Hivi ndivyo teknolojia mpya zinavyoua biashara kubwa na jinsi ya kuzuia biashara yako isife kwa mabadiliko ya teknolojia

Makirita Amani

JF-Expert Member
Jun 6, 2012
1,781
3,074
Maendeleo ya teknolojia yanatokea kwa kasi kubwa sana.

Lakini kasi hii ya maendeleo na ukuaji wa teknolojia, pamoja na kuwa na manufaa kwa watumiaji wake wa mwisho, yamekuwa na maumivu makubwa kwa makampuni makubwa yaliyo kwenye sekta ambayo teknolojia mpya inaingia.

Kuna mifano mingi sana ambayo tunaona ikiendelea, ujio wa barua pepe umeathiri sana mashirika ya posta, ujio wa mitandao ya kijamii umeathiri sana sekta ya mawasiliano na habari. Pia ujio wa magari ya umeme na yanayojiendesha yenyewe kunaathiri sana soko la magari na hata kazi za udereva.

Tukienda kwenye mfano wa kampuni moja moja, ujio wa kamera za kidigitali uliua kabisa kampuni ya Kodak ambayo ilikuwa maarufu kwa kamera za kianalojia. Ujio wa simu janja (smartphone), uliua kampuni ya Nokia ambayo ndiyo ilikuwa inaongoza duniani kwa simu za kawaida.

Swali ni je nini kinapelekea makampuni haya makubwa kufa pale teknolojia mpya inapoingia kwenye sekta yake?

Kwenye kitabu The Innovator’s Dilemma: When New Technologies Cause Great Firms to Fail, Clayton M. Christensen amechambua kwa kina sababu kubwa tano zinazopelekea makampuni makubwa kushindwa kutokana na teknolojia mpya na hatua za makampuni makubwa kuchukua ili yasishindwe pale teknolojia mpya inapoingia kwenye sekta ambayo kampuni hiyo ipo.

The Innovator’s Dilemma.jpg


Uchambuzi kamili wa kitabu hiki cha The Innovator’s Dilemma upo kwenye channel ya SOMA VITABU TANZANIA

hapa tunakwenda kuangalia kwa ufupi sana sababu kuu za makampuni makongwe kushindwa na hatua za kuchukua ili kampuni isiachwe nyuma na teknolojia.

Kwa nini kampuni kongwe zinashindwa kuwekeza kwenye teknolojia mpya?
Sababu kubwa inayopelekea kampuni kongwe kuangushwa na teknolojia mpya ni kudharau teknolojia hizo mwanzoni, kwa kushindwa kufanya uwekezaji wa kutosha kwenye teknolojia hiyo, licha ya makampuni hayo kuwa na uwezo wa kufanya hivyo.

Mwandishi kupitia tafiti anaonesha kwamba kuna sababu tatu zinazozuia makampuni makongwe kuwekeza kwenye teknolojia mpya;

Moja; bidhaa zinazotokana na teknolojia mpya huwa ni za bei rahisi kuliko zile ambazo kampuni husika inatoa. Hivyo hakuna faida kubwa ambayo kampuni inaweza kupata kwa kuwekeza kwenye teknolojia hiyo, na hapo mtaji unaendelea kuwekezwa kwenye bidhaa za sasa ambazo zina faida nzuri.

Mbili; teknolojia mpya huwa inakuwa na soko dogo, soko ambalo ni jipya na ndiyo linaanza kukua. Kampuni kubwa inahudumia soko kubwa hivyo inaona soko hilo dogo siyo uwanja wake wa kupambana.

Tatu; wateja wanaoipa faida kubwa kampuni kongwe wanakuwa hawataki bidhaa mpya inayotokana na teknolojia mpya. Sasa kwa kuwa kampuni kongwe inawasikiliza wateja wake, inawapa kile ambacho wanakitaka na hivyo kuachana na teknolojia mpya.

Kwa kiasi kikubwa, teknolojia mpya huwa inapokelewa na soko dogo ambalo halina faida. Hivyo makampuni makubwa ambayo yanawasikiliza wateja huwa hayaweki uzito kwenye teknolojia hizo mpya. Teknolojia hizo zinakua kidogo kidogo na baadaye kuja kuwa tishio kwa makampuni hayo makongwe.

JINSI YA KUZUIA KAMPUNI ISIFE KUTOKANA NA TEKNOLOJIA MPYA
Kwenye kitabu cha The Innovator’s Dilemma, mwandishi ameshirikisha misingi mitano inayopelekea makampuni makongwe kufa na kupitia misingi hiyo mitano, ameshirikisha hatua tano za kuchukua ili kuzuia kampuni isife.

Hatua tano za kuzuia teknolojia mpya isiue kampuni yako.

  1. Kutumia teknolojia mpya kwenye taasisi ambapo kuna wateja wenye uhitaji. Hata kama ni wachache, kwa kukua nao, taasisi inatawala soko.
  2. Kutengeneza timu ndogo ambazo zinafanyia kazi teknolojia mpya, timu ambayo inahamasika na mradi huo mdogo na kufurahia ushindi mdogo unaopatikana.
  3. Kuwa tayari kushindwa na kujiandaa kushindwa haraka na mapema ili kujifunza njia sahihi ya kufanya na kuwafikia wateja sahihi. Ni mwendo wa kujaribu na kushindwa mpaka kupata kilicho sahihi.
  4. Kutengeneza mfumo mpya wa ufanyaji kazi kwenye timu ndogo walizoanzisha, lakini unaotumia manufaa ya taasisi kongwe. Hii inaondoa kikwazo cha mfumo wa kampuni kongwe kushindwa kwenye teknolojia mpya.
  5. Kutafuta wateja wapya ambao wana uhitaji wa teknolojia mpya na kuwapatia hiyo, badala ya kulazimisha wateja wa sasa kukubali teknolojia mpya. Kwa kuanza na wateja wapya, pale teknolojia inapokua, wateja wa zamani wanaingia moja kwa moja.
Usikubali mabadiliko ya teknolojia yanayoendelea yawe chanzo cha biashara yako kufa, jua wapi unapoweza kuanguka na kisha chukua hatua mapema ili kujizuia usianguke. Kama upo kwenye biashara au unafanya kazi yoyote ile, basi unapaswa kusoma kitabu cha The Innovator’s Dilemma na uchambuzi wake, kitakusaidia sana.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali.
 
Shukrani sana.Nimependa jinsi ulivyo chambua, maana umetoa katika lugha ya malkia ukaleta lugha mama ili kila mtu aelewe vema tena kwa ufupi.
 
Back
Top Bottom