hivi mambo haya bado yako tanzania? | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

hivi mambo haya bado yako tanzania?

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by Ms Judith, Mar 30, 2011.

 1. Ms Judith

  Ms Judith JF-Expert Member

  #1
  Mar 30, 2011
  Joined: Dec 24, 2010
  Messages: 2,569
  Likes Received: 20
  Trophy Points: 135
  Mwenyekiti awavua nguo wananchi, awapiga

  MWENYEKITI wa Kijiji cha Nkuu Ndoo wilayani Hai mkoani Kilimanjaro, anadaiwa kuwaadhibu wananchi wasioshiriki shughuli za maendeleo kwa kuwavua nguo mbele ya watoto wao, kuwanyoa nywele, kuwafunga kamba shingoni na kuwaburuta barabarani huku wakipigwa.

  Mwenyekiti huyo, Geofrey Tito, anadaiwa kushirikiana na Mwenyekiti wa Kitongoji cha Nkweshoo, William Shoo, katika kijiji hicho Kata ya Machame Mashariki kutekeleza adhabu hiyo.

  Wananchi wanaodai kupewa adhabu hizo walitoa tuhuma hizo Jumanne katika mkutano wa kijiji ambao hata hivyo uliahirishwa na Shoo baada ya Mwenyekiti huyo wa Kijiji kushindwa kuhudhuria.

  Kabla ya kuahirishwa kwa mkutano huo, wananchi wengi wa kijiji walikuwa wakitaka ajiuzulu, kwa madai ya kuwadhalilisha kwa kuwapa adhabu sawa na za wakati wa utumwa.

  Baadhi ya watu wanaodaiwa kufanyiwa ukatili huo walitajwa kuwa ni Joseph Augustino na Jacob Ndemfoo.

  Wakielezea madai yao kwa nyakati tofauti, wanakijiji hao walidai viongozi hao waliwafunga kamba shingoni na kuwapiga mbele ya watoto wao, kutokana na wao kutojitokeza katika utambuzi wa watu ambao hawakushiriki kuchimba barabara.

  “Sisi tulikwenda kushirikiana na wenzetu katika kazi za kujenga Taifa kwa kuchimba barabara, lakini mara baada ya kumaliza kazi hiyo, Mwenyekiti wa Kijiji na wa Kitongoji waliamuru tutoe taarifa za watu ambao hawakufika.

  “Sisi tuliondoka na kwenda nyumbani bila kwenda kufanya utambuzi lakini tulifuatwa na kufungwa kamba tukaburuzwa chini na kipigo juu,” alidai Ndemfoo.

  Mbali na unyanyasaji huo, wananchi hao walidai kuwa viongozi hao wamekuwa chanzo cha uharibifu wa msitu wa asili wa Nkweshoo unaozunguka Mlima Kilimanjaro, kwa kuruhusu miti kukatwa ovyo.

  Walidai kwamba, Serikali isipowaondoa madarakani viongozi hao wananchi watajichukulia sheria mkononi, kwa kuwa zaidi ya miti ya asili 3,000 tayari imeshakatwa, na magari ya kusomba mbao yamekuwa yakipita kijijini hapo bila kuzuiwa na uongozi wa Kijiji.

  Madai mengine yaliyotolewa dhidi yao, yanahusu ugawaji wa vocha za pembejeo, ambapo walidai vocha 168 zilitakiwa kutolewa katika kijiji hicho lakini ni 153 tu ndizo zilitolewa na kusababisha watu wengine kukosa.

  Mara baada ya mkutano huo kuahirishwa, wananchi waliopandwa na jazba walitaka kumshambulia Shoo, wakidai umefika mwisho wa kuendelea kuonewa na kuishi kama watumwa, kutokana na vitendo vya ukatili na udhalilishaji vinavyofanywa na viongozi hao.

  Gazeti hili lilimtafuta Tito bila mafanikio, lakini Shoo ambaye anadaiwa kushiriki katika unyanyasaji huo alipopatikana, alikiri kutoa adhabu hiyo na kudai kuwa ni kutokana na yeye kutopewa semina za kutoa mafunzo ya uongozi na kuwa hata ufinyu wa elimu yake ambayo hakuifafanua, umechangia.

  “Ni kweli nimeteleza katika uongozi, lakini hakuna binadamu asiyefanya makosa … sijawahi kupata semina inayonipa mafunzo jinsi ya kuwaongoza wananchi, kwa makosa haya nastahili kuonywa, lakini kama hawataki kunipa onyo itabidi nijiuzulu,” alisema Mwenyekiti huyo wa Kitongoji.

  Diwani wa Kata ya Machame Mashariki, Rajabu Nkya, aliwahakikishia wananchi hao kuwa hawataendelea kuonewa tena na kuwasihi kuacha kujichukulia sheria mkononi. Nkya aliwataka wananchi kutumia vyombo vya sheria kuwasilisha madai yao.

  source: HabariLeo | Mwenyekiti awavua nguo wananchi, awapiga
   
Loading...