Historia ya Wachagga: Koo, Kabila na Falme-Mangi

Naona nisimulie kwa ufupi historia ya mangi Sina wa Kibosho kwa ajili ya msaada wa baadhi ya watu kwenye forum hii. Ukweli ni kwamba Sina halikuwa jina lake la asili alilopewa na wazazi wake. Kwa wale watakaotaka taarifa zaidi waniandikie kwenye email yangu hapo chini, ila hapa nitasema machache. Baba yake Sina aliitwa Kisaro ambaye alikuwa ni miongoni mwa watoto wa mwisho mwisho wa Iwere wa ukoo wa Urio wa Kibosho. Miaka ile ambayo Sina alikuwa ni kijana mdogo (inaaminika kama miaka 8 - 10 hivi) Machame ilikuwa ikitawala kule magharibi ya uchagani na iliikalia Kibosho kwa mkono wa chuma. Kuna wakati askari wa Machame walivamia Kibosho wakiituhumu kutengeneza silaha kinyemela. Waliua vijana wengi na watu wazima (hasa wanaume) na kuchoma moto nyumba na mashamba. Wapo walioweza kupona kwa kukimbia kujificha porini na mapangoni, na wale askari wa Machame walipokuwa wanarudi porini wakawakamata baadhi ya watu, wengine wakauawa lakini wachache walichukuliwa kama mateka wawapeleke kwa mangi wa Machame ili hatima yao ijulikane huko. Kati ya waliochukuliwa, alikuwepo kijana mdogo aliyekuwa akitetemeka sana kwa hofu (na inaelekea na baridi pia) ambaye yule jemedari wa askari wa Machame alimhurumia na kusema si vyema kumuua bali wakamwachie mangi wa Machame mwenyewe aamue.

Walipofika Machame ni ajabu kwamba mangi Ndesserua aliyekuwa akitawala Machame wakati huo ambaye alifahamika kama mtawala mkatili kupita kiasi alimpenda tu huyo mtoto na kuamuru kwamba akae katika boma la kwa mangi siku zote za maisha yake na apewe kazi za kusaidia pale kwa mangi. Hii ikamfaya yule mtoto ghafla akawa maarufu kule Machame. Inasemekana alikuwa ni mtiifu, hodari, mchapa kazi na alipendwa sana na jamii ya kwa mangi kule Machame na hata kwa watu wengine. Inasimuliwa kwamba alipenda sana kula mifupa pale kwa mangi hata wakamwita Sina (kimachame yaani kusina, kutafuna nyama na mifupa!), na hii kwa vile kwa mangi kila siku walikuwa na sherehe za hapa na pale, wakichinja ng'ombe na mbuzi kwa wingi, yaani nyama choma mbele kwa mbele na supu na mbege za kumwaga. Hili jina Sina ndilo lililokuja kuwa jina lake kabisa baadaye.

Kwa upendo mangi Ndesserua aliokuwa nao kwa Sina, alimwingiza katika jeshi lake la askari baada ya kwenda jando na hata inasemekana mara kwa mara alimwamini sana katika majukumu mbalimbali nyeti katika utawala kitu ambacho kilianza kuleta wasiwasi kwa baadhi ya wazee wa ukoo wa mangi kule Machame, wakimtahadharisha mangi Ndesserua kwamba Sina na uaminifu wote alionao lakini bado ni wa asili ya Kibosho. Hata hivyo mangi Ndesserua alimlea Sina kama jemedari na kwenda kwenye vita vingi mbalimbali hasa kule Masama, Yuri na Siha magharibi mwa uchagani. Kwa kweli Sina aliishi Machame kwa muda mrefu akiwa jemedari wa vita, mpaka wakati mangi Ndesserua alipoanza kuwa mgonjwa na kuhisi kwamba muda wake si mrefu sana, alimwambia ndugu yake Nassua (ambaye alim-recruit Sina kwenye jeshi) kwamba hali ya Kibosho si nzuri kisiasa, na ili kuepusha kuibuka kwa mtawala kama Lokilo kule Kibosho ambaye alileta matata kule uchagani, Nassua afanye hima kuhakikisha Sina anaenda kuwa mtawala kule Kibosho (ingawa hakutoka kwenye boma la Tatuo-Kirenga lililokuwa linautawala kule Kibosho). Na kwa vile mangi Wawa aliyekuwa anatawala Kibosho alikuwa ndiyo amefariki na hakuna mtawala Kibosho, waliitumia nafasi hiyo kwenda kumtawalisha Sina kwa nguvu Kibosho. Inasemekana watu wengi sana waliuawa kwa kupinga kitendo hicho na hasa ukoo wa Olotu Mallya ambao waliuawa karibu wote na waliobahatika kupona walikimbilia Old Moshi wanakoishi mpaka leo hii (kwa jina la Olotu). Kwa kutumia uhodari wake na uzoefu wake wa kivita, kwa muda mfupi Sina aliweza kuhamasisha vijana Kibosho na kuunda kikosi cha nguvu cha maaskari ambapo alifanya mashambulizi makali dhidi ya ukoo wa Tatuo-Kirenga uliokuwa maarufu kisiasa kule Kibosho ili auangamize kabisa amalize upinzani wa kisiasa dhidi ya utawala wake. Waliweza kupona wachache kwa kujificha porini, wengine waliweka yamini ya kuwa waaminifu kwake na wachache walitorokea Vunjo-Mwika wanakotumia jina la Urio hadi leo.

Haukupita muda mrefu makali ya Sina ya kulelewa kama jemedari wa vita yalianza kuwa shubiri kule uchagani. Aliiangukia Mweka ambayo ilikuwa ikitawaliwa na ukoo wa Tesha na kuilazimisha kujisalimisha. Tayari Uru ilishakaa chonjo baada ya kugundua siasa za Kibosho zimebadilika ghafula. Matukio mbalimbali ya kihistoria kwa wakati huo uchagani inaonyesha kwamba Sina alitawalishwa kuwa mangi wa Kibosho katika miaka ya 1876-1878, kwa sababu masimulizi yanaonyesha kwamba si muda mrefu sana baada ya Sina kutawala Kibosho mangi Ndesserua wa Machame alifariki (ca. 1880). Bila kutaka kwenda ndani sana katika historia, kwa kile ambacho pia kilionekana ni njama za kuitiisha Machame chini ya amri yake baada ya kufa kwa Ndesserua, mangi Sina alipeleka wapambe Machame wakipiga ukunga (tangazo la kilio) kuwa mangi Sina naye amefariki hivyo wamachame (waliomtawalisha) wakamzike na kuangalia ni nani wa kumtawalisha. Hii ilikuwa ni njama kali iliyopangwa Kibosho, kwani wamachame wengi walikwenda 'kwenye kilio' na kwa vile hawakwenda kivita basi waliangukia katika mikono ya Sina ambaye aliwaua karibu wote isipokuwa wachache waliobaki wakafanikiwa kutoroka na kurudi. Askari wa Kibosho walikwenda Machame wakachoma mashamba na nyumba na kutia hasara kubwa. Hata hivyo, wamachame walikataa kujitiisha chini yake hali ambayo ilileta vita vya mara kwa mara na Machame kuzidi kuhujumiwa na mangi Sina. Kitendo hiki alichokifanya Sina dhidi ya Machame kilizusha hofu kubwa sana uchagani dhidi yake hasa kutokana na utawala wa Machame ulivyokuwa ukiheshimika. Hali hii ni kama ilimpa morali zaidi mangi Sina ambaye aliiangukia Uru kwa kishindo na kwa muda mfupi Uru ikajisalimisha. Akaishambulia Mbokomu nayo ikajisalimisha na wakachukua mateka wengi (na hapo ndipo pia Ndegeruo aliyekuja kuitwa Marealle alipochukuliwa mateka naye kupelekwa Kibosho). Mangi Sina akatumia nafasi ya kuwa na Ndegeruo katika himaya yake kwenda kushaishambulia Vunjo na kumtawalisha Ndegeruo Marealle kule Marangu. Kufikia miaka ya mwishoni mwa 1880 mangi Sina alishatiisha maeneo mengi sana kule uchagani na kutawala anga la kivita, hofu yake ikisikika na kuhisika kila kona kule uchagani.

Hata hivyo mpinzani wake mkuu alikuwa mangi Rindi Mandara wa Old Moshi. Mangi Sina na mangi Rindi walibaki kuwa watawala wawili kule uchagani katika miaka ya 1880 waliofanya vita kila kukicha wakigombania maeneo ya mipaka ya utawala ili kuteka watu kuwauza kwa waarabu kama watumwa. Ingawa waliogopana na kuonekana kama waliheshimiana, lakini kitendo cha mangi Sina kumchokonoa mara kwa mara mangi Mandara kwa kushambulia maeneo jirani na himaya yake, kilimnyima usingizi Mandara na hata kuamua kufanya vita ya kufa na kupona dhidi ya mangi Sina katika mwaka 1888 akishirikiana na watawala wengine kule uchagani waliochoka adha za mangi Sina. Pamoja na kumchangia mangi Sina, bado Mandara na washirika wake walishindwa vibaya. Kitendo cha mangi Sina kuishambulia tena Machame 1890 huku akimsaidia Shangali dhidi ya kaka yake Ngamini, kilimtia katika hatihati kubwa na ukoloni wa kijerumani uliokuwa umeshashika hatamu kule Old Moshi. Huku wakichochewa na mangi Mandara walimvamia mangi Sina katika boma lake katika vita kali iliyopiganwa kwa siku mbili. Mangi Sina alijisalimisha katika vita hiyo, aliamua kushusha bendera ya sultani wa Zanzibar iliyokuwa ikipepea katika boma lake na kuridhia kuwa mshirika wa serikali ya kikoloni ya kijerumani. Hii vita ndiyo iliyopelekea tamati ya vita vya mangi Sina kule uchagani.

Mangi Sina ni mtawala wa Kibosho aliyejulikana sana kwa uhodari wake wa kupanga na kupigana vita. Anakumbukwa kama aliyeijenga Kibosho ikawa ni utawala uliojitegemea (kutoka katika makucha ya Machame) na kuwa wenye nguvu nyingi kabisa kule uchagani. Inasemekena wakati wa utawala wake wananchi wa Kibosho walilala mlango wazi (yaani kutokana na amani katika himaya yake), walipanda na kuvuna kwa wingi, walikula na kusaza. Ingawa madhara ya malezi yake kwa mangi Ndesserua yalionekana katika maisha yake yote ya utawala (kama waingereza wanavyosema - You will be like your mentor) kutokana na ukatili wake wa kutisha na kupenda vita kama sera ya utawala, mangi Sina alisisitiza kilimo bora kwa watu wake ambapo inasimuliwa kuwa alisisitiza kilimo cha mbolea, na kutoa usalama wa hali ya juu kwa watu wake ambao inasemekana walikuwa wakichunga mifugo yao hadi mbali bila ya woga wowote ule. Pamoja na utawala wa mkono wa chuma wa mangi Sina kule Kibosho na matatizo makubwa ya kiusalama aliyosababishia tawala zingine kule uchagani, mangi Sina bado ataendelea kukumbukwa sana Kibosho kwa maana katika utawala wake wakibosho waliishi kwa usalama mkubwa na mafanikio ya kimaisha. Hawakujua njaa wala kupungukiwa, na jina lao likawa kubwa katika historia. Mangi Sina alifariki mwaka 1897 kutokana na matatizo ya tumbo. Mtoto wake aliyeitwa Ilmollelian alitawalishwa ingawa kwa bahati mbaya siasa za uchagani zilichafuka na akanyongwa mwaka 1900 pamoja na watawala wengine wa wachaga kwa tuhuma za uhaini dhidi ya serikali ya kikoloni ya kijerumani.

Ahsanteni, email yangu ni kay.cm@hotmail.co.uk.
 
Hizi siasa za ukibosho na umachame ndizo zinazowaharibia wachaga. Bahati yao wako katika Jamhuri ya Tanzania, wangepata jamhuri yao kama alivyokuwa anataka chifu Marealle leo hii tungekuwa tunazungumzia mauaji ya kimbari kulio yale ya Rwanda. Aibu tupu!
 
Hizi siasa za ukibosho na umachame ndizo zinazowaharibia wachaga. Bahati yao wako katika Jamhuri ya Tanzania, wangepata jamhuri yao kama alivyokuwa anataka chifu Marealle leo hii tungekuwa tunazungumzia mauaji ya kimbari kulio yale ya Rwanda. Aibu tupu!

Ni kweli Kithuku. Ukifahamu historia za huko tulikotoka utashangaa sana hasa kwa wachaga. Harakati za kisiasa uchagani zilianza miaka mingi sana siyo jana au juzi kama tunavyofahamu katika historia ya nchi hii ya Tanzania. Ukumbuke pia kwamba, wakati Tanganyika inapata uhuru mwaka 1961 tayari wachaga walikuwa wana rais wao waliomchagua kidemokrasia kabisa mwaka 1960. Aliitwa Eliufoo Solomon. Kwa hiyo mambo ya kisiasa, chaguzi na mashindano ya kisera katika mambo ya vyama vya kisiasa kwa wachaga ni mambo asilia. Uchagani ndiyo mahali pekee ambapo wakoloni walinyoosha mikono kiutawala. Mpaka imefika wanafanya uchaguzi wa rais ujue kwamba wakoloni walishaona hawa ni watu wa kuwaacha waende zao maana ni wagumu sana kuwa-control. Ni kama wakoloni wakiingereza walishaona kwamba ni vyema kuwaacha wajitawale wenyewe kuliko kuendelea kupoteza muda na gharama nyingi kuwa-manipulate kiuongozi.

Ukumbuke pia kwamba hapo nyuma wajerumani walishahangaika kupita kiasi kutawala uchagani. Mwaka 1888 Carl Peters aliweka mkataba na mangi Rindi Mandara wa Moshi na kutangaza kwamba uchagani iko chini ya utawala wa Kijerumani. Hata hivyo, 1890 walikuja kugundua kwamba kumbe waliingizwa mjini na Mandara maana kule magharibi ya uchagani walikuwa wakiendelea na tawala zao na hawakuwa na habari kabisa juu ya wajerumani ni nani. Huku wakichochewa na Mandara, mwaka 1890 ndipo serikali ya kijerumani ilipopeleka majeshi kupambana na mangi Sina wa Kibosho na Sina aliposhindwa ndipo serikali ile ya kikoloni ilipotangaza rasmi kwamba uchagani yote iko chini ya utawala wa kijerumani. Hata hivyo, haikuchukua muda mrefu hali ikawa tete tena kwa wakoloni, maana mwaka 1891 boma lao kule Moshi lilivamiwa kwa amri ya mangi Meli Mandara, na baadhi ya maofisa wa kijerumani na maaskari wakauwawa na kuhitimisha rasmi utawala wa kijerumani kule uchagani. Iliwachukua miaka mitatu kurudi tena uchagani na kwa wakati huu kwa kuombwa na mangi Marealle wa Marangu akiwaahidi kwamba katika himaya yake kuna usalama wa kutosha na atawapa msaada utakaohitajika. Kwa hiyo wakoloni wale wakarudi (kutokea Zanzibar) wakaweka makazi yao Marangu. Marealle wakati huu akawa mshirika wao mkuu na kuwapa siri ya kupambana na mangi Meli wa Moshi. Kwa hiyo kutokea Marangu, wakajikusanya baada ya Marealle kuwatengenezea mazingira na hata kuwapa msaada wa askari, na kuivamia himaya ya Meli mwaka 1894. Vita vikali vilipiganwa lakini wakati huu mangi Meli alishindwa na kusalimu amri. Hii iliwezesha tena serikali ya kikoloni ya Ujerumani kurudisha makao makuu yao tena katika boma la Moshi.

Hata hivyo, si muda mrefu hali kwa wakoloni ikawa tete na vita vya kila kukicha. Inasemekana wakoloni wa kijerumani walikuwa wakiishi kwa hofu kule uchagani bila kujua nini kingeweza kutokea wakati wowote. Mpaka ilipofika 1900, serikali ya kikoloni ilikuwa imechoka kabisa na kuona njia pekee ya ku-control uchagani ni kwa kutumia vitisho, nguvu na ukatili. Hivyo wakaamua kuwabambikia kesi za uhaini watawala wa uchagani na kuwanyonga karibu wote mwaka huo wa 1900 mbele ya hadhara. Inasemekana ni watawala wawili tu walioepuka zahma hiyo, mangi Shangali wa Machame na mangi Marealle wa Marangu (ambaye alikuja kutuhumiwa baadaye kwamba ndiyo aliyewachongea na kuwapikia majungu watawala wengine). Ukatili huo hata hivyo ulileta matata sana kwa maofisa wa kikoloni kule Moshi kwani walibanwa na serikali ya Ujerumani kuthibitisha tuhuma hizo na kama haki kweli ilitetendeka. Ofisa mkuu kwa kijerumani kule Moshi ilibidi afukuzwe kazi na kurudishwa Ujerumani na mambo hayakuwa yametulia kabisa. Hicho kitendo kilisababisha uchunguzi ufanyike upya wa ushahidi uliopelekea hukumu hizo dhidi wa watawala wa uchagani na mwaka 1905 mangi Marealle akakamatwa na kutiwa ndani kwa tuhuma za kufanya kitendo kilicho hatarisha uvunjifu wa amani kwa kutoa taarifa zisizo sahihi juu ya usalama kule uchagani. Aliachiwa mwaka 1906, lakini mwaka 1907 alikamatwa tena na kutiwa ndani na serikali ya kijerumani kwa kile kilichokuwa kikidaiwa kwamba kuendelea na uchunguzi wa kilichopelekea mauaji ya mwaka 1900. Aliachiwa tena mwaka huo huo, na kwa kuona kwamba maisha yake yako hatarini huku akihofia kilichowapata watawala wengine aliamua kukimbia nchi na kuishi kama mkimbizi kule Nairobi Kenya. Mangi Marealle alirudi tena Marangu mwaka 1909 baada ya kuomba msaada kwa serikali ya kiingereza iliyokuwa ikitawala kule Kenya ambao walifanya mazungumzo na mwakilishi wa wakoloni wa kijerumani wa Afrika mashariki kule Zanzibar na alikubaliwa kurudi. Hata hivyo hakuishi muda mrefu sana baada ya hayo maana alifariki mwaka 1911, na inasemekana alikuwa ni mwenye masikitiko huku akihisi nuksi na balaa kumwanda katika maisha yake.

Hayo ndiyo mambo mwenzangu ya uchagani. Kama ni siasa, hata wakoloni waliwajua kwamba wale hatua zao ziko mbili mbele. Lakini kwa vyovyote vile wakoloni walisaidia kufuta vita vya wenyewe kwa wenyewe kule uchagani. Haikuwa rahisi. Kwanza walipiga marufuku biashara ya utumwa ambayo ndiyo ilikuwa moja ya sababu kubwa ya vita kule uchagani. Kuwanyonga watawala wa kichaga 1900 ingawa ilikuwa ni njia ya kikatili sana lakini ilisaidia pia kujenga hofu na kufuta kabisa dhana ya kujaribu kuinua silaha na kutishia maisha ya yeyote yule wakati serikali ya kikoloni ipo. Pia elimu ilisaidia sana pamoja na dini. Wamishionari walifanya kazi sana kujenga mashule, huduma za afya na makanisa. Hiyo ilisaidia sana kubadilisha mtazamo wa wachaga kutoka katika fikra za kijima za utawala wa kibabe na kuelimika na kuheshimu wengine.
 
Hahaha nimepata elimu yakutosha ndio maana nyumba za machame na kibosho milango haitazamani,hii bifu noma.sasa mbona mi ni mmachame ninamchumba kibosho itakuwaje!? nisaidieni wana JF
 
Hii nchi bila sisi wachaga isingekuwa hapa ilipo,tunahitaji Rais mchaga ili umaskini uondoke
 
Hahaha nimepata elimu yakutosha ndio maana nyumba za machame na kibosho milango haitazamani,hii bifu noma.sasa mbona mi ni mmachame ninamchumba kibosho itakuwaje!? nisaidieni wana JF

Ni kweli. Wamachame wengi waliona wamesalitiwa na mangi Sina wa Kibosho. Ingawa alishaonekana kuwa na shari lakini hawakutegemea hali ingefikia kuwa mbaya hivyo. Ndiyo maana walipoambiwa amefariki wengi walikwenda ili kumzika mtu wao waliomfahamu siku nyingi. Walikwenda majemedari wa vita na walikwenda hata watu wa ukoo wa mangi wa Machame. Ukumbuke pia kwamba pamoja na kwamba hapo nyuma Machame iliitawala Kibosho kwa mkono wa chuma lakini hawa walikuwa ni majirani walioishi kwa muda mrefu. Kulikuwa na kuoleana na wakibosho wengi walikuwa wakienda Machame kufanya biashara ndogo ndogo na kazi mbalimbali. Hata hivyo wamachame walionekana ni watu waliojisikia na kudharau wachaga wengine kitu ambacho hakikupokelewa vizuri sana na wegine kule uchagani. Kwa mfano, Baroni Von Der Decken, Mjerumani mvumbuzi aliandika (katika miaka ile ya 1860) jinsi wachaga wengine walivyojipanga kufanya hujuma dhidi ya Machame na husda ilivyokuwa kubwa dhidi ya wamachame kule uchagani. Kwa hiyo, kile alichokifanya mangi Sina dhidi ya Machame, kwa baadhi zilikuwa ni habari za mshituko lakini kwa wengine waliona kama huo ndiyo mwanzo wa mwisho wa vigogo wa kisiasa kule uchagani. Ni kitu kilichopokewa kwa hisia tofauti kule uchagani.

Kwa maelezo yaliyotolewa na Hans Meyer aliyoandika kuhusiana na safari zake kule uchagani (miaka ya 1886-1889), inaonekana ndiye mgeni pekee ambaye aliweza kugusia nyakati mauaji dhidi ya wamachame yalipofanyika. Alisimulia kwamba ni katika miaka ya 1886 (tofauti na alivyodhani Kathleen Stahl ambaye amekosea mambo kadha wa kadha ya kihistoria kule uchagani akirudisha nyuma miaka kwamba ni 1870's). Lakini hata hivyo kulikuwa na cha zaidi ya kilivyoonekana kwa wenyeji wa kawaida sehemu zile. Hii ndiyo inaonyesha jinsi siasa kule uchagani zilivyokuwa ni ngumu na zenye mambo mengi yasiyoeleweka kirahisi. Kathleen Stahl kwenye kitabu chake cha 'History of the Chagga People of Kilimanjaro' amegusia pia kitu kinachoonekana kilikuwa kikiendelea nyuma ya pazia hata kupelekea zahma ile iliyofanywa na mangi Sina dhidi ya wamachame. Ngamini Ndesserua (kaka yake Shangali) ndiyo alikuwa amejitangaza mtawala wa Machame wakati huo na watu kadha wa kadha wakawa wameambatana naye. Haifahamiki kwa uhakika nyakati lakini baada ya kifo cha mangi Ndesserua (inakadiriwa miaka ya 1879-1880) inaonekana ni watu fulani wa karibu na marehemu ndiyo waliyofahamu yaliyojiri (wanatajwa kuwa ni Nasua, Karawa, na Meenda ambao walikuwa ni ndugu waliokuwa karibu sana na mangi Ndesserua). Siri ilipikwa muda mrefu kuepuka watu kufahamu kwamba mtawala wao hayupo, lakini hata hivyo ni kwa sababu za kiusalama pia. Ilidaiwa vilevile (ni vigumu kuthibitisha hili lakini kama walivyodai hao wapambe akina Nasua) kuwa mangi Ndesserua siku za mwisho mwisho za uhai alitoa wosia kwamba mtoto wake mdogo Shangali ndiyo amrithi kwenye utawala na siyo Ngamini (ambaye ndiyo alikuwa mtoto mkubwa kwa wakati huo). Hii ndiyo iliyopelekea zengwe na mazingira tata yaliyokuja kuijiri Machame baadaye. Shangali alikuwa ni mdogo sana wakati huo (kama miaka 3 hivi) asiyeweza kabisa kupewa chochote kile cha maana kufanya katika ufalme. Hii timu ya akina Nasua baada ya kufahamu kwamba mangi Ndesserua amefariki walijikita kwenye propaganda na hadaa kwa umma kwamba mangi bado ni mgonjwa na akipona ana mambo muhimu ya kuwaeleza wananchi hivyo waendelee kutambika kumtakia heri na kupona haraka. Walipika mazingira hata ya kuleta waganga kutoka Mombasa ili ionekane kwamba kuna jitihada za kumpatia tiba wakati ilikuwa ni geresha na usanii. Hizi propaganda ziliendelea muda mrefu (inasemekana kama miaka 3 hivi) ingawa kuna dalili kwamba mangi Sina alifahamu mapema kilichotokea (inasemekana Nasua alikula yamini naye kumsaidia itakapofika wakati Shangali ana umri wa kuweza kukabidhiwa nchi). Walijitahidi kuvuta muda ili ifike kipindi cha kuweza kumtangaza Shangali kuwa ni mrithi wa mangi Ndesserua. Hata hivyo hali tata ilizidi kujiri kwenye nchi. Manung'uniko, majungu, uzushi, na hofu vilizidi kutawala kwenye jamii baada ya kupita muda mrefu bila mangi Ndesserua kuonekana kwenye 'public' kama walivyozoea miaka ya nyuma.

Hizo njama zilionekana kugomba mwamba. Kutokana na mazingira yalivyokuwa yakiendelea, moja kwa moja mtoto mkubwa wa mangi Ndesserua, Ngamini, alihisi kuna zengwe linaloendelea. Alijitosa na kutangaza kwamba sasa yeye ndiyo atakuwa akishughulikia mambo yote ya utawala wa nchi. Kutokana na jamii kuwa 'desparate', wengi walifarijika na kuambatana naye, ingawa wengine kwa kujua hatari ya mangi Ndesserua walihofia kujidhihirisha kuwa upande wake, ikiwa kweli bado mangi Ndesserua alikuwa hai. Hata hivyo, Ngamini kwa bahati mbaya hakujuwa kwamba mahasimu wake walishajipanga siku nyingi na alijiingiza kwenye mtego mbaya. Hii timu ilimpiga mkwara Ngamini kwamba alichokifanya ni uhaini na hawataweza kumtetea dhidi ya hasira za baba yake atakapopona. Ila kutokana na shinikizo la hali ilivyokuwa na jinsi ambavyo Ngamini alihisi kuwa safari zao hao jamaa (hasa Nasua) kuelekea Kibosho hazikuwa zinaelewekaeleweka vizuri, aliamua lolote na liwe lakini nchi haitaweza kuachiliwa iendelee hali ilivyo. Kuna uwezekano mkubwa hii ilikuwa ni miaka ya 1884, kabla ya mauaji yale ya kupangwa na mangi Sina hayajatekelezwa mwaka 1886. Cha kushangaza ni kwamba, wakati wakibosho wamekuja Machame kupiga ukunga kwamba mangi Sina amefariki, akina Nasua ndiyo walikuwa wa kwanza kuzipigia upambe na kuhamasisha kwamba hicho kilio kinawahusu sana wamachame na ni muhimu Ngamini kama kiongozi wa Machame aende kushughulikia mambo ya kisiasa Kibosho na kuhakikisha usalama kule. Kwa kuonekana kuafiki kile wakibosho walichokipendekeza, walihimiza pia watu wengine hasa maarufu waende Kibosho ili kushughulikia mazishi ya mangi Sina na kusaidia kumtawalisha mwingine.

Hata hivyo Ngamini alizipokea hizo taarifa kwa machale makubwa. Alihisi liko jambo. Inasemekana alipinga kabisa hilo wazo la wamachame kwenda Kibosho na alisema kwamba ili kudhihirisha kwamba ni fedheha kufanya hicho kitu atalala kwenye njia ya kuendea Kibosho akidai kwamba atakaye mruka kwenda Kibosho hatarudi. Akina Nasua waliendesha kampeni za upambe na fitina wakichochea watu kwamba Ngamini ni mtu mwoga asiyefaa kupewa hata usaidizi wa kushauri ukoo wake mwenyewe. Watu wengi waliingia kwenye mtego huu. Wengi hasa wale wa ukoo wa mangi wa Machame walimruka Ngamini wakaenda Kibosho. Wengine hasa majemedari hawakuthubutu kufanya hivyo bali waliingia porini na kutokea njia za kwendea Kibosho. Cha ajabu katika mshikemshike hiyo watu hawakugundua kwamba akina Nasua waliingia mitini na wala hawakwenda Kibosho. Inaonyesha dhahiri kulikuwa kweli na zengwe lililopikwa. Jitihada zao za kumshawishi Ngamini aende Kibosho zilishindwa vibaya. Hata hivyo yaliyojiri kule Kibosho yalisaidia sana kupunguza nguvu ya Machame na hasa Ngamini, maana majemedari wengi waliuawa na hata watu maarufu wa ukoo wa mangi wa Machame nao waliteketea. Kulikuwa na kilio kikubwa sana Machame. Ngamini alitangaza msiba mkubwa kwenye nchi na kutoa amri kwamba atakayejenga nyumba na mlango wake ukaelekea Kibosho kufa na afe, maana anaieletea nchi laana. Hii siri ya kilichojiri ilikuja kugundulika baadaye ingawa akina Nasua waliendelea kujiweka mbali na usaliti huo. Mashambulizi hayo ya 1886 yalimpa mwanya mangi Sina kufanya mashumbulizi baadaye Machame akilazimisha kwamba Ngamini akane kujitangaza kuwa mtawala wa Machame. Hiyo hata hivyo haikuwezekana kirahisi. Ilichukua mpaka 1890, baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe akina Nasua walivyovianzisha dhidi ya Ngamini wakipiga propaganda nyingi kwamba Ndesserua alitaka Shangali atawale kwa hiyo Ngamini amechukua nchi kwa nguvu. Mmishionari kutoka ufaransa, aliyeitwa Alexander Le Roy aliyefika Machame 1890, alitoa taarifa jinsi Machame ilivyokuwa imegeuka kuwa jaa la machafuko, nchi ikiwa inanuka uharibifu. Askari wa Nasua na wale wa mangi Sina waliungana dhidi ya waliomuunga mkono Ngamini na hata kufanya Machame iwe imekatika vipande vipande. Ni mwaka huo wa 1890 ndiyo Ngamini aliamua kuweka silaha chini, na kwa ushauri wa kapteni Johannes aliyekuwa bomani kule Moshi, aliamua yeye na familia yake kuhamia Moshi ili nchi itulie na kumwachia Shangali atawale Machame.

Ninakiri kwamba nimeandika kwa ufupi ufupi sana (briefly) na kuruka baadhi ya details. Mambo hayo ya wamachame na wakibosho, n.k. siku hizi yamekwisha. Ni mambo ya zamani za kale. Ninakubali lakini kwamba wako wazee ambao bado yanawasumbua. Maendeleo na maingiliano siku hizi yamefanya mitazamo ya watu ibadilike na watu siku hizi wanaoana bila kujali historia za zamani za kale. Hata hivyo, kufahamu historia ya kule unakokwenda kuoa/kuolewa ni msaada mkubwa.
 
Nitashukuru kwa darasa waungwana.
Ahsante sana Rev Kishoka...Na pia tunaomba Mnyika ambaye anagombea huko Ubungo uliko...Ajitahidi kuja hapa na kukusikiliza ili atowe ufafanuzi ili na mimi nielemishwe.
Once again nashukuru sana na ninategemea nafasii hii itatumika kutuelemisha.

wamachame,wakibosho pamoja na warombo sio wachagga
 
wamachame,wakibosho pamoja na warombo sio wachagga

Makupa kama jina lako lilivyo unajulikana kuwa wewe ni mmarangu wa mwika, mamba au kokirie na kwa asili wamarangu mnajulikana kuwa wanawake ni malaya wa kutupwa na mna dharau za kipumbavu sana hata kama ni maskini kama mbwa na ndiyo maana hauwezi kuwatambua wenzako kama wachaga shame on you! Litle Thinker.
 
Jamani@jones and others..mi ni mchagga. Ila nachangia tu kwamba,hata Wahaya walipata kuwa na historia inayofanana na hii. Mambo ya chiefdom,vita n.k.
 
Mleta mada na wachangiaji wote nashukuru kuweka akili sawa.
Niliambiwa historia ya mwanamke wa kimachame kuitwa mpalestina ni pale waume zao walipoenda huko kibosho kwenye msiba na kuuliwa pale kwenye bonde la mto weruweru.
Sasa raia sijui wa-somalia+ethiopia(walikuwa wanyenyekevu) walikuja kuomba hifadhi hapo machame kwa kujitumikisha, ndipo wakaoa wanawake wenye mali zao walizoachiwa(inasemakana mwanaume wa machame ananywele kama zao halafu ndo chanzo cha uislamu huko machame).
Na niliambiwa kwenye mto weruweru(nilikwenda kipindi nasoma umbwe) kumebaki mafuvu ya watu kwenye mapango(yapo kule kwenye maporomoko ya maji).~~~
 
Mleta mada na wachangiaji wote nashukuru kuweka akili sawa.
Niliambiwa historia ya mwanamke wa kimachame kuitwa mpalestina ni pale waume zao walipoenda huko kibosho kwenye msiba na kuuliwa pale kwenye bonde la mto weruweru.
Sasa raia sijui wa-somalia+ethiopia(walikuwa wanyenyekevu) walikuja kuomba hifadhi hapo machame kwa kujitumikisha, ndipo wakaoa wanawake wenye mali zao walizoachiwa(inasemakana mwanaume wa machame ananywele kama zao halafu ndo chanzo cha uislamu huko machame).
Na niliambiwa kwenye mto weruweru(nilikwenda kipindi nasoma umbwe) kumebaki mafuvu ya watu kwenye mapango(yapo kule kwenye maporomoko ya maji).~~~


Ninakiri kwamba kuna hizi habari watu wanazizungumzia, lakini ni vigumu kuzithibitisha. Zinaonekana kama ni uvumi hivi kwa kiasi kikubwa. Ujasiri wa wanawake wa kimachame umekuwa mara kwa mara ukihusianishwa na mauaji yale yaliyotokea miaka ile ya 1886 ambapo wanaume kadha wa kadha wa kimachame waliuliwa kutokana na fitina ile iliyosukwa na mangi Sina kule Kibosho. Hii inadaiwa ilisababisha nyumba/familia nyingi za Machame, wanawake wabaki na kuwa ndiyo walezi wa familia. Hiyo ikafanya wanawake wawe na maamuzi makubwa katika mambo ya nyumba/familia. Kwa hiyo inasemekana kuwa ndiyo ilijenga utamaduni huo Machame wa wanawake kuwa ni jasiri na hata wenye kufanya maamuzi magumu katika jamii. Hata hivyo, nadharia hii inaweza kuwa na shida kidogo ikiwa historia inayohusiana na Machame itaangaliwa kwa umakini zaidi. Sababu zenyewe ni kama zifuatazo:
  1. Pamoja na kwamba ni kweli wanaume wengi wa kimachame waliuliwa kule Kibosho, lakini ukumbuke kwamba katika tawala zote za uchagani Machame ndiyo ilikuwa na idadi kubwa sana ya watu. Hans Meyer katika kitabu chake, 'Ostafrikanische Gletscherfahrten' cha mwaka 1890 anasema kwamba Machame ndiko aligundua kwamba kuna idadi kubwa sana ya askari (warriors) kuliko sehemu zingine zote za uchagani (na hiyo ilikuwa ni kwenye miaka ya 1888-1889 baada ya mauaji yale ya 1886). Kwa hiyo, kwamba wanaume walikuwa ni wachache sana kiasi cha wanawake kuchukua uongozi katika familia na jamii, inaweza kuwa vigumu kulithibitisha hilo.
  2. Siyo wanaume tu ambao ndiyo walipata zahma hizo kule Machame. Hata wanawake nao walipitia matatizo hayo sana. Kihistoria, kulikuwa na matukio makubwa mawili yaliyotokea Machame na kusababisha wanawake wengi wa Kimachame kuondoka na hivyo kupunguza sana idadi ya wanawake kule Machame. Tukio la kwanza lilikuwa katika miaka ya 1878-1879. Katika kipindi hiki, mtawala katili sana wa Machame, mangi Ndesserua alikuwa mgonjwa mahututi lakini bado akiendelea kutawala na kutoa maamuzi na maongozo mbalimbali katika utawala. Alikuwa ameshaanza kuadimika kwenye 'public' lakini akiwa na wasiwasi mwingi wa hatima ya utawala wake na matakwa yake ya urithi atakapofariki. Inasemekana kwamba katika mkanganyiko huo wa kimawazo, alishauriana na wandani wake (akina Nasua) kuwashawishi waarusha (au wamasai) wavamie Machame na kuchukua watakachoweza kuchukua ili kuifanya nchi isitulie mahasimu wake wakajipanga kumdhuru na kuleta shari za kisiasa. Inadaiwa kwamba kulikuwa na mashambulizi makubwa mawili yaliyofanywa na waarusha kule Machame wakati Ndesserua akiwa bado hai, ingawa walikuwa wakimhamisha baada ya kudokezwa ni wapi waarusha watashambulia. Waarusha walihakikisha wamefilisi karibu ng'ombe wote na kuchukua mateka wanawake na mabinti wengi wa kimachame (Katika kitabu cha 'Mountain farmers, moral economies of land and agricultural development in Arusha na Meru, by T. Spear, anahabarisha jinsi kapteni Johannes alivyokwenda kufanya vita na waarusha na wameru mwaka 1897-99 akisaidiwa na askari wa kichaga ambapo askari wa kimachame walimlalamikia kwamba wanahaki ya kupora ng'ombe na kurudisha nyumbani wanawake wote walioporwa Machame na waarusha miaka ya nyuma).
  3. Kana kwamba tukio hilo la 1877-79 halikutosha, vilipoibuka vita vya wenyewe kwa wenyewe kule Machame mwaka 1888 vikidaiwa ni vita vya kumng'oa Ngamini, mangi Ngamini mwenyewe aliomba msaada wa marafiki wa baba yake, yaani mangi Mandara wa Moshi na mangi Fumba wa Kilema, waje kumsaidia dhidi ya askari wa Machame waliokuwa wakiongozwa na ndugu yake wa ukoo, yaani Nasua, pamoja na askari wa mangi Sina. Kama anavyosimulia mmishionari Alexander Le Roy (Au Kilimanjaro), cha ajabu ni kwamba wale askari wa mangi Mandara walipofika Machame (labda kwa kugundua kwamba mangi Sina pia alikuwa amepeleka askari wengi kule dhidi ya Ngamini), waliamua kubeba wanawake na mabinti, wakapora walichoweza kupora (ng'ombe chache zilizokuwepo, mbuzi, n.k.) wakatokomea navyo porini, wakimtelekeza Ngamini. Mmishionari Le Roy anasimulia kwamba alipofika Machame ule mwaka 1890 alikuta kuna masikitiko makubwa ya mkasa huo uliowapata, wa kuporwa mali chache zilizobaki na wakina mama na mabinti kutoroshwa na askari wa Moshi.
Kwa hiyo, wanaume na wanawake kule Machame wote walipatwa na mikasa hiyo iliyosababisha kupunguka. Hivyo basi, nadharia hiyo ya wanawake wa kimachame hata kufikia kuitwa wapalestina kwa sababu zinazodaiwa, inaonekana haina nguvu sana kihistoria. Ukumbuke pia kwamba, Machame kihistoria ni utawala ambao umekuwa na changamoto sana za kisiasa kule uchagani. Historia ya Machame ni historia ya kisiasa na wamachame wanaonekana wamekuwa hivyo, siyo wanaume wala wanawake. Ilifikia wakati mpaka msomi na mtafiti Dr. Susan Rogers aliyefanya utafiti wa chama cha ushirika na tawala kule Kilimanjaro miaka 1950 alihusisha Machame na migogoro mingi ya kisiasa iliyokuwa ikitokea kule uchagani. Kwa mfano, mwaka 1931 mgogoro mkubwa wa kahawa na migomo kule uchagani ilitokea Machame ambapo ofisi ya ushirika ilichomwa moto na mwenyekiti kulazimishwa kujiuzulu. Mgogoro huo ulihamia Kibosho ambapo nao ulisababisha mikahawa kung'olewa na migomo kwa wakulima. Hata hivyo aligundua kuwa kinara wa mgomo kule Kibosho alikuwa ni afisa wa Kilimo ambaye alitokea Machame akahamishiwa kule kikazi. Mgomo huu ulienea kwa kasi mpaka Vunjo na kuwa mgomo mkubwa uliowahi kutokea uchagani. Pamoja na hayo yote, Dr. Rogers alitanabaisha kwamba kuna uwezekano mkubwa wachaga wengine waliupokea huo mgomo kwa nia njema bila kuelewa ajenda iliyokuwa ikiendelea kule Machame (nyuma ya pazia). Kwani aliyeanzisha na kuchochea mgomo kule Machame alikuwa ni bwana anayeitwa Daudi Ngamini (kwa hiyo hapo unaweza kujumlisha 1 na 2 ukapata jibu hasa ni nini msukumo unaweza kuwa nyuma ya uchochezi huo). Pia kupanda na kushuka kwa mangi mkuu uchagani imesadikiwa kuhusishwa na nguvu ya Machame katika historia ya kisiasa kule uchagani. Kumbukumbu zinaonyesha kwamba kwenye uchaguzi wa mangi mkuu mwaka 1951, Thomas Marealle alipata zaidi ya 70% ya kura zote zikiwa zimetoka Hai (kuzidi hata zilizompigia kule alikotoka, yaani Vunjo). Watu wengi wa jimbo la Hai (alikotoka mangi Abdieli Shangali) walimkataa mangi Abdiel kwa kuwa walimtuhumu kutumiwa na wakoloni dhidi ya wazawa. Hata hivyo, baada ya Thomas Marealle kuupata umangi mkuu inaonyesha alishindwa kuliona hili akafanya Marangu kuwa ndiyo himaya ya umangi mkuu. Kilichotokea ni kwamba, mwaka 1957 aliamriwa na vijana wanaharakati kule uchagani wakiongozwa na Solomon Eliufoo (huyu ni Mmachame mpwa wake na mangi Abdieli Shangali) ajiuzulu au maandamano yafanyike uchagani kote ili ufanyike uchaguzi tena. Hata hivyo, uchaguzi haukuepukika na mangi Thomas Marealle akang'olewa kwenye uongozi kule uchagani na Solomon Eliufoo akatangazwa kuwa raisi wa kwanza wa Kilimanjaro mwaka 1960.

Kwa hiyo, wamachame wamekuwa ni wachaga waliochangamka kisiasa na wanaharakati, iwe wanaume au wanawake. Ndiyo mila, desturi, na historia yao ilivyo. Hili hata hivyo linaweza likatafsiriwa tofauti na wachaga wengine ambao wataona (hasa wanawake wa kimachame) kuwa wajanja zaidi na waliochangamka kuliko wengine. Ni kweli tofauti na wachaga wengine wanawake wa kimachame wanaonekana ni wenye kujiamini zaidi na wajasiri. Lakini hii inawezekana ni kwa sababu za kihistoria zaidi kwa ujumla wake na siyo matukio moja moja huko nyuma.
 
thnkx ndugu kwa historia yangu nzuri yenye kuvutia, imenifanya nijitambue vema na vizaz vya wazee wetu kulewalikotoka...maswali
1-kabla ya yote hayo kutokea na kupelekea wachaga kutengana kwa tofauti zao. Je! Ni lugha ipi ya pamoja uliyokuwa inatumika, ukiacha kwa sasa kuna kimachame, kimarangu, kirombo, nk?
2-Napenda kufahamu koo cha machame, kunakoo ngapi!? Ukizi orodhesha chache kubwa kabisa itakuwa vema.
 
Hahaha nimepata elimu yakutosha ndio maana nyumba za machame na kibosho milango haitazamani,hii bifu noma.sasa mbona mi ni mmachame ninamchumba kibosho itakuwaje!? nisaidieni wana JF
Wewe ndo yule Exavel Lyimo unazunguziwa na Jason Borne katika yalio mpata mwakyembe na mark mwandosya?
 
Back
Top Bottom