Historia ya Mradi wa Ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo

FbUser

JF-Expert Member
Oct 22, 2014
342
250
Mradi huu ulibuniwa na serikali chini ya ‘Bagamoyo Special Economic Zone Project’ mwaka 2004; mpango kabambe wa ujenzi wa sekta mpya ya viwanda. Japan ndiyo ilitusaidia kwenye hili. Mradi huu uliitwa ‘Tanzania-Mini Tiger 2020’ ndani ya Wizara ya Viwanda.

“Tulisikia kwamba Mamlaka ya Bandari (TPA) ilibuni mpango wa miaka 20 wa uendelezwaji wa bandari nchiniu (The Tanzania Port Development Master Plan 2009 – 2028).

“Mpango huo ulipendekeza Bandari ya Bagamoyo ijengwe na iwe tayari mwaka 2021/2022 kujaza nafasi baada ya Bandari ya Dar es Salaam kufikia ukomo wa kuweza kuongezewa uwezo.

“Kwa hiyo mambo mawili ya msingi hapa ni kwamba; kwanza, Mradi wa Ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo tuliubuni sisi wenyewe, ulikuwa sehemu ya mipango yetu ya muda mrefu na haukujengwa kwa msukumo wa Wachina.

“Pili, huu si mradi wa bandari pekee, bali ni mradi wa ukanda wa kiuchumi unaoendana na mji wa viwanda.

“Mwaka 2009, TPA kupitia Kampuni ya Hamburg Port Consulting ya Ujerumani, ilifanya upembuzi yakinifu wa Mradi wa Bandari ya Bagamoyo na kuona una manufaa ukitekelezwa.

“Mwaka 2011, Wizara ya Viwanda na Biashara, kupitia CowiConsult, nayo ilifanya upembuzi yakinifu wa Mradi wa Bagamoyo Special Economic Zone (BSEZ), kwa kufungamanishwa na Mradi wa Bandari ya Bagamoyo.

“Mipango yote hii ilikuwa ni yetu wenyewe, na tulijiridhisha kama nchi kwamba Bandari ya Bagamoyo tunaihitaji na tukaiweka kwenye Mpango wa Pili wa Miaka Mitano wa Maendeleo ya Taifa kama mradi wa taifa wa kielelezo.

“Mwaka 2013 na 2014, Kampuni ya China Merchants Ports Limited, ikiungana na Mamlaka/Mfuko wa Uwekezaji wa Oman (OIA), waliomba kuwekeza BSEZ na Bandari ya Bagamoyo.

“Baadaye kidogo, Korea Kusini nao, kupitia taasisi yao ya Science and Technology Policy Institute (STEPI) ilikamilisha upembuzi yakinifu wa kuwekeza katika kujenga na kuendeleza Bagamoyo High Technology Park kwa kushirikiana na EPZA na COSTECH.

“Kwa hiyo hoja nyingine ya kuzingatia hapa ni kwamba Bagamoyo si uwekezaji wa Wachina pekee kama inavyodhaniwa. Yapo mataifa mengine. Oman wanaweka fedha yao nyingi hapa. Korea Kusini nao wanaweka pesa na maarifa yao.

“Kama nilivyoeleza hapo awali, kwa mujibu wa Mpango wa Pili wa Miaka Mitano wa Maendeleo (FYDP II), BSEZ ni mradi wa taifa wa kielelezo unaotarajiwa kuvutia uwekezaji wa dola za Marekani bilioni 10!

“Utakuwa na viwanda 760 na hatimaye kutoa ajira 270,000 kwa awamu ya kwanza. Majadiliano ya utatu wa Tanzania, China Merchants na Oman yalikuwa yanaendelea kuelekea makubaliano na hatimaye kuingia mikataba ya uwekezaji kabla ya kusimamishwa.

“Zipo hoja kubwa tatu zinazosemwa kuhusu mradi huu: kwanza, utatutwika madeni kama Kenya na Sri Lanka, ambako Wachina walilazimika kutaifisha bandari; pili, tutaua Bandari ya Dar es Salaam; tatu, haturuhusiwi kuendeleza bandari yoyote na haturuhusiwi kutia mguu Bagamoyo kwa miaka 99!

“Hoja hizi zote si za kweli, na kwa kweli wawekezaji wa huu mradi wamekuwa wakipambana kutafuta namna ya kuzijibu bila mafanikio.

“Wawekezaji hawa, hasa wa Oman, ni mamlaka za serikali na wasingependa malumbano, hasa na Serikali ya Tanzania.

“Hoja ya kwanza, kwamba tutakopa na kujitwika deni kubwa si ya kweli, kwa kuwa kwenye mradi huu hakuna hata senti tano ya mkopo! Huu ni uwekezaji. Hakuna deni hapa, ni pesa ya kigeni inaingia kuwekezwa.

“Hoja ya pili kwamba tutaua Bandari ya Dar es Salaam haina mantiki, kwa sababu hata kabla Wachina hawajafika, ilikuwa ni ndoto na mipango ya TPA kujenga Bandari ya Bagamoyo.

“Ukisoma Mpango Kabambe wa Miaka 20 wa Uendelezwaji wa Bandari za Tanzania (The Tanzania Port Development Master Plan 2009 -2028), TPA wenyewe walitaka Bandari ya Bagamoyo iwe imejengwa ifikapo mwaka 2023. Bandari za Bagamoyo na Dar es Salaam si bandari shindani.

“Ni bandari zitakazosaidiana kuongeza shehena ya mzigo unaopita nchini. Basi! Pia Bandari ya Bagamoyo itajengwa kwa kuzingatia teknolojia ya uundwaji wa meli za kisasa (4th Generation Shipbuilding Technology Port).

“Meli hizi ambazo zitakuwa zinaongezeka kadiri miaka inavyokwenda, haziwezi kutia nanga kwenye Bandari ya Dar es Salaam. Na kama unaitazama nchi kwa miaka 50 hadi 100 ijayo, Bandari ya Dar es Salaam ina ukomo wa upanuzi. Lazima kama nchi ni muhimu kujenga bandari mpya kubwa katika ukanda huu ili kuendelea kunufaika na faida ya kijiografia.

“Hoja ya tatu kwamba Wachina wanataka tusijenge wala kuendeleza bandari nyingine yoyote kwa miaka 99 na tuwape bandari hiyo bila kutia mguu pale, si kweli. Hakuna pahala popote wawekezaji wametoa madai hayo.

“Ukweli ni kwamba kote duniani mwekezaji anapoweka fedha zake mwenyewe kwenye mradi, atataka muda wa kutengeneza faida kabla hajakukabidhi mradi. Hapa Wachina na Wa-Oman walitaka miaka 33 ya concession.

“Je, ni mingi au ni michache? Inategemea fedha iliyowekwa (dola za Marekani bilioni 10) na standard practice kwingine duniani.

“Reli ya kuunganisha UK na Ufaransa, ambayo imejengwa na sekta binafsi ina concession ya miaka 50. Kwa bandari, standard practice ni miaka 25 – 40, kutegemeana na ukubwa wa uwekezaji.

“Cha msingi kwa timu yetu ya majadiliano ni kupata financial models wa wawekezaji na kuzichambua na kuona wanaanza kupata faida baada ya muda gani.

“Na cha kutambua pia ni kwamba concession inahusu tu faida ya bandari na kwamba katika kipindi hiki cha concession bado TRA itakuwa inakusanya kodi nyingine zote husika za mizigo bandarini.

“Suala jingine la kutazama katika kufanya uamuzi ni kuangalia dunia inaelekea wapi kwenye biashara ya kimataifa. Tutake tusitake, nchi yetu inategemea biashara ya nje kimapato na China kwa sasa ndiyo kinara wa biashara ya import and exports duniani.

“Inaongoza kwa kuagiza na kuuza bidhaa nje na itaendelea kuwa kinara kwa miaka 50 ijayo. Ukifungamana nao, utashinda. Kwa mujibu mpango wa China wa Belt-and-Road-Initiative (BRI), meli kubwa za bidhaa zitakazopita katika 21st Century Maritime Silk Road kusafirisha bidhaa kati ya China, Afrika ya Kati na Kusini, zitapita katika moja ya bandari za mwambao wa Afrika Mashariki.

“Hapo ndipo patakuwa lango kuu la kupokea, kuhifadhi kwa muda na kusafirisha shehena kwa meli au usafiri wa nchi kavu. Kulingana na kudra ya kijiografia ya Tanzania ambayo inaimarishwa na uwepo wa Reli ya Kati ya Kisasa (SGR) tunayojenga pamoja na reli ya TAZARA, Bandari ya Bagamoyo ambayo itaunganishwa na reli hizo, itakuwa haina mshindani nje ya Tanzania.

“Hii ni katika dhana nzima ya ushirikiano wa maendeleo ya uchumi baina ya China na Afrika, kupitia BRI kwa muktadha wa 21st Century Maritime Silk Road.

“Mwisho, ni muhimu kutambua kwamba kuna siasa za ushindani na majirani zetu kwenye hili suala. Jirani zetu wa kaskazini wanapigana kufa au kupona mradi huu usitokee. Kwa hiyo mtaona upotoshaji mwingi wa habari kuhusu huu mradi huku baadhi ya watu wetu wakitumika bila kujijua.

“Wenzetu tayari wameanza tena kuifuata Kampuni ya China Merchant kuwashawishi wahamishie mradi kule Lamu, Kenya. Mwaka 2018 wakati wa mkutano wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC), kiongozi wao alikwenda Shenzhen, China kuwashawishi waende kwao.

“Bahati njema kwetu China Merchant walikataa na ndipo wakakutana na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa. Majuzi, Machi 25 mwaka huu, majirani zetu hawa wameandika barua tena kwa China Merchant kuomba mradi upelekwe kwao! Ni vita na mapambano.

“Namalizia kwa hadithi ndogo: mwaka 1970, wakati Dubai bado ni kamji kadogo jangwani, Wazungu waliona potential ya location yake kibiashara na wakamwendea mfalme wa wakati huo, Rashid bin Saeed Al Maktoum kupendekeza wajenge bandari na waiendeshe kwa miaka 30.

“Washauri wake wakamwambia; ‘tusiwape Wazungu bandari kwenye nchi yetu’. Sheikh akawauliza; ‘sisi tuna pesa ya kujenga?’ wakajibu; ‘hapana’, akawauliza; ‘tutaipata lini?’ wakasema; ‘hatujui’, akawauliza; ‘Dubai itaendelea kuwepo miaka 30 ijayo?’ wakajibu; ‘ndiyo’, akawauliza; ‘baada ya miaka 30 wataing’oa bandari na kuondoka nayo?’ wakajibu; ‘hapana’, akasema; ‘tuwape’.

“Wazungu wakajenga Port Rashid mwaka 1972. Miaka 30 ikapita haraka. Watu wa Dubai wakajenga uwezo wa kuendesha bandari na wakaanzisha Dubai Port World (DP World), moja ya kampuni kubwa duniani.

“Dubai sasa ni kinara wa bandari duniani. Majuzi wamechukua bandari za Senegal na Angola. Na wamejenga bandari hadi Rwanda ambapo hakuna hata bahari! Wanawasaidia Rwanda kwenye biashara ya usafirishaji.

“Mpendwa wetu Rais John Magufuli, alipenda maendeleo. Alitaka nchi yetu ipate manufaa kwenye miradi na mikataba. Namna ya kumuenzi ni kufanya makubaliano yenye tija kwa taifa katika Mradi wa Bandari ya Bagamoyo. Na hilo linawezekana kama timu yetu ya majadiliano itakuwa makini kuzingatia masilahi ya nchi.”
 

jingalao

JF-Expert Member
Oct 12, 2011
34,359
2,000
Wakazi wa asili wa Bagamoyo watasaidikaje?
Usinijibu kuhusu ajira ya vibarua.
Ni namna gani wakazi wa asili watabakia hapo na kunufaika na mradi?
So far hiyo EPZ imewamarginalize wakazi wa asili wa huko je Serikali ina mkakati gani wa makusudi wa kuwafanya wakazi wa huko matajiri na sio kusababisha wahame?
 

Kinuju

JF-Expert Member
Mar 20, 2021
2,245
2,000
Kwa nini mwaka 2009 mlisema bandari ya Dares salaam imefikia ukomo wa kuendelezwa wakati mwaka 2016 ilikuja kuendelezwa na sasa inaweza inaweza kupokea meli ya zaidi ya mita 300? Mlikuwa mnamdanganya nani kuwa bandari ya Dares salaam imefikia ukomo wa kuendelezwa?

Hao korea kusini ,china, Oman wanaoweka hapo pesa zao nyingi sana faida yao ni nini ?

Hela zao zitarudije?
 

Dezoizo52

JF-Expert Member
Jan 30, 2017
443
1,000
Moja ya bandiko lenye akili kubwa hapa jamii forum.Ndugu mwandishi sina shaka na maelezo yako hakika nakubaliana nawe,tusipo faidika sie basi vizazi vitakavyofuata.Nichukue fursa hii kuwaomba wafanya maamuzi wasicheleweshe mradi huu please.Tena kuna ule wa gesi Lindi nao uanze Mara moja
 

Gothad bonny

Member
Apr 13, 2018
38
95
Huo mkataba uwekwe wazi CCm wakati wa Mqufuri waliupinga kwa nguvu Sana ...CCM hao hao Leo wanataka tuukubari tumwamini Nan?
 

msonobali

JF-Expert Member
May 23, 2015
958
1,000
Etu Bahati nzuri majaliwa kakutana nao machi 25, kwanini hakukutana nao wakati wa Magufuri?
Acheni porojo waambieni waache tuimalishe bandari zetu Kwanza ziwe na uwezo wa ku run miaka 40 ndo wajenge ya bagamoyo na marufuku yao ya hakuna kuendeleza bandari yoyote.
 

voicer

JF-Expert Member
Jul 13, 2020
853
1,000
Hivi hata kama sio mkopo!

Je! Itawachukuwa muda gani kurudisha hizo pesa zao?

Ni nani na kwa namna gani, tutahakiki jinsi hela yao inavyorudi,ili tujuwe faida wanayopata.kama kwa uzoefu wa haraka tu kwenye migodi tumeshindwa na mali zinachotwa bure?

Sembuse mradi wa matrilioni kama huu.

Mnasema kwa haraka na kwa urahisi eti viwanda 760 vitajengwa....hivi viwanda 760 vikae eneo moja hilo sio janga la kimazingira nahatarishi kwa fukwe zetu?

Kwa nini serikali isijenge bandari kwa uwezo wake au hata kukopa, lakini iwe ni mali ya serikali,halafu hao wawekezaji wapewe eneo la uwekezaji wa hivyo viwanda EPZ?

ACHENI UKUWADI WA MABEBERU!

Wewe ,
MLETA MADA HII NI SEHEMU YA MPANGO MZIMA TOKA MSOGA.

Mko kazini.
 

UmkhontoweSizwe

JF-Expert Member
Dec 19, 2008
5,649
2,000
Bandiko zuri la kuelezea historia. Lakini tatizo ni kwamba zile hoja tatu kinzani juu ya ujenzi wa bandari umezijibu kirejareja sana. Hoja kinzani za msingi huwezi kuzijibu kwa kutumia aya fupi zenye sentensi mbili tu. Hoja kinzani zinatakiwa kutolewa ufafanuzi wa nini kitafanyika, badala ya kuzikanusha tu.
 

Samcezar

JF-Expert Member
May 18, 2014
10,537
2,000
1. Mnasema kutajengwa viwanda, swali ni je, hivi ni viwanda vya kutengeneza nini, soda na biskuti, nguo, madawa, magari au nini?!

2. Hivyo viwanda ni vya kutengeneza bidhaa za kuuzwa hapa ndani au viwanda vya kuchakata malighafi ili zisafirishwe kwenda nje ya nchi kwaajiri ya kulisha viwanda vya huko?!

3. Hizo ajira zitakazo tokana na viwanda hivi visivyojulikana ni za aina gani maana najua viwanda hutoa ajira za vibarua na si ajira za heshima na mishahara mizuri?!

4. Viongozi wadangaji wa CCM na magenge yao ya madalali wa soko huria kuchwa kutwa husema kuwa huu mradi ni kama ukombozi wa serikali kwa wananchi ila mbona ukiutazama kwa jicho la kiutaalamu na kitaaluma unaona wazi ni kuwa serikali ya ccm na viongozi wake wadangaji wamesimama kama madalali na si viongozi wazalendo wa taifa kututetea rasilimali ya raia na masilahi ya raia.

5. Kwann huu mradi unapigiwa chapuo mitandaoni na kwenye vyombo vya habari, kwan hatujajifunza mikataba iliyopita kuwa kuijadili nje ya bunge na bila kushirikisha raia ndio mwanzo mbaya?! Kwann inakuwa ni ajenda ya wachache halafu inatumika nguvu nyingi na kiburi kushawishi raia kuukubali?!

6. Hivi wewe mleta mada unajua maana ya FDI (Foreign Direct Investment)?! Unajua condition zake na implications zake katika taifa kama letu?!


Nasikitika sana watanzania tupo vizuri kukaa kimya upuuzi unapofanya na kuwaachia raia wenzetu wachache kukemea na kupiga vita tena muda mwingine wakiweka maisha yao hatarini. Ila majanga yakianza then tunakuwa mstari wa mbele kulalamika mitandao lakini inakuwa too late.
Huu mkataba si chochote kwa raia.
Maana hata ukifanyika hautasolve matatizo yetu ya Kimsingi. Huu mradi ni muendelezo wa wizi na ufujaji wa rasilimali zetu.

Hapo ndipo itakuwa lango la kupitisha rasilimali zetu kwa kasi. Kuzitoa nje ya Tanzania na afrika kwenda china na kwengineko.

Hapo bandari ya sasa macho ya wengi yatawaharibia madili yao.

Pembe za ndovu,magogo,madini,copper,gesi,madini,etc vitapitishwa hapo na hakuna mamlaka za kukagua sababu hiyo bandari ni mali binafsi hakuna cha ubia wala nini na ndipo hapo mtawajua vema wachina wakipewa uhuru hata mchanga wanachukua.

Eendeleeni kucheka na hawa mafala.

Watu miaka yote mnakalia ufala ufala utadhani hamtakufa na kuacha hizi mali mnazodhulumu mbwa nyie. MUNGU awalaaani popote mlipo na mtakayoyafanya.
 

osib

Member
Jan 19, 2017
94
150
Nyie watu wa ajabu Sana!!! Yaaani hayati magufuli alisoma mkataba wa bandari pamoja na wasaidizi wake wakaona masharti yake yalivyo Kaa kimtego....yaani mapato wakusanye wao ....hesabu wapige wao ....wakati huo ww huruhusiwi hata kuingia kwenye hayo mahesabu ....Kisha wakiona hawajapata return zao ndani ya Miaka 33 automatic mkataba unaenda Miaka 100 ....hivi huoni hapo kama kuna mtego wa kwamba concession iwe Miaka 100!?....hivi ndugu mwandishi unatuonaje lakin!? Kisha unasema sio china pekee ni oman ...na Korea kusini unazani wao hawataki pesa!? ...yaani hamuoni mifano ya nchi jirani Uganda ... Zambia nk mnatakaje nyinyi!? Yaani nikiskia mradi unafufuliwa roho yang inaumia ....shida yenu mkiahidiwa maslahi Kidogo tu ...mpo radhi mlitumbukize Taifa kwenye tanuru la moto kisa matumbo yenu
 

Kalamu1

JF-Expert Member
Jul 7, 2018
11,901
2,000
kufanya makubaliano yenye tija kwa taifa katika Mradi wa Bandari ya Bagamoyo. Na hilo linawezekana kama timu yetu ya majadiliano itakuwa makini kuzingatia masilahi ya nchi.”
Mkuu 'FbUser', umeandika vizuri sana, na mimi naomba wasomaji wanaotaka kweli kuelewa mradi huu wa Bagamoyo wakusome kwa makini na waelewe vyema mradi huu unaposimamia.

Andiko ni refu, lakini urefu huo unastahili kwa kufafanua mengi ambayo yametokea kuwa yanajadiliwa, wakati mwingine kwa upotoshaji.

Nilipokuwa nakusoma toka juu, kuna nyakati nilishawishika nisimame, ili nijibu baadhi ya uliyoandika papo kwa papo. Uvumilivu wangu mwishoni umejibiwa vizuri sana na mstari huo wa mwisho uliouweka, na mimi kuu'quote' hapo juu.

Mstari huo ndio unaojibu kila kitu katika mambo yote yanayozungumziwa kuhusu mradi wa Bagamoyo.

Tanzania tupo pazuri mno kijiografia. Kama ni biashara hii ya bandari na usafirishaji wa mizigo katika eneo hili, tushindwe tu sisi wenyewe kwa ujinga wetu.

Nasisitiza tena, mstari huo hapo juu niliounyanyua kutoka kwenye andiko lako, hilo ndilo jambo la muhimu zaidi hata kuliko ubabe wa mchina wa kibiashara katika miaka 50 ijayo. Kwa maana hiyo, hatuna lazima yoyote ya kujiuza kwa mchina kwa bei rahisi. Duniani biashara zitaendelea kuwepo tu, mchina hawezi kuhodhi kila kitu peke yake.

Nashawishika kuachia hapa, lakini kuna hili wazo linanilazimisha niendelee kidogo.

Mradi wa Bagamoyo, kiuhakika ni miradi zaidi ya mmoja, kama ulivyoeleza. Kuna mradi wa Bandari, uanohitaji uwekezaji ili bandari hiyo iwepo, halafu kuna mradi wa Special Economic Zone, mahali ambapo mwekezaji yeyote anaweza kuja kuomba nafasi na kuwekeza, kama ni viwanda, au vinginevyo.

Lakini katika uwasilishaji mwingi hapa JF, na nadhani hata huko serikalini, inakaziwa ionekane kama ni 'package' moja ambayo haiwezi kutenguliwa. Swali langu hapa, ni kwa nini iwe hivyo.
Bandari haiwezi kujengwa na yeyote yule, hata sisi wenyewe, kama Lamu inavyojengwa, halafu mambo ya SEZ yakachukua nafasi yake? Hili ni swali ambalo nadhani jibu lake linaweza kuweka mwanga kwa nini kuna masharti magumu ndani ya mradi wenyewe.

Acha nisiandike gazeti, sina mazoea hayo.

Nikushukuru tena kwa kuweka ufafanuzi huu, na jinsi ulivyouwasilisha kwa njia ambayo haiamshi mizuka ya watu juu ya mradi wenyewe.

Ahaaa, nisisahau hiyo habari ya majirani zetu wa kule juu. Ahsante kwa taarifa hiyo.
 

Wacha1

JF-Expert Member
Dec 21, 2009
16,570
2,000
SSH pamoja na mshauri wa JK ambaye ndiyo anamwongoza kwa sasa ni janga la taifa. 2025 ifike haraka na wote ambao watajihusisha na dhuluma kwa Watanzania lazima wasulubiwe kwenye sanduku la kura. Kama CCM watamweka SSH kuwa mgombea, ni lazima rais atoke nje ya CCM.
 

Kalamu1

JF-Expert Member
Jul 7, 2018
11,901
2,000
Nyie watu wa ajabu Sana!!! Yaaani hayati magufuli alisoma mkataba wa bandari pamoja na wasaidizi wake wakaona masharti yake yalivyo Kaa kimtego....yaani mapato wakusanye wao ....hesabu wapige wao ....wakati huo ww huruhusiwi hata kuingia kwenye hayo mahesabu ....Kisha wakiona hawajapata return zao ndani ya Miaka 33 automatic mkataba unaenda Miaka 100 ....hivi huoni hapo kama kuna mtego wa kwamba concession iwe Miaka 100!?....hivi ndugu mwandishi unatuonaje lakin!? Kisha unasema sio china pekee ni oman ...na Korea kusini unazani wao hawataki pesa!? ...yaani hamuoni mifano ya nchi jirani Uganda ... Zambia nk mnatakaje nyinyi!? Yaani nikiskia mradi unafufuliwa roho yang inaumia ....shida yenu mkiahidiwa maslahi Kidogo tu ...mpo radhi mlitumbukize Taifa kwenye tanuru la moto kisa matumbo yenu
Mkuu, huenda mleta mada atakuja kufafanua haya uliyoandika hapa, lakini pia nadhani amekwishayagusia humo humo ndani ya andiko lake refu.
Mimi sijui kama kweli Magufuli aliona taarifa hizo, kwa sababu hawa waliopo sasa wao hawazizungumzii kabisa, na kwa kweli litakuwa jambo la kushangaza sana ikitokea kwamba masharti hayo ndiyo kweli yatakayotumika katika ujenzi wa mradi huo. Sijui hawa viongozi watajificha wapi ikigundukika kwamba matakwa yaliyokataliwa na Magufuli, wao wameyakubali.
Ingewezekana hawa viongozi wakawa wawazi juu ya mradi huo ingependeza zaidi.

Angalizo tu ninaloomba kukupa wewe na wengine, tusichukulie tu kwa mkumbo kila kinachosemwa kuhusu China. Nchi za Magharibi sasa hivi wanatafuta kila njia ya kumpiku China, lakini hawana, na badala yake wanatumia propaganda za upotoshaji. Naomba unielewe, sisemi kamwe kwamba mchina hawezi kutunyonga, la hasha. Lakini kama anatunyonga wa kulaumiwa ni hawa viongozi wetu watakaokubaliana na masharti yasiyokuwa rafiki kwetu. Hili inabidi tulikazie zaidi, kuliko kuwalaumu wachina wenyewe.
 

Mookiesbad98

JF-Expert Member
Feb 1, 2015
1,872
2,000
JF mnatakiwa muanze kuomba mahojiano na key people waliokuwa EPZA ambao wana weza kuulezea huu mradi kwa Data na ukaeleweka mngeanza na former Director general Dr Adelhem Meru, na aliyekuwa mkurugenzi wa Biashara na uendelezaji miradi sasa hivi ni mjumbe wa bodi ya Tanesco Dada Zawadia Nanyaro hawa wanaweza lutupa majinu mazuri ya huu mradi wa Bagamoyo port kwa data.

Cc: Pascal Mayala
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom