kumuuliza PM maswali asubuhi nadhani wameona kazi ya Lissu jioni hii. Mshkaj anaongea kwa hisia mpaka noma, Ila Dr. Ndugulile amekuwa mzalendo sana kwa kutetea maslah ya nchi bila kuangalia uchama zaidi.
  It was a nice move
   
 8. N

  NDOFU JF-Expert Member

  #8
  Feb 2, 2012
  Joined: Feb 23, 2009
  Messages: 656
  Likes Received: 1
  Trophy Points: 35
  Kilichonishangaza ni Werema,jamaa ameishia kutishia kuwa hajafukuzwa ujaji na akashindwa kuitetea hoja yake! Kazi nzuri ya Ndugai,jamaa amekuwa bora kupita yule Bibi!
   
 9. F

  FJM JF-Expert Member

  #9
  Feb 2, 2012
  Joined: Apr 11, 2011
  Messages: 8,088
  Likes Received: 90
  Trophy Points: 145
  WanaJF tujadili kigodo huu usanii.

  Wabunge wa ccm waikubali hoja ya CHADEMA kuukataa huu muswada si kwa sababu kuwa ni mbovu au wanawajali bali kwa sababu wanatafuta huruma ya wanafunzi wa vyuo. Wabunge hawa wa ccm wanajua fika kuwa CHADEMA inakubalika kwenye vyuo vikuu na hivyo kama wangekataa hoja ya Lissu basi wangekuwa wamejimbia kaburi.

  Kama kweli hawa wabunge wa ccm wanajali kwa nini hawakuunga mkono hoja ya Mnyika ya kujadili mgomo wa madaktari? watu wanakufa lakini wao wameuchuna, sasa jioni hii wanajidai wanajali? tangu lini?
   
 10. Jakubumba

  Jakubumba JF-Expert Member

  #10
  Feb 2, 2012
  Joined: Mar 5, 2011
  Messages: 1,627
  Likes Received: 15
  Trophy Points: 135
  Ndugu yangu tatizo la wabunge wetu ni waoga sana! Hawasimami kama raia wa Tanzania kutetea ukweli utafikili wote wakimbizi! Yani wanawazia uchaguzi ujao kila siku badala ya kutatua kero zetu! Tusubili hii movie tuone itaishaje hapo 2015
   
 11. J

  J.K.Rayhope JF-Expert Member

  #11
  Feb 2, 2012
  Joined: Oct 26, 2011
  Messages: 316
  Likes Received: 1
  Trophy Points: 0
  Nimetamani Lissu avae kiatu cha Werema,chini ya Rais Dk.W.P.Slaa.Huyo Taata hamna kitu.
   
 12. apolycaripto

  apolycaripto JF-Expert Member

  #12
  Feb 2, 2012
  Joined: Feb 11, 2011
  Messages: 637
  Likes Received: 26
  Trophy Points: 45
  Sina mapenzi na CDM lakini kwa compilation hii ya Lissu ,namkubali kuwa ni mtu makini na mzalendo sana kwa nchi yake.Nimekuwa nikihudhuria vikao vingi vya watumishi wizarani hasa katika utungaji wa sheria ndogo za uendeshaji wa shughuli za wizara (sectoral regulations) ni aibu. Yaani ni madudu tu, hakuna kushughulisha kichwa ila ni kutekeleza tu na kulamba posho.

  Hivi kweli pamoja nakuwezeshwa kila kitu na posho lukuki, Wanasheria wa Wizara kupitia ofisi ya Mwanasheria Mkuu wameshindwa ku-brainstorm mapungufu yote haya ata kwa simple method ''cost benefit analysis'' wanakuja na miswada ya ovyo ovyo ki hivi.Hii narudia tena ni aibu kwa Taifa letu na ukosefu wa Uzalendo kabisa.

  Nchii hii asilimia 80 inauliwa na so-called wasomi na waajiriwa wa Serikali. Jamani huko no body cares ni business as usual.
   
 13. MtamaMchungu

  MtamaMchungu JF-Expert Member

  #13
  Feb 2, 2012
  Joined: Apr 10, 2011
  Messages: 3,696
  Likes Received: 507
  Trophy Points: 280
  "Ukitaka kumficha kitu mwafrika weka kwenye kitabu"
   
 14. Chakaza

  Chakaza JF-Expert Member

  #14
  Feb 2, 2012
  Joined: Mar 10, 2007
  Messages: 23,668
  Likes Received: 21,901
  Trophy Points: 280
  Wabunge wa CCM ni janga tuliLojitakia wenyewe
   
 15. B

  Bubona JF-Expert Member

  #15
  Feb 2, 2012
  Joined: Aug 31, 2011
  Messages: 449
  Likes Received: 8
  Trophy Points: 35
  Argued strongly!!! Bravo Lisu!!
   
 16. Gwalihenzi

  Gwalihenzi JF-Expert Member

  #16
  Feb 2, 2012
  Joined: Oct 21, 2011
  Messages: 5,117
  Likes Received: 51
  Trophy Points: 145
  Mh. Tundu Lisu, naamini kabisa kwamba sasa waliokuwa wanakubeza wanalazimika kuficha nyuso zao kwa viganja kama nyani wa hadithi ya Shabani Robert ya Adili na nduguze.
   
 17. Gwalihenzi

  Gwalihenzi JF-Expert Member

  #17
  Feb 2, 2012
  Joined: Oct 21, 2011
  Messages: 5,117
  Likes Received: 51
  Trophy Points: 145
  Ndugu yangu, wengi wao wanavyeti lakini hawana taaluma, kwa mazingira hayo usitegemee mchango wowote wa kisomi kutoka kwao.
   
 18. Jumakidogo

  Jumakidogo R I P

  #18
  Feb 2, 2012
  Joined: Jul 16, 2009
  Messages: 1,859
  Likes Received: 17
  Trophy Points: 0
  Kwa tuliokuwepo bungeni! Lissu aliwasilisha maoni ya kambi ya upinzani bungeni ambayo kwa sehemu kubwa ilikuwa inaukataa muswada wa marekebisho ya sheria mbalimbali na hakuunga mkono hoja. Hoja iliyoleta utata hadi kusababisha muswada kuondolewa ni kutoka kwa mbunge Faustin Ndugulile wa CCM Ndiye aliyeomba muswada huo kuondolewa. Ndipo ulipozuka utata huku upande wa serikali ukidai kiondolewe kipengele kinachohusu bodi ya mikopo tu. Hapo ndipo Tundu Lissu alipotoa ufafanuzi kuhusu hoja ya Ndugulile. Ki msingi aliyesababisha muswada kukwama ni Ndugulile, siyo Lissu kwani baada ya Lisu kumaliza hotuba yake. Mjadala uliendelea kama kawaida. Tuwekane sawa hapo.
   
 19. Donnie Charlie

  Donnie Charlie JF-Expert Member

  #19
  Feb 2, 2012
  Joined: Sep 16, 2009
  Messages: 6,580
  Likes Received: 847
  Trophy Points: 280
  kuna thread ambazo zinazungumzia hili kwa ufupi, wengine hatupo kwenye tv ndio tunapata wasaa wa kusoma hapa
   
 20. L

  LAT JF-Expert Member

  #20
  Feb 2, 2012
  Joined: Nov 20, 2010
  Messages: 4,523
  Likes Received: 86
  Trophy Points: 0
  kuna haja ya kuwa na kanuni ya utaratibu wa kuunga mkono au kutounga mkono hoja kama vile kupiga kura za siri za kuhesabu na siyo ujinga wa wabunge kusema ndiyoo, siyoo na kugonga meza kama vichaa
   
Loading...