Historia ya Katiba TANO Tanzania na Ajabu ya WANANCHI Kutoshiriki HATA KIMOJA

Uwezo Tunao

JF-Expert Member
Nov 14, 2010
6,942
0
Celina Kombani anacheza ngoma asiyoijua vyema
Joseph Mihangwa, Disemba 8, 2010
KAMA kuna waziri katika Baraza jipya la Mawaziri la Rais Jakaya Mrisho Kikwete, aliyeanza kazi kwa mikwara na mikakati iliyoshindwa kabla ya kuanza, waziri huyo ni Celina Kombani anayeongoza Wizara ya Sheria na Katiba.

Tamko la waziri huyo, hivi karibuni, kwamba suala la Katiba mpya nchini halizungumziki; kwa sababu ni la gharama kubwa, ni ishara kwamba waziri huyo anapiga jaramba kupigana na wakati asijue kwamba "wakati ukuta".

Kama ningekuwa mkufunzi msimamizi wake wa tasnifu [thesis] juu ya wizara yake, tayari ningemkata alama kabla ya kuisoma ili ashindwe mtihani hima.

Kombani anashindwaje kusoma maandishi ukutani na matukio nchini Kenya yaliyozaa Katiba mpya? Na aukubali usemi wa wahenga kwamba "ukiona mwenzio akinyolewa, wewe tia maji".

Suala la Katiba mpya haliepukiki nchini kwa mazingira ya sasa, na kujaribu kulizuia ni sawa na mtu kujaribu kutemea mate anga. Na kwa kufanya hivyo, hawezi kukwepa kujichafua uso wake mwenyewe. Au anajaribu kuzuia mafuriko ya mto kwa viganja vya mikono?

Historia ya nchi yetu inaonyesha kwamba, mabadiliko ya Katiba hayakwepeki kila panapotokea mabadiliko makubwa ya kiuchumi na kijamii; na hivyo kwamba, yanayoendelea nchini sasa yatashinikiza Katiba mpya. Kwa nini?

Katiba ya nchi ni ramani ya madaraka na ni kielelezo cha demokrasia nchini kwa sababu ni tunda la uamuzi wa dhati wa wananchi wenyewe. Kudumu kwa Katiba bila marekebisho ya mara kwa mara ni ishara ya Katiba makini; kinyume chake ni Katiba isiyozingatia matakwa ya wananchi na mabadiliko ya nyakati.

Katiba kama ile ya Marekani ambako ndiko tumeazima mfumo wa demokrasia wa sasa, imerekebishwa si zaidi ya mara nne katika kipindi cha miaka 222 tangu ianze kutumika rasmi mwaka 1788, tofauti na Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano ambayo katika kipindi cha miaka 13 pekee imefanyiwa marekebisho 14, sawa na wastani wa rekebisho moja kila mwaka!

Dhumuni kuu la kurekebisha Katiba ya nchi ni kutaka kukidhi matakwa ya jamii inayobadilika kwa lengo la kutekeleza demokrasia, haki ya kijamii utawala wa sheria na maendeleo ya nchi. Misingi yote ya Katiba huongozwa na uzalendo na si kwa mizengwe ya siasa za vyama vya siasa kwani Katiba ya nchi iko juu ya vyama vya siasa.

Katiba inayozingatia malengo haya ina uwezo mkubwa wa kuhimili mitafaruku nchini inayoambatana na mabadiliko ya jamii ya mara kwa mara na kudumu kwa muda mrefu kuliko inayokiuka malengo haya, na hivyo kusababisha mabadiliko au marekebisho ya mara kwa mara. Katiba yetu iko katika Katiba za kundi la pili. Nitaelezea kwa nini tumefikia hapo.

Tangu tupate Uhuru Desemba 9, 1961 hadi sasa, Tanzania imepata kuwa na Katiba mpya tano ambazo katika uhai wake zimeweza kufanyiwa marekebisho mara kwa mara kwa kuzingatia mazingira ya kisiasa, kijamii na kiuchumi ya nchi.

Kila Katiba mpya, na kila rekebisho au marekebisho ya Katiba yalitanguliwa na mitafaruku au migongano ya kijamii na kiuchumi iliyotishia mustakabali wa Taifa na uhusiano wa kimataifa.

Katiba ya kwanza iliyojulikana kama "Katiba ya Uhuru" [The Independence Constitution] ya mwaka 1961, ilitungwa na kutumika katika mazingira yaliyoashiria kumalizika kwa ukoloni mkongwe nchini Tanganyika.

Ilifuatiwa na Katiba ya Jamhuri [The Republican Constitution] ya mwaka 1962 iliyoashiria Watanganyika kuchukua madaraka ya nchi kutoka kwa wakoloni.

Nitafafanua kidogo. Katiba ya Uhuru ndiyo iliyotoa uhuru na ramani ya madaraka kwa Tanganyika huru bila madaraka kamili ya ndani kwa sababu nchi ilikuwa bado inasimamiwa na Uingereza kupitia mteule wake - Gavana wa Tanganyika.

Na kusema kweli, Katiba hiyo haikuwa tunda la Watanganyika; bali ilitungwa na kutolewa kwenye Ofisi ya Makoloni nchini Uingereza na kushushwa kwetu kama "Torati" yenye ukakasi bila kutoa uhuru kamili.

Kwa hiyo ilizua nguvu ya hoja kwamba uhuru kwa Watanganyika bila kuwa na Serikali yenye madaraka ya ndani [Jamhuri] lilikuwa debe tupu, na huo ukawa msingi wa kudai Serikali hiyo na Katiba mpya; madai ambayo ndiyo yaliyozaa Jamhuri.

Kwa bahati mbaya, Katiba zote mbili za kwanza – Katiba ya Uhuru na Katiba ya Jamhuri, tofauti na Katiba za nchi zingine zilizokuwa zilizokuwa makoloni ya Uingereza, hazikuwa na tamko kuhusu Haki za Binadamu.

Huo ndio ulikuwa mwanzo wa mfumo wa utawala wa rais dikteta, mwenye imla [imperial presidency], asiyeambilika au kushaurika; kwani chini ya kifungu cha 3 (3) cha Katiba hiyo, Rais alipewa mamlaka na uwezo wa kuongoza nchi atakavyo kwa vile hakulazimika kusikiliza au kupokea ushauri kutoka kwa mtu yeyote kuhusu masuala ya uongozi wa nchi.

Hali hiyo haijabadilika hadi sasa kama inavyobainishwa kwa maneno yale yale katika ibara ya 37 (1) ya Katiba yetu ya 1977 inayoendelea kutumika.

Kama kweli tunataka demokrasia ionekane kufanya kazi, tunapendekeza Rais atende kazi kwa ushauri wa Baraza la Mawaziri, na Bunge la nchi [sauti ya watu] lipewe mamlaka zaidi ya kutoa maelekezo kwa Rais bila hofu ya kuvunjwa na yeye kwa mamlaka aliyo nayo chini ya ibara ya 97 (4) ya Katiba ya sasa.

Katiba ya tatu [nayo ilikuwa ya muda] ya Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ya 1964, ilianzishwa kwa kusudi la kukidhi matakwa ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, pale nchi mbili hizo zilipoungana, Aprili 26, 1964.

Katiba hii ilikuwa ni maboresho tu ya Katiba ya Jamhuri ya Tanganyika ya 1962 kupitia Agizo la Rais [Presidential Decree] na kuitwa "Katiba ya Muda ya Jamhuri ya Muungano", wakati huo Jamhuri ya Muungano ikijiandaa kupata Katiba yake kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa na Mkataba wa Muungano pamoja na Sheria ya Muungano.

Katiba ya Nne iliitwa "Katiba ya Muda ya Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar" ya mwaka 1965 ambayo, kwa kutumia Kikao cha kawaida cha Bunge la kawaida [badala ya Bunge la Katiba kama ilivyotakiwa], ilipitishwa na kuanzisha Utawala wa Chama kimoja cha siasa badala ya vyama vingi, tofauti na ilivyokuwa kwa Katiba zilizotangulia.

Na chini ya marekebisho ya Katiba hiyo yaliyofanywa mwaka 1975, Chama cha Tanganyika African National Union [TANU], kilitangazwa "kushika hatamu" za uongozi wa nchi, ambapo vyombo vyote vya Serikali vilifanywa kuwajibika kwa Chama.

Katiba ya kudumu iliyofuata mwaka 1977 ilipitishwa mahsusi kukidhi matakwa ya vyama viwili vilivyoungana – TANU cha Tanzania Bara na Afro Shirazi Party [ASP] cha Tanzania Zanzibar, na kuimarisha zaidi "utukufu" wa Chama kipya kilichoshika hatamu za utawala wa nchi - "Chama cha Mapinduzi" [CCM] kilichozaliwa kwa ndoa ya TANU na ASP.

Katiba hii ilikamilisha zoezi la kuhodhi siasa za nchi kwa njia ya Chama kimoja ambapo jukumu la kufikiri, kutoa hoja na mawazo ya kimaendeleo liliondolewa kwa wananchi na kuwekwa mikononi mwa Chama pekee.

Yeyote aliyehoji juu ya mwenendo wa Serikali [mwanachama au si mwanachama wa CCM] aliitwa mpinga maendeleo, mpinzani wa Chama na hivyo mpinzani wa Serikali. Sheria kandamizi, ikiwamo Sheria ya Usalama wa Taifa na Mamlaka ya Rais ya kumtia mtu kizuizini, zilitumika kunyamazisha wananchi wenye hoja na maoni.

Katiba ya Kudumu ya 1977 ilianzishwa na kusimama kwenye mihimili [mafiga] mikuu mitatu: Kwanza, Rais mwenye imla, asiyeambilika au kushaurika kama sehemu ya masalia ya Katiba ya 1962. Pili, Serikali mbili – Tanganyika na Zanzibar; na tatu, Utawala wa Chama kimoja na siasa ya Ujamaa na Kujitegemea.

Katiba hii, kama ilivyokuwa Katiba ya Uhuru, si matunda ya mjadala wala maoni ya wananchi. Ni Katiba iliyopendekezwa na Tume ya Chama iliyoteuliwa kuandaa rasimu ya kuunganishwa kwa vyama vya TANU na ASP, badala ya kupendekezwa Tume ya Katiba iliyotajwa katika ibara ya 7 ya Hati ya Muungano, na kifungu cha 9 cha Sheria zote mbili za Muungano, za Tanganyika na Zanzibar.

Je, Katiba ya aina hii inakidhi matakwa na mazingira ya nchi ya sasa? Je, inakidhi matakwa ya Muungano yaliyokusudiwa?


Hatuna cha kutumaini kutokana na ukweli kwamba baadhi ya mihimili iliposimamia Katiba hii imekwishavunjika. Ukiondoa mhimili pekee wa Rais asiyeambilika uliosalia katika Katiba ya 1977 [angalia ibara ya 37, 46 na 63 ya Katiba], mihimili mingine miwili imevunjika: Itikadi ya Ujamaa na Kujitegemea imeuawa na Azimio la Zanzibar la 1992, na nafasi ya mfumo wa Utawala wa Chama kimoja imenyakuliwa na mfumo wa vyama vingi vya siasa tangu 1992.

Aidha, mfumo wa vyama vingi vya siasa na uchumi huria havikuwa katika mawazo ya Katiba ya 1977 wakati ikitungwa, na kwa sababu hiyo haujapewa nafasi inayostahili kwa tafsiri sahihi ya mfumo huo.

Kwa hiyo, nchi sasa inaendeshwa kwa kauli mbiu ya "Chama Dola" kana kwamba wananchi wengine wasio na vyama au wale wa vyama vingine ni ‘raia daraja la pili' katika nchi yao wenyewe.

Kuna tofauti kubwa kati yetu na nchi zenye demokrasia iliyokomaa. Kwa mfano katika Marekani na Afrika Kusini, rais anaweza kumteua mtu yeyote bila kujali tofauti za itikadi za siasa kushiriki katika uongozi wa nchi au katika kusimamia maslahi ya nchi. Kwa wenzetu; ni nchi kwanza, vyama vya siasa baadaye tofauti na sisi ambapo ni "Chama kwanza, maslahi ya nchi baadaye".

Nao utekelezaji wa mfumo na muundo wa Muungano uliokuwa ukifanyika kwa nguvu za Chama zaidi kuliko kutumia misingi ya sheria zilizoanzisha Muungano huo, sasa unahojika kuliko hapo zamani; na kwamba kuna kila hali kuonyesha kwamba busara inahitajika ili utekelezaji huo utazamwe upya kuondoa kero kwa manufaa ya nchi.

Vivyo hivyo kujaribu kujenga demokrasia na utawala bora nchini kwa kutumia Katiba ya sasa, ni sawa na mbio za mbilikimo katika kuisaka demokrasia. Ni mbio zisizoweza kuhimili wala kufua dafu kwa hatua ndefu za mabadiliko makubwa yanayotokea katika nyanja zote za maisha ya jamii.

Kwa hiyo; bila kuzingatia mambo haya ya kihistoria, mabadiliko yoyote ya Katiba [kwa njia ya kuweka viraka] hayatakidhi matakwa ya demokrasia, na Katiba yetu itaendelea kuwa adha kubwa kwa wananchi.

Tunapashwa kurefuka kimawazo, akili na kwa vitendo ili tusiachwe nyuma na ulimwengu wa kidemokrasia kwa maendeleo ya watu wetu. Tusikubali kubakia "mbilikimo" wakati dunia inapiga hatua ndefu katika uwanja wa demokrasia; tutasahaulika na kubaki nchi yenye udikteta unaopitwa na wakati haraka.
Itaendelea
hs3.gif

SOURCE: Raia Mwema

Simu: 0713-526 972
Barua-pepe: jmihangwa@yahoo.com
 

Uwezo Tunao

JF-Expert Member
Nov 14, 2010
6,942
0
Hoja yangu juu ya Historia ya KATIBA 5 Tanzania bila Wananchi Kushiriki Moja Kwa Moja

Kwa kipindi hiki ambapo wananchi tunadai mabadiliko ya kweli ni muhimu sana hasa kwetu sisi VIJANA tukatazama historia ya nchi yetu na NAMNA ambavyo KATIBA zote TANO katika nchi yetu zilivyopatikana na MACHUNGU TUNAYOJIFUNZA na KATIBA za nchi zinapotungwa kutoka JUU SERIKALINI au na WATAALAM wachache ama KATIBA ZA KUAGIZWA KABISA toka nchi za nje.

Hoja yangu kwa Wana-JF, je na katiba Mpya tunayoitafuta katika karne hii ya 21 NAKO PIA BADO TUKAKAE PEMBENI TUKAANDIKIWE KATIBA na wengine kama ambavyo tayari Jaji (Rtd) Bomani alivyopendekeza hivi karibuni???
 

Ronal Reagan

JF-Expert Member
Nov 4, 2010
4,890
2,000
Kwanza nimshukuru sana aliyedadavua na kutupa kitu hicho hapo juua. Na shukran za pili kwako wewe uliyeiwasilisha jamvini.

Nakubaliana sana na kuunga mkono kuwa hiyo inayoitwa katiba kwa sasa haistahili kuitwa hivyo, kwa sababu hayo mapungufu uloainisha hapo (na mengine ambayo hayakutwjwa) ni mapungufu makubwa sana kuwa nayo ktk kitu muhimu kama Katiba hivyo kuipunguzia hadhi. Matakwa ya kisheria, mahitajia ya hali halisi na mazingira ya sasa vyote havimo.

Ndio maana mtu anayesema haina mapungufu au eti mapungufu yaliyomo ni machache hivyo waendelee kuweka viraka kwa lugha yoyote ile haitakii mema Tz.

Ila wenye mapenzi mema na uchungu na Tz tusikubali hoja ya Katiba Mpya itekwe nyara na mafisadi. Wataibaka na kuchakachua wacheze sarakasi zao na kuja na kituko.
 

Ronal Reagan

JF-Expert Member
Nov 4, 2010
4,890
2,000
Eti moja ya sababu nyingine (haiko ktk bandiko hili), iliyosababisha mabadiliko ya kuwepo kwa katiba no. 3 na 4 ni "kulinda umoja wa taifa". Lipi?.

Kwa sababu hao wenye kudai kulilinda taifa ni nani aliyewapa wao ithbati na dhamana ya kufanya hivyo? .....ni sheria....ni katiba. Sasa kama mwl. Nyerere na waliounga mkono fikra zake ni wazi hawakuona mbali kuwa kwa kitendo kile walihalalisha dhana endelevu ya kuwa na watawala (hasa mkuu wa nchi na watendaji wake) wasiotokana na ridhaa ya wenye nchi wala kuwajibishwa nao.

Ndio maana wenye nchi hawajawahi kuwawajibisha watawala hao kwa madudu mengi tu na wao wakayaendeleza kama ilivyo leo. Wenye nchi hawana hiana wala shuruti nyingi, wanataka kuhuishwa kwa haki yao ya asili. Katiba mpya yenye utashi wa Tz katika nyanja zote (sio ya ki-chama) ndio jibu.
 

Uwezo Tunao

JF-Expert Member
Nov 14, 2010
6,942
0
Ndugu Reagan, masikio yangu yote yako kwako hadi sasa.

Kwa muhtasari tu ni kwamba tukuhesabu wewe kuwa ni mmoja kati ya wengi huku nje ambao msimamo ni kwamba safari hii uandikuaji upwa wa katiba ya SITA Tanzania WANANCHI KAMWE TUSIRUHUSU MADALALI kututekelezea jukumu letu la msingi sio??

Haya basi na mjadala uendelee kwani sina uhakika nao akina (1) Malaria Sugu, (2) Ndugu Dar es Salaa, Consultant na Mwanamgeuko pia watakua wanaunga mkono wazo hilo au mapendekezo ya Jaji (Rtd) Bomani??? Kama ulivyosema mwenyewe ni kwamba hoja hii tukaijadili kwa akili iliyotulia na kuweka pembeni kabisa yale yote yanayotugawa na kuyazingatia zaidi yale mambo ya msingi yanayotuleta pamoja kama taifa.

Hebu na sikilize michango ya wenzetu wengine pia humu jamvini.
 

Mahesabu

JF-Expert Member
Jan 27, 2008
5,429
2,000
Katiba kama ile ya Marekani ambako ndiko tumeazima mfumo wa demokrasia wa sasa, imerekebishwa si zaidi ya mara nne katika kipindi cha miaka 222 tangu ianze kutumika rasmi mwaka 1788, tofauti na Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano ambayo katika kipindi cha miaka 13 pekee imefanyiwa marekebisho 14, sawa na wastani wa rekebisho moja kila mwaka!

HIKI SI KILIO CHA KWANZA.....KATIBA ILISHABADILISHWA MARA KIBAO TU
 

Uwezo Tunao

JF-Expert Member
Nov 14, 2010
6,942
0
Duu!! Ndugu Mahesabu, kwa maelezo haya kinachonijia akilini kutokana na upembuzi wako ni kana kwamba unasema KATIBA inapoandikwa na WANANCHI WENYEWE humudu zaidi changamoto na mabadiliko katika jamii kwa miaka mingi zaidi. Na kwamba huenda ndi maana wenzetu Wamarekani wamebadilisha ya kwao kwa mara chache zaidi eeehhh??

Labda niongezee pia kwamba ndio maana uhiari wa wananchi wenyewe kufuata sheria bila kufuatwa kinyumanyuma pia inakua ni mkubwa huko kwao.

Basi moja kwa moja unaniambia kwamba katiba za kutungwa kwa KUTUMIA MADALALI (WATU KATI) badala ya wananchi wenyewe ina gharama kubwa (1) kwa kuhitaji kubadilishwa mara kwa mara, (2) uhiari wa wananchi kuifuata ni mdogo sana matokeo yake sisi sisi walalahoi ambao hatukushirikishwa kwenye utungaji wake moja kwa moja ndio katiba kama hiyo hufadhili sheria mbalimbali za kutufanya sisi tu na wala si watawala na familia zao kufunwafunwa gerezani.

Ukitaka kuthibitisha hili nenda Ukonga ukajionee wafungwaresho yao ilivyo; tajiri au mtawala mmoja kwa walalahoi 2000 (1:2000). Chonde tukajiandikie katiba wenyew ili hata gharama za kuendesha mi-kesi mahakama, na kutuweka selo ipate kupungua na tukaajiri polisi wachache tu na hayo mamilioni ya fedha kuelekezwa kwenye shughuli za maendeleo ya taifa letu.

Hata na sisi vijana hatupendi hata kidogo kufungwafungwa jela alimradi na tukapate kushiriki KWA UWAZI KABISA kuandika KATIBA MPYA ambayo sisi ndio wadau wake wa muda mrefu zaidi kuliko hata waze ambao KIBAYOLOJIA huenda wakatangulia mbele ya haki na kutuacha nyuma!!

Jama tunasikilizana hapa, home of Great Thinkers tusioheshimika???
 

Ronal Reagan

JF-Expert Member
Nov 4, 2010
4,890
2,000
Ndugu Reagan, masikio yangu yote yako kwako hadi sasa.

Kwa muhtasari tu ni kwamba tukuhesabu wewe kuwa ni mmoja kati ya wengi huku nje ambao msimamo ni kwamba safari hii uandikuaji upwa wa katiba ya SITA Tanzania WANANCHI KAMWE TUSIRUHUSU MADALALI kututekelezea jukumu letu la msingi sio??

Haya basi na mjadala uendelee kwani sina uhakika nao akina (1) Malaria Sugu, (2) Ndugu Dar es Salaa, Consultant na Mwanamgeuko pia watakua wanaunga mkono wazo hilo au mapendekezo ya Jaji (Rtd) Bomani??? Kama ulivyosema mwenyewe ni kwamba hoja hii tukaijadili kwa akili iliyotulia na kuweka pembeni kabisa yale yote yanayotugawa na kuyazingatia zaidi yale mambo ya msingi yanayotuleta pamoja kama taifa.

Hebu na sikilize michango ya wenzetu wengine pia humu jamvini.


Asante. Tuko pamoja mkuu wa kazi
 

Uwezo Tunao

JF-Expert Member
Nov 14, 2010
6,942
0
Wanataaluma wanasheria, wanahistoria sociologists na taaluma nyinginezo humu, hebu tupeni majibu ya KITAALAM zaidi hapa. Iweje Tanzania iwe na KATIKA hadi ya TANO katika historia yake na zote ziwe zimezaliwa toka juu bila ya raia wenye nchi kushirikiswa moja kwa moja??

Je, kwenye taaluma zenu huko katiba inayoandikwa moja kwa moja na ile wanayoandokiwa na MADALALI, ni ipi ilio na gharama kubwa zaidi kwa mtazamo wa kipindi kirefu hasa ukichukulia mazingira yetu na katiba hizo lukuki ukilinganisha mazingira ya nchi nyinginezo??

Professors Shivji, Peter Maina, Baregu, Palamagamba, Drs Mvungi, Rwikiza, Rwitama, Bana, Mama Kombani na wengine wengi tu -- Vijana tunaomba maelezo yenu ya kina hapa tunavyokaribia kuandika Katiba Mpya ya SITA nchini.
 

Uwezo Tunao

JF-Expert Member
Nov 14, 2010
6,942
0
Kulingana na maelezo ya ndugu Zakumi alipokua akimjibu Mwanakijiji kwenye THREAD mojawapo humu huyu ndugu aliubui issues nyingine nzito ambazo nazo huenda zikawakuna vichwa watafiti na wanataaluma wengine Tanzania.

(1) Huyu bwana anahoji ni kwa nini KATIBA haikua mingoni mwa vitabu vya kipaumbele kwa Mwalimu Nyerere kukibeba licha ya Bibli tu na kile kitabu cha Azimio la Arusha, na Katiba ya CCM.

Je, viongozi wengine waliofuatia wao vitabu vyao vya kipaumbele ni vitabu gani hasa??? Je, kuna uwezekano hajawahi kutawaliwa kwa mujibu wa KATIBA ambazo nazo hatukushirikishwa kuzitunga???

(2) Issue ya pili alioibua huyu bwana ni katika kuhoji kule KATIBA YETU KUANDIKWA KWA LUGHA NGUMU ambayo inafahamika kwao tu WANASHERIA wetu.

Na akaongezea kwamba katika kujitafutia elimu zaidi juu ya mambo amegungua kwamba ni rahisi sana mtoto wa umri mdogo tu akaelezea hadhara anachokielewa baada ya kusoma katiba ya watu wa Marekani kuliko kumtaja kiongozi yeyote nchini kutueleza japo ka-kipengele kimoja ndani ya katiba yetu na nini maana anayopata mara baada ya kuisoma.

Mmmmhhh, haya mapungufu mawili kati ya mengine mengi tuliyokwishaelezwa na wengine wengi tu humu ni HATARI kweli kweli. Kwa maswali ya msingi ambayo sisi vijana tumeamua KUDADISI bila unafiki kwa ajili ya kuyarekebisha pindi tutakapoanza kuandika katiba mpya bila shaka pia yanaleta kiu kuona TANZANIAN SCHOLARS wao wanafahamu nini hapa na explanations vipi wanazoweza kutupa???

Mpaka hapa naona MADALALI KUTUANDIKIA KATIBA YA SITA Tanzania hapana kabisaaaa!!!!


_____________________________________________________

Maoni ya Ndugu ZAKUMI kwa Mwanakijiji juu ya Katiba yetu ya sasa

Mwanakijiji:

Nimesoma katiba ya Marekani. Nimesoma katiba ya Tanzania. Katiba ya Marekani pamoja na kuwa na zaidi ya miaka 200 ni rahisi kuisoma na kueleweka hata kwa mtu mwenye kiwango kidogo cha elimu. Mchukue mtoto wa miaka 16 wa Marekani na muulize mambo gani yaliopo kwenye Tangazo la uhuru na katiba, atakupa jibu.

Kwa Tanzania katiba ya nchi ni kitabu cha mwanasheria. Hivyo hata sisi tuliosoma siasa hatukupitia kitabu hicho. Hata baba wa taifa alikuwa anatembea na vitabu viwili tu: azimio la Arusha na Biblia. Hivyo kwa miaka mingi, katiba ya nchi ilikuwa si kitu cha kujivunia au kutilia maanani. Na kutokana na hayo, nchi imeendeshwa kwa mazoea tu. Na wengi wanachukulia katiba kama mfumo wa utawala. Lakini kimsingi katiba inaelezea taifa na watu wake.

Hivyo moja ya tatizo la katiba iliyopo sasa ni ugumu wake. Vitu vingi katika katiba ya sasa vimeelezewa kwa undani (in detail) na sio abstract. Hivyo tunatoa mzigo kwa vizazi vinavyokuja. Vizazi vinavyokuja ni lazima kutafsiri katiba kutokana na mazingira yao na sio ya sasa. Kwa mfano wa posti yako moja, katiba ya sasa inaonyesha mfumo wa uongozi wa serikali ya mapinduzi Zanzibar.
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom