Hiki ndicho kinayakimbiza mawazo yako mazuri unapozishika fedha

Makirita Amani

JF-Expert Member
Jun 6, 2012
1,781
3,074
Rafiki yangu mpendwa,

Wengi wetu huwa tunakutana na hali hii.

Pale unapokuwa huna fedha unakuwa na mawazo mazuri sana.

Unakuwa na mipango mizuri kwamba ukipata fedha utazitumiaje vizuri ili upate manufaa makubwa.

Ukimuona mtu mwenye fedha anazitumia vibaya, unajiambia huyo hajui matumizi mazuri ya fedha.

Unajiambia ungepata fedha kama zake ungezitumia vizuri kabisa na ungepiga hatua kubwa.

Kimbembe kinakuja pale ambapo wewe mwenyewe unapata fedha.

Mawazo mazuri yote uliyokuwa nayo yanapeperuka.

Unazitumia fedha hizo kwa namna ya tofauti kabisa na mipango uliyokuwa nayo kabla hujawa na fedha hizo.

Ni mpaka fedha hizo zinapoisha ndiyo akili zinakurudi, unaona jinsi ulivyokosea na kupanga tena jinsi utakavyozitumia vizuri fedha pale utakapozipata.

Unaweza kudhani umejifunza, lakini utakapopata fedha hali ile ile inajirudia tena, mawazo mazuri yanapotea na kuja kurudi baada ya kuwa umezitumia fedha hizo hovyo.

Kuna watu wanaamini wana laana ndiyo maana hali hizo zinajitokeza kwao.
Wengine wanaamini kazi au biashara wanazofanya zimeandamwa na imani za kishirikina ndiyo maana wakipata fedha hawawezi kufanya kitu cha maana.

Lakini hayo yote siyo kweli, ni njia tu ya kuficha sababu kuu iliyo ndani ya mtu inayopelekea atumie fedha vibaya kila anapozipata.

Rafiki, huenda umewahi kufanya au imewahi kukutokea mlevi kukuambia maneno ambayo asingethubutu kukuambia kama angekuwa hajalewa.

Wengi husingizia kwamba ni pombe zimewafanya kusema waliyosema. Lakini ukweli ni kwamba pombe haimlishi mtu maneno, bali inaondoa ile aibu ya mtu kusema ya moyoni.

Yaani kile ambacho mtu anasema akiwa amelewa, ndicho ambacho amekuwa anafikiria kwa muda mrefu, pombe imeondoa tu ile aibu ya kuyatoa mawazo hayo.

Hivyo pia ndivyo ilivyo kwenye fedha, kuna tabia kuu za kifedha ambazo kila mtu anazo. Tabia hizi zimezama ndani kabisa na ndiyo zimebeba mtazamo mzima ambao mtu anao.

Wakati mtu hana fedha, huwezi kuziona tabia hizo, kwa sababu hakuna namna ya kuzionyesha.
Ni mpaka pale mtu anapopata fedha ndiyo tabia zake kuu za kifedha zinajidhihirisha.

Hivyo usiumie sana kwa yale unayofanya unapokuwa na fedha, bali jua yanafunua kile kikubwa kilicho ndani yako.

Na baada ya kuzijua tabia zako kuu kifedha, unaweza kuzizuia zisiwe kikwazo kwako pale unapopata fedha.

Baadhi ya mambo unayoweza kufanya ili kuzuia tabia zako kuu zisiwe kikwazo kwako kifedha ni kama ifuatavyo.

Moja ni kubadili mtazamo wako mkuu kuhusu fedha. Jiangalie ni fikra na msukumo upi unaoupata ukiwa na fedha, huo ndiyo mtazamo wako mkuu.

Kama kila ukipata fedha unasukumwa kuzitumia, jua mtazamo wako wa kifedha ni matumizi.

Badili mtazamo wako mkuu kifedha, ili unapoona fedha usioe tu matumizi, bali uone mengine mengi unayoweza kufanya na fedha hizo.

Mbili ni kutengana na fedha zako haraka. Pale unapopata fedha, usikae nazo kwa muda mrefu, badala yake zipeleke moja kwa moja kwenye mipango uliyokuwa nayo au ziweke kwenye gereza ambalo huwezi kuzitoa kirahisi. Mfano akaunti ya benki ambayo siyo rahisi kutoa.

Fedha huwa hazikosi matumizi ukiwa nazo, hivyo ukitengana nazo mapema, utazuia tabia yako isikuathiri.

Tatu ni kuweka juhudi zako kwenye kutafuta fedha zaidi. Haijalishi kiasi gani umepata, endelea kutafuta zaidi. Hiyo itaondoa ile hali ya kuona una fedha nyingi na hivyo kudhani unaweza kupumzika na kustarehe. Kama utaona fedha uliyopata ni kidogo kuliko unayohitaji, utasukumwa kutafuta fedha zaidi na siyo kutumia fedha uliyopata.


Rafiki, kujifunza zaid kuhusu fedha na tabia, hakikisha unapata na kusoma vitabu hivi viwili;

Cha kwanza ni ELIMU YA MSINGI YA FEDHA ambayo inakupa maarifa ya kukufikisha kwenye uhuru wa kifedha.

Cha pili ni TABIA ZA KITAJIRI ambacho kinakupa mwongozo wa jinsi tabia zako za ndani zinavyoathiri fedha zako na jinsi ya kujenga tabia sahihi kwako.

Kupata vitabu hivyo wasiliana na 0752 977 170.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda sana

Muuza Matumaini Kocha Dr Makirita Amani.
 
Back
Top Bottom