HOJA NDANI YA HOJA: Rais Magufuli na bahati nasibu ya korona - ITALIPA?

Mzee Mwanakijiji

Platinum Member
Mar 10, 2006
33,476
39,995
covid-19_phixr.png

Nilipoandika makala yangu ya ILIYOPITA kuhusiana na ugonjwa utokanao na virusi vya korona (COVID-19) Tanzania ilikuwa haijtangaza kuwepo kwa mgonjwa yeyote nchini na kuwa makala ile ililenga katika kutoa shime ya kuwahi ugonjwa huo. Nchi zote zilizowahi kuutangaulia ugonjwa huo na kuchukua hatua kali mapema wameweza kudhibiti kusambaa kwake na hata kupunguza kasi ya maambukizi (rate of infections). Nchi zilizochelewa kuchukua hatua hizo au zimechukua hatua ambazo ni za taratibu sana zimejikuta leo hii zikihangaika kuokoa na kulinda maisha ya wananchi wao. Italia, Ufaransa na Uingereza kama ilivyo Marekani na Irani ni nchi ambazo zote leo zinajikuta zinakimbizana na muda. Muda hauko upande wao.

Kwa Tanzania hadi hivi sasa kuna kitu kinachoonekana si cha kawaida (an anomaly). Nchi zote ambazo zimepata wagonjwa wa kwanza tumeona idadi ya wanaoambukizwa ikiongezeka kwa kasi kubwa (exponentially). Karibu mwezi mmoja nyuma (Februari 15) Marekani ilikuwa na wagonjwa 15; leo hii Machi 26 Marekani ina wagonjwa karibu 70,000. Hii ni nyuma ya China tu na Italia. Kasi hiyo ya kusambaa kwa ugonjwa huu imeonekana karibu nchi zote ambazo ugonjwa huu umejikita. Kwa Afrika ni Afrika ya Kusini ambayo inaonekana ugonjwa huu kusambaa kwa kasi (sasa hivi wao wana kesi zaidi ya 900)

Je, namba zetu zinaweza kuaminika?
Nimesema hapo juu kuwa hali katika Tanzania inaonekana si ya kawaida (an anomaly). Kwamba, kweli nchi yetu inaweza kuwa na wagonjwa 13 tu wakati watu wanaendelea na shughuli zao kama kawaida? Je inawezekana serikali inaficha hali halisi na kuwa labda Rais Magufuli hataki watu waone kuwa Tanzania ina wagonjwa wengi? Ukifuatilia mitandao ya kijamii unaweza ukaamini hili. Lakini hiki “kinachoonekana” ni lazima tukipime (kwa tulio pembeni) kwa kulinganisha na nchi nyingine kama za kwetu. Hadi hivi sasa inaonekana ugonjwa wa COVID-19 haujalipuka kwa kasi kubwa katika nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara kama ilivyo kwa nchi nyingine.

Kufikia leo kwa baadhi ya nchi za Afrika hali ya wagonjwa (na namba za wagonjwa wapya kwenye mabano) ni kama ifuatavyo:

Nigeria (yenye watu milioni 190) - 51

Rwanda – 41

Kenya 31 (3)

Madagascar (4)

Zambia – 16 (4)

Uganda - 14

Ethiopia (yenye watu milioni 105) - 12

Congo DR (yenye watu milioni 81) – 4


Hivyo, tukiangalia takwimu hata za majirani zetu na nchi nyingine tunazoshabihiana nazo kwa mambo mengi utaona kuwa kasi ya maambukizi bado si kubwa na kama alivyosema Waziri Ummy Mwalimu leo ni kuwa wengi wa wagonjwa hawa ni wale waliopata COVID-19 wakitokea nje. Kwa hiyo, hatuna budi kukubaliana na kile tunachokiona; ugonjwa huu ni tishio lakini kwa nchi hizi za kwetu haujaweza kusambaa kwa haraka katika jamii (community spread). Hofu ya ugonjwa huu kusambaa kwa haraka ndio ulikuwa msingi wa hoja yangu.

Hatua Zilizochukuliwa Zinatosha?
Hadi hivi sasa serikali imechukua hatua mbalimbali za kuhakikisha kuwa haya maambukizi ya ndani kwa ndani kwenye jamii hayatokei. Kufungwa kwa shule, vyuo na kutoa elimu ya usafi na kupunguza mikusanyiko isiyo ya lazima ni njia sahihi. Katika mazingira ya kawaida tulitarajia baada ya Isabela kugundulika kule Arusha tungeona mlipuko Arusha lakini hilo halijatokea. Katika mazingira tunayoyaona kwenye nchi za wenzetu mgonjwa wa kwanza anapopatikana tu basi kuna uwezekano wa kuibuka kwa wagonjwa wengi zaidi.

Na namna pekee ya kuwapata wagonjwa hao ni kuchukua vipimo kwa watu wengi kwa kadiri inavyowezekana. Hili nalo Waziri Mwalimu amelielezea leo vizuri. Kwamba serikali inafanya vipimo na kuongeza uwezo wa kupima kwa haraka. Hii yote inasaidia kuweza kujua ni sehemu gani ya watu katika nchi wanaweza kuwa wameupata ugonjwa huu.

Bahati Nasibu ya Magufuli
Ni kutokana na hili Rais Magufuli – ambaye ni mwanasayansi ameona kuwa kwa sasa nchi nzima si lazima ifungwe kama walivyofanya nchi nyingine. Amewataka Watanzania kuzingatia kanuni za usafi na kupunguza migusano isiyo ya lazima lakini wakati huo huo kuendelea na shughuli zao. Hoja hii si kwa Magufuli peke yake; tumeona hata Marekani kuna mjadala mkubwa wa kutaka watu waanze kurudi makazini ifikapo Pasaka kwani uchumi wao hauwezi kwenda bila watu kurudi makazini. Hili nalo tumelisikia kwa Rais Bosanaro wa Brazili na baadhi ya wataalamu ambao wanataka kuona jamii inatengeneza kinga ya jamii (herd immunity) ambayo inatokea endapo watu wengi wanapata maambukizi na kupona na hivyo kupunguza mahali virusi hivyo vinaweza kuambukiza zaidi.

Endapo kasi hii ya maambukizi Tanzania itaendelea kuwa ndogo namna hii mambo mawili yanaweza kutokea. Kwanza, tunaweza kujikuta hatuna wagonjwa wapya ndani ya wiki chache zijazo kwa sababu tumeweza kuzuia maambukizi ya ndani kwa ndani kwenye jamii na pili tunaweza kuonesha kuwa hofu ya kuwa Afrika itakuwa ni kiini cha mlipuko haina msingi kwani nchi zetu katika umaskini wao wote wameweza kudhibiti ugonjwa huu kwa haraka bila kulazimika kufunga nchi. Hii itaokoa uchumi wetu na watu wataendelea na maisha yao kama kawaida na kutumia fursa mbalimbali ambazo zitakuwa zimejitokeza kiuchumi.

Bahati Nasibu Ikilipa

Huku kutakuwa ni kulipa kwa bahati nasibu ya korona ambacho Magufuli ameicheza. Na ikitokea hivyo, Rais Magufuli atakuwa ameonesha namna nyingine ya kukabiliana na tishio hili kinyume na viongozi wenzake wa Afrika kama Uhuru Kenyatta, Cyril Ramaphosa na Paul Kagame. Mabezo yote ambayo baadhi ya watu wameyarusha kwa Rais Magufuli kwenye mitandao yatawarudia kwani Watanzania kwa fahari wataanza kuyarudisha mabezo hayo. Magufuli atajionesha bado ni kiongozi wa aina yake katika Afrika; umpende au usimpende. Kwamba, siyo kiongozi wa kufuata mkumbo au upepo.

Na inawezekana tukashuhudia kuwa kudhibitiwa kwa ugonjwa huu Tanzania kunaweza kutoa fursa mbalimbali za kiuchumi kwa viwanda vyetu na wajasiriamali mbalimbali. Baadhi ya nafasi zinazoweza au kupaswa kutumika mara ugonjwa huu ukidhibitiwa:

  • Utengenezaji wa vitakasa mikono (hand sanitizers)
  • Utengenezaji wa vifaa vya mtu kujikinga (PPEs) kama magauni, glovu, maski na vilemba. Viwanda vyetu vya nguo vinaweza kuchangamkia fursa hii
  • Utengenezaji wa vitanda na vifaa mbalimbali vya kitabibu (Kama dawa, maji ya wagonjwa n.k) ambavyo vinaweza kutoa nafasi kwa viwanda vyetu.
  • Kutoa mchango katika utafiti wa chanjo ya ugonjwa huu kwa wataalamu wetu (hatuwezi kuwa watu tunaosubiri wengine tu watuletee chanjo!)
Bahati Nasibu Isipolipa

Hata hivyo, bahati nasibu hii inaweza isilipe. Hili litatokea endapo vitu viwili vitatokea. Kwanza, endapo idadi ya wagonjwa wapya itaanza kuongezeka kwa kasi kama ilivyotokea nchi nyingine na kusababisha mfumo wetu wa tiba (healthcare system) kushindwa kuhimili na kubomoka (collapse). Pili, endapo itagundulika kuwa kwa makusudi serikali na taasisi zake wamekuwa hawaripoti kwa usahihi idadi ya wagonjwa na matokeo yake na hivyo kuwaacha watu wenye maambuziki kuendelea kuzurura mitaani na kusababisha hilo jambo la kwanza. Kwa vile hadi hivi sasa idadi yetu ya wagonjwa haina tofauti sana na baadhi ya nchi kama za wetu; suala la kuficha namba (under reporting) ni vigumu sana kuaminika isipokuwa kama kweli nchi nyingine zote kama za kwetu zingekuwa zinaripoti namba kubwa zaidi kulinganisha na za kwetu. Kwa nchi zetu za Afrika utaona kuwa tuoka katika wastani ukiondoa Afrika ya Kusini ambayo iko pembezoni kweli kweli (outlier).

Lakini endapo jambo la kwanza likitokea na Tanzania ikajikuta kwenye mlipuko mkubwa wa korona baadhi ya mambo ambayo yanaweza kutokea ni haya:

  • Magufuli atabebeshwa lawama binafsi za kusababisha hilo. Sidhani kama ataeleweka kama atakuja kuwalaumu Watanzania kuwa hawakumsikiliza.
  • Tanzania na Watanzania wote wanaweza kujikuta wanapigwa marufuku kwenda nchi nyingine hadi hali itakapotengemaa. Endapo mlipuko wa korona ukatokea wakati nchi nyingine zimedhibiti basi viongozi wa Tanzania watanyoshewa vidole na dunia nzima kwani wenzao walipokuwa wananyolewa wao walikuwa wanaweka kalikiti!
  • Mfumo wa afya wa Tanzania unaweza kujikuta ukiporomoka kuliko tunavyoweza kudhania. Tumeona jinsi nchi za daraja la kwanza (Italia, Ufaransa, Marekani na China) zikipata shida kukabiliana na ugonjwa huu. Imefikia mahali serikali za nchi hizo zimeomba na zinategemea misaada kutoka makampuni binafsi kupata dawa na vitendea kazi mbalimbali. Kuna hospitali Marekani manesi wake walijikuta wakitumia mifuko ya plastiki ya takataka kama mavazi ya kujikina! Marekani hiyo! Tumeona Hispania, wazee wakiachwa wajifie wenyewe kwani manesi na wahudumu wengine wamekimbia! Tumeona Italia madaktari na manesi wakifa kutokana na ugonjwa huu. Kama hili linatokea kwa mti mbichi, itakuwaje kwa mti mkavu! Kama limetokea kwa chuma cha pua, itakuwaje kwa chuma chakavu!
  • Kama hali itakuwa mbaya zaidi ya nchi hizo basi mtafaruku wa kijamii (social unrest) unaoweza kutokea utatisha. Huko Marekani sasa hivi watu pamoja na utulivu unaoonekana kwa nje lakini watu wako katika hali ya msongo mkubwa wa mawazo. Tayari takwimu zinaonesha kuwa Wamarekani wananunua bunduki na silaha ndogondogo kwa kiasi kikubwa ili kujilinda endapo utatokea mtafaruku. Ununuzi wa bunduki umeongezeka kwa zaidi ya asilimia 300 nchini Marekani kutokana na hofu ya kuvunjika kwa utawala wa sheria sababu ya korona.
Yapo na mengine ambayo yanaweza kusemwa. Lakini vyovyote vile ilivyo, swali kubwa ni je hii ni bahati nasibu holela au ni bahati nasibu inayotokana na fikra za kisayansi. Kwamba, Rais Magufuli badala ya kuangalia mambo kijamii anaongozwa na ujuzi wake wa kisayansi na hivyo anapima mambo kwa uzito wa ushahidi ulio mbele yake (empirical evidence). Kwamba, Rais Magufuli ameona kuwa uwezekano (chance) ya Tanzania kupata mlipuko mkubwa endapo tunaweza kudhibiti maambukizi yaliyopo hadi hivi sasa ni mdogo sana. Na hii ndio sababu amewataka Watanzania kutotishika na kuendelea na shughuli zao. Siyo kwamba, anapuuzia au hajali kinachotokea duniani bali hataki watu wake wajifungie ndani, waache kazi, na kuombea “siku ya mwisho ifike”. Magufuli anasema “tusitishane”. Kwamba, tunaweza kudhibiti hali iliyopo bila kulazimika kuifunga nchi nzima. Kiukweli, hayuko peke yake duniani.

Kama nilivyosema hapo mwanzoni, tayari nchi kama Marekani imeanza kufikiria namna gani ya kufungua nchi ili watu waanze kurudi makazini. Hata ndani ya Marekani yenyewe baadhi ya majimbo bado hayajatangaza kufunga shughuli zote kwa sababu hawajapata maambukizi mengi (kumbuka nusu ya kesi zote za korona Marekani zinatokea Jimbo la New York). Wenzetu Marekani kutokana na utajiri wao licha ya kuifunga nchi wameweza kutenga dola trilioni 2.2 kwa ajili ya kulinda ajira, wafanyakazi na kusaidia sekta mbalimbali ili zisilipe gharama kubwa kutokana na ugonjwa huu. Kiasi hicho ni sawa na bajeti ya sasa ya Tanzania kwa karibu miaka 75!

Ni wazi basi kila mmoja wetu afanye anachotakiwa kufanya kujikinga na ugonjwa huu. Serikali iendelee kuwa muwazi na kwa namna yeyote isiwafiche au kuonekana inawaficha Watanzania hali ilivyo. Wahenga waliposema “mficha maradhi kifo kitamfichua” walisema ukweli. Na kwa vile tumeona kuwa hadi hivi sasa hakuna sababu ya kudhania serikali haisemi ukweli ni muhimu basi Waziri Mwalimu na Waziri Mkuu kutoa taarifa za hali ilivyo kwa haraka na kwa uwazi. Katika ulimwengu wa mitandao ya kijamii, habari za uongo zinasambaa haraka na hatuwezi kuwafunga watu wote wenye kuandika au kuanzisha mijadala hiyo. La maana ni kuliwahi treni la uongo kabla yalijafika kituo cha kwanza.

Tukifanya hivyo, na kweli tukadhibiti maambukizi ya ugonjwa huu na kuhakikisha uchumi wetu hauyumbi kwa kiasi kikubwa basi bahati hii nasibu ya Magufuli; italipa na italipa na kulipa.

Niandikie: mwanakijiji@jamiiforums.com

Unaweza kufuatilia takwimu za kasi ya uambukizaji wa virusi vya korona nchi mbalimbali duniani kwa KUBONYEZA HAPA
 
Kiufupi sisi wa hali ya chini tuko pamoja na rais Magufuli.

Kwa hio watu wachache wakimlaumu Magu kwa sababu hajafungia watu ndani basi isionekane kwamba ni watu wote.

Wengi wetu tusipotoka hatuli.
Iweje tuache kuwa upande nmoja na Rais magufuli?
 
Nyie watu mna underrate Sana Rais wetu, kwa mfano, unakuta mtu anamlalamikia Rais et kwa nini hajafunga mipaka wakati hilo suala ni la kiusalama si kila mtu anapaswa kujua, mipaka ilishafungwa kitambo kabla hata ya majirani wengine kufunga
 
Umeandika makala yako ukionesha hujui matukio yanavyoendelea kutokea Tanzania kuhusu Corona; unazungumzia issue ya bahati nasibu kulipa au kutokulipa, hapo hapo unaonesha wasiwasi wako kuhusu taarifa zinazotolewa kuhusu Corona na maambukizi mapya kama ni za kweli. Kwa hali hii utatumia kigezo gani kujua kama bahati nasibu ililipa au kutokulipa kama taarifa tunazopewa haziaminiki?!

Ikumbukwe, taarifa ya mtoto wa Mbowe kupata maambukizi ya Corona ilikuja wakati tukiaminishwa hakuna maambukizi mapya, serikali imedhibiti, mpaka yule mropokaji wa taifa alipokuja kuropoka kuhusu mtoto wa Mbowe akisahau wao kama serikali walishatuaminisha hakuna tena maambukizi mapya, hivyo kuthibitisha udhaifu wao kwenye kukabiliana na hili janga, naamini mpaka hapa ungekuwa umeshapata jibu la bahati nasibu yako, kama imelipa au kutokulipa.

Hili ndilo linanifanya nitilie shaka ufahamu wako kuhusu hili suala la Corona Tanzania, na usijekuwa unajaribu kuficha kitu ambacho tayari kipo wazi.

Sent using Jamii Forums mobile app
 
Kiufupi sisi wa hali ya chini tuko pamoja na rais Magufuli.

Kwa hio watu wachache wakimlaumu Magu kwa sababu hajafungia watu ndani basi isionekane kwamba ni watu wote.

Wengi wetu tusipotoka hatuli.
Iweje tuache kuwa upande nmoja na Rais magufuli?
Raisi yupo sahihi, nachojiuliza tu ni kuwa baada ya hili janga kuisha, mataifa mengine hayawezi kututenga au kutulockdown kwa kisingizio kuwa hatukuchukua hatua zinazotakiwa kutokomeza huu ugonjwa? Hivyo kuwa na wasiwasi kuwa ndani ya jamii yetu unaweza kuwepo?
 
Hivi maelekezo ya kutosalimiana kwa mikono, kunawa mikono kwa kutumia maji yenye dawa, kutumia vitakasa mikono, kutokusanyika mikusanyiko mikubwa imetolewa na magufuli au ni wataalam wa afya ndio waliotoa kisha magufuli akasisitiza?
 
I'm too young to understand. Kwa nini mheshimiwa afanye Bahati nasibu na uhai wa raia wake wapendwa? Kitu kinachofanywa na Rais wetu mpendwa ni mikakati ya kuua ndege wawili kwa jiwe moja na inabidi tusuport na kufuata kile wizara ya afya inachoelekeza.. Na soon tu tutaanza kampeni kwa ajili ya uchaguzi mwaka 2020.
 
Nilitegemea kwenye bandiko lako ungeandika sababu kubwa zilizosababisha Rais asizuie watu kutoka badala yake umeamua kuzunguka mbuyu. Rais hajazuia watu kutoka Kwan sababu kuu mbili: Mosi , watanzania sio watu wa kuweka akiba hivyo basi, kuwazuia kutoka ni sawa na kusema kufeni kwa njaa!

Pili , serikali yetu haina hela ya kuweza ku-subsdize kwa kuwasaidia watu chakula, madawa, kulinda ajira, hduma za kijamii n.k hivyo basi kuficha hali hii Rais ameamua kujitoa mhanga kwa sababu hakuna jinsi
 
Kiufupi sisi wa hali ya chini tuko pamoja na rais Magufuli.

Kwa hio watu wachache wakimlaumu Magu kwa sababu hajafungia watu ndani basi isionekane kwamba ni watu wote.

Wengi wetu tusipotoka hatuli.
Iweje tuache kuwa upande nmoja na Rais magufuli?
Mkuu Mimi nakuelewa sana,sisi wa hali ya chini tunaugulia nyumbani kimya kimya na tunajifia kimya kimya sana sana tutasingizia kalogwa .na rais wetu anatujua vizuri,yeye amejichimbia ikulu sasa wewe kuzurule huko ukaupate na kwa kuwa yeye hajakutuma ukazurule wakati unacoronwa sisi tutakuwa tunapiga kazi ya kuchonga majeneza ili ukishacoronwa huko uje tukupige hela
 
Mkuu Mimi nakuelewa sana,sisi wa hali ya chini tunaugulia nyumbani kimya kimya na tunajifia kimya kimya sana sana tutasingizia kalogwa .na rais wetu anatujua vizuri,yeye amejichimbia ikulu sasa wewe kuzurule huko ukaupate na kwa kuwa yeye hajakutuma ukazurule wakati unacoronwa sisi tutakuwa tunapiga kazi ya kuchonga majeneza ili ukishacoronwa huko uje tukupige hela
Sasa nikifungiwa ndani siku 21 nitakufa tu.
Si bora kufa kwa corona kuliko kufa kwa njaa?
 
Nilitegemea kwenye bandiko lako ungeandika sababu kubwa zilizosababisha Rais asizuie watu kutoka badala yake umeamua kuzunguka mbuyu. Rais hajazuia watu kutoka Kwan sababu kuu mbili: Mosi , watanzania sio watu wa kuweka akiba hivyo basi, kuwazuia kutoka ni sawa na kusema kufeni kwa njaa!

Pili , serikali yetu haina hela ya kuweza ku-subsdize kwa kuwasaidia watu chakula, madawa, kulinda ajira, hduma za kijamii n.k hivyo basi kuficha hali hii Rais ameamua kujitoa mhanga kwa sababu hakuna jinsi
Wewe mwendawazimu acha kuidharirisha serikali yetu.serikali hii ya awamu ya tano pesa ipo.Wewe mwendawazimu na rais Magufuli nani anajua pesa ipo au haipo?nakuonya usirudie tena ujinga huu
 
Back
Top Bottom