Historia Ya Vita Vya majimaji. | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Historia Ya Vita Vya majimaji.

Discussion in 'Jukwaa la Historia' started by X-PASTER, Jun 16, 2010.

 1. X-PASTER

  X-PASTER Moderator

  #1
  Jun 16, 2010
  Joined: Feb 12, 2007
  Messages: 11,651
  Likes Received: 105
  Trophy Points: 160
  Historia Ya Vita Vya majimaji.

  MTU yeyote anayeijua vizuri historia ya Tanzania na akabahatika kufika Mjini Songea Mkoani Ruvuma asipotembelea makumbusho ya vita vya majimaji yaliyopo katika eneo la Mahenge Mjini Songea atakuwa amefanya kosa ambalo anaweza kulijutia katika maisha yake.

  Watu wengi kutoka nje ya Mkoa wa Ruvuma na hata wengine kutoka nje ya nchi wametembelea eneo hili maarufu katika historia ya Tanzania hasa katika harakati ambazo zilifanywa na babu zetu kupambana na wakoloni waliokuwa wanawatawala kinyama.

  Makumbusho ya mashujaa wa vita vya Majimaji Songea ni eneo ambalo limehifadhiwa vizuri na Serikali ili kuwawezesha watu mbalimbali kutembelea na kujifunza mambo mengi na ukibahatika kufika katika eneo hili utakuta kumbukumbu nyingi za kale ambazo ni kivutio kikubwa kiutalii na kiutamaduni.

  Mara unapofika katika makumbusho hayo unaongozwa na mtu maalum ambaye anafahamu vizuri makumbusho hayo ya mashujaa wa vita vya Majimaji ambaye pia ni Mwenyekiti wa kamati ya utekelezaji katika Baraza la makumbusho ya Majimaji Mzee Said Mteso.

  Mwenyekiti huyo wa Baraza la Makumbusho ya Mashujaa wa vita vya Majimaji anasema eneo hilo la Makumbusho lina historia tatu ambazo ni historia ya vita vya Majimaji, historia ya ujio wa Wangoni kutoka Afrika ya Kusini na historia ya uhuru wa Tanganyika .

  Akizungumzia historia ya vita vya Majimaji Mzee Mteso anasema vita hivyo vililenga kumkomboa Mtanzania kutoka mikononi mwa Wajerumani na kuwa si sahihi kuwa vita hiyo ilikuwa na uwezo wa kugeuza risasi kuwa maji bali ililenga kuwapa nguvu wapiganaji ili waweze kujitolea hata ikibidi kupoteza maisha yao ili mradi tu waweze kujikomboa.

  Mzee Mteso ambaye alizaliwa mwaka 1948 Songea Mkoani Ruvuma anasema vita vya Majimaji ilianza mwaka 1905 na ilianzia Kilwa na siyo Songea na kwamba hata hivyo ingawa vita hiyo ilipiganwa katika kanda ya Kusini lakini Songea inazungumziwa zaidi kwa sababu watu wote waliokamatwa walinyongwa na kuzikwa katika kaburi moja watu 68 na kaburi hilo lipo katika eneo la Mashujaa Wilayani Songea Mkoani Ruvuma.

  "Maeneo mengine ya kusini ingawa vita hivyo vilifanyika hakuna eneo lolote linaloonyesha kumbukumbu ya vita hivyo na hata mashujaa wote walizikwa Songea"
  Sisi Songea tumeweka kumbukumbu zote muhimu za historia ya vita vya Majimaji ambapo watu wengi kutoka ndani na nje ya nchi wanafika kuangalia makumbusho hayo ambayo yamekuwa ni kivutio kikubwa cha utalii" anasema Mzee Mseto.

  Anasema Songea ndiyo ilikuwa sehemu ya kwanza ya kupima uwezo wa dawa ya majimaji kabla ya kwenda katika maeneo mengine ya kusini ambako vita hiyo ilianza kupiganwa katika eneo la Kilwa Kivinje huko Utete ikiongozwa na Kinjekitile na wenzake na walifanikiwa kuchoma boma za wajerumani baada ya kwenda huko usiku na siyo mchana.

  Dawa hiyo ya Majimaji iliaminika kuwa inafaa baada ya kujaribiwa katika eneo la Songea na wajumbe wote waliokuwa wanakwenda kuchukua ile dawa ambapo Kinjekitile Ngwale alikuwa ni mwanzilishi wa dawa hiyo pamoja na vita yenyewe ya Majimaji.

  Katika makumbusho hayo ya vita vya Majimaji kuna kumbukumbu ya silaha mbalimbali walizotumia Mashujaa wa Majimaji kupigana na mkoloni ukiwemo mkuki ambao ulipatikana nyumbani kwa Chifu Songea Mbano wa kabila la Wangoni ambaye alikuwa anautumia mwenyewe katika mapigano hayo.

  Anasema Wangoni walikuwa wanapigana kwa kutumia mikuki, marungu, na vinjenje wakati wakoloni walikuwa wanapigana kwa kutumia bunduki. Katika Makumbusho hayo pia kuna barangumu ambalo walikuwa wanalitumia katika kuwasiliana katika matukio mbalimbali yakiwemo hatari, mikutano au sherehe.
  Katika Makumbusho hayo kuna vitu mbalimbali vya kale vikiwemo mafiga ya mawe, kiko, majembe ya kale.

  Pia chungu kikubwa kilichokuwa kinatumika kuhifadhia mazao kama vile karanga ambacho kilifukiwa kabla ya mwaka 1905 na kiligunduliwa mwaka 1980 katika eneo la Mputa baada ya mkulima mmoja kukiona wakati akilima shamba lake. Kwa mshangao mkubwa mkulima yule alikigonga chungu hicho na hakikupasuka na alipokiangalia akakuta karanga nyingi zimo ndani,hata hivyo inaaminika chungu hicho kilikuwa kinatumiwa na mke wa Chifu Mputa wa Songea.

  Pia ukiingia ndani ya Makumbusho hayo ya vita vya Majimaji pia kuna picha mbalimbali ambazo zinaonyesha wapigania uhuru wa kwanza akiwemo Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Marehemu Mzee Rashidi Kawawa, Picha za tukio la Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kuwa nchi moja ya Tanzania na Machifu wa kingoni na vitu vingine.

  Akizungumza namna Machifu hao walivyonyongwa na wakoloni Mzee Mteso anasema awali walikamatwa machifu 48 na baadaye walikamatwa wengine ambapo idadi kamili ya machifu walionyongwa na kuzikwa katika kaburi moja ilifikia 68 ambapo walinyongwa kwa kamba na kuwapitisha katika shimo ambalo baada ya kukanyagwa walitumbukia katika shimo na kuuawa.

  "Kati ya watu walionyongwa mmoja alikuwa ni Babu ya Babu yangu"
  Mzee Mseto anasema kuwa, kuna umuhimu kwa Watanzania kutembelea Makumbusho ya vita vya Majimaji Mjini Songea ili wajifunze mambo mbalimbali ya kale na kuona kumbukumbu nyingi za kale ambazo ni sehemu ya utalii wa kiutamaduni.

  Kwa upande wake Mzee Joakimu Ngonyani ambaye ni miongoni mwa wazee wanaounda Baraza la Makumbusho ya vita vya Majimaji, mila na desturi akizungumzia namna Mashujaa hao walivyonyongwa na Wajerumani anazitaja sababu zilizowafanya Mashujaa hao kunyongwa kuwa ni pamoja na kukataa kutawaliwa na Wajerumani.
  Ngonyani anabainisha kuwa Wazee hao kabla ya kufika kwa wakoloni hao tayari walikuwa na utawala wao wa machifu wa asili ,ndio maana waliamua kuwashambulia Wajerumani kwa mikuki na mishale wakidanganywa na Omari Kinjala kwa kutumia dawa ya majimaji ambayo haikuwasaidia.

  "Unajua Wajerumani walikuwa wakatili sana na babu zetu hawakupenda kutawaliwa kwa sababu walipigwa viboko kazini, mashambani, barabarani au wakichelewa kulipa kodi, walifanyishwa kazi bila mishahara au kulipwa ujira kidogo sana " anasema Mzee Ngonyani.

  Anaongeza kuwa, Wajerumani hao walibebwa kwenye machera na babu zetu walipokwenda safarini na kwamba wazee wetu walikuwa hawana uhuru wa kujieleza na kujitetea hivyo ili kujitawala waliamua kupigana na Wajerumani hao ili kujenga himaya yao.

  Akibainisha namna walivyonyongwa wazee hao ambao wanastahili kuitwa Mashujaa, Mzee Ngonyani anasema unyongaji ulifanyika Februari 27, mwaka 1906, Machi 20,1906 na Aprili 12,1906 katika eneo la Mahenge mjini Songea na kuzikwa kaburi moja katika eneo ambalo linaitwa Mashujaa

  "Siku ya kunyongwa watu wengine wengi walikusanywa na wakasimamishwa mahali ambapo waliweza kuwaona wanyongaji na waliokuwa wakinyongwa ili waone ukatili ule, ili wasiige ujeuri wa wazee wao kwani na wao wanaweza kunyongwa " alibainisha Mzee Ngonyani.

  Anafafanua kuwa, wanyongwaji hao waliletwa katika eneo hilo wakiwa wamefungwa kila mmoja mnyororo mkubwa na katika eneo hilo walilonyongwa hadi leo kuna nguzo kubwa mbili zilizosimikwa pande mbili wakati huo.
  Anabainisha zaidi kuwa juu ya nguzo hizo kulipigiliwa nguzo imara iliyofungwa vitanzi vinne na kwamba chini ya nguzo hizo kulikuwa na ubao uliowekwa juu ya nguzo fupi nne.

  "Basi waliwafunga wafungwa wanne toka mnyororo ule mkubwa na wakasimamisha juu ya ule ubao uliotegeshwa, wakawapachika zile kamba zilizoningi'nia kila mmoja na kamba yake huku wakiwa wamefungwa kamba mikono yote miwili ili wasiweze kujimudu na nyuso zao zilikuwa zimefungwa vitambaa vyekundu ili wasiweze kuona" anasema Ngonyani.

  Ili kuwasitiri utupu wao, Mzee Ngonyani anasema wanyongaji hao walifunga shuka ndogo ili kusitiri utupu wao na kuongeza kuwa askari alifyatua ubao na ndipo miili ya mashujaa hao ikiwa inaning'inia kwenye vitanzi mpaka walipokata roho.

  "Baada ya Mashujaa hao kukata roho katika mateso makali, wauaji hao waliiondoa miili hiyo na kuiweka kando katika sehemu hiyo waliyowanyongea na kwa sababu waliwanyonga watu wanne kwa wakati mmoja na kufanya siku ya kwanza yaani Februari, 27, 1906 kunyonga watu 40" alisema.

  Hata hivyo Mzee Ngonyani anasema Mashujaa walinyongwa vitanzini walikuwa 68, waliokufa gerezani kabla ya kunyongwa walikuwa wawili, waliopigwa risasi kuonyesha nguvu ya risasi walikuwa watano na kufanya jumla Mashujaa 75 kuuawa kikatili.

  Akizungumzia namna Mashujaa hao walivyozikwa katika kaburi moja, Mzee Ngonyani anasema kaburi kubwa lilichimbwa na wafungwa kwa mwezi mmoja katika eneo la Mashujaa mjini Songea ambako ndipo limetengwa eneo la kumbukumbu ya Mashujaa wa vita vya Majimaji na hata gereza lililojengwa na Wajerumani kwa kutumia miti lipo hadi leo.

  Anabainisha zaidi kuwa maiti za Mashujaa walionyongwa kwa siku moja ililazwa katika kaburi hilo kiubavu bila sanda na kufukiwa kidogo ili kutoa nafasi kwa maiti wengine siku nyingine ili waje kulazwa juu ya wale wa kwanza na kufukia tena kidogo mpaka wote walionyongwa walipozikwa katika kaburi moja.
  Hata hivyo anasema Chifu wa Wangoni, Nduna Songea Mbano hakuzikwa katika kaburi hilo moja na wenzake kwa kuwa yeye aliuawa siku ya peke yake baada ya wengine wote kunyongwa.

  Anasema hali hiyo ilitokea kwa sababu Chifu Songea Mbano alikuwa ndiyo Jemedari Mkuu wa Jeshi la Wangoni na alikuwa ni hodari sana asiyeogopa lolote kwa hiyo Wajerumani walitaka abakie ili wamtumie kwa malengo yao.

  "Yeye Chifu Songea alidai na yeye anyongwe kama walivyonyongwa ndugu zake, basi alinyongwa na wajerumani ambao waliondoka na kichwa chake wakiwa wamekiweka ndani ya kasha kwenda Ujerumani ambako hakijarudi hadi leo na kiwiliwili chake kuzikwa katika kaburi la peke yake" anasema.

  Eneo hilo la Mashujaa wa Vita vya Majimaji limebaki kuwa kivutio kikubwa cha wageni kutoka mbali kuja kujionee na kujifunza mambo mbalimbali lakini wazawa wanapafanya kuwa sehemu ya matambiko ya kimila hasa pale wanapokumbwa na majanga mbalimbali

  Wakati umefika kwa eneo hilo kuwa sehemu ya utalii wa kihistoria na kiutamaduni na ni muhimu Makumbusho ya Taifa ikapaangalia kwa mtazamo yakinifu, kwa sababu ni eneo mojawapo linaloweza kuchangia mapato ya kimkoa na kitaifa kutokana na wageni watakao patembelea eneo hilo na kwa faida ya vizazi vijavyo.

   
 2. Ngambo Ngali

  Ngambo Ngali JF-Expert Member

  #2
  Jun 16, 2010
  Joined: Apr 17, 2009
  Messages: 3,194
  Likes Received: 134
  Trophy Points: 160
  X-paster asante sana kwa angalizo, naomba iwe utaratibu wetu kuwasimulia watoto vitu kama hivi na kuwapeleka ili vizazi na vizazi vijue haya. Tatizo letu ni kwenda sehemu ambazo zina tija kidogo wote twapenda kwenda k.m. twanga, akudo Fm Academia kwenye clubs lakini hatukumbuki kwenda kwenye makumbusho ambamo historia na utamaduni wetu upo.

  Ukija mashuleni Historia sahihi ya nchi hii utaipata kidogo St Government shule zingine Academic hamna kitu kama hicho ukimuuliza mtoto mkwawa au Kimweri ni nani anashangaa.
   
 3. X-PASTER

  X-PASTER Moderator

  #3
  Jun 16, 2010
  Joined: Feb 12, 2007
  Messages: 11,651
  Likes Received: 105
  Trophy Points: 160
  Usemayo ni kweli kabisa ndugu yangu...!

  Alafu Wajerumani walikuwa na tabia ya kuchukua vichwa vya Machifu, sielewi ikma yake ilikuwa ni nin
  i!
   
 4. Ngambo Ngali

  Ngambo Ngali JF-Expert Member

  #4
  Jun 16, 2010
  Joined: Apr 17, 2009
  Messages: 3,194
  Likes Received: 134
  Trophy Points: 160
  Vizazi hivyo vilikuwa na akili na walikuwa na ushujaa, kuchukua kichwa cha shujaa wewe ni shujaa x2. Huoni wamasai bila kichwa ya simba hupati binti wewe sio shujaa
   
 5. FirstLady1

  FirstLady1 JF-Expert Member

  #5
  Jun 17, 2010
  Joined: Jul 29, 2009
  Messages: 16,575
  Likes Received: 541
  Trophy Points: 280
  kwani wamasai mpaka leo ni mpaka utoe kichwa cha simba?? basi mbuga zetu za wanyama simba wote wataisha
   
 6. FirstLady1

  FirstLady1 JF-Expert Member

  #6
  Jun 17, 2010
  Joined: Jul 29, 2009
  Messages: 16,575
  Likes Received: 541
  Trophy Points: 280
  Asante sana X-Paster umenikumbusha mbali sana na History za mababu zetu..sidhani kama sasa kuna mashujaa wa namna hii...Siku hizo zilikuwa ni za hatari kubwa na za kujitoa sana ...
   
 7. M

  Mama Mtalika New Member

  #7
  Jun 17, 2010
  Joined: Jun 1, 2009
  Messages: 3
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  Asante kwa Kutujuza na kutukumbusha kuhusu Historia ya Vita Vya Maji Maji.
  Pia naomba kusahihisha kidogo kuhusu Jina la Mwenyekiti wa kamati ya utekelezaji katika Baraza la makumbusho ya Majimaji. Huyu anaitwa Mzee Said MKESSO. (Babu yangu)

  Kwa sasa Makumbusho ya Vita vya Majimaji ipo chini ya Baraza la Makumbusho ya Taifa.

  Asante.

  Mama Mtalika
   
 8. Ngambo Ngali

  Ngambo Ngali JF-Expert Member

  #8
  Jun 17, 2010
  Joined: Apr 17, 2009
  Messages: 3,194
  Likes Received: 134
  Trophy Points: 160
  Imekwisha hiyo baada ya wamasai kumaliza simba katika kutafuta ndito. Si unajua jinsi wamasai walivyo warembo?
   
 9. Ami

  Ami JF-Expert Member

  #9
  Jun 17, 2010
  Joined: Apr 29, 2010
  Messages: 1,858
  Likes Received: 1
  Trophy Points: 135
  Hii Historia pamoja na urefu wake ni potofu na imeficha mengi.
  Wajerumani walionja joto ya jiwe kutoka kwa mashujaa wa kiislamu ambao ndio pekee ambao hawakuwa tayari kutawaliwa na makafiri wa kikoloni.Haya maji si maji tu bali ni maji ya zam zam kutoka Makka waislamu wanakohiji kila mwaka.
  Leo ati tunazungumzia kufaidika na utalii kutokana na ugaidi wa mjerumani kwa waislamu! badala ya kuwataka wakomeshe ugaidi wao wanaouendeleza huko Afghanistan na kuwaomba radhi waislamu.
   
 10. Companero

  Companero Platinum Member

  #10
  Jun 17, 2010
  Joined: Jul 12, 2008
  Messages: 5,475
  Likes Received: 168
  Trophy Points: 160
  Kuhusu kukata vichwa vya machifu rejea dondoo hii:

  The first case is that of Waiyaki wa Hinga who resisted British military occupation in the 19th Century. When the British captured him they removed him from his region, that is, the base of his power. In the realm of military tactics this is quite understandable. Even killing him is logically explainable. But they didn't just kill him – they buried him alive with his head facing the bowels of the earth. Why such a strange form of burial? Ngugi's explanation underscores the fact that this was an act of cultural imperialism aimed at making a statement against the cultures of those who were resisting colonialism. To Ngugi, the British applied this cultural-cum-military tactic in "opposition to the Gikuyu burial rites' requirement that the body face Mount Kenya, the dwelling place of the Supreme Deity." It is indeed an old tactic that even features in Biblical narratives of conquests whereby the vanquished's names, bearing their God, were changed. "Similarly", he notes, "in Xhosaland, the present-day Eastern Cape of South Africa, the British captured King Hintsa of the Xhosa resistance and decapitated him, taking his head to the British Museum, just as they had done with the decapitated head of the Maori King of New Zealand."

  Yes, if I may add, the Germans did the same with Mtwa Mkwawa of Uhehe – who successfully defeated them in the famous battle of Lugalo – and went on to hang in public the consortium of leaders who were inspired my Kinjeketile Ngwale of Ngarambe to resist German occupation in the legendary Maji Maji War (1905 – 1907). "The relationship between Africa and Europe", as Ngugi aptly observes, "is well represented by the fate of these figures" since a "colonial act – indeed, any act in the context of conquest and domination – is both a practice of power, intended to pacify a populace, and a symbolic act, a performance of power intended to produce docile minds." This relationship is characterized by what the author refers to as dismemberment and defines as an "act of absolute social engineering" that occurred in two stages. In the first stage "the African personhood was divided into two halves: the continent and its diaspora." Then, in the second stage, the infamous Berlin Conference of 1884-1885 "literally fragmented and reconstituted Africa into British, French, Portuguese, German, Belgian, and Spanish Africa." This tragedy and what followed afterwards is what Ngugi's Re-membering Africa aims to undo:

  The result was an additional dismemberment of diasporic African, who was now separated not only from his continent and his labour but also from his very sovereign being. The subsequent colonial plantations on the African continent has led to the same result: division of the African from his land, body, and mind…Whereas before he was his own subject, now he is subject to another (Ngugi wa Thiong'o 2009: 3 - 4).
   
 11. Ngambo Ngali

  Ngambo Ngali JF-Expert Member

  #11
  Jun 17, 2010
  Joined: Apr 17, 2009
  Messages: 3,194
  Likes Received: 134
  Trophy Points: 160
  Duh, tutafika kweli? Wajerumani walipigana na wakazi wa kusini kwa tanzania ya sasa, warefu, wafupi, weupe, weusi, wangoni, wangindo, nk ukitaja vita ya maji maji sidhani kama in afiliation ya dini au kabila. surely i dont think so. Kama waislamu walikuwepo issue ilikuwa ni kuwaondoa wajerumani na ukatili wao ndo maana hata wapagani walipigana vita hiyo. tusiwe sentimental
   
 12. X-PASTER

  X-PASTER Moderator

  #12
  Jun 17, 2010
  Joined: Feb 12, 2007
  Messages: 11,651
  Likes Received: 105
  Trophy Points: 160
  Ahsante Mama Mtalika kwa masahihisho.
   
 13. B

  Bukoba kwetu. Member

  #13
  Jan 29, 2016
  Joined: Jan 17, 2016
  Messages: 20
  Likes Received: 2
  Trophy Points: 5
  Hata wenye chokochoko zenu na huku mpo? Udini mpaka lin???
   
 14. HARUFU

  HARUFU Platinum Member

  #14
  Jan 29, 2016
  Joined: Jan 21, 2014
  Messages: 24,574
  Likes Received: 27,272
  Trophy Points: 280
  Inasikitisha sana.

  Wazee wa miaka hiyo walijitolea kupigania Uhuru kitu ambacho si rahisi hata kidogo.

  Kujitolea kwao kupambana na Mkoloni ndiko kulikotuwekea sisi kwenye mazingira ya Uhuru tulionao.

  Chifu Songea alionesha msimamo wa hali ya juu sana.

  Kitu ambacho Viongozi wetu wa kileo hawawezi.

  Sio kitu rahisi
   
 15. Nyanidume

  Nyanidume JF-Expert Member

  #15
  Feb 6, 2016
  Joined: Oct 24, 2012
  Messages: 2,156
  Likes Received: 379
  Trophy Points: 180
  Tuwaenzi mashujaa wetu!
   
 16. jingalao

  jingalao JF-Expert Member

  #16
  Dec 8, 2017
  Joined: Oct 12, 2011
  Messages: 19,263
  Likes Received: 10,448
  Trophy Points: 280
  Huyu jamaa huwa hakumbukwi kwenye historia ya Uhuru
   
 17. Nnangale

  Nnangale JF-Expert Member

  #17
  Dec 9, 2017
  Joined: Jul 20, 2013
  Messages: 1,230
  Likes Received: 302
  Trophy Points: 180
  viongozi kama kafulila kutishwa kufukuzwa chama machozi debe zima wakati mikono anayo na vyeti vyake anavyo, ndio tuliobaki nao matumbo yao ni bora kuliko kila kitu,wako wengi, ni watafuta fursa tu.
   
Loading...