Hili la wabunge kudai posho zaidi: Ni historia hasi inayojirudiarudia | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Hili la wabunge kudai posho zaidi: Ni historia hasi inayojirudiarudia

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by nngu007, Nov 17, 2011.

 1. nngu007

  nngu007 JF-Expert Member

  #1
  Nov 17, 2011
  Joined: Aug 2, 2010
  Messages: 15,871
  Likes Received: 56
  Trophy Points: 145
  • Thursday, November 17, 2011, 7:47
  • Rai-habari
  *Zama hizo malipo ya Wabunge yalikuwa Sh 4,000 tu
  *Mwalimu Nyerere ‘alifyatuka' kuhusu malipo haya

  Na Chrysostom Rweyemamu

  HISTORIA inaendelea kujirudia katika Bunge letu. Ni historia hasi isiyo na tija kwa taifa letu na wananchi wake, wakiwamo wapiga kura wanaowapeleka wabunge wetu bungeni.

  Mwanzoni mwa wiki iliyopita wabunge wameonyesha kwa mara nyingine jinsi wasivyojali wale waliowapeleka bungeni. Wanataka wao (Wabunge) waongezewe posho eti kwa sababu maisha yamepanda sana, na kwamba shilingi ya Tanzania inaendelea kuporomoka thamani kwa kasi.

  Ni kweli maisha yamepanda mno, na shilingi yetu thamani yake imedorora mno. Lakini wabunge hawa si ni wawakilishi wa wapiga kura wao? Je, maisha yanapanda kwa wabunge hao tu?

  Je, wabunge hawa huwa wananunua mahitaji yao wapi, kama si katika maduka na masoko ya vyakula yale yale ambako wananchi wote hufuata mahitaji hayo? Na wabunge kazi yao hasa ni nini bungeni?

  Mojawapo ya kazi zao si ni kuisimamia Serikali idhibiti mfumuko wa bei? Sasa kudhibiti mfumuko wa bei ni wao kujipandishia posho? Baada ya hapo wapiga kura wao, ambao wengi ni walalahoi, wafanyeje?

  Hivi ni kweli wabunge hawa hawajui kuwa nchi yetu hivi sasa inapitia katika kipindi kigumu cha hali mbaya ya uchumi, na kwamba wananchi wengi mijini na vijijini wanapata taabu sana kupata angalau mlo mmoja kwa siku? Kama hawajui, wako bungeni kumwakilisha nani? Kama wanajua, basi hawaguswi kwa namna yoyote na mateso waliyonayo wapiga kura wao!

  Hivi ni kweli wabunge hawa hawajui kuwa hospitali nyingi nchini hazina dawa? Hawajui kuwa watoto wanakaa chini shuleni, hawana vitabu na walimu na vifaa vingine vya kufundishia? Hawajui kuwa mahakama zetu ziko hoi kutokana na uhaba wa fedha, na majengo yake mengi ni aibu tupu? Hawajui kuwa wanafunzi wengi wa vyuo vikuu hawapati mikopo ya elimu? Hawajui kuwa wanafunzi wetu wanasomea chini ya miti na katika madarasa ya mbavu za mbwa?

  Hawajui kuwa hivi sasa Serikali inatumia fedha nyingi sana kununua mafuta ya kuendesha mitambo ya kuzalisha umeme katika hali ya sasa ya upungufu mkubwa wa umeme? Hawajui kuwa ujenzi wa kilomita 2,405 za barabara umesimama kutokana na makandarasi kudai malimbikizo ya Sh bilioni 287? Kuna matatizo lukuki ya msingi ambayo Wabunge wetu tungetarajia wangeanza nayo ili yatatuliwe.

  Ndiyo, kwa kuweka kipaumbele wao kupandishiwa posho na mishahara, ni ukosefu wa uzalendo na kuendekeza ubinafsi kwa kiwango cha kutisha!

  Kwa kweli kikao cha Bunge cha wiki iliyopita ambacho sehemu kubwa ya mjadala ndani ya Bunge ilihusu posho zaidi kwa wabunge kilitia kinyaa, ambapo baadhi ya wabunge waliwataka wenzao wawapuuze wale wanaopinga nyongeza ya posho!

  Madai kwamba maslahi wanayoyapata wabunge wetu kuwa hayalingani na wanayoyapata wenzao katika nchi jirani yana ‘matege na makengeza' ya kutisha kwa sababu wabunge hawa hawajui kuwa uchumi wetu hivi sasa uko ‘kwenye mawe' kinyume na ilivyo kwa majirani zetu.

  Kwa majirani wetu Kenya, kwa mfano, uchumi wao umejikita kwenye misingi mizuri ya sekta ya utalii na viwanda ambavyo vinaingiza fedha nyingi za kigeni. Hapa kwetu tumeamua kujikaanga wenyewe kwa kuingiza bidhaa nyingi nchini kutoka nje, tena nyingine za ajabu kabisa, wakati tunauza nchi za nje bidhaa kidogo!

  Kama katika kushadidia na kutoa hoja ya kuhalalisha kupandisha viwango vya posho na mishahara, mmoja wa wabunge alidhani anatoa hoja kuntu kwa kudai kuwa amepata mialiko 26 ya kwenda kuchangia ujenzi wa shule na shughuli nyingine za maendeleo katika jimbo lake, na kwamba shughuli hizo zinamhitaji atoe fedha kama mbunge. Baadaye aliuza bungeni: "Fedha hizi nitazipata wapi?".

  Wabunge wenzake waliozungumzia suala hili, hakuna aliyezungumzia matumizi ya fedha za Mfuko wa Jimbo ambazo wabunge wote wenye majimbo wamepewa! Mimi najiuliza, hivi wabunge wetu bado wanadhani Watanzania ni wale wale wa miaka ya 6o. Hawasomi alama za nyakati na kuona yanayotokea hivi sasa kila kona ya nchi hii?

  Suala la malipo ya Wabunge, hasa la posho lilikuwa limeibuka wakati wa mkutano wa Bunge kuhusu bajeti miezi miwili iliyopita, kwa hoja ambayo chimbuko lake alikuwa Mbunge wa Jimbo la Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto, ambaye alisusa posho za vikao akasema si sahihi kwa Wabunge kulipwa posho wakati tayari wanalipwa mishahara kwa kazi hiyo.

  Wabunge wengi walipinga msimamo huo kwa kudai kuwa wanaokataa posho hizo wana vyanzo vingine vya mapato. Hao ndio wabunge wetu.

  Lakini wakati Serikali ilipoongeza Sh 2,500 kwa wafanyakazi wa kima cha chini, wabunge waliitaka Serikali hiyo hiyo kuongeza posho na mishahara yao kwa madai kuwa wanaishi maisha magumu na kutegemewa na wananchi wengi.

  Hoja hiyo iliiibuka tena baada ya mbunge wa Konde, Khatib Said Haji (CUF), alipokuwa akichangia hotuba ya bajeti ya Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa mwaka 2011 / 2012.

  Haji alisema posho na mishahara ya wabunge viongezwe kwa kuwa wabunge wanaishi maisha ya taabu huko wanakotoka, na wamekuwa wakipambana na matatizo ya wananchi ambayo bila fedha hayatatuliki.

  Mwenyekiti wa Bunge, George Simbachawene, aliunga mkono hoja ya mbunge huyo kwa kusema kuwa jambo la kuboresha maslahi ya wabunge ni muhimu katika mazingira ya sasa. Simbachawene hakuendeleza hoja hiyo mbali na kusifu mchango wa mbunge huyo kuwa ni mzuri sana wenye lengo la kuangalia maslahi na mustakabali wa wabunge.

  Zitto Kabwe, alipopata nafasi ya kuchangia hotuba ya bajeti hiyo, aliwarushia makombora wabunge wenzake kwa kuwataka wawe na huruma na waelewe matatizo ya wananchi, hasa katika kipindi hiki wanachokabiliwa na matatizo lukuki.

  Zitto, alisema ni ajabu na aibu kwa wabunge kutaka kuongezewa posho na mishahara wakati hivi karibuni serkali ililazimika kutenga Sh trilioni 1.2 kwa ajili ya mpango wa dharura wa kukabiliana na tatizo la mgawo wa umeme unalolikumba taifa.

  Alisema si sahihi kwa wabunge kufikiria maslahi yao wakati wananchi wanaishi maisha magumu, hivyo ni vema wakajielekeza kushirikiana na wananchi kwenye matatizo.

  Alibainisha kuwa inasikitisha kwa mbunge anasimama bungeni na kudai nyongeza ya posho na mishahara pasi na uchungu na maisha ya wananchi.

  Hata hivyo, Zitto alikatishwa na zomea zomea ya wabunge walioonekana kukerwa na mchango wake wa kukataa posho na mishahara ya wabunge kuongezwa.

  Yeye aliwaambia kuwa "hata mkizomea, mimi sijali, ukweli ndio huo niliousema, ni lazima tuonyeshe tunawajali wananchi wetu, si kila kukicha tunasimama hadharani na kutaka maslahi yetu yaboreshwe".

  Posho za vikao vya wabunge kwa hivi sasa ni Sh 70,000; fedha ya kujikimu kwa siku Sh 80,000 ambapo kwa siku kila mbunge hulipwa 170,000.

  Mshahara wa mbunge kwa mwezi Sh milioni 2.3 ambazo hukatwa kodi ya Sh 588,000; na kiasi wanachokwenda nacho nyumbani ni Sh milioni1.7, fedha hizo ni nje ya marupurupu mengine ambapo kwa mwezi hupewa kiasi kisichopungua Sh milioni saba (7).

  Wabunge wetu kudai mishahara na marupurupu makubwa si jambo geni. Pamekuwapo na madai kama hayo tangu wakati wa uongozi wa Mwalimu Julius Nyerere.

  Kuna kipindi Mwalimu Nyerere alitishia kulivunja Bunge ili Wabunge warudi kuwauliza wapiga kura wao kama waliwatuma kudai maslahi binafsi.

  Wakati huo Wabunge walikuwa wanapata kiasi cha Sh 4,000 kwa mwezi. Walitaka, pamoja na mambo mengine, kuongezwa mshahara na kulipwa Sh 40,000 kila muhula wao wa miaka mitano unapoisha. Wakati huo hizo zilikuwa ni fedha nyingi sana, tena sana.

  Aidha, mwaka 1966 wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Mlimani) ‘walimchefua' sana Mwalimu; walikuwa wanapinga kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) wakidai kuwa huo "ulikuwa ni utumwa". Hawakuishia hapo, waliorodhesha mambo mengine mengi, likiwamo la kuboreshwa kwa chakula chao na kupewa siagi ya kupaka kwenye mikate.

  Walidai ya kuwa viongozi wa Serikali walikuwa wanalipwa mishahara mikubwa, ambayo walikuwa wanaona ‘ntimanyongo' kuboresha maisha ya wanachuo. Lakini kauli iliyomkasirisha zaidi Mwalimu ni ile ya kusema kuwa "maisha waliyokuwa wanaishi afadhali wakati wa mkoloni"!

  Wanafunzi wa shule za sekondari jijini Dar es Salaam walifanya maandamano kuwalaani wanafunzi wa Mlimani. Wananchi pia waliandamana hadi Jangwani kupinga kejeli hiyo.

  Akipokea maandamano ya wanafunzi pale ofisi kuu ya TANU Lumumba (sasa CCM), Mwalimu alikubaliana na wanachuo kuwa ni kweli mishahara ya viongozi ilikuwa mikubwa mno kwa nchi masikini kama yetu.

  "Our salaries are too high for a godamned poor country," alifoka, akimaanisha " kuwa mishahara yao ilikuwa mikubwa mno kwa nchi masikini (kama Tanzania)". Alitoboa siri kwamba yeye Rais alikuwa akipata mshahara wa Sh 4,000 bila kodi. Alisema hiyo ilikuwa fedha nyingi sana ukichukulia kwamba alikuwa akilipiwa kila kitu, yeye na familia yake.
  Hapo hapo akatangaza kupunguza mshahara wake na ya viongozi kwa asilimia mbili (2%). Uongozi ni kuonyesha njia.

  Pale Jangwani, Mwalimu aliwaambia wananchi kwamba asingeweza kuwapa siagi wanachuo wakati wananchi wa Dodoma walikuwa hawana maji ya kunywa! Mwalimu alikuwa kiongozi. Alifikiria watu wake kwanza.

  Rafiki yangu sana, kaka yangu kwa umri na mwandishi mkongwe mwenzangu, Balinagwe Mwambungu, aliwahi kunisimulia kuwa siku moja waandishi wa habari walikwenda kumpokea Mwalimu Nyerere kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dar es Salaam (sasa Uwanja wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere) akitoka safari ya nje kikazi.

  Alimwuliza Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam wa wakati huo, Mustafa Songambele: " Mustafa, lipo?" Naye kwa haraka alijibu: "Lipo". Baadaye waandishi wa habari wakamwuliza Songambele: "Lipo nini?" Aliwaambia huku akicheka: "Sembe." Mwalimu Nyerere alipokuwa akitoka safari ya nje, alikuwa anauliza kwanza kama Dar es Salaam kuna chakula.

  Watu walijua kuwa kumbe Mwalimu hata alipokuwa ‘anakula kuku kwa mrija majuu', mawazo yake yalikuwa nyumbani akiwaza kama watu wake walikuwa na chakula. Huyo ndiye kiongozi wa watu.

  Hebu tuangalie miaka ya hivi karibuni na madai ya Wabunge wetu. Wanasema mshahara na marupurupu wanayopewa hayatoshi, na wala hayalingani na hadhi yao kama viongozi! Wanataka wajengewe ofisi majimboni mwao, Serikali ilipe mishahara ya madereva, makarani na watumishi wao wa ndani, watibiwe kwa gharama za Serikali kwenye hospitali binafsi zinazolingana na hadhi yao – wao na familia zao; na waliwahi kwenda mbali zaidi kwa kutaka uhai wao bungeni uwe miaka saba badala ya miaka mitano ya sasa! Kwa maana nyingine walitaka kubadilisha Katiba ya nchi iweze kubeba matakwa yao hayo!
  Mwalimu alikataa kuwapa siagi wanachuo wa Mlimani kwa sababu alikuwa akifikiria kwanza ni namna gani angeweza kuwapa wananchi kitu cha lazima kwa maisha yao, yaani maji.
  Wabunge wetu walio wengi, bila kujali matatizo yanayoikabili nchi na wananchi wake kwa sasa – ukame na makali yanayotokana na mgawo wa umeme – hawako tayari kupewa magari ya kawaida kuwawezesha kufanya shughuli zao, wanataka ‘mashangingi ya bei mbaya'.

  Wananchi wengi majimboni kwao hawana maji. Sehemu nyingi wananchi waliowapigia kura (ili wabebe kero zao) wanakabiliwa na njaa. Hawana chakula! Wanatafunwa na umasikini wa kupindukia na maradhi.

  Watoto wao wengi hawasomi kutokana na umasikini. Maelfu kwa maelfu ya vijana wako vijiweni kwa sababu hawana ajira!

  Hawa ndio wabunge wetu! Ni wale wale tuliowapigia kura. Ni wale wale tuliodhani na kutarajia kwamba watapigania maisha bora kwa kila Mtanzania. Ni wale wale tulioshuhudia hivi karibuni wanataka ‘kumtoa roho' Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto, alipotaka posho za vikao za wabunge zisitishwe ili fedha hizo zielekezwe katika kutatua kero za wananchi!

  Hii inanikumbusha usemi wa aliyekuwa Mbunge wa Bukoba Mjini (CCM), Samwel Luangisa, aliyesema wakati wa moja ya kampeni zake za kugombea Ubunge miaka ya 80 kuwa wananchi wasije wakakosea kumpeleka bungeni mtu mwenye njaa.

  Alitoa mfano wa kumtuma mtu mwenye njaa kuangua embe, akisha kufika juu ya mti, atakula maembe kwanza yeye mwenyewe, na akisha kushiba ndipo atakapowakumbuka waliomtuma. Wakati huo tayari muda wa miaka mitano utakuwa umekwisha, naye hajafanya lolote! Falsafa yake hiyo kwa kiasi kikubwa iliwafanya wapiga kura wa Bukoba mjini wampe kura na kuweza kumwangusha mpinzani wake wakati huo.

  Kuna habari ya aliyekuwa Rais wa Bolivia, Evo Morales, ambaye alitangaza kupunguza mshahara wake na watumishi wote wa Serikali. Alisema fedha itakayopatikana itumike kuajiri madaktari na walimu. Huyu ni kiongozi aliyebeba kero za watu wake.

  Hapa nyumbani, mwanzoni mwa utawala wa Rais Jakaya Kikwete alielekea kuyaelewa matatizo na kero za Watanzania. Katika kipindi kifupi cha mwezi mmoja, alidhihirisha kwamba ni mtu wa watu aliyekerwa na hali duni ya wananchi wake. Alijitambulisha kuwa ni kiongozi asiyeweka ‘umimi' mbele. Baada ya awamu ya kwanza ya uongozi wake, bila shaka wananchi wamempima na wanaelewa upande wa kumweka hivi sasa.

  Inakatisha tamaa kusikia kwamba wale tuliowapa kura zetu ili wasaidiane na Serikali kutafuta mbinu za kukabiliana na matatizo sugu ya wananchi, sasa wako juu ya mwembe, wanataka washibe wao kwanza, hata wakati huu wa shida ya umeme na njaa! Hawako tayari kujitoa mhanga kwa ajili ya watu waliowapa uongozi!

  Tunasoma kuwa wakati wa Mapinduzi ya Kiboshelviki nchini Urusi, ‘kulianguka' njaa kali sana. Mkate ulikuwa haupatikani isipokuwa kwa mgawo, tena wa nadra. Kiongozi wa mapinduzi hayo, Vladmir Lenin, aliwahi kuzirai kwa njaa. Kisa? Mgawo aliokuwa akipelekewa ofisini alikuwa akiwapa watu waliokuwa wanakwenda kwake kumlilia njaa! Kiongozi huyu alibeba matatizo ya watu wake kuwa ya kwake.

  Sasa watu wanauliza: Hivi wabunge wanapokubali kupitishiwa marupurupu mengi, yakiwamo ‘mashangingi', wanadhani nani anayagharimia? Wanaidai Serikali, na Serikali inatoa wapi fedha? Si zinatokana na kodi za wananchi ambao wengi wao ni hoi bin taaban! Wanapoidai Serikali, si wanaiambia itutoze kodi zaidi, na mlalahoi ambaye tayari amefikia kikomo cha ufukara si ndio utakuwa mwisho wake? Ni maisha bora kwa kila Mtanzania au kejeli?

  1. "Kama Katika kushadidia na kutoa hoja ya kuhalalisha kupandisha viwango vya posho na mishahara, mmoja wa wabunge alidhani anatoa hoja kuntu kwa kudai kuwa amepata mialiko 26 ya kwenda kuchangia ujenzi wa shule na shughuli nyingine za maendeleo katika jimbo lake, na kwamba shughuli hizo zinamhitaji atoe fedha kama mbunge. Baadaye aliuza bungeni: ‘Fedha hizo nitazipata wapi?'…"

  1. "Wabunge wenzake waliozungumzia suala hili, hakuna aliyezungumzia matumizi ya fedha za Mfuko wa Jimbo ambazo wabunge wote wenye majimbo wamepewa! Mimi najiuliza, hivi wabunge wetu bado wanadhani Watanzania ni wale wale wa miaka ya 6o. Hawasomi alama za nyakati na kuona yanayotokea hivi sasa kila kona ya nchi hii?"

  3. "Posho za vikao vya wabunge kwa hivi sasa ni Sh 70,000; fedha ya kujikimu kwa siku Sh 80,000 ambapo kwa siku kila mbunge hulipwa 170,000.
  Mshahara wa mbunge kwa mwezi Sh milioni 2.3 ambazo hukatwa kodi ya Sh 588,000; na kiasi wanachokwenda nacho nyumbani ni Sh milioni1.7, fedha hizo ni nje ya marupurupu mengine ambapo kwa mwezi hupewa kiasi kisichopungua Sh milioni saba (7)"


   
Loading...