Hofu ya Kenya katika akili za Tanzania

wahid1

JF-Expert Member
Jun 26, 2014
225
279
HOFU YA KENYA KATIKA AKILI ZA TANZANIA.

Na Abbas Mwalimu.

Jumapili, 2 Agosti, 2020.

Alhamisi tarehe 30 Julai, 2020 Serikari ya Kenya kupitia Wizara ya Uchukuzi ilitangaza kanuni mpya kwa wasafiri kutoka mataifa ya kigeni.

Katika hatua hiyo, mataifa 11 yalitangazwa kuruhusiwa kuingia nchini humo kuanzia Agosti Mosi, 2020 baada mlipuko wa Covid-19 uliosababisha safari nyingi za ndege duniani kusitishwa.

Waziri wa Uchukuzi wa Kenya, James Machira alizitaja nchi hizo kuwa ni Uganda, Rwanda, China, Korea Kusini, Japan, Canada, Ethiopia, Uswisi, Namibia, Morocco na Zimbabwe.

Idadi hiyo ilitangazwa kuongezwa mnamo tarehe 31 Julai, 2020 na kufikia mataifa 19 baada ya kuongezeka nchi za Marekani (Isipokuwa kwa majimbo ya California, Florida na Texas), Uingereza, Ufaransa, Ujerumani, Uholanzi, Qatar, Umoja wa Falme za Kiarabu na Italia.

Kufuatia kanuni hizo zilizotolewa na Wizara ya Uchukuzi ya Kenya, kwa upande wake Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) imefuta kibali kilichokuwa kikiruhusu Shirika la Ndege la Kenya (KQ) kutua nchini.

Kwa mujibu wa barua iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania bwana Hamza Johari Jumamosi tarehe 31 Julai, 2020 kwenda kwa Meneja wa Operesheni za Uhandisi Ukuraji wa Shirika la Ndege la Kenya imeeleza kuwa Tanzania imeiarifu Kenya Airways juu ya hatua hiyo ya kufuta safari zote za KQ kwenda Dar es Salaam, Kilimanjaro na Zanzibar kuanzia tarehe Mosi Agosti, 2020 mpaka pale watakapojulishwa tena kama sehemu ya utaratibu wa kurejesha lililofanywa na mwingine (on a reciprocal basis).

Huu ni muendelezo wa vitendo vya nchi ya Kenya dhidi ya Tanzania mara kwa mara hali inayoonesha kuna jambo huenda limejificha nyuma ya tabia hizi za Kenya.

Hatua ya uamuzi huu wa sasa wa kuifutia KQ kibali ni wazi kuwa utaliyumbisha shirika hilo. Kwa nini?

Kwa sababu mwezi Machi, 2015 Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania ilipunguza safari za shirika hilo Tanzania kutoka 42 kwa wiki hadi 14 na kumlazimu Rais Uhuru Kenyatta kuomba mzungumzo na Rais wa wakati huo Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete ili kulinusuru shirika hilo.

Ikumbukwe kuwa mwezi Mei, 2020 Rais Uhuru Kenyatta alitangaza kufunga mipaka ya nchi hiyo dhidi ya nchi za Tanzania na Somalia kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kujikinga dhidi ya kusambaa kwa virusi vya Corona.

Hatua hiyo ilipelekea wakuu wa mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Tanga kuzuia malori yanayoingia kutoka nchini Kenya na hatimaye Kenya kupitia Balozi wake nchini, Mheshimiwa Dan Kazungu kuomba muafaka.

Baadae Rais Uhuru Kenyatta alimpigia simu Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli na kumuomba pande hizo mbili zikae katika meza ya majadiliano baada ya kuona raia wake wanaathirika kwa kukosa huduma za msingi hasa vyakula na mbogamboga kutoka Tanzania.

Historia ya vitendo vya Kenya dhidi ya Tanzania ilianza miaka mingi sana, tukumbuke hata mwaka 2010 Kenya iliwahi kuikatalia Tanzania kuuza pembe za ndovu zenye thamani ya dola za Marekani milioni 20 katika mkutano wa Nchi wanachama wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Hifadhi ya Mimea na Wanyama walio katika hatari ya kutoweka duniani uliofanyika Doha, Qatar licha ya Afrika Kusini na Zambia kuiunga mkono Tanzania.

Katika miaka ya hivi karibuni pia mwezi Aprili mwaka 2017 Kenya ilipiga marufuku uingizwaji wa ngano na gesi ya kupikia kutoka Tanzania na hivyo Tanzania nayo kuchukua hatua ya kuzuia maziwa ya ng'ombe na sigara kuingia nchini kutoka Kenya.

Baada ya kuona hali inaenda vibaya Rais wa Kenya Mheshimiwa Uhuru Kenyatta alifanya mazungumzo na Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli na hatimaye makubaliano kufikiwa tarehe 24 Julai, 2017.

JE NI NINI KINAPELEKEA KENYA KUWA NA TABIA HIZI DHIDI YA TANZANIA?

Kabla sijaeleza sababu za Kenya kufanya kile inachofanya mara kwa mara na namna Tanzania inavyojibu mapigo, kuna haja ya kufahamu kanuni zinazongoza Uhusiano wa Kimataifa.

Kwa mujibu wa Goldstein (2008) Uhusiano wa Kimataifa unaongozwa kwa kanuni kubwa tatu ambazo ni:
(i) Dominance
(ii) Reciprocity
(iii) Identity.

Hapa nitazungumzia kanuni mbili za kwanza. Kenya inaamini kuwa yenyewe ina nguvu katika Afrika Mashariki hivyo inajaribu kuonesha namna inavyoweza kutawala (Dominance) nchi nyingine za Afrika Mashariki. Nitaeleza baadae namna Kenya inavyojiona.

Tanzania kwa upande wake inatumia zaidi kanuni ya pili pale inapofanyiwa vitendo visivyo stahiki na nchi ya Kenya yaani kurejesha kile ilichofanyiwa (reciprocity). Hii kwa namna fulani inalenga kuionesha Kenya kuwa si dola lenye nguvu kama wanavyojiita kwani kila mara Tanzania inapochukua hatua hii Kenya huomba kukaa kwenye meza ya makubaliano kuondoa tofauti. Lipi ni dola lenye nguvu?

Kanuni hizi mbili zinauelezea uhusiano wa kimataifa kama mfumo wa makabiliano au ushindani (Confrontational or Competitive) zaidi.

Rochester (2010: 2018) katika kitabu chake "Fundamental Principles of International Relations" alijaribu kuondoa dhana hii ya makabiliano au ushindani kwa kujenga uwiano baina ya maslahi kinzani na yale ya pamoja kwa kutazama hali ya kutegemeana kwa nchi (Interdependence).

Baada ya kufahamu hayo sasa ni vema tukajifunza sababu za Kenya kufanya vitendo hivi mara kwa mara.

Kuna mambo matatu ambayo yanasababisha Kenya kufanya hivi, mambo haya ni:

(i) Survival of the State (Kuishi kwa Dola)
(ii)Increase in interdependency (Kuongezeka kwa kutegemeana)
(iii)Hegemony (Ukuu wa Dola).

SURVIVAL OF THE STATE (Kuishi kwa Dola).

Mambo haya yote matatu yanatazamwa katika maslahi ya taifa likiwemo hili la survival. Je maslahi ya taifa ni nini?

Hans Morgenthau (1948; 1950; 1952) alitafsiri maslahi ya taifa kwa kusema:

"The meaning of national interest is survival...power."

Brookings Institution wao walitafsiri maslahi ya taifa kwa kueleza ifuatavyo:

"What a nation feels to be necessary to its security and well being…National interest reflects the general and continuing ends for which a nation acts."

Kwa tafsiri yangu, "Kile ambacho taifa inahisi kuwa ni muhimu kwa usalama na kuwa njema kwake...maslahi ya taifa yanaakisi malengo ya jumla na endelevu yanayoendewa na taifa."

Malengo haya huwa ya kiuchumi, kiutamaduni na kisiasa. Hivyo hili la vitendo vya Kenya moja kwa moja linajikita katika malengo ya kiuchumi.

Ni wazi kuwa Kenya ina hofu kubwa ya kumalizika kwa nafasi yao ya kiuchumi dhidi ya Tanzania katika nchi za Afrika Mashariki hasa baada ya kuona uwekezaji mkubwa unaofanywa katika nchi ya Tanzania.

Tufahamu kinachofanyika nchini Tanzania kinaenda kuipa Tanzania nafasi kubwa ya kuvutia wawekezaji, hii ndiyo sababu Tanzania imezipiku nchi nyingi za EAC na SADC katika uuzaji wa bidhaa nje.

Ukitazama changamoto zote ambazo zimeainishwa na Benki ya Dunia katika "Urahisi wa Kufanya Biashara" yaani 'Easy of Doing Business' kwa kiasi kikubwa vinafanyiwa kazi, kwa mfano ujenzi wa miundombinu wezeshi ya kiuchumi na kibiashara kama vile ujenzi wa barabara, madaraja, ununuzi wa ndege, ununuzi na ujenzi wa meli, upanuzi wa bandari za Dar es Salaam, Tanga na Mtwara, Kigoma na Katavi na kuanzishwa kwa Blue Print ambayo inalenga kuondo changamoto zote za uwekezaji na biashara kunaipa nafasi kubwa Tanzania dhidi ya Kenya.

Ujenzi wa bwawa la kufua umeme la Mwalimu Nyerere katika mto Rufiji lenye kuzalisha megawatts 2115 pindi likikamilika kunatoa tafsiri ya moja kwa moja ya kushuka kwa bei ya umeme viwandani hali itakayochochea wawekezaji wengi kutokana na viwanda kupunguza gharama ya uzalishaji hivyo kuwa na uwezo wa kushindana katika soko la jumuiya za kikanda na duniani kwa ujumla.

Tunadhani Kenya watafurahia haya?

Tukumbuke Kenya wamejenga reli ya kisasa (SGR) lakini treni zake zinatumia dizeli wakati Tanzania kwa upande wake treni yake inatumia umeme na ina kasi zaidi ya ile ya Kenya, hili tunadhani haliwaumi? Tukumbuke treni hii inatarajiwa kwenda hadi Rwanda hapo baadae. Tunadhani Kenya watafurahia?

Ni lazima waumie kwa sababu Kenya inategemea umeme kutoka Uganda kwa ajili ya uchumi wake wakati Tanzania ina uwezo wa kuuza umeme wake nchi jirani. Hili ni dogo?

Sote tunakumbuka namna Kenya ilivyopigwa mweleka katika mchakato wa bomba la mafuta ambalo Tanzania ilifanikiwa kuingia mkataba na Uganda kusafirisha mafuta kutoka Hoima mpaka Chongoleani, Tanga. Hili linawauma Kenya mpaka kesho.

Mbali na hayo Tanzania inaendelea na mchakato wa kulifungua eneo la Magharibi hasa bandari ya Kigoma katika Ziwa Tanganyika na Katavi ambazo moja kwa moja zitapanua wigo wa biashara baina ya Tanzania Burundi na DRC. Bado Kenya watakuwa na amani juu ya survival yao?

Kwa ujumla ujenzi huu wa miundombinu ya kiuchumi unatishia survival ya uchumi wa Kenya ndiyo maana Kenya wanajaribu kutumia kila hila kuivuruga Tanzania ama kwa haya inayofanya au kupitia washirika wake, kwa mfano, tumekuwa tukiona mara kwa mara ubalozi wa Marekani nchini Tanzania ukiingia matatani kwa kutoa taarifa ambazo haina uthibitisho wake kama vile ulivyowahi kutoa taarifa ya kile walichoeleza kuwa ni tishio la ugaidi Masaki na pia kuitaka Tanzania itoe taarifa za Covid-19 mpaka kupeleka aliyekuwa Kaimu Balozi Imni Patterson kuitwa mara kwa mara Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kujieleza. Hivi Tanzania ina tishio la kushambuliwa na magaidi kukiko Kenya?

Tunajua kwa nini wanafanya hivi? Lengo la propaganda hii ni kuonesha kuwa Tanzania si mahala salama kwa uwekezaji hasa tukizingatia nchi ambayo Marekani imejielekeza kuwekeza yaani Kenya inapata hofu kubwa kutokana na uwekezaji unaofanyika Tanzania. Hii ndiyo sababu hasa ya Kenya kuingia mkataba wa kibiashara na Marekani ambao utaipa nafasi Marekani kuuza bidhaa zake katika soko la EAC, lengo hapa ni kuidhoofisha Tanzania kwa Marekani kuifanya Afrika Mashariki eneo la kuuza bidhaa kwa bei ya chee (Dumping). Hatujilizi kwa nini Kenya iliamua kuwalipa fidia raia wake ili Marekani ijenge base ya kijeshi pamoja na kuwapa eneo la bahari kwa ajili hiyo? Hatujiulizi?

Hatushangai Kenya ilifanya lockdown ikiwa na wagonjwa 7 lakini inakuja kuondoa lockdown ikiwa na wagonjwa elfu 7 na hapo hapo Balozi wa Marekani nchini Kenya anajigeuza bosi wa bodi ya utalii ya Kenya na kusema kuwa Kenya ni mahala salama kutalii na kusisitiza "...There is no better place to travel other than Kenya..." Kweli hatushangai?

Kama Mkataba wa Vienna wa mwaka 1961 unaohusu Mahusiano ya Kidiplomasia unaeleza kuwa Mabalozi huwawakilisha wale waliowateua ndani ya nchi zilizowapokea (soma ibara ya 3) je Balozi Kyle McCarter aliteuliwa na Rais wa Kenya?

KUONGEZEKA KWA KUTEGEMEANA (INCREASE IN INTERDEPENDENCE)

Tanzania kutangazwa kuwa nchi ya uchumi wa kipato cha kati na Benki ya Dunia Julai Mosi, 2020 kunaongeza kiwango cha kutegemeana (interdependency) kati yake na Kenya na hali inayozidisha changamoto kubwa kwa Kenya.

Haya yalibainishwa na Hanggi na wenzake (2006:27) walipoeleza:

"Confrontation or cooperation in interregional relations depends on the degree of economic interdependence and the degree of institutionalization of interregional cooperation."

Kwa bahati nzuri kwa Tanzania, ni kwamba Kenya inaitegemea Tanzania katika vitu ambavyo kama Kenya wasipovipata uchumi wao na maisha ya kawaida ya Wakenya yanaathirika kwa kiasi kikubwa.

Tanzania ni soko kubwa la bidhaa za Kenya na Tanzania ni msambaji mkubwa wa mahitaji muhimu kama chakula kwa Kenya. Haya yalibainishwa na Dkt. Duncan Onjwang alipofanya mahojiano na kituo cha luninga cha KTN katika mada iliyopewa jina, "Genesis of the tiff between Kenya and Tanzania." Wakenya wengi walichukia alichosema Dkt. Onjwang kwamba katika msuguano baina ya nchi hizi mbili, "...Kenya will suffer more..."

Ndiyo maana Hanggi na wenzake (2006:27) walisisitiza:

"The degree of interdependence can have some impact on the way in which trade disputes are resolved..." Sijui kama Kenya wanaliona hili, hasa pale wanapoanza na Tanzania kumalizia na hatimaye kujikuta wanaomba meza ya majadiliano na Tanzania.

HEGEMONY (UKIRANJA DHIDI YA MATAIFA MENGINE).

Kuna dhana ambayo imeenea vichwani mwa wakenya wengi na hasa wasomi, wao wanaamini kuwa Kenya ni Dola Kiranja au Nchi Kiongozi (Hegemonic State) katika Afrika Mashariki.

Ukimsikiliza Dkt. Duncan Onjwang katika mahojiano na KTN katika "The Genesis of tiff betwen Kenya and Tanzania utagundua hili la kujiona ni dola kiranja kama nilivyogusia awali, Dkt. Onjwang anasema, "We are the leaders in this region..." Kwamba Kenya ndiyo dola kiranja katika ukanda huu. Si ajabu kumuona Mkenya akiandika mitandaoni, "We are the super power of East Africa." Huu ndiyo mtazamo na mawazo yao.

Kuthibitisha hili, Mkenya Lee Mwiti Mugambi mwaka 2015 alifanya utafiti wake uliojikita katika kuitazama Kenya kama Dola Kiranja (Hegemony) ndani ya Afrika Mashariki. Utafiti wake ulikwenda kwa jina la "Hegemony and Regional Stability in Africa: A critical analysis of Kenya, Nigeria and South Africa as Regional Hegemons."

Katika utafiti huo Mugambi anasema na hapa ninamnukuu:

"In regard to Eastern Africa, it's sufficient to recognize the role of Kenya as another major power. It's an economic powerhouses in the region and over the years, Nairobi has become the multinational capital of the region." Mwisho wa kunukuu.

Kwa tafsiri yangu Mugambi anamaanisha kwamba "Kenya ndiyo nchi kubwa Afrika Mashariki,kwamba ina uchumi mkubwa katika eneo la ukanda huu na Nairobi ndiyo kitovu cha mitaji mikubwa ya kikanda."

Mugambi anawakilisha mtazamo wa wakenya wengi namna wanavyoitazama nchi yao dhidi ya Tanzania.

Lakini ukweli wa hili upoje?

Tuitazame nadharia ya hegemony ili kuona kama hiki wanachojiona nacho wakenya ni kweli au lah!?

Nadharia hii inayotokana na mwananadharia wa kiitaliano Antonio Gramsci na kuja kutoholewa baadae inaeleza kama ifuatavyo:

Hegemonic Stability Theory: "International system is likely to be stable if a single nation-state is dominant or outright hegemon. Conversely, the absence of such a state would be associated with disorders."

Kwamba: "Mfumo wa Kimataifa unaweza kuwa imara ikiwa nchi moja itatawala nyingine au kuwa kiranja kwa wengine. Kinyume chake, kutowepo kwake kutasababisha kutokuwepo kwa utulivu."

Brown nae aliongezea, "Hegemon is a state that has the capacity to set rules of action and by extension enforce them, the state also needs to have the alacrity to act on this ability."

Hivyo basi, wakenya wanaamini kuwa mustakabali wa uchumi wa Afrika Mashariki unaitegemea Kenya kinyume chake hakuwezi kuwa na utulivu. Kwamba Kenya inaweza kuweka kanuni na kulazimisha wengine wafuate hizo kanuni kama vile walivyofanya lockdown n.k na wanajaribu kuonesha utayari wao katika hili.

Mugambi ametazama uchumi wa Kenya na pia kulinganisha jeshi la nchi hiyo na nchi kama Ethiopia na kutoa majibu ya jumla kama walivyo wakenya wengi pasina kujua kuwa takwimu za majeshi nyingi haziwezi kuwekea wazi kwa sababu za kiusalama.

Wanachoshindwa kutambua wasomi wengi wa kikenya ni kuwa nchi kuwa hegemon kuna vigezo vingi sana ambavyo tukitazama vyote havithibiti kwa Kenya.

Aneek (2010:59-63) na Schenoni (2017) wameainisha sababu nane za nguvu ya taifa aliposema: The national power of a State is the product of a number of elements. These are; (i) Geography (ii) Population (iii) Natural Resources (iv) Popular Support (v) National Character (vi) Technology and military strength (vii) Ideology (viii) Leadership

Hivi kweli kabisa Kenya inaweza ikasema ipo eneo zuri la kimkakati kijiografia kuizidi Tanzania ambayo imezungukwa na nchi 8 zinazoitegemea moja kwa moja ikiwemo Kenya yenyewe? Kweli Kenya inaweza kusema ipo eneo zuri kwa kuwa kwake karibu na Somalia?

Tanzania ni ncho ya tatu kwa idadi ya watu katika Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi Kusini mwa Afrika (SADC) nyuma ya DRC na Afrika ya Kusini na kwa hivi sasa Afrika Kusini inaweza kuwa imeachwa. Katika EAC ni ya kwanza, hili nalo Kenya hawalipimi?

Kenya ina rasilimali gani nyingine ukiacha mbuga ya Masai Mara ambayo nayo kwa kiasi kikubwa nyumbu wanaofuatwa kutazamwa na watalii hukaa Tanzania miezi 9 na kumalizia miezi mitatu Kenya? Kipi kingine wanacho?

Walitumia propaganda nyingi kuutambulisha Mlima Kilimanjaro kuwa upo Kenya mpaka kuandika "Visit Kenya and see mount Kilimanjaro" yote ikiwa katika kuwavutia wataliii ambao walikuwa wakitua JKIA na kisha kuwavusha kuja Tanzania wakiwa tayari wameshalala kwenye hoteli za Kenya. Baada ya Tanzania kununua ndege pumzi zimewaishia. Superpower gani hawa?

Inawezekana vipi nchi ambayo mpaka sasa Rais wake na Makamu wa Rais hawaelewani inaweza kuwa na popular support dhidi ya Tanzania?

Kwa kule kutazamana kwa misingi ya kikabila na kukosa umoja wa kitaifa Kenya inaweza kuwa na national character kubwa kuliko Tanzania?

Ukiitazama Kenya imegawanyija katika itikadi (ideology) kuna maeneo wanaamini katia ujamaa na kuna maeneo wanaamini katika ubepari hasa kundi la watawala hivyo kukosa muunganiko tofauti na Tanzanian ambayo itikadi yake imeelezwa wazi katika Katiba na inajidhirisha hata katika maisha ya kawaida ya watu. Kwa Tanzania mtu kushiriki msiba wa jirani si jambo geni huu ndiyo ujamaa lakini Kenya uone kama hali ipo hivi.

Hili la leadership (uongozi) lipo wazi kwamba wakenya wenyewe wanatamani wangekuwa na Rais wa nch yetu.

Kwa bahati mbaya sana katika Uhusiano wa Kimataifa tunapozungumzia Dola Kiranja (Hegemon) barani Afrika watu wengi hutazama sifa hizo kama zilivyoainishwa hapo juu na kuacha ile nguvu isiyoonekana (Soft power), hasa ushawishi wa nchi dhidi ya nchi nyingine na namna maamuzi ya nchi moja yanavyoweza kuwa na athari kwa nyingine.

Flemes (2007 na 2009) na Ogunnubi (2014) walibainisha hili waliposema:

"Regional power studies on Africa have often excluded soft power to understand the foreign policy behaviour of contenders for regional powerhood. It is also clear domestic challenges have been an important factor in disqualifying some state contenders as regional powers despite their potential or real influence."

Tumejiuliza kwa nini viongozi wengi wa nchi za Kusini mwa Afrika hutembela Tanzania hasa nchi zao zinapokuwa na changamoto? Kwa nini wasiende Kenya? Tanzania ina hii soft power yaani ushawishi mkubwa katika nchi hizo. Hiki ndicho walichomaanisha Flemes (2007 & 2009) na Ogunnubi (2014).

Lakini pia tujiulize, kwa zile changamoto za ndani ambazo Kenya inazo hasa za kikabila na kiutawala kwamba kabila gani liongoze Kenya, wanaweza kuwa dola kiranja?

Mbali na hayo ukuu wa nchi dhidi ya nyingine hupimwa kwa namna maamuzi yake yanavyoweza kuathiri wengine ndiyo maana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alisema wazi wakati ule ncho nyingi zinafanya lockdown kuwa yeye hatofunga mipaka kwa sababu Tanzanian inategemewa na nchi 8 kufunga mipaka ni kuumiza uchumi wa nchi hizo.

Walizuia malori kule Sirali mwaka 2015, Tanzania ikapunguza safari za ndege kutoka 42 hadi 14 wakaomba kukaa mezani. Walizuia unga wa ngano na gesi ya kupikia toka Tanzania mwaka 2017, Tanzania ikazuia maziwa na sigara wakaomba kukaa mezani. Walifunga mipaka Mei, 2020 Tanzania ikazuia malori wakaomba kukaa mezani.

Tatizo linalonishangaza hadi leo ni kweli hawajui reaction ya Tanzania katika maamuzi wanayofanya? Kama wanajua reaction ya Tanzania na mimi ninaamini wanafahamu hilo, inakuaje wanafanya maamuzi ambayo mwisho wa siku yanawafanya kuwa wadogo kama sisimizi.

Hofu ya Kenya ipo kwenye kuzidiwa kiuchumi jambo ambalo hawawezi kuliepuka wakati Tanzania inatumia akili kubwa kudeal nao.

That's all.
 
Kenya inazuia nchi za Ulaya na kuruhusu za Marekani zinazoongoza kwa COVID? Hizi ni siasa za chuki hakuna chochote, ni ujinga tu.
 
Huu ukweli mchungu Sana I see, hata shubiri na muarobaini haufui dafu! God bless Tz, God bless EAC, and God bless Africa!
 
Huo uzi unasema kampuni ndio haijalipa wafanyakazi na sio kwamba wao hawajalipwa na serikali, hayo ni mambo yao ya ndani, watamalizana wao kwa wao
Afadhali we unazoakili za kusoma na kuelewa kuliko hao wanapita juujuu tu na kuanza kuipeleka lawama kusiko stahiki! Sijui walifanyaje mtihani wa STD vii😂🤣😂!
 
Back
Top Bottom