Hivi viongozi huwa wanakisoma vema hiki kiapo cha maadili?

Kichuchunge

JF-Expert Member
Dec 2, 2020
337
886
Siku zote mara baada ya uteuzi, viongozi huwa wanaapisha. Na wakishaapishwa mmoja mmoja kuna kiapo kingine, wenyewe huita ahadi ya maadili huwa wanakiimba wote. Lakini ukiisoma ahadi hiyo kifungu kwa kifungu utagundua kuwa huenda viongozi wengi huwa hawafuata wala kuzingatia yaliyomo. Serikali nayo wakati mwingine inakuwa imelala vinginevyo viongozi karibu wote wangekuwa wakiishia jela. soma kiapo chenyewe......



AHADI YA UADILIFU KWA VIONGOZI WA UMMA

Kwa kuzingatia misingi ya maadili iliyoainishwa katika Ibara ya 132 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na masharti ya Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma ya mwaka 1995, ambayo yanamtaka kila kiongozi wa umma kuzingatia viwango vya juu vya maadili ili kukuza utu, uwazi, uadilifu, uwajibikaji na kuimarisha imani ya wananchi kuhusu
utendaji wa viongozi wa umma.

Mimi ................................................................................................................................ ninauahidi umma kwamba:
1. Nitakuwa mzalendo na mtii kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
2. Nitakuwa muadilifu na mfano kwa watumishi wa umma, watumishi wa Bunge, watumishi wa Mahakama na watu wengine katika kukuza na kusimamia maadili;
3. Sitatumia cheo changu kwa maslahi binafsi au ya familia yangu, ndugu zangu au marafiki zangu au mtu mwingine;
4. Nitalinda na kutumia rasilimali za umma kwa maslahi ya umma;
5. Nitatekeleza majukumu yangu na kufanya maamuzi kwa kuzingatia Katiba, Sheria, Kanuni, taratibu, miongozo, mila na desturi za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
6. Sitatenda kitendo chochote cha rushwa;
7. Sitaomba, kutoa au kupokea zawadi au fadhila isipokuwa kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa na Sheria;
8. Sitatoa shinikizo linalokiuka Sheria, Kanuni, taratibu na miongozo katika utendaji kazi za umma;
9. Sitatoa siri ambazo nitazipata au kuzijua katika utumishi wangu isipokuwa kama Sheria itaelekeza
vinginevyo;
10. Nitatekeleza majukumu yangu kwa kuepusha mgongano wa maslahi wa aina yoyote na mara zote nitatoa uamuzi kwa kuzingatia Katiba na Sheria;
11. Nitatoa huduma bora kwa usawa kwa watu wote bila kujali misingi ya dini, siasa, kabila, udugu, utaifa, ukanda, jinsia au hali ya mtu; na
12. Nitazingatia na kulinda heshima ya nafasi yangu ya uongozi wa umma ninapokuwa kazini, nje ya mahali pa kazi na hata nitakapostaafu au kuacha kazi.

TAMKO: Ninakiri kwamba nimeisoma Hati hii ya Ahadi ya Uadilifu kabla ya kuweka saini. Ninakubali na kutambua kwamba masharti yaliyomo katika Hati hii ni ya kimaadili na kisheria na ninawajibika kuyatekeleza. Ninaelewa kwamba kuvunja masharti hayo ni ukiukwaji wa maadili yaliyowekwa kwa mujibu wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma na Sheria za nchi na hatua za kisheria zinaweza kuchukuliwa dhidi yangu iwapo nitakiuka masharti hayo.
 
Back
Top Bottom