Hofu na tafakuri za mwaka mpya/Raia Mwema, Januari 1, 2020

Rubawa

JF-Expert Member
Dec 25, 2015
1,857
2,000
BARAZANI

Hofu na tafakuri za mwaka mpya

Na Ahmed Rajab

LEO tunaufungua mwaka wa 2020 na tutauchungulia, japo kwa upenu tu, mwongo mpya unaotukabili. Tutaweza kuyafanya yote mawili, kufungua na kuchungulia, kwa kuyatia maanani yaliyokwishatokea na kwa kuziagalia dalili za yanayoweza kutokea.

Kuyazingatia yaliyopita na kuyatafakari yajayo si kazi nyepesi. Inazidi kuwa ngumu kwa sababu yanayojiri zama hizi si mambo ya kawaida yaliyozoeleka. Hizi ni zama zisizo yakinifu zilizojaa vishindo, mihemko na mishituko. Kama kweli kila zama zina kitabu chake basi hiki cha zama hizi ni kizito mno. Hakibebeki.

Tunachoshuhudia tunapoufungua mwaka mpya ni hofu kubwa, iliyo ngeni kwa wengi, iliyotanda na kuwagubika watu wa kawaida. Hofu hiyo inawashangaza na kuwababaisha kwa sababu ina mengi yenye kushangaza.

La kwanza ni kwamba hofu yenyewe inaonekana kama iliyozuka ghafla ingawa dalili zake zikionekana na mapema, tena kwa muda mrefu. Kuna waliokuwa wakionya kuhusu hatari ya kuchomoza kwa hofu ya aina hiyo lakini hawakusikilizwa.

La pili lenye kushangaza na lenye kuzidi kutisha ni kwamba hofu hiyo haikujibanza pahala pamoja tu. Lakini imezagaa kwingi duniani na inawaathiri mamilioni ya watu.

La tatu ambalo linashangaza na kusikitisha kwa mpigo mmoja, ni kwamba hofu hiyo imekuwa ikichomoza hata katika nchi zenye mifumo ya kidemokrasia iliyopea. Kwa miaka kama 70 sasa nchi hizo, au tuseme wakaazi wa nchi hizo, waliisahau hofu ya aina hiyo. Walisahau namna ya kuogopa, hasa kuwaogopa watawala wao.

Wakiamini kwa dhati kwamba katiba za nchi zao na taasisi zao za kidemokrasia zitawalinda na zitaendelea kuwalinda pengine hadi mwisho wa dunia. Pia waliamini kwamba hawatozishuhudia tena chuki kama zile zilizopelekea kuzuka kwa vita vikuu vya dunia.

Walikuwa na matumaini kwamba watu, hasa wa nchi za Magharibi, wataendelea kuvumiliana, kuendesha siasa zao kwa njia za kiungwana na kistaarabu. Uwezekano wa kurejelewa siasa za kutishana haukuwapitikia wakaazi wa nchi za Magharibi.

Zaidi ya yote kulikuwa na imani kubwa kwamba mifumo ya kikandamizi na ya tawala za kimabavu haitokuwa tena na nafasi katika siasa za nchi zao. Walishaona jinsi ubaguzi na chuki zilivyoutumbukiza ulimwengu katika nakama.

Kwa muda wote huo wakaazi wa Marekani, kwa mfano, na wa takriban nchi zote za Ulaya ya Magharibi ikiwemo Uingereza walikuwa wamo kwenye ureda. Mambo yao yalikuwa mazuri. Sasa, ghafla wanaiona hali ya mambo inawabadilikia. Hofu inaanza tena kutanda na kutamalaki katika nyoyo zao. Na imekuwa kama nge, inawauma.

Ubaya wa mambo ni kwamba hofu ya kuwaogopa watawala inachanganyika na hofu inayosababishwa na wenye kujihisi kwamba wao ndio wenye nchi, ndio wazalendo halisi. Wao huzusha hofu kwa kupalilia chuki dhidi ya watu wa aina fulani, na wawe wageni, wahamiaji, wakosoaji wa serikali au wapinzani au watu wa imani fulani za kidini.

Inasikitisha kwamba siku hizi tunashuhudia muongezeko mkubwa wa visa vya mashambulizi dhidi ya Waislamu, dhidi ya Wayahudi na dhidi watu wenye asili zisizo za kizungu katika nchi kadhaa barani Ulaya na Marekani.

Usiku wa Jumamosi iliyopita mtu aliyekuwa na pandikizi la panga aliingia kwenye nyumba ya Kuhani mmoja jijini New York na aliwajeruhi kwa panga watu wasiopungua watano waliokuwa wakiadhimisha sikukuu ndogo ya Kiyahudi iitwayo Hanukkah (“Tamasha la Nuru”). Jijini humo kumetokea visa vingine vya Wayahudi walioshambuliwa barabarani.

Katika siku mbili hizi Wayahudi wameshambuliwa katika sehemu mbalimbali za London, Uingereza. Inavoonesha ni kwamba wale wanaojihisi kwamba wao ndio wazalendo halisi wamezidi kuwa na chuki dhidi ya Waislamu pamoja na Wayahudi katika nchi mbalimbali za Ulaya na pia Marekani.

Wazee wengi katika nchi za Ulaya wanasema kwamba hofu inayotanda siku hizi inawakumbusha yaliyokuwa yakijiri katika nchi zao katika kipindi cha baina ya vita vikuu viwili vya dunia.

Kwa upande wa watawala na watawaliwa kuna mambo yanayotokea katika baadhi ya nchi za Ulaya au Marekani yenye kufanana na yanayotokea, kwa mfano, Tanzania. Ni mambo yenye kukirihisha; si mazuri hata kidogo. Na si ya lazima lakini kutokea yanatokea.

Kwingi duniani kuna hofu kwamba misingi ya kidemokrasia imo hatarini na, kwa hivyo, hofu hiyo inaifanya mifumo ya utawala katika nchi zinazohusika iwe inatisha.

Tukiitupia macho Tanzania ya leo tunaona kwamba mgongo wake umepinda kwa sababu taifa haliwezi tena kuyahimili mazito linaloyabeba. Wananchi wa hoi. Serikali inasema inajitahidi kuleta maendeleo na kuliendeleza taifa kwa kujenga miundombinu ya kisasa. Ushahidi wa miundiombiu hiyo upo lakini wananchi hawaridhiki kwa sababu miundombinu haijazi matumbo yao.

Pamoja na kuumizwa na makali ya maisha , wanaungulika na kusononeka kwa kujikuta wamegubikwa na hofu. Sijui ipi iliyo mbaya zaidi ya mwenzie, njaa au hofu.

Baadhi ya watendaji wakuu wa serikali wanatamka maneno ya ajabu, mengine yasiyoingia akilini, na mengine yanayowatia wenyewe hatiani kwani huwa wanajionesha waziwazi na bila ya kuona haya kwamba wanaikiuka katiba ya nchi. Kwa mfano, ingawa katiba inawazuia wakuu wa polisi wasijiingize katika siasa au wasikipendelee chama chochote cha siasa hata hivyo, mara kwa mara, hujitokeza wakikipigia debe chama kinachotawala.

Mkuu mmoja wa mkoa anasikika wazi kwenye video akieleza hila wanazozifanya kwa lengo la kuvisambaratisha vyama vya upinzani.

Juu ya hayo, hakuna mwenye kuwaasa na kuwaonya kwamba wanakwenda kinyume na sheria za nchi.

Yenye kuwapelekea watu wafunge midomo yao ni hofu. Wanaostahiki kuonya wanajizuia kufanya hivyo wakichelea wasije wakaikwaruza serikali wakaingia matatani.

Wenye ujasiri wa kusema wanasema, tena wanasema bila ya woga. Lakini ni wachache. Na wachache wa hao wachache ndio wenye kunusurika.

Vyombo vya dola havilali, viko macho kuhakikisha kwamba waliosalia wanachukuliwa hatua kali. Ama wanafunguliwa kesi za bandia za kuhujumu uchumi au wanatekwa na wale waitwao watu wasiojulikana au wanapotea au wanatishwa kila uchao. Ilimradi hawana salama; roho zao huwa mikononi mwao.

Wananchi, kwa jumla, wamegubikwa na hofu kiasi cha kuwafanya wawe wanazungumza kwa mafumbo. Saa zote wanahiyari wajikwae udole kushinda kujikwaa ulimi.

Hofu yote hiyo ni ishara za kwamba katika mazingira hayo demokrasia imekuwa dhaifu. Ni dhaifu sio tu katika nchi zenye demokrasia changa lakini ni dhaifu hata katika zile nchi, kama Marekani, zenye demokrasia iliyopevuka.

Hilo ni thibitisho kwamba demokrasia inaweza ikapevuka na wakati huohuo ikawa dhaifu. Au ikapevuka na kuwa imara lakini baadaye ikachimbwa na kudhoofishwa kwa kusudi na viongozi wenye dhamira ovu.

Kuna kitu tunachoweza kukibaini kwa haraka katika nchi zenye mchanganyiko kama huo. Tunachoona ni kwamba katika nchi hizo kuna viongozi wanaojaribu kutawala kimabavu. Wanajaribu kufanya hivyo kwa kuikiuka miiko ya kidemokrasia. Donald Trump, Rais wa Marekani, ni mfano mzuri wa kiongozi wa aina hiyo katika wakati huu tulionao.

Ukweli wa mambo ni kwamba yeye mwenyewe peke yake asingeweza kujaribu kuyafanya ayafanyayo, kuiminya demokrasia, lau asingekuwa na wenye kumuunga mkono. Hiyo ndiyo siri yake.

Trump ana umati mkubwa wenye kuvutiwa na sera zake za kibabe. Wanavutiwa nazo kwa sababu sera hizo zina lengo la kuufurahisha umati huo ili aweze kujipatia muradi wake. Imekuwa kama Trump na huo umati wanacheza mchezo wa “nipe, nikupe”.

Trump anawahamasisha wenye chuki dhidi ya wageni, nao hao wabaguzi wanamuunga mkono ili aweze kuendelea kutawala na kutunga sheria zenye kuzikandamiza haki za kibinadamu na za kiraia nchini Marekani. Haki hizo ndizo zenye kuwalinda na kuwahami wakaazi wote wa Marekani kwani wote wako sawa mbele ya katiba na sheria za nchi.

Kuchomoka kwa hali hii iliyopo sasa si onyo tu bali pia ni changamoto ya kuwafanya wanaharakati pamoja na wanasiasa wa itikadi tofauti wawe wakakamavu katika kuzikinga taasisi za kidemokrasi zisishambuliwe kama zilivyoshambuliwa na kina Hitler na baadaye kusababisha vita.

Inahuzunisha kuona mafanikio ya kuimarisha demokrasia yaliyopatikana kama miaka 20 au 30 iliyopita katika nchi kadhaa za Kiafrika, ikiwemo Tanzania, hivi sasa yanaporomoka.

Mporomoko huo na ule mmomonyoko wa utamaduni wa kidemokrasia katika nchi za Magharibi ni funzo kubwa kwa nchi kama Tanzania. Unatufunza kwamba nchi zenye demokrasia iliyo changa yenye kuhitaji kuengwaengwa hazipaswi kuutegemea mfumo wa kidemokrasia wa nchi za Magharibi tulioudhania kuwa ni mfumo uliokomaa.

Kinachohitajika kufanywa kwa dharura ni kuusuka upya mfumo huo hasa kwa vile kwa sasa unaonesha dalili za kuiga dosari zilizo katika tawala za kimabavu za baadhi ya nchi za Kiafrika. Hiyo bila ya shaka ni kazi pevu na changamoto kubwa kwa wanaharakati wanaotetea demokrasia halisi Afrika na kwingineko.


Baruapepe: aamahmedrajab@icloud.com; Twitter: @ahmedrajab
Sent using Jamii Forums mobile app
 

Mkaruka

JF-Expert Member
Feb 5, 2013
12,875
2,000
Mtu anaandika kuhusu hofu huku akiwa na hofu, hatimaye kaishia kuruka ruka tu mpaka kapoteza maana
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom