Historia ya lugha ya Kiswahili Pwani ya Afrika Mashariki na Kati

Rlechas_3a60

Member
Oct 4, 2018
12
27
Nadharia ya Kiswahili
Kiswahili ni lugha ya Kibantu inayotumiwa na watu katika mawasiliano hasa Afrika Mashariki na ya Kati. Lugha ni sauti za nasibu zenye mpangilio maalumu zilizokubaliwa na watu ili zitumike kwa mawasiliano.Historia ya Kiswahili imeanza takriban miaka 1000 iliyopita kwenye pwani ya Afrika ya Mashariki. Neno Swahili lina asili ya Kiarabu ‘Sahil’ ina maana ya pwani, “sawahil” “as-sawāhilī” ni wingi wake kwa kumaanisha yote yanayohusiana na pwani, watu au utamaduni wa eneo la Pwani.

Asili ya Lugha ya Kiswahili
Kuna nadharia mbalimbali zinazohusu asili ya lugha ya Kiswahili. Nadharia hizo ni kama vile Kiswahili ni Kikongo, Kiswahili ni Pijini au Krioli, Kiswahili ni Kiarabu, Kiswahili ni lugha ya vizalia, pamoja na Kiswahili ni Kibantu.

Kiswahili asili Yake ni Kikongo
Baadhi ya wataalamu hudai kuwa asili ya lugha ya Kiswahili ni huko Kongo ambayo baadaye iliitwa Zaire na sasa inaitwa Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo. Dai hili linaimarishwa na wazo lingine linalodai kwamba katika vipindi kongwe vilivyopata kuwako, sehemu za Pwani ya Afrika mashariki hazikuwa zimekaliwa na watu. Kutokana na hali ya vita, uchungaji na biashara, inadaiwa kuwa Wabantu walitoka sehemu za Kongo walisambaa na kuja pwani ya Afrika mashariki kupitia Kigoma. Baadhi ya wabantu hawa walipitia sehemu za Uganda. Wakati wa kusambaa kwao, walieneza pia lugha zao ikiwemo hii ya Kiswahili.
Sababu hizo hazina mashiko kutokana na kuwa wanahistoria hawajaeleza ni lini hasa watu hao walihamia maeneo ya pwani ya Afrika ya Mashariki.

Kiswahili ni Ki-Pijini au Ki-Krioli
Baadhi ya wataalamu hudai kuwa Kiswahili ni Ki-Pijini. Wataalamu hawa hudai kwamba Ki-Pijini ni lugha ambayo huzaliwa kutokana na kukutanika kwa makundi mawili (A) na (B) yanayotumia lugha mbili tofauti. Ili makundi haya yaweze kuwasiliana kunaundwa lugha ambayo kitabia ni tofauti na zile zinazozungumzwa na makundi yanayohusika. Lugha hii inaweza kuwa na msamiati mwingi kutoka lugha kati ya zile mbili, au inaweza kuwa na msamiati wenye uzito sawa. Lugha hiyo ndiyo inayoitwa Ki-Pijini. Mazingira yanayosababisha kuwepo Ki-Pijini ni kama vile biashara, utumwa, na ukoloni.

Nadharia hii inasema kwamba wakati Waarabu walipokuja pwani ya Afrika ya Mashariki walioa wanawake wa Afrika na hivyo kutokana na mwingiliano wa lugha zao tofauti ilizaliwa lugha mpya ambayo ni aina ya Pijini. Baadae watoto walipozaliwa walikuta lugha hiyo mpya ambayo ni Pijini. Watoto hao waliiendeleza lugha waliyoikuta na baadae ikazaliwa Krioli. Krioli ni Pijini iliyokomaa.

Kwa mantiki ya nadharia hii, wataalamu hawa hukiona Kiswahili kuwa kilianza kama Ki-Pijini kwani ni tokeo la mwingiliano baina ya wenyeji wa pwani ya Afrika Mashariki na wageni wa kutoka Mashariki ya Kati, hususan Waarabu. Aidha, husisitiza kuwa lugha ya Kiswahili haikuwepo kabla ya hapo.
Wataalamu pia wanadai kwamba watu wanaozungumza Ki- Pijini wanaweza kuishi pamoja kwa muda wa karne nyingi na kwa hiyo wakaweza kuzoeana na hata kufikia hatua ya kuoana. Wakioana watoto wao huikuta lugha ya ki-Pijini ama lugha yao ya kwanza. Inapofikia hatua ya aina hii kwa watoto wanaozungumza lugha hiyo, wao husemekana sasa wanazungumza lugha ya Ki-Krioli, lugha ambayo ni hatua ya juu ya Ki-Pijini, yaani Ki-Pijini kilichokomaa.
Nadharia hii hutumia kigezo cha msamiati wa Kiswahili kuonesha uhusiano uliopo kati ya Kiswahili na Kiarabu. Wanadai kuwa, msamiati mwingi wa Kiswahili unatokana na Kiarabu. Hivyo huhitimisha kuwa hapana shaka Kiarabu kimehusika katika kuizalisha na kuikomaza lugha ya Kiswahili.

Kiswahili ni Kibantu (Lugha ya Jamii ya Vizalia)
Wanahistoria wanaeleza kuwa Kiswahili kimetokana na Kibantu kwa kutoa sababu mbalimbali. Miongoni mwa sababu hizo ni ushahidi wa kihistoria na ushahidi wa kiisimu.
Ushahidi wa Kihistoria Kwamba Kiswahili ni Kibantu
Baada ya kuangalia ushahidi wa kiisimu kuhusu asili ya Kiswahili, katika sehemu hii Maganga (1997) aliendelea kuchambua ushahidi wa Kihistoria unaothibitisha kuwa lugha ya Kiswahili ilizungumzwa katika upwa wa Afrika Mashariki hata kabla ya ujio wa wageni kama vile Waarabu na Wazungu. Ushahidi huu ulitolewa na wageni mbalimbali waliofika hapa Afrika Mashariki. Wote wanathibitisha kuwa lugha ya Kiswahili ilizungumzwa hapa Afrika Mashariki kabla ya ujio wa wageni.

Ugunduzi wa Ali-Idris ulifanywa huko Sicily yapata mwaka 1100-1166. Kwenye mahakama ya mfalme Roger II. Licha ya kufahamika kuwa Kiswahili, kilipata kuandikwa kabla ya 10BK. Ali-Idris alikuwa wa kwanza kugundua jina la zamani la Zanzibar kuwa ni Unguja. Katika maelezo yake anaandika pia majina kama vile kikombe, mkono wa tembo, muriani, na kisukari, ambayo ni ya ndizi mbalimbali zilizokuwa zikipatikana huko.
Ushahidi wa Marco Polo ambaye alijishughulisha sana na masuala mbalimbali ya kijiografia na alisafiri sehemu nyingi duniani. Marco Polo aliandika “Zanzibari ni kisiwa kizuri ambacho kina ukubwa wa mzunguko wa maili 200. Watu wote wanaabudu (Mungu), wana Mfalme na wanatumia lugha yao, na hawalipi kodi (ushuru) kwa mtu.” Safari za Marco Polo 1958:301

Kiswahili leo
Katika Tanzania Kiswahili kimekuwa lugha rasmi ya Serikali na Taifa. Shule za msingi hutumia Kiswahili lakini shule za sekondari na vyuo bado zinaendelea kufundisha kwa Kiingereza. Februari 15 2015 Rais Jakaya Kikwete alitangaza mpango wa kubadilisha lugha ya elimu nchini kwa kutumia Kiswahili kwenye ngazi zote hadi shule za sekondari na chuo kikuu.

Kenya imetangaza Kiswahili kuwa lugha ya taifa lakini inaendelea kutumia Kiingereza katika shughuli za Serikali. Watu wa matabaka ya juu mara nyingi hupendelea kutumia Kiingereza wakiona ni lugha bora. Lakini tangu 1986 wanafunzi wote wanatakiwa kujifunza Kiswahili katika shule za sekondari. Tatizo mojawapo ni kuwepo wa makabila makubwa kama Wakikuyu au Waluo wenye wasemaji wengi sana katika eneo moja, hali isiyosaidia kujifunza lugha tofauti. Pia kaskazini na magharibi mwa Kenya wenyeji wengi si wasemaji wa lugha za Kibantu nao hawaoni Kiswahili ni lugha rahisi.

Uganda inatumia Kiswahili kama lugha ya Polisi na Jeshi, hali ambayo haikuongeza upendo wa Waganda kwa lugha kutokana na historia ya Uganda ya kuwa na vita na Serikali za kijeshi. Lakini kinasikika pia kama lugha ya biashara masokoni. Pamoja na kwamba Waganda walikichukulia Kiswahili kama lugha ya kitumwa lakini pia lugha hii ilionekana kuwa na ustaarabu wa Kiarabu zaidi, yaani Uislamu. Lugha ya Kiswahili ilitumika katika kueneza dini hiyo.
Mashariki mwa Kongo Kiswahili kimeenea sana: ni moja kati ya lugha nne za kitaifa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Kwenye visiwa vya Ngazija (Comoros) kuna lahaja mbalimbali za Kiswahili zinazotumika na wananchi.
 
Mada nzuri. Mimi huwa najiuliza lugha zote duniani zilianzaje, maana sote tunajua tulijifunza neno mojamoja tulipo kuwa watoto na kumudu kuongea lugha zetu kadiri tunavyokua. Sasa hao wa kwanza kuwepo duniani waliundaje lugha zao ikiwa hawakukuta watangulizi wao? Wajuzi tusaidieni.
 
ukiitwa mswahili, pigana-ina maanisha wewe huaminiki
Mswahili ni neno lenye maana nyingi sana anaweza kuwa alimaanisha
1 mtumiaji wa kiswahili
2 mtu anayeishi eneo duni (uswahilini)
3 mtu mwenye maneno mengi (muongeaji)
4 mkazi wa pwani ya Afrika mashariki
Usiogope kuwa Mswahili jivunie
 
ukiitwa mswahili, pigana-ina maanisha wewe huaminiki
Fikra za kitumwa kama hizi zinataendelea kupandikizwa kila siku ili watu wachukie asili yao.
Kwa hiyo na ukiitwa mzungu inamaanisha wewe mjanja?
Fikra zilipendwa za zama za mawe za kwanza.
 
Asili ya Lugha ya Kiswahili-
Swahili ni Taifa la makabila yaliopo katika Pwani ya Afrika ya Mashariki na visiwa vyake tokea Barawa hadi Sofala. Baadhi ya makabila hayo ni Wabarawa, Wapate, Waamu, Wagiriama, Wadigo, Waduruma, Wakauma, Wakambe, Wachoni, Warabai, Waribe, Wajibana, Wakilindini, Wajomvu, Wamtwapa, Wachangamwe, Watangana, Wamvita, Wapokomo, Wavanga, Wamakunduchi, Wapemba na Wangazija. Kabila hizi zote zilikuwa zikizungumza lugha ilokuwa ikijulikana kama Kingozi. Hata hivyo, makabila yote haya yalikuwa na ndimi (dialect) zao na miji yao; baadhi yao bado wangali na ndimi zao na miji yao. Ndimi zote hizi zina ukhusiano au ukuruba mkubwa wa maneno na maana zake. Kwa mfano, utakuta kwamba kuna ukuruba fulani baina ya Kipemba na Kiamu.

Kila kabila ina ndimi yake, dasturi zake, mila zake, tungo zake, na kadhalika. Haya yote ni kabla ya Waarabu na Washirazi hawajaanza kuhamia kimaisha katika Pwani ya Afrika ya Mashariki - takriba karne nane hadi kumi zilizopita (yaani baina ya miaka 800 hadi 1000).

Washirazi hawakuathiri mno mila, dasturi, mapisi, na lugha hiyo ya Watu wa Pwani. Waarabu ndiyo walioathiri sana, khususa Makabila ya Kati na Kati (kwa mfano, Wamvita, Watangana na Wakilindini). Makabila haya yaliathirika mno hadi ya kuwa majina haya yalipotea na ndimi zao za kiasili zilipotea vilevile. Ndimi ambazo bado zipo ingawa zimeazima maneno fulani ya Kiarabu (kama ambavyo pengine Kiarabu kimeazima kutoka Lugha ya Kingozi) ni ndimi za kaskazini na zile za kusini.

Ndimi za Kaskazini ambazo bado zipo na wenyewe wanatambuliwa ni kama vile Kibarawa, Kiamu, Kipokomo, na kadhalika. Ama Ndimi za Kusini ambazo hazikuathiriwa mno ni Kingazija, Kimakunduchi, Kipemba na Kivanga. Ndimi za Kati na Kati ambazo bado zikalipo ni kama vile, Kigiriama, Kiduruma, Kijibana; hizi ni miongoni mwa kabila ambazo leo zajiita au zatambuliwa kama Mijikenda (yaani miji tisia).

Utakuta ya kuwa katika makabila ya kati na kati, yale ambayo hayakuathiriwa sana ni yale ambamo watu wake hawakuwa Waislamu. Na ndiyo maana mpaka hii leo utaona ya kuwa makabila ya Mijikenda (isipokuwa Digo), ni makabila ambayo wengi katika watu wake si Waislamu. Hii ni kwa sababu makabila kama ya Mvita, Tangana na Changamwe hayakujitahidi au kujishughulisha kufanya usambazaji wa Risala ya U-Islam kwa makabila haya; Waarabu piya walipokuja hawakuwa na lengo hilo la kuingia vijijini kufanya Da’wah. Lengo lao kubwa ilikuwa ni biashara. Kama tujuavyo U-Islam ulifika Kaskazini Mashariki mwa Bara la Afrika kabla haujafika katika sehemu nyengine za bara Arabu kama vile, Yemen, Omani na hata katika mji wa Madina na sehemu nyingi za nchi tunayoijua leo kama Saudi Arabia. Yaani U-Islam ulifika Abisinia (Ethiopia ya leo) katika mwaka wa 615, miaka mitano tu baada ya Mtume Muhammad (s.a.w.) kupewa risala (610). Mtume alizaliwa mwaka wa 570. Ingawa wale Waislamu waliokuja kuomba hifadhi Abisinia walikwenda zao Madina baada ya kutawazwa kwa serikali ya kwanza ya Islam mwaka wa 623 (huu ni mwaka wa kwanza wa Hijria), walikuwa washawasilimisha watu kadha wa kadha (akiwemo Mfalme wao, Najash); hii ndiyo ilikuwa ni sababu ya kuanza kusambaa kwa U-Islam katika bara la Afrika. Kwa hivyo ni muhimu kutambua na kuamini ya kuwa makabila fulani ya Afrika ya Mashariki yalisilimu kabla ya kuja kwa Waarabu hawa tuwajuwao leo, waliokuja kwa biashara katika pwani ya Afrika ya Mashariki kutoka Yemen, Omani, na kadhalika.

Na khususa ni Waarabu hao wa Yemen na Omani ndiyo waloowana na baadhi ya hao Wangozi, au wanaojulikana leo kama Waswahili. Kwa hivyo, baadhi ya Waswahili wana damu za Kiarabu na baadhi yao hawana damu ya Kiarabu. Katika dasturi za Kizungu za kufuata ukoo, mtu anapotanganya tu damu na asekuwa Mzungu, basi azaliwae katika mtanganyiko huo katu hakubaliwi kuwa ni Mzungu. Na ndiyo twaona ya kuwa ingawa kuna asili mia thalathini (30%) ya Wamarekani Weuse (African-Americans) ndani ya Marekani, lakini wanasibishwa na U-Afrika na U-weuse (Blacks) pekee, na katu hawanasibishwi na uzungu. Kwa Waarabu nao ni rahisi zaidi kunasibishwa na taifa hilo ikiwa mtu lugha yake ya kwanza ni Kiarabu. Ama kwa Waswahili tukati na kati, yaani aghlabu mtu hunasibishwa na Uswahili kwa lugha na asili. Kwa hivyo leo wako baadhi ya Waswahili wenye damu za Kiarabu ambao wametagua, kwa sababu mbalimbali, kujinasibisha zaidi na U-Arabu kuliko U-Afrika; kadhalika, kuna baadhi yao, kwa sababu moja au nyengine, wameamua kujinasibisha zaidi na U-Afrika kuliko U-Arabu.

Hakuna yoyote atakayekataa ya kuwa neno Swahili au Sawahel ni neno lenye asili ya Kiarabu, ambalo lina maana ya Pwani au Mwambao. Kwa hivyo, ni wazi kabisa kuwa jina au neno Swahili halikuapo kabla ya kuja kwa Waarabu. Hivyo basi, wema mmoja ambao Waarabu waliwafanyia wenyeji wa Mwambao wa Afrika ya Mashariki na visiwa vyake ni kuwabandikiza neno lililoanza kutumika kama jina la taifa la wenyeji hao, litambulikanalo leo hii kama Taifa La wa-Swahili, yaani Taifa La wa-Mwambao. Watu wa taifa hili ni Waswahili, yaani Wamwambao, au kwa jina la kiasili, Wangozi. Na hapo pao napo paitwa Uswahilini. Na mila na dasturi zao ndiyo Uswahili. Na lugha ya watu hawa ni Kiswahili. Ni lugha ambayo maneno yake zaidi yatokamana na ndimi za makabila ya kati - kama vile Kimvita, Kichangamwe na Kitangana; halafu ikatukua na maneno ya Kiamu, Kivanga, Kipemba, Kingazija, Kibarawa, Kigiriama, na kadhalika. Kwa hivyo, Kiswahili ni kile kile Kingozi, tofauti ni jina tu; timbuko lake ni mtanganyiko wa ndimi za makabila ya Pwani. Piya kuna maneno ya Kiarabu, Kishirazi, Kiingereza, Kireno, na lugha za bara ya Afrika ya Mashariki. Kiswahili kimeazima maneno ya lugha nyegine kama ambavyo lugha zote zimefanya hivyo. Wao na Wahindi piya wameazimiana katika Upishi. Yayumkinika kuwa katika Kireno, Kiarabu na lugha nyenginezo kuna maneno ya Kimvita, Kijomvu, Kiamu, na kadhalika. Hili ni suala ambalo halihitaji mjadala mkubwa kwani liko waziwazi. Ikiwa baba Adamu (a.s.) na mama Hawaa walizungumza lugha moja kwa nini leo tuwe na lugha, makabila na mataifa tungu nzima? Tazama katika Quraani [Al-Hujuraat aya 13 na Ar-Rum aya 22].

Kwa mfano ukiangalia namna mataifa ya Arabu na Yahudi yalivyoanza utaona ya kuwa ni kama mtezo. Historia na dini yatueleza kuwa Mayahudi na Waarabu wanatokamana na Mtume Yaaqub (a.s.) na Mtume Ismael (a.s.). Ikiwa hii ni kweli, kwa nini iwe hivi na wote wawili wanatokana na Mtume Ibrahim (a.s.) ambae taifa lake hatulijui wala hatukuelezwa. Kwa nini wajukuu, vitukuu, vilembwe, na vilembwekeza vya Nabii Ibrahim wawe na taifa tofauti na yeye? Tena tofauti yenyewe si ya taifa moja bali mataifa mawili, angalau!

Mwana Ismael azae Waarabu na mjukuu Yaaqub (mtoto wa Is-haka) azae Mayahudi. Hii yote hapa ni kuwa tunajaribu kuonyesha ya kuwa kunahitajika sababu ndogo mno (pengine hata isiyoingia akilini mwetu) kuzaliwa kwa taifa jipya au kabila mpya. Lakini hii ni kazi ya Allah (s.w.t.) kama aya za hapo juu zinavyoonyesha. Halafu isitoshe, baada ya kuzaliwa kwa Taifa la Arabu, kukaanza Makabila kama vile Qureish, Aws, Khazraj, na kadhalika. Bado haijatosha, kukazaliwa Koo mbali mbali, kama vile kwenye kabila ya Qureish kuna koo kama Umayya, Makhzum, Alawi, Hashim na kadhalika. Ikiwa haya yote yawezekana, kwa nini visiwezekani kuapo kwa taifa la Swahili na makabila kama vile Mvita, Ngazija, Giriama, na Makunduchi? Au kwa nini kusiwe na koo kama vile Mwinjaa, Wanyali, Wamuyaka, na kadhalika?

Hii leo ni jambo gani linalomuunganisha Muarabu kutoka Sudan na yule wa kutoka Lebanon na yule wa kutoka Hijaz? Sio dini, wala rangi, wala nywele, wala tabia, wala mapishi! Huenda moja au zaidi ya mambo haya yakafanana, lakini jambo kubwa linalowafanya wote wakaitwa Waarabu ni Lugha, na labuda Asili. Labuda na Mayahudi ni vile vile, mtukue Yahudi wa Palestine, na yule wa Habashi na yule wa Urusi; kitu kitakacho waunganisha ni Asili, na pengine lugha na dini.

Kwa hivyo Swahili ni taifa ambalo lipo, na lenye makabila yasiopungua kumi na tano, tokea mji wa Barawa (kaskazini) mpaka mji wa Sofala (kusini). Ni taifa ambalo makabila yake yametapakaa katika nchi sita: Somalia, Kenya, Tanganyika, Zanzibar, Ngazija (Comoro Islands), na Msumbiji (Mozambique). Kwa hiyo, nasema tena ya kuwa Swahili ni Taifa. Ni muhimu kufahamu ya kuwa mtu anaposema kuwa yeye ni Mswahili haimaanishi kuwa kabila yake ni Swahili bali ni kuwa anatokamana na Taifa La Waswahili. Na kitu kinachowaunganisha watu katika taifa hili ni: Asili na Lugha.

KWAHERINI

Muhammad bin Yusuf
Chapa ya mara ya kwanza - Mwezi wa Ramadhan, 1415 Hijria (1995)



Madhehebu ya Lugha ya kiswahili - Ali Said Sunkar.

Kwa mtazamo wa haraka lakini wa ndani kidogo, tunapotafiti uzungumzi wa lugha ya Kiswahili hivi leo, tutapata kuwa, kuna Madhehebu matatu makubwa ambapo Waswahili wote na wazungumzi wa Kiswahili, wanaangukiya katika mojawapo ya madhehebu haya matatu.

Na kwa mara nyingine utamkuta mtu akitumiya na kuchanganya madhehebu mawili au yote matatu pindi anapoongeya au anapoandika, bila yeye kutambuwa ni mfuwasi au mtetezi wa dhehebu lipi.

Katika makala haya mafupi, tutajaribu kuangaliya kiini na chanzo cha kila dhehebu, watetezi wao, wafuwasi wao, uzuri na ubaya wa kila dhehebu na mwisho itafuatiwa na mapendekezo.

Madhehebu yenyewe ni kama yafuwatavyo:

1) Dhehebu la kwanza hapa nitaliita: "Kiswahili Lahaja yetu"
2) Dhehebu la pili: "Kiswahili Sanifu"
3) Dhehebu la tatu: "Kiswahili Asiliya".

UCHAMBUZI WA MADHEHEBU MATATU

Sasa tuchambuwe nukta zilizotanguliya moja baada ya nyingine katika kila dhehebu.

DHEHEBU LA KWANZA

1) "Kiswahili Lahaja yetu" inakusudiwa" ule uzungumzi au uwandishi wa lugha ya Kiswahili unaotegemeya lahaja moja maalum (makhsusi) miongoni mwa lahaja 23 za Kiswahili zinzotambulikanwa, kama: Kiamu, Kibajuni, Kibarawa, Kingazija, Kimvita, Kiunguja na kadhalika.

Kwa miyaka mingi sana utumiyaji wa Kiswahili ulitegemeya dhehebu hili, hivi kwamba vitabu makhtuti (nyaraka za zamani au ‘manuscripts’) ambazo ziliandikwa kuanziya karne ya nane (Eighth century C.E.) hadi karne ya kumi na tisa (19 th century C.E), zilitumiya lahaja makhsusi ya yule mwandishi au lahaja ya pale mjini alipo yule mwandishi.

Makhtuti kama hizi zilihifadhiwa kwa njiya mbali mbali katika mwambao wa pwani, kuanziya Barawa hadi Sofala na visiwa vya Bahari ya Hindi. Kwa mfano vitabu vilivoandikwa Amu au vilivyoandikwa na Waamu, utakuta kuwa vilitumiya Lahaja ya "Kiamu" na vile vilivyoandikwa Mombasa (Mvita), vilitumiya Lahaja ya "Kimvita" na hivyo hivyo vya unguja, Pemba na kwengineko.

Itakuwa ni vizuri hapa kugusiya kuwa Ndaki (Vyuo vikuu) kadhaa za Ujerumani na Uingereza zimejishughulisha sana kwa muda mrefu tangu karne ya kumi na nane kukusanya na kuhifadhi hizo Makhtuti. Ambapo hivi leo wamejilumbukiziya maelfu ya Makhtuti kama hizo kwenye zahanati za kuhifadhiya makhtuti na nyaraka za zamani.

Miaka kadhaa (80s & 90s) iliyopita wenye Makhtuti kama hizo Lamu, Malindi, Mombasa, Zanzibar, Tanga na miji mingine ya Waswahili, walilipwa karibu Shilingi elfu kumi na tano (Ksh 15,000) kwa kila makhtuti moja mtu akionyesha na wajerumani wachukuwe nakala (photocopy) yake.

Kwa bahati, makhtuti zote walizozikusanya zilikuwa zimeandikwa kwa kutumiya herufi za Kiarabu, kwa hivyo kazi nyingine iliyofanywa na Wajerumani na Waingereza, ilikuwa ni kutafuta wataalamu wa Kiswahili wa Lahaja mbali mbali na wenye uzoefu wa kufahamu maandishi ya Kiarabu, ili wazifafanuwe katika herufi za Kilatini na kadhalika kutafsiri maneno ya kizamani ambayo kwa sasa aidha hayatumiki au hayaeleweki na watu wa kawaida.

Prof. Ahmad Nabhany ni mmoja wa wataalamu waliofanya kazi hizo. Ametumiya miaka mingi akitembeleya Ndaki kadhaa za Ujerumani, Uingereza Afrika Mashariki na Marekani akihadhiri (Lecturing) juu ya lugha ya Kiswahili.

Kwa hivyo “Kiswahili Lahaja yetu” ilkuwa ni utumiyaji wa Kiswahili uliotegemeya Lahaja moja au nyingine, kulingana na mwandishi ni mtumiyaji wa Lahja gani, au yuko mji gani. Na tukizingatiya njiya nzito za mawasiliano za wakati huo ndio utaona kuwa ilikuwa sirahisi kwa Waswahili wa kawaida kujuwa tofauti ya Lahaja hizo, ila wale wataalamu waliojishughulisha na masuala ya Kiswahili, fasihi, hadithi ngano (hadithi ndefu) tunzo, mashairi na nyanja
nyingine za lugha ya Kiswahili.

DHEHEBU LA PILI

2) “Kiswahili Sanifu”: dhehebu hili lilianza kuundwa kati wa karne ya kumi na tisa na karne ya ishirini. Sababu ya kuundwa dhehebu kama hili ni ile haja ilyokuwepo ya watu (Waswahili) wote kutoka Lahaja mbali mbali waweze kukutana na waelewane katika uzungumzi au utumiyaji wa Kiswahii ambao utakuwa ni sahali kwa wote.

Fikra hii iliungwa mkono na wataalamu wengi wa Kiswahili na ikaanza kusambaa. Ndiyo wakati huu huu piya, Wanamisheni (Christian Missionaries) waliokuwa na hamu kubwa kusambaza ukiristo miongoni mwa Waswahili, na kufunguwa njiya kwa wakoloni kuingiya Kenya, kama ilivyokuwa kawaida ya wakoloni kabla ya kuja wao mwanzo hutuma wanamisheni kufunguwa mlango kwa jina la yesu kristo, walichangiya katika usambazaji wa Kiswahili.

Wanamisheni wenyewe walikuwa ni wageni katika lahaja yoyote ile ya Kiswahili. Kwa hivyo waliona kuwa wakilemeya upande mmoja watakosa wafuwasi wa pande nyingine, basi nao wakaunga mkono fikra kama hii. Na kwa kuwa wao walikuwa na uwezo mkubwa wa kifedha na kitaaluma mbali mbali, basi waliweza kwa muda mfupi sana kubuni uwandishi wa Kiswahili kwa kutumiya dhehebu hili jipya la “Sanifu”.

Kiswahili ilikuwa ndiyo lugha ya biashara, elimu, utamu wa fasihi, hisiya za ndani (emotions),mawasiliano ya rahisi. Kadhalika ni lugha ya utajiri wa maneno ikilinganishwa na lugha nyinginezo za eneo hilo la Afrika mashariki na kati, na juu ya yote ilikuwa ni lugha yenye uwezo na fursa ya kupanuka zaidi na kusambaa sehemu nyingi.

Vitabu vingi vikaanza kuandikwa, ambapo lengo kubwa kwa upande wa wanamisheni ilikuwa ni kutafsiri Bibliya kwa lugha ya Kiswahili, hasa baada ya kuona kuwa Kiswahili ilikuwa ni lugha inayoeneya kwa haraka na kuzungumzwa na watu wengi sana, hata wale wasiokuwa Waswahili, walipendeleya kutumiya Kiswahili.

Makamusi ya Kiswahili yakachapishwa, Mashule yaliokuwa tayari yameshaanzishwa na wanamisheni yakaingiza lugha ya Kiswahili katika Manhaji (Curriculum) zao, na vitabu vya shule vya Kiswahili (text books) vikatayarishwa. Matangazo ya Mongoya (radio) ya wanamisheni na serikali ya kikoloni ya Afrika Mashariki (East Africa Protectorate), yalizidi kutiliya nguvu usambazaji wa lugha ya Kiswahili.

Jambo muhimu la kutaamali kidogo ni kuwa, wakati wa usambazaji wa Kiswahili “Sanifu”, Lahaja mbili pekee ( Kimvita na Kiunguja) ndizo zilizozingatiwa. Ama Lahaja nyingine ziliachwa nyuma. Jambo hili limesababisha vizazi vilivyokuja baadaye wakawa hawajui kuhusu hizo Lahaja nyingine, hali hii imeendeleya kudhuufisha mpaka watu wa Lahaja yao kuanza kuacha Lahaja na kuisahau na badala yake wakitumiya “Sanifu”. Kwa hakika Lahaja mbili hizi zilichaguliwa si kwa sababu ni mzuri zaidi kuliko nyenginezo, au Lahaja hizo
nyengine ni mbaya, hasha, bali ni kwa sababu Lahaja hizi zilikuwa katika makao ya utawala, yaani Zanzibar na Mombasa. Na siku zote makao ya utawala kila mahali ndio yenye taathiri (influence) kubwa zaidi kwa sababu ya vifaa mabali mbali (tools and means of communications) zinazomilikiwa na serikali kwenye makao ya utawala.

DHEHEBU LA TATU

3) “Kiswahili Asiliya” Hili ni dhehebu jipya zaidi kwa upande mmoja na si jipya kwa upande mwingine. Ni jipya kwa kuwa watetezi wa dhehebu hili wamekuja na mtazamo mpya wa utumiyaji wa Kiswahili na kupinga mtazamo wa utumiaji Kiswahili “Sanifu”.

Ama si jipya ni kwa kuwa watetezi wa dhehebu hili wanapiganiya utumiyaji wa Kiswahili kwa Lahaja zote ikiwemo lahaja za Kimvita na Kiunguja. Kwa maoni yao ni kwamba lahaja zote ni lazima zichanganywe ili ziunde Kiswahili kimoja chenye utajiri wa maneno wa lahaja zote, na hivi ndio kurudi katika asili ya Kiswahili, hii ndiyo maana dhehebu hili linaitwa “Kiswahili Asiliya”

Kwa hivyo “Kiswahili Asiliya” tukitizama kwa makini tutaona kuwa si jambo geni hivyo, bali ni harakati ya usahihishaji (Reform Movement) ya ule mtazamo uliosababisha kubuniwa kwa dhehebu la “Sanifu”, la kutegemeya lahaja mbili pekee. “Asiliya”, badala yake inapiganiya utumiyaji wa Kiswahili ambao utashirikisha Waswahili (au wazungumzi wa Kiswahili) wa lahaja (ndimi) zote.

Lakini kosa au kasoro iliyofanywa na “Sanifu” ni kwamba mwishowe waliangukiya kutumiya lahaja mbili pekee na kuwacha nyuma au kutupiliya mbali lahaja nyengine. Na “Asiliya” hivi sasa inajaribu kurekebisha kosa hilo. Kwa sababu kulingana na hoja ya watetezi wa “Asiliya” ni kwamba:

utumiyaji wa “Sanifu” wa lahaja mbili pekee, unanyima lugha ya Kiswahili ule utamu wake ambao unapatikana katika lahaja nyengine. Vile vile kuna maneno mengine ambayo hayapatikani katika lahaja za Mvita na Unguja, lakini yanapatikana katika lahaja nyengine. Kwa hivyo utajiri wa Kiswahili utakamilika tu pale lahaja zote zitakaposhirikiyana na kutumika sambamba, hii ndiyo “Asiliya”

Na hivi leo watetezi na wafuwasi wa “Asiliya” wanazidi kuongezeka, na "Asiliya” yenyewe inaanza kukubaliwa na wataalamu wengi wa Kiswahili katika Ndaki mbali mbali za Kenya, Tanzania, Uganda, Ujerumani, Uingereza, Marekani na kwengineko.....




Copyright © Travel Agency. All rights​
 
Mswahili ni neno lenye maana nyingi sana anaweza kuwa alimaanisha
1 mtumiaji wa kiswahili
2 mtu anayeishi eneo duni (uswahilini)
3 mtu mwenye maneno mengi (muongeaji)
4 mkazi wa pwani ya Afrika mashariki
Usiogope kuwa Mswahili jivunie
Mchawi, ni maana nyingine ya mswahili?
 
Back
Top Bottom