Historia ya Julius Nyerere kwa maneno ya Abdallah Said Kassongo 1987

Mohamed Said

JF-Expert Member
Nov 2, 2008
20,913
30,255
SAFARI YA NYERERE SUMBAWANGA KAMA ALIVYONIHADITHIA ABDALLAH SAID KASSONGO 1987

TANU Youth League ya Tabora chini ya uongozi wa Abdallah Said Kassongo ilikuja kuwa tawi hodari sana na lenye mipango mikubwa Tanganyika nzima.

Kassongo alikuwa pamoja na wanachama wengine wa TANU Youth League kama Zena bint Malele, Jaffari Idd (aliyekuwa mpishi wa Nyerere katika mkutano wa kura tatu) Juma Salum Kisogo na Shaban Rukaya.

Miaka mitano ilikuwa imeshapita tangu kuasisiwa kwa TANU. Nyerere alikuwa amekwenda Umoja wa Mataifa mara tatu na alikuwa ametembelea takriban sehemu zote za Tanganyika isipokuwa Mpanda na Sumbawanga.

Makao makuu ya TANU iliona kuwa wakati ulikuwa umewadia kwa Nyerere kuzitembelea sehemu hizo na kukutana na wananchi kabla TANU haijapata serikali ya ndani.

Mwezi Machi, 1959 TANU Youth League Tabora iliombwa na makao makuu ya TANU kupanga safari ya Nyerere na kushughulikia mambo ya usalama wa rais wa TANU atakapokuwa katika ziara ya sehemu hizo.

Saadan Abdu Kandoro, katibu wa TANU Tabora na Rajabu Tambwe, mwenyekiti waliwataka Kassongo na kikundi chake kuchukuwa dhima ya mipango ya usalama wa Nyerere.

Kassongo alitakiwa kusafiri kwenda Mpanda na Sumbawanga kuwasiliana na uongozi wa TANU kule ili kufahamu hali ya hewa ya siasa sehemu zile na kupeleka taarifa Tabora ili uongozi wa TANU Tabora wawasilishe taarifa hiyo makao makuu ya TANU Dar es Salaam.

Kassongo alikuta hali ya hewa ya kisiasa muafaka sana kwa Nyerere kuzuru Mpanda na vijiji vyake.

Ilikuwa mipango aliyoikuta Sumbawanga ndiyo iliyomtia Kassongo wasiwasi.

Mjini Sumbawanga, Kassongo na wafuasi wake waliotangulia kule walistushwa walipoelezwa kuwa uongozi wa TANU chini ya Chief Dandis Ngua walikuwa wamepanga Nyerere abebwe mabegani kwenye machela kwa umbali wa takribani maili tano ili kuwawezesha watu wamuone vizuri.

Watu katika sehemu hizo walikuwa wamemsikia tu Nyerere lakini kamwe hawakupata kumwona uso kwa uso.

Shauku ya watu kwa ziara ya Nyerere ilikuwa kubwa sana. Mipango maalum ilikuwa ifanywe ili kuepuka msongamano na kukanyagana kwa watu watakapokuwa wakisukumana kumuona Nyerere.

Kwa kadri Kassongo alivyopendezwa na ile hamasa ya wananchi kutaka kumwona kiongozi wao, aliwasisitizia ukweli kwamba kwa kadri alivyomfahamu Nyerere, hawezi kamwe kukubaliana na mpango wao wa yeye kubebwa katika machela.

Nyerere katu hawezi kukubali kubebwa mabegani kama Wazungu walivyofanya kwa Waafrika katika siku za mwanzo za ukoloni.
Ilikuwa muhali kwa Nyerere kuwaruhusu watu wake wamuweke katika nafasi hiyo ya kudhalilisha hata kama kwa nia nzuri namna gani.

Lakini hayo yote yalikuwa nje ya hoja, muhimu kwa Kassongo ilikuwa kumbeba Nyerere juu ya vimo vya watu ilikuwa hatari sana kwa sababu wangelikuwa wanamweka wazi na hivyo kuweza kupigwa risasi.

Sumbawanga ilikuwa inapakana na Rhodesia ya Kaskazini.

Walowezi wa Rhodesia walikuwa na uadui mkubwa na harakati za Waafrika za kudai uhuru wao.

Kwa ajili hii eneo lile lilikuwa la hatari sana kwa mwanasiasa yoyote mzalendo achilia mbali Nyerere.

Majadiliano juu ya usalama wa Nyerere baina ya Kassongo na Chifu Ngua yalidumu usiku mzima na kulipopambazuka mipango ya usalama wa Nyerere ilikuwa imechunguzwa tena na tena na kukamilika.

Mpango wa kumbeba Nyerere kwenye machela ulifutiliwa mbali kutoka kwenye ratiba.

Kassongo akiwa ameridhika na ile mipango ya usalama kule Sumbawanga alisafiri kwenda Mpanda kumsubiri Nyerere.

Nyerere aliwasili Mpanda kwa garimoshi akifuatana na Rajab Tambwe, Saadan Abdu Kandoro na Sheikh Mussa Rehani.

Kulikuwapo na kundi kubwa sana la watu ndani na nje ya kituo cha garimoshi wakisubiri kumpokea Nyerere.

Aliposhuka tu kutoka garini ofisa mmoja wa Polisi Mzungu alikwenda mbele na kumpigia saluti Nyerere.

Lile kundi la watu lilishangilia.

Kitendo hicho kilikuwa hakina kifani.

Waafrika walikuwa hawajashuhudia Mzungu kuonyesha heshima kama hiyo kwa Mwafrika.

Siku iliyofuata Nyerere alihutubia mkutano wa hadhara.

Ilikuwa wakati akihutubia ule mkutano ndipo mwenyeji wake, Chifu Ngua, alipokea ujumbe wa haraka wa polisi kutoka kwa Gavana Richard Turnbull ambao ulimtaka Nyerere kurejea Dar es Salaam mara moja kwa mashauriano na serikali ili kuteuwa Waafrika watano kuingia katika Baraza la Kutunga Sheria ili wajiunge na baraza la mawaziri kama mawaziri wa serikali.

Pamoja na umuhimu wa ujumbe huo Nyerere alimsisitizia Chifu Ngua kwamba ingebidi afike Sumbawanga kuonana na wananchi hata kama itabidi atoe hotuba yake usiku wa manane.

Nyerere aliwasili Sumbawanga wakati wa magharibi kwa Land Rover ya TANU na mara moja alipofika Kassongo haraka haraka alianza kufunga vipaza sauti na kufunga vyombo vyote vya kuhutubia mikutano bila kujali kuwa usiku ulikuwa ukikigubika kiwanja cha mkutano.

Nyerere alitoa moja ya hotuba zake zenye kuvutia sana juu ya maovu ya ukoloni akiwa amesimama juu ya Land Rover.

Nyerere alizungumza kwa saa nne, hadi kupita usiku wa manane.

Hakuna mtu yeyote iliyosogea au kunyanyua mguu kwenda nyumbani.

Baada ya mkutano Kassongo na wafuasi wake walimsindikiza Nyerere mpaka Abercon, mji wa mpakani ndani ya Rhodesia ya Kaskazini ambako ndege maalum ilikuwa ikisubiri kumchukua hadi Dar es Salaam kwa ajili ya mkutano wake Government House na Gavana Richard Turnbull.

Nyerere alimpa Turnbull orodha ya TANU ya wajumbe wake wa Baraza la Kutunga Sheria: Chifu Abdallah Said Fundikira, Dereck Bryceson, Enesmo Eliufoo, Amir Jamal na George Kahama kujiunga na serikali kama mawaziri.

Historia hii na mengi yasiyofahamika katika historia ya Julius Nyerere, TANU na uhuru wa Tanganyika unaweza kusoma katika kitabu cha maisha ya Abdulwahid Sykes (1924 - 1968).

Picha: Abdallah Said Kassongo, Abdallah Said Fundikira, Nyerere na Amir Jamal.
 
Kassongo.jpg

Abdallah Said Kassongo.
 
Back
Top Bottom