Historia ya Vita ya Kagera (Part 2)

Matanga

JF-Expert Member
Nov 13, 2019
2,281
3,973
Majeshi ya Libya yaelemewa na JWTZ nchini Uganda.

#Sehemu #ya - 20.

Toleo lililopita tuliona jinsi askari wa Libya walivyo elemewa nchini Uganda na namna wengine walivyouawa na wengine kuchukuliwa mateka.

Hatimaye Iddi Amin alipoona kuwa Libya haiwezi kumuokoa katika kuzama kwake,alizigeukia nchi nyingine za Kiarabu kuomba msaada wa fedha na mali ili kujiokoa na utawala wake ambao ni dhahiri jahazi lilikuwa linazama.

Kiongozi wa Libya Muammar Gaddafi hakujua uwezo wa kijeshi iliokuwa nayo Tanzania katika medani ya kivita.
Askari wake walipata tabu kubwa walipokuwa Uganda.

Jarida la "Africa Research Bulletin" la Aprili 1—30, 1979 linasema katika mapigano ya siku mbili ya Entebbe,kiasi cha askari 400 wa Libya waliuawa na wengine zaidi ya 40 walichukuliwa mateka.

Tanzania pia ilikamata kiasi kikubwa cha silaha nzito za Libya na ndege kadhaa za kijeshi za Jeshi la Uganda,” linasema.
Kitabu cha "War in Uganda" kinasema mradi wa Muammar Gaddafi nchini Uganda uligeuka kuwa ni maafa kwa askari wake.

Makumi ya askari wa Libya waliojeruhiwa walipelekwa katika Hospitali ya Mulago mjini Kampala na baadaye waliondolewa nchini humo wakitokea kwenye Uwanja wa Ndege wa Nakasongola.
Silaha kali za kivita zikiwamo zile za kisasa zikaangukia mikononi mwa askari wa JWTZ.

Askari wapatao 60 wa Libya waliotekwa na askari wa JWTZ, kwa mujibu wa kitabu cha Iddi Amin "Speaks an Annotated Selection of His Speeches," walipelekwa Tanzania.

Hata hivyo waliachiwa baada ya miezi mitatu na waliobakia waliachiwa baada ya miezi tisa.

Kitabu cha "An Encyclopedic Dictionary of Conflict and Conflict Resolution" 1945-1996 cha John E. Jessup katika ukurasa wake wa 769 kinasema, “Mei 15, 1979, Libya iliilipa Tanzania Dola milioni 40 ili iwaachie mateka wa kivita wa waliokamatwa wakati wa mapigano nchini Uganda.”

Lakini kitabu cha "War in Uganda the Legacy of Iddi Amin" katika ukurasa wake wa 122 kimeandika:

“Hadithi za kwamba Nyerere aliwauza mateka kwa Gaddafi hazina ushahidi wowote.Gaddafi hakuonekana kama anajali ikiwa mateka watarudi nyumbani au hawatarudi.

Nyerere aliahidi Libya itawapata mateka wote Hatutawauza Hatutafanya biashara ya kuuza wanadamu kwa ajili ya fedha,sisi ni maskini sana.

Tunajali sana heshima ya utu.”
Hata baada ya kuonekana dhahiri kuwa Gaddafi hakuweza kumuokoa Iddi Amin,bado Amin alizililia nchi za Kiarabu akitaka zimsaidie kupambana na Tanzania.

Katika matangazo fulani ya redio alilalama kuwa, “Tanzania na rafiki zake Wayahudi” wanapambana na Serikali ya Uganda.

Akasema:

“Huu ni wakati ambao nchi za Kiarabu zinapaswa kuisaidia Uganda kifedha na kwa mali.”
Lakini Nyerere kwa upande mwingine,alijitahidi kuhakikisha kuwa dunia haitaona kuwa haya ni mapambano ya Waafrika dhidi ya Waarabu.

Hadi kufika jioni, kikosi cha Luteni Kanali Salim Hassan Boma kikawa kimeiteka Entebbe.
Askari wa Iddi Amin walikuwa wamekwishakimbia wakiwaacha wenzao wa Libya wakipata tabu.

Asubuhi ya Jumapili ya Aprili 8, 1979 askari wa Tanzania walianza kuvinjari katika mji wa Entebbe na wakati fulani walipofika katika kanisa moja walikuta kiasi cha askari 200 wa jeshi la anga la Iddi Amin wamejikunyata,wakiwa wamevalia nguo za kiraia, wakiwa wamejiandaa kujisalimisha.

Maduka kwenye Uwanja wa Ndege wa Entebbe, yalikuwa yameshaporwa na askari wa Iddi Amin wakati wakikimbia.

Kulikuwa na ndege tisa za kivita aina ya MiG-21 ambazo kwa mujibu wa kitabu cha "Three Thousand Nights of Terror"
Askari wa Tanzania walidai kuwa hiyo ni zawadi ya vita na ndege hizo zilichukuliwa na kupelekwa Tanzania.Lakini wakati zikiwa zinatua, moja ilianguka na kumuua rubani wake.

“Watanzania sasa walikuwa wamedhibiti vita na Ikulu ya Entebbe ilikuwa imeangukia mikononi mwao.
Walikuta Ikulu ikiwa imejaa silaha na bidhaa nyingi kama redio,pombe, televisheni.

Kimeaendika kitabu cha Three Thousand Nights of Terror"

Sasa askari wa Tanzania walikuwa wanavinjari ndani ya Ikulu ya Entebbe.

Meja Jenerali David Msuguri aliwasili Ikulu ya Entebbe saa 3:30 asubuhi.

Mpango wa mwisho wa kuivamiana na kuiteka Kampala ulifanyika kwenye chumba cha chakula cha Ikulu ya Entebbe.

Batalioni ya 19 ya Brigedi ya 208 iliyokuwa chini ya Kanali Benjamin Msuya ikapewa jukumu la kuiteka Kampala ambayo sasa ilikuwa umbali wa kama kilomita 35.

Sasa huu ulikuwa ni mpango wa jeshi la nchi moja kuteka makao makuu ya nchi nyingine.

Ni historia ya kipekee sana katika Bara la Afrika, tangu mwanzo wa vita hakuna askari hata mmoja chini ya Msuya ambaye alikuwa amepoteza maisha kwenye mapigano,na sasa alikuwa amenuia kuiteka Kampala bila kumpoteza askari wake hata mmoja.

Brigedi za 201, 207 na 208 zilijipanga kwa kazi hii muhimu.

Wakati mipango ya kuiteka Kampala ikifanyika katika Ikulu ya Entebbe, Iddi Amin naye alikuwa mjini Kampala na maofisa wa jeshi lake wakipanga namna ya kuulinda mji huo.

Mapambano makali kati ya askari wa Amin na wale wa Tanzania yalifuata,hali ya hewa ilikuwa mbaya na mvua ilikuwa ikinyesha bila kukoma,ingawa mvua ilikuwa inanyesha na askari wa JWTZ wakiwa wamelowa chapachapa, ari yao ilionekana kuwa juu sana.

Baada ya tabu yote ya mapambano ya usiku kucha kuelekea Kampala,asubuhi Msuya na kikosi chake walifika mahali wakafungua redio kusikiliza sauti ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) wakasikia taarifa kutoka Nairobi kwamba waandishi wanne wa habari,raia wawili wa Sweden na wawili wa Ujerumani Magharibi, wanaaminika kuwa wameuawa na askari wa Iddi Amin walipokuwa wakijaribu kuvuka Ziwa Victoria kwa mashua wakitokea Kenya kwenda kuandika habari za vita nchini Uganda.

Baadaye ilijulikana kuwa waandishi hao ni Arne Lemberg wa gazeti la Sweden liitwalo Expressen, Karl Bergman wa gazeti jingine la Sweden linaloitwa Svenska Bagvladet, Hans Bolinger ambaye ni mpigapicha wa shirika la habari la Gamm na Wolfgang Steins wa majarida ya Stern na Geo.

Waandishi hawa waliuawa na askari wa Amin kwa kupigwa risasi.

Walikodi mashua ndogo kutoka Bandari ya Kisumu ambayo waliitumia kuvuka ziwa,lakini walipofika upande wa Uganda wakajikuta wameangukia kwenye mikono ya askari wa Amin.

Kwa habari zaidi kujua namna mji mkuu wa Uganda Kampala ulivyotekwa na majeshi ya Tanzania pamoja na yale jeshi la uganda Tukutane tena hapa.

Itaendelea ......
 
_HISTORIA _NA _KUMBUKUMBU _YA _VITA _YA _KAGERA.

A

Wapendwa,ndugu,jamaa na marafiki zangu ,kabla sijaendelea na mfululizo wa simulizi zetu ambazo nilisitisha kuzitoa kwa takribani kipindi cha majuma mawili yaliyopita kwa sababu ambazo zilikuwa nje ya uwezo wangu

TUENDELEE NA TULIPOISHIA.

Utekaji wa kwanza wa ndege kielektroniki Duniani wafanywa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania.

#Sehemu #ya - 16.

Katika toleo lililopita tuliona wanajeshi wa Tanzania walivyopata shida sana katika mji wa Lukaya kiasi kwamba waliamua kuutangaza kuwa ni sehemu ya maafa kwa Watanzania.

Eneo la Sembabule nalo lilileta changamoto nyingine kubwa kwa askari wa JWTZ.
Katika toleo hili tutaona namna mabadiliko ya uongozi katika Brigedi ya 205 yalivyoleta tofauti kubwa na hatimaye JWTZ ikaibuka mshindi.

Katika kuipanga upya Brigedi ya 205, Brigedia Herman Lupogo aliondolewa akaingia Brigedia Muhidin Kimario.

Endelea….......

Hata baada ya Tanzania kuiteka miji ya Masaka na Mbalala,Iddi Amin alisikika katika Redio Uganda akijigamba kuwa Watanzania walikuwa wanazingirwa.
Kusikia hivyo,Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) lilianza kuchunguza taarifa hizo za kuzingirwa ambazo zilitolewa na Iddi Amin.

JWTZ liligundua kuwa ni kweli kulikuwa na kikosi kizima chini ya Kanali kilichoitwa "Tiger Regiment" kilichokuwa Mubende,katikati ya Masaka na Mbarara.

JWTZ halikuwa limeweka mpango wowote wa kukishughulikia,ila kwa kuzingatia alichosema Amin,wachambuzi wa masuala ya kijeshi wakaamini kuwa huenda kikosi hiki kilikuwa kinaelekea kusini ambako kingeanza kuwazingira Watanzania.

Brigedi ya 205 chini ya Brigedia Herman Lupogo iliamriwa kuondoka Masaka kwenda kukabiliana na kikosi hicho cha "Tiger Regiment."

Haukupita mda mrefu hadi Brigedia Herman Lupogo alipogundua kilipo kikosi hicho ambacho hadi sasa kilikuwa kimeongezewa nguvu na wapiganaji kutoka Kituo cha Mafunzo ya Kijeshi cha Kabamba na kilijichimbia eneo la Sembabule.

Vita kali ambayo ilidumu kwa wiki tatu iliaanza na majeshi ya Tanzania yalipigana kutwaa eneo moja,lakini tena wakashtukia kesho yake eneo hilo limetwaliwa tena na majeshi ya Iddi Amin.

Hata baada ya kutwaa tena eneo ambalo walinyang’anywa na askari wa Amin,wanajeshi wa Tanzania walikuwa wakikuta maiti za Watanzania katika eneo waliloliteka upya.

Baadaye wapiganaji wa Tanzania wakajikuta wakiogopa na kuvunjika moyo,vikundi na vikosi vidogo sasa vilikuwa vikikimbia wakati majeshi ya Amin yakishambulia majeshi ya Tanzania.

Katika kuipanga upya Brigedi ya 205,Brigedia Herman Lupogo aliondolewa katika kikosi hicho na akaletwa Brigedia Muhidin Kimario.

Awali Kimario alionekana ni mwanasiasa zaidi kuliko mwanajeshi,wakati mmoja alikuwa mbunge wa Moshi na kabla vita havijaanza alikuwa mkuu wa Mkoa wa Mwanza.

Alipowasili Sembabule aliikuta Brigedi ya 205 ikiwa shaghalabaghala,kiasi cha askari 20 au zaidi wa brigedi hiyo walikuwa wameuawa na wengine walikata tamaa.

Makabidhiano ya Brigedi kutoka kwa Brigedia Herman Lupogo kwenda kwa Brigedia Muhidin Kimario yalifanyika wakati brigedi ikiwa inashambuliwa vikali na askari wa Iddi Amin.

Mara moja Brigedia Muhidin Kimario aliwaita askari wake na kuwaahidi kuwa kila atakapotoa amri ya kwenda kwenye mapambano atakwenda nao bega kwa bega mstari wa mbele "front line" kupambana na maadui.

Kimario aliamua kuacha mbinu za matumizi ya vitengo vidogo vidogo katika brigedi hiyo iliyokuwa ikitumiwa na Brigedia Herman Lupogo,na badala yake akaamua kuipeleka brigedi nzima mbele kushambulia.

Mbinu ya Kimario zilizaa matunda,na ari mpya ikarudi kwa wapiganaji wa Brigedi ya 205.
Ingawa mapigano yalidumu kwa muda fulani,hatimaye "Tiger Regiment" ikaelemewa.

Katika mapigano ya mwisho ambayo katika kikosi hicho cha Iddi Amin kilikimbia,na Brigedi ya Kimario iliua askari 25 wa Amin.

Wakati wote wa mapigano ya Lukaya na Sembabule yakiendelea,Rais Nyerere alikuwa akienda Bukoba mara kwa mara kupata picha halisi ya kinachoendelea vitani badala ya kukaa ofisini na kutegemea taarifa alizokuwa akiletewa.

Baada ya ziara yake moja alirejea Dar es Salaam na hofu ya ushiriki mkubwa wa Libya katika Vita ya Kagera.

Sasa Nyerere akaona kuwa ushiriki wa moja kwa moja wa Libya katika vita ya Uganda ni uhalali tosha wa Tanzania kumchakaza Iddi Amin.

Wapiganaji waliokuwa wakikusanywa na vikundi vinavyompinga Amin havikuwa vimefikia matumaini aliyokuwa nayo Nyerere.

Kwa kukasirishwa na kitendo cha kiongozi wa Libya,Muammar Gaddafi kuliingiza jeshi lake nchini Uganda dhidi ya Tanzana,Nyerere akaiamuru JWTZ kuingia Kampala na kuuteka mjikuu huo wa Uganda.

Wakati huu silaha zaidi na wanajeshi zaidi kutoka Libya walikuwa wakiingia Uganda.
Ndege za kijeshi zilizotengenezwa Urusi, Tupelev-22, zilikuwa zikiruka kutoka uwanja wa jeshi wa Nakasongola na kwenda kurusha mabomu vilikokuwa vikosi vya Tanzania kusini mwa Uganda.

JWTZ kwa kuona ndege za Libya zikawa zinaingia Uganda mara kwa mara, ikaamua kutafuta namna ya kuziteka.

Hapo ndipo utekaji wa kwanza wa kielektroniki duniani ulifanyika.
Kabla ya hapo hakukuwahi kutokea utekaji mwingine wa aina hiyo mahali popote Duniani.

Usiku wa manane,wanajeshi wa JWTZ wakiwa Mwanza,walisubiri hadi pale walipoona kwenye rada ndege mojawapo ikielekea Entebbe upande wa Uganda,karibu na Ziwa Victoria.

Waliwasiliana na rubani wa ndege hiyo na kujitambulisha kwake kwamba wao ni waongozaji wa ndege katika Uwanja wa Entebbe na kumwonya kuwa uwanja huo wa Entebbe,unashambuliwa vikali na wanajeshi na kwa sababu hiyo haingefaa atue kwenye uwanja huo.

Wasiwasi mkubwa ulimpata rubani huyo kiasi kwamba alilazimika kuomba ushauri.Wanajeshi wa JWTZ wakamshauri kuwa uwanja wa ndege ulio karibu zaidi ni ule wa Mwanza na kwamba kwa sasa ni salama zaidi kutua kwenye uwanja huo.

Rubani alijaribu kuuliza maswali kadhaa na Wanajeshi wa JWTZ walimjibu kwa uangalifu mkubwa.

Majibu hayo na jinsi yalivyotolewa,yalimridhisha rubani huyo.
Kwa hiyo akaachana na uamuzi wake wa kwenda kutua Entebbe, akabadilisha mwelekeo akarudi kutua Mwanza.

Mara tu baada ya ndege hiyo kutua kwenye uwanja wa Mwanza ikawa tayari imezingirwa na wanajeshi wa JWTZ ambao, hata hivyo, walishangazwa sana kuona kuwa badala ya kuwa ni ndege ya Libya na yenye silaha,wakakuta ni ndege ya mizigo ya Shirika la Ndege la Ubelgiji Sabena,iliyokuwa safarini kwenda kubeba kahawa kutoka Uwanja wa Ndege wa Entebbe kupeleka Djibout.

Hakukuwa na namna ya kuiachia ndege hiyo iondoke Mwanza iendelee na safari zake kwa sababu vifaa vya kuisaidia ndege hiyo,Boeing 707 kuondoka uwanjani hapo havikuwapo uwanja wa ndege wa Mwanza.

Nyerere alipigiwa simu kuombwa ushauri na aliagiza wafanyakazi wa ndege hiyo wapelekwe Mwanza Hoteli na wapewe vyumba na mlo mzuri kadiri ilivyowezekana.

Kisha Nyerere akamwita balozi wa Ugelgiji na kumwambia kilichofanyika nin bahati mbaya na hakukuwa na lengo baya.
Kesho yake ndege ya kijeshi ilipeleka vifaa vya ndege hiyo kutoka Dar es Salaam.

Sabena iliwashwa na kuendelea na safari zake.


Itaendelea kesho sehemu ya - 17.
 
#HISTORIA #NA #KUMBUKUMBU #YA #VITA #YA #KAGERA

JWTZ yazingira miji ya Kampala na Entebbe, yasubiri amri ya kushambulia miji hiyo.

#Sehemu #ya - 17.

Jana tuliona jinsi Kiongozi wa Libya,Muammar Gaddafi alivyompa Rais Julius Nyerere uhalali wa kuingiza jeshi lake mjini Kampala baada ya Majeshi ya Libya kupigana kumsaidia Iddi Amin.

Hata hivyo,baada ya askari wa Tanzania kuizingira miji ya Entebbe na Kampala hususan katika eneo la Mpigi,Nyerere alitoa amri kwa JWTZ kusubiri kwanza mpaka hapo watakapopewa amri ya kufanya hivyo tayari kuishambulia miji ya Entebbe,pamoja na mji mkuu wa Uganda Kampala.

Baada ya mapigano ya Lukaya,eneo la katikati ya Lukaya na Kampala lilikuwa na wapiganaji wengi wa Iddi Amin na Libya waliokuwa wakikimbia mapigano.

Ndege tatu zilizobeba askari wa Libya waliojeruhiwa ziliondoka mjini Entebbe kwenda Tripoli Libya.

Wanajeshi wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) waliokuwa wanasonga mbele kuelekea mji wa Kampala walipofika eneo la Buwama walikuta basi la abiria lililokwama njiani na walipochunguza wakagundua kuwa abiria hao ni askari wa Iddi Amin waliokuwa wanakimbia.
JWTZ hawakulipua basi hilo,lakini waliwaua askari 20 wa Amin waliojaribu kuwatoroka.

Katika eneo la Mtola Maria, kwa mujibu wa "War in Uganda" askari wa Tanzania walikuta kanisa na shule,wakaona ni heri wapumzike ndani ya kanisa hilo na humo mlikuwa na kinanda.
Askari mmoja wa JWTZ aliyekuwa amechoka na kuchafuka sana matope alikitumia kinanda hicho kupiga Wimbo wa Taifa.

“Mungu Ibariki Afrika.”

Kituo kilichofuata kilikuwa ni Mpigi,kiasi cha kilomita 32 kufika mji mkuu wa Uganda Kampala.
Taarifa za kiintelijesia ziliifikia JWTZ kwamba askari wa Amin waliokuwa wamejiimarisha sana walikuwa wamejichimbia katika eneo hilo.

Kwa kuweka mikakati sawa, Jenerali David Msuguri aliamua kuwa brigedi zote mbili yaani Brigedi za 207 na 208 ziende moja kwa moja Mpigi tayari kwa mapambano na kikosi hicho cha Iddi Amini ambacho kilikuwa kimejidhatiti kwa silaha kali ili kuilinda miji ya Entebbe na Kampala,isitekwe na majeshi ya Tanzania.

Msuguri alipanga Brigedi ya 201 ifagie njia kuelekea upande wa Magharibi kudhibiti barabara na reli inayotoka Kampala kuelekea mji wa Fort Port ulioko Magharibi mwa Uganda.
Brigedi ya 201 ilipoanza kufagia njia,ilikutana na shamba la kahawa karibu na Mityana ambako askari wengine wa Libya walikuwa wameweka kambi yao.

Kabla askari wa Libya hawajajua kinachotokea, askari wa JTWZ wakawashambulia kama radi.
Ndani ya dakika chache askari zaidi ya 30 wa Libya wakawa wameuawa.
Baada ya hapo askari wa JWTZ wakaendelea kusonga mbele,lakini wakakabiliwa na changamoto nyingine.

Kwa sehemu kubwa ya barabara,askari wa Tanzania walikuwa wakitembea kwenye matope kiasi cha mabuti yao kuzama kabisa na walikuwa wamelowa chapachapa kutokana na mvua iliyokuwa ikinyesha mfululizo.
Kadiri walivyokuwa wakisonga mbele,ndivyo walivyokuwa wakikutana na vikundi vya askari wa Iddi Amin.

Sasa kwao ilikuwa ni kuua tu askari wa Amin kadiri walivyokutana nao. Waliendelea pia kuteka vifaru,mizinga midogo na mikubwa,magari mbalimbali ya kijeshi,hususan Land Rover na mabasi ya jeshi,ilimradi walinyakua chochote cha Majeshi ya Amin walichokitia machoni.

Kupitia darubini za kijeshi, JWTZ waliona gari aina ya Mercedes Benz ikiingia Mpigi na baadaye kusimama eneo hilo.
Askari wa Tanzania wakajua huyo alikuwa Iddi Amin amefika eneo hilo akiwa katika gari hilo.

Baadaye askari wa Tanzania wakawa na hakika kuwa huyo alikuwa ni Iddi Amin kwa sababu baadaye siku hiyo,Redio Uganda ilitangaza kuwa Rais wa Uganda alikuwa anahutubia mkutano wa hadhara eneo la Mpigi.

Hata baada ya kujua kuwa aliyefika eneo hilo ni Iddi Amin na kwamba wangeweza kumtia mikononi,askari wa Tanzania waliamua wasimfanye chochote.
Walimwacha hadi alipomaliza kuhutubia akajiondokea zake.

Makamanda wa JWTZ waliokuwa mstari wa mbele walikubaliana kuwa wasimuue hata kama fursa ya kufanya hivyo ingepatikana.

Sababu ya uamuzi huo ni kwamba ikiwa Amin angeuawa,huenda nafasi yake ingechukuliwa na mtu mwingine na hivyo kuwanyima askari wa Tanzania fursa ya kuishuhudia Kampala ikiangukia mikononi mwa Tanzania chini ya utawala wa Nduli Iddi Amini mwenyewe.

Hatimaye askari wa Tanzania walipoingia Mpigi,walikuta mji huo mdogo ukiwa tayari umekimbiwa na watu na uporaji ulikuwa wa kiwango cha juu sana
Askari wa Amin walichukua chochote walichoweza kubeba na kisha kukimbilia Kampala.

Sasa Iddi Amin alikuwa katika hali ngumu kuliko wakati mwingine wowote katika maisha yake tangu alipoipindua Serikali ya Dk Milton Obote miaka minane iliyopita.
Mawasiliano ya barabara na reli kutoka Kampala kwenda Fort Port sasa yakawa tayari yameshakatwa.

Njia pekee ya kutoka Kampala kwenda Fort Port ikabaki kuwa ni helikopta, lakini marubani wengi wa jeshi la anga la Uganda nao tayari walikuwa wameshakimbia kazini.

Kutoka sehemu zilizoinuka za Mpigi,sasa askari wa Tanzania wangeweza kuishambulia kwa urahisi miji ya Entebbe na Kampala mji mkuu wa taifa la Uganda.
Jeshi la Uganda sasa lilikuwa limeshachanganyikiwa huku wapiganaji na maofisa wake wakiwa katika hali ya hofu kubwa iliyowasababisha kukimbia ovyo huku na huko.

Kama ni mchezo wa karata,basi Iddi Amin alitumia vibaya karata alizopewa na rafiki yake, Muammar Gaddafi wa Libya.

Rais Nyerere, akizungumzia tishio la Gaddafi la kumuondoa Uganda, alisema "Pamoja na kwamba (Libya) wanaongeza uzito katika vita,hawawezi kubadilisha msimamo wa Tanzania. Amin atabaki yuleyule mshenzi,muuaji,haaminiki"

" Ila sasa najua atavimba kichwa zaidi kwa kujua kwamba ana nguvu na nchi tajiri nyuma yake,na nguvu hiyo sasa imetamkwa rasmi.Si ya kifichoficho tena. Amin atavimba kichwa zaidi.”
Alimalizia Nyerere kusema.

Miji mikubwa ya Uganda ambayo sasa ilikuwa imewekwa kwenye shabaha ya kutekwa ilikuwa ni Entebbe na Kampala mji mkuu wa Uganda.

Kwa wakati huo,Iddi Amin alikuwa mjini Kampala akiwahimiza makamanda wa jeshi lake waendelee kupigana vita ambayo wao walijua walielekea kabisa kushindwa.

Ingawa askari wa Libya na wale wa Amin walikuwa wanakimbia vita,bado aliamini tofauti kwamba atafaulu kuwarudisha nyuma wapiganaji wa Tanzania na kisha kuirudisha ardhi yote ya Uganda kwenye himaya yake.

Sasa askari wa Tanzania walikuwa wameizingira miji ya Kampala na Entebbe, hususan eneo la juu la Mpigi,wakisubiri amri ya kushambulia,lakini wakiwa wamejiandaa kufanya hivyo.

Rais Nyerere alituma neno la kuwaambia wasishambulie kwanza miji hiyo hadi watakapoelekezwa vinginevyo.


kwa nini Mwalimu Nyerere aliwazuia kwanza askari wake kuishambulia na kuiteka miji ya Kampala na Entebbe wakati tayari walikuwa wameshaizingira?



Itaendelea......
 
#HISTORIA #NA #KUMBUKUMBU #YA #VITA #YA #HAGERA:

Mwl Nyerere amgomea Muammar Gaddafi kusimamisha vita..

#Sehemu #ya - 18.

Katika toleo lililopita tuliona namna Rais wa Tanzania wakati huo Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alivyo zuia kwanza Jeshi la wananchi wa Tanzania JWTZ,kuitwaa miji ya Entebbe na Kampala hadi hapo watakapo amriwa vinginevyo.

Hata hivyo kiongozi wa Libya Muammar Gaddafi alituma ujumbe mzito kwa Nyerere akimtaka ayaondoe majeshi yake nchini Uganda ndani ya saa 24 vinginevyo Libya ingeingia vitani kwa nguvu zaidi ili kumsaidia Iddi Amin.

Nyerere alimjibu kwa kumwambia kama Libya wameamua kuingia vitani upande wa Amin hawawezi kubadilisha msimamo wa Tanzania.

Endelea.......

Wakati Tanzania ikiwa imejiandaa kuiteka miji ya Kampala na Entebbe,rafiki mkubwa wa Iddi Amin, Kanali Muammar Gaddafi alijaribu kumtisha Rais Julius Nyerere kwa kumwambia ayaondoe majeshi yake nchini Uganda ndani ya saa 24.

Alhamisi ya Machi 29, 1979 Rais Nyerere alilitangazia Taifa kuwa Libya imeitaka Tanzania iyaondoe majeshi yake nchini Uganda katika muda wa saa 24 la sivyo itaingia vitani kikamilifu kumsaidia Amin.

Akizungumza na wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam katika Ukumbi wa Diamond Jubilee,Mwalimu Nyerere alisema:

“Jumamosi hii iliyopita Kiongozi wa Libya,Kanali Gaddafi alimtuma mjumbe wake kuniletea risala.

Na risala hiyo inasema hivi;

NUKUU

"Tangu mgogoro umeanza baina ya Tanzania na Uganda tumejitahidi sana kusuluhisha,lakini sasa baada ya uchunguzi wa muda mrefu,tunaamini Watanzania ndio wachokozi"

“Watanzania ndio waliomvamia Amin,walioivamia Uganda na kwamba vita vinavyoendelea ndani ya Uganda sasa ni vita vya Watanzania wanaoipiga Uganda na wala hakuna Waganda ndani yake."

" Kwa hiyo inasema risala hiyo naiomba Tanzania itoe majeshi yake nchini Uganda na tunataka majibu katika muda wa saa 24."

Mwalimu Nyerere aliendelea kusema;

“Sasa napenda kutoa majibu niliyompelekea Kanali Gaddafi. Nimemwambia balozi wake ampelekee.

“Nimesema, vita hivi vimeanza Oktoba 1978. Vilianzishwa na Amin kwa kuivamia Tanzania na kuchukua eneo lake na kuitangazia Dunia kwamba eneo hilo sasa ni sehemu ya Uganda na kwamba kitendo hicho kilikuwa kinatimiza shabaha ambayo Amin alikuwa ametangaza tangu mwaka 1971."

“…Na usuluhishi ulianza wakati uleule na sisi tulikuwa tayari kukubali usuluhishi.
Na masharti ya usuluhishi tuliyatamka,tukasema kwanza Afrika ikitambue kitendo hicho cha Amin kuivamia,Tanzania kuwa ni kibaya,ni kitendo cha uvamizi.

“Akemewe huyo kusudi kesho na keshokutwa akijaribu kitendo hicho tena ajue atakemewa.
Ushahidi wa kumkemea mvamizi uwepo.
Pili, aahidi na akane kwamba hataki sehemu yoyote ya Tanzania.
Na tatu, aahidi kulipa fidia kwa uharibifu alioufanya.

“Nitaeleza kwamba haya mawili ya mwisho yangekuwa hayana maana, mtu mwenyewe hana dhamana,lakini lile la kwanza ni la muhimu."

“Nilimweleza balozi kuwa yangetokea tungesikilizana na tungeafikiana,lakini hayakutokea.

Lakini yeye Amin akaendelea kututishia kuwa si tu sehemu aliyoikalia, lakini anajiandaa kukalia sehemu nyingine zaidi za Tanzania."

“Tukaona ushahidi kuwa kweli anajiandaa tukaamua kumpiga tena.
Tukaamrisha apigwe na ndivyo vita hivyo vinaendelea hadi sasa."

“Kwa hiyo nikamwambia balozi amwambie ndugu yetu Gaddafi kuwa kama vita hivi vilikuwa halali wakati vinapigwa katika ardhi ya Tanzania,haviwezi kugeuka na kuwa haramu wakati vinapigwa katika ardhi ya Uganda,ni vita vilevile.

“Na kwamba vita tunavyopigana sisi ni vita vya usalama wa nchi yetu na hatukusudii kumtoa Amin.
Ni uongo kuwa tunataka kumtoa,tumeishi naye miaka minane tunataka kuwa na hakika kuwa anajua kuwa vita si lele-mama.

"Kuwa vita si mchezo,si jambo la kuingia katika nchi ya watu halafu unakwenda unasema uliichukua kwa dakika 25."

“Ajue hivyo tunataka ajue kuwa vita si lelemama.
Vita si mchezo akishajua hilo,mandhali tuliishi naye miaka minane, tuko tayari kuishi naye miaka mingine minane."

“…Ndugu Gaddafi alishaniletea ujumbe,na siku hiyo ukarudiwa ujumbe ule,ukarudiwa siku ya Jumamosi,kwamba tumwamini Gaddafi."
" Kwamba yeye anachukua dhamana kuwa Uganda haitaishambulia tena Tanzania,dhamana hiyo anachukua Gaddafi.

“Nilimwambia ndugu balozi amweleze ndugu Gaddafi ugumu wetu sisi kukubali dhamana hiyo nilieleza sababu mbili."

“Sababu ya kwanza, Amin haaminiki,nikamwambia balozi amuulize ndugu Gaddafi yeye anamwamini?

"Sema mimi namuuliza yeye (Gaddafi) anamwamini Amin?
Anaweza kuchukua msahafu akasema kwa jina la "Allah" namwamini Amin, Anaweza?

“Hakuna mtu mwenye akili anaweza kumwamini Amin. Yeye Gaddafi anamwamini, Kwa nini ananiomba mimi nimwamini?

"Kesho na keshokutwa atamgeuka huyo na urafiki uliopo baina ya Uganda na Libya kesho utageuka kuwa uhasama."

“Nitamuuliza nani kuhusu usalama wa nchi yangu?

Nitamwendea nani kumuuliza wakati huo Amin amekwisha mgeuka Gaddafi?

“Nikamwambia balozi, ndugu balozi, mimi nimefurahi sana tangu mwanzo wakati nilipokuwa naupokea ujumbe wa Libya kujaribu kusuruhisha ugomvi baina yetu na Uganda,lakini yalikuwa yanatokea maneno kuwa mpo ndani ya Uganda mnapigana bega kwa bega na Iddi Amin"

“Sisi tumekataa kutangaza habari hii,tumekataa kuipokea rasmi na kuitangaza,kwa nini?

Kusudi muendelee na shughuli za usuruhishi…

“Pili, huyo Amin ni mkorofi huyo,sitaki amani naye,tunataka ajifunze kuwa vita si lele-mama.

" Akishajifunza tutakuwa na amani baina ya Tanzania na Uganda,lakini hawezi kujifunza ikiwa anajua kwamba mali ya Libya iko nyuma yake."

“Hayo ni majibu kwa ufupi niliyompelekea ndugu yangu Gaddafi,na leo amerudisha ya kwake."

" Amesema tutoe majeshi yetu Uganda,na kama hatukufanya hivyo nchi yake itatoa msaada kwa Uganda."

“Lakini wakiamua kuwa wanamsaidia Amin,pamoja na kwamba wanaongeza uzito katika vita,hawawezi kubadilisha msimamo wa Tanzania.

Amin atabaki yuleyule mshenzi,muuaji,haaminiki."

“Ila sasa najua atavimba kichwa zaidi kwa kujua kwamba ana nguvu na nchi tajiri nyuma yake. Na nguvu hiyo sasa imetamkwa rasmi."

“Kwa hiyo hatari kwetu itakuwa ni kubwa zaidi,si inakuwa ndogo.
Na kwa hiyo tutajifunza zaidi kumkabili. Lakini tunamkabili Amin,nataka ndugu zangu wa Libya wajue hivyo.

"Hatuna ugomvi na Libya sisi tunapigana na Amin,hatupigani na Libya."

“Lakini usalama wa Tanzania ni dhamana ya Watanzania,utalindwa na Watanzania,siwezi kumwomba mtu mwingine nimkabidhi usalama wa nchi yangu nitaendelea kupambana na wote wanaohujumu usalama huo…."

MWISHO WA NUKUU YA NYERERE.

Inaendelea sehemu ya 19.
 
#HISTORIA #NA #KUMBUKUMBU #YA #VITA #YA #KAGERA:


Mashambulizi yaingia katika jiji la Entebbe.

#Sehemu #ya - 19.

Katika toleo lililopita tuliona namna Rais Julius Nyerere alivyolihutubia Taifa kuhusu tishio la Kiongozi wa Libya,Muammar Gaddafi akimtaka aondoe majeshi yake Uganda ndani ya saa 24 la sivyo ataungana na Amin kuipiga Tanzania.

Nyerere alimjibu kuwa Tanzania imeishi na Iddi Amin kwa miaka minane na kwamba inataka kumuonyesha kuwa vita si lelemama na akishajua hilo, mandhali tuliishi naye miaka minane,tuko tayari kuishi naye miaka mingine minane.

Siku nne baada ya Muammar Gaddafi kumwambia Rais Nyerere aondoe majeshi yake nchini Uganda ndani ya saa 24 la sivyo Libya itaingia vitani moja kwa moja kumsaidia Iddi Amin,ndege ya kijeshi ya Libya aina ya Tupolev T-22 ilipaa kutoka Uwanja wa Jeshi wa Nakasongola kwenda kupiga mabomu Tanzania.

Kwa mujibu wa kitabu cha "War in Uganda, The Legacy of Iddi Amin" ndege hiyo ilikuwa ikiruka futi chache tu juu ya Ziwa Victoria kukwepa kuonekana kwenye rada za Tanzania.

Nia yake ilikuwa ni kupiga mabomu matanki ya kuhifadhia mafuta yaliyopo Mwanza.
Lakini rubani aliwahi kudondosha mabomu hayo ambayo yalianguka kwenye Kisiwa cha Saanane kilichopo ndani ya Ziwa Victoria.

"Jarida la Summary of World Broadcasts Non-Arab Africa" liliripoti kwamba “Ndege ya Libya ya ‘Tupolev-22’ iliyotumwa na Libya kwenda Uganda kumsaidia Iddi Amin,jana saa 12:25 jioni ilirusha mabomu matano katika mji wa Mwanza eneo la Butimba katika Kisiwa cha Saanane.”

"Jarida la Daily Report: People’s Republic of China liliandika kuwa;

“Katika tukio hilo mtu mmoja alipata majeraha kichwani na mikononi ... vyanzo vya habari za kijeshi vinasema mabomu hayo yalikusudiwa kupigwa kwenye matanki ya hifadhi ya mafuta mjini Mwanza.”

Taarifa nyingine zilisema majeruhi pekee katika shambulio hilo alikuwa mfanyakazi wa hifadhi ya kisiwa hicho,swala sita waliuawa pamoja na ndege kadhaa.

Tanzania ilijibu mapigo siku mbili baadaye,ndege za Tanzania zilipaa kutoka Mwanza na kwenda kupiga mabomu katika miji ya Kampala,Jinja na Tororo.

Kwa mujibu wa "Gazeti la "Xinhua Weekly," Aprili 2, 1979 ndege za Jeshi la Tanzania ziliupiga mabomu mji wa Jinja ambao ni wa pili kwa ukubwa na mji wa viwanda nchini Uganda,kiasi cha kilomita 70 Kaskazini mwa mji mkuu wa Kampala.

Katika mji wa Jinja,rubani wa Tanzania alifanikiwa kuipiga bomu Benki ya Maendeleo ya Libya nchini Uganda.

Amin alikuwa mjini Jinja wakati mji huo ukishambuliwa.
Hata hivyo,shambulizi hilo halikudumu kwa zaidi ya sekunde 10.

Kitendo cha ndege ya Tanzania kufanikiwa kulenga shabaha na kuitwanga Benki ya Maendeleo ya Uganda-Libya kiliwashangaza sana askari wa Amin kiasi cha kuwafanya waamini kuwa Tanzania ilikuwa na silaha kali.

Ndege zote za Tanzania zilirejea salama baada ya kufanya mashambulizi na siku mbili baadaye zikafanya shambulio jingine ndani ya Uganda.

Safari hii uwanja wa ndege wa Entebbe ulishambuliwa, lengo likiwa ni kuuharibu ili ndege za Libya zisiweze kutua.

Kutoka kwenye miinuko ya Mpigi,Watanzania waliweza kuona mji wa Kampala kwa upande wa Kaskazini na Entebbe kwa upande wa Mashariki.

Ndege za Libya zilionekana zikitua na kupaa na idadi kubwa ya askari wa Amin na wale wa Libya walikuwa uwanja wa ndege wa Entebbe.

Makamanda wa vita wa JWTZ waliona kuwa ikiwa wangeutwaa mji wa Kampala kabla ya ule wa Entebbe,askari wa Tanzania wangekabiliwa na jeshi kubwa la adui nyuma yao.

Jenerali Msuguri aliamua waende kwanza Entebbe na kazi hiyo akakabidhiwa Brigedia Mwita Marwa wa Brigedi ya 208.

Kwa siku tatu mfululizo yalikuwa yakirushwa mabomu mawili au matatu kuelekea Entebbe.

Wakati bomu moja lilipodondoka eneo la maegesho ya magari la Ikulu ya Entebbe,Amin akawa na uhakika kuwa wanajeshi wa Tanzania walikuwa wamemkaribia.

Mara moja akatoka ndani ya Ikulu,akarukia kwenye helikopta iliyokuwa nje na kupaa kuelekea Kampala.

Jumanne ya Aprili 3, 1979 matangazo ya Redio Uganda yakasema;

“Amin yuko mapumzikoni na ni mwenye furaha mjini Jinja.”

Taarifa ikaendelea kusema, “Rais wa maisha wa Uganda amepuuza taarifa kwamba alikimbia na amewahakikishia wananchi wa Uganda kwamba yeye kama mshindi wa himaya ya Uingereza amejiandaa kufa akiitetea nchi yake.”

Ilipofika Aprili 6 mashambulizi ya Tanzania katika mji wa Entebbe yakaongezeka.
Asubuhi iliyofuata Brigedi ya 208 ilikuwa inasonga mbele.

Miongoni mwa mashambulizi waliyofanya siku hiyo ni kulipua gari la jeshi aina ya Land Rover lililokuwa na askari wanane wa Libya wakielekea Mpigi.

Siku hiyo ndege ya mizigo ya Libya, C-130, ikatua uwanja wa Entebbe saa nne asubuhi kujaribu kuwaokoa askari wa Libya walionasa.

Askari 30 wa Libya walikazana kuingia ndani ya ndege hiyo kabla haijageuka na kuanza kuondoka.
Lakini askari wa Tanzania walikuwa wamesha likaribia eneo hilo na kuilipua.
Ndege hiyo ilishika moto ikawateketeza askari wote wa Libya waliokuwa ndani yake.

Mashambulizi kutoka kwa askari wa Tanzania yalipoongezeka,askari wa Libya waliobaki Entebbe walizidi kuchanganyikiwa.

Waliingiwa na wazo la kukimbilia Kampala lakini hawakujua njia watakayoifuata kufika huko
Entebbe ilipozingirwa vya kutosha,askari wa Libya waliobaki nao waliamua kutafuta njia ya kukimbilia Kampala.

Malori kadhaa yaliyowabeba askari wa Libya yakisindikizwa na magari mawili ya deraya yalianza safari kuelekea Kampala.

Umbali wa kilomita nane kutoka Entebbe,Luteni Kanali Salim Hassan Boma aliwasubiri.

Aliwagawa wapiganaji wake wakae pande mbili za barabara.

Msafara uliowabeba askari wa Libya ulipofika eneo walikojificha askari wa JWTZ, askari wa Tanzania walikaa kimya na bila kujigusa.

Makamanda wa Libya walisemezana kwa muda mfupi,kisha askari waliokuwa kwenye magari hayo wakaanza kumimina risasi pande zote mbili za barabara.

Hazikuwagusa askari wa Tanzania,lakini wakiwa na wasiwasi bado waliruhusu gari moja likatangulia.

Walipoona hakuna kinachoendelea, makamanda wa askari wa Libya wakaruhusu magari mengine yaliyojaa askari wao yapite.

Ndipo Luteni Kanali Salim Hassan Boma akatoa amri ya kufanya shambulio. Magari yote ya kivita ya Libya yakashambuliwa na kuteketea kwa moto hata kabla hawajaweza kujibu shambulizi lolote.

Harufu ya kuungua kwa nyama za miili ya binadamu ikatawala eneo lote hilo la uwanja wa mapigano.
Ndani ya dakika 10 askari wote 65 wa Libya wakawa wameuliwa katika mapigano hayo.

Je,
Unataka kujua nini kiliendelea zaidi katika mapigano ya kuigombania miji ya Entebbe na Kampala baina ya Majeshi ya Tanzania JWTZ na yale ya Nduli Iddi Amin kuhakikisha kila upande utahakikisha inabaki chini ya himaya yake!?

Endelea kufuatilia
 
Mtanisamehe maana nimeanzia namba 20 kimakosa nikaja kuendelea na namba 16 maana tuliishia namba 15 tuendelee kufurahia simulizi hii ya kweli iliyoiweka nchi yetu kwenye historia yenye kuheshimika Sana
 
Back
Top Bottom