Hiki ndiyo kitu kimoja kinachokutofautisha na Viumbe wengine na jinsi ya kukitumia kwa manufaa yako

Makirita Amani

JF-Expert Member
Jun 6, 2012
1,781
3,074
Ndege wana mabawa kwa ajili ya kuruka hewani,

Samaki wana mapezi kwa ajili ya kuelea majini,

Simba wana meno makali kwa ajili ya kurarua nyama,

Chui wana mwendo mkali kwa ajili ya kukamata mnyama yeyote,

Twiga wana shingo ndefu kwa ajili ya kula majani yaliyo juu,

Miti iliyopo jangwani ima majani madogo kwa ajili ya kupunguza upotevu wa maji.

Kila kiumbe hai, kina tabia fulani ambayo inakiwezesha kiumbe hicho kuvuka magumu yaliyopo kwenye mazingira yake na kuendelea kuwa hai licha ya changamoto mbalimbali ambazo kiumbe huyo anakutana nazo.

Je, unajua ni kitu gani ambacho sisi binadamu tunacho na kinatuwezesha kukabiliana na mazingira yetu? Unajua ni kitu gani ambacho kinatuwezesha sisi kuepuka kifo na kuendelea kuwa hai kama jamii nzima ya binadamu?

Kitu hicho ni akili.

nguvu ya akili


Sisi binadamu ndiyo viumbe pekee ambao tuna akili, viumbe pekee ambao tunaweza kufikiri na kufanya maamuzi kulingana na hali fulani ambayo tunaipitia na kisha kupata njia au hatua sahihi za kuchukua.

Hatuwezi kuruka kama ndege, lakini akili zetu zimetuwezesha kutengeneza vyombo vinavyoruka hewani.

Hatuwezi kuelea majini kama samaki, lakini akili zetu zimetuwezesha kutengeneza vifaa vya kuelea majini.

Hatuna meno makali kama simba, lakini akili zetu zimetuwezesha kuwa na moto wa kupika na kulainisha chochote kigumu.

Akili tulizonazo ndiyo kitu chenye nguvu kuliko vyote duniani, ndiyo maana sisi binadamu tunaweza kuwafuga wanyama wengine.

Wanyama wengine wanaongozwa na tabia na silika, hivyo ni rahisi kuwatega na kuwafuga.

Lakini sisi binadamu tuna uwezo wa kufikiri na kubadili chochote tunachofanya, ndiyo maana ni vigumu sana kwetu kutegeka, kama kweli tutatumia akili zetu.

Jambo la kushangaza kuhusu binadamu
Mpaka sasa umeona ni kitu gani kinatufanya sisi kuwa juu ya viumbe wengine.

Sasa pata picha, ndege amepata mtoto wake na wakati anakua ndege huyo akawa anamvunja mtoto wake mabawa ili asiweze kuruka.

Au samaki anapata mtoto na kuharibu mapezi yake,

Simba anamng’oa mtoto wake meno.

Utawaelewaje wanyama hao kwa kufanya hivyo? Yaani mzazi anachagua kuondoa kitu pekee kinachomwezesha mtoto wake kuishi! Je huo siyo uuaji?

Sasa utawashangaa sana wanyama wanaofanya hivyo, lakini hicho ndiyo binadamu tunakazana kufanya.

Sisi binadamu, ni mafundi wazuri sana wa kuhakikisha tunawazuia wengine wasitumie akili zao.

Kwa kuwa tunajua akili ndiyo inampa mtu nguvu, basi tunahakikisha hakuna anayeitumia akili yake, ili iwe rahisi kwa watu kufuata mkumbo.

Hivyo watu wote wanaopata mamlaka au madaraka fulani, huwa wanahakikisha wale walio chini yao hawatumii akili zao.

Hili linaanzia kwenye malezi, wazazi kuhakikisha watoto wao hawafikiri,

Inaenda kwenye ajira, waajiri kuhakikisha wafanyakazi wao hawafikiri,

Inaenda kwenye jamii, kwa kila mtu kutegemea mwenzake afuate mkumbo na siyo kufikiri peke yake.

Na inaenda kwenye taifa na dunia kwa ujumla, kwa viongozi kuhakikisha raia wao hawafikiri kabisa.

Binadamu asiyefikiri kwa kutumia akili yake ni rahisi kutawaliwa, ni rahisi kutapeliwa, kuonewa na kutumikishwa.

Binadamu anayetumia akili yake kufikiri, hawezi kutapeliwa, hawezi kuonewa, hawezi kutapeliwa na hatakubali kutumikishwa.

Hivyo kama unataka kuwa na uhuru kamili wa maisha yako, na unataka kupata mafanikio makubwa, basi kuna kitu kimoja tu cha kufanya, fikiri kwa akili yako mwenyewe. Jua kile kilicho sahihi na ufanye hicho na acha kufuata mkumbo.

Kitabu cha Ayn Rand kinachoitwa Atlas Shrugged ni riwaya ambayo inaonesha madhara makubwa yanayoweza kutokea na ataifa likaangamia kama watu wataacha kufikiri na kufuata mkumbo.

Pale watu wanapoachana na ukweli na kufuata mkumbo, pale wanapoacha kufanya kilicho sahihi na kufanya kile ambacho wengine wanafanya, pale maoni ya wengi yanapokuwa ndiyo hukumu, ndipo watu wanageuka kuwa wanyama na kumalizana wao kwa wao.

Riwaya hii inaonesha uhalisia wa hali ambayo tunapitia kwa sasa duniani, ambapo tunaona matatizo mengi yakijitokeza, mzizi wake ukiwa ni watu kukataa kufikiri.

Tumekuwa rahisi kuacha akili zetu na kufuata kile ambacho wengi wanafanya, hata kama siyo sahihi.


atlas shrugged


Atlas Shrugged kwa ufupi.

Riwaya ya Atlas Shrugged ni hadithi ya taifa la marekani ikionesha jinsi mabadiliko ya sera za kiuchumi yanavyoweza kuliangamiza taifa.

Riwaya ina pande mbili,
Upande wa kwanza ni wa wafanyabiashara na wanasayansi, hawa wamekuwa wanakuja na uvumbuzi ambao umeweza kutatua matatizo ya watu na kuanzisha biashara kubwa ambazo zinawapa mafanikio. Upande huu ndiyo unaifanya jamii kuwa bora kwa kuleta huduma mbalimbali kama za usafiri, viwanda, mafuta, vifaa vya kielektroniki na kadhalika.

Kwa kuwepo kwa uchumi huria ambao unaruhusu kila anayeweza kujituma kufanikiwa, taifa la marekani linapata ustawi mkubwa, kupitia mfumo wa uchumi wa ubepari. Watu wanakuja na mawazo mapya, ushindani unakuwa mkali na wale wenye uwezo wanafanikiwa na mafanikio yao yanakuwa na manufaa kwa jamii pia.

Upande wa pili wa riwaya ni wa serikali ambao umejaa wanyonyaji. Serikali inapata viongozi ambao hawana uwezo mzuri wa uongozi na hivyo wanakuja na sera mpya kwamba kila mtu anapaswa kunufaika sawa na wengine. Hivyo mfumo wa ubepari unapingwa na mfumo wa ujamaa unapewa nafasi. Mfumo huo wa ujamaa unataka mawazo yote yamilikiwe na kila mtu, na kila kitu kiwe cha kila mtu, kusiwepo na umiliki binafsi, hasa wa biashara na mashirika makubwa.

Hivyo, serikali kwa kutumia nguvu na mabavu inaleta miongozo mbalimbali ambayo lengo lake ni watu kuwa sawa na kunufaika kwa pamoja, hata kama hawafanyi chochote kikubwa. Hili linafanya wale wenye uwezo kuficha uwezo wao, kwa sababu hawanufaiki tofauti na wasio na uwezo.

Hili linafanya hali ya uchumi kuanza kuzorota, uzalishaji kupungua na viwanda na biashara mbalimbali kufungwa. Serikali kwa kuona mambo ni magumu, inazidi kulazimisha mfumo huo, kwa kuongeza kodi na kutaifisha viwanda na mashirika makubwa.

Kijana mmoja (John Galt) ambaye ana uwezo mkubwa wa kiakili anakataa mfumo huo na anaamua kuanzisha mgomo wa akili (mind strike). Yeye alikuwa mgunduzi wa mota yenye uwezo mkubwa, lakini kutokana kila ugunduzi kuchukuliwa ni wa kila mtu, aliamua kuharibu mota hiyo na kuanzisha mgomo wake.

Kwenye mgomo huu aliwashawishi wale wote ambao wananyanyaswa na serikali kwa sababu ya uwezo wao, wasikubali tena kutumia akili zao kwa manufaa ya serikali iliyojaa wanyonyaji. Hivyo, mmoja mmoja katika watu ambao walikuwa wana uwezo mkubwa waliungana naye, hivyo kupelekea uchumi kuzidi kuwa mgumu zaidi.

Pamoja na hayo, serikali bado haikukubali kubadili mfumo, badala yake ilizidi kunyonya wale waliobakia na taifa lilianza kuanguka. John Galt anaongea na taifa zima kupitia redio na kueleza hali ambayo taifa linapitia na nini kimesababisha.

Anaeleza mgomo wa akili unaoendelea na anasema wazi kwamba watu wote wenye uwezo mkubwa waliopotea kwenye jamii, ni yeye amewachukua na wapo wanaendelea na mambo yao makubwa.

Anatoa sharti la watu hao kurudi ni serikali kuachana na mfumo wa kijamaa na kinyonyaji na badala yake itoe uhuru kwa watu kufikiri na kuendesha maisha yao. Serikali isimamie yale muhimu, lakini uzalishaji ubaki kwenye mikono ya wananchi. Na akaonya kwamba kama serikali haitabadilika, taifa litaangamia.

Viongozi wa serikali kusikia ukweli huo walikasirika na wakaanza kumsaka John Galt, kwa lengo la kumrubuni ili akubaliane nao na awe upande wa serikali. Wanafanikiwa kumpata John Galt, lakini anakataa katakata kujihusisha na serikali hiyo kwa kulazimishwa kwa mtutu wa bunduki.

Anawaambia njia pekee ni serikali kujiuzulu na kuacha watu wenye uwezo mkubwa kuendesha nchi. Viongozi wanakataa hilo na hivyo wanapanga kutumia mbinu za mateso kumlazimisha akubali.

Katika kutumia mbinu hizo, ambazo nyingi zilishindwa, John Galt anaokolewa na wenzake na kuelekea kwenye eneo walilokuwa wametenga na walikokuwa wanaishi wale wote waliopotea kwenye jamii.

Nchi inafikia anguko la mwisho, silaha ya maangamizi iliyokuwa imetengenezwa kuwatisha wapinzani wa serikali inatumika vibaya na kuleta maangamizi makubwa. Machafuko makubwa yanatokea na serikali kuanguka. Na hapo ndipo John Galt na wenzake wanaporudi kuanzisha utawala mpya wenye mfumo sahihi unaoruhusu uhuru wa fikra na kujali uwezo binafsi wa mtu.

Hii ni kwa ufupi, kwenye uchambuzi wa sehemu tatu za riwaya hii tutajifunza mengi sana kuhusu uchumi, uongozi, falsafa, mafanikio, usaliti na hata mapenzi na jinsi mambo hayo yanaweza kuwa kikwazo au kichocheo cha mafanikio.

Hii ni riwaya ambayo inaendana sana na uhalisia, hasa wa hali ambayo dunia inapitia kwa sasa. Ambapo kuna watu wachache waliofanikiwa sana, na wengi ambao wana maisha ya chini na hivyo viongozi wenye tamaa ya madaraka wanawaaminisha wale wenye maisha ya chini kwamba adui yao ni wale waliofanikiwa sana. Kitu ambacho siyo sahihi.

Karibu tujifunze kwenye riwaya hii, ili tuwe na njia sahihi ya kuendesha maisha yetu ya mafanikio, tuweze kutunza uhuru wetu wa kufikiri na kutumia uwezo mkubwa tulionao. Pia yale tutakayojifunza yatatusaidia kuepuka hali ya jamii kuwachukia waliofanikiwa na pale tunapopata nafasi, basi kuwashawishi wengine nao kuishi misingi hii ya mafanikio.

Riwaya hii imebeba falsafa muhimu sana kuhusu maisha, falsafa ya uwezo wa mtu binafsi na uhuru wa kifikra, ni falsafa ambayo tukiielewa na kuiishi, tutakuwa na maisha bora.

Kwenye chambuzi zitakazofuata tutapata sehemu ya kwanza, ya pili na ya tatu ya riwaya hii na yale muhimu ya kujifunza na kufanyia kazi.
 
Dr naomba kufahamu tofauti ya utashi na akili !!
naomba kufahamu tofauti ya ubongo iliopo kati ya hao viumbe wengine na binadamu
 
Kutumia akili ndio, lakini pia kutumia roho kutakupeleka pale haswa unapopaswa kuwepo kama mwanadamu.
 
Dr naomba kufahamu tofauti ya utashi na akili !!
naomba kufahamu tofauti ya ubongo iliopo kati ya hao viumbe wengine na binadamu
Akili (mind) ina kazi tatu, kufikiri (reason), kuelewa (understanding) na utashi/kuamua (will). Hivyo utashi ni moja ya kazi za akili.
Tofauti ya ubongo (brain) wa binadamu na wanyama wengine ni sisi binadamu tuna sehemu mpya na kubwa ya ubongo ambayo inafikiri (neo cortex) wakati wanyama wengine hawana ubongo huu wa juu.
 
Kutumia akili ndio, lakini pia kutumia roho kutakupeleka pale haswa unapopaswa kuwepo kama mwanadamu.
Binadamu tuna vitu vitatu, mwili, akili na roho.
Roho ndiyo inakupa maana na sababu ya kuishi,
Akili inakuwezesha kufikiri na kufanya maamuzi,
Na mwili unatekeleza maamuzi hayo ili kifikia kusudi.
Vitu vyote hivi vitatu ni muhimu sana kwenye maisha yako.
Kikikosekana hata kimoja au kikawa dhaifu, maisha yako hayawezi kuwa sawa.
 
Back
Top Bottom