Historia ya Dr. Livingston

DIDAS TUMAINI

JF-Expert Member
Nov 11, 2014
232
618
Tarehe 2 January mwaka 1845, mwanadada Mary Moffat alifunga ndoa na kijana David katika harusi iliyofanyika huko nchini Afrika Kusini. Mary ni mtoto wa kwanza kati ya watoto kumi wa mzee Robert Moffat, raia wa Scotland aliyekuja Afrika kusini kufanya kazi ya umishionari na kuwa mtu wa kwanza kutafsiri biblia kwenda katika lugha ya setswana inayozunguzwa na watu wa Botswana na baadhi ya waafrika Kusini.

Mary Moffat kama anavyoonekana upande wa kulia pichani, alizaliwa mwaka 1821 huko nchini Afrika Kusini akichukua jina la mama yake ambaye naye anaitwa Mary Smith. Mwaka 1839 aliondoka pamoja na wazazi wake kurudi Uingereza na kukaa huko hadi mwaka 1843 waliporudi tena nchini Afrika Kusini katika eneo linaloitwa Kuruman. Hapa ndio kituo cha kwanza cha wamishenari wa shirika la 'London Missionary Society LMS' na moja kati ya vitu vilivyowafanya LMS waje hapa ni ile bwawa la chemchem ya maji safi iliyopewa jina la 'Jicho la Kuruman' aliyekuwa chifu wa eneo lile 'kurumade'. Watu wa kabila la tswana waliita bwawa lile 'Gasegonyane' yaani 'kibuyu cha maji yanayotokota'. Ndio maana hata leo hii mji wa Kuruman upo ndani ya manispaa inayoitwa Gasegonyane.

Haya tuendelee!..Baada ya familia ya Moffat kurudi Afrika kusini mwaka 1843, binti Mary Moffat akapata kazi ya kufundisha hapo mjini Kuruman. Akiwa hapo Kuruman, Mary alijikuta amezama kwenye mto wa mahaba uliomsomba na kwenda kumtupa kwenye bahari ya mapenzi na kumwacha akiogelea mithili ya samaki kabla ya kunaswa katika ndoa'no ya kijana aliyeitwa David msomi mwenye taaluma ya udaktari raia Scotland aliyekuja Afrika kufanya kazi ya umishenari kupitia shirika la London Missionary Society LMS'. Ndoa yao ilifanyika tarehe 2 January 1845 hukohuko nchini Afrika Kusini.

Kijana David, kama anavyoonekana upande wa kushoto pichani ni mmishenari mashuhuri sana hapa barani Afrika akijulikana kwa jina maarufu la Dr David Livingston aliyefanya kazi ya kueneza dini ya ukristo pamoja na kufanya upelelezi 'exploration' katika bara letu la Afrika na matokeo yake tukajikuta tumeangukia mikononi mwa wakoloni. Aliingia hapa Tanganyika na kufika hadi ujiji Kigoma mwaka 1871 ambako hapo alikutana na mpelelezi mwenzake Henry Stanley. Leo hii ukienda kigoma utaona kumejengwa mnara kama kumbukumbu ya mahali walipokutana Stanley na Livingston.

Nirudi kuhitimisha kwa Mary Moffat na mumewe Dr Livingston ambao hadi kufikia mwaka 1852 walikuwa wamezaa watoto watano, Robert Agnes, Thomas, Elizabeth na William. Na katika kipindi hiko Mary alikuwa akiongozana na mumewe David Livingston katika safari zake za kimishenari na kipelelezi na hata watoto wake wawili walizaliwa katikati ya safari hizo ikielezwa kwamba wakati wa kujifungua, Mary alisaidiwa na mumewe, Livingstone ambaye ni daktari by a profession.

Mwaka 1852, Livingston ilibidi aipeleke familia yake ulaya hususani kwa ajili ya masomo ili yeye abaki Afrika kuendelea na misafara ya kipelelezi huko Zambezi ambapo alitumia takribani miaka minne. Baada ya hapo, mwaka 1856, Dr Livingstone alirudi Uingereza ambapo alipokelewa kishujaa sana kwa kazi nzuri aliyoifanya ya kupelekeza bara la Afrika. Akapewa tuzo ya dhahabu kutoka kwa shirika la 'Royal Geographic Society' akawa mtu maarufu sana wanaita 'celebrity, akitoa mihadhara kwenye vyuo na hata kutunukiwa shahada ya heshima 'Honorary degree' kutoka chuo kikuu cha Oxford na Glasgow.

Katika kipindi hicho tangu arudi Uingereza alikuwa pamoja na familia yake. Alikaa nao kwa muda wa miezi 15 hadi mwaka 1858 pale aliporudi tena Afrika, safari hii akiwa mtu maarufu huku msafara wake ukifadhiliwa na serikali ya uingereza, sio tena na shirika la LMS ambalo ameshamaliza mkataba nao. Katika msafara huu pia Dr Livingstone alikuja Afrika pamoja na mkewe Mary. Lakini kutokana na kuwa mjamzito, ilibidi Mary abaki mjini Kuruman kwa wazazi wake ili mumewe Livingstone aendelee na msafara wake huko Zambezi. Huko Karuman, mwaka huo 1858, Mary alijifungua mtoto wa sita jina lake Anna Mary. Miaka michache baadae mwaka 1862 akaenda kuungana na mumewe huko Zambezi ambapo kutokana na uwepo wa magonjwa ya Malaria, Mary alifariki tarehe 27 April 1862 katika eneo la Shupanga.

Miaka miwili baadae, Dr Livingstone alirejea Uingereza safari hii hakupokelewa kama mwanzo kwani msafara wake haukuwa na manufaa sana kama ule wa mwanzo kwani serikali haikumpa sapoti kama awali. Akajipanga tena mwaka 1866 akarudi Afrika akiwa na bajeti ndogo tofauti na ile ya mwanzo, safari hii akitegemea sapoti kutoka kwa wafanyabiashara wa kiarabu akiwemo TipuTipu. Katika msafara huu, Livingstone alilenga kutafuta chanzo cha mto Nile. Alifika Msumbiji, Zanzibar na kuingia bara na kufika hadi ujiji. Kwa miaka mitano huko Uingereza hawajui Livingstone anaendeleaje kwani hakuwa anarudisha mrejesho huko Ulaya. Hivyo ilimbidi shirika moja la habari la Marekani, kumtuma mwandishi na mpelelezi wa Uingereza Henry Stanley kwenda Afrika kumtafuta Dr Livingstone 'aliyetokomea Afrika asijulikane ni wapi alipo' ukizingatia kwamba ni mtu maarufu cerebrity ulimwenguni.

Ndipo mwaka 1871, Stanley akafatilia na hatimaye kumpata huko Ujiji Kigoma. Walikaa kwa miezi kadhaa kufatilia chanzo cha mto Nile lakini hawakufanikiwa. Stanley alimsisitiza Livingstone warudi Uingereza lakini Livingstone akakataa kurudi hivyo ilibidi waachane hapo na Stanley kurudi zake ulaya akichapisha kitabu mwaka 1872 kilichoitwa 'How I found Livingstone' kilichohuisha umaarufu wa Livingstone ambaye hakusikika kwa muda mrefu. Baada ya kuachana na Stanley, Livingstone akaendelea kupeleleza bara la Afrika safari hii akielekea kusini mwa ziwa Tanganyika. Lakini kutokana na maradhi ya kiafya yaliyokuwa yanamsumbua, kwa shida sana akisaidiwa na vijana wake wa kiafrika (Susi na Chuma)alifika nchini Zambia katika kijiji cha Chitambo ambapo alifariki hapo siku ya mei mosi 1873.

Baada ya kufariki Livingstone, wale wasaidizi wake, 'Susa na Chuma', waliuondoa moyo wa Livingstone na kisha kuuzika chini ya mti. Mwili wake ukakaushwa juani kwa muda wa wiki mbili kisha ukafungwa magome ya miti, tayari kwa ajili ya kuusafirisha kuelekea Zanzibar. Susi na Chuma waliubeba mwili wa Livingstone hadi Bagamoyo, hapo ukapokelewa na wamishionari wengine hadi Zanzibar kabla ya kupakizwa kwenye meli hadi Uingereza na kuzikwa kwenye kanisa la Westminster Abbey mjini London.

Na huo ndio ukawa mwisho wa safari ya mpelelezi (explorer), mmishenari na daktari David Livingstone aliyezaliwa mwaka 1813 huko Scotland.

Mwisho.

________________

Ahsanteni

Imeandikwa na
KichwaKikuu.
FB_IMG_1581199921634.jpeg


Sent using Jamii Forums mobile app
 
Hawa jamaa sijui kipindi hicho alipataje mawasiliano na mkewe aliyekuwa SA wakati yeye akiwa Zambia.

Na huyo Henry Stanley alijuaje kuwa Livingston yuko pale Ujiji-Kigoma? Na walisafirije wakati huo huku vita vya makabila yaliyokuwa yakichochewa na Arab Slave Masters kupitia machifu vikiwa vimepamba moto.

NB: Mateka wa vita hivyo vya kikabila walikuwa wakiuzwa utumwani kwa waarabu kwa amri ya machifu dikteta wa zama hizo.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom