Hivi kwanini vitabu vya Gamba la Nyoka na Kaptula la Marx vya Kezilahabi visitumike kufundishia Fasihi mashuleni?

Hussein J Mahenga

JF-Expert Member
Mar 5, 2012
744
633
Nimevisoma kwa yakini kubwa sana vitabu hivi viwili baada ya kuvipata kwenye moja ya maduka ya vitabu hapa mjini. Vyote viwili vinaelezeya madhila ya Ujamaa; Kaptula la Marx linaelezea zaidi kwa kebehi jinsi ujamaa ulivyoshindwa, kwa lugha ya picha hasa kwenye ile safari kuelekea kwenye Nchi ya Usawa, ambayo hata hivyo inashindwa kukamilika kutokana na kwamba njia yake ina changamoto kubwa. Vilevile, inaelezea jinsi washauri wa Rais Kapera wanavyompotosha, naye anafurahia, kwenye maamuzi mbalimbali. Mfano mzuri ni kwenye vazi lake la Kaptula alilolitoa Ujerumani kwa Marx na Shati lake ambalo amelitoa kwa Mao huko China.

Anayajaribia mavazi haya mawili ofisini kwake. Pamoja naye, yupo Katibu Muhtasi na Waziri wa Masuala ya Nje ya Nchi. Rais Kapera anapotoka akiwa ameyavalia mavazi haya, pamoja na kuwa yanaonekana kuwa makubwa kwake, Waziri anamwambia kuwa kapendeza sana, tena mavazi yale yalikuwa kwenye mtindo wa Kisasa. Lakini katibu Muhtasi anamwambia ukweli kuwa, ameonekana kama KITUKO kwani mavazi yale yanaonekana waziwazi kuwa ni makubwa kwake. Anamshauri kuwa, yeye anaye fundi cherehani mzuri huko Cuba ambaye anaweza akayapunguza. Rais Kapera, akitingishatingisha mabega yake kana kwamba kweli kapendeza, kama alivyoambiwa na waziri wa masuala ya Nchi za Nje, anakataa ushauri wa Katibu Muhtasi.

Kwa upande mwingine, gerezani wapo wafungwa wa kisiasa. Pamoja nao, yupo Africanus Mwangaza, mfungwa namba Sita, Mzee wa Makamo ambaye hata hivyo ndiye kiongozi wa wafungwa wenzake. Wanaigiza mchezo wa HAKI. Mfungwa namba Mbili ambaye ameiba kuku, anahukumiwa miaka 25 jela na Mfungwa namba Tano, ambaye kaiba fedha za serikali anahukumiwa jela kwa masaa sita.

Kwa upande wa Gamba la Nyoka, hapana shaka Kezilahabi, kwa ufundi kabisa, amejaribu kuonesha Fanaka za ujamaa, kwa kutoa ulinganishi baina ya Vijiji na Vijiji vya Ujamaa. Labda kwa harakaharaka ni kwamba, jina la Riwaya limetokana na kwamba, miaka mitano baada ya Ujamaa, Mzee Chilongo wa kijiji cha Ujamaa cha Bucho anaenda kuoga mtoni baada ya kukataa utaratibu mpya wa wakeze kumchotea nyumbani ili aoge nyumbani kwa kuwa tayari mabomba ya maji yalikuwa yameshaenea kutokana na harakati za ujamaa. Yeye aliona, mpango huu ni kinyume cha ujasiri wa enzi zao ambapo walipendelea kuoga mtoni, na wanaume wenzake, huku wakipambana na majoka na wakati mwingine wakitaniana na kuchekana juu ya nani hajatahiri na nani ana matako makubwa.

Vyote hivi yeye anayaona kama maisha ya Kijasiri. Anapofika Mtoni, anavua nguo kuyasogelea maji. Kabla hajaanza kuoga, pembeni kidogo mwa mto, anaona Nyoka mkubwa. Anatahayari na kukimbia kwa hofu. Anafika mbali kidogo, anaokota mawe na kuanza kumrushia nyoka. Jiwe moja linampata na kumpiga katikati kiasi kwamba anagawanyika kwa kukatika. Hata hivyo nyoka yule bado anaonekana yu mzima. Anasogelea kuangalia, na baadae kugundua kuwa kumbe lilikuwa ni GAMBA LA NYOKA!! Anajicheka kwa uwoga wake.

Nadhani hii ni picha halisi kabisa juu ya kile ambacho binafsi nakiita 'makombo ya Ujamaa'. Zipo sehemu nzuri ambazo msomaji akishazisoma atagungua kuwa Kezilahabi anatumia lugha kwa ufundi mkubwa wa aina yake. Kwa mfano, Mambosasa, mjamaa kindakindaki huyu, msomi wa Chuo kikuu cha Dar Es Salaam, ambaye alistaafishwa uenyekiti wa Kijiji kwa kula fedha za Kijiji. Siku moja, Rais anatembelea kijiji kile, na kwa kuwa wakati ule, wenyeviti wa vijiji walikuwa na hadhi kubwa, lazima wangeweza kusalimiana naye, kwa mkono, au hata tafrija kuandaliwa. Kweli inakuwa hivyo. Mambosasa naye anakuwa na matumaini makubwa kuwa itakuwa hivyo, kutokana na kile anachokidhania kuwa ni lazima atapata fursa ya kumsalimia Rais kwa kuwa yeye ni msomi.

Hata hivyo, anakuja kugundua kuwa, ni kweli ni msomi, lakini si mwenyekiti wa kijiji. Anafanya kila njia, anajipenyeza, na hatimaye anafika hadi kwenye ukumbi wa tafrija ya Rais. Anakuta vyakula vya kila aina, na pombe za kila aina. Anakunywa pombe na kula vyakula, na pia anabeba mabaki ya vyakula kwa ajili ya familia yake, akiwa na matarajio kuwa, mkewe Mama Werima, angeweza kufurahi sana. Anabeba mzigo huo kwa kila jitihada, mpaka anaufikisha nyumbani. Hata hivyo mkewe Tinda, (mama Werima) anamtukana sana akidai kuwa hawezi kula makombo. Anayachukua na kuyarusha nyuma ya nyumba ambapo mbwa wanagombania kila wakati. Ni picha nzuri sana.

Juu ya yote, kitabu pia kinaelezea ujamaa kwa kufanya ulinganishi na ubepari katika kasi ya maendeleo, lakini pia na mahusiano ya watu katika Nchi. Wapo vijana wawili, Mamboleo na Mambosasa, ambao ni wasomi. Kwa upande mwingine yupo Padre Madevu, hawara yake Mama Tinda, ambaye ni Beberu hasa. Padre Madevu na Mama Tinda tunakuja kugundua kuwa, wanauawa kwa sumu na Tinda, kwa jina la Mapinduzi, kwamba wote wawili hawa ni wapingamapinduzi. Hata hivyo, Tinda anajutia kwa baadae, na kumtaja kuwa Padre Madevu alikuw mtu mwema, hivyo hakupaswa kumdhulumu maisha yake.

Baina ya Mambosasa na Mamboleo, Mambosasa ni Mjamaa kupindukia, lakini kwa upande wake Mamboleo ni Mjamaa wa Staha. Wote hawa wamefukuzishwa kazi jeshini kwa sababu ya kumpiga Mwalimu wa Siasa jeshini, kama anavyowakumbusha Mzee Farjalla. Na pia wanaachishwa kazi baada ya kumshika mtoto mdogo matiti kwa lazima.

Vyote viwili ni vitabu vizuri sana, ambavyo nadhani endapo vingetumika kufundishia mashuleni, basi wanafunzi wangepata wakati mzuri wa kuujua ujamaa na madhila yake, kama kuhamishiwa kwenye vijiji vya ujamaa kwa lazima. Lakini pia mafanikio yake kama kuongezeka kwa uzalishaji wa mazao. Najua kuwa, Kaptula la Marx kilizuiwa kufundishwa kwa kuwa kinamkejeli moja kwa moja Nyerere. Sasa serikali inaweza ikaona umuhimu wa kukirejesha na kikatumika kwenye fasihi.
 
Unaujua utaratibu na vigezo vinavyotumika mpaka kitabu kiwekwe kwenye mtaala wa kufundishia?

Kaptula la Marx sidhani kama kinafaa. Suluhisho lake la kupindua serikali na kuua viongozi halikubaliki katika muktadha wetu.

Gamba la Nyoka naamini kilishawahi kutumika katika mitaala ya kidato cha sita huko miaka ya 80. Ila kinaweza kurudi. Rosa Mistika, Kichomi, Karibu Ndani, Dhifa, Gamba la Nyoka na Dunia Uwanja wa Fujo, Nagona na Mzingile vyote vinafaa. Cha muhimu tu wanafunzi na walimu inabidi wawe na welewa kidogo juu ya matapo mbalimbali ya Falsafa na hasa lile la la Existentialism kwa sababu ndilo linatawala karibu kazi zote za Kezilahabi.

Mimi natamani sana novela mojawapo kati ya Mzingile au Nagona iingizwe katika mtaala wa kidato cha sita.

RIP Kezilahabi aka Shaaban Robert wa pili
 
Kwa hiyo Kaptula la Marx hakiwezi kurudi kisa tu kina hamasa ya Mapinduzi? Mbona Betrayal in the City cha Imbuga tumekitumia na kianendelea kutumika? Nadhani huu ni uhafidhina wa kupindukia.​
 
Bujta la marksi kiliwahi kutumika advance ,pamoja na rosamistika ...
Kwa sasa vitabu hivi km maudhui ya kijamaa yameshapitwa na wakati hivyo havifai kufundishia
 
Unaujua utaratibu na vigezo vinavyotumika mpaka kitabu kiwekwe kwenye mtaala wa kufundishia?

Kaptula la Marx sidhani kama kinafaa. Suluhisho lake la kupindua serikali na kuua viongozi halikubaliki katika muktadha wetu.

Gamba la Nyoka naamini kilishawahi kutumika katika mitaala ya kidato cha sita huko miaka ya 80. Ila kinaweza kurudi. Rosa Mistika, Kichomi, Karibu Ndani, Dhifa, Gamba la Nyoka na Dunia Uwanja wa Fujo, Nagona na Mzingile vyote vinafaa. Cha muhimu tu wanafunzi na walimu inabidi wawe na welewa kidogo juu ya matapo mbalimbali ya Falsafa na hasa lile la la Existentialism kwa sababu ndilo linatawala karibu kazi zote za Kezilahabi.

Mimi natamani sana novela mojawapo kati ya Mzingile au Nagona iingizwe katika mtaala wa kidato cha sita.

RIP Kezilahabi aka Shaaban Robert wa pili
Hiki kitabu cha Rosa Mistika kinapatikana wapi? Nasikia hakipatikani,lakini inaonekana watu mmekisoma...msaada tafadhali.
 
Hiki kitabu cha Rosa Mistika kinapatikana wapi? Nasikia hakipatikani,lakini inaonekana watu mmekisoma...msaada tafadhali.
Vitabu vyote vya Kezilahabi, Shaaban Robert mpaka hadithi za Alfu Lela Ulela vimechapwa upya na vinapatikana katika maduka mengi ya vitabu jijini Dar; na kwingineko. Dar fika duka la vitabu chuo kikuu, Tanzania Publishing House n.k.
 
Kwenye kazi ngumu kidogo za kifasihi nilizowahi kusoma nibza huyu mwandishi, nilitsmani kuandika ka yeye, wahusika wake walikuwa wapo vizuri ni lazima usome sana falsafa na hata saikolojia, kwa upande wa upangaji wa matukio alikuwa vizuri...
Halafu vitabu vyake ni kama series vile, mfano mzingile kisha nagona..
 
Sisi tuliobobea kwenye ma- integration na differentiation hapa tunaona kama mjadala wa kupindua nchi....

Ngoja tuwe wapenzi wasomaji...
 
3 Reactions
Reply
Back
Top Bottom