Hii stori ya kweli inasisimua kutokea shuleni Mazinde Juu

MENISON

JF-Expert Member
Apr 26, 2013
680
1,000
Happy, binti mwenye akili, aliyetoka katika familia isiyojiweza lakini alifanya vyema katika matokeo yake ya kidato cha 4 katika shule jirani ya serikali, hivyo meneja wa shule, Padri Damian Milliken alijitolea kumsomesha Mazinde Juu na kumhudumia hadi atakapomaliza kidato cha 6 .

Baada ya kupokea msiba ule, nilijadiliana na wenzangu wa chumbani na wanadarasa wenzetu tukamuomba mkuu wa shule Sister Evetha Kilamba atupe ruhusa kuhudhuria mazishi ili mwenzetu asijione mpweke kwani aliishi karibu na shule. Sr. Evetha alikubali na tukachanga rambirambi kishasiku ilipowadia tukaenda kwenye mazishi. Tulipanda milima, hakika kulikuwa mbali. Tulipofika, wote tulishikwa na simanzi isiyo kifani, mama yake alikuwa na matatizo ya akili ya muda mrefu, hali ya nyumba waliyokuwa wanaishi ilisikitisha sana. Ilikuwa ndogo na isiyo imara.

Tulimaliza mazishi, tukarudi shule tukaketi na waliokuwa viongozi wakati nikiwa dada mkuu tukawaelezea hali ya mwanadarasa mwenzetu ilivyo. Tuliumia sana kufahamu mwenzetu alikuwa akiishi katika nyumba ile na familia yao kubwa.

Katika majadiliano ya tufanyeje kumsaidia, wazo moja TUMJENGEE NYUMBA. Kweli, tukakubaliana tumjengee nyumba. Nafahamu wazo hilo kutoka kwa mabinti wadogo linaonekana haliwezekani lakini tulipiga moyo konde tukasema kwa darasa lenye wanafunzi 117, hatushindwi kuinua nyumba kwa ajili ya mwenzetu.

Moja kwa moja nikaenda ofisini kwa Sr.Evetha, nikamueleza kila kitu hadi mpango wetu. Alifurahishwa kusikia vile, akatupa ruhusa ya kuanza kuchangishana na akakubali kututengenezea fomu za kuwachangisha ndugu jamaa na marafiki tutakapokuwa likizo.

Happy alikuwa bado hajarudi shule hivyo tukaitana wote 117 tukakubaliana kima cha chini cha mchango wa kutoa na deadline. Na papo hapo michango ikaanza kumiminika. Tulipofunga shule, kila mwanafunzi wa kidato cha 6 alipewa fomu ya kwenda kupitisha mchango. Jambo hili tulifanya kwa siri sana, ilikuwa kati yetu, Sr.Evetha, walimu wa darasa na Fr. Damian tu.

Niliporudi nyumbani nilijitahidi kukusanya michango kadri nilivyoweza, nakumbuka wazazi wangu wlainiombea michango kutoka kwa rafiki zao pia.

Kila nilipomaliza vipindi vyangu tuition pale Mapambano, nilichukua fomu yangu nikapitisha kwa walimu na yeyote yule Watu wengi sana waliisoma na kuniambia, "mnadhani nyumba kujenga ni rahisi? hamuwezi kufanikisha"Lakini nilipiga moyo konde na kuwaomba wachangie chochote kidogo.

Hii ilikuwa likizo ya mwisho tulipofungua shule tulikuwa tunaenda kumaliza na lazima nyumba ilipidi ikamilike kabla hatujamaliza shule.
Siku ikawadia, tukafungua shule.

Sikuamini macho yangu hela zilivyomiminika mkononi mwangu nikawa kila baada ya night prep watu wanakuja kitandani kwangu kuwasilisha michango.

Kumbuka, Happy alikuwa akilala kitanda cha juu, hivyo aliniuliza ile ni michango ya nini. Nikamdanganya kuwa ni zawadi za walimu kwa ajili ya graduation na hela ya kuprint tshirt za form 6, nikamwambia asihofu nimemlipia, hadi nikamuonyesha jina na kiasi akaamini kabisa.

Tukakabidhi milioni kadhaa kwa Sr.Evetha, tukamwambia aanze na kiasi hicho wakati tunaendelea kujichanga kadri tunvyoweza. Fr.Damian alipoona kiasi kikubwa tulichochanga, akasema yupo tayari kumalizia hela yote itakayobaki, kiwanja kikatafutwa, msingi ukaanza kuinuliwa.

Wakati tukiendelea kujiandaa na mitihani ya taifa, nyumba ilikuwa inajengwa na Sr.Evetha aliniita na kunionyesha maendeleo kadri alivyoweza.

Basi kwakuwa jambo jema halifichiki, wanakijiji wakayaongelea wakijua Fr.Damian na Sr.Evetha ndio wanamjengea nyumba,taarifa zikamfikia Happy.

Siku moja tukiwa tumepumziak bustanini, akaniambia, ""Wizo, nimeambiwa Sister na Father waannijengea nyumba, naomba uongee na Godson ili anitengenezee zawadi kwa ajili yao"

Niliona furaha yake, nikajifanya na mimi nimekuwa surprised, nikamwambia asiwaze nitamlipia hizo zawadi anazotaka kuwatengenezea.
Siku zikayoyoma, tarehe 13 Mei, 2015 tukamaliza mtihani wa taifa, tulikubaliana na Sister kuwa tarehe 14 Mei ndio tutaenda kumkabidhi Happy nyumba, wakati huo ilikuwa imekamilika, mafundi wa karakana ya shule walikuwa wanamalizia kutengeneza samani za ndani, makochi, vitanda, meza n.k kwa ajili ya nyumba.

Basi, shule nzima mtihani wa taifa, tulikubaliana na Sister kuwa tarehe 14 Mei ndio tutaenda kumkabidhi Happy nyumba, wakati huo ilikuwa imekamilika, mafundi wa karakana ya shule walikuwa wanamalizia kutengeneza samani za ndani, makochi, vitanda, meza n.k kwa ajili ya nyumba.

Basi, shule nzima ikaambiwa kuwa form 6 tunenda picnic (ni kawaida kwa shule kupeleka wanafunzi picnic), basi kila mtu alijua tunapendelewa kutoka out tu.

Happy akaambiwa na Sister aende na Matron Lushoto Mjini kununua viatu vya graduation ambayo ingefanyika tarehe 16 Mei, kisha akirudi ndio aende nyumbani kumsalimia mama yake. Wakati Happy akiwa mjini, form 6 tukiongozana na walimu, wapishi na masister wengine tulianza safari ya kwenda kwa kina Happy.

Ilikuwa safari ndefu kwa miguu lakini tuliinjoi sana. Wanakijiji walitushangaa kwani haikuwa kawaida kuwaona watoto wa Mazinde mtaani, hivyo vitoto vingi vilitufuata nyuma hadi tukafika.

Kwa mara ya kwanza tukayaona matunda ya kazi ya mikono yetu. NYUMBA. Nilitokwa na machozi. Niliingia ndani, sebule, vyumba vitatu vya kulala, jiko, stoo na choo na bafu. Mafundi walikuwa wakipaka rangi Tulikuwa na furaha isiyoelezeka.

Nyumba viwili tayari vilikuwa na vitanda na magodoro mapya. Nje wapishi walipika na kuandaa chai na maandazi na chakula cha mchana.
Ngoma ya kisambaa ilipigwa sote tukacheza kwa furaha tukimsubiria Happy.

Happy aliwasili akiwa na Sr.Evetha Ilikuwa surprise KUBWA kwake. Hakuamini macho yake alipotukuta wanadarasa wenzake WOTE tukimsubiri kwa bashasha. Alilia kwa furaha. Sister akamwambia, "Happy, wenzako ndio wamekujengea hii nyumba. Wao ndio walitoa wazo, wakachanga kadri walivyoweza, sisi kama shule tukamalizia na kutoa rasilimali tulizoweza"

Happy hakuamini macho yake, nakumbuka tulisimama nje tukashikana mikono kwenye duara moja akasema, "Tuendelee kushikamana kama chemical bonds"

Akanivuta pembeni akasema, "Yani wizo ulikuwa unajua siku zote, aise siamini ile michango"
Tukakumbatiana. Akakabidhiwa funguo ya nyumba, tukasali, Padri akaibariki nyumba, tukacheza ngoma tena, tukala, tukanywa kisha sote tukarudi shuleni.

Tuliporudi, ndio Sr.Evetha akatangazia shule nzima tulichokifanya kwa mwenzetu. Kila mtu hakuamini.

Ikawadia siku ya mahafali, na mbele ya wazazi waalikwa na wageni wote, wakaproject sehemu ya video iliyorekodiwa wakati wa kumkabidhi Happy nyumba.

Happy akakaribishwa, akatoa neno. Wazazi waliguswa sana na kile tulichokifanya.
Fr.Damian akasema, "Kwa walichofanya watoto hawa, sisi hatuna budi kujifunza kwao, UPENDO" Kisha akasema, "Wameniinspire hivyo nitamsomesha Happy chuo hadi atakapochoka mwenyewe kusoma", Mgeni rasmi alikuwa Mh. Ridhiwani Kikwete, naye akaongeza mchango wa kukamilisha nyumba na mahitaji ya nyumbani, ghafla wazazi, wageni kila mtu akaongeza mchango, Happy akajipatia Milioni kadhaa na ahadi kedekede.

Licha ya jambo hili kuwaacha watu na machozi machoni, lilitoa funzo kubwa ambalo halijawahi kutokea katika historia ya Mazinde Juu.
UPENDO USIOPIMIKA. Upendo wa mabinti 117 waliojitoa kubadilisha maisha ya binti mmoja, na kumfungulia mlango wa mafanikio zaidi. Nakumbuka vizuri Sr.Evetha alivyoniita pale mbele na kunitambulisha kama organizer wa kampeni hiyo. Nakumbuka tabasamu la mama huku akitokwa na machozi ya furaha namna binti yake nilivyofanya jambo jema.

Nakumbuka Fr.Damian aliponishika mkono na kunishukuru. Sijawahi kuona upendo wa namna ile.
Ni jambo linalofanya nijivunie kuwa sehemu ya familia ya Mazinde Juu.
Tumelelewa katika UDADA, UNDUGU na UPENDO.

Kuvaa viatu vya wengine na kuona magumu wanayopitia.
Leo, Happy amehitimu ni mwalimu wa Sayansi kwasababu ya UPENDO USIOPIMIKA. Tulikubaliana kumjengea nyumba kwasababu tulitaka kila siku akumbuke kuna mabinti 117 waliowasha mshumaa na kumshika mkono kutembea naye wakati wa kiza nene.

Unapogusa maisha ya mtu, hujui namna gani unaweza kumfungulia mlango mkubwa kwa msaada mdogo unaotoa.
UPENDO NI UFUNGUO. Kila mara nikiwatazama mabinti wale 117, leo hii ni wadada wakubwa, wanasoma, wana kazi, wana biashara, wameolewa na wengine wana watoto.

Nakumbuka jinsi ambavyo kila mmoja wao alitoa kidogo alichonacho ili kugusa maisha ya mwenzao.

Cheti hiki nilikabidhiwa kama shukrani. Hivyo, kamwe sichoki kuongelea Mazinde Juu, kwani ilibadilisha maisha yangu na kubadilisha maisha ya wengi sana.

MAISHA NI SAFARI, JARIBU.
Hivyo katika safari hii, usiache kugusa maisha ya wengine KWA MOYO WOTE, kama motto wa Mazinde Juu usemavyo.
Tunainuka, kwa kuinua wengine.


Imeandikwa na Kuduishe Kisowile X Head girl. Nimeitoa huko twitter.
 

Domhome

JF-Expert Member
Jun 28, 2010
2,696
2,000
Imenitoa machozi, inasikitisha sana, inatufunza Upendo walonao watoto wetu, hakika ni funzo lifunzalo na ni hekima ihekimishayo....

Nazidi kujifunza vingi ktk umri nilonao hakika tuwathamini watoto wetu. Kwani kwenye hili watoto hao 117 wamejiwekea hazina kule kusiko na Nondo wala Kutu yaani, Mbinguni.

Upendo....Upendo...Upendo
 

reyzzap

JF-Expert Member
Oct 3, 2014
5,267
2,000
Duu umenikumbusha mbali...
Nakumbuka hii issue vizuri sana,
Na niliombwa mchango, japo Nami sikuamini kivile nikahisi kizinga ila nilichanga, na hata siku ya graduation nilikuwepo.

Wewe utakua ulisoma na akina Marietha.

Mara ya mwisho kwenda pale ilikua wanazidi kuporomosha majengo tuu..

Fr. Damiani sasa kazeeka sana,
Kasaidia watu wengi sana yule mzungu.
St. evetha, Msambaa mwenyewe in control.
Mr & Mrs Chambo walistafu, Wazigua mafundi wa phyz na maths.

Moja ya shule kubwa na Bora zaidi Tz bila ubishi.

Binadamu wengi wanaumbwa na kuzaliwa wakiwa na mioyo safi, ya upendo, msaada, kugawa faraja na amani, ila Wanayo yakuta huku duniani kwa waliotangulia yanawageuza kua majuha....

Sometimes when you remember your old better days with the feelings of Love, unify, joy and happiness wish time travel was possible, that you can rejuvenate, Go there, and never come back in this terrifying folks world.
 

Paploman

JF-Expert Member
Apr 13, 2019
1,503
2,000
Duu umenikumbusha mbali...
Nakumbuka hii issue vizuri sana,
Na niliombwa mchango, japo Nami sikuamini kivile nikahisi kizinga ila nilichanga, na hata siku ya graduation nilikuwepo.

Wewe utakua ulisoma na akina Marietha.

Mara ya mwisho kwenda pale ilikua wanazidi kuporomosha majengo tuu..

Fr. Damiani sasa kazeeka sana, St. evetha yupo in control.
Mr & Mrs Chambo walistafu.
Huyo marietha lazma atakuwa wife material..vijana changamkeni
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Similar Discussions

Top Bottom